Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Doto Mashaka Biteko (7 total)

MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini kwa kuonesha mfano kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya Dhahabu ya Ishokelahela, Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Susanne Masele naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama hapa, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Imani kubwa aliyonipatia na akaona naweza kumsaidia kwenye Sekta hii ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wa Madini wadogo wa Ishokelahela Wilayani Misungwi walivamia na kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Leseni kubwa ya utafutaji wa madini inayomilikiwa na Kampuni ya Carlton KitongoTanzania Limited yenye ukubwa wa kilomita za mraba 12.4 tokea mwezi Julai, 2017. Kabla ya hapa wachimbaji hao walikuwepo lakini kwa kiasi kidogo. Mpaka kufikia sasa leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 1000 ambao wanachimba madini hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya Carlton KitongoTanzania Limited ilitolewa tarehe 5 Agosti, 2014 na itamaliza muda wake wa awali tarehe 4 Agosti 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited ambaye ni mmiliki wa leseni hiyo waliamua kutenga eneo kwa ajili ya kuwaachia wachimbaji wadogo ambalo likuwa linamilikiwa na kampuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano hayo yalihitimishwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2017 kati ya mmiliki wa leseni na vikundi ambayo viliungana kuunda kikundi kimoja kwa jina la Basimbi and Buhunda Mining Group. Nakala ya makubaliano hayo ipo Ofisi ya Madini Mwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Misungwi. Vikundi hivyo vilipatikana baada ya Wizara kupitia Ofisi yetu ya Madini Mkoani Mwanza kutoa elimu ya umuhimu ya kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za uchimbaji madini ili ziweze kuwa na tija zinazozingatia matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini, leseni za wachimbaji madini katika eneo hilo zitatolewa kwa vikundi hivyo mara tu baada ya taratibu za kisheria za kushughulikia maombi hayo kukamilika.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mgodi a Tanzanite ulioko Mererani, Wilaya ya Semanjiro ni mgodi wenye idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi katika mgodi huo na kumekuwa na historia ya matukio ya maafa kila mwaka ya vifo vya watu wengi.
(a) Je, Serikali imefanya utafiti gani ili kubaini chanzo cha maafa hayo yanayolikumba Taifa kila mwaka na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha utaratibu maalum kwa wamiliki wa vitalu vya Tanzanite kuwalipa kifuta jasho wahanga wote wanaopatwa na maafa wanapokuwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya taarifa za ajali yanaonesha kuwa ajali nyingi husababishwa na wachimbaji wadogo kutokuzingatia tahadhari ya usalama wanapotekeleza majukumu yao ya uchimbaji madini. Hivyo, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji na kuwaelimisha wachimbaji kuchukua tahadhari za usalama wakati wa kufanya kazi pamoja na kuwahamasisha kuunda timu za wakaguzi katika maeneo yao kutoka miongoni mwa wachimbaji ambao hupewa elimu ya ukaguzi na wataalam wetu wa Wizara ya Madini. Hivyo, nawasihi wachimbaji wa madini kutambua umuhimu wa kuzingatia taratibu na usalama wa kazi kwa uchimbaji ili kulinda afya na uhai wao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kupitia Sheria Namba 20 ya mwaka 2008 ya Fidia ya Wafanyakazi. Wizara itahamasisha wamiliki wa leseni na wachimbaji kujiunga na mfuko huu ili kupata kifuta jasho wanapopatwa na maafa wanapokuwa kazini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa katika Jimbo la Kwela, kwenye ukingo wa Milima ya Lyamba Iyamfipa inayoambaa katika Kata za Mfinga, Mwadui, Kalumbaleza, Nankanga, Kapeta hadi Kaoze, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiokota madini mbalimbali bila kutambua ni madini ya aina gani.
(a) Je, Serikali imeshafanya utafiti wowote katika maeneo hayo?
(b) Kama jibu ni hapana, je, ni lini utafiti utafanyika ili kujua eneo hilo lina madini gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia miaka ya 1950 Serikali imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali wa awali wa madini kwenye maeneo ya Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa yakiwemo maeneo ya Jimbo la Kwela kwenye mwambao wa milima ya Lyamba Iyamfipa. Utafiti wa awali ulibaini uwepo wa madini mbalimbali yakiwemo madini ya vito kama vile Garnet, Kyanite, Zircon na Sapphire na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za uwepo wa madini katika Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa zinapatikana kwenye ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo nachukua nafasi hii kuwashauri sana ndugu zetu wote wakiwemo wa Jimbo la Kwela kutumia Ofisi zetu za Madini za Kanda ya Magharibi iliyoko Mpanda na taarifa zilizopo kwenye ofisi ya Wakala wa Jiolojia iliyoko Dodoma, ambapo wako wataalam watawasaidia kuyachambua madini hayo pamoja na kuwashauri namna ya kufaidika na rasilimali hiyo ya madini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Mji wa Tunduru yako mabango mengi yanayoelezea ununuzi wa madini jambo linaloashiria upatikanaji mkubwa wa madini kutoka kwa Wachimbaji wadogo wadogo ambao hawatambuliwi kwa mujibu wa sheria:-
Je, ni lini Serikali itawatengea maeneo ya kuchimba madini na kuwatambua Kisheria Wachimbaji hao wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kabla sijajibu swali hili naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume mpya ya Madini.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017 inawatambua wachimbaji wadogo. Kwa kutumia sheria hiyo Serikali inatoa leseni za uchimbaji za madini (Primary Mining Licenses) kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mabango na maduka mengi yanayotangaza uwepo wa madini ya vito katikati ya Mji wa Tunduru huko Mkoani Ruvuma. Baadhi ya madini ya vito hayo yaliyopo Wilaya ya Tunduru ni pamoja na Sapphire, Ruby, Garnet na kadhalika. Maduka ya madini yenye mabango ni ya wafanyabiashara wakubwa wenye leseni kubwa (Dealers License) ambazo huhuishwa kila mwaka kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Serikali ilitenga eneo la Mbesa, Wilaya ya Tunduru, lenye ukubwa wa hekta 15,605.3 kwa tangazo la Serikali Namba tano la tarehe 22 Februari, 2013, kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini ya shaba. Hadi Aprili, 2018 jumla ya leseni hai 649 za wachimbaji wadogo wa madini yaani (PML) zimetolewa Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri taarifa za utafiti katika maeneo hayo zitakavyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili wachimbaji wadogo hao waweze kuchimba madini siyo kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, wachimbaji wadogo wanahimizwa kuomba leseni ili wafanye shughuli za utafutaji wa madini kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuinua vipato vyao kutoa ajira kwa Watanzania, kuchangia pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wachimbaji wadogo wadogo maeneo yaliyopimwa na kuwa na uwepo wa madini kama dhahabu, ikiwemo Moroko katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine yenye madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1996, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini. Tangu kipindi hicho hadi sasa, Wizara ya Madini imetenga jumla ya maeneo 46 katika sehemu mbalimbali nchini yenye ukubwa wa hekta 281,533.69. Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadiri yatakavyokuwa yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Geita Wizara imetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa leseni kama ifuatavyo: Eneo la Nyarugusu leseni 41; eneo la Rwamgasa leseni 36; eneo la Isamilo/ Lwenge leseni 22 na eneo la Mgusu leseni 22. Kwa sasa eneo la Moroko alilolitaja Mheshimiwa Mbunge lipo ndani ya leseni ya utafiti yenye Na.8278 ya mwaka 2012 inayomilikiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita. Maeneo mengine ya mkoa huo yataendelea kutengwa kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 16 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kutumia taasisi zake za GST pamoja na STAMICO itaendelea kufanya utafiti ili kubaini uwezo wa mashapo ya madini katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatenga kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini. Hii itawezesha wachimbaji wadogo wa madini kufanya kazi na kuchimba kwa uchimbaji wa tija. Ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini mgodi utafunguliwa katika eneo la Nyakafuru Wilayani Mbogwe baada ya utafiti kuchukua muda mrefu kwenye eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Nyakafuru lenye leseni ya ukubwa wa kilomita za mraba 17.53 linamilikiwa na Kampuni ya Mabangu Limited Resources, kampuni ambayo Kampuni tanzu ya Resolute Tanzania Limited kupitia leseni ya kutafuta madini PL Na.5374 ya mwaka 2008. Leseni hiyo ambayo ilihuishwa mara mbili na baadaye kuongezewa muda wa kipindi cha miaka miwili yaani extension kuanzia tarehe 24 Oktoba, 2016 ili kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na itamaliza muda wake tarehe 23 Oktoba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 yaani The Written Laws Miscellaneous Amendment Act 2017 yaliondoa uhitaji wa leseni ya utafutaji wa madini kuongezewa muda wa kufanya utafiti baada ya muda wa leseni kuhuishwa kwa mara ya pili kumalizika. Kwa sasa sehemu ya eneo hilo la leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa mashapo yanayofikia takribani tani 3.36 yenye dhahabu ya wakia 203,000 yamegunduliwa na jumla ya Dola za Kimarekani milioni 1.83 zimetumika kufanya utafiti katika eneo la mradi. Aidha, Tathmini ya Athari ya Mazingira ilishafanyika na kupewa cheti cha tarehe 16/10/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, Kampuni ya Mabangu Mining Limited kupitia Kampuni mama ya Resolute (Tanzania) Limited inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kiasi cha jumla Sh.143,077,421,804 ikiwa ni deni la kodi ambalo wanatakiwa kulilipa. Mgodi wa Nyakafuru unaweza kuendelezwa baada ya deni hilo kuwa limelipwa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa wa madini na gesi asilia aina ya carbon dioxide:-
Je, ni lini Serikali itaenda kufanya utafiti wa kutosha kwenye Kata ya Lufilyo ambapo kuna madini aina ya marble (marumaru)?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa madini ya marble katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ambapo Kampuni ya Marmo Granito inamiliki leseni moja ya uchimbaji wa kati yenye Namba ML 250 ya mwaka 2006 na leseni 10 za uchimbaji mdogo wa madini hayo zenye namba PML 0007657 – 0007666 za mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utambuzi huo ni kutokana na utafiti wa awali uliofanywa kati ya mwaka 2005 hadi 2007 na Kampuni ya BGR ya Ujerumani kwa ushirikiano wa taasisi za Serikali (STAMICO na GST). Utafiti huo ulipelekea kugunduliwa kwa madini hayo yenye rangi ya kijani na nyeupe katika Kijiji cha Kipangamansi kilichopo katika Kata ya Lufilyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itaendelea kufanya utafiti wa awali wa kijiolojia ili kubaini maeneo mengine yenye madini hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Vilevile utafiti wa kina utafanyika ili kubaini ubora na wingi wa upatikanaji wa madini hayo na kuishauri Serikali. (Makofi)