Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hamadi Salim Maalim (8 total)

MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Uvuvi ni moja ya vipaumbele vinavyosaidia kusukuma maendeleo ya wananchi wengi wa Tanzania na Taifa letu ni miongoni mwa mataifa maskini duniani:-
Je, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kwa kiasi gani ili kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo wa Tanzania ili kusaidia maendeleo ya Taifa na pia kujikwamua na umaskini uliokithiri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Maendeleo na Usimamizi Shirikishi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambao unatekelezwa Tanzania bara na Visiwani. Mradi umelenga kuboresha utawala bora kwenye jamii za wavuvi, kusaidia mitaji, kutoa elimu ya uvuvi endelevu na kuboresha miundombinu ya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Development Bank - TADB) na dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB) ili kutoa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kununua zana za uvuvi. Pia Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi wajiunge katika Vyama vya Ushirika ikiwemo kuanzisha SACCOS ili kuweza kukopesheka kwenye Taasisi nyingine za kifedha
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa wavuvi wadogo ili waweze kuvua katika bahari kuu. Hadi sasa wawakilishi wa wavuvi 99 kutoka Kamati za Uvuvi Zanzibar na Vikundi vya Usimamizi wa Uvuvi (BMUs) Tanzania Bara wamepatiwa mafunzo hayo wakiwemo 47 kutoka Pemba ikiwemo Jimbo la Kojani. Wavuvi hawa baada ya kupatiwa mafunzo hutakiwa kurudi na kufundisha wenzao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo haya ni endelevu na katika mwaka wa fedha 2016/2017 imepangwa wavuvi 50 wapatiwe mafunzo ya namna hiyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI imekuwa ikitoa mafunzo kwa wavuvi walio katika Kamati za Uvuvi na BMUs namna ya kudhibiti uvuvi haramu ili kuwahakikishia wavuvi wadogo uvuvi endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mpango kutoa ruzuku kwa wavuvi wadogo unaolenga kuwasaidia kuoata zana bora na vifaa vya kuvulia zikiwemo injini za boti kwa kuchangia asilimia 40% ya gharama. Katika awamu ya kwanza, injini 73 zimenunuliwa na taratibu za kuzisamabaza zinaendelea.
Vilevile, Serikali kupitia miradi na programu mbalimbali imejenga mialo na masoko ya samaki katika Ukanda wa Ziwa Victoria 29, Ziwa Tanganyika minne na Bahari ya Hindi mitatu. Kuwepo kwa mialo hii kumepunguza upotevu wa samaki baada ya kuvuliwa hivyo kuongeza thamani na bei ya samaki kwa wavuvi wadogo. Naomba kuwasilisha.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR (K.n.y. MHE. HAMADI SALIM MAALIM) aliuliza:-
Jeshi la Polisi ni chombo muhimu kinacholinda usalama wa raia na mali zao. Askari hawa wanapomaliza mafunzo yao kwa ngazi mbalimbali kama vile Sajenti, Staff Sajenti, Meja na nyingine, hucheleweshwa sana kulipwa maslahi yanayoendana na vyeo vyao:-
Je, ni kwa nini Askari hao hawalipwi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hamadi Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari Polisi hupanda vyeo kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na vyeo hivyo huambatana na kuongezeka kwa maslahi yao kulingana na cheo kilichopandishwa. Mwaka 2014/2015 jumla ya Askari 1,657 wa vyeo vya uongozi mdogo walipandishwa vyeo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na ucheleweshaji wa ulipwaji wa mishahara inayolingana na vyeo katika Jeshi la Polisi. Serikali mara zote imekuwa ikijitahidi kurekebisha mishahara ya vyeo vipya kwa haraka iwezekanavyo kwa Askari waliopanda vyeo. Yapo matatizo ya kiufundi yaliyojikeza wakati wa zoezi la kurekebisha mishahara na kutokea baadhi ya Askari kutorekebishiwa mishahara yao. Hata hivyo, juhudi hufanyika ili kutatua tatizo hilo mara mhusika anapowasilisha malalamiko yake Polisi Makao Makuu. Kitengo cha Maslahi Makao Makuu hupokea malalamiko na kuwasiliana na mamlaka za ulipaji ili kutatua tatizo hili. Aidha, naomba nitoe wito kwa Askari yeyote ambaye amepatwa na tatizo hili awasiliane na viongozi katika Kamandi yake au Makao Makuu ya Polisi, Idara ya Maslahi ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili haraka iwezekananvyo.
MHE. HAMADI SALIM MAALIM aliuliza:-
Je, ni kwa nini Askari wa Jeshi la Polisi hucheleweshwa maslahi yanayoendana na vyeo vyao pindi wanapomaliza mafunzo kwa ngazi mbalimbali kama vile Koplo, Sajent, Staff Sajenti, Meja na vingine?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamadi Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Kwanza nikiri, ni kweli kumekuwepo na matatizo ya Askari kupanda vyeo na kucheleweshewa malipo yanayoambatana na kupanda vyeo hivyo. Askari Polisi kupanda vyeo kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na vyeo hivyo kuambatana na kuongezeka kwa maslahi kulingana na cheo walichopandishwa. Kwa mwaka 2014/2015, jumla ya askari 1,657 wa Vyeo vya uongozi mdogo walipandishwa vyeo mbalimbali na mwaka 2015/2016, Askari wapatao 3,017 walikuwa katika Vyuo vya Polisi wakihudhuria mafunzo na hivyo kupandishwa vyeo kuwa maafisa na wakaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na ucheleweshaji kama nilivyosema wa mafao haya yanayolingana na vyeo walivyopanda kijeshi na Serikali mara zote imekuwa ikijitahidi kurekebisha mishahara ya vyeo vipya kwa haraka iwezekanavyo kwa askari waliopanda vyeo. Yapo matatizo ya kiufundi yanayojitokeza wakati wa zoezi la kurekebisha mishahara na kutokea baadhi ya askari kutorekebishiwa mishahara yao na hivyo juhudi hufanyika ili kutatua tatizo hilo mara moja na mhusika anapowasilisha malalamiko yake Polisi ama Makao Makuu.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Miongoni mwa stahiki za askari polisi anapohamishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ni nauli ya askari huyo na wategemezi wake pamoja na fedha za kusafirishia mizigo:-
Iwapo mwajiri atashindwa kumlipa askari huyo stahiki
zake zote hizo, je, askari huyo atapaswa kuhama kwa gharama zipi na kuripoti mkoa wake mpya aliopangiwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi hutoa uhamisho kulingana na mahitaji pale Inspekta Jenerali wa Polisi anapoona kuna umuhimu wa kuongeza nguvu eneo fulani ambalo ni tete kwa wakati huo. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 59(5)(a) ya Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO). Askari anayehamishwa atalipwa mafao yake kama ilivyoelekezwa katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Toleo Na. 259 iwapo hakuhamishwa kwa makosa ya kinidhamu. Aidha, askari anayeomba kuhama eneo moja kwenda eneo lingine kwa sababu zake binafsi hatalipwa mafao hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, inapotokea dharura ya askari kuhitajika kwenda kutoa huduma eneo lingine, askari husika atatekeleza amri ya uhamisho haraka wakati stahili zake zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu za fedha. Kwa taratibu za Kijeshi, askari hawezi kusubiri malipo katika mazingira ambayo anakwenda kuokoa maisha ama kulinda maslahi ya Taifa katika eneo husika.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 inatoa uhuru wa faragha kwa raia.
Je, kwa nini Jeshi la Polisi linapokwenda kupekua kwenye nyumba yenye mume na mke hutumia askari wa kiume peke yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upekuzi ni jukumu ambalo sheria imelipa Jeshi la Polisi na utaratibu wake umeainishwa wazi namna ambavyo upekuzi utafanyika kwenye maeneo mbalimbali. Kifungu cha 38 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 inatoa masharti na utaratibu wa kuweza kufanya upekuzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba, majengo na vyombo vya usafiri kama magari, boti na kadhalika endapo Afisa wa Polisi atakuwa amehisi na amejiridhisha pasipo na shaka kwamba kuna sababu ya kutosheleza kuwa kuna uwezekano wa kosa kutendeka au ushahidi kupatikana kuthibitisha kosa lililotendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, upekuzi wa makazi ya nyumba yenye mke na mume sheria haijaweka masharti ya ni askari wa jinsia gani anatakiwa kufanya upekuzi. Hata hiyo, Jeshi la Polisi kwa kutumia Kanuni ya Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) pia kwa kuzingatia busara na utu wa mwanadamu huwa inazingatia utaratibu wa kupeleka askari wa kike na wa kiume pale upekuzi unapofanyika kwenye makazi ya mume na mke.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Kwa kuwa Mabadiliko ya Kumi (10) ya Katiba ya Zanzibar yanaitambua Zanzibar kuwa ni nchi.
Je, ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itairuhusu Zanzibar kuwa na uwakilishi rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 2(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake imebainisha kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo. Aidha, Jedwali la Kwanza kwenye Katiba hiyo limebainisha kuwa masuala ya mambo ya nje ni masula ya Muungano.
Kwa muktadha huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa maslahi yote ya Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yanazingatiwa ipasavyo. Kabla ya kushiriki katika Mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kumekuwa na vikao vya maandalizi ambavyo hushirikisha pande zote mbili za Muungano ili kuandaa msimamo wa pamoja wenye kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hushiriki katika ngazi zote za Mikutano ya Wakuu wa Nchi Wanachama, Baraza la Mawaziri la Jumuiya na Mabaraza ya Mawaziri ya Kisekta yafuatayo:-
(a) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uwekezaji, Fedha, Viwanda na Biashara;
(b) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya;
(c) Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Uchumi, Mawasiliano na Hali ya Hewa;
(d) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo;
(e) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Jinsia, Vijana, Watoto na Maendeleo ya Jamii;
(f) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati;
(g) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula; na
(h) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Amani na Usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikutano hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hushiriki katika ngazi za wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri. Aidha, kati ya Wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki, Wabunge watatu wanatokea Zanzibar. Ahsante.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Wavuvi wengi nchini wanaendesha shughuli zao za uvuvi kwa kutumia njia zisizokuwa za kitaalam.
Je, ni lini Serikali itatoa mafunzo ya kitaalam kwa wavuvi wetu ili kuwawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imefanya na inaendelea kufanya tafiti zitakazosaidia wavuvi kutumia njia za kitaalam katika uvuvi kwa lengo la kuboresha uvuvi na mapato ya wavuvi. TAFIRI inao mradi wa kuyatambua maeneo yenye samaki kwa maana (Potential Fishing Zones - PFZs) katika Bahari ya Hindi ili kuwasaidia wavuvi kutumia muda mfupi na rasilimali chache kuyafikia maeneo hayo na hivyo kuboresha mavuno ambayo yataongeza pato la mvuvi na Taifa kwa ujumla. Wavuvi wanapewa taarifa za kijiografia kupitia GPS, kupitia simu zao za mkononi kujua maeneo yenye samaki kwa msimu husika. Mradi huu kwa sasa ni wa majaribio na unafanyika kwa kushirikiana na wavuvi wa maeneo ya Mafia na Tanga kwa Tanzania Bara na pia Unguja na Pemba kwa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia kupitia Taasisi yetu ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inaendelea na mradi wa vikusanya samaki yaani Fish Aggregating Devises-FADs katika Bahari ya Hindi ambapo inashirikiana na wavuvi wa Bagamoyo kwa upande wa (Tanzania Bara) na Nungwi kwa upande wa Tanzania Visiwani ambapo lengo kubwa la mradi ni kuwasaidia wavuvi waweze kwenda kuvua sehemu zilizo na samaki na kuachana na uvuvi wa kuwinda ambao unapoteza muda na rasilimali.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-

Uvuvi ni moja ya vipaumbele vinavyosaidia kusukuma maendeleo ya wananchi wengi wa Tanzania na Taifa letu ni miongoni mwa Mataifa maskini duniani:-

Je, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga namna gani katika kuwasaidia wavuvi wadogo ili kukuza maendeleo ya Taifa pamoja na kujikwamua na umasikini uliokithiri?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ina mikakati mbalimbali inayolenga kuleta maendeleo katika Sekta ya Uvuvi na kuwasaidia wavuvi ambayo ni pamoja na:-


(i) Kufanya mapitio ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kuendana na Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 na mabadiliko ya sasa ili kulinda, kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

(ii) Kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu kwa kufufua Shirika la Uvuvi la TAFICO, kujenga bandari ya uvuvi na kununua meli mbili kubwa za uvuvi ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuchakata samaki, kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, ajira na kuongeza mapato ya Serikali;

(iii) Kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu uvuvi endelevu, ukuzaji viumbe katika maji na ufugaji samaki kwenye vizimba kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa samaki ndani ya nchi; na

(iv) Kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kuendeleza Sekta ya Uvuvi Nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeanzisha Dawati la Sekta Binafsi ili kuwasaidia wavuvi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kupata mikopo kutoka Taasisi za Fedha. Pia Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Msingi, Vyama vya Akiba na Mikopo na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.