Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Othman Omar Haji (8 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Kwa kuzingatia usalama na utulivu wa nchi yetu, viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa kauli zenye msisitizo kwa wananchi kuepuka kuhubiri siasa katika nyumba za ibada na kuchanganya dini na siasa katika mikutano.
Je, ni kifungu gani cha Katiba au Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinafafanua juu ya kauli hizo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza katika utangulizi wake kuwa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.
Aidha, Ibara ya 3(1) ya Katiba hiyo hiyo inaeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ibara ya 19(1), (2) na (3) inaeleza kuwa kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ibara ya 3(2) inaeleza kuwa mambo yote yanayohusu uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba na sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo. Hivyo basi, sheria ya vyama vya siasa Sura ya 258 inaeleza bayana katika kifungu cha 9(2) kuwa chama cha siasa, hakitastahili kusajiliwa endapo katiba yake au sera zake zina mwelekeo wa kuendeleza maslahi ya imani ya kidini au kundi la kidini.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI Aliuliza:-
Moja kati ya kazi za Polisi ni ulinzi na usalama wa raia na mahali zao, uzoefu unaonesha kila zinapotokea kampeni za Uchaguzi Jeshi la Polisi hutumika kama Taasisi ya Chama Tawala hivyo husababisha ulinzi na usalama (hasa Wapinzani) kutoweka mikononi mwa Polisi:-
Je, Serikali haioni kwamba inalitumia Jeshi la Polisi kwa lengo la kudhoofisha Upinzani na kurahisisha kukipatia ushindi Chama chake cha CCM?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ambazo zinatoa mwongozo kwa shughuli za Askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ifahamike kwamba Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya Ulinzi wa raia na mali zao na siyo kwa ajili ya chama fulani cha siasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema. Ni Jeshi linalowatumikia Watanzania wote pasipo kujali vyama vyao, kabila zao, dini zao ama rangi zao. Hata hivyo, ikitokea Askari wamekiuka taratibu za kiutendaji tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kinidhamu dhidi ya wale ambao Wizara yangu inapata malalamiko rasmi kupitia dawati la malalamiko.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Moja kati ya maeneo yaliyomo kwenye mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba (1986) ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
Je, ni kwa kiasi gani Tanzania imefaidika na utekelezaji wa mkataba huo katika sekta ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Jimbo la Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Cuba katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya tangu 1986, ambapo mkataba ulisainiwa kati ya Serikali hizi mbili. Kupitia mkataba huo, Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea Madaktari Bingwa kutoka Cuba ambao wamekuwa wakifanyakazi katika hospitali za Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari hawa wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za Kibingwa kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari wanaofanya nao kazi katika hospitali hizo. Aidha, kwa kushirikiana na kampuni ya Labiofarm ya Cuba, Serikali imeweza kujenga kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kibaiolojia yaani biolarvicides kwa ajili ya kuua viluilui vya mbu waenezao malaria. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iligharamia ujenzi wa kiwanda hicho na Serikali ya Cuba ilitoa msaada wa wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yetu ni kuwa, wataalamu hao watawajengea uwezo Watanzania ili waweze kutengeneza bidhaa hizo bila kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi kwa siku zijazo. Viuadudu hivyo vimeanza kutengenezwa kuanzia mwezi Disemba 2016, na kwa sasa uhamasishaji wa Halmashauri mbalimbali nchini kununua bidhaa hizo umeanza. Endapo viuadudu hivyo vitatumiwa vizuri vitasaidia kupunguza mbu waenezao malaria na hivyo kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Madhumuni makubwa ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kilichoanza shughuli zake Julai, 1978 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 ilikuwa ni kuendesha biashara ya mikutano na upangishaji wa nyumba.
Je, ni mafanikio gani ambayo Serikali imeyapata kutokana na kuanzishwa kwa taasisi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) mwaka 1978, Serikali imeweza kupata mafanikio mbalimbali. Baadhi ya mafanikio hayo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo huchangia katika pato la Taifa kwa kulipa kodi stahiki kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa wakati, kwa mfano, kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 kituo kimelipa kodi ya jumla ya shilingi bilioni 6.05.
Pili, kituo huchangia katika bajeti ya Serikali kwa mfano kwa mwaka 2014/2015 hadi 2015/2016 kituo kimechangia jumla ya shilingi milioni 586. Aidha, kwa mwaka 2016/2017 kituo kimetoa gawio kwa Serikali la shilingi milioni 400.
Tatu, kituo kimewezesha Taasisi za Kimataifa nchini kwa kuwakodishia Ofisi na makazi yanayokidhi mahitaji yao. Kwa mfano, AICC ilikuwa ni Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia Mauaji ya Kimbari ya Rwanda. Pia ni Makao Makuu ya Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika kuhusu masuala la rushwa. Vilevile baadhi za Ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo katika eneo la AICC.
Nne, kituo kimeweza kuleta mikutano ya Kimataifa ambayo imechangia kuvutia wageni kutumia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii nchini na kutembelewa na viongozi wakubwa na maarufu duniani na kufanya vyombo vya habari vya Kimataifa kuimulika Tanzania na hivyo kuifanya nchi yetu kutambulika zaidi ulimwenguni.
Tano, kituo kimeweza kutoa ajira kwa Watanzania wapatao 132 hadi kufikia mwezi Mei, 2018.
Sita, kituo kimeweza kujenga majengo matatu ya ghorofa ya makazi kwa familia 48 Jijini Arusha, hivyo kuwawezesha wakazi wa Arusha kuishi katika makazi bora.
Saba, kituo kinahudumia zaidi ya wageni 30,000 kwa mwaka, hivyo kuchangia katika kukua kwa sekta za hoteli, usafirishaji, utalii na wajasiriamali wadogo na wakubwa katika jiji la Arusha.
Nane, kupitia hospitali ya kituo, huduma ya afya kwa jamii imeweza kutolewa kwa wafanyakazi wa Jumuiya za Kimataifa, wageni wanaokuja kwa ajili ya mikutano mbalimbali na watalii wanaofika Arusha kutembelea vituo vya utalii.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuwa na uchakavu wa mitambo ya kuongezea ndege na miundombinu duni ya usafiri wa anga nchini, TCAA imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Shirika la Usafiri wa Anga Duniani kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 na hivyo kuwa mwakilishi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Je, kupitia nafasi hii ya kipekee, Serikali kupitia TCAA ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu ya usafiri wa Anga hapa nchini, ili iweze kulingana na ile ya nchi nyingine za SADC?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) inaendelea kuboresha mitambo ya kuongozea ndege hapa nchini. Tayari mchakato wa usimikaji wa rada nne za kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Uwanja wa Ndege wa Mwanza na Songwe unaendelea. Aidha, utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 kuanzia tarehe 9 Novemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo TCAA imekamilisha mradi wa usimikaji wa mtambo Mashariki upande wa nchi yetu unaofanya kazi ya kutambua na kuongoza ndege zinazopita katika anga la juu (Automatic Dependent Surveillance Broadcast) na mtambo wa mawasiliano ya sauti katika kituo chetu cha kuongozea ndege cha Julius Kambarage Nyerere International Airport na nchi nzima kwa ujumla na hivyo kuboresha usalama katika anga la Tanzania. Aidha, TCAA wamekamilisha usimikaji wa mitambo ya mawasiliano kwa njia ya redio baina ya waongoza ndege na marubani (VHF Radios) and area cover relays na hivyo kuwa na uhakika wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na TCAA kupitia Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga nchini ni pamoja na kukarabati mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja cha Pemba na kuendelea na mchakato wa ununuzi na usimikaji wa mtambo wa kuwezesha ndege kutua kwa usalama katika kituo cha Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi zote zinazochukuliwa na Serikali zinalenga katika kulifanya anga la Tanzania kuwa salama zaidi na hivyo kuvutia mashirika mengi ya ndege ya kigeni kuja hapa nchini kwetu. Aidha, Tanzania kupitia nafasi hii ya ujumbe wa Baraza la Washirika la Usafiri wa Anga Duniani kwa kuziwakilisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) itaendelea kuhamasisha mashirika ya ndege ya kigeni kuja nchini kwa kupitia mikutano mbalimbali ya kimataifa ambayo mamlaka uhudhuria na hivyo kuongeza mapato ya mamlaka na kwa nchi kwa ujumla kutokana na miundombinu ya usafiri wa anga nchini kuendelea kuboreshwa.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-

Moja kati ya malego makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Mwaka 2017/2018 ilikuwa ni kukamilisha kuandaa Sera mpya ya Mambo ya Nje:-

(a) Je, mpango huo umefikia wapi?

(b) Je, ni maeneo gani mapya kisera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha kuandaa Rasimu ya Sera ya Mambo ya Nje kama ilivyopendekezwa na wadau wakati wa zoezi la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya 2001. Rasimu hiyo ya Sera hivi sasa ipo katika hatua ya kusambazwa kwa wadau mbalimbali kama vile Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, sekta binafsi na taasisi zisizo za Kiserikali ili kupata maoni yao yenye lengo la kuiboresha zaidi.

Mheshimiwa Spika, maeneo mapya ambayo yamejumuishwa katika Sera inayopendekezwa ni pamoja na: Kuwatambua na kuwajumuisha Diaspora kwenye juhudi za kuleta maendeleo ya Taifa; kutambua mihimili mingine kama wadau wa sera yaani Bunge na Mahakama; kuzingatia mikakati na mipango ya muda mrefu ya nchi na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa; utekelezaji wa Sera kufikia hadi ngazi ya Wilaya na Mikoa (Decentralization of Foreign Policy conduct); na vijana na tasnia ya michezo na burudani kutumia kama njia ya kuitangaza Tanzania nje. Aidha, Rasimu ya Sera inaelekeza nchi kuimarisha mahusiano na nchi nyingine yanayolenga kukuza uchumi wa nchi kwa kuzingatia mipango ya Serikali ya muda mfupi na mrefu.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACPHR) inatumia jengo la TANAPA lililopo Arusha kwa mkataba wa upangaji baina ya TANAPA na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioanza tarehe 1 Desemba, 2008 kwa kodi ya dola za Marekani 38,998.89 kwa mwezi:-

Je, kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ni nani mwenye jukumu la haki za binadamu na nani mwenye jukumu la kulipa kodi ya jengo hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwaka 2007, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Afrika Mashariki ziliingia Mkataba wa Uenyeji (Host Agreement) wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Katika mkataba huo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano ndiyo msimamizi na mtekelezaji mkuu wa mkataba huo kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 5(1) ya mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Afrika Kuhusu Uenyeji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, inaeleza kuwa Tanzania kwa gharama zake inawajibika kutoa majengo kwa ajili ya ofisi ya mahakama na makazi ya Rais na Msajili wa Mahakama hiyo. Aidha, Ibara ya 5(2) inaipa Tanzania jukumu la kutoa ofisi ya muda kwa ajili ya mahakama husika wakati ikiendelea na taratibu za kupata jengo la kudumu la mahakama. Kutokana na kipengele hicho Serikali iliingia mkataba na TANAPA wa kukodisha majengo yale ili kuwa ofisi ya muda ya Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo, ni dhahiri kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo yenye jukumu la kulipa kodi hiyo kutokana na makubaliano yaliyofikiwa. Hata hivyo, suala la kulinda haki za binadamu ni suala la kila mtu na kila taasisi sehemu yoyote duniani. Kimsingi, hata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahusika moja kwa moja katika kulinda haki za binadamu.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-

Lengo kuu la Mpango wa Kujithathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) ni kuziwezesha nchi za Afrika kuimarisha utawala bora kwa kuwawezesha wananchi wake kubainisha changamoto:-

Je, ni hatua gani ambazo zinachukuliwa na Tanzania katika kutekeleza mpango huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi 38 kati ya nchi 54 Barani Afrika zinazoshiriki katika Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) ambapo ilijiunga mwaka 2004 na Bunge la Tanzania liliridhia makubaliano hayo mwaka 2005. Hii ni kutokana na imani kubwa iliyonayo katika lengo kuu la Mpango wa APRM ambalo ni kuziwezesha nchi za Kiafrika kujitathmini kwa vigezo vinavyokubalika vya utawala bora.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini hizo ni kubaini changamoto zilizopo ili ziwekewe mikakati ya kugeuzwa kuwa fursa za maendeleo na pia kubaini maeneo ambayo nchi inafanya vizuri ili kuyaimarisha pamoja na kuigwa mataifa mengine. Tathmini hiyo hufanywa katika maeneo ya siasa na demokrasia, usimamizi wa uchumi, uendeshaji wa mashirika ya biashara na maendeleo ya jamii.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilikabidhiwa jukumu la kuwezesha utekelezaji wa APRM hapa Tanzania. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara iliandaa semina na uhamasishaji juu ya Mpango wa APRM ili kuwaandaa wananchi kushiriki kikamilifu katika mpango huo na pia kuwawezesha kuchagua Wajumbe watakaowakilisha makundi yao katika Baraza la Usimamizi la Taifa. Hivyo, mwaka 2006 Wizara iliwezesha kuundwa kwa Baraza la Usimamizi la Taifa lenye Wajumbe 20 kutoka kwenye taasisi za Serikali na taasisi zisizo za Kiserikali.

Mheshimiwa Spika, jukumu kubwa la Baraza ni kusimamia utekelezaji wa shughuli za mpango na kuhakikisha kuwa zinafanyika kwa uwazi, uadilifu na zisiingiliwe kisiasa. Kwa kushirikiana na Wizara, Baraza liliajiri Sekretarieti inayofanya shughuli za APRM za kila siku na taasisi nne za kufanya utafiti katika kila eneo la tathmini.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwaka 2019, APRM imekwishaandaa taarifa mbili za utawala bora, taarifa ya ndani ya nchi na taarifa ya nje ya nchi. Pamoja na taarifa hizo, umeandaliwa mpango kazi wa APRM wenye lengo la kutatua changamoto za utawala bora zilizobainishwa kwenye taarifa zilizotajwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha utekelezaji wa taarifa za APRM kimeundwa kikosi kazi cha APRM chenye jukumu la kuandaa taarifa za utekelezaji wa kila mwaka na taarifa hizo huunganishwa kuwa taarifa moja ya nchi. Serikali imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya kazi za APRM kila mwaka na kulipa michango yake kwa taasisi hii kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara na taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi inaendelea kutatua changamoto za utawala bora kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na kuainishwa kwenye mpango kazi wa APRM.