Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Othman Omar Haji (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. J. P. Magufuli kwa kuonesha nia na uwezo mkubwa wa kuiongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wake wote. Naomba waongeze juhudi na misimamo yao katika kuongoza Wizara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na matumizi ya soko la Marekani bila ya ushuru chini ya mpango wa AGOA. Hata hivyo, Serikali haikueleza namna itakavyochukua hatua za kuwaelimisha wananchi kujiunga na mpango huo. Ni vyema Serikali ikawaelekeza na kuwatayarisha wananchi ili kuwapa ujuzi na uelewa wa soko hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kuhusu mafuta na gesi. Hapa naanza na TPDC, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania. Kwa makala chungu nzima nilizosoma nimegundua kwamba TPDC siyo shirika la Muungano, lakini shirika hili lilipewa kazi ya kushughulikia sekta ya mafuta Tanzania nzima. TPDC katika miaka ya karibuni lilikuwa likitoa vibali na kuingia mikataba na mashirika tofauti ya Kimataifa, moja kati ya mashirika hayo lilikuwa Shirika la Shell la Uholanzi. Shirika la Shell lilifanya utafiti wa mafuta katika vitalu vilivyoko Zanzibar, ikiwepo kitalu namba Tisa, namba 10, namba 11 na namba 12, vitalu hivi vyote vinaonekana katika maeneo ya Zanzibar. Namuuliza Waziri mwenye dhamana, TPDC ilikuwa na uhalali kiasi gani kuingia katika maeneo ya Zanzibar na kutafuta mafuta bila ya idhini ya watu wa Zanzibar! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha TPDC kuingia katika maeneo ya Zanzibar na kutafuta mafuta ni sawasawa na kuwadharau watu wa Zanzibar. Tunaomba tu wenzetu waache kijicho juu ya Zanzibar kwa sababu Wazanzibari kuna rasilimali nyingi sana Tanzania Bara wao hawana habari nazo, wametosheka na umaskini wao. Tanzania Bara kuna madini ya aina chungu nzima, Tanzania Bara kuna gesi, lakini hujamsikia Mzanzibari hata mmoja kudadisi masuala ya madini, masuala ya gesi yaliyoko bara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Sheria ya Mafuta iliyoundwa mwaka jana (The Petroleum Act 2015), Sheria Na. 2 ambayo imezipa nafasi pande hizi mbili kushughulikia mafuta kila mmoja upande wake, lakini kutokana na hali ya Zanzibar ilivyo, Serikali dhalimu iliyopo, sisi hatuna imani kwamba wanaweza wakawatendea haki Wazanzibari wakaweza kudhibiti mafuta yale bila ya kuyatorosha kuyapeleka Tanzania Bara. Kwa sababu Serikali iliyopo kule ni dhalimu, ni Serikali imewekwa na Tanzania Bara na wanaketi kama ni mawakala wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi siyo Serikali ya Wazanzibari, kwa hiyo hawana uwezo, jambo lolote lile mtakalowaambia, wakiambiwa wa-pump mafuta walete Tanzania Bara wataleta, hawana uwezo wa kuyazuia mafuta. Kwa maana hiyo, hatutegemei kwamba kwa wakati huu inaweza ikaja kampuni kuchimba mafuta kule kwa muda huu. Mafuta yale yaliyoko Zanzibar, na yapo, yatakaa vilevile mpaka pale ambapo watu wa Zanzibar watakuwa na Serikali yao wenyewe waliyoichagua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie katika maeneo ya madini. Wachangiaji wengi sana hapa wamezungumzia kuhusu madini. Moja katika madini ambayo yameonekana Tanzania hii ni madini ya uranium. Pamoja na umuhimu wa madini haya ambao ni pamoja na kuzalisha umeme, kama wanavyofanya wenzetu Afrika Kusini kule, pamoja na kutengeneza silaha za nyuklia, madini haya yanatoa mionzi hatari ambayo ni hatari kwa maisha ya watu. Kuna maeneo mengi ambayo madini haya yameonekana, kama maeneo ya Bahi yaliyopo Dodoma hapa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaamini kwamba mtengamano wa kisiasa ni nguzo moja muhimu katika kujenga nchi yenye maendeleo makubwa na ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtengamano wa kisiasa unajumuisha siasa safi za kiustaarabu na zenye kuheshimu mawazo ya kila mmoja ili kukidhi katika kufikia demokrasia ya ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi washirika, ambayo ni wadau wakuu wa kusukuma maendeleo katika nchi yetu tayari wameanza kurudi nyuma kwa kukosekana sifa nilizozielezea hapa juu hasa baada ya Serikali ya CCM kuendeleza ubabe wake kwa kutoheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa miujiza gani Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaweza kufanikisha mipango yake ya kuimarisha uchumi wa nchi hasa baada ya kukosekana mtangamano wa kisiasa hapa nchini kwetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya maamuzi ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali katika Mkoa wa Dodoma, kwa kile kinachoaminika kama ni katikati ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma ni katikati kwa Tanzania Bara na sio kwa Tanzania nzima. Kwa kupunguza usumbufu kwa Wazanzibari wa kufuatilia matatizo yao Dodoma, naishauri Serikali kwamba Wizara zote za Muungano zibakie kule kule Dar es Salaam na zile zisizo za Muungano ndizo zihamishiwe Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/2016, Serikali imetoa mafunzo katika fani za mafuta na gesi kwa ngazi tofauti ndani na nje ya nchi kwa wanafunzi 159. Naomba Mheshimiwa Waziri afafanue kati ya wanafunzi hao, wamo wanafunzi Wazanzibar wangapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa wanafunzi 35 wanaogharamiwa na washirika wa maendeleo ni wangapi wanatoka Zanzibar?
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uongozi kwenye Wizara za Muungano; pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kujaribu kutatua kero za Muungano lakini bado kumeibuka kero nyingine ya kuwabagua Wazanzibari kwenye nafasi za uongozi ndani ya Wizara za Muungano. Sasa hivi zipo Wizara za Muungano kama vile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Fedha zote zinaongozwa na upande mmoja wa Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji mashirika ya Muungano; kero nyingine ya Muungano inatokana na Mashirika yanayowekeza Tanzania yanafanya uwekezaji wake Tanzania Bara pekee. Natolea mfano wa Shirika la AICC ambalo limefanya uwekezaji mkubwa Tanzania Bara na bado katika mipango yake ya baadaye haijaonyesha nia ya kufanya uwekezaji upande wa Zanzibar. Ikumbukwe kwamba mbali na pato la Serikali linalotokana na uwekezaji wa mashirika pia umekua ukitoa ajira na kunyanyua uchumi wa wananchi katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za wafanyabiashara wa Zanzibar; ni muda mrefu sasa wafanyabiashara kutoka Zanzibar wamekuwa wakilalamika TRA kuendelea na tabia yao ya kuwatoza wafanyabiashara wa Zanzibar kodi mara mbili pale wanapotoa bidhaa zao kutoka Zanzibar kuingia Tanzania bara. Tabia hii ni sawa na kupunguza harakati za wafanyabaiashara wa Zanzibar kuingiza bidhaa zao Tanzania bara na kudhoofisha uchumi wa Wazanzibari. Naomba Wizara husika ifanye ufumbuzi wa haraka wa suala hili kwa faida ya pande zote za Muungano. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii kuchangia katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpe angalizo kwanza Mheshimiwa Waziri kwamba nchi yetu kitakwimu inakuwa na idadi kubwa ya watu. Idadi hii inakwenda kuathiri kwa njia moja au nyingine katika sekta yetu ya Wizara ya Elimu, sasa sijui Mheshimiwa Waziri ameliona hili na ikiwa ameliona amejipanga namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nchi yetu imetangaza kwamba inakwenda kuwa Taifa la viwanda. Taifa la viwanda linahitaji rasilimali watu wenye ujuzi ambao wataweza kuzalisha kwa ufanisi na wenye tija. Kama ulivyozungumza katika hotuba yako page namba 42 kwamba vyuo vikuu ni nguzo moja muhimu sana katika kuhakikisha kwamba Serikali inakwenda kutekeleza malengo yake muhimu yaliyojipangia kwa kuzalisha rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vikuu kuna changamoto zake, nafikiri unafahamu Mheshimiwa Waziri kwamba vyuo vikuu kuna changamoto za wanafunzi wanaosoma elimu ya juu. Moja ya changamoto hizo Mheshimiwa Waziri ni kwamba wanafunzi wanaosoma masomo ya Uzamili, baadhi ya masomo wanachukua si chini ya miaka minne. Mafunzo hayo Mheshimiwa Waziri ikiwa utakwenda kusoma nchi za nje yanachukua si chini ya miaka miwili. Tatizo hili Mheshimiwa Waziri inakuwaje hapa nchini wanafunzi wetu wasome zaidi ya miaka minne ambapo nchi za wenzetu wanakuwa ni chini ya miaka miwili, nini kimeongezeka hapa kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika mafunzo ya Uzamivu utakwenda kusoma ikiwa hujaoa utaoa, ikiwa hujazaa utazaa, utapata wajukuu na utaota mvi bado degree hujahitimu, nini tatizo? Matatizo haya Mheshimiwa Waziri yanakwenda kusababisha uhaba wa Wahadhiri katika vyuo vyetu. Napenda Mheshimiwa Waziri hili ulione kwamba tatizo la kuwaweka wanafunzi muda mrefu katika masomo yao linakwenda kusababisha kuwa na uhaba wa Wahadhiri ndani ya vyuo. Tatizo ambalo halitakwenda sambamba na ongezeko la watu na ndiyo ukaona kuna idara nyingine pale vyuo vikuu wanachukua chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano mmoja, Idara ya Fizikia pale Chuo Kikuu ambayo katika vyuo vyote vinavyotoa Masters hapa nchini ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam peke yake, lakini wanafunzi wanaoingia kwa mwaka hawavuki wanafunzi 11. Wanafunzi 11 kweli Mheshimiwa Waziri wanatosheleza nchi nzima kwa mwaka? Hao miaka minne hujahitimu pale. Hii ni kwa sababu Wahadhiri wetu hawataki kurithiwa, hawataki wasaidiwe pale Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mhadhiri anabakia pale hawezi kutoka mpaka apelekwe kaburini pale. Namuomba Mheshimiwa Waziri suala hili la kuwatesa wanafunzi wa vyuo vikuu linawarudisha nyuma, ukitilia maanani kwamba wanafunzi wengi wanaosoma vyuo vyetu vya ndani ni watoto wa kimaskini. Hili linapelekea wengi wao warudi nyuma wasipende kusoma katika vyuo vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Wahadhiri wetu wa vyuo vikuu walione hili na waone kwamba wao wapo pale ili kulisukuma Taifa hili na Taifa linawategemea wao ili lisonge mbele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Pia napenda nifikishe salamu kwa Mheshimiwa Waziri kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Fizikia pale Dar es Salaam kwamba aende akawatembelee. Kuna maabara yao imechoka, vifaa vyao vimechoka, kwa hivyo aende wakashauriane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nieleze tu kwamba mimi ni Mwalimu, nafundisha masomo ya sayansi na hisabati. Nakumbuka katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu tatizo la masomo ya sayansi katika nchi yetu. Akasema kwamba uchumi wa viwanda unategemea kwa kiasi kikubwa rasilimali ya watu wenye ueledi wa masomo ya sayansi na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile akasema kwamba changamoto tuliyonayo hapa Tanzania mpaka sasa hivi ni vijana wetu kutopenda kusoma masomo ya sayansi na hisabati. Akienda mbali zaidi Mheshimiwa Waziri Mkuu kusema kwamba changamoto tuliyonayo ikiwa wanafunzi na vijana wetu hawatajitahidi iko hatari ya viwanda vyetu kuja kuwategemea wataalam kutoka nje na hivyo Watanzania kubakia watazamaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri nilifikiria angalau angetoa mwelekeo au kujibu hii hotuba ya Waziri Mkuu, jinsi gani anajipanga kwenda kutoa suluhisho la matatizo ya masomo ya sayansi lakini naona hotuba iko kimya. Kama Waziri mwenye dhamana wa Wizara hii tunapenda awaeleze Watanzania changamoto hii ya vijana wetu kutopenda kusoma masomo ya sayansi anakwenda kuitatua vipi? Ukitilia maanani wajibu wa Wizara yake ni kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi na mahitaji tuliyonayo ya nchi sasa hivi ni vijana waliosoma masomo ya sayansi na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajibu wa pili ni kuimarisha matumizi ya sayansi na hisabati. Tatu ni kuendeleza wataalam wa ndani wa sayansi na hisabati. Haya ni majukumu ya Wizara ambayo yameandikwa katika kitabu hichi lakini mpaka sasa hivi pamoja na changamoto hizo sijaona vipi anakwenda kulitatua tatizo hili la wanafunzi ambao hawapendi kusoma masomo ya sayansi na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimjulishe Mheshimiwa Waziri na Watanzania ni kweli usiopingika kwamba vijana wetu kusoma sayansi sasa hivi hawataki. Tatizo kubwa linalowasibu ni kwamba wale ambao wanajaribu kufuatilia masomo ya sayansi hawapendi kusoma hisabati. Huwezi ukaisoma sayansi ikiwa utaiacha hesabu, unaweza ukaisoma hesabu ukaiacha sayansi lakini huwezi ukasoma sayansi bila hisabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwalaumu sana Walimu wetu wa sekondari, kwa sababu wanafunzi hawa japokuwa wakifika pale sekondari wanaanza kuchanganyikiwa, kwa sababu hawa wanafunzi wameanza kupoteza mwelekeo kutokana na primary waliyotoka walikuwa hawana msingi mzuri wa masomo ya hisabati. Kwa hiyo, msingi wa hisabati unajengwa pale ambapo wanafunzi wako primary wakifika sekondari ikiwa hawana msingi huo wa hesabu basi masomo haya ya sayansi watayasikia tu na ikiwa watayafuata yatawaangusha njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijielekeze kwenye dhima nzima ya Wizara ya Elimu. Waziri kasema katika kitabu chake hiki hapa kwamba, moja ya dhima ya Wizara yake ni kuinua ubora wa elimu na mafunzo, pia kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania wenye kuelimika lakini pia wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika maendeleo ya Taifa hili. Nataka kupata maelezo ya Mheshimiwa Waziri hapa kwa sababu kuna idadi kubwa ya Watanzania hasa walio katika sekondari wanapenda kujielimisha lakini taratibu zilizowekwa zinawarudisha nyuma kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia mfano mimi mwenyewe mwaka 2009 nilipata nafasi ya kwenda kusoma Shahada ya Uzamili pale chuo kikuu na tulikuwa wanafunzi 11, kati ya hao wanafunzi saba walikuwa ni Tutorial Assistance kutoka vyuoni, mmoja alitoka Arusha. Hawa walikuwa wanapata mikopo kutoka elimu ya juu Mheshimiwa Waziri tulibakia wanafunzi wawili ambao tulitoka sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijiuliza kwamba wenzetu wanatoka kwenye vyuo, sisi tunatoka sekondari sote tuna lengo moja la kulitumikia Taifa hili lakini wenzetu wanasoma pale vyuoni kwa raha kabisa. Tulibakia wanafunzi wawili ambao tumetoka sekondari hatuna msaada wa aina yoyote, kwa hiyo, tukabakia tunabangaizabangaiza mpaka tukamaliza chuo. Ukiangalia hii siyo haki kuona kwamba wanafunzi wote tuna lengo moja la kujenga Taifa hili wengine wakapewa msaada huu lakini wengine wakanyimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo lililotukuta lilitupelekea sisi wawili kusoma kwa shida kubwa sana mpaka ulipofika wakati wa kuandika dissertation ilibidi tutafute njia nyingine ya kukabiliana na maisha. Mimi nilitafuta school ya karibu pale iko Kawe ambapo viongozi wengi mnapeleka watoto wenu pale. Nataka nikupe siri kidogo ya ile shule ya private ambayo iko top ten katika kiwango cha Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokigundua kinachozingatiwa pale kwanza ni ubora wa Walimu. Maslahi ya Walimu yanazingatiwa, unapoingia pale unasomesha kwa raha kabisa, unaondoka nyumbani umeacha chakula unakuja pale huna tatizo la aina yoyote. Suala la pili ni idadi ya vipindi havizidi 20 kwa wiki, ni vipindi vinne kwa siku moja. Ina maana ukiwa unafundisha vipindi vinne kwa siku moja unapata wakati wa kutosha wa kumsaidia mwanafunzi, unapata wakati wa kutosha wa kusahihisha madaftari, unapata wakati wa kutosha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji, kwa hiyo, mchango wangu utajikita zaidi kwenye eneo hilo la uwekezaji.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika zangu uzitunze. Ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji (PIC) na ninapenda mchango wangu uelekee huko kwanza. Kama tunavyofahamu kwamba lengo kubwa la mashirika ya umma haya ni kukuza mtaji ni kukuza ajira, kupunguza umasikini na kukuza uchumi wa Taifa. Tulitegemea kwamba kwamba mashirika haya yale ambayo siyo ya Muungano, mambo haya ya fursa hizi za ajira hupunguza umaskini utaenea kwa Tanzania nzima. Lakini bahati mbaya kwa masikitiko taasisi nyingi za Muungano ambazo tunategemea kueneza ajira hizi Tanzania nzima zimejikita kwenye upande mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano, tuna taasisi ya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa (AICC) kituo hiki kiliazishwa mwaka 1977 mpaka leo tunavyosema kituo hiki kina umri wa miaka 42, kituo hiki dhamira yake ni utalii wa mikutano ya kimataifa. Rasilimali kubwa za kituo hiki ziko upande mmoja wa Muungano, ajira kwa upande mkubwa unatoka upande mmoja wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile fursa au tunasema fursa za tunaweza tukasema huduma za kijamii zinazotolewa na kituo hiki zinatoka upande mmoja wa Muungano. Sasa tulitegemea kwamba kituo hiki kwa sababu shughuli yake kubwa ni mikutano ya kimataifa na kwa sababu kule Zanzibar kuna fursa nyingi, kuna maeneo mazuri, kuna mazingira mazuri ya kuweka uwekezaji, nilitegemea kwamba kituo hiki cha kimataifa kitatoa branch yake kule ili na wale wa upande wa Zanzibar wapate fursa nao za kupata ajira, kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bahati mbaya tukihoji hapa kwa nini fursa kama hizi hazipelekwi, kwa nini hatutajengewa hili jengo la mikutano angalau ya kimataifa Serikali inasema kwamba mata tunakuja kujenga Dodoma, mara tunajenga Mwanza mara Mtwara sasa tunauliza kujengwa kituo hiki Dodoma kama siyo Zanzibar kitatusaidia kitu gani? Tunaomba sana Serikali huduma hizi za mashirika ya Muungano yapendelee pia kwenda kule Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Bodi ya Wakurugenzi, nipo katika Kamati kwa muda wa miaka mitatu sasa nikiangalia Bodi za Wakurugenzi kwa kiasi kikubwa bodi zinazokuja katika Kamati hatuoni kwamba inawakilisha Muungano. Wajumbe wote wa Kamati wanakuwa upande mmoja wa Muungano, sasa tulitaka na wale wajumbe kutoka Zanzibar ambao wamo katika bodi ya Muungano wawe pia katika Kamati wanapoitwa na Kamati ya Uwekezaji ili waje washuhudie yale mambo ambayo yanaelezwa na wenzi wao kutoka huku Tanzania Bara, je, ni sahihi au siyo sahihi? Ili na sisi tupate kuwahoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapa nakwenda kwenye masuala ya TBS (Mamlaka ya Viwango), kazi ya shirika hili ni kukuza uchumi kupitia kulinda usalama wa Tanzania kwa kuhakikisha kwamba wanatumia chakula ambacho kiko salama. Lakini tatizo linalowakabili Shirika hili la TBS ni kwamba lina upungufu wa wafanyakazi, mpaka kufikia mwezi Novemba, 2018 shirika hili lilikuwa na wafanyakazi 456, shirika hili linahitaji wafanyakazi takribani 750 ukiangalia kazi ya shirika hili ukubwa wa eneo la Tanzania mahitaji wanayostahiki kuhudumiwa watanzania ni kwamba kiwango hiki cha wafanyakazi ni kidogo. Vijana tunao wengi wanaomaliza kwa hivyo wapewe fursa za ajira kwenye shughuli ili hili shirika liweze kufanya kazi yake kiufanisi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kuipongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa ushauri ilioutoa juu ya kuishauri Serikali katika suala zima la kuleta maendeleo ya uchumi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kero za taasisi tatu ambazo binafsi napenda nipate ufafanuzi wa Waziri mwenye dhamana. Mapato yatokanayo na AICC. Katika kikao cha 10 cha Mkutano wa Sita cha tarehe 10 Februari, 2017, Waziri wa Fedha nilimnukuu wakati akijibu swali la pili la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Ali Saleh kutokana na swali la msingi Na. 110 ambalo lilihusu ruzuku ya Zanzibar kutokana na Shirika la AICC. Mheshimiwa Waziri wa Fedha alijibu kama ifuatavyo nanukuu:

“AICC haijawahi kupata gawio kwamba Joint Finance Commission na Ofisi ya Msajili wa Hazina wameunda kikosi kazi ili kusaidia kituo kupata faida na kuleta gawio Serikalini kuanzia mwaka ujao wa fedha”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ya Waziri wa Fedha inakinzana na taarifa za shirika la AICC, taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje na zile za Msajili ya Hazina. Taarifa ya AICC inaeleza kwamba shirika linajiendesha kwa faida na ufanisi mkubwa na kwamba halitegemei ruzuku ya Serikali na linachangia kwenye Mfuko wa Serikali. Naomba ufafanuzi wa kina kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusu mchango wa mapato ya AICC Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), TRA inaleta usumbufu kwa Wazanzibari, unapoingiza bidhaa kwenye ardhi ya Tanzania Bara kutoka Zanzibar ushuru wake unalingana na bidhaa zinazotoka nchi nyingine. Ushuru wa bidhaa unaodaiwa na TRA na ZRB kwa mfanyabiashara wa Zanzibar inamfanya mtafuta riziki huyu kutoa ushuru mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni baadhi ya kero ambazo zinawakandamiza Wazanzibari na zinazowarudisha nyuma kiuchumi. Naomba ufafanuzi wa Waziri wa Fedha kuhusiana na TRA kwa wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Benki ya TADB tayari imeshatoa elimu ya matumizi ya benki hii na tayari imetoa mikopo na kupokea maombi ya mikopo kwa wananchi wa Tanzania Bara. Jambo la kusikitisha, Benki hii licha ya kuwa haijafanya mambo hayo Tanzania Visiwani hata kujulikana na wananchi wa Zanzibar hawaijui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha apeleke huduma ya TADB Zanzibar kama huduma hii inavyotolewa kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kuipongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa ushauri uliotolewa kwa Serikali. Mchango wangu uko katika Shirika la AICC ambalo inamilikiwa au liko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, AICC ni Shirika la Muungano ambalo kwa kipindi cha miaka 39 toka kuanzishwa kwake limefanikiwa kufanya uwekezaji wa kutosha kwa upande mmoja tu wa Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi ambayo tayari imeshaelekezwa, bado AICC inatarajia kutekeleza miradi mipya kama vile ujenzi wa Taasisi ya Kimataifa eneo la Lakilaki (Arumeru), hospitali ya kisasa, maonesho, shughuli za mikutano na burudani. Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kilimanjaro International Convention Centre (KICC), Convention Centers’ katika Miji ya Mwanza, Mtwara na Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji unalenga kutengeneza ajira na hivyo kunyanyua shughuli za kiuchumi kwa maeneo husika. Hivyo basi, ni kwa namna gani Zanzibar inafaidika na uwekezaji unaofanywa na Shirika la AICC?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema Zanzibar ni sehemu ya Shirika la AICC, je, ni kwa nini Shirika bado halijafikiria kufanya uwekezaji katika visiwa vya Zanzibar wakati uchumi wa visiwa hivi unayumba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na Zanzibar kuwa na uchumi usioridhisha, lakini Zanzibar ina mazingira mazuri ya kuvutia biashara ya utalii, biashara ambayo shirika ndiyo kiini cha shughuli zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kikao cha Kumi katika Mkutano wa Sita cha tarehe 10/02/2017, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje alijibu swali la msingi Na.110 lililohusu gawio la Zanzibar. Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kuwa gawio linapelekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya majibu hayo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alinyanyuka na akasema kwamba AICC haijawahi kupata gawio na kwamba Joint Finance Commission na Ofisi ya Msajili wa Hazina wameunda kikosi kazi ili kusaidia kituo kupata faida na kuleta gawio Serikalini kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha yanakizana na yale ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na kwa hiyo, yamelenga kuwadanganya Wazanzibari kuhusiana na mapato ya AICC. Mbali na hayo, majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha pia yanakinzana na taarifa ya Msajili wa Hazina, lakini pia na taarifa ya Shirika wenyewe la AICC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya AICC inasema, nanukuu; “AICC kwa kipindi kirefu imekuwa ikijiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali na imekuwa ikichangia ruzuku ya Serikali na imekuwa ikichangia Mfuko Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Hazina.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mgongano huu wa taarifa zinazohusu faida zinazotokana na Shirika la AICC kati ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Shirika la AICC, binafsi ninaomba maelezo ya kina na yanayojitosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwa kasi kubwa inakumbwa na ongezeko la idadi ya watu. Hali hii kwa njia moja au nyingine itaathiri utendaji wa Wizara ya Elimu. Mheshimiwa Waziri ameliona hili na amejipanga vipi katika kuwahudumia wananchi hawa kwa kuongeza idadi ya walimu na mahitaji mengine ya lazima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahitaji ya viwanda, nchi yetu inaelekea kuwa Taifa la viwanda. Viwanda vinahitaji rasilimali watu watakaofanya kazi yenye ufanisi na zenye tija. Kwa hiyo, Wizara ya Elimu ni lazima iandae mikakati kwenye vyuo vyetu vikuu ili kuwawezesha vijana wetu wanaohitimu mafunzo yao waweze kufanya kazi katika viwanda kwa ufanisi na tija ili kutimiza ndoto ya nchi yetu kufikia maendeleo waliyojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto za elimu ya juu, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema katika hotuba yake (page 42) kwamba elimu ya juu ni nguzo muhimu ya kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya maendeleo kwa kuzalisha rasilimali watu. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze katika vyuo vyetu kuna wahadhiri wa kutosha? Iwapo ni wachache, je, hawana manyanyaso kwa wanafunzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba mafunzo ya baadhi ya shahada uzamili hapa nchini si chini ya miaka minne na mafunzo hayo hayo ni chini ya miaka miwili kwa nje ya nchi? Namuomba Mheshimiwa Waziri afahamu kwamba mafunzo ya shahada ya uzamivu katika vyuo vyetu yana usumbufu. Unaweza kusoma mpaka ukajukuu bado hujapata kuhitimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaombe wahadhiri wetu wa vyuo vikuu wafanye wajibu wao kama walivyotumwa wa kuzalisha rasilimali watu kwa maendeleo ya Taifa letu. Wahadhiri wawe tayari kurithisha ujuzi wao kwa vizazi vipya na kufanya hivyo ndiyo taifa letu litakaposonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Maendeleo ya Utumishi Wizarani. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni Wizara ya Muungano wa pande mbili za Tanganyika na Zanzibar. Wizara imekuwa ikilalamikiwa kwa kutotenda haki kwenye masuala ya utumishi ndani ya Wizara. Watumishi walio wengi ni wa upande mmoja wa Muungano. Wakati Wazanzibari wanapohoji Mawaziri wenye dhamana huwa wanatoa hoja ya kuwa utumishi huhitaji weledi na vigezo. Je, Wazanzibari wamekosa sifa hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC). Wakati AICC inatimiza karibu miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, kimekuwa kikifanya uwekezaji mkubwa upande wa Tanzania Bara pekee. Pamoja na miradi hiyo iliyopo sasa hivi AICC bado ina malengo ya kujenga kituo kikubwa cha mikutano cha Mt. Kilimanjaro International Convention Center nyingine katika eneo la Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mazingira ya uwekezaji kwa shughuli za AICC yaliyoko yanaruhusu, ni sababu zipi zilizofanya Wizara isifanye uwekezaji katika Visiwa vya Zanzibar? AICC kutowekeza Zanzibar ni kuwanyima Wazanzibari fursa za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kutafuta Wawekezaji Nje ya Nchi. Miongoni mwa kazi ya Wizara ni kusimamia balozi zetu katika kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo kwa bidhaa zetu. Wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi wamekuwa wakija kuwekeza hapa nchini lakini kwa bahati mbaya wanaishia Tanzania Bara pekee. Ni kwa nini Wizara hii haiwaongozi wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika visiwa vya Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo ambao unadorora? Niombe Wizara isifanye upendeleo katika kufanya kazi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Changamoto za Utawala Bora Zilizobainishwa na APRM. APRM inaamini kwamba Tanzania ina tatizo la kutozingatia utawala bora na unaokubalika kwa wananchi wake. Hii imetokana hasa pale Tanzania inapominya uhuru wa Wazanzibari wa kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka wenyewe. Serikali ya Zanzibar iliyopo madarakani sasa hivi si chaguo la wananchi wa Zanzibar, ni Serikali iliyowekwa kwa nguvu za dola, hivyo basi Serikali hii si halali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itoe ripoti kwa APRM kwamba Tanzania haiwezi Mfumo wa Vyama Vingi kwa sababu Chama cha Mapinduzi hakiko tayari kukabidhi madaraka pale wanaposhindwa kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya usalama nchini. Pamoja na Mheshimiwa Waziri kutoa tamko kwamba watu wawe mbele ya matokeo kabla hayajatokea kwamba yaweza kudhibitiwa, kauli hii ilikuwa ni wimbo tu kwa sababu Mhariri Mchambuzi wa Gazeti la Mwananchi alitoa taarifa kwamba, maisha yake yako hatarini anatafutwa na watu wasiojulikana. Leo Msemaji Mkuu wa Serikali anasema ni usanii na upuuzi mtupu, matokeo yake Mtanzania huyu amekimbilia nchi ya Finland kuomba hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anasema, miili ya watu inayookotwa inaelea majini ni ya wahamiaji haramu, leo mwili wa tajiri wa mabasi anayemiliki Kampuni ya Mabasi ya Super Sami umeokotwa kwenye kiroba na wavuvi unaelea kwenye Mto Ndabaka, Wilayani. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuwa kauli yake haina mashiko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya chaguzi nchini; wakati Mheshimiwa Waziri anasema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wake wanaumizana kutokana na matokeo ya uchaguzi kisha Serikali ikae kimya bila kuchukua maamuzi yoyote, leo wanachama kadhaa wa upinzani wamepigwa, wameumizwa na wengine kuuawa. Je, mbona Serikali imeshindwa kuchukua hatua yoyote juu ya wahalifu waliohusika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anaposema kuwa ni aibu kwa nchi yenye vyama vingi vya siasa wananchi wake kufanyiana fujo, lakini kwa upande mwingine Serikali ya CCM, vyombo vya dola na taasisi za Serikali bila aibu zinashiriki kikamilifu katika kukivuruga Chama cha CUF. Je, kwa nini Jeshi la Polisi haliheshimu sheria na taratibu za vyama vya siasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alitoa tamko la kuwa, watu waache tabia ya kuunganisha matukio na imani ya dini, siasa au chama. Matokeo yanayotokea Zanzibar kabla, wakati na baada ya chaguzi mbalimbali huwa Serikali na vyombo vya dola vinayahusisha matokeo hayo kuwa, yametekelezwa na wafuasi wa Chama cha CUF, bila kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo husababisha wafuasi wa CUF kupigwa na kuumizwa bila hatia yoyote. Mheshimiwa Waziri tunaomba tabia hii ikomeshwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kusifia maendeleo mazuri ya demokrasia hapa nchini lakini ripoti iliyotolewa na Shirika Huru la Freedom House tarehe 10 Februari 2019 inaeleza kwamba Tanzania inashindana na maeneo yenye hatari kisiasa duniani. Hii ni kutokana na kukamata viongozi wa upinzani, kuzuia maandamano dhidi ya Serikali, kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani na sheria ya kuimarisha chama tawala na kuminya vyama vya upinzani. Ripoti ya Freedom House inaendelea kueleza kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani ambazo zilipata maendeleo ambayo yameathiri mwelekeo wake wa kidemokrasia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuridhika na hamasa za Watanzania katika uwekezaji wa ujenzi wa viwanda page 33, lakini ripoti ya taasisi ya Quantum Global Research Lab ya Machi 2018 juu ya uwekezaji Barani Afrika inaeleza kwamba Tanzania huenda isifikie lengo lake la kujenga uchumi wa viwanda. Hii inatokana na mabadiliko ya sera za usimamizi wa fedha na rasilimali ambazo siyo rafiki kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huu ulihusisha nchi 54 za Afrika ambapo Tanzania ilishika nafasi ya 13 mwaka 2018 kutoka nafasi ya nane mwaka 2017 kwa nchi zenye mazingira mazuri ya uwekezaji. Mabadiliko ya sera za fedha na mazingira magumu ya kuanzisha na kufanya biashara ambayo yanaathiriwa na ongezeko la kodi na upatikanaji wa leseni za biashara ni sababu za mkwamo wa ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) urahisi wa kuanzisha biashara Tanzania uko chini ya wastani unaotakiwa na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Naiomba Serikali kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji ili iweze kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Kitanzania wamekata tamaa kutokana na tatizo la ajira linalowakabili. Kati ya mwaka 2015 hadi Desemba 2018 jumla ya vijana 594,300 walimaliza vyuoni kati ya hao ni vijana 6,554 sawa na asilimia 1.1 ndiyo waliopata ajira. Hali hii inaonesha kushindwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia vijana wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la vijana kukosa ajira baada ya kumaliza masomo yao kunaweza kusababisha madhara ya afya zao. Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema karibu vijana milioni 3.7 wanaugua ugonjwa wa sonona (depression) kutokana na ukosefu wa ajira. Niombe Serikali kuhakikisha vijana wanapomaliza masomo yao wanapatiwa ajira ili kuwaepusha na ugonjwa huo wa sonona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi zinapunguza kasi ya kuajiri na inapunguza wafanyakazi kutokana na mazingira yasio rafiki kwao. Hivyo basi ni jukumu la Serikali kukabiliana na changamoto za ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia mishahara na maslahi katika utumishi wa Umma. Watumishi Serikalini wanakatishwa tamaa na maisha. Hii ni kutokana na kipato cha mishahara, hakikidhi mahitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, punguzo la 11% hadi 9% linatekelezwa kwa wafanyakazi wenye mishahara ya kima cha chini. Kodi kubwa hadi kufikia asilimia 30 inaendelea kukatwa kwa wafanyakazi wenye mishahara ya kima cha juu. Wafanyakazi sasa hulazimika kutafuta kipato cha ziada kwa njia nyingine, jambo ambalo linaweza kuathiri uzalishaji na kupunguza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu ajira katika utumishi wa Umma. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri haijatueleza kiwango cha Watumishi wa Umma ambao wameajiriwa, lakini kuna taarifa kwamba kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 - Desemba, 2018 takribani vijana 594,300 waliomba ajira Serikalini, lakini ni vijana 6,554 sawa asilimia 1.1 pekee ndio waliopata ajira. Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ya Desemba 10, 2018, taasisi yake ina upungufu wa wafanyakazi 1,930 ambapo athari yake ni ucheleweshwaji wa ukusanyaji wa kodi. Baadhi ya Wilaya wameshindwa kufungua ofisi na Serikali inakosa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni mpango wa kunusuru kaya masikini. Wazee wetu walio wengi ni masikini na Serikali yetu ilijipiga kifua kuwa watatoa shilingi bilioni 66.5 kwa ajili yao. Inasikitisha kuona Serikali hii inajisifu kuwa inatetea wanyonge (Serikali ya wanyonge) kwamba tokea ilipoingia madarakani (2015) mpaka tarehe ya leo imetoa shilingi bilioni 1.35 kati ya shilingi bilioni 4.35 zilizotolewa tokea kuasisiwa kwa mpango huu hapo mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utawala bora, Tanzania ni miongoni mwa nchi 16 za Afrika na ndiyo nchi pekee Afrika Mashariki iliyokataa kutia saini na kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika unaohusu demokrasia, uchaguzi na utawala bora (ACDEG). Mkataba huu unalenga kuchochea mijadala miongoni mwa wadau wanaotetea utawala bora na demokrasia Barani Afrika. Kama haitoshi, Tanzania pia imejiondoa katika makubaliano ya kuondokana na kasumba ya kuendesha mambo kwa siri kati ya Serikali na wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya Tanzania kujitoa katika mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi na ukweli (Open Government Partnership) inazua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa Sera ya Uwazi. Kutokana na hatua hizo, inaonyesha kwamba Tanzania imekusudia kuendeleza kuminya demokrasia na uhuru wa watu wake kutoa maoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Muswada huu uliopo mbele yetu. Kabla sijaendelea nami naipongeza hotuba ya Upinzani ambayo imeshiba ushauri. Namshauri Mheshimiwa Waziri auchukue ushauri huo kwa sababu ni mzuri kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi mimi nitajikita katika suala hili la leseni kwa walimu, ambalo nahisi kidogo ni geni. Kwa kule Zanzibar kwetu siyo geni, walimu wana leseni, lakini sijui kutakuwa na tofauti gani kwa leseni zinazotumika Zanzibar na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani alivyosema, tasni yetu ya elimu ina uchache wa walimu. Pamoja na Mheshimiwa Waziri kusema kwamba kuna ongezeko la walimu lakini lazima tujue kwamba kuna matataizo ya walimu. Ukienda kwenye shule huko utakuta wengine wanakamatiza tu, kuna masomo hayana walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuweka kipengele hiki cha leseni maana yake umeweka kizuizi cha wengine wasiingie katika kada hii ya ualimu. Ni jambo nzuri, lakini tukumbuke kwamba kuna baadhi ya masomo katika shule zetu, sio walimu tu wenye taaluma ya ualimu wanaofundisha. Mfano kuna masomo ya hisabati na fizikia, kuna walimu tunawategemea kama wa engineers. Ukienda kwenye shule za binafsi hawa walimu wanapatikana kwa wingi lakini hawajapitia ualimu. Je, tunapoweka kikwazo hiki huu mchango wa hawa watu utapatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu nilimsikia Mheshimiwa Waziri akisema kwamba asilimia 90 ya wanafunzi wetu wanaohitimu masomo yao, wanafeli somo la hisabati. Kwa hiyo, hiyo asilimia 10 inayopatikana Waziri ajue kwamba na hawa watu wengine wa nje wana mchango wao. Kwa hiyo, pamoja na mambo mengine kipengele hiki cha kuweka leseni kinakwenda kuzuia walimu wengine ambao watataka kusaidia hii taasisi wasipate nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kingine ni malipo ya ada ya leseni. Kama tunavyojua walimu wetu ni dhaifu kimapato. Katika wafanyakazi ambao wanawalipwa kima kidogo kabisa cha malipo ni walimu. Walimu hawana hata mahali pa kukaa. Walimu katika ya mishahara yao wanalipa income tax na kuna malipo mengine, ikiwa wataongezewa mzigo mwingine wa malipo itakuwa ni janga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, ikiwa ni malipo ya leseni kwa walimu iwe ni mara moja. Yaani pale wanapokwenda kukata leseni, iwe ni mpaka kustaafu kwake. Vinginevyo ikiwa kila mwaka wanalipa haya malipo ni kwamba mnafanya walimu ni chanzo cha mapato ya Serikali kitu ambacho hakikubaliki. Kwa hiyo, nashauri malipo ya leseni yaondolewe au yawe mara moja tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiondoka hapo, naenda kwenye ukomo wa hii leseni. Sifa ya ualimu ni ujuzi na ujuzi hauzeeki. Walimu wengi wanapostaafu wengine hutaka waendeleze ujuzi wao katika shule nyingine za binafsi. Sasa nilitaka kujua vipi huyu mtu ambaye amefika ukomo wa kustaafu, ataruhusiwa kufundisha katika shule au ni mpaka akate leseni nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hilo hilo la leseni, sasa nizungumzie hawa walimu wa kigeni. Katika shule zetu, hususan private, utakuta kuna walimu wa kutoka Uganda, Kenya, Sudan wapo mpaka Waturuki wapo, sasa hawa watakuwa na sifa zao zinazowaleta hapa. Kipengele hicho sijakifahamu mpaka sasa hivi, nataka Mheshimiwa Waziri atueleze, vipi wakiwa hapa watachukua zile zile sifa zao walizokuja nazo au tutawapa leseni kama tunavyowapa hawa walimu wa Kitanzania? Nashauri walimu watakaoingia hapa pamoja na sifa zao na wao tuwalazimishe wawe na leseni za Kitanzania kama wanavyofanya walimu wa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi langu ni hilo la leseni, naomba kuunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani.