Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ali Hassan Omar King (7 total)

MHE. ALI HASSAN OMARY KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo hata na mimi sasa nimeelewa nini tatizo na chanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zimewekwa hatua za kuchukuliwa kama ambazo tumeziona pale, namuomba Waziri ambaye anahusika na masuala haya ya mazingira na utafiti, japo siku moja twende tukaone ile hali tuweze kuangalia nini kifanyike ili tuweze kupata ufumbuzi zaidi ya hapa ambapo tumeona. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Ali Hassan King kwa jinsi alivyo na mapenzi mema hasa katika suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Ninachopenda kumhakikishia tu hapa kwamba niko tayari na tutafuatana na Mheshimiwa Mbunge tutatembelea maeneo haya yote ambayo yamedidimia na tutaungana na wataalam wengine kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Nataka nimwambie tu kwamba bila kupoteza muda siku ya Jumanne na Jumatano nitakuwa Zanzibar kwa ajili ya kazi hii na tutafuatana naye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara hii ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi yetu.
Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba katika majengo hayo ambayo yamejengwa 360 kwa misimu hiyo iliyopita ni jengo moja ninalolikumbuka mimi ambalo lipo pale Mkoa wa Mjini - Ziwani Polisi kwenye Jimbo langu. Pia Serikali imejenga jengo lingine kwa upande wa Zanzibar kule Pemba, haya majengo ukitazama ki-percentage ni madogo zaidi. Lakini mimi sina uhakika na taarifa hizi za 360; sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri katika 360 ni majengo mangapi yalijengwa kule Zanzibar na katika haya 4,130 mangapi yanatarajia yatajengwa kule Zanzibar? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili Seriklai iliji-commit katika mwaka 2011, Juni kwamba kwa kupitia bajeti wa mwaka ule ingelifanya ukarabati majengo ya Ziwani Polisi, lakini pia wangelijenga na uzio na mpaka hivi sasa ninavyozungumza kwamba askari wanajitegemea wenyewe kufanya ukarabati katika nyumba ambazo wanaishi.
Je, Waziri atanihakikishia ni lini Serikali itakuja kufanya ukarabati wa majengo yale ya Ziwani Polisi pamoja na kujenga uzio? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jang‟ombe kwa ushirikiano wake mzuri sana ambao anatupa kwani ameshiriki katika ujenzi wa Kituo cha Afya pale Ziwani pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji. Tunampongeza sana na tunamuahidi ushirikiano zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali yake mawili, ni kwamba mradi wa nyumba 4,136 ambazo tunatarajia tujenge ni nyumba 200 ambazo zinatarajiwa kujengwa Unguja na nyumba 150 zinatarajia kujengwa Pemba, kwa hiyo ukifanya jumla ya idadi ya nyumba zote 350. Pia ameuliza kuhusiana na zile nyumba ambazo zilijengwa kupitia mradi wa NSSF. Ni kwamba nyumba zilizojengwa ni kweli maghorofa yale yalikuwa ni mawili kwa maana ya Unguja na Pemba lakini yana uwezo wa kukaa familia 12 kila moja kwa hiyo kufanya jumla ya familia 24.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ukarabati wa nyumba za Ziwani ni kweli nyumba zile ni chakavu lakini kama ambavyo tunazungumza siku zote kwamba, nyumba hizi za Polisi nyingi ni chakavu. Ndiyo maana tuna mchakato wa kuweza kurekebisha nyumba hizi pamoja na kujenga mpya. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunafahamu gharama za ujenzi wa nyumba hizo, ukarabati huo ambao unakadiriwa kufika takribani shilingi milioni 400; kwa hiyo tutajitahidi kwamba pale fedha itakapopatikana tuweze kuanza hiyo kazi haraka itakapowezekana.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa nyumba za Ziwani, ikiwa ni Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na chimbuko la historia hata Mapinduzi ya Zanzibar yalianzia pale.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kodi hizo zinalipwa kwa kigezo cha usajili. Ukweli ni kwamba kampuni zote zinasajiliwa kutokana na headquarter alipo regulators. Kwa hiyo, mabenki mengi na makampuni ya simu yako Bara na regulators wake wako Bara, usajili wake unafanyika Bara wanalipia Zanzibar. Lakini ukweli upo kwamba mkaa na maiti haachi kulialia na mtegemea nundu haachi kununa, je, Serikali iko tayari kutumia kigezo cha operations za hizi kampuni kodi ikawa-charged kule ambapo zina-operate?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kodi ambayo tunaiita corporate tax inalipwa kule ambako kampuni imesajiliwa. Hilo alilolisema Mheshimiwa Ali King ni
sahihi lakini pia naomba ndugu zangu tuweze kuangalia uhalisia ulivyo. Kwa mfano makampuni makubwa kama Kampuni ya Bakhresa, Kampuni ya Zanzibar Insurance, Kampuni ya Zantel zimesajiliwa Zanzibar na kodi ya mapato inalipwa kule Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hicho anachokisema naomba nimwambie Mheshimiwa Ally King kwamba hata hizi ambazo zinakusanywa kule Zanzibar, zinakusanywa huku Bara kwa pamoja zinaingia katika mfuko mkuu wa Serikali na kwa pamoja fedha hizi zinapoingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali tunaweza pia kuhudumia
Serikali zote za pande mbili ya Bara na Zanzibar.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba uhai wa Taifa ni kodi. Lakini kuna kodi inakuwa-charged mara mbili ya VAT kwa bidhaa hizo za vifaa vya ujenzi ambavyo vinakwenda Zanzibar kwa wale ambao non registered for VAT. Je, Serikali ina maelezo gani juu ya kutatua kero hii ya double VAT?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza si sahihi kusema kodi inalipwa mara mbili kwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania Zanzibar si sahihi. Kodi ya VAT ni kodi ya mlaji inayolipwa na malaji wa mwisho na kodi hii inakuwa-charged mara moja tu, kodi ambayo najua ina changamoto ya kusema kwamba ina sura ya kulipwa mara mbili lakini kiuhalisia hailipwi mara mbili ni kodi ya import duty ambayo kwa wenzetu Wazanzibari wanapoingiza bidhaa kule Zanzibar mfumo wanaotumia haulingani na mfumo wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo na ile pia hatuwezi kusema ni double taxation ile ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa katika soko wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta na usipotibu utazika, swali langu dogo tu, namuuliza Mheshimiwa Waziri. Ni lini Serikali itakusanya mchango wa maafa kwa jengo bovu la Ziwani Polisi la Kilimanjaro pindi maafa hayo au jengo litakapoanguka. Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limeletwa mara kadhaa. Niseme tu, kwa sababu tuna siku chache kabla hatujakwenda kwenye bajeti yetu tutapa fursa tuongee na Mheshimiwa Mbunge ili tukubaliane kuhusu ni lini kwa sababu swali lake ametaka tumtajie ni lini tutachukua hatua hiyo aliyoisema yeye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimesikia jawabu la Serikali, lakini yeye amejibu mabomu hakujibu gesi. Gesi katika kuzamia haina madhara yoyote kwa sababu kwenye kina kirefu cha maji wenyewe tunaita bahari lujii inawezekana ikawa watu wanatumia nyavu kwa hiyo nyavu imekwama kule chini, kwa sababu ni kina kirefu anaweza akatumia gesi kuzamia kwenda kule. Halafu kingine, hayo mazingira ambayo anayasema Mheshimiwa Waziri kwamba yanaweza yakaharibiwa kwa mabomu kwa baharini wakati mwingine maji yanakupwa yanaweza yakafikika hata kwa miguu lakini haja ya gesi inakuwepo pale maji yanapojaa.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri azidi kuniambia chupa inaharibu kitu gani alichotaja hapa ni mabomu, chupa inaharibu kitu gani, mabomu yanaweza yakategwa hata bila ya chupa. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ugomvi wetu siyo chupa, ugomvi ni matumizi yanayotokana na ile mitungi ya gesi. Kwa maana tunafahamu kuna mahali katika bahari umbali kwa maana ya kina kilomita 40, mvuvi ni lazima awe na namna ya kuweza kumfikisha kule na kufanya shughuli yake, lakini kwa utafiti wetu hapo nyuma ilionekana wazi kwamba waliokuwa wakienda kufanya uzamiaji, ukiacha wale waliofanya uzamiaji kwa ajili ya sport fishing na utafiti, wengine wote walikuwa ni wale wanaoambatana na shughuli za uvuvi haramu na ndiyo maana Serikali ikasema kwa sababu hiyo basi tutazuia zoezi hili isipokuwa kwa kibali maalum cha wale wanaofanya utafiti na wale wanaofanya sport fishing.

Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sasa Serikali tupo katika kuboresha sheria zetu na kuboresha kanuni zetu, tumekisikia kilio hiki cha wavuvi wazamiaji na sisi tunakifanyia kazi, endapo sheria hizi zitapitishwa na kanuni hizi mpya tuna imani kwamba inawezekana katika jambo ambalo litakuwa limekwenda kuboreshwa mojawapo ni jambo hili. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na amenipa mwongozo na yametoa matumaini, lakini nina maswali mawili mdogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni wengi walioweka amana zao pale walitumia viinua mgongo vyao kuweka amana katika Benki ya FBME, hasa kule kwetu Zanzibar nilikotoka. Amesema wamelipwa wateja nusu na waliobakia bado hawajalipwa na watakaolipwa watalipwa kutokana na fedha ambazo watapata amount ambayo haitazidi 1,500,000/=; na kwa kuwa hii benki ni ya nje; na kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Financial Institutions, BOT ndio wenye dhamana ya kukaribisha mabenki ndani, swali langu;’ je, ni lini watalipwa fedha zao zote kwa sababu, benki hii haijafilisika FBME?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Benki Kuu ya Tanzania itaacha kuingiza benki hovyo hovyo kama hizi za kutoka nje zikaleta madhara katika nchi yetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Hassan King kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza alilouliza Mheshimiwa King amesema kwamba, lini wateja hao ambao wana amana zao katika benki ya FBME watapatiwa fedha zao. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, wateja waliokuwa na amana zaidi ya shilingi 1,500,000 watalipwa kiasi kitakachobaki chini ya zoezi la ufilisi wa benki ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Suala hili liko chini ya mujibu wa sheria, kwa hivyo sheria zitakapomalizika Mheshimiwa King basi, wateja wote wenye amana katika benki hiyo watalipwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; anaulizia lini benki zitatoa ukomo wa kuchukua benki ambazo hazina faida katika nchi yetu. Mheshimiwa King jibu lako la pili naomba nilichukue ili nikalifanyie kazi na nitakujibu kwa barua ili uelewe maelezo zaidi katika Serikali yetu, uweze kupata ufafanuzi zaidi wa kupata jibu lako sahihi. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nataka tu niongezee kakipengele kadogo kale ambako kanaongelea lini hawa watu watapata fedha. Kwa benki hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameuliza utaratibu huu ambao ameuelezea Mheshimiwa Naibu Waziri umekuwa mrefu kwa sababu benki hii ilikuwa ina-operate katika nchi mbili. Kwa maana hiyo, ule utaratibu wa mufilisi kuweza kukusanya madeni na kukusanya na mali zote ili azibadilishe ziwe fedha ili aweze kuwalipa wale wateja ambao amana zao zilikuwa zinazidi kile kiwango cha awali ambacho wanapewa pale benki inapokuwa kwenye mufilisi, kikamilike. Kwa hiyo, hicho kikishakamilika hapo ndipo ambapo mufilisi ataweza kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema na hawa wateja waweze kupata hizo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili ambalo Mheshimiwa muuliza swali ndugu yangu King amesema ni lini Benki Kuu itaacha kuruhusu mabenki yaingine hovyo hovyo. Nimhakikishie kwamba, mabenki hayaingii hovyo hovyo na Serikali inafanya due diligence kwa kila benki inapotaka kufanya kazi hapa nchini na ndio maana Benki Kuu iliingilia kati ilipoona baadhi ya mabenki hawaendi sawasawa na vile ambavyo yanatakiwa yafanye kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwa wananchi wetu kwa sababu, huwa kuna report zinazotolewa kila miezi mitatu na kunakuwepo na mkutano mkuu wa wadau wa benki na sisi tuwe tunafuatilia ili tuweze kuona mienendo ya benki. Tusisubirie tu Benki Kuu ambaye ni msimamizi aweze kufanya jukumu hilo ambalo linawahusu pia, wadau wadau wa benki ambao wanatakiwa watoe muongozo kwa benki yao. (Makofi)