Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. George Malima Lubeleje (45 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Waziri kwanza nakupongeza kwa hotuba nzuri kuhusu Sekta ya Kilimo na Mifugo na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naomba nichangie maeneo machache.
Sekta ya Mifugo; Kwanza Wilaya ya Mpwapwa kuna taasisi tatu za Mifugo ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya Mpwapwa (TALIRI), Chuo cha Mifugo Mpwapwa (LITA), Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo (VIC).
Mheshimiwa Waziri, taasisi hizi zote tatu zinategemeana. Taasisi ya Utafiti wa Mifugo-Mpwapwa, ng‟ombe akiugua lazima apelekwe Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo ili achunguzwe anasumbuliwa na nini au Ng‟ombe akifa lazima wapeleke mzoga huo (VIC), Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo ili afanyiwe post-mortem ili kufahamu ugonjwa gani unasababisha ng‟ombe kufa. Vile vile Mpwapwa kuna Chuo cha Mifugo cha Mpwapwa na pale kuna wanafunzi zaidi ya 360,000 wote hawa wanatumia Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa kwa mafunzo ya vitendo.
Mheshimiwa Waziri kwa sasa, Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo (VIC) Mpwapwa imehamishiwa Dodoma Mjini na kusababisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Chuo cha Mifugo (wanafunzi wake) kukosa mahali pa kuchunguza mifugo na wanafunzi kukosa mahali pa kujifunzia kwa vitendo na inabidi wasafiri kuja Dodoma na ni gharama kubwa na ni mbali, pia hupoteza muda mwingi wa masomo.
Mheshimiwa Waziri, taasisi hizi zilijengwa kabla ya uhuru na wakoloni. Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) ilianza mwaka 1905; Chuo cha Mifugo (LITA) kilianza mwaka 1936 na Taasisi hizi tatu zinategemeana. Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi alikataa Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa isihamishwe na kupelekwa Dodoma na mwaka 2015 wakati wa kampeni, Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikataa isihamishwe Dodoma Mjini.
Mheshimiwa Waziri, suala la kusikitisha taasisi hiyo imehamishwa Dodoma Mjini na suala hilo la kuhamishwa taasisi hiyo limewafanya wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kukosa mahali pa kupeleka mifugo yao wagonjwa waweze kuchungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa, Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo irudishwe Mpwapwa haraka kabla hawajamwona Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nakupongeza sana kwa hotuba nzuri sana yenye ufafanuzi mzuri sana wa Sekta ya Elimu. Pili, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na kuunga mkono hoja hii, naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI washirikiane kuhakikisha kwamba suala la madawati linakwisha na wanafunzi wote kuanzia Shule za Msingi na Sekondari wanakaa kwenye madawati siyo kukaa chini. Hii inaathiri sana taaluma na ni suala la aibu, karne ya 21 bado wanafunzi wanakaa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Mpwapwa Sekondari (Mpwapwa High School) ilianzishwa mwaka 1926. Hivi sasa shule hiyo imechakaa sana na haifanani kabisa na hadhi ya Shule ya Mpwapwa Sekondari ya zamani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati Shule za Sekondari Kongwe kama vile Mpwapwa Shule ya Sekondari, Msalato Sekondari na Kilakala Sekondari? Nashauri suala hili wasiachiwe Wizara ya TAMISEMI peke yao, lazima na Wizara ya Elimu ishiriki kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotengwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa sekondari za bweni ni kidogo sana na kusababisha kila mwanafunzi kupata shilingi 1,500/= kwa siku, yaani chai/uji, chakula cha mchana na jioni. Hela hiyo haitoshi kabisa, dola moja kwa siku. Nashauri Serikali iongeze angalau ifike shilingi 2,500/= kwa kila mwanafunzi wa bweni. Wanafunzi lazima wapate chakula ambacho ni balanced diet (carbohydrates, vitamins na proteins) siyo ugali na maharage kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufutwa kwa ada, wananchi wamelipokea suala hilo kwa furaha sana na uandikishaji wa wanafunzi Darasa la Kwanza umeongezeka sana kuliko ilivyokuwa mwanzo. Waliogopa ada na michango mbalimbali. Shule ya Sekondari ya Mpwapwa ni Kongwe lakini mpaka sasa haina gari na ni muda mrefu sana. Je, ni lini shule hii itapatiwa usafiri wa gari? (wapo Wanafunzi 600)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Ualimu cha Mpwapwa kilianzishwa mwaka 1926. Chuo hicho kinahitaji ukarabati mkubwa zikiwemo nyumba za Walimu. Kuna baadhi ya nyumba hazijafanyiwa ukarabati, sasa ni zaidi ya miaka 20, zimechoka sana. Ni lini Chuo na nyumba za Walimu zitafanyiwa ukarabati mkubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa Walimu katika shule zote za Sekondari za kutwa, naishauri Serikali ihakikishe kila shule iwe na Walimu wa kutosha na wa masomo yote ili kuboresha taaluma katika shule hizo. Maslahi ya Walimu yalipwe mapema ili kupunguza malalamiko ya Walimu. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GEORGE M. LUBELEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri sana. Pili naunga mkono hoja hii kwa asilima mia moja, pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda; kwa kuwa wananchi wa Dodoma wanalima sana zabibu lakini hawana soko la kuuza na kiwanda cha kutengeneza au kukamua mvinyo wao ndiyo maana wananchi wanakata tamaa kulima zao la zabibu. Je? Serikali itawasaidiaje wananchi wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vidogo vidogo, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma wanalima sana karanga, zao la alizeti na ufuta, lakini hawana viwanda vidogovidogo vya kukamua mafuta, Serikali isaidie wananchi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii. Kwanza niwashukuru sana wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kwa kutuchagua sisi Wabunge wawili na wote tunaitwa George, kwa hiyo tuwashukuru sana Madiwani wote thelathini na tatu wote ni wa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Hata hivyo, mwaka jana wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kwamba barabara ya kutoka Mbande - Kongwa - Mpwapwa mpaka Kibakwe itajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpwapwa ni ya zamani sana, sasa ina zaidi ya miaka mia moja tangu mwaka 1905 Mpwapwa ipo, lakini hakuna hata barabara ya lami, barabara zote za mjini ni vumbi. Kwa hiyo, naomba sana hili litekelezwe na barabara za Mpwapwa Mjini kilometa kama kumi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anaifahamu vizuri Mpwapwa, basi aweke lami katika barabara zote hizi hata Kibakwe aweke lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru, niwapongeze Mawaziri kwa bajeti zao nzuri, lakini niishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti, toka asilimia ishirini na saba mpaka asilimia arobaini. Hata hivyo, tuna tatizo, amezungumzia Mheshimiwa Tizeba hapa kwamba miradi mingi imekwama, haijatekelezwa, hapa kazi yetu Bunge ni kupitisha bajeti, ni matarajio yetu kwamba tukipitisha bajeti fedha zinapelekwa Halmashauri na fedha zile basi zifanye kazi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi imekwama katika Wilaya zetu, fedha zinachelewa kuletwa kwenye Halmashauri, hatujui sababu ni nini, ni nani anayekwamisha hii, fedha zinakuja zimechelewa, wakati fulani zinaletwa fedha kidogo, si kile kiwango ambacho Bunge limepitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano Wilaya ya Mpwapwa kwa jimbo langu na lina vituo viwili vya afya sasa ni miaka kumi havijakamilika, Kituo cha Afya cha Mima na Kituo cha Afya cha Mbori. Miaka kumi fedha haitengwi kwa nini, akinamama wanapata taabu kujifungua kupelekwa mpaka Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, wengine wanafia njiani. Kwa hiyo, naomba sana katika bajeti hii, Serikali ihakikishe vituo vile vinakamilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa, hebu simamia hizi fedha ziende kwenye miradi ya maendeleo zisichelewe, kwa nini hizi fedha zinacheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mradi wa maji katika Mji wa Mpwapwa. Mji wa Mpwapwa kulikuwa na mradi wa maji ambao gharama yake ilikuwa ni bilioni nne na milioni saba, lakini mradi umekamilika Mheshimiwa na wananchi wanapata maji, wakazi zaidi ya hamsini elfu lakini tatizo kuna mota moja imeungua, kwa hiyo, maji yamepungua wananchi wanapata shida. Hivi naiuliza Serikali hivi mota ya shilingi ishirini na tano milioni, Serikali inaweza kushindwa kununua kweli, naomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu barabara, Wilaya ya Mpwapwa ina mtandao wa barabara kilometa elfu moja na mia saba, barabara ya kutoka Mpwapwa kwenda Gulwe, Kibakwe, rudi mpaka Chipogoro ile barabara ni ya TANROAD lakini kwa sababu mvua zimenyesha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu ametuletea mvua, lakini barabara ile ni mbaya inapitika kwa shida. Kwa hiyo, naomba TANROAD ijitahidi kutengeneza zile barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Mpwapwa - Gulwe - Berege - Mima - Pufu tulikwishaomba Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina uwezo wa kukarabati au kutengeneza hizi barabara. Kwa hiyo, ombi langu kwamba zile barabara basi naomba TANROAD wachukue ili waweze kuzitengeneza iwe chini ya TANROAD ile barabara iweze kukarabatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni TASAF, ni chombo cha Serikali na TASAF inawasaidia sana Watanzania, Awamu ya Kwanza imejenga shule, zahanati Awamu ya Pili, sasa Awamu ya Tatu ni kusaidia kaya maskini, hivi karibuni tumetembelea miradi ya TASAF Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Mwanza. Tatizo wanaonufaika zaidi sio wale maskini, wanaonufaika zaidi ni Wenyeviti wa Mitaa, ndiyo wanachukua zile pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha sana kila Halmashauri ya Wilaya ina mratibu wa TASAF, kwa nini wasisimamie pesa hizi na kila bajeti tunatenga fedha kwa ajili ya TASAF, kila halmashauri. Kwa hiyo, naomba sana waratibu wa TASAF wasimamie hizi pesa zifanye kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA tumetembelea Wilaya ya Magu, wananchi wengi hawana elimu, hawajapata elimu kuhusu MKURABITA, ndiyo maana tumekwenda pale wananchi wanalalamika kwamba kununua hati shilingi elfu thelathini na tano ni nyingi sana. Kwa hiyo, wengine wameshindwa mpaka sasa tumekuta hati zaidi ya mia tisa zipo pale hazijachukuliwa, wananchi wanachodai kwamba zile hati ukipeleka benki hawazitambui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana wale waratibu wa MKURABITA kila Halmashauri wajitahidi sana kutoa elimu kwa ajili ya mradi huu. Miradi hii inasaidia sana, tunapata fedha za wafadhili, TASAF fedha za wafadhili na bajeti kidogo ya Serikali na MKURABITA. Zikitumika vibaya wale wanaotusaidia kuna siku watasema hapana tumepeleka hii fedha haikuweza kuleta maendeleo, mmeitumia vibaya, kwa hiyo sisi tunaondoa hii misaada; litakuwa ni tatizo kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana na naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Afya. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na mazingira magumu ya ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wilaya yangu ya Mpwapwa. Wilaya ya Mpwapwa ina Hospitali ya Wilaya, lakini kuna upungufu mkubwa sana wa Madaktari na wafanyakazi wa kada nyingine. Mpwapwa kuna upungufu wa wafanyakazi 285 wa kada mbalimbali, ina Vituo vya Afya viwili, Rudi pamoja na Kibakwe. Kwa utaratibu wa Wizara ya Afya Kituo cha Afya lazima kuwe na Assistant Medical Officer kwa ajili ya kufanya minor surgeries, kama kuna complicated cases pale, lakini pale kuna Clinical Officer na Kibakwe kuna Clinical Officer. Kwa hiyo, naomba watupelekee Assistant Medical Officers katika Vituo hivi vya Afya Kibakwe pamoja na Rudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mpwapwa ina Zahanati 50. Nusu ya Zahanati hizo zinahudumiwa na Medical Attendant. Nawapongeza Medical Attendants, wanafanya kazi vizuri, lakini ni kazi kubwa sana, kwa sababu mpango wa Wizara ya Afya ulikuwa ni ku-train Clinical Assistants wengi ili kuwasambaza kwenye zahanati, lakini huu mpango umeishia wapi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba anieleze mpango huo umeishia wapi ili zahanati nyingi ziwe na Clinical Assistant au Clinical Officers.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa madawa. Nimewahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya MSD, tatizo siyo MSD, tatizo MSD haina fedha. Kwa hiyo, upungufu wa fedha, uhaba wa fedha MSD ndiyo maana wanakosa madawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali itenge fedha za kutosha. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, tumeona kwamba hapa mmetenga shilingi bilioni 65, lakini umetoa taarifa kwamba kuna shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kulipa deni la MSD na vile vile kununua madawa. Naomba fedha zote zipelekwa MSD, zisipelekwe shilingi bilioni moja mwezi huu, mwezi ujao shilingi bilioni mbili, hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MSD, Bodi yetu imewahi kutembelea Sudan Medical Store pamoja na Uganda Medical Store. Medical stores zao zinakuwa full funded na Serikali na wana Vote kabisa. Pesa inatoka Hazina, wanapelekewa Medical Store, lakini hapa imekua ni tatizo. Tumezungukia hospitali nyingi, hakuna madawa na tatizo la madawa wanasema labda MSD ndiyo hawasambazi madawa, lakini tatizo ni fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri, Wabunge wengi wamechangia suala hili, nadhani sasa MSD itapata fedha za kutosha ili wanunue madawa na kusambaza hospitali zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie ugonjwa wa kipindupindu. Limekuwa ni tatizo katika nchi yetu. Kipindupindu ni ugonjwa mbaya, unaua watu wengi, lakini ni ugonjwa wa kujitakia, wala siyo ugonjwa wa bahati mbaya. Kwa sababu nakumbuka zamani kulikuwa hakuna ugonjwa wa kipindupindu. Nimewahi kuwa Bwana Afya; ilikuwa ikitokea kesi moja ya ugonjwa wa kipindupindu au mgojwa mmoja, lazima iwe reported World Health Organization kwamba Tanzania kuna ugonjwa wa kipindupindu. Sasa imekuwa cholera is endemic in Tanzania, why?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, zamani kulikuwa na Mabwana Afya. Kazi ya Bwana Afya ni kukagua usafi, unakwenda vijijini unakagua usafi; kila kaya iwe na choo, iwe na shimo la taka, iwe na kibanda cha kuweka vyombo ambavyo vimesafishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi Wizara ya Afya ni mfumo. Bwana Afya hafanyi kazi alizosomea, Bwana Afya anakuwa mratibu wa UKIMWI, Mratibu wa Malaria, Mratibu wa Chanjo. Mabwana Afya wafanye kazi walizosomea. Naomba sana Mheshimiwa Waziri; na zamani kulikuwa na utaratibu wa kupeleka kila Zahanati Health Assistant, mkafuta utaratibu huo, mkasema hapana, kuna upungufu mkubwa sana, labda uhaba wa fedha. Najiuliza, mbona Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wameweza? Kila Kijiji kina Bwana Shamba, kila Kijiji kina Bwana Mifugo. Kwa nini Wizara ya Afya ninyi mnashindwa kupeleka Mabwana Afya Wasaidizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa kazi yao kubwa ni kukagua usafi kila Kijiji. Kila kijiji unakwenda unakagua usafi, haya magonjwa ya milipuko tungeyapunguza. Kinga ni bora kuliko tiba. Pale Muhimbili tulikuwa na Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma (Health Education Unit), kazi yake ilikuwa ni ku-train Mabwana Afya wengi Wasaidizi na wanasambazwa wilaya zote kwa ajili ya kukagua usafi katika vijiji. Siku hizi sijui kama kitengo kipo; kama kipo labda Mheshimiwa Waziri anielimishe, kimeimarishwaje kitengo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya afya kwa umma inasaidia sana. Lazima kwanza pale hospitalini wagonjwa wapewe elimu ya afya kabla ya kutibiwa. Outpatient health education. Tulikuwa na outpatient health education, individual health education na public health education. Kwa mfano Daktari anapomtibu mtu anayeharisha, Daktari anamwuliza kabisa kwa nini unaharisha? Anasema mimi naharisha kwa sababu labda sijui sikuchemsha maji au sina choo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, public health education, lazima Mabwana Afya wasambae vijijini kutoa elimu ya afya, la sivyo kipindupindu kitatumaliza ndugu zangu. Naomba sana Wizara ya Afya itekeleze haya. Bwana Afya afanye kazi iliyokusudiwa na tu-train hawa Medical Attendant hao, au Clinical Assistants wengi kama ninavyosema. Upungufu wanao kama nilivyosema, MSD ni uhaba, kwa hiyo, ni vizuri MSD ikatengewa fedha za kutosha ili iweze kununua madawa mengi na kusambaza katika hospitali. Wananchi wengi wanapoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa madawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono kwa asilimia mia moja kwa mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwanza kabisa nakupongeza kwa hotuba yako nzuri. Pili, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba nichangie maeneo yafuatayo:-
(i) Sekta ya Umeme, suala la kukatikakatika kwa huduma ya umeme Wilaya za Mpwapwa, Kongwa, Gairo; je, ni sababu gani zinazofanya umeme kukatikakatika katika Wilaya hizo na kusababisha vitu vingi kuungua. Mheshimiwa Waziri ana maelezo gani kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwa ni kero kubwa sana.
(ii) Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia umeme Vijiji vya Makutupa, Bumila, Mbori, Inzomvu, Tambi, Mlembule, Mwenzele, Nana, Mafuto, Majani, Mugoma, Mzogole, Kisisi, Sazima, Igoji Kusini (Isalaza), Chamanda, Kiboriani, Makanana, Chibwengele, Pandambili (Jimbo la Mpwapwa) Makawila, Chimaligo, Kazania, Kiegea na Ngalamilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Madini, kwa kuwa Wilaya ya Mpwapwa kuna Wachimbaji wadogo wadogo Vijiji vya Winza (wanachimba rubi), Tambi, Mlembule (wanachimba copper) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mpwawa ili waboreshe hali ya uchimbaji wa madini kuliko hivi sasa wanatumia vifaa duni. Je, Mheshimiwa Waziri au Naibu watatembelea lini Wilaya ya Mpwapwa ili kukutana na wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja hoja hii na kumtakia Mheshimiwa Waziri kila la heri, bajeti yake ipitishwe na Bunge hili Tukufu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Waziri kwa hotuba nzuri kuhusu sekta ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi. Pili, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-
(i) Wananchi waelimishwe kuhusu matumizi bora ya ardhi na kutambua mipaka yao ya ardhi wanayoimiliki.
(ii) Wananchi wanapata shida kutembea mwendo mrefu kufuata Baraza la Ardhi. Nashauri Serikali ianzishe Baraza la Ardhi kila Wilaya ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa.
(iii) Wawekezaji wasichukue ardhi ya wananchi bila kulipa fidia.
(iv) Kwa kuwa Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa hukopa fedha kwa ajili ya kupima viwanja ni vema warejeshe mikopo hiyo mapema ili Halmashauri zingine nazo zikope (revolving fund).
(v) Serikali isimamie ujenzi holela wa miji yetu (squatters) na kila mji lazima uwe na master plan kabla ya kuanza kujenga.
(vi) Serikali itenge fedha za kutosha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo badala ya kutegemea wafadhili ambapo hakuna uhakika wa kuletewa fedha zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nakupongeza kwa hotuba yako nzuri sana yenye ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya Wizara yako. Pili naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-
(i) Ufinyu wa bajeti katika Wizara hii na kusababisha kufanya Wizara kushindwa kutekeleza majukumu yake na hasa miradi mingi ya maendeleo kutokamilika kwa wakati. Fedha za miradi zitolewe za kutosha na kwa wakati.
(ii) Serikali isitegemee sana fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kuwa hakuna uhakika kama fedha za nje zitaletwa zote au kidogo na kwa wakati gani. Fedha za ndani zitumike zaidi.
(iii) Uhaba wa watumishi wa sekta ya maliasili na utalii na hasa katika Wilaya zetu hakuna Maafisa Misitu, magari, pikipiki na baiskeli na maslahi duni.
(iv) Je, sababu gani zinazofanya idadi ya watalii kupungua?
(v) Je, ni sababu gani zinazofanya Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kabisa kukabiliana na ujangili na kusababisha wanyama kama tembo, vifaru wanaoendelea kupungua katika mbuga zetu, je, hakuna mbinu za kisasa za kukabiliana na majangili kwa kuwa wanaongezeka siku hadi siku.
(vi) Serikali ijitahidi kuboresha huduma kwa watalii kama hoteli, afya, barabara na ulinzi wa watalii na viwanja vya ndege.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napongeza sana kwa hutuba nzuri sana. Pili naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia haya yafuatayo:- CDA ni chombo cha Serikali Kuu na chombo hiki kipo ndani ya Manispaa ya Dodoma, Manispaa ya Dodoma ni chombo cha mamlaka ya Serikali za Mitaa. CDA wanapima viwanja na kuchukua mapato ya ardhi kodi ya ardhi ambayo ipo chini ya Manispaa ya Dodoma na Manispaa wanapima viwanja na kuchukua kodi ya viwanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri Mkuu huu sio mgogoro kati ya CDA na Manispaa ya Dodoma kwa kuwa Kisheria ardhi yote ni mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ndiyo wenye haki ya kupima viwanja na kupata kodi ya viwanja (ardhi) na sio CDA. Sheria
iliyoanzisha CDA iangaliwe upya, CDA ilianzishwa kwa ajili ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma na tayari Makao Makuu Dodoma yameanza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie machache kuhusu Wizara hii. Kwanza, niungane na Wabunge wenzangu, nakupongeza sana wewe binafsi na endelea na msimamo huo. Mimi nimo Bungeni humu sasa ni kipindi cha tano, Bunge ni mhimili, lazima uheshimike, Bunge si mkutano wa hadhara, siyo lazima kila hoja inakotoka kule, kwa mfano kuna tukio limetokea Mpwapwa sasa tuahirishe Bunge tujadili mambo ya Mpwapwa, sijawahi kuona kitu kama hicho mimi. Kwa hiyo, mimi nakuomba endelea asubuhi unakuja, jioni unakuja waendelee kutoka tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na TRA. Niwapongeze TRA wanafanya kazi nzuri sana ya kukusanya mapato lakini jiulize, kazi ya sisi Wabunge hapa ni kupitisha bajeti ya Serikali na tukishapitisha bajeti fedha zinagawanywa Wizara, Mikoa na Wilaya na mradi ukishapangiwa bajeti, kama ni barabara basi fedha yote ipelekwe. Nashangaa kwamba fedha zinapangwa, Bunge linapitisha bajeti lakini utakuta mwisho wa mwaka wa fedha karibu nusu ya fedha hazijaenda kwenye miradi.
Kwa hiyo, hii inatusababishia kuwa na viporo na vingi miradi mingi haikamiliki. Mheshimiwa Waziri hebu anieleze anayezuia/anayekata hizi fedha kule Hazina ni nani? Kwa sababu wenye madaraka ya kupitisha bajeti ni Wabunge, hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kupunguza hizi fedha kwa ajili ya kazi nyingine. Kwa hiyo, naomba sana tukishapitisha bajeti basi Wilaya, Mikoa ipelekewe fedha zile ambazo Bunge limepitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nizungumzie kidogo Mfuko wa Mahakama, hili Fungu 40. Mahakama wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hasa Mahakama za chini, tuna upungufu mkubwa sana wa mahakimu na wa mahakama. Kwa mfano, Wilaya ya Mpwapwa ina Mahakama za Mwanzo tatu tu na Kata ziko 33, kwa hiyo, wananchi wanasafiri mwendo wa kilometa zaidi ya 60-70 kufuata mahakama. Pamoja na ufinyu wa bajeti, naomba Serikali itenge fungu la kutosha kwa ajili ya kujenga Mahakama za Mwanzo na kuendelea kufundisha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Tuna chuo chetu kile cha Lushoto, hebu tuongeze idadi ya wanafunzi. Nimekitembelea kile chuo mwaka juzi, mazingira yake hayaridhishi, tuongeze majengo ili wanafunzi wawe wengi tuweze kupata Mahakimu wengi wa Mahakama za Mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee jengo langu la Mahakama ya Mpwapwa. Nashukuru sana lile jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa ni jipya lakini halijakamilika bado. Hosteli ya Majaji hakuna, mgahawa hakuna, kama ilivyo kwenye majengo mengine mfano Kongwa. Kwa hiyo, naomba lile jengo likamilishwe ili Jaji akija asilale kwenye hoteli za kawaida, hapana, siyo vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Fungu la 42, Mfuko wa Bunge, hapa nimeona fedha za miradi zilizotengwa ni shilingi bilioni saba na Wabunge wengi hawana Ofisi. Sasa labda nipate maelezo Mheshimiwa Waziri, hizi fedha ni pamoja na kujenga Ofisi za Wabunge au kwa shughuli zingine? Kwa sababu Wabunge wanalalamika hawana ofisi na zimetengwa fedha kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Sheria za Manunuzi, sheria hii inatuumiza sana. Mimi nimewahi kuwa Mjumbe wa Bodi za aina mbalimbali, kwa mfano ukichukua shule ya sekondari ya bweni, dukani sukari unanunua shilingi 2000 au shilingi 2500 lakini mzabuni ananunua shilingi 3000 au shilingi 4000. Kwa hiyo, kwa kweli sheria hii inatuumiza sana. Hivi kuna tatizo gani kuleta huu Muswada hapa Bungeni turekebishe hii sheria? Maana kila mwaka Serikali inasema italeta, italeta kwa nini msilete, watu wanaumia, fedha nyingi za Serikali zinaishia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi yangu yalikuwa ni hayo machache lakini nisisitize sana ujenzi wa Mahakama hususani Mahakama za Mwanzo na kuongeza mafunzo ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ili waweze kusambazwa kwenye Mahakama za Mwanzo. Nakushukuru na naunga mkono hoja hii lakini narudia tena uendelee na msimamo wako huo huo, asubuhi na mchana uwepo waendelee kutoka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kukupongeza kwa hotuba yako nzuri. Pia naunga mkono kwa asilimia mia moja pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni wachache sana hapa nchini. Wilaya yangu ya Mpwapwa ina Kata 33 lakini PCM wapo wanne tu na hawana usafiri, angalau PCM wote nchini wangepata pikipiki au magari madogo ya kuwasaidia kutembelea Mahakama za mbali kuliko ilivyo sasa PCM wengi wanapanda mabasi ambapo ni hatari hasa PCM akiwa na mafaili ya kesi anaweza kuporwa ndani ya basi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wajengewe nyumba za kuishi badala ya kuishi mitaani ambapo ni hatari kwa maisha yao, bahati mbaya anaweza kupanga na mtu mwenye kesi katika Mahakama yake. Maslahi ya PCM ni duni sana waongezwe mishahara ili kumudu mazingira wanayoishi au kuboresha maisha yao kuliko hali ilivyo sasa. Wilaya ya Mpwapwa tulijengewa jengo la Mahakama ya Wilaya lakini Rest House ya Mheshimiwa Jaji haikujengwa mpaka sasa. Je, itajengwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kila Tarafa zijengwe Mahakama za Mwanzo nne ili kuwasogezea wananchi huduma ya Mahakama karibu kuliko hali ilivyo sasa wananchi hutembea kilomita zaidi ya 100 kufuata huduma hiyo. Chuo cha Mahakama Lushoto waongeze wanafunzi ili kuongeza idadi ya PCM hapa nchini.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukupongeza wewe mwenyewe kwa kazi nzuri unayoifanya, tuko pamoja na wewe, uendelee kukaa hapo mpaka tarehe Mosi Julai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niipongeze sana TRA kwa kufanya kazi nzuri ya kukusanya mapato. Sasa hivi mapato yetu ni mazuri, ninachoomba tu ni kwamba hiki kinachokusanywa basi kifike kwa walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna miradi mingi ambayo haijakamilika vijijini, kwa sababu fedha za miradi hazifiki au zinafika kidogo, lakini Bunge kazi yetu ni kupitisha bajeti na tukishapitisha bajeti lazima fedha zifike kwenye miradi ya maendeleo, kama hazitafika kule miradi haitakamilika.
Kwa hiyo, ninachoomba baada ya makusanyo haya basi fedha ziende kwenye miradi ya maendeleo. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Mpwapwa nina zahanati kwa mfano zahanati ya Mgoma haijakamilika, zahanati ya Igojimbili haijakamilika, Igojimoja haijakamilika pamoja na vituo vya afya vya Mboli na Mima sasa ni miaka kumi havijakamilika, kwa sababu fedha hazijatengwa kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine huduma za afya. Sasa hivi kuna tatizo kubwa sana la dawa katika zahanati, vituo vya afya, Hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa, ni kwa sababu wanaosambaza dawa ni MSD, lakini hatuwezi kuwalaumu MSD kwa sababu hawana fedha. Fedha wanazotengewa ni kidogo sana, halafu hata zile fedha kidogo hazipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna deni la MSD shilingi bilioni 71, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, deni hili lazima lilipwe. Mheshimiwa Waziri wa Afya alitueleza Bungeni kwamba ametenga shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kupeleka MSD kwa ajili ya kununua dawa, basi naomba hizo fedha zipelekwe MSD; kwa sababu MSD bila kupeleka dawa katika zahanati itakuwa ni kazi ngumu sana, wananchi wanalalamika hakuna dawa. Wananchi wanakwenda kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali, wanaandikiwa vyeti wanaambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi. Kwa kweli hii haipendezi hasa kwa Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nizungumzie kuhusu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zetu za Wilaya na Manispaa. Mapato ndiyo uhai wa Halmashauri kwa hiyo, Halmashauri isipokusanya mapato hasa ya ndani kwa kweli, lazima Halmashauri zitayumba. Halmashauri lazima zijitegemee kwa mapato ya ndani, ninapozungumza hakuna Halmashauri ambayo inakusanya mapato zaidi ya asilimia kumi kwa kujitegemea, zote zinakusanya chini ya asilimia kumi, kwa hiyo, wanategemea ruzuku ya Serikali Kuu. Na mimi najiuliza hivi siku Serikali Kuu ikisema haitoi ruzuku, Halmashauri zitabaki? Hazitabaki! Kwa hiyo, wajitahidi kukusanya mapato, ni suala la TRA kukusanya mapato na hasa kodi ya majengo (property tax), mimi siliungi mkono kwa sababu hiki kilikuwa ni chanzo kimojawapo cha mapato ya Halmashauri ya Wilaya. Vyanzo vingi vya Halmashauri za Wilaya vimechukuliwa na Serikali Kuu, kulikuwa na hotel levy, kulikuwa na mambo haya ya mafuta, walikuwa wanakusanya Halmashauri za Wilaya, lakini baadaye Serikali Kuu ilichukua hivi vyanzo. Kwa hiyo, naomba hata kama TRA ikikusanya, lakini fedha zote zikabidhiwe Halmashauri. Siyo tena waanze kudai kama deni, hapana. Kama watakusanya TRA basi fedha hizo zipelekwe kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wetu wa Vijiji wanafanya kazi nzuri sana, lakini hawalipwi hata senti tano. Kwa hiyo, naomba katika bajeti yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha wafikirie angalau kidogo kwa sababu hawa ndiyo wanaofanya kazi za Serikali za Mitaa na kazi za Serikali Kuu katika vijiji kwa hiyo, wafikiriwe angalau kulipwa posho kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu umeme; naipongeza Serikali kwa kusambaza umeme katika vijiji na mimi vijiji vyangu vya Jimbo la Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa tumepata umeme, lakini kuna baadhi ya vijiji bado! Kwa mfano Kijiji cha Sazima nguzo zinapita karibu na kijiji, lakini hakuna umeme; Igoji Kaskazini hakuna umeme nguzo zinapita pale; Iwondo hakuna umeme; Mkanana hakuna umeme mpaka sehemu za Mlembule Tambi kule tayari nguzo zimeshapelekwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Serikali ijitahidi kusambaza huu umeme; umeme ni maendeleo, umeme ndiyo uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi. Naunga mkono kwa asilimia 100.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namkupongeza sana Waziri kwa hotuba yake nzuri yenye ufafanuzi wa mambo mbalimbali ya sekta ya afya. Pili, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na kuunga mkono hoja hii, naomba kuchangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa vituo vya afya ni muhimu sana hasa katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi wapo, vituo vya afya lazima viwe na wataalam wa kutosha na viwe na daktari msaidizi, wauguzi wa kutosha na wakunga wa kutosha. Madaktari wasaidizi wanasaidia sana kufanya operation hasa kwa akina mama wajawazito ambao hushindwa kujifungua, wakunga pia ni muhimu sana kwa ajili ya kuzalisha akina mama wajawazito. Akina mama wengi hupoteza maisha kwa kushindwa kujifungua kama vituo vya afya hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) huduma za Bima ya Afya itakuwa na maana kila kituo cha kutolea huduma kama vile zahanati, vituo vya afya, Hospitali za Wilaya na Mikoa kama vituo hivyo vitakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha badala ya wanachama wa bima ya afya wataambiwa wanunue dawa katika maduka binafsi.

Mheshimwa Mwenyekiti, kuhusu Bohari ya Dawa (MSD); kwanza ninaipongeza sana Bohari ya Dawa (MSD) kwa kazi nzuri sana ya kusambaza dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolewa huduma za afya, changamoto kubwa katika taasisi hii ni kutokupewa fedha za kutosha kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba ili kusambaza katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya. Ushauri wangu ni kwamba MSD watengewe fedha za kutosha kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Afya ni muhimu sana hasa katika kusimamia afya ya mazingira na kuzuia magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu (cholera), magonjwa ya kuharisha (dysentery),typhoid fever na kadhalika. Ipo haja ya kuimarisha Idara ya Afya Kinga (Preventive Services).

Maafisa wa Afya wakitekeleza majukumu yao vizuri hata magonjwa ya kuambukiza yatapungua. Naomba maelezo kwa nini Maafisa Afya wanahamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira? Maafisa wa Afya ni watumishi halali wa Wizara ya Afya na wamesomeshwa na Wizara ya Afya, kwa nini sasa wahamishiwe Ofisi ya Makamu wa Rais –Idara ya Mazingira? Nashauri Maafisa Afya wote warudishwe Wizara ya Afya - Idara ya Kinga na kusambazwa katika Wilaya zote hapa nchini.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hizi Kamati mbili. Niwapongeze Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe kwa kazi nzuri. Naomba nianze na hili, kwamba Bunge ni mhimili unaojitegemea na sisi Wabunge kazi yetu ni kuisimamia Serikali, lakini hatuwezi kuisimamia Serikali kwa kupata taarifa tu kutoka kwenye taasisi mbalimbali bila kutembelea miradi ya maendeleo, huko sio kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, safari hii tumeshindwa kabisa kwa sababu Bunge halina fedha. Sasa nauliza, tulikuwa na Mfuko wa Bunge, huo Mfuko wa Bunge tulikuwa na fedha, je, Mfuko wa Bunge aliyeuondoa nani? Kwa sababu Mahakama wana Mfuko wao, Serikali na Bunge lilikuwa na Mfuko wake. Kwa hiyo, Bunge lazima liwe na fedha za kutosha kuwawezesha Wabunge, Kamati kutembelea miradi, huku ndiko kuisimamia Serikali. Hatuwezi kuisimamia Serikali kila siku tunakaa Dodoma kwenye Kamati, eti tunasubiri wataalam waje watoe taarifa, hapana, lazima tuisimamie Serikali kwa kutembelea miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mwezi wa Sita tumepitisha bajeti ya Serikali, lakini cha kushangaza sasa hivi wilayani hakuna fedha ambazo zimepelekwa kule, hakuna kabisa. Hakuna barabara inayotengenezwa, hakuna kisima kinachochimbwa, kwa mfano kwangu pale Wilaya ya Mpwapwa, kuna vituo vya afya viwili, Kituo cha Afya cha Mima pamoja na Kituo cha Afya cha Mbori, ni muda mrefu, miaka 10 havijakamilika vituo vile, ni kwa sababu fedha hazipo. Sasa mwaka huu vile vituo vimetengewa, kwa mfano Mima imetengewa milioni 25, lakini hizo fedha sijui kama zimeshapelekwa au hazijapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Kituo cha Afya Mbori kimetengewa milioni 20, sijui kama pesa zimeshapelekwa au hazijapelekwa, ni miaka 10 havijakamilika. Akinamama wajawazito wanapoteza maisha kwa sababu ya usafiri kutoka Mima kwenda Mpwapwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na matatizo, haya mazingira magumu ya ufinyu wa bajeti lakini fedha zipelekwe kwenye halmashauri zetu ili miradi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuhusu utendaji wa halmashauri, halmashauri zinafanya kazi katika mazingira magumu. Halmashauri zilikuwa zinapata fedha toka TAMISEMI kwa ajili ya fidia, kwa sababu halmashauri zilikuwa zinakusanya kodi, kwa mfano kodi ya mafuta, kodi ya hoteli, Serikali kuu ilikuwa ndiyo inayokusanya na sasa kodi ya majengo inakusanya TRA. Kwa hiyo, tunaomba kama TRA watakusanya hiyo kodi, basi wapeleke hizi fedha haraka, wasikae nazo mpaka halmashauri tuanze kudai tena, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine asilimia 20; vijiji vina miradi mbalimbali, sasa vijiji vimekwama kutekeleza miradi yao kwa sababu hawana fedha na wanategemea hii asilimia 20, lakini asilimia 20 haiwezi kupelekwa vijijini kwa sababu halmashauri hazina fedha. Halmashauri nyingi hazikusanyi vizuri mapato ya ndani, usipokusanya mapato ya ndani huwezi kupeleka hii asilimia 20 kwenye Serikali za Vijiji. Nataka nijue, kwa sababu Waziri na Naibu Waziri wapo; hivi ni kweli ile fidia waliyokuwa wanapeleka halmashauri ya kufidia hii kodi ya maendeleo ambayo ilifutwa na ushuru mbalimbali wa halmashauri, wamesitisha au bado wanapeleka?
Mheshimiwa Naibu Spika, hii asilimia 10 ya akinamama na vijana, hii ni revolving fund wala siyo zawadi. Nakubaliana na Kamati, kwamba halmashauri zitenge asilimia 10 kwa ajili ya kuwapatia akinamama na vijana, lakini warejeshe hii mikopo, bila kurejesha hii mikopo vikundi vingine haviwezi kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi, pamoja na kwamba tumerekebisha Sheria ya Manunuzi hapa, lakini halmashauri nyingi bado karibu asilimia 75, fedha zinapotea kwenye manunuzi kwa sababu hawafuati utaratibu. Kwa hiyo, lazima halmashauri zisimamamiwe ili kufuata Sheria hii ya Manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utengenezaji wa magari, hivi najiuliza, halmashauri za wilaya hazina gereji au kila halmashauri inatengeneza magari inapotaka? Ndiyo maana gharama zinakuwa kubwa na halmashauri zinakosa pesa
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukaimu, ni halmashauri nyingi. Nimekuwa Mjumbe wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, nimetembelea halmashauri nyingi sana, watumishi wengi wanakaimu. Sasa kama anakaimu, Mheshimiwa Waziri, kama mtumishi huyo ana sifa kwa nini asithibitishwe kazini apate kile cheo. Ukaimu una mwisho wake, miezi sita, lakini mtumishi anakaimu zaidi ya miaka miwili, miaka mitatu, huo ni ukaimu wa namna gani, lazima wathibitishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu yalikuwa hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa hiyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja za Kamati zote mbili, Kamati ya LAAC pamoja na Kamati ya PAC.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja hizi mbili za Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Utumishi. Kwanza niwapongeze sana Mawaziri hawa wawili, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hizi kwa kazi nzuri walizofanya katika mazingira magumu sana ya upungufu wa ufinyu wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI ni chombo kikubwa sana na TAMISEMI inatakiwa ipewe bajeti ya kutosha pamoja na Utumishi kwa sababu idara zote zipo TAMISEMI, ukitaka afya – TAMISEMI, maji – TAMISEMI, ujenzi – TAMISEMI.
Kwa hiyo, inatakiwa ipate fedha za kutosha ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali. Hivi sasa kuna miradi viporo katika majimbo yetu kwa sababu fedha hazipo na zimechelewa kufika TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka kuzungumzia ni Jimbo langu la Mpwapwa hasa barabara za Mjini Mpwapwa. Mji wa Mpwapwa ulianzishwa tangu 1905, sasa una zaidi ya miaka 100 lakini hakuna hata barabara moja ambayo ina lami. Kwa hiyo, wakati umefika
sasa barabara za Mpwapwa Mjini zote ziwekwe lami ili ziweze kupitika bila wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayotaka kuzungumzia ni barabara kutoka Gulwe - Berege - Chitemo - Mima - Egoji - Sazima mpaka Seruka. Barabara hii ni mbaya sana, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anaifahamu, ni barabara mbaya inapitika kwa shida. Tangu
mwaka jana nimeomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya barabara hii ili ifanyiwe marekebisho makubwa, lakini mpaka sasa haijatengenezwa. Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina uwezo wa kukarabati barabara hii kwa sababu uwezo wao ni mdogo. Naomba sasa TAMISEMI ikabidhi barabara hii TANROADS ili iwe chini yake na iweze kufanyiwa matengenezo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu tatizo la maji vijiji vya Mima, Iyoma pamoja na Bumila. Nashukuru sana Serikali imechimba visima vitatu, imechimba kisima vijiji vya Mima, Iyoma pamoja na Bumila. La kushangaza sasa ni zaidi ya miaka nane visima hivyo
havijawekwa pampu, mabomba wala matenki kwa ajili ya kusambaza maji. Naiomba Serikali visima hivyo viwekwe pampu na kusambaza maji katika vijiji hivyo. Wananchi wa maeneo hayo wana shida kubwa sana ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni posho za Madiwani. Madiwani posho wanayopata ni kidogo. Bahati nzuri mimi nimewahi kuwa Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri miaka kumi na tano. Mwaka 2012 TAMISEMI waliunda Tume ya kushughulikia maslahi ya Madiwani na iliongozwa na Mheshimiwa George Malima Lubeleje na ikaitwa Tume ya Lubeleje. Bahati nzuri nilifanya kazi nzuri sana pamoja na wajumbe wangu mpaka Madiwani wakakongezwa posho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini posho ile waliyoongezewa sasa ni zaidi ya miaka mitano, sita haijaongezwa. Udiwani wa zamani ilikuwa ni vikao tu, lakini Udiwani wa sasa lazima Diwani usimamie miradi. Ikianza kujengwa shule Diwani ushinde pale, ikianza kujengwa zahanati Diwani ushinde pale mpaka jioni na posho yao ni ndogo sana. Kwa hiyo, nashauri waongezewe posho ili waweze kutekeleza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Madiwani wanaitwa ni civic leaders. Kwa nini waitwe civic leaders? Maana katika uchaguzi tunakwenda mafiga matatu, Diwani, Mbunge na Rais lakini baada ya uchaguzi hawa Madiwani tunawaweka pembeni, anabaki Mbunge pamoja na Rais. Kwa nini waitwe civic leaders? Kuna Sheria ya Political Leaders Retirement Benefit, nashauri kama inawezekana sheria hii irekebishwe ili
Madiwani waingizwe katika sheria ile nao wajulikane kama ni viongozi kama sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawakuwemo kwenye sheria hiyo, walikuwa kama watumishi wa Serikali. Mwaka 1999 nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala tulirekebisha sheria sasa hivi Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wapo kwenye sheria hiyo. Kwa hiyo, kazi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni contract ya miaka mitano, akimaliza miaka mitano analipwa mafao yake, basi kama atateuliwa tena na Rais anayekuja ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimpongeze sana Waziri wa Utumishi ndiye anayesimamia TASAF na MKURABITA. Tumetembelea Mikoa kama nane kwa ajili ya kuangalia utendaji wa TASAF, wanafanya kazi nzuri sana. Kila Halmashauri ya Wilaya ina Mratibu wa TASAF, ina mratibu wa MKURABITA, hawa ndio walioandikisha kaya maskini, walijua kabisa wanaandikisha kaya maskini lakini leo nashangaa kusikia kwamba walikosea na kuna wengine kati ya walioandikishwa wana uwezo wanatakiwa warejeshe hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi najiuliza mwenye kosa ni nani kati ya aliyeandikisha na kuthibitisha kaya maskini na aliyeandikishwa? Inakuwaje leo unamwambia kwamba hapana wewe una uwezo urejeshe hizi fedha? Naomba Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na TASAF mlijadili hili suala, lakini TASAF inasaidia kaya maskini kwa sababu watu wanaboresha maisha yao, wanajenga nyumba, wanasomesha watoto na wanapeleka watoto kliniki.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu MKURABITA mradi wa kurasimisha mali, mashamba yanapimwa na wananchi wanapata hati miliki, wanakwenda kukopa benki. Zamani zile hati miliki zilikuwa hazitambuliwi na vyombo vya fedha lakini nashukuru sana Serikali imeshauri mabenki kama CRDB, NMB wamekubali wanazitambua hati miliki za kimila. Kwa hiyo, wananchi wanapata mikopo, wanajenga nyumba bora
na wanasomesha watoto. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali na nashauri MKURABITA na TASAF iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, huo ndiyo mchango wangu, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie Wizara hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Engineer Mfugale ambaye ni CEO wa TANROADs na vilevile nimpongeze Manager wa TANROAD wa Mkoa wangu kwa kazi nzuri wanazofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitazungumzia barabara moja tu; na hii barabara ni ya kutoka Mbande - Kongwa kwenda Mpwapwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Nimeanza kudai barabara hii tangu mwaka 1984. Nimekuwa Diwani miaka 15; Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Mpwapwa miaka 15, nadai barabara hii. Nimeanza Ubunge mwaka 1990 nikiwa kijana, wakati huo nachana afro; ukienda Ofisi ya Makumbusho Dar es Salaam, utakuta picha yangu pale. Sasa mpaka nafika umri huu, nadai barabara. Sasa umri wangu ni mkubwa, tangu kijana nadai barabara hii, lakini Serikali hawanionei huruma, kwa nini? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa Mbunge miaka 20; 2010 - 2015, nikaenda likizo miaka mitano; sasa nimerejea tena kwa matumaini kwamba wananchi wa Mpwapwa sasa hii barabara itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana ndugu yangu, kijana wangu, sikiliza kilio cha wananchi wa Mpwapwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpwapwa ni Wilaya ya zamani, tangu mwaka 1905. Sasa umri wake ni miaka 100. Kwa hiyo, Mpwapwa ina sifa zote za kupata barabara ya lami. Ni kilomita 50 zimebaki; Mbande - Kongwa Junction; Kongwa Junction mpaka Kongwa, kilomita tano mmeshajenga tayari, bado kilomita 50. Mbande junction ya Kongwa na junction Kongwa kwenda Mpwapwa kilomita
46. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Eng. Mfugale unanisikia, wewe ndio CEO wa TANROADs, mnisaidie ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpwapwa kuna uchumi. Hii barabara ndiyo inayounganisha Majimbo matatu; Jimbo la Mheshimiwa Simbachawene, Waziri wa TAMISEMI. Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa. Hii barabara ina umuhimu kwa uchumi na maendeleo ya Wilaya ya Mpwapwa. Hii barabara Mheshimiwa Waziri inapitisha magari zaidi ya 150 kutoka Mbande kwenda Mpwapwa; magari makubwa ya mizigo pamoja na magari madogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana ndugu yangu, leo nilitamani nilie, lakini namsamehe kwa leo, maana mtu mzima kulia siyo jambo jema. Leo itakuwa ni mara yangu ya mwisho kuomba barabara. Nitakuwa nakaa kimya tu naisikiliza Serikali yangu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpwapwa kuna taasisi zaidi ya nane; kuna taasisi ya utafiti wa Mifugo ya Kitaifa, kuna Chuo cha Mifugo Mpwapwa, Chuo cha Maafisa wa Afya na Chuo cha Ualimu Mpwapwa. Mpwapwa pia kuna mabonde mazuri sana ya kilimo; Bonde la Malolo, Lumuma, Matomondo na Bonde la Chamkoroma. Mpwapwa vile vile ina madini aina ya ruby katika Kijiji cha Uinza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, CEO Mfugale, mnisikilize kilio changu. Wananchi wa Mpwapwa wananipenda na ndiyo maana wananirejesha Bungeni. Sasa nitakuja kuwaachia kumbukumbu gani jamani ndugu zangu?
Wamenirejesha kwa matumaini kwamba safari hii Serikali yangu sikivu itasikia kilio changu, watapata barabara ya lami. Kwa hiyo, nawaomba sana ndugu zangu, viongozi wakubwa watatu; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa TAMISEMI; hivi Mheshimiwa Waziri huwezi kuwaonea huruma hata wakubwa wenzako hawa kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimesema nazungumzia hii barabara, Mheshimiwa Waziri amenisikia kilio changu, Serikali yangu ni sikivu, najua wananchi wa Mpwapwa wananisikiliza na safari hii kwa kweli nina matumaini makubwa kabisa kwa baraka za Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, namshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri na CEO Engineer Mfugale, Katibu Mkuu na Viongozi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri. Ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Waziri kwa hotuba yake nzuri na pili naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ni chombo cha Serikali na TBC inafanya kazi nzuri sana ya kuwatangazia wananchi habari mbalimbali za maendeleo na uchumi wa nchi yetu TBC Taifa, TBC1, TBC FM na TBC International wote wanafanya kazi nzuri sana. TBC Taifa inasikika vizuri katika maeneo mengi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, changamoto, wafanyakazi wa TBC waboreshewe maslahi yao kwa kuwa wanafanya kazi usiku na mchana kuwatangazia wananchi habari mbalimbali, mitambo ya TBC iboreshwe Makao Makuu Dar es Salaam na Kanda zote ikiwemo TBC Kanda ya Kati Dodoma kwa kuwa hivi karibuni matangazo ya TBC Taifa yalikuwa yanakatikakatika kila wakati na kufanya wasikilizaji kukosa habari au matangazo muhimu. TBC1 pia wakati mwingine matangazo hukatika na kutokuonyesha taarifa za habari vizuri na rangi nyeupe.

Mheshimiwa Spika, Jengo la TBC1 lililopo Mikocheni likamilishwe kwa kuwa ujenzi ulianza zamani. Je, Mheshimiwa Waziri kwa nini jengo hilo halikamiliki miaka mingi? Zitengwe fedha za kutosha kukamilisha jengo hili.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Habari kwa ujumla, kwa kuwa sekta hii ni muhimu sana kwa maendeleo na uchumi wa nchi hii na sekta ya habari ni taaluma hivyo, nashauri waandishi wa habari wawe wamesomea taaluma hiyo na waandishi wa habari ambao hawana taaluma hiyo waondolewe.

Mheshimiwa Spika, Televisheni zinazoonyesha picha chafu ambazo ni kinyume na maadili ya Watanzania, zifungiwe au wapewe onyo ili wasioneshe picha chafu kwenye Televisheni na kama wataendelea kukiuka wachukuliwe hatua za kisheria. Vile vile kila Wilaya kuwe na Afisa Habari ili kuandika na kutangaza habari za maendeleo ya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa.

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa viwanja vya michezo; kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma tunampongeza sana na kumshukuru Mheshimwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kukubali uwanja mkubwa wa michezo ujengwe mjini Dodoma Makao Makuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Ligi kuu ya Vodacom;, kwa kuwa ligi kuu ya Vodacom inaendelea na katika mechi ya timu ya Simba na Kagera Sugar iliyochezwa uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba, ilithibitika kwamba Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano kinyume kabisa na kanuni za ligi kuu. TFF ilikiri kwamba mchezaji huyo alikuwa na kadi tatu za njano lakini hata hivyo Simba walinyang’anywa points tatu kwa maelezo kwamba walikosea taratibu za rufaa. Mheshimiwa Waziri naomba maelezo kwa nini Simba walipokonywa points tatu, Serikali isimamie suala hili ili timu ya Simba wepewe haki yao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Habari, Utamaduni na Michezo. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri pamoja na mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, nianze na hili la TBC, naona wenzangu wengi wameliongelea suala hili. Bahati nzuri Spika wewe ni shahidi, nilipokuwa Mbunge kipindi cha mwanzo miaka 20 nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na Utawala na Utawala ilikuwa ni pamoja na Waziri Mkuu na TBC ilikuwa kwenye Kamati yangu, nimetembelea mitambo yote ya TBC karibu nchi nzima. Hiki ni chombo cha Serikali, kwa nini vyombo vya watu binafsi vifanye kazi nzuri, matangazo yasikike vizuri kuliko TBC?

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha lakini hatuwezi kumlaumu Dkt. Rioba - Mkurugenzi wa TBC ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kwa nini Serikali isitenge fedha za kutosha kununua mitambo ya kisasa ili TBC isikike kama redio zingine za watu binafsi? Kwa hiyo, huo ndio ushauri wangu. Wafanyakazi wa TBC wanafanya kazi usiku na mchana, waboreshewe maslahi yao na ndio maana wanahama kwenda vyombo binafsi kwa sababu ya maslahi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nizungumzie habari, habari haziko mjini tu, ziko vijijini. Ukienda Wilaya ya Mpwapwa Vijijini utapata habari, kuna watu wanafanya kazi za kujitolea vijijini. Ukienda Wilaya ya Kongwa, Zoisa, Mlali, Kibakwe, Mpwapwa kule sehemu za Mima, Matomondo watu wanafanya kazi nzuri sana ya kujitolea lakini hawatangazwi, hawa waandishi wa habari wanazunguka mjini tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kila wilaya iwe na mwandishi wa habari. Mheshimiwa Waziri ananisikiliza au anaongea na Naibu Waziri? Kila wilaya iwe na mwandishi wa habari wa Serikali ili aweze kupeleka taarifa hizi za maendeleo katika wilaya zetu lakini siyo kuandika taarifa za mjini tu, kila siku mjini, hapana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, uandishi wa habari ni taaluma na ina mipaka. Huwezi kuandika jambo lolote unalotaka wewe haiwezekani, lazima kuna mipaka yake, uandike kwa kuzingatia maslahi ya nchi yetu. Siyo unaandika kwa kujifurahisha upate fedha kama biashara, no, lazima uandike taarifa kwa kuzingatia maslahi ya nchi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni michezo. Mimi ni mpenzi wa Simba Sports Club. Kila siku timu ya Simba ikicheza lazima utasikia Lubeleje anaipongeza Simba, anaitakia ushindi. Sasa tumenyang’anywa point tatu, Bwana Malinzi sitaki kuzisema sana hizo, lakini mimi ni Hakimu, kwenye court of law ukishakiri jambo, umekiri. TFF walikiri kwamba kweli yule mchezaji wa Kagera Sugar alikuwa na kadi za njano tatu, that is plea of guilty. Huwezi kusema kwa sababu umesemasema sana, mmekosea halafu mkamnyang’anya point zake, hilo naiachia TFF. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mpwapwa nilikuwa na Timu ya Mji Mpwapwa, imecheza ligi kuu miaka tisa na ilikuwa inaogopwa na timu za Yanga na Simba. Nikubaliane na mwenzangu aliyesema Timu ya Taifa siyo lazima wachezaji watoke Simba na Yanga tu, hapana, tunaweza kupata wachezaji wazuri hata wilayani huku. Kongwa kuna Timu ya Hengo ni nzuri sana. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri

arudishe michezo shule za msingi na sekondari, UMISHUMTA na UMISETA, huko ndiko tunakopata wachezaji wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuomba dakika tano na dakika tano nimemaliza, lakini nashukuru sana Wizara hii kwa kufanya kazi nzuri, waendelee hivyo hivyo ila ombi langu kila wilaya ipate mwandishi wa habari, tuache kuweka waandishi wa habari wote mjini, hapana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza na mimi nianze kuunga mkono suala la kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji. Tatizo, Hazina hawatoi fedha zote za Miradi ya Maendeleo. Hilo ndiyo tatizo! La pili, Mji wa Mpwapwa, Mheshimiwa Waziri anaufahamu, amekaa Mkoa wa Dodoma miaka mingi akiwa Wizara ya Ujenzi. Vyanzo vya Maji vya Mji wa Mpwapwa tangu Ukoloni ni vile vile. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atume watafiti wakafanye utafiti wa vyanzo vingine vya maji ili kuongeza huduma ya maji katika Mji wa Mpwapwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni uchimbaji wa mabwawa katika vijiji. Waliahidi kuchimba mabwawa Vijiji vya Chunyu na Msagali ili kusaidia bonde la Msagali ambapo kuna kilimo cha umwagiliaji. La tatu, kuna visima vitatu vya maji vimechimbwa katika Kijiji cha Iyoma, Bumila pamoja na Mima. Tayari maji yamepatikana, lakini visima vile havijawekwa pampu, mabomba, matenki ya maji ili kusambaza maji. Naomba Wizara ya Maji na TAMISEMI wasaidiane pampu ziwekwe, maji yasambazwe ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu na watendaji wao wote wa Wizara kwa kazi nzuri sana wanayofanya. Pili, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono hoja hii, naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa misitu kwanza huhifadhi maji, makazi ya viumbe hai, misitu, ni muhimu kwa matumizi mbalimbali ya binadamu kama vile mbao, dawa, chakula, kuni, mkaa na matumizi mengine. Misitu pia hutumika kwa makazi ya binadamu kama Wahadzabe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa misitu ni muhimu sana, hata hivyo ni vyema wananchi wasifanye uharibifu wa misitu; wasifyeke misitu ovyo na kusababisha jangwa/ukame ambao huleta njaa nchini. Wananchi wasichunge mifugo yao kwenye vyanzo vya maji kwa kuwa maji ni uhai, maendeleo na uchumi wa nchi yetu; wananchi wasijenge kwenye vyanzo vya maji; wananchi wasichome misitu ovyo, kwa kuwa misitu huvuta mvua na bila mvua hakuna chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote haya, Serikali iruhusu wananchi waendelee kutumia/kupikia mkaa na kuni kwa kuwa hawana mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza watendaji wa sekta ya utalii kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Pamoja na pongezi, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sekta ya utalii inachangia Pato la Taifa wajitahidi kuhakikisha kwamba watalii wanaongezeka kila mwaka ili Pato la Taifa liongezeke kuliko hali ilivyo sasa; watalii wapate huduma bora kama vile barabara ziwe nzuri na zinazopitika wakati wote wa masika na kiangazi; kuongeza vivutio kwa watalii ili waweze kuongezeka; huduma ya usafiri iwe bora ili watalii wasisumbuke; waongoza watalii wawe na lugha nzuri na tabia nzuri/njema; na huduma ya chakula na malazi iwe bora kwa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii siyo lazima wawe wa kutoka nje ya nchi tu, hata utalii wa ndani. Ushauri wangu kwa Serikali, zijengwe hoteli za bei nafuu kwenye mbuga zetu za wanyama ili watalii wa ndani waweze kumudu gharama za malazi na chakula kwenye mbuga zetu za wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti,naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyeiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la miradi ya maendeleo. Katika bajeti ya mwaka jana, hii ambayo sasa tunamalizia mwaka wa Serikali tarehe 30 mwezi Juni, Serikali imetuahidi kwamba asilimia 40 ya bajeti yake itakwenda kwenye maendeleo. Mpaka leo hii fedha ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri ni kidogo sana, hazitoshi kabisa na kuna miradi ambayo haijatekelezwa, viporo ni vingi mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka jana Bunge tumeidhinisha fedha za miradi ya maendeleo, shilingi bilioni 791.99 lakini hadi Machi mwaka huu fedha ambayo imetumika ni shilingi bilioni 18 na miradi ni mingi katika nchi hii na katika Halmashauri zetu. Nimuulize Mheshimiwa Waziri wa fedha, hii asilimia ya fedha iliyobaki ambapo miradi haijakamilika, mtaleta lini fedha zote ili tukamilishe miradi hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Jimbo langu la Mpwapwa kuna miradi mingi ya maji ambayo haijakamilika. Kuna visima vitatu sasa ni mwaka mmoja tangu vimechimbwa, hakuna cha pump, hakuna cha bomba ambalo limewekwa. Kuna vituo vya afya viwili ambavyo vimeanza kujengwa zaidi ya miaka 10 havijakamilika ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo, naishauri Serikali, TRA wanakusanya vizuri sana mapato, niwapongeze sana TRA lakini pamoja na mapato, tudhibiti fedha za Serikali ili fedha zote ziende kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu TRA kukusanya kodi ya majengo ya Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji. Nataka kupata maelezo, hii kodi ya majengo walikuwa wanakusanya Halmashauri wenyewe kuna sababu gani za msingi ikahamishiwa TRA? TRA watakwenda mpaka kwenye grass root, mpaka chini nyumba za mbali kwenye vijiji huko kukusanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wamekusanya kwa sababu Mamlaka ya Serikali za Mitaa ilikuwa imetenga kama Halmashauri thelathini ndiyo TRA ikusanye, tupate maelezo, TRA wamekusanya kiasi gani na hizo Halmashauri zimeshapelekewa fedha kiasi gani kwa sababu Halmashauri hizi zina miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, nataka nipate maelezo kwa nini suala hili limekwenda TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu vyanzo vya mapato vya Halmashauri za Wilaya. Halmashauri za Wilaya zina hali mbaya sana, hasa mapato ya ndani kwa sababu vyanzo vingi vimechukuliwa na Serikali Kuu na fedha toka Serikali Kuu zinazopelekwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha awarudishie baadhi ya vyanzo vya mapato Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ili wakusanye wenyewe kwa sababu hali ni mbaya. Wanashindwa kuendesha Halmashauri zao kwa sababu vyanzo vingi vimepelekwa kwenye Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna madeni ya ndani, wenzangu wamezungumzia pamoja na kulipa deni la nje ambalo ni lazima tulipe kwa sababu bila kulipa huwezi kupata mkopo tena lakini haya madeni ya ndani kwa mfano wakandarasi kama wasipolipwa barabara haziendelei kutengenezwa na madeni ya ndani ni pamoja na hao wazabuni wanaohudumia kwa mfano shule. Wilayani kwangu kuna wazabuni watatu wanahudumia chakula katika shule za sekondari, Mpwapwa High School, Shule ya Maza Girls’ na Shule za Berege, wanadai zaidi ya shilingi milioni 300 hawajalipwa mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, siyo Halmashauri ya Mpwapwa tu ni maeneo mengi katika nchi hii, wazabuni hawalipwi sasa kama hawalipwi watahudumia shule hizi na wanafunzi wanatakiwa kupata chakula? Hivi leo wazabuni wanaohudumia vyakula katika shule wakigoma si shule zitafungwa? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha walipe wazabuni hawa ili waendelee kuhudumia hizi shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wastaafu, wanalalamika pamoja na kuwa wanawalipa kila mwezi, lakini fedha ni kidogo waongeze fedha, wawe wanapata angalau fedha za kutosha badala ya hii Sh.100,000/= sijui Sh.200,000/=. Nataka niwaambie hapa wengi tumeshastaafu na tunakwenda kwenye uzee na sisi wengine tumefika kwenye uzee, mtu unatoka kwa mfano Rudi, Malolo unafuata Sh.100,000/= wakati nauli tu peke yake ya kwenda na kurudi ni Sh.30,000/= unapata nini hapo? Kwa hiyo, nashauri hiki kipato cha wastaafu kiongezwe ili waweze kupata fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ila ninachoomba tu ni kwamba Serikali ijitahidi kupeleka fedha za miradi ya maendeleo katika Halmashauri otherwise miradi mingi itakwama. Sisi ni Wabunge wa kuchaguliwa na tumeahidi katika Ilani ya Uchaguzi kutekeleza miradi mbalimbali, tusipotekeleza mwaka 2020 wananchi hawaturudishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hii. Wanafanya kazi nzuri lakini katika mazingira magumu ya ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo matatu; kwanza. nitaanza na suala la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI). Taasisi hii ina vituo saba; kuna kituo cha Mpwapwa, Mabuki, Kongwa, Tanga, Naliendele na Uyole, lakini mimi nitazungumzia Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kilianzishwa mwaka 1905, sasa hivi umri wake ni zaidi ya miaka 100. Hata hivyo, Kituo hiki kinakabiliwa na changamoto nyingi sana, kituo hiki ndicho kinachohudumia wafugaji Kanda ya kati, Mikoa ya Singida na Dodoma kwa sababu wanakwenda kuchukua madume bora, wanakwenda kuchukua majike yale ambayo yana mimba kwa ajili ya kufunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 na 1993, Serikali ilipunguza watumishi, lakini bahati mbaya sana Serikali ilipunguza wahudumu wote. Kwa hiyo, hata wale wahudumu wachungaji wote waliondolewa, wakamuaji wa maziwa waliondolewa, kwa hiyo wakabaki watafiti tu. Sasa najiuliza, Mheshimiwa Waziri, kama wahudumu wote walipunguzwa kazi na kituo kile kina ng’ombe zaidi ya 800, kina Mbuzi zaidi ya 400, ni nani atakaechunga? Au watafiti watapanga zamu ya kuchunga na kwenda kukamua? Wasomi wenye degree mbili, degree tatu; kwa hiyo wapange ratiba nani leo aende akachunge, nani leo aende akakamue, ni kitu ambacho hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapoamua mambo mengine kwa kweli wawe wanafikiria, wanaangalia uzito wa jambo. Sasa unapoondoa wahudumu; na namshukuru sana Mkurugenzi wa Taasisi, aliajiri vibarua 90, akawapanga wengine wanachunga, wengine ndiyo wanakumua na wengine wanafanya bush clearing yaani kusafisha mashamba yale ambayo mifugo wanachungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Hawa vibarua wameanza kazi tangu mwaka 2015 mpaka leo hawajalipwa mishahara yao; wana familia, wanasomesha. Kwa hiyo naomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, hawa vibarua wanafanya kazi nzuri, kwa sababu kama Mkurugenzi asingeajiri vibarua hii kazi ya uchungaji, ukamuaji ni nani angefanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna changamoto zingine; kuna upungufu wa magari, matrekta pamoja na pikipiki kwa ajili ya wale Extension Officers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuhusu kuhamisha kituo cha uchunguzi wa magonjwa ya mifugo na kukileta Dodoma. Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri sana; Mawaziri wote wa mifugo waliopita akiwemo Mheshimiwa Rais Magufuli aliwahi kuwa Waziri wa Mifugo alikataa ile Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa isihamishiwe Dodoma. Sasa walipoona Mheshimiwa Lubeleje mwaka 2010, 2015 amepata likizo siyo Mbunge wakaihamishia haraka haraka Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Dodoma hakuna majengo ya Maabara. Pale Mpwapwa kuna jengo zuri, mwaka juzi wamejenga jengo zuri sana la Maabara, kwa hiyo wamehama vifaa vingine wamekuja navyo Dodoma, vingine wamefungia kwenye stoo pale Mpwapwa; yale majengo Mpwapwa yanaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na sababu gani ya kuhamisha kile kituo? Kwa sababu waliojenga kituo cha utafiti wa mifugo Mpwapwa ndio waliojenga Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa kwa sababu vinakwenda pamoja. Ng’ombe akiugua kwenye Taasisi ya utafiti analetwa pale VIC kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa wanamchunguza ana tatizo gani, lakini baadaye wamejenga chuo cha Maafisa wa Mifugo kwenye Chuo cha Mifugo ili practicals wawe wanachukua pale VIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale chuo cha mifugo wanasoma theory lakini practicals walikuwa wanafanya hapa Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa, maana hawa ni wataalam wa mifugo; wanasoma anatomy physiology, animal deseases pamoja na meat inspection; sasa practicals lazima wakafanyie pale Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa hata meat inspection, maana wale wanajifunza ant-mortem inspection na post-mortem, sasa practicals lazima wakafanyie kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapochukua yule ng’ombe wanaanza kumchunguza ana tatizo gani, amekufa kwa ugonjwa gani. Kuna vidudu vingine vya magonjwa ya mifugo vinaonekana kama liver flukes, Cysticercus bovis vinaonekana, vile vile kama anthracis bacillus na Tubercle bacilli mpaka utumie darubini kali. Sasa ninyi wanahamisha kituo kile wanaleta Dodoma, hao wanafunzi wawe wanatoka Mpwapwa wanakuja kujifunza Dodoma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri arudishe kituo kile haraka sana Mpwapwa la sivyo leo nashika shilingi. Kuna mtaalam mmoja pale ndiye aliyelazimisha kituo kihame, akasema Lubeleje ndiye Mbunge ambaye anazuia sasa ameondoka na bahati mbaya amestaafu, ndiye amelazimisha kituo kuhamia hapa. Sasa Waziri anieleze ametenga fedha kiasi gani, wanafunzi watoke Mpwapwa kuja kuchukua practicals huku Dodoma? Kwa hiyo, naomba anieleze Mheshimiwa Waziri mpango wa kuhamisha kituo hiki kirudi Mpwapwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni upungufu wa chakula katika Mkoa wa Dodoma Wilaya ya Mpwapwa na Mkoa wa Dodoma. Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya Serikali hapa Bungeni kwamba kuna Halmashauri 55 zina upungufu wa chakula, alikiri mwenyewe hapa na alisema kwenye maghala yetu ya hifadhi kuna chakula cha kutosha lakini nashangaa hawakugawa hata gunia moja kwenye vijiji ambavyo vimeathirika na chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tunasema majimbo yetu yana njaa, yana upungufu wa chakula tunaomba watusikilize. Sasa kama chakula kiko kwenye maghala na hapa tunapitisha, mwaka wa jana tumepitisha bajeti bilioni 18, zimetolewa bilioni tisa, hizo bilioni tisa ndizo zimenunua chakula kwahiyo kama chakula kidogo kipo, basi wasambaze kwa maeneo ambayo hakuna chakula ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Mpwapwa na Mkoa wa Dodoma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba wagawe hicho chakula ili wananchi wasiweze kununua debe la mahindi kwa Sh.25,000/= na gunia la mahindi kwa Sh.120,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niunge mkono tu haya yote ambayo yamezungumzwa. Mipango ni mizuri sana, tunapanga vizuri sana lakini tatizo letu kubwa ni utekelezaji na utekelezaji umezorota kwa sababu fedha haziendi Mikoani, fedha haziendi Wilayani. TRA wanajitahidi sana kukusanya mapato, wanakusanya sana, lakini fedha haziendi kwenye Halmashauri, haziendi Mikoani; miradi mingi imekwama na tunategemea sana wafadhili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani wakati umefika sasa wa kupunguza hii misaada, kwa sababu tukitegemea sana wafadhili ipo siku wafadhili watasema sasa sisi tunajiondoa, Kwa hiyo, tujitahidi sana kutumia fedha zetu za ndani. Miradi mingi imekwama, kwa mfano katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna barabara hii ya kutoka Mbande, kwenda Kongwa mpaka Mpwapwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwamba ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami umeshaanza tayari, lakini bado wapo kipande cha Mbande hawajafika hata njia panda ya Kongwa.

Kwa hiyo, mimi ni mategemeo yangu kwamba wananchi wa Jimbo la Mpwapwa wategemee kwamba barabara hii itakamilika kwa wakati, kuanzia Mbande - Kongwa mpaka Mpwapwa kwa kiwango cha lami, naisubiri kwa hamu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu misamaha ya kodi. Ni kweli kisheria inaruhusu kwamba baadhi ya wafanyabiashara wasamehewe kodi, lakini hii inatupotezea mapato mengi sana. Ninaishauri Serikali kwamba ipunguze misamaha ili fedha nyingi zikusanywe ziende katika miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji wa kodi ya majengo kwenye Halmashauri zetu. Tulishaishauri Serikali kwamba utaratibu huu kwa kweli ni mgumu sana. Halmashauri nyingi zilikuwa zinakusanya kodi ya majengo vizuri sana, hii property tax.

Kuna Halmashauri ambazo zinaweza zisitegemee hata ruzuku ya Serikali kwa kutegemea mapato yao ya ndani (own source). Kwa mfano Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam walikuwa wanajitahidi sana kukusanya property tax, lakini baadaye Serikali ikaamua kwamba inakusanya yenyewe. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba taarifa, ni kiasi gani kimeshakusanywa na kiasi gani kimesharudishwa kwenye hizi halmashauri zetu. Tulikwishakataa jambo hili; tuachie halmashauri zenyewe zikusanye kwa sababu property tax ni chanzo kimoja wapo cha mapato ya ndani kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maghala yetu ya hifadhi ya chakula cha msaada. Kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa maghala na Serikali imenunua chakula kingi sana cha akiba, lakini jambo la kushangaza ukame unaendelea katika nchi yetu chakula hawagawi, njaa inaendelea hasa katika Jimbo langu la Mpwapwa na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla. Hali ni mbaya sana. Watu hawana chakula, sasa hivi wameanza kuandaa mashamba yao lakini hakuna chakula; kwa nini Serikali isianze kugawa chakula cha msaada?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatusemi kwamba kuna njaa maana Serikali inazuia neno la njaa, inasema upungufu wa chakula, lakini mimi nadhani upungufu wa chakula na njaa ni neno lilelile tu. Kwa hiyo, hakuna haja ya kuhifadhi chakula kwenye maghala na chakula kinaharibika. Serikali ianze kugawa chakula maeneo yote ambayo yana upungufu wa chakula au yana njaa, chakula kitaharibika kwenye maghala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Ujenzi wa Vituo vya Afya Jimbo la Mpwapwa. Ninashukuru sana Kituo cha Afya Mima kimepata shilingi milioni mia tano safari hii, lakini bado Kituo cha Afya cha Mbori hakijakamilika. Ninaomba sana fedha itolewe, vituo vikamilike ili huduma iweze kutolewa kwa maeneo yale. Vituo vya afya vinasaidia sana hasa wale akina mama wajawazito badala ya kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa wanahudumiwa kwenye vituo vya afya kwa sababu pale kuna Assistant Medical Officer au Clinical Officer ambao wale ni trained au wale madaktari wasaidizi wanakuwepo kwenye vituo vya afya kwa ajili ya operation ndogo ndogo. Kama akina mama wanashindwa kujifungua basi wanafanyiwa operation ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ya kwangu yalikuwa ni hayo; nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono asilimia mia moja hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, lakini tukusanye fedha na tutekeleze miradi. Fedha ipelekwe halmashauri na mikoani. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, na nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kunipa hizi dakika tano. (Makofi)

Kwanza kabisa nizungumzie REA. REA awamu ya kwanza, REA awamu ya pili usimamizi wake haukua mzuri ndiyo maana miradi mingi ilikwama. Kwa mfano kuna vijiji vya Tambi, Nambori, kijiji cha Saa Zima, kijiji cha Igoji Moja na Igoji Mbili, tayari nguzo zipo na nyaya zipo lakini transformer hakuna. Kwa hiyo nilikuwa naomba sana katika REA hii ya awamu ya tatu waweke transformer ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuna vijiji ambavyo havijafikiriwa kabisa kupata umeme. Kijiji cha Kiboriani, Ngaramilo, Mkanana, Chamanda pamoja na Iwondo hazijapelekwa nguzo wala nyaya. Kwa hiyo naomba sana hii REA awamu ya tatu wawakumbuke basi wapate umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, kukatika katika kwa umeme Mji wa Mpwapwa na maeneo mengine imekuwa ni kero kubwa sana, kila wakati kwa siku umeme unaweza kukatika mara mbili/tatu. Sasa kwanza unaweza kupata hasara ukaunguza vitu kwenye fridge, lakini pili kwa sababu wananchi wanalipa bill kwa hiyo lazima huduma ya umeme iwe nzuri. Sasa kisingizio cha TANESCO kwamba kwa sababu ya mvua na kuna baadhi ya nguzo zipo kwenye mabwawa, nguzo zingine zimeoza.

Mimi nashauri wabadilishe nguzo zote zile ambazo zimeoza. Kama inawezekana nguzo ziwekwe za chuma ambazo haziwezi kuoza, haziwezi kuliwa na mchwa hii inaweza kusaidia sana ili wananchi waweze kupata huduma ya umeme Wilaya ya Mpwapwa na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla. Kwa hiyo ya kwangu yalikuwa ni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja hii ya Kamati hizi mbili. Kwanza nizipongeze sana hizi Kamati mbili kwa kazi nzuri wanazozifanya lakini tatizo lipo, hawapewi fedha za kwenda kukagua miradi, wanakagua makaratasi tu. Sasa bila kwenda kuona miradi ile value for money kwa kweli inakuwa ni kazi bure tu. Unaweza kukuta shule imejengwa lakini kama haikukaguliwa madirisha mabovu, kuna nyufa na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuchelewa kwa fedha za miradi ya maendeleo. Bunge kama Bunge sisi ndio tunaopitisha bajeti hapa. Bajeti za Halmashauri za Wilaya pamoja na bajeti ya Serikali Kuu, lakini jambo la kusikitisha fedha hazifiki kwa wakati. Hakuna Halmashauri hata moja hapa ambayo imeshapata fedha za ruzuku zaidi ya asilimia 40 hakuna. Sasa nauliza huko Hazina kuna nini, kama TRA wanakusanya kila mwezi hela za kutosha kwa nini fedha hizi zisipelekwe Wilayani. (Makofi)

Mheshiniwa Mwenyekiti, miradi ya maji kuchelewa, nina masikitiko makubwa sana kuna visima sita vimechimbwa Wilaya ya Mpwapwa tangu Agosti, 2016, lakini mpaka leo hakuna pump, hakuna bomba wala hakuna nini. Kwa hiyo, visima vile vimechimbwa vimekuwa kama ni white elephant wananchi wanaangalia tu. Sasa namshukuru sana Waziri wa TAMISEMI, MheshimiwaJafo anajitahidi sana kutembelea miradi hii, tulifika naye Kijiji cha Mima akaona huu mradi maji, akaona ujenzi wa kituo cha afya kinavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mawaziri mtembelee miradi hii, bila kutembelea ndugu zangu, msikae maofisini mkadhani kwamba miradi inakwenda vizuri, kumbe miradi imekwama. Hata hivyo, awamu hii niwapongeze Mawaziri wanajitahidi kutembelea miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri nyingi zilikuwa zinapata hati chafu, lakini baada ya kuunda hii Kamati ya LAAC imefanya kazi nzuri sana, sasa hivi ukifanya utafiti ni Halmashauri chache tu wanapata hati chafu, kwa hiyo, niwashukururu sana lakini kama nilivyosema wapewe fedha kwa ajili ya kwenda kuona ile miradi value for money sio kukagua makaratasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kodi ya majengo bado tunasistiza sisi Wabunge kodi ya majengo irudishwe kwenye halmashauri zenyewe sasa kodi ya majengo (property tax) wanakusanya TRA ni kweli wanakusanya lakini wanakusanya mwaka mzima ndiyo waanze kugawa kwenye Halmashauri miradi hiyo si imekwama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri zilikuwa zinakusanya property tax kila quarterly wanaanza kutumia zile fedha. Kwa hiyo, nashauri kwamba kwa sababu ni chanzo kimojawapo cha mapato ya halmashauri kwa sababu halmashauri nyingi hazina vyanzo vya mapato kwa hiyo kodi ya majengo ndio kilikuwa chanzo kimojawapo. Kwa hiyo, ombi langu chanzo hiki cha mapato kirudishwe Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi kukaimu muda mrefu katika Halmashauri; ni kweli wanakaimu muda mrefu sana. Ukienda kila Halmashauri ukimuliza huyu, mimi ni Afisa Elimu Kaimu, mimi ni Mhandisi wa Maji Kaimu, mimi sijui nani Kaimu. Sasa nashauri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kama hawa watu wana ujuzi wa kutosha wana-qualification za kupandishwa vyeo kwa nini wasithibitishwe kushika nafasi hizo. Waendelee kukaimu miaka miwili, miaka mitatu hapana. Kwa hiyo, wasikaimu muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya Madiwani na Watendaji wa Halmashauri; bahati nzuri nilikuwa Diwani, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge nimejifunza mambo mengi sana. Sisi ndiyo tumeanzisha Halmashauri ya Wilaya mwaka 1984, kulikuwa na matatizo makubwa sana, lakini sasa yanaanza kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, semina au mafunzo kwa Madiwani ni muhimu. Sisi tulikuwa tunakwenda mafunzo Hombolo tunapewa mafunzo ili kupunguza migogoro kati ya Watendaji na Madiwani. Utakuta Madiwani wanamkataa Mkurugenzi inawezekana hakuna sababu zozote za msingi au Madiwani kuingilia utendaji, hilo nalo ni tatizo, lakini Madiwani wakipewa mafunzo nina hakika kabisa hii migogoro itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naunga mkono hoja hizi zote mbili za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Azimio hili ambalo ni muhimu sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, niipongeze Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa taarifa yao nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu miaka ya 1960 haikuwa hivi, ilikuwa nchi nzuri sana, ilikuwa na misitu mikubwa na mito ambayo inatiririsha maji mwaka mzima. Kwa sababu ya shughuli za kibinadamu watu wamefyeka miti, wamechoma moto hovyo na mifugo isiyozingatia maeneo ya malisho sasa hivi misitu mingi sana katika maeneo yetu imekwisha. Misitu ndiyo inayoleta mvua na hali ya hewa nzuri na mito ndiyo inayoleta maji.

Maji ni uhai, maji ni maendeleo na maji ni uchumi wa nchi yetu. Lakini vyote hivi uharibifu huu wa ufyekaji, uchomaji moto hovyo ndiyo umesababisha majangwa, umesababisha ukame katika nchi hii kama Kamati ilivyoelezea ukame, milipuko ya magonjwa, viwanda, kemikali hizi, maji machafu yanamwagwa hovyo, madawa, makemikali yanasababisha watu wanapata magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi takataka zinachomwa hovyo hata mijini utakuta mtu anachoma takataka sasa zile takataka zinatoa moshi, ule moshi unaharibu hali ya hewa badala ya watu kuvuta oxygen wanavuta carbonmonoxide, kwa hiyo ile ni pollution of air by combustion ambayo inaleta matatizo makubwa sana sana kwa Wananchi wetu wanapata matatizo ya magonjwa ya kifua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hali ya hewa inabadilika kunakuwa na joto kwa sababu ya mabadiliko hayo mpaka wakati fulani unakuta hata bahari maji nayo yanaongezeka. Kwa hiyo, wito wangu kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wazingatie kutunza mazingira, bila kutunza mazingira nchi hii ndugu zangu tutakwenda wapi? Maji yatakwisha na bila maji dunia hii tutaishi wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuiweka Wilaya Mpwapwa, naomba nisome kidogo; “Mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya vijijini, Mfumo wa ikolojia na lengo la mradi huu ni kuongezea vijiji uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi” na Mpwapwa imo. Mpwapwa ilikuwa na misitu mikubwa sana, kulikuwa na Mto Shaban Robert wote mnaufahamu mmesoma kwenye vitabu, Shaban Robert. Ulikuwa unatiririsha maji mwaka mazima, sasa hivi uko wapi? Hakuna, umekauka kwa sababu watu wamechoma, watu wamefyeka hovyo mpaka sasa hakuna na kuna baadhi ya vijiji kuna ukame umeanza, barabara zinaharibika kwa sababu watu wamechoma, watu wamefyeka hovyo kwa hiyo, maji yanakuja kwa kasi yanaharibu barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana kabisa na Mheshimiwa Waziri kwamba azimio hili naliomba Bunge wote tukubaliane liweze kupita bila kupingwa na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ya Kamati hizi mbili. Kwanza niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati na Kamati kwa kazi nzuri sana wanayofanya kwa sababu kama Kamati ya Maendeleo ya Jamii majukumu yao ni mengi na sekta zao ni nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la sekta ya afya. Sekta ya afya ina changamoto nyingi sana, sasa hivi wananchi wanajenga zahanati na vituo vya afya. Sasa unavyosema jengo la zahanati, kituo cha afya au hospitali ya Wilaya siyo jengo tu, ni dawa pamoja na watumishi. Hata hivyo, pamoja na kwamba katika bajeti hii tumetenga shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kununua dawa, vifaa tiba pamoja na vitendanishi lakini bado kuna upungufu mkubwa sana wa dawa katika hospitali zetu za wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atembelee Hospitali za Mikoa, Wilaya na Vituo vya Afya hasa vijijini ndiyo kabisa maana linakwenda sanduku moja, idadi ya watu ni 2,000 mpaka 3,000, dawa hazitoshi. Naomba viongozi wetu wa Wizara ya Afya mnapotamka kwamba hakuna upungufu wa dawa kabisa, hospitali zetu zote zina dawa za kutosha, hapana, upo upungufu mkubwa sana wa dawa. Pamoja na hii bajeti kuongezwa, lakini tujitahidi kuongeza fedha za kutosha tununue dawa za kutosha ili wananchi wetu wapate huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo hii unakwenda katika hospitali, mganga anamwandikia mgonjwa dawa anakwenda kununua duka la mtu binafsi, bado wapo na haipendezi kabisa. Tulishauri kwamba MSD wajenge maduka katika baadhi ya Hospitali za Wilaya ili dawa zinazokosekana kwenye pharmacy ya hospitali basi zipatikane pale. Kwa sababu bei ya dawa katika maduka ya watu binafsi ni kubwa zaidi kuliko haya maduka yetu ya MSD. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni sekta ya elimu. Wizara ya Elimu imeanzisha kidato cha tano na cha sita katika baadhi ya shule kwenye wilaya zetu. Hata hivyo, kuna changamoto kubwa sana ya mabweni, mabwalo, na chakula. Hizi shule zimeanzishwa form five na six lakini wameachiwa wananchi ndiyo wanaojenga. Siyo vibaya wananchi wakajenga madarasa, mabwalo na hosteli lakini tunaomba Serikali isaidie vifaa vya kukamilisha majengo haya, ni shida sana, vijana wanasoma katika mazingira magumu. Maana form five na six vijana wale hawatoki mazingira ya pale pale bali Mikoa yote ya Tanzania. Kwa mfano, tuna Shule ya Sekondari ya Wasichana Mazae, mazingira yake ni magumu sana. Tumejenga hosteli na mimi Mbunge nilitoa mifuko 200 kwa ajili ya kujenga hosteli, lakini mazingira ni magumu. Kwa hiyo, naomba Serikali isaidie vifaa vya kukamilisha majengo yale. Wananchi tunawahamasisha, wako tayari wanajenga lakini vifaa vya kukamilisha majengo hayo hatuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya chakula ni kidogo sana. Mwanafunzi mmoja anapata hela ya chakula kwa siku shilingi 1,500 kwa asubuhi, mchana na jioni kwa hizi shule za bweni. Hivi kweli unaweza kula breakfast, lunch na dinner kwa shilingi 1,500? Haiwezekani. Kwa hiyo, naomba waongeze fedha za chakula kwa siku angalau iwe shilingi 2,500, hii inaweza kuwatosha wanafunzi lakini siyo shilingi 1,500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kwa kuwa Halmashauri zetu za Wilaya zina shule za msingi pamoja na sekondari kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne, naomba Wizara ya Elimu mngewapokea form five na six muwapunguzie majukumu Serikali za Mitaa maana wana majukumu kweli. Toka elimu ya msingi, darara la kwanza mpaka darasa la kumi na mbili halafu mnaongezea tena kitado cha tano na kidato cha sita, yote Halmashauri ya Wilaya. Nashauri form five na six Wizara ya Elimu yenyewe ishughulikie hizi shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine ni kuhusu suala la UKIMWI. Ushauri wangu ni kwamba Serikali inatenga fedha nyingi sana na wafadhili wanaleta fedha nyingi sana kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI na fedha hizi zinapelekwa katika Halmashauri zetu za Wilaya lakini zisimamiwe basi ziwahudumie waathirika wa UKIMWI wenyewe. Sasa hivi wananchi wanaelewa UKIMWI ni nini lakini fedha nyingi sana zinakwenda kwenye semina makongamano wale waathirika kabisa wa UKIMWI hawafaidiki. Kwa hiyo, nashauri wale waratibu wa UKIMWI kwa kila Halmashauri wakipata hizi fedha wahakikishe walengwa ndiyo wanafaidika na hizi fedha, siyo kuanzisha semina na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi lakini la pili nipongeze sana hizi Kamati mbili kwa kazi na taarifa nzuri sana. Naunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja hizi mbili. Kwanza niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, niwapongeze Watendaji wote wa Wizara hizi mbili kwa kazi nzuri. Nchi hii ina utawala bora, ndiyo maana tumetulia, ndiyo maana tuko hapa Bungeni tunafanya vikao bila wasiwasi nchi imetulia na good governance ni kwa sababu ya political stability. Kwa hiyo, nataka kukuhakikishia kwamba ni Vyombo vya Usalama ndiyo vinafanya kazi nzuri, ndiyo maana tunatembea hata saa nane za usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni mapato ya Halmashauri. Sifa ya Halmashauri yoyote ile ni mapato, kukusanya mapato ya ndani, kama Halmashauri haikusanyi mapato ya ndani haina sifa ya kuitwa Halmashauri ya Wilaya. Kwa hiyo, wakati wa Kamati tuliwaeleza Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi Watendaji wajitahidi kukusanya mapato ya ndani wasitegemee zaidi ruzuku maana ipo siku moja Serikali ikisema kwamba ruzuku tunafuta, Halmashauri zitashindwa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niongelee suala la migogoro katika Halmashauri. Bahati nzuri mimi nimekuwa Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri miaka 15, kuna migogoro mingine inasababishwa na Wakurugenzi, Diwani ni haki yake kulipwa posho kila mwezi, lakini Madiwani wanakaa miezi miwili, mitatu, minne bila kulipwa posho hapo mgogoro lazima utakuwepo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mwingine ni kutokufahamu majukumu ya Madiwani. Tuliokuwa Madiwani zamani tulipelekwa Hombolo kwa ajili ya mafunzo ya mwezi mmoja, lakini hawa Madiwani wa siku hizi hawapelekwi na hivyo hawajui mipaka yao; mipaka ya Watendaji na mipaka ya Madiwani. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, muwapeleke mafunzo angalau wiki mbili hawa Madiwani waweze kujua mipaka yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni posho za Madiwani. Posho za Madiwani wanazolipwa, mwaka 2002 wakati Mheshimiwa Mizengo Pinda akiwa Waziri wa TAMISEMI aliunda Tume ya kushughulikia maslahi ya Madiwani na Tume ile iliongozwa na mimi mwenyewe na ikaitwa Tume ya Lubeleje. Kwa hiyo, mpaka leo wanapata kiwango kilekile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri majukumu ya Madiwani wa zamani na sasa ni tofauti. Zamani Madiwani ukiamka asubuhi unakwenda kwenye kikao ukitoka kwenye kikao unarudi nyumbani unapumuzika. Siku hizi mradi ukianza wa shule mradi wa zahanati lazima Diwani ushinde pale. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ajitahidi sana angalau wawaangalie waongeze posho kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo lingine baada ya kuongezwa hii posho kidogo, Madiwani walikopa benki, wengi walikopa CRDB, walikopa NMB, sasa bahati mbaya sana kuna Wakurugenzi hawakati zile fedha na kupeleka kwenye haya mabenki. Kwa hiyo, mgogoro mkubwa sana, vyombo vya fedha NMB na CRDB wanaanza kuwafuata Madiwani kwamba ninyi ndiyo mliokopa lakini mishahara yao imeshapelekwa Halmashauri, hawalipwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu mishahara ya watumishi, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, wakati umefika ndugu zangu tuangalie watumishi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, maisha na gharama zinapanda kila kukicha. Sasa ufinyu wa bajeti sidhani na sitegemei kuna mwaka mmoja Serikali hii itasema sasa tuna fedha za kutosha, hakuna! Kwa hiyo, tuwafikirie Watumishi wanafanya kazi ngumu sana, sifa ya Tanzania wanaleta watumishi kwa kufanya kazi nzuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kucheleweshwa kwa fedha za miradi ya maendeleo. Sasa Mheshimiwa mmoja amesema kwamba sisi ambao tunahudhuria vikao kwenye Halmashauri tusilalamike. Hii ni ruzuku ya Serikali Kuu na sheria inatamka kwamba Serikali Kuu ni lazima isaidie Halmashauri itoe ruzuku. Wabunge tunakaa hapa miezi mitatu kupitisha bajeti ya Serikali, lakini bahati mbaya sana fedha ambazo zinaidhinishwa hapa hazifiki zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wakati tunachambua bajeti ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa wengi mpaka hadi Februari, 2018 fedha ambazo wamepokea ni kati ya asilimia 51, 48, 60 lakini fedha nyingine hazifiki kwenye miradi. Kwa hiyo, ukitembelea Halmashauri nyingi kuna viporo vingi sana zahanati hazikamilishwi, vituo vya afya havikamilishwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kuniletea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Mima. Kazi inakwenda vizuri bado kuna Kituo cha Afya cha Mbori ambacho ujenzi wake bado kabisa na kile kituo kikishakamilika kitahudumia Kata Nne; Kata ya Kimagai, Kata ya Lupeta, Kata ya Matomondo na Kata ya Mlembule. Kwa hiyo, naomba milioni 500 zipelekwe tena Mbori kwa ajili ya kukamilisha kituo kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nimalizie, ni suala la upungufu wa watumishi. Serikali inasema ombeni vibali, Wilaya ya Mpwapwa tuna upungufu wa Watumishi wa huduma Idala ya Afya zaidi ya 150, tumeleta juzi kuomba kibali watumishi 150, tumepewa watumishi sita tu. Kuna Kada zingine zile ambazo ni ndogondogo mziachie Halmashauri ziajiri badala ya kuomba kibali Utumishi ndiyo tuwaajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Niwapongeze sana Mawaziri na Watendaji wao wanafanya kazi nzuri, ila wajitahidi sana kutembelea Majimbo yetu kwa sababu ukitembea kwenye Majimbo ndiyo unaona changamoto za kila Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie hii Wizara ya Afya.

Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu na watendaji wote wa Wizara ya Afya. Naipongeza Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, madaktari na wauguzi wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya ina kurugenzi kubwa mbili; kwanza Kurugenzi ya Tiba na Kurugenzi ya Kinga. Mimi niongelee kwanza Kurugenzi ya Tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati, vituo vya afya na hospitali, ili iitwe hospitali ni dawa pamoja na watumishi. Naipongeza sana Serikali kwa kujitahidi kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua dawa. Naipongeza MSD kwa kununua dawa za kutosha na kununua magari ya kusambaza dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya, hii fedha ya kununua dawa bado haitoshi. Tuendelee kuongeza hela ya kununua dawa. Hii ni kwa sababu kama alivyosema Mwenyekiti, hizi dawa kweli zinasambazwa lakini kuna baadhi ya zahanati dawa hazifiki, sasa hii inakuwa ni shida. Kwa hiyo, MSD mna Kanda, hakikisheni Mameneja wenu wanatembelea kwenye zahanati na vituo vya afya wanakagua kama kweli dawa hizi zinawafikia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa watumishi, kama nilivyosema Wizara ya Afya ilikuwa na mpango wa kuongeza Vyuo vya Clinical Officers na Clinical Assistants. Sasa kwa nini upungufu wa watumishi unaendelea? Kwa mfano, pale Mpwapwa kuna Chuo cha Afya, lakini vyuo kama vile wanaweza kupanua wakaongeza Clinical Officers wakachanganya pale Maafisa Afya, wanasoma na tunaongeza idadi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati nyingi sana Wahudumu wa Afya ndio wanaofanya kazi (Medical Auxiliaries) ndio wanaofanya kazi nzuri sana, lakini bahati mbaya sana unakuta zahanati moja ina mtumishi mmoja tu, Medical Auxiliary; hakuna Clinical Officer wala Clinical Assistant. Huyo ndio achome sindano, a-prescribe dawa na agawe dawa.

Naomba sana Wizara ya Afya itengewe fedha za kutosha ili waweze kuajiri watumishi wengi, kila zahanati iwe na Clinical Officer na Clinical Assistant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie Idara ya Afya Kinga na nizungumzie Maafisa wa Afya kuhamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais. Afisa wa Afya is a professional na wamesomea. Mimi mwenyewe ni Retired Health Officer. Wamesomea miaka mitatu mambo ya afya. Sasa tatizo linakuja wanahamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa sababu ya lile neno tu la environmental basi; lakini hawa wamesoma mambo ya Public Health and Preventive Medicine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri, ukitembelea nchi nyingine kwa mfano Kenya, Uganda, Malawi na Namibia, Idara ya Afya Kinga ni idara kamili na ina vote yake kabisa, yaani Maafisa Afya wana idara yao kamili na Wakurugenzi wao, lakini hapa sasa tunaanza kuwagawa Maafisa Afya, wengine waende Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwa hiyo, nakushauri Mheshimiwa Waziri, Maafisa Afya wote warudi Wizara ya Afya ili waweze kuimarisha kitengo hiki cha Idara ya Afya Kinga. Hawa ndio wanaoshughulika na usafi, kukagua mambo ya nyama, mahoteli na hizi food premises, lakini sasa ukiwapeleka kule, anaitwa Afisa Mazingira, haitwi tena Afisa Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vyuo nadhani mngevibadilisha majina. Sisi wakati tunasoma kilikuwa kinaitwa Chuo cha Maafisa wa Afya, lakini sasa mkishasema Chuo cha Afya ya Mazingira, Afisa Afya amesoma mambo mengi sana. Syllabus ya sasa wanasoma kama madaktari. Wanasoma mambo ya minyoo na mambo mengi sana; mambo ya preventing. Ukimuuliza Afisa Afya, kwanza ndio wanaokagua nyama (meat inspectors) wanajua ante- mortem inspection wanajua post-mortem. Unaweza ukachinja hapa ukatundika carcass ukimwambia Bwana Afya akague anakagua na anakwambia kabisa hawa ni taenia solium, hawa ni taenia saginata, wanakwambia. Ni wataalam wa haya magonjwa. Sasa kuwahamishia Ofisi ya Makamu wa Rais, it is wrong. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maafisa Afya wote warudi na muanzishe kada ya Health Assistant au Assistant Health Officer kama zamani, kwa sababu hawa Maafisa Afya, wale wenye Diploma wengi wapo katika Wilaya lakini Health Assistant wanatakiwa wakae kwenye Zahanati. Kila Zahanati iwe na Health Assistant. Kazi yao kubwa ni elimu ya afya (Health Education), kuelimisha wananchi kuzungukia vijiji kuhusu usafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Muhimbili zamani tulikuwa na kituo chetu cha Health Education Unit, wapo Maafisa Afya kwa ajili ya elimu ya afya. Hata hospitali zetu zote hizi tulikuwa tunatoa elimu ya afya kwa wagonjwa (out- patient na in-patient) lakini siku hizi sijui kama linafanyika hili. Kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba. Kinga is less expensive lakini tiba ni very expensive. Mtu akiugua kipindupindu, gharama ya kumtibu ni ngumu, lakini ukimwambia mtu achimbe choo, achemshe maji ya kunywa na atunze usafi, umezuia ule ugonjwa. Kwa hiyo, kidogo inakuwa ni gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo machache. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, lakini waongeze bidii ya kutenga fedha kwa ajili ya kununua madawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Hospitali yangu ya Mpwapwa iongezewe madawa na watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Waziri, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa. Nashukuru kwamba Mbande - Kongwa imeshaanza kujengwa, wasiwasi wangu tukisubiri barabara hii ikamilike kuanzia Mbande - Kongwa junction ndiyo waanze kujenga barabara ya Mpwapwa kwa kweli itachukua miaka 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba barabara hii ianzie kujengwa Mpwapwa kuja huku Kongwa, nadhani hii itakuwa rahisi zaidi. Mwaka jana nilisema sana, nadhani Wizara hii ni sikivu, wamenisikia, mwaka huu watanisaidia. Wananchi wa Mpwapwa wameikosea nini Serikali ya CCM? Tangu nimeingia Bungeni mwaka 1990 kila hoja naiunga mkono, sijapinga hoja yoyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Mstaafu Mheshimiwa Mwinyi aliniahidi haikujengwa, Rais Mstaafu Mheshimiwa Mkapa aliniahidi haikujengwa, Rais Mstaafu Mheshimiwa Kikwete aliniahidi haikujengwa na Rais Magufuli ameniahidi. Kwa hiyo, nina hakika kabisa Profesa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi mwaka huu asikilize kilio za wananchi wa Mpwapwa. Namwomba sana kwa unyenyekevu kabisa wanisikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimeona hapa Mheshimiwa Waziri starting construction Gulwe brigde. Daraja la Gulwe linajengwa sasa sijui linajengwa daraja lipi lingine? Daraja ambalo limebomoka kwa kuchukuliwa na mafuriko ni daraja la Godegode. Sasa hivi wananchi wanapata shida sana, wanavushwa kwa Sh.2000 kama ni pikipiki Sh.5000. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hii ni dharura wajenge daraja hilo ambalo ni kiungo kati ya Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa. Kwa hiyo, na,womba sana Mheshimiwa Waziri ashughulikie daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba barabara ya kutoka Gulwe – Berege – Chitemo - Mima mpaka Seruka ichukuliwe na Serikali. Kwa sababu wakati huo ilikuwa chini ya halmashauri wakasema hapana kwa kuwa tumeanzisha chombo TARURA, itajenga ile barabara. Ombi langu ni

kwamba TARURA wasigawane fedha na TANROAD, TARURA itengewe fedha zake za kutosha hizi za TANROAD ziachwe ili TANROAD ijenge barabara ya lami ya Mpwapwa – Mbande - Kongwa na barabara zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa asilimia mia hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie Wizara hii.

Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kufanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni Vyombo vya Habari. Vyombo vya Habari ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi hii na uchumi wa nchi hii. Serikali ilikuwa hasa vyombo vya Habari vya Umma tulishalalamika hapa Bungeni kwamba habari nyingi zinazoandikwa ni za mjini tu, lakini vijijini ndiyo kuna taarifa nyingi, tulishauri Serikali kwamba, kila Wilaya iwe na Mwandishi wa Habari. Kwa hiyo, huo ni ushauri wangu Mheshimiwa Waziri, kule habari nyingi hazifiki kwenye vyombo vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, maslahi ya vyombo vya habari. Vyombo vya habari vya umma kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja vyombo hivi vinafanya kazi nzuri sana na vinailetea sifa nchi yetu, wanaandika taarifa kila siku tunasoma magazeti, habari tusingezipata bila yale magazeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya habari kwa mfano TBC, TBC ni chombo cha umma, lakini TBC inafanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwanza vyombo vyao vimechakaa, baadhi ya vyombo kwa hiyo, kuna baadhi ya maeneo katika nchi hii TBC haisikiki. Kwa hiyo, Serikali ijitahidi kuongeza bajeti ili tuboreshe TBC iweze kusikika nchi nzima hasa TBC One pamoja na TBC Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi. TBC wanafanya kazi usiku na mchana. Hapa tunaona wanavyohangaika usiku na mchana wanafanya kazi, lakini maslahi yao ni kidogo sana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aboreshe maslahi ya watumishi wa TBC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, viwanja vya michezo. Pitch ikiwa nzuri na timu itacheza vizuri mpira...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara hii. Kwanza nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miradi ya maji; kama walivyozungumza Wabunge wenzangu, kwa nini miradi haikamiliki Mheshimiwa Waziri? Kwangu kuna visima vinne vimechimbwa katika vijiji vya Mima, Iyoma, Bumila pamoja na Mzase. Tangu mwaka juzi, mwaka 2016 umeleta wakandarasi, sawa, sasa wako pale karibu mwaka mzima hawafanyi kazi yoyote, hakuna fedha na inatakiwa upeleke shilingi milioni 426. Sasa Mheshimiwa Waziri hivi tutakuwa tunawachimbia watu visima halafu inakuwa kama white elephant, watu wanaangalia tu kwamba tuna kisima hapa, miaka mitatu, miaka minne, kisima hakikamiliki, kwa nini sisi Wabunge tusilalamike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri Miradi ya World Bank imechukua miaka kumi, mingine imekamilika juzi, mingine haijakamilika. Kwa mfano, Kijiji cha Kimagai ndiyo mradi umekamilika juzi, miaka kumi Miradi ya Benki ya Dunia. Sasa tatizo ni fedha au tatizo la wakandarasi? Naona tatizo ni wajkandarasi hamuwalipi. Bunge sisi kama Bunge tunatenga fedha, tunakaa hapa miezi mitatu, tukishapitisha bajeti haiendi kwenye miradi, inakuja nusu tu, hizi fedha zinakwenda wapi huko Hazina? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Musukuma, nadhani ipo haja ya kuunda Tume ichunguze Wizara hii fedha zinakwenda wapi? Miradi haikamiliki, miaka kumi, miaka nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa katika nchi hii ni maji, ni shida kubwa sana, kila kijiji ukienda tatizo ni maji. Sasa ahadi tulishaahidi, Ilani ya Uchaguzi kwamba mkinichagua nitahakikisha mnapata maji, sasa Mheshimiwa Waziri unatutakia mema kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana peleka Jimbo la Mpwapwa shilingi milioni 426 ili wakandarasi waweze kukamilisha miradi hii ya maji. Mpwapwa Mjini tunatumia maji ya chumvi, ni kweli wanasema siyo kila aina ya maji ya chumvi yana madhara tumboni kwa sababu yale maji yanapimwa, unachukua sample inapelekwa kwa Mkemia Mkuu wanaangalia mambo mawili, wanafanya chemical analysis pamoja na bacteriological examination. Kama yana madini yanayoweza kudhuru afya ya binadamu ama kama kuna bacteria, maana maji mengine yanaleta homa ya matumbo lakini wamepima yanafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri ukienda Wilaya ya Mpwapwa, hasa Mpwapwa Mjini, ujaribu kuonja yale maji ndiyo binadamu wanakunywa. Kwa hiyo, nakuomba na nilikwishaiomba Serikali ifanye utafiti kuna sehemu ambazo ukichimba kisima cha maji kuna maji baridi, tuwaonee huruma wananchi wa Mji wa Mpwapwa jamani wanateseka. Kweli maji yapo lakini ni ya chumvi mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Elimu.

Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii pamoja na walimu wote wa shule za msingi pamoja na shule za sekondari, wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, lakini hawana nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata mradi wa MMEM tumejenga madarasa, tukasahau nyumba za walimu, tumepata mradi wa MMES tumejenga madarasa, tumesahau nyumba za walimu. Kwa hiyo, walimu wanaishi katika mazingira magumu sana na ndiyo maana elimu inashuka. Tusilaumu walimu kwamba kwa nini elimu inashuka ni kwa sababu ya mazingira wanayoishi.

Mheshimiwa Mwenyeki, jambo la pili ni ukarabati wa vyuo na shule za sekondari kongwe. Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana, Chuo cha Ualimu Mpwapwa kimekarabatiwa vizuri sana pamoja na Shule ya Sekondari ya Mpwapwa ambayo ilianzishwa mwaka 1926. Hata hivyo, kwa nini mnakarabati vyuo na shule za sekondari, nyumba za walimu hamkarabati? Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri umefika Mpwapwa mara nyingi sana wakati wa ukarabati wa chuo cha ualimu. Ukifika Kijiji cha Mwanakianga angalia kushoto nyumba za walimu zina hali mbaya sana, nyingine zimejengwa mwaka 1926. Kwa nini hatuna huruma na hawa walimu wetu jamani? Nyumba imechakaa mtu anaishi katika mazingira magumu sana. Pangeni fungu mkarabati nyumba za walimu wa sekondari pamoja na walimu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu elimu bure. Kwa kweli wananchi wanashukuru sana likiwemo Jimbo langu la Mpwapwa na Wilaya ya Mpwapwa kwa ujumla. Hata hiyo, elimu bure ni kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne lakini kidato cha tano na cha sita wameachwa. Mheshimiwa Waziri hawa wote ni wako, hiyo shule ina form one mpaka form six, wengine wamesamehewa wengine hawakusamehewa, wanajisikiaje wale wanafunzi? Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri hawa nao muwasamehe, ni watoto wa Serikali moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa shule huko huko kuhusu chakula wanachopata wanafunzi wa bweni cha shilingi 1,500 kwa siku. Hivi kweli Mheshimiwa Waziri upewe shilingi 1,500 unywe chai asubuhi, chakula cha mchana na chakula cha jioni itatosha? Kwa nini tunawaweka katika mazingira magumu sana wanafunzi wetu? Mimi nashauri tuongeze hii posho ya chakula angalau wapate shilingi 2000 inaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni maslahi ya walimu. Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini kila Wilaya walimu wanadai maslahi yao ya likizo, mishahara na wengine wamepandishwa vyeo. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri shughulikia maslahi ya walimu wetu. Walimu wakidai posho zao muwalipe mapema. Mtu anatoka kijijini anakuja mjini kwa DEO, anakaa pale wiki nzima anafuatilia maslahi yake. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, hawa walimu lazima tuwaheshimu, hakuna mtu ambaye hakupitia darasani hapa, lazima tuwape heshima yao walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ya kwangu yalikuwa ni hayo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini nimuombe sana Mheshimiwa Waziri pangeni bajeti maalum kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu. Wananchi wamejenga shule za msingi, shule za sekondari na sasa Serikali imeanzisha kidato cha tano na cha sita katika baadhi ya shule, mfano, katika Wilaya ya Mpwapwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mazae na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Berege, lakini hakuna nyumba za walimu wala hostel, wanafunzi hawa wa form five na six wanalala madarasani. Naomba sana Mheshimiwa Waziri tuwaonee huruma wananchi wamefanya kazi kubwa sana. Shule zote za msingi na sekondari madarasa yote wamejenga wenyewe, tuwaonee huruma na Serikali nayo iweke mkono wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nikushukuru na naunga mkono kwa asilimia mia moja hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie Wizara hii ya Ulinzi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu, Mkuu wa Majeshi na Makamanda wote na Wanajeshi wote kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusicheze na amani jamani. Mimi nawasikitikia sana wanaotaka kuvuruga amani ya nchi hii. Tutakimbilia wapi sisi Watanzania, nchi zote ambazo zinaizunguka Tanzania, hakuna amani, tutakwenda wapi? Kwa hiyo, naomba sana Watanzania hii amani tuliyonayo ni tunu, kwa kweli tuilinde amani yetu ili Askari wetu hawa wasipate kazi kubwa ya kuhangaika kuzuia vurugu ndogondogo hizi. Mipaka yetu yote ni shwari, kwa hiyo naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkuu wa Majeshi kwa kurejesha Kambi ya JKT Mpwapwa. Nimeiomba Kambi ile muda mrefu bado yuko Mkuu wa Majeshi Waitara, bado yuko Mkuu wa Majeshi hawa wastaafu Mboma, mpaka ndugu yangu Mwamunyange, hawa wote nimewaomba turejeshe Kambi ya JKT Mpwapwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ile imerejeshwa, lakini bado ina matatizo makubwa, hasa miundombinu majengo ya kuishi Askari. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atenge bajeti kwa ajili ya kujenga majengo pale. Eneo lile linafaa sana kwa kilimo awapelekee matrekta, itawasaidia sana wale vijana kulima mashamba na waweze kujilisha wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu makazi ya Wanajeshi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Wanajeshi wasipange uraiani. Wanajeshi wakae pamoja lakini kukaa uraiani wakati fulani zinatokea vurugu na wananchi. Kwa hiyo nashauri wajengewe nyumba katika kila kambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa Wanajeshi kwenye makambi, haipendezi kukuta Askari wananing’inia kwenye malori. Wakati fulani huwa napita pale Ihumwa yaani nakuta Askari wako barabarani, wakati fulani napata huruma tunasimama na gari yangu napakia watatu, wanne lakini wengine wanaomba lift mpaka kwenye malori. Kwa hiyo naomba tuongeze usafiri kwenye Kambi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu posho au lishe ya Askari wetu. Posho ingeongezwa kwa sababu posho wanayopata sasa haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, yule Mkuu wa Jeshi aliyestaafu juzi anaitwa Mwakinyange ‘Jenerali Davis Mwamunyange’ samahani sana Mkuu wangu nakosea jina lako, lakini naye alifanya kazi nzuri sana pamoja na wote hao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja hii na naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja moja tu. Wilaya ya Mpwapwa ina taasisi mbili za mifugo. Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Chuo cha Mifugo. Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ndiyo Makao Makuu ya nchi nzima katika utafiti wa mifugo. Taasisi hii ina ng’ombe zaidi ya 800, lakini hawana vitendea kazi. Wana mashamba ya kulima majani kwa ajili ya mifugo, wana trekta moja na limechakaa na wana Lorry moja, nalo limechakaa. Sasa ili ng’ombe wapate chakula, watalima yale mashamba kwa majembe ya mkono? Kwa hiyo, naomba ile taasisi ipewe fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Chuo cha Mifugo, mwaka 1995 yale mabweni tulitaka tuyachukue sisi Halmashauri tuyakarabati iwe Shule ya Sekondari lakini Wizar ikayawahi. Sasa yamechakaa tena. Itolewe bajeti ya kutosha mabweni yakarabatiwe na ile Taasisi ya Mifugo ya Mafunzo iongezewe bajeti na ile maabara iongezewe vifaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono azimio hii kwa asilimia mia moja. Mji wetu wa Dodoma umekuwa ni mji wa siku nyingi na Baba wa Taifa alipotamka kwamba Makao Makuu yahamie Dodoma tangu mwaka 1973 ni miaka mingi mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa juhudi zake kuhakikisha kwamba sasa anatekeleza lile agizo au wazo la Mheshimiwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba sasa Dodoma iwe Makao Makuu. Dodoma ni Jiji kubwa, Dodoma makazi yake yamejengwa vizuri, hakuna squatters, tumefuata master plan, watu wameongezeka, kwa hiyo, kwa kweIi kuna haja ya kupata Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyopata Jiji la Dodoma, hata sisi kwenye Wilaya zetu lazima kuna mambo mengi yataboreka kuhusu barabara, huduma za shule, huduma za maji na huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono azimio hili alilosema mdogo wangu Mheshimiwa Simbachawene kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja hii. Kwanza niwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, IGP, Kamishna General wa Magereza, Kiongozi wa Zimamoto, Kiongozi wa Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na Askari wote, wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiona mtu anapambana na Polisi, nashangaa kabisa. Hawa ndio wanaotulinda. Hata hapa Bungeni, saa 24 wanalinda hawa vijana. Nchi yetu hii unatembea saa 24 hata saa 8.00 usiku, usalama upo tu kwa sababu ya hawa Askari. Naomba waongezewe posho zao na wajengewe makazi bora. Sasa hivi makazi wanayokaa kwa kweli yanatisha. Hawa ni binadamu, lazima tuwaheshimu tuwajengee makazi bora kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Wilaya ya Mpwapwa ina Kata 33, lakini Vituo vya Polisi viko viwili tu pamoja na Makao Makuu ya Polisi Mpwapwa, cha tatu; Kibakwe pamoja na Kipogoro. Kile Kituo cha Kibakwe hawana usafiri. Waliwahi kupewa pikipiki na ile pikipiki imeharibika. Kwa hiyo, naomba IGP tusaidie gari; eneo lile ni kubwa sana, pamoja na Kituo cha Polisi Kipogoro. Wanashughulikia maeneo yote ya Mtera kuhusiana na uvuvi haramu, kwa hiyo, naomba wasaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Mpwapwa Mjini ndiyo Makao Makuu ya Polisi Wilaya. Kituo kile kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati, paa linavuja. Naomba IGP akitoka hapa atembelee Kituo cha Polisi Mpwapwa. Zile nyumba wanazoishi Askari kwa kweli hazifai, wanaishi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango wa kujenga nyumba 400 kila mkoa, naomba Wilaya ya Mpwapwa isisahaulike. Tuwajengee Polisi nyumba nzuri hasa hapa Mkoa wa Dodoma. RPC anafanya kazi nzuri, mkoa wake una amani kabisa na utulivu, sisi Wabunge tupo hapa, hatujawahi kutoa malalamiko yoyote kwa RPC, lakini tunaishi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri Askari wote, IGP na vyombo vyote vilivyo chini ya Jeshi la Polisi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii nyeti sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri wote wawili pamoja na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sekta ya madini mimi nilitarajia ingechangia kiasi kikubwa sana cha pato la Taifa lakini nasikitika kwamba inachangia 4.8% tu wakati madini tunayo mengi sana hapa nchini. Mheshimiwa Waziri itabidi alieleze Bunge hili kwa nini sekta ya madini inachangia kidogo sana katika pato la Taifa? Nadhani madini mengi yanatoroshwa na ndiyo maana sekta hii inachangia kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nashauri kwamba maeneo yote ambayo wanachimba madini basi wale wananchi wanufaike, angalau watengenezewe barabara, wajengewe shule, zahanati, lakini hawanufaiki na jambo lolote wanaachiwa mashimo tu. Wilaya ya Mpwapwa ina madini, kuna rubi eneo la Winza, copper eneo la Kata ya Mlembule na Kata ya Matomondo, Vijiji vya Tambi, Mlembule Nnana, Majami, Mwenzele wanachimba sana copper. Ukienda kwenye vijiji vile hakuna chochote, barabara haitengenezwi wala hawawasaidii wananchi kwenye suala zima la shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri vilevile hawa wachimbaji wadogo wadogo hebu tuwaangalie, tuwape vifaa vya kisasa, tuwape mikopo ili waweze kuboresha uchimbaji wao kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, wapewe mikopo ili waweze kununua vifaa vya kisasa na si kuchimba kwa kutumia sululu na majembe waweze kuchimba na mitambo ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umenipa dakika tano, nakushukuru sana, huo ndiyo mchango wangu. Naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo na makamanda wote kwa kazi nzuri ya ulinzi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na kuunga mkono hoja hii naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kurudisha kambi ya JKT ya Mpwapwa. Hata hivyo kambi hiyo ina mapungufu yafuatayo:-

Kwanza ni kuhusu upungufu wa majengo, hivyo nashauri Serikali iwajengee majengo ya kutosha kwa ajili ya makazi yao na ofisi za kufanyia kazi. Pili, vitendea kazi kama vile magari, matrekta kwa ajili ya kilimo kwa kuwa eneo hilo ni zuri kwa kilimo na chakula kinachopatikana watumie wenyewe ili kupunguza gharama ya Serikali kupeleka chakula kambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT Mpwapwa ianze kuchukua vijana wa kujitolea wa form four na form six kama makambi mengine ya JKT. Katika JKT Makutupora majengo yafanyiwe ukarabati, vyombo vya usafiri viongozwe kama vile magari na kadhalika. Posho za askari Wanajeshi wa JKT na JWTZ ziongezwe. Majeshi yote yajengewe makazi badala ya kupanga uraiani, kambi zijengwe za kutosha ili wanajeshi wote wasipange mitaani. Usafiri katika majeshi yote hautoshi hivyo nashauri magari yaongezwe katika kambi zote ikiwemo Kambi ya Ihumwa, Makutupora na Mpwapwa. Posho ya chakula ya wanajeshi wote iongezwe haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia huduma ya maji iboreshwe na barabara zikarabatiwe katika Kambi ya JKT Mpwapwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GEORGE M. LUBELEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri yenye ufafanuzi. Pili, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na kuunga mkono naomba nichangie maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya mpira (football) kwa kuwa viwanja vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo vina hali mbaya sana vinatakiwa ukarabati na CCM haina fedha za ukarabati. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwa Chama cha Mapinduzi ili kuvikarabati viwanja vyake hasa ukuta eneo la Pitch ili timu zetu za ligi kuu ziweze kuchezea viwanja hivyo bila shida yoyote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waandishi wa Habari wa Umma (Serikali) kwa kuwa sekta ya habari ni muhimu sana kwa maendeleo na uchumi wa nchi yetu, Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Waandishi wa Habari kila Wilaya ambako wapo wananchi wengi na wanafanya kazi za kilimo na shughuli nyingi za maendeleo kwa ajili ya kuinua uchumi wa wananchi. Vyombo vingi vya habari vinahamasisha sana wananchi kushiriki shughuli nyingi za maendeleo badala ya Waandishi wa Habari kujazana Mijini tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyombo vya Habari hasa vya Serikali havipati maslahi ya kutosha kama vile TBC maslahi ni kidogo sana ndiyo maana watumishi wengi wanahamia vyombo binafsi ambao wanalipwa vizuri. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa TBC na Waandishi wa Habari wa Serikali ambao wapo chini ya Idara ya Habari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu nyingi za mpira wa miguu zina migogoro mingi sana. Je, ni sababu zipi zinazosababisha migogoro hiyo na kusababisha kushuka kiwango cha mchezo wa mpira wa miguu hapa Tanzania? Je, Serikali itasaidiaje kupunguza migogoro hiyo ili kuboresha soka la Tanzania hata Kimataifa.

Mheshimiwa naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Pili, naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa nyumba za Polisi, kwa kuwa nyumba wanazoishi askari polisi zina hali mbaya sana mbovu na hazina hadhi ya kuishi askari polisi na kwa kuwa Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 400, kila Mkoa na kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi, je, ujenzi wa nyumba hizo utaanza lini ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa ambapo nyumba za Askari Polisi ni mbovu zimechakaa na hazifai kuishi askari ikiwemo jengo la kituo cha polisi ambapo wakati wa kipindi cha mvua paa linavuja sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Mpwapwa halina ukuta wa ngome na hivi sasa maaskari magereza wanajitolea kujenga ukuta (ngome) na mimi kama Mbunge nilichangia mifuko 25 ya cement. Je, Serikali imetenga shilingi ngapi kwa ajili ya ujenzi wa ngome ya gereza la Mpwapwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uhamiaji, kwa kuwa passport zinabadilishwa na kwa kuwa sisi Waheshimiwa Wabunge hatujabadilishiwa, je, Idara ya Uhamiaji itabadilisha lini passport za Waheshimiwa Wabunge na hizi za sasa zinaruhusiwa kutumika kwa muda gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto, kwa kuwa magari ya zimamoto katika miji mingi ni machache sana na matukio ya moto ni mengi hapa nchini. Je, ni Serikali itanunua magari ya kutosha kuzimia moto katika miji yote Tanzania ikiwemo Makao Makuu ya Nchi Dodoma. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja Serikali kununua gari moja la kuzimia moto kila Wilaya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja hizi mbili; TAMISEMI pamoja na Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Utumishi, Manaibu Mawaziri, Wakuu wa Vitengo na Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Mapato ya Serikali za Mitaa. Mapato ya Serikali za Mitaa ndiyo uhai wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato haya yanasaidia sana kulipa Watendaji wa Vijiji…

MWENYEKITI: Utulivu ndani ya Bunge tafadhali. Kuna Senator anatoa mchango wake.

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato haya yanasaidia sana kulipa Watendaji wa Vijiji wale ambao wameajiriwa na Serikali za Mitaa, mapato haya vilevile yanasasaidia kulipa posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji na Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri zetu zilikuwa na vyanzo vingi vya mapato, lakini bahati mbaya sana vyanzo vingi vimechukuliwa na Serikali. Vyanzo hivi ndiyo vingesaidia sana kuongeza mapato katika Halmashauri zetu. Kwa mfano, hivi karibuni TRA wamechukua kodi ya majengo. Mimi sipingi, lakini ule utaratibu kwamba wakusanye mwaka mzima, miezi 12, halafu ndipo wazigawie Halmashauri. Hili kwa kweli mimi sikubaliani nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Halmashauri zina miradi na miradi ile inaendelea mwaka mzima. Sasa fedha ikae TRA mwaka mzima halafu baadaye ndiyo Halmashauri ziweze kupata hizo fedha. Kwa hiyo, nilikuwa namshauri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, hili mngeliangalia upya angalau miezi sita Halmashauri ziweze kupata mgao wa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kuhusu barabara. Naipongeza sana TARURA, inafanya kazi nzuri sana, lakini changamoto kubwa ya TARURA ni fedha. Tumeishauri Serikali kwamba hii asilimia 30 haitoshi, kwa hiyo, waongezwe angalau ifike asilimia 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Vijijini ni muhimu sana kwa ajili ya kusafirisha mazao na kusafirisha abiria. Kwa hiyo, naishauri sana TAMISEMI ijitahidi sana kuongeza fedha kwa ajili ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefika Mpwapwa na kuona barabara ya kutoka Gulwe, Berege, Chitemo, Mima, Chazima mpaka Igoji moja mpaka Seluka. Amepita hii barabara; barabara hii mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka 2018 ambayo inaendelea sasa, tulitengewa shilingi milioni 148. Barabara ile inahitaji zaidi ya shilingi bilioni moja ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha matengenezo makubwa. Sasa naomba sana mwongeze fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ile pamoja na barabara ya kutoka Mima kwenda Mkanana. Vilevile Mkanana Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba mmesitisha kugawa maeneo ya Utawala, lakini Mkanana iko milimani kilometa 35 kutoka mlimani kuja Makao Makuu ya Kata ambayo ni Chitemo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwamba Mkanana nao wapate Kata yao. Nitashukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mambo ya TASAF na MKURABITA. TASAF wanafanya kazi nzuri sana, imesambaa nchi nzima. Ombi langu Viongozi wa TASAF ni kwamba, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, tumeshatoa mapendekezo kwamba lengo la TASAF Awamu ya Tatu ni kuboresha au kunufaisha kaya masikini, lakini sasa kuna baadhi ya maeneo tumegundua fedha hizi zinakwenda kwa watu wenye uwezo. Tumeagiza chombo kinachohusika, wote ambao wameorodheshwa kwenye daftari waondolewe, kwa sababu wana uwezo, hawawezi wakapata fedha za TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za TASAF tunasaidiwa na Wafadhili na Wafadhili wakigundua kwamba kaya masikini hawapati, wanapata wananchi ambao wana uwezo, wanaweza kuleta maamuzi ambayo yatatuletea matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA ni kurasimisha mali, kwa mfano mashamba. Kuna Kijiji changu pale Jimbo la Mpwapwa kinaitwa Inzomvu MKURABITA walipima mashamba, baada ya kupima mashamba, hawakujenga ile Ofisi ya Masijala na ule mradi haujakamilika. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, afike kijiji kile, wanalalamika sana, akajibu yeye mwenyewe hoja. Mimi siwezi kukosa kura za pale kwa sababu mradi wa MKURABITA haujatekelezwa, hapana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aende akawaambie yeye mwenyewe kwamba kwa nini mradi ule umekwama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu upungufu wa watumishi. Kuna upungufu wa watumishi hasa kwenye Sekta ya Afya. Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu wa watumishi katika Sekta ya Afya zaidi ya 450. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, atusaidie tupate watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni Bodi ya Mikopo Serikali za Mitaa. Bodi ya Mikopo Serikali za Mitaa, ni chombo cha Serikali za Mitaa, ni chombo cha Halmashauri. Chombo hiki, wadau wakubwa ni Halmashauri na ndiyo wanakichangia hiki chombo. Kulikuwa na mpango wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa. Sasa Mheshimiwa Waziri: Je, mpango huu umefika wapi? Kama mpango huu haupo, basi Halmashauri ziruhusiwe kukopa kama zamani ili kujenga masoko, barabara, stendi na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuchangia hoja hii ya mipango. Kwanza kabisa nianze na sekta ya umeme; niishukuru sana Serikali imejitahidi kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinakuwa na huduma ya umeme. Kwa Jimbo la Mpwapwa ni vijiji sita tu ambavyo bado havijapata huduma ya umeme kwa hiyo, nishukuru na niipongeze sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya umeme ni maendeleo ya nchi na uchumi wa nchi kwa sababu, kijiji kikipata umeme wataanzisha viwanda vidogovidogo vya kukamua mbegu za mafuta kwa mfano alizeti, ufuta, karanga na Serikali itapata mapato pale. Kwa hiyo, naiomba Serikali, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na ameshafika Mpwapwa kutembelea kuona hii hali ya huduma za umeme, vile vijiji ambavyo bado havijapata umeme Kazania, Kiyegeya, Chimaligo, Mkanana, Kiboliani, Nana, Namba 30 Mafuto pamoja na Majami, naomba sana Mheshimiwa Waziri ajitahidi nao wapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni sekta ya ujenzi. Mawasiliano ni muhimu sana katika nchi yoyote duniani, bila mawasiliano nchi hiyo itakuwa haina maendeleo. Barabara za lami zinatengenezwa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais amesimamia hiyo kazi hasa Dar-es-Salaam ambako kuna msongamano mkubwa sana wa wananchi, lakini haya mabasi yanayokwenda kasi yamepunguza msongamano, lakini hata fly overs ambazo zinajengwa zimesaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushe suala la ujenzi wa barabara. Pamoja na kwamba, Serikali inajitahidi kujenga barabara za Kitaifa na mkoa, lakini hata hizi za wilaya kwa mfano, barabara ya kutoka Mbande – Kongwa – Mpwapwa, hili suala nimeshalizungumza muda mrefu sana hata Mheshimiwa Waziri Mkuu wiki mbili zilizopita alikuwa Mpwapwa tumeshamwambia ni ahadi ya Marais karibu wanne wote wanaahidi kwamba, tutatengeneza hii barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya Wilaya ya Mpwapwa na uchumi wa Mpwapwa, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kwa mwaka huu wameitengea fedha ni kidogo sana, milioni 500 ni sawasawa na kilometa moja tu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Waziri wa Mipango wakati anasoma alikuja Wilaya ya Mpwapwa kufanya mazoezi na barabara ile alipita, anaifahamu vizuri sana, hebu wanisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za vijijini ni muhimu. Tusiseme kwamba barabara za lami tu, ndio barabara za lami ni muhimu, lakini vijijini ndiko wanakoishi wakulima na watu wa mijini wengi hawana mashamba, hawalimi, wanategemea chakula kutoka vijijini, sasa magari yasipopata barabara nzuri za kupita watasafirishaje haya mazao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ni kweli imeundwa naishukuru Serikali, lakini iongezewe bajeti. Naomba lile fungu lile la mafuta, Mfuko wa Road Fund, basi angalau tugawane TANROADS wapate 60% na TARURA wapate 40% waweze kufanya matengenezo ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu ni mbaya sana. Waziri wa TAMISEMI ameshafika maeneo ya Mima, Barabara ya Mima ni mbaya haipitiki, sasa na mvua zinaanza, Barabara za Mkanana. Naishukuru sana Serikali imetenga milioni 48 na kwa upande wa barabara ya Mima imetengewa zaidi ya milioni 60 na tayari Wakandarasi wameshasaini mikataba kwa hiyo, hivi karibuni wataanza kutengeneza. Kwa hiyo, pamoja na barabara za Kitaifa, barabara za Mikoa, lakini vilevile Serikali izingatie barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni sekta ya maji, sekta ya maji ni muhimu sana, maji ni uhai, maji ndio uchumi wetu, maji ndio maendeleo na maji ndio kila kitu. Kwa hiyo, naiomba Serikali pamoja na juhudi kwamba, visima vya maji vimechimbwa karibu vijiji vingi sana; kwa mfano mimi katika jimbo langu visima vimechimbwa vingi, lakini bado wananchi wana tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwasaidie akinamama kusafiri mwenda mrefu, ukiwa na ndoo, ukiwa na sijui kitu gani unakwenda kutafuta maji kilometa 10 mpaka 15. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali suala la huduma ya maji ni muhimu sana. Naishauri Serikali kila kijiji kiwe na kisima cha maji ili kuwapunguzia hawa akinamama matatizo ya kusafiri mwendo mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta nyingine ni sekta ya afya, ni kweli Serikali imejitahidi sana maana afya, ukisema Wizara ya Afya ni hospitali, vituo vya afya na zahanati na zahanati, hospitali, vituo vya afya si majengo tu isipokuwa ni dawa, lazima majengo hayo yawe na dawa za kutosha na yawe na watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali kutenga fedha za kutosha karibu bilioni 269 kwa ajili ya kununua dawa, lakini bado tatizo hili ni kubwa katika hospitali zetu, watumishi ni wachache; utakuta zahanati wanaohudumia zaidi ni wale medical attendant, hatusemi kwamba, hawafanyi kazi nzuri, medical attendant ndio wanafanya kazi nzuri, ndio wanatoa dawa, wanachoma sindano na hata kuzalisha akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha vyuo vingi kwa ajili ya ku-train au kufundisha hawa Clinical Officers au Clinical Assistants, lakini mpaka sasa bado watumishi hao ni wachache sana. Naomba vyuo vile ambavyo Serikali, Wizara ya Afya iliahidi basi vifunguliwe kwa ajili ya kufundisha Clinical Officers pamoja na Clinical Assistants ili waweze kupelekwa kwenye zahanati zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na haya machache, lakini nakushukuru sana. Naiomba Serikali ikumbuke barabara za Mpwapwa, Kongwa, pamoja na Mbande pamoja na Daraja la Godegode ambacho ni kiungo kikubwa cha Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la Kibakwe. Hivi sasa wananchi wanazunguka kutoka Kata za Mbuga kuja Kata ya Lumuma, Kata ya Kitatu Pwaga wanazungukia Kibakwe ambayo ni zaidi ya kilometa 100 na nauli ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono kwa asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hii. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya lakini niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, naiunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la maji, maji ni uhai, maji ni maendeleo, maji ni uchumi wa nchi yetu. Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa tuna matatizo makubwa ya maji. Kuna miradi ya maji inayoendelea mpaka sasa lakini bahati mbaya sana imesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi niliuliza swali hapa kwamba kwa nini Serikali haiwalipi wakandarasi? Kuna miradi inachukua miaka kumi haijakamilika, kwa nini? Kwa mfano miradi kutoka Kijiji cha Bumila, Iyoma, Mima na Mnzasa, ni zaidi ya miaka kumi haijakamilika. Wakandarasi hawalipwi kwa nini na hapa Bunge tunapitisha bajeti, kama tunapitisha bajeti hiyo hela kwa nini isiwalipe wakandarasi? Kwa hiyo, nashauri wakandarasi wote nchi nzima walipwe ili miradi ya maji iendelee ili wananchi waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni ujenzi wa Vituo vya Afya katika Majimbo yetu au katika Wilaya zetu. Hili ni jambo jema, kwa sababu tunawasogezea wananchi huduma katika maeneo yao. Kwa sababu ukishajenga Kituo cha Afya, Wataalam kwa mfano Madaktari watakuwa pale, Manesi watakuwa pale hata hizo minor operations labla, mama ameshindwa kujifungua, kwa hiyo, zile operations ndogo ndogo zinafanyika pale badala ya kuwapeleka Hospitali ambako ni mbali. Kwa hiyo, hili ni jambo jema.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa shilingi milioni 500, kujenga hivi vituo, lakini nilikuwa nashauri TAMISEMI mjitahidi basi, mtoe kila Wilaya angalau fedha kidogo za kujenga Zahanati. Tusiishie tu kwenye Vituo vya Afya, hapana. Tunaomba sana, kwa sababu Vituo vya Afya viko mbali na Vijiji vingine havina Zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba pamoja na na kutoa shilingi milioni 500 kwenye ujenzi wa Vituo vya Afya, kwa mfano kama kwangu pale wamejenga Kituo cha Afya Mima na pale Jimbo la Kibakwe, pamoja na Pwaga. Kongwa vilevile wamejenga Kituo cha Afya pale, wamekarabati maana yalikuwa ni majengo ya zamani kwa hiyo, wamejenga mpya pale maeneo ya Mlali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashukuru sana, ni mpango mzuri sana. Mjitahidi sasa mwanze mpango wa kutoa fedha kidogo kidogo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Zahanati ni muhimu sana, hasa maeneo ambayo hayana huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, tunajenga zahanati; wananchi wameambiwa kila Kijiji kiwe na zahanati, lakini tatizo ni kwamba wahudumu hawatoshi kabisa. Lengo la Wizara ya Afya ilikuwa ni ku-train Watabibu Wasaidizi na Tatibu, yaani Clinical Officers na Clinical Assistants, lakini mpango huo umesimama na watumishi bado wanaendelea ni wale wale, ambao tunasema kwamba hawa Medical Auxiliary wanafanya kazi nzuri sana, lakini Medical Auxiliary amekuwa trained kwa ajili labla ya kugawa dawa na mambo mengine. Medical Auxiliary huyo ndiye atibu, huyo ndiye achome sindano, huyo ndiye a-prescribe dawa. Kwa hiyo, inakuwa ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara ya Afya mwendelee na utaratibu ule wa ku-train wale Clinical Officers na Clinical Assistants na kuwasambaza katika zahanati zote nchi nzima. Kwa hiyo, itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie mapato katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa ni Serikali kamili. Katiba Ibara ya (145), (146) inatambua kabisa kwamba tutakuwa na Serikali za Mitaa hapa Tanzania. Kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali jambo moja, mnapochukua vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa, basi mshauriane na wale wenye vyanzo vile, itasaidia kuwapa ushauri. Juzi tumepitisha Sheria ya Kukusanya Kodi ya Majengo, ni jambo jema, hatupingi sisi, lakini Kodi ya Majengo TRA wakusanye mwaka mzima, halafu ukiisha mwaka ndiyo Halmashauri zianze kupewa fedha. Hiyo miradi ya Halmashauri itakuwa imesimama! Kwa nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake miradi inatolewa taarifa quarterly kila miezi mitatu. Sasa fedha gani ukusanye halafu uziweke mpaka mwaka uishe?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba angalau wangejitahidi kukusanya miezi sita halafu wazipatie Halmashauri ili ziweze kutekeleza miradi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, sisi Wabunge tuko hapa miezi mitatu kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Serikali, lakini jambo la kushangaza, bajeti tunayopitisha na fedha inayofikishwa kwenye Wilaya zetu na Mikoani, kuna fedha mahali pengine hata asilimia 50 haifiki. Ndiyo maana kunakuwa maboma. Kuna miradi mingi sana imelala tu, haijatekelezwa. Maboma ya shule, zahanati, yamelala wala hayatekelezwi kwa sababu fedha hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Bajeti ambayo tunapitisha Bungeni hapa, basi Serikali ijitahidi kufikisha pesa mapema. Kwa mfano, kama Wilaya ya Mpwapwa imetengewa shilingi bilioni kumi, basi ziende shilingi bilioni kumi siyo zipelekwe shilingi bilioni nne, haiwezekani. Shilingi bilioni nne utatekeleza nini? Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni hali ya hewa katika Mkoa wa Dodoma. Wote ni mashahidi mnapita barabara hii…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hasa kule mwisho kule, sitaki kuwataja majina Waheshimiwa mliosimama na nini, mmeanzisha club huko, naomba mkae.

Halafu pili, naomba yaani wewe mwenyewe ukiona sauti imekuwa kubwa, unaanza kwa kushusha ya kwako kidogo. Tuelewane. Pia kuwa ma-back bencher siyo ruhusa ya kuwa ni vituo vya vikao visivyokubalika. Niendelee. Nyie mmenichonganisha eeh! (Kicheko)

Mheshimiwa Lubeleje, endelea. (Kicheko/Makofi)

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, niendelee...

Mheshimiwa Spika, la mwisho nimesema hali ya hewa. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Dodoma, kwa kweli mwaka huu hatutegemei kama tutavuna chochote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama tutakuja kuomba msaada Viongozi wa Mkoa wa Dodoma, msije mkafikiria kwamba wananchi wetu hawakulima, hawakufanya kazi, hapana. Mvua analeta Mwenyezi Mungu, lakini bahati mbaya mvua zimekatika mwezi wa Pili, mimea yote imekauka. Kwa hiyo, naomba sana, hili suala ni muhimu, lazima tupate chakula cha kutosha katika Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie na kama muda wangu bado kidogo, nimalizie la mwisho… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Lubeleje.

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, niendelee!

SPIKA: Nakushukuru sana, inatosha. Mheshimiwa Magdalena Sakaya.

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2017
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niweze na mimi kuhitimisha hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote. Muswada huu umechangiwa ukiacha taarifa za Kamati na Upinzani Muswada huu umechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wawili, na mimi napenda kuwatambua wa kwanza ni
Mheshimiwa Amina Mollel na wa pili ni Mheshimiwa Abdallah Mtolea. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa jinsi ambavyo mmepata fursa ya kuushughulikia Muswada huu kupitia kwenye Kamati ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme haya wakati nahitimisha; moja ni hili ambalo amemaliza kulisema Mheshimiwa Mtolea. Tunatambua kwamba iko sheria mahususi inayotawala Mabaraza ya Kata na kama mtafahamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine wa yale Mabaraza ya Kata sio wataalam wa sheria na Baraza lile, kusudi lake hasa ni usuluhishi. Kwa hiyo, tukitaka kufanya mabadiliko katika Sheria hii ya Mabaraza ya Kata, tunahitaji mashauriano ya kina na wananchi kwenye maeneo haya, tusije tukafanya maamuzi tu kumbe tunakwenda kuleta tatizo kubwa. Ndiyo msingi wa kwamba mabadiliko kwenye hiyo Sheria ya Mabaraza ya Kata hayapo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo tukishaelewana hivyo, hii hoja kwamba tungeleta mabadiliko pia kwenye yale Mabaraza ya Kata ambayo essentially hasa yanatumika kwenye Serikali za Mitaa, inakuwa tena haina kichwa. Kwa hiyo, ninaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Mchengerwa ametusaidia kwamba pia hata sisi Waheshimiwa Wabunge, tunayo mamlaka ya kuleta miswada, lakini pia tunayo mamlaka ya kuishauri Serikali ilete miswada mkiainisha changamoto zilizopo kule. Kwa hiyo hili la Baraza la Kata linahitaji mashauriano ya ndani kati ya wananchi, kati ya Waheshimiwa Wabunge na Serikali yenyewe waangalie, je, sasa ni wakati mwafaka yale Mabaraza ya Kata nayo yawe na watendaji wanasheria, wataalam ili sasa tuwaongezee viwango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala hilo haliwezi kuletwa hapa kwa muswada wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na Muswada wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wenyewe huwa ni mahususi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya sheria, technically yale ambayo vipengele vimeleta shida wakati wa utekelezaji. Lakini kwenye masuala yote yanayohitaji maamuzi makubwa ya kisera yanaletwa na muswada mahususi wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu hiyo, nishauri tu kwamba hata hii hoja ambayo Mheshimiwa Mtolea ameisema kwamba angetegemea kwamba ungekuja hapa muswada mahususi, mkubwa kwa ajili ya kuunganisha mifuko hii ya hifadhi ya jamii, hilo nalo lisingeweza kuletwa kwenye muswada huu kwa sababu sasa ni suala la kisera. Imekuwepo mifuko mingi, wewe mwenyewe umesema ni ya utitiri, sasa unaileta iwe pamoja, unaunganisha upi na upi na utakuja na scheme gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila naomba kushauri Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano huu wa Bunge unaoendelea sasa, Muswada huu wa Mifuko ya Hifadhi utasomwa kwa mara ya kwanza kwenye Bunge hili, ambapo pamoja na mambo mengine, utahusika pia na hiyo hoja ambayo Mheshimiwa Mtolea ameisema ya mafao ya kujitoa, itakuwa considered wakati huo, kama haitakuwemo Waheshimiwa Wabunge mtaamua ninyi wenyewe hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali inafanya kazi kwa makini sana. Naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, ninyi kuweni tu macho muisaidie wakati mnaishauri, lakini pia mtoe ushirikiano mzuri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ametushauri Mheshimiwa Mtolea ni linalohusu wepesi wa muswada. Naomba kushauri tena kwamba ndiyo asili ya miswada hii ya mabadiliko ya sheria mbalimbali. Mambo yote kama ungetaka muswada mkubwa unakuja na muswada mahususi, hayo ni mambo ya kisera. Lakini nasema hili zoezi la kutunga sheria ni zoezi endelevu kama ambavyo pia zoezi la kufanya marekebisho ni zoezi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Serikali yenyewe imekuwa kwa kweli pia ikichukua hatua za kufanya marekebisho kwenye sheria hizi kutokana na ushauri inayoupata kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, na haya ndiyo matokeo hata ya muswada huu ambao naona kama Waheshimiwa Wabunge wote mmeunga mkono. Lakini pia niwashauri, kama mnaweza kuleta miswada mingine kwa sababu mnayo mamlaka hayo kama ambavyo Mheshimiwa Mchengerwa ameshashauri, pia msisite kufanya hivyo. (Makofi)

Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Amina Mollel kwa mchango wake mzuri na sisi tunakubaliana na mchango huo na Serikali kupitia Jedwali la Marekebisho imeshafanya marekebisho kwenye hiyo hoja ya walemevu, mlemavu mnataka awe na sifa gani tena ya elimu? Kwa hiyo tumeshaweka pale kwenye jedwali la marekebisho naomba Waheshimiwa Wabunge mtambue hili ukisoma sasa kwenye Jedwali la Marekebisho Serikali imeridhia hayo marekebisho na tumeyaweka hayo marekebisho kwenye Jedwali la Marekebisho sawa sawa na mapendekezo ya Mheshimiwa Amina Mollel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja pia kuhusu kauli ya Mheshimiwa Rais. Kwanza kabla sijakwenda kwenye kauli ya Mheshimiwa Rais niseme hivi, tutofautishe Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi yaani sheria tunayoijadili leo hapa ni Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambayo ndani yake inaunda Mfuko wa Fidia kwa ajili ya wafanyakazi wanaoumia kazini.

Waheshimiwa Wabunge, sasa hii ni tofauti na Mifuko ya Hifadhi za Jamii yaani zile Pension Funds, kwa hiyo hivi vitu navyo lazima tuvitenganishe, leo tuna-deal tu na mfuko. Sheria ya Wafanyakazi ambayo ndani yake kuna mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, mfanyakazi yoyote anayeumia kazini mfuko huu umsaidie, kwa hiyo lakini nimeshalisema hili kwamba sheria inayounganisha mifuko itasmwa kwa mara ya kwanza kwenye mkutano huu wa Bunge lako linaloendelea.

Sasa hii ya Mheshimiwa Rais kauli hii ya kwamba watu wa Mwanza hawatabomolewa kwasababu walimpigia kura; kwanza siamini, hilo la kwanza, lakini la pili ameisema katika context ipi? Sikumsikia mimi hata context yenyewe tuangalie maudhui ya alichokisemea hicho kitu, hapana. Mimi sikumsikia lakini pia hawezi akasema hivyo akimaanisha hivyo, hapana tuchukue context (maudhui) yale maudhui yake. (Kicheko)

Lakini mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, ninyi ndiyo mnatunga sheria hizi muwe makini muwasaidie wananchi wenu kuzingatia hizi sheria wanapojenga na ndiyo maana tunabadilisha hizi sheria za Mipango Miji na kwenye hili la mipango miji nadhani Serikali imejisahau sana. Kama Taifa haliwezi kuendelea kama unakuwa na makazi ambayo hayakupangwa, miji ambayo haikupangwa hivi. Mipango miji na makazi yaliyopangwa vizuri ni kigezo kikubwa sana katika maendeleo na huu ubomoaji unaozungumzwa katika barabara ya Morogoro ile kwanza hiyo sheria iko tangu miaka mingi, hilo la kwanza, lakini la pili hawa watu wana taarifa wanajua waliojenga pale wanafahamu na la tatu, suala hili liko Mahakamani na watu wamekwenda Mahakamani kesi nyingine wameshindwa, wengine wameendelea.

Kwa hiyo, hili suala siyo la kuja kuletwa humu ndani. Kwa hiyo naomba kusema hilo suala, Waheshimiwa Wabunge tuwashauri wananchi wetu waishi kwa kuzingatia sheria, basi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hizi ndiyo hoja za msingi ambazo Waheshimiwa Wabunge wameshazisema na mengine nimeshayajibu.

Kwa mara nyingine tena nakushukuru sana kwa kunipa fursa mimi niweze kuhitimisha hoja hii. Naomba kuwashauri Wabunge waridhie muswada huu tuendelee hatua ya pili. Marekebisho yaliyopo kwenye muswada huu ni ya muhimu sana na tumetoa sababu zake basi naomba kutoa hoja.