Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hussein Mohamed Bashe (21 total)

MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nisikitike na samahani kwa kauli nitakayosema, ni aidha Manaibu Waziri wanapokuja kutujibu au Mawaziri hawako serious, wanatuchukulia for granted ama hawafanyi kazi yao ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Naibu Waziri anasema majengo ni mali ya mkandarasi hayawezi kurejeshwa Serikalini. Anataka kutuambia mimi na Rais tarehe 14 Oktoba, 2015, tuliwadanganya wananchi wa Nzega tukijua kwamba majengo yale ni mali ya mkandarasi na hakutakuwa na chuo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mji wa Nzega una sekondari inayoitwa Bulunde, majengo yalikuwa ya mkandarasi. Je, Serikali utaratibu ule ule iliyotumia kuyapata majengo yaliyotumika kwa ajili ya sekondari ya Bulunde, inakuwa na ugumu gani leo kuyapata majengo yanayotumiwa na mkandarasi anayejenga barabara ya Nzega - Puge ili kuanzisha Chuo cha VETA.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kilichosemwa tarehe hiyo anayoongelea, tarehe ya 14 Oktoba, 2015 ni sahihi na tulichokisema hapa kwenye jibu la msingi ni sahihi, ila tunaongelea vitu viwili tofauti. Tulichokisema hapa ni kwa mujibu wa mkataba na Mheshimiwa Naibu Spika wewe ni Mwanasheria unafahamu. Kama mkataba umesema hivyo na sisi leo tukasema tofauti, tutaiingiza Serikali kwenye hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichosemwa tarehe 14 Oktoba, 2015 na Mheshimiwa Rais akiwa na Mheshimiwa Hussein Bashe kule Nzega nacho bado kilikuwa ni sahihi, mchakato wake ndiyo huo unaoendelea ambao tumeuongelea hapa. Ni kitu ambacho Serikali itakifanya, lakini siyo kwa kulazimisha na kukitoa hadharani.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa msingi wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kutazama uwezo wa Halmashauri, kwamba haina uwezo wa kujenga madaraja haya pamoja na barabara zake, thamani ya madaraja haya mawili ni zaidi ya milioni 800.
Je, Waziri yupo tayari kuthibitishia Bunge lako na wananchi wa Jimbo la Nzega kwamba miradi hii itapalekwa TANROAD kama ambavyo Rais aliahidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na yeye kwamba kwa kulinganisha na bajeti zetu za Halmashauri, fedha hii tu peke yake inaweza ikawa ndiyo bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka mzima kwa barabara zote. Kwa hivyo ni kweli kama anavyosema Mbunge na ndiyo maana pengine Mheshimiwa Rais alisema madaraja haya yapelekwe TANROADS.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali ni moja, na ahadi iliyotolewa fedha zinatoka zote Hazina, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa dhana ya D by D hata kama Halmashauri haina uwezo ama wa kitaalamu au wa kifedha, kazi ya Wizara yangu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni coordination ambapo Wizara nyingine pia zozote zile zinaweza zikachangia ama rasilimali fedha au watu au ujuzi katika kuhakikisha kwamba Halmashauri zinafikia malengo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, hili Mheshimiwa Mbunge lisimpe shida, ndani ya Serikali tutaangalia kama linafaa kufanywa hivyo basi tunaweza tukashirikiana na Wizara ya Ujenzi kuona namna ya kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na commitment ya Serikali kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya sekondari ya Bulunde na kutoa fedha kwa ajili ya sekondari ya Chief Itinginya. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo moja;
Kwa kuwa, jitihada za wananchi na Mbunge wa Jimbo la Nzega ni kumalizaS ya Bulunde ili tuwe na high school, na kwa kuwa, mahitaji ya fedha yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya shule ya Chief Itinginya hayatoweza kumaliza ujenzi wa shule ile kuwa na high school katika sekondari ya Chief ya Itinginya, mahitaji halisi ni shilingi milioni 250.
Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ya Chief Itinginya, ili katika Halmashauri ya Mji wa Nzega tuwe na shule mbili za A-level ?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niseme wazi kwamba, Mheshimiwa Bashe kama nilivyosema pale mwanzo, ninajua una juhudi kubwa sana unaendelea kuifanya pale Nzega na umekuwa kila wakati ukija pale ofisini siyo kwa suala hilo tu, hata suala zima la kukuza uchumi wa maeneo yako ya vibanda pale, lengo ni kwamba mpate mapato muweze kuelekeza katika huduma za kijamii, kwa hiyo lazima tu-recognize juhudi kubwa unayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali kwa sababu mchakato wa bajeti wa mwaka huu umeshapita na bajeti ya mwakani tunaona ni jinsi gani tutafanya. Lengo ni kusukuma nguvu kuwasaidia watu wa Nzega. Ni kweli haiingii akilini eneo kama lile ambapo population ni kubwa, watoto wengi wanafaulu lakini wanakosa fursa ya kusoma.
Kwa hiyo, Serikali tutashirikiana nanyi kwa pamoja, Halmashauri na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia jinsi gani tutafanya kuiboresha Nzega sasa iwe na thamani hiyo ya ukuaji wake wa Mji na Mji wa kihistoria tokea enzi za madini ya almasi, basi watu waone mwisho wa siku wananchi wa Nzega waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba, juhudi ya Serikali tutakaa pamoja tutajadiliana nini kinatakiwa kifanyike na katika muda gani na kuangalia resource zilizokuwepo tuweze kusukuma watu wa Nzega waweze kupata fursa ya elimu.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza naishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Nzega, Mheshimiwa Profesa Muhongo na Mheshimiwa Kalemani wametekeleza ahadi ya kuturudishia machimbo ya Na. 7 na wiki hii wachimbaji wadogo watakabidhiwa maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali moja tu. Mwaka 2005 Rais wa Awamu ya Nne aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Nzega, hasa wa Jimbo la Bukene ujenzi wa kilometa 146 wa Barabara ya kutoka Tabora, kupita Mambali, kuja Bukene, kwenda Itobo, kwenda Kahama na Kilometa 11 kutoka Nzega Mjini kuunganisha mpaka Itobo kuweza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ya mwaka 2014/2015 Serikali ilitenga fedha za upembuzi yakinifu na tenda ikatangazwa, Wakandarasi wote walioomba wakawa wame-bid zaidi. Je, Serikali iko tayari sasa kuongeza fedha ili barabara ile upembuzi yakinifu ukamilike na ujenzi uweze kuanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Bashe kwa kunipa elimu ya kina utofauti kati ya hii barabara anayoongelea ya kutoka Tabora kupitia Mambali – Bukene hadi Kahama na ile ya kutoka Tabora kupitia Nzega Mjini hadi Kahama; ni barabara mbili tofauti na zote zina umuhimu mkubwa kiuchumi katika maendeleo ya eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi za viongozi wa Kitaifa tumekabidhiwa tuliopo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha kwamba tunazitekeleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, barabara hii kama ilivyoahidiwa, pamoja na hii nyingine ya kutoka Nzega hadi Itobo tunazishughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa suala lile la kukamilisha feasibility study na detailed design nimhakikishie Mheshimiwa Bashe kwamba tutawataka TANROADS waliangalie upya ili fedha ziongezwe na kazi ile ifanyike, kwa sababu lengo ni kukamilisha kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadri tunavyoendelea kuahirisha upatikanaji wa Mkandarasi kwa sababu ya bajeti kuwekwa kiwango cha chini, tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wale wanaohitaji huduma ya ile barabara.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mgodi mkuu uliokuwepo katika Mji wa Nzega wa Resolute ulishafungwa na kwenye ripoti ya TMAA inaonyesha Mwekezaji huyu aliondoka na fedha za Halmashauri ya Mji wa Nzega, ten billion shillings ambazo zilikuwa ni service levy: Je, kama Wizara, imefikia wapi kulifuatalia suala hili kuhakikisha haki hii ya wananchi wa Mji wa Nzega inarudi? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Bashe nakushukuru sana. Kama unatukumbusha kwamba kampuni iliondoka na ten billion sasa umetupa taarifa, tutalifanyia kazi. Mimi na wewe pamoja na wataalamu na vyombo vingine tutashirikiana pamoja, tutalifanyia kazi ili pesa ziweze kurejea. Kwa hiyo, nakushukuru Mheshimiwa Bashe. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Igunga pamoja na upatikanaji wa maji kitakwimu wa asilimia 60, lakini kutokuwepo kwa umeme wa uhakika kunapelekea upatikanaji wa maji katika Mji wa Igunga kuwa angalau kwa wiki mara mbili. Je, Waziri ama Serikali wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria, inaweza kutusaidia katika Mji wa Igunga kuwapatia angalau generator ili liwe pale ambapo umeme haupo, basi waweze kupata maji ya uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo la Igunga linafanana sana na tatizo la Mji wa Nzega; na upatikanaji wa maji katika Mji wa Nzega kwa sasa ni asilimia 30 tu ya maji na maji haya yanapatikana kwa wiki mara tatu: Je, Serikali ni lini itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa matenki matano na kuweka chujio la maji katika bwawa la Kilime na pampu ili wananchi wa Mji wa Nzega wasiendelee kupata shida wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza nashukuru amekiri kwamba asilimia 60 ya maji inapatikana katika Mji wa Igunga, lakini tatizo lililopo ni tatizo la umeme. Ameuliza kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, lakini pamoja na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa katika Bunge hili Mheshimiwa Waziri anayehusika na umeme na nishati ameshatupa majibu kwamba sasa hivi kunajengwa umeme wa msongo wa Kilowatt 400 ambapo tatizo la umeme sasa litakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, amependekeza kwamba, katika kipindi hiki kwa sababu ya tatizo la umeme, maji yanapatikana mara mbili kwa wiki, ni vyema tukafanya utaratibu wa kununua generator. Kupitia Bunge lako Tukufu, namwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, aweze kuleta andiko ili tuweze kuangalia uwezekano wa kununua generator iweze kusaidia katika kipindi hiki tunaposubiri kuwa na mradi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia Mji wa Nzega kwamba unapata 30% na maji yanapatikana mara tatu kwa wiki. Je, Serikali ni lini itajenga matenki matano yaliyoahidiwa na Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu kwamba, matenki matano makubwa yanajengwa kupitia huu mradi wa kutoa maji Ziwa Viktoria na kupeleka Miji ya Tabora, Nzega na Igunga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa kwamba matenki hayo yatajengwa kupitia mradi huu, lakini pia, mradi utahusisha ujenzi au upanuzi wa mtambo wa kusafisha na kutibu maji. Kwa hiyo, mradi huu ukikamilika, hoja zote ulizonazo Mheshimiwa Mbunge, zitakuwa zimeshapitiwa.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naomba kumuuliza swali fupi Mheshimiwa Waziri pamoja na jitihada alizozifanya katika Mgodi wa Resolute, Nzega. Je, sasa Serikali iko tayari leseni iliyokuwa chini ya MRI iweze kugawia kwa wachimbaji wadogo wa Mwaishina ambayo maarufu kwa namba saba original katika mji wa Nzega?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lililokuwa likimilikiwa na kampuni maarufu sana ya uchimbaji iliyoanza hapa nchini Resolute lilimilikiwa sasa na Serikali kupitia Chuo chetu cha Madini (MRI). Ni kweli kabisa lengo kubwa la mgodi kumilikisha kwa Serikali ili ku-plan kutoa fursa kwa wanafunzi wa Tanzania ambao wanasoma masomo kwa nadharia waweze sasa kupata eneo kwa kufanya kwa vitendo ndiyo maana tunawagawia eneo lile. Lakini nikubaliane na hoja ya Mheshimiwa Bashe tumeshazungumza naye, tumeshaweka mikakati ili tuone ni eneo gani ambalo Serikali kupitia MRI hawalihitaji ili waweze kugawia wananchi wa Nzega lakini hata hivyo tumechukua hatua mbadala zaidi ya hapo. Mheshimiwa Bashe nikuhakikishie Kampuni ya Zari Exploration imeachia kilometa nyingine kumi karibu na eneo hilo ambao wananchi wako wa Nzega tutawagawia kwa utaratibu wa Serikali.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningeomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la Itobo linafanana kabisa na tatizo la Kata ya Lusu kuwepo kwa kituo cha afya ambacho kilijengwa na ADB chenye vifaa na vitendea kazi vya namna hiyo. Je, Serikali haioni wakati umewadia wa kuhakikisha wanapeleka Wataalam na katika kituo cha afya cha Lusu ili kuweza kutatua tatizo linalowakabili wananchi wa Lusu kwa sababu wanatembea zaidi ya kilometa 20?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kituo cha afya cha Zogolo kilichopo katika Kata ya Nzega ndogo ambacho majengo yake yamekamilika na baadhi ya majengo kwa ajili ya wodi kwa akinamama na theatre yanahitaji kumaliziwa na kituo cha afya kilichopo Kata ya Mbogwe ambacho hutumika kwa ajili ya kuhudumia Kata zaidi ya saba, je, Serikali haioni wakati umewadia wa kutenga fedha kwenda kusaidia nguvu za wananchi katika vituo hivi vya afya vya hizi Kata mbili cha Zogolo na Mbogwe ili wananchi wa maeneo hayo waache kusafiri masafa marefu kwenda kufuata huduma katika hospitali ya Wilaya ya Nzega?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna vituo hivi vilivyojengwa na ADB, kuna kule Itobo, Bukene na kituo cha Lusu. Si hivyo tu hata nilivyofika Masasi nilikuta kuna vituo vimejengwa. Changamoto kubwa ya vituo hivi ni kwamba vina vifaa vizuri sana, tatizo lake ni katika suala zima la wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejielekeza, pamoja na Waziri wa Afya, kuona ni jinsi gani tutafanya katika ajira itakayokuja katika maeneo haya ambayo yana upungufu hasa wa Wataalam wale wa upasuaji na dawa za usingizi ili tukiwapata wataalam hawa tuweze kuwapeleka kwenye vituo hivyo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Hussein Bashe kwamba, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo tumeiwekea kipaumbele na hasa kutokana na vituo hivi kuwa na vifaa vyenye thamani kubwa sana, tusipovitumia kwa sasa vinaweza vikaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili katika mchakato huu unaokuja sasa hivi maeneo yale yote na maeneo mengine ambayo nimetembelea ambapo vituo vile vimejengwa, vitapewa kipaumbele katika upatikanaji wa Wataalam wanaokidhi kwa matumizi ya vile vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchakato utakaokuja maeneo yale yote na maeneo mengine ambayo nimetembelea ambako vituo vimejengwa vitapewa kupaumbele katika upatikanaji wa wataalam wanaokidhi matumizi ya vifaa vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala la kituo cha Zogolo pamoja na Mbogwe, nimesema awali, katika bajeti ya mwaka huu watu walikuwa na malalamiko kwa kusema kwamba hawaoni jinsi gani Wizara ya TAMISEMI imekwenda kuhakikisha kwamba ukarabati umefanyika. Tulisema kwamba kupanga bajeti hizi za kumalizia inaanzia katika ngazi za Halmashauri. Ndiyo maana nimesema pale awali kwamba wiki iliyopita, Wizara ya Afya na TAMISEMI na Kamati ya Bajeti imekaa pamoja kubaini upungufu kama huo. Lengo letu kubwa ni kuja na mpango mkakati mpana zaidi ili kuhakikisha vituo hivi ambavyo vina suasua tutaweza kuvikamilisha wananchi wapate huduma bora.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Kwa kuwa tatizo linalowakabili wananchi wa Mufindi Kusini linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Nzega Mjini; nilitaka kusikia kauli ya Waziri, katika kata ya Migua, jimbo la Nzega Mjini, Kata za Mwanzoli, Mbogwe, maeneo ya Bulunde pamoja na Kashishi yote haya yalikuwa yapekelewe umeme kwa miradi ya MCC na miradi hii imefutwa. Je, Naibu Waziri anasema kauli gani kuwaambia wananchi wa jimbo la Nzega wa maeneo haya juu ya upatikanaji wa uhakika wa umeme katika maneo niliyoyataja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipende tu kusema wazi kwamba miradi yote iliyokuwa chini ya MCC ambayo haikuendelea sasa itapelekewa umeme kwa bajeti ambayo tumeipitisha kupitia mradi wa REA wa Awamu ya Tatu ikiwemo pamoja na vijiji kwa Mheshimiwa Bashe alivyovitaja kwenye jimbo lake. Lakini niseme tu, kijiji cha Kashishi tulishaanza kufanyia survey lakini pia vijiji vya Mbogwe na vingine vya karibu tulishaanza kuvifanyia survey na vyote vitapelekewa umeme kwenye kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Bunge lako mimi nitatembelea kwa Mheshimiwa Kigola mara tukimaliza Bunge, pia nitatembelea kwa Mheshimiwa Bashe na maeneo mengine kuhakikisha maeneo yote yanapata umeme.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru. Nilitaka kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shilingi bilioni 5.2 ni sawa sawa na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa zaidi ya miaka mitatu, na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Nzega haina uwezo wa kifedha na ndio ilikuwa mantiki ya kumuomba Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na baadaye Rais John Pombe Magufuli kwamba miradi hii ya ujenzi wa kilometa 10 iende chini ya TANROADS.
Je, sasa Serikali iko tayari kuwaambia wananchi wa Jimbo la Nzega kwamba miradi hii ya kilometa 10 itajengwa chini ya utaratibu wa TANROADS na si kwa kutumia fedha za Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli nafahamu Halmashauri ya Mji wa Nzega mapato yake ni madogo, na Mheshimiwa atakumbuka takribani wiki tatu na nusu au wiki nne tulikuwa wote kule Nzega tukihamasisha shughuli za maendeleo. Nipende kumshukuru sana kwa juhudi kubwa anazozifanya katika Jimbo lake
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishieni kwamba hii ni commitment ya Serikali na ahadi ya Mheshimiwa Rais. Katika hivi ukiachia hata huo uchache wa mapato, hata ujenzi wa miundombinu katika maeneo mengine tunayoyafanya hivi sasa si kwamba Halmashauri hizo zinauwezo huo.
Mheshimiwa Spika, si muda mrefu tutaanza mchakato hata katika Mji wa Mpwapwa na maeneo mengine mbalimbali hapa nchini. Naomba nisema wazi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa makusudi imeamua kubadilisha miundombinu ya Manispaa na Majiji ya maeneo mbalimbali, na ndiyo maana utakuta katika miji mikubwa, Manispaa na Halmashauri za Miji sasa hivi mitandao ya barabara imeimarika.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Bashe amepata fursa kubwa, ambapo Mamlaka ya Mji wake vile vile tayari umesha-qualify sasa kuingizwa katika mipango ya ujenzi wa barabara za lami. Kwa hiyo, naomba nimtoe hofu, Serikali itahakikisha ahadi ya Mheshimiwa Rais inatekelezwa, tunajua mapato yenu ni madogo. Lakini pia ni commitment ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhakikisha kwamba miji yote inajengewa barabara za lami. Ondoa hofu Serikali itatekeleza hilo kwa kadiri iwezekanavyo.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa maeneo mengi ambayo wawekezaji wakubwa wamewekeza wameacha athari kubwa katika maeneo hayo na mojawapo ni Wilaya ya Nzega katika Mgodi wa Resolute, wananchi wameachiwa mashimo makubwa bila manufaa yoyote. Je, Serikali sasa iko tayari kumnyima mwekezaji Kampuni ya Resolute, certificate ya kumruhusu kuondoka nchini ambayo anatakiwa apewe mwezi wa sita kabla hajalipa deni ambalo anadaiwa la shilingi bilioni 10 na Halmashauri ya Mji wa Nzega?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Kampuni ya Resolute ilifunga mgodi wake miaka mitatu iliyopita. Katika utaratibu wa uchimbaji, mgodi unapoanza huwa kuna Mine Closure Plan. Kwa hiyo, wakati wanafunga mradi, kampuni ilitakiwa kutekeleza Mine Closure Plan, lakini sambamba na hilo, huwa inapewa certificate ya ku-close mgodi. Sasa Wizara ya Mazingira pamoja na NEMC wanalifanyia kazi suala hilo, watakapokamilisha taratibu Mheshimiwa Bashe utashirikishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi ni kwamba je, ni kwa nini Serikali haioni sababu ya kuwanyima certificate? Ni jambo ambalo namwomba Mheshimiwa Bashe avute subira, watu wetu wa NEMC na Mazingira wanalifanyia kazi. Nitambue ushiriki wako Mheshimiwa Bashe kwa wananchi wa Nzega. Niseme tu sambamba na hilo, ili kuwawezesha wananchi wa Nzega wapate maeneo na kuondokana na athari, mara baada ya taratibu za mazingira kukamilika, maeneo ambayo yaliachwa na Resolute ambayo yako wazi, yatamilikishwa kwa wananchi wako ili waweze kupata shughuli za kufanya kazi.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kujenga Taifa la Viwanda na sekta ya kilimo kuwa ni muhimu. Katika Halmashauri ya Mji wa Nzega tumekuwa na mradi uliokuwa unasimamiwa na Shirika lililokuwa linaitwa NZEDECO miaka ya 1970 na miaka ya 1980 la umwagiliaji katika Kata ya Idudumo, mradi huu sasa hivi umekufa. Vilevile katika Halmashauri ya Mamlaka Ndogo ya Mji wa Igunga nako katika Bwawa la Imamapuli limejaa tope.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali iko tayari
kuhakikisha kwamba miradi hii miwili katika Halmashauri hizi mbili katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 wanatenga fedha kwa ajili ya kuifufua miradi hii ili wananchi wa maeneo hayo waweze kufaidika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ipo miradi mingi ambayo inaendelea nchi nzima na ni kwamba ni suala la Wizara yenyewe kuweka vipaumbele kwa sababu katika miradi huwezi ukatekeleza yote kwa wakati mmoja kutokana na upatikanaji wa fedha.
Na kama anasema kwamba je, tuko tayari kutenga fedha kwa mwaka huu wa fedha unaokuja; itategemeana na mawasilisho ya Wilaya ya Nzega, kwa sababu ninyi ndio mnaleta mapendekezo na vipaumbele katika Wilaya yenu.
Kwa hiyo, kama mkiweka hii ndio kipaumbele Serikali basi itaangalia namna ya kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mwaka 2010 wananchi wa Jimbo la Nzega waliahidiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kilometa 10 za lami ndani ya Mji wa Nzega. Mwaka 2014, Waziri wa Ujenzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa aliwaahidi tena mbele ya Rais Kikwete ahadi hiyo hiyo. Mwaka 2015 Rais wa sasa, Rais John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Nzega ujenzi wa Daraja la Nhobola na kilometa kumi za lami ndani ya Mji wa Nzega. Waziri wa TAMISEMI ndani ya Bunge hili mwaka 2016 akijibu swali langu la msingi alisema Serikali inashughulikia ujenzi wa Daraja la Nhobola katika bajeti ya 2016/2017 na Naibu Waziri Ngonyani katika Bunge lililopita aliahidi daraja hili litajengwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Naibu Waziri anijibu ni lini ahadi ya daraja hili itatimizwa katika Halmashauri ya Mji wa Nzega? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Hussein Bashe na wananchi wa Nzega kwamba ahadi zilizotolewa na viongozi mbalimbali ama ndani ya Bunge kwa kujibu maswali, wakati wa ziara ama wakati wa kampeni kuhusu ujenzi wa hayo maeneo mawili aliyoyasema, ujenzi wa kilometa kumi pamoja na daraja la Nhobola maana yake hii siyo mara kwanza kuliuliza hili suala, nikuahikikishie kama ambavyo tumekuhakikishia siku za nyuma kwamba ahadi hii itatekelezwa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimhakikishia Mheshimiwa Mbunge hilo, na ni kweli tulisema kwamba tungeweka kwenye bajeti ya 2016/2017 na unafahamu kwamba bajeti ni mchakato, kikubwa nachokwambia ni kwamba Serikali itatekeleza ahadi hii ya viongozi mbalimbali pamoja na sisi ambao tumekuwa tukijibu maswali hapa kwa niaba ya Serikali.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninauliza swali moja la nyongeza.
Kutokana na ripoti ya BOT latest ya mwezi Juni, inaonesha kwamba export volume yetu imeshuka kutoka dola milioni 4.5 mpaka dola milioni 3.8 wakati huo huo prices za commodities kwenye soko la dunia imeendelea kushuka na import volume yetu ya capital goods imeendelea kushuka.
Je, Serikali ina mpango gani kutokana na variables hizi zote nilizozitaja kuhakikisha kwamba, miezi mitatu mpaka sita ijayo stability ya shilingi yetu inaendelea kuwa imara kwa sababu indications zote zinaonesha kwamba, shilingi yetu inaendelea kushuka kila siku kutokana na hali ya uchumi na uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa
Naibu Spika, kama ambavyo amesema ni kweli kwamba export volume yetu imeshuka, na mimi katika jibu langu la msingi nimesema katika miezi ambayo Taifa letu huwa linapanda katika exportation ni kuanzia Julai mpaka Disemba na ndio kipindi hiki. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Bashe kwamba ndani ya kipindi hiki kwa sababu ndio tunazalisha na tunavuna export yetu itapanda muda siyo mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimesema kwenye jibu langu la msingi kwamba tuendelee kuiunga dhamira ya Serikali yetu, Tanzania ya Viwanda ndiyo itakayotuwezesha kuongeza export volume yetu na kuweza kupunguza importation ya bidhaa ambazo tutazizalisha ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kumuunga Mheshimiwa Rais wetu katika dhamira yake hii na sisi kama wasaidizi wake tuko imara katika kumsaidia kuhakikisha kwamba, thamani ya shilingi yetu inaendelea kuimarika na export volume kulingana na viwanda ambavyo tayari sasa vimeanza kufanya kazi, itaongezeka muda siyo mrefu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nilitaka nimpe Taarifa tu Mheshimiwa Hussein Bashe kwamba, katika record za hivi karibuni nchi yetu ina reserve nyingi na ina over five months of imports kutokana na credibility ya Government Policy. Kwa maana hiyo, kushuka kwa imports wala hakujaathiri sana matarajio ya kuharibika kwa ustahimilivu wa mfumuko wa bei kutokana na kwamba, Serikali ina reserve nyingi za kutosha na kwa maana hiyo export zitakapokuwa zimeongezeka zitakutana na reserve za kutosha ambazo hazitaleta uharibifu wowote kwenye mbadilishano wa fedha pamoja na mfumuko wa bei. (Makofi)
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri au niombe tamko la Serikali, kwenye bajeti mwaka huu tulitaka Halmashauri zote ambazo ni class three ambazo zina madeni Serikali Kuu kupitia funds zinazokusanywa na EWURA zipelekwe Wizara ya Maji ili madeni hayo walipwe. Leo ni wiki ya pili Halmashauri ya Mji wa Nzega imezimiwa umeme na TANESCO kwa sababu ya madeni yaliyotokana na Serikali Kuu kutokupeleka fedha za utilities kwenye Halmashauri kwa miaka mingi.
Je Serikali iko tayari leo kuitaka TANESCO iweze kuruhusu watu wa Nzega waweze kupata maji?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Bashe. Tumetoa maelekezo na tumeshakaa na wadau wote kwamba taasisi zote muhimu za Serikali; afya, maji, usalama na maeneo mengi waje tukae tuweke utaratibu. Hatukati umeme kama tumeshaweka utaratibu, lakini tukishaweka utaratibu halafu utaratibu ukakiuka kwa kweli sisi tunakata umeme. Nichukue nafasi hii tutakaa na Mheshimiwa Bashe na Waheshimiwa wengine tuone namna gani ya kulifanya jambo hili ili wananchi waendelee kupata maji.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mwaka 2010 na mwaka 2015 kwa maana ya uchaguzi wa mwisho wa kumchagua Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wananchi wa Jimbo la Nzega waliahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete, vilevile ahadi hiyo imekuja kutolewa na Mheshimiwa Rais Magufuli, ya ujenzi wa daraja la Nhobola. Mwaka wa jana Desemba Mheshimiwa Rais aliwahakikishia wananchi wa Jimbo la Nzega kuwa daraja hilo linajengwa kwa commitment iliyotolewa na Wiziri wa Ujenzi. Je, ni lini daraja hilo litajengwa. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anayoyaongelea Mheshimiwa Hussein Bashe kuhusu Daraja hili Nhobola na amekuwa akiliulizia mara kwa mara, na sisi tumekuwa tukimjibu mara kwa mara kwamba tunashughulikia kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, lakini ni ahadi ambayo ilirudiwa na Mheshimiwa Rais wa sasa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Pamoja nisingependa kusema lini, lakini nimhakikishie kabla ya miaka hii haijaisha daraja hili tutakuwa tumelitekeleza kama ambavyo viongozi wetu waliahidi. (Makofi)
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo. Tatizo la maji katika Halmashauri ya Mji wa Nzega ni kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyokuwepo toka miaka ya 70 na mwaka jana Desemba tulipata ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kutatua tatizo hili. Tukapokea millioni 200. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wananchi wa Mji wa Nzega juu ya utekelezaji wa milioni 200 ambayo tumekuwa tukiisubiri toka mwezi wa Nne mwaka huu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Nzega. Milioni 200 tumeshaitoa na tumekabidhi kwenye Mamlaka ya Maji ya Tabora na mradi huo wameshaukamilisha tayari. Kwa sasa tunajiandaa kuwapatia milioni 200 nyingine ili waendelee kuboresha miundombinu ya Mji wa Nzega. Pia kupitia mradi mkubwa huo uliosainiwa juzi wa kutoa maji kutoka Solwa kupeleka Nzega na Tabora miundombinu itakarabatiwa pia. (Makofi)
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimshukuru Waziri kwa utekelezaji wa mradi wa visima katika Jimbo la Nzega. Naomba kujua mwaka 2015 moja ya hadi kubwa ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kufufua skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Idudumo katika Halmashauri ya Mji wa Nzega. Je, ni lini ahadi hii Serikali itaanza utekelezaji wake kwa ajili ya kulipitia na kulirekebisha bwawa hilo na kutekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na napenda nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge juu ni lini utekelezaji. Miradi ya utekelezaji wa umwagiliaji inategemeana na fedha. Fedha zitakapopatikana ka wakati na sisi tutatekeleza kwa wakati katika kuhakikisha mradi huu unakamilika. Ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na kazi kubwa mnayofanya, je, mko tayari sasa kwenda katika Halmashauri ya Mji wa Nzega na kulifanyia tathmini bwawa ambalo limekuwa likitumika kwa ajili ya umwagiliaji katika Kijiji cha Idudumo ili kuweza kulirudisha katika hadhi yake na miundombinu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa yote ambayo utendaji wake unasuasua baada ya kukamilisha mpango kabambe, nia yetu ni kuhakikisha wananchi wanalima mara mbili, mara tatu kwa mwaka. Tutakwenda na tutalifanyia kazi vizuri.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na shukurani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Nzega kwa kutatua tatizo la umeme katika chanzo cha maji katika Mji wa Nzega, Wizara ya Nishati nilitaka tu nipate kauli ya Waziri ama Naibu Waziri. Mradi wa REA Phase III katika Jimbo la Nzega unasuasua; mkandarasi ameonekana site mara moja alipokuwepo Waziri na kuweka nguzo. Hata hivyo mpaka sasa nguzo zile zimesimama vile vile na maeneo ambayo aliahidi kuwasha umeme mpaka leo hayajawashwa. Ni lini mradi huu utapata speed ambayo wananchi wa Jimbo la Nzega wanaitarajia?(Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Bashe anavyotupa ushirikiano kati ka kupeleka umeme kwenye Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, nitangulie tu kusema, kwa sasa Wakandarasi katika Jimbo la Nzega wanafanya kazi katika vijiji 11 na katika Jimbo la Mheshimiwa Bashe wanakamilisha kazi katika maeneo ya Migua karibu kabisa na Ziba katika Jimbo la Igunga. Kwa hiyo nimwambie tu Mheshimiwa Bashe kwamba vile vifaa vyote ambavyo vilikuwa vinasubiriwa kuja ikiwepo nyaya na transfoma vimeshafika tangu juzi; na sasa hivi katika Jimbo la Mheshimiwa Bashe kuna transifoma 12 zimewekwa juzi. kwa hiyo nimpe uhakika Mheshimiwa Bashe na wananchi wa Nzega kwamba kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji 32 katika Jimbo lake litakamilika kabla ya mwezi Julai mwaka ujao. (Makofi)
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na kuishukuru Serikali kwa mradi wa maji wa Ziwa Victoria na mradi wa visima 25 katika Jimbo la Nzega, sasa nilitaka nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutupatia commitment Halmashauri ya Mji wa Nzega kupatiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 katika mwaka wa fedha unaokuja ili kukamilisha mradi wa maji katika Vijiji vya Mhogola, Monyagula, Migua, Itangili, Igilali, Mwanzoli na Kitengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kifupi kwanza, nimpongeze Mbunge, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo lake la Nzega, lakini kubwa tunatambua utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, nimwombe basi tukutane mimi na yeye, pamoja na Wataalam wetu wa Wizara, tuangalie namna gani tunaweza tukasaidiana. Ahsante sana.