Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Selemani Jumanne Zedi (11 total)

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mwaka jana Bunge lililopita mwezi wa nne niliuliza swali hili hili la kufuatilia ujenzi wa minara hii na jibu nililopewa lilikuwa kwamba, kazi ya ujenzi imeanza na mpaka Waziri wa Mawasiliano wakati ule alinipa barua ya commitment ambayo nilikwenda kuwaonesha wananchi lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote ambacho kimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nataka kujua inakuaje makampuni ya simu...
MWENYEKITI: Swali la pili eeh?
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Inakuwaje Makampuni ya Simu pamoja na ruzuku wanayopewa kutoka kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa wote yanashindwa kukamilisha ahadi zao?
Swali la pili, Serikali ilituambia kwamba imebaini Makampuni ya Simu yanakuwa reluctant, ni wazito kwenda kujenga minara vijijini kwa sababu ya kifaida kwamba hakuna faida wanapoweka minara vijijini na wakasema kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watahakikisha kwamba, minara ya vijijini inajengwa kwa ruzuku ya 100%.
Je, mpango huo upo? Unaendelea na kama unaendelea ni vijiji gani ambavyo wameshabaini na vitanufaika kwa mpango huo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwenye Bunge hili mwaka 2014/2015, tulisemea maeneo hayo na ni kweli kwamba Makampuni mengi ya Simu, Airtel, Tigo, Vodacom, Zantel wanachelewesha kupeleka mawasiliano vijijini. Kwa mantiki hiyo ndiyo tuliamua kuleta Halotel au Viettel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini haraka. Kwa mtazamo huo huo kuanzia mwezi Mei mwaka huu mpaka mwezi Oktoba mwaka huu, Kampuni ya Halotel au Viettel itajenga takribani mawasiliano kwenye vijiji 1800. Tunaamini na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vilevile vitapata huduma hiyo.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara ambayo aliifanya katika Jimbo hili hivi karibuni na vijiji vyote vilivyotajwa kwenye swali hili vya Mwangoye, Mambali na Mbutu, Mheshimiwa Naibu Waziri alivipitia na kutoa maelekezo maalum kwa TANESCO, REA na CHICCO…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zedi, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni kwamba kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kijiji cha Mwangoye, Mambali na Mbutu, jambo ambalo limefanya wananchi wengi kufanya wiring na kuwa tayari na fedha ya kulipia, lakini kuna upungufu mkubwa wa nguzo na vifaa vya kuunganishia.
Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutumia forum hii kutoa agizo au kauli maalum kwa watendaji wa REA, TANESCO na CHICCO kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Mwangoye, Mambali na Mbutu ambao wameshajiandaa kupata umeme wanapatiwa nguzo na vifaa vya kuunganishiwa ili waweze kupata huduma muhimu ya nishati?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu niongeze maelezo kwenye shukrani alizotoa na mimi namshukuru sana Mheshimiwa Zedi kwa pongezi na shukrani za kuunga mkono. Nampongeza sana pamoja na wananchi wa Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye swali lake, kimsingi siyo swali lakini anataka wananchi wake wapate uhakika. Ni kweli kabisa nguzo zinaendelea kwenda Bukene katika vijiji vyote vitatu na katika mwezi ujao wananchi wapatao 50 watapatiwa umeme kwa sababu nguzo wameshapelekewa.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa lengo la kuchangia gharama za ujenzi wa minara maeneo ya vijijini, lakini bado speed ya ujenzi wa makampuni haya umekuwa mdogo sana, kulikuwa napendekezo kwamba sasa Mfuko wa UCSAF ugharamie asilimia 100 ya ujenzi wa minara katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto kwa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefikia wapi katika kuona umuhimu huu wa kwamba Mfuko wa UCSAF ugharamie minara ya vijijini kwa asilimia 100 badala ya kuyaachia makampuni ambayo kwa kweli yamekuwa mazito kupeleka minara vijijni kwa sababu hakuna mvuto wa kibiashara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia kuanzia asilimia kumi mpaka asilimia 100; inategemea eneo na eneo. Kama eneo hilo halina mvuto wa kibiashara kabisa mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia asilimia 100. Kuna tatizo ambalo limejitokeza ni kweli makampuni ya simu yamechelewa kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali na kwa kulijua hilo sasa Serikali itapiga faini makampuni ya simu yote ambayo yamechelewa kupeleka mawasiliano kwenye maeneo hayo. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri na hasa wazo la ku-design nyumba moja ambayo itaweza ku-accommodate Walimu sita kwa maana familia sita. Sasa swali langu ni kwamba je, Serikali haioni sasa kwamba kuna umuhimu wa kusambaza hii ramani ya design hii ambayo nyumba moja inaweza ika-accommodate Walimu sita kwa Halmashauri zote na maelekezo maalum ili shule ambazo zipo vijiji sana Halmashauri ziweze kutumia ramani hii na kujenga nyumba? Kwa sababu ukiweza kujenga nyumba mbili tu maana yake tayari ume-accommodate Walimu 12?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri katika Jimbo analozungumza Mheshimiwa Mbunge na mimi nilikuwa kule. Aliponiagiza yeye mwenyewe nitembelee Jimbo lake; nikatembelea miradi ya afya na kuona mambo mengine na changamoto za miundombinu. Naomba niseme ushauri huu tumeshaufanyia kazi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha ramani hizi zinakwenda kila Halmashauri. Tunachokifanya ni kuhakikisha tunaweka mkazo sasa, bajeti yoyote inayopatikana lazima tuelekeze katika mfumo wa ramani mpya ambayo kwa kiwango kikubwa ina tija sana katika Halmashauri zetu kuhusu suala la kupunguza tatizo la upungufu wa nyumba za Walimu katika Halmashauri zetu.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli huyu mshauri yuko site na kazi hii inaendelea, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa sababu barabara hii ilivyo sasa katika Miji ya Bukene na Itobo inapita katikati ya miji na kwa mfano Bukene ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami tutalazimika kuvunja Kituo cha Afya, jengo la Polisi, tanki kubwa la maji, ma-godown makubwa na kuvunja nyumba nyingi tu cha wananchi.
Je, Serikali itakuwa tayari kutoa kauli itakayoondoa hofu na itakayofanya kuepusha fidia kubwa kwamba usanifu huu ujumuishe kuichepusha barabara hii katika miji ya Bukene na Itobo ili isipite katikati ya Miji ya Bukene na Itobo ili kuondoa kwanza fidia kubwa ambayo itatokea baada ya kuvunja taasisi nyingi hizi na nyumba nyingi za wananchi?
Je, Serikali iko tayari kutoa kauli ili wananchi wa Bukene na Itobo wawe hawana hofu kwamba barabara hii itachepushwa pembeni ya miji hii na kuondoa gharama zote hizi ambazo zitajitokeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana hii barabara ambayo inatoka Tabora - Mambali kuja Itobo. Niseme tu kwamba upo utaratibu kwa upande wa Serikali wa kuangalia hizi gharama wakati tukisanifu hizi barabara. Kwa hiyo, niseme kwamba tutazingatia ushauri wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo geni kwa sababu zoezi hili tumelifanya katika Mji wa Nzega, kuna mchepuo; tumefanya katika Mji wa Urambo, kuna mchepuo; lakini pia tumezingatia tulivyosanifu barabara ya kule Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe wasiwasi na niwatoe wasiwasi wananchi wa Bukene kwamba tutazingatia wakati tunakamilisha zoezi la usanifu wa barabara.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza linahusu tafsiri ya kijiji kwenye huu usambazaji wa maji. Ninataka kujua anaposema maji yatafika Kijiji ya Ilagaja, Kijiji cha Ilagaja kina Vitongoji kumi. Je, maji yatafika makao makuu tu ya kijiji au katika vitongoji vyote kumi vinavyounda Kijiji cha Ilagaja?
Swali la pili, sasa maji haya yatakapofika Nzega na kwa sababu maeneo yetu ya Bukene yana shida ya water table kupata maji kutoka chini. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuanza mipango ya muda wa kati ili maji haya sasa yatakapofika Nzega yatoke Nzega yafikishwe Bukene ambako ni umbali wa kilometa 40?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameomba tafsiri kwamba maji yatafika Kijiji cha Ilagaja, je, vitongoji itakuwaje?
Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo letu ni kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanawafikia wananchi wote. Yatatoka Nzega ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, yataenda Ilagaja yakifika pale basi tutaendelea kuyaendeleza kwenda mpaka kwenye vitongoji mpaka kwenye point ya mwisho ili wananchi wote eneo la Ilagaja na vitongoji vyake wapate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na labda tu nizungumze kwamba ndio maana katika bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji tunatenga fedha kwa kila Halmashauri. Bomba la KASHWASA maji ya kutoka Ziwa Victoria yakishafika kwenye kitongoji kwa upande wa Halmashauri kile ndio chanzo cha maji, zile fedha tunazotenga basi muendeleze mpeleke kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, jibu lake ni hivyo hivyo kuwa yakishafika pale basi Halmashauri kile ndio chanzo, watenge fedha waunganishe kutoka pale kwenda kwenye maeneo ambayo hayana maji. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutupatia shilingi milioni 800 ambazo maboresho makubwa ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega yanaendelea. Sasa nataka kuuliza kwamba Serikali mna mpango gani na Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene ambavyo vina tatizo kubwa sana la wodi. Je, baada ya kumaliza maboresho ya Hospitali ya Wilaya, mtakuwa tayari sasa kuelekeza nguvu kwenye Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kimsingi tutakuwa tayari kama ambavyo tumekuwa tayari siku zote. Hatua kwa hatua tukimaliza vituo hivi ambavyo tumeanza navyo tutakwenda na Vituo vingine vya Afya.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana taarifa kwamba mchakato huu wa kuomba Mji wa Bukene upandishwe hadhi ulianza siku nyingi na mpaka Wizara ikatoa GN Namba 176 ya mwaka 1996 ambayo mpaka sasa haijafanyiwa mchakato wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye swali langu la msingi niliuliza, je, muundo wa kuwa na Kata moja inayoundwa na Kijiji kimoja tu ni sahihi? Kwa sabbau muundo huu unapelekea Mtendaji wa Kijiji kutokuwa na tofauti yoyote na Mtendaji wa Kata na Serikali ya Kijiji haina tofauti yoyote na WDC na ni sawa sawa na kuwa na Mkoa mmoja unaoundwa na Wilaya moja tu ambayo kutakuwa hakuna tofauti yoyote ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa, kwa sababu mkoa ni mmoja na Wilaya ni mmoja. Je, muundo huu ni sahihi kuwa na Kata moja ambayo inaundwa na Kijiji kimoja tu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza ananiuliza kama najua kwamba kuna GN ambayo ilikuwa imetolewa na kwamba mpaka sasa hivi GN hiyo haijafanyiwa marekebisho yoyote, taarifa hiyo ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anauliza uwezekano wa Kijiji hicho kimoja kikawa Kata, naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selemani Zedi anajua kwamba ilikuwa mchakato wa kupandisha Kijiji cha Bukene kuwa Halmashauri ya Mji Mdogo na Bukene kama ilivyo ina vitongoji vyake 11 na lengo lilikuwa hivyo Vitongoji vije vibadilike kuwa Mitaa ambayo ingeweza kutosha katika kubadilisha sasa kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bukene. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Selemani Zedi, taratibu hizo zingine ziendelee ili ukifika wakati ambapo Serikali itakuwa tayari kuongeza maeneo ya kiutawala na Bukene iwe na sifa ya kuweza kuongezeka.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Madini kwa uamuzi wake wa kuyagawa au kutoa leseni za wachimbaji wadogo kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa yana leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni kwamba kwa kuwa maeneo haya ambayo yalikuwa na leseni za utafiti za wachimbaji wakubwa yameshafanyiwa utafiti na Serikali ina taarifa za utafiti zinazoonesha wapi kuna madini, yako kiasi gani, yako umbali gani na kadhalika. Je, ili kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo waliopewa maeneo haya wasichimbe kwa kubahatisha na hatimaye kuingia hasara, Serikali iko tayari ku-share, kuwapatia wachimbaji hawa hizo taarifa za utafiti wa haya maeneo ili wachimbaji wadogo wawe wanachimba kwa uhakika wakijua hapa kuna madini na kuondokana na hali iliyopo sasa hivi ambapo wanachimba kwa kubahatisha na hatimaye wanapata hasara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kampuni kubwa na za kati ambazo zinamiliki maeneo ambayo ni ya utafiti sisi sasa hivi kama Serikali tumeamua kuyarudisha, kwa yale maeneo ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi, tumewarudishia wachimbaji wadogo waweze kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amehoji kwa nini tusiwape data zile wachimbaji wadogo kwa ajili ya kuzitumia kwa maana ya kuchimba bila kubahatisha. Ni kwamba Geological Survey of Tanzania (GST) ambayo iko chini ya Wizara yetu ina ripoti nyingi za maeneo mbalimbali ya uchimbaji. Tunawaomba wale ambao walikuwa tayari wameshaanza kufanya utafiti watupe zile data walizozipata katika maeneo waliyofanyia utafiti. Kwa kweli data tunazo, kwa wachimbaji wanaotaka kupata geological data au report kutoka GST waje wafuate taratibu na watapewa data hizo na waweze kuchimba bila kubahatisha waweze kujipatia tija katika uchimbaji.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongezea Serikali kwa kazi ambayo imefanywa kwenye barabara hii. Kimsingi wakati naandika swali hili, kuliwa hakuna kazi yoyote ambayo imefanyika, lakini sasa hivi nakubaliana kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Mshauri Mhandishi NIMETA Consult ameshaanza kazi, nami mwenyewe ni shuhuda nimemwona akifanya kazi hii ya usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa kuwa Serikali imesema kazi ya usanifu wa kina inaisha mwezi Juni, 2019 na hii barabara ni ahadi ya Rais na pia ni jambo ambalo lipo kwenye ilani:-

Je, Serikali inaweza ikatoa kauli hapa kwamba barabara hii kwa kuwa usanifu utakuwa umekamilika mwezi Juni, sasa kwenye bajeti ijayo itatengewa fedha ili Mkandarasi wa kuanza kujenga aanze kazi kabla ya Awamu hii ya Tano haijamaliza muda wake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea pongezi kwa moya wa dhati kabisa lakini napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Selemani Zedi kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana kipande cha barabara hii iliyotajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali na nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote nchini kwanza zimepitika na pili zinaunganishwa kwa kiwango cha lami. Nimhakikishie Mheshimiwa Zedi kwamba barabara yake kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kama ahadi ya Mheshimiwa Rais, tutaijenga kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020 kwisha.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, hili eneo la Sojo Kata ya Igusule ambako pameamliwa kujengwa kiwanda hiki liko jimboni kwangu na wananchi wametoa hekari 400 ili kupisha ujenzi wa kiwanda hichi muhimu. Na kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa waziri wamesema mwezi wa tisa ambayo ni miezi minne tu kutoka sasa mkandarasi anakabidhiwa eneo.

Je, nilitaka kujua kwamba Serikali inaweza kutoa commitment kwamba ndani ya kipindi hichi cha miezi minne kabla mkandarasi hajapewa hilo eneo wananchi wote waliotoa hekari 400 watakuwa wamelipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na yeye pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mradi huu mkubwa wa ujenzi wa bomba hili la mafuta na tija yake kwa wananchi wa maeneo yake hayo, kwa eneo ambalo limechaguliwa kujenga kiwanda cha kuunganisha mabomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimdhibitishie Mheshimiwa Mbunge moja ya kazi muhimu ambayo imefanyika ni kutambua mkuza ambako bomba litapita na tunatambua bomba hili ambalo litakuwa na urefu wa kilometa 1445 na zaidi ya kilometa hizo 1147 ziko upande wa Tanzania, Serikali yetu kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na TPDC imetambua ule mkuza na imeshafanya tathimini ya mali mbalimbali ambazo ziko katika huo mkuza ikiwemo eneo hilo la ujenzi wa kiwanda hichi cha courtyard.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimthibitishie tathmini imekamilika na kwa kuwa tupo katika hatua nzuri ya mazungumzo ya Host Government Agreement baada ya hapo tutaenda Share Holders Agreement na kasha kufanya maamuzi ya investment decision na hatua zote hizi zipo katika mchakato wa miezi hii ambayo imesalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge na kwa utashi wa viongozi wetu Marais wan chi mbili hizi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven wa Uganda kwamba mwezi wa tisa utakapoanza mradi huu wananchi wote watakaopisha mkuza huu wa bomba watakuwa wamefidiwa kwa sababu tathmini ile imekamilika na sasa yapo tu mapitio ya mwisho ambayo yanafanywa baina ya Wizara ya Nishatu wataalamu, TPDC, Wizara ya Ardhi, Maendeleo Nyumba na Makazi na taasisi nyingine za Kiserikali. Nikushukuru sana.