Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mussa Ramadhani Sima (11 total)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. GIMBI DOTTO MASABA) aliuliza:-
Tanzania inakabiliwa na tishio la mabadiliko ya tabianchi linalosababishwa na uchafuzi wa mazingira, hasa wa viwandani:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wamiliki wa viwanda wanaokiuka Sheria za Mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Doto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mhesimiwa Mwenyekiti, tatizo la mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kikubwa linasababishwa na uzalishaji wa gesi joto unaotokana na matumizi ya nishati kwa 47%, uzalishaji wa viwanda kwa 30% na usafirishaji 11% kwa shughuli za maendeleo katika nchi zinazoendelea kiviwanda hususan Ulaya, Marekani, Asia na Australia. Bara la Afrika kwa ujumla linachangia gesi joto kiasi kisichozidi 3%. Tanzania huzalisha kiasi cha tani 0.09 za hewa ukaa (Per Capital Emission) kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Tanzania inachangia kiasi kidogo sana katika tatizo la uzalishaji wa gesi joto ambazo ndiyo chanzo cha mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, pamoja na kuchangia kidogo kiasi hicho Tanzania imeendelea kuathirika kutokana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kama vile kupungua kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro, kuongezeka kwa usawa wa bahari, ukame, mafuriko ya mara kwa mara na mlipuko wa magonjwa. Tatizo kubwa linatokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya viwanda nchini kwa kutiririsha majitaka yenye sumu na kemikali ambazo huathiri sana viumbe hai pamoja na mazingira kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inayo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004. Sheria hii imeweka misingi ya usimamizi, tathmini na kuchukua tahadhari kuhusu madhara kwa mazingira, yakiwemo ya viwandani. Kwa kuzingatia sheria hii, Serikali imekuwa ikielimisha na kuwatoza faini wamiliki wa viwanda wanaokiuka sheria hii. Aidha, wamiliki wanaoendelea kukaidi maelekezo na masharti wanayopewa hufungiwa kufanya shughuli na hupewa masharti kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuzingatia utekelezaji wa sheria na mikakati mbalimbali iliyopo kwa ajili ya kuwezesha usimamizi endelevu wa hifadhi ya mazingira kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Wamiliki wa viwanda wanatakiwa kuhakikisha Tathmini ya AAthari kwa Mazingira na Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit) vinafanyika na kuzingatiwa. Aidha, wamiliki wa viwanda wanapaswa kutumia nishati rafiki kwa mazingira na kutumia teknolojia banifu katika uzalishaji wa bidhaa zao ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Upo uharibifu mkubwa wa mazingira katika Ukanda wa Ziwa Rukwa unaotokana na ukataji miti ovyo, wingi wa mifugo na kilimo kisichozingatia utaalamu; shughuli hizi zinahatarisha kukauka kwa ziwa hilo kwa miaka ijayo:-
Je, Serikali ina mpango gani madhubuti na wa haraka kunusuru ziwa hilo, hasa ikizingatiwa kuwa imegundulika gesi ya helium katika ziwa hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo Oktoba, 2016 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alifanya ziara ya kutembelea Mkoa wa Rukwa na moja ya maeneo aliyotembelea ni Bonde la Ziwa Rukwa ambapo alitoa maelekezo ya kuanza mchakato wa kulitangaza Ziwa Rukwa kama eneo nyeti la mazingira kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kutangaza eneo hilo kuwa eneo nyeti unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa kwa 2018. Eneo hilo litakapotangazwa rasmi kuwa eneo nyeti litakuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mzingira (NEMC) ambalo kwa kushirikiana na wadau litaandaa mpango wa matumizi ya eneo husika hivyo kuongeza nguvu ya usimamizi wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri alielekeza Halmashauri zote ambazo zina eneo katika Bonde la Ziwa Rukwa kuweka alama za kuonesha mwisho wa umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo za Ziwa Rukwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kuweka mabango ya kukataza shughuli zinazoharibu mazingira ndani ya umbali huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa eneo la Bonde la Ziwa Rukwa limebainika kuwepo kwa dalili ya gesi ya helium. Tathimini ya Athari ya Mazingira imefanyika katika hatua hii ya utafiti ili kuweza kubaini athari na madhara yoyote yanayoweza kutokea wakati wa zoezi hilo.
MHE. SAADA SALUM MKUYA aliuliza:-

Kumekuwa na changamoto mbalimbali katika Muungano ambazo zinaendelea kutatuliwa mojawapo ikiwa ni ajira za Muungano ziwe asilimia 21 kwa upande wa Zanzibar.

(a) Je, ni kwa kiasi gani makubaliano hayo yametekelezwa hadi sasa?

(b) Je, ni ajira ngapi zimepatikana kwa utaratibu huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba nichukue fursa hii sasa kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Utaratibu uliokubalika ni kwamba ajira katika taasisi za Muungano zinatakiwa kuwa kwenye uwiano wa asilimia 79 kwa watumishi wa Tanzania Bara na asilimia 21 kwa watumishi wa Zanzibar kwa utumishi wa ngazi ya utaalamu. Katika kutekeleza utaratibu wa muda wa mgao wa nafasi za ajira (quota) katika taasisi za Muungano kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Rais ilipewa kibali cha nafasi tatu, mtumishi mmoja alipangwa Zanzibar ikiwa ni asilimia 33 na watumishi wawili walipangiwa Tanzania Bara sawa na asilimia 67.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilipewa kibali cha nafasi 28 za Maafisa Mambo ya Nje na kati ya nafasi hizo saba zilijazwa na Watumishi kutoka Zanzibar ikiwa ni asilimia 25 na nafasi 21 zilijazwa na watumishi kutoka Tanzania Bara ikiwa ni asilimia 75.

(b) Tangu kufikiwa kwa makubaliano ya uratatibu wa muda wa mgao wa ajira katika Taasisi za Muungano mwaka 2013/2014 na kuanza kwa utekelezaji wa utaratibu huo mpaka sasa jumla ya wazanzibari 8 kati ya 31 wameajiriwa katika taasisi za Muungano ambao ni sawa na asilimia 25 ya waajiriwa hao. Taasisi za Muungano zina mwongozo wa utekelezaji wa makubaliano hayo na zinaendelea kuzingatia utaratibu huo wanaopata fursa ya kuajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo huu ulianza kutekelezwa mwaka 2013/2014 lakini utekelezaji wake umekumbwa na changamoto ikiwa ni kusitishwa kwa ajira Serikalini kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 kutokana na kupisha zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa na watumishi wenye vyeti feki. Hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa taasisi zote za Muungano zilipewa utaratibu huo na zitaajiri watumishi kama ilivyoelekezwa.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI aliuliza:-

Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF) hutolewa kila mwaka kwa Majimbo yote ya Uchaguzi Tanzania lakini fedha hizi zimekuwa zikichelewa sana kutolewa kwa upande wa Zanzibar tofauti na Tanzania Bara:-

Je, ni sababu zipi za msingi zinazofanya fedha za mfuko huo kuchelewa kupelekwa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Haji Ali, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Majimbo ya Uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na makubaliano hayo, Sheria Na.16 ya mwaka 2009 ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo katika kifungu cha 3 inamtaja Waziri anayehusika na Mfuko huo kuwa ni Waziri anayehusika na masuala ya Serikali za Mitaa.

Aidha, kifungu cha 4(2) cha Sheria kinasema kwamba, kwa upande wa Tanzania Bara ni Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa na kwa upande wa Zanzibar ni Waziri anayehusika na masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010, Ofisi ya Makamu wa Rais ameratibu na kufuatilia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa upande wa Zanzibar. Mchanganuo wa mgawanyo wa fedha kwa kila Jimbo kulingana na vigezo vilivyoainishwa vya idadi ya watu katika Jimbo, ukubwa wa eneo na kiwango cha umaskini hufanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kuwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zinatakiwa kufuata utaratibu wa mgawanyo kama nilivyoeleza. Utaratibu huo ni kama ifuatavyo: Fedha zinatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango (SMT), baada ya kutolewa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanya mchanganuo wa kila Jimbo, mchanganuo huo huwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo huwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango ya SMZ. Wizara ya Fedha na Mipango ya SMZ ndiyo inayoingiza fedha kwenye akaunti za majimbo ya Zanzibar. Hivyo, ni dhahiri kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha ucheleweshaji wa fedha ikilinganishwa na fedha zinazotolewa katika majimbo ya Tanzania Bara. Hata hivyo, jitihada za makusudi zinafanyika ili kuhakikisha fedha hizo zinaingia kwenye akaunti za majimbo ya Zanzibar kwa wakati.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati mifereji ya maji ya mvua na kuta za mito inayoingiza maji ya bahari katika Mji wa Mikindani ili kuirejesha katika hali yake ya awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 129(1) kinaeleza wajibu wa kila mamlaka ya Serikali za Mitaa kwenye eneo lake itajenga au kuandaa mifereji ya maji ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kumekuwepo na changamoto ya kujaa kwa maji katika maeneo mengi nchini yanayopakana na bahari kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kufanya baadhi ya mifereji kushindwa kumudu athari zake. Kufuatia hali hii, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeanza kuchukua hatua zinazolenga kuzuia na kupunguza madhara yaliyojitokeza katika maeneo yaliyoathirika nchini ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya jumla ya maeneo haya ikiwemo Mikindani ili kuwezesha kuandaa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ipo katika hatua za kuandaa Mpango Endelevu wa Kitaifa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plans) wenye malengo ya muda wa kati na muda mrefu ili kuboresha usimamizi wa mabadiliko nchini kwa kushirikiana na halmashauri zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi, tunashauri halmashauri za maeneo husika kuingiza gharama za ukarabati wa mifereji kwenye bajeti zao ili kupunguza athari zilizozidi kuongezeka kwa kuiga mfano wa Jiji la Dar es Salaam.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Moja kati ya majukumu ya kuimarisha Muungano ni pamoja na kuhakikisha kuwa kero zote za Muungano zinatatuliwa; na vikao vingi vimekaa na kujadili kero hizo:-

Je, ni kero ngapi tayari zimetatuliwa na zipi ambazo hadi sasa zimeshindikana kupatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo zimekwishapatiwa ufumbuzi ni 11 kati ya 15 zilizowasilishwa na kutafutiwa ufumbuzi. Changamoto nne zilizobaki zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi na hakuna changamoto iliyoshindikana kupatiwa ufumbuzi. Dhamira ya Serikali zetu zote mbili ni kumaliza changamoto zote zinazoukabili Muungano wetu ili uendelee kuwa nguzo pekee ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

Matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini yamekuwa na athari kubwa kwenye uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa miji yetu:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondoa matumizi ya plastiki hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka hasa kutokana na mifuko hii kutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mbalimbali. Aidha, kutokana na baadhi ya nchi jirani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuruhusu uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ya nchi, kumekuwa na wimbi kubwa la uingizaji wa mifuko ya plastiki nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hali hii na mwelekeo wa Jumuiya ya Kimataifa wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki, Serikali inadhamiria kusitisha uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeanza kuchukua hatua zifuatazo katika kuelekea kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki:-

(a) Kuhamasisha wajasiriamali, vikundi vya akinamama na vijana, sekta binafsi na viwanda kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala ikiwemo vikapu vya asilia, mifuko ya karatasi na vitambaa;

(b) Ofisi imeendesha mikutano miwili ya wadau katika Mikoa ya Dar es Salaam tarehe 6 Novemba, 2018 na Mwanza tarehe 18 Novemba, 2018, kuelimisha umma kuhusu changamoto na athari za mifuko ya plastiki na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala kutokana na dhamira ya Serikali kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikutano hii, wadau na wananchi waliishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuchukua fursa hii, kwa mara nyingine tena kuhimiza viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki na wadau wengine kujitayarisha kwa kubadili teknolojia na kutathmini fursa zinazojitokeza katika kuzalisha mifuko mbadala hasa katika kipindi hiki cha mpito wakati taratibu za maamuzi ya Serikali zikikamilishwa.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD (K.n.y. MHE. ABBAS A. H. MWINYI) aliuliza:-

Changamoto za Muungano wetu bado zipo licha ya vikao vya Kamati za pamoja kati ya SMT na SMZ kukutana mara kwa mara:-

(a) Je, ni changamoto zipi zilizopata ufumbuzi tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani?

(b) Je, changamoto hizo ni ngapi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka 2019 Serikali ya Awamu ya Tano iliyoingia madarakani, changamoto mbili zimepatiwa ufumbuzi. Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kipindi cha Serikali Awamu ya Tano ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na kutoa VAT kwa asilimia sifuri kwa umeme unaouzwa na TANESCO kwa ZECO ikiwa ni pamoja na kufuta deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi bilioni 22.9 kwa umeme uliouzwa kwa ZECO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuitisha vikao vya kisekta, kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizobakia na zinazoendelea kujitokeza. Sekta hizo ni Sekta ya Fedha, Uchukuzi, Biashara, Mifugo, Uvuvi na Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizojadiliwa ni pamoja na Taarifa ya Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa mapato yanayotokana na faida ya Benki Kuu, usajili wa vyombo vya moto, upatikanaji wa fursa za masoko Tanzania Bara, ushirikiano kati ya Taasisi ya Viwango na Zanzibar (ZBS) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Zanzibar (ZFDA), ZBS kupatiwa nakala ya usaili kiwango cha Afrika Mashariki ili kurahisisha usaili wa kiwango hicho kwa wakati; Leseni za viwanda, Zanzibar kuwa designated member country wa mashirika ya African Regional Intellectual Property Organization (ARIPO) na World na World Intellectual Property Organisation (WIPO) na upatikanaji wa fursa za miradi inayohusisha maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa kwa maendelo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo miradi inayohusu maendeleo ya wajasiriamali na kuzuiwa kwa bidhaa ya maji ya kunywa inayozalishwa Zanzibar kuingia Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali zote mbili za SMZ na SMT zimeendelea kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili yanatekelezwa na kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa ipasavyo.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD (K.n.y. MHE. MBAROUK SALIM ALI) aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa Watanzania hususan kizazi kipya, kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kutoa uelewa wa pamoja na dhamira njema za Muungano huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salum Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba, karibu asilimia 80 ya kizazi cha sasa kimezaliwa baada ya Muungano na hivyo kuna haja ya kutoa elimu ya Muungano kwa wananchi wote, hususan vijana wa Kitanzania. Elimu hii ni muhimu kwa mustakabali wa Muungano kwani inaongeza ari ya uraia, uzalendo na kujenga undugu wa Kitaifa kati ya wananchi wa pande mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2018/2019, ofisi imetoa elimu ya Muungano kupitia vipindi vya redio na television, ili kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata elimu ya Muungano, hususan vijana. Katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, shughuli za elimu ya Muungano, hususan kwa vijana, zilitolewa kupitia kongamanko la vijana, hususan fursa zilizopo katika Muungano ambapo ilifanyika Zanzibar tarehe 22 Oktoba, 2017. Wanafunzi wa shule za msingi zilizopo Dodoma ilifanyika tarehe 18 Aprili, 2018 na Kongamano la Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo Dodoma, itafanyika tarehe 21 Aprili, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ofisi ilishiriki katika maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia tarehe 31 hadi tarehe 6 Juni, 2018, ambapo wananchi walipata fursa za kujulishwa kuhusu masuala ya Muungano. Pamoja na kazi hizo, ofisi ilishiriki katika vipindi vya redio, television na magazeti katika kutoa elimu ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua faida zitakazopatikana kwa kutoa elimu ya Muungano, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, itaendelea kutoa vipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 na imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya Muungano kwa vijana kupitia makongamano na warsha, ambayo yamelenga wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Zanzibar.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF) aliuliza:-

Zanzibar kwa namna ilivyo inahitaji uchumi wa Visiwa ambapo Bandari ni kitu cha lazima:-

Je, Serikali ya Muungano inaungaje mkono nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga Bandari kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Bandari Na. 17 ya mwaka 2004 (The Ports Act No. 17), majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ni kuendeleza bandari, kuendesha shughuli za bandari, kutangaza huduma za bandari na kushirikisha na kusimamia sekta binafsi katika uendelezaji na uendeshaji wa bandari.

Aidha, Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) lilianzishwa kwa Sheria ya Bandari ya mwaka 1997, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, ZPC ina majukumu ya kuendeleza bandari, kuendesha shughuli za bandari na kutangaza huduma za bandari ndani na nje ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Nyongeza ya Kwanza imeorodhesha Mambo ya Muungano ambapo kipengele cha 11 katika orodha ya Mambo ya Muungano kinahusu Bandari, mambo yanayohusika na usafirishaji wa anga na posta na simu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo hayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya uendelezaji wa bandari nchini. Ushirikiano huo umedhihirika zaidi katika kupanga miradi ya kipaumbele na kutafuta fedha za uendeshaji wa miradi hiyo kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Washirika wa Maendeleo. TPA na ZPC zimeendelea kushirikiana kwa utaalam na kushirikiana katika kutoa huduma za bandari nchini hususan katika uongozi wa meli kutoka nje ya nchi. Aidha, tunaendelea kuboresha ushirikiano kupitia vikao vya mara kwa mara vya Sekta za Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiunga mkono nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga bandari kubwa ili kuimarisha miundombinu na huduma ya bandari nchini.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MARTHA M. MLATA) aliuliza:-

Je, ni kwa nini Sherehe za Muungano zimekuwa zikifanyika na kupewa nafasi kubwa Kitaifa tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Moses Mlata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo-

Mheshimiwa Spika, Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huazimishwa kwa kuzingatia Mwongozo wa Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa wa mwaka 2011 uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndiyo ina dhamana ya kuratibu sherehe zote za Kitaifa. Aidha, katika Mwongozo huo, Sura ya Tano katika maelezo ya Utangulizi imeelezwa kuwa “Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitafanyika tarehe 26 Aprili ya kila mwaka katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salam mahali ambapo udongo wa Tanganyika na Zanzibar ulichanganywa. Sherehe hizo zinaweza kufanyika nje ya Dar es Salam kama Kamati ya Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa itakavyoelekeza”

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzingatia Mwongozo huo wa Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa hadi hapo kutakapokuwa na sababu za msingi zitakazofanya Mwongozo huo kufanyiwa marekebisho kwa nia ya kuuboresha. Hata hivyo, Serikali inahimiza wananchi kuadhimisha sherehe hizo kwa kufanya shughuli mbalmbali za maendeleo ikiwemo usafi, michezo, makongamano na shughuli mbalimbali za kijamii.