Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Answers from Prime Minister to Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (1 total)

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa magari na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukiri kwamba wanapungukiwa sana magari, vitendea kazi pamoja na ofisi. Vilevile wana upungufu mkubwa wa rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, siku za karibuni, kwenye upande wa Jeshi la Polisi ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamejitiokeza utaratibu ambapo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanalitumia Jeshi la
Polisi kuwalinda wao binafsi wakati kuna matatizo makubwa ya kiulinzi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni hili, nikitoa mifano halisi, katika Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha analindwa na section nzima ya Jeshi la Polisi, ana motorcade, ana ving‟ora asubuhi mpaka usiku. Sasa magari kama mawili au matatu yanamhudumia Mkuu wa Mkoa na section nzima ya Jeshi la Polisi ambayo ina askari tisa na ving‟ora na hata Wakuu wa Wilaya wamejipa utamaduni huo sasa.
Je, ni nini itifaki ya Kitaifa kuhusu ulinzi wa Viongozi kama hata hawa Mawaziri wenyewe hawalindwi na Askari, lakini Wakuu wa Mikoa leo wanajilundikia Askari badala ya Askari kwenda kwenye lindo, ma-OCD wote siku hizi hawafanyi kazi ya ulinzi wanafanya kazi ya kulindana na kufuatana na Wakuu wa Wilaya. Tunaomba Wizara watueleze leo, ni nini sera ya Serikali kuhusu itifaki hii na matumizi mabaya ya Jeshi la Polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye utendaji wa kazi kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya, Mkuu wa Mkoa ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, panapokuwepo na jukumu hasa ambalo linapohusisha shughuli za kiulinzi na nje ya ofisi, ni sahihi Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya kuambatana na timu yake kwenda katika eneo husika. Inapotokea Mkuu wa Mkoa anakwenda ofisini kwake ama Mkuu wa Wilaya anakwenda ofisini kwake, maana yake OCD ama RPC ama wengine na wenyewe watakuwa kwenye ofisi zao. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi kwa mazingira ambayo nimekuwa nikipewa ni pale ambapo hawa viongozi wanakwenda katika eneo la tukio ambalo linahusisha ulinzi na usalama. Huo ndiyo muogozo kwamba kama wanaelekea katika eneo ambalo linahusisha ulinzi na usalama ni sahihi viongozi hawa kwenda na timu zao kwa sababu ni mambo ya kiusalama na sehemu ya kutolea maelekezo, lakini siyo wakati wa kwenda ofisini on daily routine, unless kama wanafanya hivyo itakuwa maeneo ambayo kila mmoja anaenda kwenye ofisi na ofisi hizo ziko katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa maelekezo haya, ni kwamba viongozi hawa wanapokwenda kwenye majukumu ambayo yanahitaji maelekezo na ni ya kiulinzi na usalama na wao ndio Wenyeviti wa Ulinzi na Usalama itifaki inataka hawa watu wawe na hao viongozi kwa ajili ya maelekezo ya site, lakini wanapoenda kazini na hawa viongozi wengine nao wanaendelea na majukumu yao.