Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ahmed Ally Salum (6 total)

MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-
Majibu ya Serikali ya Swali Na.1 la tarehe 6 Septemba, 2016 yanapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli aliyoitoa wakati akiwa kwenye kampeni katika Jimbo la Solwa:-
(a) Je, kwa nini Serikali inapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ahadi zote za Mheshimiwa Rais unafanyika kupitia mpango wa bajeti iliyotengwa kila mwaka. Hivyo, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali haipingani na agizo la Mheshimiwa Rais na kwamba Hospitali hiyo itajengwa kama agizo lilivyotolewa. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kuhakikisha ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika jibu la msingi la Swali Na.1 la tarehe 9 Septemba, 2016, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa Hospitali ile, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 40 kutokana na ukomo wa bajeti kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kutekeleza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani, ambapo tunatarajia kuongeza nguvu ya kibajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. AZZA H. HAMAD (K.n.y. MHE. AHMED ALLY SALUM) aliuliza:-
Miradi ya maji ya World Bank katika Jimbo la Solwa imesimama kwa
sababu ya Wakandarasi kutokulipwa fedha zao kwa muda mrefu sasa:-
Je, ni lini Serikali itawalipa Wakandarasi fedha zao ili miradi hiyo ikamilike.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la
Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi ya maji ikiwemo miradi ya
Jimbo la Solwa ilisimama kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji mpaka sasa imeshatuma fedha
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kiasi cha shilingi bilioni 1.17 kwa ajili
ya kuwalipa Wakandarasi kulingana na hati zao za madai walizowasilisha. Kwa
sasa wakandarasi wote wanaojenga miradi ya maji katika Halmashauri ya
Shinyanga Jimbo la Solwa wanaendelea na kazi katika Vijiji vya Mendo,
Nyashimbi, Mwanamadilana na Mwakitolyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutuma fedha katika
Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Shinyanga kwa kadri fedha
zitakavyopatikana ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyokusudiwa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-
Majengo mengi yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Solwa kama vile vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na zahanati yako katika hatua za mwisho kukamilika.
Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kukamilisha majengo hayo ili yaweze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Solwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamejenga kwa nguvu zao vyumba vya madarasa 37, nyumba za walimu 33 na zahanati 38 ambazo zipo katika hatua mbalimbali.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 695.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyoanza kwa nguvu za wananchi katika sekta ya elimu na afya. Hadi sasa Halmashauri imeshapokea shilingi 420,881,000 ambazo zimepelekwa katika ukamilishaji wa miundombiinu ya elimu na afya.
Vilevile Serikali imeongeza fedha za ruzuku ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 1.2 zilizotengwa katika Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi shilingi bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 42 kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi. Kulingana na muongozo wa asilimia 50 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika katika miradi ngazi ya Halmashauri na asilimia 50 zinatakiwa kutekeleza miradi hiyo katika ngazi ya vijiji.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-

Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga aliahidi ujenzi wa Vituo viwili vya Afya katika Jimbo la Solwa:-

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inayoelekeza kuwa na Kituo cha Afya kila Kata sambamba na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za viongozi wa Kitaifa. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yenye Jimbo la Solwa ilipewa kipaumbele na kutengewa shilingi milioni 900.0 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa Kituo cha afya Tinde, kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Samuye kilichogharimu shilingi milioni 500. Vituo hivyo vimekamilika na vimeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni miongoni mwa Halmashauri 67 zilizoidhinishiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Fedha zote zimepokelewa na ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ahmed Ally Salum Mbunge wa Solwa kuwa ahadi za viongozi zitaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-

Katika Jimbo la Solwa tayari kuna maboma 158 ikiwemo shule za msingi, sekondari na afya na tayari tumeomba fedha ili kukamilisha maboma hayo:-

Je, ni kiasi gani cha fedha Jimbo hilo limepata ili kukamilisha maboma hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya kukamilisha maboma 2,392 ya shule za sekondari ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 87.5 kwa ajili ya kukamilisha maboma saba ya shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na ukarabati/ujenzi wa vituo vya afya na zahanati 352 kwa gharama ya shilingi bilioni 184.6 ambapo kipaumbele ni ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi. Ukarabati wa vituo 352 unahusisha ukamilishaji wa maboma 199 ya vituo vya afya na zahanati.

Katika Halmashauri ya Wilaya Shinyanga, Serikali imefanya ukarabati wa Kituo cha Afya Samuye na Tinde kwa gharama ya shilingi milioni 900. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 140 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-

Usanifu na upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Mwanza – Solwa – Bulige kwa kiwango cha lami umekamilika:-

Je, ni lini mradi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Solwa – Kahama yenye urefu wa kilometa 150 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ilikamilika Desemba, 2017 kwa gharama ya shilingi milioni 798.8.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha Serikali sasa ni kuunganisha Makao Makuu ya Mkoa na nchi jirani kwa barabara za lami zilizoainishwa kwenye Shoroba za Maendeleo (Development Corridor). Barabara nyingine ikiwemo ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Solwa – Kahama itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara hii ili ipitike majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zimetengwa.