Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jumanne Kibera Kishimba (10 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya 2016/2017. Kwanza napenda kukupongeza wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa ndani ya Bunge hili. Vile vile napenda kutoa shukrani nyingi kwa wapigakura wangu wa Jimbo la Kahama kwa kunipatia kura nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita sehemu moja ya kuongeza mapato. Ni sehemu ngumu kidogo, lakini naomba nichangie na naomba Waziri wa Fedha kama anaweza kunisikiliza ni vizuri akanisikiliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania imezungukwa na nchi nyingi ambazo zina madini na maliasili nyingi na nchi hizi zinategemea nchi yetu ya Tanzania kupitishia madini haya na maliasili hizi. Vile vile zinategemea kuuza nchi za nje kupitia hapa kwetu. Ninachoomba kwa Waziri wa Fedha, kama anaweza kutukubalia, nitatoa mfano wa nchi ya Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Burundi imekuwa iki-export dhahabu tani tatu mpaka tani nne kwa utafiti unaoonesha, lakini nchi hii ina migogoro mingi ya vita na haina machimbo au mgodi wowote wa dhahabu, lakini sisi nchi yetu ina amani, ina dhahabu nyingi, imezungukwa na nchi nyingi kama Congo, Mozambique; nchi hizi zote zinataka kuuza madini yao hapa. Kuna madini ya almasi, nickel, copper, aluminium na madini zaidi ya 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, na madini haya sisi si watumiaji. Tungeomba kwenye bajeti hii, kwa kuwa haiingiliani na bajeti hii, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama atakubali yaruhusiwe yawe zero wakati wa ku-export yawe one percent. Kwa hesabu ya harakaharaka Tanzania inaweza kupata kwa wiki tani mbili na nusu za dhahabu, maana yake kwa mwezi tutapata tani kumi na mbili na nusu zikiwa za sisi nyumbani na za watu wa nje. Kama tuta-charge kwa one percent kwa bei ya leo ya Dola 40 kwa gram au Dola 40,000 kwa kilo, tutapata zaidi ya Dola milioni 500. Dola milioni 500 kwa exchange ya harakaharaka ni trilioni moja kwa mwezi, hiyo ni kwa madini ya aina moja. Tukichukua madini mengine haya yaliyobaki yanaweza kutuchangia zaidi ya bilioni 900 kwa mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua one percent pia kwenye hiyo tutakuwa karibu tuna bilioni tisa kwa mwezi. Kwa hiyo, total itakuwa na bilioni 20 kwa mwezi na pesa hii haiingiliani na Bajeti ya Serikali, ni pesa ambayo ipo tukikataa au tukikubali yenyewe iko vile vile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, attendance ya watu hawa wakija kuuza madini lazima asilimia 20 ya pesa zao wafanye shopping hapa. Kama watafanya shopping asilimia 20, maana yake watatuachia sisi bilioni 400. Bilioni 400 maana yake tutakua sisi kwa asilimia 18 ya VAT ya vitu vilivyoingia nchini ambavyo watanunua hapa, Serikali itakuwa imepata bilioni 40 tena zaidi. Kwa hiyo, madini haya yatakuwa yametuchangia zaidi ya bilioni 70 kwa mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mahali ambapo Bajeti ya Serikali itakuwa imeguswa. Ni kiasi cha Waziri wa Fedha kusema kesho kwamba, sawa amekubali na watu hawa wanaanza kupita. Maana yake hata bila kukubali au namna gani hawa watu wanaendelea kupita hapa, wanahangaika kutoka hapa mpaka Dubai kwenda kuuza; kutoka Congo mpaka Dubai ni karibu masaa tisa, lakini kuja hapa ni masaa mawili. Kwa hiyo ingekuwa vizuri Waziri wa Fedha akaliangalia sana suala hili. Suala hili ndio utajiri wa hawa tunaowaomba pesa leo na ndio wanaotunyanyasa, lakini pesa zote zimetokana na njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya, sisi hatuyatumii, yanakwenda yote Ubeligiji, yanakwenda Dubai, yanakwenda Singapore, yanakwenda China, yanakwenda Hong Kong na mwisho wake sisi tunakwenda kuwaomba pesa wao. Ingekuwa vizuri, tukarekebisha sera yetu ili madini haya yaweze kutusaidia sisi hapa na jirani zetu waweze kugeuza hapa kuwa Dubai ya kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, kwa madini haya tutapata wageni zaidi ya 10,000 kwa mwezi. Wageni hawa ni wageni ambao wana pesa, maana yake hakuna mtu anayebeba madini akiwa hana pesa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatarajia Sekta zote zitapata pesa kuanzia Usafirishaji, TRA, Uhamiaji, maduka, nyumba za kulala wageni, zote zitapata pesa na itatusaidia vile vile, kutuongezea na kutufungulia mlango mpya wa biashara ambao sisi hatukuwa nao. Sisi tumeelekeza zaidi kwenye utalii na nafikiri huu unaweza kuwa ni utalii mpya. Kwa namna hiyo, inaweza ikamsaidia Waziri wa Fedha akawarudishia na Wabunge pesa tunazozozana hapa za posho kama ataweza kukubaliana na wazo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo mchango wangu ni huo, asante sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KIBERA J. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri pole sana kwa misukosuko unayopitia. Uchumi ni soko gumu sana hasa uchumi wa dunia ya tatu na nchi maskini kama Tanzania na hasa kuwatoa kwenye maisha waliyozoea kwa miaka 25 ni kama kumwachisha mtoto ziwa, lazima kuwe na mgogoro mkubwa, vuta subira!
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu, kwanza ni maoni kuhusu Serikali kuruhusu madini yetu na ya nje ambayo yanazalishwa na wachimbaji wadogo yawe asilimia zero wakati wa kuingia, kutoka iwe asilimia moja, itatusaidia sana kama nilivyochangia kwenye mchango wa bajeti mwezi wa Saba ulio kwenye Hansard ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa Kariakoo ni wachangiaji wazuri wa uchumi kwenye importation, lakini tatizo lao kubwa liko kwenye vitu viwili: Suala la TBS kwa product ambazo siyo chakula. Mfano, Redio ya sh. 5,000 wanataka iwe na ubora, lakini wananchi wananunua na wanasikiliza habari au muziki; wanawasumbua na ukizingatia mali nyingi inanunuliwa na watu wa Malawi, Mozambique, Zambia, Congo na majirani wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tariff kwa bidhaa kwa mfano, Colgate gram 100 inauzwa sh. 2,000, Colgate herbal 100 inauzwa sh. 8,000. Kwenye tariff zinaitwa (Toothpaste) TRA anavyothamini ni sh. 8,000, muagizaji kaagiza kwa sh. 2,000, hapo ndipo mzozo unazuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufikiria upya suala la license kwenda kwenye mafuta ili kukusanya fedha kwenye ma- grader, tractor, generator na mashine nyingi, zitapunguza pia rushwa za barabarani.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nitaenda moja kwa moja kwenye Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yangu ilipata hati safi kwenye ukaguzi wa CAG vile vile kwenye mwenge tulikuwa washindi wa pili au wa tatu. Lakini kitu cha kushangaza ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri inaonyesha tuna upotevu wa zaidi ya milioni 200 na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najaribu kujiuliza hapa kwamba inawezekanaje tuna hati safi kwenye mwenge tumekuwa wa pili au wa tatu lakini mkaguzi wa ndani kwenye ripoti ambayo ninayo hapa anaonyesha tuna upotevu wa zaidi ya milioni 200 na zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi Mkurugenzi wetu wa Halmashauri ameendelea kuwaburuza Madiwani kwa kutumia ubabe kiasi ambacho ameweza kuidhinisha ujenzi wa jengo la mamalishe lenye thamani ya shilingi milioni 200. Jengo hili kwa gharama ya shilingi milioni 200 lina mapato ya shilingi 120,000 kwa mwezi. Kwa hiyo faida ya kurudisha jengo hili litachukua zaidi ya miaka 200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba waziri atakapokuwa anafanya majumuisho ajaribu kuangalia kama Serikali inakopa pesa, pesa hizo hizo milioni 200 ilizokopa kwenye mabenki ya ndani kwa riba ya asilimia kumi yenyewe italipa milioni 20. Ni vipi imeipatia Halmashauri ikajenga jengo la milioni mia mbili itapata return baada ya miaka 200 na itapata shilingi milioni 1.4 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha ubadhirifu huo unaoendelea kwa hao watu wanaitwa wateule wa Rais, Mkurugenzi huyu mpaka leo amekataa kutoa statement za benki, Mkuu wa Wilaya hawezi kumhoji, TAKUKURU hawezi kumhoji, Mkuu wa Mkoa hawezi hata sisi kamati ya fedha amekataa na kichekesho hapa ninapoongea anaendelea kupiga machinga wote wa Kahama. Namshukuru Mkuu wa Polisi amekataa kutoa polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mji wetu wa Kahama watu walioajiriwa hawafiki watu 200, na mji ule una watu zaidi ya laki tano, ni kweli watu hawa watafanya shughuli gani? Hata hivyo Mheshimiwa Rais alisharuhusu machinga na watu wa kawaida waendelee na shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Jafo wakati anafanya majumuisho ajaribu kutueleza tutafanya nini au tushitaki wapi sisi? Maana hatuna sehemu yoyote ambayo tunaweza kulalamikia. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naipokea hoja yako vizuri nafikiri Mheshimiwa Jafo uko hapo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli sisi ni Wabunge, lakini mtu ambaye anasema yeye ni mteule anapojaribu kuwa- disturb watu waliokupigia kura anatupa sisi wakati mgumu sana. Tunajaribu kila namna kutafuta pesa kutoka kila kona, ili tusaidie watu wetu, lakini mtu anafika anakataa au ana- misuse hizi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna ongezeko la wanafunzi kwenye kidato cha kwanza zaidi ya asilimia 200; kwenye darasa la kwanza tuna ongezeko la asilimia 200 pia, tuna upungufu wa matundu 2,000 ya choo, lakini Mkurugenzi huyu amechukua pesa hizo milioni 200 amepeleka kwenye jengo la mama lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hivi ninavyoongea Mheshimiwa Jafo ulipokuwa Naibu Waziri ulitoa agizo kwamba, wakati Wabunge wako Bungeni Kamati za Fedha zisikae, lakini yeye anaitisha Kamati ya Fedha kesho, ameongeza shilingi milioni 40 tena kupeleka kwenye jengo hili kwa ajili ya kuweka vigae. Kwa hiyo, naomba sana mtusaidie maeneo haya ni maeneo ambayo yanatupa matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu naomba Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Kakunda kwa kuwa mlifika Kahama mtufikirie sana suala letu la Manispaa. Ni kweli mji wetu umekua, mmeuona kwa macho na matatizo tuliyonayo. Mkitusaidia Manispaa itatusaidia vile vile kwa tatizo la barabara ambalo kwa sasa ni tatizo letu kubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa shukrani nyingi kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Elimu.

Kwanza napenda kutoa shukrani nyingi kwa Serikali kwa kutoa elimu ya bure kutoka darasa la kwanza mpaka la kumi na kbili. Mpango huu wa elimu bure umetusaidia sana kupunguza kero nyingi majimboni kwetu pia Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya Tanzania kama haitafanyiwa mabadiliko makubwa itaendelea kuwa chanzo cha mateso, umaskini kwa wazazi, watoto na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu. Wakati wakoloni walipoleta elimu zaidi ya miaka 100 iliyopita walikuwa na maana nzuri sana, leo baada ya mabadiliko makubwa ya dunia, uchumi na teknolojia kwa ujumla wake ni vigumu sana kuendelea na mfumo wetu wa elimu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwa nchi ya Uingereza; wanapomaliza wanafunzi mfano, milioni moja kutakuwa na retirement ya wafanyakazi karibu laki tisa au laki tisa na nusu ambao ni asilimia 90 mpaka 95. Kwa hiyo, wale wanafunzi laki moja ambao watakuwa hawana ajira watakuwa chini ya Serikali wanaweza kulipwa na kutafutiwa kazi polepole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu, wakimaliza wanafunzi milioni moja kutoka chuo na shule zote watakaopata kazi ni wanafunzi 50,000. Kwa maana hiyo ajira yetu ni asilimia tano peke yake ya wanafunzi. Kwa tofauti hii ya uwiano wa ajira kati ya waliotuletea mfumo huu wa elimu na waletewa, hata ikitokea miujiza hatuwezi kutengeneza ajira hata kwa asilimia 20. Ni jukumu la Wizara kuchukua mawazo ya Wabunge yanayoweza kufanyiwa maboresho ili kulitatua hili tatizo ambalo ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunaotoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa tungeomba kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne kwa shule za kutwa tupewe elimu ya kawaida na tupewe elimu ya mazingira yetu. Kanda ya Ziwa tuna shughuli zetu za kawaida kama ufugaji, uvuvi, biashara, madini, tungeomba Wizara ya Elimu itupatie elimu hii kutoka darasa la kwanza ili mtu anapomaliza form four awe ana-balance ya elimu mbili. Kwa hiyo, ataamua mwenyewe aendelee kwenda kwenye ajira ya Serikalini au sehemu nyingine au arudi akajiajiri kuliko mtindo wa sasa hivi baada ya mtu kumaliza university anarudishwa nyumbani. Akirudi nyumbani anakukuta wewe mzee umezeeka, huna kitu cha kufanya anakuja na karatasi inayoitwa degree. Tatizo hili ni tatizo la Watanzania wote, kila mtu ni mwathirika wa hili tatizo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunamuomba Waziri ajaribu kuangalia upya muda wa kukaa shuleni. Kama hatuna ajira ingekuwa vizuri mtoto amalize university akiwa na miaka 15 au 17 ili awakute baba na mama yake at least wana nguvu kwa maana hakuna kazi ili waendelee pamoja akiwa bado mdogo ni rahisi kufanya naye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo la watu wa vyuo vikuu; vyuo vikuu vinaendesha nitaita kama aina ya utapeli mamboleo. Wanachukua pesa kwa wananchi, wanalazimisha wananchi kukopa, wanachukua pesa, shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 30, baada ya miaka mitatu wanakurudishia mtoto ana karatasi inaitwa degree. Wao ndiyo kiwanda pekee kilichobaki duniani ambacho hakiwezi ku-suffer, viwanda vyote vinateseka sasa hivi lakini vyuo vikuu hakuna mahali vinateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ilete sheria hapa ili wanapotaka kusajili hao wanafunzi waeleze kazi walizonazo ili wao waende kwa waajiri waende wakatafute hizo kazi kabla hawajasajili wanafunzi. Waeleze mshahara ndiyo waseme sasa lipa kiasi hiki mtoto wako atakwenda kufanya kazi hapa. Hii itasaidia ndugu zetu maprofesa na wamiliki wa vyuo kulijua soko la ajira, itabidi wakakutane na waajiri. Kwa sasa hawakutani na waajiri, wao wanatayarisha wanafunzi wanaacha wazazi na wazee wote nyumbani wanakuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usukumani tunakaribia kumaliza ng’ombe, tunalipia vyuo tunabaki na karatasi inayoitwa degree, lakini ukienda kwa mwajiri akiikataa ina maana hiyo degree ni valueless (haina thamani yoyote). Kwa hiyo, tungemuomba Waziri alete sheria hapa Bungeni ili vyuo vikuu viweze kubanwa na vyenyewe viende vikatafute ajira, badala ya mtindo wa sasa hivi wa vyuo kutumia nguvu ya Serikali na mawazo ya kusema elimu ni ufunguo wa maisha, matokeo yake sasa elimu ni kibano cha maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kidogo suala la VETA; humu ndani wote tuna magari, lakini sijasikia mtu yeyote anasema anapeleka gari yake VETA, wote tunauliza wapi ambapo kuna garage nzuri ya Toyota tunaambiwa ipo Mwembeni, tukifika pale Mwembeni hatuulizi cheti chochote, ningemuomba Waziri awafikirie sana watu wa garage maana yake ndio wanaofanya kazi kubwa kwa sasa hivi. Kama wao anaweza kuwa-indicate kama VETA ili wanafunzi wetu wakaenda kwenye garage za Miembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri ni kwamba garage hizo hazina masharti yoyote ya kusoma, unaweza kusoma miezi sita kama umeshaelewa unaweza kuendelea na shughuli zako. Tofauti na sasa hivi unapeleka mtoto VETA kujifunza kupaka rangi miaka mitatu, fundi bomba miaka mitatu akirudi anakuta teknolojia ya bomba imeshamalizika inakuwa hakuna chochote. Hawa wakiona ametoka VETA wote huku mtaani hawamtaki, wanasema huyu ni soft, lakini anayetoka kwenye garage anapokelewa vizuri sana maana yake ni practical. Tunaweza kuwapeleka kwenye maeneo ya sofa, maeneo mengi sana ambayo yapo sasa hivi, yanatosha kabisa kuweza kusaidia VETA badala ya mtindo wa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, namuomba Waziri, pamoja na yote hayo, anisaidie kwenye Jimbo langu la Kahama shule Nne za sekondari ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu kuwa High School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni huo kwa leo, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Nitaanza upande wa viwanda na uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala ambalo linaendelea sasa hivi kwa Kiswahili linasema kuongeza thamani au kwa Kingereza ku-add value. Suala hili kama hatukulifanyia utafiti wa dhati litatuletea mtafaruku mkubwa. Maana yangu kusema hivyo ni kwamba, kila mwenye kiwanda sasa hivi anapigania kuzuia wananchi wasiuze mali zao akiwa anasema yeye yupo tayari kununua mali yote na kui-add value. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Hapa tunakatazwa kuuza mahindi nchi za nje tunaambiwa tuuze sembe lakini watu wa Kongo sembe wanachanganya na muhogo, sasa utawauziaje sembe na wenyewe wakachanganye muhogo, wanakwambia wanataka mahindi ili wakasage waweke muhogo. Kwa kuwa Waziri yuko hapa aliangalie kwa makini sana suala hili, kama mtu anasema anataka ku-add value ni lazima aoneshe uwezo wa kiwanda chake ataweza kweli kununua mali za Watanzania ili watu wasikae na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwenye ngozi. Sasa hivi karibu ngozi zote zinatupwa, zimezuiwa na zimewekewa export levy ya 80% na indication price iliyowekwa na TRA ni senti 58 ya Dola ambayo ni Sh.1,300 lakini bei ya ngozi leo duniani ni senti 35 ambayo ni Sh.800. Itawezekana vipi sasa mtu alipie Sh.1,300 auze Sh.800? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumesaini mkataba na Uganda na Kenya kwenye hilo suala la ngozi. Wenzetu Waganda na Wakenya wana-under value invoice, wanalipia kwa bei chini na kununua mali zetu, ni kwa nini na sisi wananchi wetu wasiruhusiwa kuuza mali zao ili kuondoa huu mtafaruku ambao unaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaungana na Wabunge wenzangu kwenye suala hili la Liganga na Mchuchuma ingawaje mimi mtizamo wangu uko tofauti kidogo. Mtizamo wangu mimi ni kwamba, madini haya kwa utafiti wa wataalam wetu wanavyosema yako mengi kiasi cha kutosha miaka 100 lakini miaka 100 kwa dunia inavyokwenda haraka ni kweli teknolojia hiyo au chuma hicho kitakuwa kinatakiwa duniani. Kwa nini tusiwe na option mbili, tukawa na option ya kuuza udongo wa chuma kama ulivyo na tukawa na option ya kuyeyusha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya analysis ya madini yaliyomo mle ndani nchi nyingi duniani wakati bei ya chuma au madini fulani yanapanda wanauza kwa ajili ya kupata pesa muda ule na kujikimu. Sasa hivi hapa kwetu tunalia kwamba, hatuna pesa ya maji lakini tuna mlima zaidi ya miaka 50, kuna ubaya gani kufanya analysis na baadhi ya mawe yale yakaendelea kuuzwa ili tupate pesa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Jimbo letu la Kahama au Wilaya yetu ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga mwaka huu tuna mavuno mazuri sana ya mpunga. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri hili neno la add value aliangalie. Sisi tunataka kuuza mpunga au mchele kwa Waganda lakini tunabanwa na sheria inayosema huwezi kuuza mpunga lazima ukoboe mchele, lakini wakati unasubiri kukoboa mchele hilo soko litakuwa linakusubiri kweli kule Uganda? Haiwezekani. Ni lazima Mawaziri wafikirie sana suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye suala la biashara. Kwenye mkutano wa Mheshimiwa Rais ni kweli mambo mengi sana yalijitokeza pale. Ukiangalia maswali mengi ya wafanyabiashara ilikuwa ni kwenye tatizo la Sheria ya Importation na Sheria ya Kodi ya Mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Importation inatusumbua, sisi tunatumia tarrif ambayo haisumbui sana ukienda kwenye vitu kama mafuta ta dizeli, sukari, simenti na vinywaji kwa kuwa hawa wanatumia ujazo au kilo lakini unapokwenda kwenye item ndogondogo, nitatoa mfano wa item moja, kwa mfano wewe ume-import glass, glass kwenye tarrif inaitwa glassware, lakini kuna glass ya Sh.10,000 na ya Sh.1,000 lakini TRA ata-pick glass ya Sh.10,000 kuku-charge wewe wa glass ya Sh.1,000/=. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa ni miongoni mwa kero nyingi sana ambazo wafanyabiashara wamezionesha wakati wa kufanya importation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna tatizo kubwa sisi tunaotoka mikoa ya mpakani. Kuna hii sheria mpya ya ku- declare pesa. Wananchi walioko Kongo, Burundi, Uganda wanataka kuja kununua mali kwetu Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita. Haiwezekani mtu atoke Uganda au atoke Kongo afike Mutukula aoneshe Dola zake 50,000 apande basi, ni kitu ambacho hakiwezekani hata iweje. Tumeshuhudia wote hapa mtu anatoka kuchukua pesa pale Mlimani City anavamiwa anauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa alifikirie, hili neno tume-copy kwa Wazungu, kwao ni sawa, London uki-declare hakuna mtu atakuvamia lakini ku-declare kilometa 300 upite porini ambako mpaka mabasi yanafanyiwa escort na wewe ulionesha dola, tumekwama kabisa watu wa nje wamekataa kuja kununua mali kwetu kwa sababu hiyo, hawawezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi hizo ni zile ambazo hazina mfumo wa kibenki, Kongo hakuna benki, Burundi kuna vita, watu hao wote wanatembea na cash. Nafikiri Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa ajaribu sana kulifikiria suala hili ambalo linatusumbua sana. Sisi Mwanza tunauza samaki, mchele na vitu vingi lakini mpaka sasa tumekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kwa kuwa na Waziri wa Nishati yuko hapa tungeomba sana wenzetu wa TANESCO waruhusu, kama walivyoruhusu kwenye transformer, kwa wafanyabiashara hasa wanaotaka kuanzisha viwanda kama wanaweza kuvuta umeme kwa gharama yao halafu wakawarudishia wakati wa bili inapoanza. Kwa kuwa, yeye sasa hivi analalamika kwamba hana pesa ya kununua nguzo au vifaa vya umeme itasaidia watu wanaotaka kuanzisha viwanda waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii inaonekana ndiyo Wizara ambayo itakuwa ngumu safari hii kwenye Bunge letu. Namuomba ndugu yangu Mheshimiwa Mpina ambaye anatoka eneo la wafugaji wa ng’ombe, tunaotoka maeneo ya ufugaji tunaomba hizi ranchi kwa mara ya kwanza ziruhusiwe wananchi wetu waweke ng’ombe mle, walipie officially Serikalini ili Serikali na Wizara yake ipate pesa badala ya sasa hivi pesa hizo zinaenda kwa watunzaji wa hifadhi hizo. (Makofi)

Mheshmiwa Spika, leo tunahangaika watu wanachukua ng’ombe kutoka Usukumani kwenda mpaka Lindi, lakini tuna Ranchi ya Mwabuki ambayo inaweza kuchukua ng’ombe zaidi ya 500,000 mpaka milioni moja. Wizara kama itaruhusu ng’ombe laki tano au milioni moja wakakaa pale Mwabuki, kutajengwa automatically viwanda vya maziwa, vitajengwa viwanda vya nyama bila hata shuruti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ranchi hiyo haina ng’ombe zaidi ya 500. Kuna fisi, kuna nguruwe, hakuna kitu chochote. Ingekuwa vizuri Wizara ikaanza kuchukua action.

Mheshimiwa Spika, tuna pori ambalo linatokea Kahama mpaka Kigoma, Mheshimiwa Dotto alikuwa analia sana mara nyingi maana yake amepakana nalo. Pori hilo lina urefu wa kilometa 400, upana kilometa 250. Halina wanyama, siyo National Park kwamba watalii wanaenda, kwa nini Serikali isitoe hata asilimia kumi ikaruhusu watu wakaweka ng’ombe zao na wakalipia officially Serikalini na ikapata mapato na wananchi wetu wakapata malisho.

Mheshimiwa Spika, nawalaumu sana wataalam wa mazingira, ni kweli wanatupotosha na ni waongo. Ng’ombe hali miti wala hali udongo, ng’ombe anakula nyasi. Ng’ombe akila nyasi kwenye pori wakati wa kiangazi moto unapokuja unainusuru ile miti. Wataalam wanatuletea maneno ya Ulaya ya uongo kwamba ng’ombe akiingia kwenye lile pori ataharibu, ataharibu nini.

Mheshimiwa Spika, pori lile ni nusu ya nchi ya Uganda. Ni kweli ng’ombe waliopo pale wanaweza kudhuru nini? Leo wako ng’ombe pale wanatozwa pesa na watu wanapata pesa hakuna kitu chochote. Ni vizuri Mheshimiwa Mpina Serikali yako ili ipate pesa, ruhusu watu wachunge officially, uwatoze pesa officially, lakini wananchi wetu watapata manufaa na maendeleo pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda kwenye suala la uvuvi. Mimi kwangu sina ziwa wala mto lakini makao yangu ni Mwanza. Ukweli hali inayoendelea kule Kanda ya Ziwa ni hatari na sijawahi kuiona kwa zaidi ya miaka 30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mji wa Mwanza, ukiondoa kilimo, ukaondoa na dhahabu kinachofuata ni samaki. Leo hali iliyopo kule ni hofu, sijawahi kuiona kwenye maisha yangu. Mwananchi wa kawaida anakatazwa kubeba samaki kwenye pikipiki anakimbizwa, kwenye baiskeli anakimbizwa, matokeo yake haijulikani hasa samaki wanatakiwa kupigwa marufuku au inatakiwa nini. Kama kuna tamko la Serikali, basi Serikali itamke kwamba imesitisha ulaji wa samaki kwa muda hadi hapo itakavyojulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wavuvi hawa wanaosemwa, kweli siungi mkono uvuvi haramu lakini hawezi akakosea mtu mmoja tukaamua kwenda kupiga watu wetu kwa model hiyo, kwa kweli nakataa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lawama kubwa naitupa kwa wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nchi zinazoongoza duniani sasa hivi kwa uuzaji wa samaki, siyo nchi zenye maziwa wala bahari, nchi ya Thailand ndiyo inazoongoza kwa samaki, Serikali inatoa vifaranga milioni 200 kila mwezi, inawapa raia wake wafuge ama kwenye malambo, mabeseni, ndoo, baada ya miaka miwili, samaki walio nchi kavu ni wengi kuliko waliopo ziwani. Kwa matokeo hayo, Mheshimiwa Mpina na wataalam wake ambao tunawaita wachawi wa kizungu, maana wasomi wenzetu tunawaita wachawi wa kizungu, wenyeji wanaitwa wachawi wa kienyeji ni kweli!

Mheshimiwa Spika, viongozi wetu ambao ni wasomi, msomi kugeuka kuwa mgambo kwenda kupiga raia inahuzunisha sana. Kazi hiyo ilitakiwa ifanywe na mtu ambaye hana degree, siyo kama Maprofesa alionao nao Mheshimiwa Mpina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kama wataalam wasingetengeneza mayai ya kizungu, leo mayai ya kienyeji yangekuwa shilingi 5,000. Wataalam wasingetengeneza kuku wa kizungu, leo kuku wa kienyeji angekuwa shilingi 50,000. Wenzetu wasomi wao walikaa wakafikiri, badala ya kugombana na wananchi wakaja na solution, solution hiyo ndiyo inayotufanya leo hatujaamka kwenda kugombana na wananchi wanaofuga kuku na mayai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wazalishe samaki, warudishe mbegu za samaki kila mwezi ziwani, wawagawie na wananchi mbegu za samaki bila kupeleka maneno yao ya mazingira, bila kupeleka maneno yao ya uongo ya mazingira, uongo mtupu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mpina ajaribu kupunguza jazba. Ni kweli wananchi kule hawana nyavu. Nyavu zinazotengenezwa zinatoka Kiwanda cha Sunflag, kiwanda hiki kinatengeneza vyandarua hata kama tutaficha, lakini kweli nyavu hizo zinaweza kuvua samaki? Vyandarua haviwezi kuvua samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Mpina, asituone Wabunge kama ni watu wabaya, wote tunategemea samaki, tuna biashara zetu kule ambazo siyo samaki lakini zina uhusiano na samaki, hatuwezi kukataa, maeneo yetu yote yale yanahusika na samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwangu Kahama samaki wanaliwa. Population ya watu imeongezeka, ulaji wa samaki umeongezeka, haiwezekani wataalam wetu, watu waliosoma kwa gharama kubwa wanang’ang’ana tu kupiga watu badala ya kung’ang’ana kutafuta ufumbuzi! Kama ndugu zetu wazungu walivyoleta ufumbuzi wa kutengeneza mayai, wakatengeneza na kuku wa kizungu, leo hatuna mgogoro unachagua mwenyewe unachotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kweli leo Maprofesa wazima wanaungana kwenda kupiga watu! Uzuri na Mheshimiwa Profesa Kabudi kama yuko hapa ingekuwa ni wanasheria au madaktari wangesimamishwa kwa ajili ya degree zao lakini sijui kwa degree zingine kwamba sheria inasemaje kama mtu aliyesoma anapoharibu heshima ya degree hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo yote naomba vilevile kwa Mawaziri ambao tunaendelea na migogoro mingi hapa, kwa zile sheria ambazo Mawaziri wanaziona kama zina matatizo, wazilete tena sheria hizo Bungeni zifanyiwe marekebisho kama Mheshimiwa Rais anavyofanya. Mheshimiwa Rais juzi alifanya mabadiliko akaleta Sheria ya Madini, amesema iletwe Sheria ya Mafuta ifanyiwe mabadiliko, Mheshimiwa Luhaga Mpina na Mawaziri wengine ambao wanaona kuna matatizo, leteni sheria hizo hapa zifanyiwe mabadiliko ili kuondoa ugomvi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JUMMANE J. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye bajeti yetu hii ya 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili au matatu kama muda utaniruhusu. Suala langu la kwanza alijaribu kuliongelea hapa Mheshimiwa Ngeleja. Suala hili la dhahabu tumekuwa tukiliongea leo mwaka wa tatu toka tumeingia hapa Bungeni, sijaelewa ni kwa nini Waziri Mpango hataki kulielewa. Mara ya kwanza mimi nilikuja na hoja ya one percent kwa dhahabu kwa watu wanaofanya export. Tuliongea na Mheshimiwa Mpango lakini baadaye sikupata jibu kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu ni sawasawa na dola, sijaelewi kwa nini tunapuuza dhahabu ya wachimbaji wadogo ambayo ni karibu ya asilimia 70 ya dhahabu yote ya Tanzania na leo migodi yetu mikubwa imefungwa. Sisi tunaotoka maeneo hayo ya dhahabu tunaifahamu dhahabu vizuri sana. Benki Kuu ya Tanzania ilianza kununua, kama alivyosema mwaka 1991/1992, baadaye ilisimama baada ya matatizo yaliyotokea pale kwamba uaminifu uliokuwepo haukuwa mzuri kati ya wafanyakazi wa Benki Kuu na wafanyabiashara waliokuwa wanapeleka dhahabu pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiangalia trend ya dhahabu duniani, kama alivyosema Mheshimiwa Ngeleja, kwamba tangu mwaka 1999 kwa mfano dhahabu imekuwa ikipanda kwa speed nzuri sana. Serikali ingekubali kununua dhahabu kwa ushindani kwa bei ya soko la dunia kwa shilingi za Tanzania ingeweza kupata faida kubwa na ingeweza kuifanya pesa yetu kuwa imara. Sasa hivi kinachofanyika ni kwamba, Serikali inapotaka kulipa madeni lazima ichukue pesa za shilingi ika-source dola, lakini ingekuwa inanunua dhahabu ingeuza kipande cha dhahabu wakati inapotaka kulipa deni. Hii ingesaidia shilingi yetu vile vile isiweze kuporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nafikiri kinachotusumbua hapa huenda hii dhahabu ya local kwa kuwa haimo kwenye mitaala ya shule, labda kwa kuwa haiko shuleni kwa watalaam wa uchumi inawapa kigugumizi; kwa sababu Waamerica na Waingereza wanaotoa elimu hawana hiyo dhahabu ya kuokota mitaani. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kwamba, kila ukimwambia mtu ambaye hafahamu anaona unaongea kitu ambacho si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka 1999 kweli dhahabu ilikuwa dola 270 kwa Ounce, ambayo ni kama dola nane ama tisa; leo iko dola 1400 ambayo ni takriban dola 50. Kwa hiyo imepanda kwa asilimia 800. Pesa ya Tanzania mwaka 1999 ilikuwa 1,300 leo ni 2,300, pesa ya Tanzania ime-depreciate kwa asilimia 80. Kwa hiyo kama tungekuwa na stock ya dhahabu deni la Taifa tungelifuta lote mara moja na tusingekuwa na deni lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Mpango ajaribu aidha atuite watu tunaotoka maeneo ya madini, tujaribu kuongea na watalaam wake kama kuna sababu hasa, kwa maana hatupi jibu ni kwa sababu gani. Leo dhahabu yetu Uganda wana-charge 1.5 percent kwa export levy, Burundi 1.0 percent, Rwanda 1.0 percent; na watu hawa hawana mgodi hata mmoja na wote tuko Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sisi tunaletewa plastic na Wachina, sasa itawezekanaje? Sisi tuna kiwanda cha kuchapa dola, dhahabu ni dola, ni kama una kiwanda cha kuchapa dola, hutakiwi hata kufikiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo indication ya bei ya dhahabu duniani inaonekana kwamba itaendelea kupanda; nitatoa sababu tatu ambazo zinaonesha itaendelea kupanda. Sababu ya kwanza, ni kuwepo kwa sarafu mpya duniani; kuna sarafu ya Euro, kuna sarafu mpya ya China ambayo imekuwa imara, kuna sarafu mpya ambayo inatarajiwa ya nchi za Brazil, South Afrika na nchi za Asia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile dhahabu sasa hivi imeanza kutumika kutengeneza kwenye komputa na laptop, kiasi ambacho sisi ambao tunayo dhahabu, tunayo chance nzuri zaidi ya kupata faida kutokana na dhahabu. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Madini wajaribu, kama watalaam wao wanakuwa na kigugumizi kwa ajili ya matatizo yaliyotokea mwaka 1992, teknoloji ilikuwa bado, leo teknoloji ya dhahabu ni ya kugusa simu unajua ina percent ngapi ya dhahabu ndani yake; tunaomba wasiwasi huo uondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga reli kwenda Mikoa ya Mwanza na kwenda Mikoa ya Kigoma. Wajerumani wakati wanajenga walikuwa wakati huo huo wanaandaa na mazao ya kwenda kubebwa na treni ile. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mpango awekeze kwenye mazao ambayo treni standard gauge itakapokuwa imefika kule Kigoma na kule Mwanza licha ya abiria kuwe na mazao ya kuweza kubeba kurudi nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa idea ndogo tu, kwamba Malaysia kilichofanya wakafanikiwa kwenye michikichi ni kwamba walikuwa wanampa mtu mche wa mchikichi halafu kila mwezi wanamlipa pesa yule mtu. Baada ya miaka mitatu mchikichi ilivyoanza kutoa matunda yule mtu analipa. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aweke pesa pale, awapatie wananchi wetu michikichi na mikorosho awape Sh.1000 kila mche, gharama yake itakuwa Sh.40,000 peke yake kwa mche mmoja, lakini baada ya miaka mitatu atakuwa na miche mingi ya korosho nyingi na michikichi mingi. Kwa hiyo treni yake itakapofika Kigoma atakuwa na mizigo ya kurudi nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu, ningemalizia kwenye kodi ya viwanja na majengo. Tanzania ni nchi pekee ambayo ina-charge kodi ya viwanja na majengo kwa kumfata mtu. Nchi zote duniani zinatumia kwenye bill ya maji au umeme. Mimi kama kodi ya kiwanja ni Sh.24,000 au kodi ya jengo ni Sh.24,000 tunagawa kwa 12. Kwenye bill yangu ya maji unaleta elfu mbili ambayo inakuwa indicated pale kwenye bill ya maji au ya umeme. Nafikiri Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaweza akalichukua hili litamsaidia zaidi na hatakuwa na sababu yoyote ya kushinda kutwa nzima na majembe Auction Mart, kamata huyu, funga huyu, inaweza ikatusaidia sana sana, Mheshimiwa Waziri wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba nihitimishe mchango wangu kwa kuongelea suala la bandari. Bandari yetu ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri. Hata hivyo namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie zile bidhaa ambazo zinakwenda nchi za jirani, aongee na wafanyabiashara wa Kariakoo kwamba kwa nini bidhaa hizi haziuzwi hapa, ili aone ufumbuzi. Kama zinaweza kuteremshwa bei na hazina madhara kwa viwanda vya Tanzania ni vizuri ikafikia upya suala la kupunguza kodi juu ya bidhaa ambazo zinaweza kulipishwa ushuru hapa na wewe ukapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye dhahabu. Katika Jimbo langu la Kahama ni miongoni mwa maeneo ambayo yana machimbo mengi sana madogo madogo, pamoja na mgodi mkubwa wa Buzwagi na jirani yangu Bulyanhulu. Kinachosumbua sasa hivi, kule ni Sheria ya Madini ambayo watu wa migodi mikubwa wanatumia sheria hiyo hiyo na wachimbaji wadogo wadogo wanatumia sheria hiyo hiyo. Sasa hivi wachimbaji wadogo wadogo, akitoa mifuko 10 ya mawe ya dhahabu, anatoa mfuko mmoja kwa ajili ya madini, mfuko mmoja kwa ajili ya TRA, mfuko mmoja kwa ajili ya Halmashauri na mfuko mmoja kwa ajili ya mwenye shamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu huyu akimaliza tena kusaga mchanga ule kwenda kutoa dhahabu analipa tena, mchanga ule tena ukienda kuchenjuliwa unalipiwa tena lakini huyu mwenye mgodi mkubwa akilipa ushuru wake yeye atarekebisha kwenye hesabu zake za TRA atapunguza zile gharama alizolipia, lakini huyu mchimbaji mdogo hana mahali ambapo anaweza kwenda ku-claim fedha aliyolipa. Matokeo yake inasababisha kuwa na rushwa na migogoro mingi sana maeneo yale. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Madini ni vizuri ikaoanisha kati ya sheria ya migodi mikubwa na sheria ya wachimbaji wadogo wadogo ambao ni kama wakulima wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la dhahabu nafikiri Serikali ingetamka wazi kwamba inataka kufanya kweli kazi ya dhahabu au ni kama tunataka kuruhusu uchawi lakini wakati tukiona bundi au fisi tunaogopa. Tanzania haina elimu ya biashara ya madini ina elimu ya miamba na tunachoibiwa na matatizo yetu makubwa yako kwenye elimu ya biashara ya madini ambayo haiko shuleni. Kwa hiyo, ni vizuri kama tunaamua kuruhusu biashara ya madini ionekane kwamba madini yameruhusiwa lakini hata tukiunda Tume 100, kama hatujasema wazi kabisa tunataka nini kwenye madini, bado tuna wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Uganda leo ina- charge service levy ya export 0.5%; Rwanda wana-charge 0.6%; Burundi 1%; Tanzania tuna-charge 14%. Mheshimiwa Waziri hata kama ni wewe unaweza ukapata dhahabu ya Sh.10,000,000 ukalipa Sh.1,400,000, inawezekana? Umechimba peke yako, ukapata dhahabu ya Sh.10,000,000 ukabeba kupelekea Serikalini Sh.1,400,000, inawezekana? Wafanyabiashara hawa wanafanya biashara ya madini zaidi ya miaka 10 hata mke wake hajawahi kuiona dhahabu, ni vipi Serikali inaweza ikachunga dhahabu kutoka Lindi mpaka Mara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ya wachimbaji wadogo wadogo imeajiri zaidi ya watu milioni 5. Kwa hiyo, ni kweli Serikali kwenye kitabu inaonesha wamechangia asilimia 2 lakini tunapoteza zaidi ya tani 2 au 3 za dhahabu kila wiki. Kwa nini Serikali isiruhusu dhahabu ikawa 1% na alipe anaye-export ili hawa wachimbaji wadogo wadogo waondokane na huu msururu wa usumbufu walionao halafu wale wenye migodi mikubwa waendelee na procedure ya kawaida ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia hata jirani zetu ambao wana madini wanaweza kuyaleta hapa kwetu. Ni vizuri Serikali ikafikiria sana kuruhusu madini kutoka nje. Ni kweli tuna mikataba ambayo inasema lazima wapate certificate of original lakini ni kweli sisi tunapokea wakimbizi kutoka Congo, tunapokea kila aina ya matatizo kutoka nchi jirani, tunaweza kupata ebola, mbona tunakataa kupokea dhahabu na tuko tayari kupokea dola? Ni vizuri Serikali ikafikiria upya maana dhahabu haina alama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watu hawa watanunua mali hapa na sisi tutapata pesa kutoka kwenye kodi. Sisi hatufanyi service Msumbiji, hatutengenezi barabara Congo ina maana tutapata pesa ya bure. Kwa kuwa Mwanasheria wa Serikali na Waziri wa Sheria wapo hapa waiangalie sana hii Sheria ya Madini ambapo dhahabu ni moja lakini inapatikana kutoka kwenye vyanzo viwili tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nahitimisha mchango wangu, naunga mkono hoja, ahsante sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Wabunge wote waliochangia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda nitaongelea suala la upungufu wa chakula kwa baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ukweli baadhi ya chakula kilichopo kwenye maghala na mashine za kukoboa mpunga ni chakula cha watu binafsi ambao wengi ni wakulima waliopata mavuno mengi mwaka jana, ambao ni kama asilimia15 ya wananchi hao wa vijijini na wakulima hawa ama hawataki kuuza kwa hofu ya njaa au wanasubiri bei zaidi isiyojulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu chakula hiki mpaka leo ni kingi sana kama kingekuwa cha Serikali lakini ni cha watu binafsi, kwa hiyo huenda hata takwimu zikatofautiana kadri muda unavyoenda. Itakumbukwa hata wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Wilayani Kahama nilimwomba awaruhusu wauze mchele wao nje maana soko la ndani lisingeweza kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna asilimia 25 ya wananchi ambao wanategemea kuuza mifugo yao ili wanunue chakula, lakini bei ya mifugo haipo kupelekea kurudi na mifugo yao toka minadani au magulioni bila kuuza na kuongeza hofu kubwa ya maisha kwa wananchi hawa hasa ikizingatiwa wanakabiliwa na ukame pia kwa ajili ya malisho na maji kwa ajili ya wao na mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya wananchi ambao wakiwemo watoto, wazee, wajane na watu wenye ulemavu mbalimbali na watu ambao ni maskini kabisa kundi hili ndilo linahitaji msaada wa dharura. Ni ukweli watu hawa walipata mavuno mwaka 2015/2016 lakini baada ya ukame wa mwezi wa Novemba – Desemba na Januari kuwa mkubwa ikapelekea mavuno machache na viwavi jeshi vikala kidogo kilichokuwepo kuwapelekea kupitia kipindi kigumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa historia na jiografia ya maeneo haya hakuna sehemu yoyote wanaweza kupata pesa ili waweze kununua chakula hata cha bei nafuu, hawana mifugo, hawana ndugu wa mjini ambao wanaweza kuwasaidia na hakuna hata sehemu ya kufanya kibarua ili waweze kupata pesa wanunue chakula, ikizingatiwa watakuwa kwenye njaa kuanza Juni – Januari ambapo kama hali ya hewa itabadilika katika maeneo haya ambayo ni karibu miezi saba mpaka nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri anapofanya majumuisho yake aje na jibu sahihi ili Wabunge wanaotoka maeneo haya yaliyoathirika na ukame tuwe na majibu sahihi kwa watu wetu, vinginevyo nitakamata shilingi ya bajeti.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Kamati hii ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Wataalamu wote, pamoja na Wabunge wote wa Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila, nachukua nafasi hii ingawa si Wizara yake, kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuruhusu wachungaji na wafugaji pamoja na wakulima wanaokaa karibu na Hifadhi za Serikali kwa kuwaruhusu maeneo ambayo yana mapori ambayo hayana wanyama ili wananchi waweze kuyatumia wakati wa dharura, vilevile na vijiji 300 ambavyo vimeruhusiwa virasimishwe. Namshukuru sana kwa kupokea kilio cha wakulima na wafugaji cha muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono mapendekezo ya Kamati, ila nina mawazo mawili/matatu ambayo yamo kwenye Kamati ningependa kuyafafanua na kuyaelezea vizuri, kama yataweza kuchukuliwa na kuwa msingi mzuri wa kuelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni suala hili la Liganga na Mchuchuma. Suala hili la Liganga na Mchuchuma lina takribani zaidi ya miaka 50 na kinachoonekana tunaweza tukaenda tena miaka mingine 50 kama hatukupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chuma ni bidhaa kama bidhaa zingine na ndani ya chuma cha Liganga kuna mchanganyiko wa madini mbalimbali. Kwenye mkutano wa madini Mheshimiwa Rais alieleza na analysis zilizomo kwenye mchanga ule. Pendekezo tulilonalo ni kwamba Serikali ichukue analysis za gharama za uzalishaji kama itajenga Kiwanda cha Chuma, ichukue analysis ya mali iliyomo mule ndani ya chuma ione kama inaweza kuu-peg ule mchanga kwa bei ili wanunuzi waweze kununua kwa kulipia Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ya kuongea hili ni kwamba, wenzetu Waganda leo wanachimba crude oil kutoka Uganda wanapeleka Tanga kupitia hapa lakini wananunua petroli na dizeli kutoka nje kwenda Uganda. Ni kwamba ndani ya crude ile kuna vitu ambavyo kama watachenjua hiyo crude oil kule Uganda hawawezi kuisafirisha au hawawezi kutumia ile material nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kwa Liganga ni vizuri Serikali ikafikiria upya. Sababu nyingi za msingi ni kwamba chuma ni bidhaa kama bidhaa nyingine. Tunapoongea leo bei ya chuma duniani inaendelea kuanguka na hatujui ndani ya miaka kumi bei ya chuma itakuwaje maana chuma ni bidhaa ambayo inatumika na inakuwa recycle, sio kama chakula. Kwa hiyo hata kama tutang’ang’ania tunajua nini kitatokea baada ya miaka kumi. Ni vizuri Serikali ikafikiria kufanya analysis na kuanza kuruhusu chuma hicho Serikali iuze ili iweze kununua chuma kipya na kutumia au kupata pesa kwa ajili ya matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni kwamba ndani ya chuma au ndani ya bidhaa zozote kama unataka kuzalisha hapa lazima uangalie matumizi ya yale makapi. Inawezekana sisi tunataka kutengeneza kweli hicho kiwanda, lakini kuna makapi na bidhaa nyingine ambazo huenda tukawa hatuna matumizi nazo au soko la kuziuza au ubebaji wake zikishanyofolewa mle ndani ni kazi ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la msingi ni kwamba wataalamu waangie, kama uamuzi unaweza kufanyika ili kwa mara ya kwanza baada ya miaka hamsini hiyo bidhaa tunayosema chuma iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wasukuma mtu akija kununua mpunga kwao, unachouliza kitu cha kwanza ni bei ya mchele, ukijua bei ya mchele ndipo unajua kwamba niuze mchele au niuze mpunga; lakini utaangalia gharama zako, waste na nini, ndiyo utatoa bei ya mpunga. Kwa hiyo hata hili nafikiri wataalamu wajaribu kufanya vice versa waone kama mtu anataka chuma waangalie bei ya gharama zao na waangalie bei ya waste na nini ili waamue kama wanaweza kuuza ni vizuri Serikali ikauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili tatizo la bidhaa ya mazao mbalimbali. Nimesikia wachangiaji, Waheshimiwa Wabunge hapa wameongea sana suala la mihogo kwenda kutafuta wateja China, kufanya nini; lakini mimi nilikuja hapa na wazo na kwenye Kamati tulijaribu kuliongea na kuliingiza. Lugha niliyotumia ilileta mtafaruku kidogo niliposema kwamba wananchi waruhusiwe kutengeneza gongo kutokana na mahindi, muhogo na mtama. Maana yangu, gongo ni kama kusema kitimoto kwenye nguruwe, lakini maana yangu ni spirit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gongo ni neno la mtaani kama vile kitimoto, lakini maana yake ni spirit. Pombe zote kali tunazokunywa hapa ni spirit. Hata tukiwauzia Wachina mahindi au muhogo, wakatengeneza spirit ile ile wataturudishia sisi. Kwa hiyo, sasa hivi sisi tunachokunywa ni spirit kutoka kwenye mahindi ya watu wa nje. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sawa sawa.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna ubaya gani Serikali isiruhusu gongo, iruhusu spirit itengenezwe. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iruhusu spirit kutoka kwenye mazao ya chakula ili iweze kusaidia na kuinua bei ya mazao. Najua kuna wachangiaji wengi kwenye mtandao wanajaribu kusema kwamba bei ya vyakula itapanda, lakini leo hatuna njaa ya chakula, njaa yetu kubwa ni pesa. Maana yake vyakula vimebadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchele, leo tuna competition kubwa sana ya chips. Tunalia sana mikoa inayozalisha mchele, maana yake watu wameanza kula viazi vitamu ambavyo ni chips. Na sisi watu wa Mwanza na Shinyanga hatuwezi kulalamika kwa kuwa watu wameanza kula chips, ni pamoja na sisi wenyewe; na bahati nzuri watoto wameipenda chips. Sasa sisi wenye mchele tutafanya nini? Ni lazima tutafute option nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri wataalam wetu wajaribu ku-review kidogo mawazo, itatusaidia sana. Maana yake elimu tunayotumia imeandikwa zaidi ya miaka 50 na dunia inakwenda haraka: Je, wataalam wanajaribu kweli ku- review mawazo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kumalizia kwa kuongea, suala hili limetusumbua sana hasa kwenye Kamati yetu ya Madini tulivyokuwa juzi kwenye kikao. Mheshimiwa Rais ame-invest pesa nyingi sana kwenye ndege zaidi ya shilingi trilioni moja. Ndege hizo tunatarajia ziende nje zikalete watalii na watalii watuletee dola. Hata hivyo, dola sisi hatui- charge tax, lakini dhahabu tunai-charge tax na dhahabu ni currency. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Ni fedha!

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu ni pesa na ni pesa ya kwanza kabla ya pesa hizi tunazozitumia za karatasi. Nafikiri kwa nyie wenzetu wasomi mnaelewa, pesa ya kwanza duniani ni dhahabu, lakini kwa nini tutumie gharama ya shilingi trilioni moja kufuata dola kwa Mchina Uchina? Tunakataa currency ya mtu ambaye hana viatu wala kitu chochote, hajaomba huduma ya Serikali, anatuletea dhahabu; na leo tunalia na Mheshimiwa Mpango, tuna deficit ya dola; lakini dola zipo mlangoni na watu walionazo hawana tatizo lolote. Tunataka tax ya nini? Mbona dola hatui-charge tax? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda na dola kwenye benki, unachoulizwa zaidi ni kwamba unazo nyingi tukuongeze bei? Mbona huyu wa dhahabu haambiwi kwamba unazo tukuongeze bei? Badala yake anaambiwa tutakukata. Ukimwambia utamkata, anakataa. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wataalam wetu wajaribu sana ku-review, maana yake elimu wanayotumia, hatukatai, lakini elimu isiwe kama Biblia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hata Baba Mtakatifu anafanya marekebisho kwenye Kanisa Katoliki ili kusudi Kanisa lisiwe gumu na Walokole wasimalize wafuasi. Maana yake kwa ajili ya ugumu ule, Walokole wameendelea kuchukua wafuasi. Kwa hiyo, tunaomba na ndugu zetu; Mheshimiwa Mpango, jaribu kidogo kuchukua na elimu ya Mtaani ili ijaribu kutuinua kwenye uchumi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)