Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph Kizito Mhagama (3 total)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Miradi ya maji inayojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika vijiji vya Lilondo na Maweso imekwama kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, licha ya miradi hiyo kutumia fedha nyingi na nguvu kubwa za wananchi:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha miradi hiyo?
(b) Je, ni lini miradi hiyo itakamilika ili kutatua kero za maji kwa wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Maweso na Lilondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ni kati ya miradi iliyoibuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini. Aidha, utekelezaji wa miradi hii imekuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutokana na kuwa illibuliwa na kuanza kutekelezwa wakati Madaba ikiwa ni sehemu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Maweso kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 546,792,163.2. Jumla ya shilingi 109,771,259 zimetumika kumlipa mkandarasi. Vilevile, mradi wa Lilondo kwa mujibu wa mkataba una gharama ya shilingi 1,048,875,254 na jumla ya shilingi 224, 491,637.25 zimetumika kumlipa mkandarasi. Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Songea imewasilisha hati ya madai ya wakandarasi wa miradi hiyo na Wizara imetuma jumla ya shilingi 101,444,072 ili kuwalipa wakandarasi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima kuu ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Hivyo, Serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa itahakikisha inapeleka fedha kwa kadri zinavyopatikana katika miradi hii kulingana na hati za madai zilizohakikiwa na Halmashauri, Sekretarieti ya Mkoa na Wizara ili iweze kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Zaidi ya wananchi 181 wa kijiji cha Ngadinda Halmashauri ya Madaba wanalima ndani ya Wilaya ya Namtumbo kwa sababu ya kukosa eneo katika kijiji chao. Baraza la Madiwani lilishauri sehemu ya shamba la hekta 6,000 la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililopo ndani ya kijiji hicho ambalo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ili litumike kwa shughuli za kilimo na sehemu ibaki kwa ajili ya mifugo. Hivi sasa wafugaji toka maeneo mbalimbali nchini wapo katika shamba hilo lakini wakulima hawajatengewa eneo.
(a) Je, Serikali haioni kwamba kitendo hicho ni ubaguzi na kinaweza kuchochea migogoro kati ya wafugaji na wakulima?
(b) Je, ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ngadinda cha kutengewa eneo la kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mwaka 2014 iliunda Tume ya kuchunguza matumizi ya shamba hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kubaini kuwa shamba hilo halitumiki vizuri kwa shughuli za ufugaji. Kwa msingi huo Tume ilipendekeza hekta 4000 wapewe wananchi wa Kijiji cha Ngadinda na eneo linalobaki la hekta 2000 libaki kwa shughuli za uwekezaji na ufugaji. Hata hivyo, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Songea kugawanywa na kupata Halmashauri mpya ya Wilaya ya Mababa uamuzi huo haukutekelezwa. Hivyo, Halmashauri ya Madaba inatakiwa kujadili suala hili katika vikao vya Halmashauri na kufanya uamuzi kuhusu matumizi ya shamba hilo kwa kuzingatia maslahi ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibula msingi, Halmashauri ndiyo yenye jukumu la kujadili na kukubaliana kuhusu matumizi ya shamba hilo lililokuwa linatumika kwa shughuli za ufugaji. Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha maslahi ya wakulima na wafugaji yanazingatiwa kuhusu matumizi ya shamba hilo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka, ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ikiwemo ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili waendeshe shughuli zao katika maeneo madogo lakini kwa tija kubwa na kuwaondolea adha wanazozipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwajengea uwezo wakulima na wafugaji nchini kupitia elimu na ushauri wa kitaalam ambao hutolewa na Maafisa Ugani walioko kwenye Kata na Vijiji vya Halmashauri zote nchini. Hadi Desemba, 2017 tunao Maafisa Ugani 13,532. Kati ya hao Maafisa Ugani 8,232 ni wa kilimo cha mazao, 4,283 ni wa mifugo, 493 ni wa uvuvi na 524 ni wa ushirika.
Elimu ya kilimo na ufugaji bora hutolewa kupitia mashamba darasa 11,213 nchi nzima kwa wakulima na wafugaji wakubwa na wadogo, vikundi vya ushirika vya miradi ya umwagiliaji kwa njia ya mitaro na njia ya matone (drip irrigation) na vikundi vya ushirika vya ufugaji wa kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo itakayoanza kutekelezwa mwaka ujao 2018/2019 Serikali inaandaa mradi wa kilimo cha kutumia vitalu nyumba (green house) utakaotekelezwa kwa kila halmashauri kujenga vitalu nyumba visivyopungua viwili ili kusambaza teknolojia mpya ya kilimo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha shehena ya mazao mengi katika eneo dogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kufanya sensa mahsusi ya kuwatambua wakulima wadogo na wakubwa, kuwasajili, kujua uwezo wao na kujua mahitaji yao ya mbegu, mbolea na madawa. Zoezi hilo limeanza na mazao ya kahawa, tumbaku, korosho, chai na pamba kwa mazao ya biashara; pamoja na mazao ya mahindi, mpunga, ngano na muhogo kwa upande wa mazao ya chakula. Takwimu hizo zitasaidia utekelezaji wa mikakati ya kuongeza uzalishaji kwa kuhakikisha pembejeo za kilimo zinawafikia wakulima mapema ili zitumike kwa wakati stahiki wa kilimo kwa lengo la kuongeza tija.