Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Halima Abdallah Bulembo (10 total)

MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi zenye vijana wengi, asilimia 72 ya Watanzania wapo kwenye umri chini ya miaka 29 kwa mujibu wa taarifa ya Taifa ya Takwimu ya 2013 na ajira kwa vijana hao ndiyo suluhisho la kuhakikisha kuwa vijana wanalihudumia Taifa lao:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha vijana wawe wajasiriamali kwa kuwapa mitaji, mikopo na ni vigezo gani vitakavyosimamia na kuwalinda na kuweka usawa wa upatikanaji wa ushiriki wao katika fursa hizo?
(b) Je, ni lini ahadi ya Sh. 50,000,000 kwa kila kijiji itatekelezwa na vijana watapata mgao wao wa asilimia ngapi?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa wajasiriamali na wanaweza kupatiwa mikopo na mitaji, Serikali imejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Kutambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali;
(ii) Kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana; na
(iii) Kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo maeneo ya kazi kwa wahitimu hususani wa vyuo vya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hiyo yote, vigezo ambavyo vimekuwa vikitumika katika kutoa mikopo na mitaji kwa vijana ni umri usiozidi miaka 35; kujiunga katika SACCOS za Vijana za Wilaya na kuunda vikundi na kuvisajili kisheria.
(b) Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Sh.50,000,000 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao yaani 2016/2017. Utaratibu wa kugawa fedha hizi unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo vya kulelea watoto wasio na makazi katika kila kanda nchini na kuwjajengea stadi za kazi na ujasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima, Abdallah Bulembo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua haki ya msingi ya mtoto ya kulelewa katika familia Serikali kwa sasa haina mpango wa kuanzisha vituo vya kulelea watoto wasio na makazi katika kila kanda nchini kwa sababu jukumu la kutoa malezi kwa watoto ni la wazazi ama walezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, pale ambapo wazazi ama walezi wamefariki au kwa sababu moja au nyingine wameshindwa kuwalea watoto, jukumu hio linapaswa kuchukuliwa na ndugu ama jamaa au wana jamii wengine. Lakini pale inaposhindikana watoto hao hulazimika kulelewa katika makao kwa ajili ya malezi ikiwa ni hatua ya mwisho baada ya njia nyingine kushindikana. Na wanapokuwa makaoni hupatiwa huduma zote za msingi kama chakula, malazi, matibabu, elimu ya msingi na sekondari, msaada wa kisaikolojia na kijamii na stadi za maisha, ufundi na ukasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kutekeleza Mpango wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto kwa Mwaka 2013/2017 katika jitihada za kuboresha malezi ya watoto kwa kuimarisha mfumo wa malezi, matunzo na ulinzi wa watoto katika ngazi ya familia na jamii. Kupitia mpango huo Wizara kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na wadau wa maendeleo imeanzisha timu za ulinzi na usalama wa mtoto katika ngazi ya halmashauri, kata na vijiji ama mitaa katika halmashauri 38 nchini. Zoezi la uanzishwaji wa timu hizi linaendelea ili kufikia halmasahuri zote nchini.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Serikali imeanzisha Benki ya Wanawake na Benki ya Kilimo na kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana:-
(a) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu na kuanzisha Benki ya Vijana?
(b) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa?
(c) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii ili vijana waweze kujiwekea akiba ya uzeeni, kupata Bima ya Afya na kupata mikopo ya kuendesha biashara zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b na (c). kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa umuhimu sana suala la kuanzisha Benki ya Vijana nchini ili kuwawezesha vijana kupata huduma za mikopo yenye masharti nafuu. Kwa hatua za awali, Serikali imeona ni muhimu kwanza kuwajengea vijana tabia ya kuweka akiba na kukopa kwa kuanzisha SACCOS za vijana katika kila Halmashauri ili baadaye ziweze kuwekeza hisa katika Benki itakayoanzishwa. Hatua hii itawezesha Benki ya Vijana itakapoanzishwa kumilikiwa na vijana wenyewe.
(b) Mheshimiwa Spika, suala la Serikali kuanzisha dhamana kwa vijana kwa ajili ya kukopa ni la msingi. Tunakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutaufanyia kazi. Aidha, utaratibu utategemea uwezo wa kifedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na ubainishaji muhimu wa nani apewe dhamana ya Serikali kwa lengo la kuwanufaisha vijana wote.
(c) Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeweka utaratibu wa mwanachama kujiunga katika mfuko wa uchangiaji wa hiari pamoja na kujiunga na Bima ya Afya. Serikali kwa kushirikiana na mifuko hiyo imekuwa ikiwahamasisha vijana kupitia mafunzo, mikutano na makongamano mbalimbali ili waweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Stesheni nyingi za reli hazina huduma nzuri kama maji, vyoo na sehemu za kukaa wakati wa mvua na hivyo abiria wengi hasa akina mama na watoto kupata shida.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuboresha huduma hizo ili kuwaondolea adha hiyo kubwa akina mama na watoto?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ina jumla ya stesheni 124 katika mtandao wake wa reli. Aidha, kampuni ilishaanza ukarabati wa stesheni za treni ambao pamoja na mambo mengine umezingatia uboreshaji wa mifumo ya maji, vyoo na sehemu za kukaa abiria wakati wa mvua kwa kutumia vyanzo vya ndani ya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, stesheni zilizokwisha kukarabatiwa ni Kigoma, Kaliua, Pugu, Malindi na Mwanza ambapo ukarabati kwa Mwanza bado unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni inatambua changamoto ya ukosefu wa baadhi ya huduma katika stesheni chache za reli kutokana na kuwa na miundombinu chakavu na hivyo kuweka mpango mkakati wa kukarabati na kuboresha stesheni hizo kukidhi mahitaji ya sasa hatua kwa hatua kadiri hali ya kifedha itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Kumekuwa na upandaji holela wa gharama za pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kudhibiti upandaji holela wa pango ambao unaathiri wananchi wengi kutokana na kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa linaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya Serikali. Aidha, masuala ya upingaji wa kodi huongozwa na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na sheria iliyoanzisha Shirika la Nyumba la Taifa Na. 2 ya mwaka 1990 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005. Sheria zote mbili zimeweka viwango ambavyo mmiliki wa nyumba ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa anapaswa kuzingatia katika ukadiriaji wa kodi za pango. Miongoni mwa vigezo hivyo ni ukubwa wa nyumba, mahali nyumba ilipo, hali ya nyumba na kodi za Serikali zinazolipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kurekebisha viwango vya kodi ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa husimamiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kusimamia kodi ya pango pamoja na kuidhinisha viwango vya kodi vitanavyotozwa kwa wapangaji wa nyumba za Shirika la Nyumba. Tangu mwaka 1990 shirika limefanya marekebisho ya kodi kwa miaka 6; 1994, 1999, 2001, 2005, 2007, 2008 na 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na marekebisho hayo, bado viwango vya kodi ya pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ni kati ya asilimia 42 hadi 80 ya viwango vya soko. Kwa mfano, eneo la Masaki Shirika la Nyumba la Taifa hutoza kodi ya shilingi 1,700 kwa kila mita ya mraba wakati bei ya soko katika eneo hilo ni kati ya shilingi 12,000 hadi 30,000 kwa mita mraba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya mwisho Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa iliidhinisha viwango vipya kwa kutoza kodi kwenye nyumba za shirika mwaka 2011 ambavyo ndivyo vinatumika mpaka sasa. Utaratibu wa kupandisha kodi kwa sasa hufanyika pale mkataba wa mpangaji unapomalizika na mpangaji kuomba kuhuisha mkataba wake. Ieleweke kuwa kodi zinapanda kwa mujibu wa sheria na pale mkataba wa mpangaji unapomaliza muda wake.
MHE. HALIMA ABDALLAH BULEMBO aliuliza:-
Mkoa wa Kagera upo karibu na Ziwa Victoria lakini una uhaba mkubwa wa Maji:-
Je, ni kwa nini Wizara isibuni mradi mkubwa wa kutoa Maji Ziwa Victoria kupeleka Kagera kama ule wa kutoa Maji Ziwa Victoria kwenda Tabora?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayopakana na Ziwa Victoria hapa nchini. Kwa Mkoa wa Kagera, Serikali inaendelea kutumia ziwa hilo, ambapo imekamilisha mradi wa maji Manispaa ya Bukoba na maeneo ya pembezoni yanayozunguka Manispaa hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua tatizo la maji katika Mkoa wa Kagera hususan katika Miji ya Kayanga, Omurushaka, Kyaka, Bunazi, Ngara, Muleba na Biharamulo, Serikali inaendelea na taratibu za kumpata Mataalam Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni ambapo usanifu huo utabainisha jinsi ya kutatua matatizo ya maji kwa Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekti, ushauri wa kutumia Ziwa Victoria kuwa chanzo cha maji katika Mkoa wa Kagera kama ulivyotolewa na Mheshimiwa Mbunge umepokelewa na Mtaalam Mshauri anayetarajiwa kupatikana mwezi huu wa Septemba, 2018 ataangalia uwezekano kuzingatia ushauri uliotolewa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y MHE. HALIMA A. BULEMBO) aliuliza:-

Kagera ni moja ya mikoa mitano maskini zaidi nchini kutokana na utafiti uliofanywa na Bwana Joachim De Weeidt na kuchapishwa kwenye jarida la Journal of Development Studies ambao unaonyesha kuwa kuna njia mbili za kuondoa umaskini Kagera ambazo ni kilimo na biashara:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwa na miradi maalum ya kuondoa umaskini kwa watu wa Kagera ambao ndiyo mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi zaidi za EAC na hivyo kuufanya kuwa Mkoa wa kimkakati kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ya kiuchumi na kijamii inayotekelezwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika Mkoa wa Kagera na mikoa mingine nchini ni kwa ajili ya kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya wananchi. Pamoja na ukweli huo, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mkakati wa Serikali wa kutekeleza miradi maalum ya kuondoa umaskini katika Mkoa wa Kagera imeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021, Mpango Mkakati wa Mpango wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Mipango ya Mkoa wa Kagera kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa na Serikali katika Mkoa wa Kagera ni kama ifuatavyo:-

(i) Mkoa wa Kagera umeainisha na kutenga maeneo ya uwekezaji yenye ukubwa wa hekta 58,000 kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo (Agro Processing Industries), hususan viwanda vya kusindika nyama, ngozi, maziwa, asali, ndizi, miwa, kahawa, samaki na kadhalika. Aidha, hekta 17,400 kati ya hekta 58,000 zimeshapimwa na zipo tayari kwa uwekezaji.

(ii) Kukuza sekta ya viwanda, hususan viwanda vya kusindika mazao ya maliasili na kilimo. Viwanda vinavyofanya kazi ya kusindika mazao kwa sasa ni Kagera Fish Company Ltd na Supreme Perch Ltd vinavyosindika minofu ya samaki; Kagera Sugar Company Ltd na Amir Hamza Company Ltd vinavyosindika miwa na kahawa; na Kiwanda cha Maziwa kinachosindika wine ya rosella na juisi. Aidha, Kampuni ya Josam imepatiwa eneo lenye ukubwa wa hekta 500 katika Ranchi ya Kikulula na tayari limejengwa bwawa kwa ajili ya kuvuna maji pamoja na kuanza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wapatao mia moja hadi sasa.

(iii) Kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami mfano barabara ya Kyaka - Bugene (Km 59.1); barabara ya Kagoma – Lusahunga (Km 154); barabara ya Ushirombo – Lusahunga (Km 110); barabara ya Bwanga – Kalebezo (Km 67); barabara ya Nyakanazi – Kibondo (Km 50) na ujenzi umefikia asilimia 40; na barabara ya Kyamyorwa – Buzirayombo (Km 120).

(iv) Kuanzisha Kiwanda cha Kuchakata madini ya bati katika Wilaya ya Kyerwa ifikapo Juni 2021. Kampuni ya Tanzaplus Minerals and African Top Minerals Ltd zimeonesha nia ya kuwekeza na tayari zimeanza kuleta mashine za uchenjuaji.

(v) Kuendeleza mradi wa Uwekezaji wa Madini ya Nikeli Kabanga, katika Wilaya ya Ngara ifikapo Juni, 2021.

(vi) Kukamilisha Mradi wa REA Phase III katika maeneo ambayo hayajapata umeme ifikapo mwaka 2020.

(vii) Kuanzisha na kuendeleza skimu ya umwagiliaji katika eneo la Kitengule, Wilaya ya Karagwe ifikapo mwaka 2021. Ujenzi wa daraja la kuunganisha eneo la mradi na Kiwanda cha Sukari Kagera unaendelea kwa sasa. Wakulima zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kunufaika na uwekezaji huo.

(viii) Kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MW 80 kutoka Mto Rusumo na Kakono MW 87 katika Mto Kagera ifikapo Juni 2020.

(ix) Kuimarisha usafiri wa majini kwa kukamilisha ujenzi wa meli kubwa itakayotoa huduma ya usafiri na usafirishaji kati ya Bukoba na Mwanza.
MHE. HALIMA A. BULEMBO Aliuliza:-

Mkoa wa Kagera una hekta 1,593,758 zinazofaa kwa kilimo na ni mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi za EAC hivyo Kagera inaweza kuwa Kituo cha Biashara cha EAC.

Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuifanya Kagera ifaidike na uchumi wa kijiografia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni mkoa pekee hapa nchini unaopakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki ambazo ni Uganda, Rwanda na Burundi. Ili kuuwezesha mkoa huu kunufaika na fursa za kijiografia, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwa ni pamoja na mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, kipande cha Isaka-Rusumo chenye urefu wa kilometa 371, ukarabati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo yenye urefu wa kilometa 91, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 80 katika Mto Rusumo na Mradi wa Vituo vya Pamoja katika mipaka ya Rusumo na Mutukula kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kibiashara na nchi jirani za Rwanda na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya wakulima wa Kagera na bidhaa za baadhi ya viwanda vyetu vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu vinafaidika kimasoko na jiografia ya Mkoa wa Kagera. Baadhi ya viwanda vinavyonufaika na jiografia ya mkoa ni pamoja na Kagera Fish Co. Ltd. na Supreme Perch Ltd. vinavyosinika minofu ya samaki, Ambiance Distillers Tanzania Ltd. kinachozalisha vinywaji vikali, Bunena Development Co. Ltd., NK Bottling Co. Ltd. na Kabanga Bottlers Co. Ltd. vinavyozalisha maji ya kunywa na kiwanda cha Mayawa kinachosindika wine ya rosella na juice.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Serikali kupitia Mamlaka ya Biashara (Tan Trade) ilitoa mafunzo ya kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya kurasimisha biashara mipakani katika vituo vitatu vilivyopo katika Mkoa wa Kagera. Vituo hivyo ni pamoja na Kabanga, Rusumo na Mutukula vinavyopakana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda kwa mtiririko huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalilenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika mipaka yetu na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-

Je, kwa nini mikopo ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu imekuwa ikitolewa kwa ubaguzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura 178 ya sheria zetu, ambayo inabainisha sifa za msingi ambazo ni; awe ni mtanzania aliyedahiliwa katika masomo ya shahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali; na asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Kwa mwanafunzi anayeendelea na masomo, awe amefaulu kuendelea na masomo katika mwaka unaofuata.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, bodi ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji, hivyo, bodi huandaa mwongozo unaoweka masharti kwa waombaji pamoja na maelekezo juu ya mambo muhimu ya kuzingatiwa kwa waombaji ambao ni yatima, wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada, yalifadhiliwa. Maelekezo hayo ni pamoja na kuambatanisha uthibitisho wa hali zao.

Mheshimiwa Spika, hakuna ubaguzi wowote katika utoaji wa mikopo, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hutolewa kwa watanzania wote wenye uhitaji na walioomba mikopo hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na vigezo vilivyowekwa. Hivyo, ni vyema waombaji kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na bodi wakati wa uombaji wa mikopo, ikiwa ni pamoja na kujaza taarifa zao kwa usahihi na kuambatanisha nyaraka zote muhimu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-

Katika viwango vya kidunia vya umeme vile ambavyo tunavyofuata, kuna mabadiliko ya rangi za nyaya za umeme yaliyotokea tangu mwaka 2004 kwa nchi yetu ya Tanzania:-

Je, mabadiliko hayo yanafahamika kila mahali?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya rangi za nyaya za umeme ni jambo la kawaida katika taaluma ya uhandisi wa umeme, hivyo mitaala yote ya mafunzo ya uhandisi wa umeme yanazingatia mabadiliko haya. Mabadiliko ya rangi za nyaya za umeme yalitokea mwaka 2004 na hivi sasa yanafundishwa nchini kupitia Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), Vyuo vya Ufundi Mchundo na Vyuo Vikuu. Aidha, somo la rangi za nyaya za umeme linafundishwa katika somo la Fizikia katika shule za Sekondari.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa umeme mkubwa kimazoea (high voltage) unakuwa na rangi tatu ambazo ni nyekundu, njano na bluu. Nyaya za rangi hizo huwa ni moto. Vilevile kwa umeme mdogo (low voltage) unaotumia njia tatu (three phase) unakuwa na rangi nne ambazo ni nyekundu, njano, bluu na nyeusi. Kwa upande wa umeme wa njia moja (single phase) unakuwa na rangi mbili nyekundu na nyeusi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko hayo yaliyoanza mwaka 2004 na kukamilishwa mwaka 2006 ya BS 7671 (British Standard) iliyowianishwa rangi mpya kwa umeme mkubwa (High Voltage) ni kahawia, nyeusi na kijivu kwa umeme mdogo (low voltage) three phase, rangi mpya ni kijani yenye mchanganyiko na njano, bluu kwa nyaya za moto ni kahawia nyeusi na kijivu. Kwa upande wa njia moja (single phase) unakuwa na rangi mbili za kahawia na bluu. Serikali itaendelea kutoa elimu kwa watu wote wanaohusika na matumizi ya rangi hizi ikiwemo wakandarasi, wafanyabiashara, wenye viwanda na wananchi kwa ujumla.