Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Fakharia Shomar Khamis (40 total)

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika ahsante. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Waziri amelijibu vizuri swali hili na vilevile linatoa siha kwa Watanzania, nina maswali mawili ya nyongeza (a) Mawaziri Wadogo katika miaka 1964 mpaka 1970 station yao ya kazi ilikuwa Zanzibar ili wapate kuelewa, Mawaziri wanabakia Bara, Mawaziri Wadogo ambao walikuwa na Wizara zao za Muungano huwa wanabakia Zanzibar. Je, Mheshimiwa Waziri suala hili analionaje kwa upande wa Wizara za Muungano?
(b) Kwa kuwa Mawaziri wa Muungano wana haki kuwepo Zanzibar mara kwa mara kutembelea katika taasisi zao za kazi, kwa nini wasijipangie kila baada ya miezi mitatu wabakie Zanzibar angalau kwa wiki moja kuona maendeleo ya Zanzibar na kuweza kupata ukweli wa utendaji wa kazi uliokuwepo pale? Asante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu Mawaziri Wadogo hasa wenye zile Wizara ambazo zinahusu Muungano kubaki Zanzibar, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi ni Mawaziri ambao ni wasaidizi wa Mawaziri wetu ambao tuko katika hizi Wizara za Muungano, ninachotaka nimhakikishie tu ni kwamba siyo tu kubaki Zanzibar, tutafanya kazi ya kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri katika maeneo yote yanayohusu Muungano.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kumhakikishia kwa dhati kabisa ni kwamba Mawaziri hawa na mimi mwenyewe nikiwepo, na ofisi yangu ambayo iko Ofisi ya Makamu wa Rais pale Tunguu Zanzibar, nimepanga ratiba ya kuwepo ofisini pale mara kwa mara, shida zote na majukumu yote yanayonihusu mimi kwa maana ya wananchi wa Zanzibar watanipata kwa urahisi sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa sababu ofisi hii ndiyo ambayo inaratibu mambo ya Muungano, Wizara zote zinazohusu Muungano tumeshatoa maelekezo ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhakikisha kwamba katika maeneo yao wanatenga muda mwingi wa kuwepo Zanzibar ili wananchi wa Zanzibar wasipate shida ya kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, hivyo ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi Naibu Mawaziri hatutapungua Zanzibar na wala hatutapungua upande mwingine, tupo mahali popote kwa ajili ya kushughulikia matatizo yote ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Waziri wangu wa Muungano kuwepo kule mara kwa mara ni hivyo hivyo kwamba tumeshakubaliana ofisini mimi na Waziri wangu na mpaka sasa hivi anaenda mara kwa mara tu Zanzibar. Mheshimiwa Mbunge ametutaka at least kwa miezi mitatu tuwe kule, lakini sisi karibu kila mwezi tunaenda Zanzibar na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Zanzibar hawaoni gap lolote linalohusu mambo ya Muungano.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha, je, Wizara imechukua hatua gani kuwahamasisha wazazi wenye watoto walemavu kutoa kipaumbele kwa watoto hao kupata elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kweli Wizara yetu imekuwa ikizungumza katika nyakati mbalimbali kupitia vyombo vya habari, lakini pia kupitia Wizara nyeti sana hii ya Sera, Bunge, Watu wenye Ulemavu na mambo yote yaliyoko kule, kwamba tumekuwa tukishirikiana pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu kuhakikisha kwamba tunahamasisha jamii kwa kupitia makongamano, mikutano na kupitia Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivi tunavyoona, kwamba tuna Waheshimiwa Wabunge wenye ulemavu, mtu anaanza kuona kwamba kumbe mwanangu nikimsomesha, kumbe nikimsaidia, kuna siku ataweza kuwa Mbunge, Waziri au kiongozi yeyote yule. Kwa hiyo, kwa hali hiyo niwaambie sana Waheshimiwa wazazi mlio huko, naomba muwatoe watoto wenu wenye ulemavu barabarani, msiwape kazi ya kuomba, hiyo sio kazi yao. Ninyi ndiyo kazi yenu mfanye kazi na hatimaye iweze kuwasaidia watoto hawa wenye ulemavu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Ahsante Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ajali zinazotokea huacha athari nyingi mfano vifo, ulemavu, uharibifu wa mali na hata ya mayatima, je, kwa nini Serikali sasa isianzishe Mfuko wa Ajali yaani Accident Fund kwa ajili ya wahanga wanaofikwa na matatizo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa nini wale abiria wanaopanda ndani ya gari ambao umetuambia kwamba mnawashusha na kuwarejeshea fedha zao. Ningeona kwa nini na wao wasingetozwa faini ikawa kama ni sehemu ya wengine kuogopa kupanda magari ambayo watu wamezidi? Wakiona wanatozwa faini najua na wale watakuwa kama kigezo kwamba nikiingia kwenye gari hii na mimi nitatozwa faini wakati gari imejaa? Naomba Mheshimiwa unijibu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametoa ushauri kwamba tuanzishe mfuko kwa ajili ya wahanga wa ajali hizi lakini pia ametoa ushauri kwamba abiria ambao wamezidi kwenye mabasi nao washitakiwe kwa maana ya kulipishwa faini. Naomba tu nishauri kwamba mapendekezo yake haya mawili niyachukue kwa ajili ya kuyafanyia kazi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uvuvi ni kazi inayozalisha ajira hapa nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo ambacho kitasaidia kusomesha wavuvi tukaweza kupata tija katika nchi yetu?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uvuvi ni shughuli ambayo inahitaji ujuzi fulani kama ilivyo kilimo na shughuli nyingine zote za uzalishaji. Ili kupeleka maarifa kwa wananchi kwanza Serikali inavyo vyuo kadhaa vya uvuvi. Vyuo hivi vinatumika kufundisha wataalam ambao wao sasa kama Maafisa Ugani wanapelekwa katika vijiji na halmashauri zetu ili maarifa hayo waliyonayo wayafikishe kwa wavuvi mbalimbali wanaofanya shughuli hizo. Itakuwa vigumu sana wavuvi wote nchini kuwapeleka kwenye vyuo lakini Maafisa wetu wa Ugani kwa maana ya Maafisa Uvuvi katika halmashauri zetu mbalimbali wao ndiyo wanaopaswa kufikisha maarifa ya uvuvi kwa wavuvi ili waweze kuvua kwa tija.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja ya nyongeza.
Kwa kuwa baadhi ya askari ambao wanaotumia mashine za kielektroniki njiani mle huwa zinawashinda kuzitumia na utaona wanahangaika nazo.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia elimu waliyoipata kwa askari wale ilichukua muda gani hata baadhi yao hadi leo hawajaweze kuzitumia vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametaka kujua muda ambao elimu askari wale wamechukua basi nitafanya utafiti wa kujua muda huo halafu nitampa majibu hayo baadaye.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru Mheshimiwa amenijibu vizuri ambapo Watanzania wameweza kufaidika na hili swali langu, lakini nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Ni kwa nini askari wamekuwa hawatimizi wajibu wao hasa kwa viongozi wa kisiasa wakimemo Waheshimiwa Wabunge? (Makofi)
Swali la pili, ni kwa nini Serikali isitoe maelekezo au waraka kwa askari wake ili suala hili liwe linakwenda sambamba na utekelezaji wake na viongozi wengine ambao tayari wamewataja katika waraka huu.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwa nini askari hawatimizi sharti hilo la taratibu zao za kazi za kupiga saluti kwa viongozi na hasa Waheshimiwa Wabunge, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba askari wote wanafahamu kwamba wanatakiwa kufanya hivyo. Askari yeyote ambaye atapatikana na kosa la kutotimiza matakwa hayo ya kanuni zao kawaida huchukuliwa hatua za kinidhamu; ikiwa ni pamoja na kukatwa mshahara, adhabu ya kutoondoka kambini inaitwa confinement to barracks, adhabu ya kucheza paredi, lakini vilevile adhabu ya kufanya usafi kambi au inaitwa extra duties.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba mara nyingine unakuta kwamba sio rahisi askari akafahamu kwamba Mheshimiwa ni Mbunge, lakini vilevile askari unaweza ukakuta kwamba katika namna alivyokutana na Mheshimiwa Mbunge anaweza asimtambue kwa sababu aidha hauko na bendera kwenye gari lako, lakini vile vile ukienda kwenye mazingira na kufanya vitendo ambavyo haviendani na nafasi yako ile ya Ubunge, inakuwa ni vigumu yeye kukupigia saluti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, vilevile niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba saluti hiyo tunastahili kwa sababu ya heshima ya cheo na dhamana ambayo tumepewa kama viongozi. Kwa hiyo, tunaomba badala tu ya kudai saluti lakini vilevile tuwe viongozi wenye maadili ya uongozi na ndiyo kama usipopewa heshima hiyo ni rahisi kumripoti askari yule kwa wakubwa zake na akachukuliwa hatua. Hata hivyo, kama nilivyosema askari wetu wote wanafundishwa kuhusu hizi orders na mara nyingi wanatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwamba kwa nini Serikali isitoe maelekezo askari waweze kufuata taratibu hizi. Naomba nitumie fursa hii kwa askari wote nchini wahakikishe kwamba wanafuata Police General Orders No. 102 ili waweze kutenda yale yote ambayo wanatakiwa kufanya ikiwa ni pamoja na kutoa saluti kwa viongozi wote kama wanavyotakiwa. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyaeleza kwa kirefu nilipenda pia niongezee kwa upande wa vyombo vile vya binafsi. Pia kumejitokeza vyombo hivyo vinapokuwa katika sehemu zake za lindo kutokuwa na heshima na kuzingatia viongozi wanapokuwa wanahitaji kupata huduma ikiwemo huduma za kibenki. Kwa hiyo, naomba pengine pia hilo liweze kuzingatiwa wakati pia taasisi hizi zinapowaweka hawa askari wao kwenye malindo kujua kwamba wanafanya kazi zinazoendana na ethics za kiuaskari, kwa hiyo ni vyema kuzizingatia. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwamba swali langu limejibiwa vizuri, lakini naona kajibu kwa kifupi sana, hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; je, ni lini Serikali itaanzisha mfumo wa CCTV camera katika maeneo ya vituo vya polisi ili kusaidia kubaini matendo ya uvamizi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali inasema nini kuhusu huduma za wanafamilia hususan watoto wa askari hao waliovamiwa na kuuawa; watuambie kwamba watoto wao watawapa huduma gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante!
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake ya usalama wa askari pamoja na huduma kwa wanafamilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu CCTV cameras tunaliangalia kwa ukubwa wake ambapo tunalenga kuangalia majiji kwa ajili ya usalama wa majiji, vituo vya polisi lakini pia katika maeneo ambayo askari wetu wanalinda yakiwemo mabenki pamoja na maeneo mengine ambako huduma hizo zinahitajika. Kwa hiyo jambo hilo tumelipokea na tunalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma kwa wanafamilia, kwa sasa upo utaratibu ambao fidia huwa inatolewa, lakini tunaongea na wenzetu wa bima tuweze kuangalia upande wa bima ya afya, lakini na upande wa bima ya maisha ambao utalenga utaratibu mzima wa familia zinazoachwa na askari ambao wanapata dharura za aina hiyo. Pia kwa kuwa sasa hivi Wizara ya Mambo ya Ndani inaangalia upya Police Force Act ambayo itakuja Bungeni, ambayo inafanyiwa kazi tunategemea tutapata michango mingi ya Wabunge kupitia Kamati, lakini pia na wote ambao watahusika katika kutengeneza Act hiyo mpya.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru Mheshimiwa Waziri alivyonijibu vizuri na kwa ufasaha swali langu, lakini nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Waziri, je, kwa nini Serikali haioni
umuhimu wa kuwepo vyombo vya awali vya kuhakiki aina au bidhaa mbalimbali ya vyuma chakavu kabla havijafika sokoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa nini usiwepo
utaratibu wa kutofautisha biashara ya vyuma chakavu kabla ya kuharibu miundombinu ya Serikali ambayo sasa hivi imeenea nchi nzima kila mahali vinang’olewa? Kungekuwa na uhakiki kabla ya hivyo vyuma chakavu kuweza kufika
sokoni na kuweza kuuzwa? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile dhana ya kutumia vyuma chakavu ambavyo kimsingi vinakuwa havitakiwi kwenda kuviyeyusha na kutengeneza chuma ni wazo zuri. Tatizo lililopo ni kwamba watu wenye tamaa, wahalifu ndiyo wanaharibu ile dhana nzuri, hawa ni wahalifu kama wahalifu
wengine. Sasa chombo cha awali cha kuweza kuzuia watu hawa ni wananchi, kama inavyosema Katiba ya nchi yetu, ulinzi wan chi hii ni jukumu la wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ile
miundombinu mikubwa kama ile ya TANESCO nilivyosema, TANESCO anaweka ulinzi akisaidiana na wananchi walio wema. Nina imani huo ndio mfumo mzuri wa kuweza kulinda miundombinu yetu Tanzania nzima, Wizara yangu au Serikali
haiwezi kutengeneza polisi wa kulinda vyuma kuanzia vile vya taasisi mpaka vyetu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kutofautisha, kama ilivyo kwa wale wanaoharibu miundombinu kwenda kujipatia pesa wapo hata wenye viwanda ambao wanapokea vyuma ambavyo wazi kabisa vinaonekana vimetoka kwenye miundombinu ya Serikali au ya watu, hao
mimi ndio nakula nao sahani moja. Ma-inspector wangu wanatembelea viwanda hivyo na ni vichache vinajulikana na naendelea kuwapa elimu, atakayebainika atajuta kwanini alifanya hivyo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo nchini mfano Wilaya za Manyoni na Bahi imebainika kuwa kuna madini ya uranium na inasemekana kwamba madini haya yana thamani kubwa sana na yanahitajika maeneo mbalimbali nchini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuchimba madini hayo ili wananchi wa maeneo yale pamoja na Serikali ifaidike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza Wakala wa Jiolojia wanafanya utafiti wa kubaini mbale, jiokemia, jiofizikia na jiolojia ili kujiridhisha kama maeneo fulani yana madini ya aina gani. Ni kweli kabisa katika maeneo ya Manyoni, Bahi pamoja na maeneo mengine ya Singida ikiwemo eneo la Sekenke, GST wamekuwa wakifanya utafiti. Sasa hivi wanakamilisha shughuli za utafiti kubaini kama hiyo uranium ambayo inaonekana inaweza ikatathminiwa ikachimbwa kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika maeneo ya Bahi na maeneo mengine ya Manyoni pamoja na Sekenke yapo madini ya dhahabu na madini megine. Bado GST wanajiridhisha lakini mara baada ya kukamilisha maeneo haya yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba sasa kwa uhakika. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, zoezi la ukamilishaji wa utafiti la GST likamilike na linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake marefu lakini yametoa elimu kwa Watanzania. Naomba kuuliza maswali mawili madogo.
Kwa kuwa katika kupambana na uvuvi haramu baharini na katika maziwa yetu, jambo linaloonekana ni kwa mvuvi anaevua uvuvi wa haramu kwa sababu anapatikana na nyavu zenye macho madogo; na yeye ndiye hutiwa hatiani. Kuna usemi unaosema mkamatwa na ngozi ndiye mwizi. Sasa swali, je, Serikali inasemaje kwa wale wenye viwanda vya kutengeneza nyavu, wanaoleta, wanaouza, ambao wao ndio source kubwa ya kutufanyia huu uvuvi haramu kutokana na vifaa wanavyovileta, kuliko huyu mvuvi ambaye ameuziwa akaenda akaifanya hii kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wizara italeta lini Bungeni Sheria ambayo itaweza kuwadhibiti hawa waletaji, wenye viwanda pamoja na wauzaji ili tuweze kuwadhibiti kisheria pamoja na hawa wanaozitumia nyavu hizi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nitambue kweli jitihada za Mheshimiwa Mbunge za kufuatilia masuala ya uvuvi. Si mara ya kwanza yeye kuuliza maswali katika Bunge hili, lakini amekuwa akiwasiliana na Wizara kuonesha concern yake kuhusiana na masuala mbalimbali ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuhusu kwamba ni kwa nini wavuvi tu wanaokamatwa na nyavu ndio wanachukuliwa hatua za kisheria. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa sababu kutumia nyavu ambazo haziruhusiwi kisheria ni kosa la kisheria, yoyote yule atakayehusika kwa namna moja au nyingine katika utengenezaji, uuzaji, usafirishaji, utumiaji wa nyavu hizo anakuwa amekiuka sheria vile vile, kwa hiyo hakuna ambaye ataachwa.
Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna kiwanda ambacho kinatengeneza nyavu ambazo haziruhusiwi, kama kuna mfanyabiashara atafanya, kama kuna dalali, mtu yoyote atakayejihusisha kwa namna moja au nyingine sheria itachukua mkondo wake. Ni kweli kabisa si wavuvi tu ndio wanakamatwa lakini tayari tumeshakamata bidhaa za kutengenezea nyavu kama hizo, lakini vile vile hata wafanyabiashara ambao wanahusika wameshachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la
pili kwamba lini tutabadilisha sheria yetu ya uvuvi ya mwaka 2003 ili sasa kushughulikia kwa utaratibu zaidi makosa mbalimbali yanayopelekea watu kujihusisha na uvuvi haramu. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wizara inafanya utaratibu wa kupitia sheria ile; lakini si sheria ile tu, tunaanza kufikiria sasa kama nchi kwamba suala la uvuvi haramu ni zaidi tu ya uvuvi, inahusisha vile vile mambo ya ugaidi, lakini vile vile inahusisha uhujumu uchumi. Kwa hiyo ikiwezekana sheria nyingi zitarekebishwa ili hili suala tuweze kulishughulikia kwa mapana zaidi na kwa ufanisi zaidi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari vilizungumzia kwamba baadhi ya watuhumiwa ambao walihusika na dawa za kulevya wanapokuwa gerezani wanaishi maisha ya kifahari, je, tuhuma hizi zina ukweli?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na sober house zake wenyewe ili iwe ni sehemu ya ufuatiliaji wa vita ya dawa za kulevya kutokana na hivi sasa kuwa kazi inakuwa kama ya zimamoto, haiwi endelevu? Je, wanajipanga vipi ili kuifanya kazi hii iwe endelevu isiwe ya msimu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ukweli wa tuhuma ambazo zinasambazwa, kimsingi siyo kweli. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Jeshi la Magereza linafanya kazi zake za kusimamia na kuwahifadhi wafungwa na kuwarekebisha tabia kwa umahiri, weledi na umakini wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo rahisi. Nasi katika kufuatilia kwetu ambapo tumekuwa tukifanya ziara hizi Magerezani mara kwa mara, tumeshuhudia jinsi ambavyo Askari Magereza ama Jeshi la Magereza linavyofanya kazi yake vizuri na kwa weledi wa hali ya juu. Kwa hiyo, tuhuma hizo kimsingi siyo za kweli na ninaomba Watanzania wazipuuze.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na urekebishwaji wa tabia za watumiaji wa dawa za kulevya, naomba kumjibu Mheshimiwa Fakharia kwa kumjulisha kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina utaratibu huo kwa kutumia vikundi mbalimbali vya michezo na miradi ya kuzuia uhalifu kama vile Familia yangu Haina Mhalifu, Klabu za Usalama Kwetu Kwanza na kadhalika na programu nyingine nyingi ambazo tunafanya kuhakikisha kwamba tunasaidia kurekebisha tabia za watumiaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakati huo huo kupitia sober house ambapo wadau mbalimbali wamekuwa wakizianzisha, tumekuwa tukishirikiana nazo kwa kuweza kuwapatia misaada mbalimbali kuhakikisha kwamba vijana wetu ambao wameathirika na dawa za kulevya wanaweza kutengamaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa, lakini nimevutiwa na swali la Mheshimiwa Fakharia, nimshukuru sana kwa kulileta.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaelezee Watanzania kwamba kuhusu mambo ya Sober house ni kweli, kuna baadhi ya sober house kwa sababu ya kutokuwa na standard zinazotakiwa zimekuwa zikileta matatizo. Kwa maana hiyo, tumekubaliana na Wizara ya Afya na Wizara ya TAMISEMI, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwamba tutashirikiana sisi zote ili kwenye Halmashauri zetu tukae na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya tuweze kutengeneza standard za sober houses zikiwemo zile ambazo zitakuwa kwenye Halmashauri ili watu wetu wanaokwenda kule wasije wakapata matatizo makubwa zaidi. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mhehsimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri yenye fasaha na yenye kueleweka lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, napenda kujua kwa sasa hivi Mfuko huo unatoa riba ya kiasi gani kwa wastaafu kama gawio lao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ingawa jibu la swali langu kipengele (c) ameelezea mapato yanayopatikana kwa wadau lakini hakuelezea mapato yanayopatikana kutoka kwenye miradi inayoendeshwa na taasisi hiyo jinsi yanavyowafaidisha wadau. Napenda kujua wadau wa Mfuko huo wanafaidika nini kutokana na miradi hiyo ya ujenzi wa majumba na kadhalika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza ameuliza ni riba kiasi gani wastaafu hawa wanapata. Kwa mujibu wa utaratibu wa mfumo wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu, tunatumia kitu kinaitwa defined benefits ambapo mwanachama hulipwa kutokana na michango yake na mafao mbalimbali hupatikana kutokana na mfumo huu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu riba ambayo anaipata msaafu kimsingi ni kwamba pensheni anayoipata mstaafu inatokana na michango ambayo amechangia lakini mstaafu huyu anakatwa asilimia 10 ya mshahara lakini mchango wa mwisho kwa maana mafao anayopata ya mwisho ni zaidi ya asilimia 72.5 ya mshahara wake wa miaka mitatu ya mwisho. Kwa hiyo, utaona ni kwa kiasi gani ile fedha ambayo ameiwekeza anakuja kuipata baadaye mara nyingi zaidi ya kile ambacho amekiweka. Anakatwa asilimia 10 lakini malipo yake ya mwisho ni asilimia 72.5 ya mshahara wa miaka mitatu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili alitaka kujua mapato ya miradi hii inawanufaisha vipi wanachama ambao wamechangia. Katika mfumo huu wa uwekezaji ambapo Shirika la NSSF linafanya uwekezaji katika miradi mbalimbali, fedha inayopatika kwa maana ya mapato ndiyo hiyo ambayo huwa inaingizwa kwenye kikokotoo cha mwisho cha kumpa faida mwanachama ambaye amechangia. Pia tunayo miradi ya dhahiri ambapo kupitia miradi hii, unaona kabisa imeleta manufaa makubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, mfano, tunalo Daraja la Kigamboni ambalo ni matunda ya uwekezaji wa NSSF, daraja lile limetoa ajira lakini vilevile limeongeza mapato kwa shirika na vilevile watu wengi sasa wamerahisishiwa njia ya kwenda Kigamboni kwenda kufanya uwekezaji mkubwa ambao umeongeza tija katika Taifa letu.
Vilevile tuna uwekezaji katika kiwanda cha Mbigili na Mkulanzi pale Morogoro. Katika maeneo ambayo yametengwa, asilimia kubwa ya wananchi ambao wengine ni wanachama na wengine siyo wanachama watapata fursa kutokana na uwekezaji huu kupata mapato kupitia kiwanda kile cha sukari ambacho kinajengwa pale Morogoro.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kulitamka vizuri jina langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ambapo maswali ya msingi amenijibu vizuri na yameeleweka lakini kuna kifungu cha mwisho hapa ambacho kimenifanya niweze kupata maswali ya nyongeza. Amekiri kwamba watoto 184 walipotea na 176 wamepatikana na nane hawajapatikana lakini bado wanaendelea kutafutwa. Sasa napenda kumuuliza hivi Mheshimiwa Waziri kwa hao waliopatikana na hao waliokutwa nao, Serikali imechukua hatua gani ya kuwawajibisha kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wale watoto baada ya kupatikana ambapo alikuwa hayuko kwenye mazingira ya wazazi lazima afya itakuwa ni mgogoro. Je, Serikali au vyombo vimechukua hatua gani baada ya watoto hao kupatikana kupelekwa kwenye vyombo vya utibabu ili kuangaliwa hali yao na wazee kuweza kujiridhisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba, kupotea kwa watoto hawa 184 kulitokana na sababu mbalimbali ambapo miongoni mwa sababu hizo ilikuwa ni mazingira magumu ambayo wanaishi baadhi watoto, imani na kishirikina, visasi, kukosekana uangalifu wazazi/walezi na sababu nyingine ni kupotea kwa bahati mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sababu hizi ni tofauti na hatua ambazo zinachukuliwa zinategemea na sababu husika. Kwa zile sababu ambazo zimesababishwa na njia ya uhalifu basi hatua mbalimbali zimeshachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa watu ambao wamehusika na upotevu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbukuka juzi tu kulikuwa na tukio la kijana mmoja ambaye amejihusisha na utekaji wa watoto na kuomba fedha, kijana yule alikamatwa na kwa bahati mbaya alipata majeraha na akafariki. Nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi iko makini sana kuhakikisha kwamba inalinda watoto wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu hatua ambazo watoto hawa wanachukuliwa. Kama ambavyo nimesema kwamba kwa kuwa sababu ni tofauti kwa wale watoto ambao wamepatikana na madhara mbalimbali basi nao vilevile hufikishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kuweza kupata huduma mbalimbali ili kuwaweka katika hali nzuri ya kimaisha na kiafya.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Kwa kuwa kituo cha polisi Ziwani Zanzibar kuna baadhi ya majengo yamechakaa na yanahitaji ukarabati. Je, Mheshimiwa Waziri anawajulisha nini askari hao polisi wa Ziwani kuhusu ukarabati wa majengo yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Makao Makuu ya Polisi Ziwani kuna changamoto ya miundombinu ikiwemo uchakavu wa majengo. Serikali tunalitambua hilo na tupo katika mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho hayo kadri ya hali ya upatikanaji fedha itakaporuhusu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa, Serikali inajizatiti kuzuia suala hili la madawa ya kulevya, Je, itatuhakikishia vipi kufanya kila Mkoa wa Tanzania kuwa na sober house ili kudhibiti matatizo haya?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati ambayo tumejiwekea ya kupambana na kudhibiti dawa za kulevya, moja ya mkakati ni kitu ambacho kinaitwa harm reduction. Harm reduction ni kupunguza madhara kwa watumiaji wa madawa ya kulevya hasa wale ambao wanatumia madawa ya heroin ambao wanakwenda kutibiwa kwa kutumia Methadone.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali pamoja na kuwa na mpango wa kuweka vituo vingi vya Sober houses lakini tunatumia hospitali katika Mikoa yetu kuwa na madirisha maalum kwa ajili ya kuwahudumia watu ambao wameathirika na madawa ya kulevya. Kwa hiyo, naamini huduma itasambaa Nchi nzima na wengi watapata huduma hiyo kupitia katika hospitali za Mikoa katika maeneo husika. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa hivi punde.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwanza niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania tumepewa heshima ya kuwa ni kati ya nchi chache ndani ya Bara la Afrika ambayo inafanya vizuri, kuwa na sheria nzuri na inasimamia vizuri udhibiti wa dawa za kulevya katika nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, Umoja wa Mataifa umekubaliana kwamba mwaka huu wa 2018, nchi zote za Bara la Afrika, Viongozi wanaosimamia Sheria za Kudhibiti Dawa za Kulevya katika nchi zao watakuwa na mkutano wao mkubwa sana lakini utafanyika ndani ya Tanzania ili waweze kujifunza zaidi ni kwa kiasi gani Tanzania imefanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongeza kuhusu suala hili la kutengeneza mfumo wa utengemaa kwa waathirika wa dawa za kulevya, Serikali kupitia Mamlaka kazi kubwa tuliyoifanya katika kipindi hiki kifupi ni kuandaa miongozo na utaratibu wa uendeshaji wa sober houses katika nchi yetu ya Tanzania; miongozo hiyo sasa ipo tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali kwa kuanza kujifunza model nzuri ya sober houses katika nchi yetu ya Tanzania tumetengeneza tayari tumeshajenga na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana amezindua National Rehabilitation Center katika Mji wa Dodoma na itaanza kufanya kazi baada ya muda siyo mrefu, hiyo itakuwa ni model ya Sober houses na rehabilitation centers nyingine ambazo tunazihitaji katika nchi ya Tanzania za kuwasaidia hawa waraibu wa dawa za kulevya kurudi katika hali yao. Hivyo, Serikali inafanya kazi kubwa sana katika eneo hili. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kuwa uaharibifu wa mazingira ni janga kuu nchini.
• Je, Wizara inasema nini katika kutoa motisha kwa wale wenye maeneo yaliyotunzwa na kuhifadhiwa vizuri miti?
• Je, idara ya hali ya hewa imejipangaje katika kuhabarisha umma sambamba na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaenda kwa kasi hapa nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anasema ni motisha gani ambayo inatolewa kwa watu ambao wanajitolea katika kupanda miti na kufanya shughuli za biashara hii ya miti kama Wizara na kama taasisi za Serikali. Motisha tunazotoa tunatoa katika taasisi mbalimbali kwa mfano Wakala wa Misitu. Wakala wa Misitu amekuwa akitoa motisha wa kusaidia vikundi vinavyozalisha miti na vinavyopanda miti katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kuzungumza hapa kwamba kwa sasa hivi tumefanikiwa Wakala wa Misitu sasa yuko kila wilaya na katika kazi moja ambayo tumewaekeza ya kufanya ni kuhakikisha kwamba wanapokuwepo pale wanatengeneza miche kati ya laki moja mpaka laki tano na wanagawia wananchi. Pili, wanasaidia vikundi vinavyozalisha miti na tatu wanawasaidia wananchi wanaotaka miti ya aina mbalimbali pamoja na kuwapa mafunzo au aina ya miti inayofaa kulingana na eneo fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu hali ya hewa sisi sote hapa ni mashahidi. Taasisi hii inayoshugulika na suala la utoaji wa hali ya hewa wamekuwa wakitujulisha kila wakati juu hali ya mvua kwa kila wakati na kila kipindi kwahiyo kati ya taasisi ambayo inafanya vuziri sana na mimi nachukua nafasi hii kuipongeza sana kwa sababu imekuwa ikitupa taarifa kila wakati, mwenendo wa wa mvua zilivyo, upungufu wa mvua ulivyo na jinsi ya wananchi wanavyotakiwa kuchukua hatua kulingana na hali inavyojitokeza. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali inatoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa vijana wetu wenye umri wa miaka tisa mpaka 14. Je, baada ya kupatiwa kinga hizo vijana wetu wasichana iwapo watakuwa wanafanya ngono zembe, kinga hiyo itaendelea kumkinga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imezindua chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi na tumejielekeza kwanza kwa mabinti wote wa miaka 14 na baada ya hapo tutakuja mabinti wa miaka tisa mpaka 13 na baada ya hapo tutakuja mabinti wa miaka tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zimejionyesha kwamba vijana wengi wanaanza kujamiiana wakiwa na umri mdogo, chanjo hii itawakinga mabinti dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi, haitawakinga mabinti dhidi ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama vile magonjwa ya kaswende, kisonono pamoja na UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wanaotusikiliza, chanjo hii ni salama na lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaondokana kabisa na saratani ya shingo ya kizazi ambayo inawaathiri wanawake walio wengi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu swali lake vizuri na linatia faida kwa wananchi. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yake amelezea kwamba Serikali itasimamia uuzaji wa mazao ya wakulima kwa njia ya mnada ili kuweka ushindani. Sasa mimi nataka kumuuliza hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa nini Serikali isiweke masoko huria ili mkulima aweze kuuza mazao yake popote atakapo kwa kujiridhisha na bei itakayokuwepo kwa faida yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumejitokeza mtindo baadhi ya wakulima kuuza mazao yao bado yakiwa yangali shambani ili kukidhi matakwa ya haja yake wakati inapomkumba na yeye fedha hana.
Je, Serikali itachukua hatua gani ili kusitisha tabia hiyo ambayo inamnyonya mkulima anapouza mazao yake shambani, na kwamba anatajirika ambaye yule anayekwenda kununua mazao shambani na akavuna mazao yale na kwamba wakati mkulima anapata hasara kwa pesa anayopata ni ndogo na mazao yake yote yameshamilikiwa na mtu mwingine? Ningeomba tamko la Serikali linasemaje. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye swali lake la kwanza amezungumzia Serikali kama tunaweza tukaruhusu mazao haya kuuzwa katika soko huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema kabisa kwamba Serikali imejipanga kuwa na mfumo rasmi wa uuzaji kupitia ile TMX kwa maana ya kwamba tutakuwa na soko huria lakini kupitia mfumo rasmi wa uuzaji kupitia chombo hiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali naomba nitoe rai na onyo kwa wanunuzi kwa wakulima wote ni marufuku kuuza mazao yakiwa bado kondeni/shambani, wote watakaopatikana na hilo jambo watachukuliwa hatua stahiki za kisheria, ahsante. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwamba kuna aina tofauti za maradhi ya ini lakini amesema kuna (A), (B) na (C) lakini ukipata aina ya A, B na C zinaathiri vipi ili tuweze kujielewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba nipate ufafanuzi huo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba tunapozungumzia virusi vya ugonjwa wa Hepatitis maana yake ni kwamba ni virusi ambavyo vinashambulia Ini. Katika jibu langu la msingi nilisema kwamba kuna makundi matano, kinachotofautiana pale ni jinsi gani ya virusi hivi vinaambukizwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, virusi vya type B, C na D maambukizi yake yanafanana na yanafanaa vilevile kama mtu ambaye anaambukizwa virusi vya UKIMWI kwa maana kuongezewa damu, kujitoga ama kwa kujamiiana. Virusi vya type A na E uambukizwaji wake mara nyingi ni kwa njia ya maji, mtu anapokunywa maji yasiyo safi na salama anaweza kuambukizwa virusi hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu virusi hivi vyote type A, B, C, D na E vinashambulia ini dalili zake zote huwa zinafanana kwa maana mgonjwa kuwa na macho na ngozi kuwa manjano, mkojo kuwa mweusi, kupata homa, kuumwa tumbo na wengine kuweza kuhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwa Hepatitis B tuna chanjo ambayo sasa hivi tunaitoa kwa watoto lakini Hepatitis C hii haina chanjo mpaka sasa, hizi nyingine kwa mfano Hepatitis A na E ni magonjwa ambayo athari zake sio kubwa sana kama zilivyo za Hepatitis B.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza madogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa adhabu hutolewa kwa wavuvi wanaovua kwa kutumia nyavu haramu. Je, kwa nini adhabu hiyo pia haiendi kwa yule anayemuuzia nyavu hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wavuvi wetu ili na wao waweze kuvua kwa kuitumia bahari kuu ili iweze kuwanufaisha katika maisha yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ametaka kujua kwa nini wale wanaowauzia na kuwasambazia wavuvi nyavu haramu hatuwachukulii hatua? Naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba Wizara yetu imefanya kazi ya kuwachukulia hatua wote wanaouza na kusambaza na hata wanaozalisha nyavu hizo haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini juu ya suala la elimu, ni jambo endelevu, tumekuwa tukilifanya na tutaendelea kulifanya ili wavuvi wetu waweze kuendelea kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yametoa mwangaza kwa Watanzania, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wahamiaji haramu wanapoingia nchini bila kutambuliwa kisheria baadhi yao huzaa watoto hapa nchini. Je, hawa watoto wanakuwa raia wa nchi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa wale Watanzania ambao wanawakaribisha wahamiaji haramu hapa nchi na wanajua kisheria siyo utaratibu, je, Serikali inachukua hatua gani kwa raia hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa suala la watoto wa wahamiaji haramu na wenyewe pia itakuwa ukaazi wao nchini ni kinyume na sheria za nchi yetu. Kama ambavyo tunafahamu kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji mtu anaweza kuwa raia wa nchi ikiwa angalau mmoja wa wazazi wake wakati anazaliwa alikuwa raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na suala la raia ambao wamekuwa wakihifadhi wahamiaji haramu, kwanza tunataka kutoa wito kwa wananchi wenye tabia hizo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyumbe na sheria za nchi lakini vilevile adhabu yake ni kali sana. Moja katika jitihada ambazo tunazifanya kukomesha au kutokomeza kabisa hii biashara ya uhamiaji haramu ni kushughulika na mitandao ya wale ambao wanajihusisha na biashara hii ikiwemo wanaosafirisha, wanao-organize pamoja na wanaohifadhi. Kwa hiyo, wote hawa tukiwakamata tutawachukulia hatua za kali kabisa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa kitendo hicho cha kuwachukliwa ardhi wananchi sio kitendo chema, je, Serikali haioni kwamba wananchi hao tayari imewatumbukiza katika dimbwila umaskini?
Swali la pili, kwa kuwa mwananchi huyo ameridhia zoezi la kuchukuliwa ardhi yake pasina ridhaa yake, je, kwa nini Serikali isingelitoa sehemu mbadala ili kuondoa manung’uniko kwa wananchi hao kuona wameporwa ardhi yao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema kitendo cha kutwaa maeneo ya wananchi pasipo ridhaa yao ni kwamba ni kuwaingiza katika umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Sheria ina ruhusu eneo likishatangazwa kuwa ni eneo la upangaji miji, Mamlaka za Upangaji kisheria zimeruhusiwa kuyatoa yale maeneo. Hiyo ni alternative ambayo iko kisheria, lakini katika hali halisi ambayo inaendelea sasa na kwenye kanuni ambazo zipo tumesema kwamba unapotaka kutwaa ardhi ya mtu, wananchi wanapaswa kushirikishwa. Kwa hiyo, kile kitendo cha kutwaa ardhi bado sheria inawaruhusu Mamlaka za Upangaji kuitoa ile ardhi na kupanga kile wanachoona inafaa katika utaratibu huo.
Sasa tunasema tunayo hiyo room ya kufanya makubaliano au maelewano na wananchi, lakini Serikali inapotaka kufanya jambo na eneo limeshaanishwa hauwezi tena wewe mwananchi kuzuia shughuli za Serikali zisifanyike. Sasa katika ule utoaji ndio hapa sasa tunasema hekima na busara pia itumike katika kuwaelimisha wale wananchi ili waweze kuelewa lengo na nia njema ya Serikali ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaongelea habari ya kwamba Serikali kwamba kwa nini isitoe maeneo mengine ambayo bado hayajaendelezwa ili kuondokana na taratibu hizi. Sasa labda nitoe tu rai kwa Mamlaka za Upangaji Miji. Kwa sababu suala la upangaji miji ni suala ambalo liko chini ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo kwa vyovyote vile wanapoandaa mipango yao ile ni master plan waangalie utaratibu mzima namna ya kuukuza ule mji ili uweze kwenda vizuri kutegemeana na mahitaji ya wakati huo. Lakini kikubwa kinachofanyika pale ushirikishwaji hata kama utatwaa eneo ambalo ni la wananchi ni yale makubaliano kwa mfano kama umepanga hapani eneo la biashara au la huduma za jamii maana yake mwananchi atapaswa kupisha. Kama ni biashara mpe nafasi yeye ya kwanza kama anaweza kuendeleza yeye mwenyewe apewe kipaumbele badala ya kumuondoa na kuleta mtu mwingine mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hilo tumekuwa tukilisema sana kwa sababu imekuwa ni kelele, watu wanalalamika. Kwa hiyo narudia kusema pale mnapopanga matumizi ya maeneo yenu, mnapoweka mikakati ya mipango kabambe, lazima mwananchi aliyepo afikiriwe mwanzo kama ni viwanda basi kama yeye ataweza ajenge, hawezi atauza lakini mmilikishe na umpe masharti kwamba hili ni eneo la viwanda utapaswa kujenga kiwanda, hawezi ataingia ubia, hawezi atauza ataondoka.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Dodoma ni Mji Mkuu, pia ni Jiji, lakini kukatika kwa umeme ni jambo la kawaida.
Je, nini kinachosababisha hata kukatika kwa umeme Sengia na Site Two kuwa ni jambo la kawaida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nijibu swali la mama yangu Mheshimiwa Fakharia kwamba kukatika kwa umeme kwa Mkoa wa Dodoma naomba nilichukue na tunalishughulikia, lakini wakati mwingine ni kutokana na kubadilisha tu nguzo ambazo zimeoza, nyaya na kadhalika, lakini kwa kuwa ni Jiji kwa kweli tunalifanyia kazi kwa karibu. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, kwa kuwa maradhi ya figo ni hatari sana. Je, Mheshimiwa Waziri atawasaidia vipi wananchi wanaoishi vijijini ili kujitambua mapema kwamba tayari wameshaambukizwa na maradhi hayo na wakati huo baadhi yetu hatupendi ku-check afya zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna baadhi watoto wachanga huzaliwa na maradhi ya figo wakati wazazi wao hawatambui watoto kuwa na maradhi hayo na kupelekea mtoto kusononeka. Je, Wizara inatoa elimu gani kwa wazazi baada ya kuzaa ili kuwa na hofu ya maradhi hayo kwa watoto wao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magonjwa ya figo yanazidi kuongezeka na hoja yake ya msingi ilikuwa, je, wale watu ambao wako vijijini wanawezaje kutambua magonjwa haya. Niendelee kusisitiza kwamba magonjwa haya ya figo visababishi vikubwa sana kwanza ni ugonjwa wa kisukari lakini la pili ni ugonjwa wa shinikizo la damu. Tunaweza tukazuia magonjwa haya tukizingatia mambo makubwa matatu. La kwanza ni kuhakikisha kwamba tunapata lishe bora badala ya bora lishe. Pili, kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi lakini la tatu ni kuhakikisha tunakuwa na matumizi sahihi na yasiyopitiliza kiwango ya pombe na sigara. Kwa hiyo, niendelee kuhamasisha kwamba tuendelee na utamaduni wa kufanya check-up ya miili yetu mara kwa mara na iwapo tutafanya hivi, tunaweza tukayagundua magonjwa haya mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia kwa watoto wachanga. Watoto wachanga nao wanaweza wakapata magonjwa ya figo kwa sababu ya maumbile ya figo zao kumekuwa na changamoto wanaweza wakazaliwa na tatizo la figo. Dalili gani ambazo mtu anaweza akazigundua kama mtoto anaweza kuwa na tatizo la figo? Mara nyingi mtoto anakuwa anavimba macho, sura, tumbo, miguu na sehemu mbalimbali za mwili. Mara nyingi unakuta hata ile haja ndogo haipati kwa kiwango kinachostahili. Niendelee kusisitiza kwamba iwapo mtu ataona mtoto ana dalili kama hizo afike katika vituo vya afya aweze kupata ushauri sahihi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, nina swali moja dogo tu la nyongeza. Je, ni lini Zanzibar kutakuwa na Ofisi au Kurugenzi inayoajiri kwa shughuli za Muungano badala ya kuzifuatilia Bara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Fakharia alikuwa Kamishna mwenzangu kwenye Tume ya Utumishi wa Bunge, najua kabisa uwezo wake wa kuwawakilisha Wazanzibari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hoja aliyoitoa ya kuwa na Kurugenzi kule Zanzibar siyo jambo baya, lakini nimhakikishie kwamba mpaka sasa tunavyokwenda na ndiyo maana tukaja na utaratibu wa huu mwongozo ambao tuliamini kama Serikali kwamba tunaweza tukatatua changamoto. Kikubwa ni kile ambacho Mheshimiwa Saada amesema kuzibana taasisi zinazohusika zihakikishe kwamba wanazingatia ule mwongozo katika kuajiri. Hata hivyo, wazo lake pia siyo baya.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri, amenijibu vizuri na ametoa faida kwa Watanzania katika kuona Serikali imeishupalia rushwa ili iwe mfano kwa wengine. Nina maswali mawili madogo ambayo ningetaka pia anipatie ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mtoa rushwa na mpokea rushwa ni tendo la siri kubwa ingawa wote kisheria wana. Je, ni jambo lipi na wanalithibitishaje? Kitu kinachofanyika kwa siri wanawezaje kukijua wakati kitendo hiki hakifaywi hadharani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa ziko za aina mbalimbali, mojawapo ni rushwa ya ngono na hii pia imejificha, kuitambua siyo rahisi, inataka mbinu kubwa: Je, atawasaidia vipi vijana wetu kubaini mbinu hii ya rushwa ya ngono ili kabla ya tatizo hili halijawafika wakaweza kuliabini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana kwa jinsi ambavyo amekuwa ni sehemu ya wapambanaji katika mapambano haya dhidi ya rushwa. La kwanza, anazungumzia suala la kukamatwa kwa hawa wala rushwa na anasema kabisa tuna uhakika gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba katika ile Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ina makosa 24, lakini katika kile kifungu cha 15 kinazungumzia suala la hongo, nasi kama TAKUKURU tutamkamata mtu kama tukiwa na ushahidi katika suala zima la kile kitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linategemea na circumstantial evidence, inategemea na mazingira; nasi sote humu ndani ni wanasiasa. Kwa hiyo, mfano katika ile Sheria ya Uchaguzi, mambo mengi huwa yanatokea na sote humu ndani tunaelewa. Kwa hiyo, hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu ngono ya rushwa, naomba niseme kwamba hili limekuwa ni tatizo, kubwa ngono ya rushwa iko katika kifungu Na. 25. Ninapomjibu swali lake Mheshimiwa Mbunge, hata ninyi Wabunge humu ndani mnafuatiliwa kwa sababu ni kosa na huwa linatokea hata mashuleni, vyuoni, maofisini, unakuta wanawake wananyanyaswa kutokana na tatizo hili la ngono ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama TAKUKURU…

MWENYEKITI: Waheshimiwa mmeelewa, endelea.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, tuna wataalam wa kutosha kugundua kwamba, hii ni ngono ya rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ambayo yalikuwa ni madogo ila hakutoa ufafanuzi, lakini nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa sababu jambo lolote linalokuwa linataka lifanikiwe linakuwa na ratiba au linakuwa na mpangilio maalum. Hata hivi vikao wanavyovifanya kwa vyovyote inabidi viwe na maandalizi na maandalizi yake kuwe na ratiba.

Sasa nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kabla ya kufanya hivi vikao vyao vya pamoja vya mashirikiano, wanajiandaa kwa ratiba ya pande zote mbili baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu baadhi ya Mawaziri huwa hawashiriki vikao kwa kuwa wanapotaarifiwa hivyo vikao wanakuwa nje ya nchi au wanakuwa na dharura nyingine za vikao vingine ambavyo wameshajipangia. Sasa nataka anijulishe, wanapokuwa wanakaa kufanya vikao hivyo wanakuwa wameandaa ratiba mapema baina ya SMZ na SMT ili wahakikishe kwamba viongozi wote hao wanatakiwa kushiriki? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wamesema kwamba changamoto zilikuwa 15, changamoto 11 zimepatiwa ufumbuzi zimebakia nne, sasa hizo changamoto nne ambazo anasema bado ziko katika maandalizi ya kupata ufumbuzi, ni zipi za SMT na zipi za SMZ katika hizo nne ambazo bado zimo katika changamoto zinazopatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumjibu Mheshimiwa Fakharia Shomar maswali yake mawili ya nyongeza. Moja kila kikao kinaandaliwa ratiba mapema sana na nimkumbushe tu kwamba tarehe 9 Februari, 2019 kulikuwa na kikao cha Kamati ya Pamoja cha SMT na SMZ kujadili changamoto zote hizi na hasa hizi nne nazo pia zimetolewa maelekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kweli hizi changamoto nne kwa mujibu wa swali lake la msingi alivyokuwa ameliuliza, ningependa pia nizitaje, moja ni mgawanyo wa kodi ya misaada; lakini ya pili, ni usajili wa vyombo vya moto; ya tatu, ni hisa za SMZ katika Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki na Benki Kuu; na ya nne ni Tume ya Pamoja ya Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee katika majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri katika suala hili hasa la ratiba na utaratibu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mwezi uliopita zimepitisha rasmi utaratibu mpya wa kushughulikia changamoto za Muungano na kuweka ratiba mahsusi ya vikao. Kwa hiyo, kile kikao kikubwa kabisa cha Makamu wa Rais ambacho ni cha Serikali zote Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Mawaziri la SMZ kinakutana mara moja kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kikao cha Mawaziri na chenyewe kinakutana mara moja kwa mwaka, kikao cha Makatibu Wakuu wote kinakutana mara mbili kwa mwaka na kikao cha Wataalam wa Serikali zote na chenyewe kinakutana mara mbili kwa mwaka. Kwa hiyo ratiba zimetolewa na Waraka wa Serikali (circular) imesambazwa na kueleza Wajumbe wote wa vikao hivi na utaratibu wa kuviitisha, utaratibu wa kuleta ajenda katika vikao ili kuwepo na utaratibu unaotabirika na unaoeleweka na ambao umepitishwa katika mfumo wa Serikali kushughulikia suala hili.

Vilevile, zimeundwa Kamati za hii Kamati ya Pamoja, Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ili zile changamoto ambazo ni za kutafutiwa majawabu haraka haraka zisingoje kikao kikubwa, Mawaziri waweze kukutana haraka katika hizi Kamati zao na kuzishughulikia. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeweka utaratibu madhubuti kabisa wa kushughulikia changamoto za Muungano katika Serikali hii ya Awamu ya Tano.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa ujauzito ni kawaida kwa mwanamke yeyote kwa mfungwa au mtu aliyepo uraiani. Kwa hawa wafungwa ambao tayari ni wajawazito, kuna wakunga standby ili wawasaidie? Kwa sababu uchungu unakuja time yoyote na wapo ndani ya gereza, je, mnawawekea wazalishaji/wakunga standby wa kuwasaidia uchungu unapowajia?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba kwenye Jeshi la Magereza, tunazo Zahanati na Vituo vya Afya ambapo wapo Madaktari wanaotoa utaalam wao kuhakikisha kwamba yale mahitaji yote ya akina mama katika kuhudhuria kliniki na kufuatilia siku za kujifungua wanazifanya kama kawaida. Pia tunao wakunga ambao siku zao zikifika wanawazalisha kama kawaida na hata vifaa vya kujifungulia wanavipata kama kawaida; na hata vile vyakula ambavyo akina mama, vinachochewa na mahitaji ya ujauzito; iwe ni udongo au chakula chochote kile wanaletewa kama kawaida. Ahsante sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza na pia kwa Mheshimiwa alivyonijivu kidogo inaleta afueni kwa wazee wetu lakini bado haijawa ya kuridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wazee bado wanaendelea kuteseka kupata matibabu yaliyo bora.

Je, Wizara imefanya tathmini gani ya kuona kwamba wazee hawa wanaendelea kutunzwa na kwamba hawawezi kupata shida?

Swali la pili, kwa kuwa wazee wanahaki ya kutunzwa na kulelewa lakini hakuna sheria iliyotungwa ilhali Sera imetungwa tangu mwaka 2007 lakini sheria hadi hii leo haijatungwa; unategemea nini, kwamba Sera yako hii itaweza kufanyakazi na wazee hawa waweze kutunzwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ameuliza kwamba tumefanya tathmini na changamoto ni zipi. Changamoto kama nilivyosema, ni kwamba kwanza ni utambuzi wa wazee. Taifa letu limepata bahati, sasa hivi kadri tunavyoboresha sekta yetu ya afya umri wa wazee nao kuishi unazidi kuongezeka. Sasa hivi wastani wa Mtanzania kuishi ni miaka 64 na wengi miaka 64 bado wana afya njema, na kundi hili linazidi kukua kwasababu ya maboresho haya ambayo tumeyafanya katika sekta yetu ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo moja ya changamoto ambayo tunayo ni utambuzi wa hawa wazee. Ndiyo maana tumetoa rai kuhakikisha kwamba halmashauri zinaendelea kuwatambua na kuwapatia vitambulisho. Wizara tumetoa maelekezo ya kuwa na madirisha maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee, na hili tumeendelea kulifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto nyingine ambayo tumeibaini na ambayo sasa nayo tunataka kuitibu ni magonjwa ambayo yanawaathiri wazee ni magonjwa mahususi sana; na katika jibu langu la msingi kwa swali lililopita nilijibu kwamba sasa tunataka kwenda katika National program ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo itakwenda mpaka chini kuhakikisha kwamba sasa wazee wale ambao magonjwa yao mengi ni yale magonjwa sugu basi waweze kupata huduma zao kule kule katika ngazi za kata na zahanati ambazo wanazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, changamoto nyingine ambayo tumeibaini na ambayo sasa tunataka kuitibu ni ugharamiaji wa matibabu kwa wazee ambapo sasa tunataka mwezi Septemba tuje na muswada wa sheria ambao utakuwa na bima ya wananchi wote ambao sasa utaweza kufanya ugharamiaji wa matibabu haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linauliza ni lini Serikali italeta sheria ya wazee. Sera ambayo tunayo sasa hivi sisi kama Serikali tumeona imepitwa na wakati na sasa tuko katika hatua ya kufanya mapitio ya Sera hii ya Wazee ili iweze kuendana na mazingira ya kwetu ya sasa na baada ya hapo sasa Serikali itatafakari kama kuna umuhimu wa kuja na sheria mpya ya wazee.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri ambayo yatasaidia wazazi waliokuwa hai na wanaoweza kuwatumia watoto isivyo kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kuna baadhi ya barabara wanapotembea, pembezoni mwa ile barabara utakuta mzazi na mtoto wake wanaomba ili waweze kujikimu kimaisha: Je, Wizara hii suala hili wanaliona? Kama wanaliona, wanamnusuru vipi yule mtoto ili aweze kuendelea na masomo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna baadhi ya watoto ni wadogo, wakati wa masomo utawakuta mitaani wanatembea na biashara, wengine za maandazi na matunda na wakati wazazi wao wanajulikana na sehemu wanazokaa: Je, Wizara hii itamnusuru vipi yule mtoto ili aweze kwenda shuleni kwa wakati ule wa masomo badala ya kupita mitaani na biashara akitembeza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze kwa kutoa maelezo kuhusu haki za mtoto ni zipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania tuliridhia Mikataba ya Kimataifa na tukatunga Sheria Na. 21 ya mwaka 2009 ambayo inatoa haki za msingi kwa mtoto. Naomba kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge, ni vizuri Wabunge na hata vijana na watoto ambao wako kwenye gallery waweze kuzitambua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kuendelezwa, mtoto ana haki ya kushirikishwa na mtoto ana haki ya kutofanyishwa kazi nzito. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sheria hii, Kifungu cha 14 kimeeleza vizuri tu kwamba pale haki hizi zinapokiukwa, Serikali inaweza ikamshtaki mzazi na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na faini isiyozidi shilingi milioni tano na kifungo kisichozidi miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini ambacho sisi kama Serikali tumefanya? Kwanza kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, tumeanza kufanya tathmini ya kina katika maeneo ya majiji kuweza kuwabaini watoto wale ambao wako mitaani. Ukiangalia tumefanya katika njia mbili; moja, tumefanya mchana hili na kujua idadi yao, lakini vilevile tumefanya hili zoezi usiku. Tulichokibaini ni kwamba, watoto wengi wanakuwa mtaani mchana, lakini usiku wengine wanarudi majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Watoto hawa wanafanyishwa shughuli za ombaomba na nyingine hizi za kufanya biashara. Kwa hiyo, tumekuja na Kampeni inayokwenda kwa jina la “Twende Sawa” ambapo moja ya jambo tutakaloenda kulifanya katika kampeni hii, ni kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Vilevile tumejumuisha na hili suala la watoto ambao wanatumikishwa na kufanyishwa biashara mitaani, kwa lengo la kuanza kutoa elimu katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Halmashauri kuweza kufanya zoezi hili la kufanya tathmini katika maeneo yao na kuanza kwenda kuchukua hatua kwa wale wazazi ambao wanakaidi na ambao hawasimamii majukumu yao ya msingi na kuwatumikisha watoto kama ombaomba na kufanya biashara mtaani.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kweli kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri wazee wetu watavunjika moyo. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa katika maelezo yake ametuambia hakuna sheria ya kuwatunza wazee hawa kwa kazi zao walizozifanya. Je, ni lini Wizara yake italeta hapa Bungeni sheria hiyo kwa ajili ya kuwaenzi wazee hawa ambao waliiletea nchi yetu heshima kubwa na kuifanya iweze kutambulika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa wazee walioitumikia nchi hii kwa juhudi kubwa na kuipa sifa nchi yetu na kuifanya itambulike, je, Wizara haioni umuhimu wa wa kuwapatia bima ya afya ya uzeeni angalau ikawa faraja kwa wazee hao nao wakaona kwamba Serikali na Wizara inawatambua?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Fakharia amekuwa mstari wa mbele kwanza kudumisha Muungano lakini pia na leo amekuja na jambo zuri sana kuhusiana na wazee wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile natambua mchango wa wa wazee hao wanne ambao amewazungumzia kwenye swali lake la msingi. Nichukue fursa hii kwanza kuendelea kuwaombea kheri wazee wetu hawa ambao bado wapo, wapo wawili Moshi; Bi. Khadija Rashid na Mzee Hassan Omar wako Zanzibar lakini pia Bi. Sifaeli Mushi na Mzee Elias Mrema ambao wao wako Moshi. Nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wetu walioko kwenye ngazi hizo wawashirikishe kwenye shughuli zozote zile ambazo zinahitaji kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni sahihi kabisa tunawajibika kuhakikisha tunawaenzi wazee hawa na ametoa ushauri kwamba ufike wakati Ofisi yetu iweze kuleta sheria. Nikuahidi Mhehsimiwa Fakharia tutalifanyia kazi wazo lake hili ili kuhakikisha tunawaenzi wazee hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata suala la bima ya afya na lenyewe nalo naomba tulichukue ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kuona namna gani tunawasaidia wazee wetu. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jawabu alilonipa ambalo ni zuri na linaridhisha na kaamua kusema ukweli wake hali halisi ya Kambi hiyo, lakini ni nana maswali mawili ya nyongeza:-

Kwa kuwa, uzio ambao ninaupigia kelele kila siku, sasa hivi wanataka waukarabati kufanya wa matofali na sasa bado upo wa waya, lakini hata hivyo wamejitahidi upande wa School ya Jang’ombe tayari wameufanyia ukarabati, ningeomba na upande wa Matarumbeta, upande wa kwa Alinatu, upande wa Kwahani kwa sababu hizo njia za panya zimekaa sehemu mbaya na watu bado wanazitumia kama vichaka au njia za kupitia wangelifanya kila mbinu na sehemu hizo wakafanyia ukarabati kabla hata kufanya ukarabati huo utakaozungushwa kwa matofali.

Swali la pili, kwa kuwa tayari amekubali kwamba nyumba za kambi hizo zote zimechakaa na kweli zimechakaa, maana zimejengwa kabla ya Mapinduzi ya 1964 na kwa kuwa nyumba hizo hasa zili wanazokaa Askari wa wa kawaida siyo Maofisa ambao ni kama mabanda nyumba hizo zimechakaa na haziridhishi kukaa binadamu ningeomba angalau wangeanza kuzifanyia ukarabati hizo ili Askari wetu wakaishi maisha bora.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Fakharia kwa jitihada zake kubwa anazochukua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Majimbo ya Mkoa mzima wa Mjini. Mimi ni shahidi ni Mbunge ambaye anashirikiana nami vizuri katika Jimbo langu ambalo lipo katika Mkoa wake katika kukabiliana na changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo za dhati kwa Mheshimiwa Fakharia naomba sasa nijibu maswali yake kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa amekiri ameridhishwa na jitihada ambazo tumeshaanza kuchukuwa katika kukarabati uzio kwa upande uliopo karibu na school ya Jang’ombe nimhakikishie kwamba jitihada hizo ambazo zimeanza ndizo ambazo tutaendelea nazo katika kukamilisha uzio wote lakini pamoja na kukarabati nyumba za Askari Polisi pale ambapo fedha zitakapokuwa zimepatikana kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi.(Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kuishukuru Wizara kwa jawabu zuri lenye mantiki ambalo linaeleweka na linalofahamika. Itakuwa ni hasa Watanzania wengi watalifurahia jawabu hilo kutokana na maelezo yake aliyojipanga.

Mheshimiwa Spika, lakini nina maswala mawili ya nyongeza. Kwa kweli matunda kama mananasi, matikiti, machungwa, embe n.k huwa yanazaliwa kwa wingi na yanakosa soko na yanaharibika mitaani. Je? Serikali inawaambia nini wananchi wa mikoa hiyo wanaozalisha matunda kwa wingi mbinu ya kunusuru matunda hayo ili yaweze kukaa kwa muda mrefu? (makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tunazungumza Tanzania ya viwanda na ninakubaliana na maelezo yako, lakini ningeiomba Serikali ikawahamasisha wazawa wa Tanzania wa kila mkoa wakaweza kuanzisha viwanda ili kila mkoa ukawa na viwanda vya kusindika au cha kufanya juhudi yoyote ili mikoa inayozalisha matunda kwa wingi iweze kuyanusuru matunda yao na iweze kufanikiwa na wanachokilima kiwape faida yao? Naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunajua changamoto ya upotevu wa mazao yaani (post harass losses) kwa ujumla wake na hasa katika msimu ambao kunakuwa na mavuno mengi, kwa maana ya matunda mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango Madhubuti, kwanza wa kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo Waheshimiwa Wabunge kila mmoja maeneo yake anaweza kuwa na viwanda hivyo ambavyo vinaweza kuchakata mazao haya au matunda hayo kwa muda ambao yanakuwa yamezalishwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini pili kupitia SIDO tuna teknolojia na viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vinachakata mazao ya matunda lakini pia teknolojia ya kukausha ili kuyatunza matunda hayo yasiweze kuharibika, yaweze kutunzwa ili yasiweze kupotea kabla ya kutumika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo nashukuru kwa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge; kwamba Serikali tunaendelea kuhamasisha kweli uanzishaji wa viwanda lakini pia na teknolojia nyingine ikiwemo kuwa na vyumba maalum cold rooms ambazo ni facility za kutunza matunda kabla ya kuuza yaweze kukaa kwa muda mrefu ili angalau yaweze kudumu yasiharibike haraka.

Mheshimiwa Spika, tunachukua ushauri wake lakini tunaendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo, lakini pia kupitia masharika yetu tuna teknolojia mbalimbali ambazo tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kupitia SIDO na taasisi zetu nyingine waweze kupata teknolojia hizi ili ziweze kuwasaidia katika kutunza matunda ili yasiweze kupotea wakati wa mavuno mengi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la Mkoa wa Kusini Unguja ni sawasawa na suala la Mkoa wa Kaskazini Unguja. Je, ofisi iliyokuweko Mkokotoni itamalizika lini? Maana huu mwaka wa tano unakwenda wa sita, bado kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ofisi ile ipo kwa muda mrefu na ujenzi wake ulikwama hapa katikati, lakini nimhakikishie tu kwamba, Mheshimiwa Mbunge ukarabati na kuendelea kumalizika ujenzi wa jengo lile sasa hivi umo mbioni. Na kama atakuwa ameanza kupita kwa muda huu anaweza akayaona mabadiliko ya ujenzi ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe wananchi, hasa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, jambo lao tayari lipo na linatekelezwa na muda si mrefu sana wataanza kutumia kituo kile na wataendelea kupata huduma za ulinzi na usalama katika maeneo yale, hasa ya Mkokotoni, maeneo ya Donge, maeneo ya Mkwajuni na maeneo mengine ya Mkoa wa Kaskazini Unguja. Ninakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yake mazuri kwenye swali langu la msingi. Sasa ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali ina mkakati wa kukuza uchumi wa bluu, je, Wizara yake ina mpango gani wa kutoa elimu ya teknolojia kwa wavuvi wa Bara na Visiwani ili kukuza uchumi wao na pato la Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Serikali tayari imeagiza meli nane, nne Bara na nne Zanzibar. Je, Serikali au Wizara ina mpango gani wa kutoa elimu kwa maofisa hao watakaohudumia meli hizo pamoja na ajira kwa vijana ambao ajira sasa hivi ni ngumu na meli hizo zitasaidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni juu ya kutumia vyema fursa ya uchumi wa bluu. Katika kutekeleza jambo hilo Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vyema kuhakikisha kwamba teknolojia ndiyo itakayotuongoza ili tuweze kutumia vyema rasilimali zilizopo katika bahari yetu lakini vilevile na maziwa makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia hii ni pamoja na kuwasidia wavuvi waweze kutumia vifaa vya kisasa vitakavyowafikisha katika maeneo yenye samaki kwa urahisi na kwa kutumia gharama nafuu. Vifaa hivi, hivi sasa Wizara ipo katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tunajipanga vyema watumie GPS, mvuvi anapotoka pwani anapokwenda baharini, awe tayari anazo taarifa za wapi samaki wanapatikana ili hiyo iweze kumsaidia kuweza kufanya timing ya muda, lakini vile vile hata mafuta atakayoyatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili analotaka kujua ni juu ya mkakati wa Serikali kwenye kuutumia uchumi huu wa bluu kutoa elimu na ajira kwa vijana na akinamama. Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa bluu, meli nane kama alivyotaja zitanunuliwa nne kwa upande wa Zanzibar na nne kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa kufanya hivyo Mashirika yetu makubwa mawili ya ZAFICO na TAFICO yanafufuliwa na yatanunua meli mbili kwa kuanzia katika mwaka wa fedha huu 2021/2022. ZAFICO kwa maana ya Zanzibar Fisheries Corporation itanunua meli mbili na TAFICO itanunua meli mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa zitapatikana ajira kwa vijana wa Kitanzania ambao pia watapewa elimu ya kuweza kujiandaa na fursa hiyo kubwa. Zaidi ya hapo tunao mpango wa maendeleo ya kilimo kwa maana Agricultural Sector Development Program II itakwenda sambamba na kutengeneza na kuwaandaa vijana wetu ikiwa ni pamoja na shughuli nzima za ufugaji wa samaki katika maeneo ya bahari, tunaita kwa lugha la kitaalam Mariculture. Zaidi ya vijana 1,000 kule Zanzibar na akinamama zaidi ya 15,000 watanufaika na mradi huu wa AFDP. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuunga mkono na wananchi wajipange vyema kuhakikisha tunatumia fursa hii ya uchumi wa bluu. Ahsante sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa kunijibu vizuri na Watanzania wamesikia jinsi gani vyuma chakavu vilivyokuwa vinafanya kazi ya kusaidia jamii, lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa suala la vyuma chakavu limekuwa sugu ingawa mazingira wameiwekea kanuni na kwa kuwa suala hili la mazingira limeshamiri la watu kuiba vyuma chakavu kwamba imekuwa kama ni mtaji wao na inaipa taabu Serikali katika kudhibiti ambavyo vyuma kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri.

Je, wako tayari kutuletea sheria itakayokuwa kali inayohusu vyuma chakavu ili tuipitishe hapa Bungeni iweze kusaidia jamii?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa baadhi ya wezi wanaohujumu vyuma chakavu wengi wao wanatumia vilevi ambavyo havikubaliki na jamii ambao kama mfano wanaokula unga, hao ndio jamii kubwa inayofanya kazi hizo za kubeba vyuma chakavu ambavyo vimo katika mitaro ya maji.

Je, suala hili Serikali inalijua na kama inalijua imeliangaliaje…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Fakharia umeshauliza maswali mawili tayari.

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, Insha Allah nataka nijue hayo mawili ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sheria zilizopo zinatosha kabisa, lakini ushauri unazingatiwa, kimsingi Mheshimiwa Mbunge tuondoe na tuache tu muhali wale watu ambao wamefanya makosa tuchukue hatua na kuwapeleka sehemu ambayo inayohusika. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyaweka mbele ya Bunge lako Tukufu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Fakharia, ni kweli kabisa wengi kati ya vijana ambao wamekuwa wakijihusisha na shughuli hiyo wamekuwa na dalili zote ambazo zinaviashiria vya matumizi ya dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya inachokifanya kwa sasa ni kuanzisha klabu mbalimbali katika mitaa na shule na maeneo mbalimbali kwenye nchi yetu ili kuweza pia kuwabaini hata hao vijana wanaojihusisha na shughuli hizo na shughuli nyingine tu, lakini wanaendelea kutumia dawa za kulevya na lengo letu ni kuwasaidia kuwaondoa huko na kuwaleta katika biashara ambazo hatawajihusisha tena na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa hiyo tutaendelea kufanya kazi hiyo nzuri, lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania bila matumizi na biashara ya dawa za kulevya iwezekane na tuweze kusonga mbele. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na yanaleta faida kwa Watanzania. Hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uvamizi katika vituo vya Polisi siyo jambo jema, lakini nashukuru Jeshi la Polisi wameweza kudhibiti, lakini suala kama hilo huenda likajirudia. Swali langu linasema hivi: Je, ikitokea wamevamiwa katika vituo vyao na kwa bahati mbaya askari kajeruhiwa au askari kauliwa; familia ile inayomtegemea yule askari ambapo ndio tegemeo lao kimaisha, Serikali inawaambia nini au itawasaidia nini ili waweze kuishi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wanapovamia vituo, lengo kuu ni kupata zile silaha na kuwaathiri Polisi wenyewe walioko kituoni. Je, wakati wanapozungumza au wakati taarifa tunapozipata, baadhi yao wanazipata silaha; wanapokuwa wamezipata zinakuwa katika hali gani? Katika hali ya ubora ule ule wa awali au tayari zimebadilishwa ili wasiweze kuzitambua? Ni hayo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bi. Fakharia, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa Mjini Zanzibar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeweka utaratibu maalumu wa askari wake watakapopata mitihani katika harakati za kulinda amani na utulivu wa nchi hii, lakini ni ikiwa imethibitika kwamba mtihani huo umemkuta ama ameupata akiwa katika harakati za kazi zake za kawaida za kiaskari. Kwa hiyo, kuna kanuni ya fidia ya pamoja ya Jeshi la Polisi na Magereza, hiyo hutumika. Katika kanuni hiyo imeelezwa viwango ambavyo huwa mtu anafidiwa kutokana na tatizo lililomkuta; kuna viwango akipata ulemavu, kuna viwango akikatika, na kuna viwango akifa. Kwa hiyo, Serikali kupitia Jeshi, imeweka utaratibu maalumu kupitia hii kanuni ambayo inawapa watu nafasi ya kuweza kupata fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine kwamba je, Silaha hizi tunakuwa tumezipata zikiwa zimeharibika au vipi? Silaha hizi zitakavyokuwa, zikiwa zimeharibika, zikiwa nzima, wajibu wetu tukizipata katika matukio ya kihalifu, maana yake ni kuzichukua. Kama itakuwa zimeharibika, maana yake tuna utaratibu wa kuzitengeneza. Ikiwa hazijaharibika, tunaiangalia; kama silaha ile ina kesi, tunaiacha kesi ile iendelee, ikimalizika, silaha ile inarudi Serikalini, inarudi jeshini, tunaendelea kuitumia kwa ajili ya Ulinzi na Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimepokea maelezo yake aliyonipa katika swali langu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, Serikali inafahamu kwamba, suala hili la mikopo linaathiri sana wakulima wetu. Je, Serikali haioni kwamba, sasa ni wakati wa kuwafungulia milango wakulima kuweza kuuza mazao yao wao wenyewe ikiwa ndani au nje ya nchi ili kuweza kunusuru mazao yao kuharibika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, Serikali inawajali wakulima na inawathamini. Je, kwa nini Wizara haitengi bajeti maalum kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima yale yanayorundikana majumbani ambayo yanakosa soko ili kuweza kuwasaidia wakulima wao kunusuru nguvu zao na maharibiko ya mazao yao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kufungua milango Serikali imefungua milango kwa mkulima mfanyabiashara yeyote wa mazao kuuza popote pale duniani na hatazuiliwa na mtu yeyote. Wizara ya Kilimo tunatoa vibali vya export bure kwa ajili ya kuuza mazao ndani na nje ya nchi na hakuna mfanyabiashara wala mkulima yeyote atakayezuiliwa kuuza popote anapopata soko.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuongeza bajeti kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima, sisi kama Wizara kama utakumbuka mpaka sasa hivi Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuongeza fedha za kununua mazao pale ambapo linapojitokeza tatizo na Serikali hununua mazao kwa sababu kubwa mbili.

Mheshimiwa Spika, moja kwa ajili ya kuhifadhi; lakini mbili kwa ajili ya ku-stimulate soko pale ambapo mazao ya wakulima yanaanguka bei. Na utakumbuka hapa Bunge lako Tukufu lilileta hoja na Wabunge waliibuka na hoja ya ku- rescue zao la mahindi na Serikali na Mheshimiwa Rais akaidhinisha matumizi ya shilingi bilioni 100 ambazo tumeenda kununulia mazao na mpaka sasa tunanunua mahindi kwa shilingi 500 kupitia taasisi yetu ya NFRA na ununuzi unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua ya kununua mazao tutaendelea kuifanya kadri ambavyo bajeti itakuwa inaruhusu na Bunge lako Tukufu likitupitishia fedha sisi tutaenda kutekeleza field. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa jawabu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wahitimu ambao wanashindwa kupata kazi au kujiajiri wanaamua kuondoka nchini kwenda nchi za nje kufanya kazi na wakati huo mkopo wao huku hawajalipa; ingawa kuna wazazi au wadhamini wanaambiwa wao wausimamie mkopo huo, mzazi huyu ni masikini, hana uwezo wala hajui ataipata wapi hiyo pesa: Je, deni hili hitalipika vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa baadhi ya wahitimu wako mitaani, hawana kazi, hawawezi kujiajiri na ambao elimu yao ni ya juu; na vile vile wahitimu hao wanapokuwa mitaani wanaweza kufanya mambo ambayo siyo mazuri kisheria, ingawa wao wanasema wanawapa elimu, kuna mkopo wa asilimia 10, wengine wajasiliamali.

Kwa nini wasingewakusanya wakawafundisha kazi za kujitegemea ambazo wazee wetu walikuwa wanafanya, kama upishi wa kitaalam, ufundi wa ujenzi, ufundi mchundo ila ni wa kitaalam kulingana na elimu yao waliyonayo na wakimaliza kuwapatia kitu kidogo ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye eneo la kwanza la wahitimu ambao wanamaliza na kwenda nje ya nchi kufanya kazi na huku wakiacha deni katika bodi yetu ya mkopo, kumekuwa na utaratibu mzuri wa Serikali kwa sasa wa kuendelea kuratibu watu ambao wako nje ya nchi (diaspora) wakiwa wanafanya kazi huko na kuweza kutengeneza arrangement za kuweza kuwafanya wao yale madeni yao yaweze kulipwa. Taarifa hizi tumekuwa tunazipata kutoka upande wa wadhamini wao ambao wanabaki hapa nchini. Kwa hiyo, suala hili tunaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwemyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa kwa kuliona na kuendelea kuwa mfuatiliaji ili fedha hizi zisipotee ambazo tunatarajia ziwasaidie vijana walio wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameuliza pia kuhusu wahitimu walio mtaani, kama kuna mpango wowote wa Serikali wa kuwasaidia. Tayari vijana wapo ambao wamechukuliwa na vyuo mbalimbali. Tunavyo Vyuo vya VETA ambavyo vinatoa mafunzo hata sasa. Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni tisa kwa kuwasaidia vijana zaidi ya 14,432 katika Vyuo 72 vya VETA hapa nchini na tayari wanaeleleka kuhitimu katika awamu ya kwanza katika miezi sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa sasa ukiangalia katika upande wa Wakala wa Ajira (TaESA) kumekuwa na utaratibu huo wa kuwasaidia vijana kupata ajira na pia kupata mafunzo ya namna ya kuomba kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, pia tumeingia katika mpango mwingine mpya. Sasa hivi tunafanya study ya kuangalia nchi nyingine ambazo zina changamoto kubwa ya masuala ya ajira na tunafanya study China, Marekani, Uswiss, Ubeligiji, Ufaransa, Rwanda, Burundi na Kenya ili tuweze kuangalia wenzetu kwenye eneo la ajira wamefanya kwa kiwango gani. Hivi karibuni nitatoa taarifa ya kuhusiana na changamoto za ajira jinsi nchi nyingine ambavyo wameendelea kuzikabili. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, kwa kuwa kituo cha Polisi cha Ng’ambo ambacho kipo Wilaya ya Mjini Unguja kina tataizo kama vituo kituo cha Polisi kilichozungumzwa. Na tatizo letu hasa ni uzio. Kwa sababu kituo hicho kipo katikati ya barabara pande zote, pia kimezungukwa na mitaa hatari ya magari yanaweza yakaingia ndani yakagonga kituo, au wanyama wanaofugwa mtaani wakaingia ndani na kituo hicho kipo tokea wakati wa ukolono, hakijaongezwa uzio, ulikuwa uzio wa senyenge umezungushwa na majani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuzungumza kwenye baraza hili tukufu kwamba wakati wowote utawekwa uzio toka bajeti tuliyoimaliza na tunaenda kwenye bajeti mpya hali hiyo haijatengamaa. Je, uzio huo utawekwa lini ili watu wa pale wapate amani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru, naomba sasa kujibu swala la nyongeza la Mheshimiwa bi Fakharia Mbunge wa viti maalum kutoka Mkoa wa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hichi ni moja ya miongoni mwa vituo vya Polisi ambavyo nimevifanyia ziara, na moja ya miongoni mwa vitu ambavyo tayari vimeshafanyika ni tathmini kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kituo kile, kalini wakati huo tunafanya tathmini tunaangali namna kwa sababu kile kituo ukikitazama unakuta kwamba kila pembe kimezungukwa na barabara. Kwa hiyo, the way utakavyojenga uzio kuna hatari ukaja ukajikuta kwamba unaila ile barabara. Sasa kula chote lakini usiile barabara kwasababu unaweza ukatengeneza mazingira mengine ambayo yanaweza kusababisha ajali za barabarani ambazo hazina sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba tathmini imeshafanyika na sasa tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kile, Mheshimiwa wewe kwa niaba ya wananchi muwe na subra kidogo mtusubirie na sisi tumo mbioni kuhakikisha kwamba uzio unajengwa katika kituo kile. Ahsante.