Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Ramo Matala Makani (5 total)

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza majibu mazuri ya Serikali kwa swali hili. Lakini pamoja na pongezi zangu hizo naomba kuwasilisha maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza takwimu zilizosomwa kwa ufupi zinaonesha kwamba kwa wastani uchangiaji wa mazao katika sekta ndogo hizo za kilimo, misitu na uvuvi ni 26.1%. Lakini pia wastani wa fedha za kigeni katika miaka hiyo mitano ni dola za Kimarekani milioni 864.68.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Taifa letu limepanda treni ya mwendo kasi inaitwa viwanda kwa ajili ya kukamilisha safari yake kuelekea uchumi wa kati inaonekana wazi kabisa, ushahidi upo unaoonesha kabisa juu ya umuhimu wa sekta hii ya kilimo, lakini mahususi kabisa mazao yale matano yaliyotajwa yaani tumbaku, korosho, kahawa, pamba na chai.
Mheshimiwa Mwenyeki, sasa maswali yangu ya nyongeza yatajikita zaidi kwa korosho kwa leo na nikisema kwamba swali la kwanza, kwa kuwa sasa tunataka mazao haya yachangie zaidi uchumi na kuongeza kasi hiyo yakufikia malengo ya Taifa ya kiuchumi. Je, Serikali inajipanga namna gani kuondoa vikwazo, kuondoa hali yoyote ile ambayo inawafanya wakulima washindwe kuzalisha zaidi? Kwa mfano kwa sasa hivi kule Tunduru wananchi wanapata matatizo ya upatikanaji…
Ndiyo, Serikali itaboresha namna gani utaratibu wa kibenki, unaowafanya Wananchi wa Wilaya ya Tunduru wapate shida katika kupata fedha zao baada ya kuuza mazao ya korosho miezi kadhaa iliyopita waondokane na misururu mirefu lakini pia na kusafiri kilometa nyingi zinafikia 120 na kukaa Makao Makuu ya Wilaya kwa siku mbili mpaka tatu? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili linausiana na suala la pembejeo, upande wa pembejeo ningependa kuzungumzia ubora wa pembejeo zenyewe, lakini pia ningependa kuzungumzia upatikanaji kwa wakati wa pembejeo zenyewe, lakini pia bei ya pembejeo zenyewe. Kwa ujumla Serikali inajipanga namna gani katika kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa Tunduru hasa wa zao la korosho, ni wa mazao yote lakini hususani wa zao la korosho kwa leo ili waweze kupata pembejeo hasa mbolea na madawa ya kuweza kuboresha, kilimo na hasa mazao ya ya korosho upande wa sulphur?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaifahamu changamoto hiyo ya wananchi wetu na hasa wakulima wetu wa kule Tunduru kwenda kupanga foleni katika mabenki yetu na hili hata Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda tarehe 10 Januari aliwasiliana na mimi akiwa Masasi, akiwa kwenye foleni na wananchi hao kwa ajili ya kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba kama ambavyo nimekuwa nikiliambia Bunge lako Tukufu kuanzia mwaka 1991 tuliingia katika soko uria kuhusu sekta ya kifedha na mabenki nchini. Lakini pia, mabenki yetu kwenda kufungua matawi maeneo mbalimbali huwa inahitaji kuangalia nguvu ya soko (demand and supply) katika hilo, maana na wao ni wafanyabiashara wanahitaji kupata faida wanapofungua matawi yao.
Ninafahamu kuhusu wakulima wetu wa korosho kule Tunduru na Mtwara kwa ujumla na Wilaya zake na zao hili ni la msimu kwa hiyo kunakuwa na wateja wa msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya kama Wizara ya Fedha kwa sasa ni kuongea na mabenki yetu kuona jinsi gani watafikisha huduma za mawakala (Agent Banking) au waweze kutumia Mobile Banking katika kuwahudumia Wananchi wetu wa maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili Serikali inatambua umuhimu wa mazao yote kwa ujumla na particular mazao haya matano niliyoyasema na ndiyo maana Serikali mwaka 2013 ilikuja na Regulatory Authority ambayo ni TFRA inayoshughulika na pembejeo za wakulima wetu. Tunaendelea kuimarisha wakala huu ili uweze kufanya kazi nzuri kuhakikisha wananchi wetu wanapata pembejeo wanazozihitaji hasa katika ubora na bei ambayo wanaweza kuihimili kuinunua.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa umahiri wake wa kijibu swali, siyo hili tu, hata mengine ambayo nimeshuhudia akiwa anayajibu. Naipongeza pia Wizara kwa ujumla kwa jinsi na namna ambavyo inachapa kazi kwa ufasaha na ufanisi. Pia kwa Serikali nzima ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Afya nikipita kwenye mitandao huko kote kwa kweli nataka kuipigia chapuo Serikali kwa performance hiyo. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatekeleza mpango mkakati iliyoutaja kwa mwaka 2016 mpaka 2020 na kwa kuwa katika utekelezaji wa mpango huo Serikali imezingatia maeneo matatu na moja ya maeneo hayo ni huduma wakati wa kujifungua na kwa kuwa katika huduma za wakati wa kujifungua mojawapo ya mahitaji muhimu ni chumba cha upasuaji na kwa kuwa ndani ya chumba cha upasuaji mojawapo ya vitu muhimu ni vitanda vya upasuaji ambavyo vinaitwa operation beds au operation tables; na kwa kuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru hospitali pekee katika Wilaya ambayo ina vijiji karibu 160 hali ya chumba hicho ni mbaya kwa maana ya miundombinu ya jengo lenyewe lakini pia na vifaa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kurekebisha chumba hiki cha upasuaji ili kiweze kuwa bora kabisa cha kuweza kutoa huduma kama sera inavyoelekeza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwanza naipongeza Serikali kwa kuboresha vituo vya afya hivi vichache ambavyo tunavyo. Isipokuwa vituo vyetu vya afya viko mbali sana kutoka kwenye Hospitali ya Wilaya na kwa hiyo, ili uweze kutoa huduma bora zaidi ya uzazi wa mpango au kutoa huduma vizuri zaidi kwa mpango wa uzazi na mtoto unahitaji kufikisha wagonjwa kwa wakati kwenye Hospitali ya Wilaya, lakini hatuna magari ya wagonjwa hata moja. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiomba Serikalini tuweze kupatiwa angalau...
Mheshimiwa Naibu Spika, swali sasa. Ni lini Serikali itaweza kuipatia Wilaya ya Tunduru gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwahudumia akina mama wajawazito pamoja watoto kwa ajili ya huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE, NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa kwa kufuatilia sana masuala ya afya na hususan afya ya uzazi katika Wilaya yake ya Tunduru. Takwimu zinaonyesha kwamba akina mama wa Tunduru wanafanya vizuri sana kwa kujifungulia katika Vituo vya Afya kwa zaidi ya asilimia 81 lakini vilevile katika matumizi ya uzazi wa mpango. Nawapongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na maswali yake ya msingi ambapo ameuliza kwamba, jengo pamoja na chumba cha upasuaji na upatikanaji wa kitanda cha upasuaji ni changamoto katika hospitali ya Wilaya, naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali zetu hizi pamoja na hii hospitali ya Tunduru ambayo ni hospitali ya Wilaya zina vyanzo mbalimbali. Kwanza, kupitia Serikali Kuu tumekuwa tunapeleka fedha za dawa. Naomba Waheshimiwa Wabunge, tunaposema fedha ni za dawa, haimaanishi ni dawa peke yake. Ni fedha za dawa, vitendanishi na vifaatiba. Meza ya upasuaji ni moja ya kifaatiba. Kwa hiyo, kuna vyanzo viwili ambavyo hospitali hii inaweza ikatumia ili kuweza kupata ile operating table na moja ya chanzo ni fedha zile tunazozipelekea katika hospitali yetu na katika mgao huu wa fedha mpaka sasa hivi Wilaya ya Tunduru tumeshapeleka shilingi milioni 268.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kingine ambacho wanaweza wakakitumia ni makusanyo yao ya ndani pamoja na makusanyo kupitia mfuko wa NHIF. Kwa hiyo, niendelee kumshauri Mheshimiwa Mbunge wakae katika ngazi yao ya Halmashauri na kupanga matumizi mazuri ya fedha ambazo wanazipata na wanazozizalisha katika hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, ameulizia kwamba ni lini Serikali itaipatia huduma ya Ambulance Hospitali ya Tunduru. Mimi niseme tu kwamba Serikali imeagiza magari na yatakapofika, tutaangalia vigezo vya uhitaji kulingaa na umbali na idadi ya vifo vya akina mama na watoto na Wilaya ya Tunduru itakuwa ni moja ya Wilaya ambazo tutazifikiria. (Makofi)
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napongeza majibu mazuri ya Serikali. Lakini la pili nampongeza pia huyu Mhandisi Mshauri Kampuni ya KORAIL kwa kuona kile ambacho hata kufanya upembuzi yakinifu wa wakitaalamu sana kinaonekana.
Kwa kuwa tunazungumzia mradi ambao unakwenda kuhudumia au kutafuta au kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na madini chuma, lakini pia makaa ya mawe, lakini mazao ya kilimo lakini pia urani lakini pia fursa za Ziwa Nyasa zinazotokana na shughuli za uvuvi kutaja machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali mwaka 2016 mpaka leo ni takribani miaka mitatu tangu upembuzi yanikifu ukamilishe kazi yake utoe matokeo.
Sasa je, Serikali inajipangaje kuharakisha utekelezaji wa mradi huu katika hatua inayofuata? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali naamini kwamba amesema mimi kama muuliza swali mmojawapo wa Wabunge na wenzangu wengine Bunge zima tuweze kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza jukumu letu la kuisimamia na kuishauri Serikali; na mimi nilikusududia hapo mwanzo kabisa kwamba niweze kujiandaa kwa hoja binafsi kuhusiana na mradi huu. Lakini kwa wakati huu na kwa sasa hivi na majibu haya ya Serikali ya leo yakiniridhisha basi nitaondoa ile azma yangu ya kwenda kwenye hoja binafsi.
Je, inawezekana kuunda Kamati Ndogo ya Wabunge ili waweze kushirikiana kwa karibu kabisa na Serikali katika kutafuta huyo Transaction Advisor? Ama hata hao wawekezaji ili tuweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nikuambie kwamba Liganga na Mchuchuma zimekuwepo, mali hii ni ya nchi na kwamba sasa wakati muafaka umefika kwamba sasa mali hii lazima itumike kwa ajili ya manufaa ya nchi. Tayari kama ulivyosema tangu mwaka 2016 Serikali iliona kwamba wakati muafaka umefika, tunahitaji kutumia haya madini kutokana na mahitaji ya kunyanyua uchumi wa nchi. Taratibu zimeshafanyika, Transaction Advisor sasa hivi anatafutwa ili kwenda kwenye mwelekeo sasa ya kupata mwekezaji ambaye ni mzuri atayekubalika na taratibu zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwamba shughuli hii inafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu, ushauri wako ni mzuri Mheshimiwa Mbunge. Lakini sioni kwamba sasa hivi kwa vile mambo yanaendelea kwamba Bunge. Kwa hiyo, niombe tu kwamba uiachie Serikali kwa sababu imeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na inakwenda vizuri.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini. Pia niipongeze Serikali bila hata kumung’unya maneno kwa namna ambayo kutokana na ujenzi wa barabara ya lami iliyounganisha Wilaya ya Tunduru na wilaya zingine na kuufanya Mkoa wa Ruvuma vilevile uweze kuungana na mikoa mingine kwa barabara ya lami. Wananchi wa Wilaya ya Tunduru kwa ujumla wanaipongeza na kuishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji inafanya kazi kwa kutegemeana, kusaidiana na kwa kushirikiana; baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara tumepanua fursa na kuweka mazingira ya kiuchumi na kijamii kuwa bora zaidi kwa maana ya kuvutia wawekezaji, lakini pia kuwahamasisha wananchi katika eneo hili. Sasa Uwanja wa Ndege wa Tunduru unauona umuhimu wake sasa zaidi kuliko hata ilivyokuwa hapo kabla. Je, Serikali itaingiza lini kwenye mipango ya ujenzi wa viwanja vya ndege, Uwanja wa Tunduru ukawa ni mmojawapo? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lakini kwa kuwa Serikali pia imekiri kwamba uwanja uliopo haujafungwa rasmi na unaweza ukaendelea kutumika na sisi tunahitaji utumike kwa kuwa mahitaji ni makubwa, wawekezaji wanashindwa kusafiri umbali mrefu sana kwa kutumia njia ya usafiri wa barabara. Je, uboreshaji wa kiwanja kilichopo ambacho kwa sasa hivi hali yake ni mbaya hakiwezi kutumika utafanyika lini kwa maana ya kwamba si uzio tu peke yake, runway na taxiway zinatakiwa kufanyiwa marekebisho lakini pia hata kibanda kwa ajili ya kupokea na kuruhusu abiria kuondoka?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Engineer Ramo Makani kwa jinsi ambavyo mara nyingi sana anafuatilia masuala mbalimbali yanayohusu ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kwa Jimbo lake la Tunduru Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna mradi wa ujenzi wa uwanja mpya kwa eneo ambalo tumeoneshwa na watu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduru, lakini bado kuna masuala ya fidia ndogo ndogo kwa wananchi. TAA ambao ni Wakala wa Viwanja vya Ndege wanaendelea kufanya tathmini ya malipo kwa wananchi ambao wanadai fidia zao kwa maeneo ambayo tutayachukua kwenye huu uwanja mpya ambao tunategemea kuujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba taratibu za ulipaji wa fidia kwa wananchi hao zitakapokamilika tutahitaji sasa tupate hati ya kumiliki uwanja huo kabla ya kuanza mradi wa ujenzi wa uwanja huo. Taratibu nyingine zote zitafuata baada ya kupata taratibu muhimu kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anauliza lini uboreshaji wa uwanja utaanza. Nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba tayari timu ya wataalam kutoka TAA imekwishatembelea pale kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi tangu mwaka jana mwezi wa Nne na wameshaona eneo la uwanja huo. Mahitaji muhimu kwa ajili ya kuboresha uwanja huo yameshaainishwa sasa hivi tupo kwenye taratibu za manunuzi kwa ajili ya kwenda kuuboresha uwanja huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Taarifa zinaeleza wazi na takwimu zinaonesha kwamba, takribani asilimia 45 ya bajeti ya Serikali iko upande wa miundombinu, lakini kati ya hizo asilimia 45 za bajeti nzima ya Serikali karibu asilimia 40 inakwenda kwenye maintenance. Maintenance ambayo ni matengenezo ya barabara baada ya kuwa zimekamilika na kuanza kutumia ni eneo ambalo kama Taifa tunatakiwa kuliangalia vizuri zaidi ili tuweze kuokoa fedha zinazokwenda huko kutumika kwa maintenance ziweze kutumika katika miradi mingine ya sekta mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Nikisema bajeti ya maendeleo kwa upande wa miundombinu, nazungumza ile bajeti ambayo iko Wizara ya Miundombinu pekee, lakini miundombinu pia, iko kwenye miradi mingine kama ya umeme, maji, mifugo, kilimo, elimu, afya, kote kuna miradi ya miundombinu ambayo tafsiri yake ni…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa muda unakwenda.

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, sasa nataka kuuliza swali, nilikuwa najenga mazingira ya kuuliza swali. Sasa kutoka na ukweli huo wa kwamba, fedha nyingi zinakwenda kwenye maintenance. Je, Serikali inajipanga namna gani licha ya hizi njia walizozieleza kwenye swali za kimaabara, upande wa watalaam Serikali inajipangaje kuhakikisha kwamba, wataalam wanaoshiriki katika kufanya kazi hizo wakati wa matengenezo ya barabara wanazingatia misingi ya kuwa na miundombinu bora ili isije ikasababisha kuwa na gharama kubwa upande wa maintenance?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Tunduru Kaskazini iko miradi ambayo nasisitiza kwamba, katika mipango yake Serikali inapokwenda kutekeleza iitekeleze miradi hiyo kwa kuzingatia viwango. Miradi hiyo ni pamoja na Barabara ya Mji Mwema kupitia Ngapa kwenda Nachingwea kwa kiwango cha lami, Barabara ya Mironde kwenda Kalulu mpaka Selous kwenye Hifadhi ya Taifa kule kwa kiwango cha changarawe, Barabara ya Nandembwe – Nampungu mpaka Mbatamira kwa kiwango cha changarawe na Barabara ya Kangomba kupitia Kidodoma mpaka Machemba na kule Chiwana kwa kiwango cha changarawe na pia mwisho kabisa Daraja la Fundi Mbanga. Je, Serikali itatekeleza lini mipango hii ya kutengeneza miradi hii kwa viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Makani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu nitoe shukrani sana kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kusukuma tuweze kupata fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza hii miundombinu muhimu. Pia nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi tumezungumza na ushauri wake tunaendelea kuuchukua, lakini nilishukuru Bunge kwa sababu limeendelea kututengea fedha za kutosha. Katika mwaka tu wa Fedha huu ambao tunaendelea nao Wizara yetu imetengewa trilioni 4.2, sasa hii ni fedha nyingi sana kuonesha concern ya Bunge nalo lipo pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali lake la kwanza niseme kwamba, yako mambo mengi kama Serikali kupitia Wizara hii ya Ujenzi tunafanya ili kuhakikisha kwamba, tunafanya kazi vizuri na kuboresha miundombinu. Kama unavyoshuhudia Mheshimiwa Makani sheria zimekuwa zikifanyiwa mabadiliko mbalimbali, kumekuwa na miongozo mingi inatolewa, lakini ziko programu nyingi sana ambazo hapa siwezi kuzitaja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kazi inafanyika kwa weledi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kupitia Bodi ya Wahandisi (ERB) tunaendelea kusimamia maadili ya wataalam wetu, tunaendelea kukuza namba ya wataalam katika nchi hii ili kuweza kusimamia miradi hii. Pia tutaendelea kuchukua hatua kwa wataalam hawa ambao watakwenda kinyume na utaratibu ambao tunautaka, lengo tu ni kuhakikisha kwamba, utaalam unatumika vizuri na miundombinu yetu inajengwa vizuri, lakini pia, tunaisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwango vya ujenzi wa barabara, amezungumza barabara hizi alizozitaja Mheshimiwa Mbunge. Natambua kwamba, barabara hizi karibu zote ziko kwenye upande wa TAMISEMI, lakini sisi kama Serikali, tunashirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba, barabara hizi zinaenda kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi, natambua kwamba, liko Daraja hili la Fundi Mbangai, hili daraja tayari upande wa Serikali za Mitaa kwa maana ya kupitia Halmashauri ya kwake waliomba utaalam kutoka kwenye Serikali na daraja hili limetengenezwa, isipokuwa zile approach road ndio zinahitajika kufanyiwa matengenezo. Naamini kutokana na concern ya Halmashauri yake hizi barabara zitatengenezwa, lakini Barabara hii ya Mji Mwema – Ngapa kwenda Nachingwea itaenda kutuunga na Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Ruvuma, upande huu wa Tunduru, hii Barabara kutoka Mji Mwema kwenda Ngapa tumeshaichukua na eneo la Ngapa pale tutahitaji kujenga daraja. Kwa hiyo, wananchi wa Tunduru wawe na imani kwamba, tutakwenda kujenga daraja hili ambalo litatuunga na Mkoa wa Lindi. Ahsante.