Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Ramo Matala Makani (6 total)

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Je, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni mazao yapi yaliongoza katika kuchangia Pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, mchango wa mazao ya kilimo, misitu na uvuvi katika pato la Taifa kwa kipindi cha miaka mitano iliopita ulikuwa ni asilimia 31.1 mwaka 2012; asilimia 25.0 mwaka 2013; asilimia mwaka 2014; asilimia 23.5 mwaka 2015 na asilimia 26.4 mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao yaliyoongoza katika mauzo kwenye soko la nje na kuchangia kwa sehemu kubwa katika pato la Taifa ni tumbaku, korosho, kahawa, pamba na chai. Fedha za kigeni zilizopatikana kutokana na mauzo ya mazao hayo ni dola za Kimarekani milioni 956.8 mwaka 2012, dola za Kimarekani milioni 868.9 mwaka 2013, dola za Kimarekani milioni 808.8 mwaka 2014, dola za Kimarekani milioni 793.4 mwaka 2015 na dola za Kimarekani milioni 895.5 mwaka 2016.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Serikali inatekeleza sera inayohusisha huduma bora za afya ya mama na mtoto.
Je, utekelezaji huo umenufaishaje Jimbo la Tunduru Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya mama na mtoto ni moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika Sera ya Afya mwaka 2007. Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2016 hadi 2020, ambao unajulikana kama National Road Map Strategic Plan to Improve Reproductive Maternal, New Born, Child and Adolescent Health in Tanzania, unaolenga kuboresha afya ya uzazi ya mama mtoto na vijana. Katika kutekeleza mkakati huu, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa uzazi na huduma wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, Serikali imehakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za uzazi na mtoto ikiwemo dawa ya uzazi wa mpango kwa maana ya (sindano ya depoprovera, vipandikizi na vitanzi) dawa za watoto (ORS zinc) kwa ajili ya kutibu kuharisha na dawa za antibiotics za watoto ya amoxyllin kwa ajili ya kutibu nimonia) dawa za uzazi salama ikiwepo dawa ya kuongeza uwingi wa damu kwa maana ya Fefol, dawa ya kuzuia mama mjamzito kupoteza damu baada ya kujifungua kwa maana ya oxytocin na dawa ya kuzuia kifafa cha mimba kwa maana ya magnesium sulfate.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mpango wa kukarabati na kupanua vituo vya afya 208 nchini ili viweze kutoa huduma za uzazi wa dharura, ambapo Kituo cha Afya cha Mkasale kilichopo katika Wilaya ya Tunduru kimepewa fedha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ikiwemo chumba cha upasuaji, jengo la huduma za mama na mtoto, maabara na nyumba ya mtumishi. Kituo cha Afya cha Matemanga kimetengewa fedha katika awamu inayofuata.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Reli ya Kusini (Southern Circuit) ya Mtwara - Mbambabay - Mchuchuma - Liganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali napenda kufanya rekebisho dogo ni kwamba isomeke ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, siyo Tunduma. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imedhamiria kujenga reli ya Kusini kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa mwaka 2016 na Kampuni ya KORAIL ya Korea kuonesha kuwa mradi huu unaweza kurejesha gharama za uwekezaji za sekta binafsi kutokana na fursa lizizopo katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa umbembuzi yakinifu huo Mhandisi Mshauri alipendekeza mradi huu utekelezwe kwa utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi na umma yaani PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetenga kiasi cha shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kumpata mshauri wa uwekezaji yaani Transaction Advisor wa kuandaa andiko la kunadi mradi huu na kutafuta wawezekaji kwa utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi na sekta ya umma (PPP), tathimini ya kumpata Transaction Advisor mahili inaendelea baada ya kujitokeza washauri 12 wanaoshindanishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa andiko Shirika la Reli Tanzania (TRC) litatangaza zabuni katika vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kumpata mwekezaji mahiri na mwenye masharti yanayovutia. Aidha, naomba ushirikiano wa Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kupata wawekezaji mahili katika endelezaji wa reli hii muhimu.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kujenga uwanja wa ndege mbadala katika Mji wa Tunduru baada ya uwanja uliokuwepo awali kuhamishwa kutoka katikati ya mji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa mpaka sasa hivi Kiwanja cha Ndege cha Tunduru hakijahamishiwa rasmi kutoka katikati ya Mji wa Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu ilituma timu ya wataalam wake kutembelea viwanja vya ndege vya mikoa ya kusini ili kujionea na kutathmini hali halisi ilivyo katika viwanja hivyo ikiwa ni pamoja na changamoto za kuzungukwa na makazi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Tunduru ni miongoni mwa viwanja sita vya ndege vilivyotembelewa na timu hii mnamo mwezi Aprili, 2017. Viwanja vingine vilikuwa ni Kiwanja cha Newala, Masasi, Songea na Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga eneo mbadala kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha Ndege cha Tunduru katika eno la Chingulungulu, Kata ya Muhesi, Tarafa ya Nakapanya, takriban umbali wa kilometa 17 kutoka Mjini Tunduru. Aidha, kiwanja cha sasa cha ndege cha Tunduru bado kinafaa kwa matumizi ya ndege na abiria isipokuwa kinahitaji kujengewa uzio ili kuimarisha usalama kiwanjani hapo wakati taratibu za kuhamia eneo jipya zikiwa zinaendelea.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mipango ipi ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika matengenezo ya miundombinu nchini baada ya ujenzi wake kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja, Serikali ilianzisha Bodi ya Mfuko wa Barabara mwezi Julai, 2000 kwa lengo la kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo ya madaraja. Ili kukabiliana na changamoto za matengenezo ya miundombinu ya barabara baada ya kukamilika kwa ujenzi, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya matengenezo kila mwaka kupitia Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara nchini. Bajeti ya matengenezo ambayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka inatumika kufanya matengenezo ya kawaida, matangenezo ya muda maalum, matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo ya madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu ilivyoanzishwa Bodi ya Mfuko wa Barabara bajeti ya matengenezo imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2000/2001 zilitengwa Sh.44,436,708,674 na Mwaka wa Fedha 2010/2011 zilitengwa Sh.286,907,000,000 na Mwaka wa Fedha 2018/2019 zimetengwa jumla ya Sh.908,808,000,000. Mfuko huu unaimarishwa kila mwaka ili miundombinu ya barabara na madaraja iweze kutengenezwa na kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inaendelea kudhibiti uzito wa magari kwa kujenga mizani na kupima uzito wa magari kwenye barabara zote za lami zilizokamilika na zinazopendelea kujengwa nchi nzima ili kuzinusuru barabara hizo kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na magari yanayozidisha uzito. Mizani inajumuisha mizani ya kudumu, mizani inayohamishika na mizani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo, yaani Weigh in Motion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea kufanya tafiti mbalimbali kupitia Maabara Kuu ya Vifaa vya Ujenzi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Afrika Kusini, lengo ni kubaini sababu za baadhi ya barabara hapa nchini kuharibika katika kipindi kifupi mara baada ya kukamilika. Wizara kupitia TANROADS tayari imekwishatoa mwongozo wa usanifu wa uchanganyaji wa lami, yaani Guideline for Asphalt Mix Design, unaozingatia mabadiliko ya mifumo ya miundo na vyombo vya usafiri, hali ya hewa na viwango sahihi vya vifaa vya ujenzi wa barabara. Mwongozo huu ulianza kutumika Mwezi Novemba mwaka 2018.
MHE. JEROME D. BWANAUSI (K.n.y. MHE. ENG. RAMO M. MAKANI) aliuliza:-

(a) Je, nini mpango wa Serikali kukamilisha mradi wa maji safi unaoendelea katika Mji wa Tunduru ili kuwaondolea wananchi hao adha kubwa wanayoipata ya uhaba wa huduma hiyo?

(b) Jimbo la Tunduru Kaskazini lina vijiji 92 ambapo taarifa za Serikali na takwimu zinaonesha kiwango cha upatikanaji wa maji kuwa chini sana:-

Je, ni lini mpango wa Serikali wa kuongeza kiwango hicho cha upatikanaji wa maji katika vijiji hivyo kufikia kiwango kilichowekwa kwa mujibu wa mipango ya Serikali na Ilani ya CCM itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramo Makani, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2016/2017 Mji wa Tunduru ulitengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji Mjini Tunduru na kuongeza hali ya upatikanaji wa maji. Uboreshaji huo ulisaidia kuongeza huduma ya maji kutoka asilimia 52 mwaka 2017 kufikia asilimia 66 kwa sasa. Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, kupitia mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Songea, inaendelea na utaratibu wa kutekeleza mradi wa upanuzi wa miundombinu ya maji kwa mji wa Tunduru ambapo wananchi wengi zaidi watapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Tunduru Kaskazini lina jumla ya vijiji 92 vyenye vituo vya kuchotea maji 385 vinavyohudumia wakazi wapatao 58,250. Katika kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaongezeka katika vijiji vilivyopo, Jimbo la Tunduru Kaskazini, Serikali inatekeleza miradi miwili ya Nandemo ambao umekamilika na mradi wa Matemanga ambao umefikia asilimia 85 ya utekelezaji na utahudumia vijiji vya Matemanga, Milonde, Changarawe na Jaribuni. Lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji vijijini inafikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2020 kama inavyoelekeza Ilani ya CCM.