Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ruth Hiyob Mollel (25 total)

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza. Pale Muhimbili tumepata vifaa vya kisasa vizuri sana lakini gharama za vifaa hivyo kwa mfano pacemaker ni kama shilingi milioni tano mpaka milioni sita na kitu kama angiography ni kama shilingi milioni mbili. Je, Serikali kwa nini haitoi ruzuku ili kuwawezesha wagonjwa wanaokwenda pale kupata tiba kwa bei nafuu pamoja na Hospitali ya Ocean Road ambapo chemotherapy ni ghali sana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itaendeleza utaratibu wa kuleta Majopo ya Madaktari kwa ajili ya magonjwa mengine ambayo yanawapeleka wagonjwa nje?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na la pili kwamba ni lini Serikali itaendeleza utaratibu wa kuleta Majopo ya Madaktari kwa ajili ya kutoa tiba. Jibu lake ni rahisi tu kwamba, tunaendelea kuleta Majopo ya Madaktari kutoka nchi mbalimbali rafiki na nchi yetu kwa ajili ya kutoa huduma hizi kwa Watanzania walio wengi. Mfano mzuri ni Ijumaa iliyopita nilikwenda kuwashukuru na kuwapongeza Madaktari kutoka nchi za Qatar na Saudi Arabia ambao walifanya operesheni 75 kwa watoto wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza katika nchi yetu tumefanya operesheni ya coronary bypass ambapo tunapindisha mzunguko wa damu kwenye mishipa midogo midogo ya juu ya moyo, inaitwa coronary arteries na tumefanya kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu. Kwa hiyo, utaratibu huo upo na unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi wa Mkuu wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi na timu yote ya wataalam kwenye hospitali ile kwa jitihada mbalimbali wanazofanya kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo zinapatikana hapa hapa nchini kwa kiwango cha juu na kwa maana hiyo kuipunguzia Serikali gharama na kuwapunguzia wananchi wa Tanzania usumbufu wa kusafiri nje ya nchi kufuata huduma hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kuhusu gharama za vifaa na kwamba Serikali haitoi ruzuku hiyo siyo sahihi. Gharama za afya ni kubwa mno na hivi tunavyoongea hapa Serikali inapaswa kupongezwa tu kwa kuendelea kutoa ruzuku kwenye huduma za afya nchini. Nalisema hili kwa sababu moja, asilimia 70 ya Watanzania wanaokwenda kutafuta huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma hizo kwa kiasi kikubwa wanazipata bure, hawalipi chochote na kwa maana hiyo ni subsidize services za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivi tunavyoongea, tunaweka utaratibu mpya kwenye bajeti hii kwa ajili ya vifaa alivyovisema kama vya angiogram pamoja na pacemaker viweze kutolewa kwa ruzuku na Serikali. Juzi Mheshimiwa Waziri amewaelekeza Taasisi ya Jakaya Kikwete waweke utaratibu huo na naamini kwenye mwaka huu wa fedha sasa hakutokuwa na kulipia gharama za pacemaker na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Ocean Road, matibabu yake niliyaeleza hapa jana vizuri sidhani kama Mheshimiwa Mbunge hakunisikia, naomba nitunze muda wako tu. Tumetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya chemotherapy kwenye bajeti hii.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni kwamba kwenye jibu lake la msingi la (b) anazungumzia malipo haya ya 2014, ni lini basi atatuambia pesa hizi zitalipwa ili Halmashauri ya Kaliua iweze kufanya shughuli zake kwa kutumia fedha hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni la ujumla, kwamba miradi kama hii inafanywa katika sehemu nyingi za nchi, lakini mara nyingi pamoja na kufanya social na environmental impact assessment bado wananchi huachwa mpaka wakapata mateso ndipo Serikali ikaja kuwalipa baadaye. Je, Serikali inatuambia nini kwamba sasa watakuwa wanafanya malipo kabla ya athari kupatikana kwa wananchi? Atupe majibu ni lini. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa malipo ambayo yalitarajiwa kulipwa kwa kipindi hiki cha 2014 yangekuwa yameshafanyika hadi sasa, lakini hadi sasa hayajafanyika. Napenda nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba, TANROADS imeshafanya mahesabu na imeshamwandikia sasa mkandarasi kwa ajili ya kuanza malipo. Kwa sasa tumejipanga TANROADS pamoja na wenzetu, wataanza kulipwa kuanzia Agosti hadi Septemba mwaka huu kulingana na upatikanaji wa fedha
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kuhusiana na malipo kufanyika mapema. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ni kwamba kabla ya shughuli za madini hazijaanza kufanyika, kazi inayotakiwa kufanyika kwanza ni kufanya tathmini na tathmini ikishafanyika na malipo yakakubalika na wadau wakakubaliana kuhusiana na malipo ya fidia, kawaida malipo huwa yanafanyika kabla ya shughuli kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiri tu kwamba kwa sababu wakati wanaanza uchimbaji wa kokoto wa kwenye barabara hii, tathmini zilichelewa kukamilika, kwa hiyo, malipo hayakuanza kufanyika mapema. Hata hivyo, kwa taratibu ambazo tunaanza kuanzia sasa, malipo yatakuwa yanafanyika kabla ya wananchi kuathirika. Kwa hiyo, malipo ya fidia yatakuwa yakianza kufanyika kabla ya shughuli za uchimbaji wa kokoto kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi hatuwezi kusema zitaanza lini kwa sababu walishaanza kuathirika na malipo hayajafanyika, lakini malipo yote ambayo hayajafanyika kwenye barabara hii, yatafanyika kati ya Septemba hadi Oktoba mwishoni mwa mwaka huu bila kuchelewa kwa ushirikiano wa wadau, TANROADS pamoja na Halmashauri ya Kijiji.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ufasaha wa lugha yoyote ile ni ajira na Kiswahili ni kimojawapo. Tanzania ni kitovu cha lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kufahamu Wizara ina mkakati gani wa kufunza na kutoa walimu wengi ambao wanaweza kupelekwa nchi mbalimbali, kwa mfano, Uganda, Rwanda sasa hivi wameanzisha Kiswahili kwenye shule zao na ninaamini Watanzania ndio wenye lugha fasaha ya Kiswahili. Je, kuna mkakati gani kufundisha walimu wa kutosha wa kuweza kuwapeleka nchi mbalimbali ambao wanazungumza Kiswahili na kutoa ajira kwa wananchi wetu? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba kitovu cha Kiswahili ni hapa nchini kwetu Tanzania na kwa kulitambua hili, nchi za Afrika Mashariki wameamua Makao Makuu ya Kiswahili yawe hapa nchini na yamepelekwa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na tumekuwa tukizalisha Walimu wa Kiswahili wengi kadri inavyowezekana; na siyo tu kuwazalisha, lakini kuwatafutia soko na wamekuwa wakipata masoko siyo tu katika Afrika na Afrika Mashariki, lakini hata nje ya nchi yetu na hasa China wamekuwa wakienda kwa wingi sana. Chuo Kikuu cha Zanzibar, kwa mfano SUZA, wamekuwa wakizalisha Walimu wengi sana wa Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia huu mchakato sasa wa utengenezaji wa Sera ya Lugha ambao utaipa nguvu kubwa Kiswahili kama lugha ya nchi yetu, tutaweka mikakati ya kutosha ndani mle na sheria baada ya sera kukamilika ambayo itatusaidia zaidi kukifanya Kiswahili kiendelee kuwa bidhaa na hivyo kuwapa soko kubwa walimu ambao tutakuwa tukiwazalisha nchini kwetu.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo sijayafurahia sana mimi kama mstaafu, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pensheni hii ambayo tunalipwa kila mwezi kwa kadri miaka inavyokwenda gharama zinapanda na shilingi inashuka thamani. Nimemshuhudia hata baba yangu mzazi Mungu alimjalia umri wa miaka 90 lakini ile pensheni aliyokuwa anapata na alikuwa mtu mkubwa sana Serikalini ilikuwa kidogo sana kama asingekuwa na watoto wenye uwezo angekuwa ombaomba. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba pensheni hizi za wastaafu zinawekewa hata percentage kidogo kusudi wasiwe ombaomba baada ya miaka kadhaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hifadhi hizi za jamii zimewekeza sana kwenye majengo, Mheshimiwa Rais juzi alisema wawekeze kwenye viwanda. Je, imefanyika actuarial study kuona kwamba hii mifuko haitafilisika na baadaye kuleta adha kwa wanachama?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la kwanza la pensheni kidogo na kutaka kujua mkakati wa Serikali, katika utaratibu wa ulipaji wa mafao kipo kitu kinaitwa indexation ambacho ndiyo imekuwa ni nyongeza ya kiwango ambacho kimekuwa kikilipwa kila mara kwa wastaafu. Kwa takwimu zilizopo, wastaafu wengi walikuwa wakilipwa kima cha chini cha Sh.50,000 mpaka pale ambapo lilitoka tamko kupitia SSRA ambapo sasa hivi wastaafu wanaanza kulipwa kuanzia Sh.100,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko uliobaki ni mfuko wa LAPF tu lakini mifuko mingine yote sasa wataanza kuwalipa wastaafu kima kile cha malipo kuanzia Sh.100,000 na kuendelea na wamekwishaanza. Kwa hiyo, nimwondoe tu wasiwasi kwamba mifuko hii kadri inavyozidi kufanya uwekezaji wake na kadri ambavyo returns za investment zinaongezeka, watafanya kitu kinaitwa indexation kuweza kusaidia ili wastaafu wao waweze kukidhi maisha na mahitaji ya dunia ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili lilikuwa ni la wasiwasi ya kwamba, je, mifuko hii ikienda katika uwekezaji wa viwanda haitashindwa kweli kutimiza majukumu yake ya msingi? Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, katika utaratibu wa uendeshaji wa mifuko hii, kuna kitu kinaitwa actuarial valuation ambapo huwa inafanya tathmini ya afya ya mfuko. Mpaka maamuzi haya yanafanyika ni kwamba mifuko hii tayari inao uwezo wa kwenda kufanya uwekezaji huo pasipo kuathiri michango au mafao ambayo wanachama wanastahili. Kwa hiyo, nimwondoe hofu kwamba study ya uhakika imefanyika ya kuifanya mifuko hii iende kufanya uwekezaji katika uchumi wa viwanda.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala mtambuka na watu wote wanahitajika kulinda mazingira.
Juzi au jana nafikiri, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alitoa taarifa kwamba ni marufuku kuanzia Julai kusafirisha mkaa kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine, lakini tukumbuke kwamba miti ni nishati ambayo inatumika na watu wote, hasa mijini na vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, si muda muafaka sasa kwa Serikali kutoa ruzuku au tuseme kusubsidize gesi asilia kusudi watu wengi waweze kutumia gesi badala ya kutumia nishati ya mkaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mollel, ambaye kwa kweli ndiye alikuwa Katibu Mkuu wa Ofisi hii ya Makamu wa Rais katika miaka ya nyuma iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba sasa ni muda muafaka kwa Serikali kutoa ruzuku, ndivyo
tunavyofanya na ndiyo maana mnaona mambo mengi ambayo tunayafanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba gesi
hii asilia pamoja na gesi imported zinakuwa na bei ambayo wananchi wanaweza ku-afford pamoja na jitihada
nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoweza kusema tu kwamba, ni muda muafaka sasa wa Serikali
kuendelea. Kwa hiyo, tutaendelea hivyo. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuhakikisha
tunafanya bidii kadiri inavyowezekana. Kwanza kuhakikisha kwamba, gesi asilia inasambaa nchini, lakini vilevile
kuhakikisha kwamba, imported gas inauzwa kwa bei nafuu ili wananchi wengi waweze kuitumia, waweze kuachana na nishati ambayo inapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira kwa maana ya ukataji wa miti hovyo.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini shule za Serikali hawaweki provision ya kuwa na fire extinguisher ambayo inaweza ikatumika mara tu kama huduma ya kwanza wakati magari ya zimamoto yanaposubiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukiangalia kesi hizi za majanga ya moto na siyo shuleni peke yake hata katika maeneo mbalimbali, ni kwa sababu katika kipindi kirefu tulikuwa tumejisahu kuweka fire extinguisher. Ndiyo maana sasa tumetoa maelekezo katika shule zetu mbalimbali miongini mwa vitu ambavyo tunatakiwa tuviweke viwe vya msingi ni suala la fire extinguisher. Hata hivyo, katika ujenzi wa mabweni yetu, zamani mabweni yalikuwa yakifunguka yanafungukia ndani, hata janga la moto likitokea watoto wanavyogombania kufungua mlango kumbe ndiyo wanazidi kuufunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika suala la specification tukasema na mabweni yetu sasa hivi yote milango inafungukia kwa nje ili kwamba inapotokea hatari ya moto basi watoto wakiwa wanatoka mlangoni, iwe ni rahisi sana kuweza katoka katika eneo lile pindi janga la moto linapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni agizo letu na ninaomba niwasihi sana ni waagize Wakurugenzi wote katika Halmashauri zetu kuhakikisha katika maeneo ya shule zetu zote zinakuwa na fire extinguisher as a back up strategy, endapo moto unapotokea, wakati unasubiria kupata magari ya kuzima moto yaje, tuwe na mbinu mbadala wa kuweza kudhibiti moto mapema zaidi.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ili hawa watumishi wa Serikali za Mitaa waweze kutoa huduma kwa ufanisi wanahitaji kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji wao. Kwa kuwa kwa muda mrefu mafunzo yamesimamishwa, tunategemeaje hawa watumishi waweze kutoa huduma ipasavyo? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, viongozi ambao wako karibu sana wananchi ni Watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Kata, ndio wapo karibu sana na wananchi na ndio ambao wanatoa huduma karibu kabisa na wananchi. Watendaji wanapata mshahara lakini Wenyeviti hawapati chochote. Je, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya kuwamotisha Wenyeviti ili waweze kutoa huduma vizuri kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo yamejengewa uwezo kwa hali ya juu kabisa ni hili eneo la Serikali za Mitaa. Kuna programu nyingi sana za kisekta zimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa nyakatii mbalimbali. Kuna Programu kwa mfano ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji, zote hizi zimekuwa na mafunzo mbalimbali kwa watendaji wa Serikali za mitaa kwa ajili ya kuimarisha uwezo wao, hasa hasa zile kada za fedha, ununuzi na wahandisi. Serikali inatoa commitment ya kuendelea kutoa mafunzo mara fedha zinapopatikana.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu posho za Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Vitongoji. Mwongozo uliopo ni kwamba kila Halmashauri inatakiwa iboreshe makusanyo yake ya ndani, iongeze makusanyo yake ya ndani na mwongozo uliopo ni kwamba asilimia 20 ya mapato yake ya ndani yanatakiwa yatumike kwa ajili ya posho na agizo ambalo limetolewa na kusisitizwa na Serikali ni kwamba wale ambao wanachelewesha kulipa posho za wenyeviti wa vijiji na vitongoji sasa itabidi wachukuliwe hatua.
MHE. RUTH. H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali ndiye msimamizi mkubwa wa usalama wa raia na mali zao, ningepa kufahamu ni kwa jinsi gani Serikali inasimamia kwa uhakika hizi sekta binafsi za ulinzi ili kuhakikisha wale wote walioajiriwa hawana historia ya uhalifu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia taasisi zake mbalimbali imekuwa ikihakikisha kwamba kuanzia katika eneo la usajili wa makampuni haya ambayo pamoja na kwamba utaratibu wa usajili wake ni kupitia BRELA, lakini bado Jeshi la Polisi nalo lina nafasi ya kuweza kupitia na kuyatathimini maombi ambayo yanapekwa ili kujihakikishia. Kwa sababu kazi ambayo inakwenda kufanywa hapa na sekta ya ulinzi binafsi ni kazi ambayo vilevile ni ya kulisaidia Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu kwa mujibu wa viwango vya Umoja wa Mataifa askari mmoja anapaswa kulinda watu na 450, lakini sisi kwetu askari mmoja analinda kuanzia watu 1,150 mpaka 1,300. Kwa hiyo, ndiyo maaan kama Serikali tunatoa kipaumbele na ndiyo maana katika shughuli mbalimbali za sekta ya ulinzi binfsi tunahakikisha kwamba tunashirikiana nao katika kutoa elimu, lakini vilevile na kuzisimamia kuona kwamba zinayanya kazi ile iliyokusudiwa ili hatimaye isije ikaleta madhara makubwa kwa sababu na yenyewe pia ni sehemu ya ulinzi katika nchi yetu.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa miradi mikubwa ya maji inachukua muda mrefu sana, ni kwa nini sasa Serikali haichimbi visima vifupi na virefu kwa kila mita 400 ili kupunguza adha ya maji kwa akinamama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, jambo lolote kubwa na jambo zuri lenye kuleta utekelezaji mkubwa na manufaa kwa wananchi lazima lichukue muda, lakini jambo litakalokuwa bora na lenye tija kwa wananchi. Kikubwa kuhusu suala zima la kuchimba visima vifupi; sisi kama Wizara tunafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata maji salama na yenye uhakika. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nitoe taarifa kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ametoa fedha maalum, Sh.3,900,000,000/= kwa ajili ya uchimbaji wa visima na fedha hizo tumekabidhi Mamlaka yetu ya Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA). Kwa hiyo, tunaendelea kuchimba visima Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Chalinze Wilayani Mdaula, kuna zahanati ambayo wananchi kwa nguvu zao wamekuwa wanaijenga tangu mwaka 2012. Wamejenga, wameweka plasta, wameweka madirisha, lakini bado wanasuasua kwa sababu uchumi siyo mzuri. Sasa swali langu kwa Serikali, ni lini sasa Serikali itaongeza nguvu ya Serikali kuwasaidia wananchi ile zahanati imalizike kusudi wananchi waweze kupata mahali pa kwenda kupata tiba? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Naibu Waziri wangu kwa ufafanuzi mzuri wa maswali yote ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu Mdaula na maeneo mengine kuna changamoto, wananchi wamefanya juhudi kubwa na ndiyo maana azma ya Serikali yetu ni kuhakikisha kwamba tunaunga mkono juhudi za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo, sasa hivi tunafanya uwezeshaji wa kuangalia jinsi gani tutafanya kuhakikisha maboma yote yaliyojengwa katika Halmashauri zetu tunayakamilisha. Tutatumia takribani shilingi bilioni 69 ambapo jambo hili maeneo ya Mdaula pale, hasa Halmashauri ya Chalinze tutawaelekeza wahakikishe katika umaliziaji wa maboma hayo, ile Zahanati ya Mdaula iweze kutengewa fedha katika hizo fedha ambazo tutazitoa kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo lile wanapata huduma za afya, kama azma ya Serikali ilivyokusudia.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REA linahusu pia, Kata ya Soga, Kibaha Vijijini ambapo katika Kijiji cha Zogowale umeme ulifika kwa ajili ya ku-pump maji mpaka umefika Shule ya Waamuzi, Sekondari. Wananchi wa Kijiji cha Msufini walihamasishwa kutoa mazao na kutoa ardhi kwa ajili ya kupitisha umeme wa REA, huu ni mwaka wa tatu na hiyo kazi haijafanyika. Je, Wizara ina mpango gani kuhakikisha wale wananchi ambao wameshatoa mimea yao na wametoa ardhi zile nguzo za umeme zipite mpaka ufike Msufini pale Kata ya Soga na vijiji vya karibu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na napenda nimshukuru Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani. Nimthibitishie maeneo aliyoyataja Zogowale na hapo Kijiji cha Msufini kwamba, maeneo haya yamezingatiwa katika Mradi wa Peri Urban ambapo kwa kweli Serikali baada ya kuona kuna maeneo ni vijiji ambavyo vimekuwa na ongezeko la makazi na vimekuwa vikubwa, Serikali ikaja na Mradi wa Peri Urban ambao ni nje ya REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, nimtaarifu na nimthibitishie vijiji hivyo vipo katika mradi huu Mpya wa Peri Urban ambako kazi ilitangazwa na mchakato wa kumtafuta mkandarasi sasa unaendelea. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakipata maafa makubwa sana kwenye migodi na ukaguzi mnasema unafanyika, ningependa kujua huu ukaguzi unafanyika kwa mfano kila mara baada ya miezi mingapi ili tujue kwamba kweli hawa watu wanasimamiwa ili kusudi kuepusha hizi ajali zinazotokea mara kwa mara.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi kwenye migodi ni utaratibu maalum wa Wizara yetu ya Madini kukagua mara kwa mara na hatuna muda maalum, wakati wowote kwenye migodi tunakwenda tunakagua kujiridhisha kama kuna compliance ya kufuata sheria yetu ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye migodi yote ziko Kamati ndogo ndogo za ndani kwenye hiyo migodi ambazo zinafanya kazi ya ukaguzi. Niwaombe wamiliki wote wa leseni kuzitumia Kamati hizi za ukaguzi ili tuweze kupunguza maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wachimbaji wadogo wenyewe waangalie usalama mahali pa kazi, kwa sababu mtu wa kwanza wa kuangalia usalama wake ni yeye mwenyewe mchimbaji kabla ya Serikali kuja. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu yake lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ingie madarakani annual increment zimesimama na hata kwa bajeti hii ya mwaka huu, ya Waziri wa Fedha aliyoitoa juzi hakuna mahali popote tunaona kuna increment yoyote kwa ajili ya Watumishi wa Umma. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mishahara ya watumshi inaboreshwa ili waweze kupambana na hali ya uchumi na hali ya maisha ambayo imepanda?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vile vile tangu Awamu ya Tano imeingia madarakani training ilikuwa imesimamishwa na training ni sehemu moja ya kuwapa watumishi motisha na kuwawezesha kupata weledi. Je, Serikali itaanza lini kutekeleza mpango wa mafunzo ambao upo na haujatekelezwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la annual increment nadhani kama atakuwa alifuatilia vizuri hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa Mei Mosi ilielezwa kabisa bayana kwa Vyama vya Wafanyakazi annual increment mwaka huu itakuwepo.
Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia katika bajeti ya mshahara maana yake yeye amesema kwamba hajaiona, obviously kwenye bajeti ya mshahara huwezi kusema sasa hapa hii ndio itakuwa nyongeza ya mwaka. Bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni trioni 6.6, bajeti ya mwaka huu ni nadhani trioni 7.25.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, asubiri aone katika mwaka wa fedha utakapoanza endapo annual increment hiyo itakuwepo au la! Nadhani tusichanganye na kima cha chini cha mshahara, nadhani atakuwa ameelewa kwa sababu yeye amekaa Utumishi anafahamu, lakini nimtoe hofu nimweleze tu kwamba Mheshimiwa Rais alishaahidi kupitia siku ya Mei Mosi kwamba nyongeza ya mwaka itakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kupandisha Watumishi mishahara Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mara hali ya kiuchumi inapoimarika na tumekuwa tukijitahidi na tutakuwa tukifanya hivyo kila mara kwa mujibu wa takwimu, lakini vilevile kwa kuangalia mfumuko wa bei pamoja na takwimu nyinginezo zinazotolewa na shirika letu la NBS.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mafunzo; mafunzo hayajawahi kusitishwa, mafunzo yanaendelea na hata kama mkiangalia katika bajeti mbalimbali za Mawizara zilizopitishwa, kupitia kwa waajiri wao na Maafisa Masuuli wamekuwa wakitenga bajeti zao. Niendelee kusisitiza kupitia Bunge lako Tukufu waajiri waendelee kuweka mipango yao ya mafunzo ya kila mwaka, wajitahidi kufuatilia mipango hiyo lakini zaidi waweze kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza na kutoa weledi kwa ajili ya watumishi wao.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali aliloulizia Mheshimiwa aliyezungumza sasa hivi, halina tofauti kabisa na Gereza la Keko ambalo miundombinu yake ni mibaya na pia kuna msongamano mkubwa sana wa wafungwa na wengi wao zaidi ya nusu ni mahabusu na hivyo hivyo kwenye Gereza la Segerea.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba justice inakuwa dispense, mapema watu watoke na magereza yawe na wafungwa ambao ndio wangestahili kukaa pale na hiyo miundombinu iliyokuwepo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, tunakiri juu ya tatizo la msongamano, kwani ukiangalia takribani Magereza yote kwa ujumla nchini ukiachia mbali la Keko na mengine, mpaka leo tunavyozungumza, tuna takriban wafungwa wanaokadiriwa kufika mpaka 40,000 na wakati capacity ya Magereza yetu haizidi 30,000. Kwa hiyo, utakuta tuna idadi ya wafungwa kama 10,000 hivi ambao wamezidi kiwango magerezani.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali inachukua jitihada mbalimbali kupunguza msongamano huu ikiwemo kupitia zile sheria nne tulizozipitisha hapa Bungeni za kuwapatia kifungo cha nje wafungwa kwa utaratibu wa parole, lakini pia utaratibu wa community services za EML, lakini pia kwa kupitia msamaha wa Rais. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake alizochukua za kupunguza idadi ya wafungwa mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, pia moja ya jitihada ambazo Serikali inachukua, ni kuhakikisha kwamba tunatenga bajeti ya kutosha kadri ya hali ya fedha inavyoruhusu kupanua Magereza yetu yaweze kuwa na ukubwa zaidi na kuongeza magereza mengine nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hizo ndizo jitihada ambazo tunachukua na tunaamini kabisa kadri tunavyokwenda hivi, sasa hivi uchumi wetu wa nchi, unakwenda vizuri, naamini miaka ya mbele tatizo la msongamano litapungua kama siyo kuisha kabisa.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni kweli kama wengine walivyosema tuna tatizo kubwa la ajira. Hapa Dodoma nina hakika pia kuna tatizo la ajira. Maeneo ninayokaa mimi kule Kisasa ile mitaro ya maji ya mvua imekuwa ni madampo ya takataka, kumekuwa na nyasi nyingi, kumekuwa kama mazalia ya mbu, barabara ni chafu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukusanya hao vijana ambao hawana kazi katika makundi ili kusudi kuwapa ajira ya kufanya usafi katika mji huu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, nizungumze Kitaifa mpango ni nini? Kwa kutambua kwamba katika nchi yetu ya Tanzania tunao vijana wengi sana ambao wapo katika ma-group tofauti tofauti, kwa hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mpango wa Ukuzaji wa Ujuzi kwa Vijana ambao una lengo wa kufikia vijana 4,400,000 ifikapo 2021 tumekuja na utaratibu wa kukusanya makundi haya ya vijana na kwenda kuwapa mafunzo mbalimbali ili wapate sifa ya kuajirika na kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Spika, ninapozungumza sasa tunao vijana ambao walikuwa wako mtaani hawajawahi kusoma VETA, hawajawahi kusoma Don Bosco, wana ujuzi, tuna program ya kurasimisha ujuzi wao pasipo wao kwenda kusoma, hivi sasa tumeanza kuchukua kundi kubwa la vijana katika maeneo hayo, lakini pia tunao vijana ambao wanaendelea na mafunzo katika vyuo mbalimbali. Lengo lake ni kuwapatia ujuzi stahiki ili waje wasaidie katika shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nikirudi katika swali lake la kuhusu vijana waliopo hapa Dodoma. Mwaka jana ilisomwa hapa Bungeni na maelekezo yalitoka ya kuzitaka Halmashauri za Manispaa, Halmashauri za Wilaya kuhakikisha kwamba zinachukua vikundi vya vijana waliopo mitaani na kuwapa mitaani na kuwapa shughuli mbalimbali ambazo zinaweza zikafanywa na vijana kama hiyo aliyoisema Mheshimiwa Mbunge Ruth Mollel.
Mheshimiwa Spika, kama Mbunge wa Dodoma Mjini kwa sababu limenilenga hapa, niseme tu kwamba tunalichukua hilo tuone namna bora ya kuweza kuwakusanya vijana hao katika vikundi ili kuwawezesha na mitaji wafanye kazi ya kuzoa taka na kusafisha hiyo mitaro ambayo itakuwa ni sehemu ya ajira pia. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uchafuzi wa viwanda, vilevile mifuko ya plastick ni source mbaya sana ambayo inachafua mazingira. Je, kwa nini Ofisi ya Makamu wa Rais haitumii ule Mfuko wa Technological Transfer and Adaptation Fund kuwawezesha hao wenye viwanda wabadilishe teknolojia waweze kuzalisha mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mifuko ya plastick imekuwa ikileta uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa sana. Niseme tu kwamba, Serikali tayari ilishazuia kutoa leseni mpya kwa wazalishaji ama viwanda vipya vinavyokuja kwa ajili ya mifuko ya plastic. Pia, tumeendelea ku-encourage wawekezaji wa viwanda vya mifuko rafiki ili waweze kuwekeza na hatimaye huko mbele tuweze ku-ban kabisa mifuko ya plastic.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni miaka zaidi ya 50 ya Uhuru lakini maeneo mengi ya wafugaji bado wanakunywa maji kwenye mabwawa pamoja na wanyama, binadamu wanachota maji, wanyama pia wanakunywa hapo. Nimeona hili Mkuranga Kijiji cha Beta, nimeona hili juzi Monduli katika Kata ya Nararami. Kwa nini hii shilingi milioni 50 iliyotolewa kwa kila kijiji isitumike kwenda kuchimba visima virefu katika yale maeneo ambayo hakuna maji na binadamu wanakunywa maji kwenye mabwawa na wanyama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ruth, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba maeneo mengi ya nchi yetu yana changamoto kubwa ya maji, mijini na vijijini. Serikali tumejipanga vizuri, kwa mfano tu, juzi tumepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Dunia ambapo tumepata takribani shilingi za Kitanzania bilioni 800 na pesa nyingi kati ya hizo zitapelekwa vijijini kutatua changamoto ya maji kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Siyo hivyo tu, kwenye bajeti yetu hii ya mwaka huu tuna takribani shilingi bilioni 630 kwa ajili ya kupeleka maji vijijini. Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali tumejipanga na kila kijiji tutawapelekea maji safi na salama.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wameteuliwa wengi wao walikuwa ni wana-CCM walioshindwa katika kura za maoni, nao ndio wasimamizi wa uchaguzi. Kuna wengine hata kwa mfano huyo wa Ubungo mpaka leo anahudhuria vikao vya CCM.
Swali langu, ikiwa tutaleta orodha ya Wakurugenzi ambao tunajua ni wana-CCM na walikuwa katika kura za maoni; je, Serikali itakuwa tayari kuwaondoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tunao Wakuu wa Mikoa ambao wanalipwa kwa pesa za walipa kodi, Watanzania wenye vyama na wasiokuwa na vyama, lakini wengi wameonesha itikadi za mrengo wa kisiasa; tukiangalia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu Mkoa wa Manyara na wengine; je, Serikali ina kauli gani kuhusu hilo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kumpongeza Waziri Kivuli wa Wizara yangu, mdogo wangu Mheshimiwa Ruth Mollel kwa jinsi anavyofuatilia utendaji kazi wa Wizara yangu na hiyo ndiyo kazi ya Waziri Kivuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi yeyote utakayemchagua katika nchi hii lazima kuna chama anachokipenda. Huyu yuko pale baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi na Waraka ule wa Utumishi wa Umma unasema; “Mtumishi wa umma anayeteuliwa na Rais, endapo hataridhia kufanya ile kazi, ana ruhusa ya kumwambia Mheshimiwa Rais, naomba niendelee na kazi yangu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa Wakurugenzi walipokuwa wanafanya kazi, wameshakoma kazi waliyokuwa wanaifanya, kazi iliyobaki sasa hivi ni Mkurugenzi wa Halmashauri. Nataka niseme nchi zote duniani baada ya uchaguzi, Rais anayeingia madarakani, anapanga safu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Marekani, State House yote, wahudumu, wafagizi wote, akiingia Rais mpya, anaondoa anapanga watu wake. Sasa kama Mheshimiwa Rais kafanya hivyo kwa hao Wakurugenzi, ndivyo alivyoona inafaa, nasi ndani ya Serikali, tunaona wanachapa kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule wa Ubungo kuhudhuria vikao, nataka niseme hivi, mkishakuwa na chama tawala, siku zote wajibu wenu ni kuihoji Serikali. Mkurugenzi wa Ubungo sio Mjumbe katika vikao vya CCM, lakini anaweza kuitwa saa yoyote aende kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika Jimbo la Ubungo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Wakuu wa Mikoa; kauli gani Wakuu wa Mikoa wanaoshiriki siasa, wanaoonesha wanapendelea upande mmoja, nataka niseme hivi, Mkuu wa Mkoa ndio mwakilishi wa Rais katika Wilaya ile. Mkuu wa Mkoa ndio Rais wa Mkoa ule. Rais ni neno la kiarabu, maana yake kichwa. Kwa hiyo, kichwa cha Mkoa ule ni Mkuu wa Mkoa. Huyu Mkuu wa Mkoa anamwakilisha Rais. Hutegemei huyu Mkuu wa Mkoa afanye mambo tofauti na anavyofanya Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kusema kwamba nchi hii tuna chombo kinaitwa Mahakama. Mhimili wa Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria. Pale mtu ameona kwamba amekuwa aggrieved, au pale mtu ameona kwamba ametendewa ndivyo sivyo, basi tufuate mkondo wa sheria. Baadhi yao mnaowasema, walikuja hapa kwenye maadili, wakasikiliza, wakawa cleared, wakaonekana hawana makosa. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikichoma haya makokoro kila mara tani na tani, si muda muafaka sasa Serikali ikashughulika na wale wanaoingiza na wanaotengeneza hizi nyavu haramu nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashughulika na ndiyo maana mwaka huu mwanzoni tumekamata nyavu nyingi sana za wazalishaji wa Sunflag kule Arusha ambazo tumeziteketeza. Tumeteketeza nyavu za waagizaji kutoka nje ya nchi badala ya ku-deal na wavuvi wadogo wadogo tu. Kwa hivyo, tunashughulika na wazalishaji, waagizaji na wauzaji pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkuranga mpaka leo kwa muda mrefu haina x-ray.Ni lini sasa Serikali itahakikisha hospitali ile inakuwa na x-ray kusudi kuwasaidia wananchi wa pale Mkuranga?Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ruth Mollel kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya nyongeza katika maswali ya nyongeza kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo majengo yapo, vifaa vinakuwepo na wataalam wa kutosha wanakuwepo. Kwa hiyo, ni vizuri tukajua hii Hospitali ya Mkuranga ambayo naamini ni miongoni mwa hospitali ambazo zinatakiwa ziwe na huduma hiyo, nini kilikosekana ili katika vifaa vitakavyopelekwa na yenyewe ipate hiyo X-ray.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ukiangalia bajeti ambayo imekuwa ikitengwa kila mara kwa ajili ya hii kazi ya kupima matumizi ya ardhi ni ndogo sana. Mpaka sasa miaka 57 ya uhuru tumepima asilimia 15 tu ya nchi ya Tanzania na migogoro bado ni mingi kila siku kukicha kuna migogoro. Je, Waziri atakubaliana nami kwamba, kwa style hii migogoro haitaisha na kwamba, nchi itakuwa haina amani na utulivu kwa sababu ya migogoro ya ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mikoa mingapi ambayo mpaka sasa hivi imeanzisha Benki za Ardhi ili kurahisisha uwekezaji na pia kuwawezesha wakulima wakubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Nyongeza ya Mheshimiwa Ruth Mollel kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anasema bajeti ni ndogo kiasi kwamba, migogoro bado inaongezeka kuwa mingi na huenda pengine ikasababisha kutokuwa na amani. Katika jibu langu la msingi nimeonesha takwimu ikionesha bajeti ilianza kiasi gani na sasa iko kiasi gani. Ilianza na bilioni 1.5 lakini sasa hivi tumefikia bilioni 6. 3. Kwa hiyo, ni vitu ambavyo vinaongezeka mara kwa mara, lakini kama hiyo haitoshi Wizara yangu inalo jukumu la kuwezesha halmashauri katika kuwapa uwezo wa kuweza kusimamia masuala ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha kwamba, eneo lote linapimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii imekuwa ikifanyika na mpaka sasa tunapoongea jumla ya vijiji 1,880 vimekwishafanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na sasa hivi tunazo wilaya kama 40 ambazo mpango bado unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo ni kwamba, pale ambapo halmashauri zinawezeshwa tuna imani kwamba, zoezi la upimaji litaendelea na sio kusubiri Wizara kwa sababu, sheria yenyewe inatamka wazi kwamba, mamlaka za kupanga na kupima maeneo ni halmashauri zetu za wilaya na vijiji katika maeneo. Kwa hiyo, ni jukumu pia la halmashauri zetu na sisi pia tukiwa ni washiriki katika mabaraza yetu, basi tusimamie zoezi hilo ili kila halmashauri iweze kutekeleza wajibu wake ambao inapaswa kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kuainisha ni mikoa mingapi, naomba swali hili nisimjibu kwa sababu linahusu takwimu, pia niweze kuwa na uhakika ni kiasi gani, nisije nikampa jibu lisilo sahihi. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima kila kipande cha ardhi. Ndio maana mwaka huu tumeamua kuandaa mradi mkubwa ambao utatuwezesha katika miaka mitano hii tuwe tumekamilisha upimaji na upangaji, upangaji na upimaji kila kipande cha ardhi nchini. Kwa hiyo, pamoja na hiyo fedha ya bajeti ya Serikali ya kawaida tumeamua tukope kwa sababu, ina faida kubwa zaidi kwa kupanga na kupima nchi nzima kwa wakati mmoja kwa sababu, vilevile tunajua itatusaidia katika kupata mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwananchi akimiliki kwa hati, atalipa kodi kila mwaka, kwa maana hiyo kila mtu atafaidika na upangaji na upimaji. Kwa hiyo, pamoja na hiyo ya bajeti, lakini Serikali tumeamua kuanzisha huo mradi mkubwa wa kupanga na kupima kila kipande cha ardhi na mradi huo utaanza mwaka huu baada ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza majaribio wilaya tatu, Kamati yetu ilikwenda juzi kuangalia namna tunavyoweza kufanya. Wameridhika na taarifa imetolewa jana kwamba, jambo lile linawezekana tukiwa na uwezo wa kutosha. Kwa hiyo, kutokana na ule mfano tulioufanya katika Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro tunataka kuusambaza nchi nzima mijini na vijijini. Kwa hiyo, jambo hilo Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge tunalifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumefanya uwezeshaji mikoani kwa kununua vifaa, jambo moja linalowafanya Halmashauri washindwe kupima na kupanga ni vifaa. Serikali, kupitia Wizara yangu, tumeshanunua vifaa vya kutosha vya upimaji ambavyo kila halmashauri inayotaka kupanga na kupima maeneo waende kwenye kanda wakaazime bila kukodisha ili viwasaidie katika zoezi la upangaji na upimaji kwenye wilaya zao.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pesa hizo zilizokwenda kununua hayo matrekta ni pesa za walipakodi wa nchi hii na ni nyingi sana na mpaka sasa hivi karibu 2.9 billion hazijarejeshwa. Mkakati mahususi a kuhakikisha kwamba, hii pesa inarudi, ni upi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini sasa wale wote ambao walikopa haya matrekta majina yao yasiwekwe kwenye magazeti tuwajue ni akinanani hao wanaokwamisha kurudisha mikopo ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ruth Mollel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba, fedha zilizokuwa zimekopeshwa ni bilioni tano na kitu ambazo zimesharudishwa ni bilioni mbili, yani tuko kwenye asilimia 45 ya urejeshaji, maana yake ni jitihada kubwa zimefanyika hapo na kiwango kilichobaki kitarejeshwa kwa sababu, fedha hizi hawajakopeshwa watu nje, zimekopeshwa ndani ya Mashirika ya SUMA-JKT lenyewe kwa maana hiyo wanafanya biashara mbalimbali. Sina shaka kabisa kwamba, fedha hizi zote zitarudi na faida itapatikana kwa sababu, SUMA-JKT limejiwezesha kimtaji kuanzisha biashara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu majina ya waliokopa matrekta kwamba, yawekwe kwenye magazeti. Jambo hili lilishafanyika, majina yaliwekwa kwenye magazeti na fedha hizi zimeendelea kukusanywa. Naomba nitoe taarifa kwamba, tokea Mheshimiwa Rais ametoa kauli ya kwamba, watu wote waliokopa warejeshe, tayari wamekusanya bilioni mbili na milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na jitihada hizi na kama tulivyosema SUMA-JKT itaanza kuuza mali za walikopa endapo hawatarejesha baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa madeni.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Migogoro kati ya wananchi na hifadhi zetu ni ya muda mrefu kwanza ni-declare interest kwamba nilikuwa kwenye Bodi ya TANAPA, na wakati ule walitayarisha ramani ambayo wameainisha maeneo ambayo wanaweza kuwaachia wananchi na maeneo ambayo watawatoa wananchi kwa kuwapa fidia kwa sababu ya ikolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwanini Serikali haitumi hiyo ramani ya TANAPA ambayo walishaitayarisha kuweza kutoa suluhu ya hii migogoro kati ya wananchi na hifadhi ambayo imekuwa inaendelea kwa muda mrefu.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba migogoro hii ya maeneo ya hifadhi na vijiji imekuwepo kwa muda mrefu, na nadhani kama Mheshimiwa Mbunge anafahamu, wakati Mheshimiwa Rais anatoa maelekezo ya kutokuviondoa vijiji 366 ambavyo vinapakana na hifadhi. Vijiji hivi havikuwa vimeanza migogoro miaka ya hivi karibuni vingine vipo vimesajiliwa tangu miaka ya 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Tume Maalumm iliyoundwa na Serikali kupitia jambo, hili imegundua kuna vitongoji zaidi ya 800 ambayo vina migogoro pamoja na hifadhi zetu za taifa. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ushauri wake huu wa kutumia ramani ambayo ilipendekezwa na watu wa TANAPA tumeupokea, lakini pia tuendelee kusubiri maelekezo ya Tume Maalum iliyoundwa kumaliza kabisa migogoro hii ya hifadhi.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na marekebisho ambayo yamefanyika, ni kwamba sasa ule moshi zamani ulikuwa unafika mbali, baada ya marekebisho ule moshi bado unatoka na bado unaathiri wananchi waliokuwa jirani, unasababisha watu kukohoa na harufu chafu kwa wananchi wanaozunguka lile eneo. Swali langu: Je, Serikali ilishafanya utafiti kwa sababu watu wanakohoa, tumejua ni madhara gani ya kiafya yanayosababishwa na moshi huo?

Swali langu la pili; ni kwa nini sasa NEMC wasirudi tena kule Dundani na kuhakikisha kwamba ule moshi unatafutiwa namna ambayo itaudhibiti usiendelee kuchafua mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Ruth Mollel ni Diwani wa kata husika, kwa hiyo, yeye ni mdau katika eneo hilo. Kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, kwamba mpaka sasa hivi hakuna taarifa ambayo imekuja Ofisi ya Mkurugenzi ikionesha kwamba kuna kasoro ambazo Serikali inatakiwa irekebishe, naomba Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia vikao vyake alipeleke hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sababu sisi tunajali afya ya mwananchi kuliko jambo lingine lolote, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na swali lake la pili kwamba angetaka NEMC waende kwa mara ya pili kutazama; kwa sababu mtaji wetu kwa mwananchi ni kuhakikisha kwamba ana afya bora, basi naomba nimhakikishie kwamba Serikali kwa kupitia NEMC tutakwenda kuchunguza na tujiridhishe pasi na mashaka kwamba hakuna madhara ambayo yanatokana na kichomea taka hiki.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na huduma bure kwa wazee bado tuna ule mkakati pia au huduma ambayo inatolewa kwa mama na mtoto hasa akina mama wanaokwenda kujifungua. Ni kweli inatakiwa iwe bure lakini ukweli on the ground akina mama hawa wanatakiwa kwenda na kits, na ninaushahidi wa ndugu yangu ambaye amejifungua watoto watatu juzi japokuwa hawakuwa riziki; alikwenda na kila kitu kwenda kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa changamoto hii ambayo bado watu wanakwenda na vifaa, ni kwa nini Serikali isipate taasisi zetu au REPOA au ESRF waweze kufanya utafiti kuona ni kwanini kits zinakuweko na kwanini wahusika hawapewi? maana yake mkienda nyinyi Mawaziri hamtapata ukweli lazima tupate mtu wa pembeni atakayefanya utafiti.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Mollel Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunagharamia ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kujifungulia akina mama. Ninachokiona hapa ni changamoto ya uelewa kwa watoa huduma wetu wa afya. Mama anapokwenda kliniki anaambiwa ajiandae ili atakapopata dharura kabla hajafika katika kituo cha kutoa huduma ya afya endapo atapata dharura basi awe na vifaa ambavyo vinavyomsaidia. Hata hivyo vifaa hivi si mbadala wa vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya kuwa na vifaa vya kujifungulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaipokea hii changamoto na sisi tutaweza kutoa maelezo vizuri kwa watoa huduma wetu wa afya ili waweze kuzingatia misingi hii; kwasababu sisi kama Serikali tunagharamia vifaa na vifaa hivi tunavyo katika bohari yetu ya madawa.