Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salome Wycliffe Makamba (14 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Pia ningependa kuchukua fursa hii kuipongeza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa hotuba nzuri iliyoonesha weledi na uzamifu katika suala zima la Katiba na Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeeleza yote watu watapiga makofi lakini mwenye macho na masikio atasikia neno hili ambalo watu wa Upinzani tumeeleza Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema inahitaji digrii ya ujinga kukubali kupewa kazi bila job description halafu useme huo ni uamuzi wa bosi wako kama anaweza akakupa au asikupe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba hii kwa kushauri Serikali mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa kama Wabunge kazi yetu kubwa ni kuisimamia na kuishauri Serikali ili iweze kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutekeleza hayo ningependa kushauri na kuwaomba wanasheria waliopo humu na Mawaziri waliopewa dhamna hii waishauri Serikali itekeleze majukumu hayo kwa kumshauri Rais ipasavyo juu ya utekelezaji wa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wafahamu wazi kwamba Urais ni taasisi na siyo mtu binafsi.
Mheshimwa Rais tamko lolote atakalolitoa iwe ni kwa masihara au yupo anakunywa chai au anafanya kitu chochote kwetu sisi tunaiona kama ni agizo na tunaichukulia kama ni sheria, kwa hivyo, Mawaziri wahakikishe kwamba Rais wao anapotoa matamko basi yawe ni ya kujenga na siyo kubomoa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba suala la uendeshwaji wa nchi hii, tukiangalia suala la sukari, suala la vyombo vya habari, suala la utekelezaji wa haki za binadamu, uendeshwaji wa mahakama ni suala ambalo kimsingi Rais wa nchi hii alipaswa kukalishwa chini na kuelezwa ni lipi aliongee kwenye jamii ambalo mwisho wa siku litaleta matunda na siyo kuibomoa nchi hii na kuirudisha mwaka 1980 enzi za uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhara makubwa, leo asubuhi tumepata taarifa kwamba bei ya sukari imefika shilingi 3,200...
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Na hii nayo inasababishwa na tamko ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa, tunaamini matamko, sheria, kanuni na taratibu za nchi hii zinafanyika kwa kushirikisha wadau, endapo tatizo au suala la sukari na ukuzaji wa viwanda lingeshirikisha wadau ambao ni watumiaji wa sukari pamoja na wafanyabiashara wa sukari, huenda tusingefikia kwenye hatua hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya mahakama zetu tukubaliane mbali na itikadi zetu za kisiasa ni tatizo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu. Tunakosa uhuru wa mahakama kwa sababu mahakama hizi kinyume na sheria mbalimbali zilizowekwa ikiwa ni pamoja na sheria za kimahakama na uendeshaji wa nchi hii zimekosa uwezo na uwezeshaji. Nimeshangaa sana Mheshimiwa Mbunge aliyepita aliposema kwamba tusiongelee kwa sababu hii ni mihimili inayojitegemea, lakini sisi kama Wabunge ndiyo tunaopitisha bajeti ambayo inakwenda kuiendesha hiyo mihimili mingine. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuhakikisha tunatetea na tunasimamia maslahi ili mihimili hii iweze kuwa independent na iweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mahakama zetu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto za miundombinu, malipo ya wafanyakazi na madaraja ya mahakimu; mahakimu wawili wana cheo kimoja, wana daraja moja lakini wanalipwa mishahara tofauti. Suala hili linapaswa kuzungumziwa humu kinyume na mjumbe aliyetoka kuongea anasema kwamba huo ni mhimili unaojitegemea sijui kama yeye ana mfuko wa kuwapelekea mahakama pesa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa ya rasilimali. Mwaka wa fedha uliopita Wizara ya Katiba na Sheria ilipangiwa fungu lakini pesa hazikupelekwa ndiyo tunaona inazidi kudorora siku hadi siku. Tumeshuhudia kwenye kesi za uchaguzi, Majaji wanakosa impartiality katika decisions zao, ni kwa sababu ya umaskini wa hali ya juu ulioko katika ngazi ya mahakama. Mahakimu wanapewa baiskeli kwa ajili ya kwenda kazini, wanakosa nyumba, hawawezi kujikimu na hii inapelekea kushindwa kusimamia majukumu yao wakiwa kama mhimili wa Serikali unaojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoka kwenye suala la mahakama mwaka 2012 ulitolewa waraka ambao ulikuwa unaongelea kada ya Mtendaji wa Mahakama. Lengo la kuwa na kada ya Mtendaji wa Mahakama ilikuwa ni kuboresha utendaji kazi wa kiutawala katika ngazi ya Mahakama. Kinyume na mategemeo, kada hii imeshindwa kutekeleza majukumu yake badala yake hali imezidi kuwa mbaya lakini watu hawa wanalipwa na Serikali. Ningeomba Waziri wa Katiba na Sheria aliangalie suala hili kwa umakini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba niongelee suala la Law School. Tanzania tumekuwa na mfumo ambapo mwanafunzi anapomaliza shahada yake ya sheria analazimishwa kwenda kusoma Law School, lakini Law School imekuwa tofauti na shahada ya sheria. Tanzania vyuo vinavyotoa shahada ya sheria viko Mwanza, Mbeya, Arusha na maeneo mbalimbali na Law School ya Tanzania iko Dar es Salaam. Wanafunzi wanalazimishwa kusafiri kutoka huko wanakosomea ambako walichagua mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya Law School. Usipofanya hivyo, pamoja na miaka minne aliyoipoteza wakati unasoma shahada yako ya sheria mwanafunzi yule hawezi kutambulika kama ni mwanasheria kamili na hawezi kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na tatizo hilo, wanafunzi hao walio wengi walikuwa wanasomeshwa kwa kutumia mkopo. Cha kusikitisha ni kwamba anapokwenda Law School suala la mkopo inabidi lifanyiwe pre-assessment tena na wanafunzi hawa hawapewi mkopo. Kwa taarifa tu, sasa hivi ada ya Law School ni shilingi milioni moja laki tano na zaidi. Watoto waliokuwa wanasoma shahada ya sheria walikuwa wanalipiwa mkopo na Serikali lakini linapofikia suala la kwenda Law School linakuwa ni jukumu la mzazi kujua yule mtoto atafikiaje kwenye hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili inabidi liangaliwe kwa umakini. Tunayo majengo yako UDOM pale wanakaa buibui, tunayo majengo na watu ambao wanaweza kutekeleza suala hili, lakini leo watu wachache wamejirasimisha zoezi hili wameweka Law School Dar es Salaam. Watu wanalazimishwa kusafiri mpaka Dar es Salaam, hawana makazi, wengine hawajawahi hata siku moja kufika Dar es Salaam, wanalazimishwa wakakae pale wasome Law School kwa sababu kuna maprofesa wachache au watu wachache wanaotaka kunufaika na mfumo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda suala la Law School lishirikishe wadau hasa wanafunzi wanaokwenda kwenye shule hiyo. Pia ifahamike kuna watu ambao hawakusoma Law School zamani lakini leo kila gazeti utakalolishika linatangaza kazi lazima uwe umepitia Law School. Kwa yule ndugu yangu ambaye hafahamu kiingereza kama alivyoomba afundishwe Law School ni ile shule ya sheria ambayo ni lazima uende kusoma ili uweze kuwa Wakili kwa mujibu wa Law School Act ya mwaka 2007.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, namuone huruma sana Mheshimiwa anayesimama na kusema kwamba anakaa Dar es Salaam lakini hajawahi kuona mahakama. Mahakama si kama tangazo la Vodacom au la Tigo linalobandikwa kwenye jukwaa.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mahakama ni institution ambayo iko kwa mujibu wa sheria na anachoelezwa ni fact kwa mujibu wa sheria. Unaweza ukakaa Dar es Salaam ukafahamu ratiba ya vigodoro Dar es Salaam nzima lakini usijue ziko mahakama ngapi.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Naamini nafasi hii haijaja kwangu kwa bahati mbaya kwa sababu, natokea Mkoa wa Shinyanga ambao umebarikiwa kuwa na baraka ya madini kwa sababu, nina migodi mitatu mikubwa; migodi miwili ya dhahabu, Mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi iliyoko Jimbo la Msalala na Jimbo la Kahama. Nimebarikiwa kuwa na Mgodi wa Williamson Diamonds ulioko Mwadui Shinyanga, lakini pia nina mgodi, medium scale mining wa El-Hilary ulioko Buganika, Kishapu, ukiacha migodi mbalimbali midogo midogo inayohusika na uchimbaji na uchenjuaji dhahabu ambayo imezunguka Mkoa mzima wa Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa ambao unachangia takribani asilimia tisa ya pato la Taifa hili na hii ni baada tu ya Mkoa wa Dar-es-Salaam na hii inatokana na uwepo wa nishati na madini katika mkoa huo. Pamoja na baraka hizi ambazo Mkoa wangu wa Shinyanga umebarikiwa kuwa nazo leo nikisema niondoke na watu wachache hapa kwenda kuangalia hali halisi ya mkoa huu, ukilinganisha na baraka hizi ambazo tunazo, mambo yanayoendelea kule ni mambo ya kusikitisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hasa maeneo ya uchimbaji, walipoletewa habari hii ya uwekezaji wa sekta ya madini walifikiri kwamba, itakuwa ni faraja kubwa kwao na itawakwamua na umaskini, lakini kwa bahati mbaya watu hawa, badala ya mijadala ya kuwahamisha ili kuweza kuwapisha wawekezaji kufanyika kama inavyoelekeza Sheria ya Madini ya mwaka 2002 na 2008 badala yake watu hawa walihamishwa kwa kufukuzwa kama wakimbizi kwenye ardhi yao wenyewe. Mbali na hivyo, watu hawa walilipwa fidia ambayo intervention ya Serikali katika ulipaji wa fidia hizi, ikawa ni kinyume na matarajio ya wakazi hawa, hasa maeneo ya Kakola, ambako kuna mgodi wa Bulyanhulu na maeneo ya Kahama Mjini ambako upo mgodi wa Buzwagi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa mpaka leo wamekuwa na kilio cha muda mrefu. Zaidi ya miaka 10 wanalalamika kuhusu unfair compensation iliyofanyika kwenye maeneo yale, lakini Serikali ambayo tunaamini kwamba, inaweza kushughulikia matatizo yao haioni umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na wale wananchi wa-feel kweli Serikali ipo kwa ajili ya kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ni wapole na ni watulivu, pamoja na maumivu makali waliyoletewa kwa sababu ya unfair compensation, malipo ya fidia ambayo hawakuridhika nayo, walikubaliana kuvumilia mgodi wakiamini ipo siku Serikali itakuja kutatua matatizo yao. Pamoja na Serikali kutokutatua matatizo yao na kuwaahidi kwamba, watapata kazi kwenye migodi ile, mpaka leo wananchi wale hawapati ajira na wakifanikiwa kupata ajira basi, watapewa zile ajira ambazo mwisho wa siku zitawaacha katika hali ya umaskini mkubwa na utegemezi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaozunguka eneo la mgodi wakipata kazi kubwa katika migodi hii ambayo tunaamini ni ya wawekezaji watapata kazi ya kufagia, kufyeka, upishi na hakuna program zozote za msingi ambazo ni madhubuti zimewekwa na Serikali zinazoweza kuwaendeleza wananchi wale! Japokuwa tunasema wamefanya kazi kwa muda mrefu tuna-assume kwamba, wana-on job training, basi angalau i-certify ujuzi walionao ili siku moja watu wale waweze kuja kupata kazi ambazo zitawaingizia kipato na cha akiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitishwa sana na matukio yaliyojitokeza kwenye Mgodi wa Bulyanhulu miaka ya 2000, 2002, 2005; wafanyakazi wale walipata ulemavu, wengi wao wakiwa ni ma-operator. Wale ambao tulipata bahati ya kwenda kutembelea migodini kuna Watanzania wenzetu wanaofanya kazi ya ku-operate mitambo katika migodi ile, lakini pamoja na maradhi waliyoyapata kwa sababu ya kufanya kazi ngumu na nyingine zikiwa underground, watu wale walipelekwa kutibiwa na mgodi na wakiwa wanaendelea na matibabu yale, wale watu walirudishwa kazini na kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi zao ziko Mahakamani. Mpaka leo wanahangaika wengine wanakufa kwa sababu ya magonjwa, lakini Serikali inayojiita Serikali sikivu, sijaona hatua mahususi, hatua madhubuti za kusaidia kutetea watu hawa na leo hii tunajisifu hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mbali suala la watu kufukuzwa kazi, kuna watu ambao leo migodi ya Tanzania, migodi ya wawekezaji imekuwa ni Serikali ndani ya Serikali ya Tanzania. Wafanyakazi wanapokosea katika migodi ile adhabu wanayopewa bila kujalisha ukubwa wa kosa alilolifanya anapewa adhabu ya kufukuzwa kazi na anafungiwa haruhusiwi kufanya kazi mahali popote pale maisha yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala limewaathiri watu wengi ambao kama nilivyotoka kusema awali, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga maisha yao yote yamekuwa ni maisha ya madini. Unapomwambia kwamba, haruhusiwi kufanya kazi tena ina maana unamzuia yule mtu kupata kipato halali na hakuna adhabu Tanzania hii, labda kama ni adhabu ya kifo, inayomfanya mtu kupewa adhabu ya milele, lakini hicho ndiyo kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo migodi inafungwa! Tumeona Mgodi wa Tulawaka umefungwa na Mgodi wa Buzwagi huenda mwakani ukaanza closure plan na migodi mingine itafungwa. Kinachotokea nyumba zinazozunguka migodi hii zimekuwa zikipata athari kubwa ya uwepo wa migodi hiyo, kama athari za milipuko na athari za kemikali inayoweza kuvuja kutoka migodini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo Tulawaka imeshafungwa na Buzwagi itafungwa. Vijiji vya Mwendakulima, Vitongoji vya Ikandilo, Chapulwa, Mwime, Mbulu, Kakola, kule Msalala watu wanalia, nyumba zao zimepata crack, zimepasuka kwa sababu ya athari ya milipuko! Nimewahi kushiriki kwenye Kamati kwa ajili ya kuangalia athari za milipuko na Kamati hizi zilishirikisha watendaji wa Serikali ambao ni Majiolojia na Maafisa Madini. Afisa Madini anakuja kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Athari ya Milipuko na kalamu na karatasi; utawezaje kuchunguza athari ya mlipuko kwenye nyumba bila kuwa na vifaa ambavyo vinaweza kukupa data zinazoeleweka Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea ku-improve sekta ya madini na uwekezaji, tunaongelea kuwapa vifaa Wataalam wa Serikali ili tuweze kupata ripoti ambazo zipo impartially, ambazo zinaweza kusaidia na kutetea maslahi ya wafanyakazi wetu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda Nyamongo kuna kesi, hata leo ukifungua kwenye google, kuna kesi inaitwa the Tigiti River; ile kesi watu waliripoti, Wabunge walipiga kelele Bungeni na mto ule ulikuwa unatiririsha maji yanayotoka mgodini ambayo yalisemekana kwamba yana sumu, yalitiririshwa kwenda kwenye vijiji na ng‟ombe wakafa na watu wakaathirika, lakini Serikali ikapuuza kelele za Wabunge, kama ambavyo mnafanya sasa! Matokeo yake ripoti ya Umoja wa Mataifa na Mataifa mbalimbali ndiyo iliyofanyiwa kazi. Hivyo, leo tutaendelea kupiga kelele humu ndani na kama kawaida Serikali itapuuza, lakini naamini sisi tukiongea msipofuatisha na mawe yataongea na ipo siku mtatekeleza matakwa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye suala la uchimbaji holela. Katika Wilaya ya Bukombe kuna Pori la Kigosi Moyowosi na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inasema, hairuhusiwi kuchimba madini hasa ya dhahabu except for strategic minerals. Lakini leo…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndiyo huo!
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha Mpango wake na nikazidi kupata maswali mengi ya utekelezaji wa Mpango wake kwa sababu mambo mengi ambayo ameyaandika yanaonekana kwenye nadharia na huenda yasitekelezwe au yasitokee kabisa kama Mpango uliopita. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anataka kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maendeleo ya viwanda Tanzania
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mazingira hayo mazuri ya kibiashara Mheshimiwa Waziri hakuyaeleza kinaga ubaga na hilo linanitia mashaka, kwa sababu nikifikiria moja kati ya vitu ambavyo ni vya kipaumbele ili tuweze kukuza viwanda Tanzania tunaongelea habari ya umeme, miundombinu lakini mpaka leo na hata ukiangalia katika bajeti tuliyonayo hakuna nguvu ya ziada ambayo Serikali imeiweka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano wa mazingira ambayo tunaishi Watanzania leo, bei ya umeme bado iko juu na wanasema kwamba wamepunguza kwa asilimia mbili lakini effect yake katika punguzo hilo haionekani katika uhalisia wa maisha ya Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazingira ya sheria ambazo Mheshimiwa Waziri alitakiwa azieleze kwamba ndiyo zimerahisisha utekelezaji wa sera hii ya viwanda, sioni kama ameonesha kwa njia yeyote ila ameweka sheria kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wadogo wadogo, labda kama yeye alipokuwa anaongelea maendeleo ya viwanda alikuwa anaongelea wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wawekezaji wadogowadogo hasa wale wanaohusika na mazao ya kilimo wanawekewa vikwazo, wanawekewa sheria ngumu na wanawekewa tozo mbalimbali ambazo mwisho wa siku zinawafanya wazidi kukwama katika harakati hii ya kujiendeleza katika kutengeneza malighafi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano moja katika Jimbo la Kahama Mjini, Jimbo lile kuna watu wanashughulika na biashara ya upakiaji na uchakataji wa zao la mpunga, lakini leo hii ukiangalia tozo ambazo wanatozwa watu wale mpaka wanafikia hatua ya kukata tamaa kujihusisha na zao hili la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamewekeza fedha zao kwa ajili ya kutengeneza na kupaki zao hili la mpunga, lakini kuanzia asubuhi mpaka jioni umeme hauwaki, ukiwaka jioni Polisi wanapita wanasema hairusiwi mtu kufungua kiwanda usiku. Kwa hiyo, wanajikuta ndani ya mwezi mzima watu wale wanashindwa kufanya uzalishaji, kwa hivyo hata zile fedha ambazo wamewekeza mle wanashindwa kuzirejesha kama walizikopa kwenye mabenki, lakini pia wanashindwa kuzizalisha ili ziweze kuwaletea faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ukiangalia ambao ni wazalishaji, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, anataka kuendeleza viwanda, lakini nimesikitishwa na taarifa ya Waziri anasema kwamba bei za mazao zinapaswa zizidi kushuka. Swali hasa lilikuwa limeelekezwa kwenye zao la maziwa ambapo Mkoa wa Shinyanga tunafuga sana ng‟ombe, kwa sasa hivi lita ya maziwa ni shilingi mia nne mpaka shilingi mia tano na watu wale hawanufaiki, kumfuga yule ng‟ombe ni gharama, sindano moja inakugharimu kuanzia laki nne mpaka tano kwa ngombe mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ile shilingi mia nne, shilingi mia tano kwa lita ya maziwa unaambiwa izidi kushuka sasa sijui yauzwe lita moja shilingi mia mbili, hapo sijamuelewa vizuri! Kwa maana hiyo, ni kwamba, tunawakatisha tamaa wakulima, tushushe bei ya zao la maziwa, tushushe bei ya zao la pamba, tushushe bei ya zao la tumbaku, halafu unasema watu tuko katika harakati za kuzalisha malighafi ya kutosha ili tuweze kuendeleza viwanda Tanzania!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia kauli mbalimbali za Serikali zikibeza misaada, lakini ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema wazi kwamba gharama kwa ajili Mpango huu wa Maendeleo itakuwa ni trilioni 107 na Serikali itatoa trilioni 59 tu, hiyo baki inayobaki tunategemea kuitoa wapi? Bila shaka fedha hizo huenda zingetoka kwa wahisani au wafadhili na labda kukopa kwenye mabenki ambapo mwisho wa siku inaonekana kwamba fedha hizo tunashindwa kuzirejesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kutoa kauli badala yake inazidi kuwabeza hawa watu. Sasa hivi tuko katika ulimwengu wa teknolojia, wanazipata hizi taarifa na hakuna mtu yeyote anayeshtuka na kuona kwamba yule mtu anayetusaidia angalau kidogo tunatakiwa tumheshimu, badala yake tunatoa kauli za kukejeli na kauli za dharau, wakati leo hii waziri anathibitisha wazi kwamba ana zaidi ya nusu ya gharama ya bajeti ambayo hajui atakapoitoa. Matokeo yake anategemea kwenda kuzidi kuwabana watu kwa kuchukua property tax za Halmashauri, anategemea kwenda kuwabana watu kwa kuchukua kodi mbalimbali ambazo Halmashauri inakusanya kwa ajili ya kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazao mbalimbali ambayo leo hii yalitegemewa yatunufaishe Watanzania. Wakati tunachambua sheria ndogo za Halmashauri, tulionamkulima amebebeshwa mzigo mkubwa sana. Kwa mfano, moja kati ya sheria ndogo mkulima anaambiwa achangie mpaka fedha kwa ajili ya Mwenge, hivi kweli Mwenge, kwa nini Serikali Kuu isitoe hiyo pesa kama kweli inaona hilo jambo ni la muhimu sana hata inambebesha mkulima mdogo kutoa hiyo pesa ikiwa ni moja kati ya tozo ambayo imelimbikizwa katika zao lake lile ambalo anategemea kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni sehemu ambayo Mheshimiwa Waziri ananieleza juu ya kuboresha ufundi stadi ili kuweza kupata watu ambao wataweza kufanya kazi katika hivi viwanda ambavyo vinategemewa kuanzishwa. Katika mikoa tumeona kuna VETA moja tu katika kila Mkoa na mtu anavyotaka kufungua Chuo cha Ufundi Wilayani kuna ukiritimba mwingi na process ndefu ambayo inamkwamisha mtu binafsi kuweza kufungua Chuo cha Ufundi au Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri afahamu kabisa kwamba tunayo sera ya kwamba mwekezaji anatakiwa kuajiri watu wanaozunguka eneo alilowekeza. Walio wengi na miradi mingi inawekezwa maeneo ya vijijini na maeneo yale hayana watu ambao wana elimu ya juu na wanategemea kupata watu ambao angalau wanaweza kuwa na elimu ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu ambayo ipo katika Vijiji vya Kakola na Wilaya ya Kahama, maeneo yale watu wengi siyo kwamba wana elimu ya juu, lakini hakuna Chuo cha Ufundi kwa ajili ya kuendeleza wale watu, unamkuta mtu anafanya kazi ya kibarua zaidi ya miaka minne, mitano, kwa sababu hana jinsi ya kusoma angalau masomo ya jioni ili aweze kupanda kutoka ile rank aliyopo kwenda juu, inambidi aendelee kufanya kazi ile itakayomtesa kwa miaka nenda miaka rudi halafu leo Waziri anasema anataka kuendeleza ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sijaelewa vizuri mkakati wa Waziri anaposema anataka kuuza viwanda, kwa sababu kwa upeo nilionao ni kuwa viwanda vikubwa vinatokana na viwanda vidogovidogo ambavyo vinaanzishwa na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Kahama tunalo soko la wakulima, wale watu wamejiunga kwenye ushirika na wamekusanya fedha zao wamejitahidi wameweza kutengeneza lile soko na leo linaonekana ni moja kati ya masoko makubwa katika Mji ule. Hata hivyo, leo ukiangalia soko lile Serikali imekubali ule ushirika kuupeleka ukauzwa kwa mtu binafsi, wakati Sheria ya Ushirika iko wazi kwamba soko lile lilitakiwa liuzwe kwa ushirika mwingine ulio hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaungwa mkono na Serikali, kibali kimeshatoka, soko lile ambalo wananchi wamekusanya jasho lao linapelekwa kupewa mtu binafsi, wakati wale watu waliweka nguvu. Nilitegemea Serikali iwasaidie, iwawezeshe, iwape mtaji ili lile soko liweze kuwa kubwa, liweze kukidhi mahitaji ya ndani na ya nje ya Mji ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutilia mkazo katika elimu. Kama kweli tunataka kwenda katika biashara ya viwanda ni lazima tuhakikishe tunatoa elimu ambayo ni ya ubunifu na wananchi wana uwezo wa kutoa ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda. Elimu tuliyonayo leo hii ni ile ya kukariri, ndiyo maana unasikia mara leo Mama Mheshimiwa Ndalichako anasema kuna GPA, mara anarudi kwenye Division, ni kwa sababu hatuna system ambayo inaweza kutambua njia sahihi ya utoaji wa elimu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuko serious hatuwezi kusema tunaenda kuendesha elimu kwa njia ya mtu kutoa matamko tu kwenye magazeti. Elimu inatakiwa iboreshwe kwa kufanyiwa utafiti na ikidhi mahitaji ya Watanzania na siyo kwa kukidhi mahitaji ya Serikali ya CCM inasema hivi, kesho inakuja Serikali nyingine inasema mnawayumbisha watoto mnawa- frustrate, naomba Serikali iwe serious tunapoongelea masuala ya elimu kwa ajili ya mabadiliko ya viwanda hatuongelei tu suala la kufurahisha chama fulani au chama fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ningependa kuongelea suala zima la miundombinu. Barabara za Mitaa na barabara za TANROAD, barabara hizi zimegeuzwa kama mitaji. Tunayo barabara ambayo inatoka Kahama inaelekea Kakola pale Jimbo la Shinyanga kuunganisha na Jimbo la Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inafahamika wazi kwamba uwezo wa ile barabara haiwezi kubeba magari ya ukubwa wa namna ile ambayo yanapeleka mizigo mbalimbali kuelekea mgodini na kuelekea Geita, badala yake TANROAD imegeuza ile barabara kama mtaji, kila mwaka ile barabara inafanyiwa repair, inamwagiwa kifusi na ku-level, sasa hivi ni zaidi ya miaka kumi tangu mgodi ule umeanzishwa barabara ile inafanyiwa repair kila mwaka na mamilioni ya fedha yanapotea. Naomba Waziri husika alitazame hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea maendeleo ya viwanda hatumaanishi kudunduliza pesa, bora kama fedha ni ndogo basi tuwekeze mahali ambapo tunaona kwamba italeta tija na italeta maendeleo ya nchi hii, lakini siyo tunaruhusu watu wanatumia hii kama ni njia ya kujinufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu kwa maandishi ili na mimi niweze kushauri Serikali katika kuboresha sekta hii muhimu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Elimu itoe fursa kwa watu binafsi wenye uwezo kuwekeza katika elimu ya ufundi VETA. Hii itasaidia kuipunguzia mzigo Serikali unaotokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba za wanafunzi, Wizara ilete Muswada Bungeni utakaoonesha jinsi ya kuwabana na kuwawajibisha wale wanaohusika na mimba hizo. Pia Serikali iweke mtaala maalum kwa wasichana wanaozalia shuleni ili tusije wapa haki ya kusoma na kujikuta tunakandamiza haki ya watoto waliozaliwa mfano haki ya kunyonya, kuwa karibu na wazazi lakini pia tusijeleta mzigo mkubwa wa kulea kwa bibi watakaokuwa wakilea watoto hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujitahidi kutoa motisha kwa Walimu ili kuwapa morali katika utendaji kazi wao. Natoa mifano michache ya baadhi ya Walimu niliokutana nao katika Wilaya ya Kyerwa kwenye moja ya ziara zangu. Walimu hawa walipandishwa vyeo miaka miwili iliyopita lakini mpaka leo hawajaongezewa mishahara. Nafahamu changamoto ya bajeti inayoikabili Serikali yetu ila nashauri tusiwapelekee barua za kuwapandisha vyeo kama hatuna uhakika na malipo yao. Baadhi ya Walimu hao ni kama ifuatavyo:-
(1) Rutaihwa Kazoba
(2) Geofrey Kamondo
(3) Rugeiyamu Damian
(4) Selestine Tibanyendera Ishengoma
(5) Erick Twesige Anacleth
(6) Philbert Jeremiah Kazoba
(7) Tabu Herman
(8) Ndyamukama Cylidion
(9) Heavenlight Baguma
(10) Frida Buyoga
(11) Onesmo Alphonce
(12) Philbert Kinyamaishwa
(13) Diomedes Kajungu
(14) Yohatam Samwel
(15) Diomedes Kajungu
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali hao ni baadhi ya Walimu waliopo katika Wilaya ya Kyerwa ambao nilipofanya ziara yangu ya kiutendaji niligundua hao na wengine wengi ambao majina yao sijayataja wamepandishwa vyeo kwa takribani miaka miwili sasa na mpaka leo hawajaongezwa mishahara. Naomba Mheshimiwa Waziri ufuatilie matatizo haya katika Wilaya ya Kyerwa na upatapo nafasi naomba unijibu hoja zangu hizi kwa maandishi ili niweze kupeleka mrejesho kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumwomba Waziri ashirikiane na Wizara ya TAMISEMI ili kuweza kusukuma vipaumbele ambavyo kimsingi Wizara hii mnakutana navyo moja kwa moja katika kutekeleza Sera ya Elimu nchini. Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa najiuliza swali moja, hivi hii Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo Tanzania ya Viwanda au ilikuwa ni Serikali ya Awamu ya Nne? Kwa sababu kinachofanyika sasa hivi, mwaka 2014/2015 katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge wenzetu walikuwepo humu waliipitisha, asilimia 82 ya bajeti ilipelekwa kwenye viwanda na vikaboreshwa. Leo 2015/2016 bajeti ya shilingi bilioni 35.3 tumepeleka shilingi bilioni 1.6 sawa na asilimia 5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hiyo, mwaka 2016/ 2017 tumepeleka 8% ya bajeti nzima. Mwaka 2018 mpaka Machi, taarifa tuliyopewa kwenye Kamati tumepeleka asilimia 9.4 tu yaani hakuna mwaka ambao tumepeleka angalau asilimia 50 ya bajeti ya viwanda halafu tunajinasibu kwamba tunaenda kwenye Serikali ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linanipa wasiwasi na ndiyo maana ukiona mtu anajitetea sana, ujue kuna maovu nyuma yake. Ndiyo maana ukiangalia viongozi mbalimbali wa Serikali wana matamko tofauti tofauti juu ya ni viwanda vingapi vimeanzishwa Tanzania mpaka leo hii?

Mkuu wa nchi anasema tumeanzisha viwanda zaidi ya 3,060, Waziri kwenye hotuba yake anasema kwamba ameanzisha viwanda 1,287, kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wanasema viwanda viko 50. Kila mtu anaongea statement yake, Serikali moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima ujichanganye kwa sababu Watanzania tumewaaminisha tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda. Laiti kama Watanzania wangegundua kwamba viwanda wanavyoahidiwa kwenye kampeni ni vya kutengeza juisi, zile blender, ni viwanda vya cherehani, sijui kama leo tungekuwa tunaongea haya maneno. Leo tumebadilishiliwa story tunaambia kwamba viwanda ni aina yoyote, vya kati na vidogo. Sawa, basi hivyo viwanda vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye ripoti ya CAG, SIDO wanaweza kutoa mikopo kwa asilimia 40 tu ya pesa ambazo walikuwa wame-propose kwamba wanatoa mikopo. Watu wanaoahidiwa watapewa mikopo kwa SIDO ndio hao wenye viwanda vya kati na viwanda vidogo lakini pesa hawapelekewi. Mheshimiwa Waziri anajitapa hapa ameanzisha viwanda vipya. Jamani, wengi hapa sisi ni wazazi. Hivi kweli mtoto wako hata kama una watoto wengi kiasi gani, mtoto wako mmoja akifa kwa kifo ambacho umesababisha wewe mwenyewe mzazi utajisikiaje? Viwanda vinakufa vidogo na vya kati, pesa hatupeleki halafu tunajinasibu kwamba tunatengeneza Serikali ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika bajeti ya mwaka 2018, hiyo 8% ninayosema imepelekwa siyo fedha za ndani, ni fedha za wafadhili, fedha ambazo tunapewa na watu wengine. Uangalie seriousness ya Serikali katika kukuza uchumi wa viwanda, wewe mwenyewe utaona kuna changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, ili viwanda viweze kukua, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba lazima tukuze malighafi, lazima tuhakikishe tunaboresha pamba, tumbaku na barabara. Shinyanga ni wakulima wakubwa wa pamba. Sisi mpaka sasa hivi tuna- export pamba tani 700,000. Yes, tunauza marobota 700,000 lakini tuna-import marobota ya nguo 2,000,000 kuleta Tanzania. Mbona tunafanya biashara kichaa? Kwa nini Serikali isiwekeze kwenye malighafi ili kukuza viwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namweleza Mheshimiwa Waziri, hivyo viwanda anavyovitaja kwenye kitabu chake wanampigia makofi, anapiga nao picha, anatuma kwenye mitandao, hao watu wanamwangalia waone yeye ana commitment gani kukuza viwanda? Wale watu wamewekeza Tanzania lakini Waziri unathubutu kukaa na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Kilimo kuangalia utarahisisha vipi uzalishaji kwenye hivi viwanda? Au tunafanya majaribio ya kusema tumeleta viwanda na baada ya miaka mitano viwanda vimeshindwa kufanya kazi au viwanda vyote vimefungwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi viwanda anavyotuaminisha leo Mheshimiwa Waziri, hebu jiulize swali, vinaajiri Watanzania wangapi? Juzi nimesikia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba cherehani tano ni kiwanda. Mheshimiwa Waziri tusifanye mchezo na Watanzania, wanatutegemea sisi Wabunge na Serikali kuamua hatima ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwangu Kahama, Shinyanga na Mikoa ambayo kimsingi ilikuwa imekaa strategic kibiashara, nikikueleza tangu Serikali yenu imeingia madarakani, zaidi ya asilimia 70 ya wafanyabiashara waliokuwa wanamiliki maduka na biashara wameshapokonywa mali zao na Serikali. Watu wana mikopo Mheshimiwa Waziri. Wewe unachekelea kuleta viwanda vipya, una mkakati gani kuhakikisha viwanda ambavyo vilikuwepo ambavyo kimsingi vilikuwa vinalipa kodi na vinaendesha Serikali unavi-maintain? Una mkakati gani wa kuhakikisha hawa watu pamoja na kutusaidia kuendesha Serikali, wanaendelea kuwepo kwenye circular ya uchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa nakaa namfikiria Mheshimiwa Waziri, sijui anaposema kwamba tuna viwanda 3,000 anakuwa ana-project nini? Kwa sababu kama mwisho wa siku Shinyanga pale kuna Kiwanda cha Nyama hakina uwezo wa kuajiri hata watu 2,000. Shinyanga leo maji na barabara ni changamoto, ng’ombe ndiyo kwanza mmekazana kupiga chapa mnakusanya ushuru wa Sh.5,000, umeme ndiyo kabisa, labda wanunue na power bank pale kwenye kile kiwanda, hali ni mbaya, lakini Mheshimiwa Waziri anajinasibu anasema viwanda vinaendelea, tunafanya vizuri, tunafanya vizuri wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali, tutafanyaje kuhakikisha wawekezaji wa kati na wadogo ambao ni wafanyabiashara kwa Tanzania hii na ndiyo walezi wa Tanzania hii, wanarudi kwenye hali yao ya kiuchumi kuweza kuendesha nchi hii? Nataka commitment ya Serikali juu ya huu utaratibu wenu, mtu akiamka asubuhi, TRA inapanga leo tunatoza kodi kiasi hiki, kesho asubuhi wanasema kiasi hiki, nini commitment ya Serikali? Watu wanafunga biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa leo, huyo huyo ambaye ni sehemu ya Serikali, anasema mnaofunga maduka, fungueni, njooni mezani tuzungumze, tunaweza tuka-negotiate bei ya kulipa kodi TRA.

TAARIFA . . .

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, halafu naomba kitu kimoja, tukiwa tunawashauri muwe mnatusikiliza kwa sababu Tanzania nzima haiwezi kuja hapa kuongea, sisi ni Wawakilishi wa wananchi. Tena kwa taarifa yako, kule kijijini njoo kwangu watu wanapiga chapa ng’ombe mpaka Sh.7,000 siyo Sh.5,000, ninyi mmekaa hapa sisi tunatoka kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu suala la kiwanda, mimi kwa uelewa wangu, kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania, anapokuja kuwekeza Tanzania anapewa kitu kina tax incentive. Akipewa incentive, maana yake kwa kipindi cha muda fulani yule mwekezaji hatalipa kodi mpaka ambapo ule muda wa incentive uwe umeisha. Kama hiyo haitoshi, kuna kitu kinaitwa operational cost, yule mwekezaji yuko pale hana miaka miwili, amekuwa anafanya operation pale na halipi kodi kwa sababu anasema costs zake za uzalishaji hazijalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali wanatujia hapa na mazingaombwe eti wanatafuta mbia mpya, what about the incentive? Vipi kuhusu ile tax holiday mliowapa wale wawekezaji? Jamani nyie si mnajisema kwamba ninyi ni Wataalam, ni wataalam wa nini basi? Tusifanye siasa kwenye maisha ya Watanzania. Siasa hizi zitakuja kutuadhibu, makaburi yetu yatapigwa fimbo na wajukuu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijifiche nyuma kwa kusema kwamba Serikali inatafuta mbia. Mheshimiwa Waziri hata standard gauge miujiza hii hii ilifanyika. Tumeacha mkopo wenye riba ya asilimia 1.2 tumeenda kuchukua mkopo wenye asilimia 4. Unakaa unasema umekaa na wataalam wanakokotoa mimi sijui mahesabu au biashara, lakini kwa uelewa wangu tu wa kawaida, siwezi kufanya biashara ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iwasaidie Watanzania, itengeneze miradi. Wakae pamoja, naamini Balaza la Mawaziri ni moja, wamsaidie Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara tutengeneze miundombinu kwa ajili kusafirisha malighafi na tuboreshe zao la pamba. Zaidi ya Watanzania milioni 16 wa Lake Zone wanalima pamba. Mheshimiwa Rais anasema hao ndiyo wapiga kura wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kilimo chetu tunategemea pamba. Hebu tuboreshe zao la pamba ili tuweze kufungua viwanda vya nguo na kufungua viwanda vya mafuta. Leo kelele za mafuta zisingekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikitembea tu kidogo kilometa moja kutoka nyumbani, naona maua ya pamba yametanda kila mahali, leo tuko busy tunanunua ndege, tunajenga flyover, Tanzania siyo Dar es Salaam, Tanzania ina Mikoa zaidi ya ishirini na kitu. Tanzania siyo Dar es Salaam.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuwawakilisha wananchi wangu wa Shinyanga katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kuongea na Mheshimiwa Waziri na kumwomba atusaidie matatizo ya ushirika pale Kahama. Mheshimiwa Waziri wote tunafahamu Sheria ya Ushirika namba 20 ya mwaka 2003 inasema wazi kwamba Ushirika ukifilisika mali zake zitakwenda katika Ushirika mwingine. Hilo limekuwa likifanyika tangu mwaka 1984, mwaka 1986, lakini cha kushangaza hivi karibuni pale Kahama Chama cha Ushirika kimepewa Kampuni. Wamepewa Kampuni kinyume na utaratibu na Mahakama imetengua lakini mpaka leo Chama kile cha Ushirika
kimeng’ang’aniwa na Kampuni na wale wananchi ambao walijiunga pamoja, ambao ni wakulima wadogo wadogo wakatengeneza Ushirika, wakajenga vibanda, wamenyang’anywa maeneo yao. Suala hili nimeshalipigia kelele mara nyingi humu Bungeni na hakuna msaada wowote unaoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alitazame jambo hili kwa jicho la pekee. Wale wakulima ni watu ambao ni wanyonge, hawana pesa, hawawajui watu wakubwa, lakini kwa sababu walioko pale ni mapapa, ni mafisadi, wamewanyang’anya maeneo yao wale watu, vibanda zaidi ya 200 vimechukuliwa, soko lile limemilikishwa kwa mtu mmoja ambaye ndiye mwenye hisa nyingi kwenye Kampuni ile na wale watu wanakosa pa kukimbilia. Namfahamu vizuri Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Tizeba ni mtetezi wa wanyonge. Namwomba sana aje kwetu pale atusaidie kutatua tatizo hili kwa sababu limekuwa ni tatizo sugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wale watu wakihoji kuhusu Ushirika Mheshimiwa Waziri wanakamatwa, wanaenda kuwekwa ndani, wanaanza kuhojiwa, wanatishwa, vitisho hivyo ni unyanyasaji kwa raia wanyonge wa Tanzania hii. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kutatua tatizo la ushirika kwa sababu limezidi, kwanza ni kinyume cha Sheria, Mahakama imeshatengua Kampuni ile kumiliki, ile hati iliyopo pale ya Kampuni imetenguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza wanatakatisha hati ile, wanafanya kui-renew ili ionekane kwamba ni hati halali. Kweli tatizo hili limezidi, limekuwa la muda mrefu lina miaka zaidi ya 27, tunaomba Mheshimiwa Waziri tafadhali aje atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo niongelee suala la upigaji chapa ng’ombe, tumezinduliwa mradi sasa hivi wa kupiga chapa ng’ombe. Wanasema ni kwa ajili ya sababu za kiusalama wanataka kutambua ng’ombe na wale wanaokuja kutoka nchi za jirani. Hata hivyo, wanasema upigaji chapa hawa ng’ombe gharama yake ni Sh.3,000/= kwa kila ng’ombe. Sisi Wasukuma tunasifika kwa ufugaji. Familia za vijijini Sh.3000/=, Sh.1,000/= ya kula tunahangaika kutafuta hiyo Sh.3,000/= tutaitoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndizo tozo za kero ambazo zilipigwa marufuku na Mheshimiwa Magufuli. Kama wanaleta mradi basi watafute namna ya kuutekeleza mradi ule bila kuwaumiza wananchi na Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa kwamba kupiga chapa ng’ombe kunashusha thamani ya ngozi ile inapotakiwa kuuzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, tunasema tuwakwamue wananchi kwenye umaskini, leo tunaenda kuwapiga chapa ng’ombe wao na tunawatoza Sh.3,000/=. Tunaomba majibu tunahitaji kujua ni njia gani itatumika kuwapiga chapa bila kuwabughudhi, bila kuwakera wakulima hawa ambao ufugaji kwao ni biashara, ufugaji ni maisha, lakini ufugaji kwao ndiyo chakula cha kila siku na ndio utamaduni wetu vile vile. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie sana majibu juu ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la punda. Usukumani punda wanatumika kwa ajili ya kubeba mizigo, maji, ndio usafiri kule kwetu. Hata hivyo, hivi leo nikikueleza punda wanauawa, punda wanauzwa, wamekuwa ndio biashara. Mheshimiwa Waziri, China wanabiashara ya ngozi, wananunua ngozi hizi za punda na wanatengeneza anti aging, dawa ambayo inayozuia kuzeeka na inaongeza nguvu za kiume pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri, biashara hii…

MWENYEKITI: Mheshimiwa umesemaje? (Kicheko)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la punda lina dawa ambayo inatumika kule China kupunguza kuzeeka, lakini pia inaongeza nguvu za kiume. Kwa sababu hiyo thamani ya punda ni Sh.50,000/= mpaka Sh.190,000/=, lakini thamani ya ngozi ya punda ni pound 160, ngozi peke yake. Juzi Mheshimiwa Mwijage wakati anapitisha bajeti yake hapa alisema amepiga marufuku uuzaji wa punda. Hii haitoshi, tunatakiwa tuisimamie kama tunavyopiga marufuku mambo ya pembe za ndovu na biashara nyingine, kwa sababu hii itapelekea kupotea kwa hawa punda ambao ni mifugo tunayoitegemea sisi kama njia ya usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeamua kuingia kwenye biashara hiyo basi tuwe na mechanism ya kuongeza hawa punda wawepo wawe ni wanyama wa biashara, waongezeke tuwe na jinsi ya kuboresha, kwa sababu hii mifugo iko chini ya Wizara yako na hii mifugo sisi tunaitumia kama njia ya usafirishaji kule kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia wana mifugo milioni 7.5 hii ya aina ya punda, lakini kuna nchi ambazo zimepiga marufuku na wameweka sheria, nchi kama Burkina Faso, Niger na Pakistan wameshaweka Sheria. Kusema tu haitoshi, tunafungua mianya ya wale watu ambao watakuwa wanafanya ujangili wa mifugo hii. Tusifungue mianya kwa sababu hatimaye itatuathiri sisi wenyewe. Tuweke sheria ambazo zitazuia, lakini kama unataka kufanya biashara hiyo na wafanye kwa njia halali na kuwe na misingi ya kuzuia upotevu wa wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kwa kweli Ushetu, Tarafa ya Mweli hakuna hata josho, tarafa nzima ina kata karibu sijui ngapi, hakuna hata josho la kuoshea ng’ombe. Sasa bajeti ya Kilimo na Mifugo haifiki hata trilioni moja na tunategemea eti huu uti wa mgongo wa Kilimo Kwanza; sijui hata hiyo sera iliishia wapi; tunategemea eti malighafi itokane na mazao wa kilimo na mifugo, eti uti wa mgongo wa nchi hii ni kilimo, wakati huo huo hata bajeti yenyewe haiakisi malengo ya nchi hii ya Tanzania ya kutokana na malighafi za kilimo na mifugo. Hivi kwa nini tuendelee kuwadanganya Watanzania? Mimi sina wasiwasi na ukusanyaji wa kodi katika nchi hii, wasiwasi wangu ni allocation ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atueleze mkakati wake wa kuongeza kilimo na mifugo kwa nchi hii kuelekea ku-connect na wazo la Tanzania ya viwanda ukoje? Ukiangalia ni theory tu, utekelezaji wa theory hii mimi siuoni, naona tu ni maneno yanasemwa na mwakani wanatumia kitabu kile kile wanabadilisha mwaka wanabadilisha vitu vidogo wanarudisha kitu kile kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, anaakisi vipi, anashirikiana vipi na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutengeneza barabara ili atusaidie kule Ushetu, Kinamapula, Nyandele sijui Wandele sijui wapi, anatusaidia vipi kuleta barabara tuweze kulima kilimo cha tumbaku? Pamba imeshakufa, zao la biashara tulilonalo Shinyanga sasa hivi ambalo tunalitegemea ni tumbaku, lakini hakuna miundombinu iliyoboreshwa kila siku ni hadithi mtatekeleza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami niweze kuchangia bajeti hii japo kwa dakika tano. Nimesoma vizuri kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Jambo kubwa lililopelekea tukashindwa kufanikisha bajeti iliyopita ni ukosefu wa fedha za wahisani. Kukosa fedha za wahisani Mheshimiwa Waziri anasema eti tulichelewa kufanya negotiation na wahisani ndiyo maana tulichelewa kupata pesa.

Mheshimiwa Waziri, wahisani wanatupa pesa pale tutakapokuwa tumetimiza masharti ya kupewa mikopo. Hatuwezi kupewa pesa kama Serikali yetu haizingatii utawala wa kidemokrasia, haizingatii utawala bora, uhuru wa vyombo vya habari na tunapitisha Sheria kandamizi zinazowakandamiza Watanzania. Mheshimiwa Waziri angekuwa mkweli juu ya hilo, kwamba tunahitaji tusimamie utawala bora, utawala wa sheria na kila mtu awe chini ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anasema kwenye kitabu chake, ili tuweze kupunguza deni la Taifa, ameamua kuwekeza miundombinu kwenye maeneo ambayo yanachochea uchumi. Miundombinu hiyo anataja ni barabara, reli na ndege. Bajeti inapitishwa tunakwenda kujenga kiwanja cha ndege Chato; hivi kweli Tanzania nzima tukitafuta sehemu zenye vichocheo vya kiuchumi utataja Chato kweli? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chato wameweka traffic light!

Inapita gari moja baada ya saa nzima ndiyo inapita gari pale. Wanaweka kiwanja cha ndege wanasema pale ndiyo kuna vichocheo, tupate pesa kwa ajili ya kuboresha uchumi kwenda kulipa deni la Taifa. Hizi ni ndoto ambazo haziwezi kutekelezeka. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka Sh.40/= kwenye mafuta ikiwa ni mbadala wa Motor Vehicle Licence. Kweli mafuta ya taa wataalam wetu waliosomeshwa na pesa za nchi hii wanasema tupandishe mafuta ya taa kwa sababu petroli imepanda, kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuzuia uchakachuaji magari yasiharibike. Huo ndiyo utaalam wa Wazalendo wa Tanzania waliowekwa kwamba tuwakandamize masikini kuokoa magari yasiharibiwe, mafuta yatachakachuliwa. Huo ndiyo utaalam umeishia hapo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sijaelewa vizuri kuhusu taratibu za manunuzi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha anapokuja atueleze; kweli bado tunazingatia Sheria ya Manunuzi Tanzania au ni mtu mmoja ndio anaamua tununue vipi, tufanye vipi shughuli za manunuzi Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba akija aje atueleze ni taratibu ipi ya manunuzi ilitumika kuwapa mkataba watu wanaokuja kujenga reli ya Dar es Salaam – Morogoro? Atueleze utaratibu upi ulitumika kununua zile ndege mbili ambazo mpaka sasa hivi inasemekana ndege moja iko down? Utaratibu upi ulitumika wa manunuzi kujenga barabara kwa pesa za uhuru barabara ya Mwenge – Morocco? Ni utaratibu upi umetumika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo tulitegemea kuyaona kwenye bajeti hii ambayo sisi tulipitisha hapa sheria, watu wanakwenda kinyume na sheria, Bunge linadharauliwa kile tulichokifanya, halafu tumebaki tunacheka, tunapiga makofi, tunapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi bado sijapata picha ya zile propaganda zinazoenezwa kuhusu suala la madini na migodi. Tunaonekana kwamba sisi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia. Mwaka jana tulipitisha bajeti na tukakubaliana kwamba ili tuelekee Serikali ya viwanda, Tanzania ya viwanda, kuna baadhi ya maeneo ni lazima tuyaboreshe. Tukasema tutaboresha reli, tukasema tutaboresha barabara, bandari na maeneo mengi yenye vichocheo vya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati inaonesha kwenye ukurasa wa nne, Serikali haijapeleka bilioni 14 ambazo zilipitishwa kwa ajili ya sekta ya mawasiliano, haijapeleka bilioni sita ambazo tulipitisha kwa ajili ya kuboresha bandari ya Mwanza, hawajapeleka hata senti tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijalipa Wakandarasi jambo ambalo limetuingiza kwenye deni la riba ya 3.9 bilioni, pesa hii tulipitisha lakini hazijapelekwa. Leo ni 2018 Watanzania wanaaminishwa tunakwenda kwenye Serikali ya Viwanda ilhali vichocheo ambavyo vinaweza kwenda kuhudumia viwanda kwa kusafirisha malighafi, kwa kuongeza utaalam mpaka leo havijapelekewa senti tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha hapa bilioni mbili ikiwa ni pesa kwa ajili ya feasibility study ya uwanja wa ndege wa Chato, feasibility study, lakini leo tunaongea Bunge hili halikukaa halikupitisha popote uwanja wa ndege wa Chato umepelekewa bilioni 42 na completion stage ya project ya uwanja wa ndege wa chato ni zaidi ya asilimia 62, ilipitishwa wapi Bunge halikukaa, hatukuridhia, hakuna utaratibu wowote wa Serikali wa kimanunuzi ambao ulifanyika kupitisha ujenzi wa kiwanja hiki, leo tunacheka tu hapa na Serikali. Serikali inadharau Bunge, hakuna heshima kwa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anasema asilimia 35 ya maoni yake aliyoyatoa katika ripoti yake mwaka jana haijafanyiwa kazi, Serikali imepuuza na wala hawaoni umuhimu wa kufanya hivyo, iko kwenye ripoti ya CAG. Bunge linalalamika asilimia kubwa ya bajeti yake iliyopitishwa humu Bungeni haijatekelezwa leo tunakaa hapa tunasema tunakaa kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza hapa habari ya TARURA, tukasema tatizo la barabara za Wilaya sio chombo cha kutengeneza barabara, changamoto ni pesa katika maeneo haya. TARURA leo inatengewa asilimia 30, TANROAD inapewa asilimia 70, matokeo yake ni nini? Matokeo yake imeshindwa ku-perform kufanya kazi kwa sababu hawajapelekewa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kahama ninakotoka mimi hakuna barabara inayopitika sasa hivi, ni mafuriko kila mahali, kwa sababu barabara zimeshashindwa kufanyiwa maintenance, pesa Serikali inapelekea inapotaka, halafu wanakuja hapa wanajifanya kichwa chini mikono nyuma, eti tuwape bajeti tuwapitishie, hakuna wanachokwenda kufanya ambacho tunashauri hapa Bungeni, wanatekeleza mambo yao wanayoyajua wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hawa ni Mawaziri welevu sana, yaani mimi leo ningekuwa ni hawa Mawaziri ningeomba nipumzike, kwa sababu hakuna wanachofanya pale ofisini zaidi ya kutekeleza miradi ya kuletewa na sio miradi ambayo inatokana na michango ya wananchi kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa sababu tu, sio kwamba hakuna makusanyo, kwa sababu pesa haziendi kwenye miradi. Wanawalazimisha wataalam wetu watafute njia mbadala ya kupata pesa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kabla sijaanza kuchangia, naomba Bunge hili lijue mimi ni mjumbe wako wa Kamati ya Kanuni za Bunge na wewe kama Mwenyekiti wangu umenifundisha kweli kweli kuzisoma kanuni hizi na kuzizingatia. Kwa taarifa hiyo, naomba niwakumbushe Wabunge wenzangu kwamba tutumie tu lugha nzuri pale tunapokuwa tunachangia na tusiseme uongo Bungeni, tunamlazimisha Mheshimiwa Spika wakati mwingine kutubeba lakini si jukumu lake, tuwe na busara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa quotation ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu alipokuwa akiutubia katika sherehe za utoaji za tuzo za heshima, wakati ule alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano. Mama Samia Suluhu alisema yafuatayo, imeandikwa kwa Kiingereza tafsiri nitakayoitoa haitakuwa ya moja kwa moja lakini alisema; “On the bilateral front the European Union is Tanzania key development partner both in terms of magnitude and financial support”.

Akaendelea kusema zaidi; “Let me therefore avail this opportunity to express our sincere gratitude and appreciation for the European Union in valuable assistance which has enabled the Government of Tanzania in many ways undertakes social economic development programs for sustainable development”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wajomba zangu kama Mheshimiwa Mzee Musukuma, Mama Samia Hassan Suluhu wakati anahutubia mkutano huu...(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuwa anamaanisha kwamba anatambua mchango mkubwa wa wadau wa maendeleo ambao wanatuchangia na bajeti yetu ya Tanzania. Mama Samia Hassan Suluhu ambaye sasa ni Vice President alitambua kabisa kwamba ili tuweze kutengeneza mpango wa maendeleo unaotekelezeka Tanzania haiwezi kujiendesha kwa pato la ndani peke yake.

T A A R I F A . . .

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoniita Salome ameniita kwa Kisukuma, ni mjomba wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia Hassan Suluhu, nikianza kwa kum-quote alitambua mchango mkubwa wa wadau wa maendeleo kwenye bajeti yetu akiamini kwamba ili tuweze kufikia malengo ya mipango tunayoitengeneza ni lazima tuheshimu na tuthamini wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo hivi sasa katika nchi yetu, mimi naomba nisisitize, kuna hali ya sintofahamu kubwa sana kati ya mahusiano yetu na wadau wetu wa maendeleo. Labda nianze na ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara kama tulivyoahidiwa wataishi kama mashetani wanaishi kama mashetani. Wafanyabiashara hawana security. Juzi tumeshuhudia billionaire mdogo Afrika ametekwa, amejirusha mwenyewe, halafu ameenda kuhojiwa akiwa nyumbani kwake na Serikali ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu pale Shinyanga tunao wafanyabishara wa maduka ya kati. Siku za hivi karibuni kwenye vyombo vya habari, Waheshimiwa Wabunge wenzangu mlishuhudia, Mkuu wa Mkoa amekwenda pale anafanya operesheni sijui ya ukaguzi, maana operesheni zimeshakuwa nyingi siku kila mtu anafanya; kwenye operesheni ile amefunga kwanza maduka yote ya pale mjini bila kujali athari za kiuchumi za matendo ambayo anayafanya. Kafunga maduka yale, kawachukua wafanyabiasha kaita vyombo vyote vya habari, anawasimamisha mbele ya vyombo vya habari anawaambia wafanyabiashara wale eleza ulichokifanya, haya kiri kwamba ulifanya hivi, haya eleza hivi, kinyume na haki za binadamu, utu, sera ya biashara na sera ya uwekezaji. Ndipo tulipofika kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho na kahawa zinakufa. Mazao yote ya biashara ambayo kimsingi kama walivyoeleza Wabunge wenzangu ndiyo yanayochangia kwa kiasi kikubwa tuweze kutekeleza mpango huu ambao leo tumekaa Dodoma tunaujadili yanakufa lakini nobody cares. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikupe taarifa iliyotokea jana. Jana kwenye Citizen TV kwa Wabunge wenzangu ambao mmetazama, wavuvi 36 wa Kenya wamezuiliwa kwenye Ziwa Victoria wakisemekana kwamba ni wavuvi haramu na wamekatwa na watu wa Usalama wanaambiwa hawawezi kuachiwa mpaka walipe faini ya milioni 26. Je, watu wa Usalama wanatoza faini? Uvuvi haramu mamlaka husika zinajulikana lakini sasa ndipo tulipofika leo, tunasema refa wewe, mchezaji wewe, mfunga goli wewe, mtu mmoja anafaya kila kitu na niliwahi kusema humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka kusema asubuhi habari ya watu ambao ni watetezi wa waandishi wa habari Tanzania. Kuna sintofahamu kubwa, watu wamekuwa detained hotelini wamenyang’anywa passport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema leo Serikali itoe kauli kukemea vitendo hivi ambavyo vinaweza kutuingiza kwenye migogoro ya kidiplamasia, hatuelewani humu ndani. Mpaka natamani neno diplomasia lingetafutiwa neno lingine labda ni msamiati mgumu ambao viongozi wa Serikali hawaelewi. Wale watu wamekuwa detained BBC na CNN wame-report. Hivi inaleta image gani kwa nchi yangu leo kudhalilika namna hiyo kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mahiga alitoa statement baada ya Balozi wa EU kuondoka, akasema eti ameondoka kwa anavyojua mwenyewe, amepangiwa kazi nyingine sisi hatuwezi kujua. Hata hivyo, Balozi wa EU ametoa statement kwenye tovuti yake, anasema kuwa alifanya na mazungumzo na Serikali ya Tanzania na akaeleza grievances zake kwamba Tanzania hawaelewani na EU kwa sababu kuna uvunjifu mkubwa haki za bidanamu, Tanzania kuna shida kubwa ya utawala wa sheria, ameeleza black and white. Alikuja akafanya mazungumzo mpaka anaondoka nobody cares. Serikali, Waziri mkongwe mdiplomasia ninayemuamini anatoka public anasema ameenda kupangiwa kazi nyingine mimi sijui bwana, inawezekana tukaletewa mtu mwingine, recalling of an Ambassador is not a joke ,naharibu image ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama leo hapa kutaka kukuonyesha kwamba hawa European Union inachangia…

T A A R I F A . . .

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe Watanzania wenzangu kwamba leo tunapozungumza hapa ndani kwenye kwa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka huu 2018, European Union yenye nchi 27,28 imechangia kwenye kahawa dola milioni 149.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kipekee na mimi niweze kuchangia Muswada huu wa Shirika la Simu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwa makini sana maelezo ya Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa aliyoyatoa akiomba tupitishe Muswada wake wa kumpatia shirika hili na katika maelezo yake anasema moja kati ya madhumuni yake eti anataka kulipatia Shirika la Mawasiliano ya Simu jukumu la kusimamia miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, shirika hili lilianza shirika, ikaja kampuni sasa tunarudi kwenye shirika, lina miaka zaidi ya 40. Bahati nzuri ndugu yangu Profesa Makame Mbarawa amekuwa kwenye system hii ya mawasiliano kwa muda mrefu, alikuwa huko na mpaka sasa amekuwa Waziri. Juzi alikuja hapa wakatulisha ubwabwa, wakasema kwamba wanazindua TTCL, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwepo kama mgeni rasmi, mpaka leo sijaona ushindani kati ya TTCL na makampuni mengine ya simu yaliyoko Tanzania. Sijauona ushindani wa aina yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaongea habari ya 3G, 4G, 2G peke yake line ya TTCL ukiiweka kwenye simu hizi ndogo ndogo za tochi haifanyi kazi. Line ya TTCL ukitoka three kilometers radius kutoka maeneo ya mjini au kwenye highway haishiki. Leo tunataka kumpatia Profesa na Wizara yake jukumu la kwenda kusimamia TTCL ambayo kimsingi ameshindwa kui-manage asimamie hiyo pamoja na makampuni mengine ambayo kimsingi kwake ni giants kwenye masuala ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda namna hii inabidi tuwe makini sana kwa sababu wakati mwingine inawezekana tunafanya hivi ili kujifurahisha lakini kweli leo tunarudi kwenye shirika kuipa ruzuku, kui-breast feed TTCL yenye miaka zaidi ya 40. Ina miaka zaidi ya 40 inataka breast feeding ili iweze kukua iende ikashindane na makampuni mengine maana tunasema sijui database na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inabidi Waheshimiwa Wabunge tulifikirie mara mbili suala la TTCL na suala la kwenda kwenye shirika la simu. Mimi ninachokiona hapa tunarudi kwenye ujamaa. Tunarudi kwenye Sera ya Ujamaa ya kutaka kwa vile TTCL yetu imeshindwa kushindana na makampuni mengine ya simu sasa tunataka kuyadhibiti ili angalau twende pamoja wakati tunazidi kuchelewa. (Makofi)

Mheshima Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge tujaribu kusajili line ya TTCL leo. Ukisajili line ya Tigo, Vodacom dakika tano unakuwa uko hewani, TTCL ukienda kusajili kwa wakala itakuchukua saa moja mpaka masaa mawili ili uweze kuwa hewani. Sasa mimi najiuliza Mheshimiwa Makame Mbarawa amekaa siku zote hizi, hebu kwanza atupe update tangu tumekula ubwabwa wa uzinduzi wa hili suala amefikia wapi? Au ndiyo leo anakuja na gear hii kesho unabadilisha unaingia na gear hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Mheshimiwa Waziri atueleze amefikia wapi miaka miwili na nusu akiwa kama Waziri katika Sekta hii ya Mawasiliano kuhuisha kampuni ya Kitanzania ya mawasiliano kushindana na makampuni mengine na ndiyo maana unaona hata Wabunge wakisimama humu ndani leo hawaombi upeleke mnara wa TTCL wanasema leta Halotel, wanasema leta Voda, hamna mtu anataka habari ya TTCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tumeshindwa kushindana kiuchumi kwa kufuata fair competition tusitumie mwanya kwa sababu sisi ni Serikali eti tuseme tunaenda kukandamiza private sector. Tusitumie mwanya huo kwa sababu mwisho wa siku tutakosa hata hao wawekezaji. Tunawakaribisha kwa mbwembwe na vigelegele na nini karibuni mazingira yako conducive, mwisho wa siku mbele ya safari tunaanza kubadilisha magoli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Muswada huu wameweka mazingira ya kuwa-favour wao. Wanasema ili mtu aweze kuwa Mwenyekiti wa Bodi anatakiwa angalau awe na uzoefu wa miaka nane. Kama hiyo haitoshi kufanya kazi miaka mitano, hivi kweli, hawawezi kuiga mfano kwa wenzenu?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo makampuni ya simu yaliyowekeza hapa Tanzania wanatumia wasanii tu kijitangaza na mambo yanakwenda, utasikia mara leo haliishi bundle, mara leo halichachi, mara nini, kampuni inasonga mbele, lakini sisi tulichokalia ni kutengeneza yale mazingira ya bureaucracy na urasimu mle ndani ili kusudi tu ionekane kwamba hii ni kampuni ya Serikali, kiukweli sioni sababu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Makame Mbarawa ampime mtu utendaji kazi wake kwa jinsi ambavyo alivyo creative, ampime kwa competency yake, ampime kwa jinsi gani anamletea matunda na siyo kukimbia mara anataka shirika, mara leo corporation, mwisho atasema iwe NGO. Tafadhali sana, tunamwomba awapime kwa competence. Leo mtu anayeweza kukaa kwenye Bodi akamletea mabadiliko akimchukua kwenye makampuni mengine ya simu hampati mtu wa miaka 56 au 57 anayemtaka yeye, hampati!

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo vijana wadogo wanafanya kazi, afungue boksi Mheshimiwa Waziri apate watu ambao watamsaidia kusukuma kazi siyo kila siku anacheza na makaratasi, anabadilisha sheria hii, anaweka urasimu huu, haitamsaidia wala haitaisaidia Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Simu (MTN) South Africa, leo mimi nikisikia habari ya MTN cha kwanza ninachokifikiria ni South Africa, wamei-brand ile kampuni ya simu ya nchi yao ili popote itakapokuwa inapita ionekane kwamba ni nchi yao. Tunao vijana wazuri wanaocheza mpira, wanaigiza sanaa wako kimataifa, yuko Mbwana Samatta, amtumie, anatumika kwenye matangazo mengine huko, atamsaidia hata bure kwenye Instagram yake ata-post TTCL. Kwa nini tusitumie marketing strategy na tuwe business oriented ku-push hii TTCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naiona a hidden agenda ya kurudisha hii mambo ya shirika, sijui corporate, sioni nia njema ya dhati ya Serikali kutaka kusukuma maendeleo. Tumesha-invest vya kutosha, tumeweka pesa nyingi kwenye mashirika ya umma lakini sijaona mafanikio makubwa kama nguvu inayoingia, sijayaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nimuulize Mheshimiwa Makame Mbarawa hili suala la upigaji kura, aje atueleze hapa, tukija kupiga kura kwa sababu hili suala kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 98(b) ukisoma pamoja na Orodha ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Nyongeza ya Kwanza inasema jambo la simu ni jambo la Muungano. Sasa Mheshimiwa Waziri aje atueleze hapa wakati tunapiga kura tutatafuta ile theluthi mbili ya Zanzibar na theluthi mbili ya Tanzania Bara au upigaji kura utakwendaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kufahamu kwa sababu ninavyofahamu Wazanzibari hawajanufaika kwa namna yoyote na uwepo wa kampuni hii ya simu. Leo tukisema tunarudi kwenye suala la shirika tunarudi kulekule ambako wanasema jiwe walilolikataa waashi, ndiyo tunarudi kulekule, sasa tuone kama kweli tukipiga kura watarudi kuchagua hili suala la shirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuko kwenye dunia ya ubepari siyo dunia ya ujamaa kwamba leo tukiona tumezidiwa mchezo tunabadilisha magoli, hatuko huko. Tunahitaji kuona Kampuni ya Tanzania, mimi leo utaniita siyo mzalendo natumia makampuni mengine ya simu kwa sababu hivi kweli nitasikia raha gani niko mbali na familia yangu nikishika simu yangu kutwa inaniambia hakuna network? Nitasikia faraja ya namna gani? Natamani nikishika simu nasafiri kwenda kwangu Kahama kule Shinyanga mtandao uwepo, lakini leo TTCL mikoani haipatikani na zaidi ya yote ni simu ya watu ambao ni matajiri, wanaoweza kumiliki smart phone kwa sababu inashika 3G na 4G peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, of course inaleta assurance kwamba ukiwalazimisha Ofisi zote za Serikali na Idara zake watumie TTCL utapata wateja zaidi ya milioni saba au milioni nane, lakini hivi kweli wanaturudisha kule ukienda kukata leseni unaambiwa mtandao umebuma, wanataka waturudishe kule ukienda bandarini kulipia unaambiwa mtandao uko down. Huwezi kuwalazimisha watu watumie huduma mbovu unayoitoa eti kwa sababu wewe ni Serikali na wala hatuwezi kukubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme leo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze tangu amepewa dhamana ya kuwa Waziri wa Mawasiliano amefanya nini kuhuisha TTCL ili iweze kutumika na kushindana na makampuni mengine ya simu Tanzania. Siyo tu hivyo, aje atueleze hapa nini mkakati wake atakapopewa huu uwakala wa kusimamia makampuni mengine ya simu ilhali tulishaingia kwenye mikataba tukakubaliana na wawekezaji waliokuja kuwekeza kwenye industry ya mawasiliano kwamba mchezo utakuwa fair. Nini strategy ya Serikali juu ya hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli tunasema Tanzania ni kisiwa cha amani, ni eneo ambalo unaweza kuwekeza, lakini kwa mazingira ninayoyaona, tunawatisha wawekezaji kwamba Tanzania utawekeza leo, miaka mitatu au minne mbele hali lazima itabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa nafikiria kuhusu suala la Data Centre kwamba iwe managed na TTCL. Mheshimiwa ananicheka, labda kama tunaliongea hili kisiasa lakini tukiliongea kibiashara kwamba tunatafuta biashara Tanzania TTCL ifanikiwe tupate hela halafu leo unasema lazima iwe managed na one centre source, mimi hainingii kichwani. Tushindane kwa hoja, tushindane kibiashara, tusitumie rungu la Serikali kwamba kwa sababu sisi ni Serikali tuna uwezo basi kila siku sisi tunaibuka na matamko, kila siku sisi tunaibuka na malekezo, mara tumebadilisha sheria, hapana. Tanzania ni nchi conducive for investment, hatuwezi kufikia hatua ya Mataifa mengine ambayo watu wanakimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wangu hii hoja aliyoleta Mheshimiwa Makame Mbarawa sijaielewa yaani naona anazidi kuturudisha ambako hata sisi hatukuwepo maana hiyo miaka hata sikuwepo, ndiyo anatupeleka huko. Tulisoma kwenye vitabu vya historia darasani ndiyo anaturudisha huko halafu tena anatuchanganya. Twende kibiashara, aendeshe TTCL kama kampuni ya kibiashara, watu wale wawe answerable. Huwezi kuniambia ili ufanye kazi kwenye kampuni ya simu, Joti amesomea mambo ya simu?

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukaniambia ili ufanye kazi kwenye kampuni ya simu lazima uwe na uzoefu wa miaka nane, mimi hicho kitu sikubaliani nacho, Joti amesomea mambo ya simu? Wako vijana machachari tufanye marketing, advertisements, investment, tutumie resources tulizonazo tupambane na mashirika mengine duniani. Hata ukiweka Mlima Kilimanjaro kwenye TTCL watu watanunua line ya TTCL lakini usiniambie leo unaenda kushindana na watu kwa kuwaambia eti unataka kutengeneza mkakati, wewe mkakati wa kwako mwenyewe umeshindwa kuutengeneza, utaweza kutengeneza mkakati wa mashirika mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata darasani anayechaguliwa kuwa monitor ni yule anayefaulu, huwezi kuwa monitor darasani wakati unafeli. Sisi tumeshafeli kwenye TTCL, sasa tumeona hapa tutafute ukiranja ili mwisho wa siku mtu akiongea unamwambia kaa chini, wakiibuka hawa kaa chini, kama ambavyo inafanyika kwenye mashirika mengine mengine sitaki kuyataja nitachangia siku ikifika. Tushindane kwa hoja, tushindane kibiashara, mambo ya kuleta usanii wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2018
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba na marekebisho haya ya sheria mbalimbali za nchi yetu. Kwanza kabisa siku ya leo ikiwa ni siku maaalum nianze kwa kumtakia uponyaji mwema Mheshimiwa Tundu Lissu ambaye kimsingi yeye ni moja kati ya watu waliopelekea baadhi ya marekebisho makubwa ya sheria ya Chama cha Mawakili Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pale alipoishia Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, suala la kutenganisha Chama cha Mawakili kwamba viongozi wa chama hicho wasiwe wanasiasa linakiuka Katiba kwa kiasi kikubwa na linakiuka Katiba kwa sababu siasa ni maisha na maisha ni siasa, huwezi kuvitenganisha leo humu Bungeni tunao viongozi wa vyama mbalimbali vya kitaaluma, wapo viongozi wa bodi ya mainjinia, wapo viongozi wa bodi ya wahandisina na viongozi wa Chama cha Mawakili pia wanayo haki ya kuwa Wabunge na wanaokuwa na haki ya kuwa wawakilishi katika taaluma yao. Hilo tunapaswa tuliangalie kwa makini kwa sababu mimi naliona linachukuliwa zaidi kwa kulenga baadhi ya watu fulani na sio sheria kama tulivyofundishwa utungaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbele zaidi naomba nijielekeze kwenye sheria marekebisho ya sheria inayohusiana na Administrator General wa RITA. Waziri ameleta marekebisho anasema Mkurugenzi..., wameandika kwa Kiswahili lile neno nalo ni gumu, lakini ni Administrator General na Deputy wateuliwe na Mheshimiwa Rais. Hawa watu ukisoma katika moja kati ya majukumu ya Administrator General au hiyo taasisi moja kati ya majukumu yake ni kusajili bodi za wadhamini, wanasajili bodi za wadhamini wa vyama vya siasa, mambo ya kidini na mambo ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwenyekiti wa chama cha kisiasa. Unapompa mamlaka ya kumteuwa mtu anayesajili bodi ya wadhamini wa vyama vya kisiasa na mwenye mamlaka ya kufuta bodi hiyo ya wadhamini unaondoe ile impartibility condition ambayo administrator general anatakiwa kuwa nayo. Leo tunaweza kuona ni sawa kwa sababu Mheshimiwa Rais ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, lakini sisi watunga sheria lazima tujue leo kwako kesho kwangu, kesho itakapokuwa kwa upande mwingine Mwenyekiti wa chama kingine akapewa mamlaka ya kuteua Administrator General na Deputy wake madhara yake yatakuwa makubwa kwa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaiondoa ile dhana ya demokrasia ambao imejengwa na waasisi wa Taifa hili, mimi namshauri Mheshimiwa Waziri tuweke na sio tu kwa sababu ni Mwenyekiti wa chama lakini tuangalie mambo ya cheques and balance hebu angalia Mheshimiwa Rais akikosea kumchagua Administrator General, nani anaweza kutengua jambo hilo.

Nimesikitishwa na kufutwa mfano uliowekwa kwenye kitabu cha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sababu umetolewa mfano ambao uko dhahiri. Sasa kwa sababu aliyevurunda kwenye kitu hicho yuko humu ndani amepata mamlaka ni ukurasa wa ngapi samahani naomba nisome, ukurasa wa tano imeelezwa vizuri tu Mheshimiwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge aliwahi kufanya uteuzi wa Mkurugenzi Kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa NSSF na kwa sababu alikosea Rais alipata mamlaka ya kutengua uteuzi ule, lakini kwa sababu Waziri huyo yuko humu ndani amepata Mamlaka ya kufuta kwenye Hansard na sisi tunasema Alhamdullah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kutoa mifano ambayo imetokea kwenye Taifa hili sio discussion power ya mtu mmoJa hili ni suala la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme hivi tunaposema ukimweka Administrator General ateuliwe na Mheshimiwa Rais tutakuwa tunakosa nafasi ya kurekebisha Administrator General kama a-fit kwenye ile position. Tunapomuweka Waziri awe na mamlaka yale endapo Waziri akikosea au Administrator General akishindwa ku-perform Mheshimiwa Rais an a fursa ya kumbadilisha yule Administrator General ndio mfano wangu na ndicho alichokikiri Mheshimiwa Jenista hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina nia mbaya tumeona teuzi nyingi zinafanyika kimakosa, tumeona wateule wengi wanashinda ku-perform to the expectation of the government tunawezaje kuwatoa wakiwa hawa watu ni Presidential Appointees. Wakati mwingine tujifunze kutokana na makosa kuhusiana na jambo hili ndio maana tunasema fursa inapotokea Waziri hafanyi vizuri au ameteua mtu aliyeshindwa ku-perform vizuri tunapata entrance ya kuweza kumuweka mtu atakaye-perfom kwa maslahi mapana ya Taifa hili kupitia kiti cha Rais and that is my all point. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niende moja kwa moja kwenye sheria najua hilo Mhsehimiwa Waziri amelichukua niende kwenye sheria ya urejeshwaji wa mali zitokanazo na uhalifu ambayo ni sehemu ya 13 ya marekebisho na ni Sura ya 256.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii samahani Mheshimiwa Waziri anasema Mkurugenzi wa Mashtaka kuweza kuwasilisha Mahakamani maombi ya upande mmoja yaani asikilizwe yeye peke yake, maombi ya kukamata mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu ambayo ama iko hatarini kupotea au kuharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukishuhudia kwenye Taifa hili watu wanakamatiwa mali zao, wakati mwingine ni kwa hila tu wala hakuna uhalali wowote wa kukamata zile mali, watu wanafungiwa akaunti zao kwa hila tu basi hilo tuliache. Lakini kesi inaendelea Mahakamani mali zinakamatwa mtu anashindwa kuendesha maisha yake, anashindwa kuendesha biashara hilo tumeliacha leo huyo Mwendesha Mashtaka kabla Mahakama haijaamua kama zile mali ni za uhal ifu ama sio za uhalifu anapeleka maombi mali zile ziuzwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza mazingira hapa ya kutaka kuwafanya watu wawe wanyonge ndani ya Taifa lao. Nafasi hii ni rahisi sana kuwa kutumika vibaya na Mwendesha Mashtaka na hii ni kama tu msingi wa ile hoja ya hati anayopeleka Mwendesha Mashtaka ambayo umefutwa kimahama anapeleka kuzuia mtu asipate dhamana kwa sababu yaani sababu anazozijua yeye mwenyewe na haulizwi mahali popote, ile ilifutwa kwa msingi kama huu kwa sababu Mwendesha Mashtaka anaweza kum- misuse powers alizopewa. Mimi niiombe Serikali kwanza maombi ya kuweza kuziuza mali zile yasiwe exparte, yasikilizwe kwa pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwe MWenyekiti, lakini pili maombi yale iwe ni desecration ya mahakama ku-decide kwamba mali zile ziweze kuuzwa ama zisiuzwe bila kumathiri mmiiki wa malizile kwa sababu kwa nchi hii ya leo unapokwenda najisikia vibaya kusema hivi kumekuwa na uvunjwaji mkubwa wa kanuni, sheria na taratibu hasa kwa Serikali ambayo tunaambiwa kila mtu ambaye ameteuliwa na Serikali hamna neutral, lazima kwanza mezani ukae na Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hakuna neutral lazima uegemee upande wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali tuliyofikia sasa hivi uhuru wa Mahakama hawa Mawakili huko hali ni mbaya wote wameambiwa wanatekeleze ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa hali hii tukaruhusu na mali za watu zitaifishwe na kuuzwa, watu watafilisika, mali imeshauzwa, Serikali yenyewe hii iko hoi bin taabani ikija kuonekana mtu yule mali zake ni halali atachukua miaka 100 kuja kulipwa mali zake na kuirudishiwa.

Kwa hiyo, mimi niombe ombi kwa Mheshimiwa Waziri tuondoe suala la exparte kwenye maombi ya kuuza hizi mali, lakini iwe ni desecrationya Mahakama, uhuru wa Mahakama uzingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwe Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee hili suala la ushahidi wa ku-record kweli ni mzuri, mnasema kwamba shahidi atarekodiwa ushahidi wake na atapewa nakala. Niombe tunarudi kule kule sasa hivi tumekuwa kama watu ambao tunaishi kwa tahadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuhumiwa anahojiwa yuko mahabusu, anamaliza kuhojiwa kwa video na picha anaambiwa anapewa nakala yake anaipeleka wapi? Uwezekano ni mkubwa sana kwa Waendeshwa Mashtaka
ku-temper na hizi document kwa hali ilivyo. Mimi nawapenda sana Waendeshwa Mashtaka na ni taaluma yangu lakini niseme tumefika pabaya lazima tupige ndulu. Ushahidi huu uandikwe kwa maandishi, usainiwe na chini ya yule anayechukuliwa ushahidi huu uwe chini ya mwanasheria, uwe chini ya wakili, usainiwe ndipo akabidhiwe ili...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Nakushukuru sana kwa interest ya muda nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu kwenye sheria hii muhimu kwa Taifa letu inayohusu vyama vya siasa.

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kwa kulitaarifu Bunge hili kwamba Ibara ya 20(1) ya Katiba inatoa uhuru wa kuunda vyama vya siasa na Ibara ndogo ya (2) inaeleza mambo ambayo yanapaswa kuzingatia katika uundwaji wa vyama vya siasa na ukiyakiuka mambo haya basi chama hicho kinaweza kikafutiwa usajili. Vilevile ibara ya 3 inasema Bunge linaweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kwamba vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa katika Ibara ya 2 hapo juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Katiba hii hakuna hata sehemu moja inayoonesha kwamba Msajili anaweza kumfukuza mtu kufanya kazi za siasa kwa sababu amemkosea, haipo hata sehemu moja, lakini muswada ulioletwa na Msajili wa Vyama vya Siasa unampa nafasi hiyo Msajili kinyume kabisa na Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikufahamishe kwamba jambo hili halijaja kwa bahati mbaya, tunamfahamu sote hapa Jaji Mutungi, Mheshimiwa Waziri Jenista, Attorney General na tunaifahamu Serikali vizuri hawa ni watu ambao wangeweza kukaa chini na kuleta muswada ambao unakwenda sawa na matakwa ya Katiba, lakini wamefanya hivi kwa makusudi kwa sababu Kanuni za Bunge zinataka, kwamba mapendekezo ya kamati yanayokwenda kwa Serikali yarudishwe kwenye kamati wapitie kama kweli wametimiza yale ambayo Serikali imekubaliana na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepata majibu ya mapendekezo ya Serikali leo asubuhi hapa Bungeni na kwa kukufahamisha tu kwenye mapendekezo ya Serikali yaliyoletwa yapo mambo mengi ambayo tuliafikiana kwenye Kamati hayajafanyiwa marekebisho. La yamefanyiwa marekebisho sivyo Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria walivyopendekeza.

Mheshimiwa Spika, haya mambo hayafanyiki kwa bahati mbaya… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Salome kidogo dakika mbili tu, utaendelea. Mheshimiwa Mchengerwa wewe ni Mwenyekiti wa Kamati.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, ndiyo…

SPIKA: Yuko wapi Mheshimiwa Mchengerwa?

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, nipo.

SPIKA: Haya maneno yanayosemwa ikoje maana yake tulikubaliana kwamba mtapitia kabla.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, Salome Makamba sio Mjumbe wa Kamati yangu kwa hiyo hana ufahamu wa yale ambayo yamerekebishwa na jedwali la Serikali. (Makofi)

SPIKA: Nakushukuru sana, sasa nimeelewa, kumbe Salome unaongea mambo ambayo… Salome endelea sikuwa na nia ya kumkata.

MBUNGE FULANI: (Alizungumza bila kutumia kipaza sauti)

SPIKA: No! no! no! Mimi nilitaka Salome tu nielewe maana yake alikuwa anasema kwamba hakushirikishwa ndio maana nikamnyanyua Mwenyekiti katikati ya mjadala, endelea Salome.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge mimi kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninayo haki ya kuingia Kamati yoyote na kwenda kushuhudia mwenendo wa Kamati na ikibidi naweza kutoa mapendekezo, kanuni inanikataza mimi kupiga kura tu. Kama Kanuni hii iko kwa bahati mbaya mimi naridhia na sitokwenda kwenye Kamati yoyote… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa yaani mimi ninachoona kabisa hujajiandaa. (Makofi)

Eh kabisa kabisa kwa sababu hakuna cha kuficha, ninamuuliza huyu Mwenyekiti nimekukata makusudi nimuulize kwa sababu niliagiza kwamba hii nanii ya Serikali ikishamalizika muione kabla hatujaenda Bungeni na amethibitisha. Sasa wewe ambaye hukuwa Mjumbe hebu iache ajenda hiyo maana yake unapotosha, eeh. Hiyo ajenda yaani iache tu, wenye Kamati yao wapo sio vizuri sana kupotosha mambo ambayo; wewe sema unataka kusema nini Salome?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haimruhusu Msajili wa Vyama vya Siasa kumzuia mtu kutengeneza chama cha siasa eti kwa sababu wazazi wake wote wawili si Watanzania, hairuhusu. Hayo ni masharti yalipo kwenye muswada mpya unaokuja na haya ni marekebisho baada ya mara kwanza kuwekwa sharti kwamba mtu haruhusiwi kutengeneza chama cha siasa ikiwa yeye mwenyewe si raia wa Tanzania kwa kuzaliwa. Yamefanyika marekebisho sasa wameleta aina nyingine wanasema ni lazima wazazi wako wote wawili wawe raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mimi siamui nani anizae hapa duniani, kuzaliwa na wazazi wote Watanzania sio discretion power niliyonayo, ninajikuta nimezaliwa na wazazi mmoja si Mtanzania na mwingine ni Mtanzania. Hiki kifungu hakikubaliki; kwanza ni kinyume na Katiba, lakini pili Msajili hana hayo mamlaka ya kumuamulia mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi katika section 26(2) ya muswada huu Msajili amevikwa mamlaka makubwa zaidi ya kufuta chama.

Mheshimiwa Spika, leo kwako, kesho kwangu, lakini nakuhakikishia dua la kuku halimpati mwewe, hii sheria leo tunaitunga kwa kuangalia kesi zilizopo mahakamani za CUF, leo tunaangalia kwa sababu CHADEMA ni chama cha upinzani, lakini ninakuhakikishia wanasema hii sheria itakuja kuwachinja walioitunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sidhani kama ni sahihi Bunge lako tulipotoshe kwa kumpa mamlaka makubwa namna hii Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kudhani kwamba tunakomesha upande mmoja.

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa kazi yake kubwa na namba moja ni kulea vyama vya siasa. Ukiangalia sheria hii mpya iliyokuja kwako vifungu vingi vinafanya kazi ya kubadilisha kazi ya siasa kuwa ni kazi ya jinai. Kosa dogo humu mtu anaweza akajishtukia amefungwa jela miaka mitatu mpaka miaka 20, kwa kosa dogo tu. Sheria hii inakwenda kupita kimya namna hii tunaruhusu, kazi ya siasa ni kazi ya kujitolea, hakuna watu wanaolipwa kwa ajili ya kufanya kazi ya siasa, lakini tunaruhusu mtu afungwe jela kwa kosa dogo miaka mitatu mpaka karibu miaka 20 na faini juu au vyote kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Si ungekuwa unatoa mifano Salome ili watu wakuelewe unasema kwa kosa fulani…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Nimesema section 26(2) isomwe pamoja na Ibara ya 8(c) na (e) ya marekebisho na section zingine zinazofanana na hizo, zipo nyingi sana. kwa ajili ya interest ya muda naomba nitaje hizo chache.

Mheshimiwa Spika, tulisema wazi kwamba ili kuepuka mgogoro kama uliojitokeza kwenye kikokotoo, namna ya kutengeneza coalition terms and conditions zielezwe kwenye sheria moja kwa moja na sio kwenye kanuni, tunalieleza hilo. Katika eneo la coalition nyuma tumeweka schedule tumeonesha namna gani muungano wa vyama vya siasa unaweza kuundwa, lakini katika sheria hii minister anakwenda kutafsiri yale yaliyoandikwa kwenye sheria mama juu ya muungano wa vyama vya siasa. Tunayo sababu ya kuliangalia hilo kwa kina kabla hatujafunga muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kwenda haraka niende kwenye suala la kufuta vikundi vya ulinzi. Mawakili na wanasheria wenzangu wamepotosha suala lililoandikwa kwenye Katiba la uundwaji wa majeshi. Vipo vikundi mbalimbali vya binafsi vya ulinzi tena vinakwenda mbali zaidi wanapewa rank za kijeshi, wanabeba silaha na wanapewa mafunzo ya kijeshi. Vikundi vya ulinzi tunavyoviongelea hapa ni vile vya mtu kujilinda mwenyewe au wanachama kulinda mali zao cha chama.

Mheshimiwa Spika, leo tunasema hao wamekatazwa na katiba, katiba haijakataza Wabunge wenzangu kwenye hili lazima tusome kwa makini kwa sababu tutapotoshana, haijaelezwa hivyo. Tunao KK Security na Ultimate Security hivyo ni vikundi vya ulinzi na vipo kwa mujibu wa sheria na Katiba. Kwa hiyo, sitaki kuamini kama vikundi vya ulinzi leo eti ni kosa kuwa navyo kisheria mpaka Msajili wa Vyama vya Siasa anataka kuvifuta.

Mheshimiwa Spika, ninachokiona hapa tunalo ombwe kubwa sana juu ya Serikali yetu upande wa Jeshi la Polisi kuwalinda raia. Sijawahi kumuona Katibu Mkuu wa CHADEMA Ndugu Vincent Mashinji anaongozwa na kimulimuli cha polisi wala kulindwa na polisi, tunamlinda wenyewe Katibu Mkuu wetu, lakini juzi Mizengo Pinda amefanya maandamano jambo ambalo limezuiliwa, amesindikizwa na polisi. Bashiru akizunguka mikoani anasindikizwa na polisi… (Makofi)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Sijawahi kuona hata siku moja viongozi wa Chama cha CHADEMA au chama chochote cha upinzani wanasindikizwa na polisi…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu wawili wa wastaafu wapo CHADEMA…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, Kuhusu utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wako wa Kamati ya Kanuni, mtu anaposimama anataka kutoa utaratibu anatakiwa ataje kwanza kanuni gani, wewe ndiye umenifundisha hayo, mimi naachana nayo.

Mheshimiwa Spika, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tunao Mawaziri Wakuu wawili wastaafu, lakini wanatembea/wanafanya ziara kwenye Taifa hili hakuna hata mmoja amewahi kwenda na hicho kimulimuli. Kwa hiyo, kabla hatujaenda kwenye suala la kupitisha kwamba polisi ndio watulinde nafikiri tuanze kujadili impartibility ya Police Department kwenye taifa hili. Nafikiri huo ni mjada mpana ambao ni lazima tuujalidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba hizi mbili za Katiba na Sheria na Kamati yangu ya Sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo napenda kuongea mambo machache. Kwanza, napenda kuongelea misingi miwili ya Utawala Bora katika nchi yoyote inayoendeshwa Kidemokrasia. Misingi miwili nitakayoiongelea, wa kwanza ni mgawanyo wa madaraka, kwa maana ya separation of power na wa pili ni uwajibikaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote inayotambua misingi hii miwili ya Utawala Bora, ni lazima, siyo tu itekeleza misingi hii, lakini pia ionekane kwamba inatekeleza kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, hasa kwenye upande wa mgawanyo wa madaraka, Tanzania katika uendeshaji wa shughuli za Serikali, tunayomihili mitatu, kwa maana ya Mahakama, Serikali na Bunge. Juzi tulikuwa na Siku Maalum ya Sheria hapa Tanzania. Katika siku hiyo Maalum, iliyofanyika karibu nchi nzima, kitu kinachotarajiwa kwenye siku ile, viongozi wa Judiciary wanategemewa kuitumia siku hiyo kama siku maalum kujadili changamoto na namna bora ya uendeshaji wa Mahakama katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa ambacho nilikishuhudia kinaendelea, ni namna ambavyo Judiciary wanawapa nafasi watu wa Executive (Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa) kwenda kutangaza yale ambayo wanayafanya kwenye Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko forum mbalimbali ambazo tunaweza kuzitumia kutangaza haya tunayotangaza, lakini siku ya Wanasheria Duniani Watanzania wangependa kusikia ni namna gani Judiciary wamejielekeza kupunguza mlundikano wa kesi zisizokwisha Mahakamani, ni namna gani wanapunguza mahabusu waliolundikana Magerezani, ni namna gani wanaongeza Mahakama, ni namna gani wanaongeza Mahakimu na Majaji, katika nchi hii, ili siyo tu haki itendeke, bali ionekane imetendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaona Majaji na ilitokea Iringa kule, picha moja inazunguka kwenye mitandao. Jaji na Mkuu wa Mkoa, Jaji ki-hierarchy ni mtu mkubwa sana. Sijui kama wamejawa na hofu, sielewi. Jaji anatembea pembeni, kwenye Red Carpet anatembea Mkuu wa Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali itekeleze mambo yake ya Executive na iiache mhimili wa Mahakama uweze kufanya kazi kwa uhuru, ufanye kazi kwa weledi na utashi. Kwa sababu pamoja na kuhubiri maeneo mbalimbali kwamba haki inatendeka, haipaswi...

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka niishauri Serikali, iliwekwa misingi ya Utawala Bora, iliwekwa misingi ya Uwajibikaji, yote hiyo ni kutoa sintofahamu na kutoa ombwe kubwa ambalo lilikuwepo la kuonekana mihimili hii inaingiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa wale wanaosoma, Wanazuoni, huu mjadala ni mkubwa sana. Nawaomba sana, Serikali, Mahakama na Bunge, kuepusha maneno yanayojitokeza ya kuonyesha kwamba mihimili hii inatawaliwa na mhimili wa Executive. Hebu tuoneshe kwa vitendo kwamba tunaweza kujisimamia, kwamba tunaweza kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Katiba na Sheria na Katiba inatulinda kufanya hivyo.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye hoja ya pili kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi, ni lazima kila mtu awajibike kwenye eneo lake. Leo Mheshimiwa Selasini ameeleza vizuri kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Waziri wakati anajaribu kujibu, anasema jambo hili linafanyika kwa uwazi. Sisi ni Wabunge, ni Wawakilishi wa Wananchi, tunasimama hapa kutoa maoni na mapendekezo yetu ya namna bora ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nafikiri Mawaziri wangetumia fursa hii kusikiliza maoni yetu, kuyasimamia, kuyatekeleza kwa mustakabali wa Taifa hili kuliko kusimama kuwa defensive, kwa sababu haimsaidia mtu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Chaguzi kwenye nchi hii ni moja kati ya kitu ambacho kinaweza kutuletea matatizo ambayo yanaweza kuvunja amani. Tusipoandaa uchaguzi huu kwa kufuata taratibu za ushirikishwaji wa wadau…

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sisi Wabunge, moja kati ya jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunaisaidia nchi hii kuwapa uelewa mzuri wa yale tunayoyatunga humu ndani wananchi wetu, kuwasaidia kuwafikishia taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakuja kukutana hapa Bungeni tena mwezi wa Nne, tukitoka hapa ni mwezi wa Saba. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aweke uwazi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili tunapotoka hapa, moja kati ya majukumu yetu iwe ni kwenda kuwaelimisha wananchi na kuwapa taarifa juu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, anasema hiyo kazi inafanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ndicho kinachofanya leo na kesho sisi Wabunge tutukanwe na kuonekana hatuna maana. Tunatoa ushauri, Serikali inaelewa kuliko sisi tunaowakilisha wananchi. Mwisho wa siku, ndiyo kauli zinapozuka mtaani, unazisikia zile; kama ile aliyosema CAG, sijui ameshaomba radhi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipohutubia Bunge hili kwa mara ya kwanza. Moja kati ya kitu Mheshimiwa Rais alisema, ni lazima tufute tozo za kero kwa wananchi kwa sababu zinapunguza ufanisi na zinazuia wananchi kufanya shughuli za maendeleo. Juzi Mheshimiwa Rais ameanzisha kitu kinaitwa Vitambulisho kwa Wajasiriamali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nami nichangie Muswada huu kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumshauri Waziri mwenye dhamana kwamba muda uliowekwa kwa ajili ya kutoa taarifa ya kuendeleza ardhi kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Ardhi wa miezi sita ni mchache sana. Sote tunafahamu kwamba lengo la mkopo ni kufanya biashara, sheria imelazimisha mtu achukue mkopo na aende akaendeleze eneo ambalo amekopea, kitu ambacho kwangu naona si sahihi kwa sababu akiwekeza au akiendeleza eneo lile inawezekana haikuwa malengo ya mkopo ule na hivyo anaweza akashindwa kurejesha, jambo ambalo linaweza likasababisha akanyang’anywa ardhi pia na hiyo financial institution.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme, ama kifungu hiki kiangaliwe kwa umakini zaidi au kama itawezekana muda wa kutoa taarifa ya uendelezaji uongezwe ili yule mtu aweze kuiwekeza ile pesa kwenye eneo lile kwa awamu ndogo ndogo wakati anakamilisha malengo yake ya kuchukua mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niseme kuna mkinzano mkubwa sana kati ya Sheria ya Uendeshaji wa Mabenki Tanzania na sheria hii kwa sababu benki hazitoi mkopo kwa ardhi ambayo haijaendelezwa. Kwa sababu hiyo, ni lazima ili tuweze kupata maelewano kati ya sheria hizi mbili, Serikali ione umuhimu wa kuongea na watu wa benki waelewe nini lilikuwa lengo la kuweka sheria hii ili inapofikia kwamba wanatakiwa kuwakopesha watu ambao hawajaendeleza ardhi, pesa ziweze kutolewa kwa watu wale kama ambavyo sheria inaeleza, lakini mpaka sasa bado kuna ukinzani mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe mawazo yangu kwenye huu Muswada wa Utumishi wa Umma. Nadhani wadau katika Muswada huu hawajashirikishwa vizuri. Serikali imefikia maamuzi ya kuongeza kuanzia miaka 60 kwa hiari
na miaka 65 kwa lazima lakini bado ipo haja kubwa sana ya kuweza kuangalia maoni ya wadau. Kwa sababu kuna mafunzo mbalimbali yatatoka hapo watapewa wale wataalam ambao wamefikisha miaka 65, tunadhani yatafanyika kwa ufanisi na wakati mtu huyu tayari ana umri mkubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiachana na hilo; unadhani kwa kuongeza mkataba, kwamba mtu atastaafu kwa miaka 65 kwa lazima, unadhani ndiyo inaleta ufanisi au unamlazimisha yule mtu afanye kazi hata kama hataki? Ndiyo tunarudi kwenye suala la morale; professionalism inakwenda na morale. Kwa hiyo nimshauri sana Mheshimiwa Waziri akazungumze vizuri na wadau kuhusu kuongeza umri, kwa sababu mimi naamini si wote ambao wanapendezwa na suala la kuongezwa umri wa kustaafu kama ambavyo imeelezwa katika proposal hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nimalizie kwa kusema kwamba hii Sheria ya Ardhi kuna jambo la msingi ambalo tumelikwepa la zile ardhi ambazo zinamilikiwa kimila; bado nahitaji ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana. Anasema wale wanaomiliki kimila, mabadiliko ya sheria hii hayatawagusa, lakini wapo watu wanamiliki maekari ya ardhi kimila na wanatamani kufanya uwekezaji kwa kuchukua mikopo; na hizi ndiyo zimekuwa kelele za Wabunge wengi humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi ardhi zao wanamiliki kimila na si kwa utaratibu wa Serikali na wakati mwingine sio kwa kutaka kwao, ni kwa sababu mfumo wa kupata hatimiliki ya Kiserikali bado haujakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili la wale wanaomiliki zile hati kimila; naamini ipo sababu ya msingi kama kweli tunataka kufanya uwekezaji wa ndani, kama kweli tunataka kujenga Tanzania ya viwanda na kuwapa uwezo watu ambao wanawekeza, ipo sababu ya kuzingatia umiliki wa kimila. (

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.