Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainabu Mussa Bakar (3 total)

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mtu husajili namba kwa mujibu wa mahitaji yake na mahali alipo akiwa ni Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar. Je, haiwezekani usajili huo kwa kuzingatia sayansi na teknolojia kuratibiwa pamoja?
Swali la pili, je, ni kitu gani kinachozuia mtu anayesajili namba zake Zanzibar kuweza kutumia namba hizo hizo akiwa Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi sheria hii siyo sheria ya Muungano na ndicho kitu kinachozuia namba za Tanzania Bara kutumika Tanzania Zanzibar na Tanzania Zanzibar kutumika Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tumeliona kama Serikali na Kamati kikao cha pamoja kinachoshughulikia kero za Muungano kimeliona na kikao cha mwisho kimefanyika tarehe 13 Januari, 2017 chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais na kimetoa maelekezo kushughulikia kero zote za Muungano ikiwa ni pamoja na hii ya usajili wa magari. Hivyo, kwa Serikali yetu tumeliona na tunaona kwa sababu tumepewa maelekezo Mawaziri wa pande zote mbili, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Waziri wa Fedha wa Tanzania pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, tutakaa pamoja kuhakikisha kero hii inaondoka, lakini kwa mujibu wa sheria itakapokuwa tayari sheria hii italetwa ndani ya Bunge lako Tukufu ili kama Bunge lako litaridhia, tuweze kubadilisha utaratibu huo.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; Serikali wamesema wameweka mikakati, nataka kujua ni mikakati ipi ambayo wameweka ili kupunguza ama kumaliza tatizo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana na kesi mbalimbali zinapelekwa mahakamani na baadhi ya kesi watuhumiwa wanashinda kutokana na kwamba kuna vitu ambavyo vinakosekana kama vile shahawa ama majimaji ambayo yanalingana na yule mwanaume ambaye amembaka au kumnajisi mtoto, je, Wizara ya Afya imeshusha mwongozo gani kuwashushia Madaktari ili kuwaongoza waweze kupima vitu kama hivyo ili wananchi wasikate tamaa kupeleka kesi zao mahakamani na kushindwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kubaini ukubwa wa tatizo na nianze kwa kutoa takwimu tu kwamba kati ya Januari mpaka Desemba, 2017 tulikuwa na matukio 41 ya ukatili wa kijinsia na kati ya hayo, 13,000 yalikuwa ni masuala ya ukatili dhidi ya watoto. Sisi kama Serikali tumeandaa mpango mkakati wa kuzuia ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto ambao unaitwa MTAKUWA wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha mwaka 2021/2022. Katika mkakati huu tumejielekeza katika maeneo makubwa yafuatayo:-

Moja, kuanzisha Kamati za Ulinzi na Usalama wa Wanawake na watoto ambapo mpaka sasa hivi kuna kamati zaidi ya 10,000 tumezianzisha katika ngazi mbalimbali kuanzia Taifa, Mikoa, Wilaya na katika ngazi ya Halmashauri hadi katika Kata; kuanzisha madawati ya jinsia ndani ya Jeshi la Polisi zaidi ya madawati 400 tumeshaanzisha. Sambamba na hilo, kumekuwa na kuanzishwa na mahakama maalum za watoto ili mashauri ya watoto yaweze kukaa na kusikilizwa. Tunaendelea kushauriana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba kunakwa na Walimu walezi ambao wanaweza wakatoa ushauri nasaha na kupokea baadhi ya mashauri kwa watoto ule ukatili ambao wanafanyiwa wakiwa majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kama nilivyoeleza katika jibu la msingi ni kwamba mashauri mengi tunashindwa kuyafikisha mwisho kwa sababu wanaofanya ukatili huu ni watu ambao wako ndani ya familia. Kwa hiyo, nami nitoe rai kwa jamii kwamba tusiyamalize mashauri haya kifamilia na badala yake turuhusu mkondo wa kisheria uweze kuchukua nafasi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ameelezea kwamba kushindwa kwa baadhi ya kesi kwa sababu ya ushahidi wa kitaalam kutoka kwa wataalam wetu wa afya. Hili tumeshalitolea maelekezo kwa wataalam wetu wote wa afya na tumeweka msisitizo mkubwa sana kwamba mtu yeyote katika Sekta ya Afya ambaye amepewa jukumu la kuthibitisha vipimo ambaye atakwenda kinyume na misingi na miiko ya maadili ya taaluma hatutasita kumfungia na kumfutia leseni ya Udaktari.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sijaridhika na majibu ya Serikali. Swali la kwanza, ni takribani miaka sita au saba huko nyuma, kwamba hizo nyongeza hazitolewi na Serikali. Je, hatuoni kwamba Serikali inafanya makusudi kufinya bajeti ili kuwakosesha Walimu hao nyongeza hizo za mishahara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kama hii ipo kisheria, ni kwa nini Serikali inashindwa kutoa hiyo nyongeza ya mishahara na mara ya mwisho imetoa lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hapa kwenye jibu la msingi kwamba kulingana na kanuni za kiutumishi ambazo watumishi wote Tanzania sio Walimu tu watumishi wote wanajua, kwamba Serikali inapanga kuamka, kwa mfano kwaka huu wa fedha 2019/2020 kwenye bajeti yetu, kama hatukuuingiza kipengele cha nyongeza ya mishahara ambapo najua kuna tamko pale litatolewa kwenye Sherehe za Mei Mosi, maana yake ni kwamba mwaka huu kama hawataongeza mishahara halipaswi kuwa deni. Hili kwa mujibu wa kanunu za kiutumishi watumishi wote wanajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Serikali kutathimini, tumesema mara ya mwisho nyongeza ya mishahara imetolewa mwaka 2017/2018, kwa hiyo hili kimsingi sio deni. Serikali inapanga kuinua mapato yake kama kuna uwezo wa kuongeza inaongeza na haya hayapaswi kuwa malalamiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.