Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tunza Issa Malapo (21 total)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kutoa masahihisho, Naibu Waziri wakati anajibu aliniita Malopo naitwa Malapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kuwaambia wananchi kuwa haiko tayari kutekeleza Sera ya Elimu Bure kwa maana halisi ya Kiswahili ya neno bure isipokuwa elimu inayotolewa sasa ni ya kuchangia gharama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini wito wa Serikali kwa wananchi kuhusu sera hii ili kuwawezesha walimu kufanya kazi yao bila kero kutoka kwa wazazi wanaofikiri hawawajibiki kulipa pesa yoyote kwa ajili ya elimu hiyo kwa watoto wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Kwanza naomba radhi kwa kukosea jina la Mheshimiwa Mbunge ni Malapo na nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kwamba Serikali iseme haina nia ya dhati katika suala zima la elimu bure, ndugu zangu naomba niwaambie, kama sisi ni mashahidi wa kweli vijana wengi waliokuwa wanaenda sekondari walikuwa wanashindwa kulipa hizi gharama za kawaida. Hata wale waliokuwa wanaanza elimu ya msingi mnafahamu wazazi wengi sana wanashindwa kulipa zile gharama za awali ili mtoto wake aweze kujiunga na shule na ninyi wenyewe ni mashahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi juzi kupitia vyombo vya habari wazazi wanakiri kabisa kwamba suala hili limewasaidia kwa kiwango kikubwa vijana wao kwenda shule. Hata turn over katika shule zetu imekuwaje? Hata madarasa wakati mwingine shule zinahemewa kwa sababu wazazi wote ambao mwanzo walikuwa wanakwazika na gharama hizi sasa wanapata fursa ya kuwapeleka watoto wao shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukiri kwamba Serikali katika hili imefanya juhudi kubwa sana. Naamini jambo lolote lazima lina changamoto zake, hizi changamoto ndogo-ndogo ni kwa ajili ya kuboresha ili mradi mpango uende vizuri lakini dhana ya Serikali imekamilika na inaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu ya pili, wito wa Serikali Walimu wasibughudhi wazazi, nadhani tumeshasema wazi na Waziri wangu jana alilisema wazi kwamba jambo kubwa elimu hii ni bure. Hatutarajii mwalimu awazuie watoto kwenda shule kwa kuzusha mchango wake mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tumesema tutakuwa wakali sana kwani lengo kubwa ni mtoto wa Kitanzania aweze kupata elimu ya shule ya msingi na ya sekondari mpaka form four. Lengo ni kwamba kila mwanafunzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania apate fursa ya uongozi na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri wa TAMISEMI kutokana na maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Malapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya jitihada kubwa katika suala hili la elimu bure, lakini inasikitishwa kwamba wenzetu walihoji fedha hizi zimetoka wapi kwenye bajeti na leo fedha hii iliyotolewa kwa ajili ya kusaidia jamii maskini watoto wao waende shule wanahoji tena hiyo bure gani, ni mkanganyiko ambao haueleweki. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu, katika kila shule za msingi za kutwa tutapeleka kila mwezi shilingi 600/= kwa kila mtoto kwa ajili ya uendeshaji. Kwa shule za sekondari za kutwa tunapeleka kwa kila mwezi shilingi 3,540.57/= kwa kila mtoto kwa ajili ya uendeshaji wa shule. Kwa wale wa bweni tunapeleka shilingi 7,243.39/= kwa kila mwezi. Fedha hizi zikijumlishwa uwezekano wa kuendesha elimu upo pamoja na changamoto zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninavyozungumza kutokana na mpango huu wa elimu msingi bila malipo pale ambapo tulitegemea wajiandikishwe watoto 80 kuanza darasa la kwanza wamejiandikisha 240; pale tulipotaka wajiandikishe watoto 180 wamejiandikisha karibu 700 na hiyo ni Dar es Salaam tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako baadhi ya maeneo uwezekano tu wa kuwapokea watoto hawa ni mgumu kwa sababu wazazi maskini wameona mpango huu ni muhimu kwao na umewasaidia sana.
Kwa hiyo, kuubezabeza hapa ni kwenda kinyume kabisa na wananchi ambao wanaona mpango huu umewasaidia na kwa hakika kusema kweli unalisaidia Taifa. Tupingane katika mengine lakini kwenye jambo zuri tutiane moyo kama Watanzania. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini ujenzi huo utaanza? Kwa sababu barabara hii imekuwa ikizungumzwa kwa muda mrefu. (Makofi)
Swali la pili; issue hapo ni ku-sign mkataba ama ni pesa? Kwasababu tumekaa kwenye kikao cha RCC ingawa Meneja wa TANROADS Mkoa alishindwa kusema wazi, lakini kinachoonekana pesa hakuna. Kwahiyo, issue ya msingi naomba kujua; ni kwamba mkataba haujasainiwa ama pesa zinazofanya mkataba usainiwe hazipo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Tunza Issa Malapo, kwa niaba ya Wabunge wote wa Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu walikuwa na kikao cha RCC na walikataa kuijadili barabara hii wakataka ije ijadiliwe hapa Bungeni. Naomba nikuhakikishie, hamna sababu ya kuijadili hapa Bungeni. Barabara hii imetengewa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2016/2017 barabara hii imetengewa fedha tutakayohakikisha hizo kilometa 50 zinajengwa. Tunachosubiri ni taratibu za mkandarasi ku-sign mkataba kukamilishwa. Fedha zimetengwa!
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Naomba anieleze ni tatizo gani linalofanya Mji huu usipate maji ya kutosha na ya uhakika wakati vyanzo vya maji vipo?
(b) Pia ni lini wananchi hawa walioteseka kwa muda mrefu hasa wanawake watapata maji safi na salama? Nataka time frame, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni matatizo gani yanafanya wananchi hawa wasipate maji. Ni kweli kabisa kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, katika Mikoa na Wilaya ambayo nilitembelea ni pamoja na Wilaya ya Nanyamba. Maeneo yale yana vyanzo vikubwa vya maji vya Mitema na Mkunya. Tatizo ni kwamba huko nyuma tulikotoka upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo siyo mzuri na kwa sababu tumekuwa tunaishi kwa kutegemea wafadhili vile vile. Hilo ndilo ambalo limefanya miradi ile isiweze kukamilika na kutoa maji yale yanayotakiwa kwa matumizi ya wananchi wa Nanyamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza ni lini. Sasa hivi tumeingia kwenye program ya pili ya maendeleo ya maji ambayo tunatarajia Serikali inatenga fedha na tunaanza kutenga fedha kuanzia mwaka ujao wa fedha, pia wafadhili wametuahidi na kuna juhudi kubwa ambayo inafanywa na Serikali kupitia Waziri wa Fedha, lakini na Mwanasheria wa Serikali pia ambapo tunaongea na wafadhili waweze kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha hii miradi ya Mito ya Mitema na Nanyamba ambayo itahakikisha kwamba vyanzo vya Mitema na Mkunya ili tuweze kuhakikisha maji yanapatikana kwa hizi Wilaya za Nanyamba pamoja na Tandahimba.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa vile Waziri amekiri kwamba, miradi mingi ya umwagiliaji ilikuwa na matatizo sasa je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu wakandarasi na wote waliohusika kufanya ubadhirifu wa pesa hizo nyingi, hasa ukizingatia kuna mradi wa umwagiliaji kule Kitele, Jimbo la Mtwara Vijijini mkoani Mtwara, ambalo kwa kweli wananchi walijitolea eneo lao, lakini mradi umejengwa chini ya kiwango, mifereji ina nyufa
na ule mradi haujaanza kutumika. Nini kauli ya Serikli kuhusu miradi hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kama nilivyosema hii miradi tunaifanyia mapitio, lakini pale itakapoonekana mkandarasi au kuna mtu yeyote amefanya ubadhirifu, Serikali itachukua hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, naomba asiwe na wasiwasi, lakini lengo kubwa hasa la Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi hii tunaikamilisha ifanye kazi iliyokusudiwa kwa wananchi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kupandishwa hadhi Zahanati ya Likombe katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa Hospitali ya Wilaya kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mrundikano wa wagonjwa hasa katika wodi ya wazazi. Je, ni lini Serikali itapanua wodi ile ili akinamama wale waweze kusitirika wakati wanatimiza haki yao ya msingi kama wanawake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, population ya Mtwara Mikindani sasa hivi imekuwa kubwa kutokana na kuingiliana na mambo ya gesi. Hata hivyo, hivi sasa tunaenda katika harakati za kufanya ukarabati wa vituo vipatavyo 142. Zoezi hili haliishi hapa; Serikali inajielekeza tena kupanua vituo vingine vipya ambako kuna population kubwa. Kituo hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumzia hapa tutakichukua kama sehemu ya kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kufanya commitment katika kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, hii tutaweka ni sehemu ya kipaumbele kuwahudumia wananchi wa Mikindani ili waweze kupata afya bora katika maeneo yao.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokana na ripoti ya CAG mpaka sasa hivi inaonekana ni 6% tu ya gesi inatumika, inayosafirishwa na hilo bomba na uwekezaji huu ni wa pesa nyingi. Nataka kujua Serikali imejipanga vipi kuhakikisha uwekezaji huu unaleta tija kwa Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna utata mkubwa katika uwekezaji huu kujua gharama halisi: Je, Serikali ipo tayari kumtaka CAG afanye special audit katika uwekezaji huu? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza bomba la kusafirisha mafuta au gesi kwa sasa kutoka Madimba (Mtwara) hadi Dar es Salaam ndiyo bomba kubwa tulilonalo kwa upande wa gesi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa sasa hivi gesi inayosafirishwa ni kati ya 6% hadi 10% ya uwezo wake na uwezo nimetaja ni milioni cubic feet 744. Sasa ni kwa nini? Bomba hilo lina upana wa inchi 36, ni kubwa; na mahitaji ya sasa ni megawati 668 tulizonazo kwa upande wa gesi, lakini miundombinu inayojengwa ndiyo mikakati sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunajenga miradi miwili ya kusafirisha gesi Kinyerezi I na Kinyerezi II. Kinyerezi I tunafanya extension ya kuongeza megawati 185 ili katika Kinyerezi I pekee zifikie 335.
Mheshimiwa Spika, kadhalika tunajenga mradi mwingine katika Kinyerezi II ambao utaweza kutoa megawati 240. Sasa miradi hii miwili ikikamilika, mahitaji makubwa ya gesi yataongezeka. Kwa hiyo, itazidi 6% hadi 10% na tuna matarajio inaweza kufikia asilimia 20 hadi 30.
Mheshimiwa Spika, miundombinu inayojengwa kuhitaji gesi, bado ni mingi; tunahitaji umeme wa kutosha. Kwa sasa hivi umeme hautoshi. Ni matarajio yetu kwamba mara baada ya miradi mingine, tutakwenda Kinyerezi III utakaoanza mwaka 2018 utakaohitaji megawati 600. Kwa hiyo, mahitaji ya gesi bado yatakuwa ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, lingine niseme mkakati mwingine, unapokuwa na gesi ya kutosha inakuruhusu kujenga miundombinu mingine kwa sababu una stock. Kwa hiyo, siyo hasara kuwa na gesi nyingi lakini kadhalika mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba hii gesi tunasafirisha kadri iwezekanavyo ili ichangie sana katika upatikanaji wa umeme. Mkakati wa Serikali ni kutumia gesi zaidi ili kuachana na mafuta ili kuwapunguzia mzigo wananchi, hilo ni katika ufafanuzi wa swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukaguzi, mahesabu ya Serikali hukaguliwa mara kwa mara, ni utaratibu wa kawaida. Kama ambavyo kila mwaka CAG hukagua, hata miradi hii ataendelea kuikagua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, suala la ukaguzi wa miradi ni endelevu, CAG ataendelea kukagua ili hali halisi iendelee kufahamika.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, wamesema wanaajiri walimu wa sayansi, hisabati na kadhalika, lakini bado tatizo la walimu hao ni kubwa. Nataka kujua tu, wamefanya sensa, ni walimu wangapi wa sayansi ambao kila siku wanaacha kazi kwa sababu ya maslahi duni katika Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili ni gumu sana, kwa sababu hatuna takwimu za kila mwaka kwamba ni walimu wangapi wa sayansi na hisabati wanaacha kazi.
Lakini comfort niliyonayo na ambayo nataka niwape Waheshimiwa Wabunge ni kwamba malalamiko tuliyonayo ni ya walimu kutaka kuhama haraka katika shule wanazopelekwa, yaani mwalimu anaweza akapelekwa kwenye shule fulani, akikaa baada ya wiki mbili anataka ahame. Hiyo ndiyo changamoto kubwa tuliyonayo ambayo tunaishughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuacha kazi, hilo naomba sana tutoe majibu baadae.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuendeleza viwanja vingi vya michezo, ikiwemo kiwanja cha Nangwanda Sijaona katika Manispaaa ya Mtwara Mikindani.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kurudisha viwanja hivyo Halmashauri kama ilivyofanya kwenye mashamba yasiyoendelezwa ya watu binafsi? (Makofi)
Swali langu la pili, kwa kuwa michezo ni afya, michezo ni ajira, na michezo ni furaha. Kwa kuwa chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi na kuwafanya wanamichezo wetu wacheze katika mazingira duni...
Mheshimiwa Spika, naomba unisikilize. Michezo ni afya, ni furaha na ni ajira. Kwa kuwa, Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi hatuoni kwamba Chama cha Mapinduzi kina nia ya kudunisha wanamichezo wetu kwa sababu wanapata ajali mbalimbali wanapokuwa wanachezea katika viwanja hivyo? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikuhakikishie kupitia Bunge lako tukufu kwamba, siyo kweli kwamba CCM imeshindwa kwa sababu asilimia 99 ya michezo yote nchini inaendeshwa kwenye viwanja hivyo, sasa kushindwa huko kukoje? Sasa hivi tunaanza Ligi Kuu ya Tanzania na sehemu kubwa ya michezo hiyo itachezwa kwenye viwanja hivyo hivyo.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wewe kwamba vingi haviko kwenye hali nzuri sana na Wizara ilikuwa imeiachia Shirikisho la Soka nchini kufanya majadiliano na wenye viwanja, sasa tumeona maendeleo siyo ya kasi ya kutosha, Wizara imeamua yenyewe sasa siyo tu kwa kushirikisha Shirikisho la Soka nchini, mashirikisho yote ya michezo nchini, kukaa pamoja na wamiliki tuweze kukubaliana namna ya kuboresha hivi viwanja na kuweza kupata misaada ambayo kwa kawaida itakwenda kwa urahisi zaidi kwa taasisi ambazo zina ubia na Serikali. Tunataka watuachie ubia wawe na ubia na Serikali ili tuweze kurabati viwanja, kama ambavo FIFA ilivyoweza kukarabati Kiwanja cha Kaitaba na Kiwanja cha Nyamagana.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba mitambo ni michakavu na ni kweli ni ya muda mrefu; je, imejipangaje kununua mitambo mipya ulizingatia kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme katika mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara?
Swali la pili; ni lini Serikali itaunganisha mfumo wa gesi asilia ili uweze kutumika katika majumba ya Mkoa wa Lindi na Mtwara ukizingatia kwamba kule ndiko gesi inakozalishwa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Tunza Malapo kwa kufuatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Mtwara. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi; kwanza, Serikali baada ya kuona uchakavu wa mitambo hii tisa ya Kituo cha Mtwara, imenunua mitambo miwili mipya. Hivi ninavyozungumza, kazi ya ufungaji wa mitambo hii inaendelea ambayo itazalisha megawati nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua Mikoa ya Mtwara na Lindi mahitaji yanaongezeka, Serikali imekuja na mpango wa kujenga mitambo mingine ya kuzalisha umeme megawati 300 kwa kutumia gesi na mpaka sasa Kampuni ya JICA imeendelea na upembuzi yakinifu. Kama ambavyo tumesema kwenye bajeti yetu mradi huu utaanza kutekelezwa mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeliona hilo na kwamba mradi huu mkubwa wa megawati 300 utatatua matatizo yote katika Mikoa hiyo ya Kusini na pia itaupeleka umeme katika Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameeleza ni lini mpango wa kusambaza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tunza ameulizia ni lini mpango wa kusambaza gesi asilia majumbani katika Mkoa wa Mtwara utaanza? Napenda nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo ameona hivi karibuni tumezindua mpango wa kusambaza gesi asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini Mkoa wa Dar es Salaam unakwenda sambamba na Mikoa ya Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, hii kazi itafanyika katika mwaka 2018/2019, tutasambaza gesi katika maeneo mbalimbali kwa matumizi ya majumbani kwa Mikoa hiyo. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawaili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Manispaa ya Mtwara Mikindani tatizo kubwa ni miundombinu ya usambazaji wa maji, maji yapo, lakini miundombinu ndilo tatizo. Namuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini miundombinu ile itaboreshwa, ili kusudi zile kata za pembezoni zipate maji ya uhakika? Maana tumekuwa tukiliongea suala hili siku nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kumekuwa na kero, watumiaji wa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani wanalalamika kwamba, wanabambikiwa bill na hiyo inatokana na mamlaka kushindwa kusoma bill katika nyumba zote kutokana na ufinyu wa wafanyakazi. Je, Mheshimiwa Waziri, anatambua kama kuna ufinyu wa wafanyakazi katika mamlaka na kuna jitihada gani za kuhakikisha wanapatikana wafanyakazi wa kutosha? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tumesaini mkataba wa shilingi bilioni tano kwenye Mamlaka ya Maji ya Mtwara ambayo katika huo mradi utaongeza vyanzo lakini pamoja na miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Mtwara na hiyo ni hatua ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na usomaji wa bills kwenye nyumba za watu tayari sasa hivi malalamiko yaliyokuwepo baada ya muda mfupi, yatakwisha kwa sababu, sasa tunatumia teknolojia mahususi ambayo kwanza hakutakuwa na mtu kuzidishiwa bill. Ni kwamba, zile mita zitasoma unit baada ya maji kupita sio baada ya hewa kupita, kwa hiyo, suala hilo Mheshimiwa Mbunge tutalimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo Mheshimiwa Mbunge Ilani ya Chama cha Mapinduzi tayari itatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ambao utaleta maji Mjini Mtwara na baada ya hapo Mji wa Mtwara hautakuwa na tatizo tena la maji, maji yatakuwa mengi, yatahudumia maji ya majumbani pamoja na maji ya viwanda. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira tu, Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi inafanyia kazi hili na tayari baada ya muda mfupi utekelezaji wa mradi huo mkubwa utaanza.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Mwambe nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kuna taarifa kwamba mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kukamilisha miradi hii ya REA katika Mkoa wa Mtwara, hasa Wilaya ya Masasi yenye Jimbo la Ndanda pamoja na Nanyumbu ana matatizo ya kiusajili.
Je, Serikali haioni ni wakati mwafaka wa kuachana na mkandarasi huyu na kumtafuta mwingine ambaye atakamilisha kazi hii kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, umeme ni huduma, lakini pia umeme ni biashara. Inakuaje mji mpya unapoanzishwa watu wamekaa wanahitaji huduma ya umeme lakini hawaipati kwa wakati? Serikali mnahujumu shirika hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza kwa niaba ya Mheshimiwa Cecil Mwambe na swali lake la kwanza limejielekeza kwa Mkandarasi anayefanya Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambaye kwa mujibu wa jibu langu la msingi nimemtaja, JV RADI Services.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge, nataka nimthibitishie kwamba mkandarasi huyu siyo kwamba ana tatizo la usajili, ni utaratibu wa kawaida wa kuhakiki ambao upo ndani ya Serikali. Kuna jumla ya Wakandarasi sita katika Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambao uhakiki wao unaendelea kwa vyombo mbalimbali.
MheshimiwaMwenyekiti, kwa hiyo, naomba wakazi wa Mtwara wavute subira kwamba hivi karibuni tu uhakiki huo utakamilika na ataendelea na kazi. Sambamba na hilo, pamoja na uhakiki huo, huyu mkandarasi alipewa mkataba kwa mujibu wa taratibu, lakini pia ameanza kazi. Kuna vijiji kama vitatu Mtwara Vijijini amewasha umeme, anaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kwa maeneo ya miji ambayo inakua, Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba upatikanaji wa umeme au uunganishwaji wa miundombinu ya umeme unakuwa ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na kama ambavyo tumewasilisha bajeti yetu jana, kuna miradi mbalimbali ambayo Serikali imeona ianze kutekeleza ili kukidhi mahitaji ya umeme katika miji inayokua. Mfano, kuna mradi unaokuja peri-urban Awamu ya Kwanza utakaoanza mwaka wa fedha 2018/2019. Pia hata densification ya awamu ya pili ambayo ni kwa mikoa 11 ikiwemo Mtwara, Dodoma, Kagera, Singida, Lindi, Kilimanjaro, itaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeliona hilo kwa kuwa kazi ni nyingi na tumeona tuisaidie hilo liweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza; nataka tu kujua katika ile Hospitali ya Mkoa ya Ligula kuna Madaktari Bingwa wangapi na wanatibu magonjwa gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa hospitali ile ni ya mkoa, maana yake inahudumia mkoa mzima na ni ya rufaa na sisi hatuna hospitali ya kanda, Kanda ya Kusini, bado haijaanza kufanya kazi.

Katika jibu lake la msingi amesema Madaktari wa kufanya upasuaji wa kawaida na mifupa bado wapo masomoni wanasoma na ukizingatia kuna ajali nyingi zinazotokea, anawaambia nini vijana, wananchi wa Mtwara ambao wanapata matatizo, wanataka tiba ya upasuaji wa kawaida na mifupa; wasubiri mpaka mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mtwara, Ligula tuna Daktari Bingwa mmoja katika Magonjwa ya Akinamama, lakini tunatambua kwamba tunahitaji huduma za Madaktari Bingwa katika hospitali zetu za rufaa za mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tulitangaza nafasi hizi Madaktari hawa hawako mtaani na ndiyo maana sisi kama Serikali tumewekeza katika kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo kwa Madaktari Bingwa wengi iwezekanavyo na tumeendelea sasa hata kufanya mabadiliko ya mifumo ya kufundisha Madaktari ili tuweze kupata Madaktari Bingwa wengi kwa utaratibu wa fellowship ambao na sisi ndani ya Wizara tunakwenda nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa lengo la kutibu changamoto ambazo tunazo Serikali imekuwa inafanya kambi mbalimbali za kutoa Madaktari Bingwa kutoka sehemu moja kwenda kwenye sehemu mbalimbali na hii tumekuwa tunafanya kwa kushirikiana na Bima ya Afya na kwenda katika kambi katika mikoa mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za dharura ambazo zinahitaji upasuaji nazo zinaweza zikafanyiwa kazi wakati tunasubiria kujenga uwezo wa kuwa na Madaktari Bingwa wengi zaidi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Suala la kupandishwa madaraja linaambatana na ongezeko la mishahara. Serikali hii ya Awamu ya Tano imekuwa haipandishi watu madaraja kwa wakati, mtu anakaa mpaka miaka sita, saba, hajapandishwa madaraja. Nataka tu kujua Serikali iko tayari kuwalipa wale watu arrears zao kwa ile miaka ambayo hawakupandishwa madaraja kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri amesema wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii. Hivi kweli anafikiri unaweza kumkamua ng’ombe maziwa kama humpi chakula cha kutosha? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kipekee nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala yote ya watumishi wa umma nchini. Hata hivyo, naomba niseme kwamba, katika upandishwaji wa madaraja tuna madaraja ya aina tatu, kuna kupandishwa kwa madaraja kwa maana ya salary increase, kuna annual increment na kuna salary promotion, lakini katika suala la upandishwaji wa madaraja Serikali ilitoa tamko hapa wiki tatu zilizopita kwamba, kuanzia Mei Mosi mwaka huu (2019) Serikali inatarajia kupandisha madaraja, vyeo, watumishi zaidi ya 193,000. Hilo zoezi limeshaanza, lakini vilevile mwaka 2017/ 2018 Serikali ilishalipa annual increment zaidi ya bilioni 72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile naomba niseme kabisa kwamba, Walimu walishalipwa zaidi ya bilioni 37, lakini kada nyingine za utumishi wa umma walishalipwa zaidi ya bilioni 35, lakini malimbikizo ya mishahara zaidi ya bilioni 75 zimelipwa. Isitoshe tu, lakini zaidi ya wastaafu waliokuwa wanaidai Serikali wameshalipwa zaidi ya bilioni tisa na hawa wastaafu ni zaidi ya 1,800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ni kwamba, Serikali inawajali sana watumishi. Sio lazima iwe katika nyongeza tu ya mshahara, lakini vilevile tukumbuke kwamba, Serikali ndio guarantor, watumishi wanapotaka kujenga nyumba, watumishi wanapotaka kufanya mikopo, kuna bima za afya zote hizo ni sehemu ya motisha. Kwa hiyo, naomba niseme kabisa Serikali inawajali watumishi katika njia mbalimbali na hata katika kupanda madaraja hiyo imeshaanza kutekelezwa. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, sijui mchakato utakamilika lini, lakini kuna mambo mawili; kunakuwepo mashine na kunakuwepo msomaji. Katika Hospitali hii ya Mkoa wa Mtwara kuna tatizo pia la msomaji wa x-ray, mtu amevunjika mkono sehemu ya nyuma, inaonekana amevunjika mkono sehemu ya mbele. Sasa nataka kujua Serikali imejipanga vipi inapopeleka hiyo mashine tena ya digital na kumpata mtu ambaye ataendana na hiyo mashine katika usomaji wake?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, katika Hospitali ile ya Mkoa wa Mtwara kumekuwa na tatizo kubwa la madaktari hasa upande wa wanawake. Nataka kujua Serikali imejipanga vipi na ni lini itapeleka madaktari hao ili kutoa kero hii ambayo iko kwa muda mrefu? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri na ufuatiliaji ambao anaufanya katika sekta hii ya afya na hususan katika Mkoa huu wa Mtwara. Labda niseme ni hivi kwamba katika hili eneo ambalo ameligusia kuna mambo mawili kuna suala la mpiga picha ambaye ni radiographer, yeye kazi yake ni kupiga picha, lakini tuna radiologist ambaye yeye ni msomaji wa picha. Digital x-ray tutafunga na ni kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, mashine ziko bandarini tunafanya utaratibu wa ugomboaji na tutaenda kuifunga pale Ligula, radiographer tunao.

Mheshimiwa Spika, suala la msomaji tunakuja na utaratibu mpya kwa sababu hii ni digital x-ray sisi kama Serikali na sisi tunaingia katika mfumo unaitwa telemedicine na tutakuja na kitu kinaitwa tele-radiology, kwamba hizi digital x-ray zote ambazo tunazifunga kwa kutumia Mkongo wa Taifa pale Muhimbili na pale MOI sasa hivi tumetengeneza kitu kinaitwa hub. Tutakuwa na centre moja ambayo kutakuwa na screen ambayo imeunganishwa na mtandao, picha zitakazopigwa Tanzania kote iwe ni Mbinga, iwe ni Ligula, iwe katika eneo lolote Tanzania hii zitakuwa zinatumwa, wataalam/madaktari wetu bingwa pale Muhimbili wataisoma ndani ya dakika 15 na lile jibu linarudi tena kulekule ambako linatoka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikutoe mashaka sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba matumizi ya hizi digital x-rays zinaweza zikatumika na wananchi wa Tanzania wananufaika na utaratibu mpya ambao tumeanza nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la Madaktari Bingwa; ni kweli Hospitali ya Mkoa ya Ligula ina changamoto ya Madaktari Bingwa na sasa hivi sisi kama Serikali tunawekeza katika kuhakikisha kwamba hospitali za rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Ligula tunakuwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto, madaktari bingwa wa magonjwa ya mifupa, madaktari bingwa wa magonjwa ya dharura, pamoja na mengine mengi.

Kwa hiyo, sasa hivi wapo Madaktari wapo katika mfumo wa mafunzo na tumesomesha zaidi ya madaktari 100 kwa mwaka pale watakapokamilisha masomo yao tutawapangia katika hospitali zetu ya Iligula na hospitali zingine za RRH. Lengo na kusudio la Serikali wakati tunaboresha vituo vya afya, hospitali za wilaya, tunataka sasa hospitali za rufaa za mikoa zitoe huduma za kibingwa kama ilivyokusudiwa.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa bahati nzuri nimewahi kwenda mara kadhaa kwenye Mabaraza ya Kata. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Mwanasheria wa Halmashauri anasimamia Mabaraza hayo, lakini kiukweli kabisa hakuna usimamizi wa kisheria unaopatikana pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu: Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu mahsusi ili kusudi Mwanasheria apatikane wa kueleza na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki kwa sababu unakuta Baraza la Kata linahukumu kesi ya shilingi milioni 10 wakati wao mwisho wao ni shilingi milioni tatu. Ni kwa sababu ya kukosa Mwanasheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, Serikali imejipangaje kuhusu hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Siyo kweli kwamba Wanasheria hawasimamii haya Mabaraza ya Kata. Kama nilivyosema, kwenye majibu yangu yaliyotangulia hapa, kama kuna malalamiko kwenye eneo specific, Mheshimiwa Mbunge ni vizuri akataja ili tuweze kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mfano. Kule Kivule tulikuwa na shida kwenye Baraza la Kata, tulimwita Mwanasheria wa Halmashauri ile ya Manispaa ya Ilala akaja akasikiliza malalamiko yaliyokuwepo, gharama kubwa ya uendeshaji wa kesi, uonevu na kuvuka kiwango ambacho kimewekwa kwa mujibu wa sheria, tulivunja Baraza tukaweka viongozi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna malalamiko katika eneo mahsusi tupewe taarifa. Vilevile tujue kwamba Wanasheria wako kwa mujibu wa Sheria hii ili haya Mabaraza ya Kata na yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1985 na imeendelea kufanyiwa marekebisho kadri muda unavyoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama kuna malalamiko, lazima tuchukue hatua. Hata hivyo, Mwanasheria wa Halmashauri ana uwezo, kwa sababu hazungumzi mtu mmoja, Idara ya Sheria kwenye Halmashauri ina wajibu huo. Ila kama kuna Mwanasheria kwenye Halmashauri yoyote hapa Tanzania, ameshindwa kufanya wajibu wake na haendi kila siku, Mbunge umepeleka malalamiko, wananchi wamelalamika, wamehukumu kesi kinyume na utaratibu, tupe taarifa tuweze kuchukua hatua kwa Mwanasheria huyo wakati wowote kuanzia sasa. Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwanza namshukuru Naibu Waziri, TAMISEMI kwa kujibu vizuri. Pia pamoja na hiyo aliyosema Naibu Waziri, changamoto hii kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia tumeiona kwa sababu watu wale mashauri yao mengi yanahusiana na ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Wizara yetu kwa kusaidiana na Msajili wa Mabaraza, akishirikiana na Wanasheria katika Halmashauri, tumeweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa zile Kamati zote za Mabaraza ya Ardhi ya Kata pamoja na Vijiji ili kuweza kuwapa elimu na ukomo wa namna wao wanavyotakiwa kusimamia. Kwa sababu wanapokwama, mashauri mengi yanaenda kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeona kwamba tujenge msingi kule chini ili watu waweze kufanya kazi zao vizuri kwa weledi ili kupunguza malalamiko ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayasema.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana katika Manispaa ya Mtwara Mikindani yaani Jimbo la Mtwara Mjini kumekuwa na tatizo kubwa la maji kutoka yenye tope jingi kwa muda mrefu na maji hayo yanapita katika mita za wananchi kuwasababishia kulipa bili wakati maji wanayoyapata ni machafu. Pamoja na mambo mengine chanzo kikubwa ni kukosekana kwa chujio katika chanzo cha maji cha Mtawanya.

Swali langu, ni lini Serikali itanunua chujio kubwa la uhakika kwa ajili ya kuchuja maji katika chanzo cha Mtawanya ili kusudi wananchi wanaoishi Mtwara Mikindani wapate maji safi na salama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji niseme kwa ufupi sana ni wajibu na ni haki ya mwananchi kupatiwa maji, si maji tu kwa maana yamaji safi na salama na yenye ubora. Nimefika Mtwara lakini moja ya changamoto kubwa pale ni chujio na nitumie nafasi hii kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yetu ya Maji kuhakikisha mchakato ule unakamika haraka kwa ajili ya ujenzi wa chujio na wananchi wa Mtwara waweze kupata maji safi salama na yenye ubora. Ahsante sana.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuruku, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri uko tayari kunipatia mchanganuo wa hao wafanyakazi 7,000 wanaohitajika wanatosheleza kwa kiwango gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali langu la pili, kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndiyo mamlaka iliyopewa wajibu mkubwa wa kukusanya kodi; na kwa kuwa ukirejea hotuba mbalimbali za Wizara ya Fedha utaona kuna upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi; na kwa kuwa huko mtaani kuna vijana wengi ambao wamehitimu kwenye masuala mbalimbali ya kodi lakini hawajaajiriwa. Sasa nataka kujua, ni lini Serikali itaajiri Vijana wale ili wapate ajira na Mamlaka ifanye kazi kwa ufanisi kwa maendeleo ya taifa hili? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Issa Malapo Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, anasema nimpatie mchanganuo wa hao watumishi 7,000. Mheshimiwa Tunza nimesema wanaohitajika ni 7,000 ambao tulionao Watumishi walioajiriwa ni 4,751 hawa hata leo hii nikimaliza kujibu maswali haya niko tayari kukupatia hawa 4,751. Kwa hao 7,000 pia niko tayari kukuandalia mchanganuo huo kwa kada zote ambazo zinahitajika na kukupatia ikiwezekana siku ya jumatatu tuwasiliane na nikupatie mchanganuo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, naomba kwanza niseme, si kwamba Mamlaka ya Mapato ina upungufu mkubwa wa watumishi kama alivyosema, upungufu uliopo ni wa asilimia 28 tu siyo upungufu mkubwa. Kwa hiyo kama nilivyosema tunahitaji 7,000 tulionao ni 4,751 na Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kwa kiwango kikubwa; tangu imeingia madarakani tayari tumeshaajiri Watumishi 692 na kwa mwaka huu tayari kwenye Bajeti yetu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania tutaajiri watumishi 150. Kwa hiyo tunakwenda hatua kwa hatua mpaka mwisho tutakamilisha wote Watumishi 7,000 wanaohitajika ili kuhakikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania inafanya kazi zake kwa ufanisi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Jiji la Mwanza unahusisha makazi ya watu katika Kata za Shibula na Kahama, na kwa kuwa Mwezi Januari mwaka huu timu ya Mawaziri wanane ilifika katika kata hizo na kuwaahidi kwamba watalipwa fidia zao. Sasa nataka kujua; Serikali inawaambia nini wananchi wa kata hizo kuhusu fidia hizo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kumekuwa na kusuasua katika ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Mtwara, na taarifa zilizopo ni kwamba kwa sababu hakuna fedha za uhakika. Swali langu; je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili uwanja ule uweze kukarabatiwa kwa kiwango kinachokubalika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye eneo hili la Uwanja wa Ndege wa Mwanza wapo wananchi ambao wanadai fidia. Na ni kweli kuna timu ya Mawaziri ambao wanahusika na ulipaji wa fidia hii walikuwa na jukumu la kushughulikia ili wananchi waweze kulipwa mapema. Ninawaambia nini wananchi wa maeneo haya; ninawaambia ule utaratibu unakamilishwa na ni mapema kadri itakavyowezekana watalipwa hizi fidia, kwa hiyo wasubiri tu mambo yanaendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Spika, na niseme na pia Mheshimiwa Mbunge Mabula yuko hapa, anafahamu kwa sababu karibu kila siku anafuatilia juu ya ulipaji wa fidia ya wananchi ambao wengi wako pia kwenye eneo lake. Kwa hiyo wananchi hawa wasiwe na wasiwasi, tunalifuatilia na kulishughulikia suala hili ili waweze kulipwa mapema iwezekanavyo. Lakini pia wakilipwa kuna kazi ambayo nimeitaja itafanyika ili iweze kufanyika, na utaratibu ulivyo ni wananchi walipwe kwanza fidia ili maboresho kadhaa yaweze kuendelea katika uwanja huu.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu Uwanja wa Ndege wa Mtwara, labda nimkumbushie tu Mheshimiwa Mbunge, atakuwa amesahau, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Rais alivyofanya ziara Mtwara alitoa maelekezo na sisi kama Wizara maelekezo yale kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, kuna fedha zilitolewa na kazi inaendelea vizuri katika ujenzi huu wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, na nikwambie Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu tumejipanga kuhakikisha kila wakati tunaboresha uwanja huu na mwaka wa fedha huu unaokuja Bunge hili, Bunge lako limetupitishia fedha ambazo ni takribani bilioni 4.5, mmetuidhinishia ili sasa hii kazi isilale, kwamba kwa maana ya fedha zilizokuepo katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao tuna fedha za kutosha, hatutasinzia kwenye ujenzi wa uwanja, maboresho yatafanyika tuweze kukamilisha na wananchi waweze kupata huduma ya Uwanja wa Ndege huu wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri swali hili umepewa siku nyingi na hili swali limeuliza ni lini na ni wapi, umejibu kwa ujumla naomba nifahamu hivyo viwanda vitano vya kuchakata samaki katika ukanda wa Pwani viko maeneo gani, kama na sisi watu wa Mtwara vinatuhusu vipo huko kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari umesema utakapokamilika, nataka uwe specific unakamilika lini ili hiyo bandari ipatikane kwa maendeleo ya wavuvi na nchi yetu kwa ujumla, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni wapi viwanda hivyo vipo; viwanda hivyo katika Mkoa wa Dar es salaam, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Tanga. Mkoa wa Dar es salaam tunacho kiwanda cha Alfa Cluster, Bahari Food, Pugu Road lakini vilevile Mkoa wa Pwani tunacho Kiwanda cha Abajuko kilichopo pale Vikindu Madafu, Mkuranga na vilevile tunacho kiwanda cha Alfa Cluster, Tanga Jiji ambacho kinafanya kazi ya kuchakata samaki aina ya pweza.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni lini hasa tutamaliza hii kazi ya upembuzi yakinifu ya ujenzi wa bandari ya uvuvi, tutamaliza. Mkandarasi amepewa muda wa mwaka mmoja kwa hivyo bado yupo ndani ya muda wa kukamilisha kazi yake na hatimaye atuletee ile ripoti ambayo itakuwa na ushauri wa mahala kuzuri zaidi tutakapoweza kuweka bandari yetu lakini na gharama zake za ujenzi wa ile bandari yenyewe. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mikopo hii inahusu watu wenye ulemavu; na swali langu ni kwamba, inapotokea mtu mwenye ulemavu ambaye hawezi kufanya shughuli yoyote, lakini ana mlezi ambaye anamlea. Je, Serikali sasa haioni kuna sababu ya kumkopesha yule mtu ambaye anamlea mtu mwenye ulemavu ili aweze kufanya shughuli itakayomwezesha yule mtu kuweza kumlea vizuri yule mtu mwenye ulemavu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mikubwa mpaka tulipofikia hapa. Tukumbuke kihistoria kwamba Mfuko huu ulikuwa haufanyi vizuri, lakini kwa taarifa tuliyoitoa mwaka 2020, zaidi ya shilingi bilioni 124 ziliweza kuelekezwa katika makundi haya. Mpaka leo taarifa yetu ya miezi sita mpaka mwezi Desemba, zaidi ya shilingi bilioni 22.45 zimeelekezwa katika makundi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nazishukuru Kamati za Bunge hasa Kamati ya TAMISEMIna Kamati ya LAAC katika kutoa ushauri wa uboreshaji wa Kanuni na hasa makundi ya watu wenye ulemavu. Hivi sasa tume-review kanuni zetu za kuhakikisha, hata kama mlemavu ni mmoja, aweze kupata mkopo ambapo hayo yalikuwa ni maelekezo ya Bunge. Hata hivyo, tumeenda katika suala zima la uboreshaji katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nia yetu ni kwamba Mfuko huu uende kufanya vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dada Malapo, hilo ni jambo ambalo Serikali hivi sasa inalifanyia kazi, lengo likiwa, walemavu waweze kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba viwanda hivyo viwili anavyovisema, kimoja kinabangua tani 2,000 badala ya tani 5,000 na kingine hakibangui kabisa, kinafanya kufunga. Swali la kwanza; je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha viwanda hivi vinabangua kwa ule uwezo wake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna kiwanda kikubwa cha kubangua korosho kinachomilikiwa na Kampuni ya OLAM. Kiwanda hicho kimefungwa. Kiwanda kile kilikuwa kinaajiri wafanyakazi wasiopungua 6,000 wakiwemo wanawake karibu 5,000. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanakaa na mwekezaji yule, kiwanda kile kiweze kufanya kazi ili wanawake wa Jimbo la Mtwara Mjini waweze kupata ajira wajikwamue kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa kwamba, kama nilivyosema katika jibu la msingi, kuna changamoto ya malighali kwa maana ya korosho ambazo zinahitajika katika viwanda vyetu mbalimbali vya kubangua korosho hapa nchini. Hivyo, kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Korosho, tumeandaa mwongozo ambao kwanza tunawapa kipaumbele wabanguaji wa korosho hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuanzia msimu wa 2021 mwongozo huo unataka malighafi zinazopatikana katika mnada wa awali kupitia soko la awali la korosho, viwanda vyote vya ndani ambavyo vinabangua korosho, kwanza vipate korosho, vikishajitosheleza ndiyo sasa tunafungua ule mnada wa pili ambao sasa utahusisha wafanyabiashara wote ambao wako katika soko la korosho. Hii itapelekea kuhakikisha kwamba viwanda vyote vinavyobangua korosho vinapata malighafi kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu Kiwanda cha OLAM, ni kweli kiwanda hiki ambacho kilikuwa ni sehemu ya uwekezaji katika Manispaa ya Mikindani, changamoto kubwa iliyosababisha kufungwa kiwanda kile ilikuwa ni kutokana na kukosa malighafi ambazo zilitokana na ushindani wa wanunuzi wa korosho katika minada ambayo inafanyika kwenye maeneo hayo. Ndiyo maana tunapeleka mwongozo huu ambao sasa utahakikisha kwamba viwanda vya kubangua korosho vinapata malighafi kwanza, halafu sasa zile zinazobaki ndiyo zitaingizwa kwenye mnada ambao utajumuisha wafanyabiashara wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali tayari imeshaanza mawasiliano na Kampuni ya OLAM ambao waling’oa mitambo ile na kuipeleka nchi jirani Msumbiji ambako wao walikuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha viwanda vinapata malighafi. Kwa hiyo, sasa tunataka warudi nyumbani kwa sababu nasi tayari tumeshaweka mwongozo huo ambao unawahakikishia malighafi viwanda vyote ambavyo vinabangua korosho hapa nchini. (Makofi)