Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sabreena Hamza Sungura (7 total)

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekuwa na tabia tata ya kuchukua fedha kwenye Mashirika ya Umma kama NSSF, LAPF na Mashirika mengine na kutokuzirudisha kwa wakati, ama kuwekeza katika miradi mfu kama mradi wa Machinga Complex na miradi mingine ambayo imekuwa haina tija Serikalini.
Ni lini Serikali itakoma mchezo huu wa kuchukua fedha ambazo zinawaathiri wachangiaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikichukua fedha na hii ikifuata taratibu zote na Mifuko hii kuingia katika Mikataba ili Mifuko hii iweze kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itasitisha utaratibu huu, siamini sana kwamba ni sahihi sana Serikali kusitisha, kama Mifuko inaweza kuwekeza na wakaingia katika mikataba ambayo tunaita ni Win Win Situation kati ya Serikali na Mifuko naamini ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa mifuko yetu hii. Kwa hiyo, naomba tuendele kufanya hivyo.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, kwanza kwa masikitiko makubwa nasikitishwa sana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, hii Serikali inajiita ni Serikali ya hapa kazi tu na kila siku imekuwa ikija na majibu mepesi kwa maswali mazito. Wamiliki wa mabasi ambao ni wananchi wa kawaida wenye uwezo wa kawaida wana uwezo wa kuwa na mawakala katika Wilaya mbalimbali nchini, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inashindwaje kuwa na mawakala ili kusaidia wananchi waweze kuzipata tiketi hizi kwa urahisi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtu anatoka Kasulu, mtu anatoka Kibondo, mtu anatoka Ilagala anatumia sh. 10,000, sh. 8,000, sh. 7,000, anakwenda na kurudi, anakaa saa kumi usiku mpaka nne asubuhi, tiketi zinaanza kuuzwa na anakosa tiketi anarudi kijijini. Hizo gharama kwa mwananchi anaziona ni ndogo kuliko Serikali kuweka mawakala katika maeneo husika?
SPIKA: Sasa swali!
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, swali ni kwamba anaona gharama ya Serikali kuweka mawakala katika Wilaya husika ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa usafiri ni kubwa kuliko gharama wanazozipata wananchi kuamka saa kumi ya usiku na kukosa tiketi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, …
SPIKA: Hee! Bado!
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, bado, hilo ni swali la kwanza. Swali la pili, amekiri kwamba kuna ulanguzi wa tiketi. Tiketi ya daraja la tatu ambayo inauzwa sh. 24,000 katika soko la ulanguzi inauzwa sh. 35,000 mpaka sh. 40,000. Daraja la pili kwa bei ya sh. 56,000 inauzwa sh. 75,000 mpaka sh. 85,000 na daraja la kwanza kwa bei ya sh. 76,000 inauzwa sh. 100,000 mpaka sh. 110,000. Je, Serikali, ni lini sasa mtaondoa kero hii na kutoa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ulanguzi wa tiketi ulikuwa kwa kiwango kikubwa sana kabla ya utaratibu huu ambao Serikali tumesema tumeubadilisha haujafanyika, baada ya utaratibu huu kufanyika tatizo hili la ulanguzi wa tiketi sasa halipo kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama ambazo wananchi wanazipata tutaangalia uwezekano mwingine, badala ya kuanzisha wakala, tutaanzisha huduma ya wateja katika stesheni ile ile, upate uhakika wa tiketi kabla hujakwenda stesheni kulipa fedha na tunakokwenda TRL itaanzisha huduma ya kutoa tiketi ukiwa nyumbani huko kwa kutumia simu. Hatutaleta mawakala kwa
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
22
sababu kuleta mawakala kunaongeza gharama zaidi kwa TRL na vilevile ni gharama kwa uchumi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu suala la…
SPIKA: Umesikia Mheshimiwa Sabreena, Serikali hii ya hapa kazi tu inaleta digital! Mheshimiwa Waziri endelea! (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, namhakikishia kwamba tukishaanzisha utaratibu huo, hilo tatizo la pili ambalo analiongelea halitakuwepo tena.
MHE. SABREENA H.SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna mambo ya msingi ambayo yanapelekea ajali za barabarani kuendelea kutokea ambayo hayajakuwa mentioned katika majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hususani njia inayoelekea Kigoma, kuanzia Itigi kwenda Tabora mpaka Kigoma, tumekuwa na railway cross nyingi sana katika eneo hilo, lakini nyingi katika hizo hazijawekewa alama kiasi kwamba msafiri anapokuwa anaendesha ama madereva wanapokuwa wanaendesha wanashindwa kutambua. Ni kwa mita chache sana alama hizo zipo na maeneo mengine alama hizo hakuna kabisa, kitu ambacho kinaweza kikapelekea sasa magari yetu na treni zije zisababishe ajali kubwa hapo baadaye. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wana-fix vibao vinavyoonesha railway cross barabarani katika njia hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa kumekuwa na shida kubwa sana hasa ya wafugaji, hususani wafugaji wa ng’ombe, hufuga maeneo ambayo ni pembezoni mwa barabara na wakati mwingine ng’ombe wale hupelekea ajili zisizokuwa za msingi na kwa kuwa kumekuwa na tendence ya traffic hasa katibu miji mikubwa kama Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na kadhalika, hususani Dar es Salaam ambapo taa za barabarani zinafanya kazi, hapo hapo na traffic wanafanya kazi, kitu ambacho kinapelekea ku-confuse madereva barabarani na kuweza kusababisha ajali.
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa tukikabiliana na changamoto za kukosekana katika baadhi ya maeneo alama za barabarani zinazotakiwa kuelekeza madereva kuona maeneo ambayo ni hatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilieleza kati ya mikakati 14 moja katika eneo tulilokuwa tulifanyia kazi ni eneo hilo na kwamba tumejaribu kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuwasiliana na kufanya kazi kwa karibu na mamlaka husika ili kuweza kudhibiti na kuweka hizo alama ambazo anasema kuwa zimekosekama. Bahati nzuri Makamu Mwenyekiti wa Baraza letu la Usalama Barabani ni Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, kwa hiyo tumelifanya hili kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa ambalo linasababisha alama hizi kupotea. Mara nyingi ni kutokana na tabia mbaya za baadhi ya wananchi ambao wamekuwa waking’oa kwa makusudi alama za barabarani na kuvitumia vyuma hivi kama vyumba chakavu. Naomba nitoe wito kwa wananchi kuacha tabia hiyo na kwamba mamlaka husika ziko macho kwa wale wote ambao watakiuka sheria za nchi, kwa kung’oa vibao vya alama hizi tutawachukulia hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili lilikuwa linahusiana na askari wa barabarani pamoja na taa za barabarani. Mara nyingi askari wa barabarani wanakaa wakati ambao kuna msongamano wa magari barabarani, hasa wakati wa asubuhi wakati watu wanakwenda kazini na wakati wa jioni wanapokuwa watoka kazini. Hii ni kwa sababu taa za barabarani zilipowekwa haziwezi kukidhi mahitaji ya nyakati husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kuna wakati ambao kuna msafara mwingi unatokea katika upande mmoja, kwa hiyo kutegemea taa za barabarani peke yake kunaweza kusababisha msongamano mkubwa. Kwa maana hiyo hao traffic police wanakaa pale kwa lengo la kudhibiti na kuzuia msongamano huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuhakikisha kwamba askari hao wanaendelea kutumika kusaidia kupunguza msongamano wa magari hasa katika nyakati hizo za watu ambao wanakwenda kazini na kurudi kazini asubuhi na jioni.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la vyumba vya uendeshaji wa shughuli za Mahakama hususan katika Mkoa wetu wa Dodoma na ukizingatia mkoa huu umeshakuwa Makao Makuu ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua Serikali ina mkakati gani sasa wa kupanua Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa maana ya District Court ili sasa ule mlundikano wa Mahakimu watatu kukaa kwenye chumba kimoja na kusikiliza mashauri na kesi nyingi kuchelewa, hususan kwa kesi za watoto wanaobakwa na kulawitiwa na hivyo kuathiri masomo yao uweze kwisha? Ni lini sasa Serikali itafanya upanuzi wa Mahakama hii ili kero hii iweze kuondoka kwa wananchi? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA - K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema mara zote, ni kwamba katika utaratibu tulionao sasa hivi katika utendaji kazi wa kimahakama, tunafanya kazi ya ukarabati wa majengo yetu mengi na upanuzi wa baadhi ya Mahakama. Kwa sababu sasa hivi tumeingia ubia pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi ambapo tunakwenda kujenga katika mfumo mzuri wa Moladi ambao unapunguza gharama, Waheshimiwa Wabunge waendelee kuvuta subira tu, pindi bajeti itakaporuhusu tutaendelea kufanya ukarabati na kupanua Mahakama ili kupeleka huduma za kimahakama zaidi kwa wananchi.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Mahakimu wengi wamekuwa wanaenda shuleni kwa kujiendeleza kwa maana ya shule ya sheria kwa vitendo (Law School of Tanzania), lakini wengi wao wameachwa wakifanya kazi kwenye Mahakama za Mwanzo, Mahakama ambazo haziendani na taaluma zao, huku katika Mahakama zetu za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi kuna upungufu wa Mahakimu. Nataka kujua ni lini Serikali sasa ita-upgrade wanafunzi hawa ambao wamepitia elimu ya sheria kwa vitendo ili waweze kufanya kazi kulingana na taaluma yao. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapongeza sana Mahakimu wote ambao wamechukua hatua ya kujiendeleza kielimu na pia kwenda katika Shule ya Sheria kwa Vitendo au Taasisi ya Sheria kwa Vitendo. Kwa kuzingatia hilo kila mwaka Mahakama imekuwa na mpango wa kupitia wale waliopata sifa ili waweze kupandishwa madaraja kulingana na elimu walioyoipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema ni sahihi kabisa kwamba lengo la Serikali sasa ni kuhakikisha pia kwamba Mahakimu wote wa Mahakama za mwanzo ambapo ndiko kwenye mashauri mengi wawe ni wale ambao wana Shahada za Chuo Kikuu na kwa maana hiyo baada ya miaka michache ijayo Mahakama zote za Mwanzo zitakuwa na Mahakimu ambao wana Shahada ya Kwanza ya Sheria ukizingatia kuwa huko ndiko kwenye mashauri mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo kuendelea ku-upgrade hao ambao wamejiendeleza na tunawapongeza na tunawatia moyo waendelee kufanya hivyo. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatambua kwamba zao hili la mchikichi nchi yetu iliipatia nchi ya Malaysia miaka ya 70 na limekuwa likifanya vizuri sana kwenye nchi hiyo na kukuza uchumi. Kwa kuwa zao hili linazalisha bidhaa zaidi ya 10, naweza nikataja tu chache kwa kifupi sana, linatumika kuzalisha mafuta ya mawese lakini pia mafuta ya mise kutokana na mbegu iliyoko ndani. Pia zao hili majani yake yanasaidia kuezekwa katika mapaa yetu ya nyumba, lakini pia linasaidia katika utengenezaji …
Wa sabuni za magadi ambazo hata Wabunge wako katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakizitumia na mazao mengine kutokana na muda naomba nisiyataje. Kwa nini sasa Serikali haioni ni wakati muafaka wa kutengeneza Bodi maalumu ambayo itashughulika na mchikichi na kutotegemea Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa sababu Bodi hiyo inaendeshwa kwa kusuasua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, haiwezekani zao la mchikichi kwa kiwango kikubwa lilimwe katika Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani, lakini Kituo cha Utafiti kikawekwa Mikocheni Dar es Salaam na Tabora. Kwa nini sasa wasifungue ofisi ya utafiti katika Mkoa wa Kigoma ili wakulima wetu wa michikichi waweze kwenda kufanya consultation na kupata ushauri mbalimbali katika mkoa wao? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu ndugu yangu Mheshimiwa Sabreena Sungura maswali yake mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge anayetoka Kigoma kwa kufuatilia zao zima hili la mchikichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake, swali la kwanza, kila zao linataka liwe na Bodi yake, kwa maana hiyo gharama zake zinakuwa kubwa sana. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Bodi yetu ya Mazao ya Nafaka Mchanganyiko si kwamba inasuasua, tunawashukuru sana Wabunge juzi wamepitisha bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo na sasa hivi tumejipanga kuhakikisha kwamba Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko inafanya kazi kwa kuboresha zaidi ili hili zao letu la mchikichi ambalo linasimamiwa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko liweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali lake la pili kwamba kwa nini Mkoa ule wa Kigoma usiweze kuwa na Kituo cha Utafiti. Ni kwamba hivi vituo vyetu vya utafiti hususan katika zao la michikichi vimewekwa kikanda. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba katika Mkoa wa Tabora, pale Tumbi tafiti zetu zinafanyika mahali pale. Kwa maana hiyo, hata kile Kituo cha Mikocheni kinafanya tissue culture. Naomba niseme kwamba Mkoa wa Tabora uko katika Kanda ya Magharibi ambapo Mkoa wa Kigoma upo chini yake. Ahsante.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Moja, kwa kuwa wananchi wengi sana wa Tanzania ambao wamekuwa wakipelekwa mahabusu, whether wana kesi za kujibu ama hawana, ama ni kesi zinazopata udhamini, wamekuwa wakiingia mahabusu bure, lakini kutoka ni hela; napenda kuuliza: Je, Serikali imewahi kufanya utafiti kwamba suala hili linatokea na ni hatua gani wanachukua? Kwa sababu siyo suala la kisheria kwamba mtu akiingia mahabusu kutoka lazima atoe hela ndiyo atolewe. Ni suala la practice, sisi tuliopo mitaani tunajua kwamba mtu anapelekwa mahabusu lakini siku ya kutoka wengi wao wanakuwa wanachajiwa. Je, Serikali inachukua hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kumekuwa kuna wimbi kubwa la kesi, hususan za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa vijana hasa vijana hawa kama akina Tito, Kabendera na wengine wengi ambao hatuwajui, wamekuwa wakikaa mahabusu kwa muda mrefu na kesi zao zikiendelea huko; inawezekana siku ya siku wakaja kukutwa na hatia ama wasikutwe na hatia; lakini kwa kuwa tulipitisha sheria hapa Bungeni ya pre-bargaining ambayo inamtaka mshtakiwa ama wakili wake ama mwendesha mashtaka kuomba mahakamani waweze kupata ili kupunguza ukubwa wa adhabu, kupunguza muda wa adhabu lakini kuondoa baadhi ya kesi; pia Mheshimiwa Rais kupitia maombi maalum ya barua alikuwa akiwahi kutoa msamaha; sasa Bunge halioni ni wakati muafaka sasa tuje tufanye mabadiliko ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ili kuweka flexibility kwa Majaji na Mahakimu ambao wamekuwa wakiendesha kesi hizi na wenyewe waweze kuangalia ukubwa wa kosa na kuweza kutoa dhamana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu Bunge tumetunga sheria, tumewafunga mikono kwamba hawawezi kutoa dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi. Hata hivyo, mtu anaweza akahujumu uchumi ama kufanya utakatishaji fedha kwa 20,000/=, mwingine shilingi bilioni moja, wote wananyimwa dhamana kitu ambacho kinasababisha mlundikano wa kesi.

Je, Bunge sasa halioni ni wakati muafaka wa kuleta mabadiliko ya sheria hii ili vijana ambao hawana hatia na wanateseka huko Magerezani waweze kupunguza idadi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anazungumzia kwamba kuna kauli ambayo inatapakaa katika jamii kwamba unaingia mahabusu bure na unatoka kwa pesa. Siwezi nikapingana na kauli hii kwa sababu mbali ya kazi kubwa na nzuri ambayo Askari wetu wamekuwa wakiifanya ya kusimamia usalama wa nchi hii na ndiyo maana nchi yetu iko salama, lakini tunakiri kwamba wako baadhi ya Askari ambao wamekuwa wakikiuka maadili na ndio hao ambao pengine wanatuhumiwa na mambo kama ambayo amezungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tunabaini Askari yeyote anayekiuka maadili yake kwa kufanya utaratibu kama ambao ameueleza wa kuwatoza mahabusu fedha ama kuwabambikia ama kuwaonea, tumekuwa tukichukua hatua. Wapo Askari kadhaa ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali kila mwaka ingawa ni wachache mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mabadiliko ya sheria, nadhani ni mamlaka ya Bunge hili kutunga sheria na kubadilisha pale ambapo inaona inafaa. Naye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni anazifahamu. Kama kuna utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge anadhani kuna haja ya kuleta hoja binafsi ama utaratibu mwingine ambao ataona unafaa, basi ni juu ya Mbunge yeyote kutumia haki yake ya Kikatiba na kikanuni.