Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Sabreena Hamza Sungura (9 total)

MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
Shirika la Reli Kigoma linawahudumia wakazi wa Kigoma, Burundi, Congo, Zambia na kadhalika na inawalazimu wakazi hao kulala stesheni au waamke alfajiri ili kuwahi tiketi na wakati mwingine hukosa tiketi hizo:-
Je, ni kwa nini Shirika la Reli Tanzania (TRL) wasianzishe mfumo wa uwakala wa tiketi ili kupunguza adha hiyo wanayopata wakazi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa treni katika Mkoa wa Kigoma, uuzaji wa tiketi katika Stesheni ya Reli ya Kigoma umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ubaguzi na ulanguzi wa tiketi. Ili kudhibiti ulanguzi huo, Kampuni ya Reli Tanzania iliamua kubadilisha utaratibu wa kuuza tiketi siku za safari na kwa kutumia vitambulisho, jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ulanguzi wa tiketi. Hata hivyo, utaratibu huo umekuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafiri kulala Stesheni au kuwalazimu kuamka alfajiri ili kuwahi tiketi hizo.
Mheshimiwa Spika, ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo siyo kuanzisha mfumo wa wakala ambao utaiongezea Tanzania Railway Limited gharama za uendeshaji. Tatizo kubwa lililopo ni idadi ndogo ya safari za treni ambapo huduma inayotolewa hivi sasa haikidhi mahitaji halisi ya wananchi na hivyo kuwa na uhaba wa tiketi kwa abiria. Hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatarajia kuongeza idadi ya treni za abiria kwa njia ya Kigoma ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa mkoa huo.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la mgawanyo wa fedha za TASAF ambapo wananchi wengi wasio na uwezo, wamekuwa hawapati fedha hizo.
Je, Serikali imejipangaje kutatua kero hii kwa wananchi ambao hawapati fedha hizo hususan katika Mkoa wa Kigoma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utambuzi wa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, ulianza mwezi Novemba, 2013 na hadi sasa umeshaandikisha kaya 1,100,000 katika Halmashauri 159 za Tanzania Bara, pamoja na Wilaya zote za Unguja na Pemba. Kaya hizi zinapata ruzuku kwa utaratibu wa uhaulishaji fedha baada ya kutimiza masharti ya kupeleka watoto shule na kliniki na pia kushiriki katika kazi za kutoa ajira ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaanza ulipanga kufikia asilimia 70 ya Miji, Mitaa na Shehia za Halmashauri ambavyo ndivyo vilivyofikiwa kutokana na mchakato wa kuvipanga, kutokana na viwango vya umaskini katika kila Halmashauri. Baada ya jamii kutambua kaya maskini na kuzipitisha kwenye mikutano ya hadhara iliyosimamiwa na viongozi wa Vijiji, Mitaa na Shehia. Kaya zilizotambuliwa zilijaziwa dodoso ili kukusanya taarifa zaidi za kaya na hatimaye Kaya hizo ziliandikishwa kwenye daftari la walengwa na kuanza kupokea ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa TASAF kwa kushirikiana na Halmashauri ilifanya kila jitihada kuhakikisha kwamba kaya zinatambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango ni kaya maskini sana kwenye baadhi ya maeneo Kigoma ikiwa ni mojawapo, baadhi ya jamii na viongozi walifanya udanganyifu na kuingiza majina ya kaya ambazo siyo maskini sana na kuziacha kaya zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuona changamoto hizo, TASAF imefanya mapitio ya orodha ya kaya zilizoandikishwa na kufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba na kuziondoa kwenye mpango wa kaya zote ambazo siyo maskini. Zoezi hili ni endelevu na ni la kudumu. Kaya zote ambazo siyo maskini na ziliingizwa kwa makosa au kwa makusudi katika orodha ya kaya maskini zitaondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia tarehe 30 Mei, 2016 maeneo yote 161 ya utekelezaji ambayo ni Halmashauri 159 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, zimeshaondoa Kaya ambazo hazistahili kuwemo kwenye orodha ya walengwa. Jumla ya kaya 25,446 zimeshaondolewa kwenye mpango kwa sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kukosa vigezo vya kaya maskini na kuondolewa kwa Wajumbe wa Kamati za Mpango na viongozi wa Vijiji na Mtaa na Shehia katika orodha ya kaya maskini.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza ajali za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mkakati wa kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa ambayo hupelekea ajali za barabarani kuongezeka. Mambo yaliyolengwa katika mkakati pamoja na mambo mengine ni:-
(1) Udhibiti wa madereva walevi na kuendesha kwa uzembe;
(2) Udhibiti wa mwendokasi kwa madereva na wamiliki wa magari , kuwa na madereva wenza kwa mabasi ya safari za zaidi ya masaa manane;
(3) Kuthibiti uendeshaji magari bila sifa/leseni za udereva ama Bima;
(4) Kudhibiti usafirishaji wa abiria kutumia magari madogo yenye muundo wa tairi moja nyuma;
(5) Kusimamia matumizi ya barabara kwa Makundi Maalum mfano watoto, wazee, walemavu na wasiotumia vyombo vya moto ikiwemo mikokoteni na baiskeli;
(6) Kudhibiti ajali za pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na magurudumu dumumatatu (bajaji);
(7) Kuzishauri mamlaka husika kuweka alama za kudumu za utambulisho kwenye maeneo hatarishi ya ajali;
(8) Kusimamia utaratibu wa nukta (Point System) kwenye leseni za udereva;
(9) Marekebisho ya Sheria za Usalama Barabarani;
(10) Abiria kufunga mikanda ya usalama wanapotumia vyombo vya usafiri;
(11) Kubaini maeneo tete na hatarishi ya ajali za barabarani;
(12) Kuthibiti utoaji na upokeaji rushwa barabarani;
(13) Motisha kwa askari wanaosimamia vizuri majukumu yao; na
(14) Kuwajengea uwezo wa kiutendaji askari wa usalama barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nidhahiri kwamba suala la usalama barabarani siyo la kundi au taasisi moja tu ila ni letu sote. Wabunge ni miongoni mwa wahusika wa suala la usalama barabarani, kwa maana kuwa nafasi yao kubwa ni katika kuelimisha umma na kusaidia katika ujenzi wa utamaduni wa kuheshimu alama za usalama barabarani nchini.
MARWA R. CHAHA (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Akiwa katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya lami (Kasulu Road) ili kufungua Mji wa Ujiji:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aliahidi ujenzi wa kilomita10 za barabara kwa kiwango cha lami ndani ya Manispaa ya Kigoma Ujiji. Kutokana na ahadi hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeamua kujenga barabara ya Ujiji
– Bulenga - Bangwe yenye urefu wa kilomita 7.5 ambapo usanifu umekamilika na itagharimu shilingi bilioni 11.6 ambapo ujenzi unaweza kuanza mwaka wa fedha 2018/2019 na barabara ya Ujiji hadi Daraja la Mngonya yenye urefu wa kilomita 2.5, hivyo kufanya jumla ya kilomita10 ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili uunganishe na ile barabara ya kutoka Kasulu lazima upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo ufanyike kuunganisha kutoka Daraja la Mungonya hadi barabara Kigoma - Kasulu katika eneo la Msimba lenye urefu wa kilomita tatu. Kipande hicho cha kutoka Daraja la Mngonya hadi Msimba hakijafanyiwa upembuzi yakinifu. Kwa hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kutoka Daraja la Mto Mngonya hadi Msimba kwa kiwango cha lami.
MHE. LUCIA M. MLOWE (K.n.y MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya kupokea dawa za ARV zilizokwisha muda wa matumizi (expired) kwenye vituo vya afya katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla:-
Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi katika Manispaa ya Ujiji na Mkoa wa Kigoma ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina utaratibu mahususi wa kuangalia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kabla ya kuvitoa katika Bohari ya Dawa na kuvisambaza kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya nchi. Kwa kutambua unyeti na umuhimu wa kutoa dawa salama zenye ubora kwa wananchi, Bohari ya Dawa yenye jukumu la kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi hutumia utaratibu ufuatao:-
• Mfumo wa ukusanyaji na utengenezaji wa nyaraka za ugavi una uwezo wa kuona kuwa dawa inayotakiwa kutolewa kuwa imebakisha muda gani kabla ya kwisha muda wake wa matumizi. Iwapo dawa hizo zitakuwa zimebakisha muda wa miezi sita mfumo huo hutoa tahadhari kwa afisa na kusitisha taarifa hiyo kutumwa kwa ajili ya kutoa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi husika.
• Kamati ya Dawa ya Kituo husika hupokea dawa hizo na kufanya ukaguzi kabla ya kusaini form mahususi ya kupokelea dawa na kujiridhisha kuwa dawa hizo zimekabidhiwa na kupokelewa kama ilivyoainishwa katika nyaraka za manunuzi kwa idadi baada ya kuhesabu na kuangalia kama zina ubora unaotakiwa. Iwapo kamati ama anayepokea dawa hizo ataridhika basi atasaini katika nyaraka hizo na anayekabidhi dawa huondoka na nakala. Iwapo Kituo hakitaridhishwa na dawa zilizofika, hulazimika kuzikataa na kujaza form maalum inayoitwa Discrepancy form.
Mheshimiwa Spika, tunaomba vituo au Halmahsauri hizo kuwasiliana moja kwa moja na taasisi za Serikali zinazohusika na usambazaji wa dawa katika Bohari za Dawa za Kanda au Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi ili yaweze kufanyiwa kazi mara moja pindi yanapotokea ili kwa pamoja tulinde afya za wananchi tunaowatumikia.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaunda Bodi ya zao la Mchikichi kama ilivyoanzisha kwenye mazao mengine?
(b) Je, Serikali imefanya utafiti wowote kuhusu kuendeleza zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Na.19 ya Mwaka 2009 ilianzisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo ina jukumu la kuhamasisha uzalishaji na kufanya biashara ya mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko. Kwa sasa Bodi imeanza kufanya biashara ya zao la mahindi na alizeti kwa kununua, kusafisha na kusaga unga wa mahindi na kukamua mafuta ya alizeti. Bodi itakuwa inaongeza mazao mengine kulingana mahitaji, uzalishaji na uwepo wa biashara (commercial viability) ya zao husika. Aidha, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa zao la mchikichi katika ukuaji uchumi wa Taifa na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi itatoa kipaumbele kwa zao hilo ili liweze kushughulikiwa na Bodi hii katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa usimamizi wa mazao ya nafaka na mchanganyiko katika uzalishaji na masoko, Serikali inatarajia kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko, kwa maana ya (Cereals and other Produce Regulatory Authority). Kwa maana hiyo, mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kudhibiti na kusimamia biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha mazao husika ikiwemo zao la mchikichi.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa zao la michikichi nchini unaratibiwa na Kituo cha Utafiti cha Mikocheni kilichopo Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti cha Tumbi kilichopo Tabora. Aidha, Kituo cha Utafiti Tumbi kimeweza kukusanya hifadhi nasaba (germplasm) za michikichi iliyoko nchini, wakati Kituo cha Utafiti cha Mikocheni kinatafiti namna ya kuzalisha miche ya michikichi kwa njia ya tissue (tissue culture) na baadaye kuisambaza kwa wakulima. Vilevile kituo hicho cha Mikocheni kina mpango wa kuingiza mbegu mama bora toka nje ya nchi na kuzitathimini ili kuona uwezekano wa uzalishaji wake hapa nchini.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-

Michezo ni afya, furaha, burudani, undugu na pia huondoa au kupunguza uhalifu nchini. Kuwa na viwanja vyenye hadhi kama kile cha Jakaya Kikwete Youth Park huvutia vijana wengi nchini kupenda michezo:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa viwanja vya michezo nchini si suala la Serikali peke yake bali jamii nzima ya Watanzania zikiwemo taasisi za umma, asasi za kiraia na kampuni za watu binafsi. Wajibu wa Serikali ni kuonesha njia kwa ujenzi mkubwa wa viwanja changamani kama vile Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru ulioko Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, viwanja vyote viwili sasa hivi viko katika ukarabati mkubwa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu ili kujiweka tayari kwa Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Bara la Afrika kwa watoto chini ya umri wa miaka 17 yatakayofanyika mwezi wa Nne mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ukarabati huo mkubwa Serikali imekamilisha maandalizi yote ya awali na ya kiufundi ikiwemo upatikanaji wa eneo la hati miliki, uwekaji wa mipaka ya eneo lote pamoja na beacons, ununuzi wa gari mbili za mradi huo, tathmini ya kimazingira, tafiti za eneo, upembuzi yakinifu wa mradi na michoro ya ubunifu wa ujenzi wa uwanja huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kiwanja cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha Dar es Salaam anachokiongelea Mheshimiwa Mbunge kimejengwa kutokana na mahusiano ya karibu kati ya Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ilala chini ya Mbunge wake Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na Kampuni ya Symbion kwa kushirikiana na Club ya Sanderland.

MWENYEKITI: Hampigi makofi? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kama ni kuonesha njia Serikali imeshafanyika hivyo na itaendelea kujenga viwanja vingine kadiri mahitaji yatakavyojitokeza na uwezo wa kifedha utakavyopatikana.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kulipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kwa uboreshaji wa Viwanja vya Kaitaba Kagera, Nyamagana Mwanza, na Mikoa ya Iringa, Singida na Lindi kwa kuonyesha njia katika upatikanaji wa viwanja bora vya michezo nchini.
MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-

Kituo cha Afya Ujiji kinahudumia zaidi ya wakazi 20,000 lakini kituo hicho hakina mashine ya ultrasound.

Je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya ultrasound katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Sungura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji imeidhinisha kiasi cha Shilingi 15,475,254.28 kupitia Mradi wa Malipo kwa Ufanisi (Result Based Financing) kwa ajili ya ukarabati wa chumba kitakachotumika kwa huduma za mionzi na shilingi 45,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa ultrasound. Fedha hizo zimepelekwa MSD kwa ajili ya taratibu za ununuzi wa kifaa hicho. Kwa sasa huduma ya Ultrasound inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Maweni na Hospitali Teule ya Manispaa ya Baptist.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza mahabusu katika Magereza na Vituo vya Polisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki kirefu Serikali kupitia vyombo vyake vya haki jinai nchini imekuwa ikifanya juhudi mahususi kupunguza idadi ya mahabusu katika Magereza yote hapa nchini. Kupitia mikakati mbalimbali idadi ya mahabusu imekuwa ikipungua mara kwa mara na bado juhudi zinaendelea za kuhakikisha Magereza yetu yanahifadhi wahalifu kulingana na uwezo wake kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mikakati inayotumika kutatua tatizo la mahabusu Magerezani ni pamoja na Vikao vya Kamati za Kusukuma Kesi (Case Flow Management Committee), Idara ya Mahakama kusisitiza matumizi ya Sheria ya Dhamana kwa makosa yanayodhaminika, uundwaji wa kikosi kazi cha haki jinai kupitia makosa mbalimbali (Criminal Justice System Task Force) pamoja na mikakati mingine inayotokana na Idara ya Mahakama.