Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mbaraka Kitwana Dau (9 total)

MHE. ABDALLAH H. ULEGA (K.n.y. MHE. MBARAKA K. DAU) aliuliza:-
Tafiti nyingi za mafuta na gesi zimefanywa na kampuni mbalimbali Kisiwani Mafia.
Je, ni nini matokeo ya tafiti hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni za BP na Maurel Et Prome kwa nyakati tofauti zilifanya tafiti katika eneo la Kisiwa cha Mafia kukusanya takwimu za mitetemo kwa eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 380 na 3D, lakini pia na katika Mkuza kwa kilometa 205 za 2D kuchimba visima viwili. Kati ya mwaka 1952 na 1956 kampuni ya BP ilichimba kisima cha Mafia -1 na kati ya mwaka 2006 hadi 2010 Kampuni ya Maurel Et Prome ilichimba kisima cha Mafia Deep -1. Baada ya tathmini ya takwimu hizo kufanyika matokeo yalionesha eneo hilo lina viashiria vya uwepo wa mafuta pamoja na gesi asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa leseni ya kitalu hicho imekwisha muda wake hivyo eneo hilo liko wazi kwa kampuni yoyote kuomba na kuendelea kazi ya uchimbaji mafuta na gesi katika eneo hilo.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Ujenzi wa barabara ya Kilindoni - Utende (Airport Access Road) yenye urefu wa kilometa 14 umekamilika, lakini mkandarasi CHICO ameijenga barabara hiyo chini ya viwango kwani ina viraka vingi.
Je, ni lini Serikali itaitaka kampuni hiyo kufanya marekebisho makubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni – Utende ni barabara inayounganisha kiwanja cha ndege cha Mafia na sehemu muhimu za kiuchumi, yakiwemo maeneo ya kitalii ya Fukwe za Utende na Gati la Kilindoni.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni – Utende yenye urefu wa kilometa 14 ilijengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Limited (CHICO) na kukamilika tarehe 1 Januari, 2015 na kufuatiwa na kipindi cha uangalizi cha mwaka mmoja hadi tarehe 1 Januari, 2016.
Hata hivyo, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilikataa kuipokea barabara hiyo kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa kipindi cha uangalizi na iliamuliwa ufanyike uchunguzi, ili kubaini kiwango cha mapungufu ya ubora katika ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa baadhi ya sehemu za barabara ya Kilindoni – Utende hazikujengwa katika ubora unaotakiwa, hivyo mkandarasi ameelekezwa kurudia kwa gharama zake mwenyewe maeneo yote yaliyoonekana kuwa na mapungufu kulingana na matakwa ya mkataba; kazi hiyo itaanza mara baada ya kipindi cha mvua kumalizika.
Aidha, uangalizi wa karibu wa maeneo mengine unaendelea kufanywa na TANROADS ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo inakabidhiwa Serikalini ikiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika kimkataba.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kutoka Kilindoni – Mafia – Rasi Mkumbi kwa lami ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Ilani ya CCM 2015 – 2020. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindoni -Mafia hadi Rasi Mkumbi yenye urefu wa kilometa 51 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuhusu ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kilindoni - Mafia hadi Rasi Mkumbi kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 359.52 kwa ajili ya kuendelea na matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara hii.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Wananchi wa Kisiwa kidogo cha Jibondo – Wilayani Mafia wamekuwa na shida kubwa ya maji.
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa muda mrefu wa kuvusha maji kutoka Kisiwa Kikuu eneo la Kiegeani kwenda Kisiwani Jibondo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutatua tatizo la maji katika Kisiwa cha Jibondo kwa awamu ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitumia kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa kisima, ujenzi wa nyumba ya pampu na kukiunganisha na umeme kituo cha kusukuma maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi itaanza mwanzoni mwa mwezi Juni, 2017 na kazi zitakazotekelezwa ni usanifu, uandaaji wa nyaraka za zabuni, kumpata Mkandarasi na ujenzi wa kuunganisha bomba la maji safi chini ya bahari eneo la kutoka Kiegeani kwenda katika Kisiwa cha Jibondo. Ujenzi wa mradi huo utaanza mwaka wa fedha 2017/2018 na utanufaisha wananchi wapatao 3,000.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya kuruka ndege katika Uwanja wa Ndege Mafia kwa awamu ya kwanza kwa ufadhili wa Mfuko wa Millenium Challenge Account (MCA).
Je, ni lini Serikali itajenga jengo la abiria na kuweka taa za kurukia kwenye uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mafia uliofadhiliwa na Shirika la Changamoto za Milenia la Serikali ya Marekani na kutekelezwa kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia Tanzania (Millennium Challenge Account – Tanzania) ulikamilika mwaka 2013. Mradi huo haukuhusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, barabara ya kuingia kiwanjani, maegesho mapya ya magari, maegesho mapya ya ndege (apron), barabara za viungio (taxiways) pamoja na usimikaji wa taa na mitambo ya kuongeza ndege wakati wa kutua.
Mheshimiwa Spika, kazi zilizosalia ambazo usanifu wa kina ulifanyika katika mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliohusisha viwanja saba kwa fedha za Benki ya Dunia na kukamilika mwaka 2009 hazijaanza kutekelezwa. Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali, zikiwemo fedha za ndani na washirika wa maendeleo, kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizosalia.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia kwa Wilaya ya Mafia kwa kuwa kutokana na jiografia yake kisiwa hiki kinategemea zaidi kiwanja hiki katika kuchochea shughuli za uchumi zikiwemo utalii. Hivyo, Serikali itaendelea kutafuta fedha ili kuweza kukamilisha ujenzi wa kiwanja hiki.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Papa aina ya potwe (whale shark) ni samaki ambaye duniani kote anapatikana Australia na Tanzania katika Kisiwa cha Mafia tu:-
Je, ni lini Serikali itakuja na mpango mkakati wa kumtangaza samaki huyo pamoja na vivutio vingine vya utalii kama vile scuba diving na sport fishing duniani ili kuvutia watalii nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, papa aina ya potwe (whale shark) anapatikana katika maeneo mbalimbali duniani hususan nchi zilizoko katika maeneo ya tropiki kama Australia, Taiwan, Pakistan, India, Ufilipino, Indonesia, Afrika Kusini, Kenya, Msumbiji na kwa Tanzania anapatikana katika Visiwa vya Mafia (Kilindoni), Pemba na Zanzibar. Samaki huyu ni mmoja kati ya samaki wakubwa sana duniani na uzito wake unaweza kufikia mpaka tani zaidi ya 20 na urefu kufikia zaidi ya mita nane na hivyo kuwa kivutio kikubwa cha watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania inaendelea kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi vikiwemo vivutio vya Wilaya ya Mafia ikijumuisha papa aina ya potwe kwa kutumia mikakati mbalimbali ya utangazaji kama vile vipeperushi; majarida mfano (Afrika Asilia, Selling Tanzania, Tan Travel, Tanzania Explore Magazine na Tanzania Map; tovuti yenye anuani www.tanzaniatourism.com; mitandao mbalimbali ya kijamii mfano youtube, instagram, twitter, facebook; Tanzania Tourism App inayopatikana kwenye Google Play Store kwenye simu za mkononi aina ya smart phone. Vilevile, utangazaji hufanyika kwa kutumia maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na mikoa na wilaya inaendelea kubaini maeneo ya fukwe katika mwambao wa bahari ya Hindi kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za utalii kama vile kuzamia (scuba diving), kuogelea (swimming), michezo ya kuvua samaki (sport fishing), kupiga mbizi (snorkeling) na sunbathing. Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan wavuvi ili kuwatunza samaki aina ya papa potwe. Hivi karibuni, Serikali itazindua studio ya utalii, channel ya utalii itakayokuwa chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na utambulisho wa Tanzania (Destination Branding). Hatua hii itaongeza ufanisi katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Kisiwa cha Mafia kinapata umeme kutoka kwenye jenereta kubwa ya TANESCO ambayo nayo inatumia mafuta mengi yenye gharama kubwa.
Je, ni lini Serikali itavusha umeme chini ya bahari (submarine cables) kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni takribani kilometa 50?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefanya tafiti za awali za kuona njia bora ya kuipatia Wilaya ya Mafia umeme wa uhakika na wa bei nafuu. Tafiti za awali zilizofanyika ni kuvusha umeme chini ya bahari (submarine cables) kutoka Nyamisati hadi Kilindoni na utafiti wa pili ni kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mchanganyiko (hybrid) vya umeme jua, upepo na mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti hizi za awali zimeonesha kuwa gharama za kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mchanganyiko ni nafuu zaidi na hivyo hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu zimeshaanza. Uwezo wa mitambo hii ya kuzalisha umeme itakapokamilika inatarajiwa kuwa na megawati saba ikilinganishwa na uwezo wa megawati 3.68 zilizopo kwa sasa (megawati 2.18 zinamilikiwa na TANESCO na megawati 1.5 zinamilikiwa na kampuni binafsi ya Ng’omeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tayari TANESCO imeshapata eneo la mradi Wilayani Mafia kwa ajili ya kujenga mitambo ya kuzalisha umeme na inakamilisha taratibu za kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu utakaoainisha gharama halisi za utekelezaji wa mradi huo ambapo unatarajiwa kuanza kazi mwezi Juni, 2018 na kukamilika ndani ya miezi saba. Aidha, Benki ya Maendeleo ya Ufaransa imeonesha nia ya kufadhili mradi huo mara upembuzi yakinifu utakapokamilika.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. MBARAKA K. DAU) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza urefu wa njia ya kurukia (run way) katika Uwanja wa Ndege wa Mafia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Usafiri wa Anga inataka kila mkoa kuwa na Kiwanja cha Ndege cha Daraja la 3C chenye uwezo wa kuhudumia ndege za kubeba abiria kati ya 50 na 100. Aidha, kwa mikoa inayowakilisha kanda, Viwanja vya Ndege vinavyopendekezwa ni kuanzia Daraja la 4C kwa ajili ya kuhudumia ndege za kubeba abiria kati ya 100 na 200 zinazoweza kufanya safari za kikanda na kimataifa. Kiwanja cha Ndege cha Mafia ni miongoni mwa viwanja vvya Daraja la 3C.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha Viwanja vya Ndege nchini, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilikamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja saba ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Mafia mnamo mwaka 2009. Kazi hii ilifuatiwa na ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege kwa kiwango cha lami katika ya mwaka 2011 na 2013. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege kufikia urefu wa mita 1,620 na upana wa mita 30, ukarabati wa kiungio na maegesho ya ndege kwa ikiwango cha lami, ujenzi wa mfumo wa maji ya mvua kiwanjani na ujenzi wa uzio wa usalama.

Mheshimiwa Spika, kazi hizi zilifanyika kwa ufadhili wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Serikali ya Marekani. Baada ya maboresho haya, kiwanja kipo kwenye kiwango cha Daraja la 2C ambapo kina uwezo wa kupokea na kuhudimia ndege zenye ukubwa wa aina ya ATR42, DASH 8 na Fokker 50 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria kati ya 30 na 50.

Mheshimiwa Spika, katika mipango yake ya muda wa kati na mrefu, Serikali itaendelea kukamilisha kazi zilizobaki ambazo ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria na miundombinu yake yaani barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani, maegesho ya magari, barabara ya kiungo na maegesho ya ndege pamoja na usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege. Pamoja na kuwa kwa sasa kiwanja hiki kipo Daraja la 2C, eneo la ziada limeshatengwa ili kukidhi mahitaji ya upanuzi wa kiwanja kwa siku za baadaye na kukamilishwa kwa kiwanja kuwa Daraja ya 3C.
MHE. MBARAKA K. DAU Aliuliza:-

Je, ni kiasi gani cha fedha kimepatikana mpaka sasa kwenye tozo (entrance fee) ya kuingia maeneo ya Hifadhi ya Bahari (Marine Park) katika Kisiwa cha Mafia?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na. 29 ya mwaka 1994, imekipa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu mamlaka ya kukusanyafedha zitokanazo na shughuli za utalii kwenye maeneo yaliyohifadhiwa (Hifazi za Bahari na Maeneo Tengefu) kwa ajili ya uanzishaji, usimamizi na uendelezaji wa maeneo yaliyohifadhiwa.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2001 mpaka kufika mwaka 2017/2018, Hifadhi ya Bahari ya Mafia imekusanya jumla ya fedha Sh.6,140,843,478 za Kitanzania, zilizotokana na tozo za viingilio kwa wageni walioingia kwenye hifadhi ya bahari ya Mafia kwa kipindi hicho.