Contributions by Hon. Silvestry Fransis Koka (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji usiochelewa. Nasema hivyo kwa sababu tulisimama hapa na tukasema tunahitaji Rais na Serikali ambayo inafanya maamuzi hata kama ndani yake kutakuwa na makosa madogo madogo, naye anafanya hivyo na nina imani tutakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri aikumbuke Kibaha. Tunalo eneo lapata hekta 1,500 lililotengwa kwa ajili ya viwanda na yeye kama alivyo imara kutoa viwanda basi namuomba atoe viwanda hadi eneo hili liweze kukamilika na namuunga mkono kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Tanzania ya Viwanda ni jambo linalowezekana na nia nzuri ya Serikali iliyonayo inawezekana endapo kwa uhakika tutakwenda kuondoa kero na matatizo mbalimbali ambayo yanaturudisha nyuma kwenda kufanikiwa katika azma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na azma hii tunaiomba Serikali iendelee kutengeneza mazingira bora na rafiki zaidi na wawekezaji na wafanyabiashara. Tunaiomba Serikali iondoe kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na tozo za aina moja ambazo sasa zinatozwa na taasisi ambazo ni za usimamizi (Regulatory Authority) utakuta taasisi mbili au tatu zinatoa tozo ambazo zinafanana kwa wafanyabiashara. Hili ni tatizo na ni kikwazo katika uanzishwaji wa viwanda na uendeshaji wa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kero nyingine kubwa ambapo viwanda vyetu vya ndani vinapozalisha vinashindwa hasa kushindana na mali zinazotoka nje ya nchi. Hii ni kwa sababu baadhi ya malighafi na utaratibu mzima wa mchakato wa uzalishaji katika viwanda vya ndani vinatozwa kodi, ikiwa ni pamoja na kodi ya VAT. Hii inafanya mali zinazozalishwa na viwanda vya ndani zishindwe kushindana na mali kama hizo zinazotoka nje kwa sababu wao katika uzalishaji hawalipi kodi hizo. Hili ni tatizo kubwa na ningeomba sasa Serikali kupitia Wizara yake ilitazame na kulifanyia kazi ili tuweze kushamirisha nia na madhumuni ya viwanda Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu ni wajibu wa Serikali kulea wafanyabiashara na viwanda, kwa sababu kimsingi Serikali inamiliki asilimia 30 ya makampuni na biashara zote zilizopo ndani ya nchi. Ndiyo maana siku ya mwisho biashara zote zinawajibika kulipa asilimia 30 ya faida inayopatikana na shughuli nzima ya uzalishaji au ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kulea, kutunza na kusaidia ili siku ya mwisho iweze kufaidika na kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Vivyo hivyo, kwa wafanyabiashara na wazalishaji wanatakiwa wawajibike kwa Serikali na wananchi kwa kutimiza taratibu zote kwa mujibu wa sheria zinazowahusu ikiwa ni ulipaji wa kodi na mengineyo ili kila mmoja aweze kufanya linalofaa na tuwe tunapata win win situation; kwa maana hakika mtu ambaye ana aslimia 30 kama na yeye hutamtimizia haki ni wazi kwamba biashara haitaweza kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania, wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania. Katika mkutano wa Tanzania Business Council uliokaa tarehe 6 mwezi huu, Mheshimiwa Rais alitamka wazi kwamba yupo tayari kuendelea kuwasaidia wawekezaji kwa kuwapa incentives mbalimbali ikiwa ni pamoja na tax holiday ilimradi uwekezaji huo unalenga kunufaisha na kuisaidia nchi, Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla wake. Kwa hiyo, ni wazi kwamba nafasi ipo kazi ni kwetu sisi wawekezaji na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hili ameliweka wazi na amewaagiza watendaji waende wakalitekeleze. Rai yangu kwa wawekezaji, tusilale, rai yangu kwa wafanyabiashara, tusilale. Hatuna sababu ya kuendelea kupata vikwazo kwa sababu Rais amekwisha tamka wazi na yupo tayari kufanya maamuzi yoyote ili lengo na madhumuni ya kuwaunga mkono wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na hata wa nje likamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue nafasi hii kutaka mamlaka zote husika ikiwa ni pamoja na Wizara mbalimbali ziweze sasa kushirikiana na kuhakikisha kwamba azma hii inakwenda kukamilika na tunasonga mbele katika kuimarisha viwanda na vile vile biashara na hatimaye uchumi na maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi sana nizungumzie madeni kwa kuwa kimsingi yanahusika moja kwa moja na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu mzigo mkubwa wa madeni ya nje na madeni ya ndani ambao Serikali inao, lakini naiomba sana Serikali katika utaratibu wake, ijikite sasa kupunguza mzigo wa madeni ya ndani. Lengo ni lile lile, madeni ya ndani yatakavyolipwa wafanyabiashara na wawekezaji wataendelea kuwekeza na matokeo yake manufaa yale yatakuwa ni kwa ajili ya Serikali na wananchi kwa ujumla wake, ina maana Serikali itaendelea kukusanya kodi kutokana na ile pesa kuingia kwenye mzunguko. Athari ya kupungua kwa ajira itaondoka, maana yake ajira zitaongezeka na hatimaye Serikali itafaidika zaidi pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali itapata fursa ya kutumia mitaji ya wafanyabiashara na wawekezaji katika kutekeleza malengo na mambo mbalimbali ya maendeleo. Pamoja na hilo uwekezaji wa ndani utaweza vile vile kuvutia zaidi uwekezaji wa nje ambao tunauhitaji ili kwenda kuimarisha uchumi wetu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulipwa kwa madeni ya ndani kutaisaidia Serikali kupata huduma na bidhaa kwa bei nafuu, kwa sababu kunapokuwa na tendency ya Serikali kuchelewa kulipa huduma na bidhaa zinazotokana na wafanyabiashara na za uzalishaji wa viwandani, maana yake ni kwamba kinachofuata huduma zile Serikali itaendelea kuzipata kwa bei ya juu na huku wafanyabiashara wakihofia kwamba ukifanya biashara na Serikali, basi fedha zako zitakaa muda mrefu na ikiwa umezikopa matokeo yake utapata matatizo makubwa. Kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba bei zitakuwa ni kubwa na hatimaye hatutafikia malengo ya kubana matumizi na kwenda sambamba katika utoaji wa huduma katika serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba tutasaidia wafanyabiashara wetu, maana wengi tayari wapo kwenye matatizo makubwa na mabenki. Wengine wanafilisiwa na wengine wanapoteza mali zao. Kwa hiyo kwa kuanza kuwalipa wafanyabiashara wa ndani ni wazi kwamba tutachangamsha uchumi na hatimaye wananchi watafurahia na tutasonga mbele kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya ndani yakilipwa itawasaidia vile vile Watanzania wengi ambao wanadaiwa kodi waweze kuzilipa kwa wakati na hatimaye siku ya mwisho itakuwa ni win win situation kati ya wafanyabiashara, wawekezaji na Serikali na kimsingi fedha nyingi zitatumika katika kuwekeza na hatimaye tutafikia malengo ya viwanda, ajira na ustawi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na haya machache ya kuishauri Serikali yangu, inaunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nichukue nafasi hii kwanza kuishukuru sana Serikali yetu ya Chama cha MapinduzI kwa kazi nzuri inayofanya. Wizara ya Viwanda imekuwa ikijitahidi kwa hali mali ili kuhakikisha Sera yetu ya Viwanda inakua. Nichukue kweli nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kujitoa na kujitolea kwa ajili ya wananchi wa Tanzania kuhakikisha Watanzania wenyewe tunajenga viwanda na tunakwenda kushika hatamu za uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nitoe pongezi kwa kazi kubwa ya kujenga miundombinu mbalimbali kwa sababu kupitia miundombinu hii ndiyo tunaweza kujenga uchumi wa kati na hata uchumi mkubwa. Mifano iko wazi, ujenzi wa reli, ujenzi wa miundombinu ya umeme kama Stiegler’s Gorge ni jambo ambalo tunahitaji tumuunge Mheshimiwa Rais mkono kwa nguvu zetu zote.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu mojawapo ya changamoto tuliyonayo katika uanzishaji wa viwanda ni pamoja na nguvu za kusukuma au kuendesha viwanda kwa maana ya umeme. Ndugu zangu wote tunafahamu kwamba umeme unaozalishwa kwa maji ni rahisi kuliko umeme mwingine wote. Kwa hiyo, tutakapopata umeme mkubwa unaozalishwa na maji kutoka Stiegler’s Gorge maana yake ni kwamba hata gharama za uzalishaji zitapungua, tutaweza kuzalisha kwa gharama nafuu na hatimaye kufikisha bidhaa kwa wananchi kwa gharama iliyo nafuu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wafanyabiashara wa Tanzania na Watanzania wote tumuunge mkono Rais, tujitokeze tujenge viwanda, tuunge mkono miradi ambayo ipo mbele yetu ili siku ya mwisho jihitada za kwenda kwenye uchumi wa kati ziweze kukamilika bila tatizo lolote.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ina sababu hasa ya kutazama sasa balance ya biashara ya ndani nje. Tuangalie na tuweze kuona ni namna gani tunapoanza sasa kulea viwanda vyetu tuna balance pamoja importation ya bidhaa muhimu kwa ajili wananchi. Kwa sababu lengo la biashara pamoja na kupata faida na kulipa kodi lakini ni kuwafikishia wananchi bidhaa kwa bei iliyo nzuri, nafuu na ubora. Sasa kama hatutarudi tukaangalia bado kuna watu wachache wata-take advantage na wananchi wataendelea kununua bidhaa kwa gharama kubwa na wao kujilimbikizia faida kubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kuwepo na balance kati ya bidhaa zinazoletwa kutoka nje na zinazozalishwa ili yale mabadiliko ya bei ya uzalishaji na malighafi yaweze kumnufaisha vilevile mwananchi ambaye ndiye mtuamiaji. Nina imani kwa kufanya hivi tutatimiza azma ya Serikali ya kumhudumia na kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini.
Mheshimiwa Spika, kujenga viwanda ni jambo moja lakini kuviendesha ni jambo lingine ambalo ni gumu zaidi. Nitoe mfano wa kiwanda kinachozalisha viuadudu pale Kibaha. Kiwanda hiki kilianza kujengwa mwaka 2010 kikakamilika 2015 na kikaanza uzalishaji 2016. Kiwanda hiki ni cha pekee Afrika na kina uwezo wa kuzalisha viuadudu au viatilifu vinavyoua viluilui vya mbu kiasi cha tani milioni sita kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini navyoongea na wewe kuanzia kilipoanza kufanya kazi mwaka 2016 hadi leo kimezalisha tani laki nne tu na hakuna wanunuzi. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba tarehe 22 Juni, 2017
Mheshimiwa Rais alipotembelea viwanda Kibaha alikitembelea kiwanda hiki na alifurahishwa sana na kiwanda hiki kwa sababu ndiyo njia pekee ya kumaliza malaria nchini. Alitoa maagizo kwamba kila halmashauri inunue dawa hii iweze kutumika kuuwa viluilui vya mbu na tuangamize malaria hapa nchini. Tangu kipindi kile katika ya halmashauri 81 ambazo walichukua dawa hii ni halmashauri 25 tu ndizo ambazo zimelipa, nyingine hawajalipa kiwanda kinaendelea kudorora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dawa hii ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama hamuifahamu kazi yake inashambulia viluilui vya mbu katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo maji yamesimama na kuhakikisha kwamba mbu hawawezi kuzaliwa. Nafikiri hii ndiyo njia pekee ya kumaliza malaria badala ya kutumia fedha nyingi kununua dawa kwa ajili ya malaria. Dawa hii ni nzuri sana, kwanza kabisa ni environmental friendly, yaani siyo kama dawa nyingine mfano DDT na nyingine tunazotumia kiasi kwamba unaweza hata ukainywa. Watengenezaji wali- demonstrate mbele ya Mheshimiwa Rais kwa kunywa ile dawa, haina hata madhara hata ukiinywa lakini ni sumu kwa viluilui vya mbu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa makusudi kabisa imetenga fedha nyingi kwa ajili ya huduma ya dawa na afya za Watanzania kutoka bajeti ya shilingi bilioni 30 mpaka shilingi bilioni 200 kwa ajili ya dawa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malaria inapigwa vita nchini. Sasa tunachoangalia ni watu tumeangukia, ndiyo tunahangaika kutibu malaria hatutaki kuangalia ni wapi tumejikwaa na tutapojikwaa ni kung’atwa na mbu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama kweli tunataka kusaidia viwanda vyetu vya ndani kiwanda ambacho kimejengwa kwa ushirikiano au kwa msaada kati ya Cuba na Tanzania ambacho hadi sasa tayari wenzetu wa Angola, Nigeria wameshaanza kupata hamu na kuleta order kwa ajili ya dawa hii, tusaidie kiwanda hiki kizalishe dawa na bajeti ya Wizara ya Afya itengwe kwa ajii ya kulipia dawa hizi kwa sababu lengo letu ni kuangamiza mbu si kuendelea kila siku Watanzania wanaugua tunahangaika kuwatibu kwa gharama kubwa. Niombe sana Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Wizara ya Afya ili waweze kununua dawa hizi, Watanzania wapewe elimu ya kuzitumia na hatimaye tuangamize mbu na Tanzania iwe free from malaria. Inawezekana, kiwanda tunacho, tutachekwa kama tutaendelea kuugua malaria na wakati tulishajipanga hadi kuweza kujenga hiki kwa gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki hakijasimamiwa vizuri, kiko chini ya NDC, lakini hadi sasa hakina hata Bodi ya Wakurugenzi sasa kinajiendeshaje? Kina wafanyakazi, uzalishaji ni duni na hakuna anayekiangalia ipasavyo matokeo yake tunakwenda kwenye hasara na tunatoka sasa nje ya azma na sababu ya Tanzania ya viwanda. Ni wazi kama kitasimamiwa kina uwezo mkubwa sana wa kuuza bidhaa hii ndani na hata nje ya nchi yetu na kikailetea Serikali mapato makubwa ya kigeni kwa sababu kiko pekee Afrika na dawa inayotengeneza ni pekee ambayo inakwenda kulenga mbu na kumwangamiza na kuhakiksha kwamba malaria haitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na kuhimiza ujenzi wa viwanda vilevile tushiriki katika kuhakisha viwanda hivi tunavisimamia, tunavisaidia ili viweze kuleta tija na hatimaye tuweze kufikia malengo makubwa ya Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwaasa wafanyabiashara wenzangu Tanzania, kama nilivyosema lengo kubwa la biashara mbali ya kulipa kodi na kupata faida ni kumhudumia Mtanzania. Tuna wajibu wa kuhakikisha tunapopeleka bidhaa katika masoko ya Mtanzania tunamlenga Mtanzania apate nafuu katika bidhaa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameshanyoosha mkono kwa wafanyabiashara, ameamua kutuunga mkono na kutusaidia na hata amekuwa akitoa maamuzi ya papo kwa papo kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania. Ametaka wafanyabiashara wa Tanzania tufanye biashara, tuzalishe, tujenge viwanda na tutumie soko la ndani na fedha za ndani kuboresha viwanda vyetu. Sasa kutokupeleka azma hiyo kwa wananchi na kuwafanya wananchi wakawa wanatapatapa wapate wapi mahitaji ni sawasawa na kuiudhi Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kuomba tujitahidi twende sambamba na azma ya Mheshimiwa Rais na Serikali yetu. Naunga mkono hoja tuendelee kujenga nchi yetu ya viwanda.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kupongeza na kuishukuru Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya katika miradi mikubwa ya maendeleo, bila kusahau mradi mkubwa wa umeme ambao utatutoa katika matatizo ya umeme wa Stiegler’s Gauge ambao Mheshimiwa Rais ameuvalia njuga na tunamuunga mkono; mradi wa reli ambao utaondoa tatizo la usafiri, ikiwa ni pamoja na Wabunge kuja Dodoma itakuwa ni chini ya saa tatu, tunaunga mkono na tuna imani tutainua uchumi wetu kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu ameendelea kutekeleza miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali. Pwani tuna mradi wa barabara, Awamu ya I, kutoka Ubungo mpaka Kibaha ambayo ni six lane pamoja na Daraja la Ubungo. Nilisikia mtu akisema kwamba Daraja la Ubungo halina thamani kwa wakulima vijijini lakini ukweli ni kwamba mazao ya wakulima yanayotoka katika vijiji yatafika Dar es Salaam na yatanunuliwa kwa bei nzuri na mkulima kule atafaidi lakini hata sisi watoto wa huyo mkulima na ndugu zao tutatumia daraja lile na uchumi utachangamka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya yanafanyika kwa ajili ya Watanzania. Mheshimiwa Rais na Serikali yake atajenga miradi hii, haondoki nayo inabaki, tutaendelea kuitumia na atakapomaliza kipindi chake, watoto wetu na wajukuu wetu. Jambo kubwa ni sisi tumuunge mkono Mheshimiwa Rais na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na tuishauri iendelee kufanya kazi nzuri ili maendeleo katika nchi yetu yaweze kuja kwa haraka.
Nataka niseme na kumpa moyo Mheshimiwa Rais kwamba hata wafanyabiashara walio wengi sasa voluntarily wanalipa kodi kwa sababu wanaona matokeo ya kodi zao kwamba zinakwenda kufanya mambo makubwa ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu kwamba katika miradi hii, iko miradi mikubwa na ambayo ni complicated kuiendesha kama Shirika la Ndege na ninajua ndege nyingine zinakuja, tusiogope kushirikisha experts. Tushirikishe experts wenye uzoefu kutoka nje, washirikiane na management ya Kitanzania ili tuweze kufikia malengo na mafanikio ya miradi hii mikubwa. Nina imani kama tuta-blend skills na expertism kutoka nje na ndani ya nchi ni wazi kwamba tutaweza kupeleka mbele gurudumu la maendeleo kwa kuhakikisha miradi hii inakwenda kuleta mafanikio makubwa na kuibadilisha kabisa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka vilevile nizungumzie suala la mazingira ya kufanya biashara. Nafahamu ili mipango hii ya maendeleo iweze kufanikiwa ni lazima mazingira ya ndani ya kufanya biashara yaboreke. Najua Serikali imeshachukua hatua ikiwa ni pamoja na kutengeneza ile blueprint ya kuhakikisha kwamba taasisi zinazohusika na kudhibiti ufanyaji wa biashara zinakuwa ni msaada kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachokiomba hapa sasa, Serikali ihimize utaratibu huu, ile blueprint sasa iende kwenye vitendo ili isaidie ukamilishaji na utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo na ili kila Mtanzania aweze kufanya biashara katika hali ambayo haina usumbufu na yenye tija. Masuala ya kodi yakae vizuri, masuala ya compliance mbalimbali ikiwa ni pamoja na TBS, TFDA pamoja na taasisi nyingine ziweze kumsaidia mfanyabiashara achangamshe uchumi, kodi zilipwe na hatimaye tufikie malengo yetu. Naomba blueprint sasa iende kufanyiwa kazi na iende kwenye utekelezaji na isiendelee kubakia katika vitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imechukua hatua na hatua hii ni hapohapo katika kwenda kuboresha mpango wetu wa maendeleo. Imechukua hatua ya kulinda viwanda vya ndani ikiwa ni pamoja na kuongeza baadhi ya tariffs na imechukua hatua hata ya kupunguza kodi katika bidhaa mbalimbali. Lengo na madhumuni siyo kumfaidisha mfanyabiashara peke yake bali pia kumfaidisha Mtanzania aliye kijijini anayetumia bidhaa zile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baadhi ya wafanyabishara sasa hawafanyi hivyo, matokeo yake baada ya kuweka tariffs za bidhaa za nje zikaenda juu na wenyewe wanapandisha bei ya bidhaa zao badala ya ku-capitalize katika kuuza zaidi kwa sababu bidhaa zao sasa ni bei rahisi. Niombe sana, azma ya Serikali kufanya hivyo ni kulinda viwanda na kumrahisishia Mtanzania kupata bidhaa kwa bei nzuri na kuhakikisha viwanda vinazidisha uzalishaji. Rai yangu hapa, wenye viwanda na wafanyabiashara walichukue jambo hili au wachukue hili punguzo au ongezeko la bei za bidhaa kutoka nje kuzalisha zaidi na wasiongeze bei kumuumiza yule mlaji wa mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi hii mikubwa ya maendeleo ambayo Serikali imejikita ni wazi kwamba utekelezaji wake unahitaji fedha nyingi na ili fedha ziweze kupatikana ni lazima ulipaji wa kodi uwe mkubwa na ili ulipaji wa kodi uweze kuwa mkubwa ni pamoja na Serikali kwa makusudi kuchangamsha biashara za ndani. Ili biashara za ndani ziweze kuchangamka ni pamoja na kuhakikisha madeni mbalimbali ya wafanyabiashara Serikalini yanalipwa kwa sababu, the main stimulant ya uchumi katika nchi yoyote ile ni Serikali. Katika uchumi wa nchi yetu ulio mdogo ni wazi kwamba mwajiri wa kwanza wa makampuni madogo katika nchi ni Serikali. Kwa hiyo, nina uhakika Serikali ikijikita katika kulipa madeni siku ya mwisho zile fedha zitarudi katika utaratibu wa kodi na uchumi utachangamka na miradi hii itaweza kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na hakika naunga mkono hoja na tuko pamoja katika kuhakikisha miradi na mipango hii ya maendeleo inatakamilika. Ahsanteni.