Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (1 total)

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, mpaka sasa hivi kuna baadhi ya makampuni ya watu binafsi na wafanyabiashara wanaendelea kutoza na kupanga bei kwa kutumia dola badala ya Tanzanian shillings.
Je, Serikali haioni hiyo inaidhalilisha shilingi yetu na kuonesha kwamba, hawana imani na shilingi ya Tanzania?
Swali la pili, kwa kuwa moja ya eneo ambalo linatumia fedha nyingi sana na kusababisha kutokuwepo kwa urari mzuri wa nchi ni uagizaji wa vyakula mbalimbali kutoka nje ya nchi wakati vyakula hivyo vinaweza kuzalishwa ndani ya nchi, maeneo kama mafuta ya kula, sukari na mazao mengine ambayo yanaweza kuzalishwa hapa nchini. Kwa mwaka tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya kuagiza mazao yanayotokana na vyakula vinavyoweza kuzalishwa hapa na kutoa ajira kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuzuia uagizaji wa baadhi ya vyakula kutoka nje ya nchi ili kuinua ualishaji wa ndani ya nchi na kuokoa shilingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba katika watu ambao wanaweka bei kwa kutumia dola wanaidhalilisha shilingi yetu, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tulipitisha sheria katika Bunge lako Tukufu kwamba siyo kosa kuweza kuweka bei kwa currency ambayo siyo ya Tanzania, kosa ni ni kukataa pesa shilingi ya Tanzania pale ambapo mteja anataka kulipa na yule mwenye duka akakataa kupokea hilo ndio kosa, lakini siyo kosa katika kuweka bei hiyo kwa currency ambayo sio shilingi yetu ya Tanzania, kama Taifa tuliona inafaa na ndiyo maana tunaendelea kutekeleza sheria hii tuliyopitisha mwaka 1992.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuzuia ku-import bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini. Napenda kulijibu Bunge lako Tukufu kwamba, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza kwamba uchumi wa viwanda ili tuweze kuzalisha bidhaa zetu za kutosheleza ndani ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumeweza kuzalisha bidhaa hizi kwa kiwango ambacho kinatosheleza hatuna sababu ya kuendelea ku- import na tutaweza kurekebisha sheria zetu ili tuweze sasa kutumia bidhaa zetu, lakini kusema sasa tupige marufuku wakati bado kuna uhitaji wa bidhaa hizi, haitakuwa sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika kuiendea Tanzania ya Viwanda, tuna uhakika ndani ya miaka mitano mpaka kumi tutakuwa tumeweza kujitosheleza kwa bidhaa zetu ndani ya Tanzania. (Makofi)