Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (127 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Hali ya maisha ya wastaafu wetu ni mbaya sana na Serikali imeshindwa kuongeza pensheni zinazolingana na gharama halisi za maisha kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha pensheni za wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni kwa ajili ya kuwapunguzia wastaafu makali ya ongezeko la gharama za maisha. Ili kukabiliana na changamoto za ugumu wa maisha kwa wastaafu, Serikali imekuwa ikiongeza pensheni kwa wastaafu pale ambapo hali ya uchumi inaruhusu.
Kwa mfano, mwaka 2004 pensheni ilikuwa shilingi 21,606.05 ambayo iliongezwa hadi shilingi 50,114.43 kwa mwezi wa Julai, 2009 sawa na ongezeko la 132%. Mwezi Julai, 2015 Serikali imeongeza pensheni hadi kufikia Sh. 100,125.85 sawa na ongezeko la 100%.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kiuchumi zilizopo kuanzia mwaka 2004 hadi 2015 kiwango cha pensheni kimeongezeka mara tano na Serikali itaendelea kuboresha pensheni za wastaafu kwa kadiri uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 inalenga kuwapunguzia wafanyakazi kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi kufikia tarakimu moja.
Je, Serikali imejipangaje kutekeleza jambo hilo muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kodi ya wafanyakazi uliopo sasa una viwango vya kodi kwa kuzingatia kipato cha mfanyakazi ambapo kiwango cha kodi hupanda kadri ya kipato cha mfanyakazi kinavyopanda. Kwa sasa, kima cha chini kisichotozwa kodi ya mfanyakazi ni kipato cha mshahara kisichozidi shilingi 170,000/=. Watumishi Waandamizi wanalipa kodi kubwa kutokana na mishahara yao mikubwa na kwa asilimia kubwa zaidi ya wale watumishi wa hali ya chini.
Mheshimiwa Spika, watumishi wa ngazi za chini wataendelea kuboreshewa maslahi yao kwa kupunguza kiwango cha chini cha kodi. Kiwango cha chini cha kodi kinachotozwa kwenye kipato cha zaidi ya shilingi 170,000/= ni asilimia 11; na cha juu zaidi ni asilimia 30. Serikali imekuwa ikishusha kiwango cha chini cha kuanzia kutoza kodi kwa mfanyakazi hatua kwa hatua, kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/2007, asilimia 15 mwaka 2008/2009 na kufikia asilimia 14 mwaka 2010/2011. Mwaka 2012/2013 tumefikia asilimia 13; asilimia 12 kwa mwaka 2013/2014 na sasa kufikia kiwango cha asilimia 11. Lengo la kuendelea kushusha kiwango hiki ni kufikia kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufikia kiwango hicho cha asilimia 10 Serikali itaendelea kujadiliana na Vyama vya Wafanyakazi kwa lengo la kupunguza kodi hii ya Pay As You Earn (PAYE) hadi kufikia tarakimu moja kutegemea na hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika mwaka hadi mwaka.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mwaka 2013 Serikali iliuza hatifungani ya thamani ya Dola za Kimarekani milioni mia sita (USD 600m) kupitia benki ya Standard yenye tawi hapa nchini (Stanbic); Shirika la Corruption Watch la Uingereza kwa kutumia vyanzo kama IMF imeonesha kwamba hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanzania hasara ya Dola za Kimarekani milioni themanini (USD) 80.m) na Serikali imelipwa faini Dola za Kimarekani milioni sita (USD Six Million) tu.
Je, kwa nini Serikali haiichukulii hatua Stanbic Bank ili walipe faini zaidi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mahitaji yaliyofanywa na serious fraud office ya Uingereza dhidi ya Standard Bank Group, Serious Fraud Office ilitambua kiasi cha Dola za Kimarekani milioni sita, sawa na asilimia moja ya mkopo ambao Tanzania haikupaswa kutozwa. Tozo (arrangement fee) iliyotakiwa kulipwa kwa Standard Bank Group ni asilimia 1.4. Badala yake tozo iliyoingizwa kwenye mkataba ni aslimia 2.4, na ilithibitika kwamba tozo ya asilimia moja ya ziada haikuwa halali.
Katika hukumu iliyotolewa na Mahakama huko Uingereza Standard Bank Group iliamriwa kulipa faini ya Dola za Kimarekani milioni thelathini na mbili nukta mbili. Kati ya hizo kiasi cha Dola milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania, Dola za milioni sita zikiwa ni fidia na Dola milioni moja ikiwa ni riba.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia taarifa ya hasara kwa Serikali ya Tanzania ya Dola za Kimarekani milioni themanini iliyotajwa na Mheshimiwa Zitto Mbunge wa Kigoma Mjini na hatukupata usahihi wake. Hata hivyo, taarifa ya hasara ya dola milioni themanini imetajwa katika taarifa yenye kichwa cha habari How Tanzania was Short Changed in Stanbic Bribery Payback iliyochapishwa katika gazeti la The Guardian la tarehe 16 Disemba, 2015, likinukuu taarifa ya Corruption Watch ya Uingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa haikutoa maelezo ya namna hasara ya dola milioni themanini ilivyopatikana na kwa kuwa, taarifa iliyonukuliwa kutoka corruption watch pia haielezi jinsi hasara hiyo ilivyokokotolewa, Serikali inashauri Mheshimiwa Mbunge awasilishe taarifa alizonazo tuone iwapo ina vigezo vya kutosha kuisaidia Serikali kujenga hoja ya madai ya hasara hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Benki Kuu imeiandikia Benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni tatu kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za benki na taasisi za fedha. Aidha, sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kimekwisha tarehe 30 Januari. Kwamba Stanbic imewasilisha taarifa ya utetezi wao Benki Kuu na utetezi wao unafanyiwa kazi kwa sasa. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi huo Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kwa muda mrefu uchumi wa Nchi yetu umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa mwaka:-
Je, mapato ya Serikali yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia ngapi kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2010-2015 umekua kwa wastani wa asilimia 6.74. Ukuaji halisi wa asilimia katika kipindi hicho ulikuwa asilimia 6.4 mwaka 2010, asilimia 7.9 mwaka 2011, asilimia 5.1 mwaka 2012, asilimia 7.3 mwaka 2013 na asilimia saba mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho mapato ya Serikali ambayo yanajumuisha mapato ya kodi na mapato yasiyokuwa ya kodi ya Serikali Kuu pamoja na mapato ya Halmashauri yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 17.8 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010/2011 mapato yalifkia shilingi trilioni tano nukta saba tatu na kuongezeka hadi Shilingi trilioni saba nukta mbili mbili mwaka mwaka 2011/2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.9, mwaka 2012 mapato yakafikia shilingi trilioni nane nukta tano moja, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.9. Mwaka 2013/2014 mapato yalifikia shilingi trilioni kumi nukta moja mbili ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.6 na mwaka 2014/2015 mapato yakafikia shilingi trilioni kumi nukta tisa tano, sawa na ongezeko la asilimia 7.6.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha na kumiliki Bureau de Change zake yenyewe badala ya kuacha huduma hiyo kuendelea kutolewa na watu au taasisi binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mkakati wa kufungua au kuanzisha Bureau de Change zake kwa sababu imejitoa kuhusika moja kwa moja na biashara ya fedha kama vile benki na Bureau de Change kutokana na mabadiliko ya mfumo katika sekta ya fedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991. Sekta binafsi imeachiwa jukumu la kuanzisha na kuendesha biashara ya fedha nchini chini ya usimamizi wa Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri na salama ya uwekezaji katika sekta zote, ikiwemo sekta ya fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha, kuendesha na kutoa huduma bora za kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka sheria na taratibu za kusaidia nguvu na juhudi za wananchi katika kuanzisha benki au taasisi za fedha katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.
Kwa hiyo, Serikali inategemea kuwa wananchi watatumia fursa hii ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini na kuanzisha huduma za kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo yenye uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili yaweze kutoa huduma bora na inayokidhi matakwa ya sheria na kanuni za biashara ya fedha. Hivi karibuni Benki Kuu imetoa kanuni mpya kwa lengo la kuimarisha usimamiaji wa maduka hayo. Maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni yanatakiwa kufunga mashine za EFDs ili kuiwezesha TRA na BoT kupata taarifa za moja kwa moja juu ya miamala inayofanywa kwenye maduka hayo.
MHE. CONCHESTER L. RWAMLAZA aliuliza:-
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 Serikali kupitia Waziri wa Fedha iliahidi kupandisha pensheni kwa wastaafu wanaolipwa Sh.50,000 ili walipwe Sh. 100,000/=.
Je, Serikali imetekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchester L. Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumfahamisha Mheshimiwa Rwamlaza na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali ilitekeleza ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Sh.50,114.43 kwa mwezi hadi kufika Sh.100,125.85 kwa mwezi, kuanzia Julai 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijaruhusu swali langu kujibiwa naomba marekebisho madogo kwenye majina yangu yaliyo kwenye majibu ya Waziri. Jina langu Samson halina (iiI kule mwisho na jina langu Bilago halina N katikati halisomeki Bilango linasomeka Bilago.
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wastaafu kutolipwa mafao yao baada ya kustaafu:-
(a) Je, kuanzia Januari hadi Disemba, 2015 ni watumishi wangapi wa umma wamestaafu utumishi?
(b) Je, kati ya hao ni wangapi wamelipwa mafao yao?
(c) Kama kuna ambao hawajalipwa, je, ni kwa sababu gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Idadi ya watumishi wa umma waliostaafu, kati ya Januari, 2015 na Disemba, 2015 ni 7,055
(b) Kati ya watumishi 7,055 waliostaafu, watumishi 5,057 wamelipwa mafao yao.
(c) Jumla ya watumishi waliostaafu 1,998 hawajalipwa mafao yao kutokana na sababu zifuatazo:-
(i) Upungufu wa baadhi ya nyaraka muhimu katika majadala ya wastaafu.
(ii) Waajiri kuchelewa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazotakiwa kuthibitisha uhalali wa utumishi wa wahusika kabla ya mfuko kuanzishwa Julai, 1999.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Je, ni utaratibu gani unaotumika kukokotoa kodi katika forodha zetu zinazopokea bidhaa na vitu mbalimbali vinavyotokea Zanzibar, wakati vitu vilevile vinavyozalishwa Zanzibar ni vilevile vinavyotoka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini na ukokotoaji wa ushuru au kodi ya bidhaa mbalimbali kutoka nje, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazopitia Zanzibar kuja Bara, unafanywa kwa kutumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database. Mfumo huu unatunza kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka nje na kutumiwa na Mamlaka ya Mapato kama kielelezo na rejea wakati wa kufanya tathmini na ukokotoaji wa kodi au ushuru wa forodha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyaraka za bidhaa zinapowasilishwa Central Data Processing Office, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazotoka nje ya nchi kupitia Zanzibar, bei au thamani ya bidhaa husika huingizwa kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database, ili kuhakiki uhalali wa bidhaa na bei husika na kukokota kiwango cha kodi anachotakiwa kulipa mteja. Endapo bei au thamani ya bidhaa iliyopo kwenye nyaraka itakuwa chini ya ile iliyopo kwenye mfumo wa wetu, mfumo utachukua bei iliyopo kwenye database na kukokotoa kiwango halali cha kodi. Hata hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kusafirishwa kuja Tanzania Bara hazilipiwi kodi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Fedha za miradi ya maendeleo kutotolewa kwa wananchi kwa wakati jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara na miradi ya maendeleo kuchelewa kukamilika:-
Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Bunge lako Tukufu linavyofahamu, muundo wa bajeti yetu unavyopitishwa na Bunge, una vyanzo viwili vya mapato; mapato ya ndani na mapato kutoka nje. Wakati wa utekelezaji wa bajeti, kiwango cha mgao hutegemea zaidi mapato halisi kutoka vyanzo vyote viwili. Hivyo basi, mapato pungufu au chini ya malengo kutoka kwenye chanzo chochote kati ya hivyo vilivyotajwa, yataathiri mgao wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia pekee na muafaka ya kukabiliana na changamoto hiyo ni Serikali kuongeza mapato yake kutoka vyanzo vya ndani. Hatua kadhaa za kuongeza mapato ya ndani tayari zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na kubana na kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kuwa kila anayestahili kulipa kodi, analipa kodi stahiki na kupanua wigo wa kodi kwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuweka mazingira rafiki au wezeshi kwa mlipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la hatua hizi ni kuongeza mapato ya Serikali na hatimaye kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ambayo inaambatana na masharti kadhaa, baadhi yake yakileta usumbufu na hasara kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wanatambua hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli katika kudhibiti suala la kukwepa kodi na kuongeza mapato ya Serikali. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali yetu.
MHE. KHATIB SAID HAJI (K.n.y. KHAMIS MTUMWA ALI) aliuliza:-
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inafanya ukaguzi katika Taasisi za Tanzania Bara na Zanzibar:-
Je, Ofisi hii inashirikiana vipi wakati wa kufanya ukaguzi wa Taasisi za Muungano na Ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafanya ukaguzi katika Taasisi zote za Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 143 (2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977. Ibara hiyo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mamlaka ya kufanya ukaguzi wa hesabu za mihimili yote mitatu ya dola, Serikali, Bunge na Mahakama na kutoa ripoti ya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mipaka ya kufanya kazi baina ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Jukumu la ukaguzi wa Taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Wakati jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ni kukagua Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipaka hiyo ya kazi, kumekuwepo na ushirikiano katika kufanya ukaguzi wa pamoja kati ya Ofisi hizi kuu mbili kwa lengo la kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu. Kwa mfano ukaguzi wa ujenzi wa Ofisi za Wabunge kwenye Majimbo, ukaguzi wa bahari ya kina kirefu na mradi wa kupambana na UKIMWI Zanzibar. Ukaguzi wa miradi hii ulifanywa kwa ushirikiano wa pande zote mbili.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupunguza misamaha ya kodi kufikia asilimia moja (1%) ya GDP?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ya kupunguza misahama ya kodi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa ni mkakati unaotekelezwa kwa awamu na kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi, kijamii na sheria zilizopo. Juhudi za kutekeleza azma ya kupunguza misamaha ya kodi zilianza kufanyika mwaka 2010/2011 baada ya kubaini kuwa, kwa wastani misamaha yetu ilikuwa imefikia takribani asilimia 3.2 ya pato la Taifa kwa mwaka, katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hadi 2009/2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009/2010 Serikali iliamua kupitia upya sheria zinazohusu misamaha ya kodi ili kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija katika Taifa letu. Katika mapitio hayo Serikali ilibaini kuwa takribani asilimia 60 hadi asilimia 64 ya misamaha yote ya kodi ilikuwa inatokana na kodi ya ongezeko la thamani – VAT. Baada ya kubaini hali hiyo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya maboresho ya Sheria ya VAT, Sura ya 148 na kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa, hususan za kurekebisha upeo wa misamaha inayotolewa chini ya Kituo cha Uwekezaji – TIC na Sekta ya Madini, zimesaidia kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia 1.9 ya pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 kiasi cha kodi kilichosamehewa ni shilingi milioni 564,106.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwenendo huu ni matarajio yetu kuwa kiasi cha msamaha wa kodi katika Mwaka wa Fedha 2015/2016 kitakuwa ni shilingi milioni 752,141.9 sawa na asilimia 0.84 ya pato la Taifa. Kutungwa upya kwa Sheria ya VAT ni eneo moja ambalo limeleta ufanisi mkubwa katika kutimiza azma yetu ya kupunguza misamaha ya kodi, hadi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, baadhi ya misamaha ya kodi haiepukiki katika mifumo ya kodi hapa nchini na popote duniani. Suala la msingi ni kuwa Serikali itahakikisha kuwa misamaha yote ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria za Kodi zilizopo.
Katika siku za usoni usimamizi wa misamaha utajengwa katika mifumo imara ya udhibiti inayozingatia matumizi ya teknolojia. Lengo la muda mrefu ni kuweka mfumo wa misamaha ya kodi unaokubalika Kimataifa, pia misamaha hiyo iwe ni ile inayochochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Kwa miaka mingi sasa Tanzania Investment Bank na TADB imekuwepo ila mchango wake katika kupunguza umaskini haufahamiki zaidi hata kwa Waheshimiwa Wabunge. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Benki za TIB na TADB zinajielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa sababu ndiyo mkataba wa mpango kazi wa maendeleo ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Benki ya TIB na TADB kama benki za maendeleo ni kutoa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu kwa lengo la kufadhili miradi ya kimkakati. Katika kutimiza azma ya kufadhili miradi ya kimkakati ya kufungua fursa za kiuchumi na kupunguza umaskini, TIB imetoa mikopo katika maeneo yafuatayo:
Mradi wa Maendeleo ya Makazi (Temeke na Kinondoni); Mradi wa Maendeleo ya Miji kupitia NHC; Viwanda vya Kubangua Korosho; maghala; mabomba ya maji; sukari na kilimo cha miwa; kukoboa na kusindika kahawa; kusindika matunda; mifuko ya kuhifadhia mazao; nyaya za umeme; vinu vya pamba na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na mbegu za pamba; na mahoteli. TIB umewekeza katika mashirika ya umma kama vile Shirika la Reli (TRL), imeiwezesha TPDC katika mradi wa gesi na kuipatia TANESCO mkopo kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kuweka njia mpya ya kusafirisha umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwaka jana (2015), TIB imewawezesha Watanzania wengi kupambana na umaskini kwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 550 katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Katika sekta ya kilimo, TIB imewasaidia wananchi wengi kwa kusimamia mikopo iliyotolewa na Serikali kupitia Dirisha la Kilimo inayofikia shilingi bilioni 58.8 hadi mwishoni mwa mwaka 2015. Mikopo hii ilitolewa kupitia makampuni binafsi yapatayo 121, taasisi ndogo ndogo za fedha zipatazo 11 na SACCOs 78.
Mheshimiwa Naibu Spika, TIB pia imetoa mkopo wa shilingi bilioni 489.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 181 ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA na kaya 257,000 zimenufaika na mradi huo. Aidha, vikundi 17 vya wachimbaji wadogo wadogo vimenufaika na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya TIB kwa sekta na taasisi mbalimbali imesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira mpya na kuendeleza zilizopo. Pia mikopo ya TIB imetumika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje kama vile maua, kahawa na dhahabu. Pamoja na Benki ya Kilimo kuchelewa kuanza kutoa mikopo ni wazi kabisa kuwa Benki ya TIB imejielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kama vile Dira ya Taifa (2025), Mpango wa Pili wa Maendeleo na Maendeleo Endelevu 2020 pamoja na Ajenda ya Afrika 2063.
MHE. OMAR M. KIGUA aliuliza:-
Ulipaji kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya nchi kwa ajili ya maendeleo na Serikali inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na ili Serikali iweze kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ni lazima kuwe na Ofisi za TRA katika maeneo mbalimbali nchini:-
(a)Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Ofisi ya TRA katika Wilaya ya Kilindi?
(b)Kwa kutokuwa na Ofisi za TRA Serikali haioni kama inadhoofisha maendeleo ya Wilaya hususani katika suala la mapato?
(c)Kwa kuweka Ofisi za TRA Wilaya ya Handeni na kuacha Wilaya ya Kilindi, Serikali haioni kama inawajengea wananchi tabia ya kukwepa kulipa kodi kutokana na umbali uliopo kati ya Wilaya hizo mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufungua Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Wilayani Kilindi kama ilivyo katika Wilaya zingine. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina mpango wa kufungua ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Kilindi baada ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchambuzi wa kina kuhusu fursa za mapato ya kodi zilizopo katika Wilaya zote ambazo hazina ofisi za TRA.
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya ni fursa mojawapo ya kuleta maendeleo katika eneo husika. Aidha, uamuzi wa kufungua ofisi ya Mamlaka ya Mapato unazingatia zaidi gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato. Kwa msingi huo, Serikali haidhoofishi maendeleo ya Wilaya ya Kilindi isipokuwa ni lazima tufanye utafiti kwanza kubaini gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato kabla ya kufungua ofisi.
(c)Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Kigua kuwa uwepo wa ofisi za Mamlaka ya Mapato katika maeneo yetu unaongeza ari ya wananchi kulipa kodi kwa hiari. Napenda kutoa rai yangu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa mujibu wa sheria. Aidha, wananchi wasiache kulipa kodi kwa kutumia kisingizio cha maeneo yao kukosa ofisi za Mamlaka ya Mapato kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamevunja sheria na kuikosesha Serikali yao mapato ambayo yangetumika kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Benki ya Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao (wajasiriamali) kupata huduma iliyo bora kupitia benki yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na Mchango wa wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kufungua benki mpya za wafanyabiashara wakubwa na wadogo, isipokuwa inafanya jitihada za kuimarisha benki zake zilizopo ikiwemo Benki ya Kilimo na Benki ya Wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, ni vema tukaimarisha benki za Serikali zilizopo kwa sasa kuliko kuanzisha benki zingine. Tukianzisha benki mpya tutaipunguzia Serikali uwezo wa kifedha wa kuziimarisha benki zilizopo. Mfano, Benki ya Posta ni benki ya Serikali na imeenea nchi nzima kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu, hususani wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati. Kama Serikali, tutaimarisha benki hizi zilizopo na pia kuipa sekta binafsi fursa ya kuanzisha benki zaidi kwa kadri soko litakavyoruhusu, ni imani yetu kubwa kwamba wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo watapata huduma husika.
MHE. NEEMA W. MGAYA (K.n.y. MHE. SUSAN C. MGONOKULIMA) aliuliza:-
Mfumo wa mashine za EFDs hauchanganui kwa uwazi fedha ipi ni mapato ya kodi na ipi ni faini au ni gharama za uendeshaji:-
Je, ni lini kutakuwepo ushirikishwaji kati ya waandaaji mfumo wa TRA na viongozi wa wafanyabiashara ili kodi inayotozwa iwe halali na isiwe inayoua mitaji ya wafanyabiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Chogisasi Mgonokulima, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa matumizi ya mashine za kutunza hesabu za kodi za kielektroniki ulianzishwa kwa lengo la kurahisisha na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za biashara za walipa kodi. Mfumo wa EFD ulianzishwa ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya utunzaji kumbukumbu za mauzo na utoaji wa risiti za mauzo zinazoandikwa kwa mkono. Mfumo huu umerahisisha usimamizi na ukadiriaji wa kodi kwa kuwa kumbukumbu zote za mauzo na manunuzi huhifadhiwa na kutunzwa kirahisi kwenye mashine za EFD na taarifa za mauzo ya mlipa kodi hutumwa kwenye saver ya Mamlaka ya Mapato moja kwa moja kwa njia ya mtandao kupitia mashine husika ya EFD kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa EFD haukuundwa kwa ajili ya kutoa mchanganuo wa fedha kwa mapato ya kodi, faini au gharama za uendeshaji wa biashara. Mfumo wa EFD ni kwa ajili ya kutunza kumbukumbu sahihi za mauzo na manunuzi ya mfanyabiashara pamoja na kutoa risiti. Mchanganuo wa mapato ya kodi na gharama za uendeshaji hufanywa kwa njia ya kawaida ya kiuhasibu kwa kutumia kumbukumbu za mauzo na manunuzi ya biashara zinazotunzwa katika mashine za EFD.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu la kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali yanayotokana na kodi, ada, na tozo mbalimbali pamoja na kusimamia sheria zote za kodi zilizotungwa na kupitishwa na Bunge lako Tukufu. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango ina utaratibu wa kushirikisha wadau mbalimbali wakati wa maandalizi ya bajeti ambao hutoa michango yao na ushauri kwa kupitia kikosi kazi yaani task force kilicho chini ya Idara ya Sera ambacho kazi yake ni kuchanganua maoni na ushauri uliotolewa na kuainisha mambo muhimu ya kuingiza katika bajeti ya Taifa. Utaratibu huu hutoa fursa kwa viongozi wa wafanyabiashara na wengine kutoa maoni na ushauri ili ufanyiwe kazi na kuingizwa katika mipango ya Serikali. Hakuna kodi inayotozwa kwa nia ya kuua mitaji ya wafanyabiashara wetu, kwani kiwango cha juu cha kodi ya mapato ni asilimia 30 ya mapato baada ya kuondoa gharama za biashara yaani net profit. Pale ambapo mfanyabiashara hakupata faida, hakuna kodi ya mapato itakayotozwa. Hivyo basi, kodi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato ni halali na haziui mitaji ya wafanyabiashara wetu.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:-
Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii huko vijijini lakini pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mipango ya Serikali kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake waweze kupata mikopo, napenda ikumbukwe kwamba kufuatana na mabadiliko ya mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa tangu mwaka 1991, Serikali imejitoa katika kuhusika moja kwa moja na uendeshaji wa shughuli za benki na badala yake Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ili huduma hizi ziwafikie wananchi wengi. Kupitia Benki Kuu ya Tanzania, Serikali imefanya msukumo wa kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi ili kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi mijini na vijijini. Benki kadhaa zimeanzisha huduma za kibenki kupitia mawakala na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi ambazo zimewasaidia sana wananchi sehemu ambako hakuna matawi ya benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka mazingira wezeshi na taratibu rafiki ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha. Juhudi hizi zimesaidia wananchi kuanzisha benki za kijamii na taasisi ndogondogo za fedha katika maeneo yao. Ni matarajio ya Serikali kuwa wananchi watatumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuwekeza wao wenyewe au kuzishawishi benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao. Aidha, Serikali pia itaendelea kushawishi benki nchini kupanua shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikishirikiana na Benki Kuu ipo tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama. Benki Kuu kupitia Kurugenzi yake ya Utafiti na Uchumi ina mpango wa kuelimisha umma (consumer literacy program) kuhusu utumiaji wa huduma za kifedha nchini ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za kifedha ikiwemo taratibu zinazohusu mikopo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Kufuatia taarifa zilizotolewa na vyombo vya Serikali vinavyohusika na masuala ya utafiti na takwimu, Mkoa wa Kagera ulikuwa miongoni mwa mikoa mitano maskini ya mwisho Kitaifa.
(a) Je, ni mambo gani yametumika kama vigezo vya kuingiza Mkoa wa Kagera katika orodha ya mikoa mitano maskini Kitaifa?
(b) Je, ni jitihada gani za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kuunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vilivyotumika katika kubainisha Mikoa na Wilaya maskini ni uwezo wa kaya kukidhi mahitaji ya msingi kama vile chakula chenye kiwango cha kilo kalori 2,200 kwa siku, mavazi na malazi. Kwa kutumia vigezo hivi uchambuzi wa kina wa takwimu zilizotokana na utafiti wa mapato na matumizi katika kaya wa mwaka 2011/2012 na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ulibaini kuwa Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha umaskini wa asilimia 39.3.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini, Serikali inafanya jitihada na kuchukua hatua mbalimbali kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ifuatavyo:-
(i) Kuendeleza maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda kwa kujenga miundombinu ya msingi ili kuwezesha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vidogovidogo na vya kati katika Mkoa wa Kagera.
(ii) Kuendelea kuhamasisha wananchi wote ikiwemo Mkoa wa Kagera kutumia fursa na rasilimali mbalimbali zilizopo katika mikoa husika.
(iii) Kuendeleza Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo, utafiti, na masoko ya mazao.
(iv) Kukuza sekta ya viwanda, hususan vya kusindika mazao ya maliasili, kilimo na uvuvi.
(v) Kuendeleza viwanda vya nyama vilivyopo Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Kagera, viwanda hivyo vitasaidia kuendeleza ufugaji utakaoinua kipato cha mtu mmojammoja pamoja na kuendeleza uchumi wa mkoa husika.
(vi) Uendelezaji wa viwanda vya nguo katika mikoa inayozalisha pamba ambapo Kagera huzalisha kwa asilimia 2 ya pamba yote katika Ukanda wa Magharibi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE (K.n.y MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne ilikopa fedha kwenye Benki za Nje na zile za biashara kwa mfano mwaka 2011 Serikali ilikopa shilingi trilioni 15 na kufanya Deni la Taifa kufikia shilingi trilioni 21, kabla ya mwaka 2015 ilikopa tena kiasi cha shilingi trilioni 9 na kufanya Deni la Taifa kuongezeka kufikia shilingi trilioni 39.
(a) Je, mpaka sasa Deni la Taifa linafikia kiasi gani?
(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya makusudi ya kudhibiti ongezeko hilo la Deni la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara kiasi cha shilingi bilioni 1,333.28 na mwaka 2014/2015 Serikali ilipokea mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 2,291.6. Mikopo hiyo haikufikia kiasi cha trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni tisa kabla ya mwaka 2015 kama ilivyotafsiriwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Juni, 2016, Deni la Taifa lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 19.69 mwezi Juni, 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 20.5 na deni la sekta binafsi lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 2.7.
Aidha, deni la Serikali lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja nchini, mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu Chini na Ruvu Juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya makusudi kabisa ili kudhibiti ongezeko la deni hilo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa Pato la Taifa, kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa wakandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mikataba inayoweza kusababisha mzigo wa madeni kwa Serikali. Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini (sovereign rating) kwa lengo la kupata mikopo nafuu.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Serikali imeanzisha mfumo ambao wafanyabiashara wanapouza au kutoa huduma wanatoa risiti kupitia mashine za EFD na mfumo huu umeelekezwa na Sheria na Kanuni za kodi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu ambao utawezesha TRA kupata rekodi za moja kwa moja ambayo inapata kupitia mfumo wa EFDs kwa mauzo ya huduma ambayo yanafanyika kwa njia ya Electronic Commerce.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitunga Sheria na Kanuni za matumizi ya mashine za EFDs ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi za miamala ya mauzo ya kila siku kutoka kwa wafanyabiashara. Lengo ni kurahisisha ukokotoaji na ukadiriaji wa viwango vya kodi ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kuwa Serikali inapata kodi stahiki na mlipa kodi analipa kodi stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa matumizi ya EFDs unaiwezesha Mamlaka ya Mapato kupata taarifa zote za mauzo yanayofanyika ndani ya nchi, hata kama mauzo ya bidhaa au huduma yatakuwa yamefanyika kwa njia ya mitando (E- Commerce). Ili kufanikisha azma ya Serikali ya kupata takwimu sahihi za mauzo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na jitihada ya kuhakikisha wafanyabishara wote wenye sifa za kutumia mashine za EFDs wanafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za kiteknolojia, hususan teknolojia ya kufanya manunuzi kupitia mitandao. Hatua tunazochukua ni pamoja na kuongezea wafanyakazi wa mamlaka uwezo wa kukusanya kodi kwenye biashara zinazofanyika kwa njia ya mitandao. Aidha, mamlaka inaendelea kuingia kwenye makubaliano ya kubadilishana taarifa mbalimbali na taasisi na mashirika mbalimbali (Third Party Information) ili kuweza kupata taarifa za miamala ya mauzo, hususan zile zinazofanyika nje ya upeo wa kawaida tunaoweza kuona kupitia mitandao.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Zanzibar vipo vikundi vya VICOBA ambavyo usajili wake ni lazima waje Tanzania Bara kufanya usajili:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Ofisi Tanzania Zanzibar ili kuweka unafuu kwa wananchi wa Zanzibar?
(b) Je, gharama za usajili wa VICOBA ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, VICOBA ni vikundi ambavyo vimekuwa vikiundwa na wananchi ili kupambana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya kifedha, hususan wananchi wa kipato cha chini na wale waishio mbali na huduma rasmi za kifedha. Vikundi hivi kwa sehemu kubwa vimekuwa vikiundwa na kusimamiwa na taasisi zisizo za Serikali kama vile NGOs, CBOs na kadhalika. Kwa maana hiyo, taratibu za uratibu, uhamasishaji, usajili na malezi ya vikundi hivyo hufanywa na NGO‟s au CBO‟s.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mwongozo maalum kwa sasa kwa usajili wa vikundi vya VICOBA. Hivyo basi, baadhi ya vikundi vya VICOBA kutoka Zanzibar hufuata usajili Tanzania Bara ili kukidhi matakwa ya taasisi zinazowaongoza, hususan NGOs na CBOs. Aidha, kwa kutambua mchango mkubwa wa vikundi hivyo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na huduma za kifedha katika baadhi ya maeneo na makundi maalum, Serikali imetoa fursa kwa vikundi hivyo kusajiliwa BRELA pamoja na Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar Ofisi za Ushirika zinasajili VICOBA kama Vyama vya Kuweka na Kukopa vya Awali kwa makubaliano kwamba, VICOBA hivyo vitakua na hatimaye kubadilishwa kuwa SACCOS kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya marekebisho ya Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha na Sheria yake Tanzania Bara na Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha kule Zanzibar zinazotarajiwa kuweka mwongozo rasmi wa usajili wa VICOBA na uendeshaji wake. Mapendekezo ya marekebisho ya sera yanasubiri kupangiwa tarehe ya kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia sasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za usajili wa vikundi vya VICOBA zinatofautiana kutegemeana na mamlaka zinazowasajili. Mfano, ada ya usajili chini ya NGOs ni sh. 150,000 na Halmashauri za Wilaya ni kati ya sh. 30,000 na sh. 70,000. Viwango vya ada ya usajili chini ya Halmashauri za Wilaya vinatofautiana kwa kuwa hakuna mwongozo maalum, kama nilivyosema hapo awali, unaopaswa kuzingatiwa na Halmashauri zote.Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande wa BRELA ada za usajili zinatofautiana kulingana na mtaji wa kikundi husika. Mfano ada ya usajili kwa kikundi chenye mtaji usiozidi sh. 5,000,000 ni sh. 10,000; kati ya sh. 5,000,000 na 10,000,000 ni sh. 20,000 na kati ya sh. 10,000,000 na sh 50,000,000 ni sh. 50,000.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Wafanyabiashara wanaotoa bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara hutozwa kodi Zanzibar na wanapofika Tanzania Bara hutozwa kodi tena; vilevile, wafanyabiashara wanaotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, hutozwa kodi tena Zanzibar. Hali hii husababisha wafanyabiashara kushindwa kuendelea na biashara kwani wanatozwa kodi mara mbili:-
(a) Je, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na wa kudumu kutatua suala la wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara wanoingiza bidhaa za nje Tanzania Bara kupitia Zanzibar kwa sababu Tanzania Bara inatumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database, ambao hautumiki kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, Import Export Commodity Database ni mfumo unaoweka kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu ya bei za bidhaa mbalimbali zilizopo kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database hutumiwa kama msingi wakati wa kufanya tathmini ya kodi ya bidhaa zinazoingizwa nchini pale thamani ya bidhaa husika inapoonekana kuwa hailingani na hali halisi. Hivyo basi, tofauti ya kodi inayotokana na kutotumika kwa mfumo wa Import Export Commodity Database kuthamini kiwango cha kodi kwa upande wa Zanzibar hukusanywa Tanzania Bara ili kuweka mazingira sawa ya ushindani kibiashara kwa bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara.
Mpango wa muda mfupi, muda mrefu na wa kudumu wa kutatua changamoto ya wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili, ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuridhia matumizi ya mifumo ya uthaminishaji wa kodi inayotumika ndani ya Idara ya Forodha ili kuondoa tofauti zilizopo za ukadiriaji wa kodi kati ya sehemu mbili za nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itashawishi Benki za Biashara kuwekeza katika Jimbo la Mlalo ambalo mzunguko wa fedha ni mkubwa sana kutokana na magulio ya mboga mboga na matunda?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo huduma za kibenki katika sehemu zenye shughuli za kiuchumi kama kilimo cha mboga mboga na matunda kama Jimbo la Mlalo. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na miundombinu ya umeme ili kuchochea zaidi shughuli za uzalishaji na hatimaye kuvutia mabenki kufungua matawi sehemu hizo. Ikumbukwe kuwa uanzishaji wa huduma za kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia uwezo wa kupata faida pande zote mbili yaani benki na wananchi. Hii pia hutegemea na uchumi wa eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kuendesha mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991, Serikali imekuwa ikitekeleza azma ya kujitoa katika kuhusika moja kwa moja na biashara ya mabenki. Kwa hiyo, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha benki na kutoa huduma bora za kifedha kwa wananchi wetu, hususan pale ambapo huduma hizo zitaweza kujiendesha. Serikali inaendelea na ushauwishi wake wa Benki za Biashara na taasisi nyingine za fedha kuanzisha huduma za kibenki na kifedha popote ambapo kuna mzunguko mkubwa wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushawishi wa Serikali, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Serikali yetu, kuwashauri wananchi wa Mlalo kujiunga na kuanzisha Benki za Kijamii (Community Banks) na taasisi ndogo za kifedha (Micro Finance Institutions) zinazozingatia mazingira ya mahali husika ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya Jimboni Mlalo.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Wizara ya Fedha katika juhudi zake za kukusanya mapato ya Serikali, imeweka Sheria ya Kukusanya Kodi ya Magari inayoitwa Motor Vehicle au Road License. Kodi hiyo imekuwa ikilalamikiwa sana na wananchi kwa kuwa imekuwa ikidaiwa hata kwa magari mabovu au ambayo yamepaki kwa muda wote bila kujali kipindi ambacho gari lilikaa bila kufanya kazi:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuitazama upya sheria hii?
(b) Kwa kuwa kodi hudaiwa hata kipindi ambacho gari halifanyi kazi: Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo inawaibia wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya Motor vehicle Annual License inasimamiwa chini ya Sheria ya Road Traffic Act, 1973 pamoja na kanuni zake (The Road Traffic na Motor Vehicle Registration Regulations). Sheria hii imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara kulingana na mahitaji ya wakati husika. Kodi hii ni moja ya kodi zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini na kutoa huduma mbalimbali. Hivyo hatuwaibii wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa The Road Traffic Motor Vehicle Registration Regulations ya mwaka 2001, Sura ya Pili, Kifungu cha (4) na (5) hakuna msamaha wa leseni ya gari kwa mtu yeyote na inataka ada hiyo kulipwa kila mwaka tangu gari husika liliposajiliwa. Hivyo, sheria haitoi unafuu wowote kwa gari lililosimama kwa muda mrefu bila kutembea barabarani. Ni kweli utekelezaji wa sheria hii unaleta adha kwa wamiliki wa magari na hasa pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kwamba gari husika limesimama kwa muda mrefu na kwa sababu za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa adha hii, Mamlaka ya Mapato imeanza mchakato wa kuboresha sheria hii ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuhudumia wamiliki wa magari ambayo yatakuwa yamesimama kwa kipindi kirefu bila kutembea barabarani kwa sababu za msingi. Aidha, baada ya taratibu zote kukamilika, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hii yataletwa Bungeni ili kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa kadri itakavyoonekana inafaa.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inasema kuwa idadi ya watu katika Jimbo la Lindi Mjini ni takribani 78,000, lakini takwimu za watu waliojiandikisha NIDA inafika 100,000 na sensa iliyofanywa kupitia Serikali za Mitaa inaonyesha kuwa wakazi wa Lindi Mjini ni zaidi ya 200,000 na Serikali inaendelea kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kutumia takwimu za watu 78,000 hivyo kuathiri huduma stahiki za maendeleo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuangalia upya takwimu hizo ili wananchi wa Lindi Mjini wapelekewe huduma za maendeleo stahiki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watu kwa Manispaa ya Lindi (Jimbo la Lindi Mjini) ilikuwa ni watu wapatao 78,841. Kwa madhumuni ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, eneo la Manispaa ya Lindi ni lile linalojumuisha kata 18 za Ndoro, Makonde, Mikumbi, Mitandi, Rahaleo, Mwenge, Matopeni, Wailes, Nachingwea, Rasbura, Matanda, Jamhuru, Msinjahili, Mingoyo, Ng’apa, Tandangongoro, Chikonji na Mbanja. Hivyo basi, tunapozungumzia idadi ya watu 78,841 tuna maana ya idadi ya watu katika kata nilizozitaja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilitoa makadirio ya idadi ya wapiga kura kwa kila jimbo hapa nchini. Katika makadirio hayo, Jimbo la Lindi Mjini linakadiriwa kuwa na wapiga kura 47,356. Katika zoezi hilo hilo la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo ilikadiriwa kuwa Jimbo la Lindi Mjini lina wapiga kura wapatao 42,620. Makadirio haya yalizingatia idadi ya watu kwa Lindi Mjini kama ilivyotolewa na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, Jimbo la Lindi lilionyesha kuwa na wapiga kura 48,850 idadi ambayo ni karibu sawa na ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Matokeo haya yanadhihirisha usahihi wa takwimu za sense zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya watu wapatao 100,000 waliojiandikisha NIDA ni kwa Wilaya nzima ya Lindi, ambayo inajumuisha Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na sio Manispaa ya Lindi au Jimbo la Lindi Mjini pekee kama ilivyohojiwa katika swali la msingi la Mheshimiwa Hassan Kaunje.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Matumizi ya dola katika maeneo mengi nchini ndiyo sababu kubwa ya kushuka kwa thamani ya fedha yetu:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha matumizi ya fedha yetu kwa wananchi wake pamoja na wageni nchini ili kukuza thamani ya fedha yetu na maendeleo ya nchi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakari, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo hapa nchini na hakuna sarafu nyingine yoyote iliyowahi kuidhinishwa kisheria kutumika kwa malipo hapa nchini badala ya shilingi. Hakuna sababu ya kuhamasisha matumizi ya shilingi kwa sababu Watanzania wote wanajua fedha halali kwa malipo ni shilingi na si vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanyika mwaka 2013 ulionesha kuwa, malipo ambayo hufanyika kwa dola ya Marekani hapa Tanzania ni asilimia 0.1 tu ya malipo yote na haya hufanyika zaidi katika maeneo yanayohusisha wageni kama vile mahoteli ya kitalii, mashirika ya ndege, shule za kimataifa na nyumba za kupanga kwenye baadhi ya maeneo mijini. Sababu mojawapo ya maeneo haya kuwa na bei kwa dola ya Kimarekani ni kurahisisha uelewa wa bei hizo kwa wageni na kuwarahisishia malipo. Pamoja na mambo mengine malipo kwa fedha za kigeni yanachangia upatikanaji wa fedha za kigeni hususani pale wazawa wanapouza bidhaa na huduma kwa wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya dola nchini Tanzania siyo sababu kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu. Mfano, wakati Tanzania haijafanya mabadiliko yoyote katika kanuni ya fedha za kigeni tangu mwaka 1992 thamani ya shilingi ilikuwa ikishuka na kupanda kama zilivyo thamani za sarafu nyingine duniani. Aidha, kutokea mwezi Desemba, 2011 hadi Desemba, 2014 thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilikuwa imara zaidi ya sarafu nyingine za washirika wetu kibiashara kama vile Rand ya Afrika ya Kusini, Yen ya Japan, Euro ya Jumuiya ya Ulaya na Paundi ya Uingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kuu zinazopelekea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni ni tofauti ya mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi tunazofanya nazo biashara. Nakisi ya biashara ya nje ya bidhaa na huduma ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiuchumi duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kanuni zilizotokana na sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na tamko la Serikali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni la mwaka 2007, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo. Aidha, Benki Kuu ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya fedha za kigeni ambapo miamala yote ya fedha za kigeni inatakiwa kuoneshwa. Pia, Benki Kuu imechukua hatua za kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na mabenki ni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, kidiplomasia na kijamii pekee.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Moja kati ya jukumu la Benki Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 51(2)(a) cha Sheria ya Benki Kuu, 2016 ni kutunza dhahabu safi.
Je, kwa nini Serikali imekataa kutunza dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha dhahabu safi na kwa wingi Afrika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa. Ili kufanikisha azma hii, Benki Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali zikiwemo kuuza dhamana na hati fungani za Serikali na kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki ambayo ni Interbank Foreign Exchange Market.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne. Hazina ya rasilimali za kigeni inaweza kuwa dhahabu-fedha yaani monetary gold au fedha za kigeni. Uamuzi kuhusu hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha yaani convertibility na faida inayopatikana kwa kuwekeza hazina hiyo.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu kwa muda mrefu haijaweka dhahabu kama sehemu ya hazina ya rasilimali za kigeni kutokana na bei ya dhahabu katika soko la dunia kutokuwa tulivu na hivyo kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina ya rasilimali ya nchi. Mfano, tumeshuhudia bei ya dhahabu ikishuka kutoka dola 1,745 za Kimarekani kwa wakia moja Septemba, 2012 hadi dola za Kimarekani 1,068 Disemba 2015. Aidha, ununuzi na uuzaji wa dhahabu unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki Kuu ambalo tumelieleza hapo juu, Benki Kuu haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya dhahabu.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Riba kubwa katika benki zetu nchini imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake na vijana kupata mikopo.
(a) Je, Serikali ipo tayari kuandaa utaratibu maalum wa riba elekezi itakayowawezesha wanawake na vijana kupata mikopo benki kwa riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuziagiza benki za biashara kulegeza masharti ya dhamana kwa vijana na wanawake ambayo yanarefusha mchakato wa upatikanaji wa mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye kipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha nchini ya mwaka 1991, Serikali iliruhusu benki binafsi kutoa huduma za kibenki hapa nchini kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma hizo zilikuwa zinatolewa na vyombo vya fedha vya Serikali tu. Hatua hii ilikusudia kuongeza ushindani katika sekta ya fedha na kuhakikisha kwamba huduma za kibenki zinatolewa kwa ufanisi na kwa kutegemea nguvu na mfumo wa soko huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maombi mbalimbali juu ya kupunguza viwango vya riba ikiwa ni pamoja na Benki Kuu kuweka ukomo wa riba au riba elekezi ya mikopo. Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Benki Kuu imepewa dhamana ya kusimamia sekta ya fedha na usimamizi wa mabenki hapa nchini. Kama msimamizi wa mabenki, Benki Kuu kuweka ukomo wa riba sio tu inapingana na jukumu lake la msingi la kusimamia mabenki hayo, bali pia inapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria. Kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, Benki Kuu haina mamlaka kisheria ya kuweka ukomo au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya riba katika mabenki na taasisi nyingine za kifedha hupangwa kwa kutegemea nguvu ya soko, sifa za mkopaji, ushindani katika soko, gharama za upatikanaji wa fedha, mwenendo wa riba za dhamana za Serikali, gharama za uendeshaji na matarajio ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Benki Kuu imeendelea na jukumu lake la msingi la kuhakikisha kuwa mfumo huu unaendeshwa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ili kulinda maslahi ya Taifa na uchumi kwa kusimamia na kudhibiti mambo yafuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa ingezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko kuhakikisha kuwa ongezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei;
(ii) Ongezeko la mikopo ya mabenki haliathiri uzalishaji mali na linalingana na malengo ya ujazi wa fedha;
(iii) Soko la dhamana za Serikali linaendeshwa kwa ufanisi ili liweze kutoa riba elekezi kulingana na hali ya soko na uchumi kwa ujumla; na
(iv) Mwisho kuhimiza mabenki na taasisi zote za fedha kutumia takwimu za Credit Reference Bureau.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Kituo cha Biashara cha Taifa - Tanzania Trade Center kilichopo London, Uingereza kimeripotiwa kuwa kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kukiendesha na kulipa watumishi wake kutokana na kukosa fedha kutoka Hazina jambo ambalo linasababisha kuzorota kwa kazi za kituo hicho na kukabiliwa na mzigo mzito wa madeni.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza hali ya kituo hicho kwa sasa ikoje?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hali ya kifedha na kiutendaji ya kituo hicho ambacho kimesaidia sana kutangaza Tanzania nje ya nchi inakuwa imara na kufanya kazi zake kwa ufanisi?
(c)Je, ni kiasi gani cha fedha kinachodaiwa na kituo hicho na watu mbalimbali nchini Uingereza na hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Biashara cha London kilianzishwa mwezi Oktoba, 1989 kufuatia uamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais mwaka 1989. Lengo la kituo hicho lilikuwa ni kuhamasisha biashara baina ya Tanzania na nchi za Ulaya, hususan Uingereza kwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji na kuvutia wawekezaji kutoka Tanzania na Ulaya kuchangamkia fursa hizo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwake kituo kimefanikiwa sana katika kutekeleza majukumu yake licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zitokanazo na ufinyu wa bajeti na upungufu wa rasilimali watu. Changamoto hizo zimefanya kituo hicho kushindwa kuendana na kasi inayotakiwa ya mabadiliko duniani yanayotokana na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya uenezaji wa taarifa na habari ulimwenguni. Ili kulinda heshima ya Taifa na watumishi waliokuwepo katika kituo hicho, Serikali imeamua kukifunga rasmi kituo hicho na kuhamisha majukumu yake kutekelezwa na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Mjini London.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo kimefungwa na majukumu yake kutekelezwa na Ofisi yetu ya Ubalozi Mjini London, Serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya Ubalozi wetu ili kukidhi majukumu ya ziada yaliyoongezeka.
(d) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Novemba, 2016 Wizara ilipokea na kulipa deni la jumla ya shilingi 129,896,360 kutoka kituo hicho cha London ikiwa ni madai ya pango, maji, simu, umeme na gharama za kufunga kituo hicho.
MHE. ENG.ATASHASTA J.NDITIYE aliuliza:-
Nchi yetu bado ina upungufu mkubwa sana wa sukari na kwa kuwa Wilayani Kibondo kuna ardhi oevu kwenye Bonde la Mto Malagarasi na Lupungu ipatayo ekari 52,000 na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kwa matumizi ya ardhi hiyo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta mwekezaji wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuwa katika Nchi yetu kuna upungufu wa sukari kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge. Viwanda vyetu vyote kwa pamoja vina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari ya mezani na hakuna uzalishaji wa sukari ya viwandani ilihali mahitahi ya Sukari kwa matumizi ya nyumbani na viwandani ikikadiriwa kuwa tani 610,000 hivyo uhitaji wa uwekezaji katika sekta hiyo ya viwanda vya sukari ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa upungufu huo, Serikali imeshatambua na inaendelea kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Mara, Pwani, Songwe na Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bonde la Mto Malagarasi lililopita katika vijiji kumi vya Kasaya, Kibuye, Kigina, Kukinama, Kumsenga, Kumshwabure, Magarama, Nyakasanda, Nyalulanga na Nyarugusu ni moja ya maeneo ambayo Serikali imeyaainisha kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari. Tayari Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa kushirikiana na Wananchi na Kampuni ya Green Field Plantations imefanya vikao vya uhamasishaji katika vijiji vyote kumi na hivi karibuni wataanza taratibu za upimaji wa ardhi. Mradi huu utahusisha jumla ya hekta 25,000 sawa na ekari 61,776 ambapo Kampuni ya Green Field Plantations italima hekta 20,000 na itawasaidia wakulima wadogo pembejeo na teknolojia ili waweze kulima hekta 5,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimshukuru Mheshimiwa Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Kibongo kwani barua walizotuma Wizarani ziliongeza kasi hii, tuendelee kushirikiana.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:-
Miradi mingi ya maendeleo inashindwa kumalizika kwa wakati kutokana
na Serikali Kuu kutokuleta fedha za miradi kwa wakati:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa wakati kwenye Halmashauri ili miradi
ya maendeleo itekelezwe kwa kipindi kilichopangwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, Mbunge
wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa
kutumia fedha za makusanyo ya ndani, mikopo ya ndani na nje, misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo pamoja na makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapato ya fedha za ndani (tax revenues and
non tax revenues) hupelekwa katika Wizara, taasisi na idara mbalimbali za Serikali
pamoja na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka
katika kila chanzo. Aidha, asilimia 60 ya makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa hubakishwa katika Halmashauri husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha
za mikopo ya ndani au nje, pamoja na fedha za washirika wa maendeleo, fedha
hizo hupelekwa kwenye Halmashauri zetu mara tu zinapopatikana. Hivyo basi,
uhakika wa mtiririko wa fedha kutoka vyanzo vyote vya mapato ndiyo msingi wa
kupeleka fedha kwenye Halmashauri zetu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu Waheshimiwa Wabunge
kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani katika Halmashauri zetu kupanga
mipango stahiki, kuainisha vyanzo vya mapato na kusimamia ukusanyaji na
matumizi ya mapato hayo ipasavyo ili kuziwezesha Halmashauri zetu kujenga
uwezo wa kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo
kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza
utakatishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanya nchi
nyingi duniani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa
Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za
kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza
usimamizi katika maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambapo taarifa za kila
muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa. Hatua
zimechukuliwa pia kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa
na mabenki ni ile inayohusu shughuli za kiuchumi tu ili kulinda thamani ya shilingi
yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tamko na mwongozo uliotolewa na
Serikali mwaka 2007, ulieleza kuwa bidhaa na huduma zinazowalenga watalii au
wateja wasio wakazi wa Tanzania, bei zake zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili
yaani shilingi ya kitanzania na sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa sarafu
ambayo mlipaji atakuwa nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe
kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni
hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali yetu ili
kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni. Mfano,
kufikia Desemba, 2015 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni
4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za
Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi
cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, utulivu wa urari wa biashara ya nje umetokana
na sera huru ya fedha za kigeni ambayo imechangia kuimarisha uchumi kwa
zaidi ya miaka 10 iliyopita. Wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita ulikuwa ni asilimia saba ikiwa ni wastani wa juu sana
ikilinganishwa na nchi zingine duniani. Mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 5.4 katika kipindi hicho, wakati
ule wa nchi zinazoibukia kiuchumi ulikuwa ni asilimia 5.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia zinazotumika kutakatisha fedha ni pamoja
na kuziingiza fedha haramu kwenye taasisi za fedha na kuziwekeza katika
rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya mambo yanayowapatia
wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, rushwa,
ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi na kadhalika. Fedha zinazotokana na shughuli
za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za Kitanzania, dola za Kimarekani au fedha
nyingine yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya
fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu
na siyo dola tu. Benki Kuu kupitia jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha
hufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Kuna ongezeko kubwa la maduka ya kucheza kamari yanayotaitwa Jack Pot katika miji nchini ikiwemo Dodoma; maduka hayo huchezesha kamari mchana na usiku na wateja wengi ni vijana ambao hutumia mbinu mbalimbali kupata fedha ndani ya familia ili wakacheze kamari hali ambayo husababisha uvunjifu wa maadili:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mchezo wa kamari ambao huwakosesha amani wazazi na jamii nzima?
(b) Je, Serikali haoni kuwa kuna uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana inapotea kwa kucheza kamari badala ya kushiriki katika uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo yote ya kubahatisha ikiwemo kamari inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na kanuni zake. Kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka zingine za biashara. Pia, sheria inakataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote atakayeruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo wa kubahatisha anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa faini ya sh. 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja. Aidha, endapo kosa hili litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria ya kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Hata hivyo, natoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia vijana wao kucheza michezo ya kubahatisha pale wanapoona kuwa uchezaji wao unakuwa na matokeo hasi.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya kubahatisha ni moja ya shughuli za kiuchumi inayoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli nyingine zozote. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, wote wanaoendesha michezo ya kubahatisha wanazingatia sheria na kanuni zilizowekwa. Pili, ni wajibu wetu kama wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa vijana wetu wanazingatia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania pindi wanapokuwa wanajishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya wananchi, watumishi wa umma na wafanyabiashara juu ya riba kubwa inayotozwa na benki zetu kwa wale wanaochukua mikopo hali ambayo inarudisha nyuma juhudi zao za kupunguza umaskini na kwa kuwa Benki Kuu ndiyo inayosimamia mabenki yote nchini.
(a) Je, ni lini Serikali kwa kupitia benki zetu nchini itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia 10% -12% badala ya riba ya sasa ambayo ni 17% - 20%?
(b) Kwa kuwa mikopo inayotolewa kwa watumishi wa umma ni salama zaidi kwa mabenki, je, benki hizo haziwezi kuweka riba maalum?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki. Viwango vya riba za mikopo na riba za amana, pamoja na riba za mikopo kati ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo, pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Serikali haina mamlaka kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo. Aidha, kwa sehemu kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.
Pili, ni muhimu kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa juu, ndivyo riba za amana zinapokuwa juu pia. Mfano; wastani wa riba za kukopa kwa mwaka mmoja mwezi Juni, 2016 ulikuwa ni asilimia 13.67 wakati wastani wa riba za amana za mwaka mmoja ulikuwa ni asilimia 11.52 ikiwa ni tofauti ya asilimia 2.25
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na wachongaji wa vinyago hasa pale wanunuzi wa vinyago hivyo kutoka nje wanaponyang’anywa bidhaa hiyo wafikapo airport kwa madai mbalimbali ikiwemo kutolipa kodi.
(a) Je, vinyago hivyo ambavyo ni biashara ya wanyonge baada ya kuzuiliwa hupelekwa wapi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kufanya hivyo kunawapotezea wateja na soko kwa wanaofanya ujasiriamali wa aina hiyo lakini pia kuwaingizia hasara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, vinyago sio miongoni mwa bidhaa zinazotozwa kodi au ushuru kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi. Ikiwa vinyago vilizuiliwa uwanja wa ndege au mpakani, sio kwa sababu ya kutolipiwa kodi au ushuru wa forodha. Utaratibu unaotumika kimataifa ikiwemo nchi yetu katika kushughulikia bidhaa zozote zinazokamatwa kwenye sehemu za kuingia au kutokea nje ya nchi kama viwanja vya ndege na mipakani ni wa aina mbili:-
Moja, kuziharibu au kuziteketeza bidhaa hizo au kuzipiga mnada. Bidhaa zinazoharibiwa au kuteketezwa ni zile ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi au kwa afya ya binadamu, kwa mfano, silaha, vyakula au kemikali zilizobainika kuwa si rafiki kwa matumizi ya binadamu na mazingira. Bidhaa nyingine ambazo haziangukii kwenye kundi hilo, ikiwa ni pamoja na vinyago hupigwa mnada na baada ya kuondoa gharama zozote za uhifadhi, mapato yake huingizwa Serikalini. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Tauhida halijabainisha ni lini na ni wapi vinyago hivyo vilikamatwa, idadi yake au taasisi au mamlaka ipi ilikamata vinyago hivyo ni vigumu kueleza vinyango hivyo vilipelekwa wapi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia vinyago au bidhaa nyingine yoyote inaposafirishwa nje ya nchi, hufanyika tu baada ya kubainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria na kanuni. Kwa hiyo, lengo la kufanya hivyo ni kujiridhisha kuwa wadau wote wa biashara au bidhaa hiyo wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili asiwepo yeyote mwenye kupoteza mapato yanayotokana na biashara au bidhaa hiyo ikiwemo Serikali yetu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. JAMAL KASSIM ALI) Aliuliza:-
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2013 zilikubaliana kuwa kodi ya PAYE kwa wafanyakazi wa Serikali na Taasisi zote za SMT ambao wanafanyakazi Zanzibar kodi yao ya PAYE ikusanywe na TRA Zanzibar na kuiwasilisha kwa SMZ.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa kufanya hivyo kwa kampuni zote binafsi ambazo zina matawi/ofisi Zanzibar kulipia Corporate Tax ambayo kutokana na faida inayotokana na shughuli zao za biashara ndani ya Zanzibar ili kodi hiyo iende kusaidia masuala ya maendeleo kwa
wananchi wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 66, kifungu cha 4 sehemu ya (a) na (b); Kodi ya Kampuni (Corporation Tax) ni kodi ya Muungano na inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kikatiba kodi zote za Muungano zinakusanywa na TRA. Hata hivyo, kampuni ambayo imesajiliwa Tanzania Bara na ikawa na matawi Zanzibar inatakiwa kulipa kodi ya kampuni TRA Bara. Iwapo kampuni imesajiliwa Zanzibar na ikawa na matawi Tanzania Bara inatakiwa kulipa Kodi ya Kampuni Zanzibar. Kwa msingi huo, Kodi ya Kampuni inatozwa sehemu ambapo kampuni imesajiliwa, yaani Tanzania Bara au Zanzibar.
MHE. DEO F. NGALAWA Aliuliza:-
Shirika la Posta Tanzania lilitumia fedha zake kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kulirejeshea Shirika hilo fedha hizo ili kulinusuru?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Shirika la Posta Tanzania lilitumia fedha zake kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki na kuwasilisha madai Serikalini ili lipate kurejeshewa fedha zake. Hadi sasa Shirika limelipa shilingi bilioni 5.9 na Serikali imesharejesha shilingi bilioni 2.7 kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, Novemba, 2016 Serikali ilirejesha Shilingi milioni 700; Desemba, 2016 Shilingi 1,000,000,000; na Januari, 2017, Serikali ilirejesha Shilingi 1,000,000,000. Aidha, Serikali itaendelea kurejesha kiasi kilichobaki cha Shilingi 3,200,000,000 kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Msajili wa Hazina inaendelea na jukumu la kuwalipa pensheni ya kila mwezi wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki wapatao 292.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE Aliuliza:-
Waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven ya Arusha hawajalipwa mafao yao hadi sasa:-
Je ni lini watalipwa mafao yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven - Arusha wapato 238 waliachishwa kazi mwaka 2000 na kulipwa mafao yao kwa mujibu wa taratibu na sheria. Katika zoezi la ulipaji wa mafao ya wafanyakazi hao, Serikali kupitia iliyokuwa PSRC ilitoa na kulipa kiasi cha shilingi 217,366,296 mwezi Januari, 2000 kama mafao ya wafanyakazi hao. Baada ya malipo hayo watumishi hao waliwasilisha malalamiko kuwa wamepunjwa. PSRC ilihakiki madai hayo na baada ya kujiridhisha mwezi Agosti, 2000 Serikali ilitoa idhini ya kulipa tena kiasi cha shilingili 273,816,703 kugharamia mapunjo ya mishahara na mafao ya wafanyakazi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, wafanyakazi hao tayari walishalipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria na taratibu na hawastahili kudai malipo yoyote ya nyongeza.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) lililokuwa na matawi karibu nchi nzima na assets mbalimbali lilibinafsishwa kutokana na sera ya ubinasfishaji.
(a) Je, ni matawi mangapi yamebinafsishwa na mangapi yamebaki mikononi mwa Serikali?
(b) Je, Serikali imepata fedha kiasi gani kutokana na ubinafsishaji huo?
(c) Kati ya matawi yaliyobinafsishwa ni mangapi yanaendeshwa kwa ubia wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye vipengele (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Idadi ya matawi ya Shirika la Taifa la Usagishaji yaliyobinafsishwa ni 22 na yaliyobaki mikononi mwa Serikali ni matano;
(b) Katika kubinafsisha mali za NMC Serikali imepata fedha kiasi cha shilingi 7,491,611,000; na
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matawi yaliyobaki hakuna tawi linaloendeshwa kwa ubia kati ya Serikali na mwekezaji. Matawi hayo kwa sasa yanasimamiwa na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko. Hata hivyo, tawi la NMC - Arusha maarufu kama Unga Limited limekodishwa kwa Kampuni ya Monaban Trading Company Limited.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:-
Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianza rasmi shughuli zake mwishoni mwa mwaka 2015. Hadi kufikia Desemba 2016, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilikuwa imeshatoa mikopo ya jumla ya Sh. 6,489,521,120/= kwa miradi 20 ya kilimo katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Sambamba na utoaji wa mikopo, benki inatoa mafunzo kwa wakulima na hadi sasa imeshafanya mafunzo kwa vikundi 336 vya wakulima wadogo wadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, Benki imepata nafasi kwa ajili ya kufungua ofisi katika jengo jipya la PSPF ambapo inasubiri kukabidhiwa ofisi hiyo Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi. Aidha, benki imeshaanza kutafuta miradi ya kilimo ya wakulima wadogo wadogo yenye sifa za kukopesheka iliyopo katika Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha azma hii, benki imemwandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kumwomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo. Pamoja na hayo, benki inaandaa utaratibu wa mafunzo yatakayotolewa kwa wakulima wadogo wadogo nchi nzima ikianzia na Mkoa wa Dodoma. Ni matumaini ya benki kuwa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo na wakati kwenye Mkoa wa Dodoma itaanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2017.
MHE. JULIUS K. LAIZER (K.n.y MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) aliuliza:-
Wilaya ya Siha ina changamoto ya upungufu wa ardhi jambo ambalo limesababisha wananchi kushindwa kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi na pia kuendeleza makazi yao katika maeneo hatarish.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwagawia wananchi mashamba yaliyoko chini ya Hazina kama vile mashamba ya Foster, Journey’s End na Harlington ili wananchi wayatumie kwa kilimo ikizingatiwa kuwa wananchi Kata ya Nchimeta Ngarenairobi wanaishi kwenye maporomoko hatarishi hasa wakati wa mvua na majanga ya moto?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga ardhi
kwa ajili ya ufugaji kwa wananchi wa Siha ambao kwa sasa hawana maeneo ya malisho kwa mifugo yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Siha, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mwaka 2007 Serikali ilitoa maelekezo ya kusitisha uuzaji wa mashamba ambayo yalikuwa hayajabinafsishwa yakiwemo mashamba ya Forester, Journey’s End, Harlington na Kanamodo yaliyopo NAFCO, West Kilimanjaro. Serikali ilisitisha zoezi la uuzaji wa mashamba hayo baada ya wananchi wa Siha pamoja na Uongozi wa Wilaya na Mkoa kupinga zoezi la ubinafsishaji wa mashamba na kupendekeza mashamba hayo yagawiwe kwa wananchi. Serikali ilikubaliana na maoni ya wananchi na hivyo kumtafuta Mtaalam Mwelekezi kufanya utafiti na matumizi bora ya mashamba hayo.
Mheshimiwa Spika, tathmini ilifanyika na mapendekezo yalikuwa kama ifuatavyo:-
(i) Kuyagawa mashamba hayo katika mashamba madogo madogo kwa ajili ya shughuli za kilimo cha mazao na ufugaji kwa wakulima wadogo na wa kati na kisha kuyauza kwa njia ya zabuni; na
(ii) Baadhi ya maeneo kukabidhiwa kwa Halmashauri
ya Wilaya ya Siha kwa shughuli za maendeleo ikiwemo makazi, shule, vyuo, hospitali na magereza.
Mheshimiwa Spika, kwa kutilia maanani mapendekezo ya mtaalam mwelekezi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilielekezwa kuandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wenye mapendekezo ya namna bora ya matumizi ya mashamba hayo. Waraka huo ulishawasilishwa na kufikia ngazi ya Makatibu Wakuu na kutolewa maoni kwa ajili ya marekebisho.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha marekebisho, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itauwasilisha waraka huo kwenye Baraza la Mawaziri. Baada ya kujiridhisha na mapendekezo na ushauri, Serikali itatoa uamuzi kuhusu matumizi ya mashamba husika.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kukamilisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Waheshimiwa Wabunge, sisi ni sehemu ya Baraza la Madiwani katika maeneo yetu, hivyo tunapaswa kusimamia maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha kuwa wafugaji na wakulima wanatengewa maeneo yao. Tuhakikishe kila kundi linatengewa maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi. Hapo tutakuwa tumeandaa msingi bora wa maendeleo ya kiuchumi kwa watu wetu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Kila mwaka Bunge limekuwa likipitisha Bajeti ya Serikali kuhusu Wizara, Mikoa na Wilaya lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususan katika Mikoa na Wilaya na kupelekea miradi mingi kutokamilika.
Je, ni sababu gani za msingi zinazofanya Serikali kuchelewa kuleta fedha za Miradi ya Maendeleo katika Mikoa na Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa utaoji wa fedha
za utekelezaji wa Bajeti ya Serikali hutegemea mapato ya Serikali kupitia ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo vya kodi na visivyo vya kodi, mikopo pamoja na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Katika miaka ya hivi karibuni, mwenendo wa upatikanaji wa mapato ya Serikali umekuwa na changamoto nyingi katika miezi ya mwanzo wa mwaka wa fedha ambapo mikopo ya masharti ya biashara kutoka kwenye taasisi za fedha pamoja na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo imekuwa haipatikani kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, sababu kuu zinazochangia kutopatikana kwa wakati kwa fedha hizo ni pamoja na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu, baadhi ya washirika wa maendeleo kutotimiza ahadi zao kutokana na sababu mbalimbali na kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha la kimataifa.
Mheshimiwa Spika, fedha zinazokusanywa kutokana
na vyanzo vya mapato ya ndani zimekuwa zikielekezwa kugharamia matumizi mengine yasiyoepukika kama vile ulipaji wa mishahara, deni la taifa, ulipaji wa madeni ya watumishi, watoa huduma, wazabuni na wakandarasi pamoja na utekelezaji wa miradi yenye vyanzo mahususi kama vile Taasisi ya Umeme Vijijini, Mamlaka ya Elimu Tanzania, Mfuko wa Barabara, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Mfuko wa Maji na Mfuko wa Reli.
Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya fedha za miradi
ya maendeleo katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa hutumia fedha za nje. Utoaji wa fedha hizo kutoka kwa washirika wa maendeleo huzingatia mpango kazi, masharti na vigezo mbalimbali vilivyowekwa ambavyo hupaswa kuzingatiwa na mamlaka zinazotekeleza miradi.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa miradi
ya maendeleo inatekelezwa badala ya kutegemea fedha za nje ambazo uhakika wake umekuwa hautabiriki, Serikali imeendelea kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hadi kufikia shilingi bilioni 8,702.7 kwa mwaka 2016/2017 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,366.1 mwaka 2010/2011. Aidha, Serikali yetu imeendelea kuboresha vyanzo vya ndani vya Halmashauri na kuzijengea uwezo zaidi kwa kukusanya mapato ili kutekeleza miradi mingi kwa fedha za ndani badala ya fedha za nje.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR aliuliza:-
Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Je, ni kwa nini plate number za vyombo vya moto ambazo ni za Tanzania Bara hazitumiki au haziruhusiwi Zanzibar, na ni kosa ambalo linatozwa faini ya shilingi 300,000?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usalama Barabarani ambayo husimamia usajili wa vyombo vya moto siyo sheria ya Muungano. Kwa upande wa Tanzania Bara usajili wa vyombo vya moto unasimiwa na Sheria ya The Road Traffic Act ya mwaka 1973 na Kanuni ziitwazo The Traffic Foreign Vehicles Rule za mwaka 1973. Kwa upande wa Tanzania Bara sheria hizi zinasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa upande wa Tanzania Zanzibar usajili wa vyombo vya moto unasimamiwa na Sheria ya The Road Transport Act namba 7 ya mwaka 2003. Majukumu ya usajili wa vyombo vya moto Zanzibar husimamiwa na Bodi ya Mapato Zanzibar tangu mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto Tanzania Zanzibar (The Road Transport Act No. 7) ya mwaka 2003, chini ya kifungu cha 43, magari yasiyosajiliwa Zanzibar hutumika Zanzibar bila kufanyiwa usajili upya wa siku 90 pale ambapo magari hayo yanakibali cha kukaa na kutumika Zanzibar. Hata hivyo, baada ya kupita muda wa siku 90, mmiliki wa magari hayo hutakiwa kuomba kusajili magari yao kwa namba za Tanzania Zanzibar au kuomba muda zaidi wa kutumika Zanzibar bila usajili wa Tanzania Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya kifungu cha 201 cha
The Road Transport Act Namba 7 ya mwaka 2003, mmiliki wa chombo cha moto akishindwa kusajili chombo cha moto baada ya siku 90 na kushindwa kuomba kuongezewa muda wa kutumia gari bila usajili, anakuwa amefanya kosa na faini yake ni dola za kimarekani 50 au shilingi zenye thamani ya dola hizi, na siyo shilingi 300,000.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Electronic Fiscal Device (EFD) risiti hazidumu kwa muda mrefu kwani zinafutika maandishi ndani ya muda mfupi.
Je, TRA wataridhika na maelezo ya mlipakodi bila ushahidi wa risiti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali kulikuwa na tatizo la matumizi ya risiti za EFD bila maelekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wafanyabiashara kutumia risiti ambazo zinafutika au zinadumu kwa muda mfupi. Hata hivyo, baada ya kubaini tatizo hilo, TRA ilitoa maelekezo kwa watumiaji wote wa mashine za EFD kununua na kutumia karatasi zilizoidhinishwa na Mamlaka ambazo hudumu kwa muda mrefu, takribani miaka mitano. Pili, TRA imeidhinisha waagizaji wa karatasi zenye sifa ili kuondokana na tatizo la karatasi zisizo na kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto tunayokabiliana nayo ya baadhi ya wafanyabiashara kutumia karatasi zinazofutika au kudumu kwa muda mfupi, TRA inaweza kufuatilia na kubaini kumbukumbu za mteja kutoka kwenye server iliyopo TRA na hivyo kurahisisha uhakiki wa stakabadhi, ama iliyofutika au kupotea. Hivyo basi, endapo risiti ya mtumiaji wa mashine za EFD itafutika au kupotea, ushahidi wa muamala uliofanywa na mteja kwa kutumia mashine za EFD utapatikana kwenye server kuu iliyopo TRA.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali ilitangaza kuzinyang’anya halmashauri uwezo wa kukusanya mapato ya kodi majengo (property tax) na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kupewa jukumu hilo.
(a) Baada ya TRA kupewa jukumu hilo je, ufanisi umefikiwa kwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na halmashauri?
(b) Kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za miji, manispaa na majiji na majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi hayajapunguzwa; Je, Serikali imejipangaje kufidia vyanzo hivyo vilivyopotea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimia Cecilia Daniel Paresso, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali haijazinyang’anya Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato yake hususan kodi ya majengo na badala yake imebadilisha na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo. Mamlaka ya Mapato Tanzania ndiyo yenye jukumu kuu kisheria la kukusanya mapato ya Serikali. Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399 kifungu cha 5(1), Waziri wa Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kuikabidhi TRA jukumu lolote linalohusu ukusanyaji wa mapato yoyote kama atakavyoona inafaa kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA ilianza rasmi kukusanya kodi ya majengo kwa halmashauri 30 kati ya 183 kuanzia Oktoba, 2016 baada ya tangazo la Serikali Na. 276 kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali tarehe 30 Septemba, 2016. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2016, Halmashauri zote zilielekezwa kuendelea kukusanya kodi ya majengo wakati TRA ikikamilisha taratibu za kisheria na kimfumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho cha Julai, hadi Septemba, 2016, halmashauri 30 ziliweza kukusanya shilingi milioni 3,399 ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya lengo la kukusanya milioni 14,502. Ufanisi huu ni sawa na na wastani a shilingi milioni 1,133 kwa mwezi. Aidha, katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2016 hadi Aprili, 2017 jumla ya Shilingi milioni 10,652.6 zilikusanya sawa na ufanisi wa asilimia 22 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 48,340.2 katika kipindi husika. Ufanisi huu ni sawa na wastani wa makusanyo ya shilingi milioni 1,521.8 kwa mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi ni wazi kwamba TRA imekusanya kodi ya majengo kwa ufanisi zaidi ikilinganishwa na halmashauri. Ufanisi wa TRA unatarajiwa kuongezeka kwa makusanyo ya mwezi Mei na Juni, 2017 baada ya mifumo yote kukamilika ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kupata elimu na kuitikia wito wa kulipa kodi ya majengo kwa hiari kwa tarehe za mwisho wa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna fidia inayotolewa au itakayotolea na Serikali Kuu badala yake halmashauri zitarejeshewa makusanyo ya kodi ya majengo kulingana na nakisi ya bajeti ya halmahsauri husika. Kwa mantiki hiyo, kodi ya majengo itaendelea kuwa ni chanzo cha mapato ya halmashauri na Serikali kwa ujumla kwa mujibu wa sheria na kwamba chanzo hicho hakijapotea bali mfumo wa ukusanyaji umebadilishwa na kuboreshwa.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii, pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma
ya benki vijijini ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mageuzi ya Pili ya Mfumo wa Sekta ya Fedha (Second Generation Financial Sector Reforms) Benki Kuu ilipewa jukumu la kusimamia uundwaji wa muundo wa utoaji elimu ya masuala ya fedha nchini. Muundo huu ulikamilika mwaka 2015 na kuzinduliwa mwaka 2016 mwezi wa pili na una maeneo makuu matatu ambayo ni mkakati wa elimu ya fedha, ikijumuisha makundi maalum, aina ya elimu na namna itakavyotolewa, mfumo wa usimamizi wa utoaji elimu na namna ya kupima utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu ya fedha inahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Taasisi zake, Benki Kuu inaratibu uanzishwaji wa Taasisi ya Kitaifa itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kuwezesha na kusimamia utoaji wa elimu ya fedha. Baada ya kuunda Taasisi ya Kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha, kutakuwepo na mfumo rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama wa vijijini.
Hata hivyo, taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu ya fedha kwa wateja wao wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha biashara zao kwa ufanisi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao. Pia Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kifedha nchini kuanzia mwaka 1991 Serikali ilijitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki. Uanzishwaji wa huduma za kibenki unafanywa kwa sehemu kubwa na sekta binafsi na hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia uwepo wa faida kwa pande zote mbili, yaani benki na wananchi na hii hutegemea vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na hali ya uchumi wa eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua pia mabenki mengi huendesha shughuli zake mijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kibenki. Kwa kuzingatia hilo, Serikali inajitahidi kuboresha miundombinu kama vile teknolojia ya mawasiliano, barabara, ulinzi, umeme na maji katika maeneo ya vijijini, ili kuweka mazingira bora yatakayovutia wawekezaji katika sekta binafsi kupanua huduma za kibenki kwenye maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imetoa Mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki. Utaratibu huu wa Uwakala unapanua wigo wa huduma za kibenki ili kuwezesha huduma hii ya kibenki kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa gharama nafuu, hasa katika maeneo ya vijijini. Aidha, mabenki yameshaanza kuweka mawakala maeneo mbalimbali na wananchi wa maeneo husika wameshaanza kufaidi huduma za kibenki zinazotolewa na Wakala wa Huduma za Kibenki.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Bunge lilipitisha Mpango wa Maendeleo na katika utekelezaji wake kasi ya Serikali kukopa imekuwa kubwa na bila shaka matokeo yake ni kuongezeka kwa Deni la Taifa:-
(a) Je, Serikali inaweza kuliambia Bunge hili ni kiasi gani kimekopwa hadi sasa ndani na nje ya nchi?
(b) Je, Serikali inajipangaje kulipa deni hilo pamoja na deni ambalo tayari lipo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo (2016/2017 – 2020/2021) ulipitishwa na Bunge lako Tukufu na kuidhinishwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Juni, 2016. Serikali ilianza utekelezaji wa mpango huo mwezi Julai, 2017.
Katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, Serikali ilitarajia kukopa jumla ya shilingi bilioni 9,653 kutoka katika soko la ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 5,374.30 zilitarajiwa kukopwa kutoka soko la ndani shilingi bilioni 2,177.8 mikopo yenye masharti nafuu na shilingi bilioni 2,101.0 ni mikopo ya masharti ya kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi 31, 2017, Serikali ilifanikiwa kukopa jumla ya shilingi bilioni 6,893.4 sawa na asilimia 71.4 ya lengo la kukopa shilingi bilioni 9,653.0. Kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 4,715.6 zilikopwa kutoka soko la ndani na shilingi bilioni 2,177.8 ni mikopo nafuu kutoka nje. Aidha, hatukuweza kukopa kutoka katika chanzo cha masharti ya kibiashara katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na takwimu hizi napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, si kweli kwamba tangu tupitishe Mpango wa Maendeleo Juni, 2016 kasi ya kuongezeka kwa Deni la Taifa imekuwa kubwa. Hata hivyo, hatuwezi kupima kasi ya ongezeko la Deni la Taifa ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, madeni yote ya Serikali yakijumuisha mtaji pamoja na riba yanalipwa kupitia mfumo wa kawaida wa bajeti ya Serikali. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilitenga shilingi bilioni 4,866.3 kwa ajili ya kulipa mtaji na riba ya deni la ndani na shilingi bilioni 1,586.6 kwa ajili ya kulipa mtaji na riba ya deni la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi 31,2017, shilingi bilioni 3,657.74 zilitumika kulipa mtaji wa deni la ndani, shilingi bilioni 796.16 zilitumika kulipa riba ya deni la ndani, shilingi bilioni 766.02 zilitumika kulipa mtaji wa deni la nje na shilingi bilioni 436.56 zilitumika kulipa riba ya deni la nje. Hadi sasa Serikali inahudumia au kulipa deni lake (ndani na nje) kwa mujibu wa masharti ya mikopo husika na kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 7,830.0 kwa ajili ya kuhudumia deni la Serikali litakaloiva kati ya Julai, 2017 na Juni 2018. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 5,973.8 zimetengwa kwa ajili ya deni la ndani na shilingi bilioni 1,856.1 ni kwa ajili ya deni la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, kutafuta mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na hivyo kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linaendelea kuhudumiwa kwa wakati na kwa mujibu wa masharti, sheria, kanuni na taratibu za mikopo.
MHE. KHAMIS MTUMWA ALI aliuliza:-
Taasisi za Muungano zinafanyiwa ukaguzi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Je, ni mara ngapi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeshirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukagua Taasisi za Ubalozi zilizoko nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo majukumu ya ofisi hii yameainishwa katika Ibara ya 143(2) ya Katiba hiyo, ambayo inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali, Bunge na Mahakama. Aidha, majukumu hayo pia yameanishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 na Kanuni zake za mwaka 2009.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi wa Balozi unafanyika chini ya Fungu 34, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kwa kuwa na Ofisi zote za Ubalozi ni sehemu ya Fungu 34. Hivyo basi, ukaguzi wa Balozi kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Muungano unafanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar majukumu yake yameanishwa kwenye Ibara ya 112(3) ya Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984. Kutokana na maelezo hayo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kila moja ina mipaka yake ya kufanya ukaguzi. Jukumu la ukaguzi wa taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kumhusisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ukaguzi wa Balozi au ukaguzi wowote ule kama wa Umoja wa Mataifa kwa sababu hakuna ulazima wa kufanya hivyo kikatiba na kisheria. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kusaidia sekta binafsi hasa wajasiriamali wadogo ili waweze kujiajiri, lakini tatizo kubwa la wajasiriamali hao katika sekta ya binafsi Tanzania ni tozo kubwa ya riba inayotolewa na benki hapa nchini kuwa kubwa kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki.
(a) Licha ya Tanzania kuwa na benki nyingi zaidi kuliko nchi zote Kusini na Mashariki mwa Afrika, je, kwa nini wingi huo bado haujaleta unafuu katika tozo ya riba?
(b) Je, kwa nini Serikali isiweke ukomo wa riba kisheria kwa benki hizi ili kumsaidia mjasiriamali wa sekta binafsi Tanzania kama ilivyofanya nchi ya Kenya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalisababisha Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki. Viwango vvya riba za mikopo hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, gharama ya bima, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya uhitaji na utoaji wa mikopo (demand and supply theory) si kigezo pekee kinachoweza kupunguza viwango vya riba hapa nchini. Hatari ya kutolipa mkopo ni kigezo kikubwa kinachotumiwa na benki kupanga viwango vya riba za mikopo hususan kwa wajasiriamali wadogo. Uzoefu uliopo sasa unaonesha kuwa benki zinapendelea kukopesha wajasiriamali waliojiunga katika vikundi kuliko mjasiriamali mmoja mmoja ili kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanzidata ya mikopo (credit reference bureau) ina umuhimu mkubwa katika kuwatambua wakopaji kwa kuwa huhifadhi historia na sifa za wakopaji. Kwa sehemu kubwa, historia na sifa za wafanyabiashara wakubwa zinapatikana kutoka kwenye kanzidata ya mikopo. Hivyo basi wafanyabishara wakubwa wanaaminika na kupata mikopo kwa riba nafuu ikilinganishwa na wajasiliamali wadogo kwa sababu taarifa na sifa zao zinapatikana kirahisi.
Kwa kuwa wajasiriamali walio wengi taarifa zao hazipo kwenye kanzidata ya mikopo, ni vigumu benki kuwatambua, kuwaamini na kuwapa mikopo kwa riba nafuu. Pia kiwango cha mikopo mibovu kwa wajasiliamali wadogo ni kikubwa ikilinganishwa na makundi mengine.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya mwaka 1991 iliyotungwa kwa kuzingatia misingi ya mfumo wa soko huria, Benki Kuu imepewa jukumu na mamlaka ya kusimamia na kuzichukulia hatua taasisi za fedha zinazoendesha shughuli zao kwa hasara. Kutoa maelekezo kwa benki kutumia viwango fulani vya riba, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuzichukulia benki hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na benki katika kutoa mikopo kwa wajasiliamali.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kurekebisha Road Licence au ifutwe ili ukusanyaji wa kodi hii uendane na matumizi halisi ya vyombo vya moto vya barabarani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphel Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ada ya mwaka ya magari inatozwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ambapo mmiliki wa chombo cha moto hutakiwa kulipa ada ya kila mwaka kuanzia tarehe ya mwezi ya kwanza ambao chombo kilisajiliwa. Ada hii inatozwa kulingana na ukubwa wa injini ya chombo husika. Msingi wa tozo hii ni umiliki wa chombo na siyo matumizi ya chombo barabarani. Hivyo basi, mmiliki wa chombo hutakiwa kulipa ada hiyo bila kujali kama chombo kimetumika katika mwaka husika au hakijatumika.
Mheshimiwa Spika, ada ya mwaka ya umiliki wa chombo cha moto inaweza kusitishwa kulipwa endapo mmiliki wa chombo cha moto atatoa taarifa kwa Kamishna wa Kodi na kuthibitishwa kuwa chombo hicho cha moto hakitumiki tena kutokana na sababu mbalimbali kama ajali ya barabarani, moto au uchakavu. Taarifa hizo za chombo husika zitawezesha chombo kufutwa (deregistered) kwenye kumbukumbu za mamalaka na ada hiyo itasitishwa kutozwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea mapendekezo na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Chegeni wakitaka ada hii ifutwe au ilipwe kulingana na matumizi ya chombo cha moto.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itafanya mapitio ya sheria na kanuni ya umiliki na matumizi ya vyombo vya moto ili kupata njia bora zaidi ya kukusanya ada hii, hivyo basi ada hii kwa sasa itaendelea kulipwa kwa utaratibu uliopo.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazopoteza fedha nyingi kwa ajili ya misamaha ya kodi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kigezo cha kuvutia wawekezaji na katika hotuba ya Bajeti 2013/2014 ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Mheshimiwa William Mgimwa alisema misamaha ya kodi kwa mwaka 2011/2012 ilifikia asilimia 4.3 ya pato la Taifa:-
(a) Je, hali ya misamaha ya kodi ikoje kwa sasa ikilinganishwa na ile ya mwaka 2011/2012?
(b) Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mwaka 2009/2010 Tanzania ilipoteza asilimia 15 ya pato lililotarajiwa kukusanywa iwapo misamaha isingetolewa, 2010/2011 asilimia nane na kwa mwaka wa 2011/2012 asilimia 27; je hali ya misamaha ikoje kuanzia mwaka 2013/2014 hadi sasa.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali hutolewa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi zilizopo. Baadhi ya huduma zinazotolewa katika jamii hazistahili kulipiwa kodi kwa sababu hazina manufaa ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mashirika ya Dini yanapata misamaha ya kodi kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 2014, sehemu ya pili ya jedwali kifungu cha nane (8), kwa sababu huduma zinazotolewa na taasisi hizo hazina faida ya kibiashara kama ilivyo kwa kampuni za kibiashara. Pamoja na hatua nzuri zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza misamaha ya kodi, ni vyema ikafahamika kwamba si kila msamaha wa kodi una madhara hasi katika jamii na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi kama sehemu
ya asilimia ya Pato la Taifa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013/2014 hadi sasa imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka. Misamaha hiyo ilikuwa asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2013/2014; asilimia 1.9 ya Pato la Taifa mwaka wa 2014/15; na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa katika mwaka wa 2015/16. Aidha, misamaha ya kodi ikilinganishwa na mapato ya kodi imepungua kutoka asilimia 18 ya mwaka 2013/2014 hadi kufikia asilimia 8.6 ya mapato yote ya kodi katika mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaendelea kupitia Sheria, Kanuni na Taratibu za misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha kuwa misamaha yote isiyokuwa na tija inafutwa na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza mapato kwa ajili ya kupeleka huduma za maendeleo kwa wananchi wetu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wastaafu ambao wakati wa utumishi wao walilitumikia Taifa hili kwa uaminifu na uadilifu mkubwa lakini kumekuwa na hali ya kucheleweshewa mafao yao ya uzeeni yasiyolingana na kupanda kwa gharama za maisha, hali inayosababisha kuwa na maisha magumu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko hayo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mafao ya kustaafu hukokotolewa kwa kutumia muda wa utumishi ambao mtumishi alikuwa katika utumishi na mshahara ambao mtumishi alikuwa analipwa kabla ya tarehe ya kustaafu. Ukokotoaji huo ndiyo unaotoa kiwango cha kiinua mgongo anachostahili kulipwa kwa mkupuo na kiwango cha pensheni atakachoendelea kulipwa kila mwezi. Kwa utaratibu huo, viwango vya pensheni hutofautiana kati ya mstaafu mmoja na mwingine kutegemea muda wake wa utumishi na mshahara kabla ya tarehe kustaafu. Iwapo katika ukokotoaji, itajitokeza pensheni ya mstaafu kuwa chini ya kima cha chini cha kiwango cha pensheni anacholipwa, mstaafu atalipwa kima cha chini cha pensheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni ili kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku ya wastaafu. Kwa kutambua hivyo, Serikali iliboresha viwango vya pensheni mwezi Julai 2015 ambapo kima cha chini kiliongezwa kutoka shilingi 50,114 hadi shilingi 100,125 kwa mwezi. Hata hivyo, maboresho ya viwango vya pensheni kwa wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya wastaafu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba mapato ya Serikali ni madogo ikilinganishwa na mahitaji muhimu ya kitaifa. Kwa kutambua kuwa ni miaka miwili tu tangu tuongeze kima cha chini cha pensheni, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya na elimu. Maeneo haya yana uhitaji mkubwa sana wa rasilimali fedha. Aidha, matokeo mtawanyiko ya maboresho ya maeneo haya yanaleta unafuu mkubwa wa maisha ya wastaafu wetu na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inafanya juhudi za makusudi za kuboresha mifumo ya kukusanya mapato sambamba na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kujenga uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza ya pensheni kwa wastaafu, mishahara na maslahi mazuri kwa watumishi wa umma itawezekana tu kama tutafanikisha mikakati na azma ya Serikali ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Hivyo basi, tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao ndiyo msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kumetokana na kuruhusu kutoza bidhaa mbalimbali na huduma kwa dola na kuathiri thamani ya fedha yetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani za kuimarisha shilingi yetu na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi hakutokani na kuruhusu bidhaa mbalimbali na huduma kutozwa kwa dola, bali hutokana na misingi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi (Micro Economic Fundamentals) na hali halisi ya uchumi wa nchi tunazofanyanazo biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi kunaweza kusababishwa na mambo makuu yafuatayo:-
(i) Nakisi ya urari wa biashara; nakisi ya urari wa biashara ya nje ya nchi (balance of payments) husababisha sarafu kushuka thamani kama mauzo ya bidhaa nje ya nchi ni madogo ikilinganishwa na ununuzi wa bidhaa kutoka nje. hali hiyo, hufanya thamani ya shilingi kushuka kwa sababu mahitaji yetu ya fedha za kigeni ni makubwa kuliko mapato ya mauzo yetu nje ya nchi.
(ii) Mfumuko wa bei; pamoja na mambo mengine mfumuko wa bei husababishwa na ongezeko kubwa la ujazo wa fedha kuliko uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali katika nchi. Aidha, thamani ya fedha hupungua iwapo mfumuko wa bei wa ndani ni mkubwa kuliko mfumuko wa bei katika nchi tunazofanyanazo biashara ni za nje ya nchi.
(iii) Tofauti ya misimu (seasonal factors); upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na biashara za msimu husababisha kusesereka au kutoserereka kwa shilingi ya Tanzania. Kwa mfano, mapato mengi ya fedha za kigeni kutikana na biashara ya nje huongezeka wakati wa nusu ya pili ya kila mwaka yaani kati ya Julai na Disemba, ikiwa ni kipindi cha mavuno na kilele cha utalii hivyo, thamani ya shilingi huimarika au kuwa na utulivu zaidi katika kipindi kati ya Julai na Disemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria ya kutotumia kabisa fedha za kigeni nchini Afrika ya Kusini, lakini sarafu ya nchi hiyo imapatwa na misukosuko mikubwa zaidi ya shilingi ya Tanzania. Hata thamani ya sarafu nyingine kubwa duniani kama vile Yen ya Japan, Renminbi ya China na Euro zimekuwa zikiyumba kwa kasi zaidi ya shilingi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha thamani ya shilingi Benki Kuu inaendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ili usitofautiane sana na wabia wetu wa biashara. Pia Benki Kuu imedhibiti biashara ya maoteo (speculation) katika soko la fedha za kigeni, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na sio biashara ya maoteo. Hali hii itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni katika soko la rejareja na hivyo kupunguza shinikizo la kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema ikaeleweka kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu, ufumbuzi wa kudumu wa kutengemaa kwa thamani ya shilingi hutegemea zaidi kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje. Hii itawezekana tu endapo tutaongeza uzalishaji na kuwa na ziada ya kuongeza mauzo yetu nje ya nchi na pia kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma zisizo za msingi kutoka nje.
MHE. MATHAYO D. MATHAYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuongeza ukwasi katika benki na kwa wananchi wa kawaida ili washirikiane na Serikali katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuimarisha uchumi na kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei, Benki Kuu hutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kudhibiti ukwasi ili uendane na mahitaji halisi ya uchumi. Kati ya Julai, 2016 na Julai, 2017 kiwango cha ukwasi katika mabenki kwa ujumla wake kiliongezeka kutoka asilimia 35.53 hadi asilimia 38.41 kwa mtiririko huo. Kiwango cha ukwasi wa asilimia 38.41 ni kizuri zaidi katika uchumi ikilinganishwa na kiwango cha chini cha asilimia 20 kinachotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuimarika kwa ukwasi kwa mwaka 2017 kunatokana na hatua mbalimbali za kisera zinazochukuliwa na Benki Kuu. Miongoni mwa hatua hizo ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki, kununua fedha za kigeni katika soko la jumla la fedha za kigeni (Interbank Foreign Exchange Market) na kushusha riba inayotozwa kwa benki za biashara na Serikali wanapokopa Benki Kuu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 mwezi Machi, 2017 na kutoka asilimia 12 hadi asilimia tisa mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kushusha kiwango cha sehemu ya amana ambayo mabenki yanatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 10 hadi asilimia Nane (8) kuanzia mwezi Aprili, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu, hali ya ukwasi katika sekta ya fedha, hususan benki ni nzuri na hakuna vihatarishi vya kuleta madhara hasi katika uchumi wetu. Aidha, Benki Kuu itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha masoko ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kwamba, yanaendeshwa kwa ufanisi na ushindani na hivyo kusaidia kuongeza ukwasi miongoni mwa mabenki na taasisi nyingine za kifedha.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha maeneo ya uendeshaji na usimamizi wa rasilimali ya Menejimenti, Bodi, Mabaraza ya Madiwani, Ukaguzi wa Nje, Ukaguzi wa Ndani na kuliacha eneo muhimu la Kamati za Ukaguzi (Audit Committee) kwenye Wizara, Idara, Wakala na Serikali za Mitaa.
Je, ni lini Serikali itaboresha Kanuni ili muundo wa Kamati za Ukaguzi ziundwe na Wajumbe wengi (majority) toka nje ya taasisi kuzingatia weledi na uzoefu ili kusimamia rasilimali kwa tija na ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uanzishaji wa Kamati za Ukaguzi umetajwa katika Kanuni za Fedha za Umma za mwaka 2001 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004 ambapo inaelezwa ya kwamba Kamati za Ukaguzi ziundwe na wajumbe watano; kati ya hao, mjumbe mmoja atoke nje ya taasisi. Aidha, kati ya wajumbe hao wa Kamati za Ukaguzi anatakiwa angalau mjumbe mmoja awe na uzoefu katika masuala ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mwaka 2013 Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa Mwongozo wa Utendaji Kazi wa Kamati za Ukaguzi katika taasisi za umma kuhusu idadi ya wajumbe kutoka nje ya taasisi kuwa wajumbe wawili au zaidi wateuliwe kutoka nje ya taasisi; mwongozo huo unawaelekeza Maafisa Masuuli kuwa wanaweza kuteua wajumbe kutoka nje ya taasisi kuanzia wajumbe wawili au zaidi. Hata hivyo, Wizara ya Fedha na Mipango inapitia upya Sheria ya Fedha za Umma na Kanuni zake ili tuweze kuwa na muundo mpya na huru wa Kamati za ukaguzi ili kuleta ufanisi.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitangaza kuzinyang’anya Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato ya kodi ya majengo (property tax) na kuagiza kodi hiyo kukusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).
(i) Je, baada ya Mamlaka ya Mapato kupewa jukumu hilo, ufanisi umefanikiwa kwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na Halmashauri zenyewe?
(ii) Kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji na majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi hayajapunguzwa. Je, Serikali imejipanga vipi kufidia vyanzo hivyo vilivyopotea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa (The Local Government Finance Act, Cap. 290) kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 na kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania jukumu la kukusanya kodi ya umiliki wa majengo yaani (property tax) kwa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30. Ufanisi wa Mamlaka ya Mapato ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yaliyokuwa yakisimamiwa na TRA yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 kwa mwaka 2015/2016 zilizokusanywa na Serikali za Mitaa hadi shilingi bilioni 34. 09 kwa mwaka 2016/2017 kipindi ambacho TRA ilianza kukusanya kodi hii. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 20.6 ya makusanyo ya Halmashauri husika kabla ya kodi hii kuhamishiwa TRA.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma za jamii. Hata hivyo, hatua ya Serikali ya kuhamishia jukumu hilo la ukusanyaji wa kodi za majengo TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali kuimarisha ukusanyaji wake. Takwimu nilizotoa hapo juu zinadhihirisha kuwa TRA imefanya vema katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kibajeti ambao unaziwezesha Halmashauri kupata fedha za makusanyo ya kodi ya majengo iliyokusanywa na TRA ili kuziwezesha kutimiza majukumu yao. Utaratibu uliopo ni kwamba Halmashauri zinatakiwa kuomba fedha hizo kutoka Serikali kuu kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao. Kwa mantiki hiyo, Halmashauri zinashauriwa kuzingatia utaraibu huo ili ziweze kupata fedha hizo.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliolipwa pesheni ni wale waliofungua kesi mahakamani na kushinda. Aidha, wapo ambao wanastahili malipo lakini hawakuwa na uwezo wa kumlipa Wakili katika kuendesha kesi hiyo.
Je, ni lini Serikali itawalipa wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki madai ya pesheni zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wiziri ya Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Mashariki waliolipwa pesheni ni wale tu waliofungua kesi mahakamani. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba tarehe 31 Disemba, 1990 Serikali ilisitisha mfuko wa ujulikanao kama East Africa Non Countributory Pension Scheme baada ya kushauriana na kukubaliana na Menejimenti pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baada ya kusitishwa kwa mfuko huo kila mfanyakazi alilipwa asilimia 50 ya michango yake na asilimia 50 iliyobaki ilipelekwa NSSF kwa ajili ya pesheni ya kila mwezi pindi watakapostaafu. Ni vema ikafahamika kwamba, wafanyakazi wote wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanalipwa pesheni zao na NSSF baada ya kustaafu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, baada ya malipo ya asilimia 50 kwa 50 kukamilika, wafanyakazi 254 hawakuridhika na maamuzi ya Serikali ya kusitisha mfuko wa East African Non Countributory Pension Scheme na kufungua kesi Na. 69/ 2005 Mahakama Kuu kupinga maamuzi ya Serikali. Katika shauri hilo, Mahakama Kuu iliamua kuwa uamuzi wa Serikali kusitisha mfuko huo haukuwa sahihi kisheria na hivyo wafanyakazi 254 waliokuwa katika shauri hilo walipwe madai yao ambayo yalijumuisha malipo ya mkupuo, riba pamoja na pensheni ya kila mwezi ya wafanyakazi hao.
Mheshimiwa Spika, baada ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu, Hati ya Makubaliano (Deed of Settlement) yenye tuzo ya shilingi 13,685,450,397.82 ilisainiwa mnamo tarehe 27 Agosti, 2013 na kusajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam mnamo tarehe 2 Agosti, 2013 ikiwa ni tuzo kwa wafanyakazi wote waliofungua shauri husika. Aidha, mahakama ilielekeza kuwa wadai katika kesi hiyo ambao bado wako kazini malipo yao yatafanyika mara baada ya kustaafu. Kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano malipo yaligawanywa katika awamu tatu ambapo hadi kufikia Julai 2017 awamu zote tatu zimelipwa jumla ya shilingi 12,665,994,447.92.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa wastaafu 245 wameshalipwa madai yao yote ya fedha za mkupuo ambapo kati yao wastaafu 54 wamefariki dunia na fedha zao walilipwa warithi na wastaafu 198 wanaendelea kulipwa malipo ya nyongeza ya pensheni ya kila mwezi. Kwa upande wa wadai ambao bado wapo kazini amebaki mmoja na wengine wawili wamestaafu hivi karibuni na tunatarajia kuwaombea fedha zao mwezi huu wa Novemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi huo, lilijitokeza kundi lingine la wastaafu wa TTCL waliokuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki likiongozwa na Bwana L. Mwayela na wenzake 324 na kuomba kuunganishwa katika Deed of Settlement ya kesi Na 69/2005 kati ya Bwana Berekia G. Mkwama na wenzake 254 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa kuwa Mahakama Kuu iliamua pamoja na mambo mengine kuwa wafanyakazi waliofungua kesi hiyo ndiyo walipwe madai yao na kwamba Deed of Settlement iliyosajiliwa Mahakamani ilihusisha wafanyakazi waliofungua kesi hiyo tu, wafanyakazi wengine ambao hawakuwa sehemu ya kesi hiyo hawawezi kulipwa kwa kutumia hukumu na tuzo ya kesi ambayo hawakuwa sehemu yake. Kwa msingi huo, Serikali haiwezi kulipa madai mengine ambayo hayajathibitika kisheria.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:-
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeifutia The Federal Bank of the Middle East (FBME) leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki na kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi kuanzia tarehe 8/5/2017.
Je, ni nini hatma ya wateja ambao waliweka fedha zao katika benki yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatma ya wateja endapo benki au taasisi ya fedha itawekwa chini ya ufilisi imeainishwa katika kifungu namba 39(2) na (3) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006. Wateja wa FBME Bank Limited ambayo sasa hivi ipo katika ufilisi watalipwa kwa utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza ni malipo ya fidia ya bima ya amana. Kwa mujibu wa sheria, mteja mwenye amana katika benki anastahili kulipwa fidia ya bima ya amana, kiasi kisichozidi shilingi za Tanzania 1,500,000 kutegemeana na kiasi cha salio la amana yake wakati benki inafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za kulipa fidia hiyo zinatoka katika Mfuko wa Bima ya Amana (Deposit Insurance Fund) unaosimamiwa na Bodi ya Bima ya Amana. Wateja waliokuwa na amana zisizozidi kiwango cha juu cha fidia cha shilingi 1,500,000 wakati benki inafungwa watapata fedha zote. Aidha, wateja wenye amana zinazozidi kiwango cha juu cha fidia watalipwa shilingi 1,500,000 kwanza kutoka mfuko wa bima ya amana na salio litalipwa kwa mujibu wa Sheria ya Ufilisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni malipo kwa wateja ambao fidia ya bima ya amana itakuwa ndogo ikilinganishwa na salio la amana yake wakati benki inafungwa. Malipo haya yatatokana na taratibu za ufilisi ambapo mchakato wake unahusisha kukusanya madeni, fedha iliyowekezwa katika taasisi nyingine na kuuza mali na benki. Kiasi kitakacholipwa kwa kila mteja kitategemea kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na mauzo ya mali, makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa katika taasisi zingine.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Serikali imeamua kuhamisha tozo la kodi ya umiliki wa nyumba kutoka Serikali za Mitaa kwenda TRA na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa mapato na bajeti za Halmashauri nyingi nchini zilizokwishapendekezwa na kupitishwa na vikao vya Halmashauri:-
• Je, Serikali inazipa Halmashauri ushauri gani wa kitaalam wa hatua za kuchukua ili kuziba pengo hilo la kibajeti?
• Kwa kuzingatia uwezo mdogo uliooneshwa na TRA katika kukusanya kodi mbalimbali ambazo wamekuwa wakikusanya kwa mujibu wa sheria. Je, Serikali haioni kwamba uamuzi huu ni kuzidi kuipa TRA mzigo mkubwa ambao hawatauweza?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi. Hata hivyo, hatua ya Serikali kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali ni kuimarisha ukusanyaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa kwenye ukusanyaji wa kodi ya majengo kwenye Halmashauri zetu. Changamoto hizi zipo pia kwa upande wa matumizi ya mapato hayo yanatokana na kodi ya majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Taifa letu. Aidha, Halmashauri zote zinapata mgawo wa fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yaliyokuwa yakisimamiwa na TRA yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 mwaka 2015/2016, hadi bilioni 34.09 kwa mwaka 2016/2017, kipindi ambacho TRA ilianza kukusanya kodi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ongezeko hili la makusanyo linadhihirisha kuwa TRA imefanya vizuri zaidi katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na Halmashauri hizo 30 katika mwaka wa 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018, TRA ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi cha shilingi bilioni 11.9. Hadi kufikia 30 Septemba, 2017, TRA ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 13.2 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 111. Kwa mwenendo huu wa makusanyo ni wazi kwamba TRA imefanya vizuri kwa sababu ya uzoefu walionao katika kukusanya mapato pamoja na kuwa na mifumo ya kisasa ya kukusanya mapato ikilinganishwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA)
aliuliza:-
Kukosekana kwa mpango madhubuti wa Mipango Miji pamoja na gharama kubwa za ujenzi zinazosababishwa na kodi kubwa katika vifaa vya ujenzi kumefanya wananchi kujenga kiholela.
• Je, ni kwa nini Serikali isiondoe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vyote vya iujenzi?
• Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba bora za makazi na bashara; je, ni kwa nini Serikali isiondoe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyumba za Shirika hilo ili ziwe za bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa fedha na mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa vya ujenzi hutumika kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo nyumba za makazi pamoja na nyumba za biashara. Kwa kuwa matumizi ya vifaa vya ujenzi ni mtambuka, ni vigumu kutambua kama mnunuzi atatumia kwa ujenzi wa makazi binafsi, biashara au miundombinu kama vile barabara, umeme na maji. Hivyo basi, kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi kwa lengo la kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi kunaweza kabisa kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara wachache kuliko mwananchi wa kawaida na pia kusababisha kupungua kwa mapato ya Serikali na hivyo Serikali kuwa na uwezo mdogo wa kutoa huduma muhimu kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika,kama ilivyo kwa bei ya bidhaa nyingine bei ya vifaa vya ujenzi haipangwi kwa kutumia kigezo cha kodi ya VAT pekee, bali hutokana na gharama mbalimbali zikiwemo za uzalishaji kama vile malighafi, umeme, maji, nguvu kazi, teknolojia pamoja na miundombinu ya usafirishaji na msukosuko wa nguvu ya soko. Hivyo basi, kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi si kigezo pekee kitakachopunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi.
• Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kutoza kodi ni kuiwezesha Serikali kuwa na mapato ya kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma muhimu za jamii kwa wananchi wote. Nyumba zinazojengwa na kuuzwa na Shirika la Nyumba la Taifa ni mradi wa kibiashara na si huduma.
Pili, ni vema ikaeleweka kwamba, wauzaji wa nyumba hapa nchini ni wengi, hivyo uamuzi wa kuondoa kodi ya VAT kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba la Taifa pekee utakuwa na sura ya ubaguzi kwa wauzaji wengine wa nyumba, ikiwa ni pamoja na kuikosesha Serikali mapato kwa manufaa ya Taifa letu.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
Kwa kuwa watoto wengi hasa waliozaliwa kuanzia miaka ya 1990 na kuendelea hawazijui sarafu za senti tano, kumi, 20, 50 na shilingi moja.
(a) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kurudisha sarafu hizo kwenye mzunguko wa matumizi kwa mfano kilogramu moja ya mchele kuuzwa shilingi1,892.50 au shilingi 1,895.75 badala ya shilingi 1,900?
(b) Kwa kuwa mada ya shilingi na senti inafundishwa katika shule zetu hasa za msingi, je, ni lini jambo hili litatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki Kuu ya Tanzania imepewa kisheria jukumu la kuzalisha fedha za noti na sarafu kulingana na mahitaji na mazingira ya kiuchumi yaliyopo. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, Benki Kuu imezalisha matoleo ya noti na sarafu yenye thamani mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya soko. Mambo muhimu yanayozingatiwa wakati wa kuondoa na kuingiza katika soko noti na sarafu ya thamani ndogo na kubwa ni mfumuko wa bei wa bidhaa za huduma, kulinda thamani ya shilingi na wepesi wa sarafu kubebeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuondoa na kuingiza katika soko sarafu zenye thamani ya juu ni moja ya mikakati na juhudi ya Benki Kuu katika kulinda na kuipa shilingi hadhi ya wepesi wa ubebaji. Sarafu za shilingi zenye thamani ndogo zikiwemo senti tano, kumi, 20, na 50 pamoja na shilingi moja, tano, kumi na 20 kwa uhalisia ubebaji wake ni mgumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa kuwa hatuna sera ya kupanga bei ya bidhaa na huduma kwa sasa, ni vigumu kurejesha sarafu hizi katika mzunguko wa fedha kwa njia anayopendekeza Mheshimiwa Mbunge.
Tatu, sarafu ndogo ya fedha itarejea kwa urahisi katika mzunguko ikiwa teknolojia ya kufanya miamala ya fedha kwa njia ya mitandao itasambaa kote nchini na jamii itakuwa tayari kufanya miamala hiyo kwa njia ya mitandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mada ya shilingi na senti inafundishwa mashuleni ili kuwapa wanafunzi maarifa ya kihesabu kama vile kuhesabu, kujumlisha, kutoa, kugawanya, kuzidisha, kulinganisha na kutafuta uwiano wa thamani mbalimbali ya fedha. Sambamba na maarifa ya mada ya senti na shilingi yanatolewa mashuleni, kigezo kikubwa cha kurejesha sarafu ndogo katika mzunguko wa fedha ni kuimarika kwa thamani ya shilingi au utayari wa wananchi kubeba mzigo mkubwa wa sarafu kwa ajili ya kununua bidhaa na huduma ndogo ndogo. Hata hivyo, sarafu zote zilizowahi kutolewa na Benki Kuu tangu mwaka 1966 bado ni halali kwa matumizi halali ya fedha hapa nchini za zinatumika kwenye miamala isiyo ya fedha taslimu.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Bunge lilipitisha tozo ya kodi ya majengo ya shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na shilingi 50,000 kwa nyumba za ghorofa, lakini Manispaa na Halmashauri mbalimbali nchini zimekuwa zikitoza kodi hiyo zadi ya kiasi hicho.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, kifungu cha 64 kimebainisha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania itakusanya kodi ya majengo kwenye maeneo ya Majiji, Mji na Miji Midogo yote nchini, badala ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majengo mengi hayajafanyiwa uthamini, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya uamuzi wa kuweka kiwango maalum cha shilingi 10,000 kwa majengo ya kawaida na shilingi 50,000 kwa majengo ya ghorofa kwa kila ghorofa. Viwango hivi ni vya mpito wakati Serikali inakamilisha zoezi la uthamini kwa majengo yote yanayostahili kulipiwa kodi ya majengo.
Aidha, majengo yote yaliyofanyiwa uthamini yanalipiwa viwango stahiki kulingana na uthamini. Kwa hiyo, mwenye nyumba yeyote akiona amepelekewa bili ya zaidi ya shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na zaidi ya shilingi 50,000 kwa nyumba ya ghorofa afahamu kwamba nyumba yake imefanyiwa uthamini.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Zaidi ya 70% ya Watanzania, uchumi wao unategemea kilimo.
Je, kwa nini Serikali isifute ushuru wa matrekta kuanzia matano hadi kumi kwa kila kijiji nchini kwa ajili ya kilimo ili kuwawezesha wananchi kuondokana na kilimo cha mkono?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 6(1) Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Sheria ya Kodi ya VAT ya mwaka 2014, kimebainisha misamaha ya kodi kwenye vifaa mbalimbali vya kilimo. Mojawapo ya vifaa vya kilimo vilivyosamehewa kodi ni matrekta, mashine za kuvunia (combine harvester), vifaa vya umwagiliaji, dawa za kuulia wadudu waharibifu wa mazao, vipuri vya matrekta na kadhalika. Hivyo basi, kwa mujibu wa jedwali hili, matrekta pamoja na vipuri vyake hayatozwi kodi na ushuru wa forodha.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Je, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni mazao yapi yaliongoza katika kuchangia Pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, mchango wa mazao ya kilimo, misitu na uvuvi katika pato la Taifa kwa kipindi cha miaka mitano iliopita ulikuwa ni asilimia 31.1 mwaka 2012; asilimia 25.0 mwaka 2013; asilimia mwaka 2014; asilimia 23.5 mwaka 2015 na asilimia 26.4 mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao yaliyoongoza katika mauzo kwenye soko la nje na kuchangia kwa sehemu kubwa katika pato la Taifa ni tumbaku, korosho, kahawa, pamba na chai. Fedha za kigeni zilizopatikana kutokana na mauzo ya mazao hayo ni dola za Kimarekani milioni 956.8 mwaka 2012, dola za Kimarekani milioni 868.9 mwaka 2013, dola za Kimarekani milioni 808.8 mwaka 2014, dola za Kimarekani milioni 793.4 mwaka 2015 na dola za Kimarekani milioni 895.5 mwaka 2016.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kampuni ya Chai Maruku ilibinafsishwa kwa wawekezaji ili kuendeleza uzalishaji. Tangu kampuni hiyo imebinafsishwa, wakulima hawalipwi fedha za mauzo ya chai kwa wakati na wafanyakazi hawalipwi mishahara na stahiki zao ipasavyo.
Je, katika hali hiyo, kwa nini Serikali isivunje mkataba na mwekezaji na kurejesha umiliki Serikalini au kwa mwekezaji mwingine atakayejali maslahi ya wakulima na wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2016 Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utendaji na uendeshaji wa Kampuni ya Chai Maruku.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inafanya vikao kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai kwa lengo la kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya mwekezaji, wakulima pamoja na wafanyakazi wa kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vikao hivyo haki ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala muhimu la haki za wafanyakazi pamoja na madai ya wakulima. Katika vikao vya mwezi Oktoba na Desemba, 2017 mwekezaji alikubali kulipa madai ya wakulima ya kiasi cha shilingi milioni 12. Aidha, majadiliano yanaendelea ili kutatua mgogoro wa madai ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sehemu kubwa ya mgogoro inaelekea kutatuliwa, Serikali haioni sababu ya kuvunja mkataba na mwekezaji kwa sasa. Hata hivyo, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili ili kuhakikisha kuwa haki za wakulima na wafanyakazi hazipotei.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali na Taasisi zake.
Je, Serikali inategemea kuchukua hatua gani ili kutekeleza azma hiyo ya kudhibiti matumizi ya fedha za umma katika taasisi zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imechukua hatua kadhaa katika kuboresha usimamizi wa mashirika na taasisi za umma hususan katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Hatua zilizochukuliwa zimegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni kutungwa kwa sheria mbalimbali na Bunge lako Tukufu na kundi la pili ni miongozo mbalimbali iliyotolewa na Msajili wa Hazina katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizopitishwa na Bunge lako Tukufu ni pamoja na Sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015, ambayo imebainisha hatua mbalimbali za kibajeti zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma katika mashirika na taasisi za umma. Pamoja na masuala mengine, sheria hiyo imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mpango na Bajeti (Plan and Budget Guidelines) wa Serikali unaojumuisha mashirika na taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbali mbali ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia bajeti za mashirika na taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na mipango ya Serikali inayotarakiwa kutekelezwa. Pia Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu la kupitia na kuridhia kanuni za fedha (financial regulations) za mashirika na taasisi zote za umma ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria nyingine iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 ambayo iliweka ukomo wa taasisi na mashirika ya umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara. Aidha, kati ya asilimia 40 inayobaki, asilimia 70 ya fedha hizo inarejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Hazina katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria ametoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti matumizi ya mashirika na taasisi za umma kama ifuatavyo:-
• Barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015 ya kudhibiti safari zisizo za lazima nje ya nchi kwa watumishi wa mashirika na taasisi za umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu kubwa ya fedha za umma.
• Waraka wa Msajili wa Hazina Namba 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Waraka huo umefuta posho za Vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne kwa mwaka mmoja.
• Waraka wa Msajili wa Hazina Namba 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Waraka huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kusimamia na kufuatilia miongozo yote inayotolewa na Serikali ili kuhakikisha kuwa lengo la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye mashirika na taasisi za umma linafanikiwa.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Electronic Fiscal Device (EFD) risiti hazidumu kwa muda mrefu kwani zinafutika maandishi ndani ya muda mfupi.
Je, TRA wataridhika na maelezo ya mlipakodi bila ushahidi wa risiti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali kulikuwa na tatizo la matumizi ya risiti za EFD bila maelekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wafanyabiashara kutumia risiti ambazo zinafutika au zinadumu kwa muda mfupi. Hata hivyo, baada ya kubaini tatizo hilo, TRA ilitoa maelekezo kwa watumiaji wote wa mashine za EFD kununua na kutumia karatasi zilizoidhinishwa na Mamlaka ambazo hudumu kwa muda mrefu, takribani miaka mitano. Pili, TRA imeidhinisha waagizaji wa karatasi zenye sifa ili kuondokana na tatizo la karatasi zisizo na kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto tunayokabiliana nayo ya baadhi ya wafanyabiashara kutumia karatasi zinazofutika au kudumu kwa muda mfupi, TRA inaweza kufuatilia na kubaini kumbukumbu za mteja kutoka kwenye server iliyopo TRA na hivyo kurahisisha uhakiki wa stakabadhi, ama iliyofutika au kupotea. Hivyo basi, endapo risiti ya mtumiaji wa mashine za EFD itafutika au kupotea, ushahidi wa muamala uliofanywa na mteja kwa kutumia mashine za EFD utapatikana kwenye server kuu iliyopo TRA.
MHE. JUMA HAMAD OMAR aliuliza:-
Kuna wakati mwananchi anapaswa kulipa kodi zaidi ya thamani ya bidhaa au kifaa alichonacho:-
(a) Je, Serikali haioni kwamba yanapotokea hayo yanashawishi mlipa kodi husika kulipa kwa njia ya panya au kukwepa kodi?
(b) Je, ni kiasi gani cha misamaha ya kodi kimekuwa kikitolewa na Serikali kwa kipindi cha miaka kumi nyuma na ni nini athari zake katika uchumi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Hamad Omar, Mbunge wa Ole, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi kuu zinazotozwa kwenye bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ni Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT, Ushuru wa Bidhaa na Ushuru wa Forodha. Kiwango cha Kodi ya VAT kwa bidhaa zote zinazostahili kulipiwa VAT ni asilimia 18 bila kujali kuwa bidhaa imeagizwa kutoka nje ya nchi au imezalishwa hapa nchini. Aidha, viwango vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa nyingi, isipokuwa magari, hutumia viwango maalum (specific rate) kulingana na aina ya bidhaa. Kwa mfano, bia hutozwa Sh.729 kwa lita, mafuta ya petroli Sh.339 kwa kila lita na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya Ushuru wa Forodha vinavyotumika hapa nchini ni vile vya ushuru wa pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ushuru huu unatumia viwango vinavyozingatia kiwango cha uchakatwaji wa bidhaa husika. Bidhaa za mtaji na baadhi ya malighafi hutozwa ushuru wa asilimia sifuri, bidhaa zilizochakatwa kwa kiwango cha kati na vipuri hutozwa asilimia 10 na bidhaa za mlaji hutozwa asilimia 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, mfumo wa kodi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchini unazingatia Sheria ya VAT na Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa minajili ya kulinda mazingira pamoja na viwanda vya ndani, kuna baadhi ya bidhaa ambazo zinatozwa Ushuru wa Bidhaa kwa zaidi ya asilimia 25. Mfano, sukari asilimia 100 au Dola za Marekani 460 kwa tani moja kwa kutumia kiwango chochote kilicho kikubwa zaidi na magari yaliyotumika kwa zaidi ya miaka kumi tangu tarehe ya kutengenezwa hutozwa ushuru wa ziada wa uchakavu wa asilimia 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ni kweli kuwa kuna baadhi ya bidhaa ambazo zinaweza kutozwa kodi zaidi ya bei ya kununulia ikiwa zitaangukia katika kundi hili la kulinda mazingira pamoja na viwanda vya ndani. Aidha, ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi unatokana na tabia ya waagizaji wenyewe kukosa uzalendo na si vinginevyo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha msamaha wa kodi uliotolewa na Serikali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ni shilingi trilioni 11.8 ikiwa ni wastani wa shilingi trilioni kwa mwaka.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Wilaya ya Malinyi haina kabisa huduma za Kibenki ambapo wananchi hufuata huduma hizi katika Wilaya jirani ya Kilombero au Ulanga. Serikali kupitia taasisi za kibenki zikiwemo CRDB na NMB zimeahidi kuanza kutoa huduma toka mwaka 2015, lakini hadi leo hakuna utekelezaji wowote:-
• Je, ni lini huduma hizi zitaanzishwa rasmi katika Wilaya ya Malinyi?
• Wakati benki zikisubiri ujenzi wa Matawi yao; Je, kwa nini wasianze kutoa huduma hizo kwa kutumia matawi yanayohamishika (Mobile Service)?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya mfumo wa fedha nchini ya mwaka 1991, yaliitoa Serikali katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za mabenki nchini. Hii ilifanyika ili kuruhusu ushindani huru na kuwezesha kuboresha huduma katika sekta ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za fedha katika maendeleo ya kiuchumimi, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wa Tanzania kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao. Aidha, Serikali inatambua pia kuwa huduma hizo za benki kwa wananchi lazima ziwe na faida kwa pande zote mbili yaani kwa mabenki na wateja pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua ukweli huo faida kwa pande zote na kwa kutilia maanani gharama za kuanzisha na kuendesha tawi kuwa kubwa, NMB na CRDB zinaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika Wilaya ya Malinyi. Upembuzi huo ndiyo utakaotoa mwelekeo wa kufungua tawi au la, kwani tawi linatakiwa liwe endelevu kwa kujiendesha kwa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Malinyi ni moja ya Wilaya ambazo zinanufaika na mfumo wa utoaji huduma kupitia mawakala wa Fahari Huduma (Malinyi SACCOS na Zidua Waziri Shop) zinazoendeshwa na benki ya CRDB ambapo wateja wanapata huduma za kibenki ikiwemo kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha, kuomba mikopo na kupata ushauri wa huduma za kifedha. Aidha, wananchi wa Wilaya ya Malinyi wanashauriwa kutumia njia mbadala kupata huduma za kibenki ikiwemo kupitia simu za mkononi yaani (Sim banking) ya CRDB na Banking on the Wheel ya NMB iliyoko Mlimba kwa kipindi hiki ambacho mchakato wa kufungua tawi unaendelea.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani endelevu wa kudhibiti ongezeko la watu hapa nchini, iendane na uwezo wa Serikali kupeleka huduma muhimu na za msingi kwa watu wake na wananchi kwa ukamilifu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kasi ya ongezeko la idadi ya watu hapa nchini ni asilimia 2.7 kwa mwaka. Wastani wa kiwango cha uzazi cha watoto ni watoto watano kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa, yaani tangu akiwa na umri wa miaka 15 hadi 49. Ongezeko la idadi ya watu duniani ni matokeo ya mambo makuu matatu kwa pamoja ambayo ni vizazi, vifo na uhamiaji wa Kimataifa. Kwa Tanzania, kasi ya ongezeko la idadi ya watu inatokana na vizazi au idadi kubwa ya watoto ambao akinamama wanajifungua katika uhai wa maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ambayo kwa sehemu kubwa inachangia akina mama wa Kitanzania kuzaa watoto wengi ni pamoja na ukosefu au kiwango kidogo cha elimu kwa wasichana na akinamama. Tafiti zinaonesha kuwa, akinamama ambao wana elimu ya sekondari na kuendelea huzaa watoto wachache zaidi ikilinganishwa na wanawake wasiokuwa na elimu au wenye elimu ya msingi. Wasichana au akinamama wenye elimu wanakuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango, madhara ya mimba za utotoni, madhara ya kuzaa watoto wengi pamoja na madhara hasi ya baadhi ya mila potofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina Sera ya Idadi ya Watu iliyoridhiwa na Serikali mwaka 1992 na kufanyiwa maboresho mwaka 2006. Lengo la sera hiyo ni kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu ili kuhakikisha kuwa, idadi ya watu iliyopo inaendana na huduma za jamii zilizopo. Baadhi ya mambo yaliyobainishwa katika sera hiyo ni namna Serikali ilivyojipanga kutoa elimu ya msingi na sekondari, usawa kijinsia, umri wa kuolewa, matumizi ya njia za kisasa na wajibu wa kila mdau tukiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu bila malipo, katika shule za msingi na sekondari inaonesha dhahiri kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu kupitia nyanja ya elimu. Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto wa mwaka 2015/2016 umeonesha kuwa endapo mtoto wa kike atakaa shuleni kwa kipindi kirefu, uwezekano wa kuzaa watoto wengi ni mdogo kwa vile elimu inamsaidia kujitambua na inampa uwezekano mkubwa wa kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi na matumizi bora ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa, suala la udhibiti wa ongezeko la idadi ya watu nchini ni suala mtambuka linalohitaji usimamizi wa wadau wote na kwa ushirikiano wa pamoja. (Makofi)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina hisa kiasi gani katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera?
(b) Je, kiasi cha fedha kilichokopwa na mwekezaji kwa guarantee ya Serikali kimeshalipwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haimiliki hisa katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera na Serikali kupitia PSRC ilibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Kagera Saw Mills Limited kwa kuuza hiza zake zote mnamo mwaka 2001.
• Mheshimiwa Spika, mwekezaji alikopa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 65 kwa kutumia guarantee ya Serikali mwaka 2004 ikiwa ni guarantee ya miaka 12. Hadi sasa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 56.88 zimesharejeshwa sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote. Aidha, marejesho ya sehemu ya mkopo uliobaki wa dola za Kimarekani milioni yatafikia ukomo wake mwezi Julai, 2019.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Katika mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Wilayani Rorya, kuna Ofisi za Uhamiaji na Customs za nchi yetu zipo kwenye makontena.
Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya kisasa kwa ajili ya ofisi katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha na Mpango inatambua uwepo wa mahitaji ya ofisi ya kisasa katika Kituo cha Forodha kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, Wilayani Rorya Mkoa wa Mara. Kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania ipo katika hatua za kupata umiliki wa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 22,933.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi. Mara hatua za umiliki wa eneo zitakapokamilika, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza taratibu za ujenzi wa ofisi na tuna uhakika tunaweza kuwa pamoja na ndugu zetu wa uhamiaji mara ofisi hizi zitakapokamilika na wao wakiwa wanashughulika na ujenzi wa ofisi zao.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Wamiliki wa majengo wameanza kupangisha majengo kwa kutumia fedha za kigeni kama vile dola ya Kimarekani badala ya fedha ya Kitanzania hali inayosababisha kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Je, Serikali ina mpango gani kuchukua hatua kulinda thamani ya shilingi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO aliijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania hapa nchini yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 na tamko la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.
Aidha, mwezi Desemba, 2017 Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alitoa tamko lingine kwa Umma kwamba kuanzia tarehe 1 Januari, 2018, matumizi ya fedha za kigeni hapa nchini yazingatie mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
Pili, bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi, zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na visa kwa wageni na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
Tatu, viwango vya kubadilishana fedha vitavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni benki ina maduka ya fedha za kigeni ndiyo pekee yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
Nne, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni. (Makofi)
Tano, vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matamko ya Serikali ya kupiga marufuku matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni ili kulinda thamani ya shilingi, hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei ya huduma na bidhaa, kuhamasisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kupitia programu ya Export Credit Guarantee Scheme na kudhibiti biashara ya maote katika soko la fedha za kigeni hapa nchini.
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Je, ni nini tamko la Serikali juu ya idadi kubwa ya Benki za Biashara kufunguliwa kwenye miji mikubwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi nchini unaotekelezwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, shughuli nyingi za kiuchumi hususan benki zinaendeshwa na sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sekta binafsi lengo lake ni kufanya biashara na kupata faida, uanzishaji wa huduma za Kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia zaidi fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo husika, uwepo wa miundombinu wezeshi na usalama. Kiuhalisia miji mikubwa inakidhi vigezo muhimu vya uwekezaji kwa sekta ya fedha kama vile uwepo wa fursa nyingi za kuchumi, miundombinu ya kisasa na usalama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na miji mikubwa kuvutia zaidi wawekezaji wa sekta ya fedha, Serikali inajitahidi kuboresha miundombinu katika maeneo ya vijijini ili kuweka mazingira bora na salama yatakayovutia wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi kuwa Serikali inaboresha kwa kasi miundombinu ya mawasiliano, umeme, maji na taasisi za usalama za umma ili kuhakikisha kuwa wawekezaji wanavutiwa kusogeza huduma mbalimbali zikiwemo huduma za kibenki karibu na wananchi. (Makofi)
MHE. DEO F. NGALAWA aliuliza:-
Serikali iliamua pamoja na mambo mengine ya kulinusuru Shirika la Posta kuhakikisha jukumu la kulipa pensheni za wastaafu lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki kwenye mojawapo ya Mifuko ya Pensheni:-
Je, Serikali itakuwa tayari kuhamisha jukumu hili kwenye mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jukumu la kuwalipa pensheni ya kila mwezi wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa sasa wastaafu hao wanalipwa pensheni ya kila mwezi na Shirika la Posta na kwamba Serikali hurejesha fedha hizo baada ya shirika kuwasilisha madai yake hazina kupitia kwa Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haiwezi kuhamisha jukumu la kulipa pensheni wastaafu wa Shirika la Posta na Simu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda kwenye mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa zoezi la kuunganisha Mifuko ya Pensheni halijakamilika. Ni rai ya Serikali kwamba, uamuzi wa kuhamisha au kuendelea kwa sasa utaratibu wa sasa utatolewa baada ya zoezi la kuunganisha Mifuko ya Pensheni kukamilika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Benki ya Kilimo ipo kwa ajii ya kumwezesha mkulima wa Tanzania aweze kufanya uwekezaji wenye tija katika kilimo:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi waweze kukopeshwa?
(b) Je, Serikali ipo tayari kupunguza riba kwa pesa anayokopeshwa mkulima kutoka katika benki hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango Kazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wa miaka mitano (2017 – 2021), benki inakusudia kuanzisha Ofisi za kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini pamoja na Zanzibar. Kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha, benki itatekeleza mpango wake wa kusogeza huduma karibu na wateja wa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia 30 Juni, 2018, Ofisi ya Kanda ya Kati itakuwa imefunguliwa ambayo pia itakuwa ni Makao Makuu ya Benki ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ufunguzi wa Ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika, benki itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua Ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi:-
(i) Kundi la kwanza ni wakulima wadogo wadogo kwa riba ya 8% – 12% kwa mwaka;
(ii) Kundi la pili ni la miradi mikubwa ya kilimo kwa 12% – 16% kwa mwaka;
(iii) Kundi la tatu ni wanunuzi wa mazao kwa 15% – 18% ; na
(iv) Kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko na matumizi ya mkopo huo. Hata hivyo, majadiliano kuhusu kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Katika nchi yetu suala la usawa na haki kwa wananchi wetu ni jambo linalozingatiwa sana na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano; taarifa ya hali ya umaskini nchini imebainisha kwamba ipo mikoa minne ambayo kiwango cha umaskini kipo juu sana na mojawapo ya mikoa hiyo ni Kigoma.
Je, ni hatua zipi za makusudi (kibajeti) zinazochukuliwa ili Mkoa wa Kigoma ujinasue na hali ya umaskini ambayo kwa kiasi cha asilimia 80 umesababishwa na madhila ya kihistoria (historical injustices) na Serikali kuacha au kushindwa kujenga miundombinu ya maendeleo kama barabara, vituo vya afya na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 Wizara ya Fedha na Mipango, Idara ya Kuondoa Umaskini kwa kushirikiana na REPOA ilifanya uchambuzi wa kina wa hali ya umaskini kwa lengo la kupata takwimu za hali ya umaskini katika ngazi ya Mikoa na Wilaya (poverty mapping). Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, Mkoa wa Kigoma ulikuwa na kiwango kikubwa cha watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini cha asilimia 48.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba siyo kweli kwamba Serikali iliacha au kushindwa kujenga miundombinu ya maendeleo kama barabara, vituo vya afya na kadhalika katika Mkoa wa Kigoma na hivyo kusababisha watu wa Kigoma kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Kigoma ni pamoja na Daraja la Jakaya Kikwete katika Mto Malagarasi, Kivuko cha MV Malagarasi, barabara ya Kidahwe hadi Uvinza, Kigoma – Kidahwe na Mwandiga – Manyovu. Aidha, miradi ya barabara inayoendelea ni pamoja na Kidahwe – Kasulu, Kibondo – Nyakanazi na Kibondo – Mabamba mpaka mpakani mwa Burundi. Miradi mingine ni kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kitega uchumi ya NSSF na NHC, miradi ya umeme vijijini na uwanja wa ndege Kigoma awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii yote imelenga kufungua fursa za kiuchumi kwa Mkoa wa Kigoma na hivyo kuongeza kasi ya kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/2017 hadi 2020/2021), Serikali imepanga kuendeleza eneo maalum la uwekezaji Kigoma, upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Kigoma, ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, ujenzi wa mradi wa kuzalisha megawati 44.7 za umeme wa maji kutoka mto Malagarasi na kuunganishwa na Gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imepanga kujenga reli ya Kisasa na kuimarisha reli ya zamani na kununua vichwa 63 vya treni na mabehewa ya mizigo 1,960 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa watu, bidhaa na huduma ifikapo mwaka 2020. Ni matarajio yetu kuwa kukamilika kwa miradi niliyoitaja kutafungua fursa za kiuchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Kigoma.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Madhumuni makubwa ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kilichoanza shughuli zake Julai, 1978 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 ilikuwa ni kuendesha biashara ya mikutano na upangishaji wa nyumba.
Je, ni mafanikio gani ambayo Serikali imeyapata kutokana na kuanzishwa kwa taasisi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) mwaka 1978, Serikali imeweza kupata mafanikio mbalimbali. Baadhi ya mafanikio hayo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo huchangia katika pato la Taifa kwa kulipa kodi stahiki kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa wakati, kwa mfano, kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 kituo kimelipa kodi ya jumla ya shilingi bilioni 6.05.
Pili, kituo huchangia katika bajeti ya Serikali kwa mfano kwa mwaka 2014/2015 hadi 2015/2016 kituo kimechangia jumla ya shilingi milioni 586. Aidha, kwa mwaka 2016/2017 kituo kimetoa gawio kwa Serikali la shilingi milioni 400.
Tatu, kituo kimewezesha Taasisi za Kimataifa nchini kwa kuwakodishia Ofisi na makazi yanayokidhi mahitaji yao. Kwa mfano, AICC ilikuwa ni Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia Mauaji ya Kimbari ya Rwanda. Pia ni Makao Makuu ya Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika kuhusu masuala la rushwa. Vilevile baadhi za Ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo katika eneo la AICC.
Nne, kituo kimeweza kuleta mikutano ya Kimataifa ambayo imechangia kuvutia wageni kutumia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii nchini na kutembelewa na viongozi wakubwa na maarufu duniani na kufanya vyombo vya habari vya Kimataifa kuimulika Tanzania na hivyo kuifanya nchi yetu kutambulika zaidi ulimwenguni.
Tano, kituo kimeweza kutoa ajira kwa Watanzania wapatao 132 hadi kufikia mwezi Mei, 2018.
Sita, kituo kimeweza kujenga majengo matatu ya ghorofa ya makazi kwa familia 48 Jijini Arusha, hivyo kuwawezesha wakazi wa Arusha kuishi katika makazi bora.
Saba, kituo kinahudumia zaidi ya wageni 30,000 kwa mwaka, hivyo kuchangia katika kukua kwa sekta za hoteli, usafirishaji, utalii na wajasiriamali wadogo na wakubwa katika jiji la Arusha.
Nane, kupitia hospitali ya kituo, huduma ya afya kwa jamii imeweza kutolewa kwa wafanyakazi wa Jumuiya za Kimataifa, wageni wanaokuja kwa ajili ya mikutano mbalimbali na watalii wanaofika Arusha kutembelea vituo vya utalii.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Wanawake ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kusimamia nchi yetu na kwamba ukimwezesha mwanamke umeiwezesha familia na Taifa kwa ujumla.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuboresha huduma za kibenki zitakazoweza kuwahudumia akina mama walio mikoa ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa mwanamke katika familia na Taifa kwa ujumla. Kwa kutambua hilo, Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. Suala hili lipo kisera na ni maamuzi ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wanawake wanawezeshwa na kujengewa uwezo kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuibua programu wezeshi kwa wanawake kwa kadri itakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za kisera za Serikali za kuwawezesha wanawake kiuchumi, jukumu la msingi la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili watu binafsi, taasisi za umma na binafsi ziweze kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kuzalisha mali pamoja na huduma zikiwemo huduma za kibenki. Badala ya Serikali kujiingiza moja kwa moja kusambaza huduma za kibenki hapa nchini, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, upatikanaji wa maji, umeme, mawasiliano na usalama wa watu na mali ili kuvutia wawekezaji kusambaza huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali hapa nchini yakiwemo maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara, hususan sera, miundombinu na usalama yamevutia wawekezaji binafsi wa ndani na nje kuwekeza hapa nchini na hivyo kuimarisha huduma jumuishi za kifedha kwa njia ya simbanking, wakala wa benki, mobile money, NGO’s, SACCOS na benki za kijamii. Jitihada hizi zimesaidia kuongeza matumizi ya huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 58 mwaka 2013 hadi asilimia 65 mwaka 2017. Aidha, matumizi ya huduma zisizo rasmi za fedha zimepungua kutoka asilimia 16 mwaka 2013 hadi asilimia saba mwaka 2017. Hivyo basi, ni wajibu wetu kuendelea kuwashawishi wawekezaji binafsi kusogeza huduma za fedha karibu na wananchi badala ya kuitegemea Serikali.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y. MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Katika utekelezaji wa bajeti ya 2017/2018 Serikali imekuwa ikitegemea msaada wa wafadhili (Basket Fund) ili kutunisha Mfuko wa Hazina katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kutoka Basket Fund
kimepatikana katika mwaka 2017/2018?
(b) Je, kati ya fedha hizo ni kiasi gani kimepelekwa Zanzibar kusaidia bajeti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2018 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 182.92 sawa na asilimia 32.89 ya makadirio ya shilingi bilioni 556.08 kimepokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 pamoja na marekebisho yake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapokea misaada ya mikopo ya kisekta moja kwa moja kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hivyo, basi kiasi cha shilingi bilioni 182.92 kilichopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni kwa ajili ya Tanzania Bara tu.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
TEHAMA imekuwa kichocheo cha maendeleo na hivyo kurahisisha ulipaji wa gharama (bills) mbalimbali kupitia miamala kwa njia ya simu. Mathalani, muda wa maongezi, ving’amuzi, umeme, kodi na laini mbalimbali.
Je, mlipaji aweke ushahidi wa aina gani katika kumbukumbu ngumu (hard paper) ili wakaguzi wa TRA waone au TRA itaridhika kwa kumbukumbu ya muamala?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa matakwa ya kifungu cha 35(1)(2), cha Sheria ya Usimamizi wa kodi ya mwaka 2015, kila mlipa kodi au mtu yeyote anayetakiwa kulipa kodi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatakiwa kutunza kumbukumbu za miamala katika mfumo wa kumbukumbu ngumu au mfumo wa kielektroniki. Aidha, kifungu cha 35(3) kinamtaka mlipa kodi kutunza kumbukumbu zake kwa muda wa miaka mitano kuanzia tarehe ambayo muamala umefanya au kwa muda zaidi kulingana na matakwa ya sheria.
Mheshimiwa Spika, sambamba na Sheria ya Usimamizi wa Kodi kifungu cha 69(3)(b) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (The Value Added Tax Act, 2014) kinamtaka mlipa kodi aliyesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mfumo wa malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kuwa na risiti ya EFD au ankara ya kodi (tax invoice) wakati akiwasilisha taarifa zake za mwezi (VAT return).
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kuingiza fedha zote za kodi kwenye mfuko mmoja na baadaye asilimia fulani ya fedha hizo zirudishwe kwenye Halmashauri:-
Je, kwa nini isitungwe sheria ya kuibana Serikali ikiwa haitarejesha fedha hizo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, kifungu cha 58 usimamizi wa mapato utazingatia misingi ifuatayo:-
• Mapato yote ya Serikali kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
• Yeyote aliyepewa mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika ipasavyo katika ukusanyaji wenye ufanisi, utunzaji wa hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato; na
• Mapato yote kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Bajeti, mgawo wa fedha utazingatia bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtitiriko wa fedha, utekelezaji wake, mpango wa manunuzi na mpango wa kuajiri. Aidha, hakuna fungu litakaloruhusiwa kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za kulipia matumizi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa vifungu vya 44 na 58 vya Sheria vya Bajeti vya Mwaka 2015, usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali umebainishwa vizuri na hivyo hakuna haja ya kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka fedha kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-
Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara 133 ya Katiba kupitia Sheria Na.15 ya Mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na uchumi wa Muungano usimamiwe na chombo cha Muungano:-
• Je, ni kwa nini miaka 33 sasa Akaunti hiyo haijafanya kazi yake?
• Je, gharama kiasi gani imetumika kuanzisha taasisi ambayo haina faida yoyote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Magogoni, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha pamoja na Tume ya Pamoja ya Fedha. Ibara ya 133 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha sharti la kutungwa kwa sheria itakayoweka utaratibu wa uendeshaji wa Tume ya Pamoja ya Fedha pamoja na Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Ili kutekeleza sharti hilo la kikatiba, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha ya Mwaka 1996 (The Joint Finance Commission Act, 1996) na hivyo kuwezesha kuanza kazi kwa Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 2003.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa uendeshaji wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha umependekezwa kwenye ripoti ya mapendekezo ya vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za muungano iliyoandaliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 2006. Hata hivyo, akaunti ya pamoja ya fedha haijaanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika.
(b) Mheshimiwa Spika, tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2003 Tume ya Pamoja ya Fedha imekuwa ikiidhinishiwa bajeti yake na Bunge lako Tukufu kupitia bajeti ya Fungu 10, chini ya Wizara ya Fedha na Mipango. Katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2003/2004 hadi 2017/ 2018, Tume imeidhinishiwa bajeti ya Sh.31,971,490,663 kwa ajili ya uendeshaji na utekelezaji wa majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, aidha, si kweli kwamba Tume ya Pamoja ya Fedha haina faida yoyote. Katika kutekeleza majukumu yake ya msingi, Tume imefanya stadi sita tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kutoa mapendekezo na ushauri katika eneo la uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia, Tume ya Pamoja ya Fedha imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Uendeshaji wa Akaunti ya Fedha ya Pamoja ambao unatarajiwa kutekelezwa mara majadiliano ya pande mbili za Muungano yatakapokamilika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Pamoja na nia nzuri ya Serikali kudhibiti ulimbikizaji wa madeni lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kila siku katika Idara za Halmashauri za Wilaya zinazopokea ruzuku ya matumizi ya kawaida toka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka fedha za ruzuku katika Halmashauri za Wilaya kama zilivyopitishwa na Bunge?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi. Kinachoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka husika. Pili, utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa sasa unafanyika kwa mfumo wa cash budget. Hivyo basi, ruzuku kutoka Serikali Kuu hupelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya kulingana na makusanyo halisi ya mapato ya mwezi husika. Serikali yetu kwa mtindo huo itaendelea kupeleka fedha za ruzuku kwenye Halmashauri zetu kutokana na makusanyo halisi kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Takwimu za Mpango wa Maendeleo 2016/2017 zimeonesha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa mitano (5) iliyo maskini zaidi nchini:-
• Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha Mikoa hiyo inapata rasilimali fedha na watu ili iweze kuondokana na hali hiyo ya umaskini?
• Je, nini kifanyike kwa Mkoa wa Kigoma ili kujenga ulinganifu katika maendeleo?
• Je, kwa nini Serikali isitenge shilingi bilioni 5 kwa kila mwaka kwa kila Mkoa ili kuondoa kitisho cha Mikoa hiyo kuachwa nyuma kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel N. Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasuli Mjini, lenye vipengele (a), (b), (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali yetu huzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na mwaka mmoja mmoja pamoja na Mwongozo wa Bajeti kugawa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za umaskini. Aidha, mgawanyo wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huenda sambamba na mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utekelezaji, usimamizi, uperembaji na kutoa huduma kulingana na aina ya miradi.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kujenga ulinganifu wa maendeleo katika Mkoa wa Kigoma, Serikali imebainisha maeneo na miradi ya kimkakati kwa ajili ya utekelezaji ili kufungua fursa za kiuchumi. Miongoni mwa maeneo ya kimkakati yaliyobainishwa na kuanza kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/ 2017 – 2020/2021 ni Mradi wa Upanuzi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma; Mradi wa Uzalishaji wa Umeme wa Maji katika maporomoko ya Mto Malagarasi MW 44.7; kuanzisha na kuendeleza Eneo la Uwekezaji Kigoma (Special Economic Zone); Mradi wa Gridi ya Kaskazini Magharibi KV400; na ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa.
(c) Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa rasilimali fedha huainishwa kwenye Mwongozo wa Bajeti ya Serikali kwa kila mwaka ambao huandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa; na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Hoja ya kutenga shilingi bilioni 5 kwa kila Mkoa, kila mwaka ni lazima ifungamanishwe na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kwa sasa Serikali haina Sera wala Mwongozo wa kutenga shilingi bilioni 5 kwa kila mwaka, kwa kila Mkoa ili kukabiliana na changamoto za umaskini.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inalo jukumu la kuzisimamia benki nyingine hapa nchini pamoja na kulinda haki za wateja wa benki za biashara. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa Benki ya FBME imefungwa kwa sababu ya ukiukwaji wa sheria za kifedha na mpaka sasa jambo hilo halijapatiwa ufumbuzi.
(a) Je, ni sababu gani inayofanya benki hiyo isiwalipe wateja wake haki zao au amana zao?
(b) Je, Serikali haioni kuwa BOT imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuzisimamia benki nyingine na kuwafanya wananchi kukosa imani na mifumo ya kibenki inayorudisha nyuma utaratibu wa kuhifadhi fedha?
(c) Je, Serikali haioni kuwa tunakosa mapato ambayo yangetusaidia kwa ajili ya maendeleo ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 11(3)(i), 41(a), 58(2) na 61(1) vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 Benki Kuu ya Tanzania ilisimamisha shughuli zote za Benki ya FBME na kufuta leseni ya biashara, kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi tarehe 8 Mei, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua hiyo, jukumu la kuwalipa wateja wa Benki ya FBME haki au Amana zao kisheria lipo mikononi mwa Bodi ya Bima ya Amana na siyo Benki ya FBME. Malipo ya fidia au amana kwa wateja yamechukua muda mrefu kwa sababu ya taratibu za kisheria zinazotakiwa kuzingatiwa katika zoezi zima la ufilisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, zoezi la kulipa fidia kwa wateja waliokuwa na amana katika Benki ya FBME kwa mujibu wa sheria lilianza mwezi Novemba, 2017 na bado linaendelea. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, 2018 asilimia 60 ya wateja wa benki hiyo walikuwa wamelipwa fidia ya amana na Bodi ya Bima ya Amana.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa majukumu ya msingi ya Benki Kuu ni kusimamia utendaji wa kila siku wa taasisi za kifedha hususan benki. Katika kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu kuchukua hatua kuinusuru benki husika ikiwemo kusimamia uendeshaji wa shughuli za benki au kuifutia leseni mara tu inapobaini viashiria vya kufilisika au upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na Kanuni zake. Lengo la kufanya hivyo ni kulinda walaji, amana za wateja na kujenga imani ya wananchi kuhusu mifumo ya benki na utaratibu wa kuhifadhi fedha kwenye mabenki.
Pili, Benki Kuu husimamia taratibu zote za ufilisi kwa taasisi itakayofutiwa leseni na kuhakikisha kuwa wateja wanapata fidia kwa mujibu wa sheria. Kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo, majukumu haya mawili yanaendelea kutekelezwa na kusimamiwa vizuri na Benki Kuu. Hivyo basi, siyo kweli kwamba Benki Kuu imeshindwa kuzisimamia taasisi za fedha na benki na hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani na mifumo ya kifedha nchini
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kuwa Taifa linakosa mapato ambayo yangesaidia kuleta maendeleo, ni lazima kuzingatia matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu zilizopo ili zoezi hili liweze kufanyika kwa ufanisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, zoezi la ufilisi linafanyika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za ufilisi wa kampuni. Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba, Mfilisi wa Benki kwa kushirikiana na Benki Kuu anafanya juhudi za kukusanya madeni pamoja na fedha za benki zilizopo kwenye benki nyingine nje ya nchi ili kulipa amana za wateja kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya wafanyabiashara na TRA kuhusu mashine za EFDs hususani bei za mashine na aina za mashine.
(a) Je, bei halali ya mashine ya EFD kulingana na aina na ubora wake ni shilingi ngapi?
(b) Kwa kuwa mashine za EFDs zinafanya kazi kwa niaba ya TRA, je, kwa nini Serikali isitoe mashine hizo bure kwa wafanyabiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Spika, kuna aina tano za mashine za EFD kwa ajili ya kutunza kumbukumbu na kutoa risiti za mauzo. Mfanyabiashara anaweza kununua aina mojawapo ya mashine hizo kulingana na mahitaji yake. Aidha, ubora wa mashine zote ni lazima uthibitishwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania kabla mashine hizo hazijaingia sokoni na kuanza kutumika. Bei ya kila mashine ni kama ifuatavyo:-
i. Rejista za Kielekroniki za Kodi - mashine hizi hutumiwa na wafanyabiashara wasiotumia mifumo ya kompyuta au mifumo ya kihasibu na bei yake kwa sasa ni shilingi 590,000.
ii. Mashine za kielektroniki zinazoweka alama au saini (Electronic Signature Devices) - mashine hizi hutumiwa na walipakodi wanaotumia mifumo ya kompyuta na mifumo maalum ya kihasibu na bei zake ni kati ya shilingi 1,000,000 na 1,200,000.
iii. Printa za Kielektroniki za Kodi (Electronic Fiscal Printers) - mashine hizi hutumia mfumo maalum wa kompyuta kufanya mauzo na bei zake ni kati ya shilingi 1,500,000 na 1,700,000.
iv. Printa za Pampu za Mafuta ya Petroli na Dizeli - mashine hizi hutumiwa na wafanyabiashara wanaouza mafuta ya petroli na dizeli kwa kutumia pampu na bei zake ni shilingi 6,000,000 ikijumuisha gharama za ufungaji na uunganishaji kwenye pampu za mafuta.
v. Printa za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni - bei za mashine hizi ni shilingi 2,150,000 ikiwa ni pamoja na programu ya mfumo (software).
b) Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wanaponunua mashine za EFD hulipa gharama za ununuzi wa mashine hizo na baadaye Serikali hurejesha gharama hizo kama ifuatavyo:-
i. Wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye VAT; kwa mujibu wa jedwali la saba chini ya Kanuni ya 54(2) za Sheria ya Usimamizi wa Kodi za mwaka 2016, mashine zilizonunuliwa kwa mara ya kwanza zinagharamiwa na Serikali kwa kumruhusu mfanyabiashara kujirejeshea fedha zake kwa utaratibu wa input – output tax kwenye return yake ya mauzo ya mwezi husika.
ii. Kwa wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani hurejeshewa gharama za mashine kama ifuatavyo:-
Mosi, wanaoandaa hesabu za mizania; kundi hili linaruhusiwa kujirejeshea gharama za ununuzi wa mashine kwa kuziingiza gharama husika kama gharama za kuendesha biashara kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 11(2) cha Sheria ya Kodi ya Mapato.
Pili, wafanyabiashara wasioandaa hesabu za mizania (presumptive cases) kwa mujibu wa Kanuni ya 54(2) ya Kanuni za Sheria ya Usimamizi wa Kodi za mwaka 2016 kundi hili la wafanyabiashara wanajirejeshea gharama za mashine kwenye kiasi cha kodi walichokadiriwa kwa mwaka husika. Kama hawatakuwa wamejirejeshea kwa asilimia 100 basi kiasi kilichobakia kitasogezwa mwaka unaofuata.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Zipo benki zinazotoa mikopo ya kilimo hususan Benki ya Kilimo Tanzania:-
Je, kwa upande wa Zanzibar ni wananchi wangapi wanaofaidika na mikopo ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya wananchi walionufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa wananchi wa Zanzibar hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2018 ni 3,000. Kati ya hao wanaume ni 1,800, wanawake 900 na vijana wa kike na kiume ni 300. Aidha, jumla ya mikopo iliyotolewa kwa idadi hiyo ya wananchi wa Zanzibar hadi kufikia tarehe 31Julai, 2018 ni shilingi bilioni 6.50.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitangaza kukua kwa hali ya uchumi wa nchi yetu kila mwaka:-
Je, ni vigezo gani sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, vigezo sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani ni ongezeko la pato la Taifa, ongezeko la pato la wastani la mwananchi kwa mwaka, ongezeko la uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, kupungua kwa uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, utulivu wa bei za bidhaa na huduma, utulivu wa viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na huduma za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji unaofanywa katika nchi ni kigezo kingine cha msingi cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa huongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na huduma, ajira, kipato cha mwananchi mmoja mmoja, pato la Taifa na hatimaye kupunguza umaskini katika jamii. Aidha, mchango wa Serikali katika ukuaji wa uchumi ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuwekeza zaidi kwenye shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi, kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ucheleweshaji wa mishahara kwa watumishi wa umma:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Waraka wa Hazina Na.12 wa mwaka 2004, watumishi wa umma wanatakiwa kulipwa mishahara yao kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi. Kumbukumbu za malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma zinaonyesha kuwa, kuanzia Julai, 2017 hadi Agosti, 2018 watumishi walilipwa mishahara yao kati ya tarehe 20 na 24 ya kila mwezi. Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kuwa hakuna ucheleweshaji wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Kwa kuwa Ripoti za Ukaguzi za Ufanisi unaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimeonesha kuna mapendekezo yanayotolewa baada ya ukaguzi mengi hayafanyiwi kazi na kwamba upungufu unaoibuliwa hujirudia mwaka hadi mwaka.
(a) Je, Serikali inakubaliana na pendekezo la kuanzisha kitengo maalum kitakachoratibu utekelezaji wa mapendekezo ya kaguzi za ufanisi?
(b) Je, Serikali inakubaliana na pendekezo kuwa baada ya Kamati ya PAC kujadili taarifa ya Ukaguzi wa Ufanisi ipeleke maoni yao kwa Kamati za Kisekta ili kutoa fursa kwa Kamati hizo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mapendekezo ya CAG hasa katika maeneo ya kisera na kiutendaji kwa mujibu wa Kanuni za Bunge?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa ufanisi wa miradi unaratibiwa na kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye hutoa mapendekezo yanayohitajika kutelekelezwa na wakaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya taarifa ya kaguzi za ufanisi kukamilika, huwasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana na sekta husika, mfano Kilimo, Elimu, Maji na kadhalika, tofauti na ilivyo kwa taarifa za Ukaguzi wa Serikali Kuu na mashirika ya umma, ambapo taarifa zake huwasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha na taarifa ya kaguzi za Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasilishwa Bungeni na Waziri mwenye dhamana na masuala ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vilevile utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa za ufanisi (performance audit) huratibiwa na Wizara husika. Wizara za kisekta ndizo ambazo hufuatilia na kuhakikisha kuwa mapendekezo ya CAG yanafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maelezo haya, haitakuwa vyema kuanzisha kitengo maalum cha kuratibu utekelezaji wa mapendekezo ya Taarifa ya Ukaguzi wa Ufanisi kwani kwa kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali. Hata hivyo Wizara, Idara au taasisi zinatakiwa kuwa na mpango kazi wa kuhakikisha kuwa mapendekezo yanayotolewa na CAG kupitia taarifa hizo, yanatekelezwa ipasavyo. Aidha, kupitia taarifa hizo za ufanisi, kunakuwa na masuala ambayo utekelezaji wake ni wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali siku zote ipo tayari na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni zilizowekwa zikiwemo Kanuni za Bunge. Hata hivyo, Serikali haina mamlaka ya kupanga au kuingilia majukumu yanayopaswa kutelekezwa na Kamati za Kudumu za Kisekta za Bunge. Hivyo basi, Bunge lako tukufu lina nafasi ya kuamua juu mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MASOUD A. SALIM aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 141(2) ya Katiba ya Nchi, Deni la Taifa maana yake ni deni lenyewe, faida inayolipwa juu ya deni hilo, fedha zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo polepole na gharama zote zinazoambatana na deni hilo:-
a) Je, Deni la Taifa hadi swali hili linajibiwa ni kiasi gani?
b) Je, mchanganuo wa fedha zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo ukoje?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu swali hili, naomba nikushukuru sana kwa safari yako muhimu uliyoifanya Jimboni kwangu Kondoa juzi tarehe 9 Juni, 2018. Mwenyezi Mungu akubariki na akupe afya njema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, hadi kufikia 30 Aprili, 2018, Deni la Taifa lilikuwa Dola za Kimarekani milioni 26,161.02 sawa na shilingi bilioni 59,480.74.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Deni la Taifa linajumuisha deni la Serikali na deni la sekta binafsi, Serikali inawajibika kufanya malipo ya deni la Serikali na si Deni la Taifa kwa ujumla wake. Aidha, fedha kwa ajili ya malipo ya Deni la Serikali inatengwa kwa kuzingatia taratibu za kawaida za kibajeti kupitia Fungu 22. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1,262.42 kwa ajili ya malipo ya deni la ndani na shilingi bilioni
685.06 kwa ajili ya malipo ya deni la nje. Hivyo basi, hakuna fedha iliyowekwa akiba kwenye mfuko maalum kwa ajili ya kulipia deni la Taifa.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Mfumo wa ulipaji kodi za kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unakwaza na kuvunja harakati za biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa Zanzibar kushuka:-
Je, Serikali ipo tayari kuunda Kamati kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi za mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, chimbuko la malalamiko ya kodi wakati mizigo inaposafirishwa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya kuthamini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Hali hiyo inasababishwa na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa uthaminishaji bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya TANCIS na Import Export Commodity Database ikiratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha kilichopo Dar es Salaam. Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitumii mifumo hiyo na hivyo kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia Tanzania Bara, kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa zimethaminiwa Zanzibar. Iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na ule uliofanywa Zanzibar, hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara. Ikiwa kodi iliyolipwa Zanzibar ni kidogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti ya kodi iliyozidi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara kwa kutumia mifumo ya IECD na TANCIS haina lengo la kuua biashara Zanzibar, hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya biashara na ushindani hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kujadiliana ili kuona kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Aidha, kwa kuwa Serikali zetu mbili hazijashindwa kutatua changamoto hii, ni dhahiri kabisa kuwa hakuna sababu ya kuunda Kamati ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi kwa mizigo inayotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(2), Bunge lako Tukufu ni Mhimili unaojitegemea na hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili ya jambo hili au jambo lolote lile.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Wapo Watumishi katika sekta ya afya, hususan Madaktari na Wauguzi ambao waliajiriwa katika miaka ya 1980 kupitia Serikali Kuu, lakini wakati ule hapakuwa na makato ya mfuko wa kijamii na kuanzia mwaka 1999, Serikali ilianza kuwakata mishahara yao kwenye Mfuko wa PSPF:-
Je, Serikali inawafikiriaje Watumishi hao ambao fedha zao hazikukatwa na mifuko ya kijamii wakati huo hususan Mfuko wa PSPF?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya Julai 1999, mfumo wa malipo ya mafao ya kustaafu kwa watumishi wa Serikali Kuu haukuwa wa kuchangia. Kwa mantiki hiyo, watumishi wote wa umma waliokuwa kwenye ajira ya masharti ya kudumu wanastahili malipo ya uzeeni, wakiwemo watumishi wa sekta ya afya hata kama hawakuchangia. Aidha, kwa mujibu wa Ibara ya tano (5) ya Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa PSPF, watumishi wote wa Serikali Kuu ambao waliajiriwa na kuthibitishwa katika ajira ya masharti ya kudumu na pensheni, wanakuwa wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwa mfuko huo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi Na.2 ya Mwaka 1999 kwa Watumishi wa Umma, ambayo ilianzisha Mfuko wa Pensheni wa PSPF, wastaafu wote ambao ni wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF na wanaoguswa na Sheria hii wanalipwa mafao yao ya kustaafu na Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa kipindi chote cha utumishi wao. Hii inamaanisha kwamba, mafao yao yanakokotolewa kuanzia tarehe ya kuajiriwa hadi wanapostaafu utumishi wao kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile LAPF, PSPF, PPF, NSSF na NHIF imesaidia sana kutoa mikopo hasa kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya jamii:-
Je, Serikali imefanya juhudi gani kurejesha mikopo hiyo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 Serikali ilifanya uhakiki wa deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii linalotokana na mikopo ya uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ili kuandaa utaratibu wa malipo. Jumla ya deni lililowasilishwa Serikalini kwa ajili ya uhakiki kwa mifuko yote ni shilingi trilioni 2.1 na deni lililokubalika baada ya uhakiki ni shilingi trilioni 1.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uhakiki kukamilika, Serikali ilianza kuandaa utaratibu wa kulipa deni hilo kwa kutumia hati fungani maalum zilizotarajiwa kuiva ndani ya kipindi cha kati ya miaka mitatu (3) na 20. Hata hivyo, wakati zoezi la kuandaa hati fungani likiendelea, Serikali ilipendekeza na Bunge lako Tukufu kuridhia mapendekezo ya Serikali ya kuunganisha Mifuko ya Pensheni na kuunda Mifuko miwili mmoja kwa ajili ya sekta ya umma na mwingine kwa ajili ya sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hiyo, ilisababisha Serikali kusitisha zoezi la kuandaa na kutoa hati fungani maalum hadi hapo taratibu za kuunganisha Mifuko ya Pensheni zitakapokamilika.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Viwango vya riba katika benki hapa nchini ni vikubwa na vimekuwa ni kikwazo kwa Watanzania wengi kuweza kukopa na kufanya biashara:-
Je, Serikali inachukua hatua gani ili Benki ziweze kupunguza viwango hivyo vya riba?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara huria ya sekta ya benki ilianza tangu mwaka 1991 mara baada ya kupitishwa wa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya mwaka 1991. Kupitia sheria hiyo, wawekezaji walifungua benki binafsi hapa nchini na gharama za huduma za bidhaa kuamuliwa na nguvu ya soko. Hivyo basi kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya mwaka 1991, Serikali haina mamlaka ya moja kwa moja ya kupunguza viwango vya riba katika soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba bei ya huduma na bidhaa katika sekta ya fedha inaamuliwa na nguvu ya soko, Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba katika soko zinapungua. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ni kama ifuatavyo:-
(a) Kuzitaka benki za biashara kutumia mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (credit reference bureau system).
(b) Kwa sasa Benki Kuu inatoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89.
(c) Benki Kuu imeshusha riba (discount rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.
(d) Benki Kuu imepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.
(e) Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua hizi za kisera kuchukuliwa na Serikali, baadhi ya benki za biashara hapa nchini zimeanza kupunguza riba ya mikopo. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinaendelea kupungua. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa wafanyakazi 545 wa KILTEX – Arusha ambao bado wanadai pensheni toka kiwanda hicho kilipofungwa baada ya Mwajiri wao kutowasilisha michango yao kwenye Mfuko wa Kijamii wa PPF?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Nguo cha KILTEX, kilisimamisha shughuli za uzalishaji mwaka 1994 na kuwekwa chini ya ufilisi na PSRC mwaka 1995, kutokana na tatizo la ukosefu wa mtaji na malimbikizo ya madeni. Kwa mujibu wa ripoti ya Mfilisi, kiwanda kilishindwa kutekeleza takwa la kisheria la kuwasilisha mchango wa mwajiri na waajiriwa kwenye Mfuko wa Pensheni wa PPF kati ya mwaka 1986 na 1994 na hivyo kusababisha PPF kushindwa kuandaa malipo ya mafao ya wafanyakazi kulingana na matakwa ya kisheria mara baada ya kiwanda kufungwa na kufilisiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu na nyaraka za ufilisi zilizopo, taratibu za ufilisi zilikamilika na wafanyakazi wa KILTEX walilipwa stahili zao. Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi walilipwa mafao ya kiinua mgongo kwa mkupuo na wengine walirejeshewa michango yao kwa kadri walivyochangia. Utaratibu huu wa malipo ulifanyika baada ya Mfilisi kushindwa kulipa riba, adhabu na malimbikizo ya michango kwenye Mfuko wa Pensheni wa PPF. Uamuzi huo ulifikia kutokana na ukweli kwamba mauzo ya mali za kiwanda yalikuwa kidogo ikilinganishwa na jumla ya madai na gharama halisi za ufilisi.

Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wa Kiwanda cha KILTEX walilipwa stahili zao kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 46 ya mwaka 1931 ambayo ilitumika kufilisi kiwanda mwaka 1995. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mfilisi alitakiwa kuuza mali za kiwanda na kutumia fedha za mauzo kulipa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na stahili za watumishi ndani ya muda maalum kulingana na tangazo la ufilisi. Kufuatia tangazo la Mfilisi kwenye vyombo vya habari, wadai waliwasilisha madai yao na Mfilisi alilipa madeni hayo kulingana na fedha mauzo zilizopatikana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y MHE. HALIMA A. BULEMBO) aliuliza:-

Kagera ni moja ya mikoa mitano maskini zaidi nchini kutokana na utafiti uliofanywa na Bwana Joachim De Weeidt na kuchapishwa kwenye jarida la Journal of Development Studies ambao unaonyesha kuwa kuna njia mbili za kuondoa umaskini Kagera ambazo ni kilimo na biashara:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwa na miradi maalum ya kuondoa umaskini kwa watu wa Kagera ambao ndiyo mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi zaidi za EAC na hivyo kuufanya kuwa Mkoa wa kimkakati kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ya kiuchumi na kijamii inayotekelezwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika Mkoa wa Kagera na mikoa mingine nchini ni kwa ajili ya kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya wananchi. Pamoja na ukweli huo, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mkakati wa Serikali wa kutekeleza miradi maalum ya kuondoa umaskini katika Mkoa wa Kagera imeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021, Mpango Mkakati wa Mpango wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Mipango ya Mkoa wa Kagera kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa na Serikali katika Mkoa wa Kagera ni kama ifuatavyo:-

(i) Mkoa wa Kagera umeainisha na kutenga maeneo ya uwekezaji yenye ukubwa wa hekta 58,000 kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo (Agro Processing Industries), hususan viwanda vya kusindika nyama, ngozi, maziwa, asali, ndizi, miwa, kahawa, samaki na kadhalika. Aidha, hekta 17,400 kati ya hekta 58,000 zimeshapimwa na zipo tayari kwa uwekezaji.

(ii) Kukuza sekta ya viwanda, hususan viwanda vya kusindika mazao ya maliasili na kilimo. Viwanda vinavyofanya kazi ya kusindika mazao kwa sasa ni Kagera Fish Company Ltd na Supreme Perch Ltd vinavyosindika minofu ya samaki; Kagera Sugar Company Ltd na Amir Hamza Company Ltd vinavyosindika miwa na kahawa; na Kiwanda cha Maziwa kinachosindika wine ya rosella na juisi. Aidha, Kampuni ya Josam imepatiwa eneo lenye ukubwa wa hekta 500 katika Ranchi ya Kikulula na tayari limejengwa bwawa kwa ajili ya kuvuna maji pamoja na kuanza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wapatao mia moja hadi sasa.

(iii) Kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami mfano barabara ya Kyaka - Bugene (Km 59.1); barabara ya Kagoma – Lusahunga (Km 154); barabara ya Ushirombo – Lusahunga (Km 110); barabara ya Bwanga – Kalebezo (Km 67); barabara ya Nyakanazi – Kibondo (Km 50) na ujenzi umefikia asilimia 40; na barabara ya Kyamyorwa – Buzirayombo (Km 120).

(iv) Kuanzisha Kiwanda cha Kuchakata madini ya bati katika Wilaya ya Kyerwa ifikapo Juni 2021. Kampuni ya Tanzaplus Minerals and African Top Minerals Ltd zimeonesha nia ya kuwekeza na tayari zimeanza kuleta mashine za uchenjuaji.

(v) Kuendeleza mradi wa Uwekezaji wa Madini ya Nikeli Kabanga, katika Wilaya ya Ngara ifikapo Juni, 2021.

(vi) Kukamilisha Mradi wa REA Phase III katika maeneo ambayo hayajapata umeme ifikapo mwaka 2020.

(vii) Kuanzisha na kuendeleza skimu ya umwagiliaji katika eneo la Kitengule, Wilaya ya Karagwe ifikapo mwaka 2021. Ujenzi wa daraja la kuunganisha eneo la mradi na Kiwanda cha Sukari Kagera unaendelea kwa sasa. Wakulima zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kunufaika na uwekezaji huo.

(viii) Kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MW 80 kutoka Mto Rusumo na Kakono MW 87 katika Mto Kagera ifikapo Juni 2020.

(ix) Kuimarisha usafiri wa majini kwa kukamilisha ujenzi wa meli kubwa itakayotoa huduma ya usafiri na usafirishaji kati ya Bukoba na Mwanza.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanzisha Kituo cha Forodha katika Bandari ya Manda, Ludewa ili kurahisisha huduma kwa wananchi wanaoenda nchi jirani hasa kwa shughuli za biashara?
NAIBU WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogatias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kufungua Kituo kipya cha Forodha unatakiwa kuzingatia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004 ambayo inaitaka nchi mwanachama kuwasilisha kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maombi ya idhini ya kuanzisha Kituo kipya cha Forodha na hatimaye kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kupata nguvu ya kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa ndani wa kuwasilisha maombi ya kufungua kituo kipya cha forodha unaanza katika ngazi ya mkoa ambapo mkoa husika unatakiwa kuwasilisha maombi ya kufungua kituo kipya cha forodha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Baada ya Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujiridhisha, itamfahamisha Kamishna Mkuu wa mamlaka ya Mapato Tanzania ili kufanyia kazi maombi husika kwa kuzingatia Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki na hatimaye kuwasilisha maombi hayo kwenye Sekretaieti ya Jumuiya ya Afika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia taratibu za kufungua kituo kipya cha forodha hapa nchini, tunamshauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na uongozi wa mkoa ili kuandaa andiko na kuwasilisha Serikalini kwa hatua stahiki.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-

Katika kipindi cha hivi karibuni wananchi wamekuwa wakilalamikia mzunguko wa fedha kuwa mdogo:-

Je, hali hiyo imesababishwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza Sera ya Fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendeana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kabla ya mwaka 2017 kulitokea changamoto ya kuongezeka kwa mikopo chechefu ambayo kwa sehemu kubwa ilisababishwa na baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo bila kuzingatia Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na Kanuni zake za mwaka 2008. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ilichukua hatua ya kusimamia kwa karibu Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 pamoja na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuhamisha fedha za taasisi za umma kutoka kwenye mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, kuanzia Januari, 2017, Serikali kupitia Benki Kuu ilichukua hatua za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ili kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kushusha riba ya Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 16 Machi, 2017 hadi asilimia 7 Agosti, 2018. Pili, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya biashara (Statutory Miminimum Reserve Requirement, SMR) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 mwezi Aprili, 2017. Tatu, kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10.0 ya sehemu ya SMR kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi. Mwisho, Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalumu kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

Pili, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na Benki ya Biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement) kutoka 10% hadi 8% mwezi Aprili, 2017.

Tatu, kuruhusu mabenki kutumia 10% ya sehemu ya Statutory Minimum Reserve Requirement kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi katika uchumi.

Mwisho, Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalum kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

Mheshimiwa Spika, hatua hizi za Sera ya Fedha zimesaidia kuboresha hali ya ukwasi kwenye Benki za Biashara na kupunguza riba katika Soko la Fedha baina ya mabenki kutoka wastani wa asilimia 4.6 kwa mwaka unaoishia Februari, 2018 hadi asilimia 2.3 kwa mwaka unaoishia Februari, 2019. Kuongeza kwa mikopo ya sekta binafsi kutoka wastani wa asilimia 1.7 mwaka 2017 hadi asilimia 7.3 Januari, 2019 na kupungua kwa riba ya mikopo kutoka wastani wa asilimia 21 mwaka 2016 hadi wastani wa asilimia 17 mwaka 2018.

Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa hakuna tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko baada ya Serikali kuchukua hatua hizi. Pia mzunguko wa fedha katika uchumi unaendana na malengo na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi zilizopo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Mheshimiwa Rais alitoa tamko kuwa Wazauni wote wanaoidai Serikali walipwe:-

Je, tokea tamko hilo litolewe ni Wazabuni wangapi wameshalipwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Ernespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya wazabuni 2,048 wamelipwa madai yao tangu kutolewa kwa tamko na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 3 Januari, 2018 Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Kati ya wazabuni 2,048 waliolipwa, wazabuni 1,277 walihudumia sekretarieti za mikoa na 771 walihudumia Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.

Aidha, jumla ya shilingi 199,064,014,966.64 zimetumika kulipa wazabuni hao, ambapo shilingi 3,729,605,175/= zimetumika kulipa wazabuni waliotoa huduma kwa sekretarieti za Mikoa na shilingi 195,334,409,791.64 zimetumika kulipa wazabuni wa Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali. Aidha, madai haya yalilipwa baada ya uhakiki kufanyika.

Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba, Serikali itaendelea kulipa madai mbalimbali ya wazabuni kulingana na upatikanaji wa fedha sambamba na uhakiki wa madai husika. Aidha, ili kukamilisha zoezi la uhakiki kwa wakati, wazabuni wote wanaombwa kutoa ushirikiano hususan kuwasilisha taarifa na vielelezo sahihi vya madai yao pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Je, ni lini Kituo cha Misugusugu “Check Point” kitahamishwa, kwani kimekuwa kero kutokana na vumbi linalosababishwa na miundombinu mibovu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa mizigo (One Stop Inspection Station) ili kuziwezesha mamlaka za ukaguzi wa mizigo kufanya kazi ya ukaguzi katika eneo moja. Mradi huu unatekelezwa sambamba na mradi wa mizani ya ukaguzi wa mizigo iliyopo Vigwaza Mkoa wa Pwani. Taasisi zinazohusika katika mradi huu ni pamoja na TANROADS, Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ipo katika hatua za awali za kujenga na kusimika mifumo ya ukaguzi katika eneo la mradi lililopo Vigwaza, hivyo basi kituo cha ukaguzi wa mizigo kitahamishiwa kutoka Misugusugu kwenda vigwaza mara baada ya kazi ya kujenga na kusimika mifumo itakapokamilika.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-

Thamani ya Shilingi ya Tanzania inaendelea kuporomoka kila siku, kuporomoka huko kunachangia kwa kiasi fulani ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida katika kupanga mipango yao ya kimaisha:-

Je, Serikali ina mkakati gani ya kudhibiti mporomoko huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine hutegemea nguvu za soko, yaani ugavi na mahitaji. Sababu za kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni ni pamoja na tofauti ya mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi wabia katika biashara, mauzo kidogo nje ya nchi, mahitaji makubwa ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje; kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje; kuimarika kwa fedha za kigeni kutokana na kuimarika kwa uchumi wa nchi wabia katika biashara na kuzuka kwa biashara ya kuhisia na kuotea ya sarafu za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sababu zote hizi hazikuwepo na hivyo thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani ilikuwa tulivu ikilinganishwa na sarafu nyingine dhidi ya Dola ya Marekani. Kwa mfano, thamani ya shilingi ilipungua kwa wastani wa 2% kwa mwaka 2017/2018 na 2016/2017 ikilinganishwa na wastani wa 22% mwaka 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiujumla shilingi ilikuwa imara ikilinganishwa na sarafu nyingine kama vile Franc ya Rwanda iliyopungua kwa wastani wa 5% na shilingi ya Uganda iliyoshuka kwa 3.8% katika kipindi kama hicho. Utulivu wa thamani ya shilingi ulitokana na utekelezaji thabiti wa sera za fedha na bajeti pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:-

(i) Kuhakikisha kuwa ongezeko la ujazi wa fedha linaendana na ukuaji wa shughuli za uzalishaji;

(ii) Kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma ndani ya nchi;

(iii) Kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, na;

(iv) Kudhibiti hali ya wasiwasi katika soko la fedha za kigeni inayosababishwa na hisia pamoja na biashara ya kuotea ambapo Benki Kuu hununua na kuuza fedha za kigeni katika soko la jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba jukumu la kuimarisha thamani ya shilingi ni shirikishi na pia lina wadau wengi na hivyo kila mmoja anahitajika kushiriki kwa nafasi yake ili kuleta mafanikio kwa nchi. Aidha, wadau wakuu ni Serikali pamoja na wananchi. Serikali ina majukumu makuu mawili:-

(i) Serikali kupitia Benki Kuu ina jukumu la kutekeleza na kusimamia Sera ya Fedha ili kudhibiti mfumuko wa bei, viwango vya kubadilisha fedha na ujazi wa fedha katika soko; na

(ii) Kuandaa na kusimamia sera thabiti za kibajeti, kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu na kujenga miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuchochea uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wananchi ambao ndio wawekezaji, wana jukumu la kuzalisha kwa wingi bidhaa na huduma mbalimbali hususan zile zinazoipatia nchi fedha za kigeni na/au zinazoipunguzia nchi mzigo wa mahitaji ya fedha za kigeni.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-

Je, katika mwaka 2016/2017 na 2017/2018 Serikali ilikusanya kiasi gani cha kodi ya 18% (VAT) kwa taulo za kike (sanitary pads) zote zilizotengenezwa nchini na zile zilizoingizwa nchini kabla ya kodi hiyo kuondolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/ 2017, Serikali ilikusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya kiasi cha shilingi bilioni 3.01 na shilingi bilioni 2.54 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwenye bidhaa ya taulo za kike zilizoingizwa nchini pamoja na zile zilizozalishwa hapa nchini kabla ya kodi hii kuondolewa Juni, 2018.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA Aliuliza:-

Miongoni mwa malengo ya Benki ya TPB ni kupeleka huduma ya kibenki kwenye maeneo ya vijijini na pembezoni ambayo hayafikiwi na huduma hizo:-

Je, ni kwa kiasi gani lengo hilo limefikiwa mpaka kufikia mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa malengo ya Benki ya TPB ni kupeleka huduma za kibenki na pembezoni mwa miji, kuongeza wigo na mtadao wa biashara ya benki ya kutumia teknolojia ya kisasa.

Katika kutekeleza malengo haya, Benki ya TPB imefanikiwa kuboresha huduma za kibenki kupitia mtandao wa ofisi 200 za Shirika la Posta Tanzania zilizopo katika kila wilaya na baadhi ya tarafa na kutumia teknolojia ya habari na mifumo ya kisasa kutoa huduma za kibenki ikiwemo simu za kiganjani (TPB POPOTE), mawakala wa kampuni za simu, mashine za POS pamoja na ATM katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Benki ya TPB imefanikiwa pia kuongeza idadi ya matawi makubwa kutoka 30 kwa mwaka 2017 hadi 36 mwaka 2018 na matawi madogo
yaliyoongezeka kutoka 37 mwaka 2017 hadi kufikia 40 mwaka 2018. Idadi hii ya matawi inahusisha matawi ya iliyokuwa Benki ya Twiga na Benki ya Wanawake Tanzania. Matawi yote yameunganishwa kwenye mfumo wa TEHAMA unaowawezesha wateja kupata huduma za kibenki bila kutembelea matawi walipofungulia akaunti zao.

Mheshimiwa Spika, vituo vya huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta viliongezeka kutoa 40 mwaka 2017 hadi kufikia 45 mwaka 2018. Aidha mashine za ATM ziliongezeka kutoka 51 mwaka 2017 hadi kufikia 72 mwaka 2018. Vilevile, mawakala wa SELCOM POS waliongezeka kutoka 225 kwa mwaka 2017 na kufikia 670 Desemba, 2018. Vituo vyote vua huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta vimeunganishwa pia kwenye mtandao na mfumo wa TEHAMA wa benki na hivyo kutoa fursa kwa wateja wa vijijini na pembezoni mwa miji kupata huduma kwa wakati kama ilivyo kwa wateja wengine wanaohudumiwa na matawi makubwa na madogo.

Mheshimiwa Spika, jumla ya akaunti 227,052 zilifunguliwa na wananchi wa vijijini na pembezoni mwa miji kwa kutumia mfumo wa kutoa huduma za kibenki kwa njia ya simu za kiganjani, ujulikanao kama TPB POPOTE. Mfumo huu wa TPB POPOTE unasaidia wananchi kufanya malipo mbalimbali kama kuhamisha salio, kutuma fedha, kulipa ankala za maji, kununua umeme wa luku na kununua vocha za simu bila kulazimika kwenda katika matawi ya benki ya TPB. Wateja wanaweza pia kuhamisha salio kwenda katika akaunti nyingine, kuhamisha fedha kwenda katika akaunti zao za M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na Halopesa na hatimaye kuchukua fedha kupitia mawakala.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA (K.n.y. MHE. ASHA ABDULLAH JUMA) aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kuwasadia wananchi walioweka amana zao katika Benki ya FBME.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge Vitib Maalumu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39(2) na (3), amana au akiba za wateja katika benki au taasisi ya fedha, zina kinga ya bima ya amana ya kiasi kisichozidi shilingi za kitanzania 1,500,000 tu. Endapo mteja hana salio la amana la kiasi kilichozidi shilingi 1,500,000 atapata fidia ya asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, wateja walio na amana zaidi ya shilingi 1,500,000, wanalipwa shilingi 1,500,000 kama fidia ya bima ya amana, na kiasi kinachobakia kinalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufirisi. Aidha malipo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufirisi yanategemea makusanyo ya fedha kutoka kwenye mauzo ya mali pamoja na fedha zilizowekezwa na benki katika taasisi mbalimbali za fedha za ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, zoezi la kukusanya mali na fedha zilizokuwa zimewekezwa na za benki ya FBME katika taasisi mbalimbali za fedha, hususan nje ya nchi, limekumbwa na changamoto za kisheria kati ya Tanzania na nchi ya Cyprus ambako benki ya FBME ilikuwa na tawi lililokuwa linaendesha sehemu kubwa ya biashara zake, na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa ukusanyaji na ugawaji wa fedha za ufilisi. Hivyo basi tarehe ya kuanza kulipa fedha zinazotokana na ufilisi haijulikani kwa sasa kutokana na uwepo wa kesi zinazokwamisha zoezi la ukusanyaji mali na madeni ya benki ya FBME. Serikali kupitia Bodi ya Bima ya Amana, Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo katika mazungumzo na Serikali ya Cyprus ili kulipatia suala hili ufumbuzi.
MHE. HALIMA A. BULEMBO Aliuliza:-

Mkoa wa Kagera una hekta 1,593,758 zinazofaa kwa kilimo na ni mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi za EAC hivyo Kagera inaweza kuwa Kituo cha Biashara cha EAC.

Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuifanya Kagera ifaidike na uchumi wa kijiografia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni mkoa pekee hapa nchini unaopakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki ambazo ni Uganda, Rwanda na Burundi. Ili kuuwezesha mkoa huu kunufaika na fursa za kijiografia, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwa ni pamoja na mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, kipande cha Isaka-Rusumo chenye urefu wa kilometa 371, ukarabati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo yenye urefu wa kilometa 91, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 80 katika Mto Rusumo na Mradi wa Vituo vya Pamoja katika mipaka ya Rusumo na Mutukula kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kibiashara na nchi jirani za Rwanda na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya wakulima wa Kagera na bidhaa za baadhi ya viwanda vyetu vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu vinafaidika kimasoko na jiografia ya Mkoa wa Kagera. Baadhi ya viwanda vinavyonufaika na jiografia ya mkoa ni pamoja na Kagera Fish Co. Ltd. na Supreme Perch Ltd. vinavyosinika minofu ya samaki, Ambiance Distillers Tanzania Ltd. kinachozalisha vinywaji vikali, Bunena Development Co. Ltd., NK Bottling Co. Ltd. na Kabanga Bottlers Co. Ltd. vinavyozalisha maji ya kunywa na kiwanda cha Mayawa kinachosindika wine ya rosella na juice.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Serikali kupitia Mamlaka ya Biashara (Tan Trade) ilitoa mafunzo ya kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya kurasimisha biashara mipakani katika vituo vitatu vilivyopo katika Mkoa wa Kagera. Vituo hivyo ni pamoja na Kabanga, Rusumo na Mutukula vinavyopakana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda kwa mtiririko huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalilenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika mipaka yetu na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI) aliuliza:-

TPB ni Benki ya Serikali na inamilikiwa na Serikali kwa zaidi ya asilimia 90 lakini Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yanatumia Benki nyingine katika huduma za Kibenki:-

(a) Je, ni nini msimamo wa Serikali katika kutumia huduma za Kibenki?

(b) Watumishi wa Serikali na Viongozi wote wa Serikali wanatakiwa kutumia TTCL katika huduma za mawasiliano ya simu. Je, kwa nini Watumishi na shughuli zote za Serikali zisianze kutumia huduma za Kibenki kupitia Benki hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, biashara huria ya sekta ya fedha ilianza tangu mwaka 1991 mara baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, pamoja na Kanuni zake. Kupitia sheria hiyo, Wawekezaji mbalimbali walifungua Benki binafsi hapa nchini na hivyo matumizi ya huduma na bidhaa za benki kuanza kuamuliwa na nguvu ya soko ikiwa ni pamoja na huduma na bidhaa za Benki za Serikali. Benki ya TPB, kama ilivyo kwa benki nyingine haina budi kujiimarisha na kujitangaza yenyewe kwa lengo la kuuza bidhaa zake na hatimae kuvutia wateja zaidi ikiwa ni pamoja na Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi ya nguvu ya soko, Benki ya TPB imefanikiwa kujitangaza na kuimarisha huduma zake na hivyo kuvutia baadhi ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kutumia bidhaa zake. Miongoni mwa huduma za benki ya TPB zinazotumiwa na Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma kwa sasa ni pamoja na akaunti ya muda maalumu, akaunti ya biashara, malipo kwa njia ya mtandao, kubadilisha fedha za kigeni, kukusanya mapato ya Serikali, kulipa mishahara ya watumishi, mikopo kwa watumishi, kulipa pensheni za wastaafu pamoja na mikopo kwa wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Serikali pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo ya uchumi huria, Serikali haina Mamlaka ya kumlazimisha Mtumishi au Taasisi ya Umma kutumia huduma za benki yoyote, ikiwemo benki ya TPB. Hivyo basi, ni jukumu la Benki ya TPB na benki nyingine kuboresha mifumo ya huduma na bidhaa zao ili kuvutia Watumishi wa Umma, pamoja na Taasisi za Umma kuanza au kuendelea kutumia huduma zao.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Wilaya ya Rufiji ni moja ya Wilaya kongwe nchini na inakadiriwa kuwa na watu takribani 350,000; eneo la Wilaya ni kubwa na huwalazimu wananchi kusafiri umbali wa kilometa 100 kufuata huduma za kibenki.

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma za kibenki katika Wilaya ya Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kifedha na hasa karibu na maeneo ya wananchi ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Aidha, kufuatia mabadiliko ya sekta ya fedha nchini ya mwaka 1991 Serikali ilitoa uhuru kwa mabenki kufanya tathimini na utafiti ili kuamua kuhusu maeneo ya kupeleka huduma za kibenki kulingana na taarifa za utafiti uliofanywa pamoja na vigezo vya benki husika. Kwa kuwa benki zinajiendesha kibiashara maamuzi ya kufungua tawi sehemu yoyote hapa nchini huzingatia vigezo hivyo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Wilaya ya Rufiji wanapata huduma za kifedha kupitia kituo cha makusanyo ya fedha cha NMB yaani cash collection point kilichopo Kata ya Utete pamoja na mawakala wa benki hususan Benki ya NMB na CRDB waliopo katika Wilaya ya Rufiji.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji aendelee kuwahimiza wananchi wake kutumia fursa zilizopo za kupata huduma za kifedha kupitia kituo hicho cha makusanyo ya fedha cha NMB, mawakala wa benki na simu za mkononi wakati Serikali ikiendelea kufanya jitihada za kuboresha miundombinu muhimu pamoja na kufanya majadiliano na kuyashawishi baadhi ya mabenki ili kuona jinsi ya kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyoweza kusababisha gharama za uendeshaji wa shughuli za kibenki katika Wilaya ya Rufiji kuwa juu.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imekuwa na majina mengi katika Idara ya Ukaguzi toka Ofisi ya CAG kama vile Hati safi, Hati inayoridhisha na Hati chafu:-

(a) Je, Shirika au Halmashauri kupata hati safi ni ishara kwamba Shirika au Halmashauri husika halina ubadhirifu wa mali ya Umma kwa kuwa kuna kila dalili kuwa kutolewa kwa hati safi ni dalili ya wazi ya kuficha ubadhirifu katika baadhi ya Mashirika na Taasisi za Umma?

(b) Je, lini Serikali itafuta utaratibu huo ambao umekuwa kinga ya ubadhirifu wa mali ya Umma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Boniphace Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 inampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya kaguzi mbalimbali ambazo ni Ukaguzi wa Hesabu (Financial Audits), Ukaguzi wa Kiuchunguzi (Forensic Audits), Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Audits) na Ukaguzi Maalum (Special Audits). Lengo Kuu la Ukaguzi wa Hesabu (Financial Audits) ni kutoa maoni kama Hesabu zinazokaguliwa zinaonyesha hali halisi ya mapato na matumizi ya Serikali kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Fedha. Maoni haya hutolewa kwa njia ya hati za ukaguzi ambazo zimegawanyika katika makundi manne ambayo ni hati inayoridhisha; hati yenye shaka hati isiyoridhisha na hati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hati inayoridhisha hutolewa wakati taarifa za fedha zilizowasilishwa na kukaguliwa zinapokuwa zimezingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Sekta ya Umma na Sheria na Kanuni za Fedha za Umma. Hati hii huonesha taarifa za fedha zinatoa taswira ya kweli na hali halisi ya mapato, matumizi, mali na madeni ya taasisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya kuwa ‘hati inayoridhisha’ inatoa tafsiri ya kutokuwepo kwa kila aina ya ubadhirifu siyo sahihi kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, maoni ya ukaguzi yanatolewa kwa malengo maalum ya kuwafahamisha watumiaji wa taarifa za fedha kama taarifa hizo zinaonyesha ukweli na hali halisi ya hesabu za mizania (financial positions) kwa tarehe husika, taarifa za mapato na matumizi (financial performance) pamoja na taarifa ya mtiririko wa fedha (cash flows) kwa kipindi kilichokaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, dhana ya ukaguzi wa hesabu inajikita katika masuala ambayo wakaguzi wanaamini kuwa ni mazito na yana athari kubwa kwenye taarifa za fedha za taasisi husika. Hii ina maana kuwa, mambo ambayo hayana athari kwenye taarifa za fedha yanashughulikwa na mifumo ya udhibiti wa ndani ya taasisi husika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu haya ya sehemu (a), napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, utaratibu huu ndiyo unaotumika dunia nzima, hivyo Serikali haina mpango wa kufuta hati inayoridhisha yenye maoni ya kikaguzi wala kuingilia namna taaluma ya ukaguzi nchini inavyoendeshwa. Kutoa utaratibu mwingine itakuwa ni kukiuka Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Tarifa za Fedha katika Sekta ya Umma na pia Viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi ambavyo Taifa na Serikali yetu imeviridhia vitumike.
MHE. JUMA S. NKAMIA ali uliza:-

Je, Serikali imekusanya kiasi gani cha kodi kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi nchini katika mwaka wa fedha 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Suleimani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004, Kifungu cha 7; “kila mtu anayepata mapato yatokanayo na ajira ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajibika kulipa kodi ya mapato kulingana na kipato chake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2017/2018, jumla ya shilingi milioni 1,733.6 zilikusanywa kama malipo ya kodi ya ajira kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi hapa nchini.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-

Je, ni sababu gani zimekwamisha uanzishwaji wa Benki ya Wanawake kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa hatuna Benki inayoitwa ya Benki Wanawake Tanzania, baada ya iliyokuwa Benki ya Wanawake Tanzania kuunganishwa na Benki ya TPB. Hivyo basi, huduma za iliyokuwa Benki ya Wanawake Tanzania zinaendelea kutolewa na Benki ya TPB ambapo Benki ya TPB imeanzisha dirisha maalum la akina mama katika matawi yake yote 76 yaliyopo nchini Tanzania, yakiwemo matawi ya Unguja na Pemba ili kukidhi mahitaji ya huduma za kibenki kwa akina mama kote nchini. Kwa muktadha huu, wanawake na wananchi wote wa Zanzibar wataendelea kuhudumiwa kupitia dirisha hilo maalum.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutumia Kituo cha Forodha Manyovu ili kupitisha mizigo kwenda Burundi kwa kiwango cha kutosha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Forodha Manyovu kinatoa huduma za forodha mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Mkoa wa Kigoma. Kituo hicho kinatoa huduma kidogo ikilinganishwa na uwezo wake kwa sababu ya changamoto ya umbali wa transit route ya Dar-es-Salaam hadi Burundi kupitia Manyovu.

Mheshimiwa Spika, umbali wa transit route ya Dar-es- Salaam – Isaka – Nyakanazi hadi Manyovu ni kilometa 1457 wakati transit route ya Dar-es-Salaam – Isaka – Nyakanazi hadi Kabanga ni kilometa 1330. Tofauti ya umbali kati ya transit route ya Kabanga na Manyovu ni kilometa 127. Aidha, transit route ya Dar-es-Salaam – Manyoni – Tabora hadi Manyovu ni kilometa 1273, lakini route hii pia inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa sehemu ya barabara ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto ya umbali wa transit route ya Dar-es-Salaam - Isaka – Nyakanazi - Manyovu pamoja na ubovu wa sehemu ya barabara ya transit route ya Dar-es-Salaam – Manyoni – Tabora - Manyovu wafanyabiashara wengi hutumia Kituo cha Forodha Kabanga ili kuokoa sehemu ya gharama ya usafiri na usafirishaji.

Aidha, pamoja na changamoto hizi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Kituo cha Forodha Manyovu kimeunganishwa na Mfumo wa Forodha wa Uthaminishaji Mizigo wa TANCIS na kina uwezo wa kutoa huduma za kiforodha kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu. Vilevile, taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Uhamiaji, Polisi na Wizara ya Kilimo zimeanzisha Ofisi katika kituo hicho kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiforodha.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Serikali kwamba huduma za forodha katika Kituo cha Forodha Manyovu zitaimarika zaidi baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa vipande vya barabara ya Manyoni – Tabora – Uvinza; ujenzi wa barabara ya Kasulu – Manyovu na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa, pamoja na mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-

Je ni nini maana ya dhana ya uchumi kukua ukioanisha na maisha ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali Ia Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhana ya uchumi kukua ikioanishwa na maisha ya wananchi inaweza kutafsiriwa katika dhana kuu mbili. Dhana ya kwanza ni kwa kuangalia upatikanaji, ubora na gharama ya huduma za jamii zinazotolewa na Serikali. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Mathalani, kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, muda na gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa zimepungua, sambamba na gharama za matengenezo ya vyombo vya usafiri na usafirishaji. Aidha, upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi umepunguza kwa kiasi kikubwa adha na gharama ya matibabu kwa wananchi. Pia, ugharamiaji wa elimu msingi bila malipo na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni miongoni mwa matokeo ya kukua kwa uchumi. Kwa muktadha huu, ni muhimu kutafsiri dhana ya ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi kwa kuangalia kiwango cha upatikanaji, ubora na gharama za huduma muhimu za jamii zinazotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, dhana ya pili ya kutafsiri ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi ni ushiriki wa wananchi wenyewe katika shughuli za kiuchumi. Ukuaji wa uchumi ni matokeo ya wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uzalishaji mali na huduma. Wananchi wanaoshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi hufikiwa moja kwa moja na matokeo chanya ya ukuaji wa uchumi ikilinganishwa na wale ambao wapo nje ya mfumo wa uzalishaji. Aidha, wananchi wanaoshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi wananufaika kwa tafsiri ya dhana zote mbili; yaani kupitia huduma za jamii zinazotolewa na Serikali yao pamoja na matokeo ya moja kwa moja ya shughuli wanazofanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za dhati kabisa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, ili kila Mtanzania aweze kutumia kikamilifu fursa zilizopo kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na huduma. Miongoni mwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara Nchini. Lengo ni kuhakikisha kwamba, tunapunguza kwa sehemu kubwa gharama za uwekezaji na kufanya biashara ili kuvutia wawekezaji mahiri katika sekta mbalimbali, hususan viwanda vinavyotumia malighafi za ndani. Ni matarajio ya Serikali yetu kuwa, uwekezaji katika viwanda utaongeza ajira na uzalishaji katika Sekta ya Kilimo, sekta ambayo huajiri idadi kubwa ya watu hapa nchini, lakini imekuwa ikikua kwa kasi ndogo na hivyo kuwa na mchango mdogo katika kupunguza umaskini wa wananchi walio wengi, hususan wakulima.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Miongoni mwa kero za Muungano ni wananchi wa Zanzibar waletapo magari yao Tanzania Bara kutoruhusiwa kutembea mpaka yabadilishwe namba, wakati magari yanayotoka Bara yafikapo Zanzibar yanaruhusiwa kutembea kwa muda wote bila ya bughudha yoyote:-

(a) Je, Serikali inalifahamu suala hili?

(b) Kama ndiyo, je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kutatua suala hili ili Watanzania waendelee kufaidi matunda ya Muungano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu kwamba magari yaliyosajiliwa Zanzibar hayaruhusiwi kutembea Tanzania Bara bila kibali maalumu kwa sababu sheria zinazotumika kusajili vyombo vya moto, kati ya pande mbili za Muungano siyo sheria za Muungano. Kwa upande wa Tanzania Bara, usajili wa vyombo vya moto unasimamiwa na Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 pamoja na Kanuni zake na kwa upande wa Zanzibar usajili wa vyombo vya moto unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Barabara Na.7 ya mwaka 2003. Aidha, majukumu ya usajili wa vyombo vya moto kwa upande wa Zanzibar husimamiwa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Tanzania Bara husimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na utaratibu wa sasa wa wananchi wa Zanzibar kuomba kibali maalum ili kutembelea magari yao Tanzania Bara, Serikali za pande mbili zipo katika majadiliano ili kuhuisha sheria na mifumo ya ukukotoaji kodi ya magari na hivyo kuwawezesha wananchi kutembelea magari yao pande zote za Muungano bila usumbufu. Aidha, mchakato wa kuhuisha sheria na mifumo ya ukokotoaji kodi utafuata taratibu zote zilizowekwa na Bunge lako Tukufu pamoja na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya madeni mbalimbali ya wazabuni wanaoidai Serikali:-

Je, Serikali imefikia hatua zipi katika kuhakikisha inalipa madeni ya wazabuni nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kulipa madeni yaliyohakikiwa na kukubaliwa kupitia bajeti inayoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Kati ya mwaka 2016/ 2017 na robo ya kwanza ya mwaka 2019/2020, Serikali imetoa jumla ya shilingi 2,528,619,142,345.21 kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni, wakandarasi/wahandisi washauri, watoa huduma na madeni mengineyo. Kati ya kiasi hicho, jumla ya shilingi 379,072,545,151.14 zimetolewa kulipa madeni ya wazabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupunguza madeni, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwenye bajeti kila mwaka kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa na kukubaliwa, kuweka sheria na kanuni zake kama vile Sheria ya Bajeti Sura 439 na Kanuni zake; Sheria ya Manunuzi, Sura 410; Sheria ya Fedha, Sura 348 na kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali ikiwemo Waraka Na.1 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali unaotolewa kila mwaka kuhusu utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti unaotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa, Serikali imeandaa mkakati wa kulipa madeni yaliyohakikiwa na kuzuia ulimbikizaji wa madeni. Madeni yanayohusika kwenye mkakati huo ni yaliyozalishwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa yakiwemo madeni ya watumishi, wazabuni na watoa huduma, pamoja na madeni ya wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya madeni, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa kwa kuzingatia mwelekeo ulioandaliwa wa kulipa madeni hayo kulingana na upatikanaji wa mapato.

Aidha, lengo la Waraka Na.1 wa Mlipaji Mkuu unaotolewa kila mwaka ni kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kudhibiti madeni na kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati ikiwemo kuzuia uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Wafanyakazi wa Kiwanda cha MUTEX ambacho kilifungwa tangu mwaka 1984, wamekuja kulipwa stahiki zao Disemba, 2018 na badala ya kulipwa shilingi 400,000/= kwa gharama ya kila mwezi wakalipwa shilingi 100,000 tu:-

Je, Serikali haioni kuwa inawakandamiza wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilisimamisha uzalishaji katika kiwanda cha Nguo cha Musoma (Musoma Textile Mills Limited – MUTEX) mwaka 1994 baada ya kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mtaji na ongezeko kubwa la madeni kutoka iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Kiwanda cha MUTEX kilifilisiwa na hatimaye kuuzwa mwezi Machi, 1998 kwa Kampuni ya LALAGO Cotton Ginnery and Oil Mills Company Limited.

Mheshimiwa Spika, kikao kati ya wadai, Serikali na Mfilisi kilifanyika Septemba 23, 2005 na kuridhia mapendekezo ya kulipa kiasi cha shilingi 161,347,359 kwa wafanyakazi 935 waliokuwepo kiwandani wakati Serikali ilipofanya uamuzi wa kusitisha uzalishaji. Maamuzi ya kulipa kiasi hicho cha fedha yalizingatia sheria, kanuni na taratibu za ufilisi.

Mheshimiwa Spika, baada ya zoezi la ufilisi kukamilika, wafanyakazi 512 pekee ndiyo waliojitokeza kuchukua mafao yao na wafanyakazi 423 waligoma kupokea mafao yao kwa madai kwamba, nauli ya familia na gharama za kusafirisha mizigo ni ndogo. Wafanyakazi hao 423 walifungua kesi katika Mahakama ya Kazi ya Tanzania, shauri la Uchunguzi wa Mgogoro Na. 49 wa mwaka 2007. Mahakama ilitoa tuzo mnamo tarehe 10 Juni, 2008 na kutupilia mbali shauri hilo na kuamuliwa wadai waende kwa Mfilisi kuchukua stahili zao.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, wafanyakazi hao hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama na kufungua shauri lingine la kuomba marejeo katika Mahakama ya Kazi Tanzania shauri la Maombi ya Marejeo Na. 77 la Mwaka 2008. Mahakama hiyo ilitoa tuzo tarehe 15 Februari, 2010 na kutupilia mbali shauri la marejeo. Uamuzi ukabaki kuwa wafanyakazi hao 423 waliogoma kuchukua mafao yao waende kwa Mfilisi kuchukua stahili zao kama ilivyokubalika katika kikao cha wadau.

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kupokea maombi ya malipo kutoka kwa wafanyakazi hao mwaka 2018, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya uhakiki wa wafanyakazi hao ili kujiridhisha na hatimaye kufanya malipo. Awali jumla ya wafanyakazi 219 walijitokeza na wasimamizi wa mirathi 14 na hivyo kulipwa jumla ya shilingi 44,591,559. Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya tena zoezi la uhakiki mwezi Juni, 2019 kwa wafanyakazi ambao hawakujitokeza kwa uhakiki wa awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika zoezi hilo, jumla ya wafanyakazi 115 walijitokeza tena pamoja na wasimamizi wa mirathi 27 ambao kwa ujumla wanastahili kulipwa shilingi 20,738,863. Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na taratibu za kulipa fedha hizo kwa wahusika katika mwaka huu wa Fedha 2019/2020. Aidha, Serikali inafuatilia kwa karibu malalamiko yote yanayohusu tofauti ya kiwango cha malipo yaliyofanyika hivi karibuni ikilinganishwa na kiwango kilichoidhinishwa kwenye kikao cha pamoja kati ya Mfilisi, wadau pamoja na Serikali kuona kama yana msingi na ukweli wowote.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-

Tangu TRA ianze kukusanya kodi ya majengo imekusanya kiasi gani katika Mkoa wa Kodi Temeke kwa mwaka 2017/2018 na ni asilimia ngapi ya lengo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza kukusanya kodi ya majengo (property rate) katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 baada ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura 290 kufanyika kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2016. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Mkoa wa Kikodi wa Temeke ulikusanya jumla ya shilingi 3,707,731,450 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya jumla ya shilingi 6,197,367,187.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-

ATM za Benki nyingi hapa nchini hazikidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa ATM za Benki zinawekewa mifumo inayokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ilipoanza maboresho ya mifumo ya malipo nchini mwaka 1996, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kusimamia usimikaji wa mifumo ya kisasa, mahiri na salama ili kuendana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya teknolojia. Maboresho hayo ya mifumo yanalenga pamoja na mambo mengine kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, hususan walemavu.

Mheshimiwa Spika, Mei, 2017 Benki Kuu ya Tanzania ilitoa mwongozo wa mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ikiwa ni mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa huduma za malipo kwa njia ya mtandao yanafanyika kwa usalama na kukidhi mahitaji ya makundi yote katika jamii. Miongoni mwa vipengele muhimu na nyeti, hususan kwa watu wenye ulemavu vilivyoainishwa kwenye mwongozo huo ni alama za utambuzi, usalama wa mifumo na uwezo wa mifumo wa kutunza siri za wateja. Pamoja na Serikali kutoa mwongozo huo, benki zetu zote hapa nchini hazijafanikiwa kusimika ATM maalum na rafiki kwa watu wenye ulemavu, hususan watu wenye ulemavu wa macho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba teknolojia ya ATM kwa watu wenye ulemavu wa macho ni ngeni na pia ina mfumo au mahitaji ya ziada ikilinganishwa na ATM za kawaida.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya uduni wa baadhi ya miundombinu kwa watu wenye ulemavu, hususan walemavu wa miguu imetatuliwa kwa sehemu kubwa na hivyo kuwa rafiki katika maeneo mengi yanayotoa huduma za kibenki kwa kutumia mashine za ATM. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili ili kuhakikisha kuwa mifumo ya miamala kwa njia ya ATM inakuwa rafiki kwa makundi yote wakiwemo watu wenye ulemavu.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya mtaji.

(a) Je, Benki ya Kilimo ina mtaji kiasi gani?

(b) Je, Benki ya Kilimo ina mkakati gani wa kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilipatiwa mtaji wa shilingi bilioni 60 mwezi Novemba, 2014. Aidha, tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2015, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kujiendesha na kukuza mtaji wake hadi kufikia shilingi bilioni 67.5 zilizorekodiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo inakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo na hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake, Serikali imeipatia benki hii kiasi cha shilingi bilioni 103 kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Aidha, kwa sasa benki inaendelea na mchakato wa kukamilisha masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa shilingi bilioni 103 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha huduma zake Mkoani Mbeya na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka shilingi milioni 799.9 mwezi Desemba, 2017 hadi shilingi bilioni 2.54 kwa taarifa ya mwisho wa mwezi Aprili, 2019. Mikopo hiyo imetolewa kwa miradi saba ya kilimo na kuwanufaisha wakulima 509 wa Wilaya za Mbozi, Momba na Mbarali.

Napenda pia kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kufungua ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoani Mbeya. Malengo ya ufunguzi wa ofisi hiyo ni kuhakikisha kwamba benki inasogeza huduma zake karibu zaidi na wateja wake ambao ni wakulima wote wa Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa kilimo nchini ikiwa ni pamoja na wakulima wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili waweze kupata maelekezo sahihi ya uandaaji wa miradi itakayokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na benki yao na pia kupatiwa maelezo ya fursa nyinginezo zinazopatikana katika benki yao.
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuliza:-

Idadi ya watu nchini inaongezeka kwa kasi sana na watu wanahitaji maendeleo; aidha ukuaji huu una matokeo hasi na chanya:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kutumia au kudhibiti kasi ya idadi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa idadi ya watu duniani unaonyesha kwamba idadi kubwa ya watu ni fursa kwa nchi iwapo baadhi ya mambo matano yatafanyika:-

(i) Kuboresha maisha ya watoto na kuboresha elimu na uwezeshaji kwa wanawake;

(ii) Kuimarisha uwekezaji katika afya ili kuwa na nguvukazi bora na yenye tija;

(iii) Kuimarisha uwekezaji katika elimu ya juu ili kuwa na nguvukazi yenye elimu, ujuzi na ubinifu;

(iv) Mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuharakisha ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa kazi kwa ajili ya nguvukazi iliyopo; na

(v) Mageuzi ya Sera ili kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuhakikisha uwajibikaji hasa katika rasilimali za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Mpango wetu wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 ni kujenga uchumi wa viwanda ili kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Mpango huu wa Pili umejikita zaidi katika uwekezaji wa kimkakati katika Sekta ya Viwanda kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kusambaza umeme mijini na vijijini, kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakati, kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujenga bwawa kubwa la kufua umeme katika Mto Rufiji na kuimarisha huduma za jamii kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji, hospitali na Vituo vya Afya vya Umma, shule pamoja na kutekeleza kwa ufanisi Sera ya Elimu Bila Malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kufungamanisha fursa za kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu; na jitihada hizi zinalandana na mambo yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya utafiti ya idadi ya watu duniani na athari zake. Hata hivyo, matokeo chanya yataonekana kama kila Mtanzania atashiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na huduma za jamii kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo baya kudhibiti ongezeko la idadi ya watu kama familia au Taifa limefikia kiwango cha mwisho cha kutumia rasilimali (optimal utilization) ya rasilimali zake za asili pamoja na mikakati mingine mbadala. Hata hivyo, Taifa letu bado lina rasilimali asili za kutosha kama vile ardhi ya kulima, bahari, maziwa, mito na mabonde, madini, misitu, jiografia ya usafiri na usafirishaji pamoja na fursa za utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu letu kama Taifa kuanzia ngazi ya kaya kuakisi jitihada zinazofanywa na Serikali yetu na hatimaye kutumia fursa hizi kwa ufanisi kwa lengo la kuongeza kasi ya uzalishaji mali pamoja na kuongeza kasi ya kupunguza umasikini badala ya kuogopa ongezeko la idadi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa Serikali imejielekeza zaidi katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara na hivyo kutumia ongezeko la idadi ya watu kama fursa ya nguvukazi ya kuzalisha mali pamoja na soko la bidhaa na huduma.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-

(a) Je, ni lini Benki ya FBME italipa wateja amana zao zilizokuwepo kwenye Benki hiyo?

(b) Je, Benki iko katika hali gani sasa?

(c) Je, Benki Kuu ya Tanzania ina dhamana gani katika kulinda Mabenki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango na kwa kuzingatia maombi ya Mheshimiwa Jaku, naomba kujibu swali lake lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Benki ya FBME Limited ilifutiwa leseni ya kufanya biashara hapa Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 8 Mei, 2017 kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya kutakatisha fedha huko nchini Marekani. Aidha, Benki Kuu iliteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa Mfilisi wa Benki hiyo. Katika kitimiza wajibu wake wa msingi, Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipa fidia kwa mujibu wa Sheria kwa waliokuwa na amana katika benki hiyo kuanzia mwezi Novema, 2017 na bado zoezi hilo linaendelea.

Hadi kufikia tarehe 9 Septemba, 2019 jumla ya kiasi cha shilingi milioni 2,404.2 kimelipwa kwa wateja 3,426 kama fidia ya Bima ya Amana. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 55.9 ya kiasi chote kilichotarajiwa kulipwa kama fidia ya Bima ya amana kwa wateja wote 6,628 waliopo Tanzania pamoja na wateja waliopo nje ya nchi (Tanzania International Banking Depositors). Aidha, jumla ya shilingi milioni 2,401.2 zimelipwa ikiwa ni asilimia 83.3 ya lengo la kulipa jumla ya shilingi milioni 2,882.6 kwa wateja waliopo Tanzania tu.

Mheshimiwa Spika, wateja waliokuwa na amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 watalipwa kiasi kilichobakia kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi. Kiasi kitakacholipwa kwa wenye amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya mali za benki pamoja ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wadeni wa benki hiyo.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa sasa Benki ya FBME Limited ipo katika hatua za ufilisi na hivyo haiendeshi shughuli zozote za kibenki hapa nchini.

(c) Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 imeipa Benki Kuu ya Tanzania mamlaka ya kutoa leseni, kutunga Kanuni, kusimamia benki zote zinazochukua amana za wateja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya benki zinazoendesha biashara bila kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Benki Kuu imepewa mamlaka ya kusimamia na kudhibiti benki na taasisi za fedha ili kuhakikisha kuwa amana za wateja zinakuwa salama pia kuna usalama, utulivu na uthabiti wa Sekta ya Fedha na uchumi kwa ujumla. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, ni Watumishi wangapi wanahitajika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili Mamlaka hiyo iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo Mbunge Viti maalum kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Mamlaka ya Mapato Tanzania iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi inahitaji watumishi wapatao 7,000 wa kada mbalimbali za kiutumishi.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-

Mwaka 2018 Serikali ilipitisha Sheria ya Udhibiti ya Taasisi Ndogo za Fedha SACCOS, VICOBA, Vikundi vya kuchangishana na kukopeshana, vyote vipate usajili na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania:-

(a) Je, zoezi hili limeshatekelezwa kwa asilimia ngapi na ni taasisi ngapi zimesajiliwa?

(b) Je, Serikali haioni kuwa zoezi hili ni over – regul ation na kuwanyima fursa ambayo imekuwa ikiwasaidia wakopaji na wakopeshaji wadogo kusaidiana katika jamii zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Mwaka 2018. Baada ya Sheria hiyo kutungwa Serikali ilianza mchakato wa kuandaa Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha. Kanuni hizo zinalenga madaraja manne ya watoa huduma yaliyoanishwa kwenye Sheria. Aidha, mchakato huu ulihusisha ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za walengwa ili kuweza kutengeneza kanuni zinazozingatia hali halisi ya biashara zao pamoja na matakwa ya sheria. Mchakato wa kuandaa Kanuni umekamilika na hivyo kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na. 575 tarehe 2 August Mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mujibu wa sheria hii, walengwa wamepewa makataa yaani grace period ya mwaka mmoja baada ya kununi kutolewa ili waweze kujiandaa kulingana na matakwa ya kanuni hizo. Kanuni zitaanza kutumika rasmi baada ya muda wa makataa kupita ikiwemo zoezi la usajili. Hivyo basi, hadi sasa hakuna taasisi yoyote iliyosajiliwa kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kutungwa kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha siyo kunyima jamii fursa ya kusaidiana kwa njia ya kukopesha na kukopeshana, bali ililenga kutatua changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2000. Changamoto hizo ni pamoja na kiwango kikubwa cha riba na ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda walaji na wadau wa sekta ndogo ya fedha kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio ya Serikali yetu kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, itaimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta ya huduma ndogo za fedha na hivyo kuakisi matarajio na mahitaji ya wadau, kasi ya ukuaji na mchango wake katika sekta nzima ya fedha na uchumi wa taifa letu kwa ujumla.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa kodi kwenye taulo za kike (pads) jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha ya Wanawake na Wasichana mpaka sasa ni mwaka mmoja tangu kodi hizo ziondolewe lakini bei ya taulo za kike haijashuka licha ya kuondolewa kwa kodi hizo Nchi nzima.

Je, ni lini Serikali itasimamia kwa ukamilifu suala hilo ili bei za taulo za kike zishuke na kusaidia afya za Wanawake hususani Wasichana?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye taulo za kike ililenga kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo na mojawapo ya athari chanya iliyotegemewa ni kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo. Pamoja na Serikali kuchukua hatua ya kuondoa kodi imebainika kuwa hakuna mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko. Hii inatokana na ukweli kuwa, bei ya bidhaa katika soko inaamuliwa na nguvu ya soko pamoja na gharama nyingine za uzalishaji na uendeshaji kama vile gharama za malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji, teknolojia, ushindani katika soko, umeme, maji na majitaka, usambazaji, ubora wa bidhaa n.k. Hivyo basi kutokushuka kwa bei ya taulo za kike kunabainisha kwamba kodi inachangia sehemu ndogo sana katika kupanga bei ya bidhaa kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza na kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mfumo wetu wa uchumi ni mfumo wa soko huria, bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko yaani ugavi na mahitaji ya soko. Fursa pekee iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa kwa kutumia teknolojia yenye gharama nafuu katika kutengeneza taulo za kike, kupunguza gharama nyingine sambamba na kuchochea ushindani wa bei katika soko na sio Serikali kuondoa kodi na kupanga bei ya bidhaa.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. JAKU HASHIM AYOUB) aliuliza:-

(a) Je, ni lini TRA itakaa na wafanyabiashara wa Tanzania kusikiliza vilio vyao licha ya kila Mkoa unayo Ofisi ya TRA?

(b) Je, ni sababu gani zinazofanya mizigo inayotoka Zambia, Uganda, Kenya, DRC haipati usumbufu inapoingia Jijini Dar es Salaam katika bandari lakini mizigo kutoka Zanzibar inakuwa kero kubwa inapoingia Jiji la Dar es Salaam kupitia bandarini?

(c) Je, ni lini TRA itaweka Ofisi kila Mkoa kusikiliza kero za wafanyabiashara ambao wanahisi wanaonewa na vilevile kuweka Mwanasheria kila Ofisi ili pasiwepo na manung’uniko ya wafanyabishara kuonewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, miongoni kwa kazi za kila siku za Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara ili kuwawezesha kufanyabiashara zao bila usumbufu. Mamlaka ya Mapato Tanzania hufanya mikutano au vikao na wafanyabiashara katika ngazi ya Wilaya, Mikoa na Taifa ili kutoa elimu ya kodi, kusikiliza vilio au kero zao na kuzifanyia kazi; hurusha vipindi maalumu katika televisheni na redio vinavyotoa elimu ya kodi kwa wananchi na kujibu kero za wafanyabiashara; huboresha na kuweka kwenye tovuti ya Mamlaka taarifa mbalimbali za kikodi na pia hubuni na kuanzisha mifumo, vituo na vilabu rafiki vya kikodi ili kujibu vilio vya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanzisha call centre, Makao Makuu Dar es Salaam pamoja na Kituo cha Huduma za Ushauri kwa Mlipakodi kilichopo Somara, Jijini Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuwasilisha maoni na kero za kikodi kwa wakati. Pia, Wenyeviti wa Kamati za Mapato za Mikoa na Wilaya ambao ni Wakuu wa Mikoa na Wilaya wamekuwa wakisilikiza kero za walipakodi katika Mikoa na Wilaya zao na kuzitatufia ufumbuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii, kuwahimiza wananchi kutembelea Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania zilizopo katika maeneo yao na kuhudhuria vikao vinavyoitishwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kuwasilisha maoni na kero za kikodi.

(b) Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba bidhaa za Zanzibar zinapata usumbufu ikilinganishwa na bidhaa za nchi jirani zinapoingia Tanzania Bara kwa sababu bidhaa zote zinafuata utaratibu wa forodha unaofanana. Bidhaa zinazoingia Tanzania Bara kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupata msamaha wa Ushuru wa Forodha lakini hulipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani pamoja na Ushuru wa Bidhaa.

(c) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ina Ofisi katika Mikoa yote ya Tanzania pamoja na baadhi ya Wilaya zake. Aidha, baadhi ya Mikoa ina vituo maalum vya huduma za kodi hususani Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Mheshimiwa Spika, pili, kila Mkoa una Mwanasheria na Afisa Elimu ya Kodi kwa ajili ya kutoa elimu, kusikiliza na kutatua kero za walipakodi. Pia, Mamalaka imeweka utaratibu wa Mameneja wa Mikoa ya kikodi kukutana na walipa kodi kila Alhamisi ili kusikiliza kero zao na kuzitatua. Hatua hii ina nia ya kujenga imani ya walipakodi, kutatua kero na kukuza ridhaa ya ulipaji kodi kwa hiari.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuliza:-

Kumekuwa na biashara haramu za mitandao maarufu kama pyramid schemes. Biashara ambazo zimeshamiri sana miji ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti biashara hizo ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa?

(b) Je, ni kampuni ngapi za aina hiyo ambazo zimeingia nchini na kupata kibali cha kuendesha biashara za aina hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura Na. 16 kifungu cha 171A, 171B na 171C, biashara ya pyramid schemes au upatu, ni haramu na huendeshwa kinyume na sheria na taratibu za nchi. Ili kudhibiti biashara hiyo, Serikali huchukua hatua dhidi ya wahusika kama ilivyofanya kwa taasisi ya DECI. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ubaya na madhara ya biashara ya upatu. Mathalani tarehe 14 Juni, 2017 Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ilitoa taarifa kwa umma kuhusu madhara ya biashara ya upatu na kuwahimiza wananchi kutoa taarifa kwenye vyombo vinavyohusika pindi wanapopata taarifa ya baadhi ya watu au taasisi kujihusisha na biashara ya upatu.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya upatu siyo biashara halali, hivyo hakuna mtu au taasisi yenye leseni ya kufanya biashara hiyo. Kampuni au watu binafsi wanaojihusisha na biashara hiyo wanavunja sheria na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-

Nchi Wahisani na Wa shirika wa Maendeleo wamekuwa wakishindwa kuleta misaada na ahadi zao kwenye utekelezaji wa Bajeti ya Maendeleo kwa wakati na nyakati nyingine kushindwa kuleta kabisa katika kipindi cha miaka mitatu ya fedha mfululizo iliyopita ya 2016/2017, 2017/ 2018 na 2018/2019:-

Je, Serikali inatueleza ni kitu gani kinasababisha hali hii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishirikiana na nchi Wahisani pamoja na Washirika wa Maendeleo katika kutekeleza Bajeti yake kwa kupokea fedha za Bajeti ya Maendeleo kupitia Misaada na Mikopo nafuu kwa mujibu wa makubaliano ya kimkataba.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia 2016/2017 hadi 2018/2019 Washirika wa Maendeleo wamekuwa wakitimiza ahadi zao kwa wastani wa zaidi ya asilimia 77 kwa mtiririko ufuatao:-

Mheshimiwa Spika, mw aka 2016/2017 ki asi kilichopokelewa kutoka kwa Washiriki wa Maendeleo kilikuwa ni shilingi bilioni 2,474 sawa na asilimia 69 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 3,601; mwaka 2017/2018 kiasi kilichopokelewa kilikuwa ni shilingi bilioni 3,351 sawa na asilimia 84 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 3,971; na mwaka 2018/2019 kiasi kilichopokelewa kilikuwa ni shilingi bilioni 2,082 sawa na asilimia 78 ya lengo la kipindi hicho la kupokea shilingi bilioni 2,676.

Aidha, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2019 hadi Februari, 2 020 fe dha za mis aa da na mikop o nafuu zilizopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zimefikia jumla ya shilingi bilioni 1,631.19 sawa na asilimia 90 ya lengo la kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi, siyo sahihi hata kidogo kusema kwamba kuna nyakati nyingine Washirika wa Maendeleo wamekuwa hawatimizi ahadi zao kabisa.