Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stanslaus Shingoma Mabula (8 total)

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza ujenzi wa nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilizoanza kujengwa tangu mwaka 2012 na sasa zinazidi kuwa magofu ili zisaidie hizo familia chache zipatazo 13?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilianza kujengwa mwaka 2012. Kutokana na ufinyu wa bajeti nyumba hizo hazikuweza kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga fedha katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jimbo la Nyamagana ni jimbo pekee lililochangia mradi wa ujenzi wa nyasi bandia kupitia TFF shilingi 160,000,000.
Je, ni lini Serikali itawasisitiza TFF kuhakikisha kuwa uwanja huu unakamilika kwa wakati na kuendeleza malengo yaliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamangana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uboreshaji wa uwanja wa Nyamagana wa kuweka nyasi bandia ulianza mwaka 2014 ukiwa na thamani ya dola za Kimarekani 737,886 sawa na shilingi za Kitanzania 1,193,161,662. Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) lilitoa msaada kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kiasi cha dola za Kimarekani 618,946 sawa na shilingi za Kitanzania 1,000,835,682 na Halmashauri ya Nyamangana ilichangia dola za Kimarekani 118,943 sawa na shilingi za Kitanzania 192,330,831.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi hizo bandia zimegharimu tozo kiasi cha dola za Kimarekani 100,121.93, sawa na shilingi za Kitanzania 220,268,400 ikujumuisha import duty na VAT. TFF kama msimamizi wa mpira wa miguu kwa niaba ya Halmashauri ya Nyamangana na Serikali, wameshughulikia mchakato wa kutoa msamaha wa tozo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi bandi tayari zimewasili Dar es Salaam tangu tarehe 17 Aprili, 2016. Baadhi ya vifaa tayari vimeshafika katika Uwanja wa Nyamagana na mkandarasi amekwishaanza kazi ya ukarabati wa uwanja huo. TFF sasa wako katika mchakato wa kumalizia kusafirisha vifaa vilivyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba ukarabati wa uwanja wa Nyamagana kuufanya uwe wa nyasi bandia unahitaji umakini mkubwa ili uwe mzuri, imara na wenye hadhi ya Kimataifa ni lazima mkandarasi ahakikishe kuwa ubora wa viwango vinazingatiwa. Kwa vile mpango wa ukarabati huo ulitakiwa ukamilike mwishoni mwa mwezi huu, natoa wito kwa mkadarasi huyo kuhakikisha kwamba ukarabati huo unakamilika haraka iwezekanavyo ili uweze kutumika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa.
Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igoma – Kishiri – Kanindo ina urefu wa kilometa 15 ikiwa ni mzunguko kupitia Kata za Igoma, Lwanhima na Buhongwa katika Jiji la Mwanza. Ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali katika bajeti ijayo ya mwaka 2017/2018 ikiwa ni hatua muhimu katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha Serikali kujua gharama za mradi na kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa.
Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinatakiwa kutekeleza agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zilitengewa jumla ya shilingi bilioni 56.8 ambapo hadi Machi, 2017 kiasi kilichopelekwa kwenye mifuko kilikuwa ni shilingi bilioni 16.05. Halmashauri ya Jiji la Mwanza pekee imeshapeleka shilingi milioni 147.0.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuanza kutenga maeneo rafiki ya kufanyia biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo, kupeleka fedha kwenye mifuko na kusimamia marejesho ili ziweze kunufaisha makundi mengine. Utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ni kipimo cha utendaji kwa Wakurugenzi wote nchini na kushindwa kutekeleza, sio vyema kabisa. Aidha, hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mwaka 2014 aliahidi kupatia x-ray.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya Rais hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo kwa sasa haina kifaa hata kimoja katika kitengo cha mionzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2014 wakati wa ufunguzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi 133,136,000 kwa ajili ya kununua mashine ya x-ray mpya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi hiy iliyotolewa na Mheshimiwa Rais inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu linaendelea kuwa kubwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hii kubwa hasa katika Jiji la Mwanza?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukijengea uwezo Kitengo cha Ustawi wa Jamii kukabiliana na changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali hili la msingi kwanza nikushukuru sana na kukupongeza na wewe kwa kushirikiana pamoja na Serikali katika kuhakikisha kwamba tunarudisha ule uzuri wa asili, nakushukuru na kukupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, kifungu cha 16, msamiati unaotumika katika kubainisha watoto hao ni watoto walio katika mazingira hatarishi na si watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali inatekeleza Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2021/2022, ambapo umebainisha majukumu mbalimbali ya wadau katika kuondoa changamoto hiyo. Moja ya shabaha ya mpango huo ni kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/2022 ikiwemo katika Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Jiji la Mwanza limeunda kamati 11 za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto katika mitaa 11; makao ya watoto manne yamesajiliwa; jumla ya watoto walio katika mazingira magumu (hatarishi) 5,843 walibainishwa, wakike wakiwa 3,337 na wanaume, 2,506. Kati ya watoto hao, jumla ya watoto 2,381 walitengenezewa kadi za bima ya TIKA, watoto 27 walipelekwa katika Vyuo vya VETA na watoto 741 wanasomeshwa katika shule za sekondari. Aidha, zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika kata zote 18 umefanyika mwaka 2018. Jumla ya watoto 426 wanawake wakiwa ni 21 na wanaume 405 walitambuliwa. Kati yao watoto 135 walipelekwa kwenye makao ya watoto ya muda, watoto 120 waliunganishwa na familia zao, watoto 165 walirejeshwa kuendelea na masomo na watoto 323 walipata huduma za matibabu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuona umuhimu wa huduma za ustawi wa jamii, imeanzisha Kitengo cha Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lengo likiwa ni kuboresha huduma hizi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto, haki za mtoto na uendeshaji wa mashauri ya watoto. Serikali pia imeimarisha mipango ya bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuanzisha kifungu cha malipo (cost center) na kuingiza huduma za ustawi wa jamii katika mfumo ulioboreshwa wa mipango na bajeti katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Improved Plan Rep.). (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana linalojengwa katika Kata ya Mkolani limechukua zaidi ya
miaka minne sasa bila kukamilika:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa na miradi isiyokamilika kwa wakati kunarudisha nyuma maendeleo;
(b) Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha za kukamilsha jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, lenye vipengele (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ulioanza mwaka wa fedha 2008/2009 umechukua muda mrefu. Sababu kubwa ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzi huo ni changamoto ya upatikanaji wa fedha za ruzuku ya maendeleo. Hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 1.34 kati ya shilingi bilioni 1.84 zilizokuwa zinahitajika zimetolewa na kutumika katika kujenga boma lenye vyumba 23 vya ofisi, kumbi mbili, mgahawa, chumba cha kuhifadhia nyaraka, vyoo, kuezeka jengo lote, kupiga plasta, kuweka milango, vigae, kupaka rangi, kuweka dari, kufunga milango na madirisha na mfumo wa maji safi na maji taka.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kumaliza jengo hilo, jumla ya shilingi milioni 420 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kumalizia mfumo wa usalama wa jengo ikiwemo zimamoto, mfumo wa umeme, tanki la maji na uzio. Kwa maana hiyo, ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:-

Serikali kupitia Mamlaka ya TCRA wamefungia Local Channels kuonekana kwenye baadhi ya ving’amuzi hapa nchini, mfano Azam Tv, DSTV na vinginevyo.

(a) Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo imewanyima wananchi fursa ya kujua mambo yanayoendelea kwenye Taifa lao?

(b) Je, ni lini Serikali itatoa muafaka wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata fursa ya kujua mambo yanayoendelea kwenye Taifa. Kwa misingi hiyo, imetoa leseni zenye masharti tofauti ikiwemo leseni ya public, yaani utangazaji wa umma ambapo matangazo huruhusiwa kurushwa kwa watoa huduma wenye must carry. Hivi sasa matangazo ya umma ni TBC 1 na TBC 3 maarufu kama Safari Channel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha makampuni yanayomiliki visimbusi au ving’amuzi vya DSTV, Zuku na Azam hayakustahili kutoa huduma ya kubeba channel za ndani zisizolipiwa, yaani free to air local channels, kutokana na masharti ya leseni zao. Utoaji wa huduma za maudhui kupitia visimbusi vyao uko kwenye mfumo wa kukidhi soko la kimataifa na maudhui yake kuwa ya kulipia. Masharti ya leseni hizo na mfumo mzima wa miundombinu ya utangazaji husika yamelenga soko la kimataifa na hutofautiana na masharti ya leseni za watoa huduma za maudhui ya ndani ya nchi. Kuruhusu channels za ndani kuoneshwa kwa kutumia leseni za matangazo ya kimataifa kutazifanya free to air local channels kuwa za kulipia badala ya kuonekana bure.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TCRA imefanya jitihada ikiwa ni pamoja na kukaribisha maombi ya leseni ya kubeba maudhui ya channels za ndani, yaani multiplex operator, kutoka kwa wanaohitaji kutoa huduma yakiwemo makampuni ya Azam, DSTV na Zuku ili yaweze kupata leseni stahiki na kuweza kutoa huduma za kubeba au kuonesha maudhui ya ndani kupitia visimbusi vyao. Kwa sasa TCRA inashughulikia maombi yaliyopokelewa ili iweze kushauri kuhusu utoaji wa leseni stahiki.