Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Charles Muhangwa Kitwanga (4 total)

MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Loya katika Halmashauri ya Tabora (Uyui) wameitikia wito wa Serikali wa ulinzi kwa kujenga kituo kikubwa cha polisi katika kata yao:-
(a) Je, ni lini kituo hicho kitafunguliwa hasa ikizingatiwa kuwa Loya ni zaidi ya kilometa 120 kutoka Makao Mkuu ya Wilaya Isikizya ambako ndiko kwenye kituo cha polisi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea bajeti ya mafuta ili kuwarahisishia watendaji kazi maana maeneo ya Jimbo ni kubwa na yote yanahitaji huduma za kipolisi?
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kuwashukuru wananchi na wadau wote walihusika katika kuchangia ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Loya katika Halmashauri ya Tabora (Uyui). Pamoja na mwitikio huo bado kituo hiki hakijakamilika sehemu ya kuhifadhia silaha, huduma ya choo na makazi ya askari. Pindi vitu hivi vitakapokamilika kituo hiki kitafunguliwa na askari watapelekwa. Hivyo basi, namuomba Mheshimiwa Mbunge kuendelea na jitihada za kuwahamasisha wananchi wa Kata ya Loya ili kukamilisha ujenzi huo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuongeza bajeti ya mafuta katika maeneo mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha ili kukidhi mahitaji ya doria, misako na operesheni mbalimbali katika kutoa huduma ya ulinzi na usalama kwa wananchi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:-
Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ikilinganishwa na kazi zao wanazofanya kwa jamii:-
Je, Serikali ina mpango gani kuwaboreshea makazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu askari kuboreshewa makazi, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi. Namwona rafiki yangu hapa anashusha kichwa ananyanyua. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na mpango wake wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na kwenye baadhi ya magereza kujenga nyumba na vilevile kuendelea kuona mahitaji ya nyumba na hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 4,221 hivyo kuwepo upungufu wa nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya askari kuishi nje ya Kambi za Jeshi la Magereza. Hata hivyo, kasi ya utekelezaji wa mpango huu umekuwa ni mdogo kutokana na kuathiriwa na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar kama nilivyozungumza kwenye bajeti yetu. Aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbadala ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadiri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika. Mkakati huu utakwenda sambamba na mipango. Nirudie tena, mkakati huu utakwenda sambamba na mipango ya maendeleo ya Serikali ikilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaoajiriwa baadaye.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:-
Mafunzo na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Chuo cha Polisi (CCP) katika eneo la Kata ya Donyomorwa katika Wilaya ya Siha yamesababisha maafa makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wananchi kuuawa kwa risasi na mabomu yanayotumika katika mazoezi hayo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamisha mafunzo hayo kutoka kwenye maeneo ya makazi ili kuepusha maafa yanayowapata wananchi wa maeneo hayo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Siha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina mpango wa kuhamisha mafunzo ya kijeshi katika eneo la Donyomorwa. Awali mafunzo hayo yalikuwa yakifanyika katika eneo la Kilelepori ambalo lilivamiwa na wananchi kwa kujenga nyumba na kufanya shughuli za kilimo ambapo Serikali iliamua kuhamisha mafunzo ya kijeshi katika eneo hili nililolitaja sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuepusha madhara yanayoweza kuwapata wananchi, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa jamii ya Kimasai kuacha kuchunga mifugo katika eneo hilo, kukata kuni na kuokota kitu chochote wasichokijua katika eneo hilo. Aidha, kabla ya Polisi kuanza mazoezi ya kijeshi huchukua tahadhari kama kutoa taarifa kwa Vijiji, Wilaya na Mkoa ikiwa ni pamoja na kuweka alama za tahadhari kuzunguka eneo lote kwa kuweka bendera nyekundu na kuwaweka askari katika vipenyo vya kuingia katika eneo hilo.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-
Nchi inakuwa na amani pale ambapo kuna ulinzi imara.
Je, ni utaratibu upi mzuri wa kuimarisha ulinzi Bungeni?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina utaratibu za kulinda maeneo yote tete kwa ustawi wa jamiii husika ikiwa ni pamoja na Bunge letu Tukufu. Kuna ulinzi wa kutumia vifaa vya kisasa na vinginevyo ambavyo ni automated, ulinzi unaoonekana na ule usioonekana ambao hufanywa na askari na ule unaofanywa na wanyama kama mbwa. Yote haya hufanyika kwa pamoja na tunakuwa na ulinzi imara katika maeneo yetu kwani huwezi kutegemea aina moja tu ya ulinzi.