Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Lukago Midimu (9 total)

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimuulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, watumishi wetu hawa inawalazimu kuishi Wilaya nyingine ya Bariadi ambapo kuna umbali wa Kilometa 100 kwenda na kurudi kila siku.
Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuharakisha makazi haya ili watumishi hawa waishi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inaona hilo, ndiyo maana hata Halmashauri yenyewe ya Itilima katika mkataba wao waliosaini na National Housing, bahati mbaya mkataba ule ulikuwa haujahusisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI wala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pale katika Ofisi ya RAS na ndiyo maana Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliona kwamba licha ya mapungufu yaliyokuwepo lakini ofisi iweze kutoa kile kibali kwa mkataba ule. Hivi sasa Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeshatoa kibali, na kwa sababu fedha tayari ninazo na kibali kimeshapatikana, imani yangu ni kwamba ujenzi kupitia Shirika la Nyumba utakamilika haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero ya watumishi ambao wanapata taabu kutoka katika Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri sana. Kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya Taifa, je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuwawezesha vijana wa Mkoa wa Simiyu, wajasiriamali mitaji ya uhakika na kuwatafutia masoko nje ya nchi, ambapo itapunguza ukosefu wa ajira?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu swali la Mheshimiwa Mbunge limekuwa mahususi naomba nitoe maelekezo yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, awasiliane na Meneja wa SIDO wa Mkoa wa Simiyu, atambue kikundi cha Vijana ambao wanatabia ya ujasiriamali, wataelekezwa biashara ya kufanya na katika mkopo wa NDF unaokuja watatengewa fedha kusudi tuwalee na kusudi mje mnipime kwa mwaka mmoja ujao.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Simiyu ni wajasiriamali wazuri sana. Je, ni lini Serikali itaanzisha Benki ya Maendeleo ya Wanawake ili wanawake wa Mkoa wa Simiyu waweze kujikomboa na kujinufaisha na benki hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kupeleka kila kijiji na kila mtaa shilingi milioni 50 ili kuwawezesha wanawake na vijana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kusimamia pesa hizo na kuhakikisha kwamba zimewafikia walengwa, zisije zikaishia mikononi mwa watu wachache, wajanja kama mapesa ya JK? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumbukumbu ya Wabunge yote wakati Waziri wa Afya ambaye anahusika na mambo ya maendeleo ya jamii ambapo Benki hii ya Wanawake iko katika dhamana yake, nakumbuka katika bajeti ya mwaka huu alizungumza wazi kwamba suala la ufunguaji wa matawi ya benki hii utafanyika kwa kadri rasilimali fedha inavyopatikana. Imani yangu ni kwamba kauli ile ya Mheshimiwa Waziri itaendelea kusimamiwa na katika Ukanda ule wa Ziwa benki hii itafunguliwa lengo kubwa likiwa ni kufikisha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la shilingi milioni 50, ni kweli, sisi tunafahamu kwamba katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu zile fedha zilitengwa na naamini Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahusika na kusimamia jambo hili inapanga utaratibu mzuri na ndiyo maana wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anapita maeneo mbalimbali alikuwa akitoa maelekezo kwamba watu waache kuunda vikundi vya kitapeli ambapo mwisho wa siku fedha zile zitakuja kupotea. Imani yetu ni kwamba katika kipindi tutashirikiana vizuri wananchi wote na Serikali ili tusifanye makosa yale yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma katika fedha zile za mamilioni ya JK, sasa tunasema hatutarudia tena utaratibu ule wa mwanzo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kuridhisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Maswa ni cha muda, kiko kwenye hifadhi ya barabara ambapo kinaweza kikabomolewa wakati wowote ili kupisha ujenzi wa barabara; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile tatizo lililoko Wilaya ya Maswa liko sawa kabisa na tatizo lililoko Wilaya ya Itilima, hakuna kituo cha Polisi cha Wilaya; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi cha Wilaya ya Itilima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther alitaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi Itilima pamoja na Kituo cha Kudumu Maswa. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Esther kwamba kama nilivyojibu katika swali langu la msingi ni kwamba tunatambua upungufu wa vituo 65 nchi nzima katika Wilaya 65 ikiwemo Maswa na Itilima. Kwa hiyo, pale ambapo tutafanikiwa kupata fedha za ujenzi huu tutatoa kipaumbele katika maeneo hayo kama ilivyo maeneo mengine ya Wilaya zilizobakia 65 ambazo hazina vituo vya Polisi mpaka sasa hivi.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ziwa Victoria utachukua muda mrefu ili kuwezesha Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu kupata maji, je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwapatia maji ya uhakika wananchi wa Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Maswa sasa hivi una matatizo makubwa ya maji, wanakunywa maji machafu na kuna mradi wa chujio ambao ni wa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itakamilisha ili wananchi wa Maswa wapate maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amesema kwa sababu mradi huu utachukua muda mrefu, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa wananchi wanapata huduma ya maji? Kupitia mpango wa uendelezaji wa hii sekta ya maji, tayari tumeshatekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Simiyu na kuna maeneo ambayo kwa mfano, Nyangili, Mwamanyili, Bukapile, Bulima, Lamadi, Lukugu, Manara, kuna ambayo imekamilika na mingine inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia juzi tumepitisha bajeti na katika Mkoa wa Simiyu tumeweka shilingi bilioni tisa ili Halmashauri ziendelee kutekeleza miradi ya maji kuhakikisha kwamba wakati tunasubiri ule mradi mkubwa, lakini wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji. Vilevile Bariadi kuna huu mradi wa visima vya Misri tumechimba visima pale na nimeenda mwenyewe Simiyu maji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Maswa, ni kweli ukiangalia ule mradi hata utakapoanza eneo la mwisho utakwenda Maswa. Kutokana na hilo, hata jana tulikuwa na kikao, tayari tumeagiza KASHWASA washirikiane na Halmashauri ya Maswa ili tuweze kuona uwezekano wa kutoa maji kutoka bomba lile pale Shinyanga kupeleka maji kwa muda pale Maswa wakati tunasubiri mradi mkubwa. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Serikali kwa mpango wake wa kujenga chuo kila Mkoa. Kwa kuwa vijana wengi Mkoa wa Simiyu hawana kazi na ukosefu wa ajira unasababisha vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu. Namwomba Naibu Waziri anihakikishie, ni lini sasa huo ujenzi utaanza Mkoani Simiyu ili vijana wajifunze ujuzi waweze kujiajiri wenyewe waondokane na umaskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba kwa namna tulivyopangilia tutajitahidi tusitoke nje ya mipango yetu, ujenzi unatakiwa uanze Februari mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho wakati tunasubiri chuo kikamilike, tunaendelea kuwasihi vijana wa Simiyu na wengine wa Tanzania waendelee kuachana na uhalifu kwa sababu inawezekana isiwe tiba ya changamoto iliyopo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyojitosheleza. Pia naishukuru Serikali yangu kwa kutenga hizo shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Itilima na Busega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu jengo la OPD lipo tayari na maelezo ya mkandarasi ambaye ni TBA amesema jengo hilo litakabidhiwa tarehe 28 Mei, 2018 kwa Katibu Tawala wa Mkoa. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuweza kutujengea wodi ya wazazi, watoto, wanawake na wanaume ili hospitali hiyo ianze kazi haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Hospitali Teule ya Mkoa haina kabisa gari la kubebea wagonjwa kupeleka Hospitali ya Rufaa Bugando, gari lililopo wanatumia hardtop almaarufu chai maharage; je, ni lini Serikali itatuletea gari la kubebea wagonjwa kupeleka katika Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya Wizara ya Afya ambayo tumeipitisha hivi karibuni, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikao ya Katavi, Njombe, Simiyu, Songwe na Mara. Kwa hiyo, Hospitali ya Simiyu ni sehemu ya hospitali ambazo zitaendelezwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba ya hilo, Serikali imeagiza ambulances na zitakapofika Mkoa wa Simiyu utakuwa ni mmoja ya mkoa ambao tutaufikiria kupata ambulance. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza kabisa nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya kujitosheleza. Naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa mradi wa maji wa Wilaya ya Busega, je, mradi huo utaanza lini ili kukidhi mahitaji ya wana Busega?

Swali la pili kwa vile Mkoa wa Simiyu una changamoto kubwa sana ya maji. Je, Naibu Waziri uko tayari kuongozana na mimi baada ya Bunge ukajionee mwenyewe changamoto ya maji ilivyo Mkoa wa Simiyu ili uweze kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza awali ya yote nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Esther Midimu ni miongoni mwa wa mama majasiri na shupavu katika kuhakikisha wanapigania haki za akinamama wakiwemo wamama wa Simiyu.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge langu halina wamama hili Bunge lina Waheshimiwa tu.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge, jasiri na mpambanaji katika kuhakikisha anapigania haki za akinamama wakiwemo akinamama wa Simiyu. Nataka nimuhakikishie sisi kama Wizara ya Maji tunatambua kabisa maji ni uhai hatupo tayari kupoteza uhai wana Simiyu tunatarajia mnamo mwezi wa nane mradi huo utaanza na mkandarasi atakuwa site. Lakini suala la kuongozana na mimi kwa kuwa anafanya kazi nzuri nipo tayari kuongozana naye Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupatia pesa shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ya Bariadi, Bariadi DC, Itilima na Busega. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika hospitali zetu hizo za Wilaya nilizozitaja, je, ni lini Serikali itatuletea watumishi wa kutosha hasa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali, vituo vya afya na zahanati, Serikali imeweka mkakati ambao tayari umeanza kutekelezwa wa kuajiri watumishi wa kada za afya kuanzia madaktari na wauguzi na ajira hizi zinatolewa kwa awamu. Lengo la ajira hizi ni kwenda kuhakikisha majengo yote yaliyojengwa yanatoa huduma bora za afya kama ilivyotarajiwa.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo ni kipaumbele cha Serikali na itaendelea kuajiri wataalam wa afya kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika Halmashauri za Mkoa wa Simiyu na nchini kote.