Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ester Michael Mmasi (12 total)

MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mipango ya Serikali ni pamoja na kuinua ujuzi wa vijana wahitimu kutoka vyuo vikuu kutoka asilimia 2 mpaka 12. Je, nini mpango wa Serikali katika kutekeleza mikakati hii hadi kufika mwaka 2019/2020?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, moja ya mikakati ya Serikali katika kuinua sekta ya ujasiriamali kwa vijana wa Kitanzania ni pamoja na kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kupitia Mfuko wa Vijana, Baraza la Uwekezaji la Taifa.
Je, Serikali ina mkakati gani katika kuanzisha Baraza la Taifa la Vijana ili kuongeza ufanisi lakini pia kuongeza fursa nyingi na wanufaikaji wengi kupitia Mfuko huu wa Vijana?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la tatu, kupitia …
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther, maswali ni miwili tu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza aliulizia kuhusu mpango wa ukuzaji ujuzi, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumekwishaanza mpango mkakati wa kukuza ujuzi ambao utahusisha wahitimu mbalimbali wa vyuo vikuu, lakini na wanafunzi ambao bado katika vyuo vikuu. Katika mpango wetu huu utahusisha pia mafunzo ya uanagenzi pamoja na internship na lengo lake ni kukuza ujuzi kwa wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali lake la pili ameulizia kuhusu Baraza la Vijana la Taifa na nataka nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali na Bunge hili lilipitisha Sheria Na.12 ya Uundwaji wa Baraza la Vijana la Taifa na tayari Kanuni zimekwishakamilika kwa ajili ya kuanza rasmi uundwaji wa Baraza hili ambalo litakuwa likiwakilisha matatizo mbalimbali ya vijana lakini pia litakuwa sehemu ya kisemeo cha vijana katika kuwasilisha matatizo mbalimbali ambayo yanawakabili.
Kwa hiyo, tunaamini kupitia Baraza hili, vijana watakuwa wamepata sauti na sisi kama Serikali tutakuwa sehemu ya kushirikiana nao katika kutatua kero na changamoto ambazo zinawakabili vijana.
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Waziri, kupitia mpango wa AGOA ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama sehemu ya ushiriki Nchi za SADC, tumepewa ridhaa ya kutumia soko la Marekani bila kuwepo na vikwazo vya kodi.
Je, Serikali inatupa commitment gani kuona vijana wahitimu wa Vyuo Vikuu wanaweza kutumia fursa hii ya mpango wa AGOA kuondokana na suala zima la tatizo la ajira? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa naibu Spika, ni kweli kwamba mpango wa AGOA unatoa fursa ya kuweza kuuza mazao yetu nje, na ni kweli vilevile kwamba ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri inaweza ikawasaidia vijana wetu kujiajiri na kuondokana na adha iliyopo sasa ya ukosefu wa ajira. Kwa hiyo Wizara iko tayari kushirikiana na vijana wowote ambao wako tayari kujiingiza katika uuzaji wa kahawa ili kuitumia fursa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti yetu ya mwaka huu tumetenga baadhi ya fedha ili kuweza kuona namna ya kuwasaidia vijana waweze kuingia kwenye kilimo na tutaanza eneo la Rufiji, lakini tuko tayari kufikiria namna nyingine ya kuweza kuwasaidia vijana wengi waweze kuingia katika uzalishaji huo hasa katika eneo alilosema la kahawa.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa upande wa Dar es Salaam na hususani kwa Jimbo la Kawe, ni dhahiri kwamba tumekuwa na changamoto za maji. Changamoto hizi zinatokana na kodi kubwa inayowekwa kwenye madawa ya kutibu maji, pamoja na kuhifadhi maji.
Pia tumekuwa na tatizo la miundombinu chakavu kwa upande wa DAWASA na vile vile tumekuwa na bajeti isiyokidhi mahitaji ya suala zima la upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam. Je, Serikali imejipangaje katika kutatua changamoto za maji, kwa Jimbo la Kawe zaidi sana pale Boko, Tegeta na Bunju. Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mradi wa mkubwa wa maji kutoka Ruvu Chini umekamilika na sasa hivi maji yameongezeka sana katikaJiji la Dar es Salaam. Tatizo tulilokuwa nalo ni ule mtandao. Tunao ule mtandao wa zamani ambao ni chakavu, kazi ya ukarabati inaendelea. Pia tayari tuna mkandarasi ambaye anafanya mtandao mpya maeneo hayo ya Kawe kwenda Bunju mpaka Bagamoyo, baada ya muda siyo mrefu maeneo yale upatikanaji wa maji utaongezeka sana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge na suala la kodi ya VAT kwenye madawa ya maji, Serikali imeshakubali kuondoa kodi ya VAT kwa hiyo, tunatarajia bei ya maji itapunguzwa kwa sababu itakuwa ni kigezo cha kupunguza bei maji wakati gharama za kununua madawa yale zimepunguzwa.
Mheshimiwa Mbunge uwe na imani kwamba baada ya muda siyo mrefu bei ya maji itapungua, lakini pia upatikanaji wa maji utaongezeka katika Jiji la Dar es Salaam.
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa suala zima la mazingira na changamoto zake lililoukumba Mkoa wa Mara linafanana kabisa na tatizo lililotokea hivi majuzi la mafuriko, kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kuathiri sana maeneo ya ukanda wa chini, yaani Vijiji vya Vunjo, Kahe, pamoja na Chemchem: Je, Serikali ina mpango gani, katika suala zima la uhifadhi wa mazingira kwa Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali lililoulizwa kuhusu suala zima hili la mafuriko ambalo linalikumba Taifa letu. Tukubaliane katika principle za kimazingira, ambapo sisi wote humu ndani ni wadau, kwamba kila mtu anatakiwa achukue jukumu hili la tunapambana katika zoezi zima la kuhakikisha kwamba mazingira yetu yako salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua uharibifu wa mazingira uliofanyika Mkoa wa Kilimanjaro. Tunajua hali ya mazingira nchini sasa hivi ilivyo, kwa hiyo, zoezi hili na mafuriko haya na maeneo yote aliyoyataja na tumekuwa tukitolea taarifa kwamba mafuriko haya hayawezi kuwa ya mara moja. Tatizo hili litakuwa ni permanent sasa, kutokana na uharibifu wa mazingira tulionao hapa nchini. Tuchukue jukumu wote kwa pamoja, tumeagiza, sasa hivi tumekuja na mpango mkakati wa upandaji miti. Tunajua kabisa tukipanda miti, tutazuia kwa kiwango kikubwa mafuriko ya maji ambayo yanatokea, kwa maana kwamba ni kinga, lakini vile vile katika kurekebisha hali ya hewa kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mliunge mkono zoezi ambalo linasimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais la upandaji miti, la kuhakikisha kwamba kila Wilaya inapanda miti isiyopungua 1,500,000 kwa mwaka. Nilivyotembelea Mkoa wa Kilimanjaro, nilikuta wana mkakati wa kupanda miti milioni tano kwa mwaka. Tufanyeni hili zoezi, lakini tushirikiane sana, wale watu wanaoharibu mazingira, miti inakatwa mno, hatuwezi kupona katika ukataji miti wa namna ile. Kila mwaka inafyekwa hekta laki nne, kila mwaka zinakatwa. Kwa hiyo, watu wote walioiandama misitu yetu na kuikata kiasi hicho tushirikiane kuhakikisha kwamba uharibifu huu unakomeshwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Vilevile jitihada nyingine za Serikali za kuleta nishati mbadala mnazisikia.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na uwepo wa Tume ya Vyuo Vikuu yaani TCU (Tanzania Commission for Universities), lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya kuzalisha wahitimu wasiokuwa na uwezo wa kutosha katika mustakabali wa ujenzi wa uchumi wa nchi ya Tanzania. Swali, je, Serikali imejipangaje katika suala zima la kuzalisha wahitimu wenye uwezo, weledi wenye tija na maarifa kazini? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imejipanga vizuri kabisa kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa na uwezo wanachukuliwa hatua stahiki na katika hili niseme tu wazi kwamba, Serikali itafanya uhakiki wa wanafunzi au tunaangalia upya vigezo vya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu ili tuweze kuchukua hatua mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kesho nitakuwa nawasilisha hotuba yangu, haya yote nitayaeleza kwa kina, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Ester upokee hili jibu lakini tumejipanga vizuri na mikakati yote nitakuja kuieleza hapa kesho.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo kimsingi yamejikita kwenye suala la msingi.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni dhahiri kwamba kupitia miongozo ya Serikali juu ya mishahara na posho za waendeshaji na hata walimu wa vyuo vikuu Tanzania, ni kwamba iko mikondo mathalani PGSS 13, PGSS 14, PGSS 15, hizi ni kada ambazo zinapaswa kuongozwa na waendeshaji kwa maana ya kwamba siyo academicians. Practice iliyopo sasa hivi ni kwamba viwango hivi vya mishahara havitumiki kwenye kada husika kwa kuwa nafasi hizi za uongozi wa juu ni kwamba unaongozwa na academicians.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafsiri kiwango cha mshahara PGSS 13 ambayo inashikiliwa na Wakurugenzi ambao ni wanataaluma PGSS 14 na PGSS 15 ili viwango hivi viweze kutumika kwa waendeshaji wa vyuo vikuu au taasisi za elimu ya juu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi niende tu katika ufafanuzi wa ziada kwamba baada kuona kwamba kuna malalamiko aina hiyo na mengine kwa kweli katika vyuo vyetu mbalimbali hasa vyuo vikuu, Wizara kwa kuzingatia hilo, mwezi huu wa kumi ulioisha tumeunda vikundi kazi (team) kwa ajili ya kufuatilia hayo mambo yote katika vyuo vyetu vyote vikuu vikiwemo vyuo binafsi ili kuona kwamba kwanza vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, lakini pili uongozi unapangwa kutokana na taratibu na sifa zinazostahili, vilevile kuangalia miundombinu na maslahi kwa ujumla yanayohusu viongozi wa ngazi hizo kama yapo sahihi au hayapo sahihi. Bila kusahau hata watumishi wengine ambao hawaonekani kama ni watumishi muhimu (supporting staffs), kama wapishi, kuona kwamba je, chuo kinaweza kujiendesha kiuhalali au laa!
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nizidi tu kusema haya mapendekezo yako, unayozungumza nayo yatazingatiwa katika kutafakari masuala hayo.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naitwa Mmasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu nimkumbushe Kaka yangu Jafo. Kaka yangu Mheshimiwa Naibu Waziri tulipokuja hapa Bungeni mimi na wewe tulikula kiapo kimoja, tofauti yetu ilikuwa kwenye majina. Mimi nilitamka Ester Michael Mmasi na wewe ukatamka jina lako kadri ilivyo kwenye kumbukumbu za Bunge hili. Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye maslahi ya Kibunge hususani katika payroll ya Bunge sote tuna maslahi sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu hapa yametoka kwamba hawa wenzetu kupitia Mfuko wa Jimbo wanafanya kazi za wananchi, sisi ni akina nani na tunafanya kazi za nani?Hatufanyi kazi za familia zetu, tunafanya kazi za wananchi hawa hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi ya Kenya, mathalani Wabunge...
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wabunge wa Kenya hili linafanyika. Nenda tukaangalie Wabunge wa Kenya (Woman MP’s) kwenye county level wana-Capital Development Funds for women MP’s, kwa nini Tanzania ishindikane?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba kujibu swali ambalo nadhani litakuwa swali maarufu la mwaka na limeulizwa kwa staili ambayo haijawahi kufanyika, ninakupongeza Mwenyekiti kwa utaalamu wa kujua Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili linahusu Mfuko wa Jimbo na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Ester Mmasi, Mheshimiwa Munde Abdallah na wengine wengi Wabunge wa Viti Maalum wanataka na wao wapate mgao wa fedha za Mfuko wa Jimbo. Swali hili siyo kwamba linaulizwa kwa mara ya mwanzo leo, limekuwa likiulizwa na mara nyingi tumekuwa tukitoa majawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu maarufu ambayo tumeyatoa kwamba tutakwenda kushughulikia tuone utaratibu wake, lakini kila tunaposhughulikia tunapata ugumu kwa sababu mfuko huu umezaliwa kwa mujibu wa sheria, sheria yenyewe inaitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko wenyewe unaitwa Mfuko wa Jimbo na kwa hiyo, kuupa jina linguine lolote lile ni kazi ngumu kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani kuna Wabunge
wa Majimbo, kuna Wabunge wa Viti Maalum, kuna Wabunge wa Mikoa, kuna Wabunge wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais. Bunge hili likitambua kwamba Wabunge wa aina hizi zote wapo, lilitunga Sheria ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye instrument yangu kwa mujibu wa sheria nilizopewa kuzisimamia nina sheria inayosema nitasimamia Mfuko wa Jimbo, haisemi vinginevyo. Ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi nimesema kama Bunge litaona vinginevyo suala hilo linakuja kwa utaratibu mwingine, lakini kwa sasa mimi ninasimamia Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale Wabunge waliokuwa wanadai sana mfuko huu, waliokuwa wa Viti Maalum, walipopata majimbo na wenyewe msimamo wao umebadilika, ni kwa sababu ya majukumu anayoyapata Mbunge wa Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mengine yameulizwa na Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim ambaye ameuliza suala la fedha kuchelewa Zanzibar, hili tumelichukua, tunawasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais tuone utaratibu bora zaidi wa kuweza kufanya fedha hizo ziwafikie Wabunge wa Zanzibar, hasa tunatambua yapo mapendekezo ya kwamba bora zikapita katika Ofisi ya Bunge Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine dogo limeulizwa na Mheshimiwa Paresso kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati za Fedha. Kamati za Fedha zinatambua uwepo wa Madiwani na Mbunge unapoingia kwenye Halmashauri huwi Mbunge unakuwa Diwani, kule kwenye Kamati ya Fedha wanaoteuliwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha huwa ni Madiwani. Sasa nadhani ni utaratibu wa Halmashauri zenu, kama wewe Mbunge kuteuliwa kuna baadhi ya Wabunge ambao wanaingia kwenye Kamati ya Fedha, lakini kule wameingia kwa tiketi ya Udiwani wao kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napata shida hapa
kwa sababu la kwanza, kwamba kwa Majimbo ambayo yana Wabunge wengi wa Viti Maalum, na mfahamu kikao kile kina utaratibu wa gharama zake na mambo mengine. Ingawa gharama siyo hoja kubwa, lakini kwa Jimbo ambalo lina Wabunge wa Viti Maalum nane, 10, sijui hali itakuwaje kwa sababu gharama za uendeshaji wa Halmashauri zitakuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ingelikuwa Wabunge labda ni mmoja au wawili pengine unaweza kuichukulia hili jambo likawezekana, lakini kwa hali ilivyo kuna tatizo kubwa sana na ninadhani ni vema hili jambo likabaki kama ilivyo na ndio utaratibu ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tiketi ya Udiwani, Mbunge anaweza akateuliwa na Mwenyekiti kwa utaratibu ule akawa Mjumbe wa Kamati ya Fedha.(Makofi)
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) kuja Bandari ya Tanga nchini Tanzania ulitarajiwa kuanza mwezi Juni, 2017. Kwa kuwa pia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba Serikali itakuwa tayari kuwaandaa vijana wetu kupitia mitaala ya oil and gas kwenye Vyuo vya VETA mnamo mwaka 2018. Je, Serikali kwa kufanya hivi haioni ni sawa kabisa na kuweka rehani ajira ya kijana wa Kitanzania hususan vijana wanaotoka katika Mkoa wa Tanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mchakato wa uchimbaji, uchanjuaji na uchakataji wa zao la oil and gas Mikoani Lindi na Mtwara ulitarajia kuanza mwaka 2013, lakini hakuanza kutokana na sababu za ndani ya Serikali na kubwa ikiwa ni ukamilishwaji wa local content policy pamoja na msamaha wa kodi. Nini kauli ya Serikali kwa vijana wahitimu kwa nchi ya Tanzania hasa ukiangalia kwamba vijana wengi wanahangaika kutafuta kazi pasipokuwa na imani yoyote? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mmasi, tumekuwa na yeye tangu mwaka 2013 katika jitihada za kufungua mafunzo kwa VETA kwa wanafunzi wa oil and gas. Kwa hiyo hongera sana Mheshimiwa Mmasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali yake haya mawili, la kwanza, Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa kuwapatia mafunzo hasa wanafunzi wa VETA kwa oil and gas. Ni kweli kabisa upo umuhimu na mwaka 2012/2013 kama nilivyosema, tulianza kutoa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwafundisha vijana wetu wa VETA Lindi na Mtwara kwa ajili ya uchomeleaji, ufundi sanifu pamoja na theories za kawaida za utafiti wa kuchimba na kutafiti mafuta na gesi hapa nchini. Kwa hiyo, tunaona umuhimu Mheshimiwa Mmasi na tumeshafika hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, matarajio ya mpango wa Serikali, kweli kabisa mwaka 2018 tunatarajia taratibu zote za taaluma ili kuingiza sasa mtaala katika Vyuo vya VETA kwa upande wa mafuta na gesi itafika sasa muda muafaka hasa kwa VETA ambavyo ni vyuo vipya ukiondoa vile vyuo ambavyo vimeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyowasiliana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tumefika hatua nzuri, Serikali ya Norway pamoja na Serikali yetu itatenga shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha hatua hii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mmasi, tutakapofika katika hatua hiyo tutashirikiana pamoja tuone namna ya kuwapatia vijana wetu mafunzo haya ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Kishimba linafanana kabisa na changamoto ya udanganyifu wa mitihani yaani thesis and dissertation kwa wanafunzi wa shule ya Uzamili na Uzamivu elimu ya juu.
Je, Serikali imejipangaje kuwa na mfumo mahsusi katika kudhibiti ubadhilifu wa mitihani kwa maana ya kuwa na mfumo mathalani central system plagiarism test? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika masuala haya ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafanya mtihani na wanapimwa kwa kiwango wanachostahili kwa kadri ya kuwapima uelewa wao, Serikali tumeendelea kufanya hivyo. Kwa upande wa vyuo vikuu hasa kwa upande wa wanapofanya maandishi yao, niseme thesis kwa mfano, kweli kumekuwa kunajitokeza udanganyifu wa watu kuomba ama kufanyiwa na watu, wakati mwingine kunakili maandiko ya watu wengine waliopita kiasi kwamba mtu anakuwa hajafanya kazi yake na kupimwa kwa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaliona hilo na tumeshaandaa mfumo kiasi kwamba kila mtu akishamaliza andiko lake litakuwa linapitishwa humo kiasi kwamba likioanishwa litajulikana kwamba huyu ameiba kutoka kwa andiko la mtu mwingine. Ikizingatiwa katika mfumo huu wa digital watu ni rahisi kuiba. Kwa hiyo tumeshaona namna ya kudhibiti eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya sekondari ngazi mbalimbali tunafanya uhakiki. Kwa mfano, mara hii ya mwisho hata sisi wenyewe Mawaziri tumekuwa tukitembelea baadhi ya shule za kidato cha sita kuona kwamba taratibu na sheria zinazingatiwa katika sehemu za mitihani. Mfano, safari hii nimeenda shule ya Ifunda na shule ya Iringa Girls. Hivyo tunasimamia kikamilifu.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu kwenda Wilaya ya Same na Mwanga ni mradi ambao ulipaswa uwe katika hatua za mwisho za utekelezaji, lakini mpaka ninapoongea leo mradi huu umeonekana kutokufikia hata asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Je, Serikali imejipangaje katika kuwakwamua wakazi wa Wilaya ya Same na Mwanga na especially wanawake wote na wapiga kura wangu wa Wilaya ya Same na Mwanga? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Same/Mwanga kutokutoa maji kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu, mkandarasi wa kwanza yuko asilimia 75, mkandarasi wa pili tayari anafika asilimia 30 na kazi inaendelea. Sasa hivi tank kubwa la Mlima wa Kiverenge linajengwa ambapo tank hilo likishakamilika, sasa maji yatakwenda Mji wa Mwanga na Same; na kazi inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya miezi sita wananchi wa Same na Mwanga wataanza kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa background information nzuri sana. Kimsingi nioneshe tu masikitiko yangu kwamba ukiangalia muktadha wa swali hili, itoshe tu kusema kwamba bado Mheshimiwa Waziri hakuweza kulitendea haki swali hili.
Mheshimiwa Spika, swali liliuliza; je, ni lini Serikali itafanya marekesho ya bei hizi katika kuimarisha uchumi wa Taifa hili na hususan wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro? Ingekuwa swali linauliza je, Serikali ina mkakati gani? Ndipo jibu lilipaswa kuwa hili. Kwa sababu jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri linasema Serikali imejinga kukutana na wadau. Ni kweli, lakini swali lililenga kujua ni lini hasa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni kweli kwamba moja ya kuinua mapato ya Serikali kupitia kivutio hiki cha Mlima wa Kilimanjaro ni pamoja na kuboresha mpango mkakati wa soko la utalii duniani. Nilipenda Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie, je, kupitia uwekezaji wa Shirika la Ndege la Tanzania ni kwa nini Serikali haikuona umuhimu wa kurudisha nembo ya Mlima wa Kilimanjaro katika ndege hizi za Shirika la Ndege ili basi kwa muktadha huo tuweze kuinua soko la utalii kwa nchi ya Tanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza. Najua yeye ni mdau mkubwa sana katika huu mlima na amekuwa akitushauri sana katika masuala mengi. Kuhusu maswali yake yote mawili ambayo ameuliza, suala la kuuliza ni lini? Labda nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge tumeshakutana na wadau mbalimbali katika kuzungumza masuala mbalimbali zikiwemo changamoto pamoja na gharama kubwa ambazo wanatozwa watu mbalimbali wanaopanda Mlima Kilimanjaro. Tumeshakaa tumezungumza, lakini kama Serikali tunataka kujiridhisha. Tunataka tukutane na wadau wengi zaidi kuliko wale wa vyama vyao ili tuone kama kuna haja ya kupunguza au hakuna haja ya kupunguza.
Mheshimiwa Spika, suala la kwamba ni lini? Basi niseme tu kwamba kati ya kipindi cha sasa mpaka mwezi Desemba, hili suala tutakuwa tumeshafikia muafaka kama tupunguze au tuongeze. Kwa hiyo, siyo suala la kupunguza tu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba kulikuwa na nembo kwenye Shirika la Ndege zetu la Kilimanjaro, nadhani tulikuwa na alama kwa ajili kutangaza Mlima wetu Kilimanjaro. Ilikuwemo kwenye nembo hiyo na bado itaendelea kuwemo. Mpaka sasa hivi tumeweka zaidi, lakini siyo tu kutangaza Mlima Kilimanjaro, bali tunaangalia na vivutio vingine vingi ambavo vipo, ndiyo maana ndege zetu sasa hivi tunaweka vitu vingi na alama nyingi zaidi ambazo zinaendelea kulitambulisha Taifa letu. Bado tutakaa na wadau mbalimbali kuona kama kuna haja ya kurudisha ile alama iwepo pale kama alama ya utambulisho. (Makofi)
MHE. ESTHER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali langu kwa Serikali; Vijana wanaohitimu nchini Tanzania ni takribani laki sita mpaka laki nane kwa mwaka lakini vijana wanaoingia kwenye ajira rasmi na zisizo rasmi ni takribani ni asilimia kumi mpaka 25.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali kutokana na masuala mazima ya retrenchment yanayoendelea nchini Tanzania. Kwa sasa tunayo taarifa ya kwamba kampuni ya TTCL ina mpango wa down size wafanyakazi zaidi ya 500; lakini pia ukienda kwa taasisi zisizo za Kiserikali mfano TBL tumeshuhudia hapa miezi michache iliyopita kwamba wali- retrench zaidi asilimia 80 na wakati huo huo wakihamishia sehemu kubwa ya operations mfano payroll function, lakini pia siyo hivyo tu finance Department ilipelekwa Mauritius; swali langu la kwanza; nini kauli ya Serikali haswa ukiangalia hali halisi ya ombwe kubwa la vijana wanaohitimu pasipo kuwa na ajira?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kumekuwa na utamaduni mbaya sana unaoendelea kwenye taasisi za kifedha ambapo taasisi hizi zinakuwa zinajisajili Tanzania lakini sehemu kubwa sana ya majukumu ya IT yanakuwa yanafanyika nje ya nchi. Mathalani benki ya Stanchart (Standard Chartered), Baclays, lakini Citi Bank pamoja na Stanbic bank, wamekuwa na utamaduni wa sehemu kubwa ya IT zinakuwa zinafanyika nje ya nchi. Ukiangalia NBC, supply of payment inafanyika South Afrika; ukiangalia Stanchart account opening na pia transaction process zote zinafanyika nchini Kenya. Ukiangalia Baclays function management zinafanyika nchini India, swali langu kwa Serikali. Nini kauli ya Serikali hasa ukiangalia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi hawa wanaohitimu shule ya TEHAMA? Naomba kupatiwa majibu stahiki na Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza la kuhusiana na retrenchment. Ni dhahiri kwamba sisi kama nchi katika Sera ya Ajira tunaendelea kulinda ajira za vijana katika nchi yetu kwa kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanapata fursa ya kuweza kuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, alichokisema Mheshimiwa Mbunge, kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2004 imeweka vigezo ni katika hatua gani mwajiri anaweza akafanya retrenchment. Sheria ile pia imetoa nafasi kwa vyama vya wafanyakazi kushiriki moja kwa moja katika majadiliano kabla jambo hili halijafanyika.
Mheshimiwa Spika, rai yangu kwa waajiri wote ni kwamba waendelee kufuata sheria inavyozungumza ya namna ya kuweza kuwaondoa wafanyakaza kazini kwa kuwa jambo hili lipo kisheria.Kazi yetu kama Wizara ni kuhakikisha kwamba taratibu za kisheria zimefuatwa ili Watanzania wengi haki zao za kimsingi zisiondolewe katika utaratibu huu wa uachishwaji wa kazi ambao wa sheria imeuzungumza vizuri.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kuhusu kazi nyingi kufanyika nje ya nchi. Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu anachokisema Mheshimiwa Mbunge na sisi tulikiona tumefanya ziara ya ukaguzi tumekwenda makampuni mbalimbali; na hivi sasa tumeshatoa maelekezo ya kazi hizi namna gani zifanywe.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa kwenye eneo la TEHAMA pia ni kwamba ukiruhusu mambo hayo yote yafanyike nje ya nchi ni hatari pia kwa usalama wa nchi. Kama Serikali tumechukua hatua na tumetoa maelekezo kuwataka waajiri wote kurekebisha eneo hili. Sasa hivi tunafanya follow up na vile vile tunafanya kaguzi ili kukagua waajiri wote ambao wamekiuka agizo letu tuweze kuwachukulia hatua.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa niongeze kipengele kidogo kuhusu masuala ya TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Serikali imeanzisha Tume ya TEHAMA ambayo pamoja na majukumu mengi kabisa iliyonayo inakwenda kuanzisha Bodi ya kutambua wana TEHAMA wote ili wana TEHAMA hao watambulike kutokana na elimu yao na ujuzi wao wanalionao kama wanavyotambulika Mainjinia, Madaktari na Wahasibu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba tutapata taaluma stahiki za kufanya kazi kwenye maeneo ya TEHAMA. Ahsante.