Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ajali Rashid Akibar (9 total)

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Wizara ya Fedha kwa kufanya mipango mizuri na niishukuru sana kutangaza Kariakoo kuwa Mkoa wa TRA.
Mheshimiwa Waziri, leo tumesoma kwenye magazeti yanasema kwamba, kuna mdororo wa uchumi, mpaka kufikia mahali ambapo mabenki hayakopeshi tena wananchi na wameanza kuuza bond zao. Ni nini Wizara ya Fedha inazungumza kuhusu haya mabenki kutokuwakopesha wawekezaji au waanzishaji biashara mpya ili waendelee kuuimarisha huu uchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Fedha itoe msimamo wake. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ajali, swali la msingi linahusu VICOBA, sasa maelezo ya jumla kuhusu uchumi, hayo yatamtaka Waziri alete hoja hapa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tutaendelea.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala iliamua kupambana na tatizo hili la maji wakaamua kuchimba bwawa katika Kijiji cha Chilangala, Wilaya ya Newala, lakini kutokana na ufinyu wa fedha lile bwawa hawakulimaliza. Je, Serikali iko tayari kwenda kumalizia lile bwawa ili tuweze kutatua tatizo hili la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ndiyo kwa mara ya kwanza ananipa taarifa kwamba, kumekuwa na mradi wa bwawa ambao unafanywa na Halmashauri katika maeneo ya Jimbo lake kule Newala. Niseme kwamba, niko tayari tufanye mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo tayari kupitia mkopo wa India ambao tunasubiri Financial Agreement isainiwe, hela nyingi imepelekwa kwenye maeneo hayo ili kwenda kuhakikisha kwamba sasa tunachukua maji kutoka Mkunya kule Ruvuma, tunachukua Mitema na kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya Newala yanapata maji safi na salama na hasa kwa kuzingatia kwamba, Newala iko juu sana, huwezi ukachimba kisima ukapata maji. Kwa hiyo, mradi mkubwa unakwenda kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini pamoja na hilo bwawa naomba tuwasiliane ili tuweze kuona cha kufanya.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo kuhusu barabara hii kupitia kwenye milima, tatizo langu ni uwepo wa sheria kwamba kama nilivyozungumza kwenye swali langu la msingi, mji huu wa Newala upo tangu mwaka 1800; kama wakati ule ilikuwa inaitwa Dutch East Africa. Hii sheria ya mwaka 2007 imekuta wananchi wale wakiwa na taasisi zile katika uwepo halali. Kuna polisi, mabenki na wananchi, maana yake walikuwepo kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake wanachopinga wao ni kwamba hii sheria imewakuta wao wakiwepo kisheria. Kwa hiyo, swali langu la msingi, je, ni lini TANROADS watafanya mazungumzo na wananchi hawa wa Newala ili tukaondoe kesi ile Mahakamani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kutokana na ufinyu wa Mji wa Newala, je, sasa TANROADS wako tayari badala ya kupitisha ile barabara Newala Mjini, wapitishe Kiduni hadi Nambunga kwa Mheshimiwa Mkuchika ili kuepuka mrundikano wa barabara katika ya mji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, anafuatilia sana maendeleo ya Newala na anajua eneo hili ambalo analizungumza pia ni maarufu sana kwa uzalishaji wa korosho.
Kwa hiyo, namuahidi kwamba sisi Serikali tuko tayari kwenda kufanya mazungumzo na ninampongeza sana kwa nia yake thabiti ya kuhakikisha kwamba kama shauri hii tunalimaliza, itaharakisha pia ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, tuko tayari kuzungumza ili tulimalize ili wananchi hawa waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa ule utaratibu ambao wanafikiria, na mimi eneo lile nilitembelea, ni kwamba tukiweza kupitisha bypass kwenye eneo hilo, tutaweza pia kuufanya mji upendeze lakini pia kupanua huduma, kwa hiyo, tutakuwa tuko tayari kuhakikisha kwamba tunarekebisha michoro na saa nyingine wananchi waweze kupata haki zao. Ahsante. (Makofi)
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yanayoikumba Tanga pamoja na Bagamoyo ya bandari bubu yanafanana sana na mpaka kati ya Newala na Msumbiji ambapo wananchi wa Msumbiji wanakuja kutibiwa pale Newala. Ni lini sasa Wizara ya Ujenzi itakuja kufanya iwe rasmi badala ya kuwaachia polisi wale wananchi wanaokuja kutoka Msumbiji wanakimbizana nao. Kwa nini sasa Wizara ikaja na ikarasimisha na ikawa ni rasmi? Naomba jibu lako Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge ambaye ametoa taarifa hii. Alitupa taarifa mapema na nimpe tu taarifa kwamba suala hili tumeanza kulifanyia kazi kwa nguvu zote na matokeo yatakapokuwa tayari tutakuja tumfahamishe.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Karagwe yanafanana sana matatizo ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuhusiana na barabara kutoka Newala kupitia Kitangali hadi Mtama. Je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kilometa 5 - 10, kuanzia pale Kitangali ambapo wameanza kujenga kilometa 3, kama Serikali ilivyokuwa imeahidi hasa ukizingatia ni sehemu korofi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Akbar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ujumla kwamba tunatambua mahitaji ya uboreshaji wa barabara hasa upande wa Kusini. Hii barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge niliipita wakati nikiangalia barabara ile ya Kutoka Mtwara kwenda Mnivata tunavyoendelea kujenga kwa kiwango cha lami. Nimeona barabara hii ya Newala – Mtama lakini pia hicho kipande kingine cha kutoka Tandahimba kwenda Mtama ni muhimu sana kwa vile maeneo haya kwa kweli yanazalisha sana korosho na mazao mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Newala kwa ujumla kwamba barabara hizi tunazitazama. Nami nimeziona barabara hizi na hata ile barabara ya ulinzi ina umuhimu wake. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba Serikali tunalitazama kwa macho mawili eneo hili ili tuweze kuendelea kuboresha. Tumeshaanza na hizi kilometa 3 lakini tutaendelea ili kuhakikisha barabara hii inapitika wakati wote na kuiboresha zaidi.
MHE. MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri; lakini naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Wilaya ya Newala na Masasi hatuna mgogoro wa kimpaka ila migogoro ya mipaka watasababaisha watu wa madini. Kitendo cha viongozi wa Wilaya nyingine kwenda kufanya tathmini na kusema wao watalipa fidia kwenye wilaya nyingine wakati viongozi wapo kinavunja heshima kwa viongozi wa wilaya nyingine. Kwa hiyo inaonekana kabisda kwamba viongozi wa wilaya nyingine hawafanyi kazi. Je, Serikali ipo tayari kuacha kuwadhalilisha viongozi wa Wilaya ya Newala kuonekana hawafanyikazi na wanaofanyakazi ni Wilaya ya Masasi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, itakapotokea mrabaha, kama hawa wananchi wa Newala wanakwenda kufanyiwa tathmini Masasi italipwaje na Wilaya ya Newala itapataje haki zake? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kati ya wilaya moja hadi nyingine, kwa maana ya mgogoro wa viongozi, nadhani ni kwamba ni vizuri tu viongozi hao wakakaa chini wakaelewana kwa sababu hakuna haja ya kugombana katika hatua hii wakati Kampuni ya Natural Resources inafanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu mrabaha; hatua za utafiti ni hatua za mwanzo za uchimbaji. Pale madini yatakapogundulika kwamba Kampuni hii imefanya utafiti ikagundua madini yaani katika wilaya zote mbili kwa maana ya Newala na Masasi, basi sisi kama Wizara tutakaa chini na tutaangalia namna ya halmashauri hizi mbili kuweza kuneemeka katika kupata service levy na wala si mrabaha kwa sababu mrabaha wenyewe unakusanywa na Wizara moja kwa moja, kwa hiyo hakutakuwa na ugomvi, lakini katika service levy kwa sababu ni ushuru ambao unakwenda katika halmashauri, tutaangalia na tutakaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo siyo suala jipya, kuna maeneo mengine unakuta halmashauri mbili zinaweza zikaneemeka katika service levy kwa maana katika mradi mmoja. Kwa hiyo tutaangalia namna ya service levy zitakavyogawanywa kwenda katika wilaya hizo mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, utafiti utakapokwisha tutajua kwa sababu inawezekana ile leseni ya utafiti iko wilaya mbili lakini baadaye utafiti ukaonesha kwamba madini haya yapo wilaya moja, kwa hiyo wilaya hiyo ndiyo itakayoneemeka na ushuru wa service levy. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ndogo ili niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza. Matatizo ya meli pamoja na barabara yaliyopo Ludewa yanafanana sana na matatizo yaliyopo Mtwara, Lindi hadi Dar es Salaam. Shehena kubwa ya saruji kutoka Dangote huwa inasafirishwa kwa barabara hadi kufika Dar es Salaam, vilevile shehena kubwa ya mawe kutoka Kilwa huwa inasafirishwa hadi kufika Dar es Salaam kwa njia ya barabara, tatizo ambalo lingeweza kutatuliwa kwa kutengeneza zile meli za MS Mtwara pamoja na MV Lindi. Ni lini sasa Serikali itatengeneza meli zile za MS Mtwara na MV Lindi ili barabara ile kati ya Dar es Salaam hadi Mtwara isiharibike na shehena hiyo kubwa iweze kusafirishwa na meli hizo mbili? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba zile meli alizozizungumza Mheshimiwa Mbunge zina hitilafu, lakini tayari tumeshatuma mafundi na wataalam kwa ajili ya kwenda kuangalia gharama ambazo zinahusika kwa ajili ya matengenezo ya meli hizo. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati muafaka ukifika zitatengenezwa ili wananchi wa eneo hilo wapate huduma. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna taarifa kwamba kiwanda hiki anataka kutarajia kuchakata yeye mwenyewe, mchakato wa muhogo pale Lindi. Je sisi ambao tunalima muhogo sana katika Wilaya ya Newala na Mtwara kwa ujumla, huu muhogo wetu tutauza wapi na jitihada gani Serikali imefanya kututafutia soko lingine nje kwa kuwa hili yeye mwenyewe anasema kwamba already hilo soko linamtosha kwa ajili ya kiwanda tu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa kuanzia kiwanda hiki kimepata mashamba katika maeneo ya Nankauka (a) na (b) na maeneo mengine ili kuweza kuzalisha muhogo kwa kiwango ambacho kinatakiwa. Pia kwa kufuata taratibu zinazotakiwa, lakini katika majadiliano tuliyofanya ni pamoja na kuwawezesha wakulima wanaozunguka maeneo hayo, nao waweze kuuza muhogo wao katika eneo hilo na vilevile waweze kufaidika kwa sababu kiwanda hiki kitauza, unga lakini vilevile kitauza wanga.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kuna taarifa ambazo ni rasmi, kwamba pamoja na kwamba Dangote amepatiwa gesi hii na baadhi ya viwanda vilivyopo Mkuranga, sasa vile viwanda vimeshindwa kutumia ile gesi katika kiwango ambacho ni tarajiwa. Ina maana wanatumia gesi pungufu na vingine vimetoa notice ya kufungwa.

Je, ni lini sasa Serikali itapunguza bei ya gesi hii ili viwanda hivi visifungwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, (b) nina taarifa rasmi vilevile kwamba kuna wawekezaji ambao walikuwa wametoka mashariki ya mbali; China na Uturuki, wapatao wanne ambao waliokuwa wamekusudia kuja kuwekeza hapa nchini. Ikumbukwe kwamba faida ya gesi siyo kwamba ni kwa kuuza tu, lakini vile viwanda vingeweza kulipa kodi, kutoa ajira na faida nyingine ambazo Taifa lingeweza kupata tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kwamba bei ya gesi yetu ni Dola 5.5 per metric tones wakati katika Soko la Dunia ni Dola 3.7 per metric tones. Sasa je, Serikali ina mkakati gani na kwa nini sasa isifanye sub…

MWENYEKITI: Swali, swali swali!

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni kwamba, naomba kwamba Serikali ipunguze bei ili wawekezaji hawa wasikimbie ili tupate faida nyingine zitokanazo na viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mwili ya nyongeza ya Mheshimiwa Akbar, Mjumbe wa Kamati yetu ya Nishati na Madini. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya katika ushiriki wake kwa Kamati yetu inayosimamia Sekta yetu ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili aliyojielekeza; la kwanza Mheshimiwa Mbunge ameeleza namna ambavyo viwanda vilivyounganishiwa gesi ikiwemo Dangote na viwanda vya Mkuranga kwa mfano Goodwill, kwamba vinaona bei ya gesi ni kubwa; nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo suala limewasilishwa Wizarani; na kwa kuwa wapangaji wa gesi hii ni wa bei ya gesi asilia (EWURA) pamoja na Taasisi ya PURA ambayo ina- regulate Sekta ya Nishati upande wa gesi kuhusu masuala ya upstream, ni kwamba ndani ya Serikali jambo hili limepokelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia EWURA kwa kuwa ni kazi yao kupanga hizi bei za gesi itafanyia kazi kuangalia mchakato mzima. Pia ni lazima nikiri kwamba gharama ya uzalishaji wa gesi hapa nchini hii gesi ambayo inatumika ni zaidi ya shilingi USD 5.36. Kwa hiyo, utaona, lakini nia ya Serikali ni kuwezesha viwanda kutumia gesi na kuzalisha malighafi. Kwa hiyo, hili jambo limepokelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge ameulizia kwamba kuna wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ambao wameonesha nia ya kuwekeza, sisi kama Serikali ya Awamu ya Tano kwa kweli imeandaa mazingira ya kukaribisha uwekezaji katika maeneo mbalimbali hasa viwanda vya mbolea katika Mkoa wa Mtwara na eneo la Kilwa. Hata sasa iliundwa Kamati ya Wataalam kufanya mapitio ya gesi hasa katika suala zima la kuwezesha viwanda hivi na wawekezaji katika kuwekeza kwenye suala la mbolea. Kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge suala hili limefanyika, sasa hivi kinachofuata ni kikao baina ya wawekezaji na tangu mwezi wa Nne pia kilifanyika kwa ajili ya kupanga bei na kukubaliana. Hata wale wawekezaji kwa mfano Kampuni ya Helm na AG ya WD ya Egypt walishapewa mwelekeo na namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba Serikali ipo tayari kuwakaribisha wawekezaji na waje tu na mazungumzo yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.