Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ajali Rashid Akibar (8 total)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. AJALI R. AKBAR) aliuliza:-
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Makamu wa Rais alipokuja katika Mji Mdogo wa Kitangari miongoni mwa matatizo aliyoelezwa ni tatizo la barabara kati ya Newala na Jimbo la Mtama, Mkoani Lindi yenye urefu wa kilometa 50, naye aliahidi kusaidia ujenzi pindi fedha zitakapopatikana:-
Je, ni lini sasa barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Newala hadi Mtama ina urefu wa kilometa 74.23. Kati ya hizo, kilometa 17.03 ni za lami na kilometa 57.2 ni za changarawe. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Mtwara huifanyia matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum na matengenezo ya sehemu korofi kila mwaka ili ipitike muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/20118 jumla ya shilingi milioni 783.815 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Aidha, maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii yataanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, napenda kutoa tamko kwamba barabara hii tutaipa umuhimu unaostahili.
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-
Wilaya ya Newala ni Wilaya kongwe ambayo hata utawala wa Wajerumani ulizingatia mpango bora wa matumizi ya ardhi ambao Wilaya hiyo imepangwa tangu enzi lakini hivi karibuni TANROADS wamefanya upanuzi wa barabara ulioelekea hadi Chitandi – Masasi.
Je, kwa nini Serikali kupitia TANROADS Mtwara isifanye tathmini ya nyumba za wakazi hao na kuwalipa fidia?
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-
Wilaya ya Newala ni Wilaya kongwe ambayo hata utawala wa Wajerumani ulizingatia mpango bora wa matumizi ya ardhi ambao Wilaya hiyo imepangwa tangu enzi lakini hivi karibuni TANROADS wamefanya upanuzi wa barabara ulioelekea hadi Chitandi – Masasi.
Je, kwa nini Serikali kupitia TANROADS Mtwara isifanye tathmini ya nyumba za wakazi hao na kuwalipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mbuyuni – Makong’onda – Newala sehemu ya Chitandi – Masasi yenye urefu wa kilometa 41.55 ni barabara ya mkoa inayoungana na barabara ya Mkoa ya Mtwara – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 221. Barabara hii ina upana wa eneo la Hifadhi ya Barabara ya mita 60. Kabla ya marekebisho kupitia Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 upana wa eneo la hifadhi ulikuwa mita 45, yaani mita 22.5 kutoka katikati ya kila upande wa barabara. Sehemu ya barabara hii inapita katika milima mikali ya Makong’onda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ilitenga shilingi milioni 581.586 na mwaka 2017/2018 ilitenga shilingi milioni 396.437 kwa ajili ya kuboresha ahadi ya barabara kufikia kiwango cha lami katika milima ya Makong’onda na kupunguza ajali kwenye sehemu ya miteremko mikali. Jumla ya kilometa mbili za barabara katika milima Makong’onda zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji wa upanuzi wa barabara unaoendelea, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilitoa notisi kwa wananchi wanaomiliki mali ndani ya mita 22.5 za eneo la hifadhi ya barabara ili waondoe mali zao na kuacha wazi eneo hilo kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Barabara Namba 13 ya Mwaka 2007 na kanuni za mwaka 2009.
Aidha, kwa walio ndani ya mita 7.5 ambazo ni kutoka zinapoishia mita 22.5 za eneo la hifadhi ya barabara na mita 30 zilizoainishwa katika Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007, tathmini ya mali zao itafanyika pindi Serikali itakapohitaji maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutolewa notisi hizo, baadhi ya wananchi walipeleka malalamiko yao katika Mahakama ya Ardhi ya Kanda ya Mtwara kupinga kuondoa mali hizo ambapo hadi sasa shauri hilo bado liko Mahakamani. Taratibu za Kimahakama zitakapokamilika, Serikali itachukua hatua stahiki kwa kuzingatia uamuzi wa Mahakama.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. AJALI R. AKBAR) aliuliza:-
Je, nini hatma ya Mradi wa Maji wa Makondeko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeandaa mpango madhubuti katika kuhakikisha inaboresha huduma ya maji kwa wananchi wanaohudumiwa na Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Makonde. Katika kufikia lengo hilo, Wizara inatekeleza mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi za muda mfupi, Wizara imefanya ununuzi wa mabomba ya urefu wa kilometa 24 kwa ajili ya kukarabati baadhi ya maeneo yaliyochakaa sana yenye kipenyo cha inchi mbili hadi sita, kwa maeneo ya Makote hadi Nanguruwe, Nanda hadi Kitangali, Chihangu hadi Mnyambe, Ghana Juu hadi Lukokoda na Mahuta hadi Nanywila. Aidha, ununuzi wa pampu kumi umefanyika ambazo zitafungwa katika vyanzo vitano vya kuzalisha na kusambaza maji. Matayarisho ya ulazaji wa mabomba na ufungaji wa pampu yanaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda wa kati Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo (CRIDIF) kutoka Afrika ya Kusini wametekeleza ukarabati wa visima sita ambavyo vimeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita miloni 6.72 hadi lita milioni 11.88 kwa siku katika chanzo cha Mitema.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa CRIDIF wanaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ambayo itahusu ununuzi na ujenzi wa bomba kuu kutoka chanzo cha Mitema kwenda Nanda la urefu wa kilometa
8.56 lenye kipenyo cha inchi 12; ujenzi wa mtandao wa usambazaji kutoka Nanda kwenda Kijiji cha Mtopwa na ukarabati na ujenzi wa matanki ya maji katika Vijiji vya Mtopwa, Nanywila na Mtavala.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa muda mrefu, Serikali imepanga kutumia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 84 kutoka mkopo wa masharti nafuu wa Serikali ya India ambazo zitatumika kufanya ukarabati wa mradi mzima. Kwa sasa majadiliano kwa ajili ya kusaini mkataba wa kifedha yanaendeea kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India.
MHE. DUA W. NKURUA (K.n.y. MHE. RASHID A. AKBAR) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza Bonde la Mto Ruvuma ili lilete tija kwa wananchi hasa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Mto Ruvuma liko Kusini mwa Tanzania na linapatikana katika Halmashauri za Wilaya za Songea, Namtumbo, Tunduru, Nanyumbu, Newala, Tandahimba na Mtwara. Bonde hilo lina zaidi ya skimu 75 ambazo zinatumika katika kilimo cha umwagiliaji. Serikali kwa kushirikiana na Vyama vya Umwagiliaji imeendelea kuboresha skimu hizo ili kuhakikisha skimu hizo zinaendelea kufanya kazi kama ilivyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002, maeneo mbalimbali yalibainishwa ikiwa ni pamoja na Bonde la Ruvuma na kuandaliwa mpango mkakati wa uendelezaji wa skimu zilizopo na kuanzisha skimu mpya. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango kabambe wa Taifa hususan katika Bonde la Mto Ruvuma.
MHE. MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-
Madini aina ya Coltan yamegundulika katika Wilaya za Ruangwa, Masasi na Newala, lakini Wizara ya Madini imeweka beacon katika Kijiji cha Nandimba, Kata ya Chilagala.
(a) Je, ni utaratibu gani umetumika kuweka beacon katika Wilaya nyingine?
(b) Je, Serikali haioni kupora rasilimali ya wilaya nyingine kunaweza kusababisha migogoro?
(c) Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Akbar Ajali, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini lenye sehemu (a), (b)na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ruangwa, Masasi na Newala hakuna uthibitisho wa uwepo wa madini aina ya Coltan yaliyogunduliwa. Madini yaliyogunduliwa katika Wilaya hizo ni aina ya Graphite yaani madini ya Kinywe ambapo baadhi ya Kampuni zimepewa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na Kanuni zake, mmiliki wa leseni anatakiwa kuweka alama (beacon) zinazoonesha mipaka ya leseni yake ili jamii inayozunguka maeneo hayo ijue mwisho wa leseni husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, beacon zilizopo katika Kijiji cha Namlimba ziliwekwa na Kamuni ya Natural Resources Limited wakati wa ukusanyaji wa taarifa muhimu. Kampuni hii ya Natural Resources Limited ina umiliki wa leseni ya utafiti wa madini ya Graphite yenye nambari PL 10644/2015 ambayo mipaka yake inaingia kwenye Wilaya za Masasi na Newala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina lengo la kupora rasilimali ya Wilaya nyingine bali lengo lake ni kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinazopatikana katika eneo husika, zinanufaisha wananchi wake na taifa kwa ujumla. Hadi sasa kampuni hiyo inaendelea na shughuli za utafiti wa madini ya graphite (kinywe). Pindi itakapogundulika uwepo wa mashapo ya kutosha, taratibu za kuvuna rasilimali hiyo kwa manufaa ya Watanzania wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Newala zitafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Kampuni ya Natural Resources Limited haina mgogoro wowote na wananchi wa maeneo hayo. Namwomba Mheshimiwa Rashid Akbar Ajali kama kuna tatizo la mipaka ya kiutawala katika Wilaya za Masasi na Newala suala hilo liwasilishwe kwenye Wizara husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y MHE. RASHID A. AKBAR) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Hospitali ya Wilaya ya Newala watumishi pamoja na vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuhakikisha vituo vinakuwa na vifaa tiba vinavyohitajika. Hospitali zinapatiwa rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi 198,671,475mpaka sasa shilingi 120,510,860 zimepokelewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imetenga shilingi 244,066,959.92 kwa ajili ya vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala.
Mheshimiwa Spika, uhaba wa watumishi ni changamoto inayovikabili vituo vingi vya kutolea huduma za afya nchini. Hata hivyo Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kadri vibali vya ajira vinavyopatikana. Mwezi Novemba, 2017 Halmashauri ya Mji wa Newala ilipata watumishi 12 wa kada mbalimbali za afya na katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi 60 wa kada mbalimbali za afya. Serikali itaendelea kupeleka watumishi wa afya, vifaa tiba na vitendanishi ili kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Newala.
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-

Wananchi wa Mtwara ni wakulima wakubwa wa zao la muhogo:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia masoko ya uhakika wakulima hao?

(b) Je, kwa nini Serikali isiwapatie wajasiriamali, hasa akina mama, viwanda vya kuchakata muhogo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, zao la muhogo ni miongoni mwa mazao ambayo Wizara yangu imepanga kuyapa msukumo wa kuyaongezea thamani ili yaweze kuchangia katika ukuzaji wa uchumi na kuongeza pato ya Taifa. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imekuwa na mkakati mbalimbali wa kuliongezea thamani na kupanua wigo wa soko la zao la muhogo. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 28 Juni, mwaka 2018 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa aliagiza Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuunda Kamati Maalum ya Wataalam na kupitia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima na kushindwa kuuliza zao hili katika soko la China. Kamati imeshakamilisha kazi yake na imeshatoa mapendekezo yake Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanda cha Cassava Starch of Tanzania Corporation kilichopo Mbalala Mkoa wa Lindi chenye uwezo wa kuchakata tani 60 za muhogo kwa siku umekamilika kwa asilimia 90. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji wa unga wa muhogo kwa majaribio mwezi Januari, 2019. Kukamilika kuanza uzalishaji rasmi katika kiwanda hiki kutatoa fursa ya soko kwa wakulima wa muhogo wa Mikoa ya Kusini. Vilevile kutokana na kukua kwa soko la unga wa muhogo duniani nawahimiza wajasiriamali kupata ushauri kutoka kwa wataalam wakiwemo SIDO na TIRDO kwa lengo la kuelimishwa namna bora kuchakata zao hili ili kuuza katika masoko hayo hususan China ambako mahitaji ya muhogo ni makubwa.
MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa gesi kutoka Mtwara na Songosongo inatumika kwa asilimia sita tu:-

(a) Je, kwa nini Kiwanda cha Saruji cha Dangote na Mtwara Cement Mkoani Mtwara havijapatiwa umeme wa gesi asilia hadi leo?

(b) Je, kwa nini Wananchi wa Mtwara wasiunganishiwe gesi asilia kwenye nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, Mbunge wa Newala Vijiji, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kiwanda cha Saruji cha Dangote kimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa kuwezesha matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme kwa ajili ya kiwanda cha Dongote ilikamilika na kuanza kufanya kazi mwezi Agosti, 2018.

Aidha, hadi kufikia Mwezi Aprili, 2019 kiwanda cha Dangote kimeanza kutumia wastani wa futi za ujazo milioni tano kwa siku kwa kuzalisha umeme. Awamu ya pili ya mradi ilikamilika mwezi, Desemba, 2018 na sasa kiwanda cha Dangote kinatumia gesi ya wastani wa futi za ujazo milioni 15 hadi milioni 20 kwa siku kwa ajili ya uzalishaji wa Saruji. Jumla ya gharama za mradi ni shilingi bilioni 8,200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa TPDC inaendelea na utekelezaji wa mradi kwa kuagiza na kujenga miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia majumbani, viwandani na katika Taasisi mbalimbali kwa Mikoa ya Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asilia Mkoani Mtwara imeshaanza ambapo kwa sasa kazi ya ununuzi wa vifaa, mabomba, mita za kupimia gesi pamoja na vifaa vya kupunguza mgandamizo wa gesi inaendelea. Inategemewa zaidi ya Kaya 120 za awali zitaunganishwa mabomba ya gesi Mkoani Mtwara kwa matumizi ya nyumbani ifikapo Mwezi Juni, 2019.