Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ajali Rashid Akibar (12 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nikushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili bila kuwasahau wananchi wangu wa Newala ambao wamenifanya niwe katika jengo hili, nawashukuru. Niwaambie kwamba waendelee na maandalizi ya msimu wa korosho wa 2016/2017 ambapo wamebakiza miezi miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa mchango wangu kwa Wizara hii, nianze kumpa pongezi Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchapa kazi nzuri. Pia nimpe pongezi Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Vilevile niwapongeze Mawaziri wangu na niwaambie kwamba nawapongeza sana lakini waendelee kuchapa kazi pamoja na ugumu wanaoupata katika bajeti hii, wao waendelee tu hivyo hivyo na sisi tutaendelea hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukakosa kila kitu maisha yakaendelea, lakini huwezi kukosa afya maisha yakaendelea maana huo utakuwa ndio mwisho wa uhai wako. Hii inaonesha umuhimu wa Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua nia nzuri ya Serikali yangu kwamba sera ya Chama cha Mapinduzi ni kujenga vituo vya afya kwa kila kata na kujenga zahanati katika kila kijiji. Pia kutoa maisha bora kwa watumishi wote ambao watakuwa katika hivyo vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikumsikia Mheshimiwa Waziri ambaye ndiye mwenye dhamana akizungumzia kuhusu mpango wa kujenga vituo vya afya. Maana nilitarajia Mheshimiwa Waziri angekuja na mpango mkakati wa kuonesha kwamba je, hiyo sera yetu ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga vituo vya afya kila kata utakuwaje na kwa maeneo yapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matibabu ya wazee na tumeanza kutoa michango ya matibabu ya wazee tangu tukiwa Madiwani karibu miaka mitano au sita huko nyuma, kila siku tumekuwa tukizungumzia kwamba sera ya wazee inatayarishwa na ipo mezani. Sisi ambao tulikuwa tunapita kunadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tulikuwa tunawaambia kwamba Mheshimiwa Magufuli akishapita basi tunatarajia kwamba matibabu kwa wazee yatakuwa bure. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hakuja na mpango mkakati wa kuonesha wale wazee ambao hawana uwezo watatibiwa vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa hivi wakati umefika kuwa na mkakati kuhakikisha wale wazee ambao wapo katika vijiji maana yeye amezungumzia wale wazee waliopo katika vituo kwamba wanatoa vyakula na kutoa huduma za kimsingi lakini Serikali ina mpango gani kuhusu wale wazee ambao hawapo katika vituo vya kulelea wazee? Vijijini ndiko ambako kuna wazee wengi ambao kwa kweli wengine hawana uwezo, hawana hata pesa ya kuweza kununua dawa. Kwa hiyo, ni wakati umefika Serikali kuona hawa wazee ambao hawana uwezo ni nani ambaye anaweza akawalipia hizi bima za matibabu ili na wao waendelee na maisha kwani sote hapa ni wazee watarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kule ambako kuna vituo vya afya vichache hakuna watumishi katika vituo hivyo. Mimi natokea katika Wilaya ya Newala, nina vituo vya afya viwili lakini nina kata 22 ambako kuna vijiji zaidi ya 146 lakini hatuna watumishi katika vituo hivyo vya afya. Vituo hivyo vya afya vilijengwa early 1970’s wakati Waziri wa Afya akiwa Mheshimiwa Nangwanda Sijaona lakini vilijengwa jengo tu lakini hakuna zile huduma za mama na mtoto, ina maana sehemu ya akina mama kujifungulia hakuna. Kwa hiyo, sisi tunapata matatizo kwani akina mama hawa wanajifungulia kwenye chumba kidogo hivyo kukosa uhuru na kushindwa kujifungua kwa nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hao watumishi wachache waliopo hawana sehemu ya kuishi. Mheshimiwa Waziri hakuja na mkakati wa kuonesha kwamba hawa watumishi wachache waliopo katika hivi vituo vya afya watajengewa nyumba ama wataboreshewa vipi makazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningemuomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleze vile Vituo vya afya vya Kitangali na Chihango ambavyo vilijengwa miaka ya 70 ambavyo vilishindwa kumaliziwa na Serikali za awamu mbili au tatu ambazo zimepita, Serikali hii ina mpango gani wa kuweza kuzimalizia ili ziwe na sifa ya kusema kweli kwamba hivi ni vituo vya afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu dawa au tiba tunazozipata hospitalini maana tunapokwenda tunakosa dawa lakini unapokwenda kununua katika maduka ya dawa unakuta dawa ambazo zimeruhusiwa kuingia hapa nchini ni dawa kutoka India tu. Ina maana kwamba wanaotengeza dawa ni watu kutoka India pake yake katika dunia hii na watu wote wananunua dawa kutoka India? Huko India kuna kitu gani, ina maana Wazungu wao wananunua dawa huko? Inasemekana kwamba magonjwa mengi ya ini na figo yanatokana na matumizi ya dawa ambazo hazikidhi viwango. Ina maana sisi tunakula dawa nyingi ambazo zinakosa viwango na ambazo zipo chini viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inavyosemekana baadhi ya dawa kutoka India zinakosa vile viwango na ndiyo maana watu wengi wanatumia zile dawa kwa muda mrefu bila kupata unafuu.
Kwa hiyo, naomba kama kuna dawa zinapatikana katika nchi zingine ambazo zina viwango vya juu basi Serikali ifanye mkakati wa kuingia katika hilo soko ambalo nchi zingine au nchi za Ulaya au soko la Ulaya wanaenda kununua hizo dawa siyo kufanya masihara au mchezo na maisha ya Watanzania. Maana nchi bila afya njema haiwezi kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza awali kwamba unaweza ukakosa kila kitu, ukakosa barabara, ukakosa huduma ya maji lakini ukikosa afya njema hilo Taifa haliwezi kuwa na nguvu. Naomba Wizara hii ijikite katika kuhakikisha kwamba dawa ambazo tunanunua ni zile ambazo zipo katika soko la awali au dunia ya kwanza ndizo wanazokula na sisi tule hizo ili tuwe na afya bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tumeambiwa hapa kwamba bajeti ambayo ilikuwa imetengwa mwaka jana ni asilimia 100 lakini iliyofika kule ni asilimia 39, tatizo ni nini? Kama Wizara zingine zimekwenda kule asilimia mpaka 70, afya tumeifanyia masihara. Jamani tuache kufanya masihara na afya zetu, afya ni jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe kwamba hao vijana ambao hawajaajiriwa waajiriwe ili wawepo katika hivi vituo vya afya. Mbona Wizara ya Elimu imeweza japokuwa kunakuwa na upungufu lakini ule upungufu wa Wizara ya Elimu hauwezi kufananishwa na Wizara ya Afya. Wizara ya Afya ni kweli kabisa hasa katika wilaya au mikoa iliyoko pembezoni kule hakuna kabisa watumishi. Unamkuta mtumishi au nesi, yeye ndiye anayekupokea, anaandika cheti, ndiye anayekupa dawa. Hivi inawezekana vipi ukapiga kona wewe mwenyewe na ukaenda ukafunga wewe mwenyewe, inawezekana hiyo?
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri afanye tathmini hasa kwa hii mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi hii. Kwa mfano, sisi Wilaya ya Newala ina Hospitali ya Wilaya pale lakini wale watu wanaokuja kutibiwa wengine wanatoka Msumbiji. Pamoja na kuwa na hiyo Hospitali ya Wilaya lakini nina vijiji karibu 146 na hiyo Town Council yenyewe ina vijiji karibu 80, je, vinatosha?
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kuchukua nafasi hii kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais, maana tusipomshukuru tutakuwa ni wezi wa fadhila. Mheshimiwa Rais katika Wizara hii ametoa mchango mkubwa sana kwa kuchukua jitihada zake za dhati kabisa kutafuta fedha na kuweza kununua ndege ambazo kwa kweli umekuwa mchango mkubwa sana kwa Wizara hii ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Gibson pale rafiki yangu naye ameona kwamba mchango wa Mheshimiwa Rais katika kununua ndege ni mchango mkubwa sana kwake yeye binafsi amesaidia sana kufanya contribution ili Wizara hii na yenyewe kwenye utalii ionekane machoni kwetu na watalii wa nje moja kwa moja na ndege nyingine zinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango huu ningemwomba rafiki yangu Maghembe ambaye ndiye Waziri, atambue mchango wa Mheshimiwa Rais, vilevile atengeneze nishani ya kumtambua Mheshimiwa kama Mr. Utalii namba moja baada ya hapo kila mwaka atakuwa anatengeneza nishani moja moja hii itakuwa nafasi mojawapo ya kumtangaza Mheshimiwa Rais na kuwatangaza wale wengine wote ambao watakuwa wanashiriki katika kutangaza utalii katika nchi yetu, yatakuwa ni mashindano makubwa ambapo tutakuwa tunatambua vyanzo vipya, hapo itakuwa ni sehemu ya matangazo, atashirikisha wanafunzi, atashirikisha wanavyuo na wanahabari vilevile. Mheshimiwa Maghembe asiogope, atumie jitihada zake kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo za Mheshimiwa Rais, kama Wabunge wenzangu walivyosema sekta ya utalii ni sekta ambayo ni pana sana, ili sekta hii iweze kufahamika au kama unataka kuanzia kwenye sekta ambayo ni mpya ni lazima azitambue maliasili zilizopo katika ardhi hii na akishatambua maliasili ardhi zilizopo katika ardhi hii ni lazima afanye tafiti. Akishafanya hizo tafiti hana jinsi nyingine ni lazima aingie gharama kubwa sana ya kutangaza vivutio hivyo, ukishatangaza hivyo vivutio hapo ndipo utapata rasilimali na atapata fedha Mheshimiwa Maghembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Maghembe juzi wakati tunatoa mchango hapa mimi nilitoa mfano mmoja mdogo sana kuhusu kisiwa cha Kilwa. Katika mchango wangu mkubwa sana nitazungumzia Kisiwa cha Kilwa. Inawezekana watu wengi hawajui Kilwa maana yake nini, wanasikia tu kwamba kuna Kilwa Kipatimu, Kilwa Masoko, Kilwa Pande. Hayo maeneo yote yalikuwa ni kisiwa kimoja na kisiwa hiki kina maajabu sana. Kisiwa hiki kilinunuliwa na tajiri mmoja ambaye inasadikika kwamba alinunua kwa kipande cha nguo ambacho kilifunika kwenye vijiji vyote hivi na kile ambacho kilifunika paliitwa Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilwa zote saba au nane ni maeneo ambapo yule mfalme alikuwa anamiliki, hiyo historia ni nani ambaye anayeifahamu kwa kweli, watu wengi hawaifahamu historia hiyo na kuna majengo katika hivyo visiwa pamoja na hayo maeneo kuna majengo ya Wajerumani ambayo namwomba Mheshimiwa Waziri akafanye tafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nilizungumzia kwamba kuna magofu na visiwa zaidi ya 1000 ambavyo hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani tukisema tugawane kila mmoja atapata viwili viwili, haya ni maeneo mapya ya utalii, Mheshimiwa Maghembe aende kule akafanye tafiti hayo maajabu watu wayaone. Siyo ajabu hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani wengine hawajui. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, Watalam wake wafanye tafiti za kina ili imsaidie yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ukienda Lindi Mjini, kuna eneo linaitwa Kitunda. Bahati nzuri nilikuwa nimekwenda kule kulikuwa na watu ambao wapo kule chini inasemekana kwamba wanatafuta fedha ya Wajerumani, na inasemekana kwamba kuna handaki ambalo liko ndani kama kilomita mbili ambapo Wajerumani walikuwa wanatembea chini kwa chini. Mheshimiwa sisi ambao tulikwenda kule tuliweza kuogopa, lakini Mheshimiwa Waziri nadhani akitumia watalaam wake ataangalia lile handaki lina nini ni sehemu moja ambayo ni nzuri sana ya kiutalii ya vivutio, lakini kwa kuwa havijatambuliwa haviwezi kufahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka hapo nenda Mtwara moja kwa moja kule kuna maeneo ambako Stanley alikaa siku saba kule kuna nyumba, bahati nzuri nimeiona leo katika maandishi ya Mheshimiwa Waziri, lakini yale magofu yaliyopo pale Mtwara ni mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba yale magofu ambayo au na vile visiwa ambavyo vipo kule Kilwa ambavyo watu wanaweza wakavirekebisha, tuwavutie wao hata kama wakitengeneza basi wakae navyo kwa muda mrefu na siyo kwenda kuwanyang’anya na kuwabugudhi wale. Kwa mfano, kulikuwa na yule Mama ambaye alikuwa amekuja pale akatengeneza kile kisiwa na akajenga hoteli akawa analeta watalii wake wasiopungua 70 hadi 80 na akawasomesha wanakijiji pale tusim-discourage sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye anamiliki lakini maana yake baada ya hapo ile ardhi hawezi kuondoka nayo hebu Wizara ifanye utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu ambao wanafufua au wanarekebisha hayo magofu, hayo magofu yanaendelea kubaki katika structure ya asili, provided hawachukui hatuna sababu ya kufunga biashara zao. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii kama kuna mtu anaweza kutambua hivyo na anaweza akavitangaza hivyo na kuna watu wanafanya hizo renovation basi watambue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwangu pale kuna shimo linaitwa shimo la Mungu, shimo la Mungu hilo ukiangalia liko chini ni kama kilomita mbili hivi. Kwa hiyo, maana yake ukienda ukiangalia mara moja kama siyo mzoefu lazima mtu aje akushike mkono. Vilevile kuna njia ambayo walipita Wajerumani na kuvuka kwenda Msumbiji. Hawa Wajerumani walikuwa wametokea Msumbiji wakati wanafanya research wakafika pale na ndiyo maana waka- establish Wilaya ya kwanza Tanzania ambayo ni ya Newala, lakini walikuwa wanafanyia research katika lile shimo la Mungu. Namwomba Mheshimiwa Waziri aende akalibainishe hilo shimo la Mungu ili watu walifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani anayejua kwamba leo ukienda Zanzibar kuna Kisiwa cha Chumbe ambacho kuna kobe wakubwa ambapo watu wawili tunaweza tukapanda kama ngamia tukazunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais aliyepita alizungumza kitu kimoja ‘ukitaka kula lazima uliwe’ asiogope kuliwa Mheshimiwa Maghembe! Aingize fedha, apeleke proposal mbona makusanyo ni makubwa? Ili hii sekta tuweze kuvuna fedha za kutosha ni lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa. Alikuwa ana maana ya kwamba tusiogope hasara ili tuje kupata faida na ndiyo maana alisema kwamba ukitaka kula ni lazima uliwe, maana yake wekeza mtaji mkubwa then utapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haingii akillini leo maeneo ya uwekezaji ya maajabu saba ya dunia yako Tanzania, nenda Ngorongoro crater nenda Serengeti. Serengeti kuna maajabu pale kutokana na movement ya wale wanyama ambao wana-move kutoka eneo moja la juu kwenda sehemu nyingine, lakini ile kwa kweli ni maajabu lakini tunayatangaza kwa kiasi gani? Mheshimiwa Waziri apeleke habari kote Tanzania ili watu wazijue, duniani kote tusiogope hizo gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara huwa kwanza tuna-risk, tunaingiza fedha kwa kiasi kikubwa ndiyo baadaye tunakuja kupata, usitegemee kupata bila kuwekeza haiwezekani, hayo maajabu hayapo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna bodi pale kama tatu au nne, kuna fees anazozipata Mheshimiwa Waziri, kwa nini anatumia shilingi bilioni mbili kutangaza, kwa nini asichukue bilioni 20 tukapata bilioni 300. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge katika Wizara ambazo tunaweza tukapata fedha ni Wizara ya Maliasili na Utalii, fedha ipo nje, haihitaji kutumia gharama kubwa. Kwa hiyo, nimwombe sana, zile bodi tatu kwa nini zinakuwa nyingi vile? Kwa nini asiziunganishe kama vile tunavyofikiria kuunganisha mifuko? Aunganishe zile bodi apate bodi moja ambayo itakuwa inafanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa kumalizia niongelee kuhusu utalii wa ndani. Kama vile ambavyo tumezungumza, haiwezekani utalii wa ndani Mheshimiwa Waziri akafanya peke yake. Suala la utalii ni kubwa. Naomba aunganishe nguvu na Wizara ya Habari vilevile na Wizara ya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii, lakini pili nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai sisi Waheshimiwa Wabunge. La tatu nikipongeze chama changu Chama cha Mapinduzi jana kwa kutimiza miaka 40, ni umri wa mtu mzima kwa kweli. Maana sijasikia kama Chama cha Mapinduzi kimepongezwa, kwa hiyo nitoe taarifa kwamba jana ndio kilikuwa kinatimizia miaka 40 kakweli nakipongeza sana, nampongeza Katibu Mkuu na Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nipongeze kamati zote mbili kwa maana ya Kamati ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii. Ukiangalia mustakabali wa hizi kamati zote mbili kwenye taarifa zao yaani utaona kabisa hizi Kamati zote zimefanya kazi kubwa sana tena kwa muda mfupi na kila kitu kimeelezwa humu, hakuna jambo ambalo ni geni ambalo sisi Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukalizungumza nje ya yale ambayo Kamati imeyazungumza; kwakweli Kamati nazipongeza sana kwa ufanisi wenu wa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mapungufu ambayo yanazungumzwa na mimi ningechukua nafasi hii kuchangia mapungufu ambayo nimeyaona hasa yale ambayo nimeona kuhusu dawa za kulevya. Upungufu inaonesha kabisa kwamba kulikuwa na mamlaka ambayo imeanzishwa kisheria ambayo ilikuwa imepitishwa kutoka mwaka jana lakini ukamilishwaji wa hii Kamati ndipo yote haya yanatokea leo kamata kamata inakuwa nani hajulikani akamatwe na yule ambaye asikamatwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba ile mamlaka ambayo ilikuwa imeanzishwa ule mchakato mpaka leo haujakamilika; haina commissioner, ina upungufu wa vitendea kazi na rasilimali watu. Japo kuwa kuna watu tumewasomesha lakini watu hao hawafanyi kazi, tuna polisi wa kutosha, lakini hawawezeshwi hawa watu ili wafanye kazi leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tumewahi kuwa Waheshimiwa Madiwani Jijini Dar es Salaam hili suala la kamata kamata la unga ni suala la muda mrefu sana. Vinginevyo watu watakuwa wanatuhumiwa, Wabunge wengine watakuwa wanakamatwa au watakuwa wanatajwa lakini wataambiwa wamehusika. Huu mchezo tusipokuwa makini sana itakuwa sawasawa na mchezo wa chura maana watoto walikuwa wanarusha mawe kwenye maji halafu ule mchezo watoto wanacheka, lakini chura wanalia; wakawaambia nyie watoto huo mchezo mnaoufanya ni mauti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hatujui kwamba ni nani ambaye anawajibika moja kwa moja, kwa hiyo Kamati sababu ile watu wenye mamlaka hawajapewa mamlaka wala hawajawezeshwa kufanya kazi. Kwa hiyo, wale Mawaziri wanaohusika na tasnia hii waje waileze Kamati kwamba je, ni lini sasa hizi taasisi na hizi zinaanza kufanya kazi kwa ufanisi ili tujue nani anaewajibika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye masihara ni gharama kubwa sana kutengeneza majina lakini kuyaua unaweza kuyaua kwa muda mfupi sana, tusifanye masihara kutengeneza jina. Lakini vile vile tulikuwepo pale tuliona watu ambao wametengeneza majina wameharibiwa hayo majina, lakini je, ni nani ambaye atakuja kuwajibika kwa kuharibiwa jina? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imezungumza vilevile kuhusu udhaifu ambao umejitokeza wa ukosefu wa fedha. Inaonesha kabisa kwenye tasnia ya afya, kwa sababu afya ndio lango kuu la nchi hii, tunategemea afya na elimu. Lakini utaona kabisa kwamba afya pamoja na elimu zote hizi zimepelekwa TAMISEMI. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba Wizara ya Elimu yenyewe inakuwepo pale ceremonial kama policy makers, lakini hawasimamii moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sisi tunasoma tulikuwa tunajua kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kinahusu elimu tulikuwa tunaenda Wizara ya Elimu lakini leo ukitaka kujua nini kuhusu elimu ukienda Mkoani au ukienda Wilayani Wizara ya Elimu kule, kule wewe utakuta tu TAMISEMI pamoja na Local Government kwa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana huwezi kujua kwamba kwenye ubovu wa elimu ni nani anaewajibika? Anaewajibika ni TAMISEMI au Wizara ya Elimu moja kwa moja? Kwahiyo, ningeomba hawa Mawaziri wawili wanapokuja hapa waje watueleze kwamba ni nani ambaye anawajibika moja kwa moja ili tujue kwamba ile idara ya ukaguzi iliyopo pale TAMISEMI nani ambaye anasimamia kuiwezesha fedha ili ikafanye ukaguzi ili ubora wa elimu uwe juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo upande wa afya; utadhani kana kwamba Wizara ya Afya nao ni policy makers wao wanatengeneza tu sera, lakini moja kwa moja vile vituo vya afya ambavyo vipo vijijini ambavyo havina dawa; huku tunaambiwa kwamba dawa zipo lakini ukienda vijijini dawa hazipo kabisa. Lakini vilevile tuna sera za wazee tunasema kabisa tunapokwenda kule tunaenda kujinadi kwamba aaah, sasa hivi matibabu kwa wazee zipo bure; Lakini tunaulizwa sasa hivi imeshachukua muda mrefu sisi wazee bado tunapata shida ya kupata tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya aje atueleze kwamba ni lini hii sera itakuwa imeshakamilika na hawa wazee watapata tiba ambayo moja kwa moja itakuwa bure ili nasi tuweze kujikimu kama Waheshimiwa Wabunge wamewahi kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya isipokuwa makini; mimi nadhani kwamba Wizara ambayo ninaipongeza ni Wizara ya Maji. Ukienda hata huko kwenye Local Government unakuta kabisa Wizara ya Maji inakuwa na uwajibikaji, ukienda kwenye Idara ya Maji unaona kabisa kwamba hawa watu wa maji wanajishughulisha moja kwa moja. Kwahiyo, ningeomba kwamba hizi Wizara mbili, kwa maana ya Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu na yenyewe ichukue mfumo huo huo, kwa maana kwamba wawe wanasimamiwa wanafika mpka huko chini ili kwenda kusimamia kuhakikisha kwamba haya mambo yetu yanakwenda badala ya kuwa yamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi michango yangu ilikuwa ni hiyo miwili ya kuhakikisha kwamba hawa Mawaziri wanatupa taarifa ni nani ambaye ambaye anawaibika kati ya Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa kuwa hoja yangu ilikuwa ni fupi, asante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai mpaka jioni hii ya leo, ili tuje tushiriki katika mjadala huu wa kuchangia Wizara hii muhimu. Nakushukuru wewe mwenyewe kwa kuweza kutupa nafasi hii na kutoa mchango mdogo kama huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wamezungumza Wabunge wenzangu, nami nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mpango kwa hii graph ya maendeleo ambayo inaonesha kabisa kwamba asilimia saba kwa kweli kwa uchumi kukua ni asilimia kubwa sana. Kwa kweli kwa hili, Mheshimiwa Mpango amejitahidi sana, namshukuru sana katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni juu ya Kiwanda cha Newala ambacho ameahidi kwamba, anafikiria kukichukua kukirejesha tena Serikalini. Nampongeza sana na achukue kile kiwanda sio asubiri tena aangalie uwezekano akakichukue kesho na aangalie namna gani auaweza akakigawa. Kwa sababu, vile viwanda vilikuwa vingi, Mkoa wa Mtwara na Kusini kote kulikuwa na viwanda zaidi ya 10 ambapo Serikali ilikuwa imekopa fedha nyingi sana na vile viwanda vilivyopo Newala ilikuwa ni Mkopo wa Benki ya Dunia kupitia waliokuwa wajenzi Itaro Fame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mtu yule anapewa kwa bei poa kabisa, Serikali ilikuwa imeingia kwenye deni kubwa ambalo kwa kweli ilikuwa inalilipa, lakini yule mtu mpaka leo hajafanya uzalishaji wowote wa msingi na anachokifanya yeye ni ghala tu. Sasa sio Newala tu, angalia maeneo mengine ambayo kuna viwanda kama vile, wale watu ambao tumewapa vile viwanda hawavitumii kwa yale makusudio ambayo tumewapa na badala yake wanatumia kwa madhumuni mengine. Hivyo viwanda ni vingi sana na ni kweli akichukua hatua Mheshimiwa Waziri tutamwona kwamba, sasa kweli amekuja kivinginevyo, nampongeza katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nishauri, Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano hizi taasisi kutoa fedha, kwa mfano; CAG anampa fedha kidogo sana na zile taasisi ambazo ni muhimu ambazo anadhani kwamba tunawapa mabilioni ya fedha, lakini huyu msimamizi wa fedha anampa fedha kiasi kwamba anashindwa kwenda kufanya ile kazi. Je, haitakuwa kazi ngumu sana kwa sababu, mtu umempa nyama lakini yule Mkaguzi wa kwenda kukagua kile kiwanda hana uwezo wa kwenda kumfikia yule mtu kwenda kukagua? Kwa kweli, Mheshimiwa Waziri naomba afanye jitihada zozote ili hii Ofisi ya CAG aweze kuisaidia iweze kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimepata athari vilevile kutokana na huu ukata. Toka enzi za Waziri Maghembe akiwa Waziri wa Maji, yeye likuja akaahidi pale akasema kwamba, atatupa mradi wa maji kutoka Mitema kwenda kwenye Kijiji cha Chihangu, Chilangala, Miyuyu, Mikumbi na pale maji yatakwenda kwa gravitation force hadi yafike Nnyambe. Kwa hiyo, kile chanzo cha maji kilichopo Mbwinji kikachukuliwa kikapelekwa Masasi hadi Nachingwea. Hatuna tatizo kuhusu maji kwenda Nachingwea, tatizo ni hapa toka akiwa Waziri Maghembe yule Mheshimiwa Maghembe hakuonekana tena mpaka leo kuna Waziri mwingine, kile chanzo wale watu hawajapata maji na yale maji sasa kule eneo lingine yanatoka. Kwa hiyo, wanajiuliza, hawa watu wamekuja kuchukua chanzo hiki cha maji, halafu wao waliahidi kabisa kwamba, wataleta fedha kwa ajili ya kuchukua maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kinachohitajika pale ni fedha tu kwa sababu, yale matenki alishajenga Mwalimu Nyerere yako pale Mikumbi, Miyuyi, kwa hiyo maji kutoka Mitema pale ni mabomba tu, ni kununua tu kwa kutumia fedha hadi kufika Mikumbi kupitia Chihangu. Sasa vinginevyo Mheshimiwa Waziri atakuwa ananigombanisha mimi na wananchi wangu. Sio mimi tu, vilevile wale wananchi watakuwa wanagombana kati ya kijiji na kijiji, wilaya na wilaya na mkoa na mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki wananchi wangu waende wakagombane na wananchi wa Masasi, kwa sababu wale wananchi wa Masasi ni ndugu zetu, ila nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu akae na Waziri mwenzake wa Maji, ni namna gani watawapelekea maji wale wananchi wa Newala ili wapate maji, tuangalie uwezekano wa kulitatua tatizo hili, kuliko hii ambayo sasa hivi inakuja kiduchukiduchu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuongea na Waziri wa Maji amesema kwamba tutaangalia uwezekano wa kumpata Mkandarasi, lakini hatutawaleteeni fedha; hatuhitaji fedha sisi tunachohitaji ni huduma. Mheshimiwa Waziri hebu aliangalie hilo kama limekaaje, kama limekaa vibaya, vinginevyo huu ushauri wangu utakwenda at negative attitude.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimshauri ni kuhusu wafanyabiashara na huu ugawaji wa TIN Number; inawezekana hawa TRA wanamdanganya Mheshimiwa. Mimi mwenyewe haya yamenikuta, nilienda nikasajili kampuni ambayo ilikuwa mimi mwenyewe ni Mkurugenzi pamoja na watoto wangu wanne, jumla tukawa watano, tulivyokwenda kusajili nikategemea kwamba, nitapata TIN Number bure, lakini tulivyokwenda pale tulipewa masharti kwamba, wewe ni lazima uwe na TIN Number ya kampuni, lakini na wewe mwenyewe uwe na TIN Number na Wakurugenzi wawili wawe na TIN Number.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kampuni tukailipia 1,000,000/= na kila mtu ambaye ni Mkurugenzi mle akalipia laki tano na biashara hatujafungua. Mheshiiwa Waziri haoni kama hapo ni double taxation? Hilo nimelifanya Dar-es- Salaam. Double taxation ipo nchi hii, inaonesha si kwamba unapewa tu TIN Number. Unapewa TIN Number ya kampuni ambayo ni Limited Liability Company na Wakurugenzi wote wanalipia laki tano, laki tano kutokana na ile TIN Number na biashara na duka sijafungua mpaka leo. Kwa hiyo, tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri angekuwa na alternative, hawa ni watu wake, hebu awaache wafanye biashara waingie kwenye dema, hana sababu ya kuwatafutia manati hawa watu wake, wanakuwa wengi halafu baadaye anawatoza tozo kidogo kidogo. Hiyo namwambia kabisa kwamba inawezekana ndiyo maana wale wafanyabiashara wa Kariakoo wamekimbia. Mimi ni mfanyabiashara wa Kariakoo, asituone tumekaa hapa, sisi wengine ni Wamachinga. Hicho kitu ninachomwambia na inawezekana ile milango ndiyo maana wale watu wamefunga, wamekimbia wanaogopa double taxation ya TIN Number. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika 2,500,000/= mtu hujafungua biashara. Mheshimiwa Waziri asifikirie kwamba, wananchi wake anaowadai kodi wana hela, hawa wananchi wengi milioni mbili ni hela nyingi sana, hebu afikirie, don’t look far, asifikirie mbali sana akadhani kwamba wananchi wake wana hela, hawa watu anaowaongoza ni maskini sana wana mtaji wa Sh.500,000/=, Sh.1,000,000/= na Sh.2,000,000/
=. Huyo mwenye Sh.2,000,000/= ndio ana mtaji mkubwa sana. Kwa hiyo, anapofikiria kumtoza mtu kodi ya Sh.2,000,000/= in advance na hajafungua duka asitarajie yeye akapata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Mheshimiwa Waziri aache watu wa Kariakoo wafanye biashara kama walivyokuwa wanafanya then anawatoza kodi, tena sio nyingi, hata akiwaambia kwamba, walipe laki tano atapata pesa nyingi tena za kutisha. Hayo mambo yapo, lakini inawezekana watu wanashindwa kumweleza au yeye mwenyewe aende kufanya utafiti pale Kariakoo, hayo mambo atayakuta kule, nadhani atakuja kuniambia ni kweli, sasa hayo mambo ni mazuri, hao watu wanamdanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu kama tunaingia kweli kwenye sekta ya viwanda, tuangalie namna gani wenzetu Wachina wameendelea. Kwa sababu, wale wenzetu walikuwa na mfumo wa Commune, ile Commune mwaka 1967 ilikuwa inakopa duniani, lakini leo ndio shareholder wa Exim Bank ambako leo tunataka kwenda kukopa. Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kukaa na Jeshi, kwa maana JKT aangalie pilot areas ambako wanaweza wakapeleka vijana wa JKT wakawa wanalima, lakini wakawa wanazalisha, viwanda vilevile tukawa tumekaa na mtu wa viwanda tunaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutakuwa tumetengeneza ajira, maana leo ukiwa na pilot area kama 10 na kila pilot area kuna vijana 8,000 utakuwa umeshaajiri vijana 8,000 x 10 utakuwa umeajiri vijana 80,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango mkubwa katika Wizara hii, Wizara mama ambayo kwa kweli tunaitegemea.

Mheshimiwa Spika, katika Wizara hii mimi nina wasiwasi kidogo. Wasiwasi wangu ni kwamba juzi Mheshimiwa Mpango ameonesha kwamba bajeti hii ametoa punguzo kwenye viwanda, maana yake amewasaidia wafanyabiashara wa ndani, lakini ameishia hapo hakwenda mbali zaidi, hii mimi imenitia wasiwasi sana. Kwa kuwa hakwenda mbali zaidi ina maana kwamba karibu asilimia 70 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tulitegemea kuwa hiyo asilimia 35 ambayo ameiongeza kwenye ushuru au kodi maana yake sasa angerudi tena kwa wakulima wa nchi hii ambao ni wakulima wa alizeti, korosho, mahindi na karanga ili ahakikishe kwamba anawawezesha hawa Watanzania ili tupate raw material ya kwenda viwandani; lakini hilo hakulifanya Mheshimiwa Mpango. Kwa sababu hiyo sasa kunakuwa na ugumu wa jinsi ya kupata raw material katika hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mpango atakapokuja atueleze, kwamba, je, kama amepunguza kwenye viwanda, akishapunguza au akishaongeza kodi kwenye raw material ambayo ni imported maana yake hivyo viwanda usipowezesha wananchi wa ndani vitakuwa stagnant, kwamba hakutakuwa na raw materials kutoka nje wala hakutakuwa na raw materials ambayo iko ndani. Itakuwa kama wanavyosema Wamakonde, kwamba, uchiteme wala uchimumunye, maana yake huwezi kusogea, utakuwa huna raw materials kutoka nje wala ya kutoka ndani.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini sasa kama huna raw materials kutoka nje wala huna raw material ya ndani maana yake ni hivi viwanda vyote vitasimama kwa wakati mmoja na watatengeneza shida ambayo ni kubwa sana. Kwa hiyo aangalie namna atakavyovifanya hivi viwanda. Leo tunasema hapa kwamba amewasaidia wafanyabiashara, lakini sidhani kama amewasaidia wafanyabiashara, atakuwa amewaweka njia panda kwa sababu production ya ndani ya raw material kwa ajili ya viwandani, hamna njia yoyote au hajaweka process ambayo tutahakikisha kwamba tunapata.

Mheshimiwa Spika, nina wasiwasi kwa sababu mwaka jana wananchi walipolalamikia kuhusu upande wa kilimo alisema kwamba atasaidia wakulima, kwanza kwa kufanya importation in bulk kwa upande wa mbolea. Wale wananchi hawakusaidiwa, kwenye mambo ya bulk importation. Mwaka jana alichokifanya ni kupunguza ushuru, ule ushuru wa mazao kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu. Alitengeneza nini baada ya pale? Maana yake ni kwamba waliopata nafuu ni wachuuzi, kwa sababu sheria inasema kwamba asilimia tano, maana yake kwamba ushuru utalipwa na mnunuzi, kwa hiyo unavyosema kwamba umepunguza hadi asilimia tatu unakuwa hukumsaidia mkulima na badala yake umemsaidia mnunuzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maana yake wakulima pale wakawa wamepigwa changa la macho ambalo hawakuliona, tukadhani kwamba, ok utafidia kwenye mambo ya importation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu vile vile imetokea, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba ok, sasa tunataka ushuru wa mazao, kwa mfano huu wa korosho, maana Sheria ya Korosho tunayo, anasema kwamba asilimia 35 ya mazao ya korosho yatakwenda kwenye Mfuko Mkuu na asilimia 65 itarudi tena kwenye Bodi ili kuwezesha wale wakulima wa korosho waweze kuhakikisha kwamba wanapelekwa kwenye taasisi kwa mfano Naliendele.

Mheshimiwa Spika, wakifanya tafiti zile huu ugonjwa wa mnyauko, maana yake hautakuwepo. Sasa anavyong’ang’ania pesa zote bilioni mia mbili, akitegemea kwamba mwakani atapata kutoka wapi? Nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwamba ni vizuri zile fedha za korosho ambazo anazo katika mfuko wake ambazo haku- release; maana leo mfuko wa sulphur unauzwa Sh.65,000, kwa hiyo ile production ya mwaka jana ambayo alipata bilioni mia tatu sitini na tano asitarajie mwaka huu kwamba atapata kwa sababu hiyo sulphur haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri asitarajie kupata yai la dhahabu kwa kumchinja kuku mwenyewe badala ya kumwezesha yule kuku aendelee kutaga ili apate kidogo kidogo. Kwa hiyo natarajia kabisa mwaka huu inawezekana kabisa kwa namna yoyote asipate zile bilioni mia tatu sitini na tano; kwa hiyo, maana yake atatuweka katika hali ngumu sana Mheshimiwa Dkt. Mpango. Hebu afanye utaratibu kwa kuhakikisha kwamba hawa wakulima wanapata zile pembejeo za kilimo, ili mwakani aweze kupata fedha za kutosha.

Mheshimiwa Spika, lingine, namsifu sana Mheshimiwa Mpango, kwamba ni mkusanyaji mzuri wa mapato. Hata hivyo Mheshimiwa Dkt. Mpango, halipi madeni kwa ma- supplier wa ndani. Asipowalipa ma-supplier wa ndani maana yake hakuna mzunguko wa fedha wa humu ndani, mzunguko wa ndani usipokuwepo, maana yake umaskini utakuwepo kila mahali, utakuwepo Arusha, utakuwepo Singida, Utakuwepo Dodoma, utakuwepo kila mahali. Kwa hiyo nimwombe sana alipe …

T A A R I F A . . .

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Spika, nashukuru hiyo taarifa nimeipokea na hiyo taarifa vile vile Mheshimiwa Dkt. Mpango naomba aipokee; kwamba ule mchezo alioufanya, sasa hivi unatupeleka mahali pabaya. Zile fedha ambazo mwaka huu alipata, bilioni mia tatu sitini na tano, mwaka huu alitarajia labda angepata bilioni mia saba hizo fedha hatazipata tena. Maana yake si ajabu, ule mnyauko uko kule na mikorosho inakauka na ni mikavu sana.

Mheshimiwa Spika, namwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, in future, ahakikishe kwamba hawa wakulima na hizi taasisi zake hizi, hasa Naliendele au zile ambazo ni za kilimo ahakikishe zile fedha zinaenda mapema ili production kwa wakulima iende kwa wakati na uzalishaji uende kwa wakati ili waweze kupata fedha nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kama akiendelea kung’ang’ania hizi fedha, akiwa nazo mfukoni atazitumia mwisho hata hizo kidogo hatazipata Mheshimiwa Mpango. Nimwombe sana, najua TRA kama nilivyomwambia kwamba ni kweli anakusanya vizuri na atumie mbinu ambazo kwa kweli ni shirikishi kwa wafanyabiashara, maana TRA wanajifanya kana kwamba ni polisi, wanawatisha wafanyabiashara mpaka wale wafanyabiashara wanaogopa.

Mheshimiwa Spika, namwambia Mheshimiwa Waziri wenzake tulikusanya ushuru wa mazao lakini tulikuwa tunawashirikisha hawa wafanyabiashara kiasi kwamba ukienda mtu anakulipa yeye mwenyewe; usiende pale kwa vitisho. Aangalie hii Taasisi yake ya TRA iwe shirikishi na ishirikiane na wafanyabiashara ili akusanye mapato vizuri, isiwe kwamba wakiwaona TRA wanakimbia wanafunga maduka; huo si utaratibu wa kukusanya fedha. Naomba TRA wawe rafiki kwa wafanyabiashara ili mapato ya nchi yetu yapate kuongezeka na yeye mwenyewe itakuwa rahisi katika utendaji wake wa kazi, vinginevyo atakuwa anapata ugumu kila siku.

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa hizi asilimia tano kuzipunguza mpaka asilimia tatu amezifanya halmashauri ziwe maskini. Leo halmashauri zinashindwa kulipia yale mahitaji muhimu. Anazitaka halmashauri leo zilipie bili ya maji, lakini ceiling yetu amepunguza ile kutoka asilimia tano hadi tatu, sasa hizo fedha zitatoka wapi ikiwa kila siku anatoa maagizo kwamba kuwe na miradi huko, fedha zinatoka wapi?

Mheshimiwa Spika, kana kwamba hiyo haitoshi halmashauri haziendelea kwa sababu hata hizi property tax amewanyang’anya, maana yake fedha zote sasa hivi badala ya kuwa kwenye Local Government ziko kwenye Central Government. Hii inamaanisha kwamba tunarudisha utawala wa kiimla, wa kizamani, kwamba hakuna ushirikishwaji katika miradi kutoka kwenye Local Government, miradi yote inatoka Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango kwamba, arudishe utaratibu kama Mzee wetu Mwalimu Nyerere alivyokuwa amesema kwamba tunatoa madaraka mikoani, tunapeleka huko chini ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika mapato ili miradi hii iwe shirikishi, badala ya kila kitu kwenda Serikali Kuu; inakuwa ni ngumu kiutendaji; nimwombe sana awashirikishe wananchi katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mchango wangu ni huo, ila nimwombe sana Mheshimiwa Mpango aache kung’ang’ania zile fedha za korosho, atoe release ili watu wapate kununua zile pembejeo muhimu za kimsingi za kilimo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kunipa nafasi ili nitoe mchango kwa mpango huu ambao ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango, anaufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumsifu Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha, kwa mipango yake, yeye ni mtaalam sana katika kuandaa mipango hasa ya kukusanya kodi. Ila tatizo la Mheshimiwa Dkt. Mpango ambalo mimi huwa naliona siku zote ni kwamba hafanyi coordination kati ya mpango mmoja kwa maana ya kwamba kushirikisha wale watu ambao wanazalisha, kwa mfano kushindanisha watu wa kilimo, watu wa uchumi na watu wa viwanda na kilimo kinaingiaje, yaani hao mahusiano hao watu anawezaje kuwaweka pamoja wakahusiana. Maana yake akishafanya coordination kati ya hivi vitu vyote basi Mheshimiwa Dkt. Mpango atakuwa mzuri sana katika bajeti. Kwa hiyo mimi naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango nimshauri kwa mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kabla ya uhuru au baada ya uhuru mwaka 1961 na baada ya uhuru, Mheshimiwa Rais wetu mstaafu ambaye ni hayati sasa hivi, Baba wa Taifa alikuwa na Jeshi maalum ambalo baada ya kupata uhuru aliona kwamba nchi hii haiwezi kujiongoza peke yake mpaka nchi yote ya Afrika iwe huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo baada ya kuona kwamba nchi yoyote haiwezi kuwa huru baada ya kuwa wameungana na Zanzibar kitu kilichofuata pale, Mheshimiwa Rais au Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilichofanya ni kuhakikisha Jeshi letu linakuwa Jeshi la Ukombozi la Afrika na Jeshi letu lilikuwa limepelekwa kila sehemu katika Afrika kwenda kufanya participation katika kuhakikisha kwamba zile nchi nyingine zinakuwa huru. Zile nchi huru zote leo zimekuwa huru lakini leo tulitarajia kwamba kwa kuwa kulitumia fedha zetu nyingi sana kwa kuweka makambi hapa nchini kwetu na sisi wenyewe tukabaki nyuma ndiyo hao hao ambao wametufikisha leo Tanzania tumekuwa nyuma wenzetu wamekuwa mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike Mheshimiwa Mpango ni coordination ile ile kama jeshi letu wakati ule lilikuwa la kupigania uhuru, sasa hivi jeshi letu liwe ni jeshi la kiuchumi, tutengeneze jeshi wakati ule wakati tulikuwa na watu milioni tisa leo tupo watu milioni 50, tuna rasilimali watu ambao ni wengi sana ambao tukitengeneza jeshi wale ambao tumeshawatafutia uhuru na bado wanaendelea kupigana kama ndugu wanashindwa kujiongoza sisi tunaenda kuwauliza eeh, bwana mmeshindwa kuelewana kujitawala si ndiyo, tunamgonga mmoja halafu wanatulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndivyo jeshi la kisasa lilivyo duniani kote yaani tuwe na nguvu tuwe na jeshi lenye nguvu kama watu wanapigana na tuliwasaidia kukomboa uhuru wao mbona hawakuturudishia hizo gharama tutapataje. Kwa hiyo, maana yake kwa kuwa masuala ya ulinzi mara nyingi hatuwezi kuyazungumza wazi. Niombe Kamati ya Ulinzi na Usalama ifanye coordination na Bwana Mpango tuangalie namna gani tunaweza tukatumia jeshi letu kulishirikisha kwa wale watu wanaofanya fujo wakati tuliwasaidia kukomboa uhuru ili tunaona kwamba wanashiriki vipi kutulipa zile gharama kama wao wataendelea na ugomvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo mchango kwa upande wa participation kuangalia kuona nini jeshi linashiriki kiuchumi duniani kote na ndiyo maana jeshi watu wanalitumia kiuchumi kama ninyi tumewakomboa na bado mnaendelea kupigana siyo tunakwenda tunakuja hapa kila siku kuja kuwasuluhisha bila kutulipa haiwezekani kama unazalisha mafuta haya tupe meli 200 hapa halafu sisi tunaondoka zetu itakuwa ni moja ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine Mheshimiwa Mpango ambalo nataka nikushauri ni kwamba leo umeanzisha mradi wa kimkakati uwe na miradi ya kimkakati kwa mfano ile ambayo umesema kwamba kutakuwa na reli, reli kuanzia Mtwara kwenda hadi Mbambabay ule ni mradi wa kimkakati kwa sababu pamoja na mazao ya kilimo ambayo yatakuwa yanapita, lakini kule unakokwenda kunakuwa na makaa yale Liganga ambayo na kwenyewe kule kuna madini ambayo ni ya kimkakati ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kuzalisha katika viwanda vingine. Maana yake hapo moja kwa moja hiyo miradi kama hiyo wewe unakuwa umeishirikisha kiuchumi kuliko kupeleka ile miradi ambayo inakuwa ikienda inakuwa moja kwa moja inakuwa ni mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Mpango ambalo mimi nataka kushauri nimeona jambo zuri sana wamefanya hawa watu wa Wizara na ambalo na wewe mwenyewe umeshiriki. Kuna center for excellence kwa mfano watu wa excellence kwa mfano hawa watu madini wamehakikisha kila kanda wanajenga mahala ambapo watu wenye fikra kuhusu utaalam wa madini unakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na sisi tufanye tunafanyaje sasa. Tunahakikisha kwamba yale mazao yote ya kilimo ya kimkakati yale tunaweka center for excellence kwa mfano hapa Dodoma tukiona kwamba watu wanalima zabibu, tunaangalia ile kwamba center wale Makutupora na wao wanalima zabibu ili tuweze kuuza katika viwanda vyetu, kama Singida wanalima alizeti tunahakikisha kwamba pale tunaweka national service.

Kwa hiyo, maana yake vijana wetu tutakuwa tumewaajiri maana patakuwa nacenter for excellence, lakini wale watapata kuuza kwenye viwanda vyetu vya alizeti ambavyo vitakavyokuwepo Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda Pwani kuangalia je, Ukanda wetu wa Pwani una viwanda vya samaki, tunaweka vile tunaweka camps ambao tutahakikisha kwamba kutakuwa na uvuvi, lakini vilevile tutakuwa tunaweka viwanda ambavyo vya kuhakikisha kwamba vijana wetu wanakuwa wana participation. Kwa hiyo, maana yake Mikoa yote vijana wote watakuwa wanashirikishwa moja kwa moja kiuchumi na maana yake watakuwa wanafanya kazi kwa umoja wetu na utapata upinzani na utalisha na watu ambao watakuwa hawana kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hautashirika hivo maana yake unazalisha bomu ambalo baadae litakuwa ni mzigo kwetu sisi kitaifa maana yake wale vijana wote tutakuwa na center ambazo kila mahala kama ni Mbeya, kama ni Kigoma kama kuna mawese sehemu fulani tutaweka hayo tutangalia tusifanye mipango ya kukurupuka, tukisikia korosho leo imefikia shilingi 2000 basi tuna sambaza miche nchi nzima, haya leo imeshuka tunafanyaje yaani hiyo maana yake ni mipango ambayo hatushirikishi na tunashindwa kutumia nguvu zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maana yake kwamba panapotokea jambo hata kama madini leo ni shilingi 5000 tusifikirie kuangalia madini yale peke yake, tuangalie nini ambacho kinafuata ili tukifanye ili tuhakikishe kwamba uchumi wetu unakuwa uchumi imara. Lakini tuweke uchumi ambao ni mfumo, tuweke mfumo ambao utakuwa ni endelevu, leo umetengeneza huu mpango je, huu mpango ni endelevu? Kama leo baada ya mwaka mmoja akija mtu mwingine anaweza akaubadilisha? Kamwe tusimpe loophole mtu mwingine kutokana na mpango wako ambao umeutengeneza leo akapata nafasi kuja kuuharibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie kama tumetengeneza mpango au watu wa Serikalini kwa mfano watumishi mimi nakumbuka wakati ule wakati tulipokuwa tunaajiriwa tulikuwa tunalipwa posho, kuna substance allowance mtu akishaajiriwa analipwa malundo ya posho kiasi kwamba yeye hawezi kuingia tena kwenye corruption.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maana yake hawa watumishi wa Serikali lazima uangalie masilahi yao ili wao wanapoenda kufanya kazi miguu yaani watakuwa wanaishia huko. Lakini kama utakuwa unaangalia mpango tu wa kupata fedha Serikalini bila kuangalia hawa watumishi, Mpango utakuwa unajidanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jingine ambalo Mheshimiwa Mpango ambalo unatakiwa uliangalie ni kundi la wanasiasa, kundi ambalo ni kubwa sana Waheshimiwa. Mtu atakudanganya kwamba bwana okaywewe mpango wako angalia tu mambo ya kiuchumi. Lakini wanasiasa wapo na wao wana nafasi yao katika kufanya participation katika kufanya maamuzi sasa kama wao wanafanya maamuzi wamekaa humu ndani na wewe Mheshimiwa Mpango umesikia wanalalamika hapa watu kwamba wewe unatumia la STL, lakini hapa kuna Mbunge leo anaenda pale mpaka mnafika pale Kibaigwa unamkuta Mbunge gari yake ile aliyokopa ya milioni 60 hiyo mbovu imekufa, ameificha pembeni. Hivi wewe mtu kweli atakuunga mkono, kwa hiyo maana yake lazima uangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu watakuwa wanakudanganya, watakudanganya kwamba sisi hatutaki maslahi yetu. Lakini nawasifu kwamba mmetengeneza vitu ambavyo vya kimsingi unatengeneza kabisa kuna ndege, kuna viwanda, kuna participation lakini kubwa je, maslahi ya hayo maamuzi ya hao wanasiasa inakuaje. Nakushukuru sana...

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mpango kwamba Mheshimiwa Karume wakati anaondoka pale alipojenga zile nyumba za Michenzani wale Mawaziri wake wake wote aliwajengea nyumba moja moja hawakuchukua rushwa, sasa leo wewe Wabunge badala ya kuwaona kwamba hawa Wabunge na wao wana nafasi unawaacha hivi hivi halafu unawaambia wasichukue rushwa kwa kuwa tu rushwa tu haipo, naomba uangalie wanasiasa uangalie watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, kuchangia katika hoja ya viwanda na biashara. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo kwamba nimepata nafasi ya kuweza kumshukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuchangia kwangu ni mara ya kwanza, naomba kuchukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Newala, kama wanayofanya wenzangu, kumsifu Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kura nyingi na kazi anazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Rais wa Zanzibar, ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kuwasifu Waheshimiwa Mawaziri ambao wameteuliwa ambao kwa kweli uchapaji wao wa kazi unaendana na hali halisi tuliyonayo Tanzania sasa hivi. Maana Tanzania ya leo tulikuwa tunahitaji viongozi wa design hii, maana tulishafikia mahali pabaya sana ambapo wananchi walikuwa wamekosa imani na Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika mchango wangu kwa Wilaya ya Newala. Wilaya ya Newala inalima korosho takribani tani 80,000 hadi 70,000 wakati korosho ambazo tunasafirisha nje zinakuwa ni tani 150,000. Kwa hiyo, karibu nusu ya korosho ambazo zinasafirishwa zinatoka Newala na Tandahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Newala tuna viwanda viwili vya kuchakata korosho. Kuna kiwanda kimoja au viwili vyote tulikuwa tumepata kwa mkopo wa Benki ya Dunia ambao naamini mpaka leo tunalipa zile fedha nyingi sana. Vile viwanda vilifanya kazi takriban kwa miaka miwili tu. Hivyo viwanda vikawa vimesimama, haviendelei tena kufanya kazi. Kwa hiyo, nashindwa kuelewa, kama viwanda viwili vipo na tunazalisha korosho zaidi ya tani 70,000, kinachofanyika ni nini? Kwa sababu kinachofanyika hapo unaona kwamba watu ambao wanazalisha korosho wapo, maana yake product zipo na vile viwanda vipo, tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonyesha ni kwamba hapa tatizo labda ni management. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje atueleze hapa, kwamba uchakataji wa korosho katika Wilaya ya Newala utaanza lini? Sambamba na Wilaya ya Newala, kuna viwanda vingine kwa mfano vya Mtama, Likombe pale Lindi, Mtama viwanda vyote hivyo vimesimama na hawa watu wanazalisha korosho, ni kitu gani kinachofanya kwamba tusiendelee kuchakata hizi korosho?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaingia katika mchakato mwingine wa kujenga viwanda vingine vya pili. Kwa nini tunaendelea kujenga viwanda vingine wakati vile ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa amevijenga tunashindwa kuvisimamia na kuchakata korosho? Ni kitu gani kinachofanyika? Kama kweli tumeshindwa, basi tunge-hire management.
Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonyesha ni kwamba sisi tunashindwa kuzalisha, basi tukodi management ili hivi viwanda vianze kufanya kazi. Ukiangalia kiundani, utaona kabisa kwamba hivi viwanda vyote vinatumika kama maghala leo. Wengine wameondoa mashine zile, wameuza au wamekata chuma chakavu. Sasa Mheshimiwa hapo nashindwa, tutaendaje kwenye hivyo viwanda vingine vya kisasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kama haitoshi, kuna wananchi wangu pale wa Newala baada ya kuona kwamba hizi korosho sasa hazichakatwi tena, wale akinamama wameanzisha vikundi vidogo vidogo ambavyo kwa kweli sasa wanachakata kwa kutumia mikono yao; lakini zile korosho ndiyo korosho ambazo ni nzuri in the world, lakini sasa zinapatikana kwa kiasi kidogo. Watu wa nje wanakuja wanataka zile korosho, lakini zinakuwa ni kiasi kidogo kwa sababu ile process wanayoitumia kuchakata inakuwa ni finyu kwa kuwa wanatumia mikono.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze kwamba ana mkakati gani? Kama vile viwanda ameshindwa kuviendesha, je, anawezeshaje akinamama ili waweze kuchakata korosho kwa wingi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, pale Nachingwea kuna kiwanda kikubwa sana cha kuchakata ufuta, alizeti pamoja na karanga. Sasa sisi tunalima ufuta kule, ule ufuta unalimwa kwa kiasi kikubwa sana; ni kitu gani ambacho kinazuia tusichakate ufuta tukapata mafuta ambayo ni the best in the world? Maana inasemekana kwamba mafuta ya ufuta hata wale ambao wanasumbuliwa na pressure iwe ya kushuka au kupanda, ukiyatumia kwa muda mrefu inasaidia kuweka afya yako kuwa nzuri. Kwa nini tusiendelee au tusifufue kiwanda hiki tukawa na process tena ya kuchakata huu ufuta au alizeti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Farm Seventeen pale, kwa wale ambao labda hawajafika Nachingwea, kuna Farm Seventeen, Farm Twenty One, yale yalikuwa ni mashamba ya Wajerumani ambao walikuwa wanalima karanga. Sasa Mheshimiwa Waziri aje atuambie, kama kile kiwanda kipo na yale mashamba yapo, ana mpango gani wa kutafuta watu? Maana wale Wajerumani walilima karanga pale, japokuwa wao walikosa time, lakini leo Jeshi la Wananchi wanatumia eneo lile kwa ajili ya mazoezi. Yale yalikuwa ni mashamba kwa ajili ya karanga!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwamba je, nchi yetu ina mpango gani wa kutumia yale mashamba kulima karanga ili tuweze kupata mafuta? Pia kile kiwanda kilichopo pale Nachingwea kuna mpango gani wa kufufuliwa badala ya kula mafuta mabovu mabovu ambayo tunaletewa kutoka nje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa Diwani pale Kinondoni. Kwa hiyo, mchango huu ni wa Kitaifa. Kwa mfano, pale Ilala kuna Kiwanda cha Bulb. Kile Kiwanda cha Bulb kimefungwa! Leo tuna-import bulb kutoka nje, hivi hii siyo aibu kweli? Bulb za kuweka juu; kile kiwanda leo wanatumia watu wa TATA kwa ajili ya ghala la kuuzia magari. Ile mitambo yote imeng‟olewa. Hivi ni nani ambaye alichukuwa kile kiwanda na kwa nini ile mitambo iliondolewa? Kwa nini sasa badala ya kutengeneza bulb, watu wanatumia kama maghala ya kuuzia magari?
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na East Afrika Cables. Leo wana-import badala ya kutengeneza zile nyaya ambazo zilikuwa the best katika dunia hii kutegemeana na hali halisi ya Tanzania, kwa sababu wale ma-engineer walikuwa wanajua hali halisi ya Tanzania ikoje. Leo wana-import nyaya kutoka nje, kwa nini wameshindwa kutengeneza zile nyaya ndani, leo wana-import kutoka nje? Hivi ni vitu ambavyo nadhani Mheshimiwa Waziri ayaangalie kabla hajaingia katika viwanda vingine ambavyo anasema anaweza kuhamasisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, utakuta viwanda zaidi ya 300 au 400 havifanyi kazi. Kwa nini hivi viwanda vimegeuzwa kama maghala? Kwa nini wasitafutwe wawekezaji ambao utawaambia kwamba mimi leo nina viwanda vya design fulani halafu wale wakaja ukawapa yale maghala wakaweka tu mitambo badala ya kuwatafutia ardhi ambayo haina chochote? Huoni kama huo utakuwa ni utendaji mzuri zaidi kuliko leo unaanza kutafuta ardhi lakini wale watu leo wana maghala na hayo maghala wanayatumia kwa kuhifadhia mali badala ya kuzalisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika TIC, yaani huu uwekezaji; uwekezaji should be epically ina maana kwamba huu uwekezaji maana yake lazima umnufaishe Mtanzania. Wawekezaji wengi wanapokuja hapa Tanzania, hawawanufaishi Watanzania, wao, wanaangalia rasilimali zao. Hamna nchi yoyote duniani ambapo unaweza uka-import vitu kutoka outside halafu hapa ndani ukaviuza vile vitu kwa dola. Kwa nini hawa wawekezaji zile rasilimali zao wanazozileta hapa ndani wanauziuza kwa dola? Hicho ndicho chanzo kikuu cha kushusha thamani shilingi yetu, kwa sababu sisi wenyewe tumeshaidharau fedha yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nenda India, China, nenda mpaka zile hospitali za Wilaya, haiwezekani wewe kule ukafika na dola wakakubali. Watakwambia kabadilishe upate fedha za nchi ile. Hata China, ni lazima ubadilishe zile fedha za Tanzania iwe ni dola, uibadilishe upate fedha ya nchi ile then uende ukanunue. Leo hapa tunaletewa magari ya TATA unauziwa in US Dollars. Maana yake exchange rate ya hayo magari yanabadilika kila siku kutegemeana na shilingi yetu inavyoshuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama kweli tungekuwa tunauza kwa shilingi, basi zile gari ambazo zimeingia mwaka 2015, mwaka huu zisingeweza kupanda bei. Leo gari ambayo imeingia mwaka 2015 kwa dola fulani, labda exchange rate ilikuwa shilingi 1,200/=, mwaka huu kila siku unauziwa kwa rate ya leo; uone hapo fedha yetu inakosa thamani. Kwa hiyo, tuangalie kwamba Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji washirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, waone ni namna gani tutakuwa na sheria za kuweza kudhibiti fedha yetu ikawa na thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Mchango wangu umegawanyika katika maeneo mawili. Kama hoja za Kamati zilivyozungumza, maana yake Mawaziri wanashauriwa kwamba miundombinu ifanye kazi kufuata utaratibu ule ambao kwa kweli unashauriwa na Kamati, nashauri miundombinu ishirikiane na Wizara nyingine. Kwa sababu leo TCRA haitaki kushirikiana na Halmashauri ambazo zipo huko Wilayani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu kwamba sasa hivi tunaenda kwenye bajeti, Halmashauri nyingi zinakuwa hazina mapato, lakini minara ya simu ipo katika Halmashauri zote, lakini Service Levy inakuwa hailipwi katika Halmashauri husika. Kwa hiyo, naomba Wizara ishinikize TCRA itoe takwimu ambazo ni sahihi ili Halmashauri ipate kutoza Service Levy. Kwa sababu leo minara ya simu inalipa Service Levy bila kuwa na habari, lakini TCRA ina uwezo wa kujua kwamba ni simu kiasi gani zinakuwa zinaingia kwa kila mnara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze, je, kulipa Service Levy ni sheria au mtu analipa kwa hiari yake? Kwa sababu kuna baadhi ya makampuni hayalipi kabisa na mengine yanalipa kwa kiwango kidogo sana. Kwa hiyo, Wizara ya Miundombinu iishinikize TCRA isaidie Halmashauri ili Halmashauri iweze kutoza ule ushuru kutegemeana na simu ambazo tunazitumia kutoka hayo maeneo ambayo yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama vile ambavyo nimezungumza kwamba Wizara ishirikiane na Wizara nyingine, vilevile tumezungumzia hapa kuhusu Wizara ya miundombinu. Ukiangalia sana kwa mfano kule Mtwara, leo ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa sana wanalima korosho. Kwa asilimia karibu 70 ya export ya korosho inalimwa Mtwara, lakini ukienda kuangalia kule, zile barabara zote za Kitangali, Mtopwa, Luagala na Nanyamba, zimebaki mashimo. Mapato yetu ya Export Levy, kwa mfano mwaka huu tumepata shilingi bilioni 140 na hizo fedha huwa zinapatikana kila mwaka. Hizo fedha asilimia 65 zinakwenda kule kwa ajili ya kuboresha zao la korosho, lakini zile barabara haziboreshwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuangalie uwezekano wa miundombinu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuona ni namna gani zile fedha ambazo zinapatikana zinakwenda kuboresha zile barabara ambazo zinahusiana na mambo ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani leo zile fedha zote ambazo ni asilimia 65 zinaondoka halafu asilimia 35 zinakwenda katika Mfuko Mkuu. Nasema kwamba kama kila mwaka tungeamua sisi Mtwara tutumie tu Export Levy, basi barabara zote za Mtwara zingekuwa na lami. Sasa sisi hatutaki lami, tunataka angalau kifusi kiwepo katika zile barabara ambazo zinatumika na ambapo magari makubwa yanakuwa yanapita kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba katika bajeti yake inayokuja, basi ashirikiane na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Kilimo vilevile iangalie uwezekano, ni namna gani watajitoa kusaidia zile barabara zao? Wasiangalie tu kupata zile fedha asilimia 35 ambazo zinakwenda kwenye Mfuko Mkuu na asilimia 65 ambazo zinaenda kwenye Bodi. Waangalie namna gani wananchi wananufaika kwa barabara zao kuwa bora? Isiwe kama maeneo ambayo wanachimba madini, watu wanachukua yale madini wanaondoka halafu wanaacha mashimo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada za kushirikisha maeneo yote hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu nizungumzie kuhusu REA. Mtwara ni eneo ambapo gesi inatoka kwa wingi sana, lakini mpaka leo kuna tatizo kubwa sana la umeme. Okay, sisi hatuna shida kuhusu umeme, lakini hawa wananchi wana shida ya maji. Leo maji ule umeme unaopatikana Mtwara, hauwezi kusukuma maji kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ule umeme uliopo Mtwara hautoshi, achukue hatua za dharura ili ahakikishe kwamba ananunua mashine za dharura ili tuweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo hii huwezi kupata malalamiko ya maji kwa kuwa mvua zinanyesha. Itakapofikia mwezi wa tatu it is a crisis, itakuwa ni war. Asitake Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara, Nachingwea au Lindi tuje tuombe hapa chini ya dharura, kwa sababu itakuwa ni tatizo kubwa sana kupita kiasi. Kama gesi ipo Mtwara, inawezekana vipi umeme ukosekane? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada zote za kuleta mashine mpya za gesi aende akafunge katika station ya Mtwara. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu wa leo. Ahsanteni sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara hii nyeti ya Comrade Lukuvi kwani Wizara hii ni nyeti na ndiyo Wizara ambayo kwa kweli tunaitegemea kiuchumi. Bila ardhi tunaweza tusiwe na viwanda vya kiuchumi, tunaweza tusiwe na kilimo, viwanda wala mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni muhimu na ndiyo maana inahitaji iwekwe kwa mtu ambaye ni makini tena mtu ambaye kwa kweli awe ni sahihi kweli kweli. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi amepewa yeye kwa kuwa ameonekana kwamba ni mtu makini. Ili aendelee kuwa makini, anatakiwa akemee baadhi ya Wizara. Wizara ambazo anapaswa kuzikemea ni pamoja na Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maliasili na Utalii wakitaka kujikatia eneo, wao wanaamua tu kwenda kujikatia, wanaangalia thamani ya tembo wao, lakini hawaangalii thamani ya binadamu. Naomba wafuate utaratibu kwamba pale anapostahili kuwepo mnyama aendelee kuwepo mnyama na pale ambapo panastahili kuwepo makazi yaendelee kuwepo makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wa Madini wakihitaji eneo lao, wao hawajali kama kuna watu ambao wapo ndani ama kuna mashamba ya watu. Wao wanachoangalia ni thamani ya yale madini yao. Kwa hiyo, tunahitaji watu wa madini wapewe eneo lao na wale watu wanahitaji wabaki katika eneo lao madini, waendelee kubaki katika madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza mwenzangu ambaye amepita, hii Wizara ya Ulinzi tunahitaji sana ulinzi, lakini tunapohitaji kupanua mipaka, basi wawepo ndani ya mipaka yao ili na wananchi waendelee kutumia maeneo mengine. Kwa hiyo, ni vizuri Wizara ya Ulinzi ikatengewa maeneo yao nje ya maeneo ya binadamu mahali ambapo wananchi hawawezi kuwa na mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo ambayo yamekuwa katikati sasa hivi, kwa mfano Jeshi ambalo lilo katikati, hatuhitaji tena kuwa na Jeshi katikati ya mji. Nadhani tuangalie uwezekano wa kuchukua Jeshi tuweke nje ya mMji, maana tuna maeneo mengi ili waweze kufanya mazoezi kwa nafasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba ni kuhusu Wilaya ya Newala. Wilaya ya Newala ilitangazwa mwaka 1959 kwa GN ambayo ilitoka mwaka 2000. Tulitegemea kwamba kama Wilaya ilianzishwa mwaka 1959 na GN ikatoka mwaka 2000 kuna mpaka ambao unaanzia pale Chiwata, Ndanda, Mpanyani hadi kule Mwena; hiyo mipaka ilianzishwa tangu mwaka 1959 na wale wananchi ambao walikuwa wanabeba GPS za Wazungu wapo. Kwa hiyo, tunategemea ile GN ambayo ipo, kilomita moja kutoka Ndanda ndipo ambapo Wilaya ya Newala inapoishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mshangao kuna GN ya mwaka 2010 ambayo ilitangaza Wilaya ya Masasi. Hii GN ya mwaka 2010 inatofautiana na GN ya mwaka 2000 ambazo zote zinatoka katika Ofisi moja. Inakuwaje hizo GN ambazo zinatoka katika ofisi moja zinatofautiana? Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Comrade Lukuvi, aangalie GN ya mwaka 2000 inakuwa vipi tofauti na ile GN ya mwaka 2010?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mimi naelewa kuwa kulitokea mgogoro mwaka 1994 juu ya mpaka, kwa hiyo, watu wakatumia advantage ya miaka sita ile baadaye kurekebisha ile GN na ndiyo maana hata tafsiri ya mpaka leo wa Masasi na Newala unatofautiana. Wananchi wanajua mipaka yao inaishia wapi na kila mmoja anafahamu, lakini watalaam wanatofautisha. Wale wataalam ambao siyo waadilifu wanafanya mambo ambayo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi hapa kumetokea mgogoro kati ya watalaam wa Kanda ya Mtwara na wananchi pale Mpanyani. Haiwezakani mtu ambaye amekaa kuanzia mwaka 1918 yupo pale Mpanyani uende na approach umwambie bwana wewe upo Masasi, akwambie tu leo Mheshimiwa Lukuvi wewe ni mtu wa Mbeya. Kwa kweli namshukuru sana yule Diwani wa Chilangala, alitumia busara. Vinginevyo wale watu leo tungekuwa tunaongea hadithi nyingine. Yale mambo yaliyotokea Dodoma, yangetokea Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa kutumia busara zake aende akawaite wale wazee ambao walikuwa wamesimama na wanajua ile mipaka, awaite wananchi wa Masasi na Newala ambao wanajua mipaka yao na tumekuwa tukiishi kwa amani, sisi hatuna tofauti, isipokuwa kuna madini yatatusambaratisha, nchi hii itagawanyika katika vipande. Kuna wanasiasa wengine wanataka mashamba pale, wanahonga baadhi ya watalaam ambao siyo waadilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwamba tunapomaliza Bunge hili, yeye mwenyewe Comrade aje aangalie hali iliyoko pale. Haiwezekani leo mtu ambaye hakuwa anategemea kwenda Masasi au Newala asubuhi aambiwe kwamba leo wewe upo katika Wilaya ya Newala wakati ile mipaka wao wenyewe wanaifahamu au shamba lako unaambiwa lipo Masasi au halipo Masasi lipo Newala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, kwani naamini kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja baada ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii mpya ambayo Waheshimiwa Wabunge wake au Mawaziri wake ni vijana na wapo watatu. Hawa Mawaziri wapo watatu, kwa nini waliteuliwa kuwa watatu na hii Wizara ni nyeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama Mheshimiwa Rais amewapenda sana kwa kuwapendelea ili kuwapungunguzia kazi. Mheshimiwa Rais ameonesha wasiwasi wake kuhusu Wizara hii ambayo ni nyeti. Kwa sababu matarajio ya Mheshimiwa Rais ni mapato makubwa sana katika Wizara hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja tuliwahi kusikia kwamba mambo ya madini yanatokana na mashetani, sasa haya mashetani ndiyo yanafanya nchi hii isipate madini. Kama kweli sisi hatupati madini, basi namwomba Mheshimiwa Angellah aende South Africa akamlete Sangoma aje atuchinjie ili tuwezeshwe kupata madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli madini yataendelea kuwa na unyeti na usiri mkubwa sana. Huyo aliyesababisha usiri mkubwa sana sio mtu mwingine isipokuwa ni STAMICO. STAMICO ni kubwa kuliko Wizara yako Mheshimiwa Waziri. Mawaziri lazima mfanye maamuzi magumu. Bila kuivunja STAMICO hamwezi kuleta mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ni mzigo mkubwa sana kwa sababu ni Shirika la Serikali. STAMICO leo imeingia mkataba na Tanzanite One, lakini ule mkataba wenyewe una utata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasheria wa STAMIGOLD na STAMICO wameshindwa kuelewana. Wanaiomba Serikali ninyi mkae mwapatanishe, wakati tunategemea wataalam wetu wa madini wapo STAMICO. Hivi ninyi Serikali mtawapata wapi wataalam? Hebu angalia utata huo. Kwa hiyo, maana yake STAMICO ni mzigo kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, STAMICO wamekuwa ni tatizo. Leo STAMICO walikuwa wanamiliki mradi wa makaa ya mawe. Katika mradi wa makaa ya mawe wamechimba yale makaa wamepata tani 8,000. Mradi wa Kiwira Kabulo. Wameuza wamepata shilingi milioni 500. Hebu angalia huo uwekezaji. Ukubwa wa STAMICO wanapata shilingi milioni 550 na kilo 2,200 wameweka stoo wanasema wanasubiri kuuza. Inavyosemekana ni kwamba yale makaa ya mawe siyo chochote ila ni uchafu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba hii ni kampuni ambayo ipo kwa ajili ya kuleta hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mawaziri, ningekuwa ninyi leo leo jioni hii STAMICO ninge-declare kuivunja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ina madeni makubwa kuliko uzalishaji wake ambao wale watu wa Kiwira wanadai pale. Madeni yaliyoko pale ni makubwa sana, lakini wao wanaonesha kwamba production ni milioni 550. Kuna sababu gani ya kuendelea kuwa na Kiwira tena?
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, hawa watu tena wameingia na STAMIGOLD. Kule wameumiliki ule mgodi, wamezalisha madeni ya shilingi bilioni 60. Kwa kweli haiwezekani hawa watu kuendelea kuwa ndani ya Wizara hii ambayo ni mpya, tena ina Mawaziri vijana. Wakiendelea kuwa nao, wataondoka nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, STAMICO ina majukumu makubwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia vijana. Hivi kweli itaweza kuwasaidia vijana kama wao wenyewe hawajiwezi? Wameandika hapa kwamba ni kutoa ushauri na kutoa huduma kwa vijana. Naomba vijana nchi mzima, kama wanaenda kushauriwa na STAMICO watafilisika kama STAMICO ilivyofilisika. Wao wasiifuate STAMICO, kuna utafiti hapa umefanywa na Kampuni kutoka STAMICO, wameenda kule, watu wamechimba mita 100 kwenda chini madini hawakuyapata. Maana yake ni utata uliopo ndani ya STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiria mwanzoni kwamba kama wameshindwa kwenye madini, basi hawa watu waende kwenye kokoto kule Ubena Zomozi. Hata zile kokoto pale Ubena Zomozi zimewashinda. Kama wameshindwa kuchimba kokoto, mnategemea hii STAMICO kweli itatusaidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wameomba, wamesema kwamba sasa hivi tunatafuta mwekezaji. Hivi kwenye kokoto unatafuta mwekezaji? Kokoto, yaani mtu ukiwa na shilingi milioni hamsini tu, inatosha kwenda kuchimba zile kokoto. Naomba Mawaziri, kwa kweli hatuna sababu ya kutafuta. Wamesema wanaenda kutafuta fedha, hizo hela wanaenda kutafuta wapi badala ya kuleta hapa Bungeni ili tuwape fedha wakachimbe zile kokoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotoa fedha ni sisi Waheshimiwa Wabunge, wao wanasema wanafanya mpango wa kutafuta fedha, hizo fedha wanaenda kuomba wapi? Nadhani wangeleta hapa bajeti yao, wakasema maadamu tumeshindwa madini sasa tunataka fedha, shilingi milioni 200 ili tukachimbe zile kokoto. Nadhani ndiyo kazi rahisi ambayo wanayoiweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hizi zimekuwa ni mzigo kwetu sisi; na madini, karibu asilima 90 ya Watanzania hawayajui. Ajabu asilimia hata asilimia 75 ya hawa Wabunge hatuyajui. Hata mimi ukija kunishauri leo, ukaniambia niingine kwenye biashara ya madini sitayajua. Kwa hiyo, naomba Wizara hii mpya ifanye semina kwa Watanzania, wapate kuyajua haya madini ni nini? Madini, watu wengi hatuyajui na yataendelea kuwa na utata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nimeona ni huo, kwa kuwa Wizara hii ni mpya, lakini napongeza sana jitihada ambazo anachukua Mheshimiwa Rais na kuujenga ule ukuta. Anaonesha wasiwasi na bado ameteua Mawaziri wengi kwenye Wizara moja ambayo ni ndogo, lakini ni mpya, tena vijana; anaonesha kwamba bado ana wasiwasi lakini bado anaamini kwamba Wizara hii ikisimamiwa kwa dhati itatoa production zenye tija. Nawaomba hawa vijana wasimamie. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa kuwa hii STAMICO itaendelea kuwa msiri na itakuwa mzigo kwetu sisi. Leo waivunje. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi naona dhamira ya Serikali ya REA III kwa kweli ni nzuri, isipokuwa kuna challenge ndogondogo ambazo sisi kama Wanakamati baada ya kutembelea tumekutana nazo. Kwa mfano ukosefu wa nguzo, nyaya, mashine umba; haya ndiyo matatizo ambayo yamejitokeza kwa wingi sana wakati tulipotembelea miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hii haitoshi kuna kurukwa kwa vijiji kama ambavyo Wajumbe wengi wamezungumza. Kwamba vijiji vingi vimerukwa kutokana na kukosekana kwa scope of work. Kwa hiyo, niiombe tu kwamba Wizara ifanye jitahada ya kuhakikisha kwamba sasa hili tatizo la kurukwa vijiji kutokana na kukosekana kwa scope of work lisirudiwe tena, maana yake liende hatua kwa hatua, kama Mheshimiwa Waziri anavyokuwa akizungumza siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu hawa Mawaziri wetu; Mawaziri wote kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi. Mawaziri wa Nishati wamekuwa wakijitahidi sana kufanya kazi kwa kiasi kikubwa sana, Mawaziri wa Madini wamekuwa wakifanya kwa kiasi kikubwa sana; kwa kweli production inaonekana sasa hivi. Kwa mfano, leo unaweza ukachukulia hoja ya TANESCO. TANESCO leo wana uwezo, wao wenyewe wanajikimu wao, wenyewe wana uwezo wa kulipia bili zao za umeme. Hii ni jitihada kubwa kwa sababu TANESCO haikuwa kufikia hivyo. Ina maana kwamba kuna watu ambao wanafanya kazi ndiyo maana mpaka leo TANESCO inafanya kazi kiasi hicho na ina maana hawa vijana wanajitahidi kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye makusanyo, maduhuli yamekuwa yakionekana kwa kiasi kikubwa sana kwa upande wa madini, ina maana kwamba watu wa Madini, wamekuwa wakifanya kazi kwa kiasi kikubwa na ndio maana maduhuli, yamekuwa yakionekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tulikuwa tunazungumzia, ni kuhusu Jeshi letu. Hili Jeshi letu lilikuwa la wapigania uhuru wakati ule wa enzi za Mwalimu Nyerere. Siku moja niliwahi kuongelea kwamba tuangalie namna gani sasa hivi hili jeshi letu linaweza likageuka likawa jeshi la kiuchumi, lisiwe jeshi tu ambalo sasa hivi linakwenda kwenye korosho huko Mtwara, badala yake tulitumie Jeshi hilo Kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamchukulie Mheshimiwa Keissy alivyozungumza, kwamba tulitumie lile jeshi kiuchumi, ina maana kwamba watu wote ambao tumewaondoa kwenye mikono ya mabeberu sasa hivi ni wakati wao wa kurejesha zile fadhila ambazo tulikuwa tumewaondoa katika mikono hiyo maana hakuna hata mtu mmoja anayekuja kutushukuru. Sasa kama tuna nguvu kazi ya kutosha, tuna vijana wa kutosha, kwa nini na sisi tusiwe kama wanavyofanya mabeberu wengine wa Ulaya? Kwa hiyo tuangalie, namna gani hawa vijana wetu ambao wana nguvu za kutosha tunaweza tukawabadilisha likawa ni jeshi la kiuchumi ili sisi tuishi maisha mazuri kama wanavyoweza kuishi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nimeliona ni kuwapongeza, pamoja na ukwasi ni kwamba hii, Stiegler’s Gorge hii, kwa kweli umeme tunauhitaji. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwapa vijana kazi hii na hawa vijana waendelee kuchapa kazi, haiwezekani moja kwa moja wewe ukawa unafanya kazi usisikie kelele, haiwezekani; maana mti unapopolewa ndio ambao una matunda huo. Kwa hiyo wakiona kwamba wanapigwa mawe basi wajue kwamba chochote wanachokifanya, waweke jitihada ili kuhakikisha kwamba hili bwawa la Stiegler’s Gorge linafanya kazi na linazalisha vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu ule mradi ambao tulikuwa tumekubaliana katika Kamati, kwamba zile megawatt 400, Serikali ifanye jitihada na yule Mkandarasi aanze kazi ili kuhakikisha kwamba zile megawatt 400 pale Mtwara zinajengwa kwa haraka sana; ili kuhakikisha kwamba umeme unapatikana kwa wakati kama vile ambavyo tumekubaliana na kama vile ambavyo wananchi wengi wana uhitaji umeme.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagongwa Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara hizi ambazo ni nyeti ambayo ni TAMISEMI pamoja na utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa mchango wangu, katika Wizara hizi nyeti, nami niungane na Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais jinsi anavyoweza kugawa maendeleo ya nchi hii bila kujali Wapinzani au ni Chama Tawala. Kwa kweli, namsifu sana Mheshimiwa Rais na ni kweli, tunaona juhudi zake jinsi anavyofanya kazi kwelikweli. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza hawa watendaji Mawaziri ambao wapo katika Wizara zote hizi kwa maana ya TAMISEMI, lakini pamoja na Utawala Bora. Kwa kweli, wanafanya kazi pamoja na wasaidizi wao; nawapongeza ndugu yangu Mheshimiwa Jafo na kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika. Kwa hiyo, moto mdundo waendelee kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nichukue nafasi hii naomba kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya TAMISEMI. Namwomba Mheshimiwa Jafo, kwa kuwa tulikuwa wote kwenye ziara, nami nitoe mchango kwenye upande wa barabara. Kwa kweli, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina barabara ambazo ni nyingi sana, lakini ndiyo ambayo inalima karibu nusu ya korosho za Newala. Ila kutokana na mtandao, magari makubwa ambayo yanapita katika barabara zile, nimwambie Mheshimiwa Waziri Jafo, kwa kweli, zile barabara ni mbovu nasi Wilaya ya Newala, TARURA haina gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachukua nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Jafo tupate angalao gari moja kama walivyopata Halmashauri za wilaya nyingine. Maana yule bwana anashindwa kufanya kazi na kwa hiyo, tutashindwa kusomba korosho katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuomba kwamba, nasi tunahitaji gari moja kwa ajili ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, zile fedha ambazo zinagawanywa za TARURA sisi tumepata shilingi bilioni 900. Kwa kweli hizi fedha ni ndogo sana, sijui ni kigezo gani ambacho kinatumika, lakini zile barabara zote zilizopo pale wilayani ni mbovu na magari ambayo yanatumika kusomba zile korosho ni mabovu. Kwa hiyo, vinginvyo zile barabara zikiwa mbovu tutashindwa kwenda mbele kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Jafo tuangalie kwamba kama zile barabara zitashindwa au kuongeza zile fedha, basi aangalie uwezekano yale maeneo korofi ambapo kuna milima, kwamba korosho zikishapakiwa magari yanashindwa kupanda, basi afanye utaratibu wa kuangalia kwamba, basi anaweka japo kilometa moja moja au mbili mbili za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mlima Miyuyu kwenda Ndanda; ule mlima kwa kweli ni mlima mkubwa na tulishamwandikia Mheshimiwa Waziri kuangalia uwezekano wa kuweza kupata angalau kilometa mbili za lami kutoka Miyuyu hadi kufikia Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, barabara ya Mpalu hadi Mnyambe, wale watu wanalima sana korosho, lakini kutoka pale Mpalu kuna mlima ambao ni mkali sana. Magari yakienda pale yanashindwa kusomba korosho, Kwa kweli, hatuwezi kujenga barabara yote, lakini ile kilometa moja ambayo magari makubwa yanakwama tunaomba Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Kandege Ndugu yangu waangalie uwezekano wa kuweka pale japo kilometa moja ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, pale inapoanzia chanzo cha maji Mitema pale Kitangali ambapo inakwenda barabara hadi kufika Mto Ngwele, ule mlima ni mkali sana, tunaomba vilevile japo kilometa ya lami. Ikumbukwe kwamba uchumi wote wa korosho unaotoka Newala kwa kiasi kikubwa unatoka Kitangali. Kwa hiyo, tungeomba kwamba kilometa nne au tano, itaufanya uchumi huu ukue sana na wa kitaifa maana yake tutakuwa tunapata mapato makubwa sana ya kitaifa. Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Waziri Jafo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, nashukuru kwamba tumepata milioni 200 kwa ajili ya Kituo cha Afya Mkwedu. Kuna kituo cha afya kipo Chihangu, kile Kituo cha Afya Chihangu ni cha muda mrefu sana, kipo tangu mwaka 1969 na operesheni ndogo ndogo zinakwenda pale, lakini kwa kweli hatuna jengo la mama na mtoto. Kwa hiyo, niwaombe sana Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Kandege wapeleke wataalam wakaangalie Kituo cha Afya Chihangu kwa sababu wale akinamama wanajifungulia jikoni na kulala wanalala nje, kwa hiyo inakuwa ni ngumu sana wakati wa mvua wale akinamama kuwa na sehemu ya kujistiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zile nyumba za watumishi zote karibu zime-collapse tangu mwaka 1969 ambapo kituo cha afya kile kilikuwa kimejengwa mpaka leo kile kituo ni kibovu sana. Kama hiyo haitoshi, kile kituo cha afya kipo wazi kabisa, hakina fensi, maana yake hata kama wale watu ambao wanafanya utunzaji wa vile vifaa/rasilimali kwa mfano ile OPD ambayo ilikuwa imejengwa na Wajapan leo ulinzi wake unakuwa ni mgumu. Kwa hiyo, niwaombe sanawaende wakakague ili tuweze kufanya matengenezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; niungane na Waheshimiwa Madiwani wenzangu; kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Newala Vijijini ile ni kama Halmashauri mpya, haina mapato mengine. Baada ya kuwa hizi korosho zimeingia kwenye mtandao maana yake haina mapato, wale Madiwani wanakopwa mpaka vikao maana yake sasa hivi mpaka sasa wanadai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Jafo tuangalie namna gani, kama ambavyo tumezungumza kwenye ziara ya Rais, namna gani hizi Halmashauri za Wilaya ambazo zinategemea kilimo hasa korosho na ushuru tulikuwa hatujapata, tutafanyaje ili kuwanusuru Madiwani hawa ambao wanadai malipo yao. Kwa hiyo, tuangalie namna nzuri ambayo tunaweza tukawasaidia kwa kuwalipa posho hawa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Halmashauri ya Wilaya ya Newala ni pana sana kwa maana kwamba ina Kata karibu 22 ambayo ina mtawanyiko wa wakulima wa korosho. Je, ni namna gani tutawasaidia japo pikipiki kama itakuwa imeshindikana kuwapa mikopo ya magari, basi tuweze kuwanunulia japo pikipiki kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu walivyotoa mchango kwamba tuangalie uwezekano wa hawa Waheshimiwa Madiwani ni namna gani tunaweza tukawawezesha kwa sababu wanatusaidia sana wakati wa kusimamia uchaguzi kwa maana ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hawa Madiwani wanasafiri zaidi ya siku mbili kutoka Vijijini hadi kufika ilipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Waziri waangalie namna nzuri ambazo tunaweza tukawawezesha Waheshimiwa Madiwani hawa na waangalie vilevile ni namna gani wanaweza wakawalipa posho kwa vile vikao ambavyo wameweza kuwakopa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)