Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika (27 total)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa upungufu huo wa Maafisa Ugani ni mkubwa sana kwenye Halmashauri ambazo zimeanzishwa hivi karibuni, kama Halmashauri ya Mji wa Nanyamba; je, Serikali ina mpango gani wa upendeleo kwa mamlaka hizi mpya za Serikali za Mitaa ambazo zimeanzishwa hivi karibuni?
Swali langu la pili, ukiangalia takwimu za ajira zilizotolewa hivi karibuni kwa Maafisa Ugani, na kwa kuwa nchi yetu ina takribani vijiji zaidi ya 12,000 utaona kwamba kuna vijiji vingi sana vinakosa Maafisa Ugani.
Je, Serikali ina mpango gani au mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba kila kijiji katika nchi yetu kinakuwa na Afisa Ugani ili kuleta mapinduzi ya kweli katika kilimo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Utumishi inatambua kwamba Mamlaka mpya za Serikali za Mitaa zilizoanzishwa zinahitaji upendeleo mpya, hasa katika kupanga watumishi. Nataka nimuahidi kwamba siyo Nanyamba tu, Nanyamba ni Mamlaka mpya ya Serikali za Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Mji wa Newala ni mpya, Halmashauri ya Mji wa Tarime ni mpya, Halmashauri ya Mafinga ni mpya, maeneo yale yote ambayo tumeanzisha Halmashauri mpya najua wakati wa kugawana watumishi zile mamlaka mpya hazikupata watumishi wengi. Kwa hiyo, nitakachofanya ni kuhakikisha zile mamlaka mpya zote zinapata watumishi wa kutosha ili zilingane, kama ni upungufu ulingane na zile mamlaka zilizokuwepo kabla.
Swali lake la pili, ni kweli kwamba vijiji vingi havina hawa Maafisa Ugani, hili limetokea kwa sababu muda mrefu katika nchi yetu, vile vyuo vinavyofundisha vyeti vya kilimo vilikuwa vimesimama, lakini baadae vimefufuliwa, sasa hivi kazi kubwa inaendelea. Nataka nimhakikishie kwamba tutaanzisha programu maalum kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha kwamba vyuo vile wanachukua wanafunzi wengi zaidi ili wanapomaliza waweze kuajiriwa na Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na umuhimu wa watumishi katika kada hii ya Maafisa Ugani kama kweli tunataka kuleta mapinduzi ya kilimo kwenye nchi yetu. Jambo ambalo tunaliona sasa hivi ni kwamba kutokana na kutokuajiriwa kwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata wa kutosha, baadhi ya watumishi katika kada hii ya kilimo sasa ndiyo wamekaimishwa zile ofisi za Kata kwa maana ya kuwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata.
Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi katika kada hiyo ya utendaji ili watumishi hawa muhimu wa eneo la kilimo warudi kufanya kazi ya kilimo na wananchi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pale mahali ambapo Maafisa Watendaji wa Kata hawapo, Maafisa Ugani wamekaimishwa nafasi hizo, hii imetokana na upungufu wa kutotosheleza Watendaji wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleze Bunge lako Tukufu, kazi moja wapo ya Afisa Mtendaji wa Kata ni kusukuma maendeleo ndani ya kata, watu waliofanya vizuri sana katika shughuli hii ni Walimu, Maafisa Kilimo, Mabibi Maendeleo, kwa hiyo pale ambapo Afisa Kilimo anakaimishwa Kata siyo makosa, ni nafasi nzuri ya kumuangalia keshokutwa huenda akawekwa moja kwa moja. Jambo la msingi hapa ni kwamba Wizara yangu inakubali kwamba kuna haja ya kulifanyia kazi suala hili kuhakikisha kwamba Kata zetu zote na vijiji vyetu vinakuwa na Maafisa Watendaji wa kudumu. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza.
Kwa kuwa uhaba wa Maafisa Ugani uko sawasawa kabisa na uhaba wa wataalam wa mifugo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Mifugo wa kutosha ili wananchi wasaidiwe haki katika Halmashauri zetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itashughulikia tatizo la uhaba wa Maafisa Ugani sambamba na tatizo la Maafisa wa Mifugo.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kwa kaka yangu, Mheshimiwa Kapteni Mkuchika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watumishi katika sekta ya kilimo ni sawasawa sana au zaidi ya katika sekta ya afya. Sasa hivi maeneo mengi, hasa vijijini, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili kunusuru maisha ya Watanzania, hasa akina mama na watoto? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maeneo muhimu ambayo wananchi wanategemea kupata huduma ni upande wa afya, maji, hayo ni mambo yanayogusa maisha ya kila siku pamoja na elimu na barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote Serikali inapoajiri imekuwa ikiweka umuhimu mkubwa sana upande wa watumishi wa afya, kwa sababu Waziri wa Utumishi anaajiri hawa Maafisa Afya baada ya kuwa tayari wameshafunzwa na kuhitimimu, nataka niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba nitazungumza na Waziri mwenzangu wa Elimu na Wizara ya Afya wapate mafunzo watumishi wengi zaidi katika fani ya afya ili wakazibe mapengo haya yaliyopo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na kwamba wananchi wana haki ya kupata huduma ya watumishi, hasa walimu, wauguzi na watendaji wa vijiji na kata, pia jitihada nzuri ya Serikali inayoifanya ya kupeleka fedha za maendeleo vijijini inahitaji watumishi hawa waweze kusimamia miradi hii. Kwa upande wa Karagwe kuna shortage kubwa ya Walimu wasiopungua 850, kuna shortage kubwa ya wauguzi.
Je, nini tamko la Serikali, maana kila mwaka wa fedha Serikali inasema itapanga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na watumishi wa kutosha. Nini tamko la Serikali kuhusu hii shortage ya watumishi ya sasa hususan Wilaya ya Karagwe? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa walimu na matabibu na wataalam wa idara ya afya na imekuwa ikichukua hatua kuona kwamba tunaziba mapengo haya. Kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, wakati tunaanza sekondari zetu za kata uhaba wa walimu ulikuwa mkubwa sana, lakini Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwepo walimu wa kutosha imefanya jitihada ya kuajiri walimu wengi na hivi sasa katika shule zetu za sekondari, hali ya walimu imekuwa nafuu ukiondoa labda mapungufu makubwa yaliyopo katika upande wa walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi ya kudumu ninamuahidi tu kwamba Serikali itaendelea na kasi ileile ya kuajiri watumishi wa afya na elimu ili wananchi wetu wapate huduma ya afya bora, ili watoto wetu wapate elimu inayojitosheleza. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Waziri kwa kuteuliwa kwake pamoja na Mawaziri wengine wote.
Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilikuwa na nia njema ya kuajiri watumishi 52,000; je, Serikali sasa itatekeleza mpango ule wakati gani ili vijana wetu waliopo mitaani waweze kupata nafasi ya ajira?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baada ya mchujo wa watumishi hewa, Mheshimiwa Rais ametoa idhini, Serikali imeidhinisha waajiriwe watumishi wapya 15,000, hilo zoezi linafanyika. Pia katika mwaka huu wa fedha kuna kibali cha kuajiri watumishi 52,000, zoezi hilo litaendelea, nataka nihakikishe kwamba nafasi na fedha za kuwalipa zipo, kazi hiyo itatekelezwa. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, nina maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa MKURABITA katika Wilaya ya Mpwapwa walichagua vijiji viwili; Kijiji cha Inzomvu na Kijiji cha Pwaga, lakini kwa upande wa Kijiji cha Pwaga mambo ni mazuri, mradi ulitekelezwa, masijala ilijengwa na wananchi walipewa Hati za Kimila. Lakini katika Kijiji cha Inzomvu hakuna kilichofanyika, baada ya kupima mashamba wananchi walipewa mafaili tu wakaenda nayo majumbani, hakuna chochote na ofisi ya masijala haipo.
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya Serikali kuleta muswada hapa ili tubadilishe chombo hiki MKURABITA ambao unategemea zaidi fedha za mfadhili na fedha za Serikali ni kidogo sana ili tubadilishe uwe mfuko wa urasimishaji ili wadau wengi waweze kuchangia na chombo hiki kiwe na fedha za kutosha ili wananchi wengi waweze kunufaika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kusikia kwamba Mpwapwa iliingia katika majaribio, walipata vijiji viwili, kijiji kimoja kinafanya vizuri kingine hakijafanya vizuri. Nimuombe tu ndugu yangu, Mheshimiwa George Malima Lubeleje apange muda anaoona yeye inafaa ili mimi na yeye twende katika kijiji hicho ambacho kimesahauliwa na mimi nikajifunze nikajue kimetokea nini, nichukue hatua ili vijiji hivyo pacha viweze kufanana katika utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kwamba kuletwe muswada utakaobadilisha chombo hiki, Serikali inapokea rai hii, lakini nataka nieleze kwamba kama nilivyosema tangu mwanzo tunakusudia kuanzisha Mfuko Maalum wa Urasimishaji, wakati wa kuanzisha mfuko maalum wa urasimishaji ikionekana haja iko ya kubadili sheria, suala hilo litazingatiwa na taratibu za kubadilisha sheria zinafuata ngazi kwa ngazi, itatekelezwa kadri Serikali itakapoona inafaa.
MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ambayo Serikali imeitoa ya nchi za Hungary na Russia, nchi hizi ni miongoni mwa nchi ambazo duniani zinatuhumiwa kwa kuendeshwa bila misingi ya kidemokrasia na kidikteta. Ni aibu sana kwamba nchi yetu inaweza ikaiga nchi ambazo tayari zinaonyesha kabisa kwamba hazifuati misingi ya kidemokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukwaa haya ya kimataifa yanatengeneza ushawishi wa nchi kwenye mataifa. Leo hii Mwenyekiti wa OGP ni nchi ya Canada, juzi Rais ame…
Ndio swali langu la kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Rais amesema kwamba amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Canada kuhusiana na suala la Bombardier. Je, Serikali haioni kwamba iwapo Tanzania ingekuwa imeendelea kuwa mwananchama wa OGP na Canada ndio Mwenyekiti wa OGP. Ombi hili la Rais lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi kwa sababu ya mahusiano yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa Miji 15 duniani ambayo inashiriki katika OGP kwa uhuru kabisa na haizingatiwi kama nchi iko kwenye OGP au la. Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na ushiriki si tu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo inafaidika sana kwenye OGP lakini pia na Miji mingine ya Tanzania ambayo inataka kuingia kwenye OGP, Serikali inatoa kauli gani kuhusu hili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto ametoa mfano wa nchi zailizojitoa kwamba zinaendeshwa kwa udikteta na nini na nini. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania ilipofanya maamuzi haya, imefanya kwa kupima vigezo kwa Tanzania ilivyoona inafaa, hatujamuiga mtu. Sisi ni Taifa huru, linalojitawala, linalofanya maamuzi yake yenyewe bila kushurutishwa na Taifa lolote, liwe kubwa ama dogo duniani. Kwa hiyo, kwamba nchi yetu imeiga mawazo hayo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba Rais wetu amemwandikia Rais wa Canada na kwamba Canada ni Mwenyekiti wa hili, mahusiano yetu pengine jambo lingekuwa hili. Nataka nimweleze ndugu yangu Zitto Kabwe, sisi na Canada ni wanachama wa Jumuiya ya Madola, sisi tuna ubalozi Canada, with or without OGP yaani kuwepo ama bila kuwepo OGP mawasiliano yetu na Canada haiwezi kuwa tatizo. Na juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu walikuwa kule Canada. Kwa hiyo mambo haya ya Bombardier na OGP wala sijui yanaendaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefurahi kweli, swali lako la pili nimefurahi sana Ndugu Zitto Kabwe anataka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya ushiriki wa Kigoma Ujiji. Andiko lile la mradi ule linasema nchi ikijitoa, washirika wake wote waliomo ndani ya ile nchi na wao uanachama wao shughuli zao zinakoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo taarifa kwamba Manispaa ya Kigoma Ujiji mpaka sasa wanawasiliana na OGP na OGP wamemuandikia Waziri wa Mambo ya Nje kwamba wana nia ya kuendelea kushirikiana na ninyi. Sasa nataka kupitia Bunge lako Tukufu kuionya Manispaa ya Kigoma Ujiji, nchi inayozingatia utawala bora, haiwezi Serikali Kuu ifanye maamuzi Baraza la Madiwani wakasema sisi hatuta-comply, haijatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nionye Manispaa ya Kigoma waache mara moja, watekeleze maamuzi ya Serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa Serikali itachukua hatua kali zaidi. Na ninyi mnajua Serikali kwenye Manispaa sheria kali kuliko zote ni kuvunja Baraza la Madiwani na kuweka Tume ya Manispaa. (Makofi)
Nawaomba huko mliko Waheshimiwa Madiwani wa Kigoma na ndugu yangu Zitto Kabwe, msiifikishe Serikali huko. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya na zahanati tunavihitaji sana na Serikali inajitahidi sana katika kusaidiana na wananchi kuvijenga vituo hivi na zahanati hizo. Je, si itakuwa ni kazi bure kama tutakuwa na vituo vya afya na zahanati ambazo hazina watumishi ambao watawapa huduma Watanzania? Naomba Serikali ione hilo kwa sababu huduma ya afya ni ya msingi sana watu wetu wasiendelee kuteseka. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa, lakini nataka kutoa majibu ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahakiki vyeti, watumishi wengi sana imebidi waachishwe kazi na moja kati ya idara ambayo imeathirika sana ni afya. Tumeambiwa katika baadhi ya maeneo hata zahanati zimelazimika kufungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ilikwishatoa kibali cha ajira watu 50,000. Wizara yangu katika wale 50,000 kipaumbele namba moja ni afya na nataka nisema kama kuna Halmashauri yoyote ambayo huduma zimesimama kwa sababu watu wameondolewa na hawajapata watu mbadala waandike moja kwa moja kwangu watapatikana mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala alilouliza Mheshimiwa Mary Nagu, nataka niwaambie Watanzania waondoe mashaka. Tuendelee sisi wanasiasa, viongozi kuhimiza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati pale ambapo inakaribia kukamilika au wakati inajengwa Wizara yangu ikipata taarifa itafanya maandalizi wapatikane watumishi kabla ujenzi haujakamilika. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza Halmashauri ya Kaliua hatujafikiwa kuwa asilimia 70 tumefikiwa kwa asilimia 50 tu; kati ya vijiji 102 ni vijiji 54 tu. Katika vijiji ambavyo vilipata miradi kuna baadhi ya makosa ambayo yalifanyika katika kuanisha wale ambao walikuwa ni walengwa na baada ya kulalamika wakaambiwa waandike rufaa kwa sababu kuna wazee ambao wanastahili kupata mradi hawakupewa mradi wakaenda kupewa watu ambao wana uwezo. Leo ni mwaka wa pili waliambiwa waandike rufaa na mpaka leo rufaa haijarudi wala majina yao hayajaingizwa kwenye mradi, jambo ambalo limeleta manunguniko makubwa na masikitiko kwa sababu wanashindwa kuishi lakini wenzao ambao wana hali nzuri wanaendela kupata mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba zile rufaa ambazo ziliandikwa na walengwa zinarudi ili waingizwe kwenye mradi waendelee kunufaika na mradi huu wa kunusuru kaya maskini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili mradi huu umeanza mwaka 2013, lakini kwa baadhi ya wilaya ikiwemo Kaliua tumeanza mwaka 2015, Januari. Naomba kuuliza Serikali kwa zile wilaya ambazo zilichelewa kupata mradi kwa miaka miwili, je, wataendeleza mradi kwa miaka 10 kama ilivyo kawaida au wataenda kufanya evaluation kama wanavyokwenda nchi nzima na kusahau kwamba sasa hivi mradi ni mwaka wa tatu wakati wengine ni mwaka wa tano? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Sakaya kwa jinsi anavyofuatilia kunusuru kaya maskini katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza kwamba kwake tumefikia asilimia 50 sio 70 kama katika maeneo mengine mimi kama Waziri ninayesimamia masuala ya TASAF nitafuatilia nione nini kimesababisha wao wawe chini kulingana na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, anasema makosa yalifanyika katika kuwabaini walengwa na naomba nichukue nafasi kulieleza Bunge lako Tukufu, Watendaji wa TASAF hawana kauli juu ya nani asaidiwe. Wenye kauli juu ya nani asaidiwe ni watu katika mtaa, shehia, wao ndio wanaokaa wanasema hapa kijijini fulani bin fulani hali yake si nzuri. Kwa hiyo kwa yale maeneo ambayo makosa haya yamefanyika ni makosa ya wanavijiji na hasa viongozi wa vijiji kule Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo mmetuletea watu ambao hawakuhusika wamelipishwa fedha. Juzi nilikuwa Singida vijijini, watu walilipishwa milioni tatu laki tisa ambao hawahusiki, wamesharudisha milioni tatu bado laki tisa; na kila mahali wanarudisha. Katika maeneo mengine tumewawajibisha watendaji wa TASAF ambao walishiriki katika udanganyifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zile wilaya ambazo zilichelewa nalo siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja hapa, nitalifanyia utafiti nijue walichelewa kwa sababu gani na nitachukua hatua stahiki.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuandaa mpango huu wa kunusuru kaya maskini. Katika jimbo langu Mheshimiwa Waziri alishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anajua Bonde la Yaeda Chini kwa Hadzabe kule wana tatizo hili la umaskini. Je, ataweza kutuongezea angalau Vijiji vile Mungwamono, Eshkeshi na Endagechani tukapata zaidi msaada huu wa TASAF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubali kwamba nilikuwa DC wa Mbulu 1983 mpaka 1988 na maeneo anayoyataja ya Yaeda Chini nimefika, wanakaa Wahadzabe, wanaishi kwa kuwinda tu badala ya kulima. Nataka nimwahidi kwamba kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge, wanachotakiwa wao ni kuzitambua zile kaya maskini, wakituletea sisi tutachukua hatua. Nilipita siku nyingi kule Yaeda Chini, Mheshimiwa Mbunge akinialika kwenda kuwahamasisha, nitashirikiana naye.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua inayochukua katika kusimika mifumo mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kurahisisha uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pamoja na pongezi hizo, nampongeza vilevile Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, changamoto kubwa katika utumiaji wa mifumo hii ni upatikanaji wa wataalam wa TEHAMA katika Mamlaka za Serikali zetu za Mitaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri wataalam wa kutosha wa TEHAMA hasa katika halmashauri mpya ambazo zimeanza hivi karibuni kama Nanyamba na Halmashauri ya Mji wa Newala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba kwenye Mfumo wa EPICOR kuna changamoto nyingine ambayo inapatikana hususan wakati wa kutayarisha final account katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kiasi kwamba wataalam hulazimika kutafuta taarifa nyingine nje ya mfumo. Je, Serikali ina mpango gani wa ku--repair changamoto hii ili tunapoandaa hesabu za mwisho kwa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa wataalam wategemee taarifa za kwenye system tu na si kuchukua nyingine kutoka nje?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, Mwalimu Mstaafu, Mkurugenzi Mstaafu, RAS Mstaafu, mdogo wangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuwaajiri wataalam wa TEHAMA, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora tutakuwa tayari kuajiri watumishi hao kulingana na mahitaji. Katika zile nafasi 52,000 ambazo zilipitishwa na Bunge ambazo karibuni tutaanza kuajiri, zipo baadhi ya Halmashauri ambazo zimeweka maombi ya kuajiri wataalam hao. Sasa kila Halmashauri inawahitaji hawa kulingana na mahitaji yake yanahitilafiana.
Naomba nishauri, kwa hiyo, kama mdogo wangu Mheshimiwa Chikota, kule Nanyamba uliweka katika maombi, basi itakapofika kuajiri tutaajiri na kama hawakuwekwa tunashauri Nanyamba na Halmashauri nyingine zote katika bajeti inayokuja kutuwekea maombi hayo mkishirikiana na Wizara mama ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la pili la Mheshimiwa Chikota linahusu mfumo wa EPICOR ambao unasimamiwa na Wizara ya Fedha. Kwa sababu Kwa muuliza swali anapaswa kupata majibu sahihi ninaomba nimuombe Waziri mwenzangu wa Fedha ajibu suala la EPICOR kwa sababu linasimamiwa na Wizara yake, kwa ruhusa yako.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Chikota kwa kweli kwa kujali umuhimu wa mifumo hii kuingiliana na kufanya kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo anaisema ambayo sasa wataalam wanajikuta wakitegemea taarifa kutoka nje badala ya ndani ya mifumo kimsingi inatokana na madiliko ya teknolojia ambayo tunaenda nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Chikota atakumbuka kwamba tulianza na platnum wakati ule, tukajikuta kwamba mifumo hii na ina hitilafu tukaamia kwenye EPICOR 7.0; lakini nayo kulikuwa na modules ambazo ni friendly kwa mtumiaji, lakini ikawa na changamoto nyingine tukahama tena tukaenda 7.35 tukaenda 9.05 na sasa tumefika EPICOR 10.20. Kwa hiyo, kwa kweli changamoto anayoisema ni ya kiteknolojia zaidi. Tunatarajia kwamba huu mfumo wa EPICOR 10.2 sasa to zero itajalibu kushughulikia hizi changamoto ambao zinajitokeza katika utumiaji.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kumekuwa na utaratibu wa kutengeneza mifumo yetu nyeti nje ya nchi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usiri na usalama wa taarifa zetu.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kutumia wataalam wetu wa ndani ili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kujitokeza? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeunda Wakala wa Serikali Mtandao. Serikali Mtandao iko pale kwa kusimamia mifumo yote inaayoanzishwa ndani ya Serikali na kwamba mifumo yote iliyopo sasa imeanzishwa kwa kuhusishwa Serikali Mtandao. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya Utawala na Serikali za Mitaa imependekeza na mimi nawaunga mkono kwamba Wakala wa Serikali Mtandao ibadilishwe iwe mamlaka ili iweze kusimamia mitandao yote na mifumo yote inayoanzishwa ndani ya Serikali.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba suala la uzazi wa mpango ni makubaliano ya wanandoa kuhusu idadi ya watoto wanaowataka, lini wawazae na kwa wakati gani. Sasa, je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuibadilisha hii sheria ili kuwawezesha wanandoa kupata watoto wanaowataka kutoka miaka mitatu hadi miwili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa kuna tabia kwa sekta binafsi kuwa hawawapi nafasi ya likizo wafanyakazi wao kutokana na masharti mbalimbali. Sasa, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba hawa wafanyakazi wa Sekta Binafsi nao wenyewe wanapata likizo badala ya kunyimwa mshahara ili akapumzike au aamue apumzike akose mshahara; Serikali ina mpango gani kwa wafanyakazi hawa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uzazi wa mpango sisi Watanzania tunaishi katika jamii, sisi ni wamoja. Sasa tumetafuta utaratibu gani unaweza kutuweka sisi pamoja; mwingine anataka azae kila mwaka, mwingine anataka azae kila baada ya mwaka mmoja na nusu, mwingine anataka baada ya miaka minne, baada ya mjadala mrefu Bunge hili likaweka utaratibu kwamba miaka mitatu inatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusisitiza; sheria hii kwanza inalinda afya ya mtoto mwenyewe kwamba unamwacha akue, lakini mhurumie na huyu unayemzalisha kila mwaka na yeye naye anahitaji kupumzika. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba, hii sera Serikali imeweka kwa nia moja; kulinda afya ya mtoto apate kukomaa vizuri kabla hujamtafuta mwingine, lakini pia huyo mama naye anahitaji kupumzika, kumzalisha kila mwaka ukasema ni muafaka kati yetu sisi; hao wanandoa wanaishi katika jamii ambayo ina sheria, taratibu na kanuni na hiyo jamii inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sekta binafsi kwamba hawawapi nafasi; hizi labour laws, sheria za masuala ya kazi ni za nchi nzima. Kwa hiyo zinatakiwa ziheshimiwe na watu wote; binafsi na wale waliopo Serikalini na Mashirika ya Umma. Pale inapotokea kwamba mtu kanyimwa likizo ya uzazi ati kwa sababu anafanya kwenye shirika binafsi, Waziri wa Utumishi ajulishwe na ntachukua hatua stahiki.
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini bado nina swali moja la nyongeza. Kwa wakati uliopo hivi sasa wanawake wengi wanazaa katika umri mkubwa, hasa kutokana na wengi wamekwenda shule au wakati mwingine pia uzazi kwa hivi sasa kwa wanawake wengi imekuwa ni shida, kwa hiyo utakuta wengi wanazaa…
…Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo najenga hoja, tafadhali nakuomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mtu ana miaka 40 ndipo anapata mtoto wa kwanza, mtu huyu anataka azae ndani ya miaka minne tayari awe na watoto wawili kwa sababu umri haumruhusu kwa wakati huo; hatuoni kwamba kwa sasa hivi sheria hii imepitwa na wakati na inabidi iletwe hapa ifanyiwe mabadiliko? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema watu wanaozaa katika umri mkubwa tuwalegezee masharti waende wanavyotaka. Kwanza nataka niseme hii ni sheria, sheria katika nchi hufuatwa na watu wote, lakini pia mimi kwa ufahamu wangu na utu uzima wangu mama anayezaa akiwa mtu mzima ndiye haswa anatakiwa uangalizi mkubwa kuliko yule aliyewahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo miaka 40 anayoitaja kuanzia 40 kwenda juu, kwa ufahamu wangu, ni kipindi ambacho mama akijifungua anahitaji uangalizi wa hali ya juu. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba hii sheria haijapitwa na wakati, hii sheria ni muafaka, inalinda afya ya mtoto na inajali uzazi wa mpango.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu yaliyotolewa kwa swali hili, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana kuhusu TASAF kwamba ni fedha zinazotolewa na Chama cha Mapinduzi. Hata Ndugu Polepole alipokuja jimboni kwangu aliwaambia wanufaika wa TASAF ni kwamba ni fedha zinazotolewa na Chama cha Mapinduzi. Naomba kauli ya Serikali kuhusu kuzuia upotoshaji huu unaofanywa na Ndugu Polepole pamoja na wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna vijiji 12 katika Jimbo la Buyungu havinufaiki na TASAF kama Vijiji vya Juhudi, Kewe, Rusenga, Kikulazo, Kihomoka, Ruhuru, Njomlole, Yakiobe, Kiniha, Muhange ya Juu, Nyanzige na Nkuba. Ni lini vijiji hivi vitaingia kwenye mfumo wa TASAF? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, la kwanza, sikuwepo Buyungu wala Kigoma kusikia nini alisema Katibu Mwenezi wa CCM, lakini ametaka kujua fedha hizi zinatolewa na CCM au zinatolewa na Serikali? Majibu dhahiri wazi kwamba fedha hizi ni mkopo umekopwa na Serikali ya Tanzania utalipwa na Serikali ya Tanzania unachangiwa na Serikali ya Tanzania, lakini muhimu hiyo Serikali ya Tanzania iliyoweka mipango yote hii inaongozwa na CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba viko vijiji 12 katika jimbo lake ambavyo haviko katika mpango. Napenda kuchukua nafasi hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mpango wa TASAF mpaka sasa kwa Tanzania nzima tumefikia maeneo na watu asilimia 70, hatujafika maeneo yaliyobaki asilimia 30. Maandalizi tunayofanya sasa awamu itakayokuja kuhakikisha kwamba tunamaliza asilimia 30 iliyobaki na tukifanya hivyo hapa shaka vijiji vyake 12 vilivyobaki vitakuwa vimeingia katika mpango wa TASAF.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kutokuwa na afya kwa upande wangu, niwapongeze sana Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye na Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, kwa kupokea simu kwa wakati, niwapongeze sana kwa hili na wengine naomba wafuate mfano huu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, hizo Kanuni nani anazisimamia ili hao Mawaziri ambao wamo humu ndani, hawapokei simu zikiwemo za Wabunge, mbali na za wananchi, ili hatua zichukuliwe? Ikiwa namba za ma- RPC ziko hadharani na ziko katika mtandao, sababu gani zinazosababisha Mawaziri hao namba zao zisiwe hadharani? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri kabla ya kupata Uwaziri hapa, Mheshimiwa Spika ni shahidi, alikuwa mkali kutetea wananchi wake na akawa ngangari kwelikweli. Ni lini Mawaziri namba zao zitatangazwa hadharani ili wananchi na Wabunge watakapowapigia simu wapokee?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, maswali yake kwa kweli ni moja lilelile limejirudia lakini pia nafikiri kuna mchanganyiko kidogo katika swali lake. Analalamika kwamba Mawaziri hawapatikani kwa simu lakini wakati huohuo analalamika kwamba namba zao haziko hadharani. Sasa hao ambao huwapati kwa simu ni wapi kama simu zao hunazo? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kujibu swali lake, nani anazisimamia hizo Kanuni nilizozitaja? Kanuni zinasimamiwa na Serikali, kila Wizara kuna viongozi wake na Wizara ya Utumishi inasimamia Kanuni zote za watumishi wa umma.
Mheshimiwa Spika, sasa ilimradi tumeshasema katika jibu la msingi kwamba hatuna ushahidi wa Waziri ambaye kwa makusudi hataki kupatikana, ndiyo maana hatujamchukulia hatua maana hatuna taarifa hizo. Kila Waziri hapa ana mkubwa juu yake, akizileta kama mimi siyo size yangu nitazipeleka juu, lakini atuletee na siyo kwako wewe tu, Mtanzania yeyote yule ambaye anaona kwamba hakutendewa haki, hampati Waziri kwa makusudi, hilo kwa makusudi naliweka kwenye, Wazungu wanasema inverted commas, maana yake mimi sina ushahidi nalo hilo.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kila Wizara kuna sanduku la maoni. Sanduku lile una jambo la kuishauri Wizara, una jambo umetendewa vizuri na Wizara unaandika unawapongeza, una jambo umefanyiwa vibaya na Wizara unaandika unawasema.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, fedha hizi za TASAF tunafahamu ni mkopo kutoka World Bank na fedha hizi zimekuwa zikitolewa kwa kaya maskini na fedha hizi hazijawahi kuonesha matokeo ya moja kwa moja kwa wale wananchi wanaopewa. Je, Serikali sasa iko tayari kufanya uchunguzi wa kina na tathimini na kuleta taarifa hapa Bungeni yenye kuonesha matokeo ya moja kwa moja kwa kaya hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni ukweli usiopingika kwamba fedha hizi za TASAF zimekuwa zikitolewa kisiasa kwa wana CCM na fedha hizi wakati panapotokea chaguzi ndogo zimekuwa zikitumika sana kushawishi kama sehemu ya rushwa kwa wana CCM ili CCM iweze kuchaguliwa. Nini kauli ya Serikali ikizingatia kwamba fedha hizi ni mkopo na zitarudishwa na Watanzania wote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi naomba nianze kumpongeza muuliza swali Mheshimiwa Msabaha kwa swali lake zuri, lakini pia nataka niwapongeze walengwa wa TASAF Unguja na Pemba. Katika nchi yetu mikoa inayoongoza kwa kufanya vizuri miradi ya TASAF ni mikoa ya Unguja na Pemba na kwa maana hiyo nataka nimpongeze Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed anayesimamia TASAF kule Pemba na Zanzibar ambaye anamsaidia Makamu wa Rais ambaye ndio Waziri mwenye dhamana ya TASAF Zanzibar. (Makofi)
Baada ya pongezi hizo naomba nitoe majibu ya maswali niliyoulizwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba TASAF haijaonesha matokeo; mimi ninanomba tusichanganye mambo, hoja kwamba mnaomba taarifa ya utekelezaji wa TASAF ikoje ni hoja ya msingi na inaweza ikaletwa. Mheshimiwa Mao Tse Tung anasema no research no right to speak. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndio Waziri wa TASAF na juzi nimetoka Kilimanjaro nimeona jinsi walengwa kule na wengi ni wakina mama walivyopambana na umaskini kwa kutumia TASAF wameanza biashara ndogo ndogo mwingine amenunua ng’ombe, wengine wamejenga majumba mimi ninamuomba ndugu yangu, ng’ombe ananunuliwa baada ya kudunduliza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba muuliza swali akubali ombi lake la mwanzo kwamba tupewa taarifa ya utekelezaji wa TASAF lakini kwa uhakika Kamati husika ya Bunge inapewa taarifa ya utekelezaji wa TASAF kila baada ya muda. Mheshimiwa Spika akisema taarifa ya TASAF anataka ailete humu ndani italetwa pasipo na mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba zinatolewa kisiasa, zinatumika chaguzi ndogo ndogo nini kauli ya Serikali jamaa zangu ndio yale niliyosema jambo hujalifanyaia utafiti usiliseme. Walengwa wote wa TASAF wanapendekezwa na wana vijiji wenyewe, wana vijiji wanaambiwa andika jina la mtu unayemuona kijijini kwako hapo anastahili kupata msaada wa TASAF, wakishafanyiwa hivyo sasa ndiyo Watendaji wa TASAF wanazunguka kwenda kuthibitisha kwamba je, huyu yuko na katika kuthibitisha hivyo wengine tumewafuta kwa kuona hawastahili kupata.
Mimi nataka niwaambieni hakuna mtu anayechanganya siasa katika TASAF wala hakuna ushahidi kwamba hela ya TASAF inatumika katika uchaguzi, mimi ningeweze kumuomba Spika kwamba Mheshimiwa athibitishe kauli yake, tusifike huko mimi nimekusamehe. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza mimi nikiri kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI na kwamba Kamati ilikwishafanya ziara mara kadhaa kwa ajili ya kukagua miradi ya TASAF na nikiri kwamba kuna maeneo ambayo TASAF inafanya vizuri tulitembelea Maswa pale tukakuta mama mmoja amejenga kajumba kake kwa njia hiyo vizuri, lakini sasa ni ukweli pia kwamba fedha hizi zinagawanywa kibaguzi na katika ziara tulielezwa na hofu inakuja jana tumemsikia Mheshimiwa Rais anasema ukiwa na chakula chako unawapa kwanza watoto wako halafu ndio unawapa jirani. Sasa mimi naiomba Serikali isipuuze hili suala la ubaguzi kwa sababu litagawa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara iko tayari kubeba hili dukuduku, haya mashaka na kuyafanyia kazi kwa ajili ya mtengamano wa nchi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachompenda Mheshimiwa Selasini ni mtu mkweli, maana utangulizi wake amesema maeneo mengine TASAF wanafanya vizuri, mimi nampongeza kwa kuwa mkweli, lakini tulivyo sisi binadamu katika matarajio ya utendaji hawaweze watoto wote 100 wakafanya vizuri kama unavyotaka wewe. Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya TASAF nakubali rai yake kwamba yale maeneo yenye malalamiko niyafanyie kazi na kwa uzoefu wangu mnavyo nifahamu hili jambo tutaliweka vizuri na naomba Mbunge yeyote ambaye ana ushahidi kwamba mahala fulani hizi pesa zinafanyika kwa upendeleo mimi nitalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kuuliza swali dogo. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini kwa kuwa huu sio mchango ni maswali ya nyongeza mimi naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa TASAF inafanya kazi nzuri sana hapa nchini na kwa kuwa TASAF imefanya kazi maeneo mengi sana hapa nchini kama vile upande wa afya, elimu sasa hivi TASAF inasimamia wanafunzi kwenda shuleni ambao zamani walikuwa hawaendi kutokana na kupunguza umaskini. Lakini nimesema hivi kwa uchungu kwa sababu gani TASAF kazi inayofanya haichagui vyama, haina mpango wa vyama tumeshuhudia Pemba, tumeshuhudia Unguja na tumeshughulikia na hapa Tanzania vyama vyote sichangii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize swali kwa kuwa TASAF inafanya kazi nzuri, je, Serikali ipo tayari kuwaongezea fedha ili wakidhi haja zote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kumshukuru Mheshimiwa Mchemba kwa pongezi alizolitoa kwa TASAF na sisi tutaendelea kuchapa kazi zaidi, lakini kuhusu swali lake kwamba je, TASAF iko tayari kuwaongezea fedha? Nataka niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya TASAF ni ya kuwafikia walengwa wote wanaohitaji kusaidiwa, mpaka sasa tumefikia walengwa asilimia sabini ndio maana kuna vijiji TASAF haijafika, kuna vijiji TASAF imefika lakini hatujawapata walengwa wote, huu mpango wa TASAF uko sehemu “A” na “B”. sehemu a ndio hii tunayoitekeleza sasa, TASAF ya Awamu ya Tatu “B” malengo ya Serikali ni kuwafikia walengwa wote, na ili kuwafikia walengwa wote ni dhahiri lazima tuongeze fedha.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nimuulize bwana Waziri.
Mheshimiwa Bwana Waziri TASAF One ilifanya vizuri sana, TASAF Two nayo imefanya vizuri, na pia sasa TASAF Three nayo inaendelea vizuri. Lakini Mheshimiwa Waziri vipo viporo vya TASAF Two mfano, Barabara ya Bungulwa kwenda Hundya ambayo ilitengeneza makalavati 100, yapo pale Bungulwa zaidi ya miaka mitano sasa. Barabara ya Chibuji - Upamwa miaka mitano zaidi ilikuwa ilete pesa za ukamilishaji wa miradi hiyo miwili ya barabara ni viporo.
Mheshimiwa Waziri Mkuchika ni lini viporo hivyo vya barabara hizo vitaletwa ili kusudi barabara zitengenezwe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la rafiki yangu Mheshimiwa Ndasa kama ifuatavyo kuhusu viporo anavyouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuagiza Mkurugenzi wa TASAF huko aliko anakonisikiliza apeleke timu katika maeneo hayo, nipate taarifa ya hiyo miradi na baadae nitafanya maamuzi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kulingana na majibu ya Waziri nafikiri anajua kwamba kabla ya mchakato wa kuondoa watu waliokuwa wanajulikana kama wenye vyeti feki au vya kugushi, kulikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi kwenye sekta mbalimbali zikiwemo sekta za elimu, kilimo na afya. Sasa kwa kuwa amejibu kwa data nina imani anajua upungufu mkubwa, tungependa alieleze Bunge lako; kwa kuwa kulikuwa na upungufu na wakaongoza tena upungufu ukawa mkubwa zaidi na mmeajiri kiasi hiki alichokisema, tunaomba kujua, mpaka sasa kuna upungufu wa watumishi kiasi gani?
Swali la pili, Rais wa kwanza wa Zanzibar aliwahi kusema tumesoma hatukujua, tumejifunza tumetambua. Serikali ya Tanzania inathamini zaidi vyeti kuliko kuangalia taaluma na kazi ambazo watu wamefanya. Baada ya kutumbua kuna watu walikuwa wamebakiza mwaka mmoja kustaafu. Ninapenda kujua Serikali imejipangaje kwa kuangalia mchango ambao waliutoa, kwa sababu wamefundisha watu wengine ni Wabunge, wengine ni Mawaziri… (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujua kwamba mna utaratibu gani wa kuweza kuwalipa watumishi wale ambao walitumikia Taifa hili kwa uaminifu mkubwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunapowauliza maswali Mawaziri hatutakiwi kuwataka takwimu maana hatutembei na takwimu kichwani.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, nadhani hili swali humu ndani limeulizwa tena na tena na wanasheria wakafafanua. Maelezo yako hivi, mwajiri alikuajiri wewe akiamini kwamba vyeti ulivyompa ni vyeti sahihi ndiyo maana ukaingia naye mkataba. Kile kitendo tu cha mwajiri kubaini kwamba ulimdanganya umepeleka cheti feki, Waingereza wanasema ina-nullify mkataba wako, mkataba wako unakuwa null and void, unakuwa umejifuta kwa sababu upande mmoja umewasilisha taarifa ambazo sizo.
Kwa hiyo hapa ndani hatujajipanga kumlipa mtu ambaye mkataba wake ni fake.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wameteuliwa wengi wao walikuwa ni wana-CCM walioshindwa katika kura za maoni, nao ndio wasimamizi wa uchaguzi. Kuna wengine hata kwa mfano huyo wa Ubungo mpaka leo anahudhuria vikao vya CCM.
Swali langu, ikiwa tutaleta orodha ya Wakurugenzi ambao tunajua ni wana-CCM na walikuwa katika kura za maoni; je, Serikali itakuwa tayari kuwaondoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tunao Wakuu wa Mikoa ambao wanalipwa kwa pesa za walipa kodi, Watanzania wenye vyama na wasiokuwa na vyama, lakini wengi wameonesha itikadi za mrengo wa kisiasa; tukiangalia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu Mkoa wa Manyara na wengine; je, Serikali ina kauli gani kuhusu hilo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kumpongeza Waziri Kivuli wa Wizara yangu, mdogo wangu Mheshimiwa Ruth Mollel kwa jinsi anavyofuatilia utendaji kazi wa Wizara yangu na hiyo ndiyo kazi ya Waziri Kivuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi yeyote utakayemchagua katika nchi hii lazima kuna chama anachokipenda. Huyu yuko pale baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi na Waraka ule wa Utumishi wa Umma unasema; “Mtumishi wa umma anayeteuliwa na Rais, endapo hataridhia kufanya ile kazi, ana ruhusa ya kumwambia Mheshimiwa Rais, naomba niendelee na kazi yangu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa Wakurugenzi walipokuwa wanafanya kazi, wameshakoma kazi waliyokuwa wanaifanya, kazi iliyobaki sasa hivi ni Mkurugenzi wa Halmashauri. Nataka niseme nchi zote duniani baada ya uchaguzi, Rais anayeingia madarakani, anapanga safu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Marekani, State House yote, wahudumu, wafagizi wote, akiingia Rais mpya, anaondoa anapanga watu wake. Sasa kama Mheshimiwa Rais kafanya hivyo kwa hao Wakurugenzi, ndivyo alivyoona inafaa, nasi ndani ya Serikali, tunaona wanachapa kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule wa Ubungo kuhudhuria vikao, nataka niseme hivi, mkishakuwa na chama tawala, siku zote wajibu wenu ni kuihoji Serikali. Mkurugenzi wa Ubungo sio Mjumbe katika vikao vya CCM, lakini anaweza kuitwa saa yoyote aende kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika Jimbo la Ubungo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Wakuu wa Mikoa; kauli gani Wakuu wa Mikoa wanaoshiriki siasa, wanaoonesha wanapendelea upande mmoja, nataka niseme hivi, Mkuu wa Mkoa ndio mwakilishi wa Rais katika Wilaya ile. Mkuu wa Mkoa ndio Rais wa Mkoa ule. Rais ni neno la kiarabu, maana yake kichwa. Kwa hiyo, kichwa cha Mkoa ule ni Mkuu wa Mkoa. Huyu Mkuu wa Mkoa anamwakilisha Rais. Hutegemei huyu Mkuu wa Mkoa afanye mambo tofauti na anavyofanya Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kusema kwamba nchi hii tuna chombo kinaitwa Mahakama. Mhimili wa Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria. Pale mtu ameona kwamba amekuwa aggrieved, au pale mtu ameona kwamba ametendewa ndivyo sivyo, basi tufuate mkondo wa sheria. Baadhi yao mnaowasema, walikuja hapa kwenye maadili, wakasikiliza, wakawa cleared, wakaonekana hawana makosa. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na baada ya maelezo ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Tanzania ni nchi ya Mfumo wa Vyama Vingi na kwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ndio Msimamizi wa Uchaguzi.
Je, Serikali sasa iko tayari kuleta mabadiliko ya Sheria ya Mkurugenzi wa Halmashauri asiwe msimamizi wa uchaguzi hasa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizopo sasa, zilizotungwa na Bunge hili zinasema Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa unapofika wakati wa uchaguzi ndiyo msimamizi wa uchaguzi. Pale inapotokea kwamba Bunge hili litaona haja ya kubadili, hoja iletwe, tutaijadili. Ikibadilishwa, mimi mtumishi wa Bwana nitatenda kama Bwana anavyotaka. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nianze kwa kuwapongeza Wakurugenzi wote nchini akiwemo Kayombo wa Ubungo na Arusha Mjini kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa kuwa ili kuwa thabiti katika utumishi wa umma ni pamoja na kuwajali watumishi; na Mheshimiwa Rais alianza kuonyesha mfano kwa kuwajali walimu wa shule za msingi kwa kuwapatia tablets, napenda kufahamu, je, Serikali ina mikakati gani kuwajali watumishi wa umma katika maslahi yao? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali inafanyaje katika kuwajali watumishi. Tarehe 1 Mei, 2018 Mheshimiwa Rais alipohutubia Uwanja wa Samora pale Iringa alipokuwa mgeni rasmi, alipokuwa anajibu risala ya wafanyakazi alisema; Serikali yake inatumia fedha kadri zinavyokusanywa. Kwa hiyo, ataboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alisema;“mimi sitangoja May Day, siku yoyote nitakapotosheka kwamba hali ya Mfuko wa Serikali inaniruhusu kufanya nyongeza, kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma nitafanya hivyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba Serikali inawajali watumishi, inawapeleka mafunzo, wanapewa mikopo, wengine tunawadhamini katika kupewa mikopo, tunawapeleka kusoma nchi za nje katika taaluma mbalimbali, hiyo yote ni kujali watumishi, maana kumjali mtumishi siyo lazima kumpatia fedha tu, hata ukimpeleka mafunzo, unamjali mtumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo yote niseme kwa kifupi kwamba tunaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, lakini kwa upande wa mishahara kama nilivyosema tutapandisha mishahara pale hali ya nchi itakaporuhusu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kauli ambayo Wakurugenzi walielezwa kwamba wamepewa ajira, wamepewa magari na wanalipwa mshahara na Mheshimiwa Rais, ole wake Mkurugenzi ambaye atamtangaza mpinzani. Kauli hii imeleta sintofahamu, kutojiamini na hofu katika chaguzi mbalimbali. Nini kauli ya Serikali sasa juu ya kauli hii ya tishio la uchaguzi ulio huru na haki? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ndugu yangu Mheshimiwa Waitara hajalieleza Bunge hili kwamba kauli hiyo imetoka lini? Alisema nani? Katika shughuli gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mzee wa zamani, nilifundishwa kwamba government moves on paper. Kwa hiyo, huwezi ukaja Bungeni hapa ukasema fulani alisema hivi na hivi na hivi. Kwa kifupi tu nataka nimjibu ndugu yangu Mheshimiwa Waitara kwamba Wakurugenzi tumewafundisha na tumewafanyisha semina wafanye kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo.
MHE. JOSEPH R.SELASINI: Mheshimiwa Spika, katika awamu hii umezuka mtindo kwa baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwavua vyeo baadhi ya Walimu kutokana na sababu za shule zao kutofanya vizuri, kuwavua vyeo Madaktari na hata wengine kuwaondoa kazini. Sasa mtindo huu unavyoendelea tafsiri ya jamii inaonekana kwamba ni hatua ambazo ni mahususi zilizoagizwa na Serikali. Je, Serikali iko tayari kupitia maamuzi yote haya na kuwarejeshea hao Walimu au Madaktari haki yao kama ikithibitika kwamba walionewa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wako Walimu hasa ajira mpya na hawa wengi wako katika jimbo langu. Wanapoingia kazini hawapewi zile fedha subsistence allowance za kuwasaidia kabla hawajapata mishahara yao na nadhani hata maeneo mengine katika nchi yetu iko namna hiyo. Je, ni utaratibu gani ambao Wakurugenzi au Serikali inao wa kuhakikisha kwamba hao Walimu hawapati mateso wanapoanza kazi zao kwa mara ya kwanza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, ametaka kujua je, kuwavua vyeo kunakoagizwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Serikali iko tayari sasa kuwarudisha. Nilipojibu swali la msingi nilieleza kwamba nchi hii inaendesha kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili ni kwamba yule aliyekuajiri wewe ndiye mwenye madaraka ya kukufukuza. Kwa hiyo, utaona kwamba mara nyingi wakigundua kwamba kuna makosa wanamsimamisha wakati wanasubiri yule mwenye madaraka ya ajira achukue hatua za mwisho.
Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge hili kama kuna mahali mtumishi amefukuzwa na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya wakati yeye siye aliyemwajiri niletewe suala hilo nitalishughulikia mara moja, kwa sababu kwa taratibu zetu za kiutumishi yule aliyekuajiri ndiye anayekuadhibi na ndiye anayekufuza. Nimeeleza hapa jamani sisi siyo malaika, nimeeleza kwamba wakati mwingine tunapowateua tunawapa mafunzo. Hao wanaozungumzwa tumeshawapa mafunzo, naamini nadhani hata Bunge hili kama mnafuatilia maji yametulia katika mtungi siyo kama tulivyoanza huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, Walimu hawapewi subsistence allowance kabla, moja nataka niseme, Wizara yangu ya Utumishi kazi yake ni kuajiri, nikishaajiri nakwambia wewe nenda Wizara ya Maji, Wizara ya Ushirika na kadhalika, sasa yule tajiri wako ndiye anayekushughulikia. Hata hivyo, siku za nyuma imetokea ilifanyika miaka ya nyuma namna hiyo, watu wakawa wanafanya ndivyo sivyo anakwenda anachukua hela anasema anakwenda kuripoti halafu haendei.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu kwamba kwa utaratibu tulionao sasa huingizwi wewe kwenye mfumo wa mishahara mpaka umefika, umeripoti, tuna uhakika kwamba huyu mtu kafika. Huo utaratibu unatuwezesha kupunguza udanganyifu mkubwa katika masuala ya ajira.