Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika (15 total)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo, ujuzi na maarifa ya wataalam wa kilimo unatakiwa uwafikie wakulima mara kwa mara.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha na kuwapeleka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa baada ya uteuzi, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyoonesha juu yangu, wananchi wa Wilaya ya Newala na kwa hakika wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara, wamepokea uteuzi wake kwa shangwe kubwa. Na mimi nataka nichukue nafasi hii kumuahidi Rais nitatekeleza majukumu yangu ya kumsaidia bila upendeleo wala woga na siku zote nitamuomba Mwenyezi Mungu anisaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo, ujuzi na maarifa ya watalaam wa kilimo unatakiwa uwafikie wakulima mara kwa mara. Serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira za Maafisa Ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mwaka wa fedha kutegemea uwezo wake wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2013/2014 hadi 2016/2017 jumla ya Maafisa Ugani 5,710 waliajiriwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimwa Mwenyekiti, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,487. Aidha, Serikali itaendelea kutoa nafasi za ajira kwa Maafisa Ugani kadri ya mahitaji na uwezo wa bajeti.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo lakini unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfuko wa urasimishaji utakaokuwa maalum katika Serikali za Mitaa ili kutatua tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeleza shughuli za urasimishaji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ndugu yangu, mdogo wangu, somo yangu, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo, lakini mpango huu unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ulianzishwa na Serikali kwa lengo la kuwapa nguvu ya kiuchumi wananchi kwa kuwawezesha kumiliki ardhi na kuendesha biashara katika mfumo rasmi na wa kisasa unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa tatizo la upungufu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za urasimishaji na ndiyo maana Serikali imedhamiria kuanzisha Mfuko Maalum wa Urasimishaji utakaowezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake ya urasimishaji bila vikwazo. Mfumo utakaotumika ni kwa Serikali kupitia MKURABITA kuweka fedha za dhamana katika taasisi za fedha zilizokubalika ili kuwezesha Halmashauri kukopa na hivyo kuendesha shughuli zake za urasimishaji. Kwa kutumia mfumo huu urasimishaji utakuwa nafuu, haraka na endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA kwa kushirikiana na Benki ya NMB imekamilisha utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya majaribio katika Manispaa ya Iringa na Halmashauri za Wilaya za Mbozi na Momba Mkoani Songwe. Baada ya majaribio haya ambayo yamepangwa kufanyika kwa miaka miwili, utekelezaji utaanza nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 243, fedha ambayo itatumika kama dhamana kwa ajili ya mikopo ambayo itakopwa na Halmashauri ambazo zitatekeleza miradi ya maendeleo. Aidha, urejeshwaji wa mikopo hii utatokana na michango ya wananchi wenyewe.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi kiasi cha kumwagiwa sifa duniani; na moja ya silaha kubwa dhidi ya rushwa ni uwazi.
Je, ni kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujiondoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP)?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Kuendesha Shughuli wa Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership) ulitokana na wazo la Rais wa Marekani wakati huo Mheshimiwa Barack Obama aliyekuwa na nia na lengo la kuzifanya nchi mbalimbali duniani kuwa wazi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo ulizinduliwa kama Taasisi Isiyo ya Kiserikali (NGO) tarehe 20 Septemba, 2011 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijiunga tarehe 21 Septemba 2011 baada ya kukidhi vigezo vya kujiunga ambavyo ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora. Mpango huo ni wa hiari ambapo nchi inaweza kujiunga baada ya kutimiza masharti na hata kujitoa bila kuwepo na kizuizi chochote.
Hadi sasa nchi wanachama dunia nzima ziko 70 tu na kati ya nchi hizo kumi tu ndizo zinatoka Barani Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kushiriki utekelezaji wa mpango kwa zaidi ya miaka minne imeamua kujitoa. Tanzania si nchi pekee iliyojiunga na mpango huo na kisha kujitoa, nchi nyingine kama Hungary na Urusi zilijiunga na baadae kujitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ya Tanzania tangu kupata uhuru imekuwa na mashirikiano ya kikanda na kimataifa katika kutekeleza falsafa ya uwazi na uwajibikaji. Katika kutekeleza falsafa hii , Serikali imejiunga na kutekeleza mipango ya kikanda na kimataifa kama vile Mpango wa Nchi za Kiafrika wa Kujithamini katika Nyanja za Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa (APRM), Shirikisho la Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki na Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana Rushwa kwa Nchi za Jumuiya za Madola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali yetu imesaini mikataba mbalimbali ya mapambano dhidi ya rushwa kama vile African Union Advisory Board on Anti- Corruption pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa. Ni maoni ya Serikali kuwa shughuli zinazotekelezwa kupitia vyombo hivyo zinatosha kwa nchi kuendelea kujijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi, kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania kujitoa katika Mpango wa Kimataifa wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) hakuna madhara yoyote. Mipango inayotekelezwa ndani ya nchi kama ilivyoelekezwa hapo juu inajitosheleza kuendeleza na kuimarisha misingi ya uwazi na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mradi wa TASAF awamu ya III katika vijiji ambavyo havijapata mradi katika Jimbo la Kaliua?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa dada yangu Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kunusuru kaya maskini ambao umo ndani ya TASAF awamu ya III unaendelea na utekelezaji wake katika halmashauri 159 pamoja na Unguja na Pemba. Mpango wa kunusuru kaya masikini una sehemu tatu ambazo ni uhaulishaji fedha kwa kutimiza masharti ya elimu na afya kwa watoto walioko shuleni na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki pamoja na walengwa kufanya kazi za ajira ya muda. Sehemu nyingine ni kukuza uchumi wa kaya kwa kuweka akiba na kuanzisha miradi ya kuongeza kipato na uboreshaji wa miundombinu ya elimu na afya ili kuwawezesha walengwa kutimiza masharti ya elimu na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kunusuru kaya maskini unatekelezwa katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba lakini si katika vijiji, mitaa na shehia zote. Mpango ulipoanza utekelezaji mwaka 2013, rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia asilimi 70 tu ya maeneo yote, ambayo ni sawa na vijiji, mitaa, shehia 9,989 na maeneo yaliyobaki yana vijiji, mitaa, shehia zaidi ya 5000. Kila halmashauri nchini imegusa kwa wastani wa asilimia 30 ya maeneo yake ambayo hayajafikiwa na mpango wa kunusuru kaya maskini na hili si kwa Jimbo la Kaliua pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba yapo maeneo yenye kaya zenye vigezo vya umaskini na uhitaji ambavyo bado havijafikiwa. Serikali ipo katika hatua za mwanzo za kuanza kuandaa sehemu ya pili ya TASAF awamu ya tatu ambayo itaendelea kwa miaka mingine mitano. Lengo la sehemu hii ya pili ni kuzifikia kaya zote maskini nchini na kuimarisha utekelezaji wa mpango na kuwasaidia wananchi kuwa na shughuli za kiuchumi na uzalishaji zaidi ili waweze kuondokana na umaskini.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, ni lini Mfumo wa EPICOR, LGMD na ule wa LAWSON iliyopo kwenye halmashauri itaanza kuwasiliana na si kuwa stand alone system kama ilivyo sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hii; ule wa Usimamizi wa Fedha za Umma (Intergrated Financial Management Systems – IFMS) au EPICOR, Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (Human Capital Management Information System) au Lawson na Mfumo wa Ukusanyaji Takwimu za Utoaji Huduma (Local Government Monitoring Database) ilinunuliwa kwa nyakati tofauti kutegemeana na teknolojia iliyokuwepo wakati huo na kwa madhumuni tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na teknolojia zake, ni kweli mifumo hiyo ilikuwa haiingiliani au kubadilishana taarifa (automatic data exchange). Hali hii imesababisha kuwepo kwa changamoto ya kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na usimamizi. Gharama hizi ni pamoja na mafunzo kwa watumiaji, leseni za mifumo, ununuzi wa mitambo na vifaa pamoja na gharama nyingine za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa mifumo hii inaunganishwa ili kuleta ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa sasa teknolojia imekuwa na pia uwezo wa Serikali kiutaalam umeongezeka hususan baada ya kuanzisha Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) na Idara/ Vitengo vya TEHAMA katika Ofisi za Serikali kuanzia miaka ya 2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa mifumo hii inawasiliana hatua zifuatazo zimechukuliwa:-
(a) Kuandaa miongozo ya viwango (technical specifications) kwa kuzingatiwa wakati wa kusanifu, kujenga na kuimarisha au kuhuisha mifumo kwa lengo la kufanya maandalizi ya kuunganisha na kuimarisha.
(b) Kutengeneza mfumo maalum wa ubadilishanaji taarifa kutoka mifumo mbalimbali.
(c) Kuweka miundombinu ya TEHAMA ambapo mtandao mkuu wa mawasiliano Serikalini ambapo taasisi, tumeziorodhesha 72 za Serikali, Wizara 26, Wakala wa Serikali 29, Idara zinazojitemea 17 zilizopo Dar es Salaam, Dodoma na Pwani. Aidha, Serikali imeunganisha katika mtandao huu taasisi za Serikali zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 77, Sekretarieti za Mikoa 20, Halmashauri za Majiji, Miji, Wilaya 38 na Hospitali za Mikoa 19 kwa lengo la kuwezesha kuunganisha mifumo inayotumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kulingana na mpango kazi uliopo kazi iliyobaki ya kuunganisha mifumo mbalimbali ndani ya Serikali, ikiwemo mifumo hii mikuu inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. SONIA J. MAGOGO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama ambao wanajifungua kabla ya kipindi cha kuruhusiwa kupata tena miezi mitatu ya mapumziko ili waweze kuwahudumia (kuwanyonyesha) vichanga hao huku wakiendelea na majukumu yao ya kiofisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni namba H12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, mtumishi wa umma anapojifungua hupewa likizo ya malipo ya siku 84. Hata hivyo, iwapo atajifungua zaidi ya mtoto mmoja (mapacha au zaidi), ataongezewa siku 14 na hivyo kuwa na likizo ya siku 98.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mtumishi wa umma atajifungua mtoto/watoto kabla ya kutimiza miaka mitatu atapewa likizo maalum ya wiki sita ili kuhudumia mtoto wake kwa mujibu wa Kanuni H12(6) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009. Baada ya hapo Serikali inaweza kumuongezea siku za kupumzika kulingana na ushauri wa daktari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, likizo ya uzazi hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu kwa kuzingatia Sera ya Afya ya Mama na Mtoto inayosisitiza kulinda afya ya mama na mtoto na pia kuhimiza uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sera hii, msingi wa Serikali kuhimiza likizo ya uzazi kwa utaratibu huu ni kutoa fursa kwa watumishi wa umma kupata muda wa kutosha kutekeleza majukumu ya ajira yao na kuzingatia pia uzazi wa mpango.
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Kaya zinazonufaika na Mfuko wa TASAF kwa vigezo vya umaskini baada ya kukidhi vigezo zimeanza kupata wakati mgumu na usumbufu mkubwa ikiwa mmoja wa wanakaya ni kiongozi wa Serikali ya Kijiji. Mfano baba wa kaya ndiye anakidhi vigezo vya kunufaika na mafao ya TASAF huku mama akiwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, matokeo yake anaondolewa kuwa mnufaika na kuamuliwa kurudisha fedha yote aliyokwishanufaika nayo.
(a) Je, kuwa Mjumbe wa Kijiji kunaondoa umaskini wa kaya?
(b) Je, kaya maskini inapataje uwezo wa kurudisha fedha walizotumia?
(c) Je, ni kwa nini Serikali isiangalie upya vigezo vya wanufaika wa TASAF kwa kushirikisha wadau wengi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, leo mimi nimeamka vizuri, nimefurahi sana, ndiyo maana niliwahi kuja. Nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza vijana wangu wa Yanga… (Makofi/ Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Tuliowatuma wakatuwakilishe kule Ethiopia, wamevuka, wanasonga mbele, ndiyo timu peke yake ya wakubwa nchi hii inayoshiriki mashindano ya kimataifa. (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunazidi kuwaombea wasonge mbele wapate mafanikio, wabebe vizuri bendera ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo mzuri tu, naomba sasa kuchukua nafasi hii kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mpango wa kunusuru kaya maskini una kanuni na taratibu zake za uendeshaji. Taratibu za uendeshaji wa mpango huu ziko bayana kwamba katika utambuzi wa kaya maskini, viongozi wa vijiji, mitaa, shehia hawaruhusiwi kutambuliwa kama walengwa. Hii iliwekwa hivyo ili kuondoa ukinzani wa kimaslahi kwani wao ndiyo wasimamizi wa shughuli zote za mpango katika maeneo yao. Ni kweli kwamba kuwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji hakuondoi umaskini wa kaya yake, hata hivyo, kanuni za mpango zinaruhusu iwapo kaya ya mjumbe inakidhi vigezo vingine vyote vya umaskini lakini anayo hiyari ya kuacha uongozi na kuchagua kuwa mlengwa.
(b) Mheshimiwa Spika, kaya ambazo zilitakiwa kurejesha fedha zilizopokelewa ni zile za wafanyabiashara, watumishi, viongozi na watu wenye uwezo ambao hawakustahili kupokea fedha hizi. Nakiri kwamba katika kuziondoa kaya hizo zilikuwepo zilizoondolewa kwa makosa kwa sababu tu zilikuwa zimeanza kuonyesha mafanikio na kujiimarisha kiuchumi chini ya mpango huu nazo zikatakiwa kurejesha fedha. Hali hii imeleta usumbufu mkubwa kwa kaya hizo.
Naomba kutoa wito kwa watendaji katika halmashauri na vijiji kuacha kuzidai fedha kaya ambazo zilinufaika kwa kutambuliwa kuwa ni kaya maskini na zikatolewa kwa makosa. (Makofi)
(c) Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi mazuri tuliyojifunza katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF. Aidha, tumekutana pia na changamoto ambazo zitazingatiwa katika kipindi hiki ambapo tupo katika mchakato wa maandalizi ya kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF. Ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kuhusu kuwashirikisha wadau wengi zaidi ili kupata maoni yao katika kubainisha vigezo vya kuwapata wanufaika wa TASAF utazingatiwa.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Mawaziri kama walivyo viongozi wengine wa Serikali, wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kwamba wananchi wamewachagua Wabunge na Mawaziri (Serikali) ili kuwasiliana, kushirikiana na kushauriana katika kutatua kero zao; lakini kwa bahati mbaya sana wapo baadhi ya Mawaziri ambao kupatikana kwao hata kwenye simu ni jambo gumu kupita kiasi:-
a) Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya Mawaziri wenye tabia hiyo ya kujichimbia na kutopatikana kwenye simu kuacha tabia hiyo kwa maslahi ya wananchi?
b) Je, Serikali itakubaliana nami kuwa ipo haja ya kuweka utaratibu maalum wa kuifikia Serikali iwapo wananchi kupitia Mbunge wao wana shida ya kumuona Waziri anayehusika na akawa hapatikani hata kwa simu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge anayewakilisha pia Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni B.3(1) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, simu ni moja ya njia za mawasiliano halali Serikalini. Waheshimiwa Mawaziri wanafanya kazi zao kwa lengo la kuwahudumia wananchi na wananchi nao wana nafasi ya kutoa maoni na shida zao na hatimaye kupata mrejesho. Mpaka sasa Serikali haina ushahidi wa kuwepo Mawaziri ambao kwa makusudi hujichimbia na kutopatikana kwa simu. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Spika, zipo njia mbalimbali ambazo wananchi wanaweza kuzitumia kuwasilisha maoni na kero zao ofisini kwa Waziri licha ya simu peke yake. Wananchi wanaweza kuandika barua, kupiga simu, barua pepe kwa viongozi na watendaji wa Wizara kama Makatibu Wakuu au Makatibu wa Waheshimiwa Mawaziri na taarifa za wananchi zitamfikia Mheshimiwa Waziri na kufanyiwa kazi.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. MARYAM SALUM MSABAHA) aliuliza:-
Mradi wa TASAF ni mradi wa kusaidia kaya maskini nchini. Je, ni wananchi wangapi ambao wananufaika na mradi huo katika Visiwa vya Pemba na Unguja?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulianza rasmi januari 2013. Mpango huu ni wa miaka 10 iliyogawanyika katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano na unatekelezwa hadi 2023 katika Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar. Jumla ya kaya maskini milioni 1.1 zenye jumla ya watu takribani milioni tano zimeandikishwa katika jumla ya vijiji, mitaa na shehia 9.986.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar, Unguja na Pemba kaya zilizonufaika na mpango huu kwa kupatiwa ruzuku na ajira kwa kushiriki kwenye kazi katika miradi ya kutoa ajira ya muda mfupi na vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza kwa lengo la kukuza uchumi wa kaya ni 32,262 kutoka katika shehia 168. kati ya idadi hiyo kaya 18,092 ni kutoka Unguja na kaya 14,164 ni kutoka pemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya shilingi bilioni 32 zimetumika tangu mpango uanze kama ifuatavyo:-
(a) Miradi ya kutoa ajira za muda shilingi 7,240,498,800;
(b) Ruzuku kwa masharti ya elimu na afya ni shilingi 25,24,002,721; na
(c) Vikundi vya kukuza uchumi wa kaya zilizotolewa ni shilingi 464,000,000.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti fake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Serikali imeshatoa vibali vya kuajiri watumishi 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti. Vibali kwa ajili ya watumishi hao vimetolewa katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na waajiri wote wameendelea kujaza nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa vibali vya ajira kwa mamlaka zote za Serikali za Mitaa Kumb. Na. CFC.26/ 205/01/PF/91 cha tarehe 22 Agosti, 2017 na kibali kingine cha tarehe 12, Machi, 2018 kuziba nafasi zote za Watendaji wa Vijiji na Mtaa zilizoachwa wazi kutokana na zoezi la kuhakiki vyeti kwa kuajiri watumishi wapya.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutambua umuhimu wa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali, Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22,150 wakiwemo watumishi wa kada za ualimu 6,840, fundi sanifu wa maabara za shule 160, kada za afya 8,000, wahadhiri wa vyuo vikuu 624 na watumishi 6,526 wa kada nyingine.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-
Utumishi wa umma ndiyo injini ya maendeleo katika nchi. Watumishi wa umma hawatakiwi kuwa na mrengo wowote wa itikadi ya kisiasa ili kutumikia wananchi kwa muda wote hata yanapotokea mabadiliko ya vyama tawala baada ya uchaguzi.
i. Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati gani wa kuhakikisha utumishi wa umma ni thabiti na wa kuaminika wakati wote?
ii. Je, ni watumishi wangapi wa umma ambao wamegombea vyeo katika chama tawala wakati wapo katika ajira ya utumishi wa umma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Katibu Mkuu Mstaafu, senior citizen mwenzangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 65(1), Jedwali la Tatu, Sehemu ya IX ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 ikisomwa kwa pamoja na aya ya 50 ya Taratibu za Uendeshaji Utumishi wa Umma za mwaka 2003, watumishi wa umma wanatakiwa kutokuwa na mrengo wowote wa itikadi ya siasa ili kuwatumikia wananchi kwa muda wote bila ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa kanuni hizi zimeendelea kuwepo pia katika Serikali ya Awamu ya Tano na hivyo kuendelea kuimarisha utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na.1 wa mwaka 2015 unaosimamia ushiriki wa watumishi wa umma katika uongozi wa kisiasa watumishi wote wa umma waliogombea na kupata nafasi za uongozi wa kisiasa walistaafu na hawapo tena katika utumishi wa umma.
MHE. . JOSEPH R.SELASINI - (K.n.y MHE. RUTH H. MOLLEL) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano inajinasibu kuzingati Utawala wa Sheria, Kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma. Hata hivyo, kuna ushahidi kuwa baadhi ya viongozi wanakiuka maadili na taratibu lakini wameachwa pasipo kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu:-
(a) Je, tunaweza kujenga uchumi imara bila Watumishi wa Umma kuzingatia Kanuni na Sheria za Utumishi wa Umma?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Taifa linadumisha umoja ulioasisiwa na Baba wa Taifa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazojumuisha zile zinazosimamia Utumishi wa Umma. Endapo wapo watu wanaokiuka sheria, hao wanafanya hivyo kutokana na upungufu wao na kamwe haiwezi kutafsiriwa kuwa ni Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenda kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kinidhamu huchukuliwa pale inapothibitika pasipo shaka yoyote kuwa kosa limetendeka kwa makusudi. Pale ilipogundulika kuwa utendaji usiozingatia sheria unatokana na kutoelewa misingi ya Sheria, Serikali imelazimika kutoa mafunzo maalum ili kuwajengea uwezo watendaji wake ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
(b) Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Umoja wa Tanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekhe Abeid Aman Karume unaendelezwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuadhimisha siku maalum za viongozi hawa, ambapo maoni yao huakisiwa kupitia mikutano ya hadhara na makongamano mbalimbali kwa lengo la kuenzi malengo yao.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR aliuliza:-

Walimu wote nchini wameingia katika Mkataba na Mwajiri ambao pamoja na mambo mengine unaonesha uwepo wa increment kila ifikapo mwezi Julai; tangu iingie madarakani Serikali ya Awamu ya Tano Walimu hawajapewa stahiki hiyo.

Je, ni lini Walimu watalipwa stahiki hiyo kama malimbikizo au haki hiyo imeshapotea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - MHE. MWITA M. WAITARA (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza miongozo mbalimbali iliyowekwa kuhusu maslahi ya walimu ikiwa ni pamoja na kutoa nyongeza za mwaka za mishahara kulingana na utendaji mzuri wa kazi na kwa kuzingatia tathmini ya utendaji kazi ya kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kanuni E.9(1) ya kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 Toleo la Tatu, Nyongeza ya Mwaka ya Mishahara haipaswi kuombwa au kudaiwa na Walimu, bali Serikali ndiyo yenye uamuzi wa kutoa au kutotoa nyongeza hiyo kutokana na Sera za kibajeti kwa mwaka husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watumishi wa Umma wakiwemo walimu wanastahili kupewa nyongeza ya mwaka ya mshahara iwapo bajeti ya mishahara inaruhusu. Kutokana na ufinyu wa bajeti, nyongeza hiyo haikutolewa kwa watumishi katika mwaka wa fedha 2003/2004, 2004/2005, 2008/2009, 2011/2012, 2012/2013 na 2016/2017. Hata hivyo,
kwa kutambua utendaji mzuri wa kazi, Serikali ya Awamu ya Tano ilitoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wote wakiwemo walimu katika mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kutoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wote kadri uwezo wa kulipa utakavyoruhusu. Hata hivyo, walimu hawapaswi kudai malimbikizo ya nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa miaka ambayo nyongeza hiyo haikutolewa. Ahsante.
MHE. MUSSA B. MBAROUK aliuliza:

Tarehe 12 Septemba, 2019 katika Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge yamepitishwa Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kumpa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya mwisho ya uhamisho wa watumishi wa umma.

Je, kwa kumpa Mamlaka ya Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi hakutasababisha ukiritimba katika uhamisho wa Watumishi wa Umma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Bakari Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, imefanyiwa marekebisho katika Kifungu cha 4(3) kupitia Kifungu cha 69 cha Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 13 ya Mwaka 2019 kwa kumpa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya Mwisho ya Uhamisho wa Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Mamlaka yake kama Mkuu wa Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mamlaka hayo, Kifungu cha 8(2) cha Sheria hiyo kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) Mamlaka ya kuwa Msaidizi Mkuu wa Katibu Mkuu Kiongozi. Hivyo, katika kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu Kiongozi, Kifungu cha 8(3)(h) cha Sheria husika kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) Mamlaka ya kuhamisha Watumishi wa Umma kutoka Taasisi moja kwenda nyingine Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa Katibu Mkuu (TAMISEMI) ili aweze kuhamisha Watumishi wa Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vilevile, Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ili waweze kuhamisha Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa yao. Pamoja na kukasimisha Mamlaka yake, Katibu Mkuu (Utumishi) anaweza kuhamisha Watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yeye mwenyewe pale inapobidi.

Mheshimiwa Spika, Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, yamempa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya mwisho ya uhamisho wa Watumishi wa Umma ili kuwezesha uhamisho unaofanywa naye kutopingwa au kutotenguliwa na Mamlaka nyingine. Hata hivyo, Mamlaka hayo yatatumika kwa kuzingatia masilahi mapana katika Utumishi wa Umma au pale ambapo Katibu Mkuu Kiongozi hakuridhika na uhamisho uliofanywa na Mamlaka nyingine zilizopewa au zilizokasimiwa madaraka hayo kama ilivyoelezwa.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-

Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umesaidia kuboresha hali za maisha ya Watanzania, hata hivyo baadhi ya Kaya Maskini hazikuingizwa kwenye Mpango huo:-

Je, ni lini Serikali itaingiza Kaya zote katika Mpango huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Kipindi cha Kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kilitekelezwa kwa miaka sita (6) kuanzia mwaka 2013 hadi 2019. Rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia vijiji/mitaa/shehia 9,960 sawa na asilimia 70. Katika Kipindi hiki jumla ya Vijiji/Mitaa na Shehia 5,590 nchini kote hazikufikiwa.

Mheshimiwa Spika, Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Kipindi cha Pili cha Mpango huu kimezinduliwa rasmi tarehe 17 Februari, 2020 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Wakati wa uzinduzi wa Kipindi cha Pili, Mheshimiwa Rais aliagiza kufanyika kwa uhakiki wa walengwa wenye sifa za kuwemo kwenye Mpango huo, kuhakikisha kaya zote zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanafanya kazi na kulipwa ujira katika miradi ya kuboresha miundombinu ya afya, elimu na maji na kutoa elimu kwa walengwa ili kutumia ruzuku wanazopata kujikita katika kuzalisha na hatimaye kuacha kutegemea ruzuku. Hivyo, utekelezaji wa Mpango huu utaanza rasmi mara baada ya kutekelezwa kwa maagizo hayo.

Mheshimiwa Spika, Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kitatekelezwa katika halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar katika vijiji, mitaa na shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa katika Kipindi cha Kwanza; taratibu za utekelezaji wa Kipindi cha Pili zimeboreshwa ili kuwa na walengwa wanaostahili.

Mheshimiwa Spika, aidha, kabla ya kuanza utekelezaji, Serikali itafanya tathmini ya hali ya maisha ya walengwa waliokuwemo katika kipindi cha kwanza cha Mpango huu ili kubaini kaya zilizoimarika kiuchumi na kuziondoa katika orodha ya wanufaika wa ruzuku katika kipindi cha pili. Utaratibu huu umebuniwa kwa lengo la kulinda mafanikio yao ili ruzuku kwa kaya hizi itakapositishwa wasirudi tena katika hali ya umaskini ndani ya kipindi kifupi. Utaratibu uliobuniwa ni kuipatia kila kaya mafunzo ya kuweka akiba na kuwekeza pamoja na kuwapatia mitaji ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali kulingana na eneo ambalo wana uzoefu nalo.