Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma (16 total)

MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wanawake wa Mkoa wa Morogoro wanaojishughulisha na usindikaji wa matunda wanakabiliwa na ukosefu wa soko na mikopo ya uhakika.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wanawake hao kupata soko la uhakika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mikopo ya uhakika wanawake hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuwasaidia wanawake wasindikaji matunda na mboga mboga kupata soko la uhakika na kuhakikisha wanaondokana na tatizo la kutokuwa na uhakika wa masoko ya bidhaa zao, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Wajasiriamali kushiriki kwenye maonesho ya kutangaza bidhaa zao kupitia maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Saba Saba, Maonesho ya Kikanda, Maonesho ya Juakali na Maonesho mengine ambayo huendeshwa na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.
Mheshimiwa Spika, pia wajasiriamali hao huhamasishwa kushiriki katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane na kuwapatia mafunzo ya ubora wa bidhaa na hatimaye kuhakikisha wanapatiwa alama ya ubora (TBS Mark), kwa kutambua umuhimu wa ubora kwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao. TBS inatoa huduma ya kupima ubora wa bidhaa kwa wajasiriamali bure na wajasiriamali sasa hivi wanapata huduma ya mfumo wa ufuatiliaji (traceability) na alama za utambuzi (Bar Code), humu humu nchini kupitia GS 1 wakati zamani ilikuwa ni vigumu kuzipata kwa sababu zilikuwa zinapatikana nje ya nchi tu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba mipango iliyopo ya kuwapatia mikopo ya uhakika wanawake wajasiriamali ni kama ifuatavyo:-
Mpango wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Japan na Benki ya CRDB imeanzisha Mfuko wa Dhamana kwa Wajasiriamali Wadogo (SME Credit Guarantee Scheme), wenye thamani ya shilingi bilioni mbili. Dhumuni kubwa la mfuko huo ni kusaidia wajasiriamali wadogo wakiwemo wanawake, kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu. Kwa kuanzia, Mfuko huu tayari umeanza kufanya kazi kwenye Mikoa saba ambayo ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro na Singida.
Kadiri Mfuko utakavyoimarika mikoa mingine itafikiwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujasiriamali Nchini (National Enterprenuership Development Fund) ili kuwawezesha kutoa huduma kwa wajasiriamali wadogo wengi zaidi. Hadi sasa Mfuko huo umeongeza kiwango cha mikopo kwa wajasiriamali wadogo ili kuwezesha kupanua biashara ndogo na viwanda vidogo kutoka shilingi 500,000/= hadi shilingi 2,500,000/= na shilingi 2,500,000/= hadi shilingi 5,000,000/= kwa kufuatana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha mipango ya kuvisaidia vikundi au Vyama vya Ushirika vinavyojihusisha na usindikaji wa mazao ya kilimo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na kupitia mikopo rahisi itakayotolewa na Halmashauri, hasa kwa wanawake na vijana. Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) imeendelea kutoa elimu ya mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata mikopo ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi vya kufanya shughuli zao, kuandaa michanganuo ya biashara kwa mjasiriamali mmoja mmoja na katika vikundi.
Mheshimiwa Spika, ili wajasiriamali waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi, Serikali inasisitiza wazingatie mahitaji ya soko tarajiwa kujiunga katika vikundi au Vyama vya ushirika na waweze kutumia vizuri fursa ya kuwepo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Tatizo la maji limeendelea kuwa kubwa Morogoro Mjini pamoja na Mji wa Gairo ambapo wanawake wanapata shida sana kutafuta maji:-
Je, ni lini tatizo hili la maji litaisha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Changamoto za Mileniamu, kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani (MCC) imekamilisha mradi wa maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 24,000 kwa siku hadi kufikia mita za ujazo 34,000 kwa siku kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hilo limeiwezesha Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kupanua mtandao wa usambazaji maji hadi kwenye maeneo ya Nanenane, Tubuyu, Mfuluni, Tungi, Mgudeni, Mjimwema, Tushikamane, Tuelewane, Majengo Mapya, Jakaranda, Kihonda Kaskazini pamoja na Azimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mji wa Gairo, Serikali inakamilisha mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Gairo. Ujenzi wa mradi umefikia asilimia 87 na utakamilika mwezi Juni, 2016. Mradi huu utazalisha mita za ujazo 1,279 kwa siku. Aidha, Serikali ilitekeleza mradi wa uchimbaji wa visima virefu vitatu na uchimbaji ulikamilika mwezi Agosti, 2015. Visima hivyo vimeongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 328 hadi 678. Miradi hii yote kwa pamoja itafikisha uzalishaji wa mita za ujazo 1,957 kwa siku Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuendelea kuboresha upatikanaji wa maji kwa Mji wa Gairo, Mamlaka ya Majisafi MORUWASA imetuma wataalam wake kwenda Gairo kutafiti na kuainisha maneno ambayo yatachimbwa visima vingine vitatu katika vitongoji vya Mnjilili na Malimbika. Wataalam hao wapo katika hatua ya mwisho ya kutafiti upatikanaji wa maji na uchimbaji visima ambao utakamilika Machi, 2016.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ (K.n.y. MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA) aliuliza:-
Amani na utulivu ni muhimu sana katika maisha ya binadamu.
Je, ni lini mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya za Mvomero na Kilosa, Mkoani Morogoro utaisha lini ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara katika Wilaya za Mvomero na Kilosa ambayo imesababisha uvunjifu wa amani na upotevu wa mali na maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi wa Mkoa wa Morogoro umechukua hatua mbalimbali ili kutatua migogoro sugu. Hatua hizo ni pamoja na kupima na kuhakiki upya maeneo ya Kijiji cha Mabwegere, Wilaya ya Kilosa na vijiji vinavyozunguka Bonde la Mto Mgongola ikiwemo Kijiji cha Kambala Wilaya ya Mvomero. Kutokana na upimaji upya wa vijiji hivyo, kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, kazi ya kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi inaendelea. Lengo ni kupima vijiji vyote na kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ambapo maeneo ya ufugaji yatasajiliwa. Vilevile uongozi wa Mkoa uliunda Kamati ya Usuluhisi wa Mgogoro wa Mabwegere na Kamati hiyo imekamilisha kazi, ripoti iliwasilishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya ardhi ni makubwa katika Mkoa wa Morogoro kutokana na hali ya hewa na rutuba, hali hii ndiyo inasababisha watu kutoka Mikoa mingine kuhamia Mkoa huo kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Kutokana na msukumo wa mahitaji makubwa ya ardhi na kuwepo kwa migogoro Mkoa uliamua kufanya tathmini katika Wilaya ya Mvomero na kugundua kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa. Mkoa ulimwomba Mheshimiwa Rais, afute hati za umiliki wa mashamba hayo na hadi sasa mashamba sita yeye jumla ya hekta 1,880.6 yamefutiwa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa una mpango wa kugawa mashamba hayo kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro baina ya jamii hizo. Mashamba hayo hapo katika vijiji vya Wami Luhindo, katika maana ya shamba lililokuwa la Bwana Karim B. Walji lenye hekta 500, shamba la Bwana Lusingo Kibasisi lenye hekta 200, shamba la Bwana Nicolaus Anthony la hekta 52.3, shamba la Joseph R. Hall lenye hekta 166 na shamba la D. H. Kato Farms lenye hekta 247. Vilevile katika kijiji cha Nguru ya Ndege ambapo kuna shamba la Badrun na Karim Dharamishi lenye hekta 392.6 na katika Kijiji cha Wami Valley ambapo kuna shamba la Emmanuel J. Gereta lenye hekta 545.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Benki ya Wanawake ni chombo muhimu sana hasa kwa wanawake wa Tanzania:-
(a) Je, ni lini litaanzishwa tawi la Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Morogoro ili wanawake wa Morogoro wapate kunufaika na benki yao?
(b) Je, kuna mkakati gani wa kuanzisha matawi ya Benki ya Wanawake katika Mikoa yote ya Tanzania ili wanawake waweze kukopa kwa urahisi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009 kwa lengo kuwawezesha wanawake kiuchumi hasa kupata mikopo ya fedha yenye masharti nafuu. Hadi sasa benki hii ina matawi mawili katika Mkoa wa Dar es Salaam.
minne wa 2014-2017, benki imepanga kufungua matawi angalau matatu kwa mwaka kama mtaji utakua kama inavyotegemewa. Hata hivyo, hadi sasa benki haijaweza kufungua matawi katika mikoa mingine kwa sababu haijawa na mtaji wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, benki ina mkakati wa kuuza hisa katika soko la hisa mwaka huu 2016 kwa lengo la kupata mtaji wa kutosha ili kutimiza kigezo muhimu cha kupata kibali toka Benki Kuu cha kuanzisha matawi sehemu nyingine hapa nchini ikiwemo Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuhakikisha kwamba Benki inasogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi hususan wanawake, kuanzia mwaka 2012 benki imeshafungua vituo 89 vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Njombe.
MHE. MARIA N. KANGOYE (K.n.y. MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA) aliuliza:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuanza ujenzi wa daraja la Kilombero na utakamilika lini na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa daraja la Kilombero ulianza tarehe 21 Januari, 2013, nao unaendelea vizuri. Ujenzi wa daraja hili haukuweza kukamilika kwa wakati uliopangwa ambao ni Septemba, 2016 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mvua nyingi za masika zilizosababisha Mto Kilombero kufurika na kupunguza kasi ya utekelezaji wa ujenzi. Kwa sasa ujenzi wa daraja hili umefikia asilimia 75 na ujenzi unatarajiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Desemba, 2016 na daraja kuanza kutumika.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:-
Serikali ina mpango mzuri wa kuanzisha mfumo mpya wa kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima ambao utawanufaisha zaidi.
Je, ni lini mfumo huo mpya utaanza kutumika ili wakulima waweze kupata pembejeo kwa wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya mahindi, mpunga na pamba kwa kutumia mfumo wa vocha kuanzia mwaka 2008/2009 hadi mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa vocha umetoa mafanikio mazuri ambayo ni pamoja na kueneza elimu ya matumizi bora ya pembejeo za kilimo kwa wakulima, kusogeza huduma ya upatikanaji wa pembejeo vijijijini na kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na hivyo kuongeza usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla. Aidha, kumekuwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizojitokeza katika kutekeleza mfumo huu hususan katika ngazi ya wilaya na vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa vocha, mwaka 2016/2017 Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo kwa kutumia Kampuni yake ya TFC kusambaza mbolea hadi ngazi ya vijiji. Mpaka sasa TFC imesambaza tani 25,100 za mbolea ambazo ni sawa na asilimia 85 ya lengo la mbolea ya ruzuku. Pia makampuni ya mbegu yaliyoingia mkataba na Serikali wa kusambaza mbegu za ruzuku wamesambaza tani 429.4
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuandaa utaratibu wa kupunguza au kuondoa tozo mbalimbali za pembejeo zinazochangia ongezeko kubwa la bei ya mbolea. Serikali inatarajia kuanza kutumia mfumo wa manunuzi wa pamoja (bulk procurement). Utaratibu huu utawezesha kupunguza bei ya mbolea na hivyo kuweza kuwafikia wakulima wote nchini kwa wakati na kwa bei iliyo nafuu ikilinganishwa na bei za sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa bulk procurement utaanza kutumika msimu ujao wa kilimo kwa kuanzia; na majaribio ya awali yataelekezwa kwenye mbolea za DAP na UREA.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Pamoja na jitihada nyingi zinazofanyika, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeendelea kuwa na tatizo la maji kila siku:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha na kukarabati Bwawa la Mindu ili kusaidia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kupata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Mji wa Morogoro. Serikali kwa sasa imefanikiwa kupata fedha kiasi cha Euro milioni 70 kutoka Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo (AfD) kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji safi na maji taka katika Manispaa hiyo. Mtaalam Mshauri atakayefanya mapitio ya taarifa zilizokuwepo za uboreshaji wa huduma ya maji safi amepatikana na alianza kazi mwishoni mwa mwezi Februari, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huo, kazi kubwa zitazotekelezwa ni uboreshaji wa Bwawa la Mindu kwa kuongeza kina cha tuta kwa mita 2.5 ili liweze kuhifadhi maji mengi zaidi. Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji eneo la Mafiga, upanuzi wa miundombinu ya kusambaza maji na ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia kiasi cha mita za ujazo 61,000 kwa siku kutoka mita za ujazo 33,000 kwa siku za sasa na utakidhi mahitaji ya maji katika mahitaji ya maji katika Manispaa ya Morogoro hadi mwaka 2025 na ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA aliuliza:-
Kwa muda mrefu miembe imeendelea kushambuliwa na nzi na kuoza, minazi nayo hushambuliwa na ugonjwa wa kukauka na migomba hushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondokana na magonjwa hayo ili wananchi wazidi kufaidika na matunda ya mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara imetunga mwongozo wa mafunzo ya udhibiti shirikishi wa inzi waharibifu wa maembe bila kuathiri afya ya mlaji. Hadi sasa Wizara imetoa mafunzo kwa Maafisa Kilimo 117 na vikundi 19 vya wakulima kutoka Mikoa tisa ya Dar es salaam, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Tabora na Tanga. Maafisa hao walipatiwa nyenzo na mwongozo.
Mheshimiwa Spika, Chama cha Wakulima wa maembe walipewa Starter Kit ili wawe mfano kwa wakulima wengine. Kiasi cha lita 560 za methyl eugenol au kivutia wadudu zimeingizwa nchini na zinaendelea kusambazwa katika mikoa hiyo. Wizara inaendelea na utafiti wa udhibiti wa nzi huyu kwa njia ya kibaiologia kwa kutumia mdudu maji moto katika vijiji vya Visiga na Kibamba Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Spika, utafiti wa minazi uliofanyika kwa miaka 25 umegundua kuwa minazi yote hushambuliwa na ugonjwa wa kunyong’onyea (Lethal Dieback) kwa viwango tofauti. Moja ya mikakati muhimu ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kupanda aina ya minazi yenye ukinzani au ustahimilivu wa ugonjwa huu. Utafiti umegundua aina ya minazi ya East African Tall, Mwambani, Vuo na Songosongo hustahimili ugonjwa huo.
Mheshimiwa Spika, mbegu hizi za minazi yenye ukinzani zinazalishwa katika shamba la mbegu la Chambezi Bagamoyo na zinauzwa kwa bei nafuu kwa wakulima, ni Sh.2,000/= kwa mche. Wizara inaendelea kuboresha utafiti wa zao hili ikiwa ni pamoja na kukijengea uwezo Kituo cha Utafiti cha Mikocheni na watafiti wa zao hilo.
Mheshimiwa Spika, zao la migomba ni muhimu sana katika maisha na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Kagera. Wizara imeweka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku ili kusogeza huduma hii kwa wananchi wa mkoa huu. Kazi za utafiti zilizofanyika kwa mwaka 2016/2017 Mkoani Kagera ni pamoja na usambazaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali, kanuni bora za uzalishaji ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea, mbinu za kupambana na magonjwa na wadudu waharibifu.
Mheshimiwa Spika, kiasi cha miche ya migomba 390,000 ilisambazwa kwa wakulima wa mkoa huo. Aidha, kila Wilaya Mkoani Kagera imeanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya migomba. Pia kitalu mama cha miche ya migomba kipo katika kituo cha utafiti Maruku chenye uwezo wa kuzalisha miche 5,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, utafiti umethibitisha kuwa ugonjwa wa unyanjano unaweza kudhibitiwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji zao hilo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora na safi, kutoa ua dume baada ya mkungu kutungwa, kutumia vifaa safi katika shamba la migomba, kuepuka kuchunga mifugo kama mbuzi katika shamba la migomba, vile vile kung’oa migomba iliyougua mara moja.
Mheshimiwa Spika, ili kutokomeza ugonjwa wa unyanjano ni lazima jamii ishiriki kikamilifu kwa pamoja kama ilivyoelekezwa katika Kampeni ya Tokomeza Unyanjano ya mwaka 2013. Maeneo yaliyozingatia kampeni hii yalifanikiwa kupunguza ugonjwa huu kutoka asilimia 90 hadi asilimia 10. Baadhi ya vijiji na wilaya zimefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu kwa asilimia 100. Wizara inashauri Halmashauri za Wilaya kutumia sheria ndogondogo kudhibiti magonjwa ya mazao ili kupata kilimo chenye tija.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Morogoro umekamilika lakini haina umeme wala maji:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme na maji katika hospitali hiyo ili ianze kutumika na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya mifumo ya umeme na maji katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Morogoro. Ifikapo tarehe 15 Novemba, 2017, Sh.25,240,969.33 zitakuwa zimelipwa kwa ajili ya kuingiza umeme hospitalini hapo. Hadi sasa TANESCO wameshaweka nguzo na mfumo wa umeme katika jengo la hospitali, kazi iliyobaki ni kufunga transfoma ili umeme uweze kuwashwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu ya maji hospitalini hapo utakaogharimu shilingi milioni 50 unaendelea. Kati ya hizo, shilingi milioni 21 zimeshapelekwa kulipia kazi zinazoendelea. Mifumo ya huduma ya maji itakuwa imekamilika ifikapo mwishoni mwa Januari, 2018.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wanawake wengi bado hawaelewi haki zao hasa kuhusu haki za kumiliki ardhi.
Je, kuna mkakati gani wa Serikali wa kuwawezesha wanawake waweze kujua haki zao za kumiliki ardhi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu haki ya wanawake kumiliki ardhi. Elimu hiyo imekuwa ikitolea kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipindi vya redio na luninga, mikutano ya hadhara, warsha, semina, maonesho mbalimbali kama vile Siku ya Sheria, Wiki ya Utumishi wa Umma, Siku ya Mtoto wa Afrika, Maadhimisho Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, Wiki ya Msadaa wa Kisheria pamoja na maonyesho mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikichapisha machapisho yenye kuelimisha umma kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi. Aidha, Tume hiyo imetoa elimu katika Kata 72 katika Wilaya 18 za Tanzania Bara na Shehia nane za Wilaya nne za Tanzania Zanzibar. Wilaya za Tanzania Bara ni Biharamulo, Ngara, Mpanda, Babati, Simanjiro, Mbarali, Mbeya, Mvomero, Ulanga, Ludewa, Makete, Nkasi, Namtumbo, Tunduru, Kahama, Kishapu, Kilindi na Tanga; na Wilaya za Tanzania Zanzibar ni Unguja Kusini, Unguja Kaskazini- A, Mkoani na Michweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuendelea kuelimisha umma katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar hasa kwa wanawake ili wananchi wote waweze kufurahia haki zao za msingi ikiwemo haki ya kumiliki ardhi.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Mpaka sasa inadaiwa kuwa hakuna dawa sahihi za kutibu ugonjwa wa kisukari.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti kuhusu dawa za kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa kisukari ni moja kati ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza. Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa kichochezi kiitwacho insulin. Aidha, kwa kushindwa kutengenezwa kabisa na kongosho au kwa jina kitaalam unaitwa pancreas au kwa kufanya kazi chini ya kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina tatu za kisukari. Kisukari ambacho kinategemea insulin ambayo tunaita type one ambacho huanza utotoni; kisukari kinachotegemea insulin ama type two ambacho huwapata watu kuanzia miaka 35 na kuendelea ingawa watoto na vijana wameanza kupata aina hii kutokana na kutaozingatia misingi ya lishe; na kisukari cha mimba hii ni aina ya tatu ambayo inatokea wakati wa ujauzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ambayo yanachangia mtu kuugua kisukari ni pamoja na kuwepo historia ya kisukari ndani ya familia, magonjwa ya kongosho kama saratani na maambukizi, uzito unaozidi na unene uliokithiri, shinikizo la damu, mtindo wa maisha usiofaa hususani kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa , uvutaji wa bidhaa za tumbaku na masuala mengine kulingana na aina ya kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mpaka sasa duniani kote haijagundulika dawa ya kutibu ugonjwa wa kisukari na kupona kabisa. Matibabu yote yanayotolewa mpaka sasa ni yale yanayompatia mgonjwa kiwango bora cha kuishi ikiwemo kuhakikisha kwamba kiwango chake cha sukari mwilini kinakuwa ndani ya kiwango cha kawaida kila siku ili kuvilinda viungo vingine vya mwili visidhurike na hivyo kumpunguzia mgonjwa magonjwa ya mara kwa mara, kulazwa wodini mara kwa mara na kupunguza uwezekano wa kifo. Dawa hizi ni pamoja na sindano ya aina ya insulin ambazo mgonjwa hulazimika kuchoma kila siku kwa maisha yake yote na vidonge ambavyo kila mgonjwa humeza kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tafiti nyingi ambazo zinaendelea duniani kote kutafuta dawa itakayoweza kutibu kabisa ugonjwa huu, lakini tafiti hizi bado hazijazaa matunda. Tafiti hizi ni pamoja na zile za kujaribu kutengeneza cell za kongosho na kuzipandikiza kwa maana ya Pancreas Stem Cell Transplantation ili kuweza kuweka cell mpya za kongosho na kuipa kongosho uwezo wa kutengeneza insulin kwa wingi zaidi. Njia hii pekee ndiyo itakuwa ufunguzi wa kudumu wa tiba dhidi ya ugonjwa huu. Mara tu tafiti hizi zitakapokamilika na kuonesha mafanikio, Serikali ya Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma hii inapatikana hapa nchini.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Tatizo la uvuvi haramu bado linaendelea licha ya jitihada za Serikali kuchoma nyavu za uvuvi zisizopendekezwa:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha uvuvi haramu zaidi ya kuchukua hatua hiyo ya kuchoma nyavu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara imepewa jukumu la kulinda, kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009. Katika kutekeleza jukumu hili, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu kwa kufanya doria za mara kwa mara pamoja na kufanya operesheni mbalimbali ikiwemo Operesheni Sangara ya mwaka huu wa 2018, Operesheni Jodari na za Kikosi Kazi cha Kitaifa, kwa maana ya Mult (Multi-Agency Task Team - MATT) cha kuzuia uharibifu wa mazingira ili kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo mikakati mbalimbali ya kupambana na uvuvi haramu. Mikakati hiyo ni pamoja na: Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi (BMU’s); kuendelea kutoa elimu kuhusu athari za uvuvi haramu kwa mazingira, jamii na kiuchumi; kufanya maboresho ya sheria ili kuwa na sheria kali dhidi ya uvuvi haramu hasa uvuvi wa kutumia mabomu/ milipuko, ikiwa ni pamoja na kuweka kipengele cha kuonesha uvuvi haramu ni sawa na uhujumu uchumi; na kuimarisha Mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa kwa kushirikiana na nchi mbalimbali zikiwemo nchi za SADC katika kuzuia uvuvi uisoratibiwa na usioripotiwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara inahamasisha ufugaji wa samaki ili kupunguza nguvu ya uvuvi kwenye maji ya asili. Aidha, naomba Waheshimiwa Wabunge wote watusaidie katika kuwaelimisha wananchi kuachana na vitendo vya uvuvi haramu na kushiriki katika kulinda rasilimali za nchi yetu. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi walio kwenye vijiji vilivyopo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kuwarahisishia upatikanaji wa vitabu vya usajili Wilayani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA YA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 kifungu la 21 na Kanuni ya 36, kila kijiji chenye mpango wa matumizi bora kwa ardhi inapaswa kuwa na daftari la usajili wa ardhi ambalo linatunzwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji. Daftari la usajili ni daftari ambalo hutumika kusajili hati za hakimiliki za kimila zinazotolewa katika ardhi ya kijiji husika. Utoaji wa hatimiliki za kimila hutanguliwa na zoezi la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ambayo inalenga kuboresha mipango ya matumizi ya ardhi katika kijiji kwa kuondoa mgongano wa matumizi katika ardhi za vijiji pamoja na kuiongezea thamani ardhi hiyo kuifanya kuwa ni mtaji hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na changamoto za upatikanaji wa madaftari ya usajili wa ardhi katika baadhi ya Halmashauri kutokana na uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuchapisha madaftari hayo. Katika kutatua changamoto hiyo, Wizara imekuwa ikisadiana na Halmashauri kuzipatia madaftari ya usajili wa ardhi wakati wa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Hata hivyo, Wizara imeanza kutoa hati za hakimiliki za kimila kwa kutumia mfumo wa kielektroniki katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga, Malinyi, Mkoani Morogoro. Teknolijia hii itakapoenea katika maeneo yote nchini itaondoa kabisa mahitaji ya madaftari ya usajili wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahimiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuchapisha madaftari ya usajili wa ardhi wakati tunasubiri teknolojia ya utaji wa Hatimiliki za kimila kwa njia ya kielektroniki kuenea katika nchi nzima.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Vijana na Akinamama wengi kwa sasa wamewekeza katika kilimo cha mboga mboga, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa masoko ya uhakika kwa bidhaa zao:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima hao kupata soko la uhakika la bidhaa zao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha matunda na mboga kinakadiriwa kuajiri wananchi milioni 2.4 wengi wao wakiwa akinamama. Kutokana na umuhimu huu, Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika kutambua fursa za masoko ya matunda na mbogamboga ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Horticulture Association imewapatia wakulima wa matunda na mbogamboga kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Zanzibar mafunzo ya kilimo bora cha matunda na mbogamboga ili kukidhi matakwa ya masoko ya ndani na nje ya nchi. Mafunzo haya yatafanyika pia katika mikoa iliyobaki ili kuwasaidia wakulima wananchi nzima kupata soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutafuta ufumbuzi zaidi wa soko, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uswiss inatekeleza mradi wa kukuza soko la mboga na matunda kwa kukusanya na kusambaza kwa wadau taarifa za masoko hususani uzalishaji, bei, mahali lilipo, zao na mnunuzi anayehitaji. Mradi huu umewezesha taarifa hizo kukusanywa na kusambazwa kwa wadau kwa kutumia simu za viganjani. Lengo kuu lilikuwa kuwaunganisha wakulima na soko maalum na hoteli za kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizi, wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Wizara ya Kilimo na Taasisi nyingine za Umma, inahamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kusindika matunda. Uwekezaji huo umelenga katika uendelezaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio yaliyopatikana kutokana na uhamasishaji huo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Bakhresa Food Products kilichopo Vikindu, Wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani; Sayona Fruits Limited kilichopo Mboga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani; Dabaga kilichopo Iringa; Sayona Fruits Limited kilichopo Mwanza; Elven Agri Company Limited kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani; na Iringa Vegetables Oil and Related Industry Limited (IVORY). Kwa hiyo, ni matumaini yetu kuwa viwanda hivi na vingine vinavyofuatia vitakuwa soko la uhakika la mazao ya wakulima hali itakayochochea ari ya kuzalisha zaidi. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wakulima wengi wamehamasika katika kilimo cha alizeti lakini alizeti inayolimwa haitoi mafuta kwa wingi:-
Je, Serikali ina mkakati gani katika kuimarisha utafiti wa mbegu ya alizeti inayotoa mafuta mengi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ikiwemo alizeti Serikali inatekeleza mkakati wa miaka mitano, yaani 2016/2020 wa kuendeleza zao la alizeti ambao unalenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima, kuhamasisha matumizi ya kanuni bora za kilimo, kujenga uwezo wa vyama vya wakulima kuzalisha mbegu bora za daraja la kuazimiwa yaani QDS na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya usindikaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Vituo vya Utafiti vya Ilonga (Morogoro), Makutupora (Dodoma), Tumbi (Tabora), Uyole (Mbeya), Ukiriguru (Mwanza) na Naliendele (Mtwara) inaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora za alizeti ambapo mbegu tano aina ya record, hysun 33, agura 4, NSFH 145 na NSFH 36 zimesajiliwa.
Mheshimiwa Spika, kati ya mbegu hizo, mbegu aina ya record inayozalishwa nchini tangu mwaka 1985 imefanyiwa maboresho na kuiwezesha kuwa na tija ya uzalishaji wa tani 1.5 mpaka tani mbili kwa hekta; ukinzani dhidi ya magonjwa, kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kutoa mafuta mengi kwa asilimia 48 mpaka 50. Aidha, mbegu ya record ni open pollinated variety (OPV) inayoweza kutumiwa na wakulima kwa misimu miwili hadi mitatu ukilinganisha na mbegu aina ya chotara ambazo zinaingizwa kutoka nje ya nchi na kutumika kwa msimu mmoja tu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mbegu nyingi zaidi zinazalishwa na kuwafikia wakulima, Kituo cha Utafiti Naliendele kinakamilisha utafiti wa aina tatu mpya za mbegu ya alizeti katika msimu wa 2018/2019. Aidha, Serikali imeingia ubia na sekta binafsi kufanya utafiti na kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi ambapo Kampuni ya Silver Land na Quality Food Product zipo katika hatua ya majaribio ya aina mpya ya mbegu za chotara za alizeti ambazo zitazalishwa nchini.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-

Serikali inajitahidi sana kukabiliana na tatizo la maji katika Manispaa ya Morogoro, lakini tatizo hilo lipo kwenye baadhi ya Kata:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya makusudi ya kumaliza tatizo hili katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) inaendelea na uboreshaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Morogoro kwa mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Katika mipango ya muda mfupi, katika mwaka wa fedha 2018/2019, MORUWASA imetekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Kata za Kihonda na Mkundi. Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9 na umewanufaisha wakazi wapatao 17,000 wanaoishi maeneo ya Kihonda Kilimanjaro, Yespa, Kiegea na Kihonda Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la AFD itatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Manispaa ya Morogoro. Kazi zitakazotekelezwa ni kuongeza kina cha bwawa la Mindu, ujenzi wa mtambo wenye uwezo wa kusafisha na kutibu maji, upanuzi wa mtambo wa kusambaza maji, ukarabati wa mabwawa ya majitaka kwa gharama ya Euro milioni 70. Kwa sasa Wizara inasubiri kusainiwa kwa mkataba wa kifedha kati ya Wizara ya Fedha na Shirika la Maendeleo la Ufaransa la AFD kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.