Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susan Limbweni Kiwanga (35 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme elimu kwanza iwe ya darasani au mitaani. Kama Serikali ingekuwa makini katika vipaumbele vya nchi elimu ingewekwa ya kwanza nchini ili kupata matokeo makubwa. Hivi bila elimu hata mimi nisingeweza kuchangia, Daktari, Mbunge, Waziri, Rais, Mwalimu, viongozi na wataalum wote wasingekuwepo. Sasa kwa nini Serikali inafanya mzaha katika suala la elimu? Jamani tusione aibu, tuseme tulikosea sasa tushirikishe wadau tuanze upya ni kweli tumejikwaa na kujikwaa si kuanguka, bado hatujaanguka tujipange.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mengi ya walimu nchini lakini naomba nizungumzie matatizo yanayowapata walimu katika Jimbo la Mlimba, pia miundombinu ya shule, upungufu wa walimu na elimu ya awali pia watoto walemavu wanaoishi katika Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za sekondari kata changamoto ziko tofauti, kuna uwekaji wa umeme wa jua ambako REA haifiki katika shule za sekondari za Kiburubutu, Uchindile, Matundu Hill na Mofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ununuzi wa samani (meza na stuli) za maabara kwa shule zote za Serikali zilizoko katika Jimbo la Mlimba ambazo ni Masagati, Utegule, Mutenga, Kamwene, Mlimba, Tree farms, Chisano, Chita, Mchombe, Kiburubutu, Nakangutu, Mbigu, Mofu na Matundu Hill. Pia ujenzi wa hosteli shule za sekondari za Chisano na Matundu Hill.
Aidha, kuna uhitaji wa madarasa 1,166 yaliyopo 467 hivyo hakuna madarasa 699; nyumba zinahitajika 1,036, zilizopo ni 199, hakuna nyumba 837; vyoo mahitaji ni 897, vilivyopo 290 hakuna vyoo 607
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nitawasilisha hali halisi ya hali ya elimu Jimbo la Mlimba.
Mheshimiewa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba kuna kituo kimoja tu cha ufundi kilichopo Mchombe. Kituo hicho cha ufundi stadi kina changamoto ya uchakavu wa madarasa ya nadharia na vitendo, upungufu wa zana na vifaa vya kufanyia kazi katika fani zote za useremala, uashi, chuma na sayansi kimu pia walimu. Hivyo naomba ukiangalie kwa jicho la pekee kituo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali ya shule za awali na msingi ni duni sana, hali ya walimu ndio kabisa, nyumba za walimu ndio usiseme, ukizingatia ni Jimbo la vijijini na miundombinu ya barabara ni mbaya hivyo wanahitaji kuwezeshwa usafiri angalau wa pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kuwa utalipa kipaumbele Jimbo la Mlimba kwa kuwapelekea walimu wa shule za sekondari na msingi katika ajira zijazo. Mahitaji sahihi nitakupatia, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kwa kuanza kuunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ione haja ya kutangaza Mkoa wa Ulanga ili kusogeza huduma kwa wananchi. Taratibu zote ngazi za Halmashauri na Mkoa (RCC) zimeshafanyika. Pia itangaze Halmashauri ya Mlimba ambapo wananchi wa Mlimba wanataabika kumfuata Mkurugenzi kilometa 269 na miundombinu mibovu na kushindwa kupata huduma kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Ifakara- Taweta - Madeke - Njombe. Takribani kilometa 269 haipitiki, hivi niandikavyo taarifa hii, barabara hiyo haipitiki hata mabasi ya abiria yaliyokuwa yanatoa huduma yamesitisha kutokana na ubovu wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauli zimepanda kutoka sh. 20,000/= hadi sh. 40,000/= kufika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ambako huduma zote za matibabu, mahakama na kadhalika zinapatikana. Hali hii ni mbaya, hivyo naomba
Serikali ione hitaji kubwa la kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo inategemewa sana na wananchi kusafirisha mazao yao ukizingatia barabara hiyo iko kwenye eneo la ghala la chakula (kilimo
kikubwa cha mpunga, mahindi (KPL) pia cocoa, ndizi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio kingine kikubwa kwa wananchi wa Mlimba ni maji safi na salama. Hivyo naomba Serikali ianze na kero kubwa hizi mbili, barabara na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Bila mazingira nchi hii tunakwenda kuangamiza vizazi vyote katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iongeze fedha za mazingira katika bajeti. Bajeti ya mazingira kila mwaka haieleweki ingawa suala la mazingira ni mtambuka.
Hivyo ni wakati sasa umefika wa kutilia mkazo suala la mazingira ili kuwepo na watumishi na Idara ya Mazingira. Ni ukweli usiopingika kwamba mazingira yanaharibiwa ngazi ya mitaa na vijiji, mijini na vijijini. Hivyo mkiimarisha Idara hiyo kwa kutengewa fedha za kutosha mtanusuru na kulinda mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie kwenye Wizara hii ya Miundombinu. Naibu Waziri anajua lakini bahati mbaya sana alifika wakati wa kiangazi. Hapa ninaposema, ninaposimama, naogopa hata kwenda Jimboni kwa sababu kuna vilio, kuna vifo, Mheshimiwa Naibu Waziri ile barabara imekatika kabisa. Hata kama ulimuagizia engineer siku ile kwamba ile barabara ipitike mwaka mzima ukimuuliza sasa hivi; kwanza namshukuru Meneja wa Mkoa, yule mama anafanya kazi kubwa sana lakini hela hana. Makandarasi wako kule, lakini kama unavyojua ile barabara ya Jimbo la Mlimba ina mito mingi sana, kwa hiyo kuanzia pale Idete Kalia Gogo mpaka ukifika Taweta, kule karibu na Madeke, Njombe barabara yote inakatika, mkandarasi anahangaika, leo akiziba hapa kesho imekatika hapa mito kila kona. Kwa hiyo, Jimbo la Mlimba linatakiwa litazamwe kipekee kuhusu masuala ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaposema, sisemi tu kwa kujifurahisha lakini nimeona kwenye kitabu chenu kwamba mnaboresha barabara ya mpaka Madeke - Njombe, mnaposema Madeke, Njombe ndiyo inapakana na Mlimba, na watu wa Njombe wanataka ile barabara iboreshwe na mnajenga kwa kiwango cha lami ili watu wa Njombe wapite Mkoa wa Morogoro waje Dodoma, sasa mtapoboresha kule barabara ya Njombe mpaka Madeke mkiiacha kutoka Madeke - Tanganyika - Taweta hadi Mlimba (Ifakara) mtakuwa hamjaitendea haki thamani ya ile barabara ya Madeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachoomba mnasema iko kwenye upembuzi yakinifu na kweli kabisa lakini kwenye vitabu vyenu haijazungumziwa kabisa hiyo barabara, huo upembuzi yakinifu na wa kina umeisha au vipi? Mnatarajia kujenga kwa kiwango gani? Mnasema kiwango cha lami kuanzia Ifakara mpaka Mlimba, lakini mjue kwamba ili tulinganishe Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe inatakiwa barabara ifike Madeke kule Taweta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba, tumeteseka kiasi cha kutosha miaka mingi tangu uhuru sasa na sisi angalau tufaidi matunda ya uhuru. Tunashangaa tu barabara za wenzetu lami, flyover, ndege, sisi hatutaki hata kuzungumzia ndege, tunataka barabara. TAZARA ipo inapita kule hivi wananchi wa kule wanaponea ki-peace cha kutoka Makambako mpaka Kilombero lakini ki-peace kinapita kwa wiki mara mbili au tatu.

Leo mama mjamzito anayetokea kule Masagati, Taweta, Njombe moyo unaniuma mimi, moyo unalia machozi akina mama wanakufa katika Jimbo la Mlimba, wanataka kujifungua hakuna hospitali ya uhakika, hospitali mpaka iwe Ifakara kilometa 230 hivi huyu mama mjamzito anafikaje kwenye hiyo hospitali? Wote mmezaliwa na wanawake, hebu muwaonee huruma wanawake wanaotokea katika Jimbo la Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanakufa kule jamani, kwa vile hakuna vyombo vya habari wangekuwa wanaripoti kila siku, lakini tunahangaika tu, hakuna tv nani apeleke tv yake kule sehemu ambayo haina barabara? Kwa hiyo, mimi naomba suala la barabara Mlimba ni kipaumbele. Naomba barabara, Mheshimiwa Naibu Waziri umefika Wananchi wamekushangilia ukamuagiza engineer lakini nakuambia leo hii hata hawa ma- engineer hawana bajeti ya kutosha, kinachotakiwa ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme sasa, kinachotakiwa ni kwamba barabara hii ya kilomita 230 kutoka Ifakara mpaka Madeke, mpakani na Njombe imekatika haina uwezo tena wa kupitika na haijapangiwa pesa za kutosha. Hata kama tunasubiri lami, basi tunaomba ipitike kwa mwaka mzima na nimeongea na wataalam, engineer anasema kwamba ili hii barabara ipitike kwa mwaka mzima inahitaji inyanyuliwe kwa kiwango cha juu sehemu zile korofi kilometa zisizopungua 50 angalau, lakini hela mliyoitenga kwa kukarabati hiyo barabara haisaidii, tutaendelea kuteseka wananchi wa Mlimba. Naomba mtuokoe tumo kwenye shimo, tunaonekana kama hatujapata uhuru ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kuna akina mama, kuna vijana na wazee wanahitaji huduma. Kwa hiyo basi maeneo ambayo barabara imekatika, ukianzia Jimbo la Mlimba utaanza katika kata ya Idete Kalia Gogo. Vilevile kuna maeneo mbalimbali ambayo hii barabara haipitiki, utaenda Idete, Kalia Gogo, Kiogosi, Kisegese, Tandale, Mbingu, Ngajengwa, Njage, Udagaji, Mgugwe, Mlimba Mpanga mpaka Madeke - Njombe, hili eneo lote ninalosema ni barabara ambayo ni ya TANROADS, mnatusaidiaje wananchi wa Mlimba? Hali ni mbaya tunateseka. Kwa hiyo, ni muhimu wakaliangalia kwa jicho la karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, ni Waziri wa kwanza uliyefika kuitembelea ile barabara, basi naomba uitendee haki, naomba tafadhali uitendee haki ile barabara ungepita wakati huu kwanza usingefika ingebidi urudi Ifakara, Mkuu wa Wilaya alikuwa anaenda Mlimba akashindwa akabakia pale Mgugwe maji yamejaa yanakatiza barabara akarudi Ifakara. Ndiyo maana nilikuwa nalalamika haiwezekani Mkurugenzi tumemnunulia V8 halafu gari mnamuachia Mkuu wa Mkoa, hivi huyu Mkurugenzi akitaka kuwahudumia wananchi wa Mlimba ataenda na usafiri gani? (Makofi)

Kwa hiyo tuna umuhimu wa vitu vyetu vibaki Kilombero. Yaani mimi hapa leo nalia na barabara, hela mlizotenga hazitoshi hata kwa haya matengenezo yanatakiwa linyanyuliwe matuta katika eneo korofi ya kilometa 50. Naomba mtutengee hela za kutosha. Ongeeni na wataalam wenu wanajua, na mimi haya nimeyapata kwa wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba barabara ya kutoka Mlimba, tuna Kata moja ya Uchindile ina mto mkubwa sana, huu Kilombero unaanzia kule, tunaomba ile barabara ichukuliwe na TANROADS sisi hatuna uwezo wa kuunganisha hiyo barabara kama Halmashari kutoka Mlimba mpaka Uchindile. Vilevile kutoka kijiji cha Tanganyika tumeomba mpaka mkoani ile barabara muichukue TANROADS, kuanzia Taweta mpaka Tanganyika kuna mto mkubwa wa Kilombero unakatisha. Kwa hiyo, wananchi wametengwa na kata zao, jimbo la na Mkoa wao. Chonde chonde nawaomba sana mtuangalie na mtupe haya maeneo tuhakikishe kwamba barabara inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hivyo tu kuna suala la TAZARA. TAZARA mmeandika kidogo sana. Jimbo langu limepitiwa na TAZARA, makao makuu ya TAZARA kiwilaya yako Mlimba, lakini TAZARA hiyo kuna wastaafu wanadai miaka kenda rudi, wengine mpaka wanakufa watoto wameshindwa kusoma, ninyi katika kitabu chenu sijaona mahali popote. Namna gani mnasema tu sasa hivi sijui ngapi, naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri wale wastaafu wa TAZARA waliotumikia reli kwa muda mrefu, na watoto wao sasa hivi wanateseka na wenyewe wanateseka ni nini hatima yao nchi hii jamani? Watu waliotumikia kwa moyo mkubwa kwa imani bila wizi kwa nini mnawafanyia hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muwaokoe wastaafu wa TAZARA. Mheshimiwa Waziri ukija hapa useme kidogo kuhusu wastaafu wa TAZARA, kama ndio wamesahaulika hawawezi kulipwa tena, basi mtuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano, barabara hakuna simu wengine mpaka wapande juu ya miti, sasa haya mambo gani? Kuna maeneo ambayo huwezi ukapata simu, mimi mwenyewe nikienda Jimboni kipindi fulani utanitafuta hunipati, hakuna mawasiliano ya simu, naomba mtuangalie kwa karibu watu ambao tupo remote area. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mjini mnajenga mpaka ma-flyover nyie nini? Kwa nini wenzenu mmetusahau huko? Mnazungumzia tu viwanja vya ndege sisi havitusaidii. Hivi leo usafiri wa kule ni trekta, namshukuru kijana mmoja anaitwa Muddy Kindindindi wa Ifakara alinunua mabasi yake yanaitwa Muki yakawa yanaenda mpaka Mpanda lakini kutokana na barabara mbovu sasa hivi hayaendi tena, wanasafiri na trekta. Jamani, hivi bado tupo dunia hii ya leo? Mimi naomba Waziri kama ikiwezekana Naibu Waziri umruhusu akimaliza kupitisha hii bajeti twende mimi na yeye tuongozane mpaka kulekule alikofika mwanzoni aone hiyo barabara ndipo atapata uchungu akija ataona kwamba hii hela mliyotenga hapa sio lolote sio chochote. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba tafadhali, hata kama huna mafuta mimi ntawaambia wananchi wa Mlimba wajichangishe tukuletee mafuta twende ukaikague hiyo barabara sasa hivi na watafurahi sana wakikuona. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu ni barabara...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, barabara, Mlimba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hotuba hii ya Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kabisa na kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 75 - 76, naomba kunukuu, nitakwenda pale mwishoni kidogo; “Naomba kutoa taarifa kwamba Serikali inatarajia kuwasilisha katika Bunge lako Tukufu Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Bima ya Afya. Muswada huo una mapendekezo mbalimbali ikiwemo sharti la ulazima wa wananchi wote kujiunga na Bima ya Afya na wale wote wenye uwezo kuchangia bima hiyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kipengele kimenitetemesha mwili mzima nikaikumbuka Mlimba, wananchi watakaolazimishwa kuchangia ikishakuwa sheria ya nchi hii. Mlimba yenye kata 16, yenye kituo kimoja cha afya yaani sitaki hata kusema, ndiyo maana nilikuomba Mheshimiwa Waziri ufike uone mwenyewe. Kama alivyosema Mbunge aliyetangulia kwamba unaonekana una haiba na kweli ndivyo ulivyo, lakini mzigo huu wa Wizara uliyopewa ni mkubwa sana, lakini bila pesa utaishia kulia jinsi kina mama, wazee na watoto wanavyoteseka katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri nimekukaribisha uje Mlimba, mnakwenda tu kwenye yale maeneo ambayo mmeyazoea, naomba mje Mlimba, Jimbo lenye kata 16, vijiji 61, vitongoji mia mbili na zaidi. Mimi nitakupeleka kwenye kitongoji, kutoka kwenye kitongoji mpaka kijiji ni kilometa 20 yaani kutoka kitongojini mpaka katika kijiji kilometa 20 halafu hapo kwenye kijiji hakuna zahanati, unatakiwa uende tena kilometa 30, ukiongeza na 20 zinakuwa 50, mtoto anaumwa umembeba, wakati wa mvua barabara hazipitiki, maji mpaka kiunoni unaweza kuogelea, jamani kama kuna watu wanakufa nchi hii basi ni Jimbo la Mlimba, hali ni mbaya kuliko maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuuliza ni lini katika bajeti hii itatambua kwamba Mlimba kuna wananchi? Bahati mbaya sana Mlimba tulikuwa wachache, lakini leo tumewapokea watu wa aina mbalimbali, kila kabila unaloliona humu ndani liko Mlimba, ndugu zenu wako kule. Kwa sababu gani, Mlimba ni eneo la rutuba, ukipanda ndizi twende, mpunga twende, kokoa twende, ufuta twende, miti usiseme, mahindi twende, kwa nini wasikimbilie kule, kila kitu kinakubali. Gesi ndiyo iko kule, umeme wa Kihansi upo, kuna shida tena Mlimba? Kwa hiyo, watu wameingia wengi lakini huduma sifuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimesimama hapa kuchangia hii hotuba, siwezi nikachangia maeneo makubwa sana ya Kitaifa kwa sababu nina wajibu ndani ya Jimbo la Mlimba. Naomba chonde chonde, mje mtembelee Mlimba, mlinganishe na haya ninayoyasema halafu mtaona wenyewe kama hamkulia huku mimi nawaambia. Mimi wakati wa kampeni nilikuwa nalia, hata nilivyokuwa nasikia ooh, waganga wa kienyeji wanafungiwa, fungieni huku huku, kule watu wanatibiwa na waganga wa kienyeji. Hakuna hospitali, hakuna zahanati, hakuna chochote, kwa nini mtu asiende kwa mganga wa kienyeji. Hiyo huduma mnayosema ya wazee labda mjini huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini dada yangu hapa Mheshimiwa Mollel anasema alikuwa huko Muhimbili, ameshuhudia kwa macho yake mzee amekuja Muhimbili aliambiwa aende akapimwe lakini amekwenda kule laboratory akaambiwa baba shilingi 40,000 ni mzee anatembelea mkongojo. Mheshimiwa Mama Mollel akaingilia kati kwa uchungu, kwa nini mnaacha kumtibu huyu baba, wanasema bila shilingi 40,000 hakuna bure, ikabidi atoe amalipie yule mzee apate matibabu. Sasa hii huduma ya wazee iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Dar es Salaam namna hii Mlimba kuna kitu tena kule? Giza totoro, haki ya Mungu kama hatujapata uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde, mfike Mlimba. Kwa sababu kama kuna kata 16 kituo cha afya kimoja na chenyewe kinademadema, hawana wodi ya wazazi yaani ni aibu kwa Jimbo la Mlimba. Kutoka Mlimba mpaka Ifakara ambapo kuna Hospitali ya Wilaya ama St. Francis ni kilometa 150 barabara zote kama zina makaburi ya watoto kutokana na hayo mashimo, tumewakosea nini? Kule ni hatari jamani, naomba mje muone. Halafu unamwambia ananitania tu, jamani pelekeni vitu kule Jimboni vya Bunge, aah sasa hivi hatuwezi kwenda mvua, kwani tunaoishi kule wanyama? Twendeni hata wakati wa mvua mkaone hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TAMISEMI kama mpo hapa mchukue, haiwezekani vijiji 61 kuna zahanati 18, haiwezekani! Wananchi kule wanapata wapi matibabu! Hali ni mbaya kuliko maelezo! Kina mama wanakufa kule, kina baba wazee wanateseka kule, watoto wanakufa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ukurasa wa 75 mlivyoandika kwamba mnakwenda kuleta bima ya afya lazimishi, Mlimba muitoe katika hayo mambo, hiyo sheria iseme kabisa Mlimba aah aah, tutalazimisha maeneo mengine tu. Kwa sababu haiwezekani, kwanza dawa zenyewe hawapati sasa unalazimishaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, muandae kwanza mazingira ya kuandaa vituo vya afya venye Madaktari, Manesi na dawa za kutosha, mkilazimisha hiyo ni sawa. Msilete sheria kabla hamjaandaa mazingira sahihi ya watu kupata huduma, nendeni mkakague mjiridhishe. Kwa hiyo, mimi naomba hii sheria mmeiandika tu hapa lakini ichelewe kabisa, bado tuko miaka 20 nyuma. Ni nzuri sana kwa sababu nchi za wenzetu wanatekeleza sheria hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichukua takwimu kutoka kwenye halmashauri yangu, nina takwimu hapa na nitakuletea lukuki, kama za TAMISEMI ziende TAMISEMI, kwenye Wizara yako, maana hapa tunapiga, uchungu mwingine, mateso mengine wanatuletea TAMISEMI, ninyi TAMISEMI ninyi, ni matatizo makubwa! Haiwezekani sera inasema zahanati kila kijiji lakini vijiji vyote havina zahanati. Wananchi maeneo mengine wamechangia, wamejenga zahanati, haijamaliziwa, hakuna choo, hakuna mtumishi, hakuna chochote. Kwa nini mnawafanyia hivyo Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina maneno mengi, nasema mje Mlimba mjionee wenyewe kama haya maneno ninayosema ni ya uongo ili watu wapate huduma yao kwa mujibu wa kodi wanazolipa, mtushirikishe. Kambi ya Upinzani wamesema vizuri, lakini sasa Serikali hii hata mkishauri mpango mzuri hapa, basi kwa mpango huu CHF na dawa, ili Wizara ya Afya ipate hela ingizeni hata shilingi 50,000 kwenye mafuta ya magari, uongo, kweli? Tukikubaliana hapa kama REA hela sijui mmeipeleka wapi, ninyi vipi? Yaani hapa hata tukipitisha mpango mzuri wa kukusanya shilingi shilingi kwa Watanzania mnapeleka hela sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niishie hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia hii nafasi nami nipate kuchangia kwenye hii Wizara yetu ya TAMISEMI. Ni Wizara ambayo ni pana, kubwa na inahangaika sana na makundi mengi ya kijamii yaliyoko kijiji, lakini ni Wizara ambayo haina uwezo, yaani kifedha imekuwa hoi, lakini inashughulika na watu moja kwa moja kwenye vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayeongea hapa natokea kwenye vijiji; tena vijiji hasa kule kusikokuwa na barabara, kusikokuwa na maji, wala huduma ya afya, wala kilimo bora wala na kilimo cha umwangiliaji. Ndiyo huko ninakotoka. Kwa hiyo, hata kwenye hivi vitabu wakiandika, wanaenda kuboresha barabara vijijini kwa kuweka zege na nini, mimi nashangaa, wanaboresha wapi? Mijini au vijijini? Kwa hiyo, ni muhimu watakapokuja hapa kuleta majibu ya kila eneo waeleze ni namna gani wataenda kuboresha haya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi sasa, huko nilikotoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, mpaka tunakuja hapa kwenye hili Bunge, ni asilimia 25 tu ya pesa za maendeleo zimepelekwa huko. Sasa nashangaa, tunakuja kupitisha tena, hiyo asilimia 75 mtapeleka lini? Labda mtuambie, kabla hatujamaliza mwaka huu wa fedha mnapeleka lini hizo hela ili tupate maendeleo?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamejenga maboma, lakini Serikali haijamalizia. Mnasema mnaboresha OND, lakini wananchi wameshafanya; Serikali mna mpango gani wa kumalizia hayo maeneo ambayo wananchi wameshafanya kazi ya kutosha? Matokeo yake mvua zinakuja zinaharibu majengo, kwa hiyo, nguvu za wananchi zinapotea bure. Sasa ni vema kila bajeti mkija, hapo muwe na majibu ya uhakika mlifanya nini na kila Jimbo mtuambie mmefanya nini? Hiyo jumla jumla wakati wengine tunaumia huko, haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya mipaka katika vijiji ipo. Kwa mfano, Ofisi ya Waziri Mkuu inajua, TAMISEMI mnajua. Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero; Kijiji cha Ngombo kiko Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, lakini mpaka leo Serikali haijaleta majibu Ngombo inaitika wapi? Matokeo yake mnatuachia ugomvi; Malinyi wanagombana na Kilombero. Naomba mnipe majibu, Ngombo iko wapi ili tupate maendeleo kwa wananchi wa Ngombo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sasa vijiji, tangu mwaka 2014 tulivyoingia kwenye uchaguzi wa vijiji, kuna vijiji viwili havijafanya uchaguzi mpaka leo. Kijiji cha Idandu na Kijiji cha Miomboni. Majibu ya Serikali mnasema kwamba eti kule kuna uwekezaji; mimi nashangaa, hivi mahali kwenye uwekezaji ndiyo watu hawachagui uongozi wao? Kwa hiyo, wale watu wanataabika, maendeleo yao hawajui wanafanya nini? Naomba majibu ya Serikali, ni lini mtaruhusu katika vile vijiji watu wafanye uchaguzi? Ni aibu, ni Serikali ambayo inasema ina utawala bora, lakini kule katika vile vijiji kwani wanakaa wanyama? Nataka majibu ya Serikali
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mkoa kuisimamia Halmashauri, sasa nimpe taarifa Waziri wa TAMISEMI kama hajui. Katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilombero, wananchi wa Wilaya ya Kilombero tumenunua gari la Mkurugenzi, lakini gari hilo nakwambia mpaka sasa ni miezi sita liko kwa Mkuu wa Mkoa. Leo mnasema Mkoa usimamie Halmashauri, utasimamiaje wakati wenyewe ndiyo unakwenda kubembeleza unachukua gari kwenye Halmashauri? Hawa watu wataweza wapi kuisimamia Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini msiboreshe? Kama kweli ninyi ni waungwana, kwa nini mnaishia kununua ndege, hamboreshi Ofisi za Wakuu wa Mikoa ili waende wakasimamie hizo Halmashauri? Matokeo yake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro hana gari, amechukua gari la Kilombero, moyo unaniuma na wananchi wa Kilombero tumenunua lile gari kwa pesa zetu? Pelekeni gari la Mkuu wa Mkoa pale Morogoro ili gari letu lirudi Kilombero likafanye kazi. Miundombinu yetu ni mibovu, tunahitaji gari, acheni ubabaishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo namwambia hivi, ajue nataka majibu ya Serikali apige simu kule atajua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya awali.
Usicheke hayo ndiyo mambo, mnatuumiza sana ninyi, haki ya Mungu! Yapo maneno mengi kwenye vitabu, lakini utekelezaji huko chini hamna.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya awali na msingi; sawa mnasema elimu bure, lakini nendeni field mkaone. Haki ya Mungu, watoto 400 wa chekechea na darasa la kwanza wapo nje, Walimu hakuna. Hii nini? Kwa nini hamwajiri Walimu? Tatizo liko wapi? Leo nimeona kwenye vyombo vya habari eti Mheshimiwa Rais, wale Madaktari wa Kenya Wamekataliwa, ninyi ndiyo mnasema mnaajiri. Ninyi mna matatizo gani? Kwani ninyi hamna mpango wa kuajiri mpaka wakataliwe Kenya ndiyo mwajiri?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mnasema mnapeleka Walimu wa Sayansi katika shule zetu, lakini mkae mkijua, Walimu wengi hata wa masomo ya kawaida, wamepungua katika maeneo ya Vijijini, labda wamejaa Mjini. Tunataka ajira kwa Walimu, tunataka ajiwa kwa Madaktari, tunataka ajira kwa Manesi. Mtahakiki mpaka lini? Hii ni Serikali ya kuhakiki! Haiwezekani! Leteni ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, uendeshaji wa Miji na Vijiji. Nilimwomba Mheshimiwa Jafo, hebu tembelea Jimbo la Mlimba. Kwa nini hamtembelei? Ninyi mkifika Ifakara, ndiyo mnaona mmefika Wilaya ya Kilombelo, lakini mjue kuna kilometa 265 kutoka ifakara mpaka kufikia Jimbo la Mlimba. Kwa nini hamji? Mnaogopa nini? Mnaogopa barabara kwa sababu mbaya! Njooni, tena vizuri mje wakati wa masika mwone kama hamkulala njiani siku tano na magari yenu hayo. Fikeni kule, nendeni mkahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba lina miji kama sikosei miwili au mitatu. Mlimba yenyewe, Ngeta na Chita, lakini mpaka leo hakuna mwendelezo, hakuna upimaji watu wako hovyo hovyo, hamtusaidii. Yaani Mlimba inastahili kuwa Halmashauri, Kilombelo na Ulanga na Malinyi inastahili kuwa na Mkoa, lakini leo mnatuchakaza. Sisi watoto wa wakulima hamtupi mkoa, hamtupi halmashauri, hamtupi miji, mna matatizo gani? Tunahitaji Halmashauri ya Mji wa Mlimba, tunahitaji Mkoa wa Morogoro ugawanywe mara mbili uwe Mkoa wa Kilombero. Tumeshateseka sana, sasa tunasema basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora uko wapi? Mkuu wa Mkoa kuteremka kwenye Kijiji, kuna mkutano mkubwa wa wananchi kutoka Kata mbalimbali, halafu anatangaza: “nimevunja Serikali ya Kijiji.” Huo ndiyo utawala bora? Wapeni Semina Elekezi, wanaenda kutuvuruga vijijini.
Hiyo imetokea kwenye Kijiji cha Ikule; Kata ya Mngeta Mkuu wa Mkoa alienda akiwepo na Mheshimiwa Waziri Mwinyi huyu hapa. Hivi alivyofanya vile Mkuu wa Mkoa pale ni sahihi; kwenda kuvunja Serikali ya Kijiji kwenye Mkutano wa wananchi Kata yote? Ni aibu! Waambie, wapeni elimu; wanatutesa wananchi. Wapeni Semina Elekezi, kuna umuhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwenye hiyo hotuba ya Kambi ya Upinzani naiunga mkono. Huyu Mheshimiwa Mama Mollel waliyempiga hapa, alistaafu kazi miaka mitatu iliyopita, mtu asiyekuwa na takwimu, yaani usipofanya utafiti huna right ya kusema wewe. Leo anampiga Mheshimiwa Mama Mollel, eti amestaafu siku tano; achana na hizo habari wewe! Mengine kuna watu wamekuwekea kiporo, watakuja kumalizana na wewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya vijijini kwetu ni mbaya; mnapoenda kuzuru maeneo na Waziri Mkuu anajuwa, kwenye kile kijiji mnasema kuna uwekezaji wa sukari, lakini mpaka leo wananchi wanahangaika. Vijiji havijafanya uchaguzi. Nendeni sasa mkalete hao wawekezaji, wananchi wapo tayari kuwa wakulima wa nje ili wapate maendeleo yao.
Mheshimiwa Simbachawenye naongea na wewe kila siku; tunahitaji, ingawa unasema sasa hivi huyu jamaa hataki utawala mpya. Sisi tumeshaumia sana watu wa huku; hivi wewe Jimbo moja lina kilometa karibu 300, leo linakwenda ku-report Makao Makuu ya Wilaya kilometa 265, hamwoni kama mnawatesa wananchi wale?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji utawala, tunahitaji Halmashauri ya Mji wa Wilaya ya Mlimba; tunahitaji Miji midogo ikaendelezwe; na hizo bajeti mnazosema, tunahitaji tuzipate; Vituo vya Afya ndiyo usiseme, balaa. Juzi juzi hapa tumepata shilingi milioni 500 kuendeleza Kituo cha
Afya cha Mlimba lakini hakitoshi, kwa sababu Jimbo lina kilometa zisizopungua…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mara ya kwanza kuongea katika Bunge hili la Kumi na Moja, nilikuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa miaka mitano. Kwa kutambua kwamba wanawake tunaweza bila kuwezeshwa, nikaenda kugombea Jimbo la Mlimba, na wananchi wa Mlimba bila kujali itikadi zao walinipa kura za kutosha na sasa ni Mbunge wa Jimbo jipya la Mlimba ndani ya Wilaya Kilombero Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nawashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Mlimba Mabibi na Mabwana na Wachungaji na Mashekhe waliokuwa wananiombea bila kujali itikadi yangu, bila kujali dini yangu, na jinsia yangu, nasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mara ya kwanza nachangia nikiwa Mbunge wa Jimbo kwenye haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Naomba nijikite kwenye mambo kadhaa, ambayo nikijikita nayo, nikizungumza hapa nitakuwa nawasemea na wananchi wa Jimbo la Mlimba na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango kwa sasa umekuja kama mapendekezo na natarajia haya ninayoongea hapa na Wabunge wengine wanayoyaongea, basi katika mpango kamili unaokuja basi kutakuwa na vionjo ambavyo sisi kama Wabunge tumetoa mapendekezo yetu na mpango wakauchukua ili kwenda kupatikana kwenye hiyo bajeti inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Utawala Bora; Hivi ninavyokuambia Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijaapisha Madiwani wake, hivi ninavyokuambia Halmashauri zingine zote zimeshaanza kukaa na kuangalia bajeti ili waingize kwenye Bajeti Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijawahi kufanya kikao chochote, Madiwani hawajaapishwa, uchaguzi haujafanyika, eti kwa sababu tu kwa kazi tuliyofanya ndani ya Wilaya Kilombero CHADEMA, UKAWA tumepata Madiwani wengi na Wabunge wote tumebeba, sasa ni kigugumizi Serikali ya Chama cha Mapinduzi, inashindwa kupitia Waziri wa TAMISEMI anashindwa kuruhusu wananchi wa Kilombero wapate Wawakilishi wao. Ni kilio, ni kizungumkuti, hapa hamna utawala bora bali kuna wizi, utapeli, uliokithiri kipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maendeleo ya Wilaya ya Kilombero yatarudi chini, Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo mawili, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero, leo Mbunge Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, Waziri wa TAMISEMI ameandika barua, eti asiwe mpigakura ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, shame! Hiyo haikubaliki. Sasa, katika utawala bora nataka mtuambie, Wilaya ya Kilombero mnatuweka wapi, tuko Tanzania au tuko nje ya Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti inayokuja ya Wilaya ya Kilombero itaidhinishwa na nani ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero? Naomba majibu ya Serikali maana hapa hamna utawala bora. Hili ni jambo kubwa sana kama ulikuwa hulijui ni aibu kwa Taifa hili, ni aibu Serikali kujisifu kwamba ina utawala bora lakini kuna ukandamizaji uliopitiliza, wanatutolea Wabunge wa Viti Maalum kutoka Dodoma eti waende wakaape Kilombero, wanaijua wao Kilombero? Matatizo ya Kilombero tunayajua sisi hawezi kujua mtu mwingine. Kilombero hatuna barabara, Kilombero kuna migogoro ya ardhi, Kilombero hakuna maji, Kilombero pamoja tunazalisha umeme kwenye vituo viwili, Kihansi na Kidatu, lakini vijiji vingi havina umeme. Mnatutaka nini wananchi wa Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo halikubaliki, katika utawala bora naishia hapa ingawaje kuna mambo mengi, kwa sababu katika utawala bora na haki za binadamu, tulitakiwa tuwe na kituo cha Polisi Kilombero, lakini hakuna Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero tangu uhuru. Wilaya ya Kilombero Askari wamejibana kwenye kituo cha Maliasili, hivi wakati wa mafuriko Askari wanaogelea kama bata pale, kwenye mpango nataka tujue ni namna gani Wilaya ya Kilombero, tutapata kituo cha Polisi, cha uhakika kilichojengwa na Serikali hii ili wananchi wapate huduma zao na haki zao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba ni kubwa lenye Kata 16, hakuna kituo cha Polisi, Askari wamejibana kwenye kituo kidogo kwenye ofisi za TAZARA. Mnatutaka nini wananachi sisi, mnatutaka ubaya kwa sababu gani, tumewakosea nini, lakini ukiachilia hiyo, pale pale hakuna Mahakama ya Mwanzo. Leo mahabusu wakipatikana ndani ya Jimbo la Mlimba wanawekwa Idete, haki za binadamu zinavunjwa hata miaka miwili, kwa sababu hawana usafiri wa kuwapeleka Mahakamani, hawana Mahakama ya Mwanzo, huu utawala bora na haki za binadamu ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango u-reflect ni namna gani mtatuboreshea katika utawala bora ndani ya Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi oevu, utawala bora uko wapi? Leo ninavyoongea kuna kesi Namba 161 ya mwaka 2012, wananchi, wakulima na wafugaji wameipeleka Serikali Mahakamani, hasa Wizara ya Maliasili na Mahakama Kuu ikatoa order kwamba wale wananchi wasibughudhiwe kwenye lile eneo la oevu kwa sababu, walivyoweka mipaka kule hawakuwashirikisha wadau na Wizara ilikubali inakwenda kurekebisha mipaka, tangu mwaka 2012 mpaka leo! Leo wananchi wanashindwa kulima kule! Hii njaa itaingia mwaka huu! Watu wanapigwa, wafugaji wanachukuliwa pesa zao! Hawapewi risiti, nimelalamika, nimekwenda kwa Waziri Mkuu, nimekwenda kwa Waziri wa Maliasili, Mkurugenzi wa Wanyamapori, hivi ninyi mnatutaka nini sisi? Kwa nini mnatuonea namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wasukuma wako kule wafugaji na makabila yote ukienda ndani ya Wilaya ya Kilombero Jimbo la Mlimba wapo kule, kuna uchakataji, utafutaji wa gesi, wananchi hawajui! Wanakuja tu na magari yao wanaondoka kwa nini msitoe taarifa kwa wananchi kwamba mnakwenda kuchakata kule kutafuta gesi na mafuta?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Mpango utuambie ni namna gani tunaboresha masuala mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilombero, hususan Jimbo la Mlimba. Najua kuna mradi mkubwa wa upimaji ardhi, kama nilivyoongea na Mheshimiwa Lukuvi, lakini mradi huo pamoja unavyokuja sawa, Wilaya ya Kilombero na Ulanga, lakini hivi sasa wakulima wameshindwa kulima! Mnataka mwaka huu tukale wapi? Mnataka mtuletee chakula cha msaada sisi Mlimba, hatukubali! Aisee muda hautoshi! Mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, balaa! Mnasema eti katika Mpango, Mheshimiwa Mpango naomba unisikie, mnasema tu reli ya kati, mmeisahau TAZARA? TAZARA mnaiboreshaje? TAZARA mnaifanyaje? Wafanyakazi hawalipwi! Reli shida! TAZARA mliijenga kwa gharama kubwa wakati wa Nyerere, leo mnaiua kwa sababu gani? Nataka Mpango u-reflect ni namna gani mtaboresha barabara, reli ya TAZARA, Mpango uzungumzie barabara ya kutoka Ifakara mpaka Mlimba, Mlimba mpaka Madeke-Njombe mtaiboreshaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ghala la chakula liko Jimbo la Mlimba. SAGCOT, kuna kilimo kikubwa cha mpunga pale KPL (Kilombero Planting Limited), malori yanapita pale yanye tani 30 kila siku yamebeba mchele, barabara hamna! Leo kwenye Mpango hakuna hata ile barabara hamuizungumzii! Naomba mzungumzie hiyo barabara.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Susan Kiwanga, Taarifa hiyo unaikubali au vipi?
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siikubali.
MWENYEKITI: Haya, malizia dakika yako moja!
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimpe tafsiri kwamba, shame, maana yake aibuuu! Kwa Taifaaa! Hiyo ndiyo habari ya sasa. Halafu wewe tuna wasiwasi na uraia wako!
Mheshimiwa Mwenyekiti, linda dakika zangu. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Ulikuwa na dakika moja tu.
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mpango uzungumzie kuhusu barabara ya kutoka Ifakara – Mlimba, Mlimba mpaka Madege, Njombe, hili ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mpango uzungumzie masuala ya elimu; leo ninavyozungumza kuna shule moja ya Tanganyika mwaka uliopita hakufaulu hata mwanafunzi mmoja wa darasa la nne! Elimu kule siyo nzuri sana, nitawapa takwimu baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; pamoja na kuwa Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba lina mito 38, ilikuwa mpaka 49 lakini maji hakuna! Naomba Wizara ya Maji ifanye mkakati, sisi hatuhitaji visima, mkaboreshe ile mito, ili tupate maji. Kama inatoa umeme kwa nini maji ya kunywa safi na salama tusipate?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwape vyanzo vya mapato, kimoja tu! Naomba mfanye pilot area Dar-es-Salaam kuna umeme, hebu hamasisheni mtu ukienda dukani leo mtu anakuhamasisha, nikupe risiti ya TRA au nikupe ya mkono? Hii hapa ina kodi, hii hapa haina kodi! Hivi ni nani Mtanzania leo atakubali yenye kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wekeni mfano mzuri kwa pilot area ambayo ina umeme kwamba, wale wote Watanzania na mtu yeyote atakayenunua kwa risiti ya umeme ile ya TRA, baada ya muda fulani, mwaka mmoja, mnampigia hesabu amelipa kodi kiasi gani halafu mnamrudishia kitu kidogo! Mtaona kama watu hawatadai hizo risiti madukani; hicho kitakuwa chanzo kikubwa cha kukusanya kodi ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia Mpango huu kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa Mpango huu uliowasilishwa Bungeni kuhakikisha unaendana na hali halisi ya ukusanyaji kodi na udhibiti wa mapato hayo. Mpango huu ujikite kuwezesha Mashirika ya Umma kama STAMICO, TPDC, TANAPA, TAZARA, ATC, TRL na kadhalika yajiendeshe kibiashara ili kuchangia katika bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu unapozungumzia miundombinu napenda kuona ni namna gani Serikali:-
(i) Itaboresha TAZARA.
(ii) Barabara ya kutoka Ifakara-Mlimba hadi Madeke Njombe ionekane kwenye bajeti hii ili wananchi ambao asilimia 90 ni wakulima na ni eneo linatoa mazao mengi kama mpunga, ufuta, ndizi, cocoa, miti, ng‟ombe na kadhalika. Jimbo hilo ni jipya ndani ya Wilaya ya Kilombero ambapo barabara hiyo ikijengwa itaunganishwa na Mkoa wa Njombe.
(iii) Jimbo la Mlimba halina barabara, halina Kituo cha Polisi, halina hospitali ya uhakika, halina Mahakama isipokuwa moja ndani ya Kata 16. Halina maji safi na salama ingawa lina mito mingi mikubwa ukiwemo na Mto Mpanga. Hali ya shule za msingi, awali ni tete sana, hakuna Chuo cha Ufundi wala Walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi Mpango huu na bajeti hii ione namna bora ya kuingiza hela kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishashauri Bunge lililopita na naendelea kushauri namna bora ya kuhamasisha Watanzania kusaidia Serikali kukusanya kodi. Ni hivi, Dar es Salaam uwe mkoa wa majaribio ili ukifanikiwa uende nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila anayenunua bidhaa ahakikishe anapewa risiti ya TRA (electronic receipt) ambapo ataitunza na Serikali itaweka kiwango maalum cha fedha alizotumia na mwishoni mwa mwaka mtunza risiti huyo atarejeshewa kiasi fulani cha fedha alizotumia kama motisha. Ni muhimu Serikali ikajifunza toka nchi za wenzetu mbinu za ukusanyaji kodi. Haitoshi kusema tu, Watanzania daini risiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliwezeshe Shirika la Umma STAMICO kwa kuwapa maeneo mapya ya kuchimba madini ya dhahabu na kadhalika ili ichangie pato la Taifa. Isiwe kama ilivyo sasa Shirika hilo la STAMICO linarithi migodi iliyoachwa na wawekezaji na kushindwa kuzalisha madini matokeo yake linapoteza pesa. Mfano, Mgodi wa tanzanite, Kiwira, Tulawaka na kadhalika, hata ukiangalia ni kiasi gani cha fedha zinazochangia kwenye bajeti ni sifuri, sana sana Serikali inazidi kulipa watumishi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Mpango huu umedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara hivyo katika maboresho hayo kuwepo na msisitizo wa kujenga Barabara ya Ifakara-Mlimba-Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Napenda kupata majibu ya Serikali, je, unawezaje kuzalisha vyakula kwa wingi na kuingiza fedha kwenye miradi ya kilimo bila hali hiyo kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu kama barabara na kadhalika. Ni lini Wizara hii itashirikiana na Wizara ya Ujenzi ili kuleta matokeo mazuri kwa wananchi hasa wa Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua Serikali inachukua hatua gani kwa Wawekezaji wa KPL wanaolima eneo dogo la shamba na maeneo mengine wanawakodisha wafugaji na wakulima. Pia kuhusu uhamishaji wa ubia na mali zilizopo na hadi sasa mali hizo hazipo, je zimepelekwa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata majibu ya Serikali ni lini itamaliza migogoro iliyopo kwenye maeneo ya uwekezaji mfano Rupia, Ngalimila, ambako yameonyeshwa kwenye hotuba ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itawasikiliza wafugaji waliopo Jimbo la Mlimba na kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jimbo la Mlimba lina mazao mengi ya biashara kama cocoa, ufuta, ndizi, mpunga, mahindi na kadhalika, ni lini Serikali itawapa elimu wakulima hao pia kuanzisha dirisha la mkopo kwa wakulima ili wakope na wasaidiwe utaalam wa kuboresha kilimo cha mazao hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kaya takribani 400 zenye hekari karibuni elfu moja zimeathirika na madawa ya Mwekezaji KPL, (kwa hisia zao) na Mheshimiwa Waziri ulifika na kuwapa matumaini utapeleka majibu ndani ya siku ya 21 tangu tarehe 4/5/2016 na hadi leo tarehe 4/5/2016 na hakuna majibu na wananchi hawatavuna kabisa, msimu wa kilimo umepita. Je, Serikali iko tayari sasa kupata idadi kamili ya watu walioathirika na kupeleka chakula cha msaada kwani hali ya chakula ni mbaya? Ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na leo niko hapa nawakilisha Bunge kupitia Jimbo la Mlimba kwa tiketi ya CHADEMA. Ahsante sana wananchi wa Mlimba kwa kunipa heshima hii na ahsante Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kuniteua kuwa Mbunge bila kujali jinsia yangu na nitawakilisha na nitatoa heshima kwa chama na nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitaunga mkono Kitaifa Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara hii. Sasa kwa kuwa chama changu kimeniamini na kunipeleka Jimbo la Mlimba, niwatendee haki wananchi wa Jimbo la Mlimba kwa sababu ni Jimbo jipya na mambo mengine yote yanakwenda kiupya upya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali Bungeni na nikapata jibu zuri kutoka kwa Wizara husika kwamba mwezi Juni kwenye ile barabara ya Ifakara mpaka Madeke-Njombe, inayounganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe inakwenda kumalizika kwa ule utaalam wanasema feasibility study. Sasa, baada ya feasibility study wananchi wengi wakisikia wanadhani ikimalizika hiyo ndipo wanakwenda kujenga barabara, kumbe kuna ile detailed design ambayo itahusika na mambo ya michoro, ujenzi, gharama halisi na mambo kadhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kupata majibu ya Serikali, inifahamishe na iwafahamishe wananchi, baada ya kumalizika mwezi wa Sita hiyo michoro ya ujenzi na gharama halisi ya ujenzi ni lini Serikali itakwenda kufanya na itachukua muda gani? Baada ya hapo je, Mkandarasi Mshauri atapatikana wakati gani na ujenzi wa barabara hii utaanza lini? Pia je, Serikali imejiandaa vipi kutenga fedha katika kujenga barabara hii yenye urefu wa kilometa 124.2. Nikipata majibu haya ya Serikali itanipa furaha na itanipa kujiandaa ni namna gani barabara hii itakwenda kujengwa, siyo kila wakati nilete maswali Bungeni, maana nitajua ni muda gani barabara hii inaweza ikaanza kujengwa. Naomba nipate majibu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia katika kitabu cha randama cha Waziri nimekwenda kwenye ukurasa wa 100 inaonyesha miradi ya maendeleo ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 111, miradi inayotekelezwa kwa miradi ya barabara Mlimba haimo. Nimekwenda ukurasa wa 116, mchanganuo wa miradi ya barabara za mikoa inayoendelezwa kwa kutumia Mfuko wa Barabara 2016/2017, imo Ifakara – Tawete – Madeke including crossing of Mngeta. Si Mgeta, kwenye kitabu chenu mmeandika Mgeta, mgeta si Mlimba, Mgeta iko Morogoro, iko Mvomero, naomba mrekebishe wekeni Mngeta, siyo Mgeta.(Makofi)
Sasa nimekwenda ukurasa wa 136, nikaona matengenezo ya muda maalum kutumia fedha za Mfuko wa Barabara Mlimba hakuna. Nimekwenda ukurasa wa 139 mpaka 147, barabara za mikoa za changarawe, udongo Ifakara – Taweta – Madeke, kilometa 57.59 makadirio mmetenga milioni 594, hapa kuna shida! Hii barabara naijua, naipita mara nyingi, matengenezo hayo bora mngechanganua, kama ni changarawe weka changarawe kilometa kadhaa, kama udongo weka udongo kilometa kadhaa. Mkiweka jumla hivyo hii barabara inatengenezwa kwa udongo asilimia 100. Kwa hiyo, ni vyema kuchanganua ili tujue kilometa ngapi changarawe, kilometa ngapi udongo ili wananchi wapate kufuatilia na mimi mwenyewe kama Mbunge nipate kufuatilia wakati napita hiyo barabara maana tunadanganywa sana na wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 157 mpaka 163, maeneo korofi; kutumia fedha za Mfuko wa Barabara za Mikoa Mlimba hakuna, eeh! Hapo ndipo nikashangaa. Hii barabara muda wote haipitiki na mpaka mje kujenga itachukua miaka kadhaa. Sasa kama hamtengi pesa katika barabara hii katika maeneo korofi huyu Mkuu wa TANROAD Mkoa wa Morogoro mnayempigia simu kila kukicha wakati matatizo yanapotokea atapata wapi hela za kwenda kutengeneza maeneo korofi katika barabara ya Ifakara – Mlimba mpaka Madeke-Njombe? Naomba mrekebishe vitabu vyenu, iingizeni na hiyo barabara ili tunapopata matatizo tupate kutibu haya maeneo korofi. (Makofi)
Barabara za mikoa na madaraja mmeweka, tuna madaraja saba, yaani ni hivi, katika Mkoa wa Morogoro na nchi hii, kama kuna mkoa wenye madaraja mengi basi ni Morogoro. Hata mkiangalia kwenye ile list ya madaraja utakuta tumekwenda mpaka 291, hakuna mkoa mwingine Tanzania wenye madaraja mengi. Madaraja hayo ukiangalia mengi yako katika Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba, kwa hiyo, ni bora mtuangalie kwa umakini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na mambo hayo, ngoja nieleze hali halisi ya Jimbo la Mlimba, najua Waziri hajafika, Naibu Waziri hajafika, naomba mfike mkaangalie ili mnapopanga mipango yenu muone ni namna gani mtasaidia Jimbo la Mlimba. Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha mpunga, mradi unaitwa KPL, uwekezaji, karibuni hekta elfu tano na kitu! Magari yanayotoka pale kupeleka mchele si chini ya tani 30 na barabara hiyo ni ya udongo. Kwa hiyo, muone hali halisi ya Jimbo la Mlimba na ni namna gani mtaiwekea, kama barabara zitapelekwa kwenye eneo la uwekezaji, basi Mlimba ingepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Mlimba lina mradi mkubwa wa umwagiliaji pale Kijiji cha Njagi, wasilianeni na watu wa Idara ya Umwagiliaji wa Kilimo. Kuna mradi mkubwa, Serikali inaingiza mabilioni ya fedha, sasa kama hatuna barabara ina maana hizo hela mnazowekeza Serikali ni bure. Naomba mlipe kipaumbele Jimbo la Mlimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba kuna kilimo kikubwa cha ndizi, kokoa, ufuta, kila aina, kuna mradi wa umeme Kihansi, kuna mradi wa RUBADA, unakwenda kulimwa kule katika Kijiji cha Ngalimila, hekari na mahekari. Hebu angalieni miradi inayopelekwa Mlimba na hali halisi ya barabara, barabara ni mbovu, hazipitiki mwaka mzima, sasa utajiri wa Mlimba na kuhusu miundombinu haifanani kabisa, naomba muipe kipaumbele.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika masuala ya usafiri wa treni ya TAZARA, ingekuwa treni ya TAZARA imeimarika angalau wananchi wangepata fursa ya kusafiri, lakini TAZARA bado iko kwenye mgogoro mkubwa, wafanyakazi wa TAZARA wako kwenye shida kubwa. Ni namna gani mafao yao, ni namna gani mishahara yao, kwa kweli, naomba muangalie suala la TAZARA hasa katika Jimbo la Mlimba, imepita karibuni jimbo zima, wapeni mafao yao, imarisheni reli, najua itachukua muda mrefu, basi muwaimarishe, muwape mafao yao ili wananchi wale wapate kuishi maisha yanayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano, nimekwenda nimeangalia katika kitabu cha mawasiliano ukurasa wa 18, ni kweli mmesema, kuna kata mbalimbali ambazo hakuna mawasiliano, lakini mmesema mnara haujawashwa, naona sasa, ni vyema mkawashe, kwa sababu hatuna barabara, simu hatuna, jamani, sisi tuko kwenye dunia gani? Naomba sasa mtuimarishie mawasiliano ya simu, mpeleke minara, muharakishe ili tupate mawasiliano ya barabara, maeneo korofi tupate hela na vilevile mawasiliano ya simu ili yaani ni shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ukiona akinamama na watoto wanakufa, basi wanatokea Jimbo la Mlimba kwa sababu hakuna barabara, hospitali kubwa hamna. Matatizo ni makubwa mno. Naomba mtembee, mje katika Jimbo la Mlimba muone hali halisi ili wakati mwingine mnapokuja na bajeti muiangalie kwa jicho la huruma, jicho la kweli katika Jimbo la Mlimba ili tupate maendeleo na sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi, mambo mengine nitaleta mwa njia ya maandishi katika ofisi yako, maana mnakosea majina ya maeneo yangu na vijiji, ili muone kwamba mwaka ujao nikija angalau nije sasa na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa busara na hekima kwa kunipatia angalau hizi dakika tano na mimi nipate kuzungumzia masuala kadhaa ambayo yananikera katika maisha ya Watanzania, hususan Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kwa makini hiki kitabu cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, muda hautoshi, lakini kuna mambo mengi ambayo yanaizingira nchi yetu. Kwa mfano, ukurasa huu wa 33 wanasema umuhimu wa uzalishaji wa mbegu bora nchini, sasa katika Wilaya ya Kilombero pale Ifakara tangu mimi sijazaliwa kuna kituo cha utafiti Katrin pale Ifakara, lakini mimi sijawahi kuona katika maisha yangu matokeo ya Kituo hiki cha Katrin kwenda angalau katika Wilaya ya Kilombero tu siyo Tanzania, kwenda kuwaelimisha wakulima ni mbegu gani sahihi wanatakiwa watumie na kuna magonjwa yanayokabili mpunga na kile kituo kinasema kinafanya utafiti pamoja na mpunga, lakini wananchi wa Wilaya tu ya Kilombero hawajafaidika. Sasa sielewi, Serikali naomba mtupe maelezo kwa nini kituo hiki hakina matokeo chanya? Ama hamuwapi hela au kuna kitu gani, yaani tunasikia tu lakini hatuoni faida yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi ya mpunga; wakati nakuja Bungeni nikapishana na Waziri tena nikasikia na wananchi Waziri anakuja wapi Mngeta, KPL, anakuja kufanya nini huyu kwa wawekezaji, amekwenda kule usiku kwa usiku, nikampigia simu akasema hata saa moja nitafika. Kaenda usiku wa manane, kaenda kuangalia KPL, kaenda kuangalia ghala la chakula, sijui ndiyo uliambiwa ufanye utafiti wa chakula kiko wapi, watu wanasema mna njaa ninyi hamna, lakini usiku kwa usiku mnaingia pale mnaenda kuangalia ghala la chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, KPLni eneo ambalo linazalisha mpunga na mahindi, sasa nauliza hivi, hivi akiba ya chakula ni kwa mahindi tu, je mpunga sisi tunaolima mpunga hiyo siyo akiba ya chakula, kwa nini Serikali hamuweki katika mpango kununua mazao mbalimbali ya chakula kama mpunga. Mmedharau sana lakini ndiyo kilimo ambacho kipo katika nchi hii. Kwa hiyo hata kwenye upungufu wa chakula mnaweza mkapeleka mpunga watu wapate kula. Sasa nataka majibu ya Serikali, je mpunga lini mtauingiza katika bajeti upate kununuliwa kwa ujumla? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masuala ya maji, maji Kilombero na Jimbo la Mlimba yanatokea wakati wa mafuriko, lakini mafuriko yakiisha na maji yanaondoka, lakini kuna mito ya ajabu. Sasa Wizara ya Maji hebu chukueni angalau kuwe na Wilaya moja ya mfano, maana kila Mbunge hapa akisimama maji, hebu chukueni hata Wilaya moja ya mfano muoneshe kwamba mmefanya kwa asilimia fulani na angalau Mbunge mmoja akifika hapa awapongeze, basi muende kwa awamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali njooni Kilombero ambako ni ghala la chakula, kuna mito karibu 39 lakini wananchi wa Kilombero hawana maji, wananchi wa Mlimba hawana maji, naomba mje. Naibu Waziri wa Maji ameahidi akihamia Dodoma baada ya Bunge hili atakuja kutembelea Jimbo la Mlimba, tumuoneshe miradi mbalimbali ya umwagiliaji na maji ya kunywa, miaka na miaka hela zinaingia lakini miradi haiishi, naomba mje mtagundua ufisadi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, kuhusu wafugaji na wakulima. Wafugaji na wakulima ni kero ndani ya nchi hii, lakini hawa wote wanategemeana, mfugaji anafuga mkulima analima. Hawa watu wanaowagombanisha ni Serikali kwa kutokupanga mipango bora ya ardhi ili kuwatengea maeneo wafugaji wafuge na wakulima walime, hawa wote wanategemeana, lakini katikakati kuna Serikali ndiyo inayoleta uchonganishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Kilombero…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono Hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni. Naomba Serikali ione haja ya kuwaokoa Watanzania wanaoishi Wilaya ya Kilombero, Jimbo la Mlimba ambako jimbo zima pamoja na kuwa na miundombinu mibovu lakini hakuna huduma ya uhakika ya Mahakama. Hivyo kupelekea watu wengi kukaa mahabusu kwa kukosa usafiri ama mashahidi kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, zaidi ya kilometa 260 hadi Mahakama ya Wilaya iliyopo Ifakara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Jimbo la Mlimba; pili, tupatiwe mahakama Jimbo la Mlimba; na tatu Mahakimu waajiriwe ili haki zipatikane.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
HE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nishati ya mkaa holela ni hatari kwa ustawi wa nchi yetu. Tukisubiri gesi au umeme itatuchukua karne nyingi hadi kufikia wananchi wote kuachana na mkaa wa kuni.

Hivyo basi, kwa kuwa tangu mwaka 2012 kuna shirika linalojishughulisha na mafunzo kwa wanavijiji vipatavyo 30 vya Wilaya za Kilosa, Morogoro na Mvomero uchomaji wa mkaa endelevu kwa kutenga misitu ya kuchoma mkaa. Shirika hilo linafadhiliwa na watu kutoka nje ya nchi na tija ni kubwa na ndiyo mkombozi wa misitu yetu. Hivyo Serikali itenge bajeti ya kuwezesha Halmashauri kufundisha miradi ya mkaa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda kupata majibu ya Serikali kuhusu madhara wanayopata wananchi wa Jimbo la Mlimba, kata ya Utengule na Msagati kwa kuchomewa nyumba, vyakula na kadhalika. Jambo hilo linafanywa na wamiliki na kitalu cha uwindaji (Kilombero North Safari). Tumefuatilia sana kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ambapo ufumbuzi haujapatikana wa kuainisha mipaka ili wananchi waishi kwa amani katika vijiji vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kuna timu ya pamoja iko Wilaya ya Malinyi na Ulanga inarekebisha mipaka ya eneo oevu (Ramsar Site) ambao umeleta usumbufu kwa kuwa hawashirikishi wananchi na kuweka mipaka upya na hata wanapowashirikisha hawafikii muafaka, kwani wanalazimisha mipaka.

Hivyo basi, kazi hiyo inayoendelea huko haina tija bali ni kukuza migogoro. Ushauri wangu, naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara Mlimba na maeneo yote ya Bonde oevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupata majibu ya Serikali, ni kwa nini ndani ya Bonde la Oevu mmeacha ng’ombe wengi tena inasemekana ni ng’ombe wa viongozi? Badala yake mnawanyanyasa wafugaji katika vijiji na kuwaacha wenye makundi makubwa ya ng’ombe wakiharibu Bonde la Kilombero huku mkipokea misaada ya fedha toka nje kwa madai mnahifadhi ardhi oevu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na kuwa tutaipitisha lakini matumizi ya hizo pesa mpaka leo mimi sijajua. Kwa sababu hali ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi baadhi yao, sijui wanasema wanapata maagizo, kwa hiyo, hawafuati misingi yao, maelekezo na kanuni na maadili ya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo nimeathirika na utendaji wa Jeshi la Polisi, baadhi yao. Utakuta mkubwa kabisa eti anakuita, unasalimu amri unaenda kituo cha polisi, ukifika pale umesimama tena askari mwanaume anakupiga bonge la bao, yaani sijui wakoje mimi hata sielewi.

Hivi ukatili huu hawa watoto waliozaliwa na mwanamke kama mimi wanautoa wapi?

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo neno la shetani nalitoa lakini hiyo message imeshafika. Kwa sababu kazi ya shetani ni kufanya mambo kinyume na binadamu na Mwenyezi Mungu anavyoamuru, nalitoa hilo neno la shetani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uharamia huu unaofanywa na baadhi ya maaskari wanaochafua Jeshi la Polisi lazima tuuzungumze, hatuwezi kufumba macho. Kwa sababu tusipozungumza hata ukimwendea Mheshimiwa Mwigulu ukamwambia bwana kule kuna mambo haya anasema mambo mengine wanafanya kule mimi sijui. Huyu hapa anasema kwa sababu tunamwendea na tunampigia simu tunamwambia. Sasa leo nimepata nafasi kwa sababu imekuja bajeti lazima niseme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya mimi kama kiongozi, Mwenyekiti wa Chama, Mbunge wa Jimbo la Mlimba unataka kuongea na wananchi unawekewa barua pamoja na maelekezo sema hivi, sema hivi, ndiyo kazi ya Jeshi la Polisi? Siyo kazi ya Jeshi la Polisi, acha niseme, kama unaona nimekosa, kamata, weka ndani, nipeleke mahakamani, siyo kazi yako kunizuwia kusema mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuhitaji kupewa maelekezo kwa sababu sheria, kanuni na taratibu zipo. Tunahitaji kutoa taarifa siyo kuomba kibali, hivyo vibali, vibali ndiyo vinatupeleka huko tunakofika, watu wanajiona wana nguvu sana kuliko Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kazi ya Jeshi la Polisi kwenda kuvamia kwenye lodge za watu ambao wanalipa kodi na kila kitu, usiku wa manane, eti kwa kisingizio hapa kulikuwa na watu mchana wamekaa wanataka kufanya maandamano ya tarehe 26, kimetokea Morogoro. Wanatoa wateja ndani wanawapiga, wanawaweka chini ya ulinzi, wanawalundika ndani, kuwaingiza hasara wafanyabiashara, huo ni uharamia, haukubaliki. Jeshi la Polisi fanyeni kazi zenu kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya, ukiuliza wanakwambia tumeagizwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema siku hii ya leo na kutoa mchango wangu kuhusu bajeti ya mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kabisa kwa moyo mkuu na akili zangu zote kuunga mkono maoni yaliyotolea na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge ambayo imewasilishwa Bungeni kama maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mheshimiwa Silinde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno yote yaliyozungumzwa humu yana mantiki na miaka yote bahati nzuri tangu niingie Bungeni hii ni awamu yangu ya pili kuna mambo ambayo tuliyazungumza kama Kambi na nimeona kwamba Chama cha Mapinduzi ndio kinatembea humo humo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, pamoja na kwamba yakiletwa yanabezwa lakini utakuta labda wanajifungia chumbani na kuyachukua kuona kweli haya ndiyo maoni ya wananchi. Kwahiyo, ni muhimu sana Waziri mwenye dhamana akachukua, akatendea kazi na Rais wa Nchi, akachukua akayafanyia kazi kama anavyofanya sasa, kwa hiyo, ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa ni uungwana wa hali ya juu kama Chama Tawala kingekiri na Wabunge wenzetu wa Chama Tawala kingekiri walitukosea, walituzarau, walitubeza, lakini ndio ukweli wenyewe, sasa hivi Awamu ya Tano ndio wanachukua na kuyafanyia kazi. Lakini sisi tunatimiza wajibu wetu kama Kambi tunawapa maoni, pale mnapoyatekeleza tunaona wananchi wetu ndio wanapata nafuu. Kwa hiyo, tutakwenda tu mpaka Watanzania wapate uelewa kwamba watuingize madarakani ili tuyatekeleze yale tunayowashauri. Kwa sababu mtu ukimshauri anaweza akayatekeleza, lakini wazo kwa sababu sio lake, hawezi akalitekeleza sawa sawa kwa mfano kama elimu bure, sisi tungeingia madarakani tungeifanya sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo hayo, nimeona kwenye kitabu hiki cha Waziri nataka niseme kwamba katika ukurasa 85 amezungumzia kuhusu TAZARA na nilivyokuwa naangalia nilizani anazungumzia reli ya TAZARA, lakini kibaya zaidi amezungumzia TAZARA flyover pale Dar es Salaam. Nataka nipate majibu ya Serikali ni namna gani sasa watumishi wa TAZARA walioenea katika Mikoa ya Morogoro mpaka Mbeya ni namna gani hatima yao kwa sababu hali ni tete wengine wamestaafishwa, hawajapewa mafao yao, Serikali imekaa kimya, TAZARA yenyewe ina kizungumkuti, haijulikani namna gani. Jamani hii hali inatisha watu wanateseka wameshindwa kusomesha watoto, wengine wamekufa, hawajui hatma yao, naomba nipate majibu ya Serikali, nini hatma ya TAZARA na wastaafu wa TAZARA na uboreshaji wa reli ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye barabara, kwenye kipindi cha miezi miwili iyopita hakuna mama aliyetoka Mlimba kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rufaa Ifakara, barabara haipitiki, barabara zimekatika, barabara kilometa 230 Waziri asikie, nasimama hapa kila siku kilio ni barabara, wanaoteseka ni akina mama, watoto, wazee, hivi hata nikisoma hii bajeti inazungumzia flyover, ndege na mambo mengine treni. Mimi wananchi wa Mlimba wanaionaje hiyo bajeti, wanaona kama sio yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sasa watuhakikishie wananchi wa Mlimba Waziri wa barabara amefika kule lakini hali ni tete, na Meneja wa TANROADS nimeongea naye anasema wakati Serikali inajipanga kujenga barabara ya lami, basi tupate hela za kutosha za kujenga angalau kilometa 50 ambazo tunyanyue tuta ili ile barabara ipitike mwaka mzima, lakini hela wanazopangiwa hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba hebu muwahurumie wananchi wakule na wale tuwe tumepata uhuru pamoja mwaka 1961, lakini mpaka leo wale watu kama hawajapata uhuru. Lakini eneo lile ndio linalotoka mazao ya kilimo, Kilombero Planting Limited iko pale Mngeta lakini hamna barabara. TAZARA haiboreshwi, barabara hakuna, hivi mnataka yale mazao watu wabebe kichwani na kule kuna kilimo kikubwa?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu maji, Waziri amesema atakwenda lakini maji Jimbo la Mlimba ni mtihani, hivi mji mzima mdogo wa Mlimba hivi mtu anapata maji kwa siku saba mara moja, hivi kinamama kuna Mawaziri hapa akina mama, hivi mama anaweza akakaa akapata maji siku saba mara moja,huyu mama, msichana anaishi vipi katika mazingira gani. Anaenda kujifungua inakuwaje, kwa hiyo, shughuli za maendeleo kule tunalima, shughuli za maendeleo zinarudi nyuma kwa sababu tumekosa maji. Naomba haya maendeleo twende kwa pamoja, sio wengine wanasonga mbele, wengine tunarudi nyuma, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahakama, swali linakuja lakini kule hakuna mahakama, kilometa 230 mtu anatoka anakwenda kufuata mahakama ya Wilaya Ifakara, barabara hazipitiki kwahiyo kule haki hakuna. Yaani kule kama dunia ndio imeumbwa leo, yaani ni hatari, sasa vilio vyote ninavyosema ni vya uhakika. Vilevile kuhusu vituo vya polisi Mheshimwia Mwigulu ameenda kule amejionea mwenyewe, hakuna vituo vya polisi kule, hali ni mbaya sasa watu wanakosa mahakama, wanakosa vituo vya polisi, wamekosa barabara, wamekosa maji, hawa watu hebu muwafikirie, hivi wanaishi ishi vipi wale watu kule! Kwa hiyo hivyo ni vilio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kule ni ndogo kuna mradi mmoja tu wa Njagi mito mikubwa inapita lakini hakuna umwagiliaji na kule Njagi wanamwagilia wakati wa mvua, wakati wa kiangazi hola, hicho ndio kinaitwa kilio cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu naenda kwenye makinikia, kwenye hii bajeti inazungumzia flyover, lakini wamegundua wanavyosema kwamba kuna makinikia yana grams chungu mzima za dhahabu na tutapata karibuni trilioni mia moja sijui na ngapi, sasa naomba hebu geuzeni tusubiri hizi za makinikia ambazo tunaenda kuzipata, zije zijenge reli hizo hela ambazo zipo sasa hivi kwenye bajeti hii tukaimarishe miundombinu vijijini kwa wanakijiji huko, ili hizo zinazokuja za makinikia tuweke sasa hiyo miundombinu tununue ndege nini, nini au vipi! Si hela zipo zinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mikataba na sheria, iletwe Bungeni lakini tulipiga kelele nyuma hamna kitu. Kule Mahenge, Ulanga kuna mgodi mkubwa madini ya graphite, madini ya hali ya juu duniani, lakini mpaka leo wananchi wa kule hawajui hatma yao, mikataba yenyewe ndio hivyo imefungwa fungwa, mtuletee hiyo mikataba na sheria hapa Bungeni tuone tunaendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi na mafuta, yamegundulika Wilaya ya Malinyi kule Morogoro, Kijiji cha Ipela Asilia, lakini mikataba hata wananchi wa kule hawajui itawafaidisha vipi, kwahiyo ndio haya haya tunayoyasema sasa baadaye ndio mnasema sasa tumeibiwa tumeibiwa sasa si muanze sasa? Kwa nini mnangoja mpaka tuibiwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba haya mambo twende kwa pamoja wote ni watanzania tunahitaji maendeleo, hatuhitaji matatizo kama hivi vyanzo vya Halmashauri wameshavipora huko juu, lakini kuna hiyo hoja kwamba ikifika mwaka 2025 Halmashauri zote ziwe zimejitegemea kwa 25% ile hoja mmeifuta au bado ipo? Zisije Halmashauri zikapata hoja za mkaguzi wakati zimenyang’anywa mapato zitashindwa kufikia malengo.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sera vijiji lazima vifanye uchanguzi, nasema hivi Mrimba mpaka leo kuna vijiji vitatu havijafanya uchaguzi tangu mwaka ule wa uchaguzi wanasema kuna mwekezaji, sasa kwenye uwekezaji hakuna uchaguzi. Sasa ninachokiomba ile kesi iliyoko mahakamani.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kukubali ombi la Mheshimiwa Paresso ili aniachie dakika kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na maswali, yaani ni hivi, tunajadili hapa maswali yaulizwa Bungeni na Mheshimiwa Dkt. Mpango yupo na anajua swali gani likiulizwa karibu Bunge zima linasimama. Lakini unapokuja kuweka mipango ili Watanzania wengi wanufaike unatuletea mipango ya kujenga reli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndiyo reflection ya Waheshimiwa Wabunge kwamba wao wanataka reli ya Dodoma? Ni reflection ya Watanzania kwamba wao wanataka kiwanja cha ndege cha Chato? Ni kweli ni matakwa ya Waheshimiwa Wabunge, wao wanataka bombardier? Kwa nini mnatufanyia namna hii? Kwa nini wakati Bunge watu wanauliza maswali katika mipango ya nchi hii huangalii ni nini watu wanataka ndani ya Tanzania, sisi ndio wawakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasimama wengi kwenye maji, lakini leo unatuletea mipango ya maji ya vijiji totototo, wakati Tanzania tuna mito, tuna maziwa, tuna kila kitu. Kwa nini usituletee maji ya bomba, mpango ambao utaonekana mnakwenda kutega sasa maji katika milima, katika mito ambayo tutakuwa na kilimo cha umwagiliaji na maji yatatiririka kila kijiji? Kwa nini mnakwenda kutuchokozea ardhi chini ili ituletee matetemeko ndani ya nchi ya Tanzania?

Kwani Mungu aliweka Mito hapa Tanzania alikosea nini? Naomba mipango inapokuja ndani ya maji usituletee mipango mingi ya visima. Tumia mito, maziwa ili tupate maji ya umwagiliaji na maji ya bomba salama na kunywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata umeme huo. Umeme wa maji nasikia ni rahisi. Huko nyuma katika vitabu nilisikia sana wana mipango, kwa mfano kule Mlimba kuna mto mkubwa kabisa ambako unakwenda kumwaga maji mpaka huko Kilombero, mpaka Rufiji, huko kwenye Stiegler’s, lakini kule mmekusahau kabisa. Mlisema mtazalisha umeme kwenye Mto Mpanga, leo katika mipango yenu hakuna kitu, mmedandia Stiegler’s Gorge. Nini? Tatizo liko wapi, kwa nini mnapanga mipango halafu mnaiachia njiani, kwa nini hammalizi? Kwa hiyo, mimi nilitegemea mipango iwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye gesi, Watanzania wote walijua sasa gesi imepatikana, tukasifiwa hapa kwamba gesi sasa ndiyo mkombozi wa Watanzania, kila mmoja alijua baada ya miaka fulani gesi…, sasa hivi mimi niko kwenye Kamati ya Nishati na Madini; gesi sasa hivi ni kitendawili, na wakati ule Mheshimiwa Mnyika alikuwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alisema leteni mikataba ya gesi hapa Bungeni, mikataba mnayosema tofauti na mliyoingia kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo utakuta eti Serikali imedhamini Songas imekwenda kuchukua hela huko halafu Songas hawana chochote. Mitambo ya TPDC, mitambo ya TANESCO, lakini Songas kamuajiri tena huyo mbia Pan African Energy, halafu huyo huyo anaunasibu tena wa TPDC. Hela tumekopa Tanzania; kuna gesi hapa?; halafu Serikali ndiyo inakwenda kulipa ule mkopo. Ule mkopo hailipi Serikali, inalipa kwa Watanzania, wapigakura wetu. Nini ninyi? Haya mambo gani mnatuletea hapa? Hizi figisufigisu hapa za nini? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna matatizo makubwa ndani ya nchi yetu. Labda kama unashinikizwa, maana tumuonee huruma na huyu jamaa. Hapa unaambiwa hii nchi hakijachakuliwa Chama cha Mapinduzi, amechaguliwa mtu mmoja, alichukua fomu peke yake, kwa hiyo hata ukiwa Waziri ukibisha tu imekula kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa bwana, lakini Mheshimiwa Spika jana alisema tuseme tu tusiwe na wasiwasi, sasa wasi wasi wa nini Wabunge wa CCM, lakini na mimi mwenyewe si Mwenyekiti wangu kaniambia niseme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida za Watanzania kwa mfano kule Mlimba na maeneo mengine ni kuunganishwa barabara za mikoa na wilaya kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima. Lakini leo Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie, katika mpango huu unaokuja, je, ni barabara ngapi nchini Tanzania zitakwenda kuanzishwa na kujengwa kwenye viwango vya lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasaidia nini? Inasaidia kwa sababu Watanzania wengi ni wakulima. Kwa hiyo, watapitisha mazao yao lakini itasaidia sana wanawake ambao wanajifungua katika mazingira magumu na Hospitali za Wilaya ziko mbali. Haki ya Mungu wanaokufa nchi hii ni vijijini. Kwa hiyo, barabara zitaokoa uchumi kwa wakulima, zitaokoa vifo vya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipata barabara inawezekana kabisa tutapunguza vifo vya akina mama kwa sababu sera ya Taifa kila kata kuwe kituo cha afya, kila kijiji zahanati. Hebu tuambie mpango madhubuti wa kutimiza sera ya Taifa kwamba kuna vijiji vingapi nchini Tanzania vina zahanati, kuna kata ngapi zina vituo vya afya na mpango wa Serikali ni nini katika kutatua haya matatizo. Hatuwezi kukubali wananchi wanakufa huko, hasa akina mama na watoto. Tunaomba uje na huo mpango ili utuambie tupunguze vifo, tuokoe akina mama na watoto na tuokoe wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu mimi nilitegemea uje na mpango, kwa kuwa tayari tuna vituo vya JKT na hii tunasema kwenye nchi ya viwanda, ungekuja na mpango hapa kwamba JKT itachukua vijana iwe darasa la saba, iwe vyuo vikuu, watakwenda kufanya huko stadi mbalimbali na kufundishwa uzalendo halafu wakitoka huko wanakuwa na package ya kuwakopesha kwenda kutengeneza viwanda. Mngechukua hata wataalam kutoka China, na hiyo ilikuwa Ilani ya CHADEMA, tulisema JKT itakuwa si tena mabunduki tu, kutakuwa na mpango maalum vijana kwenda huko kujifunza mafunzo mbalimbali ili kwenda kuokoa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkopo wa reli, mmechukua mkopo mnajenga reli mpaka Dodoma, lakini TAZARA mmeisahau. Tatizo ni nini? Hii TAZARA inapita hata Selous, watalii walikuwa wanatoka Dar es Salaam wanakwenda kwa treni mpaka Mlimba, au wengine wanapita kwa barabara mpaka Mlimba wanaingia Selous; lakini leo barabara hakuna, reli yenyewe haina uhakika. Tatizo liko wapi? Uje na mpango katika kukuza utalii kule Selous ili hawa watalii waje kwa barabara au waje kwa TAZARA ili tuone kwamba tunakuza uchumi wetu.

Mheshimwa Mwenyekiti, afya nimeshazungumza. Kwa ujumla naomba angalia hoja za Waheshimiwa Wabunge, angalia maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Unapokuja na mipango yako zikusanye ujue tatizo ni nini halafu ukija na mpango elekeza kule ambako Wabunge wengi wanaleta maswali Bungeni ili tutatue haya matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mengine ya bombardier na nini yatakuja tu, hivyo viwanja vya Chato, hii tumeshakula bogi umetuingizia huku mabilioni ya hela wakati wengine hata maji hatuna, umetuingizia huku mabilioni ya hela, unakopa wakati sisi hapa ulitakiwa ukope turudi vijijini kwetu tuwaambie tumekopa kwa sababu tunajenga barabara, tumekopa kwa sababu tunajenga vituo vya afya, tumekopa ili tujenge zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tungekuwa radhi kabisa kuiunga mkono Serikali kwa kukusanya kodi, tungefunga mikanda kwa sababu tunajua mpaka kufikia mwaka fulani matatizo ya maji litaisha, barabara pamoja na zahanati yataisha, lakini sasa hivi hatujui hiyo mikopo itamaliza tatizo gani. Sisi watu wa Mlimba hatuna shida ya ndege bombardier, hatuna shida ya kiwanja cha Chato lakini madeni hayo yanatupata wote, hiyo si tabia nzuri, acheni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi niende moja kwa moja kwenye point zangu; kwamba kidato cha tano na cha sita Wilaya ya Kilombero mwaka huu wametupa shule moja ndani ya Jimbo la Kilombero pale Sanji. Sasa mimi siwezi kusema sana, lakini Jimbo la Mlimba linaeleweka yaani ni kubwa, pana, miundombinu mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulikuwa tumeomba na sisi tupate kidato cha sita, kwa hiyo kwa sababu bajeti ya mwaka huu inapita na mmeshapanga hicho kwa hiyo naomba mkumbuke kunako majaliwa kipindi kijacho cha mwaka ujao wa fedha mtuwekee na sisi ndani ya Jimbo la Mlimba na tumeshapendekeza hizo shule za kuweka kidato cha sita, hiyo itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya walimu. Ukizungumzia kuhusu madeni ya walimu nchi nzima ni shida. Walimu wameshahakikiwa na katika kazi zao kule katika ofisi zao wameshaweka vizuri, sasa kwa nini Serikali hailipi hawa walimu madeni yao, kigugumizi cha nini jamani? Hamuoni kama mnawavunja moyo hawa walimu? Afadhali huku mjini watu wanapiga biashara labda ice cream nini wanauza shuleni, kule kijijini hamna wenzenu, walimu wanategemea mshahara tu na wakisema waende wakalime mara mvua imekuja imebeba mazao yote. Sasa hawa walimu wanaishi vipi katika mazingira hayo? Naomba tafadhali lipeni na mtupe majibu katika bajeti hii ni lini mnalipa madeni ya walimu nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu walimu wa sanaa mnasema wametosha. Tangu walivyoajiriwa mwaka 2014 ajira hamna tena, lakini cha kushangaza Serikali hii hii inadahili walimu hao hao wa sanaa, wazazi maskini wanasomesha hawa watoto wao na Serikali inatoa pesa kwa ajili ya kuwapa mikopo baadhi yao lakini mnasema wametosha. Sasa kama ndiyo hivyo basi msitishe hawa walimu wa sanaa, la sivyo kwa sababu nchi hii sasa inaenda kwenye viwanda basi badilisheni mtaala, badala ya kuwapeleka kwenye ualimu muwapeleke katika masuala ya ufundi hawa wanaosoma degree, waanzishe viwanda vidogo vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji watu wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na viwanda vya kati. Kwa hiyo badilisheni acheni mambo ya sanaa lakini hata mkisema walimu wanatosha, hawatoshi. Kule kijijini ratio; kwa kawaida ratio yenu ni 1:40; 1:45; 1:25. Leo nina chekechea mimi tena satellite area hakuna mwalimu lakini wanafunzi 100 chekechea, hivi kuna elimu pale? Kwa hiyo, si kwamba walimu wanatosha, lakini Serikali bado haijajipanga ni namna gani wathibitishe hiyo ratio mliyoipanga ili walimu waende wakafundishe hizo shule, hali ni mbaya kupita kiasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukariri, jamani eee, hivi kukariri hamna, sasa kukariri hamna watoto wasichana Mama Ndalichako na wewe mwenyewe ni mwanamke watoto wasichana wasipokariri waende wakaolewe wakiwa bado wadogo? Mimi naona hiyo kukariri acheni, watoto waendelee kusoma ili wapate elimu wakue shuleni baadae hata wakitupwa huko mbali kama ataolewa yeye, atakuwa mkulima yeye, lakini hiyo kukariri achanane nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa maabara. Somo la Baiolojia ni asilimia 51.5, Fizikia asilimia 43.5, huko vijijini huu upungufu huko vijijini kwetu hakuna walimu hao jamani. Sasa matokeo yake eti mtoto anayefundishwa private, anayefundishwa mjini, mwenye walimu, mwenye maabara anafanya mtihani mmoja na mtoto wa Mlimba. Huo ni uonevu ama si uonevu huo? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri akija anijibu, huo si uonevu? Kwanini mnampa mtoto wa Masagati, mtoto wa Utengule, mtoto wa Mlimba anafanya mtihani mmoja na mtoto wa Dar es Salaam au wa mijini ambaye ana maabara, ana walimu ana kila kitu, huo ni uonevu, ni ubaguzi haukubaliki ndani ya nchi yetu, haikubaliki kabisa, kwa hiyo hilo naomba mliangalie, tunaoteseka ni sisi wa vijijini siyo wa mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nauliza hivi remote area zile shule za satellite yaani kwenye jimbo langu kutoka shule ya msingi mpaka kwenye kitongoji ni kilometa 20, hapa katikati kuna mito ya ajabu. Mimi leo mpaka mfuko wa jimbo nahangaika nao nawaambia wananchi jengeni madarasa mawili halafu mimi naleta bati na nimeshapeleka bati Mpande kule Kata ya Mchombe, Ijia na sehemu nyingine nyingi. Kule Tanganyika, Masagati, Lwamate mpakani na Njombe lakini walimu hamna. Vigezo mnavyoweka mjini hebu legezeni masharti na vigezo vya vijijini jamani. Haki ya Mungu unaenda unalia, watoto 200 hakuna mwalimu, mwalimu wa kujitolea, hebu nendeni mkaangalie halafu mjue mpange mipango yenu. Hamuwezi mkalinganisha… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia bajeti hii kwa kupenda kujua na kuishauri Serikali kwamba katika Kikosi/Kambi ya JKT Chita, pamoja na kuwa na umuhimu wa uwepo wa kambi hiyo, ni muhimu kukawa na mpango wa ujirani mwema kati ya Chita JKT na Vijiji vya Makutano, Chita na Ikule kwa Kata ya Chita na Mngeta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka mingi sasa wananchi wana malalamiko ya mipaka ambapo kuna wakati Jeshi kuingia hapo, hasa Kata na Kijiji cha Chita. Ingawa kwa upande wa pili Kata ya Mngeta hawakuwa na ombi lolote kwenye Kijiji cha Mkangawalo na kuleta sintofahamu inayojitokeza ambapo wananchi wanaomba kuwepo na maelewano kwa kuwa ni miaka kadhaa sasa hawana maeneo ya mashamba na kuwafanya kuwa maskini kwani tegemeo lao ni ardhi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazungumzo ya ana kwa ana na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kuwa wananchi hao wataangaliwa kwa kuwafanya wakulima wadogo kwani kutafanyika ukulima mkubwa na SUMA JKT, lakini ni miaka sasa inapita hakuna mwananchi aliyeingizwa katika kilimo hicho. Serikali iwaonee huruma na wananchi hao wanaoteseka na kunyanyaswa katika maeneo hayo. Je, ni lini sasa Serikali itakaa na wananchi wa vijiji hivyo ili wananchi waweze kuwa na maeneo ya kilimo na kujikimu na hali ngumu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wanajeshi wenye elimu ya kiwango cha chuo kikuu. Wakati wa Rais Kikwete (Operesheni Kikwete) waliorudishwa nyumbani wangefikiriwa kupata ajira lakini hadi leo hawajaitwa. Je, ni lini sasa Serikali itawakumbuka vijana hao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione haja ya kupitia maeneo yote yanayolalamikiwa kwa kuwashirikisha wanavijiji na Jeshi na mamlaka zinazohusika ili kuleta utangamano.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu ahsante sana kwa kunipa hii nafasi adimu ili na mimi nichangie kwa dakika tano katika Wizara hii ya Kilimo ukizingatia mimi ni mtoto wa mkulima na hapa nilipo nimekulia kwenye kilimo na maisha yangu yote yapo kwenye kilimo. Uzuri zaidi katika Wilaya yangu ya Kilombero, Jimbo ambalo naliongoza mimi la Mlimba karibu asilimia 99 sisi ni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kuna haja ya kusema kwamba kilimo hiki ambacho sisi tunahangaika kwa majembe ya mkono, wengine power tiller, kwenye matope, barabara hamna, mbegu, panya tunapambana nao viwavijeshi na Maafisa wa Ugani hakuna yaani tunahangaika tu kama kuku wa kienyeji. Serikali imeshindwa kabisa angalau kuonyesha kumkomboa huyu mkulima siyo kwa maneno tu kwa vitendo kwa kutoa ajira nyingi kwa Maafisa Ugani hasa kwenye maeneo ambayo tunalima. Unaposema tu kilimo ndiyo uti wa mgongo karibu asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima lakini asilimia 100 ya Watanzania tunatumia mazao ya kilimo halafu kilimo chenyewe kinakuwa alfu lela ulela kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema inasikitisha? Pamoja na kilimo hiki kuachwa kinahangaika chenyewe lakini katika pato la Taifa kinachangia asilimia 31 lakini leo katika bajeti ya kilimo haki ya Mungu inatia huruma, hivi kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika kipindi hiki cha kupanda nilihangaika sana kwenye Wizara ya Kilimo, kwa Waziri kwa Naibu Waziri, panya walivyovamia kwenye mazao, watu wamepanda mara ya kwanza panya wamekula, mara ya pili wamekula, mbegu wanahangaika lakini kwenda Wizarani hawana bajeti. Nilitegemea kwenye bajeti hii kuwepo na bajeti kabisa ya dharura kwa sababu wadudu wengine waharibifu wanatokea bila taarifa. (Makofi)

Kwa hiyo, tunaomba bajeti ya dharura au maalum kwa ajili ya majanga kama haya katika suala la kilimo, hapo ndio mtakuwa mmeenzi kilimo kuliko kuacha watu wanahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi sisi kule tunalima mpunga, kokoa, ufuta, mbaazi kule kila kitu kinakubali hata binadamu ukimpanda kule anaota Mlimba, Wilaya ya Kilombero. Cha kushangaza pamoja na mambo yote haya kwamba tunalima wenyewe mpunga mwaka jana soko likawa kubwa kweli kweli, Tanzania nzima wakaja Ifakara. Bei ya mchele na mpunga ikapanda kwa sababu pumba ni mali chakula cha mifugo, pumba tunachomea matofali yaani hakuna kitu kinachotupwa katika mpunga, lakini ikafikia mahali bei ilivyopanda tukaambiwa soko limefungwa hakuna tena kupeleka mazao nje, ninyi vipi kwani mlitugea ninyi mitaji? Kwa nini mnatuonea wenzenu? Barabara mbovu, tunahangaika tunalima wenyewe halafu mnafunga masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba mipango hii ya Serikali ya kufunga masoko ya nje au kufunga mipaka naomba msitufanyie tu sisi wakulima. Mtuone kwamba na sisi tunastahili kuuza mazao yetu nje, siyo lazima tuuze hapa hapa Tanzania. Kwa sababu sisi Wilaya ya Kilombero hitaji letu sisi ni tani 130, tunazalisha tani 530 ziada ni tani 400 sasa mnataka tuzipeleke wapi? Kwa hiyo, ni vema sasa mkatuona kwamba na sisi tunastahili kupata maisha, kusomesha watoto, kujenga nyumba bora, kuchangia shule, elimu, hospitali tunajenga wenyewe majengo. Kwa hiyo, tunategemea tukilima, tukipata pesa ndiyo tunaenda kuchangia hizo huduma za jamii. Sasa mnavyotuacha hivi tunahangaika wenyewe huduma za jamii tutachangiaje na Serikali imesema wazi wananchi watajenga maboma Serikali ndiyo itakuja kumalizia. Sasa tunajengaje maboma kama hatuna kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushirika, hili nalo ni janga la Taifa kwa sababu hawa viongozi waliopo katika ushirika ndiyo walioua ushirika, leo zinaundwa timu kwenda kuhangaika na madeni halafu wanashirikisha viongozi hao hao. Mimi nataka nijue Serikali imechukua hatua gani kabla hatujaenda kwenye ushirika kwa wale viongozi walioua ushirika ambao wapo. Siyo mnakimbilia tu kuunda ushirika wakati wale walioharibu ushirika hamuwachukulii hatua.

Hiyo itakuwa ngumu sana mtu kujiunga katika ushirika na mtagombana na mtawafunga wengi kama mnapitisha maagizo ya namna hiyo huko chini, hayatatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba bajeti ya kilimo iongezeke na ishuke chini watu waajiriwe, tupate wataalam watusaidie katika masuala ya kilimo na masoko yawe wazi mkulima awe na uwezo wa kuuza mahali popote. Kama mnataka kudhibiti masoko basi muwe na kilimo maalum, Serikali itoe hela kwa wakulima mseme mazao haya tumetoa pesa na mbolea bure kwa wakulima kwa hiyo hayo lazima tuyauze ndani lakini aliyehangaika mwenyewe, muacheni akauze mahali popote, tutakuwa tumemstawisha huyo mkulima.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika zako hapo mezani.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie vitu vichache, katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kilombero, tuliitwa kikao cha ghafla kuonesha kwamba Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Halmashauri walikuja Dodoma ili kujumuisha ile miradi ya CGD, kwamba tusiweke kitu kidogo kidogo, tuanzishe miradi mikubwa michache ile hela tuliyopangiwa shilingi bilioni 1.5 ili tutekeleze miradi hiyo kabla ya mwaka wa fedha kwisha.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo hiyo pesa haijaisha, kigugumizi kiko wapi? Naomba Mheshimiwa akija hapa Waziri atuambie hiyo hela inapelekwa lini kutekeleza ile miradi michache tuliyokubaliana kama Baraza na wao ndio waliotushauri ili tutekeleze ile miradi waliyoanzisha wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba majibu ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Wilaya ya Kilombero kuna madeni ya walimu yameshahakikiwa na Wilaya ni kubwa, lakini mpaka leo haijulikani hawa walimu watalipwa lini? Sasa watuambie leo katika mwaka huu wa fedha kabla haujaisha haya madeni ya walimu yatakuja kulipwa lini? Wanateseka huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya Mkoa wa Morogoro kuna wazabuni ambao wamelisha tender miaka mingi katika taasisi za umma, lakini mpaka leo, hawa watu wanahangaika, wamekopa, wanataka kuuziwa vitu vyao, hela hawajapewa. Wameshafanyiwa uhakiki. Je, ni lini sasa wazabuni wa Mkoa wa Morogoro ambao wanalisha taasisi za umma watalipwa hela zao? Naomba majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, lingine ni wastaafu wa TAZARA. Jimbo langu limepitiwa na wastaafu wa TAZARA na wako wengi kweli ndani ya Wilaya ya Kilombero na huko Mkoa wa Mbeya. Tangu mwaka 2005 waliostaafu mpaka 2009 hawa watu hawajalipwa stahiki zao.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inasemaje kuhusu hawa wastaafu jamani? Mbona mnawaonea! Wametumikia TAZARA kwa moyo mkuu jamani! Hebu mtoe kauli ya Serikali, ni lini mnaenda kuwalipa hawa wastaafu wa TAZARA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine hizo shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji tunazingoja. Ni lini watatuletea hizo fedha? Wengine tunatoka kwenye vijiji ambavyo hata barabara hamna, magari hayafiki. Labda tungepata hizo, tungepata maendeleo. Ije Wizara hii sasa ituambie ni lini watapeleka hizo hela vijijini? Nadhani hata kwako Kongwa wanazisubiri kwa hamu hizo hela. Je, miaka hii inapita, tutaletewa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakusemea na wewe, huwezi kusema hapa, lakini tunahitaji hizo shilingi milioni 50 zifike kwenye kila kijiji ili tuone namna gani wananchi wetu wananufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hayo tu. Ahsante sana kwa kunipa hiyo nafasi.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu ahsante sana kwa kunipa dakika tano, ili nipate kuchangia. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye hii hotuba ya Waziri wa Maliasili nimeenda kwenye ukurasa wa 62, aya ya 5.4.5.2, kuhusu Idara ya Wanyamapori, akasema kwamba mradi na usimamizi endelevu wa ikolojia ya ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero na Mto Rufiji.

Sasa nimesimama hapa na kwa kukuomba sana ili kuzungumzia hilo suala kidogo ambapo kwenye kitabu chake ameongea kitu kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nimealikwa kwenye vikao mbalimbali vya nishati na madini kwenda na wataalam wanaoshughulikia suala la Stieglers’ Gorge kule Rufiji, kuhusu kutuelimisha namna tutakavyopata umeme. Lakini wakiwa wametujumuisha watu wa Mkoa wa Morogoro, hususan Bonde la Kilombero kwa sababu wanasema kuna asilimia karibu 60 na zaidi za maji zinategemewa kutoka Kilombero kwenda kwenye lile bwawa la umeme. Pamoja na mpango huo, lakini Wizara hii pamoja na Wizara ya Nishati haizungumzii athari za wananchi zitakazotokana na uwekezaji huo mkubwa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitiririke sasa moja kwa moja, mradi huu ndani ya Jimbo la Mlimba kuna kata zipatazo nane na vijiji vipatavyo 18 vinaenda kuathirika moja kwa moja na mradi huu, lakini mradi huu hauzungumzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo katika hizo kata na hivyo vijiji vipatavyo 18 kuna kilometa 359 inachukuliwa kwenye Kijiji cha Ngombo, chote kinaondolewa kwa ajili ya kutunza maji ili yaende Rufiji, Kata za Mlimba hizo. Katika Kata ya Mofu, Kijiji cha Idandu wanachukua ekari moja na Mwawala Kata wanachukua kilometa moja, Kata ya Idete wanachukua kilometa tatu Kijiji cha Miwangani, Kata ya Mofu wanachukua Kijiji cha Miomboni kilometa 13, Kata ya Kalenga Kijiji cha Mofu wanachukua kilometa 23, Kata ya Mofu wanachukua kilometa 31, Kata ya Ikwambi, Kijiji cha Ikwambi wanachukua kilometa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mchombe, Kijiji cha Lukolongo wanachukua kilometa mbili, Kata ya Mngeta wanachukua kilometa moja, Kata ya Chita, Chita JKT, wanachukua kilometa 74, Kata ya Melela wanachukua kilometa 27, Kata ya Kalenga Kero wanachukua kilometa 19, Kata ya Ching’anda Kijiji cha Udagaji wanachukua kilometa 37, Kata ya Chisano wanachukua kilometa sita, jumla ni Jimbo la Mlimba, ni kilometa 37. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule wanakochukua huko ndio tunakotegemea kulima, ndio tunakotegemea wafugaji wameingia wengi, wanafuga huko, tutakwenda wapi? Hawatuambii hawa watu wanakwenda wapi? Hiyo ni hatari ndani ya Jimbo la Mlimba, ni maumivu makubwa. Mradi huu hauzungumzii chochote kuhusu athari ya maeneo haya, hawa watu takribani karibuni 30,000 wanakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali, hiyo ni hatari, eti kwa sababu tu kwa Stieglers’ Gorge, jamani hata mradi mzuri angalieni athari za wananchi wanazopata. Hiyo nimesema Jimbo moja tu, kuna Jimbo la Kilombero lenyewe, kuna Jimbo la Ulanga na Jimbo la Malinyi kote wanaenda kuathirika, si kazi yangu kusemea, watasema Wabunge wao.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatari. Watuambie Serikali sisi wanatupeleka wapi? Wafugaji wamejaa kule mnawapeleka wapi? Wakulima watalima wapi? Tutaishi vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mbinu mbadala ya kutusaidia sisi, naongea hivi kwa machungu makubwa, yaani sipati jibu, hali ni hatari, sijui tutaenda wapi sisi wananchi wa Mlimba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kusema sana kwa sababu moyoni naumia sana pamoja mnacheka lakini sisi tunaenda kuathirika na sisi ni Watanzania hatuna barabara, umeme wenyewe hatuna, maji hatuna, hivi mnatufanyia nini sisi, tumewakosea nini nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ni mbaya ndani ya Jimbo la Mlimba, Serikali hebu hamieni kule mkaone watu wanavyoenda kuathirika na huo mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyosomwa na Mheshimiwa Susan Lyimo, Waziri Kivuli wa Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mazingira ya shule za kata kutokuwa na mabweni, pia umbali na kutokuwa na ulinzi wa wanafunzi hasa wa watoto wa kike huko vijijini tunakotoka, umaskini wa kipato wa wazazi hupelekea wazazi kuwapangia nyumba watoto karibu na shule au wanafunzi kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni. Watoto wa kike hukumbana na vikwazo vingi kama ubakaji, ushawishi wa pesa za kujikimu kutokana na kuishiwa kabla mzazi hajampa matumizi, elimu ndogo ya uelewa na ukosefu wa walimu na kusababisha utoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naishauri Serikali ifuatilie na iwapo mtoto wa kike (mwanafunzi) akapata mimba kwa sababu hizo au nyingine na kwa kuwa anatoka familia za maskini awekewe utaratibu wa kuendelea na masomo ili apambane na umaskini wa kipato. Pia naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya madarasa, walimu, vyoo, maji shuleni ni tete sana kupelekea kuporomoka kwa elimu. Hivyo, bajeti hii iangalie na kutatua kero hizo. Wananchi wamechangia kwa kujenga maboma ili Serikali imalizie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madeni ya walimu, kupanda madaraja walimu na posho ya mazingira magumu, navyo ni kero kubwa na kupelekea walimu kushusha morali ya kazi na kushuka kwa elimu hasa shule za vijijini kutokana na mazingira magumu. Serikali ione haja ya kuwezesha maslahi ya walimu ili kuinua elimu. Kitengo cha ukaguzi nacho kiwezeshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kitabu hiki cha Waziri, ukurasa wa 11 anazungumzia wastani wa pato la Taifa la kila mtu, anasema kwamba wastani wa kila mtu kwa mwaka 2017 ni sawa na dola za Kimarekani 1,021 ukilinganishana na mwaka 2016 ni dola 958 kwa mwaka, kwa hiyo anasema umekua. Sasa swali langu, mlishawahi kupandisha mishahara? Hawa watumishi katika nchi hii wastani wao wa pato la Taifa umepanda au umesimama pale pale? Kwa hiyo, hapa kipato chako kinatudanganya? Hawa watumishi ambao hamuwapandishi mishahara pamoja na sisi Wabunge mnasema wastani kwa dola ya Kimarekani 1,021 badala ya dola 958 huo ni uwongo wa mchana kweupe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, watumishi wanapata wapi hela nyingine, wanakula rushwa mpaka mnawapima wastani wao wa kipato kwa mwaka? Tusidanganyane. Yaani ninyi wataalam wa kuandika hivi vitabu, mnaandika peke yenu halafu mnatuletea hapa, mnawadanganya Watanzania, wastani haujakua, hivyo ni vitabu tu lakini hali halisi sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda sasa kwenye bajeti kuhusu kilimo maana mimi ni mtoto wa mkulima na naishi kwa kutegemea kilimo. Bajeti ya mwaka 2016/2017, Bunge hili tuliidhinisha bajeti ya kilimo shilingi bilioni 100.5 lakini hela zilizotolewa kwenye kilimo ni shilingi bilioni 2.252 halafu unasema pato limekua, limekua kwa nani? Labda kwako wewe lakini kwa Watanzania wa kawaida na wananchi wa Mlimba halijakua chochote, bado wanarudi nyuma badala ya kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo mwaka 2017/2018, Bunge hili tuliidhinisha kwenye bajeti shilingi bilioni 150.25 na sifuri sifuri huko, lakini hadi kufikia Machi mwaka huu pesa zilizotoka za miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 16.5 sawasawa na asilimia 11 tu, leo unasema pato la Mtanzania limeongezeka, limeongezeka wapi wakati miradi ya kilimo ni shida?

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu na karibu Tanzania nzima hivi ninavyosema ni wakati wa mavuno, wananchi sasa wanavuma pumba kwa sababu mipunga panya waliingia, mahindi panya waliingia wakahangaika wakulima mpaka sasa wakati wa mavuno watu hawavuni tena, halafu tunaambiwa ikitokea njaa Mkuu wa Wilaya, sasa kama panya wamekula halafu kilimo hamjawapa hela za kutoa wale panya hivi unadhani watu hawataomba tena msaada? Mjiandae Wizara ya Fedha kuweka fungu maalum kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania ambao wamekosa kuvuna sasa hivi mazao yao yote yaliliwa na panya. Siyo kwamba wavivu wamelima lakini uwezo wa kuvuna tena haupo, hiyo ni hali mbaya, sijui watu wengine kama wamevuna lakini kwangu hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii imeendelea katika miradi yote, tumepiga kelele hapa Bunge zima, Serikali ilitenga shilingi bilioni 251 kwenye Miradi ya Maendeleo Vijijini, (Local Government Development Grants, kwenye mwaka huu tunaomaliza, Wakurugenzi wote Tanzania nzima na Wenyeviti wa Halmashauri wakapuliza magari mafuta wakaharibu bajeti zao wakaja Dodoma, wakaambiwa mnapewa hela, leteni miradi ya mikakati, mkishaweka tu mkirudi pesa zinaingia. Mpaka leo hakuna senti tano iliyoingia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkurugenzi wetu na Mwenyekiti wa Halmashauri alirudi Kilombero tukakaa vikao wakatumia pesa kwa ajili ya kuidhinisha miradi ya kimkakati, wananchi wamejenga madarasa, maabara, zahanati, mmesema mtaleta hela na mvua zitaingia ile miradi itakwenda kubomoka, nguvu za wananchi zitakwenda bure, halafu leo mnasema bajeti iko sawasawa, sawasawa gani ninyi? Acheni mambo yenu bajeti hewa hizo. Kwani tunaposema bajeti hewa ni zipi? Si ndiyo hizo za kudanganyana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mnatuambia tupitishe tena bajeti, haya hii bajeti tunayoipitisha mtaitekelezaje wakati hii bajeti ya mwaka huu tunaoenda kuumaliza mwezi huu hakuna kitu, hewa. Mnaharibu karatasi tu hapa hamna lolote, bora mngesema tu kwamba, hatuna hela, eti ninyi mnasema mna hela pato la Taifa limekua kwa asilimia 7.1 limekuakua vipi, mmekusanya wapi? Nini mmekusanya mpaka leo? Cash budget, mmekusanyaje hiyo bajeti, mnaishia kulipa madeni lakini kibaya zaidi mnaenda kukopa kwa biashara, halafu mnalipa madeni, nyie vipi? Nyie mnadhani hatujui siri zenu mnazofanya? Mnajikazakaza tu, mnatumbua watu kila kukicha hamtaki kusema ukweli Watanzania huku wanaumia, watu hawalipwi mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wenzetu wa Uganda walimu tu hawakupandishwa mishahara wametangaza mgomo, hapa Tanzania, yaani sijui tumelogwa na nani? Ni haki kabisa ya kila mfanyakazi kupandishwa mshahara lakini mpaka leo hata senti tano, mnavunja sheria, kwa nini mnavunja sheria? Kama ninyi kweli mnakusanya pesa na mna pesa kwa nini mnashindwa kupandisha mishahara ya watu kwa mujibu wa sheria? Leo mnajitamba hapa tuna pesa, pesa ziko wapi? Pesa hamna, mkiambiwa ooh, mnakopa kopa tu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapandisheni wafanyakazi mishahara yao kwa mujibu wa sheria zilizowekwa. Hii Serikali ya Awamu ya Tano ni hatari kuliko Serikali zote zilizopita, nawaambia. Halafu leo vitabu unasema uchumi umekua, umekua kwa nani, labda umekua kwa ninyi mnaoshikashika hela huko Benki Kuu. Hela siyo zenu ni zetu halafu mnakuja hapa mnatudanganyadanganya. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii tulipofikia hali ni hatari hata wewe unajua, Waziri anajua kila mmoja anajua, lakini kwa vile mnailinda Serikali ndiyo mnasema haya hamtaki tu kusema hali mbaya. Kama hali nzuri lipeni mishahara kwa Watanzania wanaolitumikia Taifa hili, kutwa mnatumbuatumbua. Kama pato la Mtanzania limekua, wale wafanyakazi waliotumbuliwa mpaka leo hawajui hatma yao pato lao limekua au limeondoka? Watanzania gani wanaowazungumzia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiwa na kiwanja wakati wa JK utauza shilingi milioni 5 sasa hivi mpaka milioni 1 hupati mnunuzi. Ninyi nini ninyi! Eti pato limekua limekulia wapi wakati watanzania wako hoi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu chake amezungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi waliidhinishia hela kidogo wakafika mpaka asilimia 300, acheni ubabaishaji, kwa nini kutumia hela nyingi za uchaguzi? Kwa sababu kazi yenu Awamu ya Tano kununua Madiwani na Wabunge halafu mnaenda mnafanya uchaguzi matokeo yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeenda kutumia mpaka asilimia 300, acheni hizo. (Makofi)

K U H U S U U T A R A T I B U . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie muda wangu kama alivyosema ndugu yangu hapa Mheshimiwa Nsanzugwanko pamoja na mipango yenu basi muangalie na sera ya nchi hii kuunganisha mikoa. Mimi natokea Mkoa wa Morogoro, kuna Mkoa wa Njombe unaunganika kwenye barabara Jimbo la Mlimba lakini tangu nilivyoanza kusema mpaka leo, okay, wamefanya upembuzi kiasi mpaka Mlimba lakini kutoka Mlimba mpaka Madeke Njombe hakuna upembuzi, hakuna kinachoendelea. Kwenye vitabu vyao vya Serikali sioni hata mafungu yanayotengwa kujenga barabara angalau waanze kidogo ili Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe kupitia Mlimba ile barabara iunganishwe. Ndio maana wakati mwingine tunachangia hapa tunaona uchumi haujakuwa kwa sababu wananchi wa maeneo yale bado wanateseka na sera hazitekelezwi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa dakika hizi tano. Moja kwa moja naenda kwenye hiki kitabu cha TAMISEMI, ukurasa wa 12 - 13 katika masuala ya utawala bora inaonesha kwamba Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Utumishi na Mipango pamoja na Makatibu Tawala wamepewa mafunzo kuhusu utawala bora. Sasa sielewi hayo mafunzo waliyowapa yalikuwa yanahusu nini? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utawala bora kuna misingi. Misingi ya utawala bora moja ni utawala wa sheria (rule of law), waliwafundisha nini? Katika misingi ya utawala bora ninachojua mimi uwajibikaji in English (accountability), waliwafundisha nini? Katika misingi ya utawala bora uwazi katika uongozi yaani Bunge, Mahakama, vyombo vya maamuzi, transparent in English, waliwafundisha nini? Katika misingi ya utawala bora uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa watu kutoa mawazo yao bila vitisho. Sasa tukiangalia nchi yetu hivi sasa hivi kuna utawala bora ama bora utawala? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakuu wa Mikoa wame-prove failure. Wakuu wa Wilaya baadhi yao na Wakuu wa Mikoa wameonesha hawajafaulu huo mtihani wamepoteza hela za Serikali za kodi za wananchi kwa kuwapa mafunzo halafu wakienda kule hawafanyi walichojifunza. Labda wangeniita mimi mwenyewe ni Mwalimu wa utawala bora vilevile na maendeleo ya uchumi nije nitoe mada halafu wangepewa mitihani huko field, wale wanaofeli wanawatoa katika uongozi.

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Mkuu wa Mkoa wa Morogoro safari hii kafanya maajabu, Dkt. Kebwe tena alikuwa Mbunge huku, eti leo hajaitisha RCC, hajaitisha Road Board, vitabu kaleta TAMISEMI, huo ndiyo utawala bora? Wabunge hatujahusishwa katika mipango yetu ya Mkoa wa Morogoro, mkoa mkubwa, hivi kwa nini wanamkabidhi mtu kama yule mkoa mkubwa kama ule? Wananiambia ukisema
ndiyo watamwacha pale pale, muacheni lakini CCM inaenda kuondoka, mimi nawaambia, anaenda kuwadondosha jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mkoa mkubwa kama Morogoro na tulikwishaomba jamani mtupunguzie huu mkoa, mtupe Mkoa wa Kilombero mpaka leo hamna kitu. Tutaona kwenye bajeti hii, kuna majimbo wamewapa hela kama mkoa ndiyo tutakuja kushughulika na ninyi. Sisi Mkoa wa Morogoro mkoa mkubwa hamna chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja Mlimba sasa. Mlimba halafu Mheshimiwa Jafo alipokuwa Naibu Waziri…

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe dakika zenyewe ni tano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mlimba, Mheshimiwa Jafo aliniahidi atakuja Mlimba ndugu yangu mpaka leo Mlimba hawajaja wanataka nini? Kwa nini hawaji Mlimba kuangalia wakija wanaishia Ifakara na Morogoro, Mlimba ni hatari. Hivi ninavyozungumza barabara karibuni, nawashukuru TANROAD kidogo wanajitahidi kutengeneza tengeneza barabara lakini barabara imekuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mawaziri, Waziri wa TAMISEMI mimi siwezi kusema sana hapa nawaomba waje Mlimba. Kwa mfano, tulikuwa tunategemea mwaka huu tutapata hela katika Kituo cha Afya cha Mngeta, cha Mchombe lakini hamna hata shilingi. Kilometa 265 mpaka kwenda kwenye hospitali ya wilaya akinamama wajawazito wanakufa njiani jamani, watoto wanakufa, tatizo ni nini? Kwa nini hawaji wakaangalia mazingira halafu waone maeneo ambayo yalikuwa muda mrefu hayana huduma ili watuletee hizo huduma angalau, barabara tukose….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa ni la Watanzania wote na inapotokea Kambi ya Jeshi inapokuwa katika kata au jimbo au vijiji naona ni fursa na faraja kwa jamii inayopakana na kambi hizo. Hali imekuwa tofauti kwa mahusiano kati ya Chita JKT ndani ya Jimbo la Mlimba, Wilaya ya Kilombero na Kata ya Mngeta, Kijiji cha Ikule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya wananchi wa Kijiji cha Ikule inasikitisha. Ni kwa miaka mingi wananchi wa kijiji hicho wanaishi na kufanya shughuli zao za kilimo kwa maisha yao yote. Hivi nichangiapo hapa na Waziri anajua wananchi wale wamenyang’anywa maeneo yote ya kilimo. Kibaya zaidi hata mazao yao ya chakula, mahindi, ndizi, mihogo, viazi, miwa, mpunga na kadhalika vyote vilifukiwa na trekta na baadhi ya wanajeshi na kuzuia kabisa kufika huko wakidai ni maeneo ya jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa wananchi na viongozi wa Serikali ngazi ya kijiji waliopo na waliopita wanasema na wako tayari kuongea popote kuwa hawajawahi kuidhinisha mashamba yao waliyokuwa wanalima miaka yote kabla hata ya kambi hiyo kuwepo hapo kuwa walikubaliana katika Mkutano wa Kijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi kwamba wameridhia kukabidhi hiyo ardhi kwa jeshi. Hivi niwasilishapo, tokea mwaka 2016 Desemba hadi leo, wananchi na viongozi wa kijiji, kata akiwemo na Diwani wa Kata hiyo wapo mahabusu kwa madai mbalimbali na hawajui hatma yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuundwe Tume huru kwenda kijijini hapo kutafuta ukweli wa masuala mbalimbali yanayoendelea huko, kwani inasemekana katika vurugu za kugombania mashamba, yuko mwanajeshi aliyeuawa. Pia zipo taarifa kwamba wananchi wengi nao wameuawa (habari ambazo hazijathibitishwa) na hali ya kijijini hapo si shwari hata kidogo, kwani wakati wowote wanajeshi huingia kijijini na kukamata na kupekua nyumba, hata wakati wa usiku na kuleta mashaka kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema uwepo wa Kambi ya Chita ni faraja kwetu na uhakika wa kiulinzi kwa raia, isipokuwa manyanyaso ndiyo karaha kwa majirani wa Kijiji cha Ikule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipate majibu ya Serikali. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nilindiwe dakika zangu.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hiii nafasi na naanza moja kwa moja kwa sababu dakika zenyewe tano, kwamba miaka mitatu mfululizo kwa mujibu wa vitabu vyao na takwimu zinaonesha kwamba Serikali ya CCM ilikuwa tunapitisha bajeti Bungeni mabilioni ya pesa, lakini ni asilimia 26 tu ya pesa tunazopitisha na Bunge ndiyo zinaenda kufanya kazi ya maji. Ndiyo maana tunapotaka kusema kwamba hii bajeti ukilinganisha na bajeti ya ndege yaani ni mara mbili ya bajeti ya maji. Sasa tukisema Serikali ya CCM kipaumbele chake ni ndege siyo maji mnakataa nini? Tukisema Serikali ya CCM inashughulikia maendeleo ya vitu badala ya watu mnakataa nini?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatari kwa Taifa letu, ndiyo hivyo hivyo Mheshimiwa Jenista siku ile alinipunja dakika zangu unamwona yule ameshaanza. Nilindie dakika zangu Mheshimiwa Spika.

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, Bunge lingekuwa live ingekuwa tamu sana. Hii taarifa siipokei kwa asilimia 220 kwa vile umekuwa Waziri sasa ndiyo maana unasema hayo unayoyasema, ulivyokuwa unakaa hapa mbona ulikuwa husemi hivyo, acha hizo wewe. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi namuuliza huyo aliyesema hiyo taarifa kama nyumbani kwake ana shilingi 100 na chakula cha watoto kinagharimu shilingi 80 na anataka aende akajenge nyumba ya shilingi 100, je atatoa 100 kwenda kujenga nyumba au atalisha kwanza watoto? Acha hizo wewe! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninasema hapa nikiwa na uchungu mkubwa, leo ndani ya Jimbo la Mlimba Naibu Waziri nakushukuru ulienda na mimi mama yako, uliona wananchi wa Mlimba walivyokulilia na wewe ukashuka ukalia nao. Machozi yananitoka, wanaimba Mlimba maji, Mlimba maji, mito mingi lakini kuna kisima kimoja, haki ya Mungu nasema akina mama, watoto, wazee wanapata maji kwa wiki moja mpaka wiki mbili kwa mzunguko. Naibu Waziri umewaona wananchi wa Mlimba, leo unaniambia kipaumbele ndege wewe Mungu atakulaani Kigwangalla, haki ya Mungu nasema hapa nikimaanisha. Ukiniambia leo kianze nini nasema maji, wananchi wa Mlimba wanataka maji. Kuna mito mingi lakini inatuharibu wakati wa mvua, inatupasulia nyumba, barabara lakini ikiisha mvua hakuna maji, nataka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipita na Naibu Waziri kuna mradi mkubwa wa umwagiliaji pale Njage, Kata ya Mchombe Serikali imeingiza hela nyingi lakini cha kushangaza ule mradi wanamwagilia wakati wa mvua, wakati wa kiangazi hakuna maji. Ndiyo maana tunaomba tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuchimba mabwawa ili kuleta tija kwa pesa mnazopeleka, kwa mfano pale Njage Serikali itenge pesa kwa kujenga bwawa ili tukinge maji ya mvua, tumwagilie na tupate mpunga masika na kiangazi.

Mheshimiwa Spika, maji ni uhai, hapa wote mmeoga maji, mnakunywa maji, hebu mkae hapa Mawaziri wote na wote tusioge angalau siku mbili tuone kama tutafungua air condition humu ndani! Maji ni kipaumbele.(Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niseme kwa Watanzania Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inashughulikia vitu siyo maendeleo ya watu hiyo haiwezekani. Muda haunitoshi mpaka nimelia.

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa yake naipokea kwa tahadhari kwa kuwaambia kwamba wananchi wa kule Jimboni kwake wanakunywa tope, tena pamoja na punda. Naikataa kwamba, kipaumbele, eti vitu kwanza, wewe vipi? Yaani wewe uanze kwanza kujenga nyumba watoto ndani wasile? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nyumba yenyewe unajenga na maji, viwanda vyenyewe maji, umeme Stiglers’ Gorge maji, kila kitu maji, leo unasema maji siyo kipaumbele. Tunataka kipaumbele kiende kwanza, halafu hivi vingine vitakuja, hamuwezi mkatunanihii, Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inafanya maendeleo ya vitu siyo maendeleo ya watu, ndiyo maana mnapeleka asilimia ndogo sana kwenye masuala muhimu kama ya maji. Naomba wapeni pesa hawa Mawaziri ili wafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hata kwenye Jimbo lako la Kongwa tunapita barabarani tunaona watu wanavyokwangua maji. Kwanza ni aibu barabara kubwa inayokuja Makao Makuu watu wanachota maji kwenye madimbwi, shame Tanzania, shame CCM. Hebu boresheni wapeni pesa za kutosha kama tunavyopitisha, ili watuletee tuwasulubu Mawaziri, kwa sasa hivi hatuwezi kuwasulubu wanajitahidi lakini hawana pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba Mheshimiwa Mnyika badala ya bajeti hii tufanye kweli, mbona tulifanya kweli kwenye Wizara ya Ujenzi, tuliweka mguu chini wakaenda wakajadili wakaongeza pesa na safari hii tuwaoneshe Bunge kwamba hawa lazima wapewe pesa ili miradi iongezeke huku chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na Mungu atusimamie.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Napenda kuunga mkono hoja mapendekezo ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, aseme ni lini ataenda Jimbo la Mlimba katika Kata ya Namwawala, Kata ya Mofu, Vijiji vya Idandu na Miyomboni ili kuweka utaratibu wa ujenzi na kilimo cha miwa ya sukari na wananchi waweze kunufaika ili kuwaondolea tabu wanazoendelea na kupata miaka mingi sasa bila kuwa na uongozi wa Serikali za Vijiji kwa kuwa ni eneo la uwekezaji wa kiwanda cha sukari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jimbo la Mlimba ni eneo la kilimo kikubwa cha mpunga, lakini Serikali haijaweka mkakati na uendelezaji wa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao kwa kuwawezesha kuwepo kwa viwanda vya uchakataji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi wa kwanza, hasa nikiwa kwenye Kwaresma hii na wiki hii ambayo ni ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na utawala bora katika hii wiki ya mateso, tumesikia kwenye vyombo vya habari Mkuu wa Majeshi alikuwa anamwambia Rais Magufuli kwamba yeye aachiwe kazi anachunguza mambo ya uchochezi kwa wanasiasa kwa kauli ambazo zinaenda kuvunjisha amani. Sasa katika utawala bora nataka Serikali inipe majibu, je, Mkuu wa Majeshi wa nchi hii amekuwa DPP? Anasema anafanya uchunguzi yeye anajiingiza moja kwa moja kwenye siasa? Y44eye ndiyo anataka kuiingiza nchi katika matatizo makubwa. Nakemea kwa nguvu zote na ashindwe katika Jina la Yesu. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Amen. (Makofi)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda katika masuala ya TAMISEMI kwa sababu nina dakika tano, niende moja kwa moja kuhusu masuala ya walimu.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu ni tano tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumpa taarifa ili tuliweke suala hili vizuri. CDF hakusema kwamba anachunguza wanasiasa, yeye alizungumzia masuala ya amani, utulivu, ulinzi na usalama kwa ujumla wake na hakusema wanasiasa, ni lazima tuliweke vizuri jambo hili. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine kauli zile hasa ambazo hatuna uhakika, zinazohusu viongozi wengine…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Tusikilizane vizuri, hasa ambazo hatuna uhakika nazo tuwe waangalifu kwa sababu mimi nilikuwepo na alisema wanafuatilia siyo wanachunguza. Kwa hiyo, ndio maana nasema tuwe waangalifu, sisi wenyewe ni viongozi na kauli wanazotoa wengine tunapotaka kuzisema kwa namna fulani tuwe na hakika na kile kilichosemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Susan Kiwanga, endelea.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nadhani umenilindia muda wangu. Hata kama nimekosea kusema lakini kufuatilia, yeye kwa mujibu wa Katiba anafuatilia masuala ya watu mbalimbali hapa nchini? Je, DPP atafanya kazi gani? Kifungu kipi cha Katiba
kinamruhusu yeye aseme anafuatilia wachochezi? Yeye alinde mipaka bwana ya nchi yetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya walimu, katika vitabu vyao TAMISEMI wanasema wanaenda kuajiri walimu elfu nne lakini ndani ya Wilaya ya Kilombero tuna upungufu wa walimu 1,018. Kati ya hawa walimu elfu nne watakaoajiriwa, je, elfu moja na zaidi ndiyo wanaenda Kilombero na wilaya nyingine watapata nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wajiri walimu, tumechoka kusubiri, elimu haisubiri. Watu wanazidi kuwa mambumbumbu huko chini, tunazidi kuliangamiza Taifa. Leteni haraka ajira za walimu na mishahara, posho na madaraja yao wapandishwe. Wafanyakazi nchi nzima hawajapandishwa madaraja, wanasoma lakini hawabadilishiwa mishahara. Naomba TAMISEMI na Utawala Bora mshughulikie masuala haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi nchi nzima hawajapandishwa madaraja, wanasoma lakini hawabadilishiwa mishahara. Ninaomba katika Utawala Bora na TAMISEMI mwelekeze hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala maalum. Ndani ya Jimbo la Mlimba kuna masuala mengi ambayo yanahusu TAMISEMI. Kuna madaraja kuhusu TARURA. Naomba TARURA waongezewe hela ili tupate kujengewa madaraja na barabara katika maeneo yetu, kwa sababu tumechoka kusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhusu masuala ya maji, pale Mlimba hakuna maji, kuna kisima kimoja tu na ule mji unazidi kukua. Kwa hiyo, tunahitaji maji ya kutosha ili wananchi wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Mlimba, ni miji. Ndani ya Jimbo la Mlimba kuna miji kadhaa ambayo inakua ovyo ovyo. Ilishatamkwa kwamba kuna Mji Mdogo wa Mlimba, lakini mpaka leo unatamkwa vijiji. Katika bajeti hii na uchaguzi unaokuja, tunaomba Mlimba tusitoe tena vijiji, tunataka tuchague vitongoji. Kwa hiyo, TAMISEMI nawaomba chonde chonde angalau mtupe mji mmoja wa Mlimba ili tuone tunapanga vizuri mji wetu usiwe ovyo ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya uendeshaji wa miji midogo. Sasa kama Mlimba hakuna miji midogo, miji haipangwi tutaendeshaje hiyo miji. Kwa hiyo, naomba chonde chonde haya mambo yafanyike. Nitafurahi sana na wananchi wa Mlimba watafurahi sana kama mtatangaza Mji Mdogo wa Mlimba uanze kazi katika Serikali ya Mitaa hii inayokuja, wachague vitongoji siyo viji tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya Tume Huru ya Uchaguzi. Tume Huru ya Uchaguzi ni muhimu sana. Kiatu usichovaa huwezi kujua kinabanaje. Nimeshuhudia mwenyewe kule Malinyi, Sophy, Mkurugenzi anamtangaza Diwani wa CCM aliyeshindwa kwa kula 29 anamtangaza wa CCM anamwacha wa CHADEMA. Mpaka leo nina kesi Mahakamani. Ili kuvunja soo, wakanikamata wakanipeleka mahabusu ili nisifuatilie hiyo kesi Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo utawala bora sisi ndio tunaumia, sio ninyi mlioko upande huo. Nilisikitika sana na Kwaresma hii, ndugu yangu Mheshimiwa Jenista akisema Tume iko huru, sijui nini. Uhuru gani? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii kwa muda mrefu inabadili matamko kuhusu kilimo, lakini hakuna tamko hata moja lililofanikiwa katika kuboresha kilimo na kuleta matokeo chanya. Kwa mfano pamoja na Serikali kusema Mkoa wa Morogoro ni ghala la chakula, lakini ukifuatilia kwenye mkoa huo hakuna jitihada za makusudi za kuufanya mkoa huo kuwa ghala la chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kumaliza tatizo la wakulima na wafugaji, kuboresha upatikanaji wa pembejeo, kuajiri wagani hasa Jimbo la Mlimba ambapo hali ya wataalam wa kilimo na mifugo ngazi za kata hakuna. Kwa hali hii kilimo kitakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko la mchele Serikali kwa miaka yote hamumtendei haki mkulima wa mpunga na kumuacha mkulima kutokuwa na soko la uhakika na kumuongezea umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itilie mkazo uanzishaji wa mabwawa ya samaki ili kuboresha maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba lenye vijiji 61 na kata 16 maji tunayapata wakati wa mvua (masika) na yakija yanaharibu makazi, barabara, mashamba na kadhalika. Kuhusu maji safi na salama, wananchi wa Jimbo la Mlimba kwao ni tabu sana.
Mfano, katika Mji Mdogo wa Mlimba, Kata ya Mlimba kuna kisima kimoja ambapo maji yanapatikana kwa mzunguko wa wiki mara moja tu. Kata nyingine 15 na kwenye shule za sekondari, za msingi na kwenye zahanati hakuna maji kabisa. Hivyo, naomba Mheshimiwa Waziri/Naibu Waziri aje Mlimba ili ajionee mwenyewe hali ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwenye Taarifa/ Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu mradi wa mfereji wa umwagiliaji Kijiji cha Njage kuwa mradi huo unaleta tija. Ukweli ni kwamba mradi huo hauna faida wala tija kwa wananchi kwani, ingawa ni umwagiliaji mfereji huo hauna maji wakati wa kiangazi, bali wakulima hulima wakati wa masika tu, hivyo hulima kwa mwaka mara moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Mawaziri waje Jimbo la Mlimba washuhudie miradi iliyopo huko ambayo haina mwendelezo. Napendekeza pesa ikusanywe kwa kuweka tozo kwenye sigara, maji ya chupa, soda, bia, ili ziingie kwenye Mfuko wa Maji na fedha hizo mjini zipelekwe asilimia 30 na vijijini asilimia 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu katika maeneo machache ambayo napenda kupata majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ahadi ambazo Waziri Mkuu amezitoa bado kuna mgogoro wa wananchi wa Kata ya Mngeta, Kijiji cha Ikule na Vitongoji vyake na JKT Chita ambapo Jeshi limechukua ardhi kubwa ya kilimo bila maridhiano wala muhtsari wa Kijiji na JKT Chita kumiliki eneo lote kwa kulichukulia hati Wizara ya Ardhi na kujipa uhalali pasipo wanakijiji kushirikishwa na kusababisha umaskini mkubwa kwa wananchi hasa ukizingatia wote wanategemea kilimo na hawana ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu alinitamkia/ kuwatamkia wawakilishi wa Kijiji/Kata walipofika ofisini kwake Dodoma mwaka 2016 kuwa angeagiza mazungumzo yawepo ili kupata muafaka wa suala hilo ambapo alishauri katika eneo lenye mgogoro ni vema kila mmoja akapata na kupoteza na si kundi moja kutaka kutwaa eneo lote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi niandikapo hakuna utatuzi isipokuwa ni vitisho kwa wananchi. Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na Waziri wa Ulinzi wameshindwa kusimamia utatuzi wa mgogoro huu isipokuwa ni vitisho. Hali ya wananchi inaendelea kuwa dhaifu kwa kukosa maeneo ya kilimo na kusababisha umaskini mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo la vijiji viwili vya Idandu na Miyomboni vilivyopo Kata ya Mofu na Namwawala, Jimbo la Mlimba kutoruhusiwa kufanya uchaguzi wa vijiji hivyo tangu mwaka 2014 kwa hoja kuwa eneo hilo ni la uwekezaji na toka wakati huo hakuna aina yoyote ya uwekezaji uliofanyika. Hii inasababisha wananchi kukosa uongozi wa kusimamia au kuhamasisha maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni lini sasa Ofisi ya Waziri Mkuu itakwenda kuyapatia ufumbuzi masuala hayo yanayoleta kero kubwa kwa wananchi wa vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwa kuikumbusha, kuisisitiza Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya Ifakara – Mlimba – Taweta hadi Madeke Njombe. Barabara hii imeshafanyiwa upembuzi wa kina kuanzia Ifakara hadi Kihansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe. Vilevile Jimbo la Mlimba lina uzalishaji mkubwa wa mpunga, mahindi, ufuta, ndizi, cocoa na miti ya mbao (mitiki) ambapo yanapita magari makubwa ya tani 15 hadi 30 na kuifanya barabara hiyo ambayo ni ya vumbi na udongo chepechepe na ina mito mingi ambayo hutiririka mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inapita kwenye shamba kubwa la KPL la mwekezaji wa Kimarekani anayelima mpunga na mahindi kwa njia ya umwagiliaji na kufanya usafirishaji mazao kuwa mgumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa barabara hii ni kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na watoto ambapo wanaposhindwa kujifungua huhitaji kukimbizwa Hospitali ya Rufaa St. Francis iliyopo Ifakara kwa sababu Wilaya au Jimbo la Mlimba hakuna hospitali ya uhakika na kwa hiyo husababisha vifo vingi vya wazazi. Hivyo tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa daraja la Kilombero limeshaanza kutumiwa na kwa kuwa kivuko kilichokuwa kinavusha abiria hakina kazi tena hapo darajani, hivyo basi Wilaya ya Kilombero tunaomba na tulikwisha omba kivuko hicho tukabidhiwe ili kikatumike kuvusha wananchi kwenye Jimbo la Mlimba eneo la Kikoi, Kata ya Utengule, Kijiji cha Ngalimala ambako Mto Kilombero unatenganisha Wilaya ya Kilombero na Wilaya ya Malinyi. Hii ni kwa sababu miaka yote wananchi wanatumia mitumbwi ambayo ni hatari na si salama kwa usalama wa wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano katika baadhi ya kata na vijiji vya Jimbo la Mlimba yanapatikana kwa shida sana. Hivyo ni muhimu kusambaza huduma hiyo hasa kwa kuliwezesha Shirika la TTCL kwa kutumia Mkonga wa Taifa ili kuimarisha mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA ni muhimu ikawezeshwa ili itengeneze madaraja na barabara zinazounganisha kata na kata, kata na vijiji hata vitongoji ambazo zimeanzishwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlimba lina mito mikubwa inayotenganisha kata na vijiji na kusababisha wananchi wengi kukosa huduma. Pia Kata ya Uchindile imetenganishwa kabisa na Makao Makuu ya Jimbo. Hivyo naomba muone umuhimu wa Jimbo la Mlimba kutengewa pesa za kutosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni muhimu kwa maisha ya watu na kiuchumi pia, na ndiyo Wizara inayoweza kutupeleka kwenye nchi ya viwanda kwa upatikanaji wa malighafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipeleke fedha za kutosha ili kuiwezesha Wizara hii kufikia uchumi wa kati. Ili Watanzania waweze kuishi na wawe na afya bora lazima wale chakula kinachozalishwa nchini na wakulima waishio vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wakulima hao kulima kwa bidii bila hata msaada wa kitaalam, inafika mahali Serikali inamuwekea masharti mkulima huyo namna ya kuuza mazao yake. Huu utaratibu haukubaliki na unakandamiza mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi tuliyonayo ni kubwa na inafaa kwa kilimo, lakini ni kwa nini Serikali haiandai mipango bora ya kutumia ardhi hiyo kuzalisha mazao ambayo yatasababisha nchi kuuza nje ya nchi. Matokeo yake Serikali inafunga mipaka kwa mazao kama mpunga, mahindi, kahawa na kadhalika na kumzidishia umaskini mkulima mdogo kwa kushindwa kuuza mazao yake na kusababisha mazao hayo kuharibikia kwenye maghala ya kienyeji. Serikali iwe na huruma kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba ni eneo la kilimo, wananchi wanalima mazao ya biashara na chakula ambayo ni mpunga, mahindi, ufuta, ndizi, kokoa, alizeti, miti na pia ni eneo la SAGCOT lakini barabara za vijijini na barabara kuu hazipitiki kwa mwaka mzima na kusababisha mazao hayo kununuliwa kwa bei ya chini na kumuongezea umaskini mkulima. Nashauri Wizara ione haja ya kuwezesha jimbo hilo kupata pesa za kujenga masoko ya kisasa ili kupata urahisi wa kuuza mazao hayo kwa bei zinazokubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika umeleta taharuki kwa wananchi wa Tanzania hususan Wilaya ya Kilombero. Viongozi wengi takribani asilimia 95 ya viongozi wa vyama hivyo wamefanya ubadhirifu wa fedha na mali za ushirika. Matokeo yake sasa eti wameunda timu ya kukusanya madeni matokeo yake, wanatoza tozo watu na viongozi walioua ushiriki ndiyo wanaoshirikiana nao. Ushahidi upo na viongozi hao walioua ushirika wapo, lakini hawajachukuliwa hatua yoyote. Hili halikubaliki kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuunga mkono hutuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naishauri Serikali izingatie ushauri uliotolewa katika hotuba ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala uchafuzi wa mazingira na kukosekana kwa usimamizi mzuri unasababisha uharibifu wa mazingira. Nani asiyejua uidhinishaji/usajili unaofanywa wa viwanda ambavyo ni hatari kwa mazingira yetu? Hivyo basi, pamoja na kauli ya Waziri Mkuu kupiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki, je, kauli hiyo imeenda sambamba na ufungaji viwanda vinavyozalisha mifuko hiyo? Je, kauli ya Waziri Mkuu inaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi hasa vijijini? Nina mashaka makubwa na faini/ vifungo watakavyopata wananchi hasa vijijini. Naishauri Serikali itangaze kufunga viwanda vya utengenezaji mifuko hiyo mara moja na elimu itolewe kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ukataji wa miti unakithiri kila mwaka na hakuna jitihada za upandaji miti hali ambayo inasababisha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa. Serikali iweke mkazo katika upatikanaji wa gesi na umeme vijijini na mijini kwa matumizi ya viwanda, magari na majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri Serikali ipeleke miradi ya ufugaji nyuki kwa wananchi vijijini. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2010 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyosomwa na Mheshimiwa Salome Makamba kwa niaba ya Mheshimiwa Lisssu Antiphas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba lenye Kata 16, Serikali imeanza ujenzi waMahakama ya Mwanzo, Kata ya Mlimba na jengo limefika juu (boma). Ingawa boma limeisha mwanzoni mwa Machi 2019 lakini vibarua wa ujenzi ambao ni wakazi wa Mlimba ambao idadi yao yapata 19 hivi hawajalipwa. Je, huyo mkandarasi hajalipwa hadi ashindwe kulipa waliofanya kazi? Naomba mkandarasi huyo afuatiliwe na awalipe vijana hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Polisi kukamata watuhumiwa walioachiwa na Makahama na hapo hapo Askari Polisi kuwakamata kwa kutumia kifungu 225. Kifungu hicho kimepitwa na wakati kwani kinasababisha mlundikano wa mahabusu kwenye magereza na vituo vya polisi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri viongozi wa Wizara hii watembelee magereza nchini na magereza zote zaMkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwepo muda maalum wa kuchunguza kesi za jinai nchini kwa kuwa magerezani kumekuwa na wananchi wengi na wanakaa muda mrefu hadi miaka 10 mahabusu kusubiri kukamilika kwa upelelezi. Upo ushahidi usio na shaka kwa mahabusu wengi kusota maregeza muda mrefu kwa kuwa hawana msaada wa kisheria na pesa za kutoa rushwa kwa wapelelezi. Nashauri mtembelee magereza na kuongea na mahabusu ili mpate taarifa muhimu zinazohusu rushwa.