Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Philipo Augustino Mulugo (25 total)

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza na-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyoongea, kuna vikao kadhaa vinaendelea kati ya Wamiliki, Mameneja na Serikali, Ofisi ya Kamishna Wizara ya Elimu, lakini mpaka sasa hatujafikia muafaka kwa sababu ya hiki ambacho amekiongea Mheshimiwa Naibu Waziri. Tunaonekana kama vile tunafanya mchezo, lakini jambo hili ni gumu sana. Shule zimetofautiana, wapo wamiliki wamewekeza na wamekopa fedha benki. Zipo shule zina utofauti wa vijijini na mjini. Menu ya chakula huwezi kulinganisha menu ya chakula shule za Dar es Salaam na shule za Rukwa, Mbeya ama Mwanza. Hata hivyo, mpaka wiki iliyopita, tumekutana na Serikali kwamba hata hawajafanya utafiti kwenye shule za msingi lakini ada elekezi inataka kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali, ni lini Serikali itaita tena kikao cha mwisho TAMONGSCO pamoja na Serikali wakae pamoja waweze kufanya utafiti wa pamoja? Serikali ifanye utafiti na shule binafsi zifanye utafiti ili wakae pamoja waweze kufanya negotiation ili ada elekezi itolewe si kwa upande mmoja tu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshawahi kukaa na wadau hao, lakini niseme tu kwamba ni msingi huo huo ambao Serikali haitaki kuwanyanyasa wawekezaji wake ambao ni Washirika wakubwa wa elimu na ndiyo maana tumefanya tafiti katika maeneo mbalimbali. Mfano, tumeshakwenda katika maeneo hata ya vijijini, kuna shule za Sekondari kama Fingwa kule Rukwa, Idigima-Mbozi na Kitunda kule Kalambo, hizo zinatoza laki moja kule vijijini kabisa kwa Sekondari lakini ukienda kwenye shule nyingine, kama Feza yenyewe inatoza shilingi milioni 9.4, ukichukua St. Joseph shilingi milioni 5.9, ukichukua Mwanza Alliance shilingi milioni 4.8 na ndiyo maana tunafanya utafiti ili kuona kwamba bei zitakazotolewa kwanza zitapangwa kutegemeana na madaraja na shule mahali ilipo na uhalisia wa utoaji wa hiyo elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo siyo lengo la Serikali kuwatesa au kuwanyanyasa wawekezaji, bali ni kutoa bei inayofanana na uhalisia na hiyo itachochea utoaji wa elimu bora, lakini vilevile uwekezaji ulio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kikao napenda niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge, si kwamba Wamiliki tu wa shule ndiyo wanaostahili kukaa vikao, vikao hivi vitawashirikisha hata walezi pamoja na wazazi, pamoja na wananchi wengine ikiwemo Wabunge ili tupate bei zenye uhalisia.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu suala la elimu na TAMISEMI tunaguswa sana na bahati nzuri Naibu Waziri wa Elimu ametoa maelezo ya kutosha, kulikuwa na suala lini litafanyika hili, maana yake hili ndiyo suala la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba Naibu Waziri ameshazungumza kwamba, hicho kikao kitaitwa na hili naomba nikiri wazi, kwa sababu nchi yetu ni pana sana, lengo kubwa la Serikali ni kui-support private sector, lakini pia kuangalia na watu hao wanaopata huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kwamba, mchakato huu ni mpana kwa kushirikiana na wadau wote, imani yangu ni kwamba, tutakapofika mwisho wa siku hasa wamiliki wa shule na ndugu yangu Mulugo akiwa mmojawapo, tutafika maeneo ambayo Mtanzania wa kawaida wa kila level ataweza kuguswa kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi niweze kuuliza swali lanyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Songwe naomba niiulize Serikali. Rais Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Songwe ambapo sasa ni Wilaya mpya aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbalizi - Mkwajuni - Makongorosi na tayari Serikali 2013 imeshafanya upembuzi yakinifu lakini baada ya hapo hakuna kinachoendelea. Je, Serikali ni lini itaanza sasa ujenzi wa lami wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwasiliana na Mheshimiwa Mulugo kuhusu barabara hii. Najua unaifuatilia sana, ni haki yako kuifuatilia na ni wajibu wako na sisi ni wajibu wetu kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu barabara hii iko katika Ilani. Naomba tu kumhakikishia kwamba kama ambavyo tumeitaja katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kama ambavyo wewe unafuatilia utekelezwaji wa Ilani hiyo, tutatekeleza katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Sika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Songwe hatuna maji kabisa, hivi ninavyoongea ule Mji unakua, watu wanahamia kwa wingi sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura na kwa haraka tuweze kupata maji katika ule Mji ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na Mkuu wa Wilaya atakuja hivi karibuni pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wengine wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeelekeza kupitia bajeti hii tuliyonayo kwamba tumetenga fedha katika Halmashauri ili Halmashauri zile ziweze kutekeleza miradi ya maji katika maeneo yao, lakini pia tumeelekeza kwamba Halmashauri zifanye utafiti wa kujenga mabwawa na wakishafanya utafiti walete taarifa Wizara ya Maji ili tuangalie katika mwaka wa fedha utakaofuata, tuweze kutoa fedha za kujenga mabwawa kuhakikisha kwamba miji yetu hii inakuwa na uhakika wa kupata maji, lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge, ile fedha tuliyoitenga katika Halmashauri yako, naomba sana ushirikiane na Halmashauri ili ile fedha itumike katika kuhakikisha kwamba kwasababu ile Wilaya ni mpya, maji na upungufu utakaokuwa umejitokeza, basi naomba sana tuwasiliane.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza nipende tu kusikitika tu kwamba sijui Serikali inafanya kazi kwa upendeleo baadhi ya Wilaya zingine. Tumekaa RCC iliyokuwa Mkoa wa Mbeya na Mheshimiwa Mwambalaswa na Mheshimiwa Mary Mwanjelwa mashahidi hapa. Tumepitisha barabara za Chunya mbili kutoka Ngwala mpaka Kapalala na kutoka Gua ziende ziwe hadhi kwa Mkoa ziwe kwenye TANROADS, toka mwaka 2011 tulikaa RCC tukapitisha leo bado Serikali inasema tunafanyia kazi, miaka sita mnafanyia kazi? Mimi binafsi nimesikitika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti narudia tena, naomba Serikali inijibu kwasababu tayari Songwe imeshakuwa ni Wilaya mpya ni lini watatupatia fedha tupandishe hadhi barabara ya hiyo kutoka Kininga kwenda Ngwala ni kilometa 46. Nikitaka kufanya ziara kule nitembee kwa bodaboda na watu wananielewa hivyo na kuna wanyama wakali na kuna ndorobo nahangaika sana.
Naomba leo Serikali inipe majibu tunahangaika sana wenzenu. Mbona sehemu zingine barabara mnatengeneza? Kutoka mwaka 2011 mpaka leo hatujatengeneza barabara. Naomba Mheshimiwa Waziri uniambie hapa hapa, utaniletea lini barabara hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumfahamisha kwamba Serikali hii haifanyikazi kwa upendeleo. Watanzania wote sisi kwetu ni sawa na nia ya Serikali hii ni kuwajengea miundombinu ya kisasa Watanzania wote. Kama uko Mbeya, kama uko Mwanza, kama uko Shinyanga kazi yetu ni kuwajengea Watanznia miundombinu ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli imechukua muda mrefu na tatizo kubwa ambalo tunalo ilikuwa ni fedha, fedha, fedha, lakini Serikali yetu ya Awamu ya Tano sasa tumejipanga na tutahakikisha kwamba siyo muda mrefu barabara zote tutaanza kuzipandisha hadhi. Lakini naomba waelewe tu changamoto tuliyonayo ni fedha, fedha kwa sababu ukipandisha hadhi barabara maana yake ni fedha unataka utengeneze sasa kwa kiwango cha juu zaidi.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kule jimboni kwangu, Jimbo la Songwe na wilaya mpya, kuna kampuni moja inaitwa Sun Marie, walipata leseni mwaka jana mwezi Aprili kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe Kata za Magamba na Namkukwe Jimboni Songwe, lakini mpaka sasa hawaonekani walipo. Walikuwa wanafanya utafiti wa kujenga barabara mpaka sasa hatujajua wako wapi, Halmashauri haiwajui, tunaomba msaada wa Serikali, hawa watu kwanza wako wapi na ni lini wataanza kazi za uchimbaji wa madini haya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kampuni anayoitaja Mheshimiwa Mulugo ipo katika eneo lake na kwa sasa hivi imepewa miaka saba kwa ajili ya kukamilisha utafiti. Miaka mitatu iliyobaki ya utafiti ni matarajio kwamba watakamilisha na waanze kuchimba rasmi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mulugo avute subira ni matarajio baada ya miaka mitatu watakamilisha feasibility study na wataanza uchimbaji. Kwa hiyo,
baada ya miaka mitatu Mheshimiwa Mulugo atawaona wanakuja huko na magreda kwa ajili ya kuanza uchimbaji kama feasibility itaonesha kuna madini hayo
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali maswali mawili tu ya nyongeza. Katika mpango wa Serikali wa kujenga nyumba 4,136, nataka tu kujua: je, Wilaya yangu ya Songwe ambayo ni wilaya mpya, itajengewa nyumba ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mgao huo, ni pamoja na Askari Magereza pamoja na hawa Askari Polisi wa kawaida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu ya msingi ni kwamba Mkoa mpya wa Songwe ni moja katika mikoa ambayo itafaidika na awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 4,136.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kwamba Wilaya yake ya Songwe itahusika ama la, labda nichukue ili tuweze kulifanyia kazi, lakini ninachojua ni kwamba mkoa mzima utafaidika, kwa maana hiyo mgawanyo huu utafanyika kwa wilaya zote za mkoa mzima. Sasa kuhusiana na kiwango cha nyumba ngapi zitakwenda Wilaya ipi na ipi, takwimu hizo siwezi kumpatia kwa sasa hivi, lakini nitakapokuwa nimefanya utafiti, tutaweza kumjulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba je, katika suala hilo la ujenzi wa nyumba hizo Magereza wanahusikaje? Magereza wana mpango wao vile vile wa ujenzi wa nyumba ambao wao nyumba zao ni nyingi zaidi; zaidi ya nyumba 9,500 kama sikosei kwa ajili ya Magereza ambapo ni nyumba nyingi zaidi ya hizi za Polisi kwa nchi nzima.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza Naibu Waziri kwa majibu sahihi aliyoyatoa na pia nampongeza sana Mheshimiwa Mulugo kwa sababu amekuja mara nyingi sana ofisini kufuatilia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mulugo, pamoja na mikoa yote mipya kwamba tutatoa kipaumbele kwa mikoa hiyo kwa sababu, licha ya makazi ya askari kutokuwepo, hata nyumba tu za kawaida za kupanga katika mikoa ile mipya na wilaya mpya ni kazi sana kwa Askari hao kupata tofauti na maeneo mengine. Kwa hiyo, tutalizingatia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la faraja la kwanza, wakati tunaendelea kujadiliana, tutalifanyia kazi kwa umakini zaidi suala la pango allowance ambayo maaskari wetu wamekuwa wakipewa, kwanza kuwaondolea usumbufu.
Pili, kutengeneza utaratibu ambao utaendana na kiwango ambacho kina-reflect bei zaidi ya soko tofauti na sasa ambapo askari anapata asilimia 15 akiwa ngazi ya chini lakini hata akipanda, kiwango kile kinaendelea kuwa kilekile licha ya mshahara wake kupanda.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Songwe, kila wiki umeme upo siku tatu na umeme haupo siku nne mpaka hivi ninavyoongea, hata wiki iliyopita nilikuwa huko. Nini tatizo la
kukatika katika kwa umeme hasa ule unaotoka Mbeya Lwanjilo, Chunya, Makongolosi mpaka Mkwajuni. Tatizo ni nini kila mwaka maana huu ni mwaka wa nne sasa hatuna umeme wa uhakika pale Mkwajuni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa maeneo mengi umeme tulionao haujitoshelezi ndiyo maana tunarekebisha na kuimaisha miundombinu ikiwemo Mkoa wa Mbeya pamoja na mikoa
ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tuliyochukua kwa
sasa tunajenga mradi wa kusafirisha umeme wa KV 400 kutoka Mbeya kupita Sumbawanga kwenda Kigoma hadi Nyakanazi, lakini huo huo utakwenda mpaka Bulyanhulu na Geita umbali wa kilometa 1,108. Kwa hiyo, hatua hii itakapokamilika katika Mkoa wa Mbeya tatizo la umeme litapungua sana. Matarajio yetu, kufikia mwezi Julai, 2018 matayarisho, ujenzi pamoja na
uimarishaji wa njia za kuimarisha umeme katika Mkoa wa Mbeya utakuwa umekamilika. Kwa hiyo, kuanzia Julai mwakani kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Mbeya kutapungua au kutakoma kabisa kwasababu ya kutekelezwa kwa mradi huu.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ambayo kidogo hayajatosheleza, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hamu na haja ya Waheshimiwa Wabunge wengi, toka nimeingia Bungeni hapa mwaka 2010, Wabunge wengi wanahitaji sana mabadiliko ya sheria ndogo ndogo ili mambo yaweze kuendana na wakati. Iko Sheria ya Ndoa ambayo inasema lazima mtoto awe na miaka 14 kuweza kuolewa; lakini mimi nimekuwa mwalimu muda mrefu, najua miaka 14 kwa sheria ya leo ilivyo ya elimu msingi, anakuwa bado ni mtoto yupo form two na tunasema elimu msingi mtoto atoke chekechea mpaka form four na ni elimu ya lazima. Kwa hiyo, unakuta ile sheria imepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi nilisema hapa kuhusu Sheria ya TMAA ya Madini kwamba Halmashauri kule zinapata ile ruzuku (service levy) ambayo unakuta hawajui source yake imetoka wapi kwa sababu hawashiriki katika kuangalia pato lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ipo Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, imepitwa na wakati. Sasa yote hayo nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka 1980 Serikali iliunda Tume kwa ajili ya kuangalia Sheria Mbalimbali na mabadiliko ili iweze kuletwa Bungeni, mpaka leo Tume hiyo ni kama vile imeshindwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Bunge liwe na Tume yake, Serikali iwe na Tume yake ili na sisi tuonekane kweli tunatunga sheria. Maana toka nimekuja mwaka 2010 hapa sijawahi kuona Mbunge kaleta hoja binafsi hapa na ikapita. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wana hoja binafsi nyingi, lakini wakileta hapa hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iruhusu Bunge liwe na Tume ili sisi wenyewe tuanze kutunga sheria na Serikali iwe na Tume, tuzilete pamoja tuweze kujadili ili tuweze kufanya marekebisho ya sheria kadri mambo yanavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali italeta hoja ya kuruhusu Bunge iwe na Tume yake binafsi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza la Sheria kuliruhusu Bunge kuwa na Tume yake, liko nje ya mamlaka na uwezo wangu, kwa sababu ni suala la Bunge lenyewe, lakini nitalitolea indhari, haitakuwa muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kazi za Tume hii, Tume hii imefanya kazi nyingi na baadhi yake zimezaa matunda. Kwa mfano, sheria ambazo zimetokana na utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania ni pamoja na Sheria ya Upimaji wa Vinasaba wa Binadamu (The Human DNA Regulation Act No. 8 of 2009); Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act No. 21 of 2009); Sheria ya Makazi na Mahusiano Kazini (The Employment and Labour Relations Act No. 6 of 2004); Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (The Disability Act No. 9 of 2010); hizi ni baadhi ya sheria tu ambazo zimetungwa kutokana na kazi ya Tume ya Kurekebisha Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa iko Sheria ya Ndoa ambayo mchakato wake unaendelea kuhusu moja, umri wa mtoto kuoa na kuolewa. Niseme leo, kuna jambo ambalo haliko sahihi; ukiangalia kuhusu umri wa miaka 14, naomba mwende muisome ile sheria, inaruhusu mtoto wa kike kuolewa na miaka 14 na mtoto wa kiume kuoa na miaka 14.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kile mwaka 1971 kiliwekwa ili kukidhi mahitaji ya jamii mbili, Wamasai na Mabohora. Sasa ikifika wakati hali imebadilika, umuhimu huo haupo, tutalijadili. Kwa hiyo, umri wa miaka 14, someni sheria, siyo kwa msichana tu, ni kwa hata mtoto wa kiume kuruhusiwa kuoa chini ya miaka 14 kama Mahakama imeruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakubali, mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hajafikia umri wa kuoa; na mtoto wa kike kuolewa miaka 14 hajafikia umri wa kuolewa, lakini jambo hili linataka mwafaka wa kijamii kama ambavyo mwaka 1970 ilikuwa ni muhimu kuwaangalia Wamasai na Mabohora ambao ni sehemu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maadam mchakato unaendelea, tunaendelea kuzungumza Inshallah siku itafika, jambo hilo litapita.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa upendeleo wa kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Songwe lina uhaba mkubwa sana wa maji lakini niongelee Kata moja inaitwa Totowe ambapo mimi mwenyewe kwa juhudi za Mbunge niliomba mradi wa Mheshimiwa Sabodo nikachimba kisima kikubwa sana na kisima hicho mpaka ninavyosema hivi bomba hilo linatoa maji kutoka mwaka 2012 mpaka leo yanatiririka na yamesambaa pale kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuomba pale Halmashauri angalau watupe fedha hata shilingi milioni 50 tuweze kujenga tanki la kutunzia maji yale angalau yaweze kusambaa vizuri kwa kujenga mabomba kwa wananchi wa Totowe na maeneo ya Namambu. Je, Serikali inanisaidiaje mimi kama Mbunge nimefanya juhudi kutafuta maji halafu maji yanatiririka bila kujengewa tanki ili angalau wanipe fedha nikajenge tanki maji yaweze kuenea pale Totowe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mweyekiti, alichokisema ni kweli. Baada ya kumaliza Bunge mwezi wa Julai, nitamwomba Mheshimiwa Waziri nianze na Mkoa wa Songwe kwa sababu Halmashauri za Mkoa wa Songwe katika suala la utekelezaji wa miradi ya maji hawakufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Katibu Mkuu anaongea nao kule Morogoro ili kuona hizi Halmashauri ambazo haziku-perform vizuri zina matatizo gani wakati tulitoa maelekezo baada ya bajeti wanatakiwa kufanya manunuzi, lakini hawakufanya manunuzi kabisa. Nitakapokuwa nimekwenda tutaliangalia hili na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuweka utaratibu wa kwenda haraka wananchi wapate maji.(Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku nimekuwa nikilalamika hapa kwamba Wilaya ya Songwe, Mkoa mpya wa Songwe na hasa Jimbo langu lina Vijiji sita tu vyenye kutoa maji, vijiji vingine vyote 28 hakuna maji. Je, ni lini yeye mwenyewe kama Waziri anakuja Songwe mimi na yeye tutembee siku nzima nimwoneshe sehemu ambazo wananchi wa Songwe wanalalamika maji, hususan ni maeneo ya Mbangala, Mbotoe na Mkajuni. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini nitatembelea Wilaya ya Songwe, nimepanga kuanzia Jumatatu kufanya ziara katika Mikoa ya Ruvuma na Songwe. Kwa hiyo, nitakwenda Songwe kwenda kuangalia malalamiko ya Mheshimiwa Mbunge na tuweze kuona namna ya kusaidiana. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni kwangu Kata ya Mbangala nina Kampuni inaitwa Shanta Gold Mining. Kampuni hiyo imefunga Mto Lwika na kusababisha wananchi wa Mbangala kutopata maji. Miezi miwili iliyopita kulitokea vurugu kubwa sana kati ya Polisi na vijana wa pale Mbangala lakini Serikali ipo na wanaona kabisa bwawa limefungwa na mto hautiririki kwenda hata vijiji vya Maleza. Je, Serikali inaniambia nini juu ya Ashanti wafungue ili na sisi kijiji cha Mbangala tuweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kampuni ya Shanti kufunga bwawa Mbangala, Mheshimiwa Mbunge ndiyo anatoa taarifa sasa hivi. Naomba tuwasiliane ili tuhakikishe tunatatua hili tatizo kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo itakuwa ni mara ya pili nipende tu kusikitika kwamba swali hili tena halijajibiwa na Bunge lililopita mwezi Novemba, swali langu nalo halikujibiwa vizuri sasa sijui nina mkosi gani. Kwa sababu swali la msingi haliendani kabisa na majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali langu la kwanza liwe hivi. Naomba Serikali iniambie inatumia mfumo gani wa kuwajibu maswali Wabunge humu ndani, kwa sababu Wabunge wengi wamekuwa wakilalamika maswali hayo hayajibiwi vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, bado niseme namuomba Waziri tena Waziri mwenye dhamana aje Jimbo la Songwe afanye ziara aangalie jinsi ambavyo vijiji vyangu na kata vilivyo scattered ili aone umbali wa kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine, karibuni kilometa 20 hapa, ndipo wanaweza kujenga vituo vya polisi. Lakini kunijibu kwamba kipaumbele ni RPC na OCD wala haviingi akilini naomba Mheshimiwa Waziri mwenyewe anijibu.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mulugo; ni kweli anafuatilia sana masuala ya Jimbo lake na hasa haya yanayohusu askari kufuatana na aina ya Wilaya yake na aina ya Jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa sababu la msingi na ushauri alioutoa ni kufika kule, nimuahidi baada ya Bunge hili kabla ya Bunge la Bajeti nitazungukia Wilaya yake kule ili nijionee mwenyewe haya anayoyasemea ili tuweze kutengeneza utaratibu ulio mzuri wa kushughulika na jambo hilo alilolielezea.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kuweza kupata muda wa kuuliza swali moja la nyongeza. Mamlaka ya Wanyamapori maeneo ya Ngwala, Itiziro na kule Guwa wamevamia vijiji hivyo na hivyo wamewasambaza wananchi, wamewanyang’anya mashamba, wamenyang’anya mbao na mali zao nyingine; na Mheshimiwa Naibu Waziri nilikwambia. Sasa nataka Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie humu ndani mbele ya Bunge kwamba ni lini tutaongozana mimi na yeye twende tuka-solve mgogoro huo kwa ajili ya wanyamapori maeneo ya Ngwala?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kama ulivyoelekeza, ni kwamba kwanza mpaka unahusisha pande mbili na ni vigumu sana upande mmoja kusema mwingine amemwingilia mwingine kwenye mpaka wake. Nafikiri njia sahihi, wote wawili wanaweza wakawa mahali pamoja halafu kila mmoja akaangalia vigezo nani ameingia kwa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake, lini tutaweza kwenda; nilimwambia kabla na narudia tena kusisitiza, tukimaliza Bunge hili la Bajeti mimi na yeye tutapanga ratiba ambayo itakuwa ni rafiki, twende kwenye maeneo hayo, halafu tutaangalie namna gani tunaweza kutatua tatizo hilo.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na mimi kupata swali la nyongeza. Ni wiki mbili zimepita alikuja Katibu wa Hospitali ya Mwambani Bwana Kalindu na nikamwita Mheshimiwa Naibu Waziri tukakaa, tukaongelea habari ya Hospitali ya Mwambani pale Mkwajuni.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyojua Songwe ni Wilaya mpya na hatuna Hospitali ya Wilaya lakini hii Hospitali ya Mwambani ndiyo inayotumika kama Hospitali ya Wilaya au Hospitali Teule, lakini watumishi mpaka sasa ni haba na hatupati dawa na hata mgao wa Serikali hauendi kama ambavyo inatakiwa ipewe Hospitali Teule. Ni nini Serikali inatamka juu ya jambo hili na Mheshimiwa Waziri anajua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mulugo alikuja na tukakaa pamoja na Daktari ambaye alikuwa ametoka Hospitali ya Mwambani. Kimsingi Hospitali ya Mwambani kwa sababu ndiyo hospitali pekee iliyopo inatakiwa itumike kama DDH. Ni makosa tu ambayo yalifanyika na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ndani ya muda mfupi tatizo litakuwa limeshatatuliwa na hospitali ile itatambuliwa kama DDH kwa sababu ndiyo hospitali ambayo ni tegemeo kwa wananchi wa Mwambani na Chunya kwa ujumla wake. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, kwa kweli nashukuru sana kwa kuniona maana yake nikasema mbona ni mrefu kuliko wote lakini nimesimama mara 20. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nataka kumuuliza swali moja la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Nakumbuka mwezi Machi alikuja Songwe Wilaya mpya tulikuwa naye kwenye Kata ya Chang’ombe, Kijiji cha Chang’ombe na Mbuyuni na yeye mwenyewe aliona ufisadi wa maji katika mradi wa Chang’ombe uliokuwa unashikiliwa na Mkurugenzi Chunya na sasa ni Wilaya Mpya na aliniahidi kwamba atafuatilia kumrudisha yule Mkandarasi aje amalizie ule mradi wa maji Chang’ombe, lakini mpaka leo kimya. Nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli nilishafika katika Halmashauri ya Songwe na tumeona changamoto hiyo na nilikwishatoa maagizo kwa Mhandisi wa Maji katika suala zima la kusimamia. Nimwombe Mhandisi wa Maji wa Songwe asimamie maagizo ambayo niliyompa na kama ameshindwa basi ajitathmini, kwa sababu sisi tunachotaka ni kazi na wananchi wale waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya mpya ya Songwe maeneo ya Rukwa, Udinde, Guwa na Some hayana kabisa mawasiliano. Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akanihakikishia ni lini Serikali itaweka mawasiiano katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Mulugo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Mulugo kwa jinsi ambavyo anapambana kwa ajili ya Jimbo lake na wananchi wa eneo lake. Nashukuru vilevile kwa kuwa ameshaniletea barua ya maombi ya kuimarisha masuala ya mawasiliano kwenye maeneo aliyoyataja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mulugo kwamba tutafanya ziara baada ya Bunge hili kuhakikisha maeneo yake na maeneo mengine yote ambako Waheshimiwa Wabunge wameandika barua kuomba mawasiliano tunayatembelea na kuhakikisha tunaingiza kwenye bajeti ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao tutaanza kuutekeleza kuanzia mwezi Septemba, 2018. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, amenitendea haki. Kwa kweli katika mwaka huu, leo nina furaha kubwa sana, kwanza Serikali imenipatia shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Songwe, nimefarijika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mwanzo wa mwezi huu alikuja Dkt. Kalindu kutoka Hospitali ya Mwambani kuleta tatizo hili kwa ajili ya kuteuliwa Hospitali Teule ya Wilaya. Kwa hiyo, Serikali leo imejibu kwamba imepandisha hadhi na mkataba wetu umekubaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu la nyongeza. Kwa vile sasa imekubaliwa kuwa hospitali ya wilaya, naomba kujua ni lini kibali kitatoka, maana ndiyo imekuwa hospitali ya wilaya lakini watumishi pale ni wachache na tangu mwaka 2014/2015 hatujawahi kupata vibali vya watumishi. Naomba nijue ni lini Serikali itatoa kibali cha kuajiri watumishi (madaktari na wauguzi) katika Hospitali ya Mwambani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mwalimu Mulugo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mulugo kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala hili. Alikuja Daktari kutoka Hospitali ya Mwambani lakini pia na juzi imekuja Kamati ya Siasa ya Wilaya yake nao wakawa wanaulizia suala hili. Kama ambavyo nilimuahidi tutafanya mapema na hili limewezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake anataka uhakika juu ya suala zima la kupata watumishi. Naomba nimhakikishie process ya ajira iko kwenye hatua za mwisho kabisa, zaidi ya wiki mbili tayari tutakuwa tushakamilisha suala la ajira na hakika tutahakikisha tunapeleka watumishi ili wakafanye kazi kwenye ile hospitali ambayo tumekubali itumike kama Hospitali ya Wilaya kwa sasa.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Songwe au Wilaya ya Songwe kwa ujumla hatuna zao la biashara zaidi ya zao la Pamba ambalo tulikuwa tunalima mwaka 1995 wakati sisi tunasoma mpaka leo. Wananchi wa Songwe hawana zao la biashara kabisa.
Sasa naiuliza Serikali, je, toka mwaka huo wanafanya utafiti wa huyo mdudu mwekundu lakini maeneo haya ya Tanganyika kama alivyosema Mheshimiwa Kakoso na Katavi yote ni Ukanda ule ule wa kwangu Mbeya, Songwe na alikotokea Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaruhusu sasa Bonde la Songwe tuweze kulima pamba kama ambavyo leo ametoa kibali kwa Wilaya ya Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema Mkoa wa Katavi Serikali tumeruhusu baada ya utafiti wa kina kufanyika kwamba zao la pamba liweze kulimwa kwenye Mkoa wa Katavi. Kwenye jibu langu la msingi nilisema, maeneo yale yanayopakana na Mkoa wa Katavi ikiwemo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mulugo kule Songwe, ni kwamba utafiti unaonyesha kwamba bado funza mwekundu yupo katika eneo lile la Mheshimiwa Mbunge.
Kwa hiyo, naomba atoe subira kwa Serikali ili utafiti wa kina ufanyike kwamba funza mwekundu ameshaondoka katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ziwa Rukwa kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri huwa linafungwa kila wakati lakini pale Serikali inaporuhusu kufunguliwa bado samaki wale ni wadogo na wamedumaa kabisa na utafiti unafanywa lakini haufanywi ule utafiti wa wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zaidi ya miaka 20 sasa toka mwaka 1978 toka Serikali imepandikiza samaki Ziwa Rukwa. Nataka Mheshimiwa Waziri anijibu ni lini Serikali itafanya uthabiti wa kina kabisa wa uhakiki wa kuja kufanya utafiti katika Ziwa Rukwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika skimu za umwagliaji nimeona hapa ameorodhesha maeneo ya Rukwa kule Sumbawanga, Mbozi pamoja na kule Momba lakini mimi nimeuliza Bonde la Songwe maana yake ni Jimboni Songwe, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa Nanjembo ambao tayari usanifu ulishafanyika kwa ajili ya umwagiliaji, watupe fedha tuweze kufanya miradi ya umwagiliaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Mwalimu Mulugo na nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini tutafanya utafiti wa kina, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika bajeti yetu ya mwaka huu, taasisi yetu ya utafiti ya TAFIRI tumeitengea pesa na tayari tumeshaielekeza kwamba katika moja ya kazi muhimu za kufanya ni kwenda kuangalia hatma ya Ziwa Rukwa na samaki wa Ziwa Rukwa ili waweze kuwanufaisha Watanzania wa kule Songwe. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ninayoiombea ni ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya kwenda mkoani, Wilaya ya Songwe ni mpya kabisa, kwa hiyo hatuna barabara inayounganisha wilaya na mkoa, kwa hiyo ningependa Serikali ifanye uharaka zaidi kwa sababu wale wananchi wanapitia Mbalizi ambako ni mbali sana. Kama itakuwa inatenga milioni 63 kila mwaka maana yake itachukua miaka sita kuja kupata hii barabara, nataka Serikali angalau iniongezee fedha kutoka milioni 63 mpaka milioni 300 ili tuweze kumaliza hii barabara kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais alipokuja Wilaya ya Songwe tulimwomba kilometa nne kwa ajili ya kufanya Mji wa Mkwajuni, Makao Makuu ya Wilaya yawe salama na yawe safi. Sasa ni lini Serikali itatupa fedha kwa ajili ya kilometa nne za lami pale Mji wa Mkwajuni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mulugo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu kwenye majibu yangu ya msingi, yeye mwenyewe anakiri kwamba ameona nia ya Serikali ya kuhakikisha kwamba kwanza tunatambua kwamba tunataka tutumie kilometa ili wananchi wasiendelee kuzunguka na tumeanza kujenga hayo madaraja. Katika majibu yangu ya msingi nimemhakikishia kwamba ni vizuri tukawa na tathmini kujua gharama halisi ili hata hicho kiasi cha fedha kinavyotafutwa tuwe tunajua tunatafuta kwa ajili ya kazi gani ambayo inatakiwa ifanyike. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali tunatambua iko haja ya kuhakikisha kwamba wanafika Makao Makuu ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema iko ahadi ya kilometa kwa ajili ya lami ili na wao katika makao makuu ya wilaya wafanane na makao makuu ya wilaya zingine. Naomba nimhakikishie Mhesimiwa Mbunge; ahadi zote za Viongozi wa Kitaifa tunazitekeleza na kwa Mkoa wa Songwe tumeanzia Makao Makuu kwa maana ya Momba, tunaanza kuweka kilometa moja, lakini pia na Mbozi. Naomba hatua kwa hatua, hakika ahadi zote za Viongozi wa Kitaifa sisi tutakwenda kuzitekeleza.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Tunayo barabara ya kutoka Mbalizi kwenda Wilaya ya Songwe, Mbalizi ni Mkoa wa Mbeya na Songwe ni Mkoa wa Songwe na TANROADS Mbeya, TANROADS Songwe tayari kuna mgawanyiko wa kugawana hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani na kwenye agizo la Mheshimiwa Rais barabara hiyo yenye kilometa 91 na ilishafanyiwa tayari upembuzi kilometa 56 kutoka Mbalizi mpaka Galula ili iweze kupata lami, lakini mpaka leo kupo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iniambie ni lini watafanya upembuzi yakinifu ili tuweze kupata lami kutoka Mbalizi mpaka Mkwajuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amekiri kabisa kwamba kuna kipande cha barabara kutoka Mbalizi mpaka Songwe ambacho upande mmoja tayari umekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatafuta fedha hivi karibuni TANROADS upande mwingine wa pili wataanza kufanya upembuzi yakinifu ili tuwe na upembuzi yakinifu wa jumla wa kilomita 91 kwa ajili ya kuingiza kwenye mipango ya kuanza kufanya utekelezaji wa kujenga kwa kiwango cha lami.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Songwe ilipokuwa Chunya kabla hatujagawana kulikuwa na mradi mkubwa wa maji kutoka kwenye miradi ya World Bank vijiji 10 kila halmashauri. Kijiji cha Chang’ombe ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja mwaka juzi mimi na wewe tukaenda ukahutubia na mkutano na ukawaahidi wale wananchi kwamba watapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa na tatizo kubwa la mkandarasi aliyekuwa bado kwenye Halmashauri ya Chunya kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa fedha kwenye mradi wa Chang’ombe. Sasa mpaka leo hali iko hivyo hivyo na hata mwaka jana nimekuuliza swali ukasema kwamba utalifanyia kazi. Naomba na leo nisisitize kwamba ni lini unakwenda kumwambia mkandarasi akamilishe kazi pale kijiji cha Chang’ombe Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo nimeiona kwa macho katika Jimbo lake lakini kikubwa sisi kama Wizara ya Maji, jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hii ya maji na maji ni uhaki na hayana mbadala. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwakweli tulishatoa agizo na kama agizo lazima litekelezeke. Nikuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya saa saba tukutane ili tuweze kuchukua hatua katika kuhakikisha wananchi wako wananufaika na mradi wa maji. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali la nyongeza kama mwalimu kwa mwalimu mwenzangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako.

Kwa kuwa umezungumza kwamba Wabunge wengi, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Mawaziri na watumishi wengi tu wa Serikali, sasa hivi wanapendelea sana kuwapeleka watoto wao shule za english medium. Lakini kwa kuwa hizi shule za english medium zimekuwa zikitoa malalamiko mengi kwamba Serikali haijajenga chuo cha kufundishia walimu special kwa ajili ya kwenda kufundisha hizi shule za english medium.

Ni lini Serikali itajenga Chuo cha Serikali ili walimu wa Tanzania waweze kusoma na kwenda kuwafundisha walimu hao kwa sababu tunatumia walimu wa Kenya na Uganda? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana ningependa kujibu swali la nyongeza la mwalimu mwenzangu Mheshimiwa Phillipo Mulugo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake ni la msingi kwamba Serikali iandae walimu ambao watafundisha katika shule ambazo zinatumia lugha ya Kiingereza, na niseme suala hili si lazima tujenge chuo, nimwambie kwamba suala hilo Serikali imelipokea na tutangalia utaratibu ambao tunaweza ndani ya muda mfupi tukaanza kuwa hata kuwa tunatoa hayo mafunzo katika vyuo ambavyo vipo hapa nchini. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na mimi niipongeze Serikali, miaka yangu tisa ya kukaa hapa Bungeni nimekuwa nikiuliza swali la kufanya utafiti angalau Serikali sasa imeridhia na imefanya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu moja la nyongeza, kwa kuwa Serikali imefanya utafiti na imeona kabisa kwamba kweli samaki wanadumaa kutokana na sababu walizozieleza lakini upo upande mwingine wa kuweza kupandikiza samaki wa aina nyingine katika Ziwa Rukwa kama ambayo mwaka 1978, Serikali ilichukua samaki kutoka Singida wakatuletea kule Ziwa Rukwa na tulikuwa tunawaita samaki aina ya Singida ambao ndiyo wameisha.

Je, Serikali iko tayari sasa kuangalia samaki wengine upande wa Ziwa Tanganyika, Nyasa au bwawa la Mtera hapa wakachukua wale samaki wakaja kuwapandikiza kwenye Ziwa Rukwa ili kuongeza idadi ya samaki katika ziwa hili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Phillipo Mulugo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa rai yako juu ya uwepo wa madini yale na umeelekeza Wizara ya Afya itakapokuja itaendelea kujibu jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie watafiti wetu wanatazama maana viko viwango ambavyo vimekuwa recommended na WHO ikiwa kama vitaonekana vimefikia au vimezidi basi zipo hatua ambazo sisi pamoja na Wizara ya Afya tutazichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na jambo la Mheshimiwa Mulugo la namna ya kupandikiza samaki wengine kutoka maeneo mengine, naomba nichukue ushauri huu na tutakwenda kuufanyia kazi, ukionekana ni ushauri wenye kufaa basi tutautekeleza.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwanza napenda kupongeza Wizara ya Maji, Mheshimiwa Waziri Aweso na Mheshimiwa Engineer Maryprisca ya kutembelea Mikoa yetu ya Kusini, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Njombe, kazi nimeiona, mmefanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu moja la nyongeza, pale Mkwajuni Makao Mkuu ya Wilaya pana mradi mkubwa wa maji wa milioni 760 toka mwaka 2018. Mkandarasi ametumia fedha zake binafsi karibuni asilimia 80 anakamilisha mradi, lakini anakwamishwa na malipo ya Serikali baada ya kumaliza zile kazi, certificate anapeleka lakini halipwi. Galula pana mradi wa maji, Kapalala pana mradi wa maji. Hii miradi mitatu kwenye jimbo langu imekuwa ni kero sana kwa wananchi na wale wakandarasi wameshamaliza lakini wanasubiri certificate ili waweze kulipwa. Je, ni lini Serikali itawalipa fedha zao ili miradi ya maji ikamilike?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, malipo yote ambayo wakandarasi wamefanya kazi na kazi zinaonekana malipo yote yanaendelea kushughulikiwa na hivi karibuni Serikali itawalipa.