Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa (24 total)

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, sheria hiyo katika marekebisho hayo, ukija upande wa mazao ya tumbaku, iliondoa chama kikuu cha APEX cha Morogoro kwenye ushirika wa tumbaku. Baada ya kuiondoa hiyo APEX ina maana hata ile tozo ya asilimia tano ambayo APEX ilikuwa inachukua kwenye bei ya mkulima, ipo. Je, hiyo tozo sasa itarudi kwenye vyama vya msingi vya wakulima au inafanya nini?
Mheshimiwa Spika, la pili, Vyama vya Msingi vinapotaka kukopa pembejeo za zao lao vinapitia kwenye Vyama vya Ushirika vya Wilaya kwenda kwenye mabenki. Vikipitia kwenye Vyama vya Ushirika vya Wilaya kwenda kupata mkopo huo, kunakua na gharama ambapo Chama cha Ushirika cha Wilaya kinakitoza chama cha msingi, kinasema ni kwa sababu ya utawala. Je, lini Serikali sasa itatengeneza kanuni ambayo itakifanya chama cha msingi chenyewe ndiyo kiende kukopa benki pembejeo hizo?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Naibu waziri kwa majibu mazuri.
Kuhusu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Mwambalaswa, niseme tu kwamba Serikali inapanga kuyapitia upya makato yote yanayokwenda kwenye mazao, zikiwepo tozo zote hizo zinazotolewa; na pia inapanga kuangalia upya mfumo wa ugawaji wa pembejeo kwa wakulima wa mazao haya ambayo ameyataja.
Mheshimiwa Spika, nategemea kuyatolea kauli ndani ya siku mbili hizi tutakapokuwa tunatolea majibu ya hoja za Wabunge kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa sababu tayari Mheshimiwa Rais alishaonesha kukerwa na tozo nyingi zinazowaangukia wakulima kwenye mazao haya. Vilevile wakati anazunguka kwenye kampeni alishawaahidi na sisi wasaidizi wake tunatembea kwenye maneno ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tutatoa tamko kwa kuhakikisha kwamba wakulima wanaacha kubeba mzigo mzito wa makato hayo.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana yameniridhisha sana, lakini pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Serikali mwaka juzi ilitangaza kwamba itaweka vyuo vya VETA kwenye Wilaya zote nchi, lakini itaanza na Wilaya 10 ambapo Wilaya ya Chunya ni mojawapo naishukuru sana Serikali kwa kuiweka Chunya katika moja ya Wilaya 10 za kuweka Vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sana tena Wilaya ya Chunya inagawanyika kuwa Wilaya mbili, Wilaya ya Chunya na Wilaya ya Mkwajuni Wilaya ya Songwe ambako sasa ndiyo kuna heka kumi zimetengwa za kujenga Chuo cha VETA. Sasa swali, kama Serikali ilisema inaipa Chunya Chuo cha VETA, Chunya imegawanyika ziko Wilaya mbili siyo bora tu zote Wilaya zote mbili Chunya na Songwe zipate Chuo cha VETA? Hilo la kwanza na naona Mheshimiwa Mulugo ambaye ni wa Wilaya ya Songwe amefurahi sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, la pili, pale kwenye kambi ya ujenzi wa barabara ya Mbeya - Chunya kwa kiwango cha lami Serikali imesema majengo yale ni ya muda siyo ya kudumu. Je, kwa kuwa, eneo lililotengwa ni heka 25 haiwezi ikaanzia kwa majengo hayo ambayo siyo ya kudumu lakini ikajenga Chuo cha VETA kwa eneo kubwa ambalo limebaki?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambalaswa Mbunge wa Lupa kwa jinsi ambavyo amelifuatilia sana jambo hili. Pia niseme tu kwamba, kwa mujibu wa sera tuliyojipangia na mpango tuliojipangia Wizara yetu imedhamiria kuanza kujenga Vyuo vya VETA katika Wilaya zote ambazo hazina kabisa Chuo chochote cha Ufundi au VETA kwa ujumla. Kwa hali hiyo, kwa sababu ya bajeti ambayo kimsingi inahitajika katika maeneo mengi siyo rahisi kuvijenga vyuo vyote kwa siku moja.
Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Mbunge kushirikiana Halmashauri yako hilo eneo ambalo umeliangalia ni vema likatengwa na likapimwa na hati zake zikawasilishwa katika Wizara yetu ili liwe katika mpango.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, Wizara yangu inapata tatizo kubwa sana inapofikia kuanza mipango ya maandalizi ya ujenzi wa vyuo hivyo kutokana na ardhi hizo kutokupatikana na kupimwa, ni vema Halmashauri zote ambazo ziko katika mpango huu zihakikishe zinatenga maeneo hayo ili isiwe ni kikwazo tunapofikia kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, pili, nadhani nimejibu yote kwa pamoja kama ambavyo nimeelekeza kwamba ukishapima tutafanya hivyo kwa kuwa sasa Wilaya ya Songwe inajitegemea, lakini itakuwa ni baada ya kumaliza zile ambazo tumeanza nazo. Ahsante sana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Napenda kumshukuru sana Naibu Waziri amejibu vizuri sana na amejibu kitaalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesema Chunya ina mazao mengi ambayo yakibebwa ndiyo yanaharibu barabara, sasa napenda nimwambie Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba wanaosomba tumbaku, magari yanayobeba tumbaku au mbao au mkaa yanabeba lumbesa, yanakuwa mara mbili, yakifika Mbeya yanagawa kwa sababu kuna mizani kule ndiyo yawe magari mawili na Serikali hapa imesema kwamba itadhibiti hiyo kwa kuweka mobile weighbridges.
Je, ni lini itaweka kwa sababu Chunya sasa hivi sijaiona mobile weighbridge hata moja? Hilo ni swali la kwanza
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nashukuru Serikali imesema kwamba ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Chunya kwenda Makongorosi karibu utaanza, napenda nimwambie Naibu Waziri kwamba Mheshimiwa Rais akiwa Makongorosi aliwaahidi wananchi wa Makongorosi kwamba atawapa kilomita nne za lami pale Makongorosi na kwamba barabara hiyo ya Chunya Makongorosi itaanza kujengwa Makongorosi kuja Chunya.
Je, hiyo barabara itanza lini kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema kwenye jibu la msingi la swali la msingi kwamba weighbridge itaanza hivi karibuni. Naomba kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mwambalaswa kama yeye alivyo-concerned na uharibifu wa barabara hiyo na sisi ambao ndiyo wenye dhamana hiyo tuko concerned kwa kiwango kikubwa, ninamhakikishia hiyo weighbridge inatafutwa hivi karibuni itaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili naomba kumjulisha Mheshimiwa Mwambalaswa kwamba mara fedha zitakapopatikana barabara hii itaanza kujengwa na suala la ianzie wapi whether ianzie Makongorosi au ianzie Chunya nadhani ni muhimu tuwaachie wataalamu na ahadi ya kilomita Nne nayo katika eneo la Makongorosi itaangaliwa kwa umakini wake. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri amesema mwaka huu Serikali imetenga shilingi milioni 50. Hizi hela ni hela za Halmashauri, own source ya Halmashauri na mimi Mbunge nitachangia katika hela hizo. Mimi ninalosema Serikali kutoka Makao Makuu iwe Wizara ya Afya au TAMISEMI watachangia kiasi gani kwenye hospitali hiyo ambayo ni ya wananchi wa Wilaya ya Chunya hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Bunge lililopita la Kumi Serikali ilianzisha mpango wa kukarabati hospitali za Wilaya kumi, kuziinua kiwango ziweze kutibu maradhi yote ili kupunguza congestion kwenye hospitali ya rufaa na Chunya ilikuwa mojawapo katika hospitali hizo kumi katika Tanzania.
Je, huo mpango umefia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli safari hii imetengwa shilingi milioni 50 na tunapofanya mobilization of resources mara nyingi sana kuna vipaumbele, najua wazi kwamba pesa hizi ni own source. Lakini siyo kusema kwamba kwa vile ni own source basi Serikali maana yake haina jicho lake ndiyo maana mchakato wa bajeti kuna pesa nyingine zinatoka katika Serikali za Mitaa na nyingine zinatoka katika Serikali Kuu. Wakati mwingine kipaumbele cha baadhi ya vipengele inaenda katika miradi mingine. Kwa hiyo, lengo kubwa ni Serikali kupeleka mchakato huo mpana na mwisho wa siku ni kwamba wananchi kuweza kupata huduma.
Mheshimiwa Mwambalaswa naomba nikuhakikishie kwamba hela hii ni own source na ninajua kwamba na ninyi mmefanya harakati na wewe mwenyewe ulikuwa ukisimamia ile harakati ya harambee. Mimi naomba niwapongeze kwa sababu miongoni mwa watu ambao wamefanya wenyewe kuhakikisha kwamba wanafanya harambee tena ikiongezewa na Mbunge Mwambalaswa nikupongeze katika hilo. Naomba nikuhakikishie kwamba katika mchakato wetu najua hii itakapokuwa imekamilika lazima kutakuwa na mapungufu mengine yatakuwa yanajitokeza katika kuhakikisha hospitali ile inaweze kufanya kazi. Jukumu la Serikali mwisho wa siku ni kwamba hospitali ile ya Chunya iweze kuwa na hadhi sasa kama nyingine, naomba nikuhakikishie kwamba tutakuunga mkono kwa nguvu zote kwa vile umekuwa ukipigania katika hili tutashirikiana kwa jinsi zote.
Suala zima la ukarabati kama ulivyosema kulikuwa na mchakato wa ukarabati ni kweli, na maeneo mbalimbali ukarabati huu ulikuwa unaendelea. Lakini bado tukiri wazi tatizo hili bado ni kubwa sana ukiachia ukarabati; hata niliposema wiki iliyopita, kwamba ukiacha ukarabati halikadhalika kuna majengo mengine ambayo hayajakamilika. Ndiyo maana tumetoa maelekezo wiki iliyopita nimesema Halmashauri zote hata Mheshimiwa Mwambalaswa tulikuuliza kule Chunya kuwa Mkurugenzi atakuwa amepata waraka kutoka TAMISEMI, lengo letu ni nini, najua kuna mambo tumeyafanya lakini bado mapungufu yapo makubwa zaidi, tuweze kubainisha hizo changamoto tuzipangie mkakati wa pamoja sasa jinsi gani tutafanya kurekebisha matatizo haya hasa ya magofu ambayo hayajakamilika lakini kuhakikisha hadhi za hospitali zetu za zahanati ziwe sawa sawa. Nadhani mchakato huu utakuwa mpana sana ili kukidhi matakwa ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi kama tulivyoahidi wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mwambalaswa kwamba tutakuunga mkono katika juhudi kubwa ulizozifanya katika Jimbo lako la Chunya na Halmashauri yako ya Chunya.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na mimi naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika sheria ya ushirika ya mwaka 2013 tuliwaondoa watu wa APPEX kwenye mchakato wa kupata pembejeo za Vyama vya Ushirika wa Tumbaku, kwa sababu walikuwa hawana tija tukawabakiza Vyama vya Wilaya ambavyo vinawasimamia Vyama vya Msingi. Na hivi Vyama vya Wilaya vinaonekana navyo ni mzigo katika kupata pembejeo kwa Vyama Msingi vya wakulima wa tumbaku. Je, Serikali inasemaje kuhusu kuwaondoa hawa watu wa wilaya ili Vyama vya Msingi vikope vyenyewe kwenye mabenki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba Sheria mpya ya Ushirika Na. 6, 2013 ambayo imeanza kufanya kazi mwaka 2015 imeleta muundo mpya wa kitaasisi ya namna ya kuendesha vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na kuondoa utaratibu ule wa vyama vya APPEX, ilionekana kwamba msululu wa vyama vingi unaleta changamoto na kuleta gharama ambazo siyo lazima kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo lake ni kuhusu Vyama vya Wilaya kwamba navyo vinaleta mzigo katika uendesha wa Vyama vya Ushirika nimfahamishe tu kwamba Wizara inakaribisha mapendekezo yote ya kurekebisha sheria yoyote pale wadau wakihisi kwamba inakuwa na tija zaidi kama maboresho yakiletwa sisi tuko tayari kusikiliza na hatimaye kuleta Bungeni. Kwa hiyo, nimkaribishe Mheshimiwa Victor na wadau wengine kama wanataka tuirejele tena upya sheria ambayo tumeipitisha miaka miwili tu iliyopita sisi tuko tayari kuwasikiliza ndiyo kazi yetu, kwa hiyo karibu sana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mlolongo wa tozo kwenye zao la tumbaku ambazo anatozwa mkulima, ilikuwepo tozo ambayo, kabla ya marekebisho ya Sheria hiyo ya 2013 kulikuwa na AMCOS, Ushirika wa Msingi, Ushirika wa Wilaya na Ushirika wa Taifa ambao ulikuwa Morogoro wakijiita APEX. Sasa sheria hii iliporekebishwa hawa watu wa APEX waliondolewa na kuondolewa kwao ina maana tozo ambayo mkulima alikuwa anakatwa ili ikafanye uendeshaji wa APEX, ilikuwa aidha irudi kwenye AMCOS au iondolewe. Je, hiyo imeondolewa au imerudi kwa mkulima? La kwanza hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wote hapa tumemsika Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema baada ya Bunge hili atakwenda Tabora akaangalie matatizo yaliyomo kwenye eneo hili la tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na matatizo haya pia kuna tatizo la wanunuzi wa tumbaku. Makampuni ya kununua tumbaku hapa nchini yako matatu tu na mwaka 2015 yameanza ukiritimba wa kutokununua tumbaku yote ya wakulima. Je, Wizara inasemaje au ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba tumbaku yote ya wakulima inanunuliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo iliyokuwa inalipwa kwa APEX, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kuwa tuko katika utaratibu wa kupitia tozo zote katika mazao yote na tutaleta taarifa hivi karibuni Bungeni, Waziri wa Fedha atawasilisha Finance Bill na hiyo Finance Bill pamoja na mambo mengi itaonesha maeneo ambayo tumependekeza kuondoa au kupunguza kodi ambazo hazina maana. Kwa hiyo, zinashughulikiwa na atapata taarifa karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ununuzi na soko la tumbaku, ni kweli kabisa kama alivyosema, tunatambua changamoto iliyopo katika soko la tumbaku kwa sababu pamoja na mambo mengine, kuna ukiritimba mkubwa kwa sababu makampuni yanayonunua ni matatu tu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na suala la soko, ni suala la dynamics duniani, lakini nimhakikishie tu kwamba Wizara yangu tayari inafanya jitihada ili kuhakikisha kwamba tunapata wanunuzi wa ziada ili kuondoa ukiritimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango hii imekuwa ni pamoja na kufanya majadiliano na The China Confederation of Industries ili kujaribu kuwaleta wanunuzi wa tumbaku kutoka China. Nimweleze tu kwamba tumeshafikia hatua nzuri na baada ya muda siyo mrefu tuna hakika kwamba kutakuwepo na wanunuzi wa ziada kutoka China ili kuweza kuleta ushindani na hatimaye wakulima wetu waweze kupata bei nzuri.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alipojibu maswali ya nyongeza amesema kwamba makampuni ya wanunuzi ni machache yako kama matatu na yanafanya kiburi kwa sababu kwao ni cartel na amesema kwamba Wachina wana nafasi ya kununua tumbaku hapa kwetu kwa sababu Wachina ni wengi sana hapa duniani. Je, Serikali inasemaje kuyaleta Makampuni ya Kichina kuja kununua tumbaku hapa Tanzania na kuwapunguzia wakulima adha wanayopata?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali inatambua changamoto inayoletwa na ukiritimba katika ununuzi wa zao la tumbaku. Ndiyo maana Wizara yangu imechukua hatua kadhaa ili kutafuta wanunuzi wengine. Nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba wiki mbili zilizopita tumekutana hapa Dodoma na Balozi wa China ili kuangalia uwezekano wa kuwapata wanunuzi zaidi. Tumeongea nao ili confideration of China Industries waweze kuruhusu kampuni zao ziweze kuja kununua tumbaku Tanzania, mijadala hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeongea na watu wa Vietnam ili kuangalia uwezekano wa kuwapata wanunuzi kutoka Vietnam. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba jitihada zinaendelea na tuna hakika kwamba wanunuzi wengine wa tumbaku watapatikana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais kwenye Mji wa Itigi inafanana kabisa na ahadi aliyotoa kwenye Mji mdogo wa Makongorosi ambapo alisema kwamba wakati inajengwa barabara ya kutoka Chunya kwenda Makangorosi na kuelekea Itigi na Mkiwa, Serikali itawajengea wananchi wa Makongolosi lami kilometa nne; je, ahadi hiyo itatekelezwa wakati barabara hiyo inajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ahadi ya viongozi wetu, ni wajibu wetu na dhamana yetu kutekeleza ahadi za viongozi wetu pamoja na ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia kwamba ahadi hii itakamilika na hasa wakati ujenzi huu wa barabara ya kutoka Mkiwa hadi Makongorosi itakapofikia hilo eneo, kwa vyovyote na hizo kilometa nne ambazo zimeahidiwa, zitajengwa.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na pia nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba Serikali imetenga fedha sasa kwa ajili ya kujenga Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Chunya, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja Chunya ili nimwonyeshe viwanja vilivyo ambavyo Halmashauri imetenga kwa ajili ya kazi hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Jimbo langu lina tarafa mbili, Tarafa ya Kiwanja na Tarafa ya Kipembawe. Tarafa ya Kiwanja ina Mahakama za Mwanzo mbili, moja iko Chunya, nyingine iko Makongorosi. Tarafa ya Kipembawe haina Mahakama ya Mwanzo hata moja. Sasa je, Serikali inasemaje kuhusu kuleta Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Chunya ili Halmashauri iweze kumtengea eneo la kuweka Mahakama hiyo katika Tarafa ya Kipembawe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimefarijika sana kumsikia Mheshimiwa Mbunge akisema viwanja tayari wanavyo na hivi majuzi tu nimetoka kujibu swali la Mbunge wa Temeke nadhani, nikielezea tu kwamba ni vizuri Wabunge sasa hivi mkahamasisha Halmashauri zenu kutuainishia viwanja ambavyo tayari vina hati iweze kuwa rahisi kwa Mahakama kuweza ku-identify maeneo hayo na kuweza kujenga maana pesa angalau sasa hivi tunayo ya kuweza kuanza ujenzi wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na hata Mahakama Kuu. Na tunashukuru kwamba kiwanja anacho Mheshimiwa Mwambalaswa, nitamfikishia ujumbe huu Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Ningefurahi kama rai yake aliyoitoa hapa itafuatiwa na barua ili itiwe na kumbukumbu kabisa kwenye mafaili yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu Kipembawe kwamba hakuna Mahakama ya Mwanzo, ningemwomba, hiki ndiyo kipindi ambacho Mahakama inaangalia priorities tuanzie wapi katika kujenga jumla ya Mahakama 50 za mwanzo. Tafadhali tunaomba alete andiko la hayo mahitaji yawekwe pia kwenye file tuweze kuliangalia pamoja na mambo mengine.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja tu la nyongeza. Katika Mji Mdogo wa Makongorosi na Mji Mkubwa wa Chunya, matatizo ya maji ni makubwa sana. Ni makubwa kiasi cha kuweza kuvunja ndoa za watu wanapofuata maji kwenye visima mbugani.
Sasa toka alipokuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda aliona Makongorosi na Chunya, Mheshimiwa Kikwete akiwa Rais ameona matatizo ya maji Chunya na Makongorosi na Mheshimiwa Magufuli katika safari yake ya kampeni ameona matatizo ya maji katika Mji Mdogo wa Makongorosi na Mji wa Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka commitment kutoka kwa Serikali. Ni lini Waziri pamoja na kwamba ziko milioni 500 sijui anasema zimepangwa kwa mwaka huu, lakini ikija mwisho wa mwaka watasema Treasury haijaleta hela. Je, ni lini Waziri au Naibu Waziri atakuja Chunya nimwoneshe hali mbaya ya maji katika Mji wa Makongorosi na Mji wa Chunya ili tukija hapa Bungeni aweze kunijibu vizuri.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Mji wa Makongorosi na Chunya una matatizo makubwa ya maji lakini pia, kuna kikundi ambacho kilikuwa kinachimba madini eneo linaitwa Ujerumani, imeonekena pana maji mengi sana. Sasa hivi Wizara inafanya utafiti kama yale maji yanafaa ili yaweze kuwekewa miundombinu yasambazwe katika maeneo ya Makongorosi na Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwamba ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja, hakuna wasiwasi tutatembelea hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutajipanga baada ya Bunge hili.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo nimeridhika nayo, bado nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa REA Awamu ya Kwanza, jimbo langu lilibahatika kupata umeme kwenye vijiji tano au sita na kwa kuwa mradi huu wa Awamu ya Kwanza haukuwa na kipengele cha kuweka umeme kwenye majengo ya huduma za jamii kama shule na vituo vya afya. Baada ya kuona hivyo ilibidi Mbunge nije hapa Bungeni nikope fedha kama shilingi milioni 150 ili nikalipe TANESCO waweke umeme kwenye sekondari saba; na kwa kuwa REA Awamu ya Pili nimepata vijiji vitano, lakini katika Kata ya Mtanila umeme haujaend kwenye Kituo cha Afya cha Mtanila. Swali langu sasa, je, hii REA Awamu ya Pili Mheshimiwa Naibu Waziri ananihakikishia majengo ya huduma za jamii kama vituo vya afya na shule yatapata umeme? La kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa amesema REA Awamu ya Tatu karibu itaanza; je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda na mimi Chunya wakati wa ufunguzi wa mradi huo hasa hasa kuanzia Kata ya Ifumbo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambalaswa kwa kufuatilia mahitaji na maslahi ya wananchi wake katika Jimbo la Lupa na tunashirikiana naye kwa ukaribu sana hasa katika vijiji na kata ambazo zimebaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nikubali kwamba katika REA Awamu ya Kwanza na ya Pili hatukuchukua maeneo mengi sana na hii ni kwa nchi nzima, siyo katika jimbo la Mheshimiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mwambalaswa katika kata sita zilizobaki ambazo ameomba zipatiwe umeme ikiwemo Kata za Mtabila, Ifumbo, Itumbi, Kambikatoto pamoja na Matundasi A na B zote zitapelekewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyouliza, REA Awamu ya Tatu majukumu yake ya kimsingi pamoja na mambo mengine ni kusambaza umeme katika taasisi zote za umma kama hospitali, vituo vya afya, zahanati, shule, mitambo ya maji, makanisa, misikiti na sokoni.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mwambalaswa na nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwenye Halmashauri zetu tuweze sasa kutenga walau pesa kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye taasisi zetu kwa sababu hili ni jukumu letu sote, na ndiyo maana wakandarasi tunapokwenda kuwakabidhi sasa tunawakabidhi Waheshimiwa Wabunge ili waweze kufuatilia utekelezaji wa miradi hii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwambalaswa nakuhakikishia kwamba vituo vya afya na taasisi nyingine zitapelekwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili la kufuatana na Mheshimiwa Mwambalaswa, kwanza kabisa niko tayari lakini kabla sijafuatana nawe mkandarasi tumeshamtuma na tumeshazindua utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Mbeya na Songwe. Sasa hivi mkandarasi yuko Ileje na tarehe 15 atafika kwako Mheshimiwa Mwambalaswa. Kwa hiyo, tuko pamoja na niko tayari kufauatana na wewe.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka niulize Serikali kwa kuwa katika Mkoa wa Mbeya, REA III imezinduliwa tayari na mkandarasi yupo aliyeanzia Wilaya ya Rungwe. Sasa ni lini huyo mkandarasi atakwenda Wilaya ya Chunya ili akapeleke umeme kwenye Kata zilizobaki za Ifumbo, Kasanga, Nkunungu, Lwalaje, Kambi Katoto na Mafyeko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Mwambalaswa nampongeza sana, hata tulipokwenda kule ni kwa sababu pia alishirikiana na sisi sana kwa hiyo hongera kwa kazi hiyo. Nimhakikishie kwa niaba ya wananchi wake; ni kweli kabisa katika Kijiji cha Ifumbwe pamoja na Kasanga bado hatujaenda; lakini tarehe 17 mwezi huu mkandarasi atakuwa kwenye Kijiji cha Kasanga katika jimbo lake. Kwa hiyo, katika maeneo mengine yataendelea kufanya kazi hiyo hiyo na niwaombe sana Wabunge wa Mkoa wa Mbeya tushirikiane kwa kazi hiyo kwa sababu mkandarasi tayari ameshaingia mkoani.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Serikali imekiri kwamba Chunya ni kati ya Wilaya kongwe nchini Tanzania, kwa kweli mwaka huu Chunya inafikisha miaka 75 ya kuwepo kama Wilaya, kwa hiyo kutokuwa na Mahakama ya Wilaya ni kama hatuitendei haki. Kwa hiyo, haya majibu ya Serikali nayashika mwaka kesho tukijaaliwa mwezi kama huu nitaionyesha Serikali jibu lake hili. Sasa naomba niulize swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuweka mkakati wa kujenga Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Chunya, Serikali ina mpango gani wa kuweza kujenga Mahakama zingine kwenye Tarafa, kama Tarafa ya Kipembawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa sasa wa Wizara, katika ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na zingine Mahakama za Mwanzo na ukarabati wa baadhi ya majengo, tunakwenda awamu kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha na bajeti. Hivyo, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi pale bajeti itakaporuhusu tutaangalia pia umuhimu wa kushuka ngazi za Mahakama za Mwanzo ili huduma hii iweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa hivi tunatumia teknolojia mpya ya ujenzi wa majengo ya Mahakama kwa gharama nafuu, tunaamini kabisa katika miaka michache ijayo kutokana na upatikanaji wa fedha itakuwa ni rahisi pia kuweza kuzifikia Mahakama za Mwanzo ili wananchi wa Jimbo la Lupa na wenyewe waweze kupata huduma hii kwa ukaribu kabisa.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina mswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, katika uwanja huo mimi kama Mbunge nilitoa hela yangu mwenyewe shilingi milioni kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukimuona mtu anatoa hela yake mfukoni kupeleka kwenye project ya wananchi kwa zama hizi ujue kilio hicho ni kikubwa sana. Chunya ni Wilaya ambayo ni kongwe sana, sasa hivi ina miaka 76. Viongozi wengi wa nchi hii akiwemo Profesa Mark Mwandosya amesoma Chunya na viongozi wa kidunia akiwemo aliyekuwa Rais wa makaburu wa mwisho Pieter Botha alizaliwa Chunya na kusoma Chunya. Kwa hiyo, Chunya ni Wilaya ambayo inatakiwa iangaliwe kwa huruma sana. Serikali inasemaje kuhusu kututafutia Chunya wafanyabiashara wakubwa wanaoweza kutusaidia kujenga uwanja huo ili waweze kutangaza biashara zao? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje kuhusu kuja Chunya aje auone uwanja huo ili awe na uelewa mkubwa na mpana kuhusu uwanja huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa mzee wangu Mheshimiwa Mwambalaswa kwa jitihada zake kubwa ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha miundombinu ya michezo katika jimbo lake. Niseme wazi kabisa kwamba Wizara yangu pia inayo taarifa kwamba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wa Wilaya ya Chunya na Jimbo la Lupa wamechangia kiasi cha shilingi milioni 224, ambazo kati ya hizo milioni kumi ametoa Mbunge wa Jimbo la Lupa Mheshimiwa Mwambalaswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pia nichukue nafasi hii kuweza kuomba Wabunge wote kuiga mfano huu mzuri ambao Mheshimiwa Mbunge ameuonesha, lakini vilevile kuiga Halmashauri zote nchini zichukue mfano huu mzuri ambao umeonyeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya katika kuwashirikisha wadau katika kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya michezo.
Kuhusu swali lake la kwanza ambalo ameuliza kuomba wadau, kwamba Wizara imsaidie kuweza kutafuta wadau. Mimi niseme kwamba Mheshimiwa Mbunge Wizara yangu iko tayari kabisa kushirikiana pamoja na wewe, lakini vilevile na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya na Jimbo la Lupa kuhakikisha kwamba tunahamasisha wadau mbalimbali waweze kujitokeza katika kuchangia ujenzi huo wa uwanja wa michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ombi lake la pili, niseme kwamba Mheshimiwa Mbunge mimi nikutoe wasiwasi, na ni mwezi wa 12 tu nilikuwa katika Wilaya ya Mbeya Vijijini. Kwa hiyo, niseme kwamba tutakapotoka hapa naomba tukutane tukae, tujadili, tuongelee ratiba kwamba ni lini ili na mimi niweze kuja kujione uwanja huo wa Lupa.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, vilevile napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa azma yake ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Vilevile kwenye issue ya magari naipongeza Serikali kwa kuamua kununua kwa wingi (bulk procurement) ambayo inapunguza bei, na vilevile kununua kwa mtengenezaji badala ya kununua kwa mtu wa katakati ambayo nayo inapunguza bei, nawapongeza.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza.
Sasa hivi Serikali pamoja na kwamba haina sera ya magari, magari mengi yanayotumika ya Serikali ni Toyota, bei ya Toyota Land Cruiser VX bila ushuru ni shilingi milioni 220. Bei ya Toyota Land Cruiser Prado ambazo kwa sifa zote zinafanana ni shilingi milioni 120 bila kodi. Kwa hiyo, Serikali ikiamua kununua magari 20 ya VX na ikaacha ikanunua Prado ita-save karibu shilingi bilioni mbili ambayo inaweza ikatatua matatizo ya maji katika Mji wa Chunya, Mji wa Makongorosi hata Mkwajuni kwa Wilaya mpya ya Songwe. Je, Serikali inasemaje kuhusu kuachana na VX na kutumia Prado kwama inavyotumia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar?(Makofi)
Swali la pili, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali inafuata Sheria ya Udhibiti na Ununuzi wa Mali ya Umma Sura ya 410. Sheria hiyo inasisisitiza ununuzi wa mali ya umma ni kwa tender na disposal ya mali ya umma ni kwa tender. Zamani ilikuwa magari ya Serikali yale yanayochakaa yanakusanywa...

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Magari yanakusanywa MT Depot na yanauzwa kwa tender. Siku hizi hawafanyi isipokuwa Idara ya Usalama wa Taifa ndio inauza kwa tender.
Serikali inasemaje kuhusu Viongozi wa Serikali ambao wanajiuzia magari yaliyochakaa badala ya kuuza kwa tender? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema masuala ya ununuzi wa magari ni masuala yanayosimamiwa na sheria vilevile Wizara ya Fedha ndio inayosimamia GPSA. Kwa maana hiyo, nachukua maoni yake tutaenda tukayafanyie kazi kwa kushirikisha GPSA pamoja na Wizara ya Fedha pamoja na Idara Kuu ya Utumishi ili hatimaye tupate majibu sahihi na hatimae nitakueletea hayo majibu sahihi Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kuongezea kidogo hasa kuhusu magari baina ya Toyota Prado na Landcruiser VX.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati unanunua kitu unaagalia mahitaji yako, kwanza unangalia bei, unaangalia safety, unaangalia mantainance cost, vitu vyote hivi unaviangalia baada ya hapo ndio unaweza kupima. Ukinunua gari baina ya Zanzibar na Bara ni mazingira tofauti, magari yanayotumika Zanzibar yanatumika kwa siku pengine kilometa 30, hapa mtu anasafiri takribani kilometa 200, 300 mpaka 500 mpaka 1,000 kwa siku, 1,200 naambiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ukinunua gari inabidi vitu vyote hivi uviangalie, sio uangalie price tu. Uangalie comfort, uangalie safety, uangalie mainatainance cost na vitu vingine vyote. Ahsante. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la msingi lilisema ni lini Serikali itamalizia Skimu ya Ipatagwa, Kongoro/Mswiswi na Motombaya, itamalizia lini? Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie Serikali itamalizia lini skimu hii ambayo ilishaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, matatizo ya wananchi wa Mbarali yanafanana sana na matatizo ya wananchi wa Chunya ambako kuna Bwawa kubwa la Matwiga ambalo linajengwa kwa msaada wa Serikali ambalo limefikia asilimia karibu 80. Je, Serikali ni lini itamalizia ujenzi wa bwawa hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi kama Wizara ya Maji tunatambua kabisa umuhimu wa umwagiliaJi na tunatambua asilimia kubwa ya wananchi wanaishi vijijini na kilimo wanachotegemea ni kilimo cha kudra za Mwenyezi Mungu kwa maana ya kwamba mpaka mvua inyeshe. Hata hivyo, kwa kuwa sasa hivi tunaenda katika Tanzania ya viwanda, tunatambua tunapoenda katika kilimo cha umwagiliaji tutaweza kuwa na kilimo cha kisasa na tutaweza kupata mazao ambayo yatakuwa toshelevu kwa chakula lakini hata katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo cha umwagiliaji, sisi kama Wizara ya Maji tumeona kumekuwa na changamoto nyingi sana; moja, kumekuwa na miradi mingi lakini haijakamilika, tumekuwa na skimu za umwagiliaji lakini hakina chanzo cha maji, kinalima msimu mmoja. Waziri wangu ameona haja ya kupitia masterplan ya kilimo kile cha umwagiliaji ili tuwe na njia bora sasa, tuwe na miradi michache lakini itakuwa na tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia sasa, moja ya miradi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameorodhesha Mbarali na eneo lake, tutatekeleza kwa wakati katika kuhakikisha tunakipa nguvu kilimo hiki cha umwagiliaji.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Swali la kwanza, majibu ya Serikali yanaonyesha kwamba uchapishaji wa mara kwa mara wa ripoti hizi ni muhimu sana, kwanza kwa best practice, openness na ease of reference.
Ni kitu gani kimefanya ripoti hizi zisichapishwe kwa miaka minne mfululizo? La kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naiunga mkono sana Serikali kwa juhudi zake za kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani kwa ku-appoint Majaji wengi. Hata hivyo, kuna practice hii ya Majaji kwenda likizo mwezi Desemba na Januari ambayo ni ya historia tu. Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa wa kuwapangia Majaji likizo wakati wowote wa mwaka (Januari mpaka Desemba) badala ya kuwaweka wote kazini na kwenda likizo Desemba mpaka Januari?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu iliyosababisha Law Reports kutotoka kwa wakati, kwanza ilikuwa ni mabadiliko makubwa sana ya Editorial Board. Editorial Board ya Law Reports hizi ni Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pamekuwa na mabadiliko makubwa pale ambayo yalifanya kazi ya uhariri wa hizo kesi ichukue muda kwa sababu siyo kuzihariri tu ni pamoja na kuzichambua na kuzihariri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo hilo limeonekana na ndiyo maana tumeamua kuchapa ripoti zote nne kwa wakati mmoja na baada ya hapo Mahakama na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumekubaliana kwamba sasa tutaanza kutoa annual reports.
Napenda tu kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari katika huu mwaka wa 2018 tumekwishaandaa asilimia 42 ya mashauri yaliyoamuliwa. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu mwisho wa mwaka tutatoa ripoti ya mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, kuhusu likizo ya Majaji mwezi Desemba mpaka Januari, nikubaliane na wewe kabisa kwamba ni utamaduni wa nchi za Commonwealth kwamba Desemba na Januari Majaji wote wanakwenda likizo kwa sababu huko kwa wenzetu Uingereza mwezi Desemba na Januari kila kitu kinasimama na miezi hiyo watu hawafungwi ili wamalize Krisimasi ndiyo waende jela. Ni utamaduni tumeurithi, kwa hiyo, nitamshauri Mheshimiwa Jaji Mkuu tuuangalie kwa mukhtadha na mazingira ya Tanzania. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana. Kwanza kabisa wananchi wa Busokelo Kata ya Lufilyo wanakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kukushukuru sana kwa utendaji wako. Ulienda Kata ya Lufilyo ukiwa Naibu Waziri wa Elimu, ulisaidia sana katika uanzishwaji wa ujenzi wa Kituo cha VETA pale kwenye kata hiyo. Wanakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza; la kwanza; madini ya granite ni mazito sana na ndiyo maana katika kuyabeba kutoka Lufilyo kwenda mpaka Mbeya inaharibu miundombinu hasa hasa ya barabara sababu ya uzito.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wawekezaji waweze kuweka mtambo wa kutengeneza madini hayo hapo hapo sehemu ya Lufilyo ili tusiharibu miundombinu? La kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, uwekezaji katika Kata ya Lufilyo na Jimbo la Busokelo unafanana kabisa na uwekezaji katika Wilaya ya Chunya. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara Chunya mwanzoni mwa mwaka huu na alishuhudia uchenjuaji wa tailings (makinikia) kwa wazawa na wageni na alifurahishwa sana na uchenjuaji huo uko Chunya. Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba sasa hivi Serikali iko kwenye mchakato wa kuweza kuweka mtambo wa kuchenjua makinikia hapa nchini na akapendekeza kwamba Chunya inaweza kuwa sehemu mojawapo ya kuweka mtambo huu wa kuchenjua makinikia (smelter). Je, mchakato huo wa kuweka smelters nchini hasa Chunya umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kwanza kabisa nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba kweli granite zina uzito mkubwa, lakini katika hatua za ku- process ni mwekezaji mwenyewe ndiye ana jukumu la kuangalia ni sehemu gani anaweza akaweka mtambo wa ku-process ili uweze kumtengenezea faida. Kwa hiyo, anatakiwa afanye cost benefit analysis kusafirisha na ku- process katika eneo husika na sisi kama Wizara ya Madini tunapendekeza mtu a-process madini katika eneo la uchimbaji ili atengeneze ajira katika eneo lile, hiyo moja.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika uchenjuaji wa tailings kwa manufaa ya Wabunge wote kufahamu kwanza tailings na makinikia ni vitu viwili tofauti. Tailings ni mabaki ya dhahabu katika udongo ambao umechenjuliwa katika hatua za awali yaani unapochenjua kwa kutumia mercury zinabaki tailings kwa ajili ya ku-process katika CAP yaani katika process ya aina nyingine. Sasa kutengeneza mtambo wa makinikia ni kweli kabisa Wizara ya Madini inashirikiana na makampuni makubwa kutoka nje kuweza kuwekeza katika mitambo mikubwa ya kuweza kufanya smelting. Mpaka sasa hivi tuna kampuni 27 ambazo zimekuja kuonesha nia za kuwekeza, kuanzisha smelters pamoja na refineries na mpaka sasa hivi tayari tuna kampuni 10 zime-qualify, kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na hizo kampuni za nje muda si mrefu tutaanzisha zile smelters hapa nchini. Ahsante.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Serikali imekiri kabisa katika majibu haya kwamba sheria iliyopo sasa hivi ni ya mwaka 2001 na kanuni za mwaka 2012. Ni ya zamani kweli kweli, lakini vilevile mwaka 2006 Serikali ilisaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku na mwaka 2008 Bunge lako liliridhia mkataba huo. Sasa hivi ni ziadi ya miaka 10, mkataba huo bado haujawa domesticated ndio maana nasema sheria hii haijaletwa hapa Bungeni ili iweze kurekebishwa.
Je, majibu haya ya Serikali ni kweli mwaka huu wataleta sheria hiyo Bungeni hapa sio kuniridhisha mimi? La kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwa bahati mbaya sana zao la tumbaku uzalishaji wake unashuka kila mwaka badala ya kupanda bahati mbaya sana na mwaka huu imekuwa mbaya zaidi kwamba hivi ninavyoonge viko vyama vya msingi vya wakulima ambavyo havijapata makisio. Kwa hiyo hawajui kwamba mwaka huu watalima tumbaku au hawatalima na mwezi huu wa tisa ni wa mwisho wa matayarisho.Kwa mfano, Jimboni kwangu kuna Chama cha Msingi cha Upendo...
... na Kikola. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na namshukuru Mheshimiwa Mwambalaswa kwa swali nzuri. Ni kweli kama Serikali tuliridhia mkataba huo tamko hilo kwa ajili ya kupunguza matumizi ya tumbaku duniani ikiwemo Tanzania na ni kweli kwamba Serikali kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba tuko kwenye mchakato wa kufanya marekebisho mbalimbali na tumedhamiria mchakato huu ukikamilika tutaileta haraka iwezekanavyo katika Bunge lako hili tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba ni kweli matumizi ya tumbaku au mahitaji ya tumbaku kila mwaka yanaendelea kupungua kutokana na hili hili azimio ambalo tulilisaini na nchi nyingi ambao wamelisaini pia. Kwa hiyo, zao la tumbaku lina masharti mengi sana sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka jana tulitakiwa kwamba Tanzania kuzalisha tani 72,000 lakini mwaka huu ni tani 55,000 tu kwa sababu tumepata masharti mapya, sasa hivi uzalishaji wa tumbaku kwamba sharti mojawapo kwamba yale mabani yatumie muda miti iliyopandwa na mzalishaji mwenyewe. Na wameshatoa notice ikifika mwaka 2020 kama bado tumbaku yetu tunakausha kwa kutumia miti ya asili maana yake tunaharibu mazingira hawatanunua tumbaku yetu hata kilo moja.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima wote tuzingatie sheria hii kwa sababu tumesharidhia, tuanze kupanda miti yetu ya kisasa kwa ajili ya kufanya ukaushaji wa tumbaku hiyo, la sivyo, soko hilo tutakuwa tumelipoteza kabisa na kilimo hichi kitakuwa kimekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ni vizuri tukafanya diversification of crops yaani tukaangalia na mazao mengine kulima. Kwa sababu zao hili kila siku linaendelea kupigwa vita na wahitaji wenyewe, ahsante.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo nimeyaelewa yameeleweka nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, utafiti ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kilimo lakini nao ustawi wa wananchi kwa kujipatia kipato nayo ni muhimu. Kwa kuwa wananchi hawa wana eneo dogo la kulima na nyuma ya kitongoji hicho ni hifadhi. Je, Serikali haioni umuhimu wa angalau kugawa pori hili ambalo ni zaidi ya heka mia tano, kugawa kidogo kuwapatia wananchi waweze kulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu sana kitongoji hicho na hiyo kata anaifahamu kwani wapiga kura wake wako huko. Je, yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kwenye kitongoji hicho kwenda kuwaelimisha wananchi hao kwamba utafiti ni bora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana, kwa sababu ni Mbunge ambaye anajitoa kwa dhati katika lile Jimbo lake la Chunya kuhakikisha kwamba wakulima wote hususani wa zao la tumbaku na hata hiki kituo kidogo cha utafiti wanatendewa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba niseme tu kwamba, kile kituo chetu cha utafiti pale Mtanila ni kweli kuna wapiga kura wangu wako pale na mimi nakifahamu na nimefika lakini kinachukua eneo la hekari mia tano na ni hekari tatu tu zinatumika tu kwa ajili ya kituo hicho kwa sababu vituo vya utafiti huwa vinachukua eneo kubwa sana. Kwa maana hiyo nimtake kabisa Mheshimiwa Mzee wangu Kilasile Mwambalaswa kwamba eneo hilo linatumika kwa ajili ya utafiti na ndio maana hata Kituo chetu kile cha Uyole kinatumia eneo hilo katika suala zima la mazao ya mahindi na maharage pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la nyongeza la pili niko tayari kufika Chunya na baada ya Bunge lako Tukufu nitafanya ziara ya kwenda huko. Ahsante.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaishukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa hivi mkandarasi yupo Wilayani Chunya kwa kupeleka umeme REA III, anafanya upimaji katika Vijiji vya Ifumbo, Soweto, Mawelo na vinginevyo. Kuna Kijiji kinaitwa Itumbi katika Kata ya Matundasi, kijiji hiki Serikali kupitia Wizara inajenga kituo cha mafunzo kwa wachimbaji wadogo (center of excellence) lakini Kijiji hiki hakimo kwenye Awamu namba tatu ya kupeleka umeme. Je, Serikali haiwezi kukiangalia Kijiji hiki kwa jicho la pekee na kupeleka umeme katika awamu hii ya tatu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge katika swali lake. Kwa kweli kituo cha Matundasi pamoja na Itumbi ni kati ya maeneo ambayo yapo kwenye center of excellence kwa upande wa madini na baada ya kufanya survey Mheshimiwa Mbunge, kijiji kipo kwenye mpango sasa kwa sababu ni maeneo ya vipaumbele kwenye miradi ya maendeleo, kwa hiyo, kipo kwenye mpango wa fedha wa mwaka huu. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Serikali imetoa majibu kitaalam sana na Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba uwepo wa gereza mahalI unapunguza gharama za usafiri, unaharakisha uendeshaji wa kesi, vilevile unapunguza msongamano magerezani ambao ni kubwa sana kwa sasa. Pamoja na majibu hayo mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Chunya ni Wilaya kongwe sana hapa nchini. Katika Wilaya tatu kongwe Chuya imo, mwaka huu inatimiza karibu miaka 80. Je, rasilimali fedha itakapopatikana Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwamba ataipa Chunya kipaumbele kujenga gereza Wilayani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika kipindi cha mpito kabla ya kujengwa kwa gereza hilo, je, Serikali ipo tayari kujenga walau chumba, siyo gereza, chumba cha mahabusu ili kuweza kupunguza gharama hizi ambazo Serikali imezisema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Rukwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale bajeti itakapokaa vizuri Chunya itakuwa eneo la kipaumbele. Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza yeye binafsi kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo kuanza mchakato ambao unaendelea wa ujenzi wa bweni moja na jengo la kuishi Askari ambao umefikia 90%.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kwamba litakapokamilika kwa 100% tutaanza kupeleka wafungwa na kuanzisha kambi ambapo wafungwa hao tutawatumia kwa ajili ya kufyetua matofali ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa gereza. Wakati tunasubiri bajeti ikae vizuri Serikali tutaunga mkono nguvu hizo kwa kuhamasisha wafungwa na kutumia rasilimali zilizopo Chunya ili tuweze kutatua tatizo hili angalau kwa kuanzia gereza la mahabusu ili kupunguza msongamano.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Bado narudi kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kuhusu tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye kalenda ya Bodi ya Tumbaku ili pembejeo zifike nchini mwezi Agosti na Septemba, makisio hutolewa tarehe 31 Machi, ndiyo deadline. Sasa makisio yametolewa kwa makampuni matatu ambayo yanafanya biashara hapa nchini; kampuni moja haijatoa makisio, hiyo ina maana wakulima wa Tabora, Chunya, Ruvuma, Mpanda watakosa kulima tumbaku msimu ujao. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuitisha kikao cha dhararu kati ya Bodi ya Tumbaku na Wabunge wanaolima tumbaku ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nakubaliana na yeye kwamba kukaa na wanunuzi kufanya makisio mapema iwezekanavyo ikiwezekana mapema mwezi Machi, ni jambo la msingi kwani litasaidia wakulima wetu kujua ni kiasi gani wanahitaji kuagiza kupitia bulk procurement system.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni kwamba tuko tayari kukaa na huyu mnunuzi mmoja ambaye bado hajatoa makisio? Jibu ni kwamba Mheshimiwa Mwambalaswa niko tayari na baada ya hapa nitatafuta namba zao na kuwapigia simu na kuona kwa nini mpaka sasa hawajatoa makisio kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa matatizo ya wananchi wa Rungwe kuhusu barabara yanafanana kabisa na matatizo ya wananchi wa Chunya hasa hasa kwa barabara inayotoka Chunya – Kiwanja - Ifumbo - Mjele, ambayo sasa hivi inaunganisha Mikoa miwili ya Songwe na Mbeya; na kwa kuwa Mamlaka ya Wakala wa Barabara (TARURA) toka imeanzishwa Chunya hakuna barabara hata moja ambayo wameikarabati. Je, Mheshimiwa Waziri anatoa maagizo kwa TARURA ili waikarabati barabara hiyo iweze kupitika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri kijana mchakapa kazi yupo tayari kuongozana name kwenda Chunya ili akaangalie kazi ambazo wanafanya TARURA katika Halmshauri ya Chunya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwa barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja na mipango iliyopo na kwa sababu michakato hii inaanzia kwenye ngazi ya Halmashauri, inakuja kwenye Mkoa mpaka ngazi ya TAMISEMI, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane baadaye tupate taarifa sahihi ya eneo hili na tuweke mipango mahususi ambayo inaweza kutatua shida hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anauliza kama nipo tayari. Mimi nipo tayari sana wakati wowote. Tupande ratiba twende tuone eneo hili, turudi kufanya mipango ya kukamilisha na kuondoa kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.