Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (5 total)

MHE. MAULID S. MTULIA Aliuliza:-
Taifa lina tatizo kubwa la ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana. Vijana wa Jimbo la Kinondoni wameamua kujiajiri katika sanaa mbalimbali kama vile maigizo, maonesho ya mitindo na michezo mbalimbali:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea vijana hawa vifaa, mitaji na menejimenti ili kuongeza tija katika kazi zao;
(b) Je, Serikali imefikia wapi katika suala la hatimiliki ili Wasanii, Wanamichezo na Wanamitindo wetu waweze kupata haki zao.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA
MICHEZO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, nianze wa kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kutambua mchango wa sanaa mbalimbali kama sehemu ya chanzo cha ajira kwa vijana wetu kama Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge ambaye amelionesha hilo katika Jimbo lake la Kinondoni. Wizara yangu kwa sasa iko katika mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa, ambapo dhima kubwa ya mfuko huo ni kusaidia kuinua kipato, kuongeza tija, kukuza uwezo na weledi kupitia utaratibu wa upatikanaji fedha utakaowekwa na hivyo kuwawezesha wasanii kuzalisha kazi bora za sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ya ndani na ya nje.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa unaandaliwa, Serikali inashauri Halmashauri zote ziwasaidie vijana wanaojishughulisha na sanaa kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa kuwa sanaa pia ni sehemu ya ujasiriamali na ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wetu kwa sasa. Aidha, sekta binafsi, mashirika, Serikali za Mitaa na taasisi mbalimbali zinaombwa kushirikiana nasi katika kuinua, kukuza na kuboresha vipaji kwa wasanii ili
waweze kujikwamua kiuchumi.
(b) Kuhusu Hakimiliki, Wizara yangu kupitia Bodi ya Filamu, COSOTA na BASATA zimeendelea kuwaelimisha wasanii wa fani mbalimbali kuzisajili kazi zao ili ziweze kutambuliwa, kupata udhibiti na ulinzi kutokana na wizi wa kazi za sanaa. Aidha, Serikali imeendelea kushughulikia migogoro na biashara haramu ya kudurufu kazi za sanaa ili wasanii waweze kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Spika, haki na maslahi ya wasanii yanalindwa kwa Sheria Na. 7 ya mwaka 1999 ya Hakimiliki na Hakishiriki, Sheria Na. 4 ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya 1976 na Sheria Na. 23 ya Baraza la Sanaa la Taifa ya 1984. Serikali inaendelea na urasimishaji wa tasnia ya filamu na muziki ambapo kazi za wasanii hawa zinawekwa stempu za TRA ambazo huwezesha kubaini nakala halisi. Serikali na taasisi zake itaendeleza zoezi la urasimishaji kwa fani nyingine.
MHE. MAULID S.A. MTULIA aliuliza:-
Sera yetu ya Afya ni kuchangia gharama ili kupata huduma ya afya isipokuwa kwa wazee, mama na mtoto:-
Je, ni fedha kiasi gani zimekusanywa kutokana na tozo za uchangiaji gharama ndani ya miaka mitano na ni nini matumizi ya fedha hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mwongozo, fedha za uchangiaji zinakusanywa katika vituo vya kutolea huduma na zinatumika mahali zilipokusanywa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma. Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015, jumla ya Sh.62,244,000,000 zimekusanywa kutoka katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Mheshimiwa Spika, kulingana na mwongozo huo, fedha hizi zinapaswa kutumika kwa kuweka kipaumbele katika ununuzi wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba lakini pia ukarabati mdogo, kulipia maji, umeme na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa.
MHE. ZAYNAB M. VULLU (K.n.y. MHE. MAULID S. MTULIA) aliuliza:-
Serikali inafanya juhudi kubwa ya kuzuia biashara ya ukahaba kwa kuwakamata wauzaji na wanunuzi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Pamoja na jitihada hizo bado biashara hiyo haramu inaendelea kwa kasi ileile:-
Je, Serikali ina mpango gani mbadala wa kuzuia biashara hii haramu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikipambana na watu wanaojihusisha na vitendo vya ukahaba nchini. Jeshi la Polisi limekuwa likifanya misako kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kubaini na kukamata watu ambao wanajihusisha na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya Kitanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukahaba ni suala mtambuka ambapo kulikabili kunahitaji ushirikiano wa wadau wengi. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi, imeandaa mkakati wa kushirikisha taasisi nyingine za Serikali kama vile TAMISEMI, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii na kupunguza hatimaye kumaliza vitendo hivi ambavyo vinautia doa utamaduni wa nchi yetu. Aidha, mkakati huu unahusisha ujenzi, kutoa elimu ya madhara ya ukahaba, faida za ujasiriamali na kuwashirikisha viongozi wa dini katika kufundisha maadili.
MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:-

Walemavu wana mahitaji maalum ukilinganisha na watu wasiokuwa na Ulemavu na idadi ya walemavu imekua ikiongezeka siku hadi siku kutokana na ajali za barabarani hasa zitokanazo na usafiri wa bodaboda:-

(a) Je, Serikali inaweza kutoa orodha ya idadi ya watu wenye ulemavu nchini kwa kuzingatia makundi yao kwa asilimia?

(b) Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuwajengea uwezo wa kujitegemea watu wenye ulemavu hasa Vijana, Watoto na Wanawake ili kuondoa utamaduni wa kuendesha maisha yao kwa kuombaomba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni lenye kipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, idadi ya Watu wenye Ulemavu kwa kuzingatia makundi yao na kwa asilimia ni kama ifuatavyo:-

Watu wenye Ualbino ni 16,477 sawa na 0.04%; walemavu wasioona ni 848,530, sawa na 1.93%; walemavu ambao ni viziwi ni 425,322, swan a 0.97%; walemavu wa viungo ni 525,019, sawa na 1.19%; walemavu wa kumbukumbu ni 401,931, sawa na 0.91%; walemavu wa kujihudumia ni 324,725, sawa na 0.74%; na Ulemavu mwingine, yaani kwa ujumla wake ni 99,798, sawa na 0.23%. Kulinganisha na takwimu hizo jumla ya watu wenye ulemavu, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 ni watu 2,641,802.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hivi sasa inakamilisha zoezi la uanzishwaji wa regista ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Faida nyingine ya kuanzisha regista hizi zitatusaidia pia kutambua sababu za kuongezeka kwa ulemavu katika kila eneo na changamoto zinazowakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha watu wote wenye ulemavu hasa vijana, watoto na wanawake hawaachwi nyuma kiuchumi, Serikali inaendelea kuwajengea uwezo kuhakikisha watoto wote ikiwa ni pamoja na wenye ulemavu wanapata elimu ya msingi na sekondari ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea. Pia inatoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi ya vijana na wanawake wenye ulemavu kupitia vyuo vya watu wenye ulemavu na programu ya kukuza ujizi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawezeshwa kiuchumi, Serikali inatoa mkopo wa fedha ya asilimia mbili (2%) zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Hata hivyo, mipango yote ya uwezeshaji kiuchumi nchini ni jumuishi ikiwajumuisha pia watu wenye ulemavu.
MHE. MAULID S. A. MTULIA aliuliza:-

Vijana wetu wanafanya kazi za sanaa nzuri sana lakini kipato wanachokipata hakilingani na ubora wa kazi zao:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana hawa kupata stahiki ya kazi zao?

(b) Je, sera na sheria zinasaidiaje wasanii wetu kumiliki na kunufaika na kazi zao za sanaa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 inaelekeza kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia hakimiliki ambayo ni sehemu muhimu ya dhana pana ya haki bunifu (intellectual property). Hivyo, mwaka 1999 ikatungwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ambayo chini yake maslahi ya watunzi wa kazi za Sanaa, watafsiri, watayarishaji wa kuhifadhi sauti, wachapishaji na kadhalika yanalindwa kisheria na chombo cha kusimamia haki hizo, yaani Chombo cha Hakishiriki Tanzania (COSOTA).