Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Boniphace Mwita Getere (26 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Bunda na kwa bahati nzuri nina Kata saba, kwa hiyo, niwashukuru wapiga kura wa Nyamang’uta, Nyamswa, Salama, Mihingo, Mgeta na Hunyali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Wabunge wote nikiwemo mimi mwenyewe, hatua ya kufika hapa ni ndefu sana. Kwa kweli, Mwenyezi Mungu ametusaidia tumefika hapa wote, jambo la kwanza naomba tupendane, hii habari ya kushabikia vyama na kunyoosheana vidole itakuwepo, lakini iwe kwa wastani, kwa sababu wote tunaishi kama binadamu na tukifa au tukifiwa tunaenda kupeana pole, kwa hiyo tunapokuwa humu ndani naomba tupendane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Wabunge wa CCM wajue kwamba, nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumekabidhiwa sisi, hawa jamaa zetu wapo tu kwa kupinga na kupiga kelele. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye kila la maana kuwatendea haki Watanzania ili tunapofika 2020 hawa watakwenda kuuliza, tuliwaambia CCM hamuwezi sasa mnaona mmefanya nini? Kwa hiyo, tufanye kila la maana ili nchi yetu iweze kupata maendeleo ikifika 2020 tuwaoneshe kwamba tumefanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, sijui huwa najiuliza mara mbili mbili hivi kuna nini? Kwa sababu kabla ya mambo yote tunasema nchi inaliwa, nchi mbovu, hali mbaya, tunalia kila mahali, leo tumepata jembe, tingatinga anapiga kila upande bado watu wananung’unika nini? Hivi nchi hii tusipopata Rais nje ya Magufuli tunapata Rais wa aina gani? Kilichobaki ni kusahihishana tu pale na hapa mambo yanakwenda sawa, lakini Rais anafanya kazi nzuri sana.nn(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye utawala bora. Katika utawala bora naangalia mafunzo ya Halmashauri za Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata. Tumekuwa na tabia ya kuchagua viongozi halafu hatuwapi mafunzo, hata humu ndani Wabunge tumo tu, hatukupata mafunzo bora, juzi nilikuwa namuuliza mwenzangu hapa, hivi maana ya mshahara wa Waziri ni nini? Ananiambia na mimi sijui! Unashika mshahara wa Waziri, mshahara uko benki wewe unaushikaje? Anasema sijui. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulitakiwa kuelezwa kwamba hivi vitu vinakwendaje, kuna Vote, kuna sub-vote, kuna program tulitakiwa tupewe mafunzo. Mafunzo kwa Watendaji wa Vijiji ni jambo la msingi sana, lakini imezungumzwa hapa habari ya Wenyeviti wa Vijiji kulipwa mshahara au kupewa posho. Serikali za Halmashauri au Halmashauri za Wilaya haziwezi kutoa posho, hilo tukubaliane!
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote tumetokea maeneo hayo, tumetoka kwenye vijiji, tumetoka kwenye Kata tunakuwaje hatuwatetei watu hawa wapate posho nzuri? Tunapaswa kufanya kila namna Watendaji wa Halmashauri za Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji wapate posho nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo nizungumzie habari ya migogoro ya mipaka. Kuna migogoro ya mipaka ya Wilaya na Wilaya, kuna migogoro ya mipaka kati ya Kata na Kata, kuna migogoro ya mipaka kati ya Vijiji na Vijiji na ni mingi sana, kwenye Jimbo langu ipo katika kila eneo. Tunaomba Wizara zinazohusika na maeneo hayo, TAMISEMI na Ardhi washirikiane kumaliza migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Shule za Msingi, jambo ambalo Bunge la Kumi na Moja tutafanya na tutapata heshima ni kupata madawati ya watoto, madawati ya wananfunzi katika shule za msingi. Ukienda shule ya msingi ukiingia darasani watoto wanaamka wanakusalimia shikamoo mzazi, unasema marahaba, halafu unawaambia kaeni chini au unafanyaje? Wanakaa kwenye vumbi! Huwa najiuliza, naomba Waziri Mkuu afanye kazi mmoja, tufanye kazi moja au kazi mbili tu na nitoe njia. Kwanza, tukubaliane kwamba Bunge hili Bajeti yoyote kutoka Wizara mbalimbali ikatwe tupate bilioni 150 za kuweka madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga hesabu hapa yamepungua madawati 1,500,000 kama milioni nne, kwa hiyo, tukipata bilioni 160 au 170 maana yake madawati nchi nzima yanakuwepo. Waheshimiwa Wabunge tukitoka hapa tutakwenda kupambana na tatizo la madawati hamtakwepa, saa hizi kuna meseji zinazotoka kwa DED ooh! Mheshimiwa Mbunge hela yako ya Mfuko natengenezea madawati, nani kakutuma utengeneze madawati mimi sijafika huko?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tukubaliane kwamba madawati ni jambo la kwanza katika Bunge hili. Tutoke humu tujue kwamba tunakwenda kupata madawati nchi nzima, tukisema hii ya Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa tumetofautiana kipato katika Mikoa. Dar es salaam watatengeneza, Arusha watatengeneza, Bunda je, ambayo ni Wilaya ya maskini? hawawezi kutengeneza madawati! Kwa hiyo, nafikiri kwamba jambo la msingi sana kufanya mambo kama haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kama hatuwezi kuweka bajeti bilioni 160 kutoka Wizara mbalimbali, tukubaliane na Waziri Mkuu aunde Kamati ihusishe Kambi zote, Kamati itafanya kazi moja ya kujua idadi ya madawati nchi nzima, lakini kujua mashirika mbalimbali. Kwa mfano, tukasema hivi ukiweka shilingi tano katika Makampuni ya Simu, ukiweka shilingi tano kwa Makampuni ya Mafuta, ukiweka taasisi mbalimbali tulizonazo, hatuwezi kupata bilioni 160? Inawezekana! Waziri Mkuu aunde Kamati ili tuweze kupata watu, wafanye tathmini, watuletee hapa, wote tuchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Bunge letu limechanga, tumechanga bilioni sita au uwongo jamani?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumechanga bilioni sita kutokea Bungeni humu ndani, tunataka Mashirika mengine yote na Taasisi zingine zichange.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwa leo yalikuwa hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo.

Nachukua nafasi hii kuwashukuru Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na wafanyakazi wote wa Wizara hii wakiongozwa na Katibu Mkuu wao. Nachukua nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa nguvu na juhudi kubwa anazozifanya katika kuokoa mali ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili iko dhana inajengwa hapa kwamba Rais Magufuli anafanya kazi yake bila kuhusisha Chama cha Mapinduzi. Sasa leo nimekuja hapa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuonesha wenzetu kwamba Rais hafanyi mambo yake, anafanya ya Chama cha Mapinduzi. Baadaye kama kuna mtu anahitaji Ilani hii tutampa aisome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kunukuu maandishi ya Chama cha Mapinduzi kwa ujumla wake. Na. 4 inasema:-

“Katika miaka mitano ijayo 2015 - 2020, CCM ikiwa madarakani itaelekeza Serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendeleza na kupambana na changamoto kubwa nne.

(i) kuondoa umaskini; kupambana na makinikia, kuzia wizi ni kupambana na umaskini;

(ii) Kupunguza tatizo la kukosefu wa ajira hasa kwa vijana wetu. Kutafuta fedha zinazoibiwa ni kuleta ajira ambayo tutaitumia baadaye kwenye viwanda; na

(iii) Kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hii ni ilani inayozungumza mambo hayo, maana yake CCM tunaelekeza kwamba Rais wa kwetu atakayepatikana atatekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikutosha tukasema, sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, Serikali pia zinaelekezwa na CCM, zinatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma. Kwa hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John PombeMagufuli anatekeleza yale tuliyomwelekeza Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ile dhana inayojengwa kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya yake, siyo kweli na yako mengi humu ndani. Mkitaka tutawapa mwendelee kusoma hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo nayashangaa humu ndani, nayashangaa sana. Leo duniani kote, Korea Kusini pamoja na vita waliyonayo na Korea Kaskazini wamemfukuza Rais wao kwa sababu ya ubadhirifu; leo Brazil pamoja na umaskini ambao umekithiri, wamemfukuza Rais wao. Leo Urusi pamoja na juhudi kubwa za Putin lakini leo wanaandamana kwamba anakula rushwa. Sasa leo Rais wetu anapopambana kutoa rushwa na ubadhirifu, Venezuela nao wamemtoa Rais, naambiwa hapa. Rais wetu anapopambana kwenye mambo ya ubadhirifu, tunashindwa kumshangilia na kumpa na pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba siyo jambo jema, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wote tukaungana pamoja, tukashughulikia ubadhirifu huu na bahati nzuri sasa taarifa zilikuwa hewani kwamba wale watu ambao mlikuwa mnasema watatupeleka Mahakamani, wameshakubali kulipa. Sasa shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelekezo haya sasa, niende kuchangia, nijielekeze kwenye mambo ya viwanda na kilimo. Tunapozungumza viwanda maana yake tunazungumza kilimo; tukiendeleza kilimo chetu, ni lazima tubadili kilimo chetu cha mazao mbalimbali ili kupata nakisi ambayo itasaidia kwenda kuendeleza viwanda. Ni lazima ufugaji wetu tuubadili ili tuweze kupata mazao bora kwa ajili ya kupata viwanda. Malighafi itakayopatikana katika kilimo na katika mifugo isaidie kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kwenye Jimbo langu la Bunda ni tatizo kubwa sana na namshukuru Mheshimiwa Rais kwamba anapopambana na ufisadi huu hela zitapatikana ili zije kwenye maji katika Jimbo la Bunda. Tuna miradi mitatu ya maji; kuna mradi wa Nyamswa wa World Bank, mradi wa Kiloleli na Salamakati. Miradi yote hii haijaenda kwa sababu fedha hazijaenda kwenye maeneo yangu. Mheshimiwa Waziri anapokuwa kwenye bajeti yako, naomba ufikirie namna ya kupeleka fedha Bunda kwa ajili kuendeleza miradi yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya barabara. Tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, barabara ya Makutano
– Sanzati – Nata na tuna barabara ambayo inakwenda kukasimiwa kuwa barabara ya TANROAD ya Mgeta – Siolisimba – Mikomalilo. Kwa hiyo, naomba maeneo haya tuzingatie wakati tunapokuwa tunafanya bajeti hiyo waone namna gani mnasaidia miradi yangu kwenye Wilaya ya Bunda na Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Kongwa Mkoa wa Mara, ni ya muda mrefu sana na tumeisemea sana. Tunaomba kipindi hiki cha bajeti waikumbuke Hospitali ya Kongwa ambayo ni Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bandari yetu ya Musoma, hii ni bandari ya muda mrefu sana na kwa sasa hivi imechakaa. Tunaomba waitengee fedha na niliona wanaenda kuishughulikia. Kwa hiyo, waone namna gani ya kusaidia ili Mkoa wa Mara nao upate bandari na iweze kutumika vizuri. Bahati nzuri kuna meli ya MV Butiama ambayo iko Mwanza inatengenezwa. Kwa hiyo, ikitengemaa tuone namna ya kuifikisha Musoma kwa ajili ya kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna reli ya kutoka Tanga – Arusha – Musoma, tumeizungumza sana. Pamoja na kwamba tuna reli ya kati ambayo tunaipigia upatu, lakini hata reli hii inayotoka Tanga – Arusha – Musoma inaweza kusaidia katika maeneo yetu na kuendeleza uchumi wa watu wetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunazungumzia mambo ya wakulima, lazima tukubaliane namna ya kuboresha zao la pamba. Katika Mkoa wa Mara hakuna zao lingine la kibiashara, ni zao la pamba ambalo liko pale. Kwa hiyo, tunapokuwa tunazungumza haya mambo, ni lazima tuone ni namna gani tunapandisha bei ya pamba. Miaka mingi sana tumekuwa tukitegemea Soko la Dunia, lakini lazima tutegemee viwanda vyetu vya ndani ili tuweze kukuza bei ya pamba katika Mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya wafugaji. Tumekuwa na Kamati mbalimbali; kuna Kamati zimeundwa kwa Wizara tatu. Tunaomba zile Kamati zifike Mkoa wa Mara na hasa eneo moja linaitwa Kawanga kwenye Jimbo langu la Bunda ambako kuna migogoro mikubwa sana ya wafugaji kati ya Pori la Akiba la Ikorongo na eneo langu na Vijiji 15 vilivyopo kwenye maeneo haya ili tuweze kuona namna gani tunaweza kusaidia katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo mengi sana ya ndovu kwenye maeneo yetu. Tunaomba zile fidia ambazo zinahitajika kwenye maeneo haya; kuna Kijiji kimoja ama Vijiji vitatu vimebaki vya Maliwanda, Mgeta na Kyandege. Tuone namna ya kuvisaidia hivyo vijiji ambavyo havikupata fidia ya kifuta jasho ambapo vijiji vingine vimepata lakini vyenyewe havikupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda viwili vidogo vidogo vya maziwa, havifanyi kazi muda mrefu sana; kimoja kipo Kyandege na kingine kipo Mgeta. Kwa hiyo, tunaomba waone namna gani hivyo viwanda vinaweza kusaidiwa ili viweze kutoa mazao yao kwa ajili ya kuwapa faida wakulima wa maeneo hayo. Hivi viwanda vilijengwa enzi hizo za miaka ya nyuma tukiwa na Kiwanda cha Maziwa Musoma ambacho kimekufa, sasa tuone namna gani ya kuvifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya pamba viwili; Ushashi na Bramba. Kwa hiyo, tunaomba tuweze kusaidiwa kuvifufua viwanda hivi kwa ajili pia ya kuongeza zao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii zana inayozungumzwa ya tozo ya road license. Gharama za mafuta kwa miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikishuka sana, lakini hatujawahi kuona nauli ya kutoka Bunda kuja Dodoma inapungua. Kwa hiyo, hata tukipunguza habari ya mafuta, wala hawa watu wanaofanya biashara ya usafirishaji hawapunguzi gharama zao za nauli. Kwa hiyo, naona kwamba hii Sh.40/= tuliyoiweka tungeongeza Sh.10/= ili tuipeleke kwenye maji kwa ajili ya kusaidia akinamama wanaohangaika na maji kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tukiwa tunazungumza suala la walemavu, ni vizuri tukaona namna gani ya kupunguza baadhi ya gharama. Pamoja na kwamba zimepungua, lakini bado. Tuwasaidie walemavu katika maeneo mbalimbali na hasa wale watoto wanaotakiwa kusoma ili wapewe vifaa bora kwa ajili ya kujifunza na kwa ajili ya kupata manufaa katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ni kuhusu umiliki wa akinamama katika suala la ardhi. Sasa ni vizuri tukiwa tunazungumza hapa, tuone kama bajeti hizo zinawekwa kwenye maeneo haya ili tuweze kuona, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi na kwa Mkuu wake, jemedari wetu Mkuu Dokta John Pombe Magufuli, kwa kuongoza kazi nzuri anazozifanya, anatekeleza vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na hili niliseme tu, kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ninavyomuona namkumbukia sana Simba wa Nyika, Marehemu Mheshimiwa Mfaume Kawawa ambaye enzi hizo alikuwa akiagizwa kutekeleza jambo anatekeleza, Mungu amrehemu mahali alipo. Waziri Mkuu kila anapopewa nafasi ya kutekeleza mambo anatekeleza vizuri sana. Nimpongeze kwa kweli kwa mambo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza mambo madogo tu kwenye hii bajeti na kwenye hii hotuba ninayotaka kuitoa hapa au kwa maelezo ninayotaka kutoa; kwamba, hivi mtu akipata nafasi ya kuchangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, hivi mwaka ujao yale aliyoyasema atayaona mawili, matatu yametendeka au ni kusema tu halafu yanaishia hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kusema kwamba kwa nafasi hii nitakayokuwa nayasema hapa nataka kuyapima kwamba mwaka ujao nitakuja kuona nafasi nilichangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, yale niliyoyasema japo mawili matatu yametendeka? Kwa hiyo, nafikiri hili jambo litakuwa bora zaidi kwa Bunge kuchangia hii ofisi kwa sababu ndiyo eneo kubwa ambalo Waziri Mkuu analiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze kwenye miradi ya Jimbo langu la Bunda. Tuna miradi ya maji, katika miradi ya maji ya Jimbo la Bunda iko miradi mingi sana. Nimpongeze Waziri wa Maji, amekuja pale mara nyingi sana, kuna Mradi mmoja unaitwa Nyang’alanga – Mgeta ambao ulianza kwa bajeti ya milioni 495, sasa una milioni 910 mradi haujaisha na maji hayajatoka. Kila siku ripoti zinakwenda na hakuna ukaguzi unaofanyika wa kutoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ahati nzuri Naibu Waziri wa Maji amesema wale wote wanaohujumu fedha za maji watakipata cha moto. Namwomba afike pale sasa aone namna ya kuwashughulikia mradi wa maji Nyang’alanga ili kuweza kumuondoa mtu ambaye amekaa pale kwa muda mrefu na hakuna kazi inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Malambo. Bunge lililopita nilizungumza hapa malambo 12 yaliyokuwa yanataka kutengenezwa ya zamani kuyafufua. Tunayafufua kwa sababu kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Jimbo langu ni kilometa 25 lakini sisi maji hatuna tuna tabu sana ya maji katika Jimbo la Bunda. Tunataka kufufua malambo ya zamani yaliyochimbwa na Mtemi Makongoro na tumeleta bajeti kwenye Wizara ya Maji na Katibu Mkuu Wizara ya Maji alipokea huo mradi wetu na tunaomba aushughulikie, ninashauri haya mambo yafanyike mapema ili tuweze kupata maji kwenye Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya wanyama waharibifu kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 11 ambavyo wanyama waharibifu wapo kila siku, kila mazao yanayolimwa yanaliwa, hata katani zinazopandwa zinaliwa, hata pamba inayolimwa sasa hivi inaharibika. Tunaomba Serikali sasa ichukue hatua za kutosha za kuzuia wale wanyama wasiwe wanakuja kuharibia wananchi mazao ili wananchi waweze kujineemesha kwa sababu yale mazao ndiyo kipato chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu fidia. Toka haya mazao yameanza kuliwa tunadai zaidi ya milioni 360, kulikuwa na milioni 400 wameshalipa karibu milioni 182, kwa hiyo bado milioni 360 zinadaiwa, tunaomba Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na nimwombe Waziri Mkuu ahimize hii fidia ya wakulima iweze kupatikana kwa Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya afya katika Jimbo langu. Tumejenga zahanati tano na mpaka zahanati zingine tumeshaezeka, tunaomba Serikali, kwa sababu Bunge lililopita Wabunge walisema hapa, maboma yote ya zahanati zote na maboma ya vituo vya afya wakasema na Bunge la Bajeti hapa tulizungumza na Bunge lililopita tulizungumza, kwamba maboma yote yashughulikiwe na yaletwe hapa Bungeni na tuweze kutengeneza mkakati maalum wa kuyamaliza, sasa sijui hatua imefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa maboma matano ya vijiji vilivyotengeneza kwenye jimbo langu, Kijiji cha Kambubu, Chiling’ati, Komalio na Malambeka ili waweze kupewa fedha za kuweza kumalizia majengo haya. Nimuombe Waziri wa Afya aweze kutusaidia na Wizara ya TAMISEMI iweze kutusaidia katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya barabara, habari ya barabara ya lami kutoka Makutano kwenda Nyamswa hadi Sanzati, inaitwa makutano ya barabara ya lami kutoka Makutano – Sanzati. Ninavyozungumza hii barabara bila unafiki, Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana alikuja Mkoa wa Mara na akapita kwenye ile barabara akaiona, ni vitu vya aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayopita kwenye maeneo ya kaburi la Baba wa Taifa imekaa miaka zaidi ya sita haimaliziki na wale watu wanaotengeneza hiyo barabara wale wakandarasi hawaguswi, hivi ni akina nani hawa? Barabara ipo kila siku na vumbi zinakwenda kwenye kaburi la Mwalimu pale, hakuna mtu anamaliza hiyo barabara, why?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii tupo tunavuta upepo, huu upepo tunaovuta ni wa Mwalimu. Jamani mambo gani hayo? Aibu hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameliona hilo, nadhani atalishughulikia haraka iwezekanavyo ili tuweze kuzungumza haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, tuliahidiwa kupewa mkandarasi lakini hajaenda. Tuna Barabara ya Sanzati – Nata, mkandarasi hajapatikana, na kuna barabara ya kutoka Bunda kwenda Buramba na Buramba – Kisoria, mkandarasi bado naye anasuasua hajawa kwenye uwezo mzuri. Tunaomba Serikali ione namna gani ya kumaliza zile ahadi zake na hasa ile miradi ya muda mrefu ambayo inahitaji kumalizika. Barabara ya Makutano – Nyamswa – Sanzati ni ya muhimu sana, imeleta kero kubwa sana kwa wananchi wa Butiama na wananchi wa Kata ya Nyamswa na maeneo mengine yaliyopakana na barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi; namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Mkoa wa Mara, amezungumza na ametusaidia mambo mengi, lakini migogoro ya Vijiji vitatu vya Silolisimba, Lemuroli na Mkomalilo bado vina matatizo ingawaje Mkuu wa Mkoa anajitahidi kumaliza tatizo hilo, lakini bado, tunamuomba na bahati nzuri siku moja Mheshimiwa Naibu Spika alitamka hapa Bungeni kwamba Serikali ishughulikie namna ya kumaliza tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuone namna gani ya kulimaliza ili wananchi waweze kukaa vizuri kwa sababu kila siku ni mapanga. Bahati nzuri miezi miwili iliyopita wananchi wawili walikufa kwa ajili ya mapigano ya hiyo mipaka, kwa hiyo tunaomba tuone namna ya kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya Watendaji; katika jambo ambalo Wabunge tunashauri kwa kila mara na kama tuko Kikatiba katika kushauri jambo hili, hili suala la Watendaji hawa ambao tumepanga kuwafukuza, nadhani katika jambo ambalo tunaweza kulihimiza Bunge lifanye ni namna gani ya kuwaacha wale Watendaji wamalize muda wao, kwa sababu wengi wamemaliza miaka miwili, mitatu, minne, mitano, kuna haja gani ya kuwatoa sasa hivi? Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri tuone namna gani na tupate majibu mapema ili tujue namna ya kuwasaidia hao Watendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina miradi ya REA vijiji 21, Jimbo langu katika Mkoa wa Mara ndiyo Jimbo lenye vijiji vingi ambavyo havijafikiwa na umeme ingawaje Mheshimiwa Waziri amenisaidia vijiji vingine huko nyuma vilikuwa 32 sasa vimebaki 21. Tunamwomba yule mkandarasi wa REA kwenye Jimbo langu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alifungua mradi wa REA kwenye Jimbo langu, ajitahidi kumhimiza mkandarasi aweze kuimaliza ile miradi kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya Bandari ya Musoma, kuna miradi mikubwa pale ya Kimkoa, kuna mradi wa bandari na kuna mradi wa kiwanja cha ndege Musoma na mradi wa Hospitali ya Kwangwa. Kwa hiyo, Mkoa wa Mara kuna miradi mikubwa kimkoa, tunaomba Serikali iangalie namna ya kuimaliza ili wananchi wa pale waweze kupata huduma za kutosha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu la Bunda na Bunda nzima na Jimbo la Bunda, ardhi yetu imechoka sasa, tunaomba kama kuna uwezekano wa kupata pembejeo kwa ajili ya wakulima sasa na sisi tuingizwe kwenye mradi huo wa kupewa pembejeo ili wakulima waweze kupata mazao mazuri kwa sababu ardhi yao imechoka kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya Walimu wa sayansi shule za msingi na sekondari. Katika maeneo mengi ya Jimbo la Bunda kuna sekondari zaidi ya tisa hakuna Mwalimu hata mmoja wa sayansi. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri sasa Waziri anayehusika aweze kuona namna gani ya kutusaidia Walimu wa sayansi kwenye sekondari tisa katika Jimbo la Bunda ambazo hazina Walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine naviona hapa nikivisoma huwa vinanitia kichefuchefi kidogo. Kuna deni la watumishi wa Serikali, lakini ukiangalia deni la watumishi wa Serikali kuna vitu vingine vya kujitakia. Hivi inawezekanaje leo tuna watumishi wanaokaimu wengi katika Wizara mbalimbali na kila mtumishi anayekaimu anapewa nusu ya mshahara wa mtu aliyekuwepo katika nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama Mkurugenzi aliyetoka alikuwa anapokea mshahara wa milioni tano na yeye anaenda kukaimu anapokea milioni mbili na nusu na anakaa miaka kumi, mitano, saba, kumi na tano. Sasa hii kwa nini tunaitafutia Serikali madeni, kwa nini tusibadili sheria hizi za utumishi za kukaimu na sheria zile za kwenda kwa wakati wanakaimu kama ni mtu kwenda kukaimu tumwambie akaimu bure, sio akaimu kwa kulipa mshahara, tunatia madeni Serikali bure na tuangalie ile sheria namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kuangalia sheria ndogo hizi au sheria za Wanyamapori, Maliasili na Utalii na hasa zile sheria za fidia. Fidia imekuwa ndogo sana lakini mbaya zaidi kuna sheria zile za fidia ambazo hazijakaa sawa. Kwa mfano, kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa wananchi wanasema iwe ni mita 500, mita 500 ni nusu kilometa, lakini kutoka hiyo nusu kilometa buffer zone kwenda mpaka kilomita 1000 mkulima anatakiwa kulipwa kama amelima shamba heka 20 halafu tembo amekwenda amekula mazao yote, anatakiwa kulipwa heka tano tu, heka 15 nyingine ni sadaka, hii sheria ya wapi tena? Nafikiri kwamba ni vizuri wakaangalia hiyo sheria...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani zangu za awali kwa wote walioandaa hotuba hii ya Wizara ya Elimu na hasa Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Naibu Waziri.
Matatizo ya Jimbo langu la Bunda Vijijini; moja ni kutoa kibali cha ufunguzi wa sekondari ya (High School) ya Makongoro (Makongoro High School). Tunahitaji msaada wa Wizara, wananchi wamejenga vyumba vya madarasa, mabweni na jengo la utawala, tunahitaji shilingi 72,000,000 ili kumaliza ujenzi wa high school hii. Tunaomba msaada ili kupunguza makali ya michango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili ni upungufu wa walimu wa sayansi, (kemia, fizikia, biolojia na hesabu). Zaidi ya sekondari 30 wanahitajika walimu 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni matatizo ya mazingira ya vyoo. Zaidi ya shule za msingi 40, zina matatizo ya vyoo vibovu vya shule na tatizo la maji shuleni, hivyo naomba Wizara ya Elimu kupitia mashirika yake ya kutoa huduma za msingi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo la vyoo magonjwa ya watoto shuleni yameongezeka sana, (typhoid, kuhara, U.T.I). Naomba msaada wa suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba nne, matatizo ya maabara, madarasa na nyumba za walimu. Wizara iangalie namna ya kusaidia Jimbo hili jipya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kwa maeneo yanayohusu Jimbo langu la Bunda Vijijini. Jimbo la Bunda lina Vijiji 39. Matatizo ya umeme ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, REA I vijiji vilivyopata umeme ni Kyandege, Migeta, Mariwanda, Salama „A‟ na Hunyuri Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo umeme wa REA Phase I uliwekwa katika maeneo ya center (Barabara kuu). Aidha, maeneo yote ya Taasisi; Mashuleni, Hospitali, Ofisi) hakuna umeme. Aidha, katika Vijiji vya Mariwanda, Hunyari, umeme uliwekwa katika volt ndogo (muhimu). TANESCO Bunda wanajua.
REA II: Vijiji vilivyopata umeme ni Kiloreli, Kambubu, Nyamuswa, Marambeka, Salama Kati, Kurusanga, Mikomariro na Mibingo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo vijiji vya REA II nilivyovitaja kuanzia cha 1 – 6 umeme umewaka katika maeneo ya center tu. Taasisi zote za Umma hakuna umeme. Wizara imetoa agizo kupitia Mheshimiwa Muhongo (Waziri) kuwa Taasisi zote za Umma zipate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA III; vijiji ambavyo vinahitaji umeme ni Manchimaro, Tingirima, Nyangiranga, Rakana, Tiringati, Bigegu, Nyaburundu, Mahanga, Mmagunga, Nyariswori, Sarakwa, Majengo, Nyangere, Nyabuzame, Mmuruwaro, Nyang‟ombe, Nyanungu, Rubimaha na Bukoba,
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kuwa maeneo yote hayo yatapewa umeme wa REA Phase III kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni.
N.B. Vijiji vya Bukoba na Samata vimewekewa transformer, tunahitaji umeme uwake. Mungu ibariki Wizara, Mungu ibariki Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitangulize shukrani zangu za dhati kwa Serikali yangu ya CCM. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Fedha na Sekretarieti yake kwa kuthubutu kutoa mapendekezo yao kwa Mpango huu wa Maendeleo wa Mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya ni mazuri kwa sehemu kubwa. Mchango wangu katika mapendekezo yangu upo katika sehemu tatu:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni Elimu ya Bure Shule za Msingi na Sekondari. Kwa maoni yangu, fedha hizi zinazotolewa mashuleni na hasa shule za msingi, hazifanyi kazi iliyokusudiwa. Mfano, Shule ya Msingi „A‟ kwa mwezi itapata shilingi 230,000/=. Fedha hizi hugawanywa kwa asilimia ishirini ishirini. Kwa maoni yangu, fedha hizi hazitoshi hata kununua mpira.
Kwa mahitaji makubwa ya shule ni chaki, mitihani na utawala. Kwa nini Serikali isifungue akaunti maalum kila Halmashauri na fedha hizi zikawa katika akaunti hii na kila shule ikapewa mahitaji muhimu ya wanafunzi na utawala. Napendekeza style iliyokuwa inatumika enzi za Mwalimu, kila mwanafunzi alikuwa anapewa vitabu, madaftari, chaki na vitu vingine muhimu kuliko fungu la fedha hizi ambazo sehemu kubwa hazifanyi kazi. Fanyeni utafiti.
(b) Nashauri Serikali itenge fidia ya wakulima kwa mazao yaliyoharibiwa na wanyama waharibifu (ndovu) Jimboni kwangu. Wakulima wanadai zaidi ya shilingi milioni 400. Serikali ihakikishe fidia kwa wakulima, inalipwa.
(c) Malambo kwa wafugaji. Maeneo mengi ya hifadhi ya Taifa hayana maji kwa mifugo. Serikali iwe na mpango maalum wa kuchimba malambo Jimbo la Bunda.
(d) Vile vile Serikali iwe na mpango maalum wa kujenga vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu kwa shule za msingi na sekondari. Mfano, Jimbo langu la Bunda lina upungufu wa vyumba vya madarasa 586 vyenye thamani ya shilingi milioni 687. Serikali iwe na mkakati maalum wa kujenga/kutatua kero hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushuru kwa kunipa nafasi hii, namshukuru Ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi; Mheshimiwa Mabula ambaye ni jirani yetu Kanda ya Ziwa. Tumshukuru Rais kwa kuwapa nafasi hiyo, mnafaa kupewa nafasi hiyo na Mungu awasaidie muweze kutongoza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nimeangalia taarifa hizi za Kamati ya Ardhi na Kambi Rasmi ya Upinzani wamesema vizuri sana. Wametofautiana kitu kimoja tu, hawa waCCM wameunga mkono, wale wa upinzani wameunga mkono kwa kushauri kwamba Serikali ikae pamoja itatue migogoro, jambo zuri sana.
Namshukuru rafiki yangu wa Bukoba Town na leo ni mnada, kwa hiyo, tutajua namna ya kufanya huko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye mambo muhimu na naomba niulize maswali ambayo natakiwa wakati unakuja hapa ku-wind up uweze kuyatolea ufafanuzi. Ni nani anapima mipaka kati ya vijiji na hifadhi za wanyamapori? Kama ni Wizara ya Ardhi inapima, inakuwaje mpaka huo buffer zone moja iwe na kilometa kadhaa na buffer zone nyingine au kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa binadamu ni nusu kilometa; lakini kutoka mpaka wa wananchi kwenda porini ni zero. Nani anapima mipaka hiyo na kwa upendeleo gani wa aina hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanapima wataalamu wa wanyamapori, kweli wanaweza kutenda haki? Mipaka ya Jimbo langu la Rubana, kwa Mto Rubana, ukiingia mtoni, ukivuka tu, umekamatwa. Ukivuka mto tu, umekematwa; lakini wao kutoka mpakani, mita 500 ambayo ni nusu kilometa. Kwa hiyo, ina maana mita 500 hizo kama kuna mazao yakiliwa na wanyamapori, hakuna kulipwa. Hakuna malipo! Hawa jamaa wamejiwekea sheria, unalipa kutoka kilometa moja mpaka kilometa tano ndiyo unalipwa na unalipwa kwa heka moja shilingi 100,000. Kwa hiyo, kama tembo amekula mazao heka 20, unalipwa heka tano, heka 15 ni sadaka ya Serikali. Nani alifanya maneno ya namna hii? Tunataka kujua nani anapima hii mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nani anatatua migogoro kati ya hifadhi ya wanyamapori na wananchi? Maana yake wamelalamika mika nenda-rudi, hakuna mtu anaenda. Tuna eneo moja linaitwa Kawanga; mpaka uchaguzi wa mwaka 1995 ulimtoa Waziri Mkuu, hiyo Kawanga. Aliuliza swali, nani atatatua mgogoro wa Kawanga? Akasema hii ni sheria, tutakwenda kufanya. Wakasema hapana, sisi tumeshachoka. Mpaka leo mgogoro upo, Mawaziri wameenda watano, sita, wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Mawaziri wengine mlioko humu ndani, hebu tuambieni, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Waziri wa Ardhi, wametamka humu Bungeni kwamba watakaa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii watatue migogoro ya wakulima, wafugaji na Hifadhi za Taifa, mtakaa mtatue. Uchaguzi tumetoka juzi! Mheshimiwa Rais wetu mtiifu amesema wafugaji sitawangusha. Tumetoka juzi tu, lakini operation zinaendelea kukamata watu. Hii maana yake nini hasa? Migogoro haijatatuliwa, watu wanakamatwa, watu wanatolewa; nani sasa amesema wewe uko sahihi kutoa watu? Tupo tu tunaangalia. Mheshimiwa Lukuvi, nafasi yako naitaka, ikifika miaka miwili na nusu miaka ijayo kama migogoro haijaisha angalau hata robo, wewe toka tu mimi niingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mgogoro wa Jimbo la Bunda, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameandika vizuri sana hapa. Mgogoro wa Bunda kati ya Wilaya tatu; kuna Serengeti, Bunda na Musoma Vijijini. Mgogoro wa mwaka 1941 mpaka leo haujaisha. Watu wanapigana, wanauana mgogoro upo tu. Mheshimiwa Mabula, wewe ulikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, unaujua mgogoro. Mara uko TAMISEMI, mara uko Ardhi, mara uko wapi, toka miaka hiyo mpaka leo. Mimi sitaunga mkono hoja hii kama kweli mgogoro huu hautaniambia unaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la Kyandege na wameliandika vizuri hapa. Sasa haya ni mambo ya ajabu. Wakati fulani hawa wenzetu wakisema maneno hapa, ingawaje sisi hatuna mpango wa kutoka madarakani, lakini wana maneno yao mazuri. Hivi inakuwaje? Kwa mfano, inakuwaje GN ya kijiji imetoka; na imetoka Makao Makuu ya Ardhi, imekwenda kijijini; imeandika mpaka kati ya kijiji ni kaskazini na kusini, lakini anayekwenda kukata mipaka kutoka Halmashauri au sijui kutoka wapi, anaenda anakata Magharibi Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamelalamika toka 2007 mpaka leo; eneo hilo tu moja, Muliyanchoka kweli hii? Hapana, hii hapana! Kwa hiyo, naomba kujua hili tatizo litaisha lini? Kwa kweli kusema kweli yapo mambo ya msingi ya kufanya, lakini vinginevyo nakushukuru sana unajitahidi kufanya. Tatizo tulilokuwa nalo, Waziri ulielewe na Mawaziri wote mlielewe, mnafanya kazi sana ya kutumikia watu lakini watumishi wenu wakati fulani wanasema ninyi wanasiasa tu. Watumishi wenu wanawaangusha sana ninyi. Kila ukisema maneno wanakwambia huyu ni mwanasiasa tu. Sasa muangalie, hao wanaosema wanasiasa waondoeni kwanza mbaki ninyi ambao mnafanya kazi. Nashukuru sana.
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda, kwa kunipa nafasi ya kuja hapa Bungeni na mimi nijumuike na wenzangu katika kuwatetea Watanzania wenye matatizo mengi. Nianze kwa migogoro ya moja kwa moja, migogoro ya wafugaji na hifadhi za wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa, lakini kwenye Jimbo langu la Bunda kuna eneo maarufu linaitwa Kawanga, na mimi niombe kwa kusema wazi tu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, ng‟ombe ana laana, toka mmetunga Sharia hii ya wanyama pori ya kukamata ng‟ombe mnamfanya kama nyara, mnamkamata porini hachungi na mnampiga risasi, Mawaziri zaidi ya tisa wamesha toka humu ndani; ng‟ombe ana laana. Kwa hiyo, yeyote anayeshughulika na ng‟ombe vibaya ajue mambo yake yatakwenda vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu eneo la Kawanga. Eneo hili mwaka 1974 alikuja Mwalimu Nyerere pale kama kijiji cha ujamaa, akawashauri wananchi wa maeneo yale kwamba jamani acheni maeneo ya malisho. Wakavuka Mto Lubana wakaacha eneo la Kawanga, wakawa wamechimba malambo mawili makubwa ya Chifu Makongoro, wananywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 ukaja ujanja ujanja eneo hili likachukuliwa kama game reserve, Ikolongo Game Reserve na Grumeti Game Reserve, pori la akiba.
Mheshimiwa Mwwenyekiti, kwanza huwa najiuliza hivi pori la akiba maana yake ni nini? Mwalimu alisema hivi vitu vya akiba viwepo pale ambapo wananchi wana shida wapewe nafasi.
Sasa inavyoonekana mapori ya akiba yote ni ya wanyama pori, ikija kwa binadamu nongwa. Leo ikitokea operation ya kuzuia tembo asiende kwenye mashamba ya watu na operation ya kwenda kuzuia ng‟ombe wasiende porini, operation ya ng‟ombe inachukua nafasi. Kwa sababu ng‟ombe wanakuwa na faida ukiwatoa kwenye operation unawakamata unawatoza, wanatoa hongo na mnawauza sijui hela za ng‟ombe zinazouzwa zinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Kawanga wakahama watu, mkalifanya Pori la Gruneti, malambo mawili yako upande ule, mpaka wetu ni mto, na mto ule maana yake ng‟ombe akivuka tu, amekamatwa ndivyo mpaka ulivyo. Lakini kutoka kwenye mpaka wa Mto Rubana kwenda kwenye watu, unatembea nusu kilometa kwenda pale mbele, ndiyo buffer zone yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza kama wananchi wa maeneo yale tembo wanakula mazao yao, ngo‟mbe hawavuki kwenye Mto Rubana, malambo yao mmechukua na hamkufidia halafu mnasemaje tuna mahusiano mabaya na ninyi? Profesa Maghembe mimi naomba nikuambie hivi, pengine kule Mwanga ninyi Ubunge wenu wakati fulani akisema fulani mnapata. Sisi Ubunge wetu ni wa kazi, kuna maeneo mengine Ubunge akisema mkubwa fulani watu wanapewa, lakini sisi Ubunge wetu mpaka utoe jasho ndipo upate. Sasa naomba uje Kawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugonvi na wewe, na mimi nikuambie wazi wala huna ugonvi na Wabunge, tatizo lako ni kwamba una-attack ng‟ombe, kwa nini una- attack ng‟ombe sisi tunaolea ng‟ombe. Mimi mke wangu ametoka ng‟ombe namuita Nyabulembo, sasa wewe una-attack ng‟ombe mara kwa mara kwa nini? Tunataka ng‟ombe kweli watoke porini sawa, lakini watoke kwa mpango maalum. Hivi kwa nini majangili wamewashinda porini mnang‟ang‟ana na ng‟ombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa kwenye ripoti ya wapinzani hapa, anasema kwamba ujangili ni mfupa uliowashinda CCM. Na kila siku asubuhi, hata leo asubuhi nimesikia, kwamba kiongozi mmoja mhifadhi wa wanyama pori sijui amekamatwa na pembe za ndovu. Sasa kwa nini msishughulike na hawa mnashughulika na ng‟ombe? Profesa achana na mambo ya ng‟ombe watakulaani hapa. Naomba uje Kawanga uangalie mpaka ulivyo ni mbovu. Lakini ndugu zangu Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya wafugaji, naomba niwaambie wazi, hizi kanuni na sheria za wanyama pori zitaua watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zitaua humu ndani, sheria hii imeandika ng‟ombe ni kama nyara, akikamatwa anapelekwa mahakamani, akionekana ameingia porini auzwe. Ng‟ombe wa Usukumani, ng‟ombe wa Jimbo la Bunda, ng‟ombe wa Tarime na maeneo mengine ana tofauti gani na ng‟ombe wa Ngorongoro? Ng‟ombe wa Ngorongoro anachunga na wanyama, kwani ile sheria ya Ngorongoro imekuwa ni sheria ya Mungu haibadiliki? Sheria ya Ngorongoro ambayo ng‟ombe wanachunga na wanyama haibadiliki imekuwa ni sheria ya Mungu? It’s too rigid haiwezi kubadilika. Tuone maeneo mengine ambayo yanahitaji uhitaji wa Ngorongoro wapelekewe hiyo sheria. Profesa nakuomba uje Bunda, uangalie eneo la Kawanga tuone ni namna gani tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo. Nakupongeza kwa maana ya kwamba msimu mdogo uliopita umenisaidia sana, tembo kidogo, watu wamevuna. Lakini ndugu zangu Wabunge na ndugu zangu Watanzania, mnyama tembo, mama mmoja tulienda kwenye mkutano akatuuliza hivi, hivi hao tembo hawana uzazi wa mpango? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana kama wamezidi tuwafanyie uzazi wa mpango, tembo siku hizi wanakwenda kwenye maghala, wanaangusha maghala wanakula mazao. Maeneo ya Bunda, Unyari, Kiumbu, Mariwanda na kwa Mheshimiwa Ester Bulaya pale Bukore na Mihale wanakula mazao asubuhi na mchana na Profesa upo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipiga kelele hapa mnasema tumekuwa wabaya, watu hawa wanaozunguka wanyama pori hawa, mazao yao yanaliwa fidia haipo. Tunadai fidia zaidi ya milioni 400 hamjalipa kutoka mwaka 2012 mpaka leo, na wanakula mazao kila siku na magari mnayo, watu mnao, mkiambiwa mnasema kwamba Halmashauri ndiyo ilinde wale wanyama. Halmashauri ina askari pori mmoja na gari bovu halipo na Halmashauri hazina own source. Halmashauri hazina hela unawaambia walinde tembo watalinda saa ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mbaya zaidi Halmashauri alinde tembo, asipolinda tembo anakula mazao, wakila mazao mnalipa nyie hivi kwa nini mpo hasara sasa? Kwa hiyo nilikuwa nafikiri kwamba ni vizuri ukaangalia. Lakini mambo mengine niseme mapambano ya kuzuia ujangili yaendelee kuwepo, kuimalisha misitu yetu muendelee kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze kidogo juu ya TFS. Hao TFS ulionao nikushukuru kwanza umewashughulikia, ni jipu. Haiwezekani kwenye makusanyo yao, kila mwaka asilimia 100, asilimia 200, asilimia 150 uliona wapi? Yaani kila makusanyo ya TFS asilimia 100, asilimia 250, asilimia 300 uliona wapi? Angalieni makusanyo yao asilimia walizokusanya kila mwaka, asilimia 120, asilimia 110, asilimia116 kila mwaka, wao makadirio yao yanakuwaje mpaka wapate hizo asilimia? Kwa hiyo, mliangalie hili nalo hao watu inawezekana wakawa jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya shilingi milioni 400 watu wa Bunda unawalipa lini? Hii fidia sijaiona kwenye bajeti yako. Profesa ukija hapa uniambie kwamba hii kitu unalipa lini. Lakini naomba kuanzia leo na kwenda muda unaokwisha, kwa muda wa mwezi mmoja na nusu naomba mtusaidie kupata magari ili watu wale wapate mavuno yao. Wamebakiza mwezi mmoja tu, tembo leo wanaenda usiku na mchana na kama hamuwezi, Profesa ngoja nikuambie, Marekani ni wanjanja sana lakini wanaishi na Mexico. Waliona haiwezekani kuishi na Mexico maskini na wao wakiwa matajiri, ikabidi wawafadhili wao wapate hela. Hamuwezi mkafanya wananchi wanaozunguka maeneo ya pori, mkasema eti mtakuwa marafiki wakati ninyi mnawanyonya haiwekani, lazima muwafadhili ili waweze kuishi na wanyama vizuri. Na ninyi niwaambie huku Serikalini… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia uhaba wa chakula. Kwanza niwashukuru watoa hoja wote, Kamati ya Ardhi na Kamati ya Kilimo, wamezungumza vizuri kwenye vitabu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua tu kwa Mawaziri wanaohusika na Wizara hizi au wa Serikali sijawahi kuona kwamba kwa nini kila siku tunazungumza hivi vitu vinavyohusu mifugo, vinavyohusu ardhi kutopimwa na sina hakika kwamba hivi muda huu toka Wabunge wamekuja toka mwaka 1961, haya mambo ya kupima ardhi yalikuwa hayajazungumzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba kwa Wabunge wenzangu mkitaka Bunge hili tulitendee haki tuondoeni maneno yanayohusu U-CHADEMA na U-CCM. Mkiondoa haya maneno haya mtajenga Bunge ambalo ni imara na litasimamia Serikali. Tukifika humu tumebaki kubishana tu, tunabishana upande huu mara mwingine azushie Magufuli maneno, mara sijui Rais amefanya nini hatutafika hiyo. Tuzungumze mambo yanayohusu wananchi tuwaulize Serikali kwa nini kila siku tunazungumza migogoro ya mifugo na haitatuliki. Kama hakuna majibu tuseme sasa itakuaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila siku tunakuja hapa maneno tu kama ngonjera tu, tukubaliane kwamba kama sisi ni wasimamizi wa Serikali, tuiulize Serikali kwa nini sasa mipango hii ya ardhi ambayo wakulima na wafugaji wanauana, kwa nini haifiki mwisho? Tutapata majibu siku hiyo. Kama haifiki mwisho hatuendi kwenye bajeti, tutapata majibu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kwenye eneo langu la Bunda. Amekuja Waziri Mhagama, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ndugu yangu hapa Ramo Makani, amekuja Naibu Waziri Kilimo, Mheshimiwa Ole-Nasha wamejionea hali halisi ya uharibufu ya wanyama tembo katika maeneo yangu, kata saba na Bunda Mjini. Wameona hali ilivyo, ikaahidiwa kwamba watapeleka chakula hakijaenda. Sasa nimeona humu wanaandika tupeleke mbegu bora, unaipanda wapi? Unapanda mbegu bora lakini tembo anaishi pale kila siku, wale Wazanzibar wanaita ndovu, anaishi pale pale kwenye shamba, tunapeleka mbegu bora ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hao tembo au ndovu hawawezi kutoka kwenye Jimbo lile watu watalima lini? Nawashukuru siku hizi wanajitahidi wapeleke na magari, lakini tembo au ndovu zimewashinda kutoa. Wanaishi pale pale kila siku, wamepeleka tochi imeshindikana. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri Serikali ituambie kama mpango wa eneo langu, vijiji vya Unyali, Maliwanda, Kihumbu, Nyamang’unta, Tingirima, Mgeta na kule kwa neighbour wangu Mheshimiwa Ester Bulaya, vijiji vya Nyamatoke na Mihale, watuambie kama maeneo haya hayawezi kulimwa basi Serikali ijiandae kwenda kuwapa chakula cha bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo sasa hivi wamefika wakati sasa wanavunja maghala, wanachukua chakula wanakula, hawana uwezo sasa wakulima pale, ngombe hawaendi porini wanakamatwa, sasa tunafanyaje? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika hili kuwa wepesi wa kupeleka chakula cha msaada au chakula cha bei nafuu wapeleke katika Kata Saba za Jimbo langu. Hali ni mbaya na Kata Tatu za Jimbo la Bunda Mjini. Hali ni mbaya sana kwenye maeneo haya, njaa ni shida.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimpa rafiki yangu, jirani yangu anaitwa Ryoba dakika tano uwe unanichunga kama zikizidi itakuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo, niseme tu kitu kimoja…
MWENYEKITI: Mheshimiwa zimekwisha dakika tano zako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yangu yote ya Ofisini kwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu yazingatiwe.
(i) Kukasimu barabara ya Mugeta – Misingo – Mekomariro (Bunda) hadi Sirorisimba (Butiama) na Serengeti.
(ii) Kutangaza mkandarasi wa barabara ya Nyamuswa – Bunda (ahadi ya Mheshimiwa Waziri 31/12/2016) aliposimama Kata ya Nyamuswa na kuahidi kutangaza mkandarasi ifikapo Februari, 2017.
(iii) Kutangaza mkandarasi kipande cha Sanzate hadi Nata. Nasikitika kuona kipande hiki kimerukwa badala yake Wizara ilitangaza barabara ya Nata. Kwangu naona kama sikutendewa haki na hasa ikizingatiwa hii Lot ilitakiwa kwisha kabla ya kutangaza huku. Naomba haki itendeke.
(iv) Uwanja wa Ndege Musoma, Mheshimiwa Waziri alishasema anatafuta shilingi bilioni 10 za ukarabati wa uwanja huu mapema 2016/2017. Nasikitika kuona bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni tatu badala ya shilingi bilioni 10. Naomba suala hili lizingatiwe.
(v) Reli ya Arusha – Musoma. Reli hii toka mwaka 1975 inapewa ahadi hadi leo. Tunaomba kwa miaka mitano watu wa Musoma waone jitihada ya Serikali katika kujenga reli hii.
(vi) Bandari ya Musoma ilikuwa ikipokea meli ya MV Victoria, MV Butiama na MV Umoja. Nimeona juhudi za Wizara za kutengeneza meli hizo, tunaomba meli hizo zikitengenezwa zifike Musoma. Matengenezo ya Bandari ni kidogo sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwnyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru Waziri na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niendelee kutoa pongezi kwa Jemedari wetu, Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya, sina mashaka na yeye. Wasiwasi wangu ni kwamba akimaliza miaka yake kumi atakuja mtu mzuri kama yeye au vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Hospitali ya Mkoa wa Mara. Sijajua kwa Mkoa wetu wa Mara ni kitu gani kinatokea kwa sababu vitu vingi haviendi vizuri. Hospitali hii imechangiwa karibu miaka 32 na haijaisha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kongwa, imekuwa ikitengewa fedha kidogo kila mwaka na mpaka leo haijulikani itaisha lini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleza kwa mwaka huu wa fedha imetengewa kiasi gani na ni lini hospitali inaweza kwisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, nadhani ukurasa wa 149, anazungumzia habari ya kupeleka fedha za vijana na akina mama katika vikundi. Katika Wilaya ya Bunda wameandika kwamba imepeleka shilingi milioni 106, nikashangaa! Sasa nataka kujiuliza haya maandishi humu ni ya kweli au mtu ameyabandika tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nimempigia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kumuuliza hii hela mmepeleka ninyi? Anasema sisi tumepeleka shilingi milioni 20 tu. Maana Bunda yenyewe kukusanya shilingi milioni 100 ni kesi. Sasa nataka kujiuliza hizi fedha zimetoka Wizarani za muda mrefu au za namna gani? Kwa hiyo, kama ni za Wizarani ni sawa lakini kama ni za kutoka kwenye Halmashauri na ni own source, hizi fedha hazijatoka. Kwa hiyo, nataka kuuliza suala hili limekaaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nizungumzie habari ya watumishi katika Jimbo langu la Bunda. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ametembelea katika Jimbo langu la Bunda ameona katika kila kituo nurse ni mmoja-mmoja tena wale wa daraja la chini na akaahidi mtakapopata nafasi mtatuletea watumishi katika Jimbo la Bunda. Zahanati zote zina nurse mmoja-mmoja na Naibu Waziri ameshuhudia mwenyewe. Kwa hiyo, naomba katika nafasi zitakazopatikana mnisaidie kupata watumishi wa maeneo hayo. (Makofi)

Lakini pia mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii. Tumetembelea Muhimbili, Ocean Road na maeneo mengine mengi, fedha haziendi kwenye vituo vyote vikuu. Tunaiomba Serikali katika bajeti inazotenga fedha ziende kwenye maeneo muhimu ambayo imezitengea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona Mloganzila, tumeambiwa kile Kituo cha Ufundishaji cha Tiba kimeisha lakini hakina watumishi. Kinahitaji fedha kiasi cha shilingi bilioni nne ili kianze kazi. Tunaomba Serikali ipeleke pale madaktari na kituo kile kiweze kuanza kazi mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa iko hapa, tunaomba watumishi waende maeneo hayo ili waweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna Hospitali ya Nyamuswa, ni kituo ambacho tumekijenga kiko kwenye hali nzuri. Tunaomba pale mtakapopata x-ray na nimesikia Waziri anasema mtapata x-ray basi mtupelekee kwenye Kituo cya Nyamuswa ili watu waweze kupata huduma katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika haya mambo ya vijana mimi nadhani sasa kuwepo na mkakati maalum kupitia hii Wizara na Wizara ya Kazi tujue sasa hizi fedha za taasisi za kijamii zinazoenda kwa ajili ya kuwakopesha akina mama na vijana zina mfumo mzuri ambao unaeleweka. Maana inaonekana kwamba kuna maeneo mengine yanapata fedha kutoka makao makuu na wengine wanapata kutoka own source sasa haijulikani ni wapi wanapata manufaa. Nashauri tuweke mfuko mmoja wa hizi fedha zijulikane kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanyama waharibifu. Serikali iwe na mikakati ya wazi katika kuzuia wanyama waharibifu katika Vijiji vya Hunyari, Kisambu Nyangere, Mariwanda, Sarakwa, Mugeta Kyandege na Tingirima. Maeneo haya kwa muda mrefu yameathirika sana kwa wanyama kula mazao yao ya chakula na biashara toka msimu wa 2011/2012 hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya kifuta jasho. Tunaomba Serikali kulipa fidia ya kifuta jasho na kifuta machozi zaidi ya shilingi milioni 360 zinadaiwa na wakulima wa Vijiji vya Nyangere, Mariwanda, Kihumbu, Sarakwa, Tingirima, Mugeta na Sarakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msaada wa kumalizia majengo matatu ya zahanati, kuna maeneo yaliyo mbali na huduma za afya, wakazi wa vijiji husika wamejenga zahanati ili kusaidia kupata huduma za afya. Majengo matatu yameezekwa bado samani, lipu, floor, nyumba ya Mganga katika Vijiji vya Tiring’ati, Kambubu na Mihingo. Tunaomba Serikali kusaidia vijiji hivi ambavyo vipo mbali na huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji katika Jimbo langu kuna uhaba mkubwa wa maji ya binadamu na mifugo na hapa ieleweke kuwa katika vyanzo vya maji katika Jimbo langu maji ya malambo na mabwawa ndio maji ya binadamu na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kukarabati malambo ya zamani ya Kyandege, Mugeta, Tingirima, Nyang’aranga, Manchim, Wero, Mahanga, Salama A, Sarzate, Rakanaa, Mihingo, Mekomariro (Malambo mawili) na Sarakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malambo haya yalipangwa kuchimbwa sana budget ya 2016/2017 hadi leo hakuna dalili, Mheshimiwa Waziri wa Maji aliahidi humu Bungeni, Bunge la Mwezi wa Pili, 2018 na kwamba Bunda imetengewa bilioni moja kwa kazi hiyo. Malambo yanatumika zaidi kwa maji ya binadamu kwa visima kukauka kila kiangazi. Suala la Malambo katika Jimbo langu yana umuhimu zaidi kuliko visima, maana visima hukauka kila kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Kitengo cha SENEPA wamekubali kutoa vifaa na ufundi kusaidia kukarabati malambo haya, tunaomba Serikali ikubali kusaidiana na Wizara ya Maji kukarabati malambo haya yaliyochimbwa miaka ya 60 lakini ni chanzo cha uhakika cha maji katika jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kabla sijatoa hoja yangu ya kuunga mkono niwape pole wakazi wa Jimbo langu la Bunda kwa taabu kubwa waliyonayo ya upungufu mkubwa wa chakula na niwahakikishie kwamba Serikali kwa maelekezo yake hivi karibuni inaweza kuwasaidia kupunguza tatizo walilonalo.

Suala la pili, niwape pole wanavijiji wa barabara ya Bukama, Salamakati, Mihingo na Mgeta ambayo imevunjika daraja zake kwasababu ya mvua na mkandarasi wiki ijayo au wiki mbili zijazo atakuwa kwenye site, kwa hiyo wategemee watapata huduma, kwamba Serikali inawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu kwamba humu ndani pamoja na kwamba tupo Wabunge wengine wa miaka mingi lakini pia kuna wazee humu ndani, hili suala la bajeti ya maji tumelisema sana, watu wameonyesha njia, lakini iko hoja ya msingi kwamba sasa litakwenda kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itakaa na kulitazama upya. Sasa kama hiyo ndiyo hoja basi hakuna haja ya kulipinga ni kuliunga mkono tu kwamba pengine katika ongezeko litakalokuja litatusaidia kufanya mambo.

Kwa hiyo, mimi nitaiunga mkono hii bajeti mkono kwa sababu itakwenda na itarudisha majibu ambayo yataleta neema. Mambo mengine haya ya kuota kwamba CCM itakufa lini, unaweza ukakaa miaka mingi tu hujapata jambo hilo kwa sababu CCM pia ni nembo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jimbo langu la Bunda. Haihitaji kusoma sana kujua kwmana asilimia 72.6 ya huduma ya maji inayopatikana vijijini haihitaji kwenda darasa la saba wala la ngapi. Hivi kwa mfano, kama asilimia 72.6 ndiyo huduma ya maji vijijini, kwa lugha nyingine ni kwamba kama una watu milioni moja maana yake watu 726,000 wanapata maji vijijini. Yaani kama tuna vijiji 1,000 ina maana vijiji 726 tu vinapata maji sasa jamani hivi ni kweli? Maana yake ni kwamba vijiji 274 ndivyo havipati huduma ya maji. Hivi Waziri, wazee wangu hawa mmetoka sijui engineer sijui nini inahitaji hilo kutuuliza? Hivi takwimu hizi tunazipata wapi? Waheshimiwa Wabunge sisi wote tuko humu ndani, kwanini usituambie kila Mbunge atuletee vijiji vyenye huduma ya maji na wewe ukaviona kwenye asilimia? Msikariri bajeti hizi kwa mambo ya kukariri kwenye vitabu jamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wangu nyie ndiyo mnamalizia hivi, mkishatoka hapa na uwaziri unaacha. Kwa hiyo naomba mjikite kutusaidia sisi. Mbona Waziri wa Nishati na Madini ametuambia leteni vijiji ambavyo havina umeme, tumempa na ameviona vijiji vinaonekana, ninyi kwa nini hamfanyi hivyo? Mnakariri bajeti sio wataalam? Mimi ninawaambia kumekucha hali si nzuri sana. Kwenye Jimbo la Bunda amezungumza mwenzangu hapo, lakini niseme tu nimeandika barua tarehe 26/10/2016, utata wa miradi ya Jimbo la Bunda nikataja mradi wa maji Mgeta-Nyangaranga. Nashukuru kwa sasa hivi mkandarasi yupo lakini bado anasuasua tu, anaweka leo bomba moja kesho haweki, hakuna kinachoendelea pale, mradi una miaka sita unahangaika tu, haiendi vizuri. Barua hii haikujibiwa; hata sikujibiwa mimi kama Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupewa nilichoandika jamani ni sawa? Mheshjimiwa Waziri nimekuja kwako, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuja kwako, kwa Katibu nimeenda, sasa mnataka tuende wapi? Wazee wangu mnataka tuende wapi tuseme? Mradi wa Maji Mgeta matatizo, Mradi wa Nyamswa Salama Kati mmetenga shilingi 367,291,127, wanasema mradi umetengenezwa kwa asilimia 55 umekufa una miaka mitatu; mnataka twende wapi? Nimezungumza mkasema mtarekebisha miradi ya zamani iendelee, lakini hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi wa Kilolei shilingi milioni 400, vijiji vya Nyabuzume, Kiloleni na Kambugu shilingi milioni 400, ile mnasema visima kumi. Nimewaambia ofisini hakuna kinachoendelea, mnasema tuseme nini sasa kwenye hili? Ameandika Mhandisi wa Wilaya ya Bunda tarehe 1 Juni, 2016 miradi ya viporo vya madeni ya wakandarasi wa mradi wa maji Wilaya ya Bunda; mmeleta shilingi bilioni tano. Miradi karibu asilimia sabini na kitu asilimia haifanyi kazi, ninyi mkija kwenye asilimia hapa mnaandika maji yanapatikana Bunda, hayapo, hayapo Bunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu wamekuja watu wa JICA tumewapa taabu kubwa sana, tumewaambia watusaidie kwa sababu kwenye Jimbo langu la Bunda lina ukame mkubwa, wametuambia tufanye bajeti tumewapelekea bajeti ya dola 63,879 ya ukarabati ya marambo yaliyoingiliwa na magugu maji.

Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mliwahi kujibu hapa Bungeni kwamba mwaka huu mtafanya ukarabati wa malambo sita, iko wapi mzee wangu? Sasa mnafikiria sisi Wabunge tufanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, JICA hawa hawa wamesema tutengeneze malambo, tumewapa bajeti ya dola 255,237.17 tusaidieni basi, tusaidieni kwenye JICA hawa ambao wametuona kwenye tatizo mtusaidie kutusemea watusaidie. Jimbo la Bunda lina ukame wa kutisha, Jimbo hilo hilo ndio lina tembo wanaokula mazao ya watu kila siku, lina watu wana taabu zao kule; tunaomba mtusaidie kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mradi wa umwagiliaji Bunda. Mradi wa umwagiliaji maji wa Nyatwali hauko Jimbo la Bunda, haupo Wilaya ya Bunda uko Bunda Mjini. Bunda DC kuna mradi wa umwagiliaji wa Maji unaoitwa Mariwanda pamoja na mradi wa Kasugutwa wa Buramba, haiku kwenye bajeti yanu; na kwenye takwimu zenu mnaonesha kwamba Mradi upo Bunda DC lakini upo Bunda Mjini. Kwa hiyo, naomba mlirekebishe hili na mradi wetu wa Mariwanda muufanyike kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hebu tusaidieni, kama mmepewa hiyo Wizara na hali ndio hii inaenda miaka miwili sasa inaenda miaka mitatu na ninyi wazee ma-engineer mpo hapo, watu wazima ambao tunawategemea mtusaidie na hamna plan mpya ya kukomboa mambo ya maji, tunakaa na ninyi humu kufanya biashara gani? Maana sasa lazima tuwaambie kwamba miaka mitatu ijayo mtuambie mmeingia humu ndani mmekomboa nini au ndiyo zile asilimia mnazoimba tu asilimia 72 wakati hazipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimeandika kwenu, nimewaleta, kwenye Jimbo langu mnasema kwamba miradi ya zamani iendelee kuwepo; na kwangu miradi ya zamani ipo, endeleeni kunisadia au mnampango wa kuniondoa huko ndani? Mniambie sasa mapema nijue.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo na watendaji wote wakiongozwa na Katibu, Mkuu Meja Jenerali Milanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa nchi yetu kwa kuwateua hawa lakini kwa kulinda maliasili ya nchi yetu na kuonesha kwamba ana nia nzuri ya kuendeleza utalii kwa kununua ndege ambazo zitakuwa zinatoa watalii maeneo mbalimbali na kuwaleta hapa kwa ajili ya kuongeza mapato ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze leo kwa kutumia hotuba zote hizi mbili ya Waziri na Kamati, yote ambayo tulitegemea kusema humu ndani hasa mimi naona wamezungumzia maeneo mengi. Nianze kwa kuangalia kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 17, ibara 36 wanasema:-
“Dhana ya ushirikishwaji jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanashiriki katika uhifadhi na kunufaika kwa mujibu wa Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maeneo yangu ya Bunda na kwa bahati mbaya lugha inakuwa tofauti nikisema tembo inakuwa kosa basi niseme ndovu. Nimshukuru Waziri katika msimu wa kilimo wa mwaka jana na mwaka huu wametusaidia kuleta magari na askari ili kuzuia ndovu wasije kwenye maeneo ya makazi ya watu na kula mazao yao. Nina ombi maalum kwa Waziri kwamba kwa sasa wakulima wale wamelima sana na mazao yao yako kwenye hatua nzuri, kwa mwezi wa Tano, Sita na Saba watusaidie kupeleka magari na askari wa wanyamapori ili wananchi waweze kuvuna kwa msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu hiki cha hotuba ukurasa wa 19, ibara ya 39 inasema, jumla ya shilingi milioni 567.5 zimelipwa kwa wananchi ambapo shilingi milioni 504 ni kifuta jasho. Miongoni mwa Wilaya zilizolipwa hizo hela ni Bunda, nikushukuru Waziri kwa sababu amewakumbuka watu wa Bunda kwa Vijiji vya Unyari na Kiumbu. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Kijiji cha Maliwanda ambacho kimeathiriwa sana na wanyamapori lakini kwa bahati mbaya katika malipo haya hawakupata na Kijiji cha Sarakwa. Nilishaenda Ofisi kwao wakaniahidi kwamba watafanya marekebisho na hawa watu watapata malipo yao ya kifuta jasho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo nizungumzie hili la kifuta jasho. Mwaka jana katika hotuba hii ya bajeti tumezungumzia marekebisho ya kanuni za wanyamapori kuhusu kifuta jasho. Wanasema kutoka kwenye mpaka, mpaka kwenye eneo ambalo ni kilomita tano kutoka kwenye mpaka ambao wananchi na wanyamapori wanaishi, mwananchi atakayeliwa mazao yake zaidi ya kilomita tano analipwa shilingi laki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuseme ndovu amekula mazao kilomita arobaini kutoka eneo la mpaka analipwa shilingi laki moja kwa heka moja. Iko sheria pale kwamba kama umelima heka arobani halafu ndovu wamekuja kwenye shamba lako wamekula heka arobaini unalipwa heka tano tu kwa shilingi laki moja. Kwa lugha nyingine unalipwa shilingi laki tano, kwa heka 40 unalipwa heka tano tu heka 35 inakuwa sadaka. Sasa ni vizuri tukaangalia namna gani ya kurekebisha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye kitabu hiki namna gani watu wanaozunguka wanyamapori wananufaikana nao. Katika eneo langu la Unyari miaka mitatu iliyopita ndovu walivunja jengo la watoto na akina mama wajawazito. Tukajitahidi kujenga jengo hilo na Serikali ikaahidi kwamba itaezeka na kufanya finishing. Niishukuru Wizara imetoa shilingi milioni 50 jengo lile linaendelea vizuri lakini alipokuja Waziri wa Afya amesema jengo lile kwa sababu tumelijenga vizuri liwe kituo cha afya. Kwa sababu ya sera yetu, nafikiri Mheshimiwa Waziri ni vizuri sasa akatusaidia hela nyingine kwa sababu inahitajika pale shilingi milioni 50 nyingine ili kubadilisha maeneo yale yote yawe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba tutasaidiana katika jengo hili ili kiwe kituo cha afya na ikiwezekana hata kama litaitwa Profesa Maghembe siyo mbaya ili mradi tu umetutengenezea eneo limekuwa zuri zaidi kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya mipaka kati ya vijiji kumi na tano na Pori la Akiba la Grumeti. Mgogoro huu ni wa muda mrefu, tumesema sana na tunafikiri ile Kamati iliyoundwa ya Wizara tatu itafika kwenye eneo letu na kuweza kuangalia mipaka hii. Ipo hoja kwamba mwaka 1994 wakati eneo hilo linachukuliwa kutoka open area kuwa game reserve (pori la akiba), wananchi hawakushirikishwa. Kwa hiyo, tunafikiri kuwa sasa ni muda muafaka kuangalia mipaka hiyo na Kamati imesema ili tuweze kujua ukweli uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba wakati hilo pori la akiba linachukuliwa ambalo maarufu kule kwenye maeneo yangu kama Kawanga kulikuwepo na malambo mawili yaliyochimbwa na wananchi kwa ajili ya kunywesha mifugo. Yale malambo mawili sasa wanyamapori ndiyo wanakunywa maji lakini sisi huku chini hatuna maji ya kunywa. Mheshimiwa Waziri anajua mpaka wetu ni Mto Rubana, sasa watu wakienda katika maji yale wanafukuzwa kwa sababu wakivuka Mto Rubana tu wameenda porini. Kwa hiyo, tulifikiri ni muhimu sana Serikali kuja kuangalia namna ya kuchimba malambo upande wa pili ili ng’ombe wawe wanapata maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kero ya mipaka ambayo ni ya muda mrefu lakini kuna vijiji vya Mgeta, Tingirima, Kandege na vyenyewe havikupata huu mgao wa kifuta jasho. Ni vizuri sasa tukaona ni namna gani wanaweza kuzingatiwa, lakini Maliwanda ni kijiji cha kwanza kuzingatiwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka nichangie hayo, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia. Kwanza nawashukuru Wenyeviti wa Kamati, Mawaziri wote wa Wizara hizi tatu na Watendaji wao na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanatufanyia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia nijielekeze kwenye Wizara ya Nishati. Wizara ya Nishati kuna maeneo mawili; kuna eneo la Densification na eneo la REA III, lakini yote inatoka kwenye REA. Kasi ya utendaji kazi wa Wakandarasi katika Jimbo la Bunda kwa upande wa densification ni mdogo sana, ninavyozungumza hapa, wako site lakini wanaenda pole pole sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, REA katika vijiji, kasi yake nayo imekuwa ndogo ingawa Mheshimiwa Waziri anafanya kazi kubwa sana ya kuanzisha hii miradi katika maeneo mbalimbali. Nami wakati fulani namhurumia, anatembea sana, lakini Wakandarasi wanaenda slow sana. Sasa, sijui ni upungufu wa hela au ni nini, sielewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri sasa awahimize hawa Wakandarasi katika maeneo na hasa Wilaya ya Bunda, hususan Jimbo la Bunda katika maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri alikuja akafanya uzinduzi wa Mradi wa REA III katika eneo la Maiwanda katika Jimbo la Bunda. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri Mheshimiwa Waziri akahimiza wakaja kwenye kutenda hiyo kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika REA kuna mambo huwa siyaelewi vizuri. Moja, ni kitu kinaitwa kilometa. Unakuta kuna upungufu kati ya watu wa survey ya TANESCO na survey ya Mkandarasi, TANESCO ukiwauliza, nani amefanya survey ya kumpa Mkandarasi aende kujua Kijiji ‘A’ kila kilometa tatu, kina kilometa moja na Kijiji ‘B’ kinawekewa transfoma mbili na Kijiji ‘A’ kinapewa transfoma tatu au kilometa mbili. Sasa ukiuliza TANESCO, wanasema ni REA; ukiuliza REA, wanakuja na takwimu, hawahusishi wanakijiji wale kujua toka mwanzo kwamba kijiji hiki kitapata kilometa mbili au mtandao wa umeme wa kilometa mbili na transfoma tatu na voti ngapi katika hiyo transfoma. Kwa hiyo, hilo nalo ni tatizo liko hapa, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie vizuri ili tuweze kwenda vizuri katika suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Wizara ya Miundombinu. Kuna masuala ya barabara ya lami kutoka Nyamswa kwenda Bunda na kutoka Bunda kwenda Bramba na Bramba kwenda Kisorya, imechukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri anayehusika aweze kuiangalia kwa makini zaidi kwenye hiyo barabara. Kuna barabara ambayo inatoka Sanzati kwenda Mgeta na Mgeta kwenda Nata, nayo tunaomba Mheshimiwa Waziri anayehusika aweze kuiangalia vizuri hiyo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema mambo yafuatayo:-

Kwanza, ni kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Mkoa wa Mara. Sisi Mara hatuna upungufu wa kupata Rais, tumewahi kupata Rais miaka 24, kwa hiyo, hatuwezi kulalamika kwamba Rais amefanya nini kwa miaka miwili iliyokuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kwenda India kumshuhudia mtu anafanyiwa operesheni; kuna operesheni ndogo na kubwa. Operesheni kubwa ni zile zinazohusisha matumbo kwa ndani; unatoa labda figo na vitu vingine. Mtu yeyote atakayekatwa kisu kwa operesheni kubwa lazima agune na lazima arushe miguu. Kwa hiyo, ninachoona wenzangu hapa wanarusharusha miguu, naona kama operesheni ya Mheshimwia Dkt. Magufuli imewafikia. Kwa hiyo, sioni matatizo ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo yote anayoyafanya. Kwanza, ni kutupa Mkoa wa Mara shilingi bilioni 10 za uwanja wa ndege. Kwa mara ya kwanza Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwa madarakani, juzi Waziri Mkuu ametua pale na ndege kubwa. Sasa tunamlaumuje kwa mambo haya? Tunapozungumza, site watu wanaendelea na kazi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Mkoa wa Mara shilingi bilioni nne kwa ajili ya Hospitali ya Kongwa ambayo imekuwepo toka mwaka 1975. Inaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Niabu Spika, kwa hiyo, sisi Mara tunamlaumu kwenye jambo gani? Kwa hiyo, mambo mengine yapo, yanaendelea. Naona watu wanarusha miguu tu, lakini hali ya hewa ni nzuri. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais pia kwa kudhibiti rushwa, kuweka nidhamu ya kazini, kudhibiti wazembe na wala rushwa, kutoa elimu bure, kuanzisha miradi mikubwa ya Stigler’s Gorge na miradi mingine inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunachokiona hapa ni kitu kimoja; wenzetu wameshaona Messi wa CCM ni Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Kwa hiyo, ni lazima mshikeshike miguu. Wana-CCM lazima tukae tayari kumlinda Messi wetu asiumizwe, asilete madhara katika mambo hayo. Kwa hiyo, nafikiri kwamba haya ni mambo ya msingi ya kufanya, lakini naomba Wizara zinazohusika ziangalie Jimbo la Bunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze tu kwa kuwashukuru na niseme tu kwamba Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wanafanya vizuri. Nimefuatilia mambo mengi wanayoyafanya na nchi nyingi zinazofanya mambo ya barabara, wanafanya vizuri sana, tunatakiwa kuwashukuru sana. Tumpongeze Waziri Mbarawa, Katibu wake, Naibu Waziri na wote wanaohusika na Wizara hii kwa kweli wanafanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nianze tu na barabara za Mkoa wa Mara na niseme wakati fulani huwa najiuliza sijui kwa sababu mtangulizi wa Taifa hili alitoka Mkoa wa Mara na kwa sababu alikuwa anajumuisha Taifa hili kwa kuliona kama mtoto wa nyumbani kwake na akahusika kufanya maendeleo kwa kila eneo la nchi hii, lakini sasa Mkoa wa Mara kwa maeneo mengi hayaendi vizuri kwa kweli. Ukitazama barabara zetu barabara ya Nyamswa - Bunda tumeahidiwa toka mwaka juzi na iliwekewa shilingi bilioni nane mpaka leo iko kwenye utafiti tu hakuna kinachoendelea hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Buramba inatengenezwa haiendi, barabra ya Makutano - Sanzati haiendi, barabara ya Sanzati - Makutano - Mugumu haiendi, reli ya Arusha - Tanga - Musoma haiendi na Uwanja wa Ndege Musoma hauendi. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli Mheshimiwa Waziri uutakapokuja hapa uje na majibu kamili kwamba hizi barabara tulizozitaja hapa zinakwenda vizuri na unaandaa namna gani unaweza kusaidia vinginevyo tunaweza kung’anga’ania shilingi yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mawasiliano, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuzungumzia masuala ya mawasiliano, niliomba kata tano, kwa maaa ya mawasiliano, nimepata kata moja kwa mtandao wa Halotel. Kuna vijiji vya Nyangere, Tingirima, Nyabuzume, Marambeka, Nyagurundu vyote havina mawasiliano. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri mnapokuja hapa muone ni namna gani ya kutusaidia, na ndugu yangu Nditiye uko hapo nadhani utanisaidia katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema mambo mengine madogo madogo haya lakini ni makubwa kwangu, nashangaa kuona vitu vingi vinazungumzwa hapa, sijui kuna shilingi trilioni 1.5, kuna ngapi, lakini sisi ambao tumeingia humu bado ni wageni kwenye Bunge hili tunajua utaratibu wa CAG unafuata kanuni ya kwenda kwenye Kamati ya PAC ambayo ndiyo inaita watu wote wanaohusika na ile mijadala kule ndani na kuona kile kinachohusika na kama uthibitisho utakuwa haupo ndipo tunajua kwamba hizi hela zimepotea au hazijapotea. Sasa naona watu hapa mishipa imewatoka, trilioni zimepotea, wapi sasa? Nani amekwenda kuthibitisha kwamba hela zimepotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika report ya CAG tumeona mengi, tumeona kuna vyama hapa vimepoteza hela nyingi, tumeona kuna vyama vingine vimeshindwa kupeleka hela hatusemi wameiba, tunasema ni vitu vimo ndani, kwa nini watu wameshupaa? Lakini mbaya zaidi inaonekana ni kama kwamba hizi hela ni kama vile zimechukuliwa na Rais wakati Rais si mtu wa masuhuli sasa ni maneno gani haya? Yaani kuna vitu vingine vinanga’ang’aniwa kiasi kwamba wakati mwingine huwezi kujua kama vina maana gani hivi. Jamani katika mtu ambae atakuwa wa mwisho kuhukumiwa katika Taifa hili kwamba ni mdhulumati, kwamba ni mwizi, kwamba ni mtu anayekula rushwa ni Rais John Pombe Magufuli, wananchi wanamjua ndiye namba moja kwa uaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara hii sana kwa mambo mazuri sana waliyowatendea wakazi wa Jimbo langu, kama vile ujenzi wa nyumba vya madarasa primary na secondary. Wizara hii imesaidia sana ujenzi wa sekondari ya Makongoro kwa mabweni na nyumba. Shule hii ina kidato cha kwanza na cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba shilingi milioni 72 kumalizia ujenzi wa bwalo la Chalanda, watoto wanalia nje, mvua na jua lao. Sekondari ya Mekomariro tunajenga bweni, tunaomba samani za bweni (vitanda, meza na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni sekondari za Nyamangita, Salama Rihingo na Chamriho, Nyamangutu. Naomba ujenzi wa maabara. Kwa upande wa Salama, jengo la maabara lipo katika kata, tunaomba fedha za kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chamriho na Mihingo watoto wanasafiri kilometa 17 kutoka eneo la shule ya sekondari. Tunaomba Wizara mtusaidie maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii, akiwepo Naibu Katibu Wizara ya TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, nilitoa taarifa ya kubomoka na kuanguka kwa shule za msingi Sarawe na Stephen Wasira ambapo watoto wawili walifariki.

Mhshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kutoa msaada wa dharura kwa shule hizi mbili. Naomba ahadi hii itekelezwe, kwani mwakilishi na Serikali (Mkuu wa Mkoa) kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Elimu waliahidi kusaidia kutoa msaada wa dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo sugu ambalo liko kimya, tatizo la mikopo ya watumishi na hasa walimu ambao ndio wengi. Walimu wanakopa kuliko uwezo wao, hakuna limit ingawa zipo sheria za mikopo, lakini hazifuatwi. Naomba Wizara ifanye tathmini ya kuhusu jambo hili. Tafuteni udhibiti wa namna mikopo ya mabenki katika eneo la walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya wanafunzi iwe kwa wanachuo toka Diploma hadi Chuo Kikuu na mikopo iwe kwa ngazi zote au mwaka wa kwanza hadi wa tatu bila kujali hakuna mwaka wa kwanza au wa pili au wa tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunashuhudia Wizara hii kwa muda mrefu, lakini kwangu nilichokiona muhimu sana katika hii Wizara ni uadilifu wa Wizara. Uadilifu wa Wizara ya Elimu sasa hivi umekuwa mkubwa sana kwa sababu fedha zote zinazotoka kwenye Wizara zinakwenda chini zinafika salama na zinafanya kazi salama. Zamani ilikuwa fedha zikija huku zinarudi tena Wizarani huko huko lakini siku hizi zinafanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, nisifu uadilifu wa Wizara hii umekuwa mkubwa, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Katibu, Naibu na wote wanafanya kazi vizuri sana, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko machache ambayo naona pale vijijini kwa sababu vitabu vile vya wanafunzi wa darasa la nne wanafanya mitihani havijaenda, lakini nimepiga simu kule wameniambia ndio vimeanza kwenda. Kama vinaenda kweli naomba vifike salama kwa sababu wanafunzi wanavihitaji vifike kwa wakati lakini tunafikiri kwamba Serikali imefanya vizuri kupeleka hivyo vitabu mapema na vinaendelea kusambazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Jimbo langu la Bunda na hili nimelisema muda mrefu. Wizara ya Elimu imetupa majengo mazuri sana kwenye Shule ya Makongoro ambayo ina wanafunzi wa high school na wale wa kidato cha nne lakini jengo la Bwalo la Makongoro
limejengwa mpaka kwenye lenta limeshindwa kumalizika na fedha yake ilikuwa imepungua. Tunaiomba Wizara itusaidie kwenye hilo jengo ili liweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekondari ya Nyamang’unta na Sekondari ya Salama kuna majengo ya maabara yameshindwa kukamilika. Tunaomba mtusaidie ili yaweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Salawe na Shule ya Msingi Stephen Wassira, majengo yalianguka na watoto wawili walifariki na taarifa zilitolewa kwenye vyombo vya habari na tukatoa taarifa Wizarani, TAMISEMI inajua na Wizara ya Elimu inajua. Mliahidi kutusaidia tunaomba mtusaidie hizo shule mbili ziweze kupata majengo yake kwa sababu watoto walipotea na wananchi walipata mateso ya kuhangaika muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Chamriho Sekondari na Mihingo Sekondari watoto wake wanatoka kilometa 17 kutoka eneo la kijiji wanachokaa na wasichana wale wakianza 50 wanamaliza 12 au watano. Kwa hiyo, tunahitaji shule hizi mbili zipate mabweni ili watoto wa kike waweze kusoma katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala muhimu sana ambalo mimi sijui kama mnaliona lakini lina-affect sana hii industry ya elimu kwa maana ya kiwanda cha elimu hiki ambalo ni masuala ya mikopo. Kama hatutaweza kudhibiti mikopo ya mabenki kwa walimu; mwalimu anapokea mshahara wa shilingi 2,000,000 lakini anaenda kupokea mshahara wa shilingi 150,000 na siyo walimu tu na watumishi wengine wote wa Serikali hii, kama hizi sheria za mikopo za mabenki kwa watumishi wa Serikali hatuwezi kuzidhibiti vizuri maana yake ni kwamba hakuna uaminifu utakaokuwepo. Ni lazima tuone mshahara unabaki kama sheria inavyosema. Mtu anapokea mshahara shilingi 300,000 anapokea shilingi 50,000 wengine wanapokea shilingi sifuri. Kwa hiyo, tufanye tathmini ya kujua hii mishahara ya watumishi na hasa walimu ambao wakati fulani hawana hela za akiba tuone tutadhibiti vipi ili walimu waweze kutumika vizuri kwenye shule zetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni kiwanda na tatizo liko hapa elimu yetu nzuri au mbaya? Ili kutambua elimu nzuri au mbaya ni namna gani tunazalisha? Je, tunazalisha watu wenye ubora kulingana na soko lilivyo au ni watu wasio na ubora kulingana na soko? Kwa sababu unaweza kuzalisha jambo, kwa mfano sasa hivi tunazungumza habari ya viwanda na kama tunazalisha watu wa historia, tunazungumzia watu ambao hawako kwenye mambo ya ustawi wa jamii na kwenye mambo ya ufundi kama walivyosema wenzangu, shule za ufundi hazipo, hivi tunalenga nini hasa?

Kwa hiyo, kwenye soko letu tunakokwenda huku mbele halitakuwepo, hatutapata watumishi wanaoweza kwenda kwenye viwanda. Elimu inataka unazalisha nini, ni suala la demand and supply. Kwa hiyo, tuweze kujua kwamba elimu yetu hii tunayozalisha watoto wakoje, ndiyo hilo wanasema quality education na quality in education, ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, tuangalie michango yetu inakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la matangazo la Baraza la Mitihani. Mimi huwa mara kwa mara najiuliza sana, mtu anakaa pale kwenye tv anatangaza, mitihani kidato cha kwanza au mitihani primary shule bora, St. Mary, St. Augustine, sasa unalinganisha na nini? Shule yangu ya Mihingo ina mwalimu mmoja toka inaanza. Shule yangu ya msingi watoto wanasoma nje, wana matatizo mbalimbali, unakuja kusema imekuwa ya mwisho kwa kulinganisha na nini, unalinganisha nani sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwamba mambo haya tuweze kuweka categories ili tulinganishe maana sasa hii mitihani tunalinganisha na nani? Huyu amekuwa bora kwa kulinganisha na nani? Hivi kweli leo unaweza kuleta hapa Barcelona ukasema inacheza sijui na Yanga halafu useme imekuwa ya kwanza eti kwa sababu tu ni sheria inaruhusu?

Kwa hiyo, nafikiri hata mitaala hii nayo tuiangalie upya wakati fulani haileti maana sana kwenye mambo haya ambayo yanakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi tumezungumza kwenye mambo ya sera. Mimi nafikiri huo mfumo unaouzungumza kwamba kuwepo na kongamano zito, alizungumza Mzee Mkapa, akazungumza Mzee Jakaya na hata Mheshimiwa Magufuli akitoka mtasema Mheshimiwa Magufuli alizungumza. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hii mijadala hii iendelee kuwepo na hakuna mtu anazuia mjadala, nami nawaomba Wizara ya Elimu pale watu wanapotaka kufanya mijadala ya elimu basi tuwaunge mkono ili tuweze kuona kitu bora tutakachokuja kufanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia jioni ya leo katika bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchangia Wizara hii ya Maji kwangu mimi naomba Mungu anisaidie nipate akili ya kusema vizuri kwa sababu ninaweza nikaruka humu Bungeni. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu aliwahi kusema ni bora kuongoza maskini mwenye matumaini kuliko kuongoza maskini asiye na matumaini na maskini mwenye matumaini ni yule aliyelima mihogo au ana shamba anaweza kumkopa mwenzake fedha kwa kumuomba kwamba mahindi yake yakifika atauza atamlipa lakini yule ambaye hana kitu kabisa huyo ni maskini asiye na matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili mimi naona ni maskini nisiye na matumaini maana kila bajeti inayokuja sioni kwenye Jimbo langu la Bunda kuna chochote mle ndani. Kwa hiyo, inavyofika wakati huu naona kwamba hivi Bungeni humu nafanya biashara gani humu ndani? Si bora tu nitoke nikachunge ng’ombe huko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Bunda na Bunda kwa ujumla kuna miradi mbalimbali na mimi nashangaa watu wanasema hamna fedha, nadhani fedha zipo ila usimamizi wake ni kidogo sana au tuna ugonjwa unaoitwa D by D, hii ambayo wataalam wametupatia. Wizara ya Maji inatoa fedha kwenda kwenye Halmashauri, mamilioni ya fedha yanaenda, watekelezaji wa miradi ile ni watu wa TAMISEMI, wahandisi wako TAMISEMI na pengine hata Waziri wa TAMISEMI au Naibu wake, watumishi wake hawajui fedha ngapi imeenda huko, inajulikana kwa Wizara ya Maji tu peke yake. Waziri wa Maji anapokwenda kukagua maji anakuta fedha zimeliwa. Ukimuuliza Waziri sasa huyu achukuliwe hatua gani anakwambia mimi hao siyo wangu mpaka niende kushauriana na Mheshimiwa Jafo, hii biashara hatuiwezi hii, hii biashara itakuwa ngumu sana.

Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia huu ugonjwa wa D by D tunaufanyaje katika hizi Wizara mbili, vinginevyo tutapata shida sana na ndiyo maana tumeshauri hapa mara kwa mara kwamba Wakala wa Maji Vijijini uwepo ili Waziri apewe vitu vyote, fedha na watu wake aweze kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie miradi ya Wilaya ya Bunda kwa ujumla, tuna Mradi wa Kibara shilingi milioni 400, zimetumika pale kama shilingi milioni 300 na zaidi maji hayatoki, lakini kwenye taarifa utaonesha maji yanatoka. Kuna Mradi wa Buramba, shilingi milioni 353, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kinyambwiga shilingi milioni 395, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kwing’ombe shilingi milioni 700, mradi umeisha na Mwenge ukafungua, maji hayatoki, kuna Mradi wa Nyamswa Salamakati, shilingi milioni 252 zimetumika, maji hayatoki, kuna Mradi wa ufadhili wa Bomamaji, walikuja wafadhili pale Bomamaji wakatoa shilingi milioni 987 zimeliwa, ripoti ikatolewa haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mkubwa wa maji wa Bunda ambao bomba lake linatoka Nyabeho nao unasuasua. Mbaya zaidi kuna mradi wa Mgeta, Nyang’aranga zikatolewa shilingi milioni 495 zimefika shilingi milioni 910 maji hayatoki na Waziri ameshafika pale akiwa Naibu Waziri. Sasa hili linakuwa ni tatizo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba ukimuuliza Waziri hapa nimezungumza habari ya malambo kule kwetu sisi Bunda malambo hayo ndiyo visima tunaita, ndiyo ng’ombe na binadamu wanakunywa. Tukamwambie atutengenezee malambo ambayo yalitengenezwa na Chifu Makongoro yatatusaidia huko tunapokwenda, akakubali hapa Bungeni kwamba atatengeneza hayo malambo akasema leteni mpango. Tumepeleka mpango tukamkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara, kuidhinisha huo mpango uende kujengwa ukija kumuuliza Waziri anakwambia malambo sichimbi mimi, anachimba Wizara ya Kilimo lakini Wizara hii ya Maji ndiyo yenye malambo. Sasa najiuliza hii ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba kiasi cha shilingi bilioni moja bajeti ya 2016/2017 hatukuitumia, Halmashauri ya Bunda haikupata taarifa. Bajeti ya mwaka 2017/2018 tumewekewa shilingi bilioni moja tumeleta mpango wa maji wa malambo sita hayachimbwi wala hamna kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Bunda una mradi mkubwa wa maji na kuna kitu kinaitwa chujio. Mimi nimwombe Waziri, pale wanasema kuna shilingi bilioni 12, wanasema ni nyingi labda hizi ni za wizi. Sasa kama ni za wizi ngapi zinatosha sasa kwa sababu katika kuchimba, mimi siyo mtaalamu lakini katika mambo ya kuchimba hilo chujio kuna vitu vinaitwa clarifier, flocculant, rapid stand, refilter, mitambo na kuna vitu vingi mle ndani. Wataalam wa Wizara si waende waangalie kwamba ni fedha ngapi zinatosha kuweka hiyo chujio. Kwa sababu maji ya Bunda kila siku yanaletwa maji machafu, kila Waziri anayekuja mnanywesha maji machafu kwa nini sasa msipeleke wataalam watuambie hili chujio badala ya shilingi bilioni 16 ni bilioni ngapi? Wakati fulani tunaweza tukawa tunawalaumu watu tu kwamba mkandarasi amekula, amefanyaje, twendeni tukajiridhishe na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya fedha, tumezungumza mwaka jana kwenye bajeti Sh.50 kuongezeka kwenye mafuta kwa ajili ya kupata fedha za kuhudumia maji lakini imekuwa wimbo. Sasa Wabunge tukubaliane, wakati fulani mimi nasema na tutaendelea kusema, humu ndani tukifa wote watasema Wabunge wa Tanzania wamekufa, hawatasema CCM wala CHADEMA. Ifike muda tukubaliane kwamba kwenye mambo yale ambayo tunakubali ni halali tuache UCCM wala UCHADEMA tukubaliane hoja. Kwa nini tunaweka shilingi 50 kwenye mafuta iende kwenye maji halafu haiwekwi, nani anaizuia na sisi ndiyo wawekaji wa fedha? Kwa hiyo, nafikiri Waziri anapokuja hapa atuambie anafanyaje kuhakikisha kwamba hiyo fedha kwa kipindi hiki itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri, najua wakati fulani tukisema haya mambo yanamgusa Waziri, Naibu na watendaji wake, lakini watu hawa nao ni wapya. Hebu tuweke mtazamo mzuri, hivi Waziri anaposema shilingi bilioni moja imekwenda Bunda, lakini haikutumika, anatulaumu sisi Wabunge, hivi nani ana utaratibu wa kuwaambia Halmashauri fulani kwamba jamani kuna fedha zenu hapa mbona hatujaona proposal yenu ya kuanzisha miradi? Kwani wataalam wa Wizara ya Maji wana kazi gani? Kwani nani anaweza kujua mradi Bunda iko miradi mitano wanaandika imekamilika lakini haitoi maji, nani anaweza kujua? Ina maana Wizara ya Maji haina watu wa IT ambao wanaoweza kujua vitu hivi? Siku hizi watu wanafanya vitu kwenye computer kwa nini haya mambo hayafanyiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua bajeti tutampitishia Mheshimiwa Waziri najua na wewe una bidii sana ya kufanya kazi lakini mimi kwangu uadilifu si hoja. Kwangu mimi mtu awe mwadilifu na awe mbunifu. Unaweza kuwa na mwadilifu anakaa na hela tu kwenye droo hapo watu wanakufa bila maji. Kwa hiyo, tunajua Waziri wewe ni mwadilifu jitahidi kufanya innovative na creative kwenye ofisi yako ili watu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ile proposal yangu ya Bunda ya malambo, sisi malambo ndiyo visima, atupitishie ili watu wakapate maji. Toka mwaka 2008 hii miradi imeanza kuzungumzwa humu ndani na bajeti zinakuwepo, lakini haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza niwashukuru tu watendaji wa Wizara tukianza na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kasoro wale tu wanaodhulumu ng’ombe hao siwezi kuwashukuru hao ambao wanadhulumu ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, naliona jambo moja muhimu sana ambalo unaweza ukalifanya wewe kwa ujasiri wako. Wizara tulipokuja hapa Bunge hili tulikuwa tunataka kushughulikia masuala ya wafugaji na ardhi ya migogoro ya mipaka. Zikawekwa Wizara tano kushughulika matatizo hayo, zimeshindwa, zimeshindwa kushughulika matatizo ya wananchi katika mipaka na mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nakuomba wewe sasa ama uunde Kamati Maalum ya Bunge kushughulikia migogoro hiyo au ukiona hilo ni gumu utuachie Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii washughulikie hiyo migogoro. Kwa maana sasa watendaji wa Maliasili wanaoshughulika na mapori ya akiba na hifadhi wanachokifanya ni kile ambacho umekizungumza sasa hizi hapa wanakwenda na ramani, hata kama hiyo ramani mipaka yake ya asili ilikuwa Bahi, lakini ramani yao inaonesha wamekuja vigingi UDOM, watafika UDOM halafu wanamwambia mwanakijiji vigingi vyetu vipo hapa kwa hiyo tuamue hapa. Haliwezi kuisha, hauwezi kuachia mgogoro wa mtu aliyeweka mwenye mali halafu aamue mgogoro wake, haiwezekani.

Kwa hiyo, tukubali sasa ile Wizara ya Ardhi na zile Tume zilizounda zimefeli. Sasa ni jukumu lako uunde Tume au uwaambie watu wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii waendelee ku-solve hiyo migogoro uwape mamlaka hayo, nilikuwa nafikiri kwamba hilo ni la maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Stiegler’s Gorge nilikuwa naliona kwangu kwa mawazo yangu, kwa sababu wafadhili hawawezi kujenga ule mradi, kama Serikali yetu ina uwezo wa kujenga huo mradi na wana fedha za kujenga huo Mradi wajenge na kama fedha hizo za mradi huo zitahujumu maeneo mengine ya miradi kwa mfano kwenye kilimo, ardhi, viwanda kama fedha zetu hazitoshi kujenga Stiegler’s Gorge kwa maana kwamba tuna mambo mengine yanagusa wananchi tuangalie upya juu ya mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake isije ikawa tukachukua fedha zote kama hatuna ufadhili tukazipeleka kwenye Stiegler’s Gorge halafu maeneo mengine ya nchi yakaathirika na mradi huo. Lakini kama ni mazingira, mimi mwenyewe nimesoma mazingira, mazingira yapo kwa ajili ya binadamu na binadamu yupo kwa ajili ya mazingira. Habari ya kukata miti milioni ngapi hiyo sawa, lakini miti mingapi tunakata kwenye nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuangalie kama tuna fedha ya kujenga hiyo ndo muhimu ili maeneo mengine haya tusije tukamalizia fedha. Kwa sababu wafadhili hawapo tayari kufanya ule mradi, nimeusoma muda mrefu wafadhili wamekuwa wakitukataza mambo mengi tu hata barabara ya Loliondo, hata maeneo ya kujenga viwanja vya ndege hata nini hawajengi viwanja hivyo. Kwa hiyo, suala ni moja tu tukubali tu Wabunge watuambie na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ituambie ina fedha za kujenga? Je, fedha hizi hazitaathiri maeneo mengine ya uchumi wetu? Basi hilo ndiyo jambo muhimu la kufanya kwenye mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumza kwenye maeneo yangu ya Bunda kwamba niwashukuru Wizara wamekuwa wanafanya maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka vijiji vinavyozunguka mbuga za wanyama, niwashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kunijengea Kituo cha Afya Kunyali, wanafanya maendeleo, niwashukuru Wizara kwa kuleta barabara zile za kuvuka vijiji 15 vya kwangu havina uwezo wa kwenda porini kwenye eneo la Serengeti wamesema watafungua barabara ya kutoka Mgeta kwenda kule. Nimshukuru Mtu wa TANAPA, ndugu yangu Kijazi kwa kuona hili kwamba sasa mnaenda kufanya maendeleo kwenye maeneovijiji vinavyozunguka maeneo yanayotuzunguka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru kwa mpango wenu wa kupima vijiji vinavyozunguka maeneo haya ili vipate hati waweze kufanya biashara na mambo mengine na vijiji vyangu 15 mmsema vitakuwemo katika vijiji hivyo Unyali, Mgeta, Maliwanda, Kihumbu na maeneo mengine ambayo amezunguka maeneo haya. Niwashukuru sana kwa mpango huo ambao mtaufanya kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna zile vitu vya buffer zone, sasa buffer zone nashangaa buffer zone za National Park au Hifadhi ya Taifa kwa maana Mapori ya Akiba, TAWA na TANAPA zinakwenda kuweka kwenye maeneo ya vijiji mpaka ambao siyo wao, wao wanaweka mipaka kwa nini sasa? Kwa nini buffer zone isiende kwenye upande wako wewe? Nadhani kwa kuunda hiyo Kamati ambayo tumeisema tutashughulikia matatizo kama haya nadhani yanaenda kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla niseme jamani timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga vizuri. Kigangwalla wanaweza wakakutafsiri kwa maana umekaa kimya upo hivi, lakini una uwezo wa kufanya kazi, Naibu wako anauwezo wa kufanya kazi, Makatibu wana uwezo wa kufanya kazi kwa hiyo tuwashukuru waendelee kufanya kazi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea. Ni dakika ngapi Mheshimiwa?

SPIKA: Dakika kumi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hizo dakika kumi.

Mheshimiwa Spika, nchi zetu za Afrika zilikuwa zinatawaliwa na wakoloni kwa miaka mingi tu ikiwemo Tanzania nayo ilitawaliwa na Waingereza lakini kwa sasa wakoloni hawawezi kutawala nchi za Kiafrika, kilichobaki ni kuwatawala katika fikra zao yaani fikra za Waafrika wengi viongozi wengi na hasa wasio kwenye chama tawala wamekuwa colonized na Wazungu. Ndiyo maana utawakuta wapo maeneo mbalimbali wanazungumza mambo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Nilikuwa naangalia hapa kwenye takwimu mbalimbali wanasema top ten best performing President in Africa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli yumo. Ana miaka mitatu tu toka ametawala nchi hii lakini ameingia ni wa nane, amemzidi mpaka wa Rwanda miaka mingapi ametawala? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama mtu anazungumza mambo ya Stiergler’s Gorge namshangaa. Nataka ni-declare interest kwamba mimi nimesoma diploma, certificate na degree ya mazingira. Sheria ya Mazingira inasema hivi utawale mazingira na mazingira yakutawale. Ukiangalia nchi zote duniani zilizoendelea zina mabwawa ya hydroelectric power; Marekani, China, Uingereza zote wanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu, China sasa ina mahali panaitwa Gorges Dam capacity yake ni MW 22,500. China imechukua mito kama mitatu imekusanya yote, ina watu bilioni sijui 3 leo tunazungumza Tanzania MW 2,400 watu ng’e, ng’e, ng’e, hivi wamekuwaje? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, Marekani wana bwawa linaitwa Grand Coulee Dam, capacity yake ni 6,809. Sasa Marekani wametengeneza mto unaitwa Colombia, ule China unaitwa Yangtze, leo wale waliokuwa-colonized kwenye akili they are talking about mambo ya wazungu, sasa akili gani hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe tu angalizo, nampenda sana rafiki yangu Msigwa na tupo Kamati moja, mimi Mungu alinisaidia kuwa mkweli, ni vizuri tuwe wakweli. Kwanza amezungumza kwamba kwenye Kamati yetu hakuna taarifa lakini taarifa hiyo imo. Kamati imempongeza Rais kwa kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi nchini. Wewe ulitaka tuseme kwamba wamenyang’anya mashamba ya Sumaye? Rais anapofanya kazi nzuri ni kumpongeza. Naishukuru Kamati yangu ya Ardhi imefanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, tumempongeza Rais kwa kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Rais hanyang’anyi watu mashamba na Rais yeye hafuti umiliki. Nataka nitoe mfano, Bunge lako ndiyo linatunga sheria, leo mwanafunzi wa darasa la kwanza, la pili au la tano akiulizwa nani anatunga sheria za Tanzania watasema Bunge la Tanzania lakini hizo sheria haziwezi kwenda kufanya kazi bila Rais kupitisha. Kwa hiyo, Rais akipitisha ndiyo inakuwa sheria. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, matatizo ya hawa jamaa ndiyo hayo hayo, yaani wao ni kukuza maneno, Mwenyekiti wetu sisi anafanya kazi nzuri, kama amejiuzulu, amejiuzulu kwa utaratibu wa kawaida wa watu kujiuzulu. Mimi nampongeza Mwenyekiti kama amejiuzulu kwa utaratibu wa kawaida basi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee, hakuna siku kwenye Kamati yetu na Mwenyekiti wangu yupo hapa tumewahi kuita watu wenye mashamba walionyang’anywa wakalalamika, tumeita watu wa porini, tourism na watu wa kila mahali, Kamati tuna majina.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, tuna orodha ya mashamba mengi nchi hii yanayotegemea kufutwa na mengine yamefutwa na sheria iko wazi…

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nadhani huyu ana jambo analo kichwani ndiyo linalomsumbua, kwa hiyo, tuendelee na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuja na orodha ya mashamba yanayopendekezwa kunyang’anywa au kufuta miliki siyo kuleta wadau waliolalamika. Ni kweli kwamba Kamati ilikuja na mashamba mengi tu ya wakulima wadogo na wakulima wakubwa. Sheria ya Ardhi iko wazi inakutaka ukipewa uwekezaji miaka mitatu uwe umeendeleza.

MBUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Sheria hiyo inasema tukitaka kunyang’anya shamba tutakupa siku 90 za kujitetea. Nani aliwahi kuleta hiyo barua wewe ukaiona? (Makofi)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, niombe nchi yetu tufanye kazi moja kuwaelimisha Watanzania waelewe nini maana ya kuwa mzalendo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kuzishukuru Kamati zote mbili, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo. Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati hizo na Mawaziri walioshughulika na Kamati hizo kusaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natazama vitu katika Kamati hizi na nimeona kuna jambo nataka nilizungumze la Kamati Ndogo kuhusu kile kipengele cha Kodi ya Majengo. Kipengele hiki cha kodi ya majengo wakati kinatekelezwa katika maeneo yetu kimekuwa na vitisho vingi sana. Kwa hiyo, naomba wakati wanafanya ufuatiliaji wa kipengele waangalie kwa sababu huko vijijini kuna nyumba za nyasi na nyumba za bati, ilifika wakati ukijenga nyumba ya bati unadaiwa kodi, ikaonekana kama ni Kodi ya Kichwa hivi. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie vizuri kwenye kodi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa ni letu wote na kama kuna watu wana ndoto kwamba nchi hii ni ya Rais John Pombe Magufuli na chama chake na wako tayari kuiharibu kwa wakati wowote wanavyotaka kwa maslahi yao watakuwa wamekosea sana. Hotuba nyingi zinazokuja hapa hata ya ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kubenea anauliza habari ya ma-DED kwamba ni makada wa CCM, lakini hapa tuna Wabunge zaidi ya 100 kwenye uchaguzi uliopita na wametangazwa na ma--DED hao wanaosema ma-DED wa CCM. Sasa DED amemtangaza kuwa ameshinda, amekuja Bungeni halafu anamsema ni mbaya, sielewi kinachoendelea huko mbele katika mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanazungumzwa hapa. Nilikuwa natazama sana wakati Rais wa United State, Trump, alivyo-tweet juu ya White House, kuhusu ya Wazungu wale weupe wa South Africa kwamba anataka kuwalinda wale Wazungu kwa maana ya ardhi ya South Africa. Nikamtazama Julius Malema, nikamtazama Ramaphosa ambaye ni Rais, wote walikusanyika pamoja kutetea ardhi ya South Africa bila kujali upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimuona Malema alienda mbali zaidi anawaandaa wanachama wake anawaambia tuko tayari kufa kwa ajili ya ardhi yetu, hatuko tayari kutoa ardhi yetu kwa sababu ya umasikini wetu au kwa sababu hatuna uwezo wa kufanya jambo hili. Huyu ni mpinzani wa South Africa lakini nchi yetu leo hata tungezungumzia habari ya kugeuzwa kuwa wanawake tayari watu wanatetea. Mimi sielewi kama katika nchi hii hali ya hewa inavyoenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza democracy lakini wanashindwa kutofautisha democracy and futures of democracy…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa heshima ya Paroko nafuta hilo neno, tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine wakati fulani unaweza ukaongea hata ukachanganyikiwa kwa sababu leo kama tuna watu ambao ni Watanzania wanaodhani kwamba Rais au utawala wa nchi hii ambao tuliupata bila kumwaga damu na kuna watu walihangaika kuupata kwa kuzunguka tukapata uhuru, leo ni mwaka wa 48, wanadhani kwamba nchi za Ulaya, za Mabeberu wanaweza kuamrisha Watanzania wakampa mtu Urais kwa kupitia nchi za Ulaya, haya ni mambo ya ajabu na ya aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais aliyekuwa maarufu sana hapa duniani na Afrika, Nelson Mandela, alifungwa miaka 27. Alipotoka jela wala hakwenda Ulaya kutafuta Urais, alikaa kule kwake na wala alipotoka jela wala hakutafuta nani alimweka jela. Alikaa kwenye nchi yake akawaambia uhuru tunautafuta na uhuru akapewa na Wazungu waliomweka ndani miaka 27 akaishi nao, ni historia kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu akikosewa dakika mbili, dakika tatu, imekuwa matatizo. Leo tuna Rais bora kabisa katika nchi za Afrika, ameandikwa humu ndani ukisoma, ana miaka mitatu lakini ameandikwa anafanya vizuri. Leo nchi yetu ni ya 10 kwenda kwenye uchumi bora katika nchi za Kiafrika. Sasa leo wanapita tu wanachafua nchi yetu ambayo ni yai letu la kulea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale wote ambao wana mawazo hayo warudi tufanye kazi ya ndani wasichanganye demokrasia na utekelezaji wa demokrasia. Kama kuna utekelezaji mtu anazungumza ni watu wanafungwa na kesi zinacheleweshwa, mmeona juzi Mheshimiwa Rais ameteua Majaji na anaendelea kuteua ili mambo ya kesi yaende vizuri na mambo mengine pia tunaendelea kuyatendea haki, mfano, uchaguzi tumechagua vizuri na tunaendelea kuchagua. Tunapozungumzia demokrasia maana yake nchi yetu inatekeleza demokrasia. Tumechagua Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais hiyo yote ni demokrasia, sasa demokrasia inayozungumzwa ni ipi, mimi sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasilete hofu kwamba utendaji mzuri wa Mhesimiwa Dkt. Magufuli watakosa vyeo, ukikosa cheo ni Mungu ameamua, siyo wewe sasa. Mungu akisema wewe huwezi kuwa Mbunge huwezi kuwa Mbunge. Kwa hiyo, tukubali kwamba nchi ni yetu tumsaidie Rais afanye kazi vizuri ili tuendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, chama ni chenu na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezwa ni yenu, tufanye kila namna tumsaidie Rais afanye kazi yake vizuri. Pale ambapo tunahitaji kumshauri, tumshauri vizuri, pale tunapotakiwa kutenda, tutende vizuri. Tukianza kuwa tofauti maana yake ni kwamba chama chetu kinakwenda kufa, kwa sababu aliye na dhamana ya kusimamia Chama cha Mapinduzi kwa sasa ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Huyo ndiye mchezaji wetu wa Chama cha Mapinduzi, tukimyumbisha wakamkanyaga mguu ukavunjika maana yake chama chetu kinaenda kupata matatizo, kwa hiyo, lazima tumlinde kwa heshima zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru tumeupata, nchi yetu ipo, ina miaka 48 na ina sifa, ni nchi pekee duniani yenye Muungano. Nataka niwakumbushe watu, tusipokuwa watetezi wa mambo mazuri tuliyoyafanya, kama mwaka 1995 Muungano wetu ulivyotaka kuyumba, asingesimama imara Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere, akaita Bunge na Halmashauri Kuu ya CCM na tukakubali kuendelea na Muungano leo Muungano usingekuwepo. Kama hatuwezi kuungana kutetea nchi yetu maana yake wote tunaweza kwenda kwenye matatizo. Nchi yetu ni ya amani na watu wetu hawakuzoea mabomu na timbwilitibwili nyingi, kwa hiyo, tunaomba watu wawe na amani na tuombeane amani ili tuweze kuishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema kwamba suala la kum-support na kumpa nguvu za kutosha Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli sio la majadiliano tena, ni suala la kumuunga mkono kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kila kitu. Na yale anayoyafanya hayawezi kutufaidisha sisi tuliopo, yatawafaidisha wanaokuja na huku mbele kama wenzetu wa upande wa pili wa Gaza kama watakuja kupata nafasi watafaidi haya matunda ambayo Rais anayafanya kwa sasa, kwenye miaka milioni 200 inayokuja huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze mambo matatu leo, la kwanza nataka nizungumze habari ya TANAPA. Shirika hili linatunza hifadhi 16 lakini hifadhi zenye faida ni tano tu, na juzi tumeongeza hifadhi nyingine za BBK, Burigi, Kimisi na hifadhi nyingine zimeongezeka nyingi, hifadhi tano ndiyo zenye faida. Na sasa shirika hili lina michango na kodi ambayo inalipwa kodi ndani ya kodi, likitoa mchango wa kujenga Kituo cha Afya Hunyari, Bunda kodi inakatwa, likilipa cooperative tax ndani ya kadi inakatwa, na tumezungumza sana na Kamati ya Bajeti nadhani imepewa hiyo taarifa. Ninafikiri Serikali ione namna gani ya kulipunguzia hili shirika hizi kodi ndani ya kodi ili liweze kujiendesha lenyewe kwa sababu lina mzigo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote mashirika kama haya huwa yanapewa ruzuku lakini TANAPA inajitegemea, kwa hiyo naomba waipe nafasi ili iweze kuleta namna ya kujenga miundombinu kwenye maeneo mbalimbali ili tuvutie wawekezaji na kuleta watalii wengi kama inavyoonesha kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kwamba wameongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 67 fursa za ajira, lakini nikasoma Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukurasa wa 23 unasema; upatikanaji wa pembejeo, hatua iliyofikiwa ni kununuliwa kwa lita elfu mbili mia mbili sitini na tisa elfu na kilo elfu tatu vya viatilifu zenye thamani ya shilingi bilioni tisa na hivyo viatilifu vya bilioni tisa vinaua panya, nzige, wadudu viwavijeshi, sasa mimi leo nataka nizungumze fursa ya viwavijeshi na fursa ya vipepeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya leo kuna soko la mende, kuna soko la panya, kuna soko la mbwa, kuna soko la kwerea kwerea ambalo tunatumia bilioni tisa kuwaua, kuna soko la senene, kuna soko la kila kitu. Nchi yetu tumegawana katika maeneo mawili, eneo moja lina asilimia 36 ambayo ina mambo ya mapori haya, Mapori ya Akiba, TANAPA, maeneo tengefu na maeneo yote yaliyoko hapa. Eneo 64 ni letu sisi tunaotumia Watanzania, sasa kama tunalitumia tuna vitu vinaitwa mende, nyoka, mbwa, vinatakiwa kupata masoko ya nje, tutafute namna ya kufungua masoko hayo vinginevyo tunaua ajira, wamezungumza hapa ukurasa wa 67 fursa ya ajira tunatafuta fursa ya ajira katika mende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mende leo ni zao kubwa sana Brazil, ukifuga mende wewe ni bilionea, kwa mfano mkate mmoja Brazili ni laki moja ambayo ni dola 44,000.4 ya Brazil ambayo ni sawasawa na laki moja na watu wanafuga mende sasa hivi wameanza kufuga Njombe. Leo tunapozungumza nyoka tunazungumza soko kubwa sana na viwanda vikubwa sana China. Kwa hiyo, tunafikiri kwamba kuanza leo watu wafuge nyoka kupeleka huko. Tunapozungumza kipepeo leo ni nafasi kubwa sana Malaysia na maeneo mengine.

Kwa hiyo tunapozungumza Kwelea kwelea, mmoja ni dola mia mbili hamsini ambayo ni pesa nyingi sana. Sisi tunasema tunatumia bilioni tisa kuua wadudu na kibaiologia na mimi ni mtu wa environment, unavyotumia ndege kuua wale wadudu maana yake unaua vyura vinavyohitajika, unaua nyoka wanaohitajika kule chini, unaua nzige wanaohitajika huko juu. Kwa hiyo, tunataka kujua ni namna gani eneo la uwekezaji litatumia viumbe hai hivi vilivyopo hapa kutengeneza njia kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wakenya wanashirika la KWS ambao wanatumia vibali hivi, kwa hiyo wenzetu wanatumia leo wanyama wetu hai, wanatumia mbwa, nyoka na membe kufunga katika maboksi kwenda nje. Kwa hiyo, tunaomba sasa Serikali najua Mheshimiwa Rais aliwahi kusema katika mambo, wakati huo tunafanya mambo ya ovyo, nasema yalikuwa mambo ya ovyo kupeleka twiga nje na wanyama wengine, lakini mzee alivyokuwa anakemea nchi sasa nchi imetulia, arudi aangalie ni fursa gani sasa ipo ambayo watu wanaweza kuitumia bila kuangalia mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumza hilo ili ieleweke kwamba kuna kuna soko kubwa sana la Afrika la wanyama hao. Pia kuna kitu kinaitwa konokono, Ghana ni chakula kibwa sana konokono na konokono kama mnavyomjua tunaita ni double entry anajizalisha mwenyewe, female and male yaani ukimfuga konokono mmoja akila majani mazuri hahitaji mume wala mke anajizalisha mwenyewe, anapata soko na ni dola elfu 25. Kwa hiyo ukienda Ghana ni soko kubwa sana kwenye maeneo hayo. Hivyo, naomba hili tatizo tusiogope kutafuta fursa ya mambo ambayo yapo wazi, tulizungumze wazi na vijana wapate ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia habari ya jimboni kwangu. Sisi kule jimboni tumejenga maboma tisa ya maabara za sekondari hayajamalizika kwa sababu nguvu za wananchi zimekuwa kubwa kwenye maeneo haya, tunaomba sasa maeneo yanayohusika waweze ku-support wananchi wa Jimbo la Bunda kwenye mambo ya maabara waweze kupata nafasi ya watoto wao kusoma sayansi ambapo kwa sasa sayansi inakuwa ngumu sana kuisoma kwa sababu maabara hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la barabara, ambapo barabara ya kutoka Nyamswa kwenda Bunda haijatangazwa na ni muda mrefu sasa tumekuwa tukisema barabara hii itatangazwa itapata mkandarasi tunaomba Wizara inayohusika na wamesikia na Rais amekuja pale akasema itatangazwa hivi karibuni, lakini haijatangazwa. Vile vile barabara ya kutoka Sanzati-Mugumu - Nata haijatangazwa na Rais amefika pale akasema itatangazwa hivi karibuni. Kwa hiyo, tunaomba kwa wanaohusika urekebishaji wa mambo hayo uweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la Silolisimba Mgeta limekatika na Meneja wa TARURA Bunda amelifunga na sasa ni wiki moja. Tunaomba wanaohusika sasa waone namna ya kufungua ile barabara ili wananchi waweze kupeleka ng’ombe zao mnadani na watoto waende shule kwa sababu hali siyo nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka kusema hayo tu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani zangu za dhati kwa Wizara hii, kwa kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa Wizara hii kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, AGP na watumishi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iwe inakumbuka ahadi zake Budget 2015/2016, 2016/2017, niliomba fedha za ujenzi wa vituo vya polisi, Nyamuswa na Mugeta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya makazi ya nyumba za askari polisi ni mbaya sana, tunaomba suala hili Serikali ilione na kulifanyia kazi haraka. Jimbo la Bunda ni wakulima wa pamba, naomba Kituo cha Polisi, Kata ya Haonyori, ambayo wakazi wake ni wakulima wazuri wa pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba askari watumie weledi wao wakati wa kufanya operation. Tarehe 12 Novemba, 2018, kulitokea mauaji ya watu wawili katika mapigano ya vijiji viwili, Remung’orori na Mekomariro lakini askari waliokuja kufanya operation katika tukio hili, walichukua bidhaa zote madukani, walikunywa bia zote katika baa na kupekua masanduku na kuchukua fedha clip zipo na tukio hili siyo zuri, askari watumie weledi.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu. Kwanza, nampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuletea hii miswada mizuri sana; inaonekana wamefanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikutie moyo na wewe Mama Mchapakazi; inavyoonekana ni kwamba kuna watu hawaelewi. Kuna mambo mawili duniani yanapatikana tu kwa kufanya kazi, kwamba busara na umaarufu, hakuna chuo cha busara wala umaarufu. Kwa hiyo, umaarufu wako na busara yako ni kushinda matatizo. Kwa hiyo, nawe unaelekea kushinda matatizo, tunakupongeza kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nilikuwa naangalia hizi sheria, sasa najiuliza, kwanza nimeangalia mambo hapa. Kuna watu tunazunguza mambo hapa bila kujali tunapoelekea. Nchi yetu hii tuna watoto wa mitaani au watoto kwa mfano tunaita mayaya sijui, wale wanaofanya kazi nyumbani wanaitwaje? Wamejaa hata kwenye nyumba za Wabunge humu ndani, lakini sasa tunaangalia tu jambo hili, jambo hili; la pili hatuangalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukiangalia hapa ni kitu kimoja, ninachoomba ni Serikali itafute vipimo vya DNA, vitapakae kwa kila Halmashauri na kila vituo vya afya ili tuweze kujua nani kampa mtoto huyu mimba? Maana watoto wa mitaani hata tunaowaona Dar es Salaam, wengine ni wa watu wakubwa tu. Tumeona kesi kubwa kabisa inaendeshwa na watu, viongozi wakubwa tu wana watoto. Sasa nataka tujue, Mwanasheria aniambie, hivi vipimo vya DNA vinapima muda gani? Kabla au baada? Tujue maana yake! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi nimempa mtu mimba halafu kwa ushahidi wa mazingira, ukanifunga miaka 30. Waziri wa Sheria uko hapa, nikapigwa miaka 30, nikarudi baada ya miaka 30, nikafanya utafiti mtoto aliyezaliwa DNA ikaonesha siyo wangu na wamenipiga miaka 30 inakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba hivi vitu tuviangalie inavyokuwa. Vile vile sheria hii ukiisoma vizuri hapa kwa Mwanasheria alivyotuletea hapa, inamzungumzia mwanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari, ndiyo inavyozungumza. Sheria kuu inasema, anayepewa mimba ni mtoto wa chini ya miaka 18. Sasa kwa elimu yetu kuna watoto wanasoma kwa mfano Sekondari, kuna mwanafunzi ana miaka 18, akipigwa mimba inakuaje? Anahukumiwa kwa uanafunzi au kwa umri wake? Maana nataka kuliona hili nalo limekaaje hapa ili tuweze kujua wanahukumu kwa umri au utoto? Kwa sababu inaonekana hapa tunazungumzia wanafunzi wa Primary na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninachokiona ni ile adhabu tunayotaka kuitoa. Tunatoa adhabu ya miaka 30, sasa najiuliza, hii adhabu tunamwadhibu mhalifu au tunaiadhibu Serikali? Kwa mfano, unamfunga mtoto wa Chuo Kikuu, inawezekana akampa mtoto wa Primary au wa Sekondari mimba, tukampiga miaka 30, lakini miaka 30 hiyo Serikali inatoa chakula, inamhudumia Gerezani. Sasa tunaimpa adhabu Serikali au mhalifu? Kwa sababu mhalifu atakwenda atasoma, atafanya ufundi na kadhalika. Tuangalie na hii miaka ambayo tunaitoa.
Mheshimiwa naibu Spika, kingine ambacho nataka kukizungumza hapa ni wale wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi; na wakati fulani sasa tunamwacha mzazi miaka 18. Halafu tumesema kwamba atakayesaidia mtoto kupata mimba huyu naye tumshitaki. Sasa tunajiuliza, ni nani anayesaidia? Kwa mfano, chini ya miaka 18, wale wanaomaliza Darasa la Saba wako wa miaka 7, 8, au 9; Je, akitoroka yeye amekwenda mjini, wako wanaokwenda kusalimia mjini, sijui wanaenda kusalimia shangazi wapi, wakitoroka huko, halafu unamkamata mzazi wake? Una maana gani? Unamwonea. Wanaosaidia ni akina nani hawa? Pengine nafikiri wanaosaidia ni wale ambao kwa mfano, Serikalini wamekwenda wamefanya mkataba wa mtoto kuolewa. Amepita kwa Mwenyekiti wa Kitongoji amekubali, amepita kwa Mtendaji wa Kijiji amekubali au Mzazi wake amechukua mahari, hapo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kama mtoto ametoroka, halafu unasema mzazi wake amemwoza Dar es Salaam, anajuaje? Tutaonea watu hapa. Lazima tuangalie ni namna gani tunafanya katika kutetea haya mambo. Vinginevyo kikubwa ninachokiona mimi ni DNA. Serikali ilete DNA itapakae kila mahali, tuipeleke kwenye Vituo vya Afya ikae pale halafu tulete wataalam ili mtu ahukumiwa kwa ukweli. Kama amempa mtu mimba, ioneshe kwamba hii mimba ni ya mtoto kabla hajazaliwa ili mtu akahukumiwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nipate kuchangia katika miswada hii miwili. I declare interest kwamba ni member wa Kamati hii sasa kwa bahati mbaya unasema Kiswahili lakini lugha yenyewe ya chemistry na yenyewe inahusu Kiingereza sana. Sasa ndio maana…
NAIBU SPIKA: Kwa mfano neno member ni mjumbe huna haja ya kusema member unasema mimi ni Mjumbe wa Kamati, sio? (Kicheko)
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kuleta miswada hii mzuri sana. Waziri na Naibu Waziri wake tunawashukuru sana, Kamati na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kwa ujumla sisi tumepitia sana hii miswada yote miwili lakini kwangu leo mimi nitajikita kwenye Muswada huu wa Government Laboratory Authority Act 2016 ambao ukija hapa utachukua page namba 16 mpaka 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nizungumze mambo yanayohusu Wabunge kwa ujumla, mjue hali halisi ilivyo kwenye maisha yetu Watanzania. Kunazungumzwa mambo ya sample au sampuli. Kuna sampuli za aina mbili, kuna zile signal ambazo zinachukuliwa na polisi wakati mtu akihisiwa kwamba amekunywa sumu au ameuawa kwa sumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo sasa hapa ni namna gani hiyo sample au hivyo vipimo vya mtu aliyefariki inachukuliwa na polisi kutoka kijiji A mpaka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Kuna matatizo makubwa sana ya kufanya hiyo postmoterm anapokwenda kuchukua daktari, anapokwenda polisi. Polisi mwenyewe kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali mpaka alipwe na analipwa na mtu ambaye amefiwa. Sasa imagine kwa mfano mtu huyu ni maskini anafanyaje, inakuwa ni shida na Mkemia Mkuu wa Serikali ukipeleka lazima uwalipe. Sasa hii naishauri Serikali kwamba katika hivi vipimo ruzuku zitolewe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali katika maabara hii ili pale ambapo watu hawana uwezo wa kupima vipimo hivyo waweze kupimiwa bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zile sample zinapochukuliwa kutoka kwenye viwanda, environmental pollution, yale maji machafu yanatoka kwenye viwanda wanakwenda kupima, mathalani ni kijiji A kimepata athari, wamepiga kelele amekuja mtaalam wa NEMC amechukua vipimo amepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali anataka hela, mtu wa NEMC wa kupeleka hiyo sample anataka hela na vipimo kutoka kwenye viwanda kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali unalipa milioni tatu mpaka milioni saba.
Sasa ni lini wanakijiji watapata haki hiyo? na anayelipa hizo hela milioni tatu, milioni saba ni mwenye kiwanda. Ambaye anatuhumiwa ndiye mlipaji wa hizo hela. Kwa hiyo, hapa tunafikiri kwamba Serikali iweze kutoa hela nyingi kwenye maabara hii ili tuweze kupimiwa, kwa mfano wanavijiji ambao hawana uwezo waweze kupimiwa bure ili waweze kupata haki yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho mimi nakizungumzia hapa ni suala la DNA. Nimezungumza kwenye kipindi kilichopita kwamba wakati fulani hiki kitu usipopima vizuri watu wataozea magerezani. Mathalani unapelekwa kufungwa kwa hisia tu kwamba mimi nimempa mtoto mimba, mtoto wa shule miaka 10, 20, unaenda unafungwa miaka 20 au 30. Siku unatoka kwa sababu kipimo chenyewe kinasema mpaka mtoto apatikane, sasa miezi tisa imepita, mtoto amepatikana amekwenda kufanya utaalam wakasema mimi siye niliyeweka hiyo mimba na mimi nimeshaozea magerezani, sasa haya ni maneno gani haya? (Makofi)
Kwa hiyo nafikiri kwamba wataalam nao wajikite zaidi kujua vipimo hivi kabla mtoto hajazaliwa ili mtu aweze kuokoka kwa kujua kama mtoto si wake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vingine katika hii DNA ni suala la kuangalia, wamezungumza wengi, Kambi ya Upinzani imezungumza sisi kamati tumezungumza. Hivi hawa watu wakemia hawa! Kwa mfano mimi nahisi mtoto si wangu, nimekwenda kusoma Marekani nimerudi, sura nikiangalia mpaka kidole sio changu sasa naanza kujihisi, hapa kuna nini? Sasa napeleka kutafuta DNA, sasa huyu mtu ana nafasi kubwa sana ya kusema mtoto huyu ni wako. Wakienda wakakubaliana na mke wangu kwenye mambo fulani hivi akasema ni wako sasa halafu mimi nikagundua si wangu namfungia wapi? Tunawapa nafasi kubwa sana hawa, tutafute vifungu vya kuwabana ili waweze kuona kwamba namna gani itaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mimi nimefurahi sana jana. Jana tumepitisha muswada mzuri hapa, nimshukuru Mheshimiwa Halima Mdee na Mheshimiwa Mama Profesa pale, wametuletea vifungu, huu ni muswada unahitaji vifungu, sasa maneno ya kebehi ya nini hayana maana humu ndani. Kwa hiyo, nafikiri kwamba muswada wa jana ulikuwa mzuri sana na huu unaokuja tukubaliane kwamba hali ndivyo ilivyo. Kwa mfano leo tunasema Waziri asiteue, lakini Mawaziri wote wanateua. Sasa kama tunataka Waziri asiteue Baraza basi tulete sasa muswada humu ndani au maombi rasmi ya kuondoa Mawaziri wote wasiteue Mabaraza. Sasa huyu Mheshimiwa Ummy Mwalimu tutakuwa tunamuonea sisi hapa. Kwa hiyo, tumruhusu kwamba hii kazi ni ya kwake lakini naye aweze kukaa na management yake huko tunakokwenda mbele tufanye mabadiliko kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo niishukuru Serikali, niwashukuru na Wabunge wote, tufanye mambo kama ya jana, tuonekane Bunge liko vizuri tusizomeane, sisi sote ni ndugu, unanizomea mimi ndugu yako!
Mheshimiwa Katekista Selasini, unanizomea wakati tunasali wote? Mimi ndugu yako! Sasa unanizomeaje? Kusema kweli mimi nilifikiri kwamba iko siku kama haya mambo yataendelea mturuhusu tuingie humu na rungu basi tupigane halafu tuendelee kushindana humu ndani. Naunga mkono hoja.