Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa uwasilishaji mzuri pamoja na heka heka ambazo tumezipata mwanzoni mwa wiki, lakini Wahenga wanasema kawia ufike. Naomba nijielekeze moja kwa moja katika Hotuba na mapendekezo ya Serikali kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja, pamoja na vipaumbele vyote ambavyo tumeviweka, ningependa kuona Serikali inaweka kipaumbele katika ujenzi wa reli ya kati. Naungana na Wabunge wote wa mikoa yote ambao wamekuwa wanaliongelea suala la reli ya kati. Tukitaka kupaisha uchumi wetu, tukitaka kuimarisha uchumi wetu bila ya kuwa na reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge naamini kabisa tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali itakapokuja kufanya hitimisho tunataka kauli iliyokuwa thabiti na wala isiyopinda kuhusiana na nini mikakati yetu ya kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, tumeliongea sana, tuliliongelea katika Bunge la Kumi, sasa umefika muda wa utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tungependa kusikia na kuona Mpango wa Serikali katika kuimarisha Bandari ya Dar es Saalam, tuipanue, kuna kazi kubwa ambayo mmeweza kuifanya na nimpongeze sama Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya ya maboresho katika bandari. Bado tunahitaji kupunguza muda wa utoaji mizigo pale na kuongeza ufanisi na ikiwezekana bandari yetu iwe inafanya kazi saa 24. Hii iendane sambamba na upanuzi wa Bandari ya Mtwara, ni bandari ambayo inakuja kwa kasi, tukiweza kuwekeza katika Bandari ya Mtwara, hakika kabisa tutakuwa tumepiga hatua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie, ni ushirikishwaji wa sekta binafsi. Nchi yetu ina sera nzuri sana ya ushirikishaji wa sekta Binafsi (Private Public Partnership) na tuna sheria ambayo inaendana na hiyo sera ambayo tunayo. Katika upande wa utekelezaji tumekuwa na changamoto kubwa sana, sasa nadhani umefika muda muafaka, miradi yote hii, mipango yetu yote hii, hatuwezi tukaifanya kwa hela ya Serikali, tuishirikishe sekta binafsi katika baadhi ya hii miradi ili sasa Serikali ijikite katika ile mipango mingine mahususi, haya mambo mengine tuweke mazingira mazuri ya uwezeshaji ili sekta binafsi iweze nayo kufanya kazi na tuwape support.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto moja ambayo imekuwa ipo ni kwamba Serikali imekuwa na bureaucracy kubwa sana na tumekuwa tunawa-frustrate sana wawekezaji ambao wanataka kuja kushirikiana na sisi Serikali. Kwa hiyo, naomba sana Serikali itengeneze mazingira mazuri ili kwa wawekezaji binafsi tuweze kuwashirikisha kwa kupitia mpango wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuligusia ni eneo la barabara hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tumekuwa tunaliongelea sana jambo hili, Dar es Salaam sasa hivi kwa mtu kutoka maeneo anayoishi kuweza kufika mjini si chini ya masaa mawili na masaa mawili tena wanayatumia kutoka katika maofisi kwenda majumbani. Tumekuwa tunaongelea masuala ya barabara ya mzunguko (ring roads). Niiombe sana Serikali ifike sasa wakati tuwekeze na tuwe na dhamira ya dhati kuwekeza katika barabara za mzunguko katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuondokane na hii adha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kufanya investment kubwa kwa wakati mmoja, tunaweza tukawa tumeondokana na hili. Tuna miradi mingi ambayo tumeweza kuifanya, tuna Mradi DMDP, lakini tuje na mradi mahususi ambao utaondoa kero ya usafiri katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tunashukuru kwa kuona kwamba zile flyovers zimeanza kujengwa, lakini niongelee kwa upande wa mimi kama Mbunge wa Kigamboni, tumejenga daraja, linakamilika mwezi Machi, lakini tuna changamoto ya approach roads kwa upande wa Kigamboni lakini vilevile kwa upande wa Kurasini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili daraja halitakuwa na manufaa iwapo zile approach roads kuanzia Bendera Tatu mpaka Kamata hazitajengwa. Niiombe sana Serikali, tumefanya investment kubwa sana ya over two hundred billion pale katika Daraja la Kigamboni lakini tuhahitaji zile approach roads ili sasa lile daraja liweze kutumika kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuligusia ni upande wa maji. Inasikitisha kuona kwamba nchi yetu ni asilimia ndogo sana ya wananchi ambao wana huduma ya maji. Ni jambo ambalo nalo tumekuwa tunaliongelea kwa muda mrefu sana, tumeweka mikakati na nakumbuka katika Bunge la mwaka jana au mwaka juzi tuliweka mikakati mahususi na tukatenga bajeti, kwamba, Serikali itumie fedha hii katika kuhakikisha kwamba huduma ya maji tunaisambaza. Naungana mkono na Wabunge wengine ambao wana mtazamo tuwe na Agency kama REA kwa ajili ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, hii itasaidia sana na tu-specify vyanzo vya mapato ambavyo vitakwenda pale kuhakikisha kwamba kama tulivyokuwa na Mfuko wa Barabara na Mfuko wa Umeme Vijijini, basi tuwe na chanzo cha fedha kwa ajili ya maji vijijini, itatusaidia sana kuweza kupiga hatua katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena katika eneo hilo la maji, tuna mradi wa maji ya chini kule Kimbiji, Kigamboni, mradi ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia, unachimba visima 20,000. Niwaombe sana, mradi ule unasuasua mno na ni mradi muhimu sana kwa sisi wakazi wa Kigamboni ambao hatuko katika mfumo wa maji salama kwa DAWASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba mradi ule uharakishwe na usambazaji uweze kufanyika na wanufaika wa kwanza wawe wananchi wa Kigamboni. Hatutakubali maji yale yakaondoka Kigamboni bila wananchi wa Kigamboni kuwa walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka kugusia katika sekta ya afya, tuna changamoto kubwa sana. Burden of disease inazidi kuongezeka, tuna magonjwa ya kuambukizwa na sasa hivi tunaanza kuona magonjwa yasiyoambukizwa, none communicable diseases. Idadi ya wananchi wa Tanzania inaongezeka kwa kasi kubwa sana, sijui kama wachumi wetu na sisi mnakaa mnaliona hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunaongeza Watanzania takribani milioni moja, Watanzania hawa wanahitaji huduma za jamii, bajeti ya afya inashuka kila mwaka, sasa hivi tuko kwenye eight to nine percent. Kuna umuhimu sasa wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha sekta ya afya na mimi ni muumini mkubwa sana wa universal coverage, wananchi wote tuwaingize katika mfumo wa bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la UKIMWI linatufedhesha sana. Asilimia 90 ya fedha za kuendesha mradi wa UKIMWI nchini zinatoka kwa wafadhili na sasa hivi tuko katika hali ngumu kidogo, wafadhili wametuambia tuweke Matching Funds ambayo sisi hatujaweka. Mwaka jana tumepitisha Sheria ya Aids Trust Fund, ni hatua nzuri, lakini niombe sana twende mbali zaidi ku-specify, kwa sababu mwaka jana tuliweka kwamba tuwe na three hundred billion Serikali haiku-commit hiyo fedha. Kwa hiyo, niiombe sasa twende mbali, tu-identify vyanzo na tuweze kuwa na fedha za kuendesha Mfuko wa UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana na naipongeza Serikali kwa uwasilishaji mzuri. (Makofi)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, napenda kuwashukuru sana wachangiaji wote ambao wamechangia hoja hii, walikuwa wengi sana waliochangia kwa maandishi, lakini vilevile ambao walichangia kwa kuongea. Lakini kwa nafasi ya kipekee nimshukuru sana Waziri wa Sera na Bunge, Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye alishiriki vikao vyetu vyote na kwa ukamilifu kuanzia asubuhi mpaka muda ambao tulikuwa tunamaliza, namshukuru sana na kumpongeza sana.
Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati mpya ya UKIMWI kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya kuhakikisha kwamba taarifa hii inakamilika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema kwamba vita dhidi ya masuala ya UKIMWI na vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji dhamira ya dhati. Bila dhamira ya dhati tutakuwa tunapiga porojo na tutakuwa tunaongea lakini vita hii hatutaiweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize katika maeneo machache na la kwanza nisisitize katika suala la sera. Katika Bunge la Kumi tulifanya mapitio ya Sera ya UKIMWI na Sheria ya UKIMWI lakini vilevile Sheria ya Tume ya Dawa za Kulevya ambazo zilielezea kuhusiana na muundo na mamlaka ambazo sheria hizi zimepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwa kusema, kwa kweli Sera ya UKIMWI nayo ni ya muda mrefu, ni ya mwaka 2001 sasa hivi ni mwaka wa 16, tunahitaji tuipitie upya sera ile ili iweze kuendana na mazingira ya sasa. Vivyo hivyo, kuhusiana na Sera ya Dawa za Kulevya ni ya mwaka 2004, mbinu zimebadilika, mahitaji yamebadilika na aina ya dawa za kulevya yamebadilika, tunahitaji sera mpya ambayo itaendana na mazingira ambayo tunayo sasa. Sheria tulizozipitisha zimeelekeza kuhusu muundo mpya, tuiombe Serikali, ili kama tuna dhamira ya dhati katika vita hii, basi miundo hii ya hizi taasisi ambazo zimeundwa upya kisheria basi ziweze kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kupewa watumishi ambao wanahitajika kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo nataka nigusie ni suala la fedha, taasisi zote mbili. Tumeanzisha Mfuko wa Masuala ya UKIMWI, ni jambo jema, Serikali iliahidi shilingi bilioni tano imetoa shilingi bilioni 1.5, mahitaji ya masuala ya UKIMWI kwa mwaka ni takribani shilingi trilioni 1.3, hivi sasa fedha ambazo zinapatikana katika masuala ya UKIMWI ni shilingi bilioni 800, tuna gap ya takribani shilingi bilioni 500, tunahitaji tuongeze nguvu zaidi. Fedha za wafadhili zinapungua, ni lazima sasa tujielekeze katika vyanzo vya ndani. Niiombe Serikali na Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja, ni muda muafaka sasa kuungana, tuhakikishe katika bajeti inayokuja Serikali ije, au sisi kama Wabunge tupendekeze vyanzo mahsusi, kama ilivyokuwa katika Mfuko wa Barabara, kama Mfuko wa Mawasiliano na Mfuko wa Elimu, sasa tuwe na source maalum kwa ajili ya kuwezesha shughuli za UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais leo asubuhi. Katika Kamati yetu na kama mtasoma katika mapendekezo yetu, tulikuwa tunataka kauli za viongozi wa Kitaifa kukiri kwamba suala la dawa za kulevya ni janga, na leo asubuhi Mheshimiwa Rais ameitamka hiyo kauli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na mimi niwaombe viongozi wengine, tuendelee kuibeba kauli ya Mheshimiwa Rais na sisi twende tukayasemee. Ndugu zangu, UKIMWI ulipoanza mwaka 1979 tulisema UKIMWI ni tatizo la sehemu fulani katika Tanzania yetu, hivi tuvyoongea hakuna familia ambayo haijaguswa. Na ninyi mtakuwa mashahidi, katika vijiji vyetu, vitongoji vyetu katika Wilaya zetu na Majimbo yetu, tuna wagonjwa ama tuna watu ambao wanatumia dawa za kulevya na waathirika wa dawa za kulevya. Tunapokwenda ni kubaya zaidi, tunahitaji tuweke nguvu sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu na sisi tungependa kusisitiza; tuna Kamati zetu katika halmashauri ambazo zinasimamia masuala ya UKIMWI na sisi kama Wabunge ni wajumbe wa zile Kamati za UKIMWI. Tunapendekeza na tungewaomba Serikali na hili mliwekee msisitizo, zile Kamati zipewe majukumu ya ziada ya kuwa ni Kamati za Halmashauri kusimamia masuala ya UKIMWI na dawa za kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati tunaunga mkono suala la viroba linaharibu vijana wetu, linaharibu kizazi chetu, linaharibu Taifa letu. Tanzania tunapoelekea sasa hivi tunakuwa ni Taifa la watu walevi, na bahati mbaya sana tumezi-package hizi pombe kwa kiwango cha chini sana. Leo nilikuwa naongea na Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema kule Kanda ya Magharibi pombe hizi zinauzwa shilingi 300, mpaka watoto wadogo ambao wanapewa nauli ya kwenda shuleni wana uwezo kununua ile pombe. Sasa niiombe Serikali, kwa kweli kama ni mapato yote yanapatikana kwa njia hii haramu haiwezekani, tupige vita viroba na sisi kama Wabunge tutawaunga mkono ili tuondokane na hili janga tuweze kujenga kizazi imara kwa miaka ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamegusia suala la tohara; ni kweli katika suala la kitaalam ni intervention ambayo imeonekana inaweza ikasaidia katika kupunguza ugonjwa ya UKIMWI, ni kitu ambacho kimekuwa proven. Lakini hatuwezi tukalazimisha mtu akafanye tohara, muhimu tuwekeze katika elimu na watu waelewe umuhimu na faida ambazo wanaweza kuzipata kutokana na jambo hili, naamini hilo tukiweza itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kubwa sana; tumetoa elimu, na tuliwekeza sana katika elimu ya UKIMWI lakini inaonekana bado tuna changamoto kubwa. Maambukizi kwa vijana kati ya miaka 15 mpaka 19 ni makubwa sana, kwa mujibu wa takwimu ambazo zimetoka hivi karibuni za Tanzania Demographic Health Survey zinaonesha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniruhusu kuendelea. Nilikuwa nasema kwamba, katika rika la vijana wa miaka 15 mpaka 16, hususan kwa wasichana, asilimia 27 wameshapata ujauzito. Sasa tunahitaji kwa kweli tuwekeze nguvu kubwa sana katika rika hili kupunguza mimba za utotoni, lakini vilevile katika kupunguza maambukizi. Na hili suala la elimu naomba sana, tunahitaji sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tujielekeze huko, lakini vilevile katika jamii nzima kuhakikisha kwamba jamii na sisi kama wadau tunashiriki katika kuwajenga vizuri kimaadili watoto wetu, lakini vilevile kuwapa elimu jinsi ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuligusia ni hususan katika upande wa dawa za kulevya, kuna intervention ama mkakati ambao unasaidia kupunguza athari kwa wagonjwa ambao wanatumia dawa za kulevya. Niseme jambo moja ambalo limeongelewa hapa, watumiaji wa dawa za kulevya sio vichaa, na watumiaji wa dawa za kulevya sio wahalifu na hawapaswi kuwekwa jela, ni watu ambao wanahitaji kupata msaada wa tiba na magereza sio sehemu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwatia moyo, tumeipiga vita na baadhi nimesikia ni maneno yapo ya kupiga vita sober houses, hatuhitaji kupiga vita sober houses, tunahitaji kuziboresha kuwasaidia na kuzisimamia na kuziratibu. Lakini vilevile Serikali iongeze nguvu kuhakikisha kwamba tuna rehabilitation center yetu ambayo tumekuwa tunaijenga pale Dodoma na tuliliongea hilo, Serikali iweke msukumo tuimalize ile pale. Watumiaji wa dawa za kulevya wasiwekwe Isanga ili sasa wawekwe kule wakapate tiba, wapate msaada wanaohitaji ili warudi katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashauri Waheshimiwa Wabunge maana yake na mimi nasoma kwenye mitandano na magazeti, kutoka katika dawa za kulevya sio shughuli ndogo. Ni sawasawa na huyu ambaye anatumia sigara, kuna mwingine anaweza akaacha papo kwa papo, lakini kuna wengine wanaweza wakachukua hata miaka mitano; anaingia, anatoka, anaingia anatoka. Wanahitaji msaada mkubwa sana badala ya kuwanyanyapaa tuwasaidie waweze kurudi kwenye mstari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na niokoe muda wako, nishukuru, mapendekezo yetu tumeyatoa na tumeyatoa kwa kirefu sana. Niombe sana Serikali ijaribu kuzingatia ili tutakapokutana tena katika Kamati basi itupe mrejesho wametekeleza kwa kiasi gani na wapi wamekwama na kiasi gani wamekwama ili na sisi kama Kamati ya Bunge ambayo inasimamia suala hili tuweze kutoa na kushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana kwa kunipa fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nitoe hoja kwamba yale mapendekezo ambayo tumetoa kupitia katika taarifa yetu yaweze kupokelewa na kufanyiwa kazi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi kwa rehema yako kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kuta hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Katika kipindi hiki cha utendaji wa kazi nikiwa kama Naibu Waziri nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Shukurani za pekee kabisa nazielekeza kwa Mheshimiwa Dkt. Ummy Mwalimu namuita daktari, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ujuzi wake na ubobezi katika sekta ya afya na kwa ushirikianoa ambao amenipa katika kutkeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha napenda kuwashukuru Makatibu Wakuu Dkt. Mpoki Ulisubisya pamoja na Sihaba Nkinga kwa mchango wao kwa kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Vilevile nawashukuru Profesa Mohamed Bakari - Mganga Mkuu wa Serikali, na pia nachukua fursa hii kuwashukuru watendaji wa wizara taasisi za Wizara pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati; Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile natoa shukurani zangu kwa ushirikiano ambao wameendelea kutupa katika sekta ya afya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii na wananchi wote kwa ushirikiano.

Mwisho natoa shukurani zangu za dhati kwa watoa huduma wote katika sekta ya afya kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuitoa na uzalendo wao. Sifa tunazipata sisi Mawaziri lakini kazi kubwa zinafanyika huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge na la kwanza nitajiekeza katika hoja ambazo Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na masuala ya miundombinu katika sekta ya afya. Serikali imekuwa inafanya kazi kubwa sana kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa mujibu wa Mpango wetu wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ambapo zinaelezea kwamba kila kijiji kitakuwa na zahanati na kila kata itakuwa na kituo cha afya. Tumeboresha kwa kiasi kikubwa sana vituo vya afya na Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani mtakuwa mashuhuda kwamba vituo vingi vya sasa hivi vimeboresha, zaidi 208 .

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya TAMISEMI ambayo tumeipitisha hivi karibuni tumesema kwamba tutajenga Hospitali za Wilaya 67; katika mapendekezo ambayo tunaleta katika Bunge lako tukufu hili baada ya Serikali kutukabidhi Hospitali za Rufaa za Mikoa tutaanza ujenzi wa hospitali sita za rufaa za mikoa pamoja na kuboresha hopsitali nyingine za rufaa katika maeneo ya afya ya mama, mtoto na huduma za dharura. Kwa hiyo, tumeendelea pamoja na hilo kuboresha huduma mbalimbali katika Hospitali zetu za Kikanda, Hospitali zetu Maalum na Hospitali za Rufaa za Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na kuboresha masuala ya miundombinu tumejielekeza katika kuboresha ubora wa huduma za afya. Moja ya jambo ambalo tumeweza kulifanya kama Serikali ni kuanzisha mfumo wa star rating ambao unaweka viwango vya ubora katika utoaji wa huduma na kwa kiasi kikubwa tumeweza kufanikiwa sana. Tuliweza kufanya tathimini ya awali ambapo zaidi ya asilimia 33 ya vituo vya kutoa huduma ya afya vilikuwa na viwango vya nyota sifuri; lakini baada ya kuja kufanya tathimini na maboresho makubwa viwango vile vimepungua sna kwenda chini ya asilimia 10 ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaka tujielekeze zaidi kwenda mbali zaidi, tutatoa viwango vya ubora katika utoaji huduma. Sambasamba na hilo tunataka tuanzishe utaratibu wa kutoa leseni kwa vituo vyetu vya utoaji huduma vya afya ambavyo sasa badala mtu kuwa kutoa huduma tu pasipokuwa na kuzingatia viwango vya ubora tutaanza kutoa leseni na leseni hii inahuishwa na viwango vya ubora ambavyo anavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo iliibuka kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba ni nani mwenye mamlaka ya kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati. Niseme tu, kwa mujibu wa instrument tuliyo nayo Wizara ya Afya ndio mamlaka pekee ambayo ina mamlaka kisheria ya kupandisha hadhi zahanati na vituo vya afya; na hii inaendana sambamba kabisa na majukumu ambayo Wizara ya Afya inayo. Wizara ya Afya itasimamia sera, masuala yote ya viwango na miongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Wizara ya Afya itasimamia Wizara zote za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali za Taifa. Wenzetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI majukumu yao ni kusimamia utekelezaji wa sera, viwango na miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya, lakini sambamba na hilo watasimamia Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya; huo ndio mgawanyo wa majukumu ambao tunao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kidogo katika suala la dawa, na hoja zimekuwepo nyingi na Waheshimiwa Wabunge wamechangia sana. Niseme tu kwamba katika awamu hii ya tano bajeti ya dawa imeongezeka kutoka bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufika bilioni 269 katika mwaka huu wa fedha na mwakani tutakuwa na bilioni 270. Tumekwenda mbali zaidi kuimarisha mifumo yetu, takribani kama wiki tatu/nne tulikuwa tunazindua magari mapya 181, na mfumo ambao tunautumia ni kuhakikisha kwamba dawa tunazipeleka mpaka katika kituo cha kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo tumeweka mwongozo wa utoaji wa huduma na hili nilitaka nilisisitize. Tumeweka mwongozo wa kutoa huduma za afya za dawa, tunasema dawa gani itatolewa wapi kwa ngazi gani kwa ugonjwa gani. Kwa sababu tulikuwa tunapata changamoto katika hospitali kubwa kwamba kampuni za dawa zilikuwa zinaenda kwa watoa huduma, wanawaambia andika dawa hii na utakapokuwa umeandika dawa hii ikawa inanunuliwa kwa wingi na sisi tutakuwa tunakupa commission. Na hii wakati ikasababisha zile dawa zisiwe zinapatikana pale kwa sababu tu wale wafanyabiashara walikuwa ndio wanatoa mwongozo wa jinsi gani ya dawa kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tumeweka mwongozo wa kutoa dawa ambao sasa utatoa mwongozo dawa gani inatumika wapi na katika aina gani ya ugonjwa. Lakini sambamba na hilo, tumekwenda mbali kuweka label katika dawa zetu. Kwa hiyo, ninaamini mifumo hii ambayo tunaendelea kuiboresha itahakikisha kwamba dawa tunazipata kwa kiasi cha kutosha. Hata hivyo nitoe rai, na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wengi wameniuliza mbona dawa fulani haipatikani. Kuna dawa zipo katika ngazi tofauti tofauti, hatutegemei tukakuta dawa kwa mfano insulin katika zahanati, hatuwezi tukazikuta zile. Zile dawa ziko katika ngazi tofauti kwa sababu dawa zile zinategemea na aina ya utaalam ya wale ambao wanatakiwa kuzitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunatambua kwamba magonjwa yasiyoambukizwa yanazidi kuongezeka na sisi tutakuwa tunapitia miongozo yetu mara kwa mara kuangalia wapi tunahitaji kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuja na hoja nyingine ya masuala ya CT Scan na MRI katika hospitali za Rufaa za Mikoa. Kwa sasa hivi kwa mujibu wa miongozo yetu, huduma hizi haziwezi zikapatikana katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Ngazi ambazo CT Scan na MRI zinaweza zikaanzia, kwa mujibu wa miongozo yetu ni katika ngazi ya Rufaa za Kanda. Hata hivyo kadri nchi yetu inavyozidi kuongezeka na huduma zinazidi kuboreshwa tutafanya mapitio kuangalia kama tunaweza sasa tukaruhusu teknolojia hizi zikaweza kutumika katika ngazi hii kwa sababu changamoto hii si suala tu la kuwa na vifaa hivi ni suala vilevile kuwa na wataalam ambao wanaweza kusimamia vifaa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lilikuwa ni suala la rasilimali watu. Tunakiri kwamba tumekuwa na changamoto kubwa ya rasilimali watu na nimshukuru sana Mheshimiwa Mkuchika, ameainisha vizuri sana kwamba katika mgao utakaokuja na sisi tutapata mgao katika watumishi wa afya. Naamini katika hili litatusaidia sana kupunguza changamoto ya watumishi ambayo tunayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo lilikuwa limeongelewa na hili nataka niwapongeze watoa huduma kwa kweli kwa kiasi kikubwa sana, kelele za wananchi kuhusu utoaji wa huduma zimepungua sana. Lugha za matusi na masuala ya rushwa kwa watumishi wa afya tumepunguza sana; na hii niwashukuru sana na kuyapongeza mabaraza ya kitaaluma na maadili ambayo yako chini ya Wizara ya Afya. Tumezidi kuyaboresha na tumeendelea kuhakikisha kwamba tunafanya mabadiliko ya kisheria kuhakikisha kwamba taaluma hizi tunazisimamia vizuri. Moja ya mikakati ambayo tumeiweka ni kuhakikisha kwamba sasa kada zetu zote tunatoa leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, msije mkashangaa, tumepitisha Sheria ya Madaktari ambayo itahitaji hata mimi Naibu Waziri ambaye nimesimama hapa ni daktari, baada ya muda mtakuwa na mimi mnaniona dispensary pale natoa huduma au Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuhakikisha kwamba tunapata mafunzo endelevu kuhakikisha kwamba na mimi ili niendelee kuitwa daktari na ku-practice kama daktari ninakuwa na leseni yangu na ninapata mafunzo endelevu na yote hii ni mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wanakuwa… muda umekwisha?

NAIBU SPIKA: Endelea.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze sasa katika ngazi ya maendeleo ya jamii. Kuna hoja kama mbili/tatu ambazo nazo ziligusiwa sana na Waheshimiwa Wabunge na moja lilikuwa suala la NGO’s, kwamba kuna NGO’s nyingi hapa nchini. Nyingi ni NGO za Kimataifa lakini zimejisajili kama NGO za hapa nchini. Sambamba na hilo kuna fedha nyingi ambazo zinakuja kwenye NGOs na hazijulikani zinakwenda wapi. Tatu, ilikuwa ni kwamba kuna baadhi ya NGO’s zimekiuka majukumu yao ya kikatiba na kuanza kujiingiza katika mambo mengine ikiwa ni pamoja na siasa.

MheshimiwaNaibu Spika, kupitia idara yetu ya NGO tumefanya tathmini ya NGOs zote, kuangalia usajili wao, kuangalia mifumo yao ya fedha, kuangalia wanafanya shughuli gani, kuangalia kama je wanawasilisha taarifa muhimu zote ambazo zinatakiwa kwa mujibu wa sheria na tumekuta NGOs nyingi ambazo zimekuwa zinakiuka masharti haya na baadhi tumeshazifuta na nyingine zimepewa maonyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumewekeza nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba sasa tunazisimamia vizuri hizi NGOs ili ziweze kutimiza majukumu yake. Hatuna shida na NGO’s; ni wadau wakubwa sana wa Serikali na sisi kama Serikali tuna-appreciate sana kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la mwisho ambalo nilitaka nigusie lilikuwa ni suala la wazee. Sisi kama Serikali kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007 tunatambua umuhimu wa wazee na katika sera yetu imesema kwamba wazee watapewa matibabu bure. Mheshimiwa Waziri amekuwa kinara katika hili kuhakikisha kwamba tunatenga madirisha ya wazee na wazee wetu wanapata vitambulisho vya kuweza kuwatambua na kuweza kupata matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba tumekuwa na changamoto kidogo katika utekelezaji wa hili, lakini na sisi tutaongeza juhudi zaidi kuhakikisha kwamba tunasimamia kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuja hoja ambayo ilikuwa raised hapa kuhusiana na Sheria ya Wazee. Tuna Sera ya Wazee ya mwaka 2003, sasa hivi tunaifanyia mapitio na baada ya hapo tutaileta kwa ajili ya kuleta hiyo rasimu ya sheria ili iendane na mazingira ya sasa ya hali ya wazee tuliokuwa nao hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, mimi nikushukuru sana na niwashukuru watoa hoja wote kwa michango mizuri ambayo wameweza kuitoa katika bajeti yetu. Sisi tunaamini kwamba michango hii itatusaidia sana kuboresha utendaji wetu wa kazi. Nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika maeneo mawili ambayo yaligusiwa na wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni mabadiliko ya kisheria, kuna sheria mbili ambazo tunatarajia kuzileta Bungeni kwa mara ya kwanza. Tunatambua kumekuwa na changamoto katika ugharamiaji wa matibabu na hivyo kama Serikali tunakusudia kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tunatambua vilevile katika kufikia malengo ya 90-90-90 kwa maana ya asilimia 90 ya watu wote ambao wanaishi na Virusi vya UKIMWI tuweze kuwafikia na kuwapima, asilimia 90 ya wale ambao wamepimwa waweze kupata matibabu na asilimia 90 ya wale ambao watapata matibabu tuweze kufubaza kabisa Virusi vya UKIMWI, tumeona kwamba kumekuwa na changamoto hususani katika kundi la vijana na wanaume, hivyo tunataka kuja na mabadiliko ya sheria ili kuruhusu upimaji binafsi lakini vilevile kushusha umri wa upimaji kufikia miaka 15. Taratibu zote za mabadiliko haya ya sheria yako katika ngazi mbalimbali ndani ya Serikali na pindi taratibu hizi zitakapokamilika Miswada hii italetwa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo liligusiwa na wachangiaji ni kuhusiana na hali ya magonjwa nchini. Kwa muda mrefu tumekuwa tunapambana na magonjwa ya kuambukiza lakini sasa hivi tumeanza kuona ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa kwa maana ya kisukari, pressure, kiharusi na magonjwa ya figo. Sisi kama Serikali tumeona tunahitaji tuanze kujipanga upya, hivyo tunataka tuangalie mtiririko mzima wa huduma za afya kama alivyokuwa ameongelea Mheshimiwa Mukasa kuangalia masuala ya elimu, kinga, tiba na huduma ya utengamao. Awali tulikuwa tumejikita sana katika masuala ya tiba tukaacha haya maeneo mengine. Ili sasa tuweze kupambana vizuri na magonjwa yasiyoambukiza tunahitaji tuhakikishe kwamba huu mtiririko mzima tunauzingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya tuko katika hatua za mwisho kuanzisha Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yasiyoambukiza kama ilivyo kwa magonjwa ya UKIMWI, TB na Malaria. Tunataka tuje na Mpango wa Magonjwa Yasiyoambukiza ili tuweze kuwa na utaratibu mzuri wa kudhibiti magonjwa haya. Tutaweka utaratibu ambao utaanzia katika ngazi ya Taifa mpaka ngazi za kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa nami nichangie katika bajeti kuu. Nianze kwa kusema kwamba kauli mbiu ya bajeti hii naikubali ambayo imelenga kuongeza uzalishaji viwandani na kupanua fursa kwa ajira. Niseme tu kwamba nasi kama Jimbo la Kigamboni tumeshajipanga vizuri, tayari tumeshapima ekari 1,000 na tumetoa viwanja vipatavyo 461 vya viwanda ambavyo viko tayari kwa uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niseme tu kwamba bajeti hii mwelekeo wake ni mzuri, kutoka asilimia 26 mpaka asilimia 40 ya fedha za ndani kutengwa katika kuelekea katika bajeti ya maendeleo, ni jambo jema. Jambo jema lingine ni kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto ambazo nami naziona. Pamoja na juhudi ambazo zinaendelea za kuongeza ukusanyaji wa kodi za ndani, bado tuna changamoto ya wigo wa kukusanya kodi, kwa maana ya tax base, hilo bado ni tatizo kubwa sana. Bado naona tunaendelea kuvikamua vyanzo vile vile ambavyo tumekuwa tunavitumia siku zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kwamba sasa hivi inabidi tuangalie na vyanzo vingine. Sekta ya Kilimo, Uvuvi pamoja na Utalii vinaweza vikachangia kwa kiasi kikubwa. Tuweke pesa ili tupate pesa. Kwa hiyo, nataka kuishauri Serikali ijaribu sasa kuangalia vyanzo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kushauri ni kuhusiana na matumizi makubwa ndani ya Serikali. Tunaziona juhudi ambazo mnazifanya katika kupunguza matumizi ya Serikali. Asilimia 49.5 ya mapato ya ndani yote yanaenda kwenye mishahara. Hii ni gharama kubwa sana. Ni lazima sasa mwangalie upya ndani ya Serikali, kuangalia reforms za kuboresha ufanisi lakini na kupunguza gharama ambazo zinaingia katika masuala ya mshahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuangalie tena maeneo mengine ambayo tunaweza tukapunguza matumizi makubwa. Katika eneo la ununuzi wa magari, matumizi ya magari ya Serikali bado ni mbovu. Tunayanunua magari kwa gharama kubwa. Ni muda muafaka sasa kuweka sera nzuri ya ununuzi, matumizi na matengenezo ya magari ya Serikali; yanatumia gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni ushirikishwaji wa sekta binafsi. Tuna Sheria nzuri ya PPP na sera nzuri sana ya PPP; lakini ukiangalia katika hotuba hii ya bajeti kwa kiasi kikubwa sana, miradi yote mikubwa tunategemea sana Serikali kwenda kukopa fedha kwa ajili ya kuendesha hiyo miradi. Kwa nini tusi-engage sekta binafsi tuka-freeup some resources kwa ajili ya huduma nyingine za jamii kama afya, elimu na maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali ijaribu kuangalia hii, miradi mingine kuna watu wana fedha zao, tuwashirikishe ili hizo fedha nyingine tuweze kuziokoa kwa ajili ya mambo mengine katika huduma za jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilikuwa nataka kuchangia ni concern. Sisi kama Bunge jukumu letu ni kupitisha bajeti ya Serikali. Nilipokuwa nasoma hotuba ya Kamati ya Bajeti, imenishtusha kidogo kuona kwamba Serikali inatumia fedha kupita kile kiwango ambacho kimeidhinishwa na Bunge, hilo ni kosa. Tuanze sasa kujenga msingi wa Serikali kuheshimu maazimio na zile idhini ambazo zimepitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupeleka fedha asilimia 140, 120, 150 zaidi ya zile zilizopitishwa na Bunge bila kuleta maombi hayo Bungeni ni kuvunja sheria na kuvunja Katiba. Kwa hiyo, lazima sasa tufike mahali turudi kwenye ile misingi ya matumizi ya fedha ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali izingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulichangia ni hususan ushirikishwaji wa Kamati ya Bajeti. Kamati ya Bajeti inafanya kazi kwa niaba ya Bunge. Serikali ione kuwa, wanapofanya kazi na Kamati ya Bajeti, wanafanya kazi na Bunge. Ni muhimu sana wakawashirikisha. Bajeti itakuwa nyepesi kama Kamati ya Bajeti itakuwa imeridhia kwa niaba yetu sisi. Sasa Serikali inapokuwa inaleta bajeti na vitu vingine havijapitishwa katika Kamati ya Bajeti mnaifanya kazi ya kujadili na kupitisha bajeti inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, Bunge linaweza likawa rafiki pale mnapokuwa mnatoa ushirikiano kwa Bunge, lakini kazi inaweza ikawa ngumu pale mnapokuwa hamuwashirikishi Wabunge kikamilifu. Sasa nawaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, msiwaone Kamati ya Bajeti kwamba wale ni maadui, wale ni marafiki zenu na wako pale kwa niaba yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema, nami nataka kugusa suala la kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge na nataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha naye ajaribu kunisaidia, nini hasa lengo la kuiweka hoja hii katika bajeti yake? Kwa sababu Bunge letu hili ndiyo limeanza 2015 litakwisha 2020; unapoliweka hili suala la kukata kodi katika kiinua mgongo, lengo lake ni nini? Ama ilikuwa kama hivyo alivyokuwa anasema Mheshimiwa Kangi Lugola, kuwa-beep Waheshimiwa Wabunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, huwezi ukaleta usawa katika kupofua wenzako. Kama kuna watu vipofu nawe ukawapofua wengine ili wote tuwe sawa, nadhani hiyo siyo mantiki sahihi. Suala kubwa la msingi hapa, kama tunaongelea masuala ya kiinua mgongo, lets cut across board. We should not single out a single group. Kwa hiyo, hili nataka niliseme kwa Mheshimiwa Waziri ili liweze kueleweka. Maana yake unapokuwa na single out a single group, inaleta mashaka kuhusu dhamira ya lengo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika Azimio hili, kuhusiana na Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Madawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu umekuja umechelewa lakini ni mkataba ambao ni muhimu sana. Kama walivyotangulia kusema wenzangu michezo ni afya, michezo ni ajira, michezo ni mahusiano na michezo inajenga undugu na amani. Katika dhana hii ya michezo kumekuwa na tatizo kubwa tena kubwa sana kuhusiana na baadhi ya washindani kutaka kupata ubora ama ushindi katika njia za mkato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi katika dunia ambao wanafuatilia vyombo vya habari watakuwa wanajua wanariadha wa Kenya ambao wamekuwa wanasifika sana duniani wamepata kashfa ya matumizi ya madawa ya kulevya. Vilevile kwa upande wa Urusi maabara ambazo zimekuwa zinapima matumizi ya madawa ya kulevya nazo zimeingia matatani. Mara nyingi nchi ambazo zinapata matatizo haya huwa zinakosa sifa na zile ambazo zimekuwa zimejengeka kwa muda mrefu kuhusiana na washindani wao na inatia mashaka kuhusiana na wanariadha wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Daktari athari za madawa ya kulevya ni kubwa sana, wachangiaji waliopita wamezisema, siyo tu kwa kipindi kile ambapo wanariadha wanashiriki katika michezo lakini hata baada ya miaka kumi, ishirini, thelathini baada ya kuacha kutumia madawa haya watu bado wana athari za kimwili, kisaikolojia na kiakili. Kwa hiyo, mkataba huu umechelewa na naunga mkono tuuridhie na nitawaomba Waheshimiwa Wabunge wote na sisi tuukubali kwa sababu una manufaa makubwa sana katika suala zima la michezo katika nchi yetu. Hata hivyo, wakati tunaelekea kuuridhia mkataba huu nitaomba tu vile vile tuangalie katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja; tuhakikishe kwamba tunatoa elimu ya kutosha kuhusiana na hivi vitu ambavyo ama madawa ama zile njia ambazo zimedhibitiwa katika mkataba huu; sio kila mwanamichezo anaelewa hili na siyo mamlaka zote zinaelewa hili. Kwa hiyo, tujikite zaidi kupitia Wizara husika kuhakikisha kwamba tunajenga, tunatoa elimu ya kutosha kwa wanamichezo vilevile katika mamlaka mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; tujenge uwezo wetu wa ndani wa kuweza kubaini matumizi ya madawa haya; maana yake ni kwamba sasa tuwe na maabara zetu, zitasajiliwa na ambazo zitakuwa zinatumika katika mashindano yetu ya ndani tuwe na uwezo wa kuweza kubaini baadhi ya matumizi haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo naliomba ni kutoa elimu vilevile kwa Madaktari wa michezo. Inawezekana mtu akapewa dawa pasipo kujua dawa hii inakuwa na athari ama inaweza kuwa ni stimulants ama ikawa na madhara ama ikawa ni sehemu ya yale madawa yasiyoruhusiwa na mtu ameitoa tu. Kuna madawa kwa mfano, kuna dawa zingine tu za mafua ambazo mtu akipewa zinakatazwa kwa mujibu wa mkataba huo. Kwa hiyo, nataka tutoe hii elimu kwa Madaktari wa michezo, lakini sasa tuwe na mtatibu wa kusajili Madaktari wa michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nami naunga mkono hoja hii ya kuridhia Mkataba huu, umechelewa kuja, lakini ni Mkataba muhimu sana katika ushiriki wa Tanzania katika masuala ya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia, na kama itakupendeza ntaomba dakika zangu mbili nimpatie Mheshimiwa Zitto Kabwe aweze kuendelea nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa uwasilishaji wa taarifa nzuri ambayo imesheheni mambo makubwa ya msingi. Nitajielekeza moja kwa moja katika suala la Mji mpya wa Kigamboni. Katika ukurasa wa sita wa taarifa hii Kamati hii ya Bunge ilitembelea Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni na naomba ninukuu walichokisema:-
“Kamati ilifanya ziara katika Ofisi ya Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni tarehe 18 Machi, 2016 na kupokea taarifa kuhusu maendeleo ya mradi. Kamati haikuridhishwa na hatua ya Serikali katika utekelezaji wa mradi huu na hadi wakati Kamati inapokea taarifa za utekelezaji wa miradi hakukuwa na fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya uendelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kulipa fidia katika maeneo yatakayojengwa miundombinu.
Kutokana na hali hii hakukuwa na mradi wowote ulioonekana kuanzishwa na hivyo kupoteza maana halisi ya kuwa na mradi na uanzishwaji wa Wakala. Hali hii imesababisha Serikali kupoteza fedha za kulipia pango za wakala na kuwa na watendaji ambao hawana majukumu ya kutekeleza. Kamati inashauri Serikali iachane na mradi huu kwa kuwa umechukua muda mrefu bila kuwa na utekelezaji wowote.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naunga mkono hoja hii, ni mwaka wa tisa tangu Serikali itoe azimio la kujenga Mji wa Kigamboni. Hadi hivi sasa wananchi wa Kigamboni hawawezi wakajenga wala wakauza ardhi yao wala kuiendeleza, inawaletea umaskini mkubwa sana. Nami naunga mkono ripoti ya Kamati. Katika mwaka wa jana wa fedha Serikali haikutoa hata senti tano na wala hivi tunavyoongea hakuna hata senti tano ya fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana niliitisha mikutano ya wadau wa Kigamboni, Wenyeviti wangu wote wa Serikali za Mtaa, Madiwani na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Temeke kabla halijavunjwa na tukatoka na azimio kwamba moja, KDA ivunjwe na mamlaka yake yakabidhiwe katika Halmashauri mpya ya Kigamboni.
Pili, suala zima la uendelezaji wa Kigamboni sasa kwa kuwa Kigamboni sasa hivi ni wilaya inayojitegemea, ni halmashauri inayojitegemea, ina Idara ya Mipango Miji ambayo ina sifa na vigezo vya kusimamia uendelezaji wa Kigamboni; muda wa miaka tisa umetosha sasa tunaomba sisi kama Wanakigamboni tuivunje KDA na shughuli zote zikabidhiwe katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaliomba sasa Waheshimiwa Wabunge hili nalo, pamoja na kwamba mmelitoa kwenye preamble, naomba liingie kama azimio ili sasa Serikali itoe msukumo zaidi, pamoja na mapendekezo ambayo tumeyaleta sisi kama Wanakigamboni hili sasa liwe ni azimio la Bunge ili sasa baada ya hapo Serikali iweze kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi ya kusema, naomba niishie hapo. Nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa ya kwanza ya kuwa mchangiaji katika hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri Mheshimiwa William Lukuvi, Naibu Waziri Mheshimiwa Angeline Mabula, Katibu Mkuu Dkt. Kayandabila na safu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika Wizara ya Ardhi. Kwa mara ya kwanza nitaanza kuiongelea vizuri Wizara ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitano ambayo nimekuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sijawahi kuunga mkono bajeti ya Wizara ya Ardhi, inawezekana leo ikawa ndiyo mara yangu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la kwanza ambalo nilitaka niligusie ni suala la premium. Mheshimiwa Waziri ameongea katika hotuba yake kwamba amepunguza premium kutoka 7.5 percent kwenda asilimia 2.5. Tunatoa pongezi nyingi sana kwa Serikali, lakini bado tunaamini kwamba kiwango hiki bado ni kikubwa sana. Waende wakaliangalie tena. Katika suala la mashamba makubwa ambayo wamekuwa wanayahimiza wananchi wayapime, kikwazo kimoja cha kupanga Miji na upimaji imekuwa ni premium. Kwa hiyo, naomba waende wakaiangalie upya ili kama ikiwezekana tuipunguze zaidi na itatoa hamasa kwa wananchi kupima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni viwango vya land rents; kodi za ardhi nazo bado kuna wakati walipandisha, nadhani sasa wamefanya marekebisho. Suala hapa siyo kupandisha viwango, suala hapa ni kuhamasisha wananchi waweze kuwa wanalipia. Tukiongeza viwango vikawa vikubwa sana, ulipaji nao utakuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nataka sana Wizara nayo itusaidie, asilimia 30 ya mapato yale ya land rent yanayotakiwa kurudishwa katika Halmashauri, mpaka wakati tunatengana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tulikuwa tunaidai Wizara ya Ardhi takribani Sh.3,000,000,000/=. Ni fedha nyingi sana ambazo zingeweza kutusaidia katika maendeleo ya Halmashauri zetu. Sasa nadhani ifike mahali kama inashindikana fedha ile kwenda na wao wakaturejeshea 30 percent, kwa nini sasa tusipitishe sheria tufanye mabadiliko tu-retain ile 30 percent na sisi tuwapatieni ile hela nyingine iliyobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nataka kuligusia ni master plan ya Mkoa wa Dar es Salaam. Dar es Salaam inakuwa kwa kasi kubwa sana, lakini utengenezaji wa master plan umekuwa unakwenda muda mrefu sana. Nimeona katika ripoti yao wanaongelea mwezi Agosti, naamini Agosti itakuja nayo itakwisha. Tungependa kuona ifikapo mwisho wa mwaka huu tuwe na master plan ya Dar es Salaam, ujenzi holela unatapakaa kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ambalo ninataka kuligusia ni mradi wa viwanja 20,000 katika Jimbo langu la Kigamboni, hususan katika eneo la Kibada. Wananchi walionunua viwanja vile, walilipa premium ambayo inaendana na utengenezaji wa miundombinu. Mpaka sasa hivi tunavyoongea kuna wananchi wa Kibada wanaelea, kuna viwanja wamewapa kwenye mabonde, sasa hivi kuna wananchi wa Kibada wanashindwa kufika majumbani kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kibada hawana miundombinu ya kufika katika makazi yao na nitamwomba sana Mheshimiwa Waziri baada ya bajeti yake twende Kibada akawaone wananchi wale ambao walilipa fedha na wanalipa kodi ya ardhi, wanaishi kwa shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo nataka kuliongelea ni suala la Kigamboni. Serikali ilikuja na mpango wa Kigamboni mwaka 2008 tunavyoongelea sasa hivi ni mwaka wa tisa, wananchi wale hawajengi, hawakarabati, hawauzi wala hawakopesheki. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri tangu ameingia katika Wizara ile, tumeweza kufanya kazi kubwa sana mimi na yeye na namshukuru sana chini ya uongozi wake, yale ambayo wananchi wa Kigamboni tuliyokuwa tumesimamia, ameweza kuyasimamia na kuyatekeleza kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana yeye na safu nzima ya Wizara yake. Hatua tuliyofikia ni nzuri sana na ndiyo maana mnaona Mbunge wa Kigamboni sasa hivi ametulia, la sivyo siku za nyuma hapa pangekuwa hapatoshi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna lile ombi ambalo tumeleta kwenu Serikalini na ambalo nashukuru Mheshimiwa Waziri ameligusia kwa kidogo. Kuwepo mamlaka mbili za kupanga mji inaleta kero na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuvunja CDA. Sisi pia sasa
tunasema KDA hatuitaki. Tunaomba mradi ule uletwe chini ya Halmashauri mpya, chini ya uongozi mpya wa Kigamboni ili sisi wenyewe tukausimamie. Mheshimiwa Waziri akiweza kulitekeleza hilo, tutakuwa marafiki wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, machache nakushukuru sana na kwa mara ya kwanza naunga mkono bajeti ya Wizara ya Ardhi. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kupata fursa ya kuchangia, lakini nianze kwa kusema kwamba nilitarajia kwamba schedule of amendments ya muswada unaohusu Chief Government Chemist Authority uwepo hapa ili na sisi tuweze kukaa na kupitia kuona yale marekebisho ambayo Serikali imeyafanya kupitia Kamati ambazo tulikuwa tumekaa imezingatiwa. Sasa niiombe Serikali watusaidie kupata amendments ili sasa na sisi tuweze kufuatilia kuangalia kwamba yale tuliyokuwa tumeyasema yameweza kufanyiwa kazi, hilo lilikuwa la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Chief Government Chemist kwa kuja na huu muswada na nina amini umekuja katika muda muafaka sana hususani wakati fani hii ya kemia inazidi kukua. Niseme tu kwamba ni mdau na ni mjumbe katika kamati ya huduma ya Jamii na Maendeleo ya Jamii. Ni kweli kabisa kwamba Chief Government Chemist alikuwa anadandia katika sheria za watu wengine. Kwa hiyo, sasa hivi sheria hii inakuja katika muda muafaka kuanzisha amakuwa na sheria ambayo itakuwa inasimamia taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Vilevile itakuwa ni vizuri muswada huu mwingine ambao umekuja muda muafaka lakini vilevile umekuja sambamba na huu wa taasisi ni huu ambao unakuja sasa kuanza kusimamia taaluma ya wakemia nchini na hii ni hatua kubwa sana na ambayo kwa kweli tunataka tuipongeze sana Serikali na ukizingatia mkemia namba moja ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, naamini sheria hii itakapoanza baada ya yeye kusaini na ninyi mtamuomba ajisajili kama mwana taaluma katika fani hii ilikuendelea kuhamasisha fani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ni Mjumbe katika Kamati, mapendekezo yetu tuliyatoa katika taarifa ambayo niliisoma asubuhi. Kwa hiyo, nitaongelea mambo ya ujumla kwa sababu mapendekezo na ndio maana nilikuwa nataka kuiona schedule of amendments kama yanazingatia yale ambayo tuliyasema katika Kamati. Sasa kwa sababu hiyo schedule haipo hapa nitajikita katika maudhui tu ya jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ni ushauri wa ujumla na hii na yenyewe ni ka upande wa Serikali. Nadhani sasa hivi tunapokwenda huko mbele tujaribu kuangalia bodi badala ya kuwa ni za uteuzi tujaribu kuangalia kama tunaweza kutoa fursa watu wakaomba. Tuweke sifa na vigezo, tuwaachie Watanzania waombe; kuwe competitive na tuangalie watu kutegemeana na competency zao badala ya utaratibu wa sasa hivi ambao tunakwenda nao ili tuweze kupata watu wazuri katika hizi bodi ambazo wanaweza kutushauri katika taasisi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka niligusie ni kuhusiana na utendaji kazi wa taasisi hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Ni taasisi muhimu na taasisi nyeti sana, lakini ina mchango mkubwa sana hususani katika makosa ya jinai, na moja kati ya jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa sana ni ucheleweshaji na wazungu wanasema justice delayed is justice denied. Kwa hiyo, tuwaombe wenzetu waendelee kujipanga vizuri kuhakikisha kamba huduma hizi hususani katika vile vipimo ambavyo vinahusiana na kesi za jinai vinaharakishwa na kufanyika kwa haraka ili sasa wale ambao wanategemea haki kutokana na vipimo hivyo waweze kuvipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu katika hili ambalo nilikuwa nataka kushauri kwa sababu tuna maabara nyingi na tumesema maabara hii itakuwa ndio supreme and referral katika masuala ya uchunguzi. Ni muhimu sasa tukauhisha majukumu ya maabara hii na maabara nyingine ambazo zipo chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali zikawa na mahusiano pamoja na mawasiliano na hususani hapa nilikuwa nalenga maabara nyingine kama za Jeshi la Polisi ambao nao wana forensic laboratory yao. Ni kuangalia jinsi gani ambapo wanaweza kufanya kazi kwa pamoja pasipo kuleta migongano, ni kuangalia ni jinsi gani wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na maabara ya TFDA, maabara za TBS, maabara nyingine za Wizara ya Maji na taasisi nyingine zote ambazo zina maabara ili kuleta ufanisi na kujenga mahusiano yaliyokuwa mema na kuondoa duplication katika kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine nilitaka kugusia ni masuala tu ambayo yapo katika jamii yetu. Sisi ambao tunaishi Dar es Salaam mboga nyingi zinalimwa katika Bonde la Mto Msimbazi na katika Bonde la Mto Msimbazi pale hatuna uhakika sana na usalama wa maji ambayo yanatumika kunyweshea zile mboga. Tulikuwa tunaiomba sana Serikali itutoe mashaka wana Dar es Salaam lakini watutoe mashaka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na wananchi kwa ujumla kwamba mboga tunazokula za kutoka Bonde la Msimbazi zipo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tumekuwa na changamoto hususani katika uhifadhi wa nafaka ndani ya maghala ya Taifa, lakini vilevile katika maghala ya watu binafsi, tumekuwa na changamoto kubwa sana kuhusiana na uhifadhi wa nafaka. Ni muhimu sana maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikawa proactive badala ya kuwa reactive kuhakikisha kwamba hizi nafaka ambazo zipo katika maghala yetu nazo zipo salama. Isijekuwa tunatoka kwenda kushuhudia matukio ama kushughulikia matukio wakati tungeweza kufanya kazi ya kuzuia matukio. (Makofi)
Mwisho mimi niipongeze Serikali sana, Mheshimiwa Ummy Mwalim, Mheshimiwa Dkt. Hamis Kigwangalla, Profesa Manyele, Mwenyekiti wa Bodi ya Mkemia Mkuu - Profesa David Ngasapa, mwalimu wangu kwa kazi kubwa sana ambayo wameifanya kuhakikisha kwamba miswada hii inakuja kwa muda muafaka, tunakuwa sasa na sheria ambayo itaisimamia chombo hiki, sheria mbayo itasimamia taaluma hii. Na nina hakika kabisa sheria hizi zikishapitishwa basi taasisi hii inaweza ikasimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie na sisi kama Wabunge tunaomba tuwaunge mkono taasisi hii na sisi kuhakikisha kwamba tunapigia debe waweze kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kuendesha taasisi hii. Nashukuru sana.