Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Devotha Methew Minja (1 total)

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, umekiri kwamba ni kweli Serikali inadaiwa, lakini umesema kwamba kuna dosari ambazo zimejitokeza katika uhakiki wa zoezi hilo na toka mwaka 2014/2015 – 2015/2016 ni muda mrefu. Serikali kwa nini haiwezi kuona kwamba kuna haja sasa ya kuharakisha zoezi hilo kama watu wanastahiki zao wakalipwa kwa maana hivi sasa ninavyozungumza ziko taarifa kwamba kuna baadhi ya mawakala hivi sasa wameuziwa nyumba zao, kuna baadhi ambao hivi sasa wanashindwa kusomesha watoto wao shule na kuna baadhi ya mawakala ambao wamefariki kwa mshituko baada ya kuona nyumba zao zinauzwa na mabenki. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kazi hii kama hawa watu mmewatambua na wamefanya kazi yao kwa uadilifi. Serikali kwenye hii Kamati ya kuandaa mawakala ilijumuisha Serikali wakiwemo wa TAKUKURU, Polisi, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya. Sioni ni kwa nini uhakiki wa namna hii na ucheleweshaji wa namna hii kwa hawa watu ambao wamefanya kazi yao kwa uadilifu. Mheshimiwa Waziri Mkuu umetoa commitment kwa mawakala hawa kwa siku….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Devotha Minja muda wako unakwisha naomba uulize swali sasa ili uweze kujibiwa.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Waziri Mkuu ulitoa siku 25 kwamba zoezi hili la uhakiki liwe limefanyika Tanzania nzima kwa mawakala zaidi ya 940. Ni kwa nini mpaka sasa kwa miaka hiyo toka mwaka 2014 watu hawa Serikali haitaki kuwalipa haki yao ya msingi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kupitia mazungumzo yetu kwa pamoja na mawakala wote tulitoa muda ambao tumejipanga kufanya uhakiki wa madeni yaliyobaki ili tuweke utaratibu wa kulipa na tarehe hiyo imeishia jana tarehe 31. Kwa hiyo, sasa nasubiri taarifa kutoka Halmashauri za Wilaya zote zitakazokusanywa kwenye ngazi ya Mikoa na Mikoa itatuletea takwimu na baada ya kupeleka Wizara ya Kilimo ikishapitia watapeleka Wizara ya Fedha na malipo hayo yatalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baadhi ya mawakala kwa mujibu wa mazungumzo yetu walieleza adha
hiyo ambayo wanaipata, lakini kupitia kauli hii wanasikia pia hata wale wadai kwamba, wale wote ambao watakuwa na madeni sahihi baada ya kuhakikiwa ni watu wema na ndio ambao pia tunajua tunatakiwa tuwalipe. Kwa hiyo, hakuna umuhimu wa kuharakisha kunyang’anya nyumba, na kufanya vitu vingine ni jambo la kuona kwamba taratibu hizi tunazozitumia ni taratibu ambazo zinaleta tija kwa Watanzania, zinaleta tija kwa Serikali kwa sababu tungeweza kupoteza mabilioni ya fedha ambayo yangeweza pia kusaidia kwenye miundombinu nyingine, lakini sasa tumebaini kwamba hayakuwa ya ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kutoa wito kwa watumishi wa Serikali wote ambao wamehusika katika hili ambao pia tutawabaini kwamba wao walihusika kwenye wizi, ubadhirifu na udanganyifu huo wote tutawachukulia hatua kali, hilo moja.

Pili, wale wote ambao wameshiriki katika hili, nirudie tena kuwahakikishia kwamba madeni hayo yakishathibitishwa kwamba fulani anadai kiasi fulani tutawalipa kama ambavyo tumetangaza, ahsante sana.