Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (20 total)

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka niseme nimesikitika sana kwa majibu yaliyotolewa na Serikali na nataka niwahakikishie Bunge lako kwamba wananchi wa Tarime hawatakubaliana na hali hii. Nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mhesimiwa Spika, katika sehemu ya kwanza ya majibu yaliyotolewa na Serikali, maeneo yote yaliyotajwa hapo, yalifanyiwa tathmini na mgodi wa North Mara na wakati fulani hivi baada ya tathmini, mgodi ulikwenda mbele zaidi kufyeka mazao ya wananchi na Mheshimiwa Spika kwa mujibu wa sheria ya madini, wananchi wanatakiwa wakae umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo uchimbaji unafanyika.

Mheshimiwa Spika, wakati wote wananchi walipofanyiwa tathmini wamezuiliwa kuendeleza maeneo yao, mashamba yao yameharibika, nyumba zimebomoka na nyingi zimebomoka kutokana na blasting inayofanywa na mgodi lakini naambiwa hapa kwamba hawatalipwa wakati walifanyiwa tathmini.
Sasa swali langu ni hili, ni kwa nini mgodi ulifanyia tathmini nyumba, maeneo na mazao ya watu na kuzuia kuyaendeleza na sasa inasema kwamba haiwezi kulipa wakati ilifanyia tathmini yaani evaluation?

Swali la pili, haya majibu ya kukurupuka yasiyo na research, Serikali imesema kwamba wanalipa kwa mujibu wa viwango na North Mara inalipa fidia kubwa kweli kuliko ya Serikali, sasa mimi nina cheque hapa mbili za wananchi wa Tarime waliolipwa na haya ni matusi!

Mheshimiwa Spika, Nyamakaya Mbusiro amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 3,871/= kama fidia ya shamba lake na nitawasilisha mezani kwako, cheque ya pili Chacha Muhabe Mwita amelipwa na Mgodi wa North Mara shilingi 7,273/= na ni nyingi mno, mashamba ya wananchi masikini. Nauli ya kutoka eneo la Nyamongo, Nyamwaga mpaka kufika Tarime Mjini ni shilingi 15,000/=.

Je, hii fidia ndiyo Serikali ya CCM inawaambia wananchi kwamba ni kubwa kuliko viwango ambavyo vinatakiwa kulipwa?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mambo ya fidia ya Nyamongo historia yake imeanza toka miaka ya 1980 na Mheshimiwa Mbunge atastaafu bado madeni yale yakiwepo. (Makofi)

Mimi mwenyewe nimekaa na wenyeji pale, kuna kitu kinaitwa ‘mtegesho’ na mtegesho umefanywa hata na wafanyakazi wa Serikali.

Kuna mtu anakuwa na nyumba, anamkaribisha mtu, watu wamejenga nyumba za thamani hata ya milioni 200 wakitegea mgodi uwalipe. Nimefanya vikao wakati ule na wenyeji wa Tarime, wenyewe baadaye wakasema hawa wenye mitegesho ndiyo wanakuja kuharibu taratibu za hayo malipo.

Kwa hiyo, hayo mashamba na hiyo ni kwamba tathmini ilifanyika na niliitisha kikao nikiwa na DC na wenyeji wananchi wa pale, nikaleta na wazee nikajaribu hata kuweka viongozi wa madhebu ya dini, Mheshimiwa Heche tumeongea naye nikasema baada ya Bunge suala la Nyamongo itabidi tuende tukae pale kama siku tano na itakuwa ya ukweli.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Heche asiondoke tutaenda, hayo mashamba saa zingine ni mtu anatafuta kaeneo, anaweka mimea usiku, asubuhi anataka tathmini ndiyo maana inakuja shilingi 3,000/=.

Kwa hiyo, kutatua tatizo la Nyamongo, itabidi mimi, Mheshimiwa Heche, DC, wale wananchi na viongozi wenyewe twende eneo moja baada ya lingine.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa lengo la saba la Maendeleo Endelevu ya Duniani ni kuwa na umeme nafuu wa uhakika, endelevu na wa kisasa kwa wananchi wote; na kwa kuwa sekta ya nishati ni sekta nyeti; uzalishaji wa umeme, usafirishaji wa umeme na usambazaji wa umeme, Serikali imefikia hatua gani ya kuhakikisha uzalishaji na usambazaji unakuwa na ubia; na usafirishaji ukamilikiwa na Serikali ili effectiveness katika upatikanaji wa nishati uweze ukawa kwa wote?
Pili, kwa kuwa Kata zilizotajwa kwenye Jimbo la Kibamba, matatizo yake ni sawa sawa na Kata za Kahe Mashariki, Kahe Magharibi, Njia Panda Makuyuni katika Jimbo Vunjo, je, Serikali haiwezi ikaona kwa kuwa hili ni Bunge jipya, ikaleta mpango kazi wa usambazaji wa umeme kwa Majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima ili Wabunge waweze kupata ikawa ni rahisi kufuatilia katika Majimbo yao ya uchaguzi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza swali la usambazaji, siyo kwamba tuna mipango, tunayo miradi. Kwa hiyo, kwa sasa tunaongeza usambazaji wa umeme unaotokea Iringa kwenda Dodoma, Dodoma mpaka Mikoa ya Kaskazini Magharibi, tunatoka kwenye kilovoti 220 kwenda kilovoti 400.
Mheshimiwa Spika, nadhani waliosafiri kwenye hiyo barabara wameona nguzo zile za chuma kubwa, halafu tunajenga transmission line kutoka mpakani mwa Zambia kwenda mpaka Namanga, kutoka kilovoti 220 mpaka kilovoti 400. Ni kwa sababu tunaingia kwenye biashara ya kuuziana umeme kama inavyofanyika duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiwa pale Canada unaangalia wanauzia umeme Marekani Niagara Falls, ukiwa kule Iceland, Polland na nchi zote; kwa hiyo, Tanzania inayokuja ni ya umeme mwingi na wa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nije umeme wa bei nafuu. Ni kwamba kwa sasa hivi ukichukua umeme wote tulionao nchini, hata wa watu binafsi, hatuvuki megawati 1,500; lakini mimi nitachangia siku ya mwisho kuonyesha namna gani tunajenga viwanda vyenye umeme wa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, kama tunataka kuingia nchi ya kipato cha kati miaka 10 ijayo lazima tuwe na Megawati zaidi ya shilingi 10,000/=. Ndiyo maana nakaribisha hata nyie Wabunge kama mnataka kuwekeza kwenye umeme, njooni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bei ya umeme, wengine wanasema nilisema bei ishuke, haijashuka. Mheshimiwa Mbatia ni hivi nilisema tunapiga hesabu; hizi bei huwezi ukaongea kwenye majukwaa. Kwa hiyo, mategemeo yangu ni kwamba TANESCO na EWURA wanapiga hesabu, nitakaa nao. Umeme sasa hivi tunauziwa kwa senti 12 kwa unit moja. Tunataka kuushusha bei, lakini siyo kwenye majukwaa. Hesabu inapigwa na tarakimu mtazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile usambazaji wa umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam, katikati ya jiji, kwa mara ya kwanza kabisa tunataka kuachana na matatizo ya umeme. Nyaya zote zinapita chini ya ardhi. Ile ya TANESCO kufukuzana na magari kutafuta wapi nyaya zimeharibika tunataka kuachana nayo kuanzia mwezi wa Nne. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, station ile inatizamana na Hospital ya TMJ ambayo itakuwa inaangalia wapi kuna matatizo. Huo mradi nadhani Mkandarasi nimemwambia ikifika mwezi wa nne, mvua sijui miti imeangukia kule katikati ya Dar es Salaam tutaachana nayo.
Ndugu zangu wa Mbagala na Temeke, tunajenga transfoma kubwa sana ambayo itatatua matatizo ya usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mnyika kote tunatoa transfoma ambazo zilikuwa za kVA100, kwenda 200.
Kwa hiyo, miradi ndugu yangu ni mingi sana Mheshimiwa Mbunge, tukileta hapa, mimi nadhani tuonane huko huko, field mnaziona. Ahsante. (Makofi)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, tarehe 26 mwezi wa kwanza hapa Bungeni, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, alitoa Kauli kwamba wananchi wengine wanashindwa kupata haki ya malipo stahiki kutokana na kitendo alichoita utegeaji. Kwamba wananchi wengine wanapanda wakati ule wanasubiri kwamba waweze kulipwa kwa wakati unaofuata. Sasa kutokana na hicho lakini naamini kwamba Mheshimwa Waziri, anafahamu ya kwamba wananchi huwa wanalipwa kutokana na asilimia ya ukuaji wa mmea husika, kwa hiyo kama mtu amepanda mgomba stahiki ni 50 kama mmea huo umekuwa kwa asilimia 10 basi utalipwa kwa asilimia hiyo 10. Je, kutokana na kauli hiyo ya Mheshimiwa Waziri, haoni kwamba Wizara hiyo itakuwa inashirikiana na migodi hiyo katika maeneo hayo ambako madini yanapatikana ili kuweza kuwanyima wananchi malipo stahiki kutokana na kazi yao katika maeneo yao husika?
Vilevile swali la pili, Geita ni sehemu ambayo inazungukwa na dhahabu kwa kiasi kikubwa, lakini katika maeneo mengine ambayo yameshalipwa fidia wananchi wamelipwa milioni moja na nusu kwa eka nzima, kwa maana ya fidia ya ardhi katika lile eneo. Lakini ukiangalia kwa maana ya wale wananchi hao hao wa Halmashauri hiyo ya Mji wa Geita, walipewa tena na Serikali kwa kuuziwa ardhi na kiwanja cha ishirini…
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, najenga hoja. Kwa maana ya 25 kwa 30, wananchi hawa waliweza kununua eneo hilo hilo kwa milioni tatu. Maana yake ni kwamba ile milioni moja na nusu ambayo walilipwa haikuweza hata kutosha kununua heka nzima.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ambayo yana madini waweze kulipwa malipo ya ardhi kulinganisha na bei ya soko iliyopo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli yangu, naomba uelewe Mgodi wa Geita Gold Mine, watu wameanza kulipwa enzi ya plasadom, miaka ya 1980. Kwa hiyo huo mtegesho ni kweli na bahati nzuri tumepanga tarehe 10 mpaka 14, nakukaribisha na wewe uwepo Nyamongo kwa sababu nitakuwa na Mbunge wako hapa. Halafu hili suala la tathmini siyo kufikiria kwamba mtu anahitaji fedha kiasi gani ili akanunue shamba au akawekeze, anayefanya thathmini ni Ofisi ya Serikali na kila Wilaya inafanywa chini ya DC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunafuata taratibu za sheria ambazo zipo, tathmini siyo kukufanya wewe upate fedha kwa sababu umeshalenga mradi fulani. Ahsante.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, swali hili linafanana kabisa hali ilivyo na katika Wilaya ya Mkalama, mkandarasi yuko site lakini aliondoka kwa muda mrefu sasa ndiyo amerudi je, mradi huu utakamilika lini wa usambazaji umeme?
Pia kuna kata nyingi ambazo hazikupitiwa na mradi huu, Kata ya Kikonda, Kinankundu, Msingi, Pambala na Mwanga, je, lini vijiji vilivyopo kwenye Kata hizi vitajumuishwa katika mradi huu?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mbali na majibu mazuri ya Naibu Waziri naomba nitoe ufafanuzi ufuatao, tarehe 6 na tarehe 7 mwezi huu tunafanya tathmini ya REA Awamu ya Pili, kwa hiyo, REA watakuja na orodha ya miradi iliyokamilika REA Awamu ya Kwanza, REA Awamu ya Pili tunataka na Wakandarasi tujue waliopewa kazi, malipo waliyopewa na kazi inakamilika lini. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania vuteni subira baada ya hiyo tathmini mimi na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu tutasambaa nchi nzima kwenda kuthibitisha tuliyoambiwa kwenye kikao chetu ambacho tutakifanyia Mtera.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo REA awamu ya tatu inatayarishwa, lakini REA awamu ya tatu haitaanza wala orodha haitakamilika mpaka kwanza REA awamu ya pili ikamilike na turidhike kwamba imekamilika. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tukiwa huko naomba ushirikiano wenu na ambaye anaona REA awamu ya pili haijaenda vizuri ni vizuri sana anipatie orodha kabla ya kikao chetu cha tarehe 6 na tarehe 7. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ahadi ya Serikali na Waziri mwenyewe humu Bungeni aliwaahidi Watanzania kwamba Miradi ya REA II itakamilika yote Juni, 2015; siyo mara moja wala mara mbili; ni sababu ipi iliyopelekea miradi hii kutokukamilika kama Mheshimiwa Waziri alivyosema? (Makofi)
La pili, kwa sababu huyu Mkandarasi mara kwa mara amekuwa akiwachangisha Watanzania shilingi 200,000/= au shilingi 300,000/= kwa kila nguzo ya umeme wale wanaohitaji; Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wananchi hao wapate huduma hii kama ilivyotarajiwa? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tulikusudia kwamba ikifika Juni, 2015 miradi iwe imekamilika, lakini tuwe na ukweli wa kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pato letu la Taifa ni karibu dola bilioni 53 na mwaka jana tulikuwa na uchaguzi, tulikuwa na Katiba, uchumi wetu hauna uzito wa kukabili vitu vikubwa kwa wakati mmoja. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni ukweli wa kifedha na kiuchumi. Kwa hiyo, ndiyo maana sasa Serikali imemaliza majukumu makubwa fedha zinaenda REA, kwa hiyo, miradi itakamilika kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuongezea kwamba miradi ya REA na Miradi yote ya umeme, ndugu zangu Watanzania inahitaji fedha nyingine za kutoka nje. Kwa hiyo, sisi Wizara tumeanza kutafuta fedha kutoka nje. Kwa mfano, Tanzania ndiyo iliwakilisha Afrika kuweka hizi taratibu za umeme kwa kila raia wa sayari hii (Sustainable Energy for All 2030). Ni sisi ndiyo tuliwakilisha Bara la Afrika na tutahakikisha sisi ndiyo tutapata fedha nyingi kutoka huko na tumeishaanza kuzipokea. Kwa hiyo, miradi itaenda kwa kasi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Chico, tumewaambia Wakandarasi kwamba endapo pataonekana kuna rushwa, adhabu kubwa kabisa ni kwamba huyo mkandarasi hatapata miradi mingine ya REA. Kwa hiyo, kama huyu mkandarasi anachangisha, ni kwamba na wiki ijayo tunafanya tathmini adhabu yake nyepesi sana ni kutopata mradi wowote wa REA kuanzia mwaka huu.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa huu Mradi wa REA umesambazwa sana vijijini na nguzo zimewekwa sana vijijini, lakini nguzo hizi zimeanza kuoza. Je, ni lini Serikali itahakikisha nguzo hizi zinawekwa na wananchi wa vijijini wanapata umeme? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza labda iwe ni miujiza, hizi nguzo kuharibika siyo chini ya miaka kumi. Kwa hiyo, kuoza kisayansi hatukubaliani na hilo, la kwanza hilo. (Makofi)
La pili, Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba jumla Tanzania tuna vijiji 15,029. Vijiji ambavyo vimepata umeme hadi sasa ni 5,900, sawa na asilimia 33. Kwa hiyo, tukiingia REA Awamu ya Tatu, ya Nne na ya Tano, nadhani Tanzania itakuwa katika nchi pekee Barani Afrika kwamba umeme umetapakaa vijijini kote.
Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana ni wiki moja kutoka sasa tunafanya tathimini ya REA Awamu ya Pili, ili tuingie REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, nguzo haziozi na hazitaoza, umeme utapatikana. Ahsante.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yasiyoridhisha, ni dhahiri kwamba Serikali haijajipanga kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo. Kinachonisikitisha zaidi, eti Serikali imejipanga kwenye kituo cha madini, kitakachoanzishwa na AICC na Wizara, kijengwe Arusha. Mjini Sri-Lanka, geuda sapphire...

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Sri-Lanka. Kwa kuwa Sri-Lanka imejipanga kwenye geuda sapphire red stone, kwenye Mji wa Ratnapura; Madagascar Afrika, kwa nini Serikali ya Tanzania isijipange kati ya Mererani na Naisinyai, ianzishe kituo hiki ili heshima hii ipewe Simanjiro? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kati ya Disemba na Januari, Wizara ikishirikiana na Jeshi la Polisi, wamewakamata vijana wasio na ajira wa Simanjiro kati ya Mererani na Arusha, wamenyanganywa madini yao, vijana hawa hawajasoma, wanajitafutia maisha. Ni lini Serikali inayojitapa inatafutia vijana ajira, itawasaidia vijana hawa kupata ajira na kutowanyanyasa kwenye nchi yao? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Serikali haijawasaidia wachimbaji wadogo. Kama ingekuwa hivyo, kama kweli wachimbaji wadogo wasingefaidika, kwenye Kikao chao cha Geita, wasingenichagua mimi niwe mlezi wao Kitaifa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ruzuku ya kwanza tuliyoitoa, sisi Wizara ndiyo tuliitafuta, tuliitoa kwa vikundi zaidi ya 10 na kila Kikundi kilipewa ruzuku ya dola 50,000. Awamu ya Pili, tumetoa ruzuku ambayo kiwango cha juu kabisa ni dola 100,000 ambavyo ndiyo Naibu Waziri alikuwa anasema, tumetoa kwenye vikundi 111.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) limefungua desk, wameweka Idara kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Sasa hivi tunavyofanya ni kwamba eneo la wachimbaji wadogo likitengwa (geological survey). Wakala wa jiolojia hapa anaenda kwa gharama ya Serikali, wanafanya utafiti kabla hatujawapatia wachimbaji wadogo maeneo. Kwa hiyo, kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye Tanzanite. Ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge, tumejadili naye na kwa heshima kabisa, nimekusanya watu kesho ofisini na mwenyewe anajua. Namleta Kamishna, naleta watu kutoka Arusha, waje wakae naye kwanza wampe somo la mambo ya biashara ya Tanzanite. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga naye anafahamu hivyo. Mbali na hapo Mheshimiwa Mbunge atakubali kwamba wakati sisi tunatengeneza mambo ya Tanzanite, watu walilalamika wakasema wamejitokeza Watanzania wapewe huo mgodi. Nawe unajua kuanzia jana wananchi wamegoma, hawawataki hawa wawekezaji mliokuwa mnawashabikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kutatua suala la Tanzanite kwa jinsi linavyotatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifano aliyoitoa Mheshimiwa Mbunge ya Sri-Lanka na Madagascar, kwa heshima zote siyo kweli. Kwa sababu mimi nimeenda Madagascar mara nyingi sana; na nilikuwa nashughulikia gem stones za Madagascar na Sri-Lanka. Ukienda Madagascar utakuta badala ya vijana kuuza karanga na njugu, wao wanauza gemstones wamezichonga, wameweka kwenye kama viberiti. Huko labda ndiko tutakapokwenda. (Kicheko/Makofi)
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nataka kujua tu, Serikali inipe majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuzuia branding za Tanzanite externally, nayo yana sovereign ownership ya Tanzania na kuthibiti mapato ya Serikali; kulikuwa na Mkataba ambao ulisainiwa Afrika Kusini mwaka 2003 unaitwa Kimberley Process. Certification ya madini haya ilikuwa pamoja na Diamonds, kipindi kile kulikuwa na conflict diamonds, lakini waka-incorporate na madini ambayo yana thamani kama Tanzanite.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, je, Tanzania tumo katika mkakati huo wa certification ya Tanzanite ili kudhibiti sovereign ya mali hii ibaki nchini na itambulike kuwa ni mali ya Tanzania tu? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Kimberley Code yenyewe ilikuwa controversial. Kuna wengine waliikubali, wengine wameikataa, ikaanzishwa nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jibu la kifupi ni ndiyo tunataka Tanzanite. Hata Ofisi yetu ya London, wale wafanyakazi wa kwetu kule waliokuwa wanasimamia uuzaji wa diamonds, wakiwa wana Ofisi London, tuliifunga, tunataka haya madini yauzwe nchini hapa. Jibu ni ndiyo!
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niuliza swali la nyongeza. Mji wa Maramba una tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme kama ilivyo Mji wa Korogwe. Je, Waziri atatuhakikishia kwamba katika mipango hiyo anayoizungumza ina-consider vile vile Mji wa Maramba?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kukatikakatika umeme, sababu mojawapo ni miundombinu kuwa inasafirisha umeme mdogo ambao haulingani na matumizi. Kwa hiyo, project kubwa kabisa ambayo tuna nyingine tunaizindua mwezi wa tisa ni kutoka kwenye miundombinu inayosafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kwenda 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wa Tanga, hii inatoka Dar es Salaam inapita Tanga ikielekea Arusha halafu kuna nyingine inatoka Iringa, Dodoma kuelekea Shinyanga. Ni lazima tuwe na umeme mwingi ndiyo tutakomesha ukatikaji wa umeme mara kwa mara na hilo tatizo linatatuliwa. Ahsante.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shida kubwa ya maji katika Mkoa wa Arusha especially Jiji la Arusha inatokana na tatizo la mgao wa umeme tatizo ambalo katika nchi yetu tunaona kabisa haliishi leo wala kesho. Kwa mfano, Arusha Mjini tulikuwa tunapata maji lita laki moja kwa siku lakini mwaka 2013 tunapata maji lita 45,000 na katika Kata ya Mushono ni magaloni matano kwa siku hadi kufikia sasa kwa wiki mbili unapata maji mara mbili. Tatizo hili limekuwa kubwa sana na hatuoni kama kuna mkakati madhubuti wa Serikali kusaidia tatizo hili kwa sababu shida kubwa ni ya umeme na umeme wa nchi hii hata siku moja haujawaka frequently. Ni nini mkakati wa Serikali kuhusu kusaidia kutatua changamoto hii kwa sababu umeme katika nchi hii bado ni wa mgao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mradi huu ni wa muda mrefu, lakini shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni shida ya kudumu na ya muda mrefu sana kama ulivyosema katika jibu lako …
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi huu ni wa muda mrefu na shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni ya muda mrefu, nini mkakati wa Serikali kutatua kwa haraka tatizo hili ili wananchi wa Arusha wapate maji kwa haraka?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimfahamishe Mbunge vitu asivyovifahamu. Kwanza pale KIA tumeweka sub-station kwa ajili ya umeme wa KIA na maeneo ya pale tu. Ukienda Mererani, katika wachimbaji 10 wa Tanzanite wachimbaji tisa wanatumia umeme bila kulipa, wanaiba umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba ukitaka umeme wa uhakika shughulika na wezi wa umeme wa Arusha, ahsante.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu sehemu ya pili ya swali lake kwamba mradi huu ni wa muda mrefu, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ili tuweze kufanya kazi nzuri lazima kwanza tufanye usanifu ili tuwe na uhakika kabisa kwamba maji yatakuwepo ya kutosha maeneo yote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avumilie na mpango unaoletwa na Serikali ni wa uhakika kwamba tupate maji ya kutosha mpaka mwaka 2025.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pia kwa kuniona.
Suala la umeme katika vijiji vingi hapa nchini bado halijawekwa wazi kuhusiana na maeneo ya visiwa. Jimbo langu tu kwa mfano linavyo visiwa 25. Nisizungumzie Jimbo la Mheshimiwa Mwijage huko Gozba, Bumbire na maeneo mengine.
Sasa mimi ningependa tu Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini labda atuambie ni kwa namna gani Wizara au Serikali kwa ujumla imejipanga kufikisha umeme katika maeneo haya ambayo kimsingi si rahisi sana kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba visiwa vyetu vinahitaji kupata umeme na cha kwanza vilivyopata umeme ni visiwa vya Zanzibar ambapo tumejenga cable chini ya bahari. Wao wana megawati 100 lakini mahitaji ya Zanzibar ni megawati 50, kwa hiyo wanayo 50 zaidi. Na Mheshimiwa Tizeba yeye mwenyewe anafahamu kisiwa cha kwanza kabisa katika Ziwa Victoria kupata umeme ni kisiwa chake ambacho kwa mara ya kwanza tumepitisha cable chini ya Ziwa Victoria, na tumemuomba Waziri Mkuu akazindue huo umeme kwa sababu ni wa kipekee kabisa. Na hivi sasa Kisiwa cha Ukara vilevile wamepatiwa umeme na ni mtu binafsi aliyewekeza umeme pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Wabunge wote ni kwamba hivi visiwa vingi vidogo vidogo hatutaweza kujenga cable kwa kila kisiwa, ila umeme watakaoupata ni umeme wa jua.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, mradi wa ORIO ulikuwepo toka mradi wa umeme vijijini Phase II ambao ulihusisha vijiji vitano, vya Kabungu, Ifukutwa, Igalula na Majalila. Mradi huu ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha, Serikali ilishindwa kuwekeza fedha ambazo zinge-support kampuni ya ORIO. Je, Serikali ina majibu yapi sahihi ambayo yatawezesha miradi hii iweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nilikuwa nataka kufahamu uwiano wa miradi hii ya umeme vijijini. Yapo maeneo mengine ambayo sasa hivi yana asilimia mpaka 80, yamepata miradi hii, maeneo mangine bado hayajakuwa na fedha zinazopelekwa kwenye maeneo husika kama Jimbo la Mpanda Vijijini. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya mgawanyo wa fedha zinazofadhili Mradi wa Umeme Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge, kwamba mradi wa ORIO ni wa Uholanzi. Ni kweli kwamba sisi tulikuwa hatujalipa fedha, lakini sasa fedha zimelipwa na hiyo mitambo imetengenezewa Ubeligiji na itafungwa. Ndio maana engine nyingine ambazo zilikuwa Ngara na kwingine tutahamisha, kwa sababu engine zinakuja zimeshatoka na wanazifunga kule; kwa hiyo mradi huo utatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza juu ya uwiano, ni kweli napenda kukiri, kwanza Awamu ya Kwanza ya Umeme Vijijini, ilikuwa ni ya majaribio, ilifanyika ndani ya mkoa mmoja tu, Awamu ya Pili, tumejaribu kwenda nchi nzima. Lakini ukweli ni kwamba uwiano sio mzuri, na ndiyo maana Awamu ya Tatu tumekubaliana kwamba itabidi tufanye tathimini mkoa kwa mkoa, tuone mikoa ambayo imefaidika kwa kupata umeme Awamu ya Kwanza na ya Pili, safari hii watapata vijiji vichache kusudi vijiji ambavyo havijapata umeme vipewe kipaumbele.
Ninapenda kukiri kwamba mikoa ambayo kusema ukweli hawajapewa umeme sana ni mikoa ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na REA Awamu ya Tatu inaweka mkazo hapo
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Machi, REA walikuwa wamepata karibia asilimia 40 tu ya fedha za kwenda kumalizia katika REA ya Awamu ya Pili. Nilitaka kujua, mpaka sasa hivi Wizara yako imepokea kiasi gani ili vijiji vyangu ambavyo vilikuwa viporo kabla ya hii REA ya Awamu ya Tatu, kama Kunzugu, Mihale, Nyamatoke, Bukole, Kamkenga, Kangetutya, Rwagu na maeneo mengine yapate umeme katika ule ule mpango wa REA ya Pili na huu wa REA ya Tatu?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tulikuwa asilimia 40, lakini kwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 75, kwa hiyo jinsi ambavyo tunakusanya fedha na ndivyo jinsi ambavyo Hazina inatupatia fedha. Kwa hiyo, kwa mipangilio inavyokwenda na wakandarasi tumewaambia huu mwezi Mei tutafanya tena tathmini kwa kila mkandarasi amefanya kazi kiasi gani, nadhani hadi kufikia mwezi Mei tutakuwa tumefika karibu asilimia 80. Mheshimiwa Mbunge nataka kukuhakikishia na ndiyo maana tumekubaliana na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama miradi yako ya REA Awamu ya Pili haikukamilika ni lazima itapewa kipaumbele kwenye REA Awamu ya Tatu.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa pesa ambazo MCC walikuwa waipatie Tanzania zingeshiriki kutatua tatizo kubwa na kero kubwa ya umeme na sasa wamesitisha kutoa pesa hizo. Je, Serikali inaweza kutuambia ni athari gani zinaweza kupatikana kwa wananchi kwa kukosa msaada huo wa MCC?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wasikilize kwa makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna hata dola moja, hata senti moja ya MCC ilikuwa iko kwenye Miradi ya Umeme Vijijini. Hiyo hawezi kunibishia Mheshimiwa Msigwa kwa sababu mimi mwenyewe ndiyo nimeenda kukaa na watu wa MCC, nimekaa na Waziri wa Nishati na wa Fedha wa Marekani, hizo fedha zilikuwa haziji Bungeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MCC halafu fedha zote za MCC hazikuwa za umeme vijijini. Hilo nalo ni kosa lingine ambalo lazima watu waelewe, kuna fedha za barabara halafu kuna fedha za maji na vitu vingi sana, katika zile fedha za MCC zilizokuwa za umeme hazivuki theluthi moja. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kwamba mimi tunaongea kwa takwimu, siyo ubishi, ni takwimu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote naomba hili jambo tulielewe hivi, mimi hapa ninataka kulima heka nane za mahindi, ndugu yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema Mheshimiwa Muhongo kwa nini ulime heka nane? Mimi naomba nikuongezee heka mbili, ili zitimie ziwe kumi na mimi nasema ahsante ndugu yangu nipatie. Kwa hiyo, asiponipatia hizo heka mbili mimi bado za kwangu nane nitalima.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri. Kama majibu yalivyo yanadhihirisha kabisa kwamba kuwataka au watu wa Kahama kuendelea na umeme wa jenereta wakati Watanzania wote na yeye mwenyewe anafahamu kwamba Wilaya ya Kahama ni kati ya Wilaya ambazo ni kitovu cha uzalishaji wa chakula especially mchele na kwa jinsi hiyo kuwazuia kwa namna moja au nyingine wasifanye uzalishaji wenye tija. Nimeshukuru amesema kwamba utaratibu umeanza wa kuwapatia umeme wa uhakika. Ningetamani sana kuona kuwa hili linapatiwa ufumbuzi haraka na ningetaka sasa aseme ni lini ambapo umeme huo utapatikana kwa uhakika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tatizo la kukatika kwa umeme siyo la Kahama peke yake, ni la maeneo mengi sana Tanzania, likiwepo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo kule mnaamka mnaulizana kwenu upo? Leo umeme upo? Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anaweza kutusaidia kujua kwamba eneo la Kigamboni sasa litaacha kukatiwa umeme kila siku, kila mara especially siku za Jumapili kuanzia lini? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Kahama imeunganishwa kwenye lane ya Shinyanga ambayo msongo wake ni wa KV 33 na sisi tunajua kwamba umeme huo ni mdogo, ulitosha kwa wakati huo lakini siyo kwa sasa. Kwa hiyo kinachofanyika, nadhani hata kabla ya bajeti yangu kwisha, Ijumaa atawaona watu wa TANESCO wako pale, wameondoka leo, wamekubaliana na Mgodi wa Buzwagi, Buzwagi ndiyo iko karibu sana na Kahama. Kwa hiyo, umeme utavutwa kutoka Buzwagi 33 KV kwenda Kahama. Kwa hiyo, huku watakuwa na wa Shinyanga, huku watakuwa na wa Buzwagi, tatizo hilo litakwisha.
Mheshimiwa Spika, mbali ya hilo la umeme kukatika katika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote lazima tufanye maamuzi. Tukiwa tunajenga hii miundombinu kuna wakati lazima tuzime umeme. Watu wa upande wa Ziwa Victoria kila Jumapili umeme unakatika, lakini wanatangaziwa kwamba tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme mwingi kutoka Iringa mpaka hapa Dodoma, tunatoka kwenye KV 220 mpaka KV 400. Tunatoka hapa Singida, Shinyanga mpaka Nyakanazi KV 400. Sasa hii tunaizindua Septemba.
Mheshimiwa Spika, sehemu zingine Tanzania nzima, hata ndugu zangu wa Arusha waliokuwa wanasema umeme unakatikakatika, tunajenga kutoka Singida kwenda Arusha KV 400, halafu kutoka Da es Salaam kupitia Tanga kwenda Arusha KV 400. Hiyo ndiyo TANESCO mpya. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utafutaji wa madini katika eneo la Kalambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, sasa hivi kule mitaani kuna malalamiko kwamba utafutaji umepungua sana, wawekezaji hawaji kwa sababu ambazo hazielezeki. Kwa nini Serikali sasa isichukue hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba utafutaji unakua na tuweze kupata migodi mingine siku za usoni? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, msemaji ni geologist nilikuwa nadhani anajua jiolojia na madini duniani yanakwendaje. Hayo yaliyoko mitaani sio ya kitaalam kwamba utafiti umepungua. Ni kwamba kila baada ya miaka fulani madini yanatafutwa yanawekwa store yanakuwa mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vita ya kwanza, Wajerumani na Wafaransa walileta vijana wao kutafuta madini Afrika. Kufika mwaka wa sitini, madini yakawa ni mengi sana duniani ndiyo maana utafutaji ulizorota hata sekta yetu ya madini miaka ya 70, 80 ikazorota. Miaka ya 90, madini yakapungua dunia, utafutaji ukawa wa nguvu sana na Afrika ilichukuwa asilimia 30 ya bajeti ya utafutaji wa madini duniani kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hata China ambayo ndiyo mchimbaji na mtumiaji mkubwa wa chuma duniani vilevile amepunguza kutumia chuma na ndiyo maana unaona hata Zambia uchumi wao umeyumba kwa sababu walikuwa wanategemea sana shaba iliyokuwa inapelekwa China. Kwa hiyo, hili sio jambo la Tanzania ni kwamba dunia ina madini mengi, utumiaji wa chuma,shaba umepungua sio kwa Tanzania tu lakini utafutaji utakuja tena, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, teknolojia ya dunia inabadilika huwezi ukang‟ang‟ania kila siku dhahabu, chuma au shaba. Sasa hivi madini yanayotafutwa kwa wingi sana duniani ni haya nilivyosema yanayotumika kwenye simu zetu, rare earth elements. Madini hayo hayajapungua duniani yanatumika kwenye simu, televisheni, kwa hiyo, yanatafutwa kwa nguvu sana.
Kingine ambacho kinatafutwa madini ya kutengeneza mabetri kwa sababu hesabu inaonyesha kwamba itakapofika karibu mwaka 2040, asilimia kubwa ya magari mengi duniani yatakuwa ni yanayotumia umeme. Kwa hiyo, madini kama graphite na mengine ndio yanatafutwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba utafutaji umepungua bali ni madini gani utafutaji wake umepungua. Sababu ni teknolojia ya dunia inabadilika na sisi Tanzania tunajielekeza kwenye madini ambayo ni adimu na ambayo yanatakiwa duniani. Ahsante.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, hata hivyo napenda kusema kwa mfano wananchi wa Nyarugusu ni kipindi kirefu sana ni ahadi Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi wananchi hawa waweze kupewa eneo hili na harakati mbalimbali, viongozi wengi wamekuja katika eneo hilo kuahidi lakini hakuna kilichofanyika kwa hiyo wananchi wote wa Nyarugusu wanahitaji kusikia kwamba ni lini sasa wataweza kupewa eneo hilo la STAMICO?
Swali la pili, wananchi wa Geita wanategemea sana shughuli za uchimbaji ndio maana Wanyamatagata pamoja na Sami na maeneo mengine kama vile Mkaseme maeneo ya Magenge wananchi wanahitaji kupewa maeneo ya uchimbaji, ningependa kujua sasa nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapewa maeneo ya uchimbaji? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, na ndugu zangu wa Nyarugusu, nadhani unataka tutoe jibu la ukweli kabisa na hili ndiyo litakuwa la ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hilo eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea ni leseni kati ya STAMICO na kampuni ambayo kuna Watanzania na Wacanada, kilichotokea ni kwamba kuna mgogoro mkubwa kweli na Mheshimiwa Naibu Waziri nilivyomuagiza aende kule alivyotoa tamko tu, lile tamko likasambazwa dunia nzima.
Kwa hiyo, naomba wananchi wafahamu kwamba eneo hilo halitatolewa mpaka hiyo kesi iishe. Watanzania tuwe makini sana, tumesaini mikataba na makampuni na mkataba mkubwa ni ule MDA (Mineral Develepment Agreement), tukicheza na hiyo kesi na Wabunge kama wanataka tuandikishiane na Wabunge kwamba Serikali ikishtakiwa Wabunge husika watabeba gharama za hiyo kesi kwenye mahakama za nje ya Tanzania. Kesi bado ipo, wananchi wavute subira mpaka hiyo kesi ikamilike kuhusu huo mgodi wa Nyarugusu na huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, ahadi zitatolewa, ahadi zisitolewe tena hapa mpaka hiyo kesi iishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo sasa wa Geita na sehemu zingine, ni kwamba tunatoa maeneo kwa wachimbaji wadogo, na hivi juzi nilikuwa naenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu, lakini tumegundua kwamba ruzuku awamu ya pili waliochukua fedha kwa kupitia TIB hawakuchukua fedha walipewa vifaa, vile vifaa vingine havipo huko kwenye migodi.
Kwa hiyo, kabla hatujatoa ruzuku ya awamu ya tatu imesimamishwa mpaka tufanye tathmini ya awamu ya pili na awamu ya kwanza, hapo ndipo tutaenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu. Lakini wachimbaji wadogo Serikali ina dhamira kubwa kwelikweli ya kuwaendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuheshimu sheria, na ninawaomba Wabunge, tuna Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inatambua utoaji wa leseni na MDAs hizo. Sasa Wabunge wenyewe hatuwezi kushabikia kuvunja sheria ambazo tuliziweka. Ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Katika Sekta ya Gesi utafiti wa gesi na mafuta katika Bonde la Ziwa Tanganyika pamoja na Chepechepe na Bonde la Mto Malagarasi, tungependa kujua utafiti huo umefikia wapi?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa majibu mazuri, niongezee lile swali la awali; matumizi ya gesi na mambo ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba sasa hivi Mikocheni na nyumba za TPDC 70 wanatumia gesi, wana mabomba mawili mle ndani; bomba la maji na bomba la gesi. Matumizi yake kwa mwezi hawajavuka sh. 25,000/= hata wakipika vyakula kama maharage, makongoro, ni sh. 25,000. Hiyo tumefanya. Halafu kuna viwanda 37 vinatumia gesi. Hili jana liliongelewa. Tumepata fedha dola milioni 150 kutoka African Development Bank kwa ajili ya kusambaza gesi Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Waheshimiwa Wabunge, maana ya uchumi wa gesi ni kwamba hii gesi ni lazima tujenge mabomba mengi. Sasa hivi bomba kubwa la Mtwara – Dar es Salaam liko kwenye asilimia 10 lakini likijaa kabisa gesi, ni mita za ujazo milioni 784 (784 million cubic feet of natural gas) ndiyo inapaswa kupita mle kwa siku. Sasa hivi bado tuko ten percent, lakini ikishafika pale Kinyerezi, ni lazima tujenge mabomba kwenda Morogoro, Dodoma, kila mahali, mpaka Mbeya. Hiyo ndiyo maana ya uchumi wa gesi na ndiyo maana tunasema hii nchi lazima tujenge mabomba mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ya matumizi ni kwamba elimu itakayotolewa Mheshimiwa Mbunge, nadhani siyo muhimu. Gesi ya zamani ndiyo ilikuwa inalipuka, lakini gesi ya kisasa hailipuki. Hii gesi ni CNG (Compressed Natural Gas). Kwa hiyo, ukweli ni kwamba huenda hata elimu haihitajiki, ni kununua unakwenda kutumia tu na ndiyo inaingia kwenye magari. Kwa hiyo, hatuwezi kuweka gesi kwenye gari halafu tena inalipuka. Kituo cha kwanza cha gesi kiko pale Ubungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye swali lako Mheshimiwa Nsanzugwanko, ni kwamba mkutano wa kwanza, tena nilikuwa sijamweleza Naibu Waziri, naye itabidi aniwakilishe, mzee niwakilishe; kikao cha kwanza kitafanyika Kalemee wiki ijayo cha exploration kwenye Ziwa Tanganyika. Ni kwamba Congo, Tanzania, Burundi na Zambia ni lazima tukae chini; tunajua kwamba kuna gesi na mafuta. Hiyo tunaweza kujua kwa sababu ya ugunduzi kule kaskazini Lake Kivu. Kabla hatujaanza kuzozana, ni afadhali tuanze majadiliano kwamba gesi na mafuta yakipatikana tutakuja kugawana kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, exploration ile tunaifanya pamoja na Mto Malagarasi, tunajua dalili kwamba kuna ama gesi au mafuta, lakini huku gesi tumeshaiona huku Kipili kusini mwa Ziwa Tanganyika huku, ipo. Sasa tunataka kujua ni kiasi gani na ni mafuta kiasi gani.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini swali langu hasa lilikuwa linahusu upande wa umeme. Naomba niulize maswali mawili madogo, kwa kuwa Waziri wa Nishati yuko hapa kama ataona anaweza kumsaidia basi anaweza akajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ambalonalielekeza Wizara ya Maji; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Kilolo kuna vyanzo vingi vya maji, lakini sasa hivi wakulima walio wengi walikuwa wanategemea sana vilimo vya mabondeni, kwa lugha ya kwetu tunaita vinyungu ambavyo ndiyo vimewapelekea kuwasomesha watoto zao na kuendesha maisha ya kila siku lakini sasa hivi wamezuiwa. Kwa kuwa Serikali ilipokuwa inazuia ukataji wa miti ilihamasisha watu watumie umeme na kupunguza bei ya gesi sasa Serikali imezuia watu wasilime kwenye vyanzo vya maji, Wizara imejipangaje ili kuhakikisha wale wananchi wanaendelea kupata fedha kwa kutumia kilimo cha vinyungu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nilitegemea ningejibiwa na watu wa umeme, kwamba kwa kuwa vyanzo vingi vimekwenda Kihansi na Kihansi ndiyo inatoa maji wananchi wa Kilolo wananufaika vipi kwa sababu wametumia muda mwingi kutunza vyanzo vile? Naomba maswali yangu yajibiwe.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa kwanza ni hivi, sio wananchi wa Kilolo peke yake ni suala la dunia nzima, unahitaji maji kuzalisha umeme, lakini unahitaji maji kwa ajili ya umwagiliaji. Huu ni mjadala ambao dunia nzima wataalam wa maji na wa umeme wanaendelea kujadiliana. Kwa hiyo, siyo kitu cha ajabu kwa kwetu hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la umwagiliaji tulivyoenda huko vijijini kusema ukweli zile mbinu wanazozitumia ni za kizamani, mtu anakuja anajenga yale mataruma kwa zege, wakati wa mvua anamwagilia, wakati wa kiangazi anamwagilia. Kwa hiyo, nadhani Serikali imefanya utafiti hasa watu wa Kilimo kwamba kuna njia bora za umwagiliaji. Cha kwanza ni kutumia njia bora za umwagiliaji, lakini wote wawili wanahitaji maji, wakulima na watu wa kuzalisha umeme, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la wanafaidikaje, tuna mradi mmoja katika miradi ya REA III ambayo tutakuja kuieleza kwenye bajeti yetu kuna mradi wa kuwapatia watu umeme walio kwenye mkuza mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Iringa - Dodoma mpaka Shinyanga kama ambavyo tulivyofanya kuwapatia watu umeme walioko kwenye mkuza wa bomba kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam, huo mradi tayari unatekelezwa.
Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto afahamu kwamba ndani ya REA III huo ni mradi mmojawapo, wanaotutunzia vyanzo vya maji watapata umeme ule wa jogoo wawili shilingi 27,000, ahsante.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Najua Naibu Waziri haya majibu amepata kwa wataalam, lakini ukweli ni kwamba katika Jimbo la Mlimba hakuna Kijiji kinachoitwa Ipela Asilia. Ipela Asilia ipo Wilaya ya Malinyi, Halmashauri mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyofuatilia Malinyi, Madiwani hawana taarifa yoyote, hata Baraza la Madiwani halina taarifa yoyote kuhusu hizi taarifa, wanaona tu watu wanaingia na kutoka. Ni kweli kabisa pale uwezekano wa mafuta upo mkubwa sana, wameshachimba kisima kimoja cha mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu; kwa kuwa eneo hilo ni eneo nyeti, wanapatikana wale wanyama wasiopatikana duniani (puku), lakini Serikali inakwenda kutoa kibali cha kuchimba hayo mafuta na wananchi wanaozunguka hili eneo wamekatazwa kabisa kufanya shughuli za kibinadamu katika eneo hili.
MHeshimiwa Mwenyekiti, nataka majibu ya Serikali,
ni lini sasa watakwenda kuwaelimisha hawa wananchi na kuwapa wao maeneo ambayo wanaweza wakaendeleza shughuli zao za kilimo wakati mradi huu unaendelea na elimu haijatolewa katika kijiji hicho ambapo ni Kata ya Njiwa na Kata ya Itete; nimezungumza na Madiwani usiku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi; kwa kuwa amesema Mlimba; Mlimba katika Kata ya Mofu, Bwawa la Kibasila kuna utafiti ulifanyika na Mzee Magoma alikuwa Mkalimani wa wale Wazungu na ukweli ni kwamba Bwawa la Kibasila Kata ya Mofu, Kijiji cha Ikwambi kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta kwa sababu kuna mikondo miwili inayotoka Ihenga na Mofu na Ikwambi na mkondo mwingine unatokea Mngeta, inakutana pale, kwa hiyo, wakasema kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta.
Sasa nauliza swali hili kuhusu Jimbo la Mlimba; ni lini
sasa Serikali itakwenda katika Jimbo la Mlimba ikibidi waonane na huyu Mzee Magoma awaambie hali halisi, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta, lakini leo wamenijibu swali la Malinyi. Kwa hiyo, swali langu bado halijakidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipande kusema tu kwamba hatutakwenda kwa mzee yeyote kumuuliza uwezekano wa mafuta kupatikana, kwa sababu hili ni suala la kitaaluma, tutachukua utafiti uliofanywa Seismic Surveys ambayo kuna 2D na 3D, hizo ndizo zitakazotupeleka kule. Kwa hiyo, hatutakwenda kwa mzee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tena, mbali ya mchanganyiko wa majina, tunaomba radhi kama tumechanganya majina, lakini utafutaji wa mafuta, nataka kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, sehemu nyingine duniani watu wametafuta mafuta wameyakosa, lakini baada ya kubadilisha mbinu na namna ya kutafuta mafuta, wengine wakaja wakayapata. Kwa hiyo, hili ni jambo la kitaaluma na kitaalam, halina mjadala wa mambo ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.