Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainab Athman Katimba (13 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nitambue kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa uhakiki wa vigezo vinavyotumika kutoa mikopo kwa wanafunzi, ili kuhakikisha wanaopata mikopo ni wenye sifa na uhitaji na sio wale ambao wanafanya udanganyifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mfumo huu wa utoaji mikopo utaendelea kuwa himilivu na endapo idadi ya wanafunzi itaendelea kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Bodi inatakiwa kuhakikisha kuwa kumbukumbu za wote wanaoomba mikopo zinakuwa kamilifu kwa kushirikiana na vyuo ambavyo vina wanafunzi wanaopewa mikopo hiyo. Kila chuo kinatakiwakuwa na dawati maalum ambalo linashughulikia mikopo, lakini pia katika kutoa mikopo ni lazima kuzingatia vigezo na sifa ambazo zimewekwa. Hivi karibuni Wizara imepitia vigezo hivyo na vigezo vinazingatia hasa uhitaji, uraia, lakini pia uombaji lazima upitie kwenye mtandao na vilevile kwa kuzingatia mahitaji ya nchi, yaani kipaumbele katika taaluma ambazo zinahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuona kwamba, mikopo hiyo inakuwa endelevu ni kwamba, Wizara baada ya kuangalia matatizo yaliyokuwa yakijitokeza katika ulipaji wa mikopo, imeangalia upya Sheria ya Bodi ya Mikopo na hivyo tuko katika kutaka kuileta Bungeni, ili kuona kwamba, inarekebishwa kuweka mikopo kuwa ni deni la kipaumbele kwa mwombaji ambaye ameshamaliza chuo. Lakini vilevile kuhakikisha kuwa waajiri wanahusika nao moja kwa moja katika kuhakikisha mikopo hiyo inalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika sambamba na hiyo tunaangalia namna ya kuboresha upya mifumo mizima ili kuona mfumo huo unaweza kuongea na taasisi nyingine zinazohudumia raia, ikiwemo ya Vitambulisho vya Taifa. Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Serikali ina mpango kabambe wa kupima na kurasimisha ardhi nchi nzima na imekuwa ikishirikisha sekta binafsi katika kufanya hivyo. Aidha, kumekuwa na gharama kubwa sana katika upimaji na urasimishaji huo wa ardhi. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya gharama hizo ili kuweza kuwapunguzia wananchi mzigo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zainab anazungumzia habari ya gharama kubwa katika suala zima la upimaji. Lakini naomba nimkumbushe tu bajeti ya mwaka jana ilivyosomwa gharama zile zilishuka kutoka shilingi 800,000 kwa heka mpaka shilingi 300,000 kitu ambacho ilipunguza sana gharama zinaongezeka kulingana na ukubwa wa eneo ambalo linaenda kupimwa. Kwa mwaka huu pia katika bajeti yetu nadhani kuna maeneo ambayo Serikali imeyafanyia kazi mtayasikia wakati tunatoa bajeti.
Kwa hiyo, niseme kwamba gharama tunaziangalia
na namna bora ya kuweza kumuwezesha mwananchi wa kawaida aweze kupima ardhi yake na kuweza kumiliki ili kumletea maendeleo katika shughuli zake.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza.
Kwa niaba ya vijana wote wa Tanzania ambao wanaweza kuwa wanufaika wakubwa sana wa michezo naomba kuuliza swali la nyongeza lifuatalo:
Je, Serikali haioni umuhimu wa kwamba ni wakati muafaka wa kuwa na shule maalum kwa ajili ya kukuza vipaji katika michezo kama sports academy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninampongeza kwa kuwatetea vijana kimichenzo, kama alisikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ni kwamba tumedhamiria. Serikali sasa hivi imekwishatenga shule takribani 55 ambazo ziko katika Mikoa yote ya Tanzania, hizi ndizo ambazo tutazichukulia kama ndizo academy zetu. Vilevile michezo ya UMISETA, michezo ya UMITASHUMTA itasaidia sana kuibua vipaji, hata hivyo tunashirikiana sana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba michezo inafundishwa katika ngazi zote za elimu tangu awali, sekondari na vyuoni. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na niseme ninatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha elimu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati gani katika mabweni haya 155 ambayo inatarajia kuyajenga katika mwaka wa fedha 2017/2018 kuhakikisha kwamba, inazingatia kipaumbele katika ujenzi wa mabweni katika shule zetu za kata?
La pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mamlaka ya Elimu ya Juu Tanzania ambayo inaonekana inapata changamoto kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha, inatengewa fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kujenga mabweni kwa kushirikiana na Halmashuri na wananchi, kama ambavyo tumekuwa tukifanya na hivi natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kule kwenye maeneo yao ambako kuna ujenzi wa mabweni, basi wasaidie kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu kwenye mkakati huu, lengo ni kuhakikisha kwamba, tunakamilisha ifikapo mwezi Juni mwakani, kama ambavyo tumejipanga.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tutaweka fungu maalum kwenye bajeti kwa ajili ya kuisaidia taasisi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja pamoja na taasisi nyingine ambazo zinasaidia maendeleo ya elimu nchini. Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imefanya jitihada gani ili kuhakikisha kwamba wavuvi wanaweza kuzifikia na kunufaika na hizi fursa alizozizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha inasimamia kwa ukamilifu sekta hii ya uvuvi ili kuhakikisha inaepusha uvuvi haramu ambao utaleta uharibifu kwa mazingira?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni jitihada gani ambazo Serikali imeshakufanya. Kama nilivyojibu katika swali la msingi ya kwamba, la kwanza, tumeendelea kuhamasisha wavuvi kujiunga katika vikundi mbalimbali ili waweze kutumia fursa zinazojitokeza, kama vile fursa niliyoitaja ya ruzuku ambapo katika mwaka huu wa 2017/2018 tumeshatenga shilingi milioni 100 ili kuweza kuendelea kuwasaidia wavuvi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Sheria ile ya Fedha ya mwaka 2007 tunaendelea kuisimamia kuhakikisha ya kwamba zana za uvuvi zinaendelea kupatikana kwa bei nafuu. Pia tunalo dirisha katika Benki yetu ya Rasilimali ambalo linahusu wakulima, wavuvi na wafugaji ili waweze kupata mikopo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni juu ya hatua gani Serikali inachukua kukomesha uvuvi haramu ili kulinda rasilimali zetu. La kwanza kabisa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wavuvi na jamii za wavuvi ili kulinda rasilimali zetu kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imejishirikisha katika kufanya doria mbalimbali ambazo zimeleta matunda chanya ya kuhakikisha kwamba uvuvi haramu unapigwa vita ikiwa ni pamoja na uvuvi wa matumizi ya mabomu na uvuvi wa nyavu zisizoruhusiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika kupambana na uvuvi haramu, Serikali inakusudia kuleta maboresho ya Sheria yetu ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 ili kuipa meno zaidi kuhakikisha tunaendelea kulinda rasilimali za nchi yetu. Nashukuru sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninaswali moja la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba ina hakikisha wavuvi hawa wanapata sokola uhakika baada ya kuhamasisha uzalishaji kwa kuhakikisha kwamba kuna jengwa kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki katika ukanda wa Lake Tanganyika na hasa ukizingatia kwamba kuna specie ya kipekee katika Ziwa Tanganyika ya samaki anayeitwa migebuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ina mkakati gani kuhakikisha viwanda vinajengwa katika ukanda ule? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI:Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa uvuvi katika Ziwa Victoria tumejenga mwalo wa kisasa pale Kibirizi ambapo mwalo ule tumeuwekea vifaa vyote muhimu ambavyo samaki akivuliwa anaweza kutunzwa hata kwa zaidi ya wiki mbili. Yote haya ni kuwafanya wavuvi wanapovua samaki kabla hawajafika sokoni wasiharibike yaani waweze kupata soko kabla hawajaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tumejenga pale mradi mkubwa sana wa ziadi ya takriban shilingi bilioni mbili zimetumika kwa ajili ya kutengeneza mwalo ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili la pili linalokuja ni la kujenga viwanda sasa kwa sababu tayari tumeshapata mwalo mzuri ambapo samaki wanapokelewa na kutunzwa. Kinachofuata sasa ni maandalizi ya kujenga kiwanda ili tuweze kuchakata samaki katika ukanda ule na tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini pia nashukuru kwa kuchukua ushauri wangu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda unalenga pamoja na mambo mengine kutatua changamoto ya ajira hususan kwa vijana, na kwa kuwa viwanda vya ngozi nchini vinakabiliwa na changamoto ya kodi kubwa katika malighafi ya kuchakata ngozi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa tax incentives kwa viwanda vinavyozalisha mazao yanayotokana na mifugo ili kufikia malengo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali haioni haja ya kuwa na breeding program ili kuongeza kiwango na ubora wa mazao yanayotokana na mifugo Tanzania. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba sasa nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba na naomba nimpongeze sana kwa maswali yake mazuri yanayolenga katika kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inapatikana lakini pia tunazalisha ajira kupitia sekta yetu muhimu ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linaeleza juu ya suala la kufanya mkakati au Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuvipendelea viwanda vyetu vya ndani katika tasnia ya ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu tayari imeshapeleka mapendekezo Wizara ya Fedha ya kuhakikisha kwamba kodi zote zinazotozwa katika accessories za uchakataji wa ngozi ziweze kupunguzwa ama kuondolewa kabisa ili kusudi kuweza kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye tasnia hii ya ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tumehakikisha tunapendekeza Wizara ya Fedha iweze kuongeza viwango kwa bidhaa za ngozi zinazotoka nje ya nchi kuingia nchini hasa za mitumba ili kusudi kuweza ku- discourage uagizaji wa bidhaa hizo na uwekezaji zaidi ufanyike ndani ya nchi yetu, na huu ndio mtazamo wetu kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linahusu mpango mkakati wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa kuweza kupata mifugo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mpango wa kuhamasisha, tunaita artificial insemination au uhimilishaji wa mifugo yetu na hii tumefanya kwa kuanzisha vituo maeneo mbalimbali takriban vituo sita katika nchi, na tunacho kituo kikubwa sana pale Arusha cha NAIC pale Usa River ambacho kinazalisha mbegu bora. Vilevile zile mbegu zinatawanywa katika hivyo vituo vingine vilivyopo kote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mkakati huo tumekuwa tukinunua mbegu bora hata kutoka nje ilikuweza kuja kuongeza ubora wa mifugo yetu tuliyonayo hapa nchini. Vilevile tunakwenda katika kuhakikisha kwamba tunaboresha sheria yetu ya mbali za mifugo ili kusudi kuweza kwenda sambamba na mabadiliko hayo tunayoyataka ya kuboresha mifugo yetu hapa nchini ili tuweze kupata nyama bora na tuweze kupata maziwa bora na kwa wingi, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nilipenda tu niongezee, kwanza nilitaka nithibitishe kwamba mapendekezo yaliyotoka Wizara ya Mifugo ni kweli yamefika Wizara ya Fedha na hapa mkononi mwangu nina bangokitita lina kurasa 53 ya mapendekezo ya maboresho ya kodi mbalimbali zikiwemo hizi za tasnia ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Zainab avute subira kidogo Serikali itaji- pronounce kupitia hotuba kuu ya Serikali. Nimuhakikishie kwamba kabisa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vya ndani vinapewa ahueni ya kodi mbalimbali kadri itakavyowezekana. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kwanza kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuelekea katika uchumi wa viwanda, lakini ningependa kuuliza swali moja la nyongeza. Changamoto zinazokabili zao hili la tangawizi ni zilezile ambazo zinakabili zao la mchikichi.
Je, Serikali haioni ni wakati wa kuendelea kuongeza nguvu kuhamasisha wakulima waweze kuongeza uzalishaji wa michikichi na kujengwe kiwanda cha kuchakata na kusindika mawese ili kuweza kuongeza kipato kwa wakulima na kuleta manufaa kwa Taifa hili?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo, mpango wa Serikali kwa Mkoa wa Kigoma ni kuainisha kaya 100,000 ambapo kila kaya itapanda michikichi na tunawasiliana na Wabunge wa Kigoma akiwemo Mzee Nsanzugwanko na Mheshimiwa Peter Serukamba ili tuweze kupata vikonya vya kupandikiza kutoka nchi za Malaysia ambazo zitatumia kituo cha Arusha kuzalisha vikonya zaidi kusudi tuzalishe miche ya michikichi tuwagawie wananchi kwa bei nafuu tofauti na shilingi 5,000 ambazo mnanunua mchikichi, tunakuja Kigoma.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwanza ningependa kutambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli katika vita dhidi ya madawa ya kulevya na ningependa kuwatia moyo na waweze kuendelea na jitihada hizi. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka katika mitaala ya elimu ya msingi pamoja na sekondari mafunzo kuhusu athari ya dawa za kulevya?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, hawa vijana 3,000 waliopatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau, je Serikali inafahamu vijana hawa wako wapi katika muda huu, yaani kwa sasa na wanafanya nini?(Makofi)
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ningependa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainab Katimba kuhusiana na kipengele cha mpango wa Serikali kuweka kwenye mitaala masuala ya madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Spika, ningependa kusema kwamba mitaala ya kuanzia shule za msingi, Sekondari pamoja na masuala ya kitaaluma lakini pia inakuwa imebeba masuala mtambuka. Kwa hiyo, masuala yanayohusiana na masuala ya madawa ya kulevya, masuala ya jinsia, masuala ya UKIMWI yapo katika mitaala yetu na tutaendelea kuyaimarisha ili kuhakikisha kwamba tunaenda sambamba na azma ya Serikali ya kupambana na hili janga la madawa ya kulevya nchini. Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, pia nashukuru kwa kuchukua mapendekezo haya na kuona umuhimu wa kutunga sera hii ya mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu.
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza, sisi tunafahamu kwamba ili kijana/mhitimu awe na uzoefu, uzoefu hujengwa kwa kuanza. Sasa pamoja na kwamba Serikali itatunga sera hii kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu, lakini haioni haja kwamba kuna kazi zingine ambazo hazihitaji kuwa na experience, kwa sababu ukiangalia leo hii ajira zilizotolewa utakuta kuna kigezo, two years experience, three years experience, five years experience. Sasa hawa vijana wanaohitimu, wataanza lini kupata huo uzoefu kama kila kazi inayotolewa inahitaji wawe na uzoefu?
Mheshimiwa Spika, sasa pamoja na kwamba Serikali itatunga sera hii ambayo itaweza kusaidia kuondoa hilo umbwe kati ya elimu waliyopata wahitimu pamoja na mahitaji ya soko la ajira lakini Serikali haioni haja kwamba kuna kazi zingine ambazo hazihitaji huo uzoefu na vijana waweze kupata fursa ya kuajiriwa ili na wenyewe waweze kujikwamua na changamoto ya kukosa ajira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Zainab Katimba kwa namna ambavyo anawapigania vijana wa Taifa hili la Tanzania na vile alivyokuwa mstari wa mbele kuhakikisha maslahi ya vijana yanalindwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na changamoto kubwa katika masuala ya uhitaji wa uzoefu katika nafasi za kazi ambazo zimeombwa na kama itakumbukwa, wakati wa kampeni mwaka 2015 Mheshimiwa Rais pia aliwahi kulisema hili juu ya kigezo hiki cha uzoefu. Sisi kama Wizara tukaona kwa sababu asilimia kubwa ya vijana wanaotoka katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu wamekuwa wakipata taabu sana kwenda kujifunza kivitendo na wengi wao ni mashahidi huwa wanatembea na ile barua ya to whom it may concern na wengine mpaka kumaliza soli za viatu bila kupata eneo la kwenda kufanyia kazi. Kama Serikali tukaona sehemu ya kwanza ya kuanzia ni kuhakikisha tunatengeneza mwongozo huu na mwongozo huu tumefanya kati ya Serikali, waajiri na Vyama vya Wafanyakazi ili tutoe nafasi kwa vijana wale wahitimu wa Vyuo Vikuu wakimaliza masomo yao na tumeshazungumza na haya makampuni yatoa nafasi, tunawapeleka moja kwa moja katika makampuni na taasisi mbalimbali kwenda kujifunza kuanzia miezi sita mpaka mwaka mmoja. Lengo letu ni kuondokana na kikwazo cha kigezo cha experience ili akitoka pale akienda sehemu awe ana reference.
Mheshimiwa Spika, hili ni eneo la kwanza ambalo tumelianzia, naamini kabisa kupitia mpango huu utawasaidia sana vijana wasomi wa nchi yetu ambao wamekuwa wakipata tabu na kikwazo cha uzoefu. Kwa hiyo, hivi sasa atapata nafasi ya kujifunza katika kampuni kwa muda huo wa mwaka mmoja na baadaye tutampatia cheti cha kumtambua ili iwe kama reference yake katika sehemu inayofuata. Tunafahamu ni tatizo kubwa, ni changamoto kubwa lakini kama Serikali tumeona tuanzie hapa kwenda mbele na jinsi Waheshimiwa Wabunge watakavyotushauri tutaona namna nzuri ya kuboresha mpango huu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba kuongeza majibu machache katika swali hili na hasa nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amekwisha kuyasema.
Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kuona tatizo hilo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema tumeshatengeneza hiyo miongozo. Tunafikiri sasa kazi yetu kubwa ambayo tumeanza kuifanya ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuji-link sisi Ofisi ya Waziri Mkuu na miongozo tuliyonayo na wenzetu wa Wizara ya Elimu, lakini kupitia vyuo vikuu vyote kuhakikisha kwamba tunatambua mahitaji na tunawasaidia hawa vijana kuwaandaa vizuri, ili awingie kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Spika, tumekubaliana pia ndani ya Serikali na ndio maana mmeona hata ajira na matangazo ya ajira yanayotolewa sasa hivi, ajira hizo zinazotolewa sasahivi kwa kweli, kimsingi wengi wanaoajiriwa kwenye ajira hizi ni wale ambao ni fresh kutoka kwenye vyuo vyetu vikuu na taasisi nyingine ambazo zinatengeneza ujuzi. Wakati mwingine tunaweza kuwa tunataka ajira katika position fulani ambazo zina matakwa rasmi. Kwa mfano, Mkurugenzi labda wa kitu fulani kwa matakwa fulani kwa hiyo, huko ni lazima tuone sasa wale walioenda internship, lakini vilevile wale ambao wana uzoefu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie vijana wetu kwa kweli, baada ya kuona hiyo gap ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu tumeifanyia kazi vizuri sana, sasa hivi waajiri na Serikali kwa pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi tumeanza kulifanyia kazi vizuri sana eneo hilo. Na tunawaondoa hofu vijana wetu kwa kweli sasa tunataka kuwapa assurance ya ajira bila kupata vikwazo vyovyote katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa jitihada za kutoa mitaji kwa vijana na wanawake inabidi ziende sambamba na kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendeleza biashara. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatumia hawa Maafisa Biashara katika kuwajengea uwezo vijana wanaokuwa katika vikundi ambao wananufaika na asilimia 10 inayotengwa kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kwa dhati kabisa nimshukuru na kumsifu sana Mheshimiwa Zainab Katimba kwa sababu yeye amekuwa anashughulikia sana sana maslahi ya vijana katika Bunge hili Tukufu. Aliwahi kuleta mpaka mapendekezo ya hoja kutaka kutetea vijana wanaomaliza shule ili kusudi waajiriwe bila kuwa na experience. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie kwamba vijana katika nchi hii wana idara nyingi sana za kuweza kuwasaidia mawazo ya kujikwamua kutoka pale walipo kwenda mbele. Katika Halmashauri kuna Idara ya Vijana, Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Mipango sasa Maafisa Biashara tunawongezea sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nitumie nafasi hii kuwaomba vijana wa nchi hii ambao hata fursa ambayo ziko katika Halmashauri hawazitumii ipasavyo, ukienda katika Halmashauri unakuta maombi ya vijana yako asilimia 10 ya maombi yote yaliyowasilishwa. Kwa kweli, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tujitahidi kuwaelimisha na kuwaomba vijana wajitokeze na wajiunge katika vikundi na watumie fursa zilizopo kwa ajili ya kujiendeleza na Serikali tuko macho katika kuangalia suala hilo linatekelezwa vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza nianze kwa kupongeza maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na shule za sekondari na sisi wote ni mashahidi ni kwa namna gani maamuzi haya yameweza kuleta tija kwa Taifa letu. Aidha, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kumekuwa na matukio ya adhabu za kuchapa wanafunzi zilizopitiliza mashuleni ambazo zimesababisha madhara makubwa ya kisaikolojia na kwa wakati mwingine zimesababisha vifo vya wanafunzi. Japokuwa kuna mwongozo wa namna gani adhabu hizi za kuchapa...

SPIKA: Mheshimiwa Zainab swali.

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Okay, japokuwa kumekuwa na mwongozo wa namna ya kutumia adhabu hii ya kuchapa wanafunzi mashuleni lakini mwongozo huu umekuwa hauzingatiwi.

Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masuala haya ya adhabu mashuleni?

Swali la pili, je, wenzetu ambao wamefanikiwa katika sekta ya elimu walifanikiwa kwa sababu ya kuwapo kwa adhabu hizi za kuchapa wanafunzi mashuleni au walifanikiwa kwa sababu ya kuwekeza katika mifumo, mitaala pamoja na miundombinu ya ufundishaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utekelezaji wa kanuni na waraka unaohusiana na viboko bado haujafuatwa kikamilifu. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuwataka viongozi wote wanaosimamia elimu pamoja na walimu, kuhakikisha kwamba wanafuata Waraka ule Namba 24 wa mwaka 2002, lakini vilevile Kanuni ile inayofahamika kama The Corporal Punishment Regulations wa mwaka 2002.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike kwamba kwa wale walimu ambao hawatafuata waraka na kanuni hiyo,
wanakuwa wanafanya kosa na wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria inaitwa The Teacher Services Act ya mwaka 1989 kama ilivyorejewa mwaka 2002. Kwa hiyo, nawataka wote wafuate taratibu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba wenzetu wamefanikiwa vipi kuboresha elimu bila kutumia adhabu ya viboko.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge, pamoja na Wabunge wengine ni kwamba viboko havitumiki Tanzania pekee, hata Marekani huko ambapo ndio tunafikiri wameendelea sana majimbo 19 kati ya majimbo 50 ya Marekani mpaka leo hii yanatumia viboko. Naomba nimwambie kwamba Serikali haitumii tu viboko kama njia ya kuboresha elimu, kuna mengine mengi tunafanya, tunaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, viboko ni sehemu ndogo tu na tena tunatumia kidogo sana. Kwa hiyo asije akafikiri kwamba sisi tunatumia viboko tu. Kwenye hilo la viboko hatupo peke yetu duniani tunafahamu mtindo wowote wa kufundisha lazima uhusishe adhabu na zawadi (punishment and rewards).
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na natambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Serikali katika kuongeza uzalishaji wa umeme lakini nina swali moja tu la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha na kuwezesha kisera uwekezaji wa miradi midogo midogo ya uzalishaji wa umeme hususan katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa kama vile Mkoa wa Kigoma?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la Mheshimiwa Katimba. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia wazalishaji wadogo wadogo katika nishati kwa upande wa maeneo ambayo hayana gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kama ambavyo tumeeleza katika jibu la msingi, pamoja na kuzalisha umeme mkubwa katika maeneo mbalimbali yenye gridi ya Taifa, bado Serikali inahamaisha sana uzalishaji wa umeme mdogo mdogo katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa. Katika maeneo ya Kigoma mathalani; wazalishaji wadogo wameshajitokeza, Kampuni ya Nexgen Solar White imeanza kuzalisha megawatts tano ambazo sasa wanafanya majadiliano na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuingiza kwenye gridi ya Taifa. Kwa hiyo ni matumaini yetu maeneo mbalimbali ya Ujiji ambayo yameshafanyiwa utafiti kwenda mpaka Kaliua kuja mpaka Mkoa wa Tabora wazalishaji wataongezeka zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza maelezo ya upana zaidi kwenye suala la nyongeza la Mheshimiwa Katimba ni kwamba katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma na Uvinza ambayo hayajapitiwa na umeme wa gridi ya Taifa, hivi sasa Serikali imeanza kujenga njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa gridi ya Taifa ili Mikoa ya Kigoma na Katavi nayo ifikiwe na gridi ya Taifa. Sasa hivi ujenzi unaanzia Tabora kupitia Jionee Mwenyewe-Juhudi-Nguruka mpaka Kidawe Mchini-Kigoma, kwa hiyo, hata wazalishaji wadogo wa umeme mdogo mdogo nao wataingizwa kwenye gridi ya Taifa.