Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rose Cyprian Tweve (14 total)

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu yako Mheshimiwa Waziri, kwangu naona hayajitoshelezi. Nilitegemea ungenipa ni kiasi gani pesa zilitolewa kwenye hivi vikundi vya akinamama kila Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na urasimu mkubwa sana wa utoaji wa hizi pesa kwa akinamama especially kwa Wilaya zangu za Mufindi, Iringa Mjini, Kilolo na Iringa Vijijini: je, huoni umuhimu wa kutoa tamko rasmi kwa Wakurugenzi ambao watakwenda kinyume na utaratibu wa utoaji wa pesa hizi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, huoni wakati sasa umefika kwa Wabunge wa Viti Maalum kusimamia zoezi zima la utoaji wa pesa hizi kwenye vikundi vya akinamama? After all, wao ndio wametuchagua sisi kuwa wawakilishi wao. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza dada yangu Mheshimiwa Rose Tweve kwa ajenda yake na swali lake. Ni kweli, katika analysis, maana yake nilizungumza jinsi gani wanawake na vijana wamefikiwa. Nilichambua mchanganuo mbalimbali katika kila Halmashauri. Kwa figure halisi ni kwamba wanawake walipata sh. 339,487,000/= wakati vijana walipatana shilingi milioni 98. Hapa kuna mchanganuo mdogo wa kila Halmashauri kuona ni jinsi gani ilishiriki katika vile vikundi ambavyo i nimevibainisha awali kwamba vilipewa zile fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika Mkoa wa Iringa ni kwamba, kila Halmashauri, kama nilivyosema, kwa figure, akinamama walipata karibu shilingi milioni 339 na vijana milioni 98. Kwa suala zima la kutoa maagizo kwa Wakurugenzi, hili lilikuwa ni jambo langu la msingi zaidi. Nilizungumza siku tulipohitimisha bajeti yetu hapa, tukasema kwa sababu mwaka huu karibu takriban shilingi bilioni 56 zitakwenda kwenye vikundi vya akinamama na vijana, katika ule mgao wa asilimia tano tano. Nilisema katika bajeti yetu kwamba Wakurugenzi wote wa Halmashauri wana kila sababu kuhakikisha wanatekeleza hili.
Pia niliainisha tena, nikasema kwa sababu pesa za ndani maamuzi yake yanafanyika ndani ya Halmashauri, baada ya kupokea kwamba ni kiasi gani kimekusanywa, Kamati ya Fedha sasa inaweza kuhakikisha kwamba katika mwezi ule ule inatoa ule mgawanyo wa asilimia tano kwa tano kwa vijana na kwa akinamama.
Kwa hiyo, niliwahimiza Wabunge wote, kwa sababu sisi ni Wajumbe katika hizo Halmashauri zetu, tuhakikishe tunapokusanya own source tuwe wa kwanza kuhakikisha kwamba tunazielekeza pale pale, kwa sababu pesa hizi haziendi Hazina wala haziendi TAMISEMI, zinaishia katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Wakurugenzi wetu kwamba waende wakalisimamie hili. Vile vile niseme tena, Madiwani wote wanaingia katika Kamati ya Fedha na yale Mabaraza yetu ya Madiwani wahakikishe fedha hizi tano kwa tano zinakwenda kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Wabunge Wanawake kusimamia jambo hili kwa karibu; naomba niwaambie, hili ni jukumu letu sisi sote. Akinamama, vijana na Wabunge wote humu tuna jukumu hilo. Mimi lengo langu ni nini? Ni kwamba kila Mbunge ataona kwamba jambo hili ni la kwake. Mama akinufaika katika Jimbo hilo, maana yake unakuza uchumi wa watu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, vijana wakinufaika, maana yake unakuza uchumi wa vijana katika eneo hilo. Kwa hiyo, ni jukumu letu sisi sote, twende sasa tukalisimamie hili kwa nguvu kubwa kwa ajili ya mustakabali wa uchumi wa nchi yetu.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa asilimia kubwa ya wanawake hapa Tanzania wako kwenye vikundi vya ujasiriamali hususani Mkoa wangu wa Iringa na changamoto kubwa ya hivi vikundi havina miradi endelevu ambayo ingekuwa msaada mkubwa sana kuwasaidia hawa akinamama kuendelea kupambana na hizi changamoto zao wanazopambana nazo kila siku.
Sasa Mheshimiwa Waziri huoni hii ni fursa kubwa pamoja na kazi nzuri ambayo mmewasaidia vijana. Huoni hii ni fursa nzuri sasa kuwasaidia akina mama wote sio tu wale wanaozunguka ule msitu bali akina mama wote wa Mkoa wa Iringa na Wilaya zote, Iringa Mjini, Iringa Vijijini, Kilolo na Mufindi ili waweze kunufaika na msitu huu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana naye kabisa na huo ndiyo mwelekeo wa Serikali kuongeza ajira miongoni mwa vijana, lakini pia kuongeza ajira miongoni mwa akina mama. Sasa misitu ni eneo moja ambalo Serikali inaweza kufikia malengo yake ya kuweza kufanya vijana na akina mama wakaweza kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mwelekeo wa Serikali nitoe wito kwa Halmashauri zinazohusika katika Mkoa wa Iringa, baada ya akina mama kuwa wamejiunga katika vikundi basi waweze kupewa maeneo, halafu baada ya pale kwa shughuli zile za kiutaalam na utoaji wa mbegu na pia hata usimamizi wa kutoa utaalam na kuhakikisha kwamba mashamba hayo yanastawi vizuri wataupata kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuanzia sasa tuwe na mwelekeo wa kuhakikisha kwamba sekta ya misitu ichangie sana kwenye lengo la Serikali kuweza kutoa ajira za kutosha upande wa akina mama na kwa vijana.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa, kumekuwa na uhitaji mkubwa wa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, hususan Mkoa wangu wa Iringa na Wilaya ya Mufindi tuna Community Bank, sasa Serikali haioni kuwa hii ni opportunity nzuri kufungua dirisha pale kwa Benki ya Wanawake ili wanawake wote wa Mkoa wa Iringa waweze kunufaika na hii mikopo yenye riba nafuu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Rose Tweve kwa kuendelea kuwaseme wanawake, mtu yeyote yule akiwasemea wanawake maana yake anarahisisha kazi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya swali lake ni kwamba, wazo hilo la kufungua dirisha kwenye benki ya Mufindi Community Bank pale ni zuri sana na Serikali tunalichukua. Natumia jukwaa lako hili kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake kufanya jitihada za haraka kabisa za kuweza kutumia fursa hii ya pendekezo linalotolewa na Mheshimiwa Rose Tweve na kuangalia maeneo mengine yote nchini ambako kuna Community Banks.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kuna Meru Community Bank, kuna Mwanga Community Bank; tuna uwezo wa kufanya nao ushirikiano kwa kufungua madirisha maalum ya wanawake ili tuweze kuwafikia wanawake wengi zaidi katika nchi yetu. Hivyo, wazo lake tunalichukua.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Kwako Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na majibu hayo mazuri pia nikupongeze umekuwa champion mzuri wa vijana, watoto na wanawake na unatambua kuwa wanawake wengi hususani Mkoa wa Iringa wanakiu kubwa ya kujitafutia maendeleo ya kwao pamoja na watoto wao. Na kikwazo kikubwa kimekuwa upatikanaji wa hii mitaji na mikopo yenye riba nafuu. Pamoja na jitihada za Serikali za kufungua hivi vituo viwili pale Mkoa wa Iringa na kama ulivyokiri huu mchakato wa kufungua dirisha pale MUCOB umechukua muda mrefu, sasa ningeomba pia utupe kipaumbele na time frame ni lini sasa pale MUCOB tutegemee kituo hiki ili hawa akinamama waepukane nah ii adha ya kupata mitaji yao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, namshukuru Mheshimiwa Rose Tweve kwanza kwa kunipa compliment, mara chache sana Wabunge huwa wanawapongeza Serikali wanapofanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, time frame ni mpaka tutakapopata fedha kwa ajili ya kutunisha mtaji wa benki yetu. Lakini jambo la faraja ni kwamba kwa ahadi niliyoitoa hapa hapa Bungeni kwake yeye mwenyewe na kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba tuna-cosider kufungua dirisha pale MUCOB bado iko pale pale na ndio maana tumeiingiza kwenye mpango mkakati wetu.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Pamoja na maelezo hayo, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kabisa kwamba kumekuwa na dhana potofu kuwa kilimo kimekuwa kama last resort. Hata ukiongea na watoto wetu wa shule, ukiwauliza unataka kuwa nani? Mmoja atakwambia daktari, mwanasheria, engineer na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka nipate maelezo ya Mheshimiwa Waziri, ni mikakati gani sasa kama Wizara au incentives gani mmeziweka ili iwe kivutio kwa hawa Watanzania na vijana wetu ambao kuna tatizo kubwa la unemployment? Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika maelezo yangu ya mwanzo niliongelea suala la wataalam nashukuru kuwa Mheshimiwa Waziri ameli-address lakini kwenye ukosefu wa vitendea kazi, Watanzania wamekuwa wakiwalaumu sana wataalam hasa hawa Maafisa Ugani kuwa wamekaa tu Maofisini, lakini ukiangalia tatizo kubwa ni ukosefu wa vitendea kazi. Sasa napenda nipate maelekezo, ni mkakati gani kama Wizara mmeweka kuhakikisha hawa wataalam wetu wanapata vitendea kazi kama vile pikipiki na zana za kufundishia ili tuweze kuleta mapinduzi ya hii Sekta ya Kilimo? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuweka mazingira ya kilimo kuvutia watu wengi zaidi hususan vijana, naomba nimahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kilimo kinavutia sana na ndiyo maana hata baadhi yenu Waheshimiwa Wabunge ni wakulima hodari. Kwa hiyo, kizuri kinajiuza, kilimo kinalipa, tayari kuna watu wengi wamenufaika na hivyo niwasihi tu vijana kwamba kilimo kina manufaa. Vilevile Serikali imeweka mazingira mazuri sana ya kuwavutia vijana na ndiyo maana tumeweka taratibu za wao kupata mitaji, tumeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo, tuna Mfuko wa Pembejeo, lakini vilevile hata Benki za binafsi zinatoa mikopo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kilimo kinavutia, kuna uwezeshaji, kwa hiyo, vijana wanakaribishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na wataalam, Maafisa Ugani kutokuwa na vitendea kazi. Hili limezungumzwa sana, lakini mara nyingi vilevile imekuwa ni ksingizio. Kinachohitajika kwa Afisa Ugani anapokuwepo kwenye eneo lake la kazi ni elimu ile aliyonayo ajaribu kuitumia kuwafikishia wananchi. Mara nyingi katika ngazi ya kijiji huwezi kulalamika kwamba kwa sababu sina pikipiki, basi siwezi kuwafikia wananchi. Watendaji wengine wa Serikali walioko katika ngazi hizo wanafanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na ukweli kwamba kuna hitaji la kuhakikisha kwamba hivyo vitendea kazi viweze kupatikana lakini tunawasihi kwamba isiwe ni kisingizio. Lazima watumie elimu ambayo wanayo kwa sababu ni ajira yao ili kujaribu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kilimo bora.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pia naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa ambayo inaendelea kuwafanyia wakulima wetu. Nitakuwa na swali ndogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa wakulima wetu wengi especially Mkoa wangu wa Iringa wamekosa mwongozo na baadhi hawana uelewa ni kitu gani wanatakiwa kufanya ili bidhaa zao ziweze kufika kwenye Soko la Kimataifa, sasa Serikali iko tayari kuwa na Kitengo Maalum ambacho kitakuwa kinafanya kazi usiku na mchana, siyo tu kwa kutafuta masoko, bali kwa kutoa taarifa kwenye mikoa yetu juu ya hali ya masoko ya bidhaa ambazo wanazalisha? Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Tweve kwa swali zuri.
Kuanzia mwaka 2017 maelekezo ya Serikali ni kwamba Shirika la TanTrade lina jukumu la kuhakikisha kwamba linatafuta masoko ya mazao na bidhaa zote za Tanzania na lina wajibu wa kuhakikisha linatengeneza mtandao kupitia Halmashauri za Wilaya kwamba waweze ku-identify wakulima wana nini na masoko yako wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu tulionao sasa ni kwamba Wizara yangu kwa kushirkiana na Wizara ya Kilimo na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisa Biashara ngazi ya Wilaya watakuwa waki-link na TanTrade na hizi Wizara za kisekta katika kuhakikisha kwamba wakulima wanapata masoko ya mazao yao. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri mimi nilikuwa very specific kwenye swali langu la msingi, niliuliza ni watu wangapi waliomba fidia na wangapi wamelipwa mpaka sasa hivi. Kwa maelezo yako Mheshimiwa Waziri inaonesha jumla ya vifo na majeruhi ni zaidi ya elfu 14, hiyo ni kwa mwaka 2016 mpaka 2018 na ambao wamelipwa fidia mpaka sasa hivi ni watu 1,583, ni kama asilimia zaidi ya 10 kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa mwaka 2009 Bunge lilipitisha Sheria namba 10 ili kuwalinda waathirika wa ajali hizo. Sasa Mheshimiwa Waziri hawa wenzetu ambao wanaoshughulikia hili suala la bima hawa wenzetu wa TIRA (Tanzania Insurance Regulatory Authority) inaonesha kabisa kuna upungufu. Ambao wamekuwa beneficiary wakubwa wa hii issue ya bima ni hizi kampuni ambazo yanakatisha bima, lakini ajali inapotokea inaonesha kabisa Watanzania wamekuwa ni waathirika wakubwa ambao wameachiwa mzigo mkubwa. Sasa Mheshimiwa Waziri huoni ni wakati muafaka sasa tuanzishe idara maalum ambayo itakuwa inatoa elimu kwa Watanzania pale ajali inapotokea ili wajue hatua stahiki ambazo wanatakiwa kuchukua ili walipwe fidia zao? Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rose Tweve kwa ku-take serious concern ya Watanzania wanaopata matatizo hayo na kutokupata fidia ama kuchelewa kupata fidia. Niseme tu kama Serikali tunapokea wazo lake na kwa sababu tuna wataalam wazo hilo litachambuliwa kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Watanzania kuchukua hatua haraka za kufuata taratibu zinazotakiwa badala ya utaratibu ambao maeneo mengi wamekuwa wakifanya panapotokea matatizo ya aina hiyo; kuamua kuchukua sheria mikononi ama kuamua kufanya taratibu za njia za mkato ambazo zinasababisha wao kukosa kile ambacho walitakiwa wapate.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa demand ya zao hili la tangawizi imekuwa kubwa sana, kama Mheshimiwa Waziri alivyokiri hata majirani zetu Njombe wanalima zao hili, sasa ni mkakati gani wa makusudi ambao Serikali imeweka kuhakisha tunawajengea uwezo hawa wakulima wetu ili kilimo chao kiwe na tija? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Tanzania wana uwezo na wanaelewa, kinachoamua ushindi ni mahitaji ya soko (the market pool). Kwa hiyo tulichofanya, jambo la kwanza; Serikali kwa kushirikiana na Mbunge Mheshimiwa Anne Kilango tunaweka bilioni 1.7 kwenye kiwanda cha Tangawizi cha Same, tuchukue tangawizi yote tuichakate Same, tuweze kwenda kwenye soko. Soko likivuta zaidi wananchi watavutiwa na bei na watazalisha. Watanzania wanajua kinachoamua ni soko, panapokuwa na bei nzuri wananchi watazalisha hawahitaji ruzuku yoyote.
Kwa hiyo tunamuwezesha mama Kilango makusudi, tumempa bilioni 1.7 kiwanda kile cha Same kifanye kazi tutachukua tangawizi yote ikonekana mahitaji zaidi tutaweka Buhigwe, tutakwenda Ileje tutaweka kiwanda basi viwanda vitakuwa vinasababisha wananchi wanalima zaidi.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na mikakati mizuri ambapo Wizara inahakikisha tunatokomeza hivi vitendo vya ubakaji nadhani Walimu wana nafasi kubwa ya malezi ya watoto wetu. Kwa nini tusiweke kipengele maalum kwenye mitaala yao jinsi ya kubaini na kuwafanyia counseling hawa watoto mara wanapobaini kuwa wamebakwa? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli jambo hili kwanza linakera na linaudhi lakini si muda mrefu tulikuwa na kikao cha Maafisa Elimu wote wa Mikoa na Wilaya na jambo hilo tumeliwekea msisitizo hasa katika suala zima la kuhakikisha kwamba, watoto wa kike wanalindwa. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa ni mzuri, Serikali tumeuchukua na tutakwenda kuufanyia kazi kwa kadri tutakavyoona inafaa.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo yake Mheshimiwa Waziri amekiri kabisa kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi. Pamoja na mikakati mizuri ambayo Wizara mnaifanya, mtambue kabisa kwamba walimu wetu wa sayansi wana work load kubwa sana uki- compare na walimu wengine. Tuna shule moja Wilaya ya Kilolo inaitwa Shule ya Lukosi ina mwalimu mmoja wa sayansi kati ya watoto 700.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa Mheshimiwa Waziri; ni incentives gani kama Wizara imejipanga kuhakikisha inawapa motisha hata hawa walimu wachache waliopo ili wawe chachu kwa watoto wetu waweze kufanya vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo ameonesha concern kubwa kuhusu walimu wa sayansi, namna ambavyo tunaweza tukawafanya wajisikie kwamba Serikali inawajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo tumefanya kama Serikali, ni kuhakikisha kwamba tumeweka package ambayo ni nzuri zaidi kwa walimu wa sayansi hata wanapoanza kazi kuliko hata walimu wa sanaa. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu ya motisha kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasisitiza sana kwamba wanapofika katika shule, Walimu Wakuu na Maafisa Elimu wawapokee vizuri, wawape counseling ili wakubali kuishi katika maeneo wanayopelekwa, hilo ndiyo jambo la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tutaendelea kuboresha kwa sababu mengine hatuwezi kuweka motisha kubwa sana, kwa sababu nao ni watumishi sawasawa na watumishi wengine. Sasa kama utabagua, una watumishi ambao ni walimu halafu unabagua; huyu lazima apewe nyumba, huyu kwa sababu una uhasama naye, asipewe nyumba. Hicho nadhani itakuwa ni kitu ambacho siyo kizuri sana katika Taifa letu.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Changamoto ya Walimu wa Sayansi iliyoko Masasi pia inaukumba Mkoa wangu wa Iringa. Nataka commitment ya Mheshimiwa Waziri kwamba watakapopewa vibali vya kuajiri Walimu wa Sayansi mtaupa kipaumbele Mkoa wa Iringa? Nilitoa mfano last time kuwa Shule ya Lukosi ina watoto 700 na tuna Mwalimu mmoja tu wa Sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose Tweve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yale yote ambayo yana upungufu mkubwa wa Walimu wa Sayansi ndiyo hayo ambayo hasa yanaanza kupelekewa Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niutake Mkoa wa Iringa kwa ujumla wake watupe stock, maeneo ambayo yana upungufu mkubwa hayo ndiyo yawe ya kwanza katika kuhakikisha kwamba walimu wanapelekwa kwa ajili ya kwenda kuziba pengo hilo. Naamini na Iringa nao watafanya hivyo.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu limeshapatiwa majibu, lilikuwa linafanana na swali la Mheshimiwa Lwakatare.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, naomba nitoe ufafanuzi mdogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maswali ambayo yameulizwa sisi kwenye Wizara ya Kilimo tuna mpango mkakati wa kuendeleza kilimo ambao pia ulikuwa umezinduliwa juzi na Mheshimiwa Rais. Na suala la vijana pia limezungumzwa na hili jambo lipo, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tunatakiwa tuwe na vitalu nyumba kwenye kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ni kwamba kama Wizara ya Kilimo tuna mfuko wetu ule wa pembejeo ambao unatoa mikopo kwa riba asilimia saba hadi nane ili kumuwezesha mkulima aweze kunufaika. Vilevile niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote kupitia halmashauri zao waweze ku-endorse kule kwenye halmashauri ili mfuko wetu wa pembejeo uweze kutoa hii mikopo ya bure kabisa ambayo ni asilimia saba hadi nane; huo ulikuwa ni ufafanuzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tatizo la ubakaji na ulawiti kwa watoto bado ni changamoto kubwa sana, hasa kwa Mkoa wetu wa Iringa. Sasa wenzetu wa Chuo cha Mkwawa na RUCO walifanya utafiti na walibaini kuwa wazazi na walezi wamekuwa wanaachwa na mzigo mkubwa sana kugharamia matibabu ya watoto hao.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kuweka utaratibu maalum kwa matibabu, ukizingatia hawa watoto huwa wanaachwa na physical damage na psychological damage kubwa ili waweze kuwalea watoto hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Rose Tweve kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tulishalitolea tamko suala hili kwamba wahanga wote wa ukatili wa kijinsia Serikali itatoa matibabu bure.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nakubaliana kabisa na maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuwa pale Polisi anapokuta kuna umuhimu wa kusimamisha gari ambalo limevunja sheria ni muhimu wafanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa tumekuwa na hivi vituo maalum vya ukaguzi, sasa hivi kumekuwa na changamoto kubwa hasa kwenye mabasi ya daladala. Kumekuwa na unnecessary stop na kusababisha ucheleweshaji wa wananchi kwenda kufanya shughuli zao. Nitakupa mfano, unakuta daladala imesimamishwa na Traffic yuko pembeni ana-argue na Konda kwa nini hana proper uniforms? Haya ilibidi yafanywe kabla huyu abiria hajaingia kwenye gari.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilitaka kujua sasa kama Serikali na Jeshi la Polisi tumejipanga vipi kuhakikisha sasa tunakuwa na hii mandatory car inspection tofauti na utoaji wa stika wa sasa ukizingatia hizi stika zimekuwa zinatolewa kwenye magari yasiyo na viwango na kusababisha ajali kubwa za barabarani. Nakushuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana na ya msingi. Baada ya pongezi hizo sasa nitoe majibu ya maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mbali ya sheria ambayo nimeinukuu inayotoa mamlaka kwa Askari kusimamisha gari popote anapoitilia hitilafu, ambapo madhumuni ya sheria ile kimsingi inatokana na baadhi ya madereva wetu nchini ambao wamekuwa wakikiuka Sheria za Barabarani mara kwa mara, kwa mfano, utakuta mtu anaendesha gari kwa speed. Kwa hiyo, Askari akiona utaratibu wa uendeshaji kama huo, lazima achukue hatua.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe wito kwa wananchi hasa madereva kutii Sheria za Barabarani ili kuepusha usumbufu. Pili, nataka nichukue fursa hii pia kutoa wito kwa Askari wetu wa usalama barabarani nchi nzima ambao kama wapo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge najua atakuwa ame-experience hiyo, kama wapo ambao wanafanya utaratibu wa kusimamisha magari kiholela kwa kujifichia chini ya mwamvuli wa sheria hii bila kuwa na makosa yoyote, basi waache mara moja.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa lazima, nataka nimwelezee Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tumeshalitafakari kwa kina suala hilo na tunatambua kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa lazima ni jambo ambalo ni muhimu na haliepukiki katika karne hii tuliyokuwa nayo, siyo tu kwamba litasaidia kutoa fursa kwa magari yetu kukaguliwa vizuri zaidi na hivyo kuwa na magari salama barabarani, lakini itasaidia kuiongezea mapato Serikali na hususani Jeshi la Polisi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo tunazikabili. Kwa hiyo, kwa kutambua hilo tumekuja na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunatamani kwamba katika mabadiliko ya sheria ambayo itakuja, utaratibu huo utakuwa unasimamiwa na baraza jipya la usalama barabarani ambalo tunatarajia lije na muundo mwingine. Kwa hiyo, ni Baraza Tendaji, lakini hata kama matamanio yetu hayo bado hayajafikiwa au yatakuwa yamechelewa kufikiwa, tumeshatoa maelekezo kwa Shirika la Jeshi la Polisi (Police Cooperation Soul) kuanza mchakato wa kuanzisha utaratibu huo wa ukaguzi lazima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nichukue fursa hii vilevile kuwaelekeza Jeshi la Polisi kupitia Shirika hilo la Maendeleo kuharakisha huo mchakato ili uweze kuanza mapema ikiwezekana hata kabla ya Awamu hii ya Kwanza ya utawala wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijamaliza muda wake.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.