Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rose Cyprian Tweve (5 total)

MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Serikali imeweka utaratibu wa kuzitaka Halmashauri zote za Wilaya kutenga asilimia tano ya mapato ili kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo:-
Je, ni akinamama wangapi au vikundi vya wanawake vingapi vimenufaika na mikopo hiyo katika Halmashauri za Wilaya ya Mufindi, Kilolo, Iringa Mjini na Iringa Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake, Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimewezesha vikundi vya wanawake 430 na vikundi vya vijana 47 kupata mikopo.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi iliwezesha vikundi vya wanawake 331, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi vitatu, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 73 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa vikundi 23.
Kwa upande wa vikundi vya vijana; Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi vikundi 13, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi sita, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 28 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa hakukuwa na kikundi hata kimoja.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kupitia mfumo wa electronic ili kuongeza mapato yanayokusudiwa kufanya mifuko hiyo kutengewa fedha zaidi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila Halmashauri ilikuwa ni kuonesha kiwango kilichotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Napenda kulihakikishia Bunge lako kuwa tutaendelea kusimamia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua yoyote itakayobainika kuhujumu mpango huu wa kuwawezesha wananchi.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Ni azma ya Serikali ya CCM kumuinua mwanamke kiuchumi na azma hiyo ilipelekea Serikali kuanzisha Benki ya Wanawake.
Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kufungua madirisha ya benki hiyo mikoani hasa Mkoa wa Iringa ambapo kuna Community Bank (MUCOB) iliyopo Wilayani Mufindi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Desemba, 2016 Benki ya Wanawake imefanya kazi katika mikoa saba ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma. Mwaka 2014 madirisha mawili yalifunguliwa Iringa Mjini na Makambako na hadi kufikia Desemba, 2016 jumla ya wajasiriamali 6,850; wanawake wakiwa 5,350 na wanaume wakiwa ni 1,500 walipata mikopo kupitia madirisha hayo ambayo wajasiriamali wa Mufindi nao wamefaidika. Aidha, benki imefungua vituo vya kutolea mikopo 252 kufikia Desemba, 2016 na Mufindi kuna kituo kimoja kilichopo Mafinga ambacho kimetoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 120 kwa wateja 146, wanawake wakiwa 117 na wanaume wakiwa 32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania imeingiza suala la kufungua dirisha katika Benki ya Wananchi ya Mufindi (MUCOB) kwenye mpango mkakati wa mwaka 2012 mpaka 2017. Tunatarajia dirisha hili litafunguliwa mara tu tutakapopata fedha za kutekeleza mpango huu. Benki ya Wanawake ina mkakati wa kuenea nchi nzima, lakini kikwazo kikubwa ni ukosefu wa mtaji. Endapo benki itafanikiwa kupata mtaji wa kutosheleza itaweza kufungua ofisi zaidi mikoani ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi na kwa ukaribu.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Pamoja na kwamba sekta ya kilimo ndiyo yenye kuajiri Watanzania walio wengi, lakini sekta hiyo imekuwa na maendeleo hafifu kutokana na watumishi wachache wenye ujuzi wa kutosha na ukosefu wa vitendea kazi kama vile pikipiki, zana za kufundishia na kadhalika.
Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuwa na wataalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye kuajiri Watanzania wengi, hivyo mapinduzi ya kilimo pamoja na mambo mengine yatachangiwa uwepo na wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze kushauri matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuleta mapinduzi ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ugami wenye ujuzi ili kila Kata na kijiji kiwe na Afisa Ugani mmoja. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha na kuwezesha Vituo vya Kilimo na Vituo vya Rasilimali za Kilimo za Kata kwa ajili ya kufundisha teknolojia mbalimbali za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwaka 2016/2017, Serikali imeajiri Maafisa Ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya mahitaji ya Maafisa Ugani 20,374 katika ngazi ya kijiji, Kata na Wilaya. Jumla ya wataalam wa kilimo 8,000 ngazi ya Astashahada na Stashahada waliohitimu mafunzo katika Vyuo vya Kilimo wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali inaendelea kusomesha vijana tarajali na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa kusambaza teknolojia za kilimo bora kwa wakulima kwa kutumia njia mbalimbali hususan shamba darasa, vipindi vya redio na luninga, mchapisho na Maonesho ya Kilimo - Nane Nane.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo na mafunzo ya huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima nchini.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Kumekuwa na idadi kubwa ya ajali nchini zinazosababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali:-
• Je, kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2016
– 2018 ni ajali ngapi zimetokea na kusababisha vifo au majeruhi?
• Je, ni waathirika wangapi waliomba fidia na wangapi mpaka sasa wamelipwa fidia zao kutoka kampuni za bima?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani lilichukua hatua za makusudi kupunguza ajali ambapo mpaka kufikia Disemba, 2017 limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 kulitokea jumla ya ajali 9,856 ambazo zilisababisha vifo 3,256 na majeruhi 2,128. Mwaka 2017 kulitokea ajali 5,310 ambazo zilisababisha vifo 2,533 na majeruhi 5,355 wakati kwa kipindi cha Januari hadi Februari, 2018 zimetokea ajali 769 ambazo zimesababisha vifo 334 na majeruhi 698.
• Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 jumla ya waathirika wa ajali 1,583 walilipwa fidia yenye jumla ya thamani ya fedha za kitanzania bilioni 7.3 kutoka kampuni mbalimbali za bima.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Imekuwa ni kawaida sasa kwa Askari wa Usalama barabarani kusimamisha magari ya usafiri wa Umma kama vile daladala na mabasi na kadhalika:-

Je, ni lini Serikali itaandaa utaratibu wa kuwa na Vituo Maalum vya Ukaguzi huo ili kuokoa muda wa wasafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002 Kifungu cha 81, kinampa uwezo Askari Polisi wa kulisimamisha gari lolote barabarani au sehemu yoyote anapolitilia shaka na kulikagua au pindi linapokuwa limetenda kosa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani limeshaandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi wa mabasi ya Umma katika vituo vikuu vya mabasi vyote katika kila Mkoa ambapo mabasi ya abiria hufanyiwa ukaguzi kabla ya kuanza safari na pale yanapofika mwishoni wa safari.

Mheshimiwa Spika, aidha, ukaguzi wa pembezoni mwa barabara (road side inspection) ambao huhusisha mabasi ya daladala na vyombo vingine vya moto hufanyika katika vituo vya ukaguzi maalum (check points) ambavyo vipo katika barabara kuu na katika barabara nyingine za Miji pamoja na Majiji.