Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Najma Murtaza Giga (15 total)

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nihitimishe hoja ya kutambua na kuenzi mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza kusema, hakika kwake mola tumetoka na kwake ni marejeo, Bwana ametoa Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Watanzania tumepata pigo tumelia na uchungu kutokana na mapenzi makubwa tuliyokuwa nayo kwa jemedari wetu aliyetangulia mbele ya haki, iliyobaki ni kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu ampumzishe salama huko aliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa vile lisilobudi kutendwa naomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tuendelee na maisha yetu ambayo Mwenyezi Mungu ameturuzuku sisi ambao tuko hapa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutambua na kuenzi mchango wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuongea tu, haitosaidia kitu chochote. Kutambua na kuenzi mchango wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuongea tu haitasaidia chochote. Hivyo basi, niungane na wote waliounga mkono azimio hili kwa lengo la kuendeleza na kudumisha yale yote ambayo tumeyatambua na kukusudia kuyaenzi. Endapo tutafuata njia aliyotuonesha Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli nina imani tutakuwa tumeuenzi mchango wake kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan na Makamu wake Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, kuwa azimio hili litaweza kutekelezeka chini ya uongozi wao mahiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema na uwezo wa kumudu majukumu yao katika Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Najma, toa hoja ili niweze kuwahoji Wabunge.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa ni lazima nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananiwezesha kila jambo. Hata hivyo, pia sina budi kuushukuru Umoja wa Wazazi Tanzania kwa imani yao juu yangu kwa kunikubalia na kuniwezesha kuwa Mbunge ninayewawakilisha kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile sina budi kukushukuru wewe pamoja na Wabunge wote kwa imani yenu juu yangu ya kunikubalia kuwa miongoni mwa Wenyeviti wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee kabisa lazima nizipeleke kwenye uongozi mpya wa Awamu hii ya Tano unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli dhamira yao njema imeshaanza kuonekana, kwa hiyo tuwaombee tu Mwenyezi Mungu azidi kuwaendeleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia sina budi kabisa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Ummy pamoja na msaidizi wake, Naibu Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi nzuri waliyoanza nayo. Sina haja ya kuwalaumu kabisa, ni lazima niwapongeze. Changamoto ndiyo sehemu ya maisha na kazi yetu ni kuwashauri.
niongelee kwenye suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo Mheshimiwa ameainisha humu katika kiambatanisho namba 10.
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumza hapa kuhusiana na suala hilo kwa maoni tofauti, lakini naomba nielekeze moja kwa moja kwenye ushauri kwenye mambo sita tofauti ambayo ameainisha.
Suala la kwanza ni ukatili wa kingono. Hilo limezungumzwa, lakini nasema, pamoja na elimu ambayo itatolewa ambayo wamejipangia katika Wizara hii lakini ushirikiano wa karibu kabisa ni lazima kwa vitengo vya sheria. Mwanasheria Mkuu atanielewa nikisema zaidi kwamba ushahidi katika suala hili la hao wahalifu ni mgumu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bila ushirikiano wa karibu na vitengo vya sheria na kuhakikisha kwamba tunapunguza masharti ya sheria za ushahidi ili tuwadhibiti hao wenye vitendo vinavyofanya mporomoko wa maadili katika nchi yetu na kusababisha idadi inayoripotiwa kwa mwaka 2015 kufika 6,722 ambapo naamini kabisa idadi hii ni ya wale walioripotiwa tu, lakini kuna wengine huku ambao hawakuripotiwa wapo wanaathirika na janga hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukaribu baina ya Wizara pamoja na Wizara nyingine, ukajenga mnyororo madhubuti, tutaweza. Naamini kabisa mkituletea hapa Wabunge tujaribu kurekebisha hizi sheria za ushahidi wa jambo hili, basi hawa watakamatwa na watadhibitiwa na hivi vitendo vitapungua, vinginevyo tutaongeza vitendo hivi jamani. Kwa sababu hata Mwenyezi Mungu kwenye kitabu chake kitukufu cha Qurani amesema tusikaribie zinaa, hakusema tusifanye, amesema, tusikaribie kwa maana, tusipokaribia hatutofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ikiwa tutawadhibiti hawa kwa ushahidi mwepesi wakapatikana, wataacha na wao watakoma na Taifa letu litanusurika na janga la huu ukatili wa ngono kwa akinamama na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja suala la pili, utupaji wa watoto na wizi wa watoto, vitu viwili sambamba. Kuna watu wanahitaji watoto hawana, wanaiba. Kuna watu wanapata watoto wanatupa na wanakufa. Kwa hiyo, nashauri kwa Wizara hii hebu tujaribu, kama Wizara itakuwa ni vigumu labda kifedha, basi hebu tutoe uhamasishaji kwa wananchi waweze kujitolea kujenga vituo vya kulelea yatima ili wale akinamama ambao wanaona watoto wale hawawahitaji, wawapeleke wakalelewe kule na wale wezi waache kuiba wakachukue kule. Kwa hiyo, huo ni ushauri ambao pengine Serikali inaweza ikashindwa lakini wadau wengine watakubali. Kwa hiyo, naomba sana hilo tulifanye.
Mheshimiwa Spika, katika hilo hilo kuna suala la utoaji mimba. Hili naomba pia Wizara ilishughulikie, baadhi ya mimba zinazotolewa wanashirikiana na wakunga na manesi. Kwa hiyo, sasa hawa manesi wenye tabia hizi wadhibitiwe kwa sababu ni watu wachache wenye ujasiri wa kutoa mimba wenyewe, lazima wasaidiwe na wanaoelewa wanakuwa ni wakunga ama manesi. Kwa hiyo, sasa Wizara hii inabidi katika upande wake, katika sera zake na mambo yake, ihakikishe kwamba hao wanaofanya vitendo hivi wanadhibitiwa ipasavyo na kuadhibiwa ili kuondoa tatizo la utoaji mimba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiondokana na hayo nakuja kwenye mauaji ya vikongwe. Ni kweli inawezekana hawa vikongwe wanatuhumiwa, inawezekana ni kweli lakini kwa nini tuchukue sheria mkononi? Kwa nini, hakuna Serikali za vijiji? Hakuna uongozi wa vijiji? Kwa nini tusiende tukatoa taarifa kule. Kwa hiyo Wizara hii naomba sana kwa kushirikiana na vitengo vya sheria, narudia tena tudhibiti jambo hili kwa kuhakikisha tunatoa elimu tosha ya kuelekeza wananchi wetu vijijini ili waende wakatoe taarifa wanapoona kwamba kuna wazee wanahatarisha jamii yetu, basi waende wakashughulikiwe kisheria kuliko kuchukua hatua au sheria mkononi ya kwenda kuwaua wazee wetu, inawezekana wengine si kweli. Kwa hiyo, naomba sana hilo nalo tulifuatilie kwa uzuri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija suala la nne, mashambulio ya kudhuru na lugha za matusi. Hii zamani ilikuwa haipo kabisa jamani. Utamaduni wetu sasa unaporomoka, ni tatizo kubwa. Naomba sana niwashauri Wabunge wenzangu humu ndani, tuanze sisi na lugha nzuri. Sioni sababu ya kutoa lugha ya matusi wakati tunaambiwa maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Kwa hiyo, sasa wale wanaotusikia nje au wakihadithiwa nje kwamba Wabunge ndani wanazungumza lugha mbovu, tutakuwa hatuna mfano mzuri kwa wananchi wetu. Haya matendo yanazidi, idadi yake ni kubwa mno hapa tunaambiwa 14,561 mashambulio ya kudhuru pamoja na lugha za matusi. Kwa hiyo, naomba sana sisi Wabunge tuwe mfano ili image yetu iwe reflected nje, watu waweze kuwa na adabu nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tano ni utelekezaji wa familia. Naunga mkono kweli elimu ni ndogo, pengine vijana wetu wengi hawajui nini maana ya familia, lakini bado narudi tena pamoja na kutoa elimu kuna akinababa wengine wazima zaidi ya miaka 40, anatelekeza familia yake anakwenda kutafuta mwanamke mwingine. Hili ni baya sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kabisa hii Wizara inayohusiana na jinsia jamani Mheshimiwa Ummy, hawa akinababa wenye tabia hizi na wana uwezo wao wengine wanafanya kazi na wana uwezo tuwadhibiti, tukiwajua wakatwe baadhi ya mshahara wao ama vipato vyao viende kwenye familia zile.
Mheshimiwa Spika, pia sisi akinamama nao wake wa pili, nyumba za pili, tusiwe na roho mbovu, tusidhibiti kila kitu. Tuwaachie akinababa wawashughulikie na akinamama wenzetu wengine na familia zao. Hili ni jambo zuri sana, naomba jamani kwa heshima kubwa sana hili tulifikirie na tulizingatie, litaondosha kabisa tatizo hili jamani.
SPIKA: Mheshimiwa Najma, sijakusikia vizuri. (Kicheko)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, nasema kwamba kuna tabia ya akinababa hawa ambao ni watu wazima zaidi ya miaka 40, wanaacha familia zao za kwanza, yaani nyumba ya kwanza wanatafuta nyumba nyingine, ile wanaitelekeza. Kwa hiyo, hili ni jambo baya. Hawa wadhibitiwe na kama wanafanya kazi wana uwezo basi kile kinachopatikana wagawiwe familia ya kwanza.
Pia na akinamama hawa wa nyumba za pili, tuwe na huruma kwa akinamama wenzetu wa nyumba za kwanza. Nafikiri hili limeeleweka vizuri na naamini kabisa utelekezaji huu utapungua, tukifanya hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, namalizia kuhusu mimba za wanafunzi. Mimba za wanafunzi zinaweza kuleta madhara kwa wasichana wetu na kuwayumbisha kimaisha jamani! Hapa tunaambiwa idadi ya ripoti ni 412 lakini naamini ziko nyingine ambazo hazijaripotiwa. Kwa hiyo, hili suala nalo tulidhibiti vizuri kwa kushirikiana tena na vitengo vya sheria. Ikiwa ni mtu mzima amempa mimba mwanafunzi, basi huyu asiachiwe, adhabu iwe kali. Vilevile ikiwa ni mwanafunzi na mwanafunzi waadhibiwe wote wawili ikiwezekana, kwa sababu wengine wakome. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yangu kwa kweli yalikuwa ni hayo. Nakushukuru sana kwa muda huu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Najma….
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja wala sina haja ya kupinga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niende direct to the point na naingia kwenye ukurasa wa 101 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu haki na maendeleo ya mtoto. Ninashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri mwenyewe kwamba ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini na asilimia 28 ambayo imeoneshwa kuongezeka katika wanaoripoti kuanzia mwaka 2016/2017 mimi ninasema bado hiyo itakuwa ni kidogo ikiwa Watanzania wengi watalielewa hili suala. Kwa hiyo, tunaweza tukafika hata kwenye asilimia 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi tena kwenye ombi langu, namwomba Mheshimiwa Waziri kigezo cha kusema kwamba hawa wabakaji sugu, nikisema wabakaji sugu wa watoto wa kike na wa kiume sikusudii mtu mwingine yoyote, sikusudii mbakaji wa mume kwa mke, hilo ni lao. Nakusudia watoto wadogo wa kike na wa kiume. Naomba sana tuache hii ya kufikiria kwamba tunapowaamulia au kuwatungia sheria hawa wabakaji sugu kuhasiwa, ni kosa au ni haki za kibinadamu, naomba nije kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ninukuu; “Haki na uhuru wa binadamu ambapo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.”

Pili, inasema: “Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo kwa ajili ya:- (a) kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutumia ibara hiyo, ninaomba nikushawishi na ninaomba nishawishi Bunge, mwisho wa siku tusipolivalia njuga jambo hili litakuwa ni janga la kitaifa. Ninasema hivi nawaambieni mfano, mwisho wa siku hatima yake, kiongozi ambaye yupo mbele yetu sasa hivi ni mwanaume, atakuja kiongozi ambaye ana ndoa ya jinsia moja, hilo ndiyo mwisho wa siku. Kwa hiyo, naomba tusifanye masihara wala tusione hili jambo ni la utani. Taifa letu la kesho linakwenda kuangamia. Taifa letu lenye utamaduni bora Tanzania linakwenda kutoweka ikiwa tutakuwa hatupo makini katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema, Mheshimiwa Waziri kaa na Wizara husika tuangalie namna bora ya kutengeneza sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wetu wa kike na wa kiume ili tuweze kuondokana na janga hili sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu ya leo.
Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kwanza. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika mwezi huu wa Ramadhani tukiwa wazima na kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hotuba ambayo imetolewa na Wizara hii ya Nishati na Madini. Kwa kweli Serikali kwa upande wa Wizara hii imejitahidi. Vyovyote tutakavyofanya na kusema hatuna budi kuishukuru Serikali kwa jitihada inazochukua katika suala la sekta hii ya nishati na madini hasa tukizingatia usimamizi imara uliopo katika Awamu hii ya Tano ya Serikali yetu chini ya uongozi makini kabisa wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia sina budi kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa namna ambavyo amepokea wito wa uungwana kabisa na busara kulipokea deni ambalo ZECO inadaiwa na TANESCO na kuahidi kulilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile dawa ya deni ni kulipa, Mheshimiwa Rais amechukua hekima na busara kuweza kukubali na mpaka hivi sasa deni la shilingi bilioni 11.8 limeshalipwa ambapo shilingi bilioni 10 zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shilingi bilioni 1.8 zimelipwa kupitia ZECO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hatuna budi kuipongeza Serikali kupitia TANESCO, tusipoipongeza tutakuwa hatuna shukrani. Pamoja na upungufu yote ambayo TANESCO inayo lakini kazi inayofanywa lazima tuishukuru na kuithamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwenye kitabu humu miradi mbalimbali imeshatekelezwa ikiwemo Kinyerezi I na II ambazo zinaendelea lakini pia tuna REA, usambazaji wa umeme vijijini, kazi inafanywa kubwa kwa mazingira magumu. Tukipita sisi wengine tunaona juu ya milima kuna nguzo huko, tunashangaa zimetandazwaje, chini ya mabonde huko tunakuta nguzo tunashangaa zimetandazwaje, lazima tuwe wenye kushukuru na lazima tuwapongeze. Naamini kwamba Serikali kupitia TANESCO itatatua changamoto hatua kwa hatua ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utaelekea huko huko kwenye nishati ya umeme na hapa nitazungumzia mfumo uliopo baina ya Shirika la TANESCO na ZECO. Niseme wazi kwamba kutokana na mfumo uliokuwepo siku za nyuma na pengine huu uliopo sasa hivi, ndiyo umepelekea ZECO kuwa na deni kubwa kwa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee yale ambayo yamepeleka mfumo huu kuonekana kama unaendelea kuipa deni ZECO. Kwanza ni tozo ya KVA. Hii nikizungumza wataalam wanaelewa, ni tozo ya watumiaji wakubwa wa umeme kwa mfano viwanda na kadhalika. ZECO tunachukua kilovoti 132 kwa bei ya shilingi 16,550 lakini watumiaji hawa wa kilovoti 33 ambao wanachukua kwa Tanzania Bara wanatozwa shilingi 13,200 kwa kilovott moja. Kwa hiyo, utaona difference iliyopo ya mfumo katika uendeshaji na kuipelekea ZECO kuweza kulimbikiza deni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wawekezaji ambao wana tamaa ya kuwekeza Zanzibar wanashindwa kuwekeza kwa ajili ya tozo hii, hivyo naomba sana Serikali ilizingatie. Kwa mfano, mwaka 2011 utaona pia mtiririko wa mabadiliko ya tozo unavyobadilika, naweza kutoa mfano mwaka 2011 ZECO iliongezewa tozo ya asilimia 81.1 wakati Tanzania Bara iliongezwa tozo ya asilimia 19.4 tu, ni difference kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali izingatie sana kupitia Shirika hili la Umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa mfano pia mwaka 2013 TANESCO na ZECO walikubaliana kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwamba sasa umefika wakati hizi kilowatts per hour Zanzibar ipunguziwe kwa asilimia 31. Matokeo yake, TANESCO iliendelea kuingiza hiyo asilimia 31 hatimaye deni hili likatajwa mwisho wake kuwa ni shilingi bilioni 121.9 ambayo round figure ni shilingi bilioni 122 wakati ZECO wanaendelea kuhesabu kwamba wameshatolewa punguzo la asilimia 31 na kulikubali deni hilo kuwa ni shilingi bilioni 65.5. Kwa hiyo, tunaweza kuona difference hizo na naomba sana Mheshimiwa Waziri husika na timu yake waweze kuangalia kwa upande huu wa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la ZECO kuwa end user, nikizungumza end user anakuwa kama mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara anapelekewa umeme kupitia miundombinu ya TANESCO lakini ZECO tunaletewa umeme kwa bei ambayo mtumiaji wa Tanzania Bara anapewa with operational costs za ZECO, miundombinu na gharama zote ni za ZECO. Kwa hiyo, tuangalie hali inavyokwenda tuone mfumo uko vipi, nia yangu ni kueleza mfumo huu tuweze kuusahihisha ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hili tunasema kwamba ZECO na TANESCO ni mashirika ya Serikali, moja kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na lingine kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. ZECO yenyewe inakuwa na madeni ambayo inadai Taasisi za Serikali ikiwemo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Wizara yake imeweza kupunguza shilingi milioni 400 deni ambalo tulikuwa tunawadai na sisi ndiyo tumeweza kurudisha TANESCO. Kwa hiyo, tuangalie haya mambo ili sisi tuweze kulipa deni na Serikali taasisi zake iweze kulipa. (Makofi)

Kwa hiyo, hilo ni moja ambalo nilipenda nizungumzie kwa upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna huduma nyingine za jamii ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja. Kwa mfano, ZAWA ambayo inashughulika na masuala ya kusambaza maji Zanzibar, tunaidai zaidi ya shilingi bilioni 20. Tunashindwa kuwafungia umeme kwa sababu Watanzania wanaoishi Zanzibar watakosa maji. Kwa hiyo, inabidi shirika hili tuone mfumo gani ambao utaweza kuwa bora na mzuri ili tusije tukaingia kwenye migogoro ambayo mimi sipendi kuiita kero, nasema bado ni challenge, tuzirekebishe hizi challenge ili Watanzania wote wanaoishi Tanzania Bara na wale walioko Zanzibar ambao wote ni wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania waweze kunufaika na huduma hii bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili Shirika la ZECO linafanya kazi kubwa kuikusanyia mapato TANESCO. Mbali na hayo madeni ambayo yametokana na hizo sababu nilizozitaja, tunatumia umeme kuanzia shilingi milioni 400 hadi shilingi milioni 500 kwa mwezi na bahati nzuri kuanzia mwaka 2015 Desemba tunalipa current bill kwa maana kwamba ankara kamili ya kila mwezi. Kwa hiyo, ili kuweka sawa mambo haya, tuonekane na sisi ZECO kule kwamba tunaifanyia biashara TANESCO ambayo ni taasisi ya Jamhuri yetu ya Muungano Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mwingine, tumeweza kuikusanyia shilingi bilioni 41.8 katika kipindi cha miezi tisa kuanzia 2016 hadi kufikia Machi, 2017. Kwa hiyo, sasa nachoshauri mbali na kuwekwa huyu Mtaalam Mwelekezi nitaomba ushauri wake ufuatwe ili twende sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kwamba sisi ZECO basi angalau tupewe fursa ya kuwa agent wa TANESCO ili tuweze kulipwa na kuweza kugharamia operation cost ili tusiweze kuleta migogoro katika Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, pamoja na kuunga mkono hotuba hii naomba sana ushauri huu uweze kuzingatiwa ili tuweze kuimarisha Muungano wetu. Ahsanteni sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii kuwa mchangiaji wa mwanzo kwa siku ya leo katika kuboresha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa hai na wazima hadi leo na afya njema tukaweza kuendelea na majukumu yetu, kwa hiyo naomba nianze moja kwa moja kuboresha mpango wetu huu ambao umeletwa mbele yetu katika eneo la uwezeshaji wanawake lkiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili ni muhimu sana na ndiyo maana nimelitenga kwa upekee wake niweze kulichangia kwa siku ya leo. Pamoja na kuipongeza sana Serikali kwa mkakati ambao unafanywa katika kuongeza juhudi za kuwawezesha Wanawake kiuchumi katika maeneo mbalimbali hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu mimi naomba nielekee kwenye maeneo hayo ambayo yanashughulikiwa hasa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mpango wa TASAF, najua nia ya Serikali ni njema hapa lakini niseme tu kwamba mpango huu unawanufaisha wale wanawake ambao wako mfuko tu na pia hao wanawake ambao wako kwenye mfuko huu wa TASAF au mpango huu wa TASAF wananufaika kwa kiasi gani hilo hatujui, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri labda pengine ukija utueleze namna gani wanawake ambao wako kwenye mpango huu wa TASAF wananufaika kwa kiasi gani, lakini ambao awamo kwenye mpango huu hawana manufaa yoyote wanayoyapata kwa hiyo bado mpango huu haujawafikia wanawake kwa namna ambavyo inastahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna Benki ya Wanawake ambayo imeunganishwa sasa na TPB na kufunguliwa dirisha maalum kwa ajili ya wanawake, mimi nashauri sana Mheshimiwa Waziri dirisha hili likusudiwe kwa lengo lililokusudiwa yaani lifanyiwe kwa kazi kwa lengo lililokusudiwa ikiwa ni dirisha la wanawake liwe ni la wanawake tu na kisingiie kitu kingine chochote na isiwe kwavikundi ianzie from individuals to the group ili mwanamke wa kitanzania afaidike na hii benki ambayo imewekwa kupitia TPB au dirisha hili la wanawake ambalo limewekwa kupitia TPB. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukija kwenye mpango mwingine ambao umeanzishwa na Serikali ni uanzishwaji wa jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi nawapongeza sana dhamira ni njema lakini hatujui bado jukwaa hili kwa kiasi gani litaweza kuwafikia wanawake wote Tanzania na kuweza kuwezesha ili tuone uchumi wetu unazidi kupaa kwa kasi kabisa. Kama amabvyo nimesema benki ya TPB ambayo tuna dirisha ya wanawake bado kuna umuhimu wa kuonyesha kwamba benki hii itawafikiaje wananchi wanaoishi vijijini kwa sababu lengo si kuwasaidia wanawake walioko mijini tu uwezeshaji wa wanawakekiuchumi ni kwa watanzania wanawake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukija kwenye suala la asilimia nne ya vijana; asilimia nne ya akina mama na asilimia mbili inayoenda kwa watu wenye ulemavu katika Halmashauri zetu hii bado ni changamoto kwa sababu ile asilimi nne inaenda kwenye vikundi maalum, kwa hiyo hitaji la mwanamke kama mwanamke na familia yake bado haijafikiwa kwa lengo lililokusudiwa, watapata mahitaji kwa kiasi cha chini, mahitaji madogo kama ya chakula kwa hiyo si mbaya lakini tuzidi kuiboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa nataka nijue hii asilimia mbili ambayo inaenda kwa wenzetu wenye ulemavu hawa hawana makundi, lakini kuna walemavu wenye ngozi na waliokuwa hawaoni, kuna ambao walemavu wa masikio, wako kila aina sasa sijui utekelezaji wake unakuwaje labda Mheshimiwa Waziri utakapokuja utuoneshe namna gani asilimia mbili hii inayoenda kwa wenzetu wenye ulemavu inatekelezwa na inawafikia na labda faida zake zilizopatikana mpaka sasa hivi katika hiyo asilimia mbili ambayo inaenda labda itapatikana vipi faida katika hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa heshima zote nimeamua kusudia kuweka kwenye eneo hili la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa sababu nina sababu nyingi sana, wanawake Tanzania tuko wengi, wanawake Tanzania tunajiweza kwa mambo mengi, kwa hiyo tunapopata fursa ya uchumi katika nchi hii Mheshimiwa Mpango na mipango yako mizuri uliyonayo basi uchumi wa Tanzania utakwenda kwa kasi kuliko hiyo ambayo umefikiria. Kwa hiyo mimi nasema hili kwa maana ya kwamba nina sababu za msingi, mwanamke anapojiweza kiuchumi familia yake inaimarika, hatokubali mtoto asiende shule, ataelimisha kwa kadri ya uwezo wa mtoto kusoma. Lakini pia lishe ya nyumba itakuwa safi ya baba na watoto, pia afya itakuwa imezidi kuimarika katika familia tutapunguza matatizo mengi yaliyo changamoto katika Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utekelezwaji wa watoto litapotea itakuwa si changamoto tena, mwanamke anajiweza kiuchumi, wewe mtelekeze yeye anaendelea na shughuli zake. Kwa hiyo jamani kuwezeshwa mwanamke kiuchumi ni jambo la msingi kabisa katika Taifa letu. (Makofi)

Naona wanawake tumefurahi lakini ndio ukweli ulivyo hivyo kwamba wanawake Tanzania Mheshimiwa Waziri Mkuu unanisikia ikiwa tutawezeshwa vizuri basi nakwambia uchumi wa nchi hii utapaa kwa namna ambayo ni ya ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa wana baba nawaombeni tuna Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kabisa ambaye anajaribu kuweka njia ya kuinyoosha Tanzania tuelekee kule ambako tunakutaka na mimi naomba aendelee hivyo nashukuru sana Mwenyezi Mungu ametuletea kiumbe ambaye anajaribu kunyoosha pale tulipopinda. Kwa hiyo, naomba Mungu atujalie tuendelee hivyo kwa hiyo lakini turudi siharibu hebu niacheni.

Sasa naomba nirudi kule kwa sababu kama hili ambavyo anatunyoosha kuelekea kwenye mambao mazuri tunayoyataka na wanawake atunyooshee tuendelee hivyo hivyo tutafika pahala pazuri sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mpango huu ambao nimeusoma baada ya kutoka kwenye ajenda yangu hiyo, huu mpango mimi wala sina pingamizi nao najua kazi unayofanya ni nzuri na hii kazi ni nzuri zaidi kwa sababu pembeni yako kuna mwana mama hapo ambaye yuko vizuri, ana upendo, ana huruma na yuko makini sana hapo, kwa
hiyo haya mambo yanakwenda vizuri mimi naamini Wizara zikiwa na mama na baba mambo yatakwenda vizuri kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naendelea kusema kwamba huu mpango kwa kweli naomba niwaambie Watanzania najua lazima mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni kazi zinazofanywa sio mbaya na tusiwadanganye Watanzania si kila jambo litakalofanywa na Serikali litawanufaisha watu wote ndege zinapoboreshwa Tanzania, watakaonufaika wapo na ambao watakuwa hawajui faida yake wapo lakini wakiwa wanufika si wananufaika katika nchi hii. Kwa hiyo sasa leo ndege yetu inakwenda China wafanyabiashara wataacha Ethiopian Airline, wataacha Kenya Airways, watapanda ndege yetu ya Tanzania watakwenda kufanya biashara zao kwa hiyo na mambo mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaboresha umeme ukawa umeme mzuri zaidi tutafaidika na viwanda ambavyo tunavipigania, yote ni sahihi tuna changamoto, changamoto ni sehemu ya maisha, hizi changamoto ambazo amesema hapa Mheshimiwa Mpango ziko dunia nzima. Kwa hiyo hayo sio tatizo lakini na conflict (migogoro) katika dunia ipo sehemu zote kuna migogoro ya kisiasa, kuna migogoro ya kiuchumi, muhimu ni namna gani ya control ile migogoro isilete madhara katika dunia. Kwa hiyo, hayo naomba tuweke umakini sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala langu ambalo nimelizungumzia huu mpango huu pamoja na uzuri wake wote suala la uwezeshaji wanawake kiuchumi ndio mpango mzima, kama nilivyosema kwamba hii mipango ni mizuri sana lakini sekta tukimuweka mwanamke akawezeshwa basi mipango yote hii imeshamalizika haina jambo jingine ambalo litakuwa la ziada.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nitachangia katika taarifa ya Kamati ya Katiba na Sheria katika maeneo machache, lakini la kwanza nitaanza ni katika suala la kuwajengea uwezo kiuchumi vijana ambalo linafanyika kwa kutumia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Naomba nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada ambazo zinafanyika katika kuwawezesha hawa vijana ambao ndiyo inapunguza kasi ya changamoto ya ajira katika nchi yetu. Hilo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo ya kwamba sehemu hii mwaka 2015/2016 zimetolewa bilioni moja; 2017/2018 zimetolewa bilioni 2.7; na naamini baadae wataendelea kutoa zaidi na zaidi, hii ni nia njema. Tatizo ndiyo hilo changamoto imeonekana, naomba niiseme ili iweze kufanyiwa kazi na Serikali, ni usimamizi wa hivi vikundi vya vijana ambao wanapewa hizo fedha, yaani hizi SACCOS. Kwa kweli imeonekana kwamba hizi fedha zimetolewa kwa lengo jema, lakini vikundi ambavyo vinapewa vinaonekana kwamba vinatumia hizo fedha kinyume cha malengo waliyojiwekea, hiyo ni changamoto. Pia inaonekana kwamba hizo fedha pia zinatolewa bila kuelewa kama hicho kikundi kweli kipo ama hakipo. Kwa hiyo wito wangu ni kwamba Serikali iweze kuzisimamia au kuzishinikiza halmashauri zetu ziweze kusimamia hivi vikundi vya vijana ili lengo jema kabisa la Serikali ambalo limekusudiwa liweze kufanikiwa. Hiyo ni sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la ufinyu wa ukomo wa bajeti kwa baadhi ya taasisi zinazosimamiwa na Kamati ya Katiba na Sheria ambayo ni miradi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika sehemu ya Bunge, Kazi, Vijana na Ajira na Wenye ulemavu. Hii imeonekana kwamba miradi mingi inategemea fedha za nje, hii ni changamoto. Kutegemea fedha za nje ni changamoto na kwa nini nasema hivyo? Nasema kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaligundua hilo kama ninavyoliona mimi na Watanzania wengi naomba waelewe hivyo. Fedha za ndani ni muhimu, kwa hiyo ili tuweze kupata fedha za ndani lazima wananchi tuhimizwe kukusanya kodi kwa wakati, tulipie, tuwe watiifu, tutengeneze miradi mingine kupitia Serikali yetu ili tuongeze vyanzo vya mapato ya ndani ya nchi yetu na hili jambo linafanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuongeze jitahada ya kuunga mkono Serikali kuongeza mapato ya ndani ya nchi. Misaada ina madhara, Waheshimiwa pamoja na Watanzania naomba tuelewe hivyo, ukiona unasaidiwa, basi kuna lengo fulani linatakiwa huko. Kwa hiyo sasa hii tuikwepe kwa njia yoyote na napongeza sana kwa kweli jitihada za Mheshimiwa Rais ameliona hilo na ameligungua na ndio maana anakwepa hii misaada ya nje kwa gharama yoyote. Kwa hiyo na sisi tumuunge mkono tuendelee kupigania fedha zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo kubwa ambalo nimeona pia ni upande wa magereza, naomba nizungumzie kwa upana wake. Lengo la kuweka magereza ni kuwapa mafunzo wale wanaofanya makosa ya aina mbalimbali ili wakitoka nje uraiani waachane na hayo, wafanye mambo mema ili wawe kama raia wa kawaida waweze kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo naomba niielezee hapa kwa undani, ni jinsi ambavyo magereza yetu pamoja na mahabusu zinavyokusanya wafungwa wa aina tofauti; mwizi wa kuku, mbakaji, muuaji, jambazi sugu, wote wako pamoja wanafungwa pamoja. Si hivyo tu, mwenye miaka 18 ambaye anajulikana huyu sasa ni mtu mzima na kuendelea hadi kufika 30 humo humo ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokusudia hapa ni hivi, tunawaweka kule ili wapate mafunzo, wakija uraiani wawe watu wema, badala yake mule ndani watoto wetu ambao ni vijana kuanzia miaka 18 ni kijana tunavyosema kwa mujibu wa sharia, wanatoka mule ndani wamebakwa, wamelawitiwa, wanarudi uraiani wameisha hawana nguvu kazi ya vijana, kwa hiyo hilo nalo tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufanye mpango maalum wa magereza yetu kupitia Serikali ili tuone utaratibu maalum hawa wabakaji sugu wawekwe tofauti na watu wengine, wananitia uchungu mimi wanawaharibu watoto wetu vijana. Pia hawa wauaji, majambazi sugu nao wanafundishana vitendo viovu, wanaweza wakawafundisha vijana wetu mambo ambayo yatawajengea uwezo, wakitoka huku nje badala ya kuwa mwizi wa kuku anakua muuaji, kwa hilo jamani naomba sana Serikali itafakari kwa kina kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina pingamizi na hukumu zinazotolewa mahakamani, hata ukija kwenye hiyo money laundering yaani utakatishaji wa fedha, inawezekana yule mtu ambaye amefungwa kwa kutakatisha hizo 300,000, hizo 300,000 zimepatikana labda pengine kwa mafunzo ya ugaidi, kwa mafunzo ya uuaji, kwa hiyo anaweza akafungwa hata miaka sita, hata miaka 10 hata zaidi there is no ploblem. Kwa hiyo hiyo mimi sina pingamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba upande mwingine nimalizie kwenye challenge ambayo tunayo kwenye mazingira wezeshi ambayo wenzangu wamezungumza na mimi nitumie fursa hii kupongeza uongozi mzima wa Bunge naona jengo letu linakarabatiwa kwa hiyo kutakuwa na lift karibuni na itakuwa ni mazingira wezeshi kabisa kwa wenzetu wenye ulamavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwamba sasa Serikali iweze kuona mpango mzuri wa kutekeleza sheria ya mwaka 2010 ili Baraza hili sasa la Watu Wenye Ulemavu liweze kuanzishwa lakini pia na Mfuko wa Maendeleo ambao umekusudiwa kwenye sheria hii uweze kuanzishwa na kuweza kuwasaidia kwa umakini hao wenzetu wenye ulemavu. Suala la mwisho katika upande wa watu wenye ulemavu ni kwamba, halmashauri zetu ziweze kushughulikiwa kwa ukamilifu kuona kwamba ile asilimia mbili inawafikia walengwa kwa wakati mahususi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo natumia fursa hii kukubali hoja hii ya Kamati ya Katiba na Sheria kwa maana ya taarifa nzima kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais, sina pingamizi, mambo yanakwenda vizuri, changamoto ndogo ndogo naamini zitafanyiwa kazi, lakini
kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu nao pia nitumie fursa hii kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Mifuko ya WCF, OSHA na Taasisi zote zinafanya kazi kuwawezesha wafanyakazi wetu katika hali nzuri kufanya kazi, pia malipo ya fidia nayo yanafanya kazi kwa uzuri, kwa hiyo nitumie fursa hiyo, kama kuna changamoto ndogo ndogo tuzirekebishe. Kwa ujumla wake natumia fursa hii kukubali hoja zote za Kamati kama zilivyo, lakini na kuipongeza Serikali kwa kadri ambavyo wanajitahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa dakika hizo tano. Kwanza kabisa, naanza kwa kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Muungano. Nitumie fursa hii kumuunga mkono sana na kuwapongeza Waziri wa Muungano, Mheshimiwa January Makamba na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Mussa, kwa kazi nzuri wanayofanya lazima niwapongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natumia fursa kwa kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameondoa changamoto iliyokuwa inatukabili muda mrefu ya deni la ZECO. Hilo lazima tushukuru sana na kupongeza na hii inathibitisha kwamba Mheshimiwa Rais ni muumini wa kweli wa Muungano wetu. Hilo lazima tulioneshe na Watanzania lazima waelewe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mazuri yanayofanywa na Mheshimiwa Janauary na timu nzima, napenda kusema kwamba sote tunaupenda Muungano, mimi ndiyo muumini wa kwanza wa Muungano. Katika kuupenda Muungano tunaomba hayo ambayo mmeyakusudia na kuyaendeleza muyafanyie kazi inavyostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize maeneo matatu kwa haraka haraka. Fursa za kiuchumi Zanzibar ni jambo linalopigiwa makelele siku zote. Miaka ya 1985 mpaka tunakwenda 2000 wenzetu wa Tanzania Bara walikuwa wanakuja kufanya biashara Zanzibar, wanabeba mali kule na wanatunufaisha Wazanzibari. Sijui kimetokea nini hapa katikati, ndugu zetu wa Tanzania Bara mnahamia Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda mnatuacha jirani zenu, hebu angalieni hapo tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kwenye masuala ambayo tunaungana, nakwenda kwenye Balaza la Mitihani la Taifa, hapo bado hapajakaa vizuri. Kuna communication, coordination na cooperation ndogo, tuweke sawa hapo. Balaza la Mitihani lile na chombo maalum kinachotambulika kisheria ili ku-coordinate, cooperate na ku-communicate baina ya Wizara zetu mbili, tutakwenda vizuri, tunaupenda Muungano. Pia NACTE kwenye elimu ya juu, tuangalie kinachotambulika Tanzania Bara na Zanzibar kitambulike. Tunaomba tufanye hayo kwani tutakwenda vizuri na Muungano wetu Mheshimiwa January na timu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine zuri kabisa, naomba niliseme kwa Watanzania wote kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga misingi imara ambayo inaweza kulidumisha Taifa letu miaka mia ijayo. Kwa hiyo, yale marekebisho madogo madogo ambayo tunaomba yanaendelea kufanyika siku zote isiwe ni neno la kuleta mjadala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na marekebisho madogo madogo, Katiba yetu iko vizuri na tutakwenda nayo vizuri hata miaka mia ijayo kwa sababu kila kilicho ndani ya Katiba ile kinatafsirika vizuri. Hiyo implementation ni jambo lingine wala siingilii lakini Katiba yenyewe kama Katiba inatufaa na ndiyo maana ikatufikisha miaka 55 hii na tukiwa tunasifiwa na mataifa yote ulimwenguni kwa Muungano ambao tunao, kwa nini tusiringe? Lazima turinge na Taifa letu kwa sababu Muungano wetu ni mzuri, uko very unique, inatakiwa na mataifa yote waige kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kuendeleza haya, hizo changamoto tuzimalize kwa muda unastahiki ili tuweze kujivunia zaidi Muungano wetu na kuupenda zaidi Muungano wetu. Mimi naipenda Zanzibar, naipenda Tanzania Bara lakini nakupenda Muungano zaidi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote ambayo ametujaalia lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuchaguliwa tena kwa kura nyingi kama ambavyo wametangulia kusema wenzangu na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika pamoja na Wabunge wote ambao tumebarikiwa kurudi tena kwa awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi pia nimshukuru kiongozi wangu wa Umoja wa Wazazi na timu yake yote pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini kwa mara nyingine tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Rais imejimwaga katika maeneo mengi ambayo ndiyo mwelekeo na dira ya miaka mitayo iliyopo. Pia mwisho wa hotuba yake aliwaelekeza Mawaziri ambao atawateua ambao tayari wako mbele yangu hapa kwamba warudi wakaisome Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa maeneo ambayo yeye hakuweza kuyafafanua kwa siku ile. Kwa hiyo na mimi nitaenda moja kwa moja katika eneo ambalo hakulifafanua siku hiyo ambalo liko kwenye ukurasa wa 144 hadi 145 ambayo inahusu ustawi wa jamii kwenye suala zima la ustawi wa Watoto na familia.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado ina changamoto katika suala hili, lakini nitumie fursa hii kushukuru sana wote waliopanga timu hii ya Ilani iliyotengeneza kwa kuweza kufafanua vifungu ambavyo sasa vitatuelekeza tunaondokana vipi na mporomoko wa maadili unaosababisha kuondoa furaha na amani ya watoto wetu, ndoa zetu ndani ya nyumba zetu na mambo yote yawe yameelekezwa hapo kuanzia kifungu (a) mpaka (n) vya Ilani katika ukurasa huo wa 144 na 145.

Kwa hiyo, nitaomba sana waheshimiwa Mawaziri kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliomba kwamba mfanye kazi hiyo kupitia ilani mimi nitakuwa na ninyi sambamba katika miaka mitano hii kuhakikisha kwamba vile vifungu vyote ambavyo vimeelekezwa kwenye ilani tunavishughulikia ipasavyo. Kama ni kutunga sheria, kama ni kurekebisha sheria, kama ni kutoa elimu kwa jamii basi nitawahamasisha na Wabunge wenzangu tuhakikishe tunakwenda Tanzania nzima kuhakikisha kwamba suala la mporomoko wa maadili ambao unasababisha matatizo mengi mojawapo likiwa ni mimba za utotoni tunalitokomeza Tanzania. Lakini pia, suala la talaka za hovyo nchi yetu imezidi jamani Waheshimiwa Wabunge! Tunashindwa kudumisha ndoa zetu na badala yake tunasababisha kutelekezwa kwa familia zetu na watoto wetu ambao mwisho wa siku ndiyo wanaenda kupata mimba za utotoni. Kwa hiyo, hilo ni janga ambalo kama hatukuliendea vizuri na tukalitilia mkazo basi haya maendeleo ambayo tuanzungumzia huko baadae tutakuja kukosa maendeleo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sio hilo tu, kuna suala zima la kuwarudisha nyuma watoto wa kike katika kutafuta elimu. Bado ni changamoto katika nchi yetu. Kwa hiyo nitashirikiana na Wabunge wenzangu, lakini pia kuna suala zima la udhalilishaji wa watoto wadogo. Hili jamani mara hii litakuja kwa mwendo mpya. Ninaomba Mheshimiwa Dorothy Gwajima ajiandae kwa hilo. Mimi sitakubali kwa sababu tunashindwa kabisa ni nini tufanye jinsi ambavyo watoto wetu wanaharibiwa katika nchi yetu hii. Hilo ni jambo la kusikitisha, tumelizungumza miaka mingi, lakini safari hii naomba kutokana na haya yaliyoandikwa kwenye Ilani yetu kwenye vifungu hivi 14 nina hakika kabisa kama tutavisimamia ipasavyo na tutaisimamia ipasavyo Serikali katika vifungu hivi vilivyoainishwa kwenye Ilani kumlinda mtoto katika nchi yetu naamini kabisa miaka mitano hii tutafika mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa na hayo tu. Naipongeza kabisa hotuba ya Mheshimiwa Rais na naomba tushirikiane kuitekeleza ambavyo ameelekeza. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NAJMA MURTAZA. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi anavyokuwezesha Mheshimiwa Waziri (mwanamke mwenzetu) kufanya kazi zake kwa ujasiri na uweledi unaothibitisha kuwa wanawake tunaweza kabisa.

Mheshimiwa Waziri hoja yangu inajikita moja kwa moja kwenye hotuba yako kwenye ukurasa wa 101 hadi 107 na ukurasa wa 109 hadi 110. Umekiri kabisa kuwa ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini, na mimi ninakiri pia kwa kauli yako hii. Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kwa asilimia 28 kutoka mwaka 2016 hadi kufikia mwaka 2017, ninaamini kabisa elimu sahihi kuhusu vitendo hivi ikiwafikia Watanzania walio wengi na kuweza kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto, asilimia hii inaweza kuzidi hadi kufikia asilimia 60 au zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sichoki na wala siyachoka kutoa ushauri wa kuangalia adhabu mbadala kwa makatili wazoefu wanaoharibu maisha ya watoto wetu ambao ni Taifa letu la kesho.

Mheshimiwa Waziri inasikitisha sana kuona kuwa haki za binadamu zinapewa kipaumbele kwa hawa makatili wa watoto wetu na hasa wabakaji watoto wa kike na wanaolawiti watoto wakiume, mbali na kutumikia kifungo kwa miaka 30 makatili hawa sugu (ambao wanathibitika kuwa wazoefu katika kuwaharibu watoto wetu) wafikiriwe adhabu mbadala ya kuhasiwa uume wao ili iwe funzo kwa wengine na kuwaokoa watoto wetu kutokana na janga hili ambalo tukizidi kuwaonea huruma kwa kisingizio cha haki za binadamu tutaliangamiza Taifa la kesho kwani hili janga mwisho wa siku litakuwa janga la kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza wazi kwamba haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambavyo itasababisha kuingiliana kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma; kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru wa haki za watu bibafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali kuwa ibara hii ya Katiba ikionekana kuvunjwa kwa namna yoyote kwa mujibu wa ibara 30 mtu anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu. Hili suala la kufungua shauri katika mahakama zetu bado inaonekana siyo muafaka sana kwa maslahi ya watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakushukuru Mheshimiwa Waziri ukiwa kama mwanamama mwenzangu ulitafakari na kukaa na timu yako kutafakari zaidi suala la kuleta muswada wa sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wa kiume na wa kike, tukizingatia ibara hizo hapo juu za Katiba yetu zinaturuhusu kutunga sheria katika jambo la aina hii, tuache kabisa kisingizio cha kuvunja haki za binadamu wakati hawa wabakaji wanaendelea kuvunja haki za binadamu wadogo.

Naomba sana Wizara yako ijaribu kutafiti na kuona uwezekano wa kutungwa sheria hii ya adhabu ya kuhasi kwa kulinganisha na nchi nyingine ambazo tayari zina hukumu za aina hii. Mfano Mheshimiwa Mary Karooro Okurut, Waziri wa Jinsia Kazi na Maendeleo wa Uganda anaunga mkono suala hili la kuwahasi wabakaji hawa.

Mheshimwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na natumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza lakini kuwatakia Waheshimiwa Wabunge wote heri zote za mwaka mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kuchangia katika Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 5 wa mwaka 2017. Sheria hizi ukitazama zimeletwa kwa uchache kwa maana ni kidogo lakini zina impact kubwa na maslahi mapana sana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa sheria hii ya Ufilisi ni sehemu ndogo tu lakini lengo lake nalo pia ni zuri katika kufanya utekelezaji uwe mwepesi katika Sheria ya Ufilisi kwa kuweka tafsiri ya neno hili la official receiver. Kwa hiyo hili halina mjadala mkubwa na naamini wote mtakubalina na mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sheria ya Bajeti hii inadhamiria kuweka hali sawa katika Bunge letu baina ya kanuni zetu na sheria. Kwa hiyo hili nalo nafikiri ni jambo zuri na naamini wote tutakubaliana, kwamba kupokea Mpango wa Bajeti wa Serikali katika kipindi cha Oktoba na Novemba itakuwa ni vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali kwa kuona kwamba kuna umuhimu wa kuweka exception katika ule mwaka ambao tutafanya uchaguzi na kuweza kupokea mpango huu sasa katika mkutano wa pili wa Bunge. kwa hiyo, nalo hilo limekaa vizuri halina tatizo lolote na naamini wote tutakubaliana hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la ardhi, yaani masharti kuhusu kutumia ardhi kwa ajili ya kupata mkopo. Hapa lazima niseme kidogo zaidi. Kwanza naiunga mkono na kuipongeza sana Serikali kwa kuweza kuona kwamba umuhimu wa kuendeleza ardhi yetu ya Tanzania. Hili ni jambo muhimu sana, tusilione kwa udogo tukaitizama kwa urahisi lakini inaonekana muda mrefu Serikali yetu inapata hasara, watu wanakopa kwa kutumia ardhi iliyopo Tanzania ambayo haijaendelezwa na wanaweza kuendeleza maeneo mengine ambayo yapo nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuwepo au kuletwa kwa marekebisho ya sheria hii, yatasaidia ardhi ya Tanzania kuweza kuendelezwa. Haiwezekani leo mtu anakopa kwa kutumia rasilimali ya ardhi ya Tanzania na kuendeleza sehemu nyingine ambayo si ya Tanzania. Kwa hiyo, sheria hii naamini Watanzania wote wazalendo wa nchi hii wataunga mkono na kukubaliana na marekebisho haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye sehemu ya mwisho ambayo ni Sheria ya Utumishi wa Umma, kuongeza umri wa wastaafu hasa tukienda kwenye kada ya maprofesa na madaktari bingwa. Kuhusiana na hili Serikali pia imeleta hoja nzito na hoja za msingi. Ni kweli kabisa kada hii ni muhimu sana kwa Taifa letu na hao watu bado tunawahitaji kwa uchache wao kwa maslahi ya Taifa letu, hii haina mjadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunakubali kurekebisha sheria hii kwa maslahi mapana ya Taifa letu lazima Serikali ione namna mbadala wa ku-fill gap, hiyo ndiyo itakuwa solution ya kudumu. Tutaenda na sheria hii tutarekebisha leo, tutaweza kuitumia na naamini itatufikisha pazuri ili kuondoa gharama kubwa ambayo tumeitumia siku zote katika Serikali yetu katika kuongeza mikataba ya watu hawa ambao tunawahitaji katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida zipo pande mbili, kwamba kuna wengine ambao wanaongezewa muda wanajiweza bado wapo na afya nzuri na bado wataleta maendeleo katika Taifa letu. Pia tutawakwepa wale ambao wanasomeshwa na Taifa hili halafu wanafika umri wa miaka 55 wanasema wanataka kustaafu kwa hiyari anakwenda kutafuta mpango mwingine wa binafsi na anaacha maslahi mapana ya Taifa letu yanakwenda pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo hayo mawili yamesaidia kuonesha hoja ya msingi ya Serikali na kwa kweli naunga mkono suala hili, lakini narudi pale pale tena, Taifa letu bado lina uchache wa kada hizi, kwa hiyo naomba tupange tu mpango endelevu wa kuona kwamba tunaondoa urasimu kwanza katika kuhakikisha hawa wasomi wetu wanafikia level hizi ambazo tumezikusudia za Maprofesa na Madaktari Bingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu pia kwa upande mmoja urasimu ndio unaosababisha, mtu anaandika paper miaka mitatu mizima hasogezwi popote au hajibiwi lolote. Kwa hiyo hii inarudisha nyuma kuongeza hizi kada za Mprofesa au Lectures wa vyuo vyetu. Kwa hiyo, naomba hilo suala la urasimu liangaliwe sana na Serikali ili tuweze kuwasogeza mbele hawa wasomi wetu ambao wanatakiwa wafike katika kada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba gharama ya kusomesha Madaktari bingwa nje ya nchi ni kubwa sana lakini bado nasisitiza kuna umuhimu mkubwa sana wa Serikali yetu kupanga fungu maalum la kuweza angalau basi tusiwafikie wenzetu wa nchi nyingine za jirani ambao wanaweza kupeleka wasomi wetu kwenda kutafuta hii fani ya udaktari bingwa nje ya nchi, basi angalau na sisi tuweze kufanya japo kidogo tuanze taratibu ili kuona kwamba gap hili linaweza kuondoka miaka ya mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini nimeeleweka kwa machache haya, naomba na wengine waweze kuchangia. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba moja kwa moja nianze kwa kusema kwamba, marekebisho ambayo tunayafanya leo ya Muswada wa Sheria hii yana malengo makuu mawili naomba tuelewe hivyo Watanzania wote. Lengo la kwanza ni kuhakikisha kwamba katika mfumo wetu wa vyama vingi katika Tanzania, lazima amani na utulivu idumu daima milele. Hili ndilo lengo la kwanza la sheria hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la pili ni kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vyote Tanzania vinashiriki kikamilifu katika hatua ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. Hiyo inathibitishwa katika vifungu vyote, lakini naomba niende na kifungu kimoja kutokana na muda. Kwa mfano, Section 6A(5) ukurasa wa nane inazungumzia ulazima wa chama cha siasa kuenzi na kudumisha mambo yote ya kitaifa ambayo yameorodheshwa katika Muswada huu na yamelenga katika maeneo matatu ya vyama vya siasa katika kuunda sera zake za chama cha siasa, lakini katika uteuzi wa wagombea na pia katika uchaguzi wa viongozi, lazima udumishe na kuenzi mambo haya ambayo yametajwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza moja baada ya moja. Naanza na Muungano, naamini muungano hakuna atakayepinga hapa, muungano lazima udumishwe kwa heshima zote katika ya Taifa, ni tunu ya pekee ya nchi hii. La pili ni Mapinduzi ya Zanzibar, Mapinduzi ya Zanzibar ni uhuru wa Wazanzibari, mapinduzi ya Zanzibar ndio alama inayothibitisha uhuru wa Zanzibar, ni lazima iwepo na ienziwe maisha na maisha. Chama chochote ambacho kitakuwa kimekwenda nyuma na makubaliano ya Mapinduzi ya Zanzibar hakifai katika sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye demokrasia wote tunakubaliana hakuna anayepinga, tulikuwa tunapiga kelele demokrasia hakuna, sijui nini na nini, sheria imethibitisha kwamba demokrasia iko ndani ya sheria na vyama vyote vitastahiki kuhakikisha kwamba vinakwenda kwa mujibu wa demokrasia inavyotakiwa. Utawala bora hakuna anayekataa, sheria imeweka wazi mambo yote yanakwenda kwa namna ambayo vyama vinatakiwa vifanye utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija rushwa hakuna mtu anayetaka rushwa, sidhani kama kuna mtu anakubaliana na rushwa, kila chama kinatakiwa kiheshimu hayo. Pia tunakwenda kulinda maadili na misingi ya maadili ya Taifa letu, ndio utakuta kuna vifungu vya utoaji wa elimu, tunadhibiti namna gani elimu ya uraia, vinaingia hapa hapa. Kwa hiyo lazima tulinde maadili ya Taifa letu kupitia sheria hii. Vilevile tunakwenda kwenye uzalendo, jamani uzalendo si rangi, si kabila wala si dini, uzalendo ni kulipenda Taifa lako, kulitetea kwa hali yoyote, kuhakikisha kwamba unaleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine, Mwenge wa Uhuru, Uhuru torch, Uhuru torch ni symbolization ya Uhuru wa Tanganyika, ile pale, ni alama ambayo itabidi ienziwe milele, daima. Si hivyo, malengo ya mwenge wa uhuru hayajaisha Tanzania. Malengo ya mwenge wa uhuru ni kuleta upendo kwenye chuki na ni kuleta heshima kwenye dharau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amani na utulivu halina mjadala, lakini tumeongezewa jembe vyama vyetu havifuati, vina mfumo dume. Kuna chama humu kina Wabunge karibu Ishirini kutoka Zanzibar, hakina mwanamke hata mmoja jimboni, lakini vijana wameingizwa huku kwa sababu ndio Taifa la kesho. Kwa hiyo chama ambacho hakijali vijana hakitakiwi kwenye sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jamani naomba nirudie tena kusema, vifungu vyote vya sheria hii vinaendeleza vyama kushiriki kikamilifu katika Taifa letu. Naunga mkono mkono Muswada huu kwa maana hiyo ambayo nimeieleza. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2018
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi nitajikita katika katika Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Na. 4 ya mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Muswada huu una marekebisho madogo sana ambayo naungana moja kwa moja na Serikali kwa vipengele vile ambavyo wameweka katika Sheria hii ya Serikali za Mitaa ambayo ina jambo ambalo ni la muhimu kulifanyia marekebisho kwa wakati huu, kwa maana ya kuongeza faini kutoka ile shilingi 50,000 kwa maana ya faini isiyozidi shilingi 50,000 kwenda faini isiyozidi shilingi 300,000 ili iweze kulingana na Sheria za Serikali za Mitaa na isiweze kukinzana na Sheria hiyo ya Serikali za Mitaa Sura ya 288 kifungu cha 97. Ili ziiweze
kwenda sawa na kifungu cha 156(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa, kwa hiyo haina tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia kwamba mabadiliko yanatokea na shilingi inapanda kwahiyo hatuwezi kuwa na adhabu ile ile kwa muda mrefu bila kufanyiwa marekebisho. Kwa hiyo, haina tatizo na naunga mkono kwa asilimia zote hiyo hoja ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna sehemu ya tano inahusu Sheria ya Bodi ya Utalii Sura ya 364 kifungu cha
3. Hii imemuwezesha sasa Mwanasheria Mkuu ambaye ndiye Mshauri Mkuu wa Serikali kuweza kuingilia masuala au mashauri yanayofunguliwa mahakamani dhidi ya Bodi hii ya Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile yeye ndio Mshauri Mkuu wa Serikali na hii Bodi ni chombo cha Serikali, kwa hiyo, kuna umuhimu wa yeye kuingilia masuala haya na kuona namna gani Bodi yetu ya Utalii inaweza kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika sehemu hiyo hiyo wameongezea majukumu ya Bodi hii ya Utalii ambayo mwanzo yalikuwa pengine hayakukaa sawa, lakini sasa hivi ili kuziba mianya hiyo na ili kuweka sheria iwe nzuri zaidi, majukumu hayo yamewekwa kwa ufanisi zaidi ili tuweze kupata tija katika shughuli yetu ya utalii na kukuza nje na ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile, nimesema Muswada huu ni mfupi sana na hayo niliyozungumza ni ya muhimu sana, lakini pia nichukue fursa hii kuwapongeza sana Serikali kwa kuikubalia Kamati kutoa kifungu cha 3 na cha 4 ambacho kilikuwa kinahusu mafao kwa Watumishi Wastaafu wa Kisiasa, Sura ya 255, lakini pia na haki ya watumishi kwa pass za kidiplomasia. Naishukuru sana Serikali, wamechukua uamuzi mzuri wa kutufuata Kamati na ninaamini watakwenda kulifanyia kazi kwa uzito unaostahiki. Kwa sababu tunachokiomba sisi tumekiona kidogo, lakini kwa upande wao wanaweza kuona kwamba kuna ugumu fulani lakini naamini watakapokwenda kukaa watatuingiza na sisi Waheshimiwa Wabunge baada ya kustaafu tuweze kupata pass za diplomasia. Hilo ndiyo lilikuwa lengo kubwa la Kamati yetu.

Kwa hiyo, wamelichukua hilo na wameliondoa kwa pamoja kwenye vifungu vyote viwili ili wakakae sawa sasa na kuweza kuirudisha kwa namna nzuri ambayo sisi Wabunge tutapata privilege hiyo na yule ambaye kwamba atakuwa amekosea jamani, basi atakuwa na haki ya kufutiwa hiyo pass. Kwa ambaye atatumia vizuri, basi tumwachie apate privilege kwa sababu Waziri na Mbunge tunafanya kazi zinazofanana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya ndiyo niliyokuwa nayo. Nashukuru sana, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza lakini pia nitumie fursa hii…

MWENYEKITI: Dakika kumi…

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Niseme sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniongezea mwaka mmoja wa umri wangu nikiwa na afya njema na uzima. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake yote pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kufikiria kuleta marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.4 ya mwaka 2019 kwa wakati huu ambao naamini ni muafaka kabisa. Lengo na dhamira ya kuleta marekebisho haya ni kuziba mianya (gaps) ambazo zipo katika sheria hizo ambazo ni 11 katika Muswada huu ulioletwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana na kumpongeza AG kwa usikivu na umakini wake wakati tunashirikiana na Kamati kiasi kwamba ameweza kupokea ushauri mwingi wa Kamati na kuufanya marekebisho kama ambavyo tumeona kwenye Jedwali la Marekebisho. Kwa hiyo, usikivu wake umeweza kuleta Muswada ulio bora kwa maslahi ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na Sheria ya Mawakili, Sura ya 341. Ni lazima nikubaliane na Serikali kwamba mfumo wetu wa sheria unaendana na mfumo wa Sheria ya Jumuiya za Madola na wenzetu katika nchi hizo kwa muda mrefu wamegundua kwamba taaluma hii ya sheria inapokuwa katika mazingira ya Serikali ikiwa itachanganywa na private sector inaweza kuleta migongano mikubwa ya kimaslahi katika nchi yetu tofauti kabisa na taaluma nyingine kama vile madaktari, walimu na wengineo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukubaliana na maono hayo ya Serikali ili tuendane na International Standards za nchi za wenzetu ambao tunaiga mifumo yao ya sheria, Serikali hatuna budi pia kufikiria mazingira halisi ya nchi yetu na wananchi wake. Kwa hiyo, nina imani kubwa Mwanasheria Mkuu na Serikali kwa ujumla wanaweza kuyafikiria maoni na ushauri uliotolewa kwenye Kamati kuhusiana na hawa Mawakili ambao wanafanya kazi Serikali na kuweza kuweka mfumo bora ambao utasaidia kurahisisha kazi ndogo ndogo ambazo hazileti migongano ya kimaslahi kwa maslahi ya wananchi wa nchi yetu lakini pia kwa manufaa machache ya Mawakili wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini ushauri huo Serikali yangu sikivu itasikiliza na kuweza kuweka mfumo bora na kuwaruhusu hawa Mawakili ambao wanafanya kazi Serikali ambao utasaidia kuwasaidia hasa wananchi wetu walioko vijijini ambapo pengine kwenye Halmashauri kuna Mawakili wawili tu Serikalini kwa hiyo ili kuwafuata sasa Mawakili wengine ili kupata huduma ya hati za viapo, mikataba pamoja na hati nyingine basi tufikirie namna bora ya kuweza kuruhusu kulingana na mazingira ya Kitanzania na mazingira ya wafanyakazi wetu. Naamini hilo utakuwa umelisikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukija kwenye Sheria ya Vizazi na Vifo, hii nayo imekuja wakati mzuri, wakati Taifa letu bado tunaendelea kuzaa na vifo vinaendelea lakini na wale ambao watakuwa nje ya nchi basi sheria hii itakuwa imewafaidisha kuweza kujua takwimu sahihi na hata katika sensa zitakapotokea itakuwa imesaidia sana katika uweka idadi kamili ya Watanzania tuliopo na wale ambao wamepoteza maisha yao. Sheria hii pia inakwenda kutekeleza misingi bora ya Sheria ya Mtoto ile ya mwaka 2019 ambayo inataka tutimize haki na ustawi wa jamii wa mtoto katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuwepo kwa sheria hii iliyoletwa hapa kama ni marekebisho ya sheria hii itasaidia kurahisisha kazi hasa baada ya kushusha yale mamlaka ya usajili kwa Wasaidizi Wasajili ambao wako katika kata na halmashauri zetu badala ya kumuachia Msajili Mkuu. Kwa hiyo, kazi itarahisika na mambo yatakwenda vizuri na ndiyo maana nasema kwamba kazi hii ni nzuri na imekuja kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Red Cross (Chama cha Msalaba Mwekundu). Sheria hii imekuwa katika nchi yetu kwa muda mrefu sana na ni chama ambacho kimefanya kazi kubwa sana katika kuokoa maisha ya watu wetu katika nchi yetu popote pale yanapotokea majanga Tanzania nzima. Hata hivyo, Tanzania Zanzibar pia imekuwa ikifanya kazi kwa miaka mingi ya nyuma pamoja na kwamba sheria hii ilikuwa ikitumika Tanzania Bara tu. Kwa hiyo, kuletwa kwa marekebisho haya kutasaidia na Zanzibar kuonekana ni sehemu ya sheria hii na hivyo wigo wake mpana kufanyika bila uvunjaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, sheria hii inakuja kuweka wazi maana halisi ya Chama cha Msalaba Mwekundu. Dhana potofu ya watu wachache katika nchi hii ni fikra kwamba chama hiki ni cha dini fulani lakini sheria hii inakuja kuweka sawa kwamba Chama cha Msalaba Mwekundu ni chama ambacho kinatoa msaada Tanzania na dunia nzima bila kujali dini au kundi la aina yoyote. Kwa hiyo, sheria hii inakuja kuweka sawa mambo hayo na wigo mpana wa chama hiki utasaidia Taifa letu katika viwango vya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni makubaliano ya awali baina ya Mwendesha Mashtaka na mtuhumiwa katika kesi hizi za jinai ambazo zimeelezewa hapa (Plea Bargaining) ambayo imeletwa kwa madhumuni ya kupunguza mrundikano wa kesi Mahakamani lakini pia kupunguza kiwango cha adhabu ambacho pengine mtu angepewa wakati ameshajua kwamba hili kosa mimi nimefanya. Kwa hiyo, iko vizuri na naamini itasaidia sana katika kupunguza hayo mambo ambayo tumekusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni marekebisho ya Sheria ya Mali itokanayo na uhalifu, Sura ya 256. Nchi yetu kwa muda mrefu imekuwa kimya na kuachilia watu wachache wakijilimbikizia mali kwa njia ambayo siyo ya halali na kujinufaisha wenyewe huku Watanzania walio wengi wakiumia na hali ngumu ya maisha. Kwa hali hii tunayoenda nayo sasa na Awamu ya Tano ya Serikali yetu ambayo inapinga vikali suala hilo, sheria hii imekuja sasa kuweka sawa hali nzuri ambayo itasaidia watu wanaojilimbikizia mali kuzikosa mali hizo itapothibitika kwamba wamepata kwa njia isiyo ya halali. Kwa hiyo, watu kama hao wakae tayari na wajue kwamba mwisho wa kufanya ubaya ni kuona haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuwadhulumu Watanzania kwa kujilimbikizia mali ambazo siyo halali na kuwafanya wengine waendelee kuwa wanyonge sio jambo zuri kwa sheria za nchi wala sheria za Mungu. Kwa hiyo, hilo ni jambo zuri na naunga mkono sheria hii lakini ni matumaini yangu makubwa kwamba Serikali itazingatia Katiba ya nchi na misingi yake kwa kutowahusisha wale ambao wanahisi kwamba wanashirikiana na hao wahalifu wakubwa kwa kuzishika mali zao na pengine kuzitaifisha wakati ushiriki wao si wa principal offender ambaye yeye ndiye mhusika mkuu. Naamini kabisa Serikali yangu itazingatia Katiba na kutekeleza sheria hii kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono Muswada huu na naomba tuupitishe kwa moyo mmoja. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2019
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi,na mimi ningependa kuchangia katika muswada huu ambao umekuja kwa hati ya dharura katika maeneo matatu, Sehemu ya pili, ya tatu na ya nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni sehemu ya pili ambayo inahusiana na masuala ya kampuni. Kwa muda mrefu sana nchi yetu imekuwa na kampuni, taasisi binafsi ambazo si za Serikali, pamoja na taasisi nyingine za kijamii, bila kuwa na mfumo uliokuwa sahihi katika kuzisajili hizi taasisi. Kwa hiyo kuletwakwa muswada huu wa dharura sijambo la ajabu, kwa sababu kama kuna jambo linaweza kuharibika katika nchi basi kuja kwa dharura siyo tatizo, na hii ni kazi yetu Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyokuletwa kwa Muswada huu mbele yetu kunakuja kuweka sasa usajili uliokuwa rasmi. Hapo nyuma unakuta kampuni imesajiliwa lakini malengo yake si ya kibiashara hivyo inabidi iende ku- fall under NGO’s Act;na zile ambazo zimesajiriwa na zinafanya kazi ya kibiashara basi inabidi ziende kwenye Company’s Act. Kwa hiyo hiki ndicho kilicholetwa na Serikali, si jambo baya; ni dhamira njema ya kuweka mfumo uliokuwa unafaa katika nchi ili kuweka sawa mambo yaende kwa lengo la kusaidia Watanzania, hilo ndilo jambo muhimu na wala siyo baya na ninaomba watanzania waamini hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,hakuna NGO ambayo itakuwa inafanya kazi zake kwa mujibu wa utaratibu ikafutwa, wala kampuni ambayo itakuwa inafanya kazi zake kwa mujibu wa utaratibu ikafutwa, hayo ni dhana potofu za watu wasiopenda maendeleo ya nchi yetu. Hilo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, l la pili, malengo ambayo yamekusudiwa katika hizi taasisi je, yanatekelezwa. Tumeshuhudia NGO’s nyingi latika taifa letu zinasajiriwa kwamalengo yaliyopangwa, zinafanya kazi malengo mengine kabisa;hayo hayatakiwi wala hayafai katika nchi hii kwa maslahi au usalama pamoja na maslahi ya Watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja;taasisi inasajiriwa kwa ajili ya kuhubiri mambo ya dini inakwenda kuhubiri siasa, wapi na wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni mifano midogo tu michache, hatuwezi kuachilia nchi inakwenda hovyo hovyo kama hivyo, nchi ina watu wenyewe na ni wananchi, ambao sisi humu ndani tunawawakilisha leo hii. Kwa hyo, hilo haliwezi kukubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hizi taasisi, zinaingiza ma-Trilions of money, kwenye nchi yetu, je, zinatumika kwa maslahi ya Watanzania waliokusudiwa?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,so transparence, uwazi katika kuziangalia hizi taasisi zetu ambazo zinaendeshwa bila ya kuingia na Serikali ziwe zinafuatiliwa na kuwa monitored kuangaliwa kwamba je, yale malengo yanakusudiwa, lakini je kile kinachoingia kwa maslahi ya Watanzania kinatumika kwa walengwa au kinapenya pembeni na kwenda kwa wanufaika wachache?Hiloni muhimu sana katika nchi yetu kuzingatia na wala haina ubaya na mimi naomba Watanzania waelewe hivyo, na wala halina tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya tatu, kuhusu Copy Right(Haki Miliki). Watu wengi wanatushangaa duniani, tuache mataifa ya nje kabisa yaliyoendelea sana kama Marekani;wana mifumo mizuri ya kuweka sheria za kudhibiti haki miliki za sanaa zao, filamu zao, kuzilinda, kuhakikisha kwamba zinaleta manufaa katika nchi zao.

Vilevile nchi nyingine za Afrika pia watatushangaakwa sababu Tanzania hatuna mfumo bora. Vijana wetu waKitanzania wanajitahidi sana katika tasnia ya filamu.Wanatunga michezo, wanafanya mambo mengi, wanachora, wanachonga, wanaimba nyimbo nzuri zinazopendwa mpaka nje ya Tanzania; lakini je, haki miliki ya sanaa zao imedhibitiwa na kutunzwa?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sheria hii inakwenda kuwalinda vijana wetu wa Tanzania ambao wanajitolea kujiajiri kwa kufanya kazi za sanaa. Mimi nitaiomba sana Serikali iweze kuangalia katika utengenezaji wa sera zake ziwe mbili ambazo zinakwenda kudhibiti haya mambo ya NGO pamoja na mambo ya Sanaa na Filamu. Tuwe makini katika kutengeneza sera zilizo borana imara zitakazoweza kutudumisha nchi yetu kwa miaka mingi mbele katika kusaidia tasnia hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwasababu, mtu anachonga kinyago chake hapaTanzania kizuri kabisa, kikishatoka nje ya nchi ndiyo amekwisha, hana faida nyingine yoyote. Watakwenda ku-duplicate, watatengeneza wanavyoweza wao, faida ya haki miliki ya yule mtengenezaji wa kwanza iko wapi?Wenzetu wana brands zao ikishatoka nje inalipwa na kulipwa ma-Trilions yanaingia. Kwa hiyo hilo ndilo kusudio na lengo la sheria hii iliyokuja kwa hati ya dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja sehemu ya nne, hii Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza. Sheria inakuja vizuri kabisa, inakuja kulinda maslahi ya hawa vijana wetu wanaoendesha hizi kazi. Hiyo ni moja, lakini pia inakuja kuweka mfumo bora wa kulinda utamaduni wa nchi yetu. Hakuna upotoshaji hapo utakaokwenda kupotosha tamadi za nchi yetu. Nikitolea mfano, labda vibanda hivi vya filamu ambavyo vinaonyesha, tukiweka udhibiti wa hivi vibanda, tutaweka mfumo bora ambao hata wanafunzi hawatatoroka shule kwenda kuangalia filamu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutaweza kudhibiti maudhui yanayotolewa kwenye vile binada. Tumegundua kwamba watoto wanaangalia, vijana wanaangalia, lakini pia ukiingia kwenye mabasi ambayo tunapanda, yanayosafiri mikoani, filamu zinawekwa baba yuko pale mtoto yuko pale lakini ukitazama maudhui yaliyopo; tunaburudisha, of course mimi sikatai watu waburudike; lakini utakuta maudhui, mavazi yaliyokuwamo ndani, hayawezi kukidhi utamaduni wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali, itakapokwenda kutengeneza sera na kuweza kurekebisha sheria katika masuala hayatuzingatie na maadili ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu umekwisha.

MBUNGE FULANI: Bado, endelea.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA:Mheshimiwa Naibu Spika, bado, ahaa, maana hawa wananichanganya hapa wananiambia umeisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa heshima kubwa kabisanasema tena, narudia kwa mara nyingine, kwamba kazi ya Bunge ni kusimamia wananchi wetu na kuwawakilisha, lakini kazi yetu nyingine ni kutunga sheria, hata iwe ya dharura iwe yoyote, kwa hiyo wananchi tusichoke na tusikate tamaa. Kuna watu wana dhana kwamba ikishakuja sheria hapa ndiyo ije imetimia. Nasema hivi, sheria si Vitabu Vitakatifu vya Mungu, sheria zinatakiwa kubadilika kwa kadri ya mahitaji yanapohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ikiwa kwamba Mheshimiwa Rais atakuwa amesaini leo nabaada ya miezi mitatu ikaonekanahuko nje imegonga inarudi hapa tunarekebisha.Hilo halina mjadala, kwanini tunakuwa wakaidi? Tusiwe wavivu Waheshimiwa Wabunge katika kufanya kazi zetu, hilo ndilo linalohitajika, kwa sababu sheria hizi siyo za kudumu, mahitaji yanabadilika…(Makofi)

MBUNGE FULANI: Siyo amri ya Mungu.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Siyo amri ya Mungu, kama hivyo unavyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi ninaomba sanasana sanatuipokee sheria hii, tuifanyie kazi, tuipitishe leo hii, kwa maslahi mapana ya nchi yetu na si kwa lengo lingine lolote. Mwenye mawazo tofauti huyo kwa kweli anapotosha watu, aondoke katika hisia hizo arudi tujenge Serikali yetu. Wapinzani nawaomba muingine na nyinyi muunge mkono hii hapa, iende ili tuweze kunufaika, ninyi pamoja na sisi na watanzania wote.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono yote na naomba Muswada huu uweze kupita kwa heshima zote. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nitangulie kusema kwamba tuwe pole kwa msiba wa mwenzetu aliyetutangulia mbele ya haki na sisi Mwenyezi Mungu atujalie hatma njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni dakika tano basi moja kwa moja mimi naomba niende kwenye Muswada huu wa Sheria ambao umeletwa mbele yetu Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2021 ambayo inakwenda kubadilisha vifungu vitatu Tafsiri ya Sheria Sura Kwanza; Sheria ya Mahakama ya Mgogoro wa Ardhi na Sheria ya Mahakama za Mahakimu Mura ya Pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo la ajabu na wala siyo geni katika ulimwengu huu kwa sababu tunaelewa siyo Tanzania ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Madola ambazo muda mrefu tumekuwa tukitumia mienendo katika sheria zetu za mahakama na maeneo mengine ya sheria kwa lugha ya kiingereza lakini pia na Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hizi ambazo nyingi zimetawaliwa na koloni la Uingereza ambazo tulikuwa tukizitumia muda mrefu toka wakati huo wa enzi za ukoloni mashitaka mengi yalikuwa yakiendeshwa kwa lugha za kienyeji pamoja na kwamba lugha ya kiingereza ilikuwepo ndiyo official. Lengo jamaa na lugha ya rasmi. Kwa hiyo jambo hili ni zuri kwetu litaleta mambo mengi ya faida mimi naweza nikasema mawili tu kwa muda ni mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza tutarahisisha katika utoaji haki. Watanzania walio wengi asilimia kubwa sana wanatumia lugha ya Kiswahili, hawaelewi lugha ya kigeni au ya kitaalamu ambayo inatumika katika sheria zetu. Kwa hiyo itarahisisha namna gani mtua ataweza kupata haki yake kwa urahisi kwa lugha ya Kiswahili kwa kuelewa yale ambayo yanayoendeshwa na yanayotolewa. Lakini hii itakuwa ni endelezo kwa sababu mahakama zetu kama ambavyo wamezungumza wenzangu Waziri wa Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati kwamba mashauri mengi yameshakuwa yanaendeshwa kwa Kiswahili kuanzia ngazi za chini hadi Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata ukienda kwenye Mahakama nyingine kubwa hukumu zinatolewa kwa Kiswahili, kwa hiyo siyo jambo kubwa sana. Lakini tukija kwenye mifano mingine mimi nitaenda mfano mmoja wa nchi za Jumuiya ya Madola yaani India. India bahati nzuri kwenye Katiba yao Ibara ya 348(2) wamepewa ruhusa Magavana kuomba ruhusa ya kutumia lugha zao za kienyeji kwa Mheshimiwa Rais na hata hivyo nimeona mfano mmoja Haryana wameshaomba mwaka 2020 kwa Mheshimiwa Rais ili watumie lugha ya Hindi katika Mahakama zao. Kwa hiyo hili siyo jambo la ajabu ni jambo la kawaida na kwetu hapa kwa hiyo litakuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa sababu Katiba yetu ya Tanzania nayo imetoa ruhusa hiyo Ibara ya 67 sifa za Mbunge awe anajua kusoma na kuandika Kiswahili ama Kiingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutasema siku moja tuamue kutoa hoja kwa lugha ya kiingereza shughuli itakuwepo, kwa sababu hata Wabunge pamoja na usomi wetu, lakini tumeshazoea kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo hili ni jambo ambalo lazima tulitilie mkazo.

Lakini faida nyingine ni promotion ya lugha ya Kiswahili yaani kuiendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili, lugha ya Kiswahili inatumika na watu zaidi ya milioni 100 katika dunia hii kwa hiyo kuna nchi nyingi ambazo zinatoa taarifa zake kwa lugha za Kiswahili; kuna BBC London tunajua tuna Deutch Welle Ujerumani, kuna Iran, nchi nyingi sasa hivi zinazungumza Kiswahili na zinatoa taarifa ya habari kwa lugha ya kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia utakuta Mabunge yetu haya SADC tayari tumeshatoa fursa hiyo, lakini hata na maeneo mengine mengi tutaweza kuzungumza, East Africa Community tayari inatumia Kiswahili. Kwa hiyo niseme tu ushauri uliotolewa na Kamati ni mzuri kwa sababu muda ni mfupi, lakini tusifikirie kwamba itakuwa ni jambo rahisi najua tutakuwa na gharama zitakuwepo za kutafsiri lugha hii kuingia Kiswahili haina shida jambo zuri lote linatakiwa gharama, lakini pia na muda kama alivyosema Mwenyekiti wangu lazima tuanze vile vitu vya vipaumbele kwanza tutizame nini tunaanza nacho kwa awamu alafu baadae tunaendelea na vingine hadi tutafikia mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, na pia wataalamu wetu wasiwe na hofu ya kutafsiri lugha kutoka kiingereza kuja Kiswahili. Kiswahili ni lugha ya kirafiki kabisa jamani ni lugha nzuri ambayo inaenda kwa namna zote lazima tukubaliane kwamba asilimia 30 ya maneno ya Kiswahili yanatokana na lugha za kigeni tumeyatohoa kutoka kwenye lugha za Kiarabu, Kihindi na Kingereza, lakini pia tuna asilimia kama kumi kutoka nchi za Kiafrika kwa maana bantu languages au lugha za kibantu tuna maneno mengi tumeyatohoa kama asilimia kumi.

Kwa hiyo, haitakuwa tatizo tukiona kuna tatizo wanasheria/wasomi kwamba lugha hii kwamba tunashindwa kuitafsiri basi tutohoe tu kwa mfano naweza kutumia neno moja locus stand tukiitafsiri kwa urefu wake itakuwa ni shida kwamba lazima mtu awe na haki ya uwezo wa kufikisha shauri mahakamani au kulisimamia, litakuwa ni neno refu kwa hiyo tukishindwa tuna sema hana locus ama anayo locus. Kwa hiyo nafikiri tutaelewana kwa sababu sote tunakubaliana hapa kwa maneno mengi tunayotumia hata katika ibada zetu makanisa na misikiti malaika, shetani, thawabu, dhambi zote zinatokana na lugha za kigeni lakini tumezitohoa zimekuwa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana, naomba tuupitishe Muswada huu kwa heshima zote. (Makofi)