Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Munira Mustafa Khatib (9 total)

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, je, ni lini Serikali itahakikisha imeondoa changamoto zilizopo katika huduma ya afya na wananchi kuweza kupata huduma zilizo bora katika vituo hivyo?
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Munira Khatib tafadhali rudia swali lako uikaribie microphone.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itahakikisha changamoto zilizopo katika huduma ya afya zinaondoka na wananchi wanafurahia huduma hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku Serikali inafanya kazi ya kuondoa changamoto zilizopo kwenye mfumo wa sekta ya afya. Serikali ya Awamu ya Tano kupitia maelekezo ambayo tunayapata kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 inajielekeza kwenda kuanzisha mfumo wa bima ya afya ambapo Watanzania wote watapaswa kuwa na kadi ya bima ya afya kwa lazima. Azma hii ya Chama cha Mapinduzi ya kuweka utaratibu wa Bima ya Afya kwa kila mtu tunaamini itaondoa changamoto kwa kiasi kikubwa zinazoukabili mfumo wa afya nchini kwetu.
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni wanachama wa CCM kwa kule Pemba; Je, Serikali haioni umuhimu wa chama hiki cha CUF kukifutia usajili na kuweza kupata amani ndani ya Tanzania yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa upande wa Pemba matukio haya, wakati wa uchaguzi wa marudio na baada ya uchaguzi kumalizika, Pemba kulikuwa na amani, ambapo mpaka sasa hivi amani ipo. Matukio haya ya kihalifu ya kukatakata mikarafuu na kufanya mambo mengine ya hovyo zaidi yalijitokeza baada ya viongozi wa CUF, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kufanya ziara kule Pemba. Ndiyo maana nikasisitiza kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba wanachukua sheria kali kwa Kiongozi yeyote wa chama chochote kiwe cha CUF au chama kingine ambacho kinahatarisha ama kinachochea amani ya nchi yetu.
Kuhusiana na suala la kukifutia usajili chama hiki nadhani hayo ni mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuona kama kuna haja hiyo kulingana na taratibu na sheria za nchi yetu zilivyo. Si jukumu la Serikali ama Jeshi la Polisi kuamua.
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, nakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu yake mazuri ambayo amenijibu, lakini napenda kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Je, ni utaratibu gani uliotumika kugawa hivi vifaa katika hospitali zetu za wilaya na mikoa kwa sababu vifaa hivi ndani ya hospitali zetu za wilaya na mikoa havionekani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni utaratibu gani unaotumika kuwapa elimu akinamama wajawazito kuweza kuwalea watoto hawa?
NAIBU WAZIRI, WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Kangaroo Mother Care haihitaji vifaa vyovyote vile, kwa sababu ni huduma ambayo inatolewa na aidha mzazi mama, baba, ama mtoa huduma yeyote yule ambaye atakuwa amechaguliwa na familia kutoa huduma hiyo. Huduma hii inahusisha kumchukua mtoto kumweka kifuani ngozi kwa ngozi na mzazi huyo, mara nyingi inakuwa ni mama. Kwa maana hiyo, hakuna vifaa vinavyohitajika pale zaidi ya mashuka na mablanketi ambayo yanagawanywa kwenye hospitali zote nchini kwa utaratibu wa kawaida wa kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa kupitia Wizara ya Afya ina encourage zaidi kutoa huduma kwa kutumia njia hii ya Kangaroo Mother Care na ndiyo maana hatuwekezi sana kwenye kujenga vituo maalum pembeni kwa ajili ya kuwatenga watoto na wazazi wao, kwa sababu imeonekana wakikaa na wazazi wao wanajengwa afya zao kisaikolojia zaidi.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nipende kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathimini inaonesha kwamba kila mwaka akina mama zaidi ya 400 wanapoteza maisha kutokana na vifo vinavyosababishwa na kujifungua. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza vifo hivi 400 kwa mwaka vinavyojitokeza wakati wa kujifungua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni kwa
nini vituo vya huduma ya upasuaji katika Tanzania yetu ni vichache hasa ukizingatia maeneo ya vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa hali aliyo nayo na nimtakie kila la kheri yeye na mwanaye na niwahakikishie kwamba watamaliza safari yao salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu maswali yake naomba niyajibu kwa pamoja tu kwamba tuna mkakati gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati tuliyonayo ni mingi na kwa kiasi kikubwa Serikali kwa sasa imewekeza nguvu zake zote kwenye huduma zijulikanazo kitaalamu kama Comprehensive Emergency Obstetric and Neonatal Care (CEmONC). Hizi ni package ya medical interventions ambazo zinahusisha kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, kumsaidia mama kwa kutumia njia za manual, lakini kumsaidia mama wakati wa kujifungua kama mtoto amekwama kwenye njia, pia kumuongezea damu mama mjamzito wakati wa kujifungua ama baada ya kujifungua, vile vile huduma za kutoa dawa ambazo zinajulikana kama urotonic ambazo zinasaidia ku-contract ile placenta wakati wa kujifungua ili kupunguza damu nyingi kupotea kwa mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile huduma za dawa zinazopunguza magonjwa ya kifafa cha mimba, magonjwa kama eclampsia, pre-eclampsia, gestational hypertension na magonjwa yote yanayohusiana na akina mama wajawazito. Sasa hii package inapaswa kutolewa kwenye vituo vya afya nchini, inaitwa CEmONC. Huduma hizi kwa kweli zilikuwa za kiwango cha chini sana. Katika vituo vya afya takribani 484 tulivyo navyo nchini vinavyomilikiwa na Serikali tulikuwa na vituo 113 tu vinavyotoa huduma hizi; lakini kwa mujibu wa sera vituo vyote vingepaswa kutoa huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana katika bajeti iliyopita hata kwenye bajeti hii tumejikita zaidi kwenye kuongeza idadi ya vituo ambavyo vitaweza kutoa huduma za CEmONC, na pia mkakati wetu umeendana sambamba na kuhakikisha hizo dawa nilizozisema kama oxytocin na magnesium sulphate zinapatika kwenye vituo vyote, hiyo ndiyo mikakati tuliyonayo. (Makofi)
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja dogo tu. Mheshimiwa Waziri nyumba zilizopo ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba, hasa Wilaya ya Mkoani ni chakavu sana. Je, Serikali ina mkakati gani kukarabati nyumba hizo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta swali hili. Ni kweli, hata mazingira ya kazi tu katika Mkoa wa Pemba ni magumu sana kufuatana na uchache wa nyumba za askari. Jambo hili Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilipigia sana akiwemo Balozi wa Askari, Mheshimiwa Faida Bakar.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, kama ambavyo nimesemea katika maeneo mengine ambayo yana hali tete za makazi ya askari, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ambaye nay eye amekuwa akifuatilia sana masuala ya askari, yakiwemo nyumba pamoja na haki zao nyingine yakiwemo madai kwamba, tutatoa kipaumbele kwa ajili ya nyumba hizo kwa sababu, mazingira ya kazi yanakuwa magumu pale askari wanapokosa makazi bora ya kukaa.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Elimu ya Watu Wazima imekuwa ni elimu dhaifu ndani ya mikoa yetu, ndani ya mikoa yetu iko chini yaani mikoa mingine hata haitambuliki kama kuna Elimu ya Watu Wazima. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia na kuboresha elimu hii ya watu wazima ili waweze kukabiliana na majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali ina mpango wa kuimarisha Vyuo vya Maendeleo (FDCs). Je, ni lini sasa Serikali itaimarisha Vyuo hivi vya Maendeleo ya Wananchi ili vijana waweze kupata elimu katika vyuo hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kwamba Elimu ya Watu Wazima imedhoofika katika baadhi ya maeneo, ni suala la mtizamo lakini kama tulivyosema rekodi tulizonazo ni kwamba karibia katika mikoa yote kuna vituo kwa ajili ya kutoa Elimu ya Watu Wazima. Mheshimiwa Mbunge labda kama atakutana na mimi ataniletea orodha ya mikoa ambayo anafikiri haifanyi kazi lakini nimhakikishie kwamba Elimu ya Watu Wazima bado ipo pale. Ni ukweli vilevile kwamba kadri tunavyozidi kuimarisha na kuboresha elimu ya mfumo rasmi mahitaji ya Elimu ya Watu Wazima kwa baadhi ya watu yanaanza kuonekana kwamba yamepungua lakini ukweli wa mambo ni kwamba bado kuna watu wengi ambao wanajifunza na kupata elimu kwa kupitia Elimu ya Watu Wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile swali lake kuhusiana na namna Serikali inavyoboresha Vituo vya Maendeleo vya Wananchi (FDCs), nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango unaoitwa ESPJ ambao pamoja na mambo mengine utajenga na kukarabati miundombinu ya Vyuo vya Wananchi 55 na baadae tutahakikisha watakuwa na rasilimali watu wa kutosha. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kupata fursa ili vijana wengi waweze kujifunza stadi za kazi na ufundi na hasa kwa sasa hivi ambapo tunakazania kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye uchumi wa kati ambapo rasilimali watu wa aina hiyo inahitajika.
MHE. MUNIRA M. KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kiwanda cha Urafiki hakizalishi kwa kiwango kinachotakiwa na kiwanda hiki kinamilikiwa na Wachina. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kiwanda hiki kinamilikiwa na Serikali ili kuongeza uzalishaji na kupata ajira kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Urafiki kimsingi kinamilikiwa na Wachina na kuna hisa ambazo ni za Serikali. Tumekuwa tukiwasiliana juu ya uboreshaji wa kiwanda hiki na kuhakikisha kwamba tunazalisha kwa kiwango kikubwa zaidi, hata hivyo, bado uzalishaji hauridhishi. Kwa hiyo, Serikali bado inaendelea kulifanyia kazi.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwa kuwa watumishi wengi hasa wanaoanza kazi wamekuwa wakiunganishwa kwenye mikataba ya wafanyakazi bila ya ridhaa yao.

Je, Serikali haioni haja sasa ya kutoa mwongozo kwa maafisa utumishi juu ya kulinda haki za watumishi hao?

Swali la pili, Serikali ina mkakati gani wa kujiondoa kuwa mawakala wa makato ya wafanyakazi?

SPIKA: Swali la pili liweke vizuri.

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, Je, Serikali ina mkakati gani wa kujiondoa kuwa mawakala wa vyama vya wafanyakazi?

SPIKA: Kivipi yaani, ili ujibiwe swali lako.

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu yake ya msingi, amesema vyama vya wafanyakazi, naomba ninukuu” watumishi wa vyama vya wafanyakazi licha ya kuwa na mamlaka nchini, wafanyakazi husika, vyama vya wafanyakazi hupitia vikao vyao , katiba kwa kufanya mabadiliko katika…

SPIKA: Ahsante sana Munira, Mheshimiwa Waziri jibu hilo swali la kwanza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, utaratibu wa wafanyakazi kujiunga katika vyama vya wafanyakazi ni utaratibu ambao umewekwa kwa mujibu wa sheria na kuna uhuru wa wafanyakazi kujiunga ambapo chama husika kwa kuzungumza na mwajiri, hufanya mikutano na kutoa elimu mbalimbali na baadaye ndiko wafanyakazi wanajiunga.

Mheshimiwa Spika, hivyo, niseme tu kwamba wafanyakazi wengi wanajiunga kwa mujibu wa taratibu za kisheria ambazo zimewekwa na Katiba na katika mazingira ambayo wafanyakazi wanalazimishwa kujiunga pasipo wao kufahamu na ridhaa yao, hiyo ni kinyume na utaratibu na nitoe tu maelekezo kwamba vyama vyote vya wafanyakazi vihakikishe kwamba vinazingatia sheria za kazi ili wanachama wote wanaojiunga wawe wanajiunga katika uhuru na ridhaa yao.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kudhibiti makampuni haya haramu kufanya biashara hii, ila yamekuepo baadhi ya makampuni haya yanayoendesha biashara hii kinyume na sheria. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia waathirika ambao fedha zao zimetapeliwa katika makampuni haya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; waathirika wakubwa wa biashara hii ni akina mama na vijana kutokana na mikopo yenye riba kubwa kwa mabenki, je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana na akinamama kuwapa mikopo yenye riba nafuu ili kuepukana na biashara hii haramu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kuwasaidia waathirika wa fedha hizi. Napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba washiriki wa biashara hii haramu wote, yule anayewashajihisha watu kufanya biashara hii na wale wanaoshiriki biashara hii wote wameshiriki kwenye biashara haramu kutokana na Sheria ya Makosa ya Jinai kama nilivyotaja kifungu 171A, B na C, wote wawili wanatenda kosa na wote wawili hawatakiwi kusaidiwa chochote zaidi ya kupata adhabu ya kushiriki katika biashara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; ni vipi Serikali inawasaidia vijana na akina mama; kwa dhamira njema kabisa Serikali yetu ilileta sheria hapa ya microfinance, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2018 ambapo kanuni zake zinakamilika na zitaanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 ili kuhakikisha vijana na akina mama wanapata mikopo kutoka kwenye taasisi halali ambazo zinatoza riba yenye kulipika, riba ambayo ni nafuu kabisa kwa vijana wetu na akina mama.

Lakini pili, Serikali yetu kupitia Bunge lako tukufu mwaka 2018 ilipitisha mabadiliko ya sheria kwenye Sheria ya Fedha kuhakikisha asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri inakuwa sasa ni lazima na ni sheria kwa Wakurugenzi wote wa halmashauri kutoa asilimia kumi hii na asilimia kumi hii ya mikopo inapotolewa haitozwi riba yoyote, riba yake ni sifuri ili akina mama na vijana wapate fedha hii waweze kufanya biashara zao bila kulipa riba yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia chini ya Wizara ya Fedha na Mipango tuna Taasisi ya Self Microfinance Bank ambayo inatoa mikopo katika riba nafuu sana kwa akina mama na vijana na imefanya vizuri katika mikoa mbalimbali. Naomba niwaombe na niwatake vijana wetu na akinamama wasijihusishe kwenye biashara haramu ila waende kwenye taasisi ambazo ni halali zenye dhamira njema ya kujenga uchumi wa taifa letu.